TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KUMI Juzuu 10

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA

IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED

IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.

Kama lilivyo jina la Tafsiri yenyewe ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo. Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.

Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea, hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho 'Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah' (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka hivi karibuni Inshaallah).

Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasyansi kama kina Enstein, Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.

Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.

Mwisho: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.

MAKOSA YA CHAPA

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa, Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146). Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua), Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa "Fawqahum ila yawmil qiyama” badala ya “Fawqahum yawamal qiyama", Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu jabal amail 'Makosa ya chapa.'

Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: " Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"

Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.

Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa, kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu."

Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubali- ayale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH


1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

Mwendelezo Wa Sura Ya Nane: Surat Al-Anfal

وَاعْلَمُوا أَنَّمَا غَنِمْتُم مِّن شَيْءٍ فَأَنَّ لِلَّـهِ خُمُسَهُ وَلِلرَّسُولِ وَلِذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ إِن كُنتُمْ آمَنتُم بِاللَّـهِ وَمَا أَنزَلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا يَوْمَ الْفُرْقَانِ يَوْمَ الْتَقَى الْجَمْعَانِ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٤١﴾

41. Na jueni kwamba chochote mlichopata ghanima, basi khumsi yake ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume na jamaa na mayatima na masikini na msafiri. Ikiwa nyinyi mmemwamini Mwenyezi Mungu na tuliyoteremsha kwa mja wetu siku ya upambanuzi, siku yalipokutana majeshi mawili. Na Mwenyezi Mungu ni muweza juu ya kila kitu.

KHUMS

Aya 41

LUGHA

Neno; Ghanima kwa lugha ya kiarabu lina maana ya kupata kitu. Wametofautiana kuhusu maana ya Fay-u kwa kauli mbili: kauli ya Kwanza kuwa ni ghanima, na kauli ya pili kuwa ni mali inayochukuliwa bila ya vita.

Ama kuhusu Nafal yametangulia maelezo yake mwanzo wa Sura hii. Makusudio ya jamaa ni jamaa za Mtume. Yatima ni yule aliyefiwa na baba yake kabla ya kubaleghe. Na Khums ni humusi (sehemu moja ya tano).

MAANA

Na jueni kwamba chochote mlichopata ghanima, basi khumsi yake ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume na jamaa na mayatima na masikini na msafiri.

Wafasiri wamefanya utafiti katika pande nyingi kuhusu Aya hii, Ama sisi tutatosheka na pande mbili tu:

Kwanza: dhahiri ya Aya inafahamisha pande hizo mbili.

Pili: kwamba upande mwingine hautumiki. Katika pande hizo mbili tutakazozitaja ni kueleza maana ya neno ghanima na kubainisha wale wanaostahiki Khumsi.

Wametofautiana Sunni na Shia kuhusu makusudio ya neno ghanima katika Aya. Sunni wamesema ni ngawira wanayoiteka waislamu kutoka kwa makafiri kwa vita.

Kulingana na kauli yao hii, suala la Khums linakuwa kwao halipo siku hizi; sawa na suala la utumwa. Kwa vile hakuna dola ya kiislamu inayopigana jihadi na makafiri na washirikina hivi sasa.

Shia wamesema kuwa ghanima ni zaidi ya ngawira ya vita inayochukuliwa na Waislamu kutoka kwa makafiri, na kwamba inakusanya madini; kama vile mafuta ya petroli, dhahabu nk. Vile vile dafina ikiwa haijulikani mwenyewe na wanavyovitoa watu kutoka baharini kwa kuzamia; kama vile lulu.

Nyingine ni mali inayozidi gharama za mtu yeye na watoto wake katika chumo la mwaka, mali ya halali iliyochanganyika na ya haramu na haijulikani kiwango cha haramu.

Pia ghanima ni ardhi aliyoinunua kafir dhimmi kutoka kwa Mwislamu. Ufafanuzi uko kwenye vitabu vya Fiqh, kikiwemo Fiqh Imam Jaffer As Sadiq Juz.2. Kulingana na kauli ya Shia suala ya khums linakuwa bado lipo.

Kama walivyotofautiana katika maana ya ghanima, vile vile wametofau- tiana katika idadi ya mafungu ya khums na wanaostahiki.

Shia wamesema: khums hugawanywa mafungu mawili: La kwanza litagawanywa mafungu matatu: Fungu la Mwenyezi Mungu, la Mtume wake na la jamaa. Lile la Mweneyzi Mungu ni la Mtume na la Mtume ni la jamaa zake.

Na msimamizi wa jamaa baada ya Mtume ni Imam anayesimamia kazi za Mtume. Akiweko atapewa yeye; kama hayuko basi ni wajibu kulitoa fungu hilo katika maslahi ya kidini, ambayo muhimu zake ni kuutangaza Uislamu na kazi ya kuusambaza na kuutukuza.

Ama fungu la pili, nalo lina sehemu ya mayatima wa ukoo wa Muhammad(s.a.w.w) , masikini wao na wasafiri wao. Wanaohusika katika fungu hilo ni ukoo wa Muhammad(s.a.w.w) tu peke yao, Kwa sababu Mwenyezi Mungu anawaharamishia sadaka akawawekea Khums.

Tabari katika tafsir yake na Abu Hayan Al-Andalus katika Bahrul-Muhit wanasema: “Amesema Ali bin Abu Talib(a.s) :Mayatima na maskini ni mayatima wetu. Anaongeza Tabari: “Ali bin Hussein (r.a) alimwambia mtu mmoja kutoka Sham: Je, hukusoma katika Sura Anfal:“Na jueni kwamba chochote mlichopata ghanima, basi hakika khums yake ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume na jamaa na mayatima na masikini na msafiri.

Akasema yule mtu: “Naam! Kwani ndiyo nyinyi? Akasema: ndiyo” Ama wasemavyo Sunni, tuwaachie maulamaa wawili wakubwa, mmoja wao ni wa zamani, Razi, na mwingine ni wa hivi karibuni, Maraghi, mmoja wa Masheikh wa Az-har na rais wake wakati wake.

Razi anasema: “Kauli zilizo mashuhuri ni kwamba hiyo humusi ni sehemu tano:

1. Mtume wa Mwenyezi Mungu.

2. Jamaa zake katika Bani Hashim, na Bani Muttwalib, sio Bani Abdu Shams (Umayya) na Bani Naufal.

3. Mayatima.

4. Masikini.

5. Wasafiri.

“Hiyo ni katika uhai wa Mtume wa Mwenyezi Mungu. Ama baada ya kufa kwake(s.a.w.w) , kwa upande wa Shafii sehemu ni tano.

Ya Mtume wa Mwenyezi Mungu, inatolewa kwenye maslahi ya Waislamu, ya jamaa matajiri na makufara, ilyobaki ni ya mayatima, maskini na wasafiri.

Abu Hanifa anasema kuwa sehemu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu inaondoka baada ya kufa kwake kwa saba Na hugawanywa Khums kwa mayatima, maskini na wasafiri. Malik naye anasema: “Mambo ya khums huachiwa rai ya Imam.”

Sheikh Maraghi anasema: “Amepokea Bukhari kutoka kwa Mut’im bin Jubair wa Bani Nawfal, kwamba yeye alikwenda na Uthman bin Affan wa Bani Abd Shams kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) akawaambia: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Umewapa Bani Muttalib na ukatuacha na hali sisi na wao ni daraja moja. Akasema Mtume(s.a.w.w) : “Hakika Bani Muttalib na Bani Hashim ni kitu kimoja.”

Sheikh Maraghi anaongezea juu ya Hadith hii kwa kusema, na siri ya hilo ni kwamba Makuraish walipoandika maazimio yao ya kuwatoa Bani Hashim Makka na kuwazuia katika Shii’b waliingia humo pamoja na Bani Muttalib, na wala hawakuingia Bani Abu Shams wala Bani Nawfal kwa uadui waliokuwa nao na Bani Hashim wakati wa Jahaliyya na wakati wa Uislamu.

Akawa Abu Sufyan anapigana na Mtume(s.a.w.w) na kuungana na washirikina na watu wa Kitab dhidi yake, mpaka Mwenyezi Mungu alipompa ushindi Mtume wake na Waarabu wakaingia kwenye dini kwa ushindi wa Makka. Vile vile baada ya Uislamu Muawiya alimtokea Ali na akapigana naye.

Nasi tunaungia maneno ya Sheikh Maraghi kuwa vile vile Yazid mjukuu wa Abu Sufyan alimuuwa Hussein Bin Ali, mjukuu wa Mtume(s.a.w.w) . Mshairi anasema kuhusu uadui huu wa kurithiana baba na babu.

Bin Harb na Mustwafa, Aliy na mwana wa Hind, Husein hawakumfaa, alipambana na Yazid

Ikiwa nyinyi mmemwamini Mwenyezi Mungu na tuliyoteremsha kwa mja wetu siku ya upambanuzi, siku yalipokutana majeshi mawili. Na Mwenyezi Mungu ni muweza juu ya kila kitu.

Wafasiri wanasema kuwa makusudio ya siku ya upambanuzi na siku yalipokutana majeshi mawili ni siku ya Badr. Kwa sababu Mwenyezi Mungu alifarikisha baina ya ukafiri na imani kwa kuuweka Uislamu juu ya shirk. Vile vile ni siku yalipokutana majeshi mawili, la waumini na la washirikina ambapo jeshi la washirikina waliipata.

Maana ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakubali kumwamini yeye, vitabu vyake na Mitume yake kama nadharia tu, bila ya vitendo, isipokuwa anakubali imani ya anayehukumu na kufanya amali kwa anavyohukumu Mwenyezi Mungu.

Razi anasema: “Kauli yake Mwenyezi Mungu: Mkiwa mmemwamini Mwenyezi Mungu, inafahamisha kuwa ikiwa haukupatikana ugavi huu, kama alivyohukumu Mwenyezi Mungu, basi imani nayo haipo.”

Nasi tunaongezea juu ya kauli ya Razi kuwa vile vile ikiwa hukumu haikupatikana katika usiokuwa ugavi huu, kama alivyohukumu Mwenyezi Mungu, basi imani nayo haitapatikana. Kwa vile, sababu inayowajibisha ukafiri ni moja nayo ni kuhalifu hukumu ya Mwenyezi Mungu makusudi. Kimisingi ni kwamba sababu hii haikubali kufungwa wala kuhusishwa na jambo moja tu.

Tumeeleza mara nyingi kwamba makusudio ya ukafiri katika mfano huu ni ukafiri wa kimatendo, yaani ufasiki sio ukafiri wa kiitikadi.

إِذْ أَنتُم بِالْعُدْوَةِ الدُّنْيَا وَهُم بِالْعُدْوَةِ الْقُصْوَىٰ وَالرَّكْبُ أَسْفَلَ مِنكُمْ وَلَوْ تَوَاعَدتُّمْ لَاخْتَلَفْتُمْ فِي الْمِيعَادِ وَلَـٰكِن لِّيَقْضِيَ اللَّـهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا لِّيَهْلِكَ مَنْ هَلَكَ عَن بَيِّنَةٍ وَيَحْيَىٰ مَنْ حَيَّ عَن بَيِّنَةٍ وَإِنَّ اللَّـهَ لَسَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٤٢﴾

42. Mlipokuwa kando ya bonde lililo karibu, nao wako kando ya bonde lililo mbali; na msafara upo chini yenu, Na lau mngeliagana mngelihitalifiana katika miadi. Lakini ili Mwenyezi Mungu alitimize jambo lililokuwa lifanyike Ili aangamie wa kuangamia kwa dalili dhahiri na awe hai wa kuwa hai kwa dalili dhahiri. Na hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kujua.

إِذْ يُرِيكَهُمُ اللَّـهُ فِي مَنَامِكَ قَلِيلًا وَلَوْ أَرَاكَهُمْ كَثِيرًا لَّفَشِلْتُمْ وَلَتَنَازَعْتُمْ فِي الْأَمْرِ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ سَلَّمَ إِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ ﴿٤٣﴾

43. Alipokuonyesha katika usingizi wako kuwa ni wachache. Na lau angelikuonyesha kuwa ni wengi mngelivunjika moyo na mngelizozana katika jambo hilo, lakini Mwenyezi Mungu alilinda. Hakika yeye ni mjuzi wa yalimo vifuani.

وَإِذْ يُرِيكُمُوهُمْ إِذِ الْتَقَيْتُمْ فِي أَعْيُنِكُمْ قَلِيلًا وَيُقَلِّلُكُمْ فِي أَعْيُنِهِمْ لِيَقْضِيَ اللَّـهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا وَإِلَى اللَّـهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ ﴿٤٤﴾

44. Na alipowaonyesha machoni mwenu mlipokutana kuwa ni wachache Na akawafanya nyinyi kuwa wachache machoni mwao ili Mwenyezi Mungu alitimize jambo lililokuwa lifanyike.

MLIPOKUWA KANDO YA BONDE LILILOKARIBU

Aya 42 – 44

MAANA

Aya hizi zinaonyesha baadhi ya sababu ambazo aliziandaa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ushindi wa waislamu kwa washirikina katika vita vya Badr. Miongoni mwa sababu hizo ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwapa ilhamu waislam kujiweka mwenye bonde lililo karibu na Madina. Ama washirikina wao walikuwa upande ulio mbali zaidi na hapa; na kati ya pande mbili kulikuwa na kilima kinachotenganisha.

Kulingana na mfumo wa maneno, inaonyesha kuwa upande wa waislamu ulikuwa ndio mahali pa vita walipomkusudia adui yao, Ni katika mipango yake Mwenyezi Mungu kuliweka kila jeshi mahali pake bila ya kujuana. Kwani lau waislamu wangeliwaona maadui zao kwa macho, wangeliogopa na kukata tamaa ya kuwashinda.

Vile vile ni katika mipango yake Mwenyezi Mungu, kwamba yeye – imetukuka hekima yake – aliwafanya wachache washirikina kwenye macho ya waislam walipokutana. Yote hayo ni kwa ajili kuidhirisha dini yake juu ya dini zote, hata kama watachukia washirikina.

Pia ni katika hekima yake kuwa Abu Sufyan aupeleka msafara wa ngamia kwenye mwambao wa bahari, ili majeshi mawili, ya batili na haki, yakutane na wala waislamu wasifuate msafara tu wakaacha jeshi.

Baada ya utangulizi huu, sasa tunaingilia kufasiri Aya:

Mlipokuwa kando ya bonde lililo karibu, nao wako kando ya bonde lililo mbali.

Msemo unatoka kwa Mwenyezi Mungu kuelekezwa kwa waislamu, akiwakumbusha mahali walipokuwa - kando ya bonde lililo karibu ya Madina, na mahali walipokuwa washirikina nao ni upande wa mbali: Vile vile anawakumbusha kugeuza njia kwa msafara wa ngamia kuelekea mwambao wa bahari, ambako Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekuashiria kwa kauli yake:

Na msafara upo chini yenu.

Lengo la ukumbusho huu ni kwamba mambo yote yalikuwa kwa masilahi yao; kama ilivyobainika.

Na lau mngeliagana mngelihitalifiana katika miadi.

Waislamu walitoka pamoja na Mtume(s.a.w.w) kufuatia msafara wa ngamia na mizigo yake, bila ya kukusudia kupigana, lakini Mwenyezi Mungu akaigeuza safari hii ya kufuatia mali kuwa ya kupigania jihadi katika njia yake.

Hilo likawa ni heri kubwa kwao. Lau kama tangu mwanzo wangelijua kuwa wanakwenda kupigana na washirikina; kisha wakajua wingi wao, basi baadhi ya waislamu wangeligeuka kwa hofu, na kutofautiana na wale watakaotaka kupigana, Matokeo yake ushindi usingelipatikana.

Lakini ili Mwenyezi Mungu alitimize jambo lililokuwa lifanyike.

Yaani lakini Mwenyezi Mungu alipanga kukutana huku bila ya ahadi, ili litimie alilokukusudia la kutukuka dini na kudhalilika washirikina.

Ili aangamie wa kuangamia kwa dalili dhahiri na awe hai wa kuwa hai kwa dalili dhahiri.

Makusudio ya mwenye kuangamia ni kafiri, na mwenye kuwa hai ni yule mwenye kuamini. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwanusuru vipenzi vyake na kuwashinda nguvu maadui zake, siku ya Badr ili hilo liwe ni hoja mkataa kwa yule mwenye kupinga na hoja dhahiri kwa mwenye kuamini.

Utauliza : Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa mwenye kushindana na haki atashindwa, lakini tujuavyo, wabatilifu mara nying si wanaishinda haki?

Jibu : Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaahidi ushindi waislamu kupitia kwa Mtume wake, kabla ya vita, ingawaje walikuwa wachache na wanyonge; kama alivyosema katika Aya ya 7 ya sura hii: “Na alipowaahidi moja ya makundi mawaili kuwa ni lenu.” Mwenyezi Mungu akatekeleza ahadi hiyo, ukathibiti muujiiza wa Muhammad(s.a.w.w) aliyewapa habari ya ushin- di wakati ambapo dalili zote zilionyesha ni kinyume na hivyo.

Zaidi ya hayo walisaidiwa na malaika, kama inavyofahamisha Aya ya 9 na fumba la mchanga au changarawe alilowatupia mtume(s.a.w.w) ; kama ilivyo katika Aya ya 17. Yote haya na mengineyo yalikuwa ni muujiza wa wazi uliodhihiri mikononi mwa Muhammad, siku ya Badr. Na ndiyo makusudio ya dalili dhahiri kwa anayekufuru na dalili dhahiri kwa anayeamini; na wala sio ushindi tu.

Kwa maneno mengine ni kutoa habari ya ushindi kabla ya kutokea kwake pamoja na miujiza; na wala sio makusudio ya ushindi wenyewe.

Na hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kujua.

Hakifichuki chochote katika kauli na vitendo na yanayopita nyoyoni.

Alipokuonyesha katika usingizi wako kuwa ni wachache. Na lau angelikuonyesha kuwa ni wengi mngelivunjika moyo na mngelizozana katika jambo (hilo), lakini Mwenyezi Mungu alilinda.

Huu nao ni muujiza mwingine wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Nao ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwonyesha usingizini kwamba washirikina ni wachache tena madhaifu; na kushujaika. Lau Mwenyezi Mungu angelimuonyesha kuwa maadui wana nguvu, basi azma ya waislamu ingelidhoofika, wakawa wanyonge wa kupigana na kutofautiana. Hilo lingelifuatiwa na kushindwa. Lakini Mwenyezi Mungu alilinda tatizo hili na akawahurumia waja wake waumini.

Hakika yeye ni mjuzi wa yalimo vifuani.

Yaani anajua kuwa nyoyo za waislamu zitahisi hofu ya kupigana zikijua wingi wa adui; ndipo akiziweka mbali, Mwenyezi Mungu, hisia hizi kwa alivyoona Mtume uchache wa maadui usingizini.

Na alipowaonyesha machoni mwenu mlipokutana kuwa ni wachache ili muwe imara enyi waislamu, na muwe na ukakamavu na uthabiti katika kupigana na adui yenu. Na akawafanya nyinyi kuwa wachache machoni mwao ili wasijiandae sana kupigana nanyi na kuchukua hadhari.

Hivyo ndiyo ilivyokuwa; hata Abu Jahl akasema: “Watu wa Muhammad ni mboga tu.” Mwisho wa dharau hii ulikuwa ni balaa na udhalili.

Matukio yamethibitisha kuwa silaha kubwa iliyo mkononi mwa adui ni kudharau na kutojiandaa vizuri.

Ili Mwenyezi Mungu alitimize jambo lililokuwa lifanyike.

Wafasiri wamesema: Jumla hii imekaririka kwa vile sababu yake katika Aya ya kwanza ni kukusanyika waislamu na washirikina katika vita bila ya miadi. Ama sababu katika Aya hii imekuja kwa kufanyisha uchache kila kundi machoni mwa mwenzake.

Nasi tumetangulia kusema kuwa kukaririka katika Qur’an ni aina ya utangazaji uliofaulu.

Na kwa Mwenyezi Mungu hurejeshwa mambo yote.

Hutokea kwake na huishia kwake. Yeye ndiye mwenye kuyapanga kwa uadilifu wake na hekima yake.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا لَقِيتُمْ فِئَةً فَاثْبُتُوا وَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٤٥﴾

45. Enyi mlioamini! Mnapokutana na jeshi, basi kazaneni, na mumkumbuke Mwenyezi Mungu sana ili mpate kufaulu.

وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ وَاصْبِرُوا إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ ﴿٤٦﴾

46. Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala msizozane, msije mkavunjika moyo na zikapotea nguvu zenu, na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri.

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ خَرَجُوا مِن دِيَارِهِم بَطَرًا وَرِئَاءَ النَّاسِ وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَاللَّـهُ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ ﴿٤٧﴾

47. Wala msiwe kama wale waliotoka majumbani mwao kwa fahari na kujionyesha kwa watu, na kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu: Na Mwenyezi Mungu ameyazunguka wanayoyafanya.

وَإِذْ زَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ وَقَالَ لَا غَالِبَ لَكُمُ الْيَوْمَ مِنَ النَّاسِ وَإِنِّي جَارٌ لَّكُمْ فَلَمَّا تَرَاءَتِ الْفِئَتَانِ نَكَصَ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ وَقَالَ إِنِّي بَرِيءٌ مِّنكُمْ إِنِّي أَرَىٰ مَا لَا تَرَوْنَ إِنِّي أَخَافُ اللَّـهَ وَاللَّـهُ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٤٨﴾

48. Na shetani alipowapambia vitendo vyao, na kusema: Leo hakuna wa kuwashinda na hali mimi ni mlinzi wenu. Yalipoonana majeshi mawili, alirudi nyuma na kusema: Mimi si pamoja nanyi, mimi naona msiyoyaona, mimi namwogopa, Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

إِذْ يَقُولُ الْمُنَافِقُونَ وَالَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ غَرَّ هَـٰؤُلَاءِ دِينُهُمْ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَإِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٤٩﴾

49. Waliposema wanafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao: Hawa imewadanganya dini yao, Na mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu, basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.

MNAPOKUTANA NA JESHI KAZANENI

Aya 45 – 49

MAANA

YANAYOLETA USHINDI

Enyi mlioamini! Mnapokutana na jeshi, basi kazaneni, na mumkumbuke Mwenyezi Mungu sana ili mpate kufaulu.

Makusudio ya jeshi ni lile linalofanya ufisadi katika nchi. Kauli yake Mwenyezi Mungu ili mpate kufaulu yaani mlishinde.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja mambo mawili yanayoleta ushindi katika Aya hii:

La kwanza: ni uthabiti na ushupavu, aliposema; “Kazaneni.”

La pili: ni ikhlas, aliposema “Mkumbukeni Mwenyezi Mungu sana.” Makusudio ya kumkumbuka Mungu vitani sio dhikri ya takbira na tahalili tu; isipokuwa ni kuwe kupigana na ukakamavu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu; kwa maana ya kutoathirika vita na hali yoyote isipokuwa kwa ajili ya kuthibitika haki na kubatilika batili; kwa ajili ya kuhifadhi amani ya watu na usalama wao; na kuwapiga waovu wanaoeneza ufisadi katika nchi kwa kunyanganya na kupora huku wakileta vita na fitina ili watawale miji na riziki za waja.

Na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala msizozane, msije mkavunjika moyo na kupoteza nguvu zenu, na subirini. Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja katika Aya iliyotangulia mambo mawili ya kuleta ushindi; na katika Aya hii anataja matatu: Kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume, kujiepusha na mizozo na kusubiri (kuvumilia.) Lakini kuwa na subira ndiko kukazana. Kwa hiyo kauli yake Mwenyezi Mungu: Subirini ni ibara nyingine ya kazaneni; kama ambavyo kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake ndiyo ikhlasi. Ama kutofautiana kwingine ni kuzuri na kwengine ni kubaya, Ufafanuzi utafuatia.

Kwa ufupi mambo yanayoleta ushindi wa hakika yaliyoelezwa katika Aya mbili ni matatu:

1. Subira na kukazana, nako ni kujitolea mhanga kwa moyo wote ili kuinusuru haki ishinde batili; kama ambavyo haki inashinda kwa kuondoka batili, vile vile haki inashinda kwa kufichuka batili na kuidhihirisha kwa watu.

Subira ni lazima katika kufika lengo lolote. Hakuna mwanafunzi, mwalimu, mgunduzi, au mfanyi biashara yeyote anayeweza kupata kitu bila ya subira (uvuumilivu) na kukazana. Kiwango cha kuvumilia kwake mashaka na uchungu ndicho kiwango cha kufaulu kwake, Na hii ndiyo siri ya kauli yake Mwenyezi Mungu.

Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri

وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ ﴿١٥٥﴾

“Wape habari njema wanaosubiri (2:155)

وَلَا يُلَقَّاهَا إِلَّا الصَّابِرُونَ ﴿٨٠﴾

Wala hawatapewa hayo isipokuwa wanaosubiri” (28:80)

وَلَئِن صَبَرْتُمْ لَهُوَ خَيْرٌ لِّلصَّابِرِينَ ﴿١٢٦﴾

“Na kama mkivumilia hiyo ni kheri kwa wanaosubiri” (16:126) na Aya nyinginezo.

Mimi nimejaribu kuwa na subira nilipokuwa mwanafunzi na mtunzi. Sikuona kitu chenye mwisho mtamu na manufaa kama hicho. Tumezungumzia kuhusu kuwa na subira na uvimilivu katika Juz.2 (Sura 2:155)

2. Ikhlasi: Kukusudia kitendo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kumtegemea yeye sio mwingine na kuamini kwa imani mkato kwamba yaliyoko mbele ya Mwenyezi Mungu ni bora na yatasalia kuliko jaha, mali na watoto, kisimwaathiri chochote katika hivi na kumtii Mwenyezi Mungu na radhi yake.

Mtu huweza kufikia malengo yake ya kishetani, lakini haya hayahisabiwi kuwa ni ushindi, ila kama tukizingatia batili ni fadhila, wizi ni ghanima na ufisadi ni takua na utengenevu.

3. Kujiepusha na aina yoyote ya kutofautiana. Inaweza kutokea kutofautiana katika maoni na mtazamo kwa ikhlasi. Kutofautiana huku hakupingani na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wala hakuzuii kuafikiana lengo; kama vile kupigana jihadi na wafisadi. Mara nyingi huko kunakuwa ni njia ya kufunguka uhakika.

Vile vile inaweza kuwa sababu ya kutofautiana ni hawaa, na ubinafsi na kupupia dunia. Hayo ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu: “Wala msizozane msije mkaharibikiwa na kupoteza nguvu zetu.”

Mifano ya madhara ya kuzozana na kushindana haina idadi, na katika Historia ni mamia. Hatuna haja ya kutoa mfano wa historia ya mbali, Historia yetu tu ya sasa hivi inatutosha kwa mifano yote. Hivi karibuni nimesoma makala ya mwandishi wa Kimarekani, Salz Bridge aliyoiandika katika gazeti la Herald Tribune. Ninamnukuu:

“Washington inapima tofauti ya idadi ya waarabu na Israil; na inasisitiza kwamba, hata kama si kwa masilahi ya Israil, lakini daima kipimo kitakuwa ni kugawanyika kunakoendelea baina ya dola za kiarabu. Kwa sababu kugawanyika huku kunaifanya idadi ya waarabu iwe ni nambari tu, isiyokuwa na thamani yoyote.”

Kabla ya mwandishi huyu viongozi wa Israil wametangaza mara nyingi kuwa wao walifaulu katika vita vya tarehe 5 Juni kwa msaada wa Marekani na kutofautiana kwa waarabu. Na ni kitu gani kilichowapendeza waisrail kuliko kushikiana silaha waarabu wenyewe kwa wenyewe, badala ya kuwashikia Israil? Kwa ajili hiyo wakoloni wa kizayuni wamefanya kila wawezalo kuwagombanisha waarabu. Jambo la kusikitisha ni kuwa wamepatikana waliowaitikia, bali wanaozungumza kwa niaba yao, Hata hivyo, mapambano bado yanaendelea. Ni lazima wakoloni na vibaraka wao watashindwa, sasa au baadaye.

Wala msiwe kama wale waliotoka majumbani mwao kwa fahari na kujionyesha kwa watu, na kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu, Na Mwenyezi Mungu ameyazunguka wanayoyafanya.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwaamrisha waislamu mambo matatu wakiwa wanawaelekea vitani, sasa anawakataza mambo matatu: fahari, kujionyesha, na kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu.

Amenasibisha sifa hizi tatu kwa makafiri wa kiquraish kwa sababu wao waliotoka kuelekea Badr kumpiga vita Mtume(s.a.w.w) wakiwa wanajifaharisha, wanajionyesha na kuwazuilia waislamu na njia ya Mwenyezi Mungu.

Wafasiri wanasema: Abu Jahli alipokuwa akiwaongoza maquraish kumpiga vita Mtume huko Badr, njiani alijiwa na Ibn Al-Hiqaf Al-Kinaniy na zawadi kutoka kwa baba yake. Akamwambia Abu Jahli: “Baba yangu anakwambia, kama unataka atakuongozea watu, na kama unataka nitaungana nawe.” Abu Jahli akasema “Ikiwa tunapigana na Mwenyezi Mungu, kama anavyodai Muhammad, basi Wallahi hatumuwezi Mwenyezi Mungu na ikiwa tunapigana na watu, basi sisi ndio watu wenye nguvu zaidi, wala hatutarudi nyuma kupigana na Muhammad mpaka tufike Badr tunywe pombe na watuimbie watumwa na waarabu wasikie.”

Kujifaharisha kunadhihiri katika maana yake pana kwa kauli ya Abu Jahl: “Na sisi ni watu wenye nguvu zaidi.” Ama kujionyesha kuko katika kauli yake: “Na waarabu wasikie” Kwa ajili hii basi nasi tunaelemea kwenye kauli ya mwenye kusema kuwa Aya hii imemshukia Abu Jahli.

Ama mwisho wa fahari hiyo na ria ni kuuawa waliouawa, akiwemo Abu Jahli na kutekwa waliotekwa na kushindwa waliobakia.

Na shetani alipowapambia vitendo vyao, na kusema: Leo hakuna wa kuwashinda na hali mimi ni mlinzi wenu. Yalipoonana majeshi mawili, alirudi nyuma na kusema: Mimi si pamoja nanyi, mimi naona msiyoyaona, mimi namwogopa, Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

Aya hii inasema waziwazi kuwa kuna kitu kinachoitwa Shetani kiliwachochea maquraish kumpiga vita Mtume huko Badr na kuwapa dhamana ya ushindi, na kwamba yeye alipoyakinisha mwisho wao alijitoa.

Tumekwishaelezea mara nyingi kwamba sisi tunaamini kila linaoelezwa na wahyi na lisilokataliwa na akili; na kwamba tunaiachia ghaibu ufafanuzi. Hakuna kitu katika hukumu ya akili kinachozuia kupatikana kitu kinachoonekana au kisichoonekana kinachowatia mshawasha watu kwenye batili na kuwahadaa. Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwamrisha Mtume wake mtukufu ajilinde na shari ya mwenye kutia wasiwasi katika nyoyo za watu, awe jini au mtu.

Waliposema wanafiki na wale wenye maradhi nyoyoni mwao: Hawa imewadanganya dini yao. Na mwenye kutegemea kwa Mwenyezi Mungu, basi hakika Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.

Wanafiki ni wale wanaodhihirisha Uislamu na kuficha ukafiri. Ama wale ambao nyoyoni mwao mna maradhi, ni wanafiki, makafiri na mafasiki.

Kwa hiyo kuunganisha wenye maradhi nyoyonni juu ya wanafiki ni kati- ka kuunganisha jumla juu ya mahsusi.

Mwenyezi Mungu amesimulia, katika Aya hii, kuhusu wenye maradhi ya moyo, kwamba wao walishangaa walipoona kujitokeza kwa waislamu wachache wa kupigana vita na makafiri; wala hawakufahamu tafsir ya kujitokeza huku isipokuwa kujiangamzia kwa waislamu na kuhadaliwa na matumaini ya kufuzu pepo. Kwao hayo ni maneno yasiyo na maana. Kwa sababu kila kitu kwao ni biashara tu; hata dini.

JE WAKOMBOZI NI WAHARIBIFU?

Wakati huu ambapo nguvu za shari zimeungana kuwafanyia njama waarabu na waislamu na kuwafukuza wazalendo wa Palestina katika ardhi zao na kuwatupa ufuoni wanawake, wazee na watoto; wakati huu ambapo wakombozi wanawanyima usingizi waisrail na kuwakosesha raha; na kutamka neno, uhuru juu ya ukombozi wa ardhi iliyovamiwa, ndipo anaposema Sheikh mwenye kilemba kwenye mpaka wa Israil katika kijiji kimoja cha kaskazini, akinadi kwa kupaza sauti kadamnasi na kusema: “Wakombozi ni waharibifu” sawa na anavyosema Moshe Dayan.

Ewe mheshimiwa! Wakombozi ni waharibifu! Je, wewe na Israil ndio watengenezaji? Kwa nini wakombozi wawe waharibifu? Je, ni kwa kuwa wanapigania haki zao, katika njia ya kuuawa na kuua; au ni kwa vile wao wamebadilisha jina la wakimbizi na kuwa wakombozi? Na, je, wewe katika kauli yako hii unamtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kupigana jihadi kutekeleza wajibu wa kidini na wa kiuzalendo?

Ni dini gani hiyo inayokataza kujitolea mhanga kwa ajili ya kulinda mtu nchi yake na kutaka kuishi huru na kuheshimiwa; hata kwa thamani ya namna gani?

Mimi nimeelewa mantiki yako ewe Sheikh, Wewe unasema kuwa Israil inajibu mashambulizi ya wakombozi kwa kuwatesa wanyonge, nasi twakuuliiza: Walikuwa wapi wakombozi mnamo tarehe 29 Juni 1897, wakati Uzayuni ulipofanya mkutano mkuu huko Uswisi, na kupitisha azimio la kuwafukuza waarabu Palestina na waikalie Mayahudi? Je, azimio hilo lilitokana na wakombozi wakati huo?

Kisha utasema nini kuhusu mauaji ya Diryasin na uchinjaji ulofanywa na Mayahudi kwa wakazi wasio na hatia, kabla ya jeshi kuingia Palestina?

Inakupasa ujue ewe mwenye kilemba cha usheikh na kila Mwarabu kwamba waisrail hawatosheki tu na Palestina, Jordan, Lebanon, Syria na Iraq; isipokuwa lengo lake ni kuwadhalilisha waarabu wote wanyenyekee Uzayuni na ukoloni kisiasa na kiuchumi. Israil inatamani mafuta ya Kuwait, Qatar, Abu Dhabi na Saudia.

Tamaa yao hii wameipanga na kuiwekea mkakati kwa kula njama pamoja na dola za kikoloni, Harakati za wakombozi ndizo zilizoharibu mikakati hii ya waisrail kiasi cha kufikiria kuwa Israil haitakuwako.

Ni bora mara elfu tuvumilie maumivu yanayosababishwa na vitendo vya wakombozi, kuliko kuwacha yatimie malengo ya Israil ambayo haiatoshe- ki na chochote; hata mto Nail na Furat.

Zaidi ya hayo, hivi sasa inatulazimu kumkabili adui kwa kupatikana wakombozi wa kujitolea mhanga; kama hatua ya kwanza na tuvumilie taabu zote zitakazosababishwa nao ili kukinga ambalo ni baya na kubwa zaidi.

Baada ya hayo, ewe Sheikh! Unasemaje kuhusu vikosi vilivyokuwa vikitumwa na Muhammad(s.a.w.w) kukata njia ya maadui zake washirikina na kuchukua mali zao, kuua na kuchukua mateka na kuwakosesha amani majumbani akiwa yeyey mwenye binafsiakiongoza baadhi ya mashmbulizi hayo; kama alivyowapiga Mayahudi wa Bani Quraidha baada ya kuvunja ahadi na kujiiunga na Abu Sufyan, adui wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika vita vya Ahzab.

Mtume(s.a.w.w) aliliamrisha jeshi lake alilokuwa akiliongoza yeye mwenyewe lichome mimea ya mayahudi, na kukata miti yao na kuvunja majumba yao, Je, kitendo chake hicho Mtume kilikuwa cha utengezaji au uharibifu?

Imepokewa Hadith Mutawatir aliposema Mtume(s.a.w.w) : “Mwenye kufa akilinda mali yake amekufa Shahid” Je vipi kwa yule atakayokufa katika hali ya kumzuia Mwisrail adui wa Mwenyezi Mungu, wa nchi na wa binadamu wote?

Mwenyezi Mungu anasema:

إِنَّ اللَّـهَ اشْتَرَىٰ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ أَنفُسَهُمْ وَأَمْوَالَهُم بِأَنَّ لَهُمُ الْجَنَّةَ يُقَاتِلُونَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَيَقْتُلُونَ وَيُقْتَلُونَ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ وَالْقُرْآنِ وَمَنْ أَوْفَىٰ بِعَهْدِهِ مِنَ اللَّـهِ فَاسْتَبْشِرُوا بِبَيْعِكُمُ الَّذِي بَايَعْتُم بِهِ وَذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿١١١﴾

‘Hakika Mwenyezi Mungu amenunua kwa waumini nafsi zao na mali zao kuwa wao watapata pepo. Wanapigana katika njia ya Mwenyezi Mungu, wanaua na wanuawa. Hii ni ahadi aliyojilazimisha kwa haki katika Tawrat na Injili na Qur’an, Na ninani atimiziaye ahadi kuliko Mwenyezi Mungu? Basi furahini kwa biashara yenu mliyofanya naye, Na huko ndiko kufuzu kukubwa” (9:111)

Wala hakuna anayeitumia Aya hii katika umma wa Kiarabu isipokuwa wapiganaji ukombozi; na kujitolea kwao ndio jiwe la msingi la mapinduzi ya mataifa yote ya kiarabu.


2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

وَلَوْ تَرَىٰ إِذْ يَتَوَفَّى الَّذِينَ كَفَرُوا الْمَلَائِكَةُ يَضْرِبُونَ وُجُوهَهُمْ وَأَدْبَارَهُمْ وَذُوقُوا عَذَابَ الْحَرِيقِ ﴿٥٠﴾

50. Na lau ungeliwaona Malaika wanapowafisha wale waliokufuru wakipiga nyuso zao na migongo yao na (kuwaambia) ionjeni adhabu iunguzayo.

ذَٰلِكَ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيكُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ ﴿٥١﴾

51. Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyokwishatangulizwa na mikono yenu, Na hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.

كَدَأْبِ آلِ فِرْعَوْنَ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ كَفَرُوا بِآيَاتِ اللَّـهِ فَأَخَذَهُمُ اللَّـهُ بِذُنُوبِهِمْ إِنَّ اللَّـهَ قَوِيٌّ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٥٢﴾

52. Ni kama ada ya watu wa firaun na wale waliokuwa kabla yao; walizikufuru ishara za Mwenyezi Mungu, kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa sababu ya makosa yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mkali wa kuadhibu.

ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ لَمْ يَكُ مُغَيِّرًا نِّعْمَةً أَنْعَمَهَا عَلَىٰ قَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ وَأَنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٥٣﴾

53. Hiyo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi kabisa neema alizowaneemesha watu, mpaka wao wabadilishe yaliyomo nafsini mwao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kujua.

كَدَأْبِ آلِ فِرْعَوْنَ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ كَذَّبُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ فَأَهْلَكْنَاهُم بِذُنُوبِهِمْ وَأَغْرَقْنَا آلَ فِرْعَوْنَ وَكُلٌّ كَانُوا ظَالِمِينَ ﴿٥٤﴾

54. Ni kama hali ya watu wa firaun na wale waliokuwa kabla yao; walizikadhibisha ishara za Mola wao, kwa hiyo tukawaangamiza kwa sababu ya dhambi zao, na tukawazamisha watu wa firaun, Na wote walikuwa madhalimu.

LAU UNGEONA

Aya 50 – 54

MAANA

Na lau ungeliwaona Malaika wanapowafisha wale waliokufuru wakipiga nyuso zao na migongo yao na (kuwaambia) ionjeni adhabu iunguzayo.

Maneno yanaelekezwa kwa kila mwenye kuona, kwa sababu makusudio ni mawaidha na mazingatio. Makusudio ya wale waliokufuru ni kila kafiri, kwa kuchukulia dhahiri ya tamko kama lilivyo. Imesemekana kwamba makusudio ni kuwahusu makafiri wa Kiquraish waliopigana na Mtume(s.a.w.w) katika vita vya Badr, kwa kuchukulia mfumo wa maneno. Kwa sababu bado maneno ni ya tukio la Badr.

Kupiga nyuso na migongo yao ni fumbo la adhabu wanayoipata makafiri wakati wa kufa. Inawezekana kuwa ni kupiga hasa kwa kiuhakika, hata kama hakuonekani. Vyovyoote iwavyo ni kwamba makafiri wanahizika wakati wa kufa na baada ya kufa; wala hatuna umuhimu wa kutaja aina ya hizaya yenyewe.

Hayo ni kwa sababu ya yale yaliyokwishatangulizwa na mikono yenu, Na hakika Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.

Vipi adhulumu naye anaikataza dhuluma na kuiwekea adhabu? Sunni wanasema kuwa akili inajuzisha kwa Mwenyezi Mungu mtukufu amwadhibu mtiifu na kumpa thawabu mwasi, Vile vile akili inajuzisha Mwenyezi Mungu ahalifu ahadi yake. Tazama Mawaqif 8 sehemu ya 5 na sita. Na Madhahibul-Islamiya cha Abu Zuhura uk. 104.

Shia wanasema: Akili haijuzishi kwa Mwenyezi Mungu amwaadhibu mtiifu na inajuzisha kumpa fadhila mwasi. Kwa sababu mwadilifu hamwadhibu mtiifu na mkarimu mpole humsamehe mwenye kumfayia uovu.

Ni kama ada ya watu wa firaun na wale waliokuwa kabla yao; walizikufuru ishara za Mwenyezi Mungu, kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa sababu ya makosa yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mkali wa kuadhibu.

Yaani yaliyowapata washirikina siku ya Badr, kuuliwa na kutekwa, ni kwa sababu wao walimkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) . Yaliyowapata hawa yanafanana na yaliyowapata washirikina waliotangulia. Kwa sababu wali- wakadhibisha Mitume wao; kama watu wa Firaun na waliokuwa kabla yao.

Hiyo ni kwa sababu Mwenyezi Mungu habadilishi kabisa neema alizowaneemesha watu, mpaka wao wabadilishe yaliyomo nafsini mwao. Na hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kujua.

Dhahiri ya neema hapa ni riziki na kuibadilisha ni kuiondoa.

Hapa linajitokeza swali kuwa : dhahir ya Aya inafahamisha kwamba watu aliowaneemesha Mwenyezi Mungu kwa riziki hubakia kwao maadamu ni watiifu, Wakiasi hunyang’anywa. Lakini tunavyoona ni kuwa waasi wengi, kila wanavyozidi uasi ndivyo wanavyozidi utajiri wala hakibadili kitu kwao je ni vipi?

Jibu : Aya haikutaja tamko la maasi wala ukafiri. Lililofahamisha Aya ni kuwa Mwenyezi Mungu haondoi neema kwa watu wake ila wakibadilisha yaliyomo nyoyoni mwao, lakini Mwenyezi Mungu hakubainisha aina ya mabadiliko. Mfano wake ni Aya isemayo:

إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ ﴿١١﴾

“Hakika Mwenyezi Mungu habadilishi yaliyoko kwa watu mpaka wabadilishe yaliyomo nafsini mwao.. “ (13:11).

Watu wa Firaun, aliowatolea mfano Mwenyezi Mungu katika Aya iliyotangulia, walikuwa washirikina kabla na baada, Wao walizidisha kupetu- ka mipaka baada ya Musa kuwajia.

Kwa hiyo tutachukulia Aya tuliyonayo, kwenye maana ya kuwa Mwenyezi Mungu hawaangamizi watu duniani ila ni baada ya kuwapelekea Mtume na kuwalingania kwa Mwenyezi Mungu ana kwa ana; kisha waukatae mwito wake; kama vile watu wa Firaun na waliotangulia; wakiwemo watu wa Nuh, Lut na wengineo. Na kama hakuwapelekea Mtume, basi huchelewesha adhabu yao mpaka siku ya hisabu na malipo, Ama kuhusu Aya (13:11) tuna maoni katika tafsir yake tutayabainisha huko inshallah.

Ni kama hali ya watu wa firaun na wale waliokuwa kabla yao; wal- izikadhibisha ishara za Mola wao, kwa hiyo tukawaangamiza kwa sababu ya dhambi zao, na tukawazamisha watu wa firaun.

Umepita mfano wake katika Juz.3 (3:11)

Na wote walikuwa madhalimu.

Yaani kila mmoja katika watu wa Firaun ambao walimkadhibisha Musa(a.s) na makafiri wa Kiquraish ambao walimkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) . Wamejidhullumu wao wenyewe na wakawadhlumu watu kwa kuwazuilia njia ya Mwenyezi Mungu.

إِنَّ شَرَّ الدَّوَابِّ عِندَ اللَّـهِ الَّذِينَ كَفَرُوا فَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿٥٥﴾

55. Hakika wanyama waovu kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale wanaokufuru, basi hawataamini.

الَّذِينَ عَاهَدتَّ مِنْهُمْ ثُمَّ يَنقُضُونَ عَهْدَهُمْ فِي كُلِّ مَرَّةٍ وَهُمْ لَا يَتَّقُونَ ﴿٥٦﴾

56. Ambao umepeana nao ahadi kisha wanavunja ahadi yao kila mara; wala hawaogopi.

فَإِمَّا تَثْقَفَنَّهُمْ فِي الْحَرْبِ فَشَرِّدْ بِهِم مَّنْ خَلْفَهُمْ لَعَلَّهُمْ يَذَّكَّرُونَ ﴿٥٧﴾

57. Basi ukiwakuta vitani wakimbize kwa hao walio nyuma yao ili wapate kufahamu.

وَإِمَّا تَخَافَنَّ مِن قَوْمٍ خِيَانَةً فَانبِذْ إِلَيْهِمْ عَلَىٰ سَوَاءٍ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْخَائِنِينَ ﴿٥٨﴾

58. Na kama ukihofia hiyana kwa watu, basi watupie kwa usawa, Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wafanyao hiana.

وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا سَبَقُوا إِنَّهُمْ لَا يُعْجِزُونَ ﴿٥٩﴾

59. Wala wale waliokufuru wasifikirie kwamba wao wametangulia; kwa hakika wao hawatashinda

وَأَعِدُّوا لَهُم مَّا اسْتَطَعْتُم مِّن قُوَّةٍ وَمِن رِّبَاطِ الْخَيْلِ تُرْهِبُونَ بِهِ عَدُوَّ اللَّـهِ وَعَدُوَّكُمْ وَآخَرِينَ مِن دُونِهِمْ لَا تَعْلَمُونَهُمُ اللَّـهُ يَعْلَمُهُمْ وَمَا تُنفِقُوا مِن شَيْءٍ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ يُوَفَّ إِلَيْكُمْ وَأَنتُمْ لَا تُظْلَمُونَ ﴿٦٠﴾

60. Na waandalieni nguvu kama vile muwezavyo na kwa farasi waliofungwa ili mumtishe adui wa Mwenyezi Mungu na adui yenu, na wengineo msiowajua nyinyi, Mwenyezi Mungu anawajua, Na chochote mtakachotoa katika njia ya Mwenyezi Mungu, mtarudishiwa, wala nyinyi hamtadhulumiwa.

وَإِن جَنَحُوا لِلسَّلْمِ فَاجْنَحْ لَهَا وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٦١﴾

61. Na kama wakielekea kwenye amani, nawe ielekee, na mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika yeye ni mwenye kusikia mwenye kujua.

وَإِن يُرِيدُوا أَن يَخْدَعُوكَ فَإِنَّ حَسْبَكَ اللَّـهُ هُوَ الَّذِي أَيَّدَكَ بِنَصْرِهِ وَبِالْمُؤْمِنِينَ ﴿٦٢﴾

62. Na kama wakitaka kukuhadaa, basi Mwenyezi Mungu atakutoshelezea. Yeye ndiye aliyekupa nguvu kwa msaada wake na kwa waumini.

وَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ لَوْ أَنفَقْتَ مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مَّا أَلَّفْتَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ أَلَّفَ بَيْنَهُمْ إِنَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٦٣﴾

63. Na akaziunganisha nyoyo zao; lau ungelitoa yote yaliyomo ardhini usingeliweza kuiunganisha mioyo yao, lakini Mwenyezi Mungu amewaunganisha, Hakika yeye ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.

KANUNI NA HUKUMU KATIKA AMANI NA VITA

Aya 55 – 63

MAANA

Aya hizi zimekusanya kaida na hukumu katika hali ya usalama na ya vita. Tutazifafanua kulingana na mpango ufuatao:-

Hakika wanyama waovu kabisa mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale wanaokufuru, basi hawataamini. Ambao umepeana nao ahadi kisha wanavunja ahadi yao kila mara; wala hawaogopi

Asili ya neno mnyama (Dabba) ni kila anayetembea ardhini. Kisha ikawa neno hilo linatumiwa sana na wenye miguu mine.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema kuwa jamaa waliokufuru, ambao imani yao haitarajiwi walielewana na Mtume(s.a.w.w) kuishi kwa amani na ujirani mwema. Lakini kumbe wamedhamiria uhaini na wakauvunja ahadi zaidi ya mara moja; hawakuogopa balaa wala adhabu itakayotokana na hayo. Mwenyezi Mungu amewataja hawa kuwa ni waovu zaidi kuliko mnyama.

Kuna kundi la wafasiri wamesema kuwa ni Mayahudi wa Bani Quraidha, waliahidiana na Mtume kisha wakavunja ahadi na kusaidiana na washirikina wa Makka siku ya Badr. Mtume(s.a.w.w) aliposhinda waliomba msamaha, akawakubalia na kuwasamehe.

Kisha wakawaahidiana mara ya pili, wakavunja ahadi siku ya Khandaq, Si ajabu kwa Mayahudi kufanya hiyana na kuvunja ahadi; isipokuwa ajabu ni kuwa na ukweli na uaminifu.

Basi ukiwakuta vitani wakimbize kwa hao walio nyuma yao ili wapate kufahamu.

Maneno haya anaambiwa Mtume(s.a.w.w) , Mwenyezi Mungu anabainisha hukumu ya hawa makafiri wasio na ahadi; kwamba akiwapata awatie adabu kali kabisa; hata wengine wanaotaka kufanya hiyana wapate funzo. Kwa hivyo basi inatubainikia kuwa makusudio ya walio nyuma yao ni wengine.

Na kama ukihofia hiyana kwa watu, basi watupie kwa usawa.

Makusudio ya kuhofia hapa ni kujua; na usawa ni kuwa sawa wewe na wao katika kujua kuvunja ahadi.

Maana ni ikiwa baina yako wewe Muhammad na watu kuna mapatano na ukajua kabisa kwamba wao watavunja ahadi, kwa kuonyesha alama wazi wazi kuwa wao wana dhamira mbaya au hiyana na kuyafanya mapatano ni pazia ya kupanga njama zao, basi yatupilie mbali mapatano yao na uwafahamishe kuwa umevunja mapatano yao; wala usianze kupigana kabla ya kuwafahamisha ili usinasibishiwe uhaini; kwani

hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wafanyao hiana.

Kwa maneno mengine ni kwamba Uislamu unawajibisha kutekeleza ahadi kwa watekelezao ahadi. Ama wale wanaofanya ahadi ni nyenzo ya uhaini basi Uislamu unaamrisha kuivunja, kwavile hiyo si ahadi bali ni vitimbi.

وَأَنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي كَيْدَ الْخَائِنِينَ ﴿٥٢﴾

Hakika Mwenyezi Mungu haongozi vitimbi vya wahaini” (12:52).

Imam Ali(a.s) anasema:Kuwatekelezea ahadi wavunja ahadi ni kuvunja ahadi na kuvunja ahadi kwa wavunja ahadi ni kutekeleza ahadi.”

Wala wale waliokufuru wasifikirie kwamba wao wametangulia; kwa hakika wao hawatashinda.

Maana ya wametangulia ni wameponyoka. Na hawatashinda, ni hawatanishinda mimi. Maana ya Aya kwa ujumla ni kuwa asifikirie yeyote kwamba Mwenyezi Mungu anapitwa na jambo.

Na waandalieni nguvu kama vile muwezavyo na kwa farasi waliofungwa.

Aya zilizotangulia zimeonyesha mfungamano wa mapatano na hukumu ya anayeyavunja. Katika Aya hii, Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawaamrisha Waislamu kujianda kwa nguvu na kukamilisha maandalizi dhidi ya adui.

Makusudio ya nguvu ni chochote kile kinachotia nguvu. Katika kumkabili adui, iwe ni Mkuki, Roketi, au chochote. Mwenyezi Mungu amehusisha kutaja Farasi, kwa sababu wakati huo ndio ilikuwa silaha ya kutegemea.

Imepokewa hadith kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) kwamba yeye alisoma Aya hii na kusema:

“Tambueni kwamba nguvu ni kurusha” Alilikariri mara tatu, Makusudio ni kubainisha umuhimi wa kurusha na athari yake katika vita.

Historia imethibitisha umuhimu wa nadhari hiyo aliyoitamka Mtume(s.a.w.w) kiasi miaka elfu moja na mia tatu; ambapo hakukua na makombora wala mizinga. Wataalamu wameelekeza akili zao kila mara kukaza nguvu za kurusha kuanzia mishale hadi risasi; na kutoka kwenye mizinga hadi mabomu ya Atomic na Haidrogeni. Waislamu walitumia, pamoja na Mtume, teo katika vita ya Khaibar.

Ili mumtishe adui wa Mwenyezi Mungu na adui yenu, na wengineo msiowajua nyinyi, Mwenyezi Mungu anawajua.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewagawanya maadui aina mbili: Aina iliyo dhahir ambayo waislamu waliwajua na aina isiyodhahiri ambayo waislamu hawakuwajua uadui wao; nao ni kila anayetamani uislamu ushindwe, kwa kuhofia utawala wao; yakiwemo mataifa ya jirani; kama vile Fursi na Roma ambao baadae walishindwa na waislamu ulipopata nguvu.

NGUVU ZA KUJILINDA NA NGUVU ZA UCHOKOZI

Hebu tusimame kidogo kwenye kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu: “Ili mumtishe adui wa Mwenyezi Mungu na adui yenu.” Kwa sababu ina- fungamana na msingi wa kuilinda jamii ya binadamu kutoka na vurugu, na kuwazuia mataghuti kuchezea maisha ya binadamu na kuwakandamiza.

Msingi huu ni kupatikana nguvu, kwa watu wa haki na uadilifu, itakayoweza kuwazuia madhalimu na wavunjaji na kuwafanya wawe chini ya hukumu na sharia ya Mwenyezi Mungu inayowataka watu wote waishi kulingana na kanuni ya maisha na desturi yake, wala asikengeuke yeyote. Akitamani tu kupotoka basi nguvu hiyo imzime na kumrudisha kwenye desturi hiyo.

Lau mabingwa na wenye akili watafanya utafiti wa sababu ya matatizo ya maisha na maangamivu ni kudhoofisha nguvu ya kukinga maovu na kuipa ubabe nguvu ya uchokozi.

Mfano mzuri wa hilo ni ni nguvu wanazomiliki Marekani na kuzitumia katika uporaji na unyang’anyi bila ya pingamizi wala kizuizi, isipokuwa kutapatapa kwa wananchi wasiokuwa na silaha.

Anasema Nicholas Sparekman “Sisi Wamerekani tunaweza kutekeleza matakwa yetu na kuyalazimisha kwa wale wasiokuwa na nguvu kwa njia yoyote ile, ikiwemo kutumia nguvu; kama vile vita vya kubomoa”

Vile vile Leon Walsh anasema katika kitabu chake American strategic in world politics (Mbinu za Marekani katika siasa za ulimwengu)

“Wajibu wetu ni kutekeleza maongozi yetu ya sawa kwa nguvu duniani, kisiasa kiuchumi na kijamii. Na hilo sio jambo lenye muda maalum tu bali ni lazima kuendele haifai kuliacha.”

Hakuna siri ya kujifaharisha huku kwa maadui wa Mwenyezi Mungu na kudhihirisha uchokozi kwa waja wa Mwenyezi Mungu bila ya kujali, isipokuwa kutohofia nguvu yoyote ya kujikinga ambayo italiinua neno la Mwenyezi Mungu na kuiweka chini batili.

Viongozi wa Marekani wametekeleza yaliyoandikwa katika Kitab hicho na kukichikulia kama ni Injil yao takatifu badala ya Kitab cha Mwenyezi Mungu.

Wametekeleza njia zote za nguvu na za kuumiza, ikiwa ni pamoja na vita vyenye kuangamiza ili watekeleze matakwa yao kwa wale wasiokuwa na nguvu; wakatupa makombora ya kuunguza kwa watoto, vikongwe na waja wazito na wakatupa mabomu ya sumu kwenye nyenzo za riziki na uhai, wakiwemo wanyama na mimea ili waliobaki wafe kwa njaa.

Ni kwa lengo hilo ndipo Marekani ikaanzisha ngome za mauti katika ardhi yake, wakaanzisha humo uchunguzi wa kutafuta mikrobu kali zitakazoma- liza maisha ya binadamu, wanyama na mimea, na kwa ajili ya kutafuta gesi inayoondoa akili na kulemaza mishipa.

Kuna ajabu gani baada ya hayo yote kwa Marekani kuanzisha ngome ya mauti na kuweka silaha za kuharibu katika ardhi ya Palestina na kuipa jina la taifa la Israil? Hapana ajabu! Isipokuwa ajabu ni kwa madola, yakiwemo mataifa madogo yaliyo dhaifu, kuitambua ngome hii iliyosimamishwa kwa msingi ya uadui kwa binadamu wote, na kuwa na mwakilishi anyeitetea na kuangalia masihi yake katika Umoja wa Mataifa.

Pamoja na yote hayo, sisi hatukati tamaa kabisa kuwa iko siku haki itashin- da na batili itashindwa, Hicho kilio dhidi ya wachokozi kinasikika kila mahali ulimwenguni; hata katika Amerika. Huyu hapa mwananchi wa Vietnam ameiangamiza haiba ya Wamerekani, na kuua maelfu ya wanajeshi wao na kuwalazimisha kupoteza mabilioni ya dola zao[1] .

Na chochote mtakachotoa katika njia ya Mwenyezi Mungu; mtarudishiwa, wala nyinyi hamtadhulumiwa.

Hii ni kuhimiza kutoa mali ambayo hapana budi kuitoa ili kuandaa nguvu na kujikinga. Yametangulia malezo katika Juz.2 (2:196) na mwanzo wa Juz.4 (3:92)

Na kama wakielekea kwenye amani, nawe ielekee, na mtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika yeye ni mwenye kujua.

Amani ni ya ujumla, ikiwa ni pamoja na kusimamisha vita na suluhu, kutoa kodi na kusilimu. Kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu kumwambia Mtume wake ‘nawe ielekee’ ni amri ya lazima ya kumpa amani mwenye kutaka amani, vyovyote atakavyokuwa, ila kukiwa na dalili mkato kuwa amani yake ni vitimbi na maandalizi ya uvamizi na kuvunja mkataba.

Ni lazima ifahamike kuwa makusudio ya amani katika Aya hii ni amani ya wote, mwenye kupigana na asiyepigana. Wala sio amani ya pande zinazozana tu; kama vile kuishi kwa amani baina ya Urusi na Marekani ambako nyuma yake kuna mipango ya njama na mapinduzi katika mataifa yasiyofungamana na upande wowote, na kupinga ukombozi katika Asia,

Afrika na Latin Amerika, ili wazidishe faida katika mashirika yao ya kilanguzi kupitia damu ya wazalendo, chakula chao na mustakbali wao.

Utauliza : Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya anasema: ‘Wakielekea kwenye amani nawe ielekee, na katika Aya nyingine anasema:

فَلَا تَهِنُوا وَتَدْعُوا إِلَى السَّلْمِ وَأَنتُمُ الْأَعْلَوْنَ وَاللَّـهُ مَعَكُمْ ﴿٣٥﴾

“Basi msilegee na kutaka amani na hali nyinyi mko juu, na Mwenyezi Mungu yu pamoja nanyi” (47:35)

Je, kuna wajihi gani wa kujumuisha Aya hizi mbili?

Jibu : Hakuna kupingana baina ya Aya hizi. Aya ya kwanza inawaamrisha waislamu kumpa amani mwenyewe kutoa amani na Aya ya pili inawataka wawe na moyo wa kupigana wakazane na wasilegee wakamkimbia adui. Hilo linatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Mwenyezi Mungu yu pamoja nanyi’.

Kwa hiyo Aya hii: “Basi msilegee” ni sawa na Aya isemayo:

وَلَا تَهِنُوا فِي ابْتِغَاءِ الْقَوْمِ إِن تَكُونُوا تَأْلَمُونَ فَإِنَّهُمْ يَأْلَمُونَ كَمَا تَأْلَمُونَ وَتَرْجُونَ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا يَرْجُونَ ﴿١٠٤﴾

“Wala msilegee katika kuwafuatia hao watu, ikiwa mnaumia basi na wao wanaumia kama mnavyoumia nyinyi. Na nyinyi mwataraji kwa Mwenyezi Mungu ambayo wao hawayataraji”

Juz.5 (4:104)

Na kama wakitaka kukuhadaa, basi Mwenyezi Mungu atakutoshelezea. Yeye ndye aliyekupa nguvu kwa msaada wake na kwa waumini.

Mtume anaambiawa kuhusu hao walioelekea kwenye amani; kuwa kama wanakupangia njama za uhaini nyuma ya mwelekeo wao wa amani, basi usiogope njama zao. Wewe uko katika amani ya Mwenyezi Mungu na atakutosheleza na shari yao naye amekupa nguvu kwa msaada wake na kwa waumini.

Utauliza : Punde tu, yamepita maelezo ya kauli yake Mwenyezi Mungu akimwamrisha Mtume wake kuvunja mapatano ikiwa anahofia kwao hiyana na hadaa. Na katika Aya hii anamwamrisha kuwakubalia wakitaka amani bali hata kama wanataka kufanya hiyana, Je, kuna wajihi gani?

Jibu : Kule Mwenyezi Mungu, alimwamrisha kuvunja mapatano akiwa na yakini na kujua hiyana zao, kwa kumdhihirikia alama. Na, hapa ameamrishwa kuwapa amani hata kama wanakusudia hiyana, ikiwa hakuna dalili mkato za njama zao isipokuwa uwezekano tu wa hilo. Katika hali hii Mtume atachukulia dhahiri na kuamiliana nao kulingana na dhahiri. Kwani dhahiri ni ya watu na batini ni ya Mwenyezi Mungu.

Na akaziunganisha nyoyo zao; lau ungelitoa yote yaliyomo ardhini usingeliweza kuiunganisha mioyo yao, lakini Mwenyezi Mungu amewaunganisha, Hakika yeye ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.

Hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyeunganisha nyoyo za masahaba baada ya kuwa na uhasama uliozoeleka; hasa baina ya Ausi na Khazraj ambao uliendelea kiasi cha miaka 120.

Vile vile hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) hupitisha mambo kulingana na desturi, kanuni, sababu na visababishi vyake. Sababu ya kuunganisha nyoyo za masahaba wa Mtume Muhammad ni Uislamu na imani yao kinadharia na kimatendo. Na, Uislamu unatoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa hiyo imesihi kunasibishiwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Tumesema katika kufasiri Aya ya pili ya Sura hii kwamba dini haioteshi ngano isipokuwa inaotesha penzi na ikhlasi. Mfano wa Aya hii, tunayoifasiri, ni kama Juz.4 (3:103). Huko utakuta tafsiri yake kwa ufafanuzi.


3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَسْبُكَ اللَّـهُ وَمَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٦٤﴾

64. Ewe Mtume! Mwenyezi Mungu anakutosheleza wewe na wale waliokufuata katika waumini.

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَرِّضِ الْمُؤْمِنِينَ عَلَى الْقِتَالِ إِن يَكُن مِّنكُمْ عِشْرُونَ صَابِرُونَ يَغْلِبُوا مِائَتَيْنِ وَإِن يَكُن مِّنكُم مِّائَةٌ يَغْلِبُوا أَلْفًا مِّنَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَفْقَهُونَ ﴿٦٥﴾

65. Ewe Nabii! Wahimze waumini wende vitani; wakiwepo miongoni mwenu ishirini wenye subira, watashinda mia mbili; na kama wakiwa mia moja miongoni mwenu watawashinda elfu moja katika waliokufuru, maana hao ni watu wasiofahamu.

الْآنَ خَفَّفَ اللَّـهُ عَنكُمْ وَعَلِمَ أَنَّ فِيكُمْ ضَعْفًا فَإِن يَكُن مِّنكُم مِّائَةٌ صَابِرَةٌ يَغْلِبُوا مِائَتَيْنِ وَإِن يَكُن مِّنكُمْ أَلْفٌ يَغْلِبُوا أَلْفَيْنِ بِإِذْنِ اللَّـهِ وَاللَّـهُ مَعَ الصَّابِرِينَ ﴿٦٦﴾

66. Sasa Mwenyezi Mungu amewahafifishia na anajua kuwa kuna udhaifu miongoni mwenu. Kwa hiyo wakiwa mia moja miongoni mwenu wenye subira watawashinda mia mbili, na kama wakiwa elfu moja miongoni mwenu watawashinda elfu mbili kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri.

ANAKUTOSHELEZA MWENYEZI MUNGU

Aya 64 – 66

MAANA

Ewe Mtume! Mwenyezi Mungu anakutosheleza wewe na wale waliokufuata katika waumini.

Imesemekana kuwa maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu anakutosha wewe Muhammad na pia anawatoshea waumini waliokufuata. Ama sisi tunaelemea kwenye kauli ya aliyesema kuwa maana yake ni: Ewe Muhammad! Anakutosha Mwenyezi Mungu na waumini kwa Utume wako. Dalili yetu katika hilo ni Aya iliyotangulia (62): “Basi Mwenyezi Mungu atakutoshelezea.

Yeye ndiye aliyekupa nguvu kwa msaada wake na kwa waumini.” Aya hii inaeleza wazi kuwa Mwenyezi Mungu na waumini walimsaidia Muhammad, basi ni hivyo hivyo “Anakutoshelezea wewe Mwenyezi Mungu na wale waliokufuata katika waumini.”

Vyovyote iwavyo, makusudio ni kumtuliza Mtume kwamba vita vyake na makafiri vimedhaminiwa katika hali yoyote ile, Kwa sababu nguvu inayomsaidia haishindiki.

Ewe Nabii! Wahimze waumini wende vitani; wakiwepo miongoni mwenu ishirini wanaosubiri, watashinda mia mbili; na kama wakiwa mia moja miongoni mwenu watawashinda elfu moja katika waliokufuru, maana hao ni watu wasiofahamu.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anamwambia Mtume wake washujaishe na vita Ewe Muhammad, watu wako, na uwape habari kwamba wao ni kufu ya maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zao, hata kama watazidi zaidi ya mara kumi. Hilo ni kwa kuwa waumini wanafahmu amri ya Mwenyezi Mungu na wanaitakidi siku ya mwisho; na kwamba heri itapatikana kwa jihadi na kufa shahidi. Kwa hiyo wanakwenda kwa nia njema, Ama makafiri hawafahmu amri ya Mwenyezi Mungu wala hawaitakidi ahadi. Kwa hali hii wao wanabania maisha yao.

Sasa Mwenyezi Mungu amewahafifishia na anajua kuwa kuna udhai- fu miongoni mwenu. Kwa hiyo wakiwa mia moja miongoni mwenu wenye subira watawashinda mia mbili, na kama wakiwa elfu moja miongoni mwenu watawashinda elfu mbili kwa idhini ya Mwenyezi Mungu na Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaosubiri.

Wafasiri na mafakihi wamerefusha maneno kuhusu Aya hii. Kuna waliosema kuwa Aya hii ni Nasikh (inayofuta hukumu) ya Aya iliyotangulia ambayo imemlazimisha Mwislamu asiwakimbie watu kumi. Wengine wakasema ilikuwa uzito kwa Waislamu kukabili mmoja kwa kumi, ndipo ikaja tahfifu hiyo. Mafakihi nao kwa kutegemea Aya hi wamefutu kuwa ni haramu kukimbia vitani ila ikiwa idadi ya jeshi la adui ni maradufu ya idadi ya jeshi la Waislamu.

Katika kufasiri Aya 15 katika Sura hii, tumebainisha kuwa mafakihi hawana fatwa katika suala hili; na kwamba anachiwa suala hili, kamanda mkuu peke yake mwenye ujuzi na mwaminifu.

Kwa ajili hii tunatilia nguvu kuwa Aya mbili hizi na ile iliyo kabla yake, hazikuja kubainisha hukumu ya kukimbia, isipokuwa zinahusika na Mtume na sahaba zake tu; na Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi wa makusudio yake.

مَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَكُونَ لَهُ أَسْرَىٰ حَتَّىٰ يُثْخِنَ فِي الْأَرْضِ تُرِيدُونَ عَرَضَ الدُّنْيَا وَاللَّـهُ يُرِيدُ الْآخِرَةَ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٦٧﴾

67. Haimfalii Nabii yoyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda sawasawa katika ardhi, Mnataka vitu vya dunia Na hali Mwenyezi Mungu anataka Akhera. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.

لَّوْلَا كِتَابٌ مِّنَ اللَّـهِ سَبَقَ لَمَسَّكُمْ فِيمَا أَخَذْتُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿٦٨﴾

68. Lau isingelikuwa hukumu iliyotangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bila shaka ingeliwapata adhabu kubwa kwa yale mliyoyachukua.

فَكُلُوا مِمَّا غَنِمْتُمْ حَلَالًا طَيِّبًا وَاتَّقُوا اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٦٩﴾

69. Basi kuleni katika vile mlivyoteka ni halali na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّمَن فِي أَيْدِيكُم مِّنَ الْأَسْرَىٰ إِن يَعْلَمِ اللَّـهُ فِي قُلُوبِكُمْ خَيْرًا يُؤْتِكُمْ خَيْرًا مِّمَّا أُخِذَ مِنكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٧٠﴾

70. Ewe Nabii! Waambie wale mateka waliomo mikononi mwenu: Kama Mwenyezi Mungu akijua heri yoyote nyoyoni mwenu, basi atawapa bora kuliko vilivyochukuliwa kwenu na atawasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

وَإِن يُرِيدُوا خِيَانَتَكَ فَقَدْ خَانُوا اللَّـهَ مِن قَبْلُ فَأَمْكَنَ مِنْهُمْ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٧١﴾

71. Na kama wanataka kukufanyia hiyana, basi walikwishamfanyia hiyana Mwenyezi Mungu kabla, na akakupa ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.

KATEKA

Aya 67 – 71

MAANA

Haimfalii Nabii yoyote kuwa na mateka mpaka awe ameshinda sawa-sawa katika ardhi.

Wameafikiana wafasiri kwamba Aya hii imeshuka kuhusu mateka wa Badr, Dhahir ya mfumo inafahamisha hivyo. Wametofautiana katika tafsir yake, nasi tutaileta kwa njia ya swali na jawabu:

Ikiwa kuna vita baina ya Waislamu na waabudu masanamu. Na, Mwenyezi Mungu akampa ushindi Mwislamu kwa kafiri, je, ni wajibu kwa Mwislamu kumuua kafiri huyo? Au inajuzu kumchukua mateka? Na kama akimchukua mateka, je iko hiyari kwa Mtume baina ya kumuua na kumwacha kwa fidia? Na kumwacha bila ya fidia?.

Jibu : ni lazima lifafanuliwe katika hali mbili: Kwanza, ni kutokea vita baada ya dini kuwa na nguvu katika ardhi na watu wake kuwa na nguvu kwa namna ambayo hila na vitimbi vya maadui haviwadhuru, kwa kuwa ipo nguvu ya kujikinga.

Katika hali hii, Mwislamu anayepigana, anahiyarishwa baina ya kuua na kuchukua mateka. Na akichukua mateka itakua hiyari kwa Mtume baina ya kuua mateka na kumwacha kwa fidia au bila ya fidia. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

فَإِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا فَضَرْبَ الرِّقَابِ حَتَّىٰ إِذَا أَثْخَنتُمُوهُمْ فَشُدُّوا الْوَثَاقَ فَإِمَّا مَنًّا بَعْدُ وَإِمَّا فِدَاءً ﴿٤﴾

“Basi mnapokutana vitani na wale waliokufuru wapigeni shingo mpaka mkiwashinda sawa sawa, hapo wafungeni pingu, Baadae waacheni kwa ihsani au kwa kujikomboa” (47:4)

Siri katika hilo iko wazi, nayo ni kupatikana nguvu ya kujikinga.

Hali ya pili ni kutokea vita kabla dini haijamakinika vizuri na kuwa na nguvu katika ardhi. Hapo Mwislamu anayepigana, akimmudu kafiri anayepigana naye amuue sio kumchukua mateka. Siri ya hili ni kutia hofu moyo wa kila anayejaribu kutangaza vita dhidi ya waumini.

Haya yanafahamika kutokana na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Haimfalii Mtume kuwa na mateka mpaka ashinde sawasawa’ Yaani hakuna kuchukua mateka wa kikafiri mpaka dini iwe na nguvu kamili ya kujihami ambayo makafiri na mataghuti watakuwa chini yake.

Mnataka vitu vya dunia

Maneno haya yanaelekezwa kwa mwenye kuteka mateka kwa kukusudia ngawira na kuchukua fidia bila ya kujali kuharibika maisha yake katika ardhi.

Na hali Mwenyezi Mungu anataka Akhera.

Mwenyezi Mungu anawatakia waja wake malipo ya akhera kwa sababu ndiyo bora na yenye kubaki kuliko mapambo ya dunia.

Na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.

Anawapa nguvu waumini hata kama hawana mateka; na ni mwenye hekima katika kupanga mambo yake na amri yake na makatazo yake.

Lau isingelikuwa hukumu iliyotangulia kutoka kwa Mwenyezi Mungu, bila shaka ingeliwapata adhabu kubwa kwa yale mliyoyachukua.

Ilitangulia hukumu ya Mwenyezi Mungu kuinusuru dini yake na Mtume wake pamoja na watu wachache aliokuwa nao Badr, na kuteswa makafiri, pamoja na wingi wao, kwa kuuliwa na kutekwa kwa mikono ya waumini.

Lau si kupitisha kwake huku Mwenyezi Mungu, wangeliadhibiwa waumini ambao waliwachukua mateka maadui wa Mwenyezi Mungu kwa tamaa ya kupata fidia. Kwa sababu Mwenyezi Mungu Mtukufu anataka jihadi na amali iwe ni kwa ajili yake yeye Mwenyezi Mungu tu.

Kuna hadith isemayo “… ambaye hijra (kuhama) yake ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hijra yake ni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na ambaye hijra yake ni kwa ajili ya kupata dunia au kuoa mwanamke, basi hijra yake ni kwa lile alilolihajira.”

Ilivyo ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu hakubainisha aina ya adhabu ambayo angeliwapa wachukuaji mateka katika masahaba, lau si kupitisha alivyopitisha. Je, ilikuwa ni adhabu ya kidunia au ya kiakhera.

Utauliza : Ikiwa kuchukua mateka kulikuwa ni haramu kabla ya kushamiri dini yake Mwenyezi Mungu juu ya dini zote, ilikuwaje kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) kuwaruhusu masahaba siku ya Badr na akakubali kuchukua fidia kabla ya ushindi kamili? Na vita vya Badr vilikuwa ndio vya kwanza na kukafuatiwa na vita vilivyoendelea hadi mwaka wa kuchukuliwa Makka?

Wafasiri na wengineo wamedangana katika kujibu swali hili au mushkeli huu; na yakagongana maneno yao. Wengine wakajiachia na kusema ‘Mtume sio maasum aweza kukosa. Lakini hapana, hayuko hivyo Mtume wa Mwenyezi Mungu ambaye hatamki kwa hawa yake

Tunalotilia nguvu ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) alivua uharamu wa kuchukua mateka kwa kila mateka aliyeachwa huru na Mtume(s.a.w.w) siku ya Badr. Wengi wao walisilimu na kuwa watu wazuri; bali hata walikuwemo waliochukuliiwa vitani kwa kulazimishwa.

Ibn Athir katika Tarikh yake Juz: 2 katika kifungu; vita kuu ya Badr, anasema: “Mtume(s.a.w.w) aliwaambia sahaba zake siku hiyo:“Ninajuwa watu katika Bani Hashim na wengineo wametolewa kwa kulazimishwa. Kwa hiyo atakayekutana na yeyote katika Bani Hashim asimwue”

Miongoni mwa mateka alikuwemo Suhail bin Amr. Umar bin Al-Khattab akasema. “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: Acha nimwue asije akakuudhi.”

Mtume akasema:“Mwache atakuwa na jambo utakalomsifia.” Mateka mwingine alikuwa Abul As bin Rabii mume wa Zainab binti ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) .

Zainab akapeleka fidia ya kumkombolea mumewe ukiwemo mkufu wa mama yake Khadija. Mtume alipouona aliingiwa na huruma nyingi sana, na kuwaambia Waislamu:“Kama mtaonelea ni vyema kumwachia na kumrudishia vitu vyake basi fanyeni” Basi Waislamu walimwachia na kumrudishia mkufu, Abul As akasilimu baada ya hapo.

Mtume(s.a.w.w) aliua, miongoni mwa mateka waovu ambao haitarajiwi heri kwao, na wala hakukubali fidia yao. Ibn Athir anasema: “Miongoni mwa mateka alikuwemo Nadhr bin Harith na Uqba bin Abi Muiti. Mtume akaamuru wauliwe akasema Uqba: “Je, mimi si kama mateka hawa?” Lakini Mtume hakujali kauli yake hiyo, kwa vile anajua uovu wake na uhaini wake, na kwamba maisha yake ni shari na ufisadi katika ardhi.

Kwa hiyo kuwaachia huru baadhi ya mateka na kuwaua wengine, kunafahamisha kuweko masilahi kwa Uislamu na Waislamu katika kuwaacha walioachwa; nayo yalidhihiri, baadae, kama tulivyoelezea. Kwa ajili hii ndipo ikasihi kuvua hukumu ya uharamu katika mateka wa Badr.

Basi kuleni katika vile mlivyoteka ni halali na vizuri, na mcheni Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Maneno yanaelekezwa kwa waliopigana vita Badr pamoja na Mtume. Yana madhumuni ya kuidhinisha kula walivyochukua ngawira katika vita, iwe ni fidia au ngawira yenyewe. Hii ni dalili kwamba kuchukua mateka katika Badr kuliruhusiwa. Kwa sababu kuruhusu moja ya badali mbili (kitu na thamani yake) ni kuruhusu ya Pili; yaani ikiruhusiwa thamani ndio imeruhusiwa mali yenyewe. Kuna Hadith isemayo: “Mwenyezi Mungu akiharimsha kitu basi pia huharamisha thamani yake.”

Ewe Nabii! Waambie wale mateka waliomo mikononi mwenu: Kama Mwenyezi Mungu akijua heri yoyote nyoyoni mwenu, basi atawapa bora kuliko vilivyochukuliwa kwenu na atawasamehe. Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Baada ya Mtume kuchukua fidia kutoka kwa mateka aliamrishwa kuwaambia hao mateka kuwa ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu atawapa badali bora kuliko fidia, duniani na akhera.

Wafasiri wanasema kuwa baadhi ya mateka walidhihirisha Uislamu, ndipo Mwenyezi Mungu akamwaamrisha Mtume wake kuwaambia kuwa ikiwa mliyoyasema ni haki basi Mwenyezi Mungu anajua na atawapa badali bora kuliko vile vilivyochukuliwa kwenu na atawasamehe. Na ikiwa ni unafiki basi mmekwisha kufuru na mkafanya vitimbi kabla ya hapo na Mwenyezi Mungu akampa ushindi Mtume wake juu yenu.

Kisha wakaendelea kusema wafasiri, akiwemo Razi na Tabrasi, kwamba Mtume(s.a.w.w) alimwambia ami yake, Abbas: Jikomboe wewe na watoto wawili wa nduguyo, Aqil na Naufal. Abbas, akasema: Nilikuwa Mwisilamu wakanilazimisha kutoka. Mtume akamwambia Ikiwa uyasemayo ni kweli, basi Mwenyezi Mungu atakulipa. Abbas akasema: Sina chochote. Mtume akasema: Iko wapi ile dhahabu uliyompa mkeo,

Ummul Fadhi na kumwambia: Nikitokewa na lolote basi ni yako na watoto wako?[2] Abbas akashangaa na kumuuliza: Ni nani aliyekuambia?

Mtume akasema: Mwenyezi Mungu ndiye aliyeniambia. Abbas akasema: Nashuhudia kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu; Wallahi hakujua habari hii yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu. Baada ya hapo Abbas alisema: Amesema kweli Mwenyezi Mungu na Mtume wake, hakika Mwenyezi Mungu alinibadilishia ziada nyingi baada ya kutoa fidia.

Na kama wanataka kukufanyia hiyana, basi walikwishamfanyia hiyana Mwenyezi Mungu kabla, na akakupa ushindi juu yao. Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.

Dhamir katika kama wanataka, inawarudia mateka ambao aliwaacha huru Mtume(s.a.w.w) . Maana ni kuwa usiogope hiyana ya mateka uliowaachia, kwani wananini wakitaka kufanya hiyana? Walikupiga vita kabla na haikuwa lolote:

وَمَنْ عَادَ فَيَنتَقِمُ اللَّـهُ مِنْهُ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ ذُو انتِقَامٍ ﴿٩٥﴾

“Na atakayerudia, Mwenyezi Mungu atampa adhabu; na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye nguvu mwenye kuadhibu” Juz.7 (5:95)

Hii ni dalili nyingine kuwa Mwenyezi Mungu aliwahalilishia waislamu mateka katika vita vya Badr.

Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu amewajibisha kuwaua washirikina katika vita yao na waumini ikiwa vimetukia kabla ya dini kuwa na nguvu; isipokuwa katika vita vya Badr.

Kwani Mwenyezi Mungu alihalalisha kwa Mwislamu anayepigana kuchukua mateka kwa masilahi ya Uislamu na waislamu.

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَالَّذِينَ آوَوا وَّنَصَرُوا أُولَـٰئِكَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يُهَاجِرُوا مَا لَكُم مِّن وَلَايَتِهِم مِّن شَيْءٍ حَتَّىٰ يُهَاجِرُوا وَإِنِ اسْتَنصَرُوكُمْ فِي الدِّينِ فَعَلَيْكُمُ النَّصْرُ إِلَّا عَلَىٰ قَوْمٍ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُم مِّيثَاقٌ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٧٢﴾

72. Hakika wale walioamini na wakahajiri na wakapigania dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao; na wale waliokaribisha hao ndio wanaosimamiana wao kwa wao. Na wale walioamini na wasihame, hamna haki ya kuwasimamia hata kidogo mpaka wahame. Lakini wakiwaomba msaada katika dini, basi ni juu yenu kuwasaidia, isipokuwa juu ya watu ambao yapo mapatano baina yenu na wao, Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.

وَالَّذِينَ كَفَرُوا بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ إِلَّا تَفْعَلُوهُ تَكُن فِتْنَةٌ فِي الْأَرْضِ وَفَسَادٌ كَبِيرٌ ﴿٧٣﴾

73. Na wale waliokufuru wanasimamiana wao kwa wao; msipofanya hivyo itakuwa fitina katika ardhi na ufisadi mkubwa.

وَالَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَالَّذِينَ آوَوا وَّنَصَرُوا أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا لَّهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ ﴿٧٤﴾

74. Na wale walioamini waka- hajiri na wakafanya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale waliokaribisha na kusaidia, hao ndio waumini kweli, wana wao maghufira na riziki njema.

وَالَّذِينَ آمَنُوا مِن بَعْدُ وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا مَعَكُمْ فَأُولَـٰئِكَ مِنكُمْ وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٧٥﴾

75. Na wale walioamini baadaye wakahajiri na wakapigania jihadi pamoja nanyi, basi hao ni katika nyinyi. Na ndugu wa tumbo wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe katika Kitab cha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.

WAHAJIRI NA ANSAR

Aya 72 – 75

MAANA

Aya hizi zimewagawanya waumini kwenye mafungu; na zikaonyesha muungano wa kusaidiana ulioko baina yao kwa sababu ya imani na Hijra. Pia Aya zimeonyesha muungano wa makafiri na mirathi ya wenye udugu.

Ufafanuzi ni kama huu ufuatao:

1.Hakika wale waliaomini na wakahajiri na wakafanya juhudi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao.

Hao ni wale wahajiri (wahamiaji) wa kwanza. Mwenyezi Mungu amewasifu kwa imani, kuhama mji na kufanya juhudi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa hali na mali.

Ni kwa kujitolea huku, sio imani tu, ndipo Qur’an ikawasifu na kuzungumza mengi ya kumwitikia kwao Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Utauliza : Ilivyo ni kuwa wahajiri waliingia Madina wakiwa hawana kitu ndio maana Ansar waliwakaribisha majumbani mwao wakawapa chakula na mavazi, wakiwatanguliza wao kuliko wenyewe; kama asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Na wale waliokaribisha,’ sasa walitoa wapi mali waliyoijitolea katika njia ya Mwenyezi Mungu?

Jibu : Kwanza: wahajiri walikuwa wakiwasaidia mafukara waislamu kabla ya Hijra.

Pili: wao waliacha majumba yao na mashamba yao yaporwe na washirikina, kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu. Hakuna kitu kikubwa kama mtu kuacha nyumba yake, na ardhi yake na yote aliyoyachuma kwa ajili ya maisha yake na watoto wake.

2.Na wale waliokaribisha na kusaidia hao ndio wanaosimamiana wao kwa wao.

Hao ni Ansar. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewasifu kuwa wao walimkaribisha Mtume na walioahama naye katika majumba yao, wakawapendelea kuliko nafsi zao na watoto wao.

Na kwamba wao walimpa amani aliyewapa amani wahajiri na kuwa hasimu waliowafanyia uhasimu. Kwa hali hiyo ndipo, Mwenyezi Mungu akawapa sifa hii mpaka likawa neno ‘Answar’ (wasaidizi) ndio nembo yao siku zote.

Kauli yake Mwenyezi Mungu hao ndio wanosimamiana ni kuashiria Wahajiri na Answar kwa pamoja; na kwamba kila mmoja anamsimamia mwenzake kama anavyojisimamia kimsaada na kiulinzi. Kuna Hadith isemayo: “Mfano wa waumini katika kuhurumiana na kupendana; ni kama mfano wa mwili, kiungo kimoja kikiwa na tatizo, basi huacha mwili mzima ukeshe na kuwa na homa.”

Baadhi ya wafasiri wamewatofautisha Wahajiri na Answar, wakawafanya bora hawa kuliko hao. Ama sisi tuko katika upande wa kuwa wote wako sawa. Hilo lafahamishwa na Aya tuliyo nayo, vile vile Aya isemayo:

وَالسَّابِقُونَ السَّابِقُونَ ﴿١٠﴾

“Na waolitangulia wametangulia” (56:10)

Hawa waliwatangulia wenzao kwa imani na kuhama na wale wakawatangulia wenzao kwa kukaribisha na kusaidia. Yakawa makundi yote ni katika waliotangulia. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewasifu hivyo katika Aya isemayo: “Na waliotangulia wa kwanza katika wahajiri na Answar”

Na wale walioamini na wasihame.

Hawa ni wale walioamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, lakini walikataa kutoka mji wa shirki na kuhamia mji wa Uislamu, pamoja na kuwa Qur’an imewaamrisha na kuwahimiza, lakini wao walishikamana na mali zao na kuhofia masilahi yao.

Yametangulia maelezo ya hawa na hukumu ya Hijra katika Juz.5 (4:97)

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amebainisha hukumu ya hawa ambao hawakuhama kwa kusema:

Hamna haki ya kuwasimamia hata kidogo mpaka wahame, Lakini wakiwaomba msaada katika dini, basi ni juu yenu kuwasaidia.

Yaani hawa hawazingatiwi kuwa ni sehemu ya jamii ya Kiislamu; wala haiwathibitikii haki yoyote ya waislamu wanaokaa katika mji wa Kiislam. Kwa sababu wao wamechagua hukumu ya shirk na washirikina kuliko hukumu ya Uislamu na waislamu.

Ndio! wakiacha nchi ya washirikina kuelekea nchi ya Uislamu, basi wanayo haki ya kulindwa na kusaidiwa. Vile vile kama akiwachokoza mchokozi kwa ajili ya dini na itikadi yao na kujaribu kuwafitini na Uislamu.Lakini si wajibu kuwasaidia katika yasiyokuwa hayo. Kwa sababu, mfungamano wa dini unamlazimisha kila mmoja kulinda dini ya ndugu yake, hata kama ni fasiki. Kwa maneno mengine ni kuwa kuilinda itikadi ya fasiki ni kulinda dini hasa sio kumlinda fasiki mwenyewe.

Kama kwamba muuliizaji aliuliza: Ikiwa kafiri amemchokoza Mumin ambaye hakuhama: na baina ya kafiri mchokozi na Mumin aliye katika nchi ya Kiislam kuna mkataba, na Mumin aliyechokozwa akataka msaada kwa Mumin aliye katika nchi ya Kiislamu, Je, hapo ni wajibu kumsaidia aliyechokozwa?

Mwenyezi Mungu (s.w.t) akajibu kwa kusema:

Isipokuwa juu ya watu ambao yapo mapatano baina yenu na wao, Na Mweneyzi Mungu anayaona mnayoyatenda.

Yaani usaidizi haupasi katika hali ya namna hii kwa kulinda mkataba. Kwani Uislamu hauruhusu kwa hali yoyote kufanya hiyana, hata na kafiri.

JINA LA DINI HALINA ATHARI

Na wale waliokufuru wanasimamiana wao kwa wao.

Dhahiri ya Aya inaweza kutoa dhana kwamba kushirikiana katika ukafiri kunapelekea kusaidiana, Lakini hali haiko hivyo, Historia ya makafiri wao kwa wao ni historia ya vita na umwagikaji wa damu, Vile vile historia ya waislamu.

Majarabio yamefahamisha kuwa masilahi ndiyo yanayowaweka watu pamoja, Ama matamko tu na majina ya kidini, kama vile Mwislamu na Mkristo, yanaweza kuwa na athari, lakini haifikii kiwango cha kusimami- ana kwa kusaidiana.

Yaani huyu amsimamie mwenzake; kama anavyojisimamia kiasi cha kutoa mhanga masilahi yake yote, hata nafsi yake na watu wake na mali yake! Hapana, ila ikiwa ni kwa ajili ya dini.

Hayo ndiyo yanayokusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu. ‘Hao ndio wanaosimamiana’ na pia kauli yake:

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ﴿٧١﴾

Waumini wanaume na waumin wanawake ni mawalii wao kwa wao. Huamrishana mema na kukatazana maovu (9:71).

Yaani mema kwao ndio masilahi Ama makusudio ya kauli yake: ‘Na wale waliokufuru wanasimamiana wao kwa wao” na kauli yake:

وَإِنَّ الظَّالِمِينَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ﴿١٩﴾

Na hakika madhalimu wanasimamiana (45: 19).

Pia kauli yake:

الْمُنَافِقُونَ وَالْمُنَافِقَاتُ بَعْضُهُم مِّن بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمُنكَرِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمَعْرُوفِ ﴿٦٧﴾

“Wanafiki wanaume na wanafiki wanawake ni hali moja, Wanaamrisha maovu na kukataza mema” (9:67)

Makusudio ya Aya hizo tatu ni kuwa makafiri, wanafiki na madhalimu wanakuwa kitu kimoja dhidi ya haki, pamoja na uadui na kupigana baina yao. Kwa sababu masilahi yanawakusanya na kuwaweka safu moja, masi- lahi yenyewe ni kulinda manufaa na faida.

Hilo limekwishafanyika mara nyingi zamani na saa. Katika historia ya saa ni muungano wa wakoloni na wanyonyaji dhidi ya wazalendo na wanamapinduzi; na jinsi mashirika ya kilanguzi yanavyoshindania faida.

Na historia ya zamani ni kuafikiana washirikina wa kiarabu na mayahudi wa Hijaz na wanafiki kwa kauli moja kuupiga vita Uislamu na waislamu. Hakuna lililowapa msukumo huo isipokuwa masilahi ya pamoja; kwani uadui baina ya washirikina na mayhudi, kabla ya Uislamu, ulikuwa umepita kiasi.

Kwa maelezo hayo ndio tunafasiri kauli yakeMwenyezi Mungu: “Na wale waliokufuru wanasimamiana wao kwa wao.” Ama walioyoyaeleza wafasiri wengi kuwa makusudio ni kuwa makafiri wanarithiana, tafsiri hii iko mbali na dhahiri ya tamko.

Tumezungumzia mfano wa Aya hii na masilahi ya pamoja baina ya mayahudi na wakristo wengi hivi sasa, katika Juz.6 (5:51) kifungu cha mayahudi petroli na wakristo.

Msipofanya hivyo itakuwa fitina katika ardhi na ufisadi mkubwa.

Yaani: Enyi Waislamu! Mlioamini msipowasaidia waislamu wenye kuwataka msaada dhidi ya makafiri ambao wanajaribu kuwafitini na dini yao na kuwarudisha kwenye shirki, basi itakuwa chokochoko na ufisadi kwa sababu ya shirki kutawala imani na batili kutawala haki.

Hakika wale waliaomini na wakahajiri na wakafanya Jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao. Na wale waliokaribisha na kusaidia hao ndio waumini wa kweli. Wana wao maghufira na riziki njema.

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewataja wahajiri na Ansari kwa tamko hili hili kubainisha wajibu wa hilo kwa kila mmoja juu ya mwenzake katika kumlinda na kumsaidia. Kisha hapo amerudia kwa ajili ya kuwasifu kuwa wao ndio waumini wa kweli na kubainisha alivyowaandalia keshomsamaha na thawabu ambazo amezielezea kwa ibara ya ‘riziki njema.’

Sijasoma ibara fasihi zaidi kushinda wasifu wa Imam Zainul-Abidin(a.s) kwa wahajiri na Ansari huku akimlingani Mola wake na kuwatakia rehema na radhi, kwa kusema:“Ewe Mola! Hasa maswahaba wa Muhammad ambao walikuwa na usuhuba mzuri, wakawa na majaribu mema katika kumsaidia kwake.

Wakamwitikia alipowaaeleza hoja ya ujumbe wake.

Wakapigana na mababa zao na watoto wao ili kuithibisha unabii wake na wakashinda kupitia kwake.

Waliozingirwa na mapenzi wakitarajia biashara isiyo na hasara kwa ajili ya kumpenda kwake.

Wakatengwa na jamaa zao waliposhikamana na kamba yake, Udugu ulikwisha walipotulia chini ya kivuli cha udugu wake.

Basi ewe Mola usiwasahu kwa yale waliyoyawacha kwa ajili yako. Na uwaridhie kwa radhi zako.

Na walikuwa wakilingania kwako pamoja na mjumbe wako”

Hii ni sehmu ya kwanza ya dua namba nne inayopatikana katika kitabu cha dua kinachoitwa Asswahifatussajjadiyya ambacho Shia wanakiadhimisha na kuitukuza kila herufi yake.

Hili ni jawabu tosha la yule anayesema kuwa Shia wanawavunjia heshima maswahaba.

Na wale walioamini baadaye na wakahajiri wakapigana jihadi pamoja nanyi, basi hao ni katika nyinyi.

Hawa ni wale waliomwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wakahamia Madina na kupigania dini ya Mwenyezi Mungu kwa nafsi zao na mali zao, baada ya wale waliotangulia kwanza. Wote hukumu yao ni moja tu katika wajibu wa kuwasaida na kuwalinda.

Na ndugu wa tumbo wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe katika kitabu cha Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.

Wafasiri wanasema baada ya Mtume kuwafanyisha ndugu masahaba zake, na yeye akawa nduguye ni Ali; walikuwa wanasaidiana na kustahikiana katika mirathi; yaani warithiane kwa udugu huu sio kwa nasabu na akraba.

Kisha ikafutwa hukumu ya kurithiana huku, kukarudi kurithiana kwa udugu wa tumbo na akraba.

Aya hii wameitolea dalili Shia kwamba aliye karibu na marehemu kinasabu ndiye anayestahiki zaidi mirathi yake kuliko aliye mbali, ni sawa awe na fungu au la; au awe na nasaba au la, Kwa hiyo Binti wa marehemu anamzuia ndugu wa marehemu kurithi kwa vile yuko karibu naye zaidi; na dada wa marehemu anamzuia ami wa marehemu, Kwa sababu hiyo hiyo. Namna hii wa karibu zaidi humzuia wa mbali katika daraja zote.

Tumeyazungumzia hayo na kauli za Sunni na Shia kuhusu jambo hilo; kama tulivyoonyesha kurithiana kwa udugu na sabababu za kurithi wakati wa Jahilia, Yote hayo tumeyazungia katika Juz.4 (4:11).

MWISHO WA SURA YA NANE


4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

Surah Ya Tisa: Suart At – Tawba.

Vile vile inaitwa Surat baraa na fadhiha, kwa vile inawafedhehi wanafiki. Aya zake ni 129. Imeshuka Madina.

Wameafikiana Masahaba na watalaamu wa kisomo cha Qur’an (qurrau) kutokuwa na Bismillahi mwanzo wake, kwa sababu ni Sura iliyoshuka kuondosha aibu na Bismillahi ni amani kutokana na Mwingi wa Rehema Mwenye Kurehemu. Imesemekana kuwa hiyo na Sura Anfal (iliyotangulia) ni Sura moja.

بَرَاءَةٌ مِّنَ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ إِلَى الَّذِينَ عَاهَدتُّم مِّنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿١﴾

1. (Tangazo la) Kujitoa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina.

فَسِيحُوا فِي الْأَرْضِ أَرْبَعَةَ أَشْهُرٍ وَاعْلَمُوا أَنَّكُمْ غَيْرُ مُعْجِزِي اللَّـهِ وَأَنَّ اللَّـهَ مُخْزِي الْكَافِرِينَ ﴿٢﴾

2. Basi tembeeni katika nchi miezi minne; na jueni kwamba nyinyi hamuwezi kumshinda Mwenyezi Mungu, na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuwadhalilisha makafiri.

وَأَذَانٌ مِّنَ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ إِلَى النَّاسِ يَوْمَ الْحَجِّ الْأَكْبَرِ أَنَّ اللَّـهَ بَرِيءٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ وَرَسُولُهُ فَإِن تُبْتُمْ فَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ وَإِن تَوَلَّيْتُمْ فَاعْلَمُوا أَنَّكُمْ غَيْرُ مُعْجِزِي اللَّـهِ وَبَشِّرِ الَّذِينَ كَفَرُوا بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٣﴾

3. Na ni tangazo litakalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa watu siku ya Hijja kubwa ya kwamba Mwenyezi Mungu amejitoa na washirikina na pia Mtume wake. Basi kama mkitubu ndiyo heri kwenu, na kama mkikengeuka, basi jueni kwamba nyinyi hamuwezi kumshinda Mwenyezi Mungu na wabashirie waliokufuru adhabu iumizayo.

إِلَّا الَّذِينَ عَاهَدتُّم مِّنَ الْمُشْرِكِينَ ثُمَّ لَمْ يَنقُصُوكُمْ شَيْئًا وَلَمْ يُظَاهِرُوا عَلَيْكُمْ أَحَدًا فَأَتِمُّوا إِلَيْهِمْ عَهْدَهُمْ إِلَىٰ مُدَّتِهِمْ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُتَّقِينَ ﴿٤﴾

4. Ispokuwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina kisha hawakuwapunguzia chochote wala hawakumsaidia yeyote juu yenu, basi watimizieni ahadi yao mpaka muda wao Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wenye takua.

KUJITOA

Aya 1-4

MAANA

Mwaka wa nane wa Hijra Mtume(s.a.w.w) aliiteka Makka, mwaka wa tisa ilishuka Sura hii, katika mwaka wa kumi Mtume alihiji hija ya mwisho, na katika mwaka wa kumi na moja akafariki. Kwa hiyo Sura hii siyo ya mwisho kushuka, lakini ni katika Sura za mwisho mwisho. Hivoyo imekusanya hukumu za mwisho za uhusiano wa waislamu na washirikina, Twaha Hussein anasema katika kitab Mir-atul-Islam.

“Waarabu walizidi kuukubali Uislamu baada ya Hijja aliyohiji Abu Bakr mwaka wa tisa. Katika Hijja hii alimtuma Ali amuwahi Abu Bakr na awasomee watu Qur’an. Ikawa ni upambanuzi wa zama mbili: Zama ambazo Uislamu ulikuwa unapata nguvu kidogo kidogo, huku ushirikina ukiwa umebaki katika baadhi ya makabila ya Kiarabu. Na zama ambazo bara ya Arabu yote ilikuwa na Uislamu.

Qur’an yenyewe - ambayo Ali aliwasomea watu na kutenganisha baina ya zama hizo mbili - ni Aya hizi tukufu za Sura ya baraa, akatangaza kujitoa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na washirikina, akawaharamisha, katika tangazo hilo, washirikina wasikurubie Ka’aba au kuipitia au kutufu uchi’.

(Tangazo la) Kujitoa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina.

Tumetangulia kueleza kuwa Sura hii ilishuka mwaka uliofuatia kutekwa Makka ambapo Uislamu ulikuwa na kuenea bara Arabu yote, lakini pamoja na hayo ushirikina ulikuwa umebakia vifuani mwa baadhi ya makabila ya Kiarabu ili vifua hivyo visiwe kikosi cha tano[3] katika jamii ya Kiislamu, Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake katika Sura hii kutangaza kujitoa katika dhima na washirikina.

Kwa ufasaha zaidi kumpa onyo la vita kila mshirikina anayekaa bara Arabu mpaka aseme: Lailaha Illa Llah na aingie waliyoingia wenzake.

Onyo hilo liliwahusu washirikina wote, hata wale waliowekeana mkataba wa amani na Mtume; isipokuwa katika hali moja tu ambayo Mwenyezi Mungu ameiashiria kwa kusema:

Ispokuwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina kisha wasiwapunguzie chochote.

Tafsir yake inafuatia.

Basi tembeeni katika nchi miezi minne; na jueni kwamba nyinyi hamwezi kumshinda Mwenyezi Mungu, na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kuwadhalilisha makafiri.

Yaani semeni: Enyi waislamu kuwaambia washirikina: Tembeeni katika nchi kwa usalama katika muda huu. Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwatangazia vita washirikina, aliwapa muda wa miezi minne wahame kwa amani waende watakako bila ya kuguswa na yeyote.

Wakisilimu baada ya hapo basi wamesalimika na kufuzu duniani na akhera. Wakiendelea na ushirikina basi malipo yao ni kuuawa katika dunia na adhabu kali katika Akhera na hawataweza kuheba hayo.

Utauliza : kupigana na washirikina mpaka watamke shahada, hakuafikiani na kauli ya Mwenyezi Mungu:

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ﴿٢٥٦﴾

“Hakuna kulazimishwa katika dini” Juz.3 (2:256)

Pia hakuafikiana na kauli ya Mwenyezi Mungu:

أَفَأَنتَ تُكْرِهُ النَّاسَ حَتَّىٰ يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ ﴿٩٩﴾

“Je, wewe utawalazimisha watu wawe waumini?”. (10:99)

Na Uislamu ni dini ya usalama si dini ya vita?

Jibu : ni kweli kuwa Uislamu hamlazimishi yeyote kutamka: Lailaha Illa Llah; isipokuwa unalingania kwa hekima, na dalili. Mwenyezi Mungu anasema:

وَقُلِ الْحَقُّ مِن رَّبِّكُمْ فَمَن شَاءَ فَلْيُؤْمِن وَمَن شَاءَ فَلْيَكْفُرْ ﴿٢٩﴾

“Na sema haki inatoka kwa Mola wenu basi atakaye aamini na atakaye akufuru” (18:29)

Lakini hutokea, katika hali maalum, haja ya kutokuwepo washirikina kwa sababu wao wanaeneza ufisadi katika ardhi. Katika hali hii inajuzu kwa kuwalazimisha washirikina watamke kalima ya shahada. Na, washirikina wa bara Arabu wakati huo walikuwa ni kikosi cha tano katika jamii ya kiislamu mpya.

Kwa ajili hiyo ndipo ikawa hukumu kwao ni kuuawa au kudhihirisha Uislamu na wawe na walionayo Waislamu. Kwa maneno mengine ni kwamba hukumu hiyo ilikuwa ni maalum kwa washirikina wa bara Arabu wakati huo tu, yametangulia maelezo kuhusu hayo katika Juz.3 (2:256)

Na ni tangazo litokalo kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa watu siku ya Hijja kubwa ya kwamba Mwenyezi Mungu amejitoa na washirikina na pia Mtume wake. Basi kama mkitubu ndiyo heri kwenu, na kama mkikengeuka, basi jueni kwamba nyinyi hamuwezi kumshinda Mwenyezi Mungu na wabashirie waliokufuru adhabu iumizayo.

Siku ya Hijja kubwa ni ile siku ya kuchinja (siku ya kumi ya Dhul-Hijja). Miezi minne ilianzia hapo, mnamo mwaka wa tisa wa Hijra na kumalizikia siku ya kumi, Rabiul-Akhar, mwaka wa kumi Hijra. Baada ya muda huo ndipo ikawa sasa washirikina wa bara Arabu wachague mawili. Kusilimu au kupigwa, kwa sababu ilikuwako haja ya kufanya hivyo kama tulivyoashiria.

Wafasiri, akiwemo Tabari, Razi na Abu Hayan Al-Andalusi, wamesema kwamba: iliposhuka Sura Tawba Mtume(s.a.w.w) alimwamrisha Ali awaendee watu kwenye msimu wa Hijja awasomee. Akaambiwa: kwa nini usimpe Abu Bakr, akasema: Hanitekelezei ila mtu anayetokana na mimi. Ali akasimama kwenye Jamratul-Aqaba siku ya kuchinja na kusema: “Enyi watu! Mimi ni mjumbe wa mjumbe wa Mwenyezi Mungu” Akawasomea Aya hizo.

Ispokuwa wale mlioahidiana nao miongoni mwa washirikina kisha hawakuwapunguzia chochote wala hawakumsaidia yeyote juu yenu, basi watimizieni ahadi yao mpaka muda wao.

Baada ya Mwenyezi Mungu kumwamrisha Mtume wake(s.a.w.w) kuwapa muda wa miezi minne washirikina; hata wale ambao walivunja ahadi na waislamu, aliwatoa katika washirikina wale waliokuwa na mkataba wa amani na waislamu na hawakuvunja mkataba huo.

Aliwatoa hawa na kuwapa muda wa miezi minne tu, bali aliwapa muda wao kadiri watakavyokuwa wanatekeleza mkataba wao. Wafasiri wengi wanasema kuwa washirikina hao waliotekeleza mkataba ni watu wa Kinana, na muda wao ulikuwa umebakia miezi tisa, Ndipo mtume akawatimizia muda wao.

Aya hii inafahamisha kwamba si wajibu kutekeleza mkataba ila ikiwa upande wa pili nao unatekeleza. Ukiharibu kipengele chochote, basi huhis- abiwa uhaini na uvunjaji ahadi. Wala hapana ahadi kwa anayevunja ahadi.

Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wenye takua ambao wanaogopa kuvunja ahadi na ufisadi mwengineo.

فَإِذَا انسَلَخَ الْأَشْهُرُ الْحُرُمُ فَاقْتُلُوا الْمُشْرِكِينَ حَيْثُ وَجَدتُّمُوهُمْ وَخُذُوهُمْ وَاحْصُرُوهُمْ وَاقْعُدُوا لَهُمْ كُلَّ مَرْصَدٍ فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَخَلُّوا سَبِيلَهُمْ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٥﴾

5. Ikisha miezi mitukufu, basi waueni washirikina popote mtakapowakuta, na wakamateni na muwazingire na wakalieni katika kila njia. Lakini wakitubu na wakasimamisha swala na wakatoa zaka, basi iacheni njia yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

وَإِنْ أَحَدٌ مِّنَ الْمُشْرِكِينَ اسْتَجَارَكَ فَأَجِرْهُ حَتَّىٰ يَسْمَعَ كَلَامَ اللَّـهِ ثُمَّ أَبْلِغْهُ مَأْمَنَهُ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَعْلَمُونَ ﴿٦﴾

6. Na kama yeyote katika washirikina akikutaka hifadhi, basi mhifadhi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu, kisha mfikishe mahali pake pa amani. Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasiojua.

كَيْفَ يَكُونُ لِلْمُشْرِكِينَ عَهْدٌ عِندَ اللَّـهِ وَعِندَ رَسُولِهِ إِلَّا الَّذِينَ عَاهَدتُّمْ عِندَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ فَمَا اسْتَقَامُوا لَكُمْ فَاسْتَقِيمُوا لَهُمْ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُتَّقِينَ ﴿٧﴾

7. Itakuwaje ahadi kwa washirikina mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya Mtume wake. Isipokuwa wale mlioahidiana kwenye msikiti mtakatifu. Basi maadamu wanakwenda na nyinyi sawa nanyi nendeni nao sawa, Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wenye takua.

كَيْفَ وَإِن يَظْهَرُوا عَلَيْكُمْ لَا يَرْقُبُوا فِيكُمْ إِلًّا وَلَا ذِمَّةً يُرْضُونَكُم بِأَفْوَاهِهِمْ وَتَأْبَىٰ قُلُوبُهُمْ وَأَكْثَرُهُمْ فَاسِقُونَ ﴿٨﴾

8. Itakuwaje! nao wakiwashinda hawaangalii kwenu ujirani wala ahadi. Wanawafurahisha kwa midomo yao tu, hali nyoyo zao zinakataa. Na wengi wao ni mafasiki.

MIEZI MITUKUFU IKIISHA

Aya 5-8

MAANA

Ikisha miezi mitukufu, basi waueni washirikina popote mtakapowakuta, na wakamateni na muwazingire na wakalieni katika kila njia.

Kuwakamata ni kuwachukua mateka. Kuwazingira, kuwafunga na kuwakalia kila njia ni kuwachunga katika kila njia wanayopita na kutowaacha wasichomeke.

Ama miezi mitukufu tumetaja katika Juz.2 (2:194) kwamba Mwenyezi Mungu ameharamisha kupigana katika miezi minne: Dhul-Qaada, Dhul- Hijja, Muharram na Rajab[4] .

Miezi hii siyo iliyo kusudiwa hapa; isipokuwa makusudio ya miezi mitukufu hapa ni miezi minne ambayo Mwenyezi Mungu aliharamisha ndani yake kupigana na washirikina wa Bara Arabu. Akawahalalishia ndani ya muda huu watembee kwa amani katika nchi, kuanzia tarehe 10, Dhul-Hijja 9 A.H mpaka tarehe 9 Rabiul- Akhar 10A.H.

Baada ya hapo aliamrisha kuwapiga washirikina na kuwateka na kuwafunga na kuwaandama popote watakapoelekea, ikiwa hawakusilimu au wahame kabla ya kwisha muda. Hiyo ni kwa ajili ya kuchelea shari yao na ufisadi wao.

Lakini wakitubu na wakasimamisha swala na wakatoa zaka, basi iacheni njia yao. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Yaani wakisilimu kabla ya kwisha muda na wakaendeleza nembo za dini ambazo miongoni mwa zilizo muhimu ni kuswali na kutoa zaka, basi wao wako katika amani. Watakuwa kama waislamu wengine bila ya tofauti yeyote.

Na kama yeyote katika washirikina akikutaka hifadhi, basi mhifadhi apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu, kisha mfikishe mahali pake pa amani.

Yaani mshirikina yeyote ambaye inajuzu kumwua, akijitolea au kutaka hifadhi ya amani kwa waislamu basi wamhifadhi na kumpa amani ya nafsi yake na mali yake, na kumlingania kwenye Uislam kwa hikima na mawaidha mazuri.

Akikubali basi atachukuliwa kama waislamu wengine, na kama akikataa basi si halali kumuua na ni wajibu kwa waislamu kumfikisha mahali atakapo kuwa salama.

Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasiojua.

Hayo ni ishara ya kutoa hifadhi kwa mshirikina, kumwambia maneno ya Mwenyezi Mungu na kumfikisha mahali pa salama yake. Kusema kwake Mwenyezi Mungu: ‘Hayo ni kwa kuwa wao ni watu wasiojua’ ni kubainisha sababu ambayo ni kutojua wale washirikina wanaotaka hifadhi Uislamu na hakika yake.

Wametoa fat-wa mafaqih kwamba waislamu wawape amani washirikina kwa sharti ya kutokuweko uchafuzi wa amani, kwa yule mtaka hifadhi asiwe ni jasusi na wala jihadi isiyumbe kwa kumpa amani.

Itakuwaje ahadi kwa washirikina mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele ya Mtume wake.

Aya hii inakamilisha Aya ya kwanza na ya nne ya Sura hii. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewajibisha, katika Aya ya kwanza, kuvunja mkataba na washirikina waliofanya hiyana, Hawa ndio wanaokusudiwa hapa. Na amewajibisha, katika Aya ya nne, kutekeleza mkataba na washirikina wanaoheshimu mkataba bila ya kupunguza kitu, hao ndio wanaokusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

Isipokuwa wale mlioahidiana kwenye msikiti mtakatifu. Basi maadamu wanakwenda na nyinyi sawa nanyi nendeni nao sawa, Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wenye takua.

Yaani bakieni nao na mkataba wa amani maadamu wao wamebaki hivyo. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anawachukia watu wa hiyana na anawapenda wanaotekeleza wenye kumcha Mwenyezi Mungun (takua).

Kusema kwake kwenye msikiti mtakatifu, ni kuashiria mahali palipofanyi- ka mkataba wa amani na Bani Kinana. Kwani Mtume(s.a.w.w) aliwekeana nao mkataba aliopatana nao Hudaibiya karibu na Makka.

Itakuwaje! nao wakiwashinda hawaangalii kwenu ujirani wala ahadi. Wanawafurahisha kwa midomo yao tu, hali nyoyo zao zinakataa. Na wengi wao ni mafasiki.

Dhamir inawarudia wavunjaji mkataba, Amewataja, Mwenyezi Mungu, kwa mambo matatu mabaya:

1. Uovu, kwa sababu wao lau wangeliwashinda waislam wangewalifanya vya kuwafanya bila ya kuchunga ahadi wala ubinadamu.

2. Unafiki kwamba wao wanasema mdomoni yale yasiyokuwa nyoyoni mwao.

3. Ufasiki.

Sifa moja tu miongoni mwa sifa hizi tatu inawahukumu kuadhibiwa na kuwatoa katika haki zote za ubinadamu, sikwambii kuwatekelezea ahadi tena. Sasa itakuwaje wakisifika na zote tatu kwa pamoja!

Utauliza : makafiri wote ni mafasiki kwa sababu, ukafiri ni ufasiki na zaidi. Sasa vipi Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewatoa wengine kwa kauli yake. ‘Na wengi wao ni mafasiki?.

Jibu : maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu na wengi wao ni mafasiki ni kwamba makafiri wengi huendelea na ukafiri na ufasiki wao, wala hawatarajiwi kuongoka kwa hali yeyote.

Na wako wachache miongoni mwao wanaoacha upotevu wao, Kwa hiyo makusudio ya ufasiki hapo ni kuendelea na kutouacha. Aina ya ibara kama hii ni nyingi katika Qur’an.

اشْتَرَوْا بِآيَاتِ اللَّـهِ ثَمَنًا قَلِيلًا فَصَدُّوا عَن سَبِيلِهِ إِنَّهُمْ سَاءَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٩﴾

9. Wamenunua thamani ndogo kwa ishara za Mwenyezi Mungu, kwa hiyo wakazuilia na njia yake. Hakika ni mabaya waliyokuwa wakiyafanya.

لَا يَرْقُبُونَ فِي مُؤْمِنٍ إِلًّا وَلَا ذِمَّةً وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُعْتَدُونَ ﴿١٠﴾

10. Hawaangalii kwa Mumin ujirani wala ahadi; na hao ndio warukao mipaka.

فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ وَنُفَصِّلُ الْآيَاتِ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ ﴿١١﴾

11. Kama wakitubu na wakasi- mamisha Swala na wakatoa Zaka, basi ni ndugu zenu katika dini na tunazifafanua Aya kwa watu wanaojua

وَإِن نَّكَثُوا أَيْمَانَهُم مِّن بَعْدِ عَهْدِهِمْ وَطَعَنُوا فِي دِينِكُمْ فَقَاتِلُوا أَئِمَّةَ الْكُفْرِ إِنَّهُمْ لَا أَيْمَانَ لَهُمْ لَعَلَّهُمْ يَنتَهُونَ ﴿١٢﴾

12. Na kama wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao na wakatukana dini yenu, basi piganeni na viongozi wa ukafiri, Hakika hao hawana viapo (vya maana), Ili wapate kukoma.

أَلَا تُقَاتِلُونَ قَوْمًا نَّكَثُوا أَيْمَانَهُمْ وَهَمُّوا بِإِخْرَاجِ الرَّسُولِ وَهُم بَدَءُوكُمْ أَوَّلَ مَرَّةٍ أَتَخْشَوْنَهُمْ فَاللَّـهُ أَحَقُّ أَن تَخْشَوْهُ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٣﴾

13. Je, hamtapigana na watu waliovunja viapo vyao na wakawa na hamu ya kumtoa Mtume nao ndio waliowaanza mara ya kwanza? Je, mnawaogopa? Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumuogope ikiwa nyinyi ni waumin.

قَاتِلُوهُمْ يُعَذِّبْهُمُ اللَّـهُ بِأَيْدِيكُمْ وَيُخْزِهِمْ وَيَنصُرْكُمْ عَلَيْهِمْ وَيَشْفِ صُدُورَ قَوْمٍ مُّؤْمِنِينَ ﴿١٤﴾

14. Piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu, na awafedheheshe, na awanusuru muwashinde na avipoze vifua vya kaumu ya waumin.

وَيُذْهِبْ غَيْظَ قُلُوبِهِمْ وَيَتُوبُ اللَّـهُ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿١٥﴾

15. Na aondoe hasira ya nyoyo zao Na Mwenyezi Mungu humkubalia toba amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni mjuzi, mwenye hekima.

WANAZIUZA AYA ZA MWENYEZI MUNGU

Aya 9-15

MAANA

Wamenunua thamani ndogo kwa ishara za Mwenyezi Mungu, kwa hiyo wakazuilia na njia yake. Hakika ni mabaya waliyokuwa wakiyafanya.

Dhamir inawarudia washirikina ambao Mwenyezi Mungu ameamrisha wauawe, Maana ni kuwa hawa wameupinga Uislam wakaupiga vita na kuzuilia watu nao, kwa kuhofia masilahi yao waliyoathirika nayo kuliko ishara za Mwenyezi Mungu na ubainifu wake uliowajia.

Aya hii sio kama inahusika na washirikina na watu wa Kitab tu, bali inawakusanya ambao wanaiharibu dini kwa ajili ya kuafiki matakwa ya wakoloni na wanyonyaji.

Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 4 (3:187).

Hawaangalii kwa Mumini ujirani wala ahadi; na hao ndio warukao mipaka.

Utauliza kuwa : Aya hii ni mfano wa Aya iliyotangulia (ya nane) kwa nini imerudiwa?

Jibu : Mwenyezi Mungu (s.w.t), katika Aya iliyotangulia, alikuwa akiwambia maswahaba wa Mtume(s.a.w.w) na kuwa lau washirikina watawashinda basi watafanya maajabu. Huenda hapo mtu akadhania kwamba washirikina wanadhamiria chuki na uadui kwa Mtume(s.a.w.w) na maswahaba tu.

Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akaondoa dhana hii kwamba uadui wa washirikina, kwa waislamu wakati huo ni uadui wa msingi wenyewe, sio uadui wa watu; ni uadui wa kufuru kwa imani na batili kwa haki:

وَمَا نَقَمُوا مِنْهُمْ إِلَّا أَن يُؤْمِنُوا بِاللَّـهِ الْعَزِيزِ الْحَمِيدِ ﴿٨﴾

“Nao hawakuwachukia ila ni kwa vile wamemwamini Mwenyezi Mungu mwenye nguvu mwenye kusifiwa”. (85:8)

Kama wakitubu na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka, basi ni ndugu zenu katika dini na tunazifafanua Aya kwa watu wanaojua.

Aya hii inaafikiana na Aya ya tano katika sharti (wakitubu na wakasimamisha Swala na wakatoa Zaka), lakini inatofautiana katika jawabu la sharti. Jawabu katika Aya iliyotangulia ni kuwachia njia na mambo yao na kutowataaradhi na chochote. Jawabu katika Aya hii ni kuwa ni ndugu zenu, yaani nyinyi na wao mkeo sawa katika haki, hakuna bwana wala mtumwa; mwenye kula au kuliwa; kama ilivyokuwa hali ya washirikina.

Kwa kutofautiana huko katika jawabu la sharti,kunafutika kukaririka, ingawaje kukaririka katika Qur’an sio jambo la nadra.

Na kama wakivunja viapo vyao baada ya kuahidi kwao na wakatukana dini yenu, basi piganeni na viongozi wa ukafiri, Hakika hao hawana viapo (vya maana), Ili wapate kukoma.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameleta ibara ya kupigana na makafiri kwa kusema ‘piganeni na viongozi wa makafiri,’ kwa vile wao ndio wanaowaon- goza kwenye vita na kuvunja ahadi, na wanatukana na kuwahimiza wafuasi wao wamtukane Mtume(s.a.w.w) na Qur’an.

Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘ili wapate kukoma’ inaashiria makusudio ya kupigana, - Kuwazuia washirikina wasiendelee kupigana na waislam.

Je, hamtapigana na watu waliovunja viapo vyao na wakawa na hamu ya kumtoa Mtume nao ndio waliowaanza mara ya kwanza?

Maneno yanaelekezwa kwa waislamu na dhamir inawarudia makafiri wa Kiquraish, kwa sababu wao ndio waliomwahidi Mtume wa Mwenyezi Mungu kuacha kupigana miaka kumi, kuishi kwa amani makundi yote mawili na walioungana nao.

Hapo ilikuwa ni mwaka wa sita wa Hijra. Lakini hawakudumu na mkataba huo. Vile vile wao ndio waliodhamiria kumuua Mtume(s.a.w.w) mpaka akalazimika kuhama na ndio wao walioanza kupigana siku ya Badr.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwakumbusha waislam walivyofanya washirikina kuvunja ahadi na kumtoa Mtume na kuanza vita, aliwahimiza jihadi na kupigana, ambapo hakuna njia nyingine isiyokuwa hiyo.

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawaondolea hofu waumini kwa kusema:

Je, mnawaogopa? Basi Mwenyezi Mungu anastahiki zaidi mumuogope ikiwa nyinyi ni waumin.

Kauli yake Mwenyezi Mungu ikiwa nyinyi ni waumini, inaashiria kwamba kumwogopa Mwenyezi Mungu kiuhakika hasa, hakuwi wala haku-takuwa ila kwa anayemwamini Mwenyezi Mungu kiuhakika hasa.

Ama mwenginewe, hamwogopi Mwenyezi Mungu hasa, ispkokuwa kumwogopa kwake ni kama njozi tu zinazopita.

Imam Ali anasema: “Kila hofu ina uthibitisho, isipokuwa kumhofia Mwenyezi Mungu, huko kuna ila”. Yaani Mtu kumwogopa asiyekuwa Mwenyezi Mungu ni jambo la uhakika, lakini kumhofia Mwenyezi Mungu hakuwi na uhakika halisi, isipokuwa ni njozi tu zinazoondoka kwa kitu kidogo.

Piganeni nao, Mwenyezi Mungu awaadhibu kwa mikono yenu, na awafedheheshe, na awanusuru muwashinde na avipoze vifua vya kaumu ya waumin na aondoe hasira ya nyoyo zao.

Sifa hizi zinanasibiana na ushindi wa kuiteka Makka. Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwadhalilisha na kuwafedhehesha vigogo vya Maqureish na kuwapa ushindi waislamu na kuvipoza vifua vya waumini ambao walikandamizwa na waonevu wa Kiqureish kabla ya Hijra, na kuwepo aina kwa aina ya mateso.

Na Mwenyezi Mungu humkubalia toba amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni mjuzi, mwenye hekima.

Makka ulikuwa ndio makao makuu ya nchi ya Hijaz na kituo cha harakati zote katika Bara Arabu. Wakuu wake walikuwa wakimchomolea upanga wa dhulma na utisho kila mwenye kutaka kujiunga na Mtume Muhamad(s.a.w.w) .

Baada ya kutekwa, Makka ilikuwa chini ya kivuli cha Uislamu na wakasilimu wale mataghuti. Hata hivyo baadhi yao walisilimu kwa kupenda sio kwa kuhofia. Wakasilimu kidhati na kindani. Hawa ndio wale ambao Mwenyezi Mungu amewakubalia toba na atawalipa kwa ikhlasi yao na ukweli wa nia yao.

Baada ya hayo, hakika kila hukumu iliyofungamana na Aya hizi inahusika na washirikina wa Kiarabu wakati huo. Kwa sababu wao ndio waliomtoa Mtume(s.a.w.w) , wakampiga vita na wakaacha kuheshimu mkataba.

Lakini kwa kukadiria kwamba Aya hizo zinawajibisha jihadi dhidi ya washirikina kila mahali na kila wakati, basi jihadi hiyo haijuzu ila kwa uongozi wa dola ya Kiislamu kwa kuongozwa na Maasum au naibu wake.

Yuko wapi huyo hivi sasa? Amedai hayo mwenye kudai, akaanzisha chama kwa ajili kwa uongozi wake, kisha akabainika kuwa ni kibaraka, wakamuepuka wale aliowahadaa waliokuwa wameghafilika na wala hajulikani alipo mpaka sasa.

Hata hivyo, jihadi ya mtu kulinda uhuru wake, mali yake na nchi yake haingoji kupatikana dola ya Kiislam wala haihitaji idhini ya maasum au asiyekuwa maasum.

Kwa sababu kulinda nafsi na nchi na kuwapiga wakoloni wanyonaji ni haki inayotukuzwa na sharia zote na kanuni zote. Tumeyaeleza katika kufasiri Juz.1 (2:19-193) Juz.4 (3:95) na katika Juzuu hii tuliyonayo sura (8:47).


5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تُتْرَكُوا وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّـهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَلَمْ يَتَّخِذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ وَلَا رَسُولِهِ وَلَا الْمُؤْمِنِينَ وَلِيجَةً وَاللَّـهُ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿١٦﴾

16. Je, mnadhani kuwa mtaachwa na hali Mwenyezi Mungu hajawabainisha wale wanaopigana jihadi miongoni mwenu, na hawakumfanya mwandani asiyekuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na waumin? Na Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyafanya.

مَا كَانَ لِلْمُشْرِكِينَ أَن يَعْمُرُوا مَسَاجِدَ اللَّـهِ شَاهِدِينَ عَلَىٰ أَنفُسِهِم بِالْكُفْرِ أُولَـٰئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ وَفِي النَّارِ هُمْ خَالِدُونَ ﴿١٧﴾

17. Haiwi kwa washirikina kuamirisha Misikiti ya Mwenyezi Mungu, hali wanajishuhudia wenyewe ukafiri, Hao vitendo vyao vimeporomoka, Nawatadumu katika moto.

إِنَّمَا يَعْمُرُ مَسَاجِدَ اللَّـهِ مَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَأَقَامَ الصَّلَاةَ وَآتَى الزَّكَاةَ وَلَمْ يَخْشَ إِلَّا اللَّـهَ فَعَسَىٰ أُولَـٰئِكَ أَن يَكُونُوا مِنَ الْمُهْتَدِينَ ﴿١٨﴾

18. Wanaoamirisha misikiti ya Mwenyezi Mungu ni wale tu wanaomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na wakasimamisha swala na wakatoa zaka na wasiogope ila Mwenyezi Mungu, Basi hao huenda wakawa miongoni mwa waliongoka.

MNADHANI MTAACHWA

Aya 16-18

MAANA

Je, mnadhani kuwa mtaachwa na hali Mwenyezi Mungu hajawabain- isha wale wanaopigana jihadi miongoni mwenu.

Imetangulia tafsir yake katika Juz.4 (3:142)

Na hawakumfanya mwandani asiyekuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na waumin?

Utiifu bora zaidi kwa Mwenyezi Mungu ni kuwapiga vita wabatilifu- maadui wa haki na ubinadamu. Ndipo akadokeza Mwenyezi Mungu: ‘Na hali hajawabainisha wale wanaopigana jihadi miongoni mwenu.”

Na maasi makubwa zaidi ni kuwapondokea, hapo akaeleza Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa kusema: “Na hawakumfanya mwandani”

Kila mwenye kuwategemea watu wa dhulma na uadui na kuyaunganisha maslahi yake na yao, basi yeye ni adui wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na waumin. Ni juu ya kila mwenye ikhlas kumtangaza na kufichua njama zake ili watu wamtofautishe yeye na mwaminifu na kumweka kila moja anapostahiki.

Na Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyafanya

Ndio yeye ni mjuzi mwenye habari, lakini hamwadhibu yeyote kwa anay- oyajua kwake, bali hata kwa yanayofichuka katika vitendo vyake na tabia zake.

Haiwi kwa washirikina kuamirisha misikiti ya Mwenyezi Mungu.

Katika vitabu vya lugha husemwa, Nyumba imaamirika kwa wakazi wake, yaani wamekuwa wakazi humo au fulani amemuamirisha Mola wake, yaani amemwabudu. Ikaenea midomoni mwa watu Misikiti inaamirishwa kwa kutajwa Mwenyezi Mungu. Kuna Hadith isemayo: “Mwenyezi Mungu anasema: Majumba yangu katika ardhi ni misikiti, na wanaonizuru humo ndio wanaoiiamirisha.”

Hayo ndiyo maana yanayochukuliwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu kuamirisha misikiti, Yaani washirikina wasiingie na kufanya ibada zao za mizimu, kama walivyokuwa wakifanya siku za jahiliya. Ni bora pia wasiwe na usimamizi. Maana hiyo yanatiwa nguvu zaidi na kauli yake Mwenyezi Mungu:

Hali wanajishuhudia wenyewe ukafiri.

Kwa sababu kuabudu kwao masanamu na kuwaomba Lata na Uzza ni ushahidi wao juu yao wenyewe kwamba wao wanamkufuru Mwenyezi Mungu, Na mwenye kumkufuru hastahiki kuingia majumba ya Mwenyezi Mungu.

Hao vitendo vyao vimeporomoka.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu haikubali amali pamoja na shirk.

Na katika moto watadumu.

Kwa sababu shirk imeangusha vitendo vyao vyote, hata vilivyokuwa vizuri.

Wanaoamirisha misikiti ya Mwenyezi Mungu ni wale tu wanaomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na wakasimamisha swala na wakatoa zaka na wasiogope ila Mwenyezi Mungu.

Yaani haijuzu kwa yeyote kuingia msikitini na kufanya ibada humo au kusimamia jambo lake lolote ila zikikusanyika humo sifa hizo. Kumwamini Mungu na Siku ya mwisho, na kuwa na nembo za dini ambazo muhimu zaidi ni kuswali na kutoa zaka na kumhofia Mwenyezi Mungu, yaani kumfanyia ikhlas katika kauli na vitendo.

Basi hao huenda wakawa miongoni mwa waliongoka kwenye haki na kuitumia.

Neno huenda kutoka kwa Mwenyezi Mungu, linamaanisha yakini kwa sababu shaka ni mahali kwake.

أَجَعَلْتُمْ سِقَايَةَ الْحَاجِّ وَعِمَارَةَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ كَمَنْ آمَنَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَجَاهَدَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ لَا يَسْتَوُونَ عِندَ اللَّـهِ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴿١٩﴾

19. Je, mnafanya kuwanywesha mahujaji na kuamirisha msikiti mtukufu ni sawa na yule aliyemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na akapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu? Hawawi sawa mbele ya Mwenyezi Mungu Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.

الَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ أَعْظَمُ دَرَجَةً عِندَ اللَّـهِ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَائِزُونَ ﴿٢٠﴾

20. Wale walioamini na wakahama na wakapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kwa mali zao na nafsi zao, wana cheo kikukbwa mbele ya Mwenyezi Mungu, na hao ndio wenye kufuzu.

يُبَشِّرُهُمْ رَبُّهُم بِرَحْمَةٍ مِّنْهُ وَرِضْوَانٍ وَجَنَّاتٍ لَّهُمْ فِيهَا نَعِيمٌ مُّقِيمٌ ﴿٢١﴾

21. Mola wao anawabashiria rehema kutoka kwake na radhi na pepo ambazo watapata humo neema zitakazodumu.

خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا إِنَّ اللَّـهَ عِندَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ ﴿٢٢﴾

22. Watadumu humo milele, Hakika kwa Mwenyezi Mungu kuna malipo makubwa.

KUWANYWESHA MAHUJAJI

Aya 19-22

MAANA

Je, mnafanya kuwanywesha mahujaji na kuamirisha msikiti mtukufu ni sawa na yule aliyemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na akapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu?

Makusudio ya kunywesha mahujaji ni kuwapa watu maji ya kunywa katika Hijja na kuamirisha msikiti hapa ni kuuhudumia.

Tafsir nyingi, ikiwemo tafsir ya Tabari, Razi, Naisaburi na Suyuti, imeelezwa kuwa Abbas bin Abdul Muttalib alikuwa akiwanywesha maji watu katika Hijja, na Twalha bin Shayba kutoka ukoo wa Abduddar alikuwa na funguo za Al-Kaaba. Twalha akasema mimi ndio mwenye Al-Kaaba, nina funguo zake. Abbas naye akasema mimi ndio mwenye kunywesha, Ali Bin Abutalib akasema.

Sijui mnasema nini? Mimi nimeswali kibla miezi sita kabla ya watu wengine na mimi ni mwenye jihadi ndipo, Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hiyo.

Kwa hiyo Ali ndio makusudio ya ‘yule aliyemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho na akafanya jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu’

Hiki ndicho kipimo cha ubora mbele ya Mwenyezi Mungu - imani na kupigana jihadi katika njia yake. Ama wadhifa na vyeo mara nyingi humwongoza mtu kwenye ufisadi na maangamizi.

Hawawi sawa mbele ya Mwenyezi Mungu katika malipo na thawabu, Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu madhalimu.

Baada ya kuwalingania kwenye uongofu na kukataa kwa chaguo lao ovu.

Wale walioamini na wakahama na wakapigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu, kwa mali zao na nafsi zao, wana cheo kikukbwa mbele ya Mwenyezi Mungu, na hao ndio wenye kufuzu.

Wapi na wapi kunywesheleza mahujaji na kutumikia miskiti kulinganisha na imani, Hijra na Jihadi?

Umekwishapita mfano wa Aya hii katika Juzuu hii Sura (8:72). Neno cheo kikubwa hapa halina maana ya kuzidiana, isipokuwa ni kuthibitisha ubora wa waumini tu, kwani makafiri hawana cheo hata kile kidogo mbele ya Mwenyezi Mungu.

Mola wao anawabashiria rehema kutoka kwake na radhi na pepo ambazo watapata humo neema zitakazodumu, Watadumu humo milele. Hakika kwa Mwenyezi Mungu kuna malipo makubwa.

Anasema mwenye Bahrul-Muhit: “Waumin wamesifika na sifa tatu: Imani, Hijra na Jihad. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akawakabili na matatu Rehema, Radhi na Pepo”

Razi amerefusha maneno katika kubainisha tofauti ya sifa hizi, Ama sisi tunaona kuwa sifa hizo pamoja na kufuzu na malipo ni kwa maana moja kwamba waumin wenye kufanya amali wako katika hifadhi ya Mwenyezi Mungu. Na neno ‘Radhi ya Mwenyezi Mungu’ lingetoshelezea yote, kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema:

وَرِضْوَانٌ مِّنَ اللَّـهِ أَكْبَرُ ﴿٧٢﴾

“Na radhi za Mwenyezi Mungu ndizo kubwa zaidi” (9:72)

Lakini Mwenyezi Mungu na Mtume wake(s.a.w.w) alitaka kuwatukuza na kuwahimiza waja wake kwenye Imani na Matendo mema.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّخِذُوا آبَاءَكُمْ وَإِخْوَانَكُمْ أَوْلِيَاءَ إِنِ اسْتَحَبُّوا الْكُفْرَ عَلَى الْإِيمَانِ وَمَن يَتَوَلَّهُم مِّنكُمْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٢٣﴾

23. Enyi mlioamini! Msiwafanye baba zenu na ndugu zenu kuwa mawalii ikiwa wamestahabu kufuru kuliko imani, Na atakayewafanya mawalii katika nyinyi basi hao ndio madhalimu.

قُلْ إِن كَانَ آبَاؤُكُمْ وَأَبْنَاؤُكُمْ وَإِخْوَانُكُمْ وَأَزْوَاجُكُمْ وَعَشِيرَتُكُمْ وَأَمْوَالٌ اقْتَرَفْتُمُوهَا وَتِجَارَةٌ تَخْشَوْنَ كَسَادَهَا وَمَسَاكِنُ تَرْضَوْنَهَا أَحَبَّ إِلَيْكُم مِّنَ اللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَجِهَادٍ فِي سَبِيلِهِ فَتَرَبَّصُوا حَتَّىٰ يَأْتِيَ اللَّـهُ بِأَمْرِهِ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ ﴿٢٤﴾

24. Sema ikiwa baba zenu na wana wenu na ndugu zenu na wake zenu na jamaa zenu na mali mlizozichuma na biashara mnazohofia kuharibikiwa, na majumba mnayopenda, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na jihadi katika njia yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu mafasiki.

MSIWAFANYE BABA ZENU NA NDUGU ZENU MAWALII

Aya 23-24

MAANA

Enyi mlioamini! Msiwafanye baba zenu na ndugu zenu kuwa mawalii ikiwa wamestahabu kufuru kuliko imani.

Makusudio ya uwalii hapa ni kusaidia. Uislamu unaamrisha kutokata udugu, ukazingatia kuwa kuwaudhi wazazi ni katika madhambi makubwa, ukausia ujirani, kutekeleza haki ya urafiki na mikataba na ahadi zote.

Vilevile waislamu wamehalalishiwa kuwafanyia wema na uadilifu washirikina na yote hayo yanajuzu, lakini kwa sharti la kutoharamisha halali au kuhalalisha haramu.

Kwa mfano baba akiwa upande wa batili, haijuzu kwa mtoto kumsaidia, bali ni juu ya mtoto kumzuia na kumkataza akiweza.

Kwa hiyo kauli yake Mwenyezi Mungu ‘ikiwa wamestahabu kufuru kuliko imani,’ inakusanya maasia yote, Ikiwa baba yako au ndugu yako ni Mwislamu na akamdhulumu mwingine, basi ni juu yako kumsaidia aliyedhulumiwa dhidi ya huyo baba yako au ndugu yako.

Na atakayewafanya mawili katika nyinyi basi hao ndio madhalimu.

Kuna Hadith isemayo “Mwenye kufanya dhuluma na mwenye kuisaidia na mwenye kuiridhia ni mshiriki” Kwa maneno mengine ni kuwa haki iko juu ya ndugu na urafiki.

Sema: ikiwa baba zenu na wana wenu na ndugu zenu na wake zenu na jamaa zenu na mali mlizozichuma na biashara mnazohofia kuharibikiwa, na majumba mnayopenda, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na jihadi katika njia yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu mafasiki.

Inasemekana kuwa Aya hii ilishuka kwa ajili ya tukio maalum. Inawezekana kuwa ni kweli, lakini tamko lake ni la ujumla, pia hukumu yake.

Aya hii inawaelezea mumin kwa maelezo wazi na ya uhakika. Mwenye kuathirika na haki kuliko maslahi yake binafsi wakati yana-pogongana na haki basi huyo ni mumin mwema, vinginevyo basi ni mnafiki mwovu.

Hiyo ndiyo njia inayomtofautisha mumin na asiyekuwa mumin, kama ilivyoelezewa na Aya. Kutajwa ndugu mali na majumba ni mfano tu wa kuweka mbele manufaa kuliko haki ambayo Mwenyezi Mungu ameitolea ibara ya kumpenda Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Zaidi ya hayo yako manufaa mengine; kama vile kupupia maisha, kupenda jaha, utawala n.k.

Mtu kwa maumbile yake hujipenda na kupenda watu wake na mali yake, na dini haikatai hilo, wala haimzuii yeyote kustarehe atakavyo na kumpenda amtakaye, mradi tu amwogope Mwenyezi Mungu katika starehe hiyo, na yote hayo yamekutana na juhudi yake sio juhudi za wengine.

Imepokewa kutoka kwa Bukhari kwamba Umar Bin Al-Khattab alimwambia Mtume(s.a.w.w) . Kwa hakika wewe unapendeza kwangu kuliko chochote isipokuwa nafsi yangu iliyo mbavuni mwangu”

Mtume(s.a.w.w) akamwambia: Hapana! Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake, ni mpaka niwe napendeza kwako kuliko nafsi yako iliyo mbavuni mwako”

Wala hakuna maana ya kumpenda Mtume(s.a.w.w) isipokuwa kumtii na kufanya mambo kulingana na sharia yake. Tumeyazungumzia haya katika Juz.5 (4:135)

لَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّـهُ فِي مَوَاطِنَ كَثِيرَةٍ وَيَوْمَ حُنَيْنٍ إِذْ أَعْجَبَتْكُمْ كَثْرَتُكُمْ فَلَمْ تُغْنِ عَنكُمْ شَيْئًا وَضَاقَتْ عَلَيْكُمُ الْأَرْضُ بِمَا رَحُبَتْ ثُمَّ وَلَّيْتُم مُّدْبِرِينَ ﴿٢٥﴾

25. Hakika Mwenyezi Mungu amewasaidia katika mwahala mwingi, kama vile na siku ya Hunain ulipowafuraisha wingi wenu. Lakini haukuwafaa chochote, na ardhi ikawa finyu juu yenu ingawa ilikuwa pana, kisha mkageuka mkirudi nyuma.

ثُمَّ أَنزَلَ اللَّـهُ سَكِينَتَهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ وَعَلَى الْمُؤْمِنِينَ وَأَنزَلَ جُنُودًا لَّمْ تَرَوْهَا وَعَذَّبَ الَّذِينَ كَفَرُوا وَذَٰلِكَ جَزَاءُ الْكَافِرِينَ ﴿٢٦﴾

26. Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha utulivu wake juu ya Mtume wake na juu ya waumin, Na akawateremshia majeshi ambayo hamkuyaona. Na akawaadhibu wale waliokufuru, Na hayo ndiyo malipo ya makafiri

ثُمَّ يَتُوبُ اللَّـهُ مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٧﴾

27. Kisha baada ya haya Mwenyezi Mungu atamkubalia toba amtakaye, Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

MWENYEZI MUNGU AMEWANUSURU

Aya 25-27

KISA CHA HUNAIN

Hunain ni bonde lilioko baina ya Makka na Taif, Vita vilvyopiganwa hapo vinaitwa vita vya Hunain, vita vya Autas au vita vya Hawazin. Vita hivyo vilikuwa mwezi wa Shawwal (mfunguo mosi) mwaka wa nane Hijra.

Mtume(s.a.w.w) alipoiteka Makka walimlia njama Hawazin na Thaqif wakakusanya maelfu kumpiga vita Mtume. Ilipomfikia Mtume(s.a.w.w) habari hiyo, alijiandaa na kukusanya jeshi la watu elfu 12, Elfu kumi kati yao ni Maswahaba wake aliotoka nao Makka na elfu mbili walikuwa ni Tulaqau[5] akiwemo Abu Safyan na mwanawe Muawiya.

Mtume(s.a.w.w) akaelekea kwa Hawazin njia yake ilipitia bonde la Hunain na ilikuwa nyembamba yenye maporomoko. Jeshi la adui lilikuwa limewatangulia kufika kwenye uchochoro wake wakajificha.

Mara tu jeshi la Waislamu lilipofika katikati ya bonde, maadui waliwamiminia mishale, watu wakaanza kusambaratika na Abu Sufyan ndiye wa mwanzo wao.

Sheikh Ghazali katika kitabu Fiqh Sera, Anasema: “Wengine walirudia ukafiri wao. Abu Sufyan akasema: ‘Kushindwa kwao hakutakoma mpaka baharini.’ Hilo si ajabu kwani mburuga alizokuwa akiagulia wakati wa Jahilia bado ziko mkobani mwake”.

Ali akabaki na Mtume wa Mwenyezi Mungu akiwa ameuchomoa upanga wake, huku Abbas ameshika lijamu ya farasi wake, Al-fadhl bin Abbas akiwa kuumeni kwa Mtume pamoja na Mughira Bin Harith Bin Abdul Muttalib, Zaid Bin Usama na Aiman Bin Ummu Aiman. Wakapigana mbele ya mtume wa Mwenyezi Mungu.

Washirikina walipoona waislam wanasamabaratika, walitoka kwenye ngome za bonde wakimfuatia Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mtume(s.a.w.w) akamwambia Ami yake Abbas aliyekuwa na sauti kubwa. Waite watu na uwakumbushe ahadi.

Akanadi kwa sauti kubwa: “Enyi watu wa Baia ya mti! (Mliombai mtume chini ya mti) Enyi watu wa Sura ya Baqara! Mnakwenda wapi? Kumbukeni ahadi mliyomwahidi Mtume wa Mwenyezi Mungu. Ansar waliposikia mwito wa Abbas walirudi na wakavunja ala za panga zao wakiwa wanasema: Labeka! Labeka! Wakamkabili adui na makundi mawili yakapambana vikali

Mshika bendera na shujaa wa washirikina alikuwa ni Abu Jarwal. Huyu alikuwa akiwashambulia waislamu na kuwaua. Ali Bin Abu Talib akapambana naye na kumuua. kwa kuliwa kwake jeshi la washirikina lilitawanyika na ushindi wa Mtume(s.a.w.w) na wa waumin ukapatikana.

Tulaqau walipojua kuwa waislamu wameshinda na kuna ngawira nyingi, walirudi kwa Mtume(s.a.w.w) , Katika Tafsir Bahrul-Muhit imeelezwa kuwa Tulaqau walikimbia wakikusudia waumin washindwe”.

Sharqawi naye anasema katika kitabu Muhammad Rasulul-Huriyya (Muhammad Mtume wa uhuru): “Maquraish elfu mbili wakiongozwa na Abu Suffin walisilimu kwa hofu au tamaa. Walikuja hiyo siku si kwa ajili ya kuusaidia Uislamu bali ni kwa ajili ya kuudhalilisha na kueneza ulegevu kwa wapiganaji jihadi waliowatangulia”.

Hivi ndivyo walivyo wanafiki na watu walio huku na kule. Wanajifanya ni wenye ikhlas, wanajiingiza katika safu za wapigania ukombozi na kupanga mambo. Wakichunguza mbinu zao, kisha wanapanga njama, zikifaulu njama zao, inakuwa wamepata waliyoyataka, au wakifaulu wakombozi, basi husema sisi na nyinyi tuko pamoja, Yametangulia maelezo ya hawa katika kufasiri Juz. 5 (4:141)

Hakika Mwenyezi Mungu amewasaidia katika mwahala mwingi.

Kama vile vita vya Badr, Quraidha, Nadhr, Hudaibiya, Khaibar na kuiteka Makka.

Na siku ya Hunain ulipowafurisha wingi wenu.

Razi anasema, “Mtu moja katika waislam alisema, Hatutashindwa kwa uchache leo. Akaona vibaya Mtume wa Mwenyezi Mungu. Inasemekana kuwa aliyesema hayo ni Mtume(s.a.w.w) na ilisemakana ni Abu Bakr. Kutegemeza neno hili kwa Mtume ni mbali”

Lakini haukuwafaa chochote, na ardhi ikawa finyu juu yenu ingawa ilikuwa pana, kisha mkageuka mkirudi nyuma.

Kuanzia kufura kichwa hadi kulemewa kabisa kiasi cha kutopata hata upenyo wa kujiokoa na adui yao. Huu ndio mwisho wa kila mwenye kujigamba na kumdharau adui yake.

Kisha Mwenyezi Mungu akateremsha utulivu wake juu ya Mtume wake na juu ya waumin.

Utulivu ni kuwa na mategemeo na umakini. Maana ya kuuteremsha kwa Mtume(s.a.w.w) ni kubakia kwake mwenye kuthibiti katikati ya vita akiwa makini na mwenye ushupavu akipangilia mambo, ingawaje wanajeshi wake, waliokuwa kiasi cha watu elfu kumi na mbili, wamekimbia wote, isipokuwa watu wasiozidi kumi, na huku jeshi la maadui likiwa na idadi ya maelfu.

Wapokezi wanasema Mtume(s.a.w.w) alikuwa akimchochea nyumbu wake kuwaelekea maadui huku akiwalingania wale waliokimbia. Njooni enyi waja wa Mwenyezi Mungu! Mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi ni Mtume sisemi uwongo mimi ni mwana wa Abdul-Muttalib.

Waumin ambao Mwenyezi Mungu aliwateremshia utulivu ndio wale waliothibiti bila ya kumkimbia, na wale waliorudi baada ya kushindwa na kuitikia mwito wa Mtume(s.a.w.w) wakiwa wenye ikhlas. Maana ya kuteremshiwa utulivu ni kuwa na utulivu katika nyoyo zao na kuwaondokea hofu.

Na akawateremshia majeshi ambayo hamkuyaona.

Razi anasema: “Hakuna tofauti kwamba makusudio ni kuteremshwa Malaika”. Ama sisi tunaitakidi kwamba Mwenyezi Mungu ana jeshi la Malaika na lisilokuwa Malaika kwa aina isiyokuwa na idadi. Miongoni mwa aina hizo ni nguvu ya nafsi na silika yake na nguvu za nje, Aya haikubainisha aina hii ya jeshi aliloteremsha Mwenyezi Mungu siku ya Hunain. Kwa hiyo ujuzi wake tunamwachia Mwenyezi Mungu aliyesema:

وَمَا يَعْلَمُ جُنُودَ رَبِّكَ إِلَّا هُوَ ﴿٣١﴾

“Na hakuna ajuaye majeshi ya Mola wako ila yeye tu” (74:31)

Na akawaadhibu wale waliokufuru.

Aliwaadhibu duniani kwa kuuliwa kutekwa, kushindwa na kuchukuliwa mali na atawaadhibu Akhera kwa moto wa Jahannam na ni marejeo mabaya.

Kisha baada ya haya Mwenyezi Mungu atamkubalia toba amtakaye, Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Mwenyezi Mungu ni mkarimu, hashindwi kusamehe dhambi kubwa, na mlango wake uko wazi kwa kila mwenye kubisha. Aliyekimbia Mtume wa Mwenyezi Mungu katika waislamu, kisha akatubia basi Mwenyezi Mungu anawapenda wanaotubia. Na mwenye kukufuru na akampiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake(s.a.w.w) kisha akatubia na akaamini na akafanya amali njema basi yeye ni katika waliofaulu.

Wanahistoria wanasema baada ya kwisha vita na ngawira kugawanywa ulikuja ujumbe kutoka Hawazin hali ya kuwa ni waislamu. Wakasema Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu wewe ni bora wa watu na mwema wao, wake zetu na watoto wetu wametawaliwa na mali zetu zimechukuliwa. Basi Mtume(s.a.w.w) akawakubalia Uislamu wao na wakarudishiwa wake na watoto wao.


6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْمُشْرِكُونَ نَجَسٌ فَلَا يَقْرَبُوا الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ بَعْدَ عَامِهِمْ هَـٰذَا وَإِنْ خِفْتُمْ عَيْلَةً فَسَوْفَ يُغْنِيكُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ إِن شَاءَ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٢٨﴾

28. Enyi Mlioamini! Hakika washirikina ni najis, kwa hivyo wasiukaribie Msikiti Mtakitifu baada ya mwaka wao huu. Na kama mkihofia umasikini, basi hivi karibuni Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake akitaka. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.

WASHIRIKINA NI NAJISI

Aya 28

MAANA

Enyi Mlioamini! Hakika washirikina ni najis, kwa hivyo wasiukaribie Msikiti Mtakitifu baada ya mwaka wao huu.

Yaani mwaka wa tisa wa Hijra, mwaka ambao Ali(a.s) aliwasomea watu Aya za kujitoa katika dhima.

Aghlabu Qur’an hulitumia neno washirikina kwa wanaoabudu masanamu; hasa washirikina wakiarabu. Na hutumia neno ‘Watu wa Kitab’ kwa mayahudi na wanaswara (wakristo). Kuunganisha washirikina na watu wa Kitab katika Aya isemayo:

مَّا يَوَدُّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَلَا الْمُشْرِكِينَ ﴿١٠٥﴾

“Hawapendi waliokufuru miongoni mwetu wa Kitab wala washirikina” (2:105)

na ile isemayo:

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ وَالْمُشْرِكِينَ ﴿٦﴾

“Hakika waliokufuru katika watu wa Kitab na washrikina…”(98:6)

Kunafahamisha kuwa kinachounganishwa si sawa na kinachouganishiwa, ingawaje inawezekana kuunganisha maalum kwenye ujumla, lakini ni kulingana na jumla yenye ilivyo.

Mafakihi wametofautiana kuhusu kuwazuia makafiri kuingia msikitini, Shafii anasema wanazuiwa mskikiti mtukufu (Masjidul-haram) tu, Malik anasema watazuiwa misikiti yote, Abu Hanifa anasema hazuiwi msikiti wowote, Hayo yamo katika Tafsir ya Razi katika kufasri Aya hii.

Tuonavyo sisi ni kuwa ni wajibu kuzuia najisi kwenye msikiti wowote na ikiwemo ndani ni wajibu kuitoa, ni sawa iwe ni ya mtu, mnyama au kitu kingine chochote. Iwe ni najisi ya itakayochafua msikiti na kuivunjia heshima yake au la. Dalili ya hayo ni kwamba hukumu ya kuharamisha imeachwa bila ya kufungwa na kitu chochote.

Tukisema mtu aliye najisi tuna maanisha mkanushaji na mwabudu masana- mu na mizimu. Ama watu wa Kitab tumethibtisha utohara wao katika Juz. 6 (5:5)

Unaweza kuuliza kuwa : kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘kwa hivyo wasiukaribie Msikiti Mtakitifu” inafahamisha kusihi kauli ya Shafii, kuwa kuzuia kunahusika na Msikiti Mtakatifu (Masjidul-haram) tu, sio mwengineo, Kwa sababu hakusema wasikaribie kila msikiti.

Jibu : mkusanyiko wa Aya unafahamisha kuenea, sio mahsusi. Kwa sababu linalokuja haraka kwenye fahamu ni kuwa sababu ya kuzuiwa kuingia ni najisi na kuheshimu msikiti mbele ya Mwenyezi Mungu.

Hakuna mwenye shaka kwamba kila msikiti unaheshimiwa mbele ya Mwenyezi Mungu kwa sababu unanasibishiwa kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na hukumu inakwenda pamoja na sababu yake kwa kuthibitisha na kukanusha.

Ndio maana mafakihi wakakongamana kuwa wiski ni haramu, ingawaje hakuna kauli wazi juu yake, kwa kutosheka na sababu ya kuharimishwa ulevi.

Na kama mkihofia umasikini, basi hivi karibuni Mwenyezi Mungu atawatajirisha kwa fadhila yake akitaka. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye hekima.

Washirikina katika pembe zote za bara Arabu walikuwa wakielekea Makka kuhiji na kufanya biashara. Watu wa Makka walikuwa wakinufaika na hilo, wakiuza na kununua kutoka kwao, pia walikuwa wakiwakodisha majumba. Na Makka iko katika jangwa lisilokuwa na mmea.

Basi Mwenyezi Mungu alipowazuia washirikina baadhi ya watu wa Makka walihofia ufukara, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawaambia hivyo; yaani mkihofia ufukara kwa sababu ya kukatika mawasiliano ya washirikina na Makka, basi Mwenyezi Mungu atawapa badali kwa njia nyingine.

Kwani sababu za riziki mbele yake ni idadi ya matone ya mvua; kama ilivyoelezwa katika Hadith.

Amesema kweli Mwenyezi Mungu na Mtume wake, aliwafungulia waislamu miji na ngawira, wakaingia watu kwa makundi katika dini yake, wakaelekea Makka kwa mamilioni pamoja na nyoyo zao na mali zao.

Watu wa Makka wakaona faida ambayo hata hawakuiota.

Utauliza : nini lengo la kauli yake Mwenyezi Mungu ‘Akitaka’ pamoja na kuwa alikwishataka?

Jibu : Yanaweza kuwa makusudio ni kudokeza kuwa visababishi vinapita kwa sababu zake na inaweza kuwa makusudio ni kuwafundisha waja wake wamtegemee Mwenyezi Mungu katika mambo yao yote na malengo yao wayaambatanishe na matakwa yake Mwenyezi Mungu pamoja na juhudi; kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَلَا تَقُولَنَّ لِشَيْءٍ إِنِّي فَاعِلٌ ذَٰلِكَ غَدًا ﴿٢٣﴾ إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ ﴿٢٤﴾

“Wala usiseme kamwe kwa jambo lolote lile: Hakika nitalifanya kesho ispokuwa Mwenyezi Mungu akitaka (inshaallah)” (18:23-24)

قَاتِلُوا الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَلَا بِالْيَوْمِ الْآخِرِ وَلَا يُحَرِّمُونَ مَا حَرَّمَ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَلَا يَدِينُونَ دِينَ الْحَقِّ مِنَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ حَتَّىٰ يُعْطُوا الْجِزْيَةَ عَن يَدٍ وَهُمْ صَاغِرُونَ ﴿٢٩﴾

29. Piganeni na wale wasiomwamini Mwenyezi Mungu wala siku ya mwisho wala hawaharamishi aliyoharamisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawashiki dini ya haki, miongoni mwa waliopewa Kitab, mpaka watoe kodi kwa mkono hali wametii.

وَقَالَتِ الْيَهُودُ عُزَيْرٌ ابْنُ اللَّـهِ وَقَالَتِ النَّصَارَى الْمَسِيحُ ابْنُ اللَّـهِ ذَٰلِكَ قَوْلُهُم بِأَفْوَاهِهِمْ يُضَاهِئُونَ قَوْلَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَبْلُ قَاتَلَهُمُ اللَّـهُ أَنَّىٰ يُؤْفَكُونَ ﴿٣٠﴾

30. Na mayahudi wanasema, Uzair ni mwana wa Mwenyezi Mungu; na wanaswara wanasema Masihi ni mwana wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo kauli yao kwa vinywa vyao, wanayaiga maneno ya wale waliokufuru zamani. Mwenyezi Mungu awangamize! Wanageuzwa wapi?

اتَّخَذُوا أَحْبَارَهُمْ وَرُهْبَانَهُمْ أَرْبَابًا مِّن دُونِ اللَّـهِ وَالْمَسِيحَ ابْنَ مَرْيَمَ وَمَا أُمِرُوا إِلَّا لِيَعْبُدُوا إِلَـٰهًا وَاحِدًا لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ سُبْحَانَهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٣١﴾

31. Wamefanya makuhani wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu na Masih mwana wa Maryam. Wala hawakuamrishwa isipokuwa wamwambudu Mungu mmoja hakuna Mungu ila yeye Ametakata na wanayomshirikisha nayo.

يُرِيدُونَ أَن يُطْفِئُوا نُورَ اللَّـهِ بِأَفْوَاهِهِمْ وَيَأْبَى اللَّـهُ إِلَّا أَن يُتِمَّ نُورَهُ وَلَوْ كَرِهَ الْكَافِرُونَ ﴿٣٢﴾

32. Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao, Na Mwenyezi Mungu amekataa isipokuwa kuitimiza nuru yake, ijapokuwa makafiri wamechukia.

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ ﴿٣٣﴾

33. Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokwa washirikina wamechukia.

PIGANENI NA WASIOMWAMNI MWENYEZI MUNGU

Aya 29 – 33

MAANA

Piganeni na wale wasiomwamini Mwenyezi Mungu wala siku ya mwisho wala hawaharamishi aliyoharamisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala hawashiki dini ya haki, miongoni mwa waliopewa Kitab, mpaka watoe kodi kwa mkono hali wametii.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuamrisha kupigana na washirikina ikiwa hawakusilimu wala hawakutoka, katika Aya hii ameamrisha kupigana na watu wa Kitab ikiwa hawakutoa kodi na kunyenyekea hukumu ya Kiislam.

Mwenyezi Mungu amewasifu kuwa hawamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho wala hawaharamishi haramu ya Mwenyezi Mungu au kufuata dini ya haki.

Ilivyo ni kwamba neno ‘miongoni’ katika kauli yake Mwenyezi Mungu ‘miongoni mwa wale walopewa Kitab’ ni la kubainisha jinsi. Na imesemekana ni la kufanya baadhi.

Hapa kuna maswali mawili:

Swali la Kwanza : Aya imeawakanushia watu wa Kitab kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho pamoja na kwamba wao wanaamini kuweko Mwenyezi Mungu. Kwa sababu neno watu wa Kitab hilo lenyewe linafahamisha kumwamini kwao Mwenyezi Mungu ambaye ameteremsha Tawrat na Injil.

Vile vile wanaamini siku ya mwisho kwa nukuu ya Aya isemayo:“Na wanasema: hautatugusa moto isipokuwa kwa siku chache tu” Juz. 1 (2:80) Ingawaje ni kweli kuwa wao hawafuati dini ya haki. Mayahudi wanaabudu mali na kanisa linauza cheki za msamaha?

Jawabu la swali hilo tunalipata katika Aya iliyo baada yake, bila ya kuweko kati kitu kingine:

Na mayahudi wanasema, Uzeir ni mwana wa Mwenyezi Mungu; na wanaswara wanasema Masihi ni mwana wa Mwenyezi Mungu.

Njia ya jawabu ni kuwa Mayahudi na Wakristo wamemfanya Mwenyezi Mungu kuwa na mtoto. Maana yake ni kuwa wanamwamini Mwenyezi Mungu asiyekuwepo ila katika mawazo yao tu, Ama Mungu aliyeko kweli, wao hawamwamini. Wameleta picha ya kua ni Mungu mwenye watoto. Ama Mola wa uhakika ambaye hakuzaa wala hakuzaliwa wao hawamwamini wala hafungamani nao kwa mbali au karibu.

Kwa ufupi ni kuwa Mungu aliyeko hawamwamini na wanamwamini mungu asiyeko. Natija ya yote hayo ni kuwa wao hawamwamini Mwenyezi Mungu.

Kimsingi ni kwamba asiyemwamini Mwenyezi Mungu haamini akhera kwa imani sawa, wala hafuati dini ya haki, hata kama itafikiriwa kuwa yeye ni katika wanaoamini akhera na wenye kufuata dini ya haki. Kwa sababu kumwamini Mwenyezi Mungu ndio asili (shina) mengineyo ni matawi, yaani yeye anaamini akhera na dini ambayo haina athari yoyote isipokuwa katika mawazo yao tu; kama kusema kwao: Hautatugusa moto isipokuwa kwa siku chache tu. Dini hiyo ndiyo ile iliyotajwa na yule aliye- sema: “Dini inatengenezwa na mawazo na njozi.”

Swali la pili : Uislamu haumlazimishi yeyote kuukubali kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

لَا إِكْرَاهَ فِي الدِّينِ ﴿٢٥٦﴾

“Hakuna kulazimishwa katika dini….”Juz: 3(2:256).

Na pia kauli yake Mwenyezi Mungu:

أَفَأَنتَ تُكْرِهُ النَّاسَ حَتَّىٰ يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ ﴿٩٩﴾

Basi je, wewe unawalazimisha watu hata wawe waumini? (10: 99).

Sasa imekuwaje kuamrishwa kupigana na watu wa Kitab mpaka waamini au watoe kodi?

Swali hili tumelitaja katika kufasiri Aya ya pili katika Sura hii, ambayo imeamrisha kupigana na washirikina.Tukajibu kwamba : amri ya kupigana nao ilikuwa ni hukumu maalum ya wakati huo, kwa sababu mahsusi, kwamba jamii ya Kiislam ndio ilikuwa inaanza na washirikina walikuwa ni kikosi cha tano[6] walifanyia vitimbi Uislamu na watu wake.

Masilahi yakawa ni kuwatoa bara arabu au kuwaua. Na amri ya kupigana hapa ni mahsusi kwa watu wa Kitab ambao walikuwa wakiungana na washirikina kuwapiga vita waislamu kama walivyofanya Mayahudi wa Madina na walio pembeni baada ya kuwekeana mkataba wa amani na mtume na kufanya muungano nao.

Zaidi ya hayo, kiini cha Sura hii ni vita vya Tabuk, kama itakavyoelezwa katika Aya 38 na zinazofuatia. Na, Mtume(s.a.w.w) alipata habari kwamba Warumi wakiwa Sham wanaanda majeshi kwa ajili ya kuumaliza Uislamu na watu wake. Na dalili zilionyesha wazi kuwa watu wa Kitab walikuwa ni wasaidizi na mawakala wa wakristo wa Roma; na kwamba wao walikuwa wakila njama nao dhidi ya Mtume na wafuasi wake waumini.

Kwa ajili hiyo ndipo ikawa hukumu ni kupigana nao au waweke silaha chini na wawe chini ya hukumu ya Kiislamu, pamoja na kutoa kodi ambayo itaonyesha usalama wao na kutekeleza kwao ahadi yao. Wakitoa kodi basi ni wajibu kuwapa amani kuwahami na kuwapa uhuru katika dini yao. Wakisilimu watapata waliyonayo waislamu, Vinginevyo basi ni kuwaua kujikinga na shari yao.

Wafasiri na mafakihi wamerefusha maneno kuhusu kodi, kiasi chake na sharti zake. Maneno yao wakati huo yalikuwa na faida ambapo uislamu ulikuwa na dola yake na nguvu zake. Ama leo mazungumzo kuhusu kodi ni kuongeza maneno tu.

Na mayahudi wanasema: Uzair ni mwana wa Mwenyezi Mungu; na wanaswara wanasema, Masihi ni mwana wa Mwenyezi Mungu.

Kauli ya Wakristo kuwa Masih ni mwana wa Mwenyezi Mungu ni maarufu na tumeizungumzia katika Juz.6 (5:18)

Ama kauli ya Mayahudi kuhusu Uzair, mwenye Tafsir Al-Manar amenukuu kuwa jina la Uzair liko katika vitabu vitakatifu vya mayahudi,Vile vile amenukuu kutoka Daira tul-Maarifil-Yahudiyya kwamba zama za Uzair ndizo zama nzuri za Historia ya mayahudi. Katika Tafsir ya Tabari, Razi na Tabrasi imeelezwa kwamba kikundi cha Mayahudi walimwambia Mtume(s.a.w.w) : Tutakufuata vipi nawe umeacha Qibla chetu na wala hudai kuwa Uzair ni mwana wa Mwenyezi Mungu, ndipo ikashuka Aya.

Kwa vyovyote ilivyo ni kwamba Mtume aliwakabili Mayahudi wa zama zake kwa Aya hii, na haikunukuliwa kutoka kwa yeyote katika wao kumkosoa au kumpinga pamoja na kumkadhibisha kwao sana Mtume, Kwa hiyo inafahamisha kuwa wao waliamini hivyo wakati huo.

Hiyo ndiyo kauli yao kwa vinywa vyao, wanayaiga maneno ya wale waliokufuru zamani. Mwenyezi Mungu awangamize! Wanageuzwa wapi?.

Yaani kauli ya mayahudi inafanana na kauli ya washirikina waarabu ambao walisema: Malaika ni mabinti wa Mwenyezi Mungu, vile vile kauli ya waabudu mizimu wa zamani, waroma, wayunani, wabudha na wengineo.

Wamefanya makuhani wao na watawa wao kuwa ni miungu badala ya Mwenyezi Mungu na Masih mwana wa Maryam.

Hii ni dalili nyingine kwamba wao hawamwamini Mwenyezi Mungu bali wanaamini wanayoyasema watu wa dini yao na itikadi yao. Imam Jaffer As-sadiq(a.s) anasema:“Wao hawakuwafungia swaum au kuwaswalia, lakini waliwhalalishia haramu na wakawaharamishia halali, wakawafuata na kuwaabudu bila ya kutambua.”

Haya ni sawa na yaliyo katika Hadith kwamba Udey bin Hatim alimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) : Sisi hatuwaabudu wao.

Mtume akamwambia: Je, hawaharimishi aliyohalalisha Mwenyezi Mungu mkayaharamisha; na kuhalalisha aliyoharamisha Mwenyezi Mungu mkayahalalisha? Udey akasema: Ndio, Mtume akasema: huko ndiko kuwaabudu.

Voltare anasema: Makasisi wetu hawajui chochote isipokuwa sisi ni wepe-si wa kusadiki wayasemayo.

Wala hawakuamrishwa isipokuwa wamwambudu Mungu mmoja hakuna Mungu ila yeye Ametakata na wanayomshirikisha nayo.

Razi katika Tafsir yake anasema: Maana yako dhahiri. Lakini mfasiri mwingine ambaye alitaka asema tu: “Yaani wamwabudu Mola Mkuu”.

Wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao.

Makusuido ya nuru ya Mwenyezi Mungu hapa ni Uislamu. Maana ni kuwa watu wa Kitab walijaribu kuumaliza Uislamu kwa kila njama na uwongo; ikawa ni kama mtu anayejaribu kuzima nuru, ambayo imeenea ulimwenguni, kwa pumzi yake.

Na Mwenyezi Mungu amekataaa isipokuwa kuitimiza nuru yake, ijapokuwa makafiri wanachukia.

Hii ni ahadi ya Mwenyezi Mungu, kupitia mdomoni mwa Mtume wake, kuunusuru Uislamu na kuudhihirisha mashariki ya ardhi na magharibi. Amesema kweli Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na ahadi ambayo inafahamisha utume wa Mohammad(s.a.w.w) ikathibiti na ukweli wake katika kila alilolitolea habari.

Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokwa washirikina wanachukia.

Aya hii ni ubainifu na ufafanuzi wa Aya iliyo kabla yake. Mwenyezi Mungu aliwajalia waislamu kuwashinda washirikina katika miji ya Kiarabu, Mayahudi walipowatoa huko, wakristo katika Sham na Majusi katika Fursi. Imam Ali anasema: “Hakika huu Uislamu umedhalilisha dini (nyingine) kwa utukufu wake, ukaziondoa mila kwa utukufu wake na ukawatweza maadui zake kwa utukufu wake.”

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّ كَثِيرًا مِّنَ الْأَحْبَارِ وَالرُّهْبَانِ لَيَأْكُلُونَ أَمْوَالَ النَّاسِ بِالْبَاطِلِ وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَالَّذِينَ يَكْنِزُونَ الذَّهَبَ وَالْفِضَّةَ وَلَا يُنفِقُونَهَا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ فَبَشِّرْهُم بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٣٤﴾

34. Enyi mlioamini! Hakika wengi katika watawa na makuhani wanakula mali za watu kwa batili na kuwazuilia njia ya Mwenyezi Mungu. Na wale walimbikizao dhahabu na fedha na hawazitumii katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi wabashirie adhabu iumizayo.

يَوْمَ يُحْمَىٰ عَلَيْهَا فِي نَارِ جَهَنَّمَ فَتُكْوَىٰ بِهَا جِبَاهُهُمْ وَجُنُوبُهُمْ وَظُهُورُهُمْ هَـٰذَا مَا كَنَزْتُمْ لِأَنفُسِكُمْ فَذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَكْنِزُونَ ﴿٣٥﴾

35. Siku zitakapotiwa moto kati- ka moto wa Jahannam, na kwazo vitachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao; Haya ndiyo mliyojilimbikizia, basi onjeni yale mliyokuwa mkiyalimbikiza.

WALE WANAOKUSANYA DHAHABU NA FEDHA

Aya 34 – 35

MAANA

Enyi mlioamini! Hakika wengi katika watawa na makuhani wanakula mali za watu kwa batili na kuwazuilia njia ya Mwenyezi Mungu.

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewataja mayahudi na wakristo kwamba wao wanawafanya viongozi wao wa kidini ni waungu badala ya Mwenyezi Mungu. Katika Aya hii amewataja hao viongozi kwa kula mali ya batili na kuzuia watu na njia ya Mwenyezi Mungu.

Makusudio ya kula mali kwa batili ni kuchukua bila ya njia ya sharia; kama vile rushwa na riba ambayo ilienea sana kwa mayahudi. Pia uuzaji wa cheki ya msamaha kwa wakatoliki nk. Wanahistoria wanasema watu wa kanisa waliwahi kuwa ndio matajiri zaidi.

Makusudio ya kuzuia watu na njia ya Mwenyezi Mungu ni kuwazuilia akili zao na kuzuia watu kukubali Uislam, bali na kuwafanya wautuhumu na Mtume wake.

Voltaire alilichagiza kanisa na kuwalaumu wakubwa wake kwa ulafi wao wa mali; akaituhumu Tawrat kutokana na mgongano. Akazuiliwa na kanisa na baadhi ya kubwa wake wakataka afungwe maisha. Akaogopa sana mwanafalsafa huyu wa kifaransa[7] . Hakupata njia yoyote ya kuokoka isipokuwa kutetewa na baba mtakatifu Bendedict xiv kwa kutunga Kitab cha kumtukana Muhammad. Akafanya hivyo na akasamehewa na kanisa; kikabarikiwa kitabu na mwandishi wake.

ABU DHAR NA UJAMAA

Na wale walimbikizao dhahabu na fedha na hawazitumii katika njia ya Mwenyezi Mungu, basi wabashirie adhabu iumizayo.

Kuna maneno mengi kuhusu Aya hii, Baadhi wakaitolea dalili juu ya kuweko ujamaa (usoshalist) katika Uislamu, Wengine wamediriki hata kusema kuwa Abu dharr alikuwa mjamaa kwa vile yeye alikuwa akiwatisha, kwa Aya hii, wale walioathirika na mali ya Mwenyezi Mungu kuliko watu wa Mwenyezi Mungu.

Tutaonyesha maana ya Aya na kila linalofugamana nayo kwa karibu au mbali, na kwayo tutaihukumu kauli ya anayeutolea dalili ujamaa wa Abu dhar kwa Aya hii:

1. Muawiya bin Abu Sufyan alisema kuwa Aya hii ilishuka kwa watu wa Kitab tu na wala haiwahusu Waislamu. Yaani, kwa mtazamo wake, Waislamu wanaweza kurundika mali wanavyotaka na wala wasitoe chochote katika njia ya Mwenyezi Mungu. Alinukuu kauli hii kutoka kwa Uthman bin Affan.

Kwenye Durrul Manthur ya Suyuti imeelezwa kuwa Uthman alipoandika msahafu walitaka kuondoa herufi wau (na) katika kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na wale walimbikizao dhahabu na fedha…” ili iwe ‘Walimbikizao ni sifa ya makasisi na watawa. Sahaba mmoja akapinga na kusema: Mtaiweka wau au ni uweke upanga wangu begani kwangu, ndipo wakaiweka.

Ilivyo hasa ni kuwa Aya inamhusu kila mwenye kukusanya mali na asitoe katika njia ya Mwenyezi Mungu, awe Mwislamu au si Mwislamu, kwa kuchukulia kuwa tamko ni la kuenea.

Imepokewa kutoka kwa Zaid bin Wahab kwamba alipita Rabdha, akamuona Abu dharr huko, akamuuliza: Kitu gani kilichokufikisha hapa? Akasema: Nilikuwa Sham nikasoma: ‘Na wale walimbikizao dhababu ….’ Muawiya akasema Aya hiyo haituhusu sisi ni ya watu wa Kitab. Nikasema: Hakika hiyo inatuhusu sisi na wao. Basi akanishtaki kwa Uthman ndipo wakanifukuza hadi hapa unaponiona.

2. Neno dhahabu na fedha ni Mahsus, lakini hukumu ni ya ujumla kwa aina zote za mali, hata ardhi madini miti majengo mifugo, magari na viwanda. Kwa sababu waliotishiwa adhabu iumizyao na Mwenyezi Mungu ni matajiri bahili na wala sio wanaomiliki dhahabu na fedha tu. Vingenevyo ingekuwa matajiri wa mafuta na wengineo ndio watu wema na watukufu zaidi kwa Mwenyezi Mungu duniani na akhera.

Linalotufahamisha kuwa, makusudio ni ya ujumla ni kuwa Aya hii iliposhuka iliwashughulisha waislamu kwa sababu wao walifahamu mali zote. Walipomuuliza Mtume(s.a.w.w) aliwathibitshia walivyo fahamu na kuwambia: “Hakika Mola hakufaradhisha zaka ila kwa kuifanya njema iliyobakia katika mali zenu; na hakika amefaradhishia warithi mali zinazobakia baada yenu.”

3. Kutumia katika njia ya Mwenyezi Mungu ni pamoja na jihadi ya kupigania dini na nchi, kujenga madrasa, mahospitali na nyumba za mayaitma. Vile vile kuwapa sadaka mafukara kumtunza mke na watoto. Sehemu nzuri ya kutumia ni ile inayoienzi na haki na watu wake.

4. Madhehebu mane yamekongamana kuwa katika mali hakuna haki yoyote isiyokuwa zaka; kama ilivyoelezwa katika Ahkamul Qur’an cha Abu Bakr Al-Muafirir Al-andalusi.

Mafakihi wengi wa Kishia wamesema katika mali hakuna haki zaidi ya khumsi na zaka. Sheikh Tusi anasema “Iko haki nyingine nayo ni ile aliyoiaishiria Imam Saffer As-Sadiq kwa kauli yake: “Hakika Mwenyezi Mungu amefaradhisha katika mali za matajiri haki nyingine zisizokuwa zaka.

Kwa sababu yeye amesema:

وَفِي أَمْوَالِهِمْ حَقٌّ لِّلسَّائِلِ وَالْمَحْرُومِ ﴿١٩﴾

“Na ambao katika mali zao iko haki maalum kwa ajili ya aombaye au ajizuiaye” (51:19)

Haki maalum ni kitu chochote anachojilazimisha mtu kwa kadiri ya uwezo wake, atatoa kila siku akipenda, kila Ijuma au kila mwezi; kiwe kichache au kingi, mradi tu kiwe ni cha kudumu. Lakini kauli ya Imam, atajifaradhishia yeye mwenyewe, inatambulisha suna sio wajibu, kwa sababu wajibu unatokana na Mwenyezi Mungu si mwenginewe.

Tuonavyo sisi, baada ya kufuatilia Aya za Qur’an Tukufu, ni kwamba matajiri wanao wajibu, sio suna, kujitolea mali zao zaidi ya zaka na khums; kwa ajili ya kuipigania dini na nchi ihitajika; na ni juu ya mkuu wa waislamu kuwalazimisha hilo. Bali pia ni wajibu wajitolee kwa nafsi ikihitajika, Aya za namna hii ziko chungu nzima.

5.Siku zitakapotiwa moto katika moto wa Jahannam, na kwazo vitachomwa vipaji vya nyuso zao na mbavu zao na migongo yao; Haya ndiyo mliyojilimbikizia, basi onjeni yale mliyokuwa mkiyalimbikiza.

Hili ni fumbo la adhabu kali na vituko vyake. Aya hiyo ni mfano wa Aya isemayo: “Watatiwa mandakozi ya hivyo walivyofanyia ubakhili siku ya kiyama” Juz.4 (3: 180).

6. Kutokana na yaliyotangulia imetubainikia kuwa Aya inafahamisha kwa kinukuu na kimaana kwamba ni wajibu juu yao matajiri kutoa sehemu ya mali zao katika njia ya Mwenyezi Mungu, na kama wataifanyia uchoyo, basi Mwenyezi Mungu atawadhibu kwa adhabu kali. Ama kiwango cha fungu hili, na kwamba je, ni khumsi au ushuri, zaidi au chini na kwamba je, ni zaka au zaidi, Aya haifahamishi kwa Ibara wala kwa ishara.

Sasa basi ni wapi panapofahamisha ujamaa. Ujamaa ni siasa ya kiuchumi ambayo, kabla ya chochote, huangalia nyenzo za uzalishaji, kama ardhi nk, na kuweko viwango vya kumiliki; kisha huangalia uzalishaji wenyewe na njia za kukua kwake na mgawanyo wake. Hili ni jambo jingine na kuhimiza matajiri kutoa ni jambo jingine.

Kwa hiyo inatubainikia kuwa kauli ya mwenye kusema kuwa Abu Dhar alikuwa mjamaa kwa vile aliwakaripia matajiri kwa Aya hii, kuwa ni makosa na kuchanganyikiwa. Abu Dhar hana habari na ujamaa wala kitu chochote isipokuwa Uislamu. Mfano wake katika hilo ni mfano wa Mwislamu yeyote. Lakini yeye alikuwa mwenye Ikhlasi na dini yake, aliufanyia ikhlasi Uislamu na kutupilia mbali tamaa na malengo mengine.

Ikhlasi yake hii ndiyo iliyomfanya awapinge Maquraish na kuwatusi waungu wao siku aliposilimu, pale aliposimama kwenye Al-Kaaba akinadi kwa sauti kubwa: Hapana Mola mwingine ispokuwa Mwenyezi Mungu. Akikinadi tamko la Uislamu juu ya vichwa vya Maquraish siku waislamu walipokuwa hawana nguvu wala uwezo na hakuna aliye kuwa akithubutu kutamka jina la Mwenyezi Mungu na Mohammad isipokuwa kwa kujificha.

Aliendelea kuwa na msimamo huu hata mbele ya Uthman na Muawiya. Kama ambavyo alipata mapigo ya kuumiza kutoka kwa washirikina, pia kwa Uthman alipata pigo la kufukuzwa na kuwekwa mbali na watu, lakini halikumkasirisha kwa sababu yeye hakukasirikia katika maisha yake yote isipokuwa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu peke yake.

Kwa ufupi alilofanya Abu Dhar ni kuwataka viongozi watawale kwa uadilifu na kuchunga haki pia aliwahofisha na adhabu kali na kuwahimiza wanaodhulumiwa kuwapinga madhalimu na kurudisha haki zao kutoka kwa madhalimu hao.

Sasa wapi na wapi hayo na Ujamaa? Tumezungumzia kuhusu kunasibish- wa ujamaa kwa Abudhar katika Kitab Maashiah Al-Imamia kwenye kifungu ‘Je Abudhar ni mjamaa?’ Na katika Kitabu Ma’ulamainnajaf Al-Ashraf kwenye kifungu ‘Abudharr’.


7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

إِنَّ عِدَّةَ الشُّهُورِ عِندَ اللَّـهِ اثْنَا عَشَرَ شَهْرًا فِي كِتَابِ اللَّـهِ يَوْمَ خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ مِنْهَا أَرْبَعَةٌ حُرُمٌ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ فَلَا تَظْلِمُوا فِيهِنَّ أَنفُسَكُمْ وَقَاتِلُوا الْمُشْرِكِينَ كَافَّةً كَمَا يُقَاتِلُونَكُمْ كَافَّةً وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُتَّقِينَ ﴿٣٦﴾

36. Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu (tangu) siku alipoumba mbingu na ardhi. Katika hiyo iko mine mitakatifu, Hiyo ndiyo dini iliyo sawa, Basi msidhulumu nafsi zenu humo. Na piganeni na washirikina nyote, kama wanavyopigana nanyi wote, na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye takua.

إِنَّمَا النَّسِيءُ زِيَادَةٌ فِي الْكُفْرِ يُضَلُّ بِهِ الَّذِينَ كَفَرُوا يُحِلُّونَهُ عَامًا وَيُحَرِّمُونَهُ عَامًا لِّيُوَاطِئُوا عِدَّةَ مَا حَرَّمَ اللَّـهُ فَيُحِلُّوا مَا حَرَّمَ اللَّـهُ زُيِّنَ لَهُمْ سُوءُ أَعْمَالِهِمْ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ ﴿٣٧﴾

37. Hakika kuahirisha ni kuzidi katika kufru, kwa hayo hupotezwa wale walio kufuru. Wanauhalalisha mwaka mmoja na kuuharamisha mwaka Ili wafanye sawa idadi ya ile aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu, hivyo huhalalisha aliyoharamisha Mwenyezi Mungu. Wamepambiwa ubaya wa vitendo vyao, Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri.

IDADI YA MIEZI

Aya 36 – 37

MIEZI MIANDAMO NDIYO MIEZI YA KIMAUMBILE

MAANA

Hakika idadi ya miezi kwa Mwenyezi Mungu ni miezi kumi na mbili katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu (tangu) siku alipoumba mbingu na ardhi.

Makusudio ya kwa Mwenyezi Mungu na katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu ni kwamba miezi kumi na mbili iko kihakika katika ulimwengu wa kimaumbile, sawa na mbingu na ardhi si katika ulimwengu wa mazingatio na sharia, kama vile halali na haramu.

Makusudio ya siku alipoumba mbingu na ardhi ni kwamba yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu aliumba ulimwengu kwenye hali ambayo idadi ya miezi ni kumi na mbili, tangu siku ya kwanza ya kupatikana mbingu na ardhi; yaani idadi ya miezi hii, sio kwamba imewekwa na binadamu na ugunduzi wake; isipokuwa ni desturi na nidhamu ya maumbile.

Haya ndiyo maana ya Aya, Kimsingi ni kwamba binadamu hupima wakati na kuupanga kwa anavyoona na kuhisi. Tukiangalia maumbile ambayo yatatuongoza katika kujua wakati, hatupati zaidi ya jua na mwezi. Jua kila siku linakwenda kwa mfumo mmoja kutoka mashariki na kutua magharibi, bila ya kuweko tofauti.

Kupitia hilo jua twajua wakati wa asubuhi mchana na jioni, na wala halihusiki na kujua mwezi si kwa karibu wala mbali. Lakini mwezi ni kinyume na hivyo. nHuwa unajitokeza kwa picha maalum kuanzia siku ya kwanza, ya kila mwezi, ambao ndiyo siku ya kwanza ya mwezi, Tunapojua mwezi ndio tunajua mwaka.

Na kwa ajili hii ndipo ikawa miezi miandamano, ndiyo miezi inayo kwenda na maumbile, kinyume cha miezi mingine, na kwa ajili hii ndio Mwenyezi Mungu ameiwekea wakati wa Hijja, Swaumu eda ya watalikiwa na kunyonyesha, kama ambavyo wakati wa swala amuweka kwa jua, kwa vile ndio njia ya kujua mafungu ya siku. Kwa maneno mengine, jua ni la kujua saa na mwezi mwandomo ni wa kujua miezi. Binadamu alikuwa akihisabu muda wake kwa misingi hii.

Anasema Razi: “Desturi ya Waarabu tangu zamani ni kuwa na mwaka wa mwezi na sio wa jua Hukumu hii walirithi kutoka kwa Ibrahim na Ismail”

Katika baadhi ya tafsir imeelezwa kuwa hekima ya kujaaliwa Hijja na Swaumu katika miezi miandamo ni kuwa izunguke katika vipindi vyote vya mwaka; mara inakuwa nzito na mara nyingine inakuwa sahali[8] , Lakini jitihadi hii haitegemei asili yoyote, hata hivyo haina kizuizi kwani haikukusudiwa kuthibitisha hukumu ya sharia, isipokuwa kubainisha masilahi ya hukumu yenye kuthibiti kisharia.

Katika hiyo iko mine mitakatifu.

Mitatu katika miezi mine hii, inafuatana: Dhul-qaada, Dhul-hajj na Muharram[9] , Na mwezi mmoja, Rajab, uko peke. Imeitwa mitakatifu kwa kukatazwa kupigana katika miezi hiyo wakati wa jahiliya na wa Uislamu, Hayo tumeyaeleza zaidi ya mara moja.

Hiyo ndiyo dini iliyo sawa.

Yaani kugawa miezi kwa idadi ya kumi na mbili kwa hisabu ya mwezi mwandamo ndio magawanyo sahihi wala haijuzu kufanya upotofu kwa hawa na matakwa mengine katika miezi hiyo wala katika miezi mitakatifu.

Basi msidhulumu nafsi zenu humo.

Kwa kuhalalisha kupigana katika miezi mitakatifu, au kufanyiana uadui katika wakati wowote, Kila anayemwasi Mwenyezi Mungu katika dhambi kubwa na ndogo, basi ameidhulumu nafsi yake kwa kujiingiza kwenye adhabu ya Mwenyezi Mungu na ghadhabu yake.

Na piganeni na washirikina nyote, kama wanavyopigana nanyi wote.

Hii ndiyo dawa; watu wote jihadi, ni desturi ya Mwenyezi Mungu na huwezi kupata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu. Ama vikao vya kutatua ugomvi ni kumyenyekea adui na kusalimu amri kwake. Wazayuni wote na wakoloni wamejitokeza kuwapiga waarabu na waislamu wote; wakaweka kambi ya kiadui katika ardhi ya waarabu, na kuipa jina ‘Taifa la Israil’, ili wapitishie mashambulizi yao kutokea hapo!

Hivi tuko katika mwezi Novemba 1968, katika umoja wa mataifa, inaendelea mipango ya kutafuta suluhisho la kudumu kutatua tatizo la mashariki ya kati kwa njia ya mazungumzo ambapo adui anatoa masharti, kila anapopata fursa, ambayo yanamzidisha mori wa uadui na kupata yote ayatakayo, kisha arudie tena mazungumzo. Mambo yatakuwa hivyo hivyo mpaka atawale sehemu zote.

Dawa pekee ya kuondoa mzizi wa fitina ni ile aliyoipanga Mwenyezi Mungu kwa kauli yake:

Na piganeni na washirikina nyote, kama wanavyopigana nanyi wote, na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yu pamoja na wenye takua.

Ambao wamejikomboa na chuki na tamaa na kuungana pamoja wote kwa ajili ya kupigana na adui wao na adui wa Mwenyezi Mungu na wa utu.

Hakika kuahirisha ni kuzidi katika kufru, kwa hayo hupotezwa wale walio kufuru. Wanauhalalisha mwaka mmoja na kuuharamisha mwaka mwingine.

Washirikina walikuwa wakiahirisha utukufu wa mwezi, kama vile Muharram, mpaka mwezi mwingine, kama vile Safar.

Ikiwa ni masilahi yao kupigana katika mwezi mtukufu basi hupigana bila ya kujali, lakini wanautukuza mwezi mwingine badala yake, katika miezi ya halali, ili ipatikane miezi mitukufu minne ya mwaka.

Ili wafanye sawa idadi ya ile aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu, hivyo huhalalisha aliyoharamisha Mwenyezi Mungu.

Tafsiri wazi zaidi kuhusu hii ni yale yaliyonukuliwa kutoka kwa Ibn Abbas aliposema: “Hakika wao hawakuhalalisha mwezi katika miezi mitakatifu ila huharamisha mahali pake mwezi wa halali. Na hawakuharamisha mwezi katika miezi ya halalali ila huhalalisha mahali pake mwezi mtakatifu. Wanafanya hivyo ili idadi ya miezi mitukufu iwe minne kwa kufuata aliyoyataja Mwenyezi Mungu” Haya ndiyo makusudio ya kufanya sawa.

Wamepambiwa ubaya wa vitendo vyao.

Matamanio na malengo mengine ndiyo yanayompofusha mtu na ubaya wa amali yake. Anaiona shari kuwa ni heri na uzuri kuwa mbaya.

Na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu makafiri.

Yaani anawaacha kama walivyo baada ya kukata tamaa na kuongoka kwako. Angalia Juz. 5 (4:88).

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا مَا لَكُمْ إِذَا قِيلَ لَكُمُ انفِرُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ اثَّاقَلْتُمْ إِلَى الْأَرْضِ أَرَضِيتُم بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا مِنَ الْآخِرَةِ فَمَا مَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا فِي الْآخِرَةِ إِلَّا قَلِيلٌ ﴿٣٨﴾

38. Enyi mlioamnini! Mna nini mnapoambiwa nendeni katika njia ya Mwenyezi Mungu mnajitia uzito katika ardhi?. Je, mmeridhia maisha ya dunia kuliko ya Akhera?. Lakini starehe za maisha ya dunia kulinganisha na Akhera ni kidogo tu.

إِلَّا تَنفِرُوا يُعَذِّبْكُمْ عَذَابًا أَلِيمًا وَيَسْتَبْدِلْ قَوْمًا غَيْرَكُمْ وَلَا تَضُرُّوهُ شَيْئًا وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٣٩﴾

39. Kama hamwendi atawaadhibu kwa adhabu iumizayo na atawaleta watu wengine badala yenu, wala hamtamdhuru chochote Na Mwenyezi Mungu ni muweza wa kila kitu.

إِلَّا تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللَّـهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لَا تَحْزَنْ إِنَّ اللَّـهَ مَعَنَا فَأَنزَلَ اللَّـهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ لَّمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُوا السُّفْلَىٰ وَكَلِمَةُ اللَّـهِ هِيَ الْعُلْيَا وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٤٠﴾

40. Kama hamtamsaidia, basi Mwenyezi Mungu alimsaidia walipomtoa wale waliokufuru Alipokuwa wa pili katika wawili alipomwambia sahibu yake: Usihuzunike hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja nasi. Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamsaidia kwa majeshi msiyoyaona. Na akalifanya neno la wale waliokufuru kuwa chini, na neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.

MNANINI MNAPOAMBIWA

Aya 38 – 40

VITA VYA TABUK

Aya hizi ziko karibu na mwisho wa sura iliyoshuka katika vita vya Tabuk. Kwa ufupi ni kuwa Roma ilikuwa ikimiliki Sham iliyopakana na Bara Arabu. Walisikia nguvu ya Uislamu na kukua kwake. Hercules, mfalme wa Roma, aliwahofia waislamu akasema: “Nikiwaacha mpaka wanikabili basi dola yangu haitakuweko mashariki” Akaazimia kuanza vita.

Mtume(s.a.w.w) naye kwa upande wake akaona asingoje mpaka ajiwe na Hercules na jeshi lake Madina. Akawataka watu watoke wakapigane na Waroma. Wakati huo joto lilikuwa kali sana.

Wanafiki wakapata fursa na kuwahofisha waislamu kwa umbali wa safari, joto kali na wingi wa adui. Wakaitikia mwito wao wale wadhaifu wa imani; wakatoa udhuru na kutafuta sababu, lakini Mtume akatangaza jihadi na kwamba watu wote. Hakutoa ruhusa kwa yoyote isipokuwa mgonjwa na asiye na cha kutoa Pamoja na njama za wanafiki, lakini walijotokeza wapiganaji kiasi elfu thelathini.

Kabla ya Mtume(s.a.w.w) kutoka na jeshi lake alimweka Ali bin Abu Talib kuwa kaimu wake kwa watu wake na familia yake. Muslim katika sahih yake, Sahih Muslim J2 uk 108 chapa ya mwaka 1348 A.H, anasema: “Ali akamwambia mtume: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu unaniacha nyuma na wanawake na watoto? Mtume(s.a.w.w) akasema: Je, huridhiii kuwa wewe kwangu mimi ni daraja ya Harun na Musa; isipokuwa hakuna Mtume baada yangu?”

Jeshi la Waislamu likaosonga; wote wakawa wako jangwani kwenye mvuke unachoma nyuso na mili. Njiani walimkuta sahaba mtukufu Abu Dhar akitembea kwa miguu kwa vile hakuwa na cha kupanda; wakati ambapo kiongozi wa wanafiki Abdallah bin Ubayya alijitoa na sehemu ya jeshi wakarudi Madina. Wanawake wakawapokea kwa kuwazoma na kuwarushia michanga nyusoni.

Baada ya mwendo wa siku saba, jeshi la waislamu likafika mpakani mwa dola ya Roma. Mkuu wa mji akataka suluhu na Mtume(s.a.w.w) kuwa atoe jiziya, Mtume akakubali. Akaendelea mbele na jeshi lake mpaka akafika katika mji wa Tabuk ulioko kati kati ya njia baina ya Damascus na Madina. Wakati huo ilikuwa ni mwezi wa Rajab mwaka wa 9 A.H.

Ikatokea kuwa kiongozi wa Tabuk ametoka nje kwenda kuwinda. Waislamu wakamteka na kuuchukua mji. Mtume akawa anatoka mahali fulani hadi mahali pengine mpaka akawashinda nguvu walinzi wa mpakani, akakomboa makabila ya kiarabu kutoka katika serikali ya Roma, Haya yote yalifanyika ndani ya siku ishirini.

Waislamu wakarudi Madina wakiwa na ngawira; na Mtume(s.a.w.w) akatoa agizo la kuwasusia waliorudi nyuma, akazuia wasizungumze na kuamiliana na watu hata wake na watoto. Ufafanuzi zaidi utakuja katika Aya zitakazofuatia; hasa Aya 117 na 118 katika sura hii.

MAANA

Enyi mlioamnini! Mna nini mnapoambiwa nendeni katika njia ya Mwenyezi Mungu mnajitia uzito katika ardhi.?

Mtume(s.a.w.w) alipowataka waislamu watoke kwa ajili ya vita vya Tabuk, liliwatia uzito hilo baadhi yao wakaathirika kubaki ardhini mwao na majumbani mwao.

Ilikuwa ni desturi ya Mtume(s.a.w.w) , anapotoka kwa ajil ya vita, kuwapa dhana watu kuwa anatokea jambo jingine kwa masilahi ya siri katika vita, lakini katika vita hivi alisema wazi wazi, ili watu wajue taabu zinazowangojea.

Baadhi ya wafasiri wamewatolea udhuru wale waliojitia uzito kutoka, kwamba wakati ulikuwa wa joto kali, watu wanadhiki ya chakula na mazao yamekwisha komaa tayari kwa kuvunwa.

Vyovyote iwavyo maneno kwa hali ilivyo – yanaelekezwa kwa waliojitia uzito na jihadi. Na Mwenyezi Mungu akawalaumu kwa kuwaambia:

Je, mmeridhia maisha ya dunia kuliko ya Akhera.? Lakini starehe za maisha ya dunia kulinganisha na Akhera ni kidogo tu.

Je, ni sawa imani yenu na akili zenu kuathirika na neema ya dunia inayokiwisha kuliko neema ya Akhera iliyo adhimu na yenye kudumu?

Kama hamwendi atawaadhibu kwa adhabu iumizayo na atawaleta watu wengine badala yenu, wala hamtamdhuru chochote.

Yaani kama hamtaitikia mwito wa Mtume wa kutoka naye kupigana na Waroma, basi Mwenyezi Mungu atawateremshia adhabu iumizayo, enyi wanafiki mnaojitia uzito; na atamsaidia Mtume wake kwa mikono ya wengine, wala kurudi nyuma kwenu hakuwezi kumdhuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Na Mwenyezi Mungu ni muweza wa kila kitu.

Hashindwi kuwaadhibu wala kuinusuru dini yake na Mtume wake kwa watu bora zaidi yenu.

Kama hamtamsaidia, basi Mwenyezi Mungu alimsaidia walipomtoa wale waliokufuru;

Inadokeza tukio la vitimbi na njama walizopanga makafiri wa Kiquraish, kumua Mtume(s.a.w.w) akiwa amelala kitandani kwake, jinsi alivyomwokoa nao kwa kulala Ali mahali pake na alivyo hama kutoka Makka kwenda Madina baada ya Mwenyezi Mungu kumfichulia njama zao, Hayo tumeyaeleza katika kufasiri (8:30).

Alipokuwa wa pili katika wawili alipomwambia sahibu yake: Usihuzunike hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja nasi.

Makusudio ya wa pili katika wawili na sahibu ni Abu Bakr, kwa vile yeye alikuwa pamoja na Mtume katika kuhama kwake na walijificha pamoja katika pango Thawr. Razi anasema: “Washirikina walipofuata nyayo na kukurubia pango, Abu Bakr alilia akimhofia Mtume(s.a.w.w) , Mtume(s.a.w.w) akamwambia usihuzunike, hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja nasi. Abu Bakr akasema: Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja nasi, Mtume(s.a.w.w) akasema ndio.

Mwenyezi Mungu akamteremshia utulivu wake, na akamsaidia kwa majeshi msiyoyaona.

Amesema Abu Hayan Al-Andalusi katika tafsir yake: “Amesema Ibnu Abbas: Utulivu ni rehma, na dhamir katika akateremshia inamrudia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , kwa vile yeye ndiye anayezungumziwa.”

Hayo yanafikiana na kauli ya Sheikh wa Al az-har, Al Maraghi, aliposema katika tafsir yake, ninamnakuu: “Yaani akateremsha utulivu wake, unao tuliza moyo, kwa Mtume wake(s.a.w.w) , akampa nguvu kwa majeshi kutoka kwake ambao ni Malaika.” Vile vile yanaafikiana na mfumo wa Aya Kwa sababu dhamir katika kumsaidia na kumtoa inamrudia Mtume(s.a.w.w) .

Na akalifanya neno la wale waliokufuru kuwa chini, na neno la Mwenyezi Mungu ndilo la juu. Neno la Mwenyezi Mungu ni Tawhid na neno la waliokufuru ni shirk na ukafiri.

Na Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.

Hekima yake ilipitisha kumnusuru Mtume wake(s.a.w.w) kwa nguvu yake na kuidhihirisha dini yake juu ya dini zote.

انفِرُوا خِفَافًا وَثِقَالًا وَجَاهِدُوا بِأَمْوَالِكُمْ وَأَنفُسِكُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٤١﴾

41. Nendeni mkiwa wepesi na wazito, na mpiganie jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu. Hilo ni kheri kwenu mkiwa mnamjua.

لَوْ كَانَ عَرَضًا قَرِيبًا وَسَفَرًا قَاصِدًا لَّاتَّبَعُوكَ وَلَـٰكِن بَعُدَتْ عَلَيْهِمُ الشُّقَّةُ وَسَيَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ لَوِ اسْتَطَعْنَا لَخَرَجْنَا مَعَكُمْ يُهْلِكُونَ أَنفُسَهُمْ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ إِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ ﴿٤٢﴾

42. Lau ingekuwa ni faida iliyo karibu na safari nyepesi wangelikufuata. Lakini imekuwa ndefu kwao yenye mashaka, Na wataapa kwa Mwenyezi Mungu lau tungeliweza bila shaka tungelitoka pamoja nanyi. Wanaziangamiza nafsi zao, Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa hakika hao ni waongo.

عَفَا اللَّـهُ عَنكَ لِمَ أَذِنتَ لَهُمْ حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكَ الَّذِينَ صَدَقُوا وَتَعْلَمَ الْكَاذِبِينَ ﴿٤٣﴾

43. Mwenyezi Mungu amekusamehe! Kwa nini umewapa ruhusa kabla ya kubainika kwako wanaosema kweli na ukawajua waongo.

NENDENI MKIWA WAZITO NA MKIWA WEPESI

Aya 41-43

KWENDA WOTE

MAANA

Nendeni mkiwa wepesi na wazito, na mpiganie jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu.

Makusudio ya wepesi nikwenda kupigana jihadi kwa wepesi, na uzito ni kupigana kwa mashaka. Aya inafahamisha wajibu wa kutoka wote. Ufuatao ni ubainifu:

Adui akijaribu kuichokoza dini ya Kiislam kwa kukipotoa kitabu cha Mwenyezi Mungu na yaliyothibiti katika sunna ya Mtume wake, au kuwazuiya waislamu kutekeleza wajibu wao na nembo za kidini; akijaribu kutawala mji katika miji yao, basi hapo itakuwa ni wajibu kwa waislam kumpiga jihadi adui huyu na kuzuia upotevu wake.

Ikiwa baadhi wanaweza kumzuia, basi wajibu utakuwa ni kutosheana (kifaya) kwa maana kuwa wakitekeleza baadhi, basi jukumu litawaondokea wote, na wakipuza wote, basi jukumu ni lao wote na watastahiki adhabu wote.

Na kama haiwezekani ila kwa watu wote, basi itakuwa ni lazima kwa vijana, wazee, wanawake, vilema, vipofu na hata wagonjwa, kadiri mtu atakavyoweza.

Mwenye Jawahir anasema!” Adui akishambulia waislamu na kuhofiwa kuutia doa Uislamu au kafiri akitaka kutawala miji ya waislamu na kuwateka na kuchukua mali zao, basi ni wajibu kupigana kwa mungwana, mtumwa, mwana mume, mwanamke, mzima, mgonjwa, kipofu, mlemavu na wengineo; iwapo kuna haja ya kufanya hivyo.

Wala lilo halitahitajia kuweko Imam wala idhini yake; na wala halitahusika na wale waliochokozwa tu, bali ni wajibu kwa kila atakayelijua hilo, hata kama hakuchokozwa, Kama hakujua kuwa waliochokozwa wanaweza kumkabili adui.”

Hii ni ahadi aliyoichukua Mwenyezi Mungu kwa kila mwislamu kwa maafikiano ya madhehebu yote; sawa na walivyoafikiana juu ya wajibu wa Swaum, Swala, Hijja na Zaka.

Waislamu na waarabu hivi sasa wamejaribiwa kwa uchokozi wa Uzayuni wa kikoloni juu ya dini yao na miji yao. Wameuliwa wamefukuzwa na wakafungwa kwa maelefu. Kwa hiyo ni juu ya kila Mwarabu na Mwislamu popote alipo, Mashariki au Magharibi apigane kwa nguvu zake zote dhidi ya genge hili linalojiita dola ya Israil.

Hilo ni kheri kwenu.

Yaani hilo la kutoka ni kheri kwa waislamu katika dini yao na dunia yao.

Mkiwa mnamjua.

Ndio sisi tunajua kwamba kutoka kuwapiga jihadi waisrail ni wajibu kwa kila Mwislamu, lakini linalotuzuia kuwapiga jihadi waisrail ni viongozi wahaini. Kwa hiyo basi ni wajibu kuwapiga jihadi hawa kabla ya chochote. Kwa sababu wao ndio sababu ya sababu; lau si hiyana yao kwa dini yao, uma wao na kuwatii kwao wazayuni na ukoloni, basi Israil isigekuwako kabisa.

Lau ingekuwa ni faida iliyo karibu na safari nyepesi wangelikufuata.

Dhamiri ya wangekufuata inawarudia walio rudi nyuma katika vita vya Tabuk, Faida ya karibu ni ngawira baridi. Maana ni kuwa Ewe Muhammad! lau ungeliwaita kwenye manufaa ya haraka wangelikuitikia haraka haraka.

Lakini imekuwa ndefu kwao yenye mashaka.

Safari ya Sham kupitia jangwani kwenye vumbi la upepo na joto kali na adui Mrumi ndiye mwenye nguvu wakati huo, vipi watakuitikia?

Sifa hizi hazihusiki na wale waliorudi nyuma katika vita vya Tabuk tu, bali nafsi hupendelea raha na manufaa. Lakini watu wa imani wanaojiridhia kwa takua, wanaona chepesi kila kitu anachokiridhia Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Imam Ali(a.s) anasema:“Amali bora ni ile inayokirihisha nafsi yako.”

Yametangulia maelezo yanayoambatana na hayo katika Juz.5 (4:37).

Na wataapa kwa Mwenyezi Mungu lau tungeliweza bila shaka tungelitoka pamoja nanyi.

Hii ni habari kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake kwamba wanafiki waliorudi nyuma ya vita vya Tabuk, wamemwandalia viapo na nyudhuru za uwongo atakaporudi. Kimsingi ni kwamba sifa ya uongo haiepukani na mnafiki; kama si hivyo basi asingelikuwa mnafiki.

Wanaziangamiza nafsi zao.

Kwa vile wao wameiangamiza dini yao kwa uwongo na unafiki.

Na Mwenyezi Mungu anajua kuwa hakika hao ni waongo katika nyudhuru zao na viapo vyao.

Inasemekana kuwa hasemi uwongo isipokuwa mwoga, nasi tunaogozea kuwa anayeangamizwa na tamaa pia ni mwoga.

Mwenyezi Mungu amekusamehe! Kwa nini umewapa ruhusa kabla ya kubainika kwako wanaosema kweli na ukawajua waongo.

Mtume(s.a.w.w) alipotoa mwito wa kwenda kwenye Jihadi, baadhi walimwomba ruhusa ya kutokwenda, wakatoa sababu kadhaa. Mtume akawakubalia kabla ya kujua ukweli wao na uwongo wao katika nyudhuru.

Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamlaumu kwa hilo, akamwambia, ingekuwa vizuri kungoja kuwapa ruhusa mpaka ikufunukie hakika yao.

Hayo ndiyo yanayofahamika kutokana na dhahiri ya Aya.

Utaweza kuuliza kuwa : Mtume(s.a.w.w) ni Maasumu, na kauli yake Mwenyezi Mungu ‘Amekusamehe’ inaonyesha kuweko kosa (dhambi), pia kauli yake Mwenyezi Mungu ‘kwa nini umewapa ruhusa.’

Jibu : Msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu haulazimishi kuweko dhambi. Mara nyingi inakuwa ni ibara ya thawabu yake na rehema yake, Mitume wote walikuwa wakiomba msamaha kwake Mwenyezi Mungu. Ama kusema “Kwa nini”, hilo ni jambo jepesi ambapo inasihi katika mambo ya halali na mengineyo. Unaweza kumwambia sahibu yako; kwa nini umefanya hivi?, Bila ya kuona kuwa amefanya jambo baya, isipokuwa unakusudia angefanya jingine.

Lengo la lawama hapa inayotoka kwa Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake, ni kubainisha uwongo wa wanafiki katika nyudhuru zao, na kwamba hilo lilikuwa ni kukimbia jihadi tu. Mfumo huu ni fasaha zaidi katika kukanusha udhuru kuliko mifumo yote. Zaidi ya hayo Mwenyezi Mungu amesema katika Aya 117 ya Sura hii: “Mwenyezi Mungu amekubalia toba wahajir na answar waliomfuata katika saa ya dhiki Ikiwa toba haifahamishi kuweko dhambi, basi msamaha na kuuliza kwa nini, ndiko kusikofahamisha zaidi dhambi.

لَا يَسْتَأْذِنُكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ أَن يُجَاهِدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِالْمُتَّقِينَ ﴿٤٤﴾

44. Hawakuombi ruhusa ambao wanamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho ya kuacha kupigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwajua wenye takua.

إِنَّمَا يَسْتَأْذِنُكَ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَارْتَابَتْ قُلُوبُهُمْ فَهُمْ فِي رَيْبِهِمْ يَتَرَدَّدُونَ ﴿٤٥﴾

45. Hakika wanaokuomba ruhusa ni wale tu wasiomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Na nyoyo zao zikatia shaka, kwa hiyo wanasitasita katika shaka yao.

وَلَوْ أَرَادُوا الْخُرُوجَ لَأَعَدُّوا لَهُ عُدَّةً وَلَـٰكِن كَرِهَ اللَّـهُ انبِعَاثَهُمْ فَثَبَّطَهُمْ وَقِيلَ اقْعُدُوا مَعَ الْقَاعِدِينَ ﴿٤٦﴾

46. Lau wangelitaka kutoka bila shaka wangeliandalia maandilio, Lakini Mwenyezi Mungu alichukia kutoka kwao, kwa hiyo akawazuia Na ikasemwa: Kaeni pamoja na wakaao.

لَوْ خَرَجُوا فِيكُم مَّا زَادُوكُمْ إِلَّا خَبَالًا وَلَأَوْضَعُوا خِلَالَكُمْ يَبْغُونَكُمُ الْفِتْنَةَ وَفِيكُمْ سَمَّاعُونَ لَهُمْ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِالظَّالِمِينَ ﴿٤٧﴾

47. Lau wangelitoka pamoja nanyi wasingeliwazidisha ila mchafuko na wangelikwenda huku na huko kati yenu kuwatakia fitina, Na miongoni mwenu wako wanawaosikiliza, Na Mwenyezi Mungu anawajua madhalimu.

لَقَدِ ابْتَغَوُا الْفِتْنَةَ مِن قَبْلُ وَقَلَّبُوا لَكَ الْأُمُورَ حَتَّىٰ جَاءَ الْحَقُّ وَظَهَرَ أَمْرُ اللَّـهِ وَهُمْ كَارِهُونَ ﴿٤٨﴾

48. Walikwishataka fitina tangu zamani na wakakupindulia mambo. Mpaka ikaja haki na ikadhihiri amri ya Mwenyezi Mungu na wao wamechukia.

HAWAKUOMBI RUHUSA AMBAO WANAWAMWAMINI MWENYEZI MUNGU

Aya 44 – 48

MAANA

Hawakuombi ruhusa ambao wanamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho ya kuacha kupigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao.

Kutakuwa na sababu gani ya kuomba ruhusa ikiwa jihadi ni wajibu. Je, mumin wa kweli anaweza kuomba ruhusa ya kuacha kuswali na kufunga na kusema lailaha illa llah, Muhammad Rasullah?

Hakika wanaokuomba ruhusa ni wale tu wasiomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.

Kila moja katika Aya mbili hizi inafahamisha juu ya mwenzake, Kwa sababu maana ya kuwa Mumin hakuombi ruhusa nikuwa asiyekuwa mumin hukuomba, Na maana ya asiyekuwa mumin anakuomba ruhusa ni kuwa mumin hakuombi. Mwenyezi Mungu amechanganya Aya mbili hizi kwa kusisitiza maana.

Na nyoyo zao zikatia shaka, kwa hiyo wanasitasita katika shaka yao.

Yaani kwamba wao wanajionyesha kuwa ni waislamu, lakini kumbe walivyo ni kuwa wanashaka shaka, hawasemi kuwa ni kweli au ni uwongo. Huu ndio unafiki, Kwa sababu mkweli mwenye ikhlasi hufanya vile inavyoonelea akili yake na kudhihirisha kwa watu, iwe ni shaka au yakini.

Lau wangelitaka kutoka pamoja na mtume kwenye vita vya Tabuk,bila shaka wangeliandalia maandilio ya vipando na masurufu ya njiani; nao walikuwa wakiliweza hilo.

Lakini Mwenyezi Mungu alichukia kutoka kwao, kwa sababu hawana wanalolitokea isipokuwa ufisadi na fitina; kama walivyofanya katika vita vya Hunain, wakati Abu Sufyan na walio mfano wake walipotoka na Mtume vita vilipochacha waligeuka wakakimbia na likalegea jeshi la waislamu.

Kwa hiyo akawazuia.

Mwenyezi Mungu aliwaamrisha kutoka kwa ajili ya Jihadi, lakini wao waliazimia ufisadi kwa kuleta migongano katika jeshi la wislamu; kama alivyosema katika Aya inayofuatia:

Lau wangelitoka pamoja nanyi wasingeliwazidisha ila mchafuko.

Kwa hiyo aliwazuia Mwenyezi Mungu na hili la fitina sio na jihadi, ambayo amewaaamrisha.

Na ikasemwa: Kaeni pamoja na wakaao.

Yaani kaeni pamoja na wanawake, watoto na vikongwe.

Mwenyezi Mungu hakubainisha aliyewaambia hivyo, Je, ni nafsi zao, au hali yenyewe ilivyokuwa au waliambiana wenyewe? Mwenyezi Mungu ndiye ajuae.

Unaweza kuuliza : Katika Aya 43, Mwenyezi Mungu amesema: Kwa nini umewapa ruhusa na katika Aya hii anasema: Mwenyezi Mungu hakupenda kutoka kwao, Sasa tutazichanganya vipi Aya hizi?

Jibu : litaeleleweka kulingana na tuliyoyasema katika kufasiri kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Kwa nini umewaruhusu’ kwamba hiyo sio lawama na swali la kiuhakika; isipokuwa lengo ni kubainisha uwongo wa wanafiki katika nyudhuru zao.

Lau wangelitoka pamoja nanyi wasingeliwazidisha ila mchafuko na wangelikwenda huku na huko kati yenu kuwatakia fitina.

Huu ni ubainifu wa hekima ya Mwenyezi Mungu wa kutopenda kwake Mwenyezi Mungu na Mtume kutoka wanafiki pamoja na jeshi la waislam. kwamba wao wangefanya mbinu za kuwatenganisha na kuleta vurugu ndani ya jeshi. Watu wa aina hii wapo kila mahali na kila wakati. Siku hizi wanajulikana kwa jina la kikosi cha tano (Fifth Column).

Na miongoni mwenu wako wanawaosikiliza.

Nao ni wale wenye akili za juu juu ambao wanachukua maneno ya waongo ni bendera wanaofuata upepeo.

Walikwishataka fitina tangu zamani na wakakupindulia mambo.

Mwenyezi Mungu anadokeza vitimbi vyao na hadaa zao kwa Mtume kabla ya vita vya Tabuk, ikiwa ni pamoja na kukimbia Abu Sufyan katika vita vya Hunain, na kujitoa bin Ubayya pamoja na theluthi ya jeshi katika vita vya Uhud.

Mpaka ikaja haki na ikadhihiri amri ya Mwenyezi Mungu na wao wamechukia.

Kila aliyopenda Mwenyezi Mungu ni haki na kila aliyoyachukia ni batili. Mwenyezi Mungu alipenda Uislam pamoja na Mtume wake ushinde. Kwa hiyo yakatimia aliyoyataka Mwenyezi Mungu na akamwandalia sababu kwa ushindi wa kuiteka Makka, ushindi katika vita vya Hunain na Tabuk na kusafika bara Arabu kutokana na uchafu wa Mayahudi waovu.

Makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Na ikadhihiri amri ya Mwenyezi Mungu’ ni kwamba ushindi huu waliushuhudia watu wote, na mpaka leo hivi hadi siku ya mwisho jina la Muhammad bin Abdullah linatajwa pamoja na la Mwenyezi Mungu kote - Mashariki mwa Ardhi na Magharibi.


8

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

وَمِنْهُم مَّن يَقُولُ ائْذَن لِّي وَلَا تَفْتِنِّي أَلَا فِي الْفِتْنَةِ سَقَطُوا وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمُحِيطَةٌ بِالْكَافِرِينَ ﴿٤٩﴾

49. Na miongoni mwao kuna anayesema: Niruhusu wala usinitie katika fitina, Hakika wamekwishatumbukia katika fitina, Na hakika Jahannam imewazunguka makafiri.

إِن تُصِبْكَ حَسَنَةٌ تَسُؤْهُمْ وَإِن تُصِبْكَ مُصِيبَةٌ يَقُولُوا قَدْ أَخَذْنَا أَمْرَنَا مِن قَبْلُ وَيَتَوَلَّوا وَّهُمْ فَرِحُونَ ﴿٥٠﴾

50. Ukikupata wema unawachukiza, Na ukikusibu msiba husema: Tuliangalia vizuri mambo yetu tangu mwanzo na hugeuka kwenda zo wakiwa wamefurahi.

قُل لَّن يُصِيبَنَا إِلَّا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَنَا هُوَ مَوْلَانَا وَعَلَى اللَّـهِ فَلْيَتَوَكَّلِ الْمُؤْمِنُونَ ﴿٥١﴾

51. Sema halitatusibu ila alilotuandikia Mwenyezi Mungu. Yeye ni Mola wetu, basi waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu.

قُلْ هَلْ تَرَبَّصُونَ بِنَا إِلَّا إِحْدَى الْحُسْنَيَيْنِ وَنَحْنُ نَتَرَبَّصُ بِكُمْ أَن يُصِيبَكُمُ اللَّـهُ بِعَذَابٍ مِّنْ عِندِهِ أَوْ بِأَيْدِينَا فَتَرَبَّصُوا إِنَّا مَعَكُم مُّتَرَبِّصُونَ ﴿٥٢﴾

52. Sema: Nyinyi hamtutazami ila moja ya mema mawili Na sisi tunawatizamia kuwa Mwenyezi Mungu awafikishie adhabu itokayo kwake au kwa mikono yetu, Basi ngojeni nasi tunangoja pamoja nanyi.

NA MIONGONI MWAO KUNA ANAYESEMA: NIRUHUSU

Aya 49 – 52

MAANA

Na miongoni mwao kuna anayesema: Niruhusu wala usinitie katika fitina.

Wamekubaliana wafasiri kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alipotoa mwito wa kwenda kwenye vita vya Tabuk, Jad bin Qays, aliyekuwa ni katika wakuu wa kinafiki, alisema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ni ruhusu, kwa vile mimi ni mtu ninayependa wanawake, ninaogopa nikawaona wanawake wa Kirumi nitafitinika nao”, ndipo akashuka Aya hiyo. Mnaafiki huyu alidai kuwa anahofia dhambi kwa wanawake kama atapigana pamoja na Mtume(s.a.w.w) , lakini asiogope kuingia katika ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Hakika wamekwishatumbukia katika fitina.

Yaani walidai kukimbia dhambi na wakaingia katika dhambi waliyoikimbia au zaidi yake.

Na hakika Jahannam imewazunguka makafiri katika pande zote wala hawatapa kimbilio.

Mtume aliwapa mwito wa kujitakasha kwa kutubia dhambi zao ambazo zimewazunguka kila upande, lakini wakakataa mwito wake, ndipo ikawazunguka adhabu kila upande.

Ukikupata wema unawachukiza.

Kama ilivyo kawaida ya mtu mbaya, huchukia sana watu wema wanapopata yanayowapendeza; na hufurahi sana wanapopatwa na yanayowachukiza.

Na ukikusibu msiba husema: Tuliangalia vizuri mambo yetu tangu mwanzo, na hugeuka kwenda zao wakiwa wamefurahi.

Mfumo unafahamisha kwamba makusudio ya msiba ni kuvunjika jeshi la waislamu. Kwa sababu kusema kwao: ‘Tuliangalia vizuri mambo yetu,’ maana yake ni kuwa waislamu walipokuwa wakipata machukivu, basi wanafiki walikuwa wakizungumziana kwa furaha na kuambiana kuwa sisi tulichukua tahadhari, umetangulia mfano wa hayo katika Juz. 4 (3: 120) na Juzuu hii (8:49).

Sema: halitatusibu ila alilotuandikia Mwenyezi Mungu.

Yaani sema ewe Mtume kuwaambia wanafiki, Sisi ndio ambao tumezinduka na kuchukua tahadhari, sio nyinyi kwa sababu nyinyi mmekaa tu, na sisi tumepigana jihad baada ya kujiandaa; na tumepitia desturi ya Mwenyezi Mungu katika vita, kuna siku yetu na siku yao, mapambano bado yanaendelea, mambo huangaliwa mwisho wake, ushindi ni wetu mwishoni na kila lijalo likaribu.

Yeye ni Mola wetu, basi waumini wamtegemee Mwenyezi Mungu.

Ambao wanajiandaa kisha wakaendelea kwa jina la Mwenyezi Mungu. Wakipatwa na vizuri husema: Hii ni katika fadhila za Mwenyezi Mungu na rehema yake, na wakipatwa na msiba husema hiyo ni kudura ya Mwenyezi Mungu; wakiwa katika hali ya ikhlas na yakini ya dini yao; na kwamba Mwenyezi Mungu ataidhihirisha kuliko dini zote wajapochukia makafiri.

Sema: Nyinyi hamtutazami ila moja ya mema mawili, ambayo ni ushindi au kufa shahidi.

Katika ushindi kuna kuwadhalilisha makafiri na wanafiki; na katika shahada kuna thawabu kubwa. Yote mawili ni utukufu na heshima.

Na sisi tunawatizamia kuwa Mwenyezi Mungu awafikishie adhabu itokayo kwake au kwa mikono yetu, Basi ngojeni nasi tunangoja pamoja nanyi.

Kwa vyovyote mwisho wa wanaopigana jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu ni moja ya mambo mawili mazuri: ushindi au kufa shahidi.

Na, mwisho wa wanafiki na makafiri ni moja ya maovu mawili: Ama adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu au kupigwa na waumini wanapopata idhini ya Mwenyezi Mungu.

قُلْ أَنفِقُوا طَوْعًا أَوْ كَرْهًا لَّن يُتَقَبَّلَ مِنكُمْ إِنَّكُمْ كُنتُمْ قَوْمًا فَاسِقِينَ ﴿٥٣﴾

53. Sema: toeni kwa kupenda au kuchukia haitakubaliwa kwenu, Hakika nyinyi mmekua watu mafasiki.

وَمَا مَنَعَهُمْ أَن تُقْبَلَ مِنْهُمْ نَفَقَاتُهُمْ إِلَّا أَنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّـهِ وَبِرَسُولِهِ وَلَا يَأْتُونَ الصَّلَاةَ إِلَّا وَهُمْ كُسَالَىٰ وَلَا يُنفِقُونَ إِلَّا وَهُمْ كَارِهُونَ ﴿٥٤﴾

54. Na hawakuzuiliwa kukubaliwa michango yao, ila ni kwamba wao wamemkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Wala hawaiendei swala ila katika hali ya uvivu, wala hawatoi ila kwa kuchukia.

فَلَا تُعْجِبْكَ أَمْوَالُهُمْ وَلَا أَوْلَادُهُمْ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ لِيُعَذِّبَهُم بِهَا فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَتَزْهَقَ أَنفُسُهُمْ وَهُمْ كَافِرُونَ ﴿٥٥﴾

55. Basi zisikushangaze mali zao wala watoto wao, Hakika Mwenyezi Mungu anataka tu kuwaadhibu kwayo katika maisha ya dunia. Na roho zao zitoke na hali wao ni makafiri.

وَيَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ إِنَّهُمْ لَمِنكُمْ وَمَا هُم مِّنكُمْ وَلَـٰكِنَّهُمْ قَوْمٌ يَفْرَقُونَ ﴿٥٦﴾

56. Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao ni katika nyinyi, na wala wao si katika nyinyi. Lakini wao ni watu wanaogopa.

لَوْ يَجِدُونَ مَلْجَأً أَوْ مَغَارَاتٍ أَوْ مُدَّخَلًا لَّوَلَّوْا إِلَيْهِ وَهُمْ يَجْمَحُونَ ﴿٥٧﴾

57. Lau wangelipata pa kukimbilia au mapango au mahali pa kuingia wangeligeukia huko kwa kasi sana.

SADAKA ZA WANAFIKI

Aya 53 – 57

MAANA

Sema: toeni kwa kupenda au kuchukia haitakubaliwa kwenu.

Baada ya Mtume(s.a.w.w) kujiandaa kwa vita vya Tabuk, mnafiki mmoja alimtaka amruhusu asiende kwenye jihadi, akatoa kitu kidogo katika mali yake.

Mwenyezi Mungu akamwamuru Mtume wake amwambie mnafiki huyu na mfano wake kuwa Mwenyezi Mungu haana haja na mali zenu na zichukueni wenyewe, hata kama mmetoa kwa kupenda au kutopenda.

Utauliza : Tunajua njia ya kukataa ikiwa kutoa ni kwa kutopenda; sasa kuna wajihi gani wa kukataa ikiwa kutoa ni kwa kupenda?

Jibu : Wao hawakutaka kutoa kwa kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, isipokuwa walitaka umashuhuri na jaha. Hakuna tofauti kati ya kutoa kwa lengo hili na kutoa kwa kutopenda kwa kuhofia kutojulikana hakika yao – yote mawili ni kwa ajili ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Kwa ajili hii ndipo Mwenyezi Mungu akawaambia:

Hakika nyinyi mmekua watu mafasiki.

Na,kuwaita mafasiki kunaashiria kuwa ufasiki ndio sababu ya kutokubaliwa.

Na hawakuzuiliwa kukubaliwa michango yao, ila ni kwamba wao wamemkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake,

Wanafiki walitoa mali zao ili tu waambiwe kuwa nao wametoa kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na huku wanamkanusha. Na, unafiki huu na ria hii ndio sababu ya kutokubaliwa wanachokitoa.

Lau wangelitoa kwa ubinadamu tu, kama vile mlahidi anapomlisha mwenye njaa, ingeliweza kusemwa: ‘Hakuna malipo ya hisani ila hisani.’ Lakini unafiki ni uovu; na mwenye kufanya uovu atalipwa Kwa maelezo zaidi angalia Juz.4 (3:177) Kifungu cha ‘Kafiri na amali ya Kheri’

Wala hawaiendei swala ila katika hali ya uvivu, wala hawatoi ila kwa kuchukia.

Hali hiyo ndiyo natija ya ukafiri kwa sababu kuswali kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kutoa kwa ajili yake ni matawi ya imani.

Basi zisikushangaze mali zao wala watoto wao, Hakika Mwenyezi Mungu anataka tu kuwaadhibu kwayo katika maisha ya dunia.

Unaweza kuuliza kuwa: mali na watoto inaweza kuwa ni sababu ya adhabu ya Akhera, ambapo watu wengi, siku za shida wamewahi kuahidi wema, lakini wanapojiwa na fadhila za Mwenyezi Mungu hupetuka mpaka na kufanya uovu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

كَلَّا إِنَّ الْإِنسَانَ لَيَطْغَىٰ ﴿٦﴾ أَن رَّآهُ اسْتَغْنَىٰ ﴿٧﴾

“Hakika binadamu hupetuka mpaka kwakujiona ametajirika” (96:6-7)

Na akasema:

وَاعْلَمُوا أَنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ ﴿٢٨﴾

“Na jueni kwamba mali zenu na watoto wenu ni fitna” Juz.9 (8:28)

Lakini kuwa mali na watoto ni sababu ya adhabu katika dunia, hilo ni kinyume; hasa mali iliyotafutwa chini ya ardhi na ndani ya bahari na wa kati ambapo teknolojia imeendelea kufikia kuitafuta mwezini na kwengineko. Zaidi ya hayo, kauli hii haiafikiani na kauli isemayo:

الْمَالُ وَالْبَنُونَ زِينَةُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ﴿٤٦﴾

“Mali na watoto ni pambo la maisha ya dunia” (18:46)

Na kama itakuwa mali ni sababu ya adhabu katika maisha haya, basi adhabu haitahusika na wanafiki tu, bali itawaenea watu wote” Sasa itakuwaje?

Jibu : Ni kweli huu ni mushkel, lakini ikiwa Aya inawahusu wote. Ama ikiwa inakusudia tukio maalum, basi hakutakuwa na mushkeli wowote.

Mfumo wa maneno ulio kabla ya Aya hii na iliyo baada yake, unafahamisha waziwazi kwamba dhamiri katika ‘Anataka kuwadhibu”, inarudia kuhusisha wanafiki waliokuwa wakati wa Mtume na kuwahusu hasa wale waliojitoa katika vita vya Tabuk ambao walikuwa kiasi watu themanini na kitu, kama ilivyosemekana, na walikuwemo wenye mali nyingi na watoto wengi.

Ili isisemwe kuwa vipi watu hawa ni wafasiki na Mwenyezi Mungu amewaneemesha kwa mali na watoto. Ndipo Mwenyezi Mungu akasema: “Hakika tu Mwenyezi Mungu anataka kuwaadhibu kwayo katika maisha ya dunia”.

Na, kweli Mwenyezi Mungu aliwaadhibu kwa watoto wao. Kwani watoto wao walikubali Uislam na wakawa na ikhlasi, kinyume na mababa zao. Hakuna hasara mbaya kwa mzazi kuliko kuwa mwanawe ana dini nyingine na itikadi nyingine. Mwana wa Abdallah bin Ubayya, alisilimu na kupendekeza kwa Mtume(s.a.w.w) amuue baba yake, mkuu wa wanafiki, lakini Mtume akakataa.

Vile vile aliwaadhibu kwa mali zao, kwa vile wao walikuwa na yakini kuwa itawageukia wale ambao hawako katika dini yao na njia yao.

Kwa hiyo Aya inahusika na wanafiki waliokuwa katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Na kwa hali hiyo basi hakuna wajihi wowote kwa waliyoyataja wafasiri, kwamba kuadhibiwa na Mwenyezi Mungu kwa mali zao ni kutabika kuitafuta, na kwamba kuadhibiwa kwa wototo wao ni kuona uchungu wakiugua na wakiwakosa. Kwani tabu hiyo na machungu hayo hayahusiki na wanafiki peke yao, bali ni kila mwenye mali na familia.

Na roho zao zitoke na hali wao ni makafiri.

Yaani watakufa wakiwa makafiri na Mwenyezi Mungu atawaadhibu kwa kufuru yao huko Akhera, kama alivyowaadhibu kwa mali zao katika dunia.

Tabrasi katika Majmaul-bayan anasema: “Matakwa ya Mwenyezi Mungu yamefungamana na kutoka roho zao sio ukafiri wao; kama kusema: Nataka kumpiga akiwa asi, Hapa kutaka kumefungamana na kupiga sio kuasi.”

Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwamba wao ni katika nyinyi, na wala wao si katika nyinyi.

Kuna faida gani ya kiapo hiki na Mwenyezi Mungu ameshuhudia kwamba wao wamesilimu kwa kuhofia, sio kwa kukinai.

Lakini wao ni watu wanaogopa.

Nyoyo za wanafiki zilijazwa na hofu kwa nguvu ya waislamu

Lau wangelipata pa kukimbilia au mapango au mahali pa kuingia wangeligeukia huko kwa kasi sana.

Yaani wangelikimbilia huko kwa kasi sana. Wanafiki hawakuweza kutoka Madina, pia hawakuthubutu kudhihirisha ukafiri kwa vile Uislamu ulikuwa umeingia katika kila nyumba ya Aus na Khazraj. Kwa hiyo wakalazimika kusilimu kwa ncha za ndimi zao wakiwa ni makafiri nyoyoni wakingoja fursa ya kuufanyia vitimbi Uislamu.

وَمِنْهُم مَّن يَلْمِزُكَ فِي الصَّدَقَاتِ فَإِنْ أُعْطُوا مِنْهَا رَضُوا وَإِن لَّمْ يُعْطَوْا مِنْهَا إِذَا هُمْ يَسْخَطُونَ ﴿٥٨﴾

58. Na miongoni mwao wako wanao kulaumu katika sadaka, Na wanapopewa katika hizo huridhika, na wasipopewa katika hizo huchukia.

وَلَوْ أَنَّهُمْ رَضُوا مَا آتَاهُمُ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ وَقَالُوا حَسْبُنَا اللَّـهُ سَيُؤْتِينَا اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ وَرَسُولُهُ إِنَّا إِلَى اللَّـهِ رَاغِبُونَ ﴿٥٩﴾

59. Na lau wangeliridhia kile alichowapa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosheleza, Mwenyezi Mungu atatupa katika fadhila zake, na Mtume wake; hakika sisi ni wenye kumtaka Mwenyezi Mungu.

WANAPOPEWA HURIDHIA

Aya 58 – 59

MAANA

Na miongoni mwao wako wanao kulaumu katika sadaka.

Dhamir ya miongoni mwao inawarudia wanafiki, Maana ni kuwa baadhi ya wanafiki walikuwa wakimsema Mtume(s.a.w.w) na kumtia ila katika kugawa kwa kudai kuwa anapendelea.

Katika Tafsir Tabari imepokewa kutoka, kwa Said Al-Khudri, amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alipokuwa akigawa mafungu, alijiwa na Ibn Dhulkhuwayswara Tamimi, akasema: Fanya uadilifu ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu. Mtume akasema: Ole wako! Ninani atafanya uadilifu ikiwa mimi sikufanya? Umar akasema: Niruhusu ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nikate shingo yake. Mtume(s.a.w.w) akasema: Mwache yeye ana wenzake ambao mmoja wenu atadharau kuswali nao na kufunga nao, watachomoka katika dini kama unavyochomoka mshale kwenye upinde; alama yao ni mtu mweusi[10] , moja ya mikono yake ni kama titi la mwanamke” Ndipo ikashuka: ‘Na miongoni mwao wako wanao kulaumu katika sadaka’.

Anaendelea kusema Abu Said: Ninashuhudia kuwa mtume alisema haya na nashuhudia kuwa alipouawa Ali (rehema za Mwenyezi Mungu ziwe kwake) aliletwa mtu aliyekuwa na sifa hizo”

Na wanapopewa katika hizo huridhika, na wasipopewa katika hizo huchukia.

Mtume alikuwa akigawanya sadaka, kama alivyobainisha Mwenyezi Mungu. Waumin walikuwa wakiridhia na wanafiki wakichukia na kumlaumu katika kugawanya kwake.

Aya inamchanganya kila asiyeridhia fungu lake. Lau watu wote wangeliridhia wanayostahiki, watu wote wangeliishi katika amani na raha.

Na lau wangeliridhia kile alichowapa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakasema: Mwenyezi Mungu anatutosheleza, Mwenyezi Mungu atatupa katika fadhila zake, na Mtume wake; hakika sisi ni wenye kumtaka Mwenyezi Mungu kututoshea na sadaka na mengineyo ya kuwahitajia watu.

Aya hii inahimiza mtu kujizuilia na vilivyo mikononi mwa watu, kumtege- mea Mwenyezi Mungu na kula jasho lake.

Imam AIi(a.s) anasema:“Utajiri mkubwa ni kutokuwa na tamaa na vilvyo mikononi mwa watu” .

Sijui kama kuna anayestahiki kudharauliwa kuliko yule anayetarajia watu na huku anaweza kujitosha nao japo kwa subira.

إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاءِ وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِّنَ اللَّـهِ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٦٠﴾

60. Hakika sadaka ni ya (hawa) tu: Mafukara na masikini na wanaozitumikia na wanaotiwa nguvu nyoyo zao Na kuwakomboa watumwa na wenye madeni na katika njia ya Mwenyezi Mungu na mwana njia. Ni faradhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kujua mwenye hekima.

WANASTAHIKI ZAKA

Aya 60

MAANA

Makusudio ya sadaka hapa ni zaka ya wajibu. Mafakihi wameizungumzia zaka, hukumu zake, sharti zake, vitu ambavyo ni wajibu vitolewe zaka na wenye kustahiki kupewa. Sisi tumezungumzia kwa ufafanuzi katika Kitab Fiqhul-Imam Jaffer Assadiq Juz: 2. Katika Juz: 3 (2:272) tumeizungumzia zaka kama msimamo uliothibitishwa na Uislamu.

Hapa tutazungumzia aina nane za wanaostahiki kupewa zaka kulingana na Aya tukufu:

1.Hakika Sadaka Ni Ya(Hawa) Tu. Mafukara.

Shia Imamia wanasema: Fukara wa kisharia ni yule asiyemiliki gharama yake ya mwaka na ya watoto wake. Hanafi wanasema ni yule anayemiliki chini ya kiwango cha zaka. Shafii na Hambal wanasema mwenye kupata nusu ya mahitaji yake hahisabiwi kuwa fukara. Shia Imamia, Shafii na Hambal wanasema: Mwenye kuweza kuchuma si halali kwake zaka, lakini Hanafi na Malik wamesema ni halali.

2.Na Masikini.

Wamesema jamaa, kuwa neno fukara na maskini yakiwa pamoja kila moja linakuwa na maana nyingine; na yakiwa mbali mbali basi yanakuwa na maana moja. Wakasema tofauti ni kuwa fukara haombi na maskini huomba. Vyovyote iwavyo la kuzingatia ni haja, na wote ni wahitaji.

3.Na Wanaozitumikia.

Ni wale wanaokusanya zaka, waliowekwa na Imam au naibu wake, kusimamia kukusanya zaka na kuihifadhi; kisha kuitoa kwa atakayeigawanya kwa anayestahiki. Kile wakichukuacho wakusanyaji kinazingatiwa kuwa ni malipo ya kazi yao, sio sadaka. Kwa hiyo wanapewa hata kama ni matajiri.

4.Na Wanaotowa Nguvuu Nyoyo Zao.

Ni wale wanaovutiwa kwenye Uislamu au wanatakiwa msaada na Waislamu kwa manufaa ya Uislamu.

5.Na Kuwakomboa Watumwa.

Yaani inatolewa zaka kwa ajili ya kuwakomboa watumwa wawe huru. Mambo haya hayako siku hizi.

6.Na Wenye Madeni.

Ni wale walio na madeni yanayowashinda kuyalipa watapewa zaka, kwa sharti yakuwa wawe hawakutumia madeni hayo katika dhambi.

7.Na Katika Njia Ya Mwenyezi Mungu.

Njia ya Mwenyezi Mungu ni kila analoliridhia ambalo hutakiwa kujikurubisha kwake, kwa namna yoyote itakavyo kuwa, kama vile kutegeneza njia, kujenga zahanati au vyuo. Bora zaidi ni kutoa katika kupigania dini na nchi.

8.Na Mwana Njia.

Huyo ni msafiri aliyeishiwa njiani, atapewa kiasi kitakachomfikisha kwao; hata kama ni tajiri, kwa sharti ya kuwa safari yake isiwe ya maasi.


9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

وَمِنْهُمُ الَّذِينَ يُؤْذُونَ النَّبِيَّ وَيَقُولُونَ هُوَ أُذُنٌ قُلْ أُذُنُ خَيْرٍ لَّكُمْ يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَيُؤْمِنُ لِلْمُؤْمِنِينَ وَرَحْمَةٌ لِّلَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَالَّذِينَ يُؤْذُونَ رَسُولَ اللَّـهِ لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٦١﴾

61. Na miongoni mwao wako wanaomuudhi Mtume na kusema: Yeye ni sikio tu. Sema: ni sikio la heri kwenu. Anamwamini Mwenyezi Mungu na ana imani na waumini. Na ni rehema kwa wale wanaoamini miongoni mwenu. Na wale wanaomuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu wana adhabu iumizayo.

يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ لَكُمْ لِيُرْضُوكُمْ وَاللَّـهُ وَرَسُولُهُ أَحَقُّ أَن يُرْضُوهُ إِن كَانُوا مُؤْمِنِينَ ﴿٦٢﴾

62. Wanawaapia Mwenyezi Mungu ili wawaridhishe na hali Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ndiye mwenye haki zaidi ya kumridhisha, ikiwa wao ni waumini.

أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّهُ مَن يُحَادِدِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَأَنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدًا فِيهَا ذَٰلِكَ الْخِزْيُ الْعَظِيمُ ﴿٦٣﴾

63. Je, Hawajui kuwa anayeshindana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi huyo atapata moto wa Jahanamu adumu humo? Hiyo ni hizaya kubwa.

WANASEMA YEYE NI SIKIO TU

Aya 61-63

MAANA

Na miongoni mwao wako wanaomuudhi Mtume na kusema: Yeye ni sikio tu.

Mtume(s.a.w.w) alikuwa akiwachukuliwa wote kwa dhahiri yao, bila ya kumtafuta mtu undani wake, kwa kuchukulia msingi wa kuwa dhahiri ni ya watu na undani ni wa Mwenyezi Mungu.

Hiyo ni miongoni mwa misingi ya Kiislamu ya sharia inayochukuliwa hukumu nyingi. Waliitumia wanafiki; wakawa wanaepuka kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakitoa udhuru na Mtume akiwakubalia.

Ajabu ni kwamba wao walitumia fadhila hii kuwa ni njia ya kumtukana na kumnasibisha kuwa anakubali haraka kila analolisikia bila ya kufikiria na kupambanua lipi la kukubalia na lipi la kukataa.

Lau kama Mtume angeliwakubalia kwa uwongo wao na unafiki wao, na kuwapa adhabu inyostahili, basi ingelikuwa shari kwao na wangelisema ni mwenye moyo mgumu na mwenye hasira.

Hiyo ndiyo ajabu kumwaibisha na lile lenye manufaa yanayowarudia wao! Lakini mwenye kulaumu hilo si ajabu kwake. Kwa vile anaangalia kila kitu kwa kioo cha nafsi yake kilicho cheusi; hata yule anayemfanyia wema pia.Amesema kweli yule aliyesema: “Asiyejua kizuri si mzuri yeye”.

Sema: ni sikio la heri kwenu.

Hili ni jibu la Mwenyezi Mungu kwa hao wanafiki. Kwa ufupi ni kwamba mtume ni sikio la heri sio la shari. Anawakubalia yale yasiyo na mad- hara kwa mtu na anakataa yaliyo na madhara; kama vile kusengenya na kufitini.

Anamwamini Mwenyezi Mungu na ana imani na waumini.

Yaani anawasadiki wakweli, kusadiki kwa kukinai, Ama wanafiki anawasadiki katika ambayo hapana madhara kuyasadiki.

Na ni rehema kwa wale wanaoamini miongoni mwenu.

Haya yanaungana na sikio la heri. Hiyo ni katika kuunganisha jumla kwenye mahsusi. Kwa sababu sikio la heri ni rehema vile vile.

Na wale wanaomuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu wana adhabu iumizayo.

Kwa sababu mwenye kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu ndio amemuudhi Mwenyezi Mungu.

Wanawaapia Mwenyezi Mungu ili wawaridhishe na hali Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ndiye mwenye haki zaidi ya kumridhisha, ikiwa wao ni waumini, kama wanavyodai.

Maneno ya wanawaapia na kuwaridhisha yanaelekezwa kwa Mtume na waumini. Mwenyezi Mungu amewapa habari katika Aya hii kwamba wanafiki walipojua kuwa mmewagundua waliwahofia; wakakimbilia viapo vya uwongo, Afadhali wao wangemridhisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa toba na ikhlasi.

Kuna hadith isemayo: “Mwenye kuapa kiapo cha uwongo, akiwa anajua kuwa yeye ni mwongo, basi amejitokeza kupambana na Mwenyezi Mungu”.

Ibara ya kusema ‘ndiye mwenye haki zaidi ya kumridhisha’, badala ya ndio wenye haki zaidi ya kuwaridhisha,’ ni kufahamisha kua kumridhisha Mtume ndio kumridhisha Mwenyezi Mungu; kama ambavyo kumuudhi ndiko kumuudhi yeye pia.

Je, Hawajui kuwa anayeshindana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi huyo atapata moto wa Jahanamu adumu humo? Hiyo ni hizaya kubwa.

Aya hii ni msisitizo wa Aya iliyotangulia. Sheikh Ismail Haqi anasema, katika tafsiri yake Rawhul Bayan: “Kila Mtume aliudhiwa kiasi kisichosemeka, na Muhammad(s.a.w.w) alikuwa ni zaidi; kama alivyosema mwenyewe: Hakuudhiwa Mtume kama nilivyoudhiwa mimi.”

Kwa kuwa kuudhiwa ni sababu ya kuimarika, basi maana ni kuwa hakuna Mtume aliyeimarika kuliko yeye. Hasan alipewa sumu na Husein akachinjwa kwa sababu ukamilifu ulikuwa ukiwakabili kwa kufa shahidi.

Mtume(s.a.w.w) alikuwa anaweza kuwaokoa kwa kuwaombea, lakini aliona ukamilifu wa daraja yao ulikuwa na nguvu kuliko kuokolewa; kiasi ambacho Mtume alimpa mmoja wa wakeze chupa mbili na kumwambia, kama moja ikiwa rangi ya njano, basi Hasan atakuwa amekufa shahidi kwa kupewa sumu; na kama nyingine ikiwa nyekundu basi Husein atakuwa shahidi kwa kuchinjwa, Na kweli hayo yakawa”.

يَحْذَرُ الْمُنَافِقُونَ أَن تُنَزَّلَ عَلَيْهِمْ سُورَةٌ تُنَبِّئُهُم بِمَا فِي قُلُوبِهِمْ قُلِ اسْتَهْزِئُوا إِنَّ اللَّـهَ مُخْرِجٌ مَّا تَحْذَرُونَ ﴿٦٤﴾

64. Wanaogopa wanafiki kuteremshiwa sura itakayowatajia yaliyomo nyoyoni mwao, Sema: Fanyeni mzaha tu, hakika Mwenyezi Mungu atayatoa mnayoyaogopa.

وَلَئِن سَأَلْتَهُمْ لَيَقُولُنَّ إِنَّمَا كُنَّا نَخُوضُ وَنَلْعَبُ قُلْ أَبِاللَّـهِ وَآيَاتِهِ وَرَسُولِهِ كُنتُمْ تَسْتَهْزِئُونَ ﴿٦٥﴾

65. Na ukiwauliza, kwa hakika watasema: Sisi tulikuwa tukipiga porojo na kuchezea tu. Sema: Je, mlikuwa mkimfanyia mzaha Mwenyezi Mungu na Aya zake na Mtume wake?

لَا تَعْتَذِرُوا قَدْ كَفَرْتُم بَعْدَ إِيمَانِكُمْ إِن نَّعْفُ عَن طَائِفَةٍ مِّنكُمْ نُعَذِّبْ طَائِفَةً بِأَنَّهُمْ كَانُوا مُجْرِمِينَ ﴿٦٦﴾

66. Msitoe udhuru, mmekwisha kufuru baada ya kuamini kwenu, Tukisamehe kundi moja miongoni mwenu tutaliadibu kundi jingine kwa vile wao walikuwa wakosefu.

WANAOGOPA WANAFIKI

Aya 64 – 66

MAANA

Wanaogopa wanafiki kuteremshiwa sura itakayowatajia yaliyomo nyoyoni mwao, Sema: Fanyeni mzaha tu, hakika Mwenyezi Mungu atayatoa mnayoyaogopa.

Wanafiki hawakuogopa hasa kushukiwa na wahyi kuwahusu wao, isipokuwa walidhihirisha hadhari kwa njia ya dharau na stihzai – walikuwa wakimbeza Mtume(s.a.w.w) huku wakiambizana kwa dharau: Angalieni, msije mkateremshiwa Sura!

Kwa upande mwingine wanafiki hawaamini wahyi, vipi watauogopa kiuhakika? Wafasiri wengi wamesma kuwa dhamiri katika ‘kuteremshiwa’, inawarudia waumini, na ile ya nyoyoni mwao inawarudia wanafiki. Lakini hayo yako mbali kwa sababu zifuatazo:

Kwanza : waumini hawakutajwa katika Aya na kwamba waliotajwa wazi- wazi ni wanafiki; kama ambavyo Aya iliyotangulia imewataja wao tu.

Pili : katika kufasiiri hivi, itabidi kuweko kutopatana dhamiri jambo amba- lo halina dalili.

Kwa ajili hii tunatilia nguvu kauli ya anayesema kuwa dhamiri zote zinawarudia wanafiki, Kwa hiyo maana yanakuwa wanaogopa kwa dharau, wanafiki kuteremshiwa Sura itakayofichua uadui wao kwa Uislamu na waislamu.

Mwenyezi Mungu naye akawapa kiaga cha kuwa Sura itakyowafichua itashuka tu, na itawakabili wao ana kwa ana; waombe msamaha usifae msamaha wao.

Na ukiwauliza, kwa hakika watasema: Sisi tulikuwa tukipiga porojo na kuchezea tu.

Jamaa katika wanafiki walisema yale yasiyostahiki kuhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Alipowauliza walisema tulikuwa tunafanya mchezo tu.

Wafasiri wametofautiana kuhusu majina ya walio sema hayo na aina ya maneno waliyoyasema. Aya haidokezi chochote katika hayo; nasi tunanya- maza kama alivyowanyamazia Mwenyezi Mungu.

Sema: Je, mlikuwa mkimfanyia mzaha Mwenyezi Mungu na Aya zake na Mtume wake?

Kusema kwao kuwa tulikuwa tukichezea ni kubaya zaidi kuliko dhambi waliyoitakia msamaha. Je, Mwenyezi Mungu ambaye umetukuka ukuu wake ni wakufanyiwa mchezo? Je, amewatuma Mitume wake waje wachezewe? Aya inafahamisha kwamba kila mwenye kuifanyia mchezo dini na huku- mu yake yenye kuthibiti kwa uwazi basi huyo ni kafiri.

Msitoe udhuru, mmekwisha kufuru baada ya kuamini kwenu.

Utauliza : Je, si hii inafahamisha kuwa wao walikuwa waumin kabla ya kufanya mzaha; na kwamba sababu ya kuyawajibisha ukafiri wao ni istihzai; na inajulikana kwamba wao walikuwa makafiri kabla; na huo ukafiri wao ndio sababu ya mchezo wao?

Jibu : Kabla ya kukiri kwao kuifanyia mchezo dini walikuwa ni makafiri kwa hali halisi, lakini walikuwa ni waislamu kihukumu, Kwa sababu wao walidhihirisha Uislamu,Kwa hiyo zikawapitia hukumu za waislam ambazo zinaangalia dhahiri sio hali halisi.

Mara tu baada ya kukiri kwao kuifanyia mchezo dini wamekuwa ni makafiri kwa hali halisi na kwa kihukumu, wakiwa sasa kwenye hukumu ya waliortadi.

Tukisamehe kundi moja miongoni mwenu tutaliadhibu kundi jingine kwa vile wao walikua wakosefu.

Wanafiki walikuwa aina mbili: Viongozi wanaofuatwa ambao wana utakia mabaya Uislamu, kumfanyia vitimbi Mtume wake na kumchezea. Kundi jingine ni wale madhaifu wanaofuata.

Ndipo akamwamrisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) Mtume wake mtukufu kuwasamehe hao wanyonge kwa unyonge wao na kuwaadhibu wale wengine.

Kwa sababu wao ndio sababu, Inasemekana kuwa Mwenyezi Mungu aliwasamehe waliotubia na kuwaadhibu waliog’ang’ania ukafiri na unafiki.

الْمُنَافِقُونَ وَالْمُنَافِقَاتُ بَعْضُهُم مِّن بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمُنكَرِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمَعْرُوفِ وَيَقْبِضُونَ أَيْدِيَهُمْ نَسُوا اللَّـهَ فَنَسِيَهُمْ إِنَّ الْمُنَافِقِينَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿٦٧﴾

67. Wanafiki wanaume na wanafiki wanawake ni hali moja. Wanaamrisha maovu na kukataza mema na wanafumba mikono yao. Wamemsahau Mwenyezi Mungu na yeye amewasahau, Hakika wanafiki ndio mafasiki.

وَعَدَ اللَّـهُ الْمُنَافِقِينَ وَالْمُنَافِقَاتِ وَالْكُفَّارَ نَارَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا هِيَ حَسْبُهُمْ وَلَعَنَهُمُ اللَّـهُ وَلَهُمْ عَذَابٌ مُّقِيمٌ ﴿٦٨﴾

68. Amewaahidi Mwenyezi Mungu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake na makafiri moto wa Jahanam hali ya kudumu humo.Ni tosha yao, Na Mwenyezi Mungu amewalaani, Na wana wao adhabu ya kudumu.

كَالَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ كَانُوا أَشَدَّ مِنكُمْ قُوَّةً وَأَكْثَرَ أَمْوَالًا وَأَوْلَادًا فَاسْتَمْتَعُوا بِخَلَاقِهِمْ فَاسْتَمْتَعْتُم بِخَلَاقِكُمْ كَمَا اسْتَمْتَعَ الَّذِينَ مِن قَبْلِكُم بِخَلَاقِهِمْ وَخُضْتُمْ كَالَّذِي خَاضُوا أُولَـٰئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿٦٩﴾

69. Ni kama wale waliokuwa kabla yenu. Walikuwa na nguvu zaidi kuliko nyinyi na mali nyingi na watoto. Basi walistarehea sehemu yao, na nyinyi mwastarehea sehemu yenu kama walivyostarehe kwa sehemu yao wale waliokuwa kabla yenu na mkazama (katika batili) kama walivyozama. Hao zimeporomoka amali zao katika dunia na akhera, Na hao ndio waliopata hasara.

أَلَمْ يَأْتِهِمْ نَبَأُ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ قَوْمِ نُوحٍ وَعَادٍ وَثَمُودَ وَقَوْمِ إِبْرَاهِيمَ وَأَصْحَابِ مَدْيَنَ وَالْمُؤْتَفِكَاتِ أَتَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيَظْلِمَهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿٧٠﴾

70. Je, hazikuwafikia habari za wale walio kuwa kabla yao, kaumu ya Nuh na Ad na Thamud na kaumu ya Ibrahim na watu wa Madyan na miiji iliyopinduliwa. Basi Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwadhulumu, lakini wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe.

WANAFIKI WANAUME NA WANAWAKE

Aya 67 – 70

MAANA

Wanafiki wanaume na wanafiki wanawake ni hali moja.

Hilo ni fumbo la kufanana kwao kisifa na kimatendo. Kisha akabainisha jinsi walivyofanana, kwa kauli yake:

Wanaamrisha maovu na kukataza mema na wanafumba mikono yao. Wamemsahau Mwenyezi Mungu na yeye amewasahau.

Maovu waliyoyamrisha ni ukafiri na unafiki; na wema walioukataza ni imani na kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ama mikono yao wameifunga kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu. Kumsahau Mwenyezi Mungu ni kuacha kwao kumtii; na yeye kuwasahau ni kuwanyima rehema yake.

Hakika wanafiki ndio mafasiki wenye kuacha njia ya Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema na kufuata njia ya shetani.

Amewaahidi Mwenyezi Mungu wanafiki wanaume na wanafiki wanawake na makafiri moto wa Jahanam hali ya kudumu humo.

Baada ya kubainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) maovu ya wanafiki, aliwa- pa kiaga na kumpa kiaga kila kafiri moto wa Jahanam.

Ni tosha yao.

Yaani malipo yanatoshana na matendo yao

Na Mwenyezi Mungu amewalaani Amewaweka mbali na rehema yake.Na wana wao adhabu ya kudumu Haipungui wala kukatika

Ni kama wale waliokuwa kabla yenu. Walikuwa na nguvu zaidi kuliko nyinyi na mali nyingi na watoto. Basi walistarehea sehemu yao, na nyinyi mwastarehea sehemu yenu kama walivyostarehea sehemu yao wale waliokuwa kabla yenu na mkazama (katika batili) kama walivyozama.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawambia: Enyi wanafiki mlio wakati wa Muhammad! Ni sawa na wanafiki waliopita. Walistarehe na maraha ya dunia, tena walikuwa na nguvu, mali na watoto kuliko nyinyi; basi na nyinyi stareheni na mmezama katika batili kama walivyozama.

Hao zimeporomoka amali zao katika dunia na akhera.

Yaani mema yao yamebatilika, ikiwa wanayo, kama vile kuishi kwa jasho lao. Kubatilika katika akhera ni kutolipwa hayo. Ama kubatilika kwake duniani ni kwamba hilo si chochote kwa makafiri na manafiki mbele za watu wenye mwamko na imani.

Na hao ndio waliopata hasara.

Kwa vile wao wamejichokesha kupanga njama kwa waumini wema, kisha ubaya wa dunia na akhera ukawarudia wao. Kwa ufupi ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaaambia wanafiki waliokuwa wakati wa Mtume(s.a.w.w) . Acheni ukafiri na unafiki na chukueni funzo kwa wale waliokuwa kabla yenu kabla ya kuchukua funzo watakao kuja baada yenu.

Je, hazikuwafikia habari za wale walio kuwa kabla yao, kaumu ya Nuh na Ad na Thamud na kaumu ya Ibrahim na watu wa Madyan na miiji iliyopinduliwa.

Watu wa Madyan ni kaumu ya Shuaib, na wa miji iliyopinduliwa ni kaumu ya Lut.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawakumbusha wanafiki kuhusu watu hawa, kwa sababu miji yao ilikuwa karibu na miji ya waarabu; nao walikuwa na mali nyingi na watoto:

Watu wa Ibrahim waliangamizwa kwa kunyang’a nyangwa neema, wa Adi kwa upepo, wa Nuh kwa gharika, wa Thamud kwa ukelele, na wa Madyan kwa adhabu ya wingu, na wale wa miji iliyopinduliwa ni kwa kupinduliwa juu chini, Yametangulia maelezo ya hayo katika sura ya 7.

Basi Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwadhulumu, lakini wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe kwa kung’anga’ania kwao makosa na dhambi.

وَالْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ يَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَيُطِيعُونَ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ أُولَـٰئِكَ سَيَرْحَمُهُمُ اللَّـهُ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿٧١﴾

71. Na waumini wanaume na waumin wanawake ni mawalii wao kwa wao. Huamrishana mema na kukatazana maovu, Na husimamisha swala, Na hutoa zaka. Na humtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.

وَعَدَ اللَّـهُ الْمُؤْمِنِينَ وَالْمُؤْمِنَاتِ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَمَسَاكِنَ طَيِّبَةً فِي جَنَّاتِ عَدْنٍ وَرِضْوَانٌ مِّنَ اللَّـهِ أَكْبَرُ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿٧٢﴾

72. Amewaahidi Mwenyezi Mungu waumini wanaume na waumin wanawake bustani (Pepo) zipitazo mito chini yake; hali ya kudumu humo na maskani mema katika mabustani ya milele, Na radhi za Mwenyezi Mungu ndizo kubwa zaidi, Huko ndiko kufuzu kukubwa.

NA WAUMIN WANAUME NA WAUMINI WANAWAKE

Aya 71 – 72

MAANA

Na waumini wanaume na waumin wanawake ni mawalii wao kwa wao.

Makusudio ya walii hapa ni kusaidiana. Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja wanafiki na uchafu wao, anawataja waumin kwa fadhila zao; na kwamba wanasaidiana. Yeyote anayedai kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala asimsaidie ndugu yake katika imani hii basi yeye ni mnafiki aliyetajwa na Aya iliyotangulia, iliyowashukiwa wanafiki.

Huamrishana mema na kukatazana maovu Kinyume na wanafiki ambao wanaamrisha maovu na hukataza mema.Na husimamisha swala kiuhakika, sio ria kama wanafiki.

Na hutoa zaka Wala hawafanyi ubakhili kama wanafiki. Na humtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake

Na wanaendelea na utiifu huo vyovyote iwavyo.

Hao Mwenyezi Mungu atawarehemu.

Ama wanafiki amewalaani na kuwaandalia moto wa Jahannam hali ya kudumu humo.

Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hekima.

Mwenye uwezo wa kuwapa nguvu waumini na kuwadhalilisha wanafiki na makafiri.

Amewaahidi Mwenyezi Mungu waumini wanaume na waumin wanawake bustani (Pepo) zipitazo mito chini yake; hali ya kudumu humo na maskani mema katika mabustani ya milele. Na radhi za Mwenyezi Mungu ndizo kubwa zaidi

Kila anayemridhisha Mwenyezi Mungu katika amali zake na makusudio yake, basi Mwenyezi Mungu atamridhia.

Huko ndiko kufuzu kukubwa

Huko ni ishara ya huko kupata bustani na makazi mema. Umetangulia mfano wake katika Juz.(3:15).

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ جَاهِدِ الْكُفَّارَ وَالْمُنَافِقِينَ وَاغْلُظْ عَلَيْهِمْ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿٧٣﴾

73. Ewe Mtume! Pambana na makafiri na wanafiki na uwawekee ngumu. Na makazi yao ni Jahanamu, nayo ni marejeo mabaya.

يَحْلِفُونَ بِاللَّـهِ مَا قَالُوا وَلَقَدْ قَالُوا كَلِمَةَ الْكُفْرِ وَكَفَرُوا بَعْدَ إِسْلَامِهِمْ وَهَمُّوا بِمَا لَمْ يَنَالُوا وَمَا نَقَمُوا إِلَّا أَنْ أَغْنَاهُمُ اللَّـهُ وَرَسُولُهُ مِن فَضْلِهِ فَإِن يَتُوبُوا يَكُ خَيْرًا لَّهُمْ وَإِن يَتَوَلَّوْا يُعَذِّبْهُمُ اللَّـهُ عَذَابًا أَلِيمًا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَمَا لَهُمْ فِي الْأَرْضِ مِن وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ ﴿٧٤﴾

74. Wanaapa kwa Mwenyezi Mungu, hawakusema na hakika wamekwisha sema neno la kufuru, Na wakakufuru baada ya kusilimu kwao, Wakajihimu kufanya wasioyoweza kuyafikia. Na hawakuchukia ila ni kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake amewatajirisha kwa fadhila zake. Wakitubia, itakuwa heri kwao; na kama wakikengeuka, Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu iumizayo duniani na Akhera, Hawana mlinzi katika ardhi wala msaidizi.

SHINDANA NA MAKAFIRI NA WANAFIKI

Aya 73 – 74

MAANA

Ewe Mtume! Pambana na makafiri na wanafiki na uwawekee ngumu. Na makazi yao ni Jahanamu, nayo ni marejeo mabaya.

Mtume(s.a.w.w) aliwachukulia upole wanafiki, lakini haikufaa, bali ndio walimtusi na kumwambia kuwa ni sikio; ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamwamrisha kuwawekea ngumu na kupambana nao, Lakini hakubain- isha aina ya kupambana nao. Je, ni kwa upanga ulimi au kwa njia nyingine. Maana yake ni kuwa Mwenyezi Mungu amemwachia Mtume(s.a.w.w) kukadiria vile hekima na masilahi yanavyotaka.

Wanaapa kwa Mwenyezi Mungu, hawakusema na hakika wamekwisha sema neno la kufuru.

Waliosema ni jamaa katika wanafiki. Kwani wao walitamka neno la kufuru kuhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , Alipowauliza waliogopa, wakaapa. Ndipo Mwenyezi Mungu akawakadhibisha na yakathibiti yale yaliyonasibishwa kwao.

Mwenyezi Mungu, mtukufu hakutaja majina ya walioapa kiapo cha uwon- go wala hilo neno la kufuru walilolitamka ili waislam wasiliabudu kwa kulisoma.

Sheikh Maraghi anasema: “Yamesahihika, yaliyopokewa, kwamba Mtume(s.a.w.w) alipokuwa amelala chini ya kivuli cha mti, alisema: Atawajia mtu atawangalia kwa macho ya shetani, Akija msizungumze naye. Mara akatokea mtu mwenye mandhari ya kiuadui.Mtume akamwita na kumwambia: Kwa nini unanishutumu wewe na sahaba zako? Yule mtu akaondoka na kuleta wenzake; wakaapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa hawakusema. Akateremsha Mwenyezi Mungu Aya hii

Na wakakufuru baada ya kusilimu kwao.

Mfano huu ni kama wa Aya 66 ya Sura hii.

Wakajihimu kufanya wasioyoweza kuyafikia.

katika Tafsir Razi, Bahrul-muhit Al-Manar, Maraghi na nyinginezo imeelezwa kuwa kikundi cha wanafiki kiliafikiana kummaliza Mtume. Mwenyezi Mungu akamfahamisha hilo akajiepusha nalo bila ya kutimia makusudio.

Katika Kitabu Ala’yan, cha Sheikh Muhammad Al-amin, kuna maelezo haya: “Mtume(s.a.w.w) alipokuwa akirudi kutoka Tabuk akielekea Madina, ali- fanyiwa njama na watu katika maswahaba zake, Wakala njama ya kumtupa kutoka katika njia inayopitia juu mlimani, Basi Mtume akapewa habari yao”.

Na hawakuchukia ila ni kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake amewatajirisha kwa fadhila zake.

Dhamiri inawarudia wanafiki, Wengi wao walikuwa katika dhiki ya maisha wakiwa na hali ngumu sana ya ufukara kabla ya kusilimu. Baada ya kutamka tamko la kusilimu kwa midomo yao tu, ziliwamiminikia riziki. Kwa vile Mtume alikuwa akiwagawanyia ngawira sawa na waislam wengine. Vile vile baadhi yao aliwalipia madeni yao.

Malipo yao yakawa ni hayo waliyoyasema na kuazimia kumua. Ndipo Mwenyezi Mungu akawatahayariza, na kukufuru kwao neema, kwa mfumo huu; sawa na kumwambia mtu uliye mfanyia wema kisha akakuudhi “Ubaya wangu ni kukufanyia wema?!”.

Wakitubia, itakuwa heri kwao

Mlango wa toba uko wazi kwa kila mwenye kuubisha. Njia ya kuuendea ni nyepesi sana, kiasi ambacho makafiri na wanafiki hawatakiwi lolote zaidi ya kuomba msamaha kwa yaliyopita na kusadikisha yajayo.

Na kama wakikengeuka, Mwenyezi Mungu atawaadhibu adhabu iumizayo katika duniani na Akhera.

Adhabu yao huko Akhera inajulikana ama adhabu katika dunia ni kwamba wanafiki daima watakuwa katika hofu ya kuwafedheheka na kufichuka.

Kwa ajili hiyo wanaogopa kila kitu na wanadhani kuwa kila neno wanaambiana wao tu; kama alivyowatajia Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kauli yake:

وَإِذَا رَأَيْتَهُمْ تُعْجِبُكَ أَجْسَامُهُمْ وَإِن يَقُولُوا تَسْمَعْ لِقَوْلِهِمْ كَأَنَّهُمْ خُشُبٌ مُّسَنَّدَةٌ يَحْسَبُونَ كُلَّ صَيْحَةٍ عَلَيْهِمْ ﴿٤﴾

“Na ukiwaona miili yao inakupendeza, na wakisema, unasikiliza usemi wao; wao ni kama boriti zilizotegemezwa, wanadhani kila kishindo ni juu yao” (63:4).

Hawana mlinzi katika ardhi wala msaidizi.

Ninani anayeweza kumsaidia au kujaribu kumsaidia ambaye aibu yake na maovu yake yamefichuka kwa watu wote.

وَمِنْهُم مَّنْ عَاهَدَ اللَّـهَ لَئِنْ آتَانَا مِن فَضْلِهِ لَنَصَّدَّقَنَّ وَلَنَكُونَنَّ مِنَ الصَّالِحِينَ ﴿٧٥﴾

75. Na miongoni mwao wako waliomwahidi Mwenyezi Mungu: Akitupa fadhila zake hakika tutatoa sadaka na hakika tutakuwa miongoni mwa watendao wema.

فَلَمَّا آتَاهُم مِّن فَضْلِهِ بَخِلُوا بِهِ وَتَوَلَّوا وَّهُم مُّعْرِضُونَ ﴿٧٦﴾

76. Lakini alipowapa katika fadhila zake, walizifanyia ubakhili wakageuka na huku wakipuuza.

فَأَعْقَبَهُمْ نِفَاقًا فِي قُلُوبِهِمْ إِلَىٰ يَوْمِ يَلْقَوْنَهُ بِمَا أَخْلَفُوا اللَّـهَ مَا وَعَدُوهُ وَبِمَا كَانُوا يَكْذِبُونَ ﴿٧٧﴾

77. Kwa hiyo ukawalipa unafiki katika nyoyo zao mpaka siku ya kukutana nao. Kwa sababu ya kumhalifu Mwenyezi Mungu yale waliyomwahidi na kwa sababu ya kusema kwao uwongo.

أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ سِرَّهُمْ وَنَجْوَاهُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ عَلَّامُ الْغُيُوبِ ﴿٧٨﴾

78. Je,hawajui kwamba Mwenyezi Mungu anajua siri zao na minong’ono yao, na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye sana mambo ya ghaibu.

MIONGONI MWAO WAKO WALIO MWAHIDI MWENYEZI MUNGU

Aya 75 – 78

MAANA

Na miongoni mwao wako waliomwahidi Mwenyezi Mungu: Akitupa fadhila zake hakika tutatoa sadaka na hakika tutakuwa miongoni mwa watendao wema. Lakini alipowapa katika fadhila zake, walizifanyia ubakhili wakageuka na huku wakipuuza

Watu wa Tafsir wamesema kuwa Aya hii ilimshukia mtu mmoja katika Ansar anayeitwa Tha’lab bin Hatib. Alimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) : Niombee kwa Mwenyezi Mungu aniruzuku mali.

Mtume akamwambia: Ee Tha’laba! Kichache unachoweza kishukuria ni bora kuliko kingi usichokiweza. Kwani hupati kiigizo chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu! Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi kwake! Lau ningelitaka jabali linigeukie dhabu na fedha, lingegeuka.

Lakini Tha’laba, hakukinai, akamnaga’ang’ania Mtume na kusema: Naapa kwa ambaye amekupa utume kwa haki! Kama Mungu akiniruzuku mali nitampa kila mwenye haki haki yake. Mtume akasema: Ewe Mola wangu! Mruzuku Tha’alaba mali.

Basi Tha’laba akawa na mbuzi wakazaana kama wadudu, Pakawa pale mjini, hapamtoshi, akahamia nje, Ikawa tena hawezi kuhudhuria Swala ya Jamaa wala ya Ijumaa.

Mtume akamtumia mtu akachuke zaka kwake, akakataa na kufanya ubakhili, akasema. Hii tena ni kama kodi. Mtume akasema: Ole wake Tha’laba, Ndipo zikashuka Aya hizo.

Iwe ni kweli Aya hizi zimeshuka kwa Tha’laba au kwa mwengine, lakini tukio hilo linabainisha kwa ufasaha sana makusudio ya Aya hizi. Tumezungumzia kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 4 (3:143) kifungu cha: ‘Mabadiliko ya hulka na fikra’

Kwa hiyo ukawalipa unafiki katika nyoyo zao mpaka siku ya kukutana nao.

Katika Tafsir Albahrul Muhit kuna maelezo kuwa Hasan, Qatada na Abu Muslim, walisema kuwa dhamir ya ukawalipa inarudia kwenye ubakhili.

Pia kauli hiyo ameichagua Tabrasi na Maraghi. Yaani ubakhili umewalipia unafiki hautaachana nao mpaka siku ya kukutana na malipo ya ubakhili.

Mwenyezi Mungu ametaja sababu mbili za hayo:

1.Kwa sababu ya kumhalifu Mwenyezi Mungu yale waliyomwahidi.

2.Kwa sababu ya kusema kwao uwongo.

Sifa hizi mbili za kuhalifu ahadi na uwongo ni sifa mahsusi za wanafiki zilizoelezwa katika Hadith. Anasema Mtume Mtukufu(s.a.w.w) : “Alama za mnafiki ni tatu: Akizungumza husema uwongo na akiahidi huhalifu na akiaminiwa hufanya hiyana.”

Je, hawajui kwamba Mwenyezi Mungu anajua siri zao na minong’ono yao, na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye sana mambo ya ghaibu.

Siri ni ile iliyo moyoni, na mnong’ono ni maneno ya siri wanayoizungumza wawili au zaidi na ghaibu ni ile wasiyoijua viumbe wote. Maana ni kuwa vipi hawa wanafiki wanathubutu kuficha ukafiri na kuunong’ona? Hawajui kuwa Mwenyezi Mungu anajua yaliyo katika nyoyo zao na yanayozunguka katika ndimi zao, na kwamba halifichiki kwake lolote la kufichika katika ardhi na mbingu?


10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI

الَّذِينَ يَلْمِزُونَ الْمُطَّوِّعِينَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ فِي الصَّدَقَاتِ وَالَّذِينَ لَا يَجِدُونَ إِلَّا جُهْدَهُمْ فَيَسْخَرُونَ مِنْهُمْ سَخِرَ اللَّـهُ مِنْهُمْ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٧٩﴾

79. Wale wanaowabeza waumin wanaotoa sana sadaka na wale wasiopata ila juhudi yao, wakawafanyia maskhara; Mwenyezi Mungu atawafanyia maskhara na wana wao adhabu iumizayo.

اسْتَغْفِرْ لَهُمْ أَوْ لَا تَسْتَغْفِرْ لَهُمْ إِن تَسْتَغْفِرْ لَهُمْ سَبْعِينَ مَرَّةً فَلَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَهُمْ ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْفَاسِقِينَ ﴿٨٠﴾

80. Uwaombee msamaha au usiwombee, hata ukiwaombea msamaha mara sabini Mwenyezi Mungu hatawasamehe, Hayo ni kwa sababu wao wamememkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu mafasiki.

WANAOWABEZA WANAOTOA SADAKA

Aya 79 – 80

MAANA

Wale wanaowabeza waumin wanaotoa sana sadaka.

Bado maneno yako kwa wanafiki. Aya mbili hizi tulizo nazo zinaonyesha aina nyingine ya dhambi zao na maudhi yao kwa Mtume na kwa waumin.

Wakati ambapo Mtume(s.a.w.w) alihimiza kutoa katika njia ya Mwenyezi Mungu na waumini wakamwitikia miongoni mwa sahaba zake; wakawa wengine wanajitolea maelfu na wengine pishi ya tende, kila mtu kwa uwezo wake, basi wanafiki wakawabeza wakamwambia aliyetoa kingi kuwa ni ria, na yule aliyetoa kichache kuwa anajikumbuka yeye tu.

Kawaida ya wanafiki ni kufanya ria kwa wanayoyasema na wanayoyafanya, kwa hiyo wanawakisia wengine vile walivyo wao, Kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu.

Na wale wasiopata ila juhudi yao, inaashiria mafukara waliotoa kichache, kwa vile ndio uwezo wao.

Wakawafanyia maskhara kwa kudharau kile walichokitoa.

Imam Ali(a.s) anasema:Usione haya kutoa kichache, kwani kuzuia ndio uchache zaidi.

Mwenyezi Mungu atawafanyia maskhara na wana wao adhabu iumizayo

Maana ya maskhara ya Muumbaji Mtukufu ni kwamba yeye atawalipa wafanyao maskhara kwa adhabu iumizayo.

Uwaombee msamaha au usiwombee, hata ukiwaombea msamaha mara sabini Mwenyezi Mungu hatawasamehe.

Sabini ni fumbo la wingi. Bado waarabu wanafanya wingi kwa saba na sabini.

Kuna msemaji mmoja aliyesema kuwa: Mwenyezi Mungu ameacha hiyari ya kuzindua kuwaombea msamaha wanafiki au kuacha kuwaombea.

Kwamba au katika Aya ni ya hiyari, kama anavyodai. Lakini huu ni mkanganyo, kwa sababu kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu ‘hatawasamehe’ ni dalili mkataa kwamba hakuna njia ya kuwasamehe wala kuwaghufiria. Kwa hiyo ‘au’ katika Aya, ni ya usawa.

Kuna riwaya isemayo kuwa ilipo shuka Aya ‘wale wanaowabeza,’ wanafiki walimtaka Mtume awatakie msamaha, ndipo Mwenyezi Mungu akataremsha: ‘Uwaombe msamaha au usiwaombee ’ Unaweza kuuliza kuwa Mwenyezi Mungu anapenda wenye kutubia na huwaghufuria dhambi zao vyoyvote zitakvyokuwa kubwa. Sasa kuna siri gani katika kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Hatawasamehe?’ Mwenyezi Mungu (s.w.t) amelijibu swali hili pale aliposema:

Hayo ni kwa sababu wao wamemkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na Mwenyezi Mungu hawaongozi watu mafasiki

Wao walitaka udhuru na wakamtaka Mtume awaombe msamaha, lakini ni kwa unafiki na ria. Ama katika hali yao halisi wao wanaendelea na ukafiri na inadi. Anaowatakabalia Mwenyezi Mungu ni wanaogopa tu, sio wanafiki ambao wanasema wasiyoyafanya.

فَرِحَ الْمُخَلَّفُونَ بِمَقْعَدِهِمْ خِلَافَ رَسُولِ اللَّـهِ وَكَرِهُوا أَن يُجَاهِدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَقَالُوا لَا تَنفِرُوا فِي الْحَرِّ قُلْ نَارُ جَهَنَّمَ أَشَدُّ حَرًّا لَّوْ كَانُوا يَفْقَهُونَ ﴿٨١﴾

81. Walifurahi walioachwa nyuma kwa sababu ya kubakia nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na walichukia kupigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao katika njia ya Mwenyezi Mungu. Wakasema: Msiende katika joto. Sema: Moto wa Jahanamu una joto zaidi lau wangelifahamu.

فَلْيَضْحَكُوا قَلِيلًا وَلْيَبْكُوا كَثِيرًا جَزَاءً بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٨٢﴾

82. Basi nawacheke kidogo na walie sana, ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

فَإِن رَّجَعَكَ اللَّـهُ إِلَىٰ طَائِفَةٍ مِّنْهُمْ فَاسْتَأْذَنُوكَ لِلْخُرُوجِ فَقُل لَّن تَخْرُجُوا مَعِيَ أَبَدًا وَلَن تُقَاتِلُوا مَعِيَ عَدُوًّا إِنَّكُمْ رَضِيتُم بِالْقُعُودِ أَوَّلَ مَرَّةٍ فَاقْعُدُوا مَعَ الْخَالِفِينَ ﴿٨٣﴾

83. Basi Mwenyezi Mungu akikurudisha kwenye kundi miongoni mwao, Na wakakutaka idhini ya kutoka, Sema: Hamtatoka pamoja nami milele, wala hamtapigana na adui pamoja nami. Hakika nyinyi mliridhia kukaa mara ya kwanza, basi kaeni pamoja na watakaobaki nyuma.

WALIFURAHI WALIOACHWA NYUMA

Aya 81 – 83

MAANA

Walifurahi walioachwa nyuma kwa sababu ya kubakia nyuma ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na walichukia kupigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Amesimulia Mwenyezi Mungu (s.w.t), katika Aya zilizotangulia, kauli ya baadhi ya wanafiki kwa Mtume kuwa waruhusiwe kukaa nyuma wasiende kupigana Jihadi. Katika Aya hii anatoa habari ya furaha yao kwa kukaa huko baada ya Mtume; wakachukia kupigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao katika njia ya Mwenyezi Mungu; hasa katika vita vya Tabuk; Kwa sababu Aya ilishuka katika vita hivyo.

Wakasema: Msiende katika joto. Sema: Moto wa Jahanamu una joto zaidi lau wangelifahamu.

Walizihurumia nafsi zao kwa joto la dunia, lakini hawakujihurumia na moto wa Jahanamu ulio na joto zaidi na muda mrefu zaidi. Zaidi ya hayo ni kwamba mwenye kuacha Jihadi dhidhi ya Mataghuti amejivisha nguo ya udhalili duniani. Waarabu hawakupigwa vita ndani ya miji yao ila pale walipozembea na kujidhalilisha; wakaona ni heri wadhalilike kuliko kufa shahidi kulinda heshima yao.

Basi nawacheke kidogo na walie sana, ni malipo ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

Amri ya kucheka na kulia, maana yake ni kutoa habari kwamba wanafiki hata kama wakifurahi kukaa kwao nyuma na Jihadi, lakini furaha hii si chochote kuliganisha na hizaya na udhalili watakaokutana nao katika dunia na huko Akhera ni zaidi.

Basi Mwenyezi Mungu akikurudisha kwenye kundi miongoni mwao.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume. Maana ya kukurudisha ni kukurudisha kutoka vita vya Tabuk hadi Madina. Makusudio ya kundi ni wanafiki na miongoni mwao ni wale waliorudi nyuma kwenye vita vya Tabuk. Kwa sababu baadhi ya hawa walirudi kwa udhuru wa kweli.

Na wakakutaka idhini ya kutoka nawe kwenda kwenye vita au mahali pengine, Sema: Hamtatoka pamoja nami milele, wala hamtapigana na adui pamoja nami.

Walirudi nyuma ya Jihadi ya wajibu ndipo Mwenyezi Mungu akawaadhibu kwa kuwanyima kusuhubiana na Mtume(s.a.w.w) na kutoka naye kwenda vitani au kwengineko. Hii ni mojawapo ya adhabu iliyo kali kwenye nafsi kuliko kuchomwa mshale.

Yatakuja maelezo katika Aya 95, Kisha akabainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) sababu ya kukataza kutoka pamoja na Mtume na kushirikiana nao katika kupigana na adui kwa kauli yake:

Hakika nyinyi mliridhia kukaa mara ya kwanza, basi kaeni pamoja na watakaobaki nyuma.

Walibaki nyuma ya Mtume wakati wa shida, basi hawawezi kukubaliwa baada ya hapo. Na yeyote anayejichagulia utwevu, Mwenyezi Mungu humwacha na alilochagua. Makusudio ya walio baki nyuma ni watoto, vikongwe na wanawake.

وَلَا تُصَلِّ عَلَىٰ أَحَدٍ مِّنْهُم مَّاتَ أَبَدًا وَلَا تَقُمْ عَلَىٰ قَبْرِهِ إِنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَمَاتُوا وَهُمْ فَاسِقُونَ ﴿٨٤﴾

84. Wala usimswalie kamwe yeyote miongoni mwao akifa, wala usisimame kaburini kwake, Hakika wao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakafa wakiwa ni mafasiki.

وَلَا تُعْجِبْكَ أَمْوَالُهُمْ وَأَوْلَادُهُمْ إِنَّمَا يُرِيدُ اللَّـهُ أَن يُعَذِّبَهُم بِهَا فِي الدُّنْيَا وَتَزْهَقَ أَنفُسُهُمْ وَهُمْ كَافِرُونَ ﴿٨٥﴾

85. Wala zisikushangaze mali zao na watoto wao. Hakika Mwenyezi Mungu anataka tu kuwadhibu kwa hayo katika dunia na zitoke nyoyo zao wakiwa ni makafiri.

وَإِذَا أُنزِلَتْ سُورَةٌ أَنْ آمِنُوا بِاللَّـهِ وَجَاهِدُوا مَعَ رَسُولِهِ اسْتَأْذَنَكَ أُولُو الطَّوْلِ مِنْهُمْ وَقَالُوا ذَرْنَا نَكُن مَّعَ الْقَاعِدِينَ ﴿٨٦﴾

86. Na inapoteremeshwa sura kuwa mwaminini Mwenyezi Mungu na piganeni jihadi pamoja na Mtume wake, wanakutaka idhini, wale wenye nguvu miongoni mwao, na husema: Tuache tuwe pamoja na wanaokaa.

رَضُوا بِأَن يَكُونُوا مَعَ الْخَوَالِفِ وَطُبِعَ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَهُمْ لَا يَفْقَهُونَ ﴿٨٧﴾

87. Wameridhia kuwa pamoja na wanaobaki nyuma, Na nyoyo zao zimepigwa muhuri kwa hiyo hawafahamu.

لَـٰكِنِ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ جَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ وَأُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْخَيْرَاتُ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿٨٨﴾

88. Lakini Mtume na wale walioamini pamoja naye walipigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao. Na hao ndio wenye heri; na hao ndio wenye kufaulu.

أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ذَٰلِكَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ ﴿٨٩﴾

89. Mwenyezi Mungu amewaan- dalia Bustan (pepo) zipitazo mito chini yake, hali ya kudu- mu humo; huko ndiko kufuzu kukubwa.

USIMSWALIE YEYOTE MIONGONI MWAO

Aya 84 – 89

SWALA YA MAITI MNAFIKI NA FASIKI

MAANA

Wala usimswalie kamwe yeyote miongoni mwao akifa, wala usisimame kaburini kwake, Hakika wao wamemkataa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakafa wakiwa ni mafasiki.

Maneno anaambiwa Mtume, na makusudio ya miongoni mwao ni wanafiki.

Iilikuwa ni desturi ya Mtume afapo mmoja wa maswahaba zake kumswalia na kusimama makaburini mwake akimwombea msamaha na kuwaambia waliohudhuria muombeeni msamaha mwenzenu na uthabiti, kwa sababu yeye hivi sasa anaulizwa.

Baada ya kushuka Aya hii Mtume(s.a.w.w) alijizuia kuwaswalia wanafiki na kusimama kwenye kaburi zao kuwaombea dua. kwa sababu Aya iko wazi katika kulikataza hilo.

Ama sababu ya katazo hili ni kule kung’angania kwao kumkufuru Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kuendelea hivyo hivyo kung’ang’a- nia ukafiri wao ambao umeelezewa na kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu: ‘Na wakafa wakiwa ni mafasiki.’

Haya ndiyo maana ya dhahiri ya Aya, na yanaambatana nayo masuala haya yafuatayo:

1. Mnaafiki ni fungu katika mafungu ya makafiri, bali yeye hali yake ni mbaya kuliko huyo. Kwa sababu anaficha ukafiri na kudhihirisha Uislamu. Ni kwa ajili hii imekuwa haramu kuswalia jeneza lake. Na kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Wala usimswalie kamwe yeyote katika wao,’ zimeliweka wazi hilo. Iliyoweka wazi zaidi ni ile kauli yake iliyo katika Aya 114 ya sura hii.

Ama fasiki ni katika waislamu kwa sababu yeye anamwamini Mwenyezi Mungu na Mtume kwa dhahiri na batini, lakini yeye anamwasi Mwenyezi Mungu katika hukumu zake. Kwa hiyo ni wajibu kumswalia, haifai kuacha.

Siku moja alinijia ulama kutoka Jabal Amil, tukawa na mazungumzo na majibizano haya:-

Alisema: Nimeitwa kumswalia maiti ninayemjua kuwa ni fasiki, je, itafaa nimswalie?

Nikasema: Bali ni wajibu kifaya kwako, Akasema: Na ufasiki je?

Nikamsomea kauli ya Imam Jaffer Assadiq(a.s) :“Mswalie aliyekufa kati- ka waislamu na hisabu yake iko kwa Mwenyezi Mungu.”

Akasema: Lakini mwenye kuswali ni lazima amwombee dua baada ya Takbira ya nne, na imezoeleka kumwombea kwa kusema: “Ewe Mola wangu sisi hatujui kwake isipokuwa heri” Ikiwa nitasema si nitakuwa mwongo.

Nikwambia: Sema: Ewe Mola wangu sisi tunajua kwake heri, ukusudie Uislamu.

2. Wamehitalifiana wafasiri kwa kutafutiana Riwaya kuwa je, Mtume(s.a.w.w) aliswalia jeneza la kiongozi wa wanafiki Abdallah bin Ubayya?

Kuna kauli tatu katika hilo: Kwanza, kwamba yeye alimswalia kwa kutu- maini kupata waislamu wengi, lakini hiyo ni dhana tu ambayo haifai kuithibitishia au kuifasiria chochote katika vitendo vya Maasum. Ya pili, kwamba hakumswalia.Alitaka kumswalia lakini Jibril akamshika nguo na akamsomea Aya hii, Ya tatu, kwamba yeye hakumswalia. Kuna maelezo katika Majmaul Bayan: “Riwaya nyingi zinasema kuwa yeye hakum- swalia.”

Bora ya niliyoyasoma kuhusu maudhui haya ni maelezo yaliyo katika Tafsiri ya Sheikh Maraghi juu ya kutosihi hadith iliyopokewa na Bukhari na wengineo kuwa mtume alimswalia bin Ubayya, na alipoulizwa, akasema: Mwenyezi Mungu amenihiyarisha kuwaswalia wanafiki, kwa vile yeye amesema: Uwaombee msamaha au usiwaombee.

Kisha akaongezea Maraghi, kwamba maulama wengi wame hukumu kutosihi hadith hii; Kwa sababu Aya ya kukataza kuwaswalia wanafiki ilishuka kabla ya kufa bin Ubaya na ni muhali kwa Mtume Mtukufu (saw) kuhalifu Kitab cha Mwenyezi Mungu. Vile vile ni muhali kusema kuwa Mwenyezi Mungu amenihiyarisha, kwa sababu kauli yake Mwenyezi Mungu hatawasamehe ni dalili mkataa kwamba au hapa si hiyari. Kwa hiyo hadith hiyo yenyewe inajifahamisha kuwa ni uwongo na uzushi kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

3. Tabrasi katika Majamaul Bayan anasema: “Katika Aya hii kuna dalili kwamba kusimama kaburini kuomba dua na ibada iliyowekewa sharia.”

Hakuna faqih yoyote anayepinga kuwa kuwaombea Mungu maiti kunajuzu kisharia sawa na kuwaombea Mungu waliohai, bali kuna haja zaidi kwa waliokufa, maadamu tunaitakidi ufufuo, hisabu na adhabu; wala hakuna tofauti baina ya kuwa dua ni kaburini au pengine.

Ama kuzuru makaburi mafakihi wote wamegongana kuwa inajuzu isipokuwa Maimamu wa Kiwahabi. Sunni wamepokea, katika vitabu vitatu vya Sahih yao, Hadith inayoeeleza waziwazi kujuzu hilo; kama vile Hadith isemayo:“Alizuru Mtume kaburi la mama yake na akasema; Nimemtaka idhini Mola wangu kuzuru kaburi la mama yangu na akanipa idhini, basi yazuru makaburi, kwani yanakumbusha mauti”.

Sahih Muslim sehemu ya pili Juz:1 mlango wa kutaka idhini Mtume(s.a.w.w) kazuru kaburi la mama yake.

Amesema Ibn Hajar al-Asqalani katika Kitab Fathul-Bar Sharhil-Bukhar J3 Mlango wa Ziyara ya Makaburi: “Ametoa Muslim kutoka kwa Mtume (saw) kwamba yeye amesema: Nilikuwa ni kiwakataza kuzuru makaburi, sasa ya zuruni”.

Amezidisha Abu Daud na Nisai, wakiwa ni miongoni mwa wenye sahih, kuwa aliendelea kusema: “…Kwani yanakumbusha Akhera.” Hakim naye akazidisha: “… hulainisha moyo na huliza macho basi msiseme ni mahame…”

Hayo tumeyazungumzia katika Kitab Hadhihi hiyal wahabiyya (Huu ndio uwahabi), kisha tukaweka mlango maalum kwa anuani ya ziyara ya makaburi. Ama hisabu ya makaburi tumeizungumzia kwa ufafanuzi katika Juz: 3 (2:259), Tunaweza huyarudia maudhui haya ikihitajika.

Wala zisikushangaze mali zao na watoto wao. Hakika tu Mwenyezi Mungu anataka kuwadhibu kwa hayo katika dunia na zitoke nyoyo zao wakiwa ni makafiri.

Umetangulia mfano wa Aya hii katika Aya 55 ya Sura hii. Wafasiri wamesema kuwa amerudia Mwenyezi Mungu kwa kusisitiza hadhari ya kuishangaa mali na watoto na kujishughulisha zaidi nao. Lakini tumesema mara nyingi kuwa kukaririka, katika Qur’an, ni jambo la kawaida.

Na inapoteremeshwa sura kuwa mwaminini Mwenyezi Mungu na piganeni jihadi pamoja na Mtume wake, wanakutaka idhini, wale wenye nguvu miongoni mwao, na husema: Tuache tuwe pamoja na wanaokaa.

Wenye nguvu hapa ni wale wenye nguvu na utajiri, nao ni wale mataghuti wapenda anasa ambao wanajiepusha na kila linalogusa masilahi yao kwa mbali au karibu. Na, kumwamini Mwenyezi Mungu maana yake ni kuwa sawa na watu wengine, kupigana jihadi maana yake ni kuwa dhidi ya dhulma na ufisadi; yaani kuwa dhidi yao.

Ikiwa kumwamini Mwenyezi Mungu na kupigana jihadi kunapinga masilahi yao, basi wao ni wa vita wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Lakini sasa wana tatizo, kuwa watakataa vipi na hali wao wanandai kuamini utume wake? Mwisho wakapata ufumbuzi – kutaka idhini ya kukaa, Lakini idhini hii imewafedhehesha na kufichua kufuru yao na unafiki wao na kwamba wao wanajificha kwa jina la Uislam wakihofia nafsi zao.

Wameridhia kuwa pamoja na wanaobaki nyuma, ambao ni vikongwe, watoto na wanawake.

Hilo linatosha kuwa ni utwevu.

Na nyoyo zao zimepigwa muhuri kwa hiyo hawafahamu malengo mengine na tamaa zimepofusha nyoyo zao na haki na kuwazuia kuifuata haki.

Lakini Mtume na wale walioamini pamoja naye walipigana jihadi kwa mali zao na nafsi zao.

Yaani, ikiwa wanafiki watabaki nyuma, basi wako waumini wenye ikhlasi waliosimama na Mtume. Huo ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu katika Juz.6 (6:89).

Na hao ndio wenye heri; na hao ndio wenye kufaulu

Heri na kufaulu duniani na akhera ni natija ya kuwamini Mwenyezi Mungu na kupigana jihadi katika njia ya haki na uadilifu. Wale haihusiki heri na faida kimaada tu, bali ni maada na maana. La kushangaza ni kauli ya mfasiri mmoja anayesema kuwa makusudio ya heri hapa ni Hurilaini, Inaonekana anaelezea jambo analolipenda zaidi.

Mwenyezi Mungu amewaandalia Bustan (pepo) zipitazo mito chini yake, hali ya kudumu humo; huko ndiko kufuzu kukubwa.

Umetangulia mfano wake katika Aya 82 ya Sura hii na Juz. 2 (3:25)

وَجَاءَ الْمُعَذِّرُونَ مِنَ الْأَعْرَابِ لِيُؤْذَنَ لَهُمْ وَقَعَدَ الَّذِينَ كَذَبُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ سَيُصِيبُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِنْهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٩٠﴾

90. Na walikuja wenye kutoa udhuru katika mabedui ili wapewe idhini. Na wakakaa wale waliomwambia uwongo Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Itawafika wale waliokufuru miongoni mwao adhabu iumizayo.

لَّيْسَ عَلَى الضُّعَفَاءِ وَلَا عَلَى الْمَرْضَىٰ وَلَا عَلَى الَّذِينَ لَا يَجِدُونَ مَا يُنفِقُونَ حَرَجٌ إِذَا نَصَحُوا لِلَّـهِ وَرَسُولِهِ مَا عَلَى الْمُحْسِنِينَ مِن سَبِيلٍ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٩١﴾

91. Hapana lawama juu ya waliodhaifu, wala juu ya wagonjwa, wala juu ya wale wasiopata cha kutumia, wakimsafia nia Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hakuna njia (ya kuwalaumu) wanaofanya wema; na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa msamaha mwenye kurehemu.

وَلَا عَلَى الَّذِينَ إِذَا مَا أَتَوْكَ لِتَحْمِلَهُمْ قُلْتَ لَا أَجِدُ مَا أَحْمِلُكُمْ عَلَيْهِ تَوَلَّوا وَّأَعْيُنُهُمْ تَفِيضُ مِنَ الدَّمْعِ حَزَنًا أَلَّا يَجِدُوا مَا يُنفِقُونَ ﴿٩٢﴾

92. Wala (si lawama) juu ya wale waliokujia ili uwachukua ukasema: Sina cha kuwachukukulia; wakarudi hali macho yao yanamiminika machozi kwa huzuni ya kutopata cha kutumia.

إِنَّمَا السَّبِيلُ عَلَى الَّذِينَ يَسْتَأْذِنُونَكَ وَهُمْ أَغْنِيَاءُ رَضُوا بِأَن يَكُونُوا مَعَ الْخَوَالِفِ وَطَبَعَ اللَّـهُ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٩٣﴾

93. Njia (ya kulaumu) iko tu juu ya wale wanaokuomba ruhusa hali wao ni matajiri, wameridhia kuwa pamoja na wanaobaki nyuma. Na Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao; kwa hivyo hawajui.

WALIKUJA WENYE UDHURU

Aya 90-93

MAANA

Na walikuja wenye kutoa udhuru katika mabedui ili wapewe idhini.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kubainisha hali za wanafiki ambao walikuwa Madina, hapa anawaelezea mabedui waliokaa nyuma ya jihadi na kwamba wao ni aina mbili:

Kwanza ni wale waliomwendea Mtume(s.a.w.w) , wakatoa udhuru na kutaka idhini ya kubaki nyuma. Aina hii ndiyo iliyokusudia na kauli hio ya Mwenyezi Mungu mtukufu: “Na walikuja wenye kutoa udhuru....”

Aina ya pili ni wale waliokaa wakiwa wanamwambia uwongo Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Hao wameashiriwa na kauli isemayo:

Na wakakaa wale waliomwambia uwongo Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Kuwagawanya wale waliobaki nyuma kwenye mafungu mawili, wenye udhuru na waongo, kunafahamisha kuwa makusudio ya wenye udhuru ni wale waliobaki nyuma kwa udhuru sahihi. Ndio maana Mwenyezi Mungu akawanyamazia wenye udhuru bila ya kuwatishia na adhabu iumizayo; kama alivyowatisha waongo kwa kauli yake:

Itawafika wale waliokufuru miongoni mwao adhabu iumizayo.

Utauliza : Mfumo wa Aya unataka neno ‘miongoni mwao liondolewe,’ Kwa sababu wanaomuongopea Mwenyezi Mungu na Mtume wake wote ni makafiri, sio baadhi yao.

Jibu : Razi amejibu kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa akijua kwamba baadhi yao wataamini na kuepuka adhabu, ndipo akataja neno miongoni, kufahaamisha baadhi.

Tuonavyo sisi ni kuwa wale waliokaa wakamdanganya Mwenyezi Mungu na Mtume wake wako aina mbili: Miongoni mwao wamo waliotoa udhuru wa uwongo kwa kutaka raha na kuepuka taabu ya jihadi, wakiwa wanamwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa dhahiri na batini. Na hawa sio makafiri bali ni wapuuzaji.

Aina nyingine ni wlae waliotoa udhuru wakiwa wanakanusha utume wa Muhammad(s.a.w.w) kwa ndani, Hawa ndio makafiri wanaostahiki kudumu katika adhabu. Ndipo likaja neno ‘miongoni mwao’ kufahmisha kuwa makafiri waliobaki nyuma kwa kupinga utume, kinyume cha wale waliobaki kwa kupuuza si kwa kukanusha.

Hapana lawama juu ya waliodhaifu, wala juu ya wagonjwa, wala juu ya wale wasiopata cha kutumia.

Mtume(s.a.w.w) alipiga mbiu ya jihadi wakajitokeza waliojitokeza na wengine wakabaki nyuma wakiwemo wanafiki, kama ilivyotangulia kuelezwa na yataaendelea kuelezwa. Vile vile walikuwemo wenye udhuru wa kiuhakika.

Hawa ndio ambao hawana dhambi wala lawama, Wao wako aina tatu:

1. Waliodhaifu wasioweza kupigana kwa uzee au wenye maumbile dhaifu wasioweza kupigana kwa hali yoyote.

2. Wagonjwa. Tofauti ya ugonjwa na udhaifu ni kuwa ugonjwa sio ila ya kimaumbile.

3. Mafukara ambao hawana posha wala mdhamini. Kwani kuweko watu wa hawa ndani ya wapiganaji kunawaletea matatizo ya kufikia lengo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewahalalishia watu hawa watatu kubaki nyuma ya jihadi – wakimsafia nia Mwenyezi Mungu na Mtume wake kuwa wenye ikhlasi katika imani yao wakisimamia majukumu yaliyobaki; kama vile kuulinda mji, kuchunga familia na mali za wapiganaji nk.

Hakuna njia (ya kulaumu) wanaofanya wema, Na Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Kila mwenye kutekeleza wajibu wake wowote kwa ukamilifu, basi huyo ni mfanya wema, katika mtazamo wa Kiislamu. Na kila asiyetekeleza basi ni mwovu. Mwenyezi Mungu amewaondolea jihadi wagonjwa na mafukara, wakitekeleza wajibu mwingine basi hao ni wema, na haifai kwa yeyote kuwalaumu kwa njia yoyote.

Mafakihi wamechukua, kutokana na Aya hii, asili ya kisharia walionyumbua hukumu nyingi. Miongoni mwa hukumu hizo ni hizi zifuatazo:

Mtu akiweka amana mali yake kwa mtu mwingine na mali ile ikaharibika, basi hatalipa, ila ikiwa amezembea au kukusudia kuiharibu.

Hakimu wa Sharia, mwenye masharti kamili, akikosea katika hukumu, basi hakuna chochote kwake, ikiwa alifanya bidii kujua ukweli.

Ikiwa mtu anaona mali ya mwingine inataka kuangamia, akatumia sehemu ya mali ile ili kuukoa sehemu nyingine, basi hatalipa ile aliyoitumia au kuiharibu. Na mengineyo mfano wa hayo Kwa sababu wote hao wanafanya wema na: ‘Hakuna njia ya (kuwalaumu) wanaofanya wema.’

Wala si lawam juu ya wale waliokujia ili uwachukue, ukasema: Sina cha kuwachukulia; wakarudi hali macho yao yanamiminika machozi kwa huzuni ya kutopata cha kutumia.

Wameafikiana wapokezi wa Hadith na wafasiri kwamba Aya hii iliwashukia jamaa katika waislamu waliomjia Mtume(s.a.w.w) akiwa anajiandaa kwa vita vya Tabuk; wakamwambia: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Sisi hatuna chombo cha kusafiria pamoja nawe kwenda kwenye Jihadi, Wakamtaka Mtume(s.a.w.w) awapatie kipando; Mtume akasema sina cha kuwapandishia; wakalia machozi kwa kutoweza kwenda kwenye jihadi na Mtume(s.a.w.w) .

Kisha wafasiri wakatofautiana kuhusu majina ya hawa na idadi yao; lakini hilo halina umuhimu wowote maadamu Aya iko wazi kufahamisha tukio hilo; na wala hakuna aliyelikanusha.

Utauliza kuwa : hawa wanaingia kaitka aina ya mafukara waliodokezwa na kauli yake Mwenyezi Mungu wala juu ya wale wasiopata cha kutumia, Sasa je, kuna faida gani kurudia?

Baadhi ya wafasiri wamejibu kwamba mafukara hawakuwa na chakula wala cha kupanda, na hao waliolia walikuwa na chakula, lakini hawana cha kusafiria. Au huenda ikawa faida ni kutaja ukweli wa waliolia, ikhlasi yao na nafasi yao mbele ya Mwenyezi Mungu .

Vyovyote ilivyo ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameondoa jukumu kwa waliobaki nyuma kwa kushindwa; ni sawa iwe wameshindwa kwa maradhi, kukosa chakula au cha kupanda.

Njia (ya kulaumu) iko tu juu ya wale wanaokutaka idhini hali wao ni matajiri. wameridhia kuwa pamoja na wanaobaki nyuma. Na Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao; kwa hivyo hawajui.

Maana ya Aya hii inaafikiana na madhumuni ya Aya mbili zilizotangulia (86 na 87). Ufupi wa maana yaliyokusudiwa, ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya kuondoa majukumu kwa mafukara na wagonjwa, ameyathibitisha majukumu hayo kwa matajiri walio na afya ambao wanabaki nyuma ya jihadi.

Ni muhali kwa watu hawa kufanya kitu kwa maslahi ya uma na kusaidiana na wenye ikhlas katika jambo ambalo linagusa masilahi yao kwa mbali au karibu. Siku zote wao wako tayari kuiuza dini yao na nchi yao kwa mashetani ikiwa watawapatia faida.

Ndio hivyo, tangu zamani, Wanyonge wanapopambana kwa ujasiri kuondoa dhulma, kwa upande mwingine kunakuwa na matajiri wanaoongoza upinzani dhidi ya mapinduzi, kila wanapopata nafasi; vinginevyo wataficha vichwa vyao vyumbani wakingojea, kwa hamu, balaa liwafike wanapigana jihadi.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA JUZUU YA TISA


YALIYOMO

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI1

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA 1

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA 1

IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED 1

IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU 1

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI 1

MAKOSA YA CHAPA 2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI 3

KHUMS 3

LUGHA 3

MAANA 3

MLIPOKUWA KANDO YA BONDE LILILOKARIBU 6

MAANA 6

MNAPOKUTANA NA JESHI KAZANENI 9

MAANA 9

YANAYOLETA USHINDI 9

JE WAKOMBOZI NI WAHARIBIFU? 12

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI 14

LAU UNGEONA 14

MAANA 14

KANUNI NA HUKUMU KATIKA AMANI NA VITA 17

MAANA 17

NGUVU ZA KUJILINDA NA NGUVU ZA UCHOKOZI 18

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI 22

ANAKUTOSHELEZA MWENYEZI MUNGU 22

MAANA 22

KATEKA 24

MAANA 24

WAHAJIRI NA ANSAR 28

MAANA 28

JINA LA DINI HALINA ATHARI 29

MWISHO WA SURA YA NANE 32

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI 33

KUJITOA 33

MAANA 33

MIEZI MITUKUFU IKIISHA 36

MAANA 36

WANAZIUZA AYA ZA MWENYEZI MUNGU 39

MAANA 39

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI 42

MNADHANI MTAACHWA 42

MAANA 42

KUWANYWESHA MAHUJAJI 44

MAANA 44

MSIWAFANYE BABA ZENU NA NDUGU ZENU MAWALII 45

MAANA 45

MWENYEZI MUNGU AMEWANUSURU 46

KISA CHA HUNAIN 47

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI 50

WASHIRIKINA NI NAJISI 50

MAANA 50

PIGANENI NA WASIOMWAMNI MWENYEZI MUNGU 52

MAANA 52

WALE WANAOKUSANYA DHAHABU NA FEDHA 55

MAANA 55

ABU DHAR NA UJAMAA 56

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI 59

IDADI YA MIEZI 59

MIEZI MIANDAMO NDIYO MIEZI YA KIMAUMBILE 59

MAANA 59

MNANINI MNAPOAMBIWA 62

VITA VYA TABUK 62

MAANA 63

NENDENI MKIWA WAZITO NA MKIWA WEPESI 64

KWENDA WOTE 65

MAANA 65

HAWAKUOMBI RUHUSA AMBAO WANAWAMWAMINI MWENYEZI MUNGU 67

MAANA 67

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI 70

NA MIONGONI MWAO KUNA ANAYESEMA: NIRUHUSU 70

MAANA 70

SADAKA ZA WANAFIKI 72

MAANA 72

WANAPOPEWA HURIDHIA 74

MAANA 74

WANASTAHIKI ZAKA 75

MAANA 75

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI 77

WANASEMA YEYE NI SIKIO TU 77

MAANA 77

WANAOGOPA WANAFIKI 79

MAANA 79

WANAFIKI WANAUME NA WANAWAKE 81

MAANA 81

NA WAUMIN WANAUME NA WAUMINI WANAWAKE 82

MAANA 82

SHINDANA NA MAKAFIRI NA WANAFIKI 83

MAANA 83

MIONGONI MWAO WAKO WALIO MWAHIDI MWENYEZI MUNGU 85

MAANA 85

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI 87

WANAOWABEZA WANAOTOA SADAKA 87

MAANA 87

WALIFURAHI WALIOACHWA NYUMA 88

MAANA 88

USIMSWALIE YEYOTE MIONGONI MWAO 90

SWALA YA MAITI MNAFIKI NA FASIKI 90

MAANA 90

WALIKUJA WENYE UDHURU 93

MAANA 93

SHARTI YA KUCHAPA 96

MWISHO WA JUZUU YA TISA 96

YALIYOMO 97



[1] . Kumbuka m andishi aliandika kitabu hiki katika miaka ya sitini

[2] . Akil bin Abu twalib alisilimu kabla ya vita ya Badr, lakini washirikina walim- lazimisha kwenda vitani kupigana na binamu yake Muhammad (s.a.w.w).

[3] . Kikosi cha tano (fifth column) ni jina linalotumiwa kwa wale wanaofanya ujasusi wakijifanya ni miongoni mwao, Jina hili lilianza kutumiwa katika vita ya Uhispania mnamo mwaka 1936. Emilio Mola, kiongozi aliyekuwa chini ya Franco, alisema: "Nina vikosi vine dhidi ya Madrid kuongeza cha tano kitakachotokea kwao wenyewe." Mwandishi amelitu- mia neno hili hapa, kama lugha ya kufananisha – Mtarjumu.

[4] . Mfunguo Pili, Mfunguo tatu, Mfunguo nne na mfunguo kumi (Rajab).

[5] . Mahuria: walioachwa huru siku ya kutekwa Makka

[6] . Askari wa siri (Fifth Colomn)

[7] . Angalia Kitabu Voltaire cha Gustave Lanson

[8] . Usahali huu na uzito wake, pengine sisi tulio karibu au kwenye msitari wa ikweta (equator) hatuwezi kuhisi sana, lakini katika nchi nyingine tofauti ya usiku na mchana ni kubwa sana, lau isingefuatwa kalenda ya mwezi mwandamo, basi nchi nyingine zingekuwa na usahali daima wa ibada, kama swaumu nk, na nyingine ugumu daima –Mtarjumu.

[9] . Mfunguo pili, mfunguo tatu na mfunguo nne.

[10] . Ieleweke kuwa mtu mweusi si lazima awe mwafrika, hata kwa warabu na wengineo pia kuna weusi –Mtarjumu.

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KUMI Juzuu ١٠

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KUMI

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu
Kurasa: 13