TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KUMI NA MBILI Juzuu 12
Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad MughniyyaQurani tukufu
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI
IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA
IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA
IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED
IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU
UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI
Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.
Kama lilivyo jina la Tafsiri ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo.
Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.
Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.
Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea.
Hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka kwa lugha ya kiswahili hivi karibuni Inshaallah).
Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.
Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasayansi kama kina Enstein, wasanii kama Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.
Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.
Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.
Mwisho : Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.
MAKOSA YA CHAPA
Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa. Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.
Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146). Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.
Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawamal qiyama. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.
Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu Jabal amil 'Makosa ya chapa.'
Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"
Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.
Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa.” Kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.
Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu."
Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).
MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH
1
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI
Mwendelezo Wa Sura Ya Kumi na Moja: Surat Hud
وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ رِزْقُهَا وَيَعْلَمُ مُسْتَقَرَّهَا وَمُسْتَوْدَعَهَا كُلٌّ فِي كِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿٦﴾
6. Na hakuna mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu. Na anajua makao yake na mapitio yake yote yamo katika Kitabu kinachobainisha.
وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ وَكَانَ عَرْشُهُ عَلَى الْمَاءِ لِيَبْلُوَكُمْ أَيُّكُمْ أَحْسَنُ عَمَلًا وَلَئِن قُلْتَ إِنَّكُم مَّبْعُوثُونَ مِن بَعْدِ الْمَوْتِ لَيَقُولَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ هَـٰذَا إِلَّا سِحْرٌ مُّبِينٌ ﴿٧﴾
7. Naye ndiye aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita. Ili awajaribu ni nani miongoni mwenu mzuri zaidi wa vitendo? Na kama ukisema, hakika nyinyi mtafufuliwa baada ya kufa, bila shaka waliokufuru watasema, hayakuwa haya ila ni uchawi ulio wazi.
وَلَئِنْ أَخَّرْنَا عَنْهُمُ الْعَذَابَ إِلَىٰ أُمَّةٍ مَّعْدُودَةٍ لَّيَقُولُنَّ مَا يَحْبِسُهُ أَلَا يَوْمَ يَأْتِيهِمْ لَيْسَ مَصْرُوفًا عَنْهُمْ وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٨﴾
8. Na kama tukiwacheleweshea adhabu mpaka muda uliohisabiwa bila shaka watasema, nini kinachozuia hiyo adhabu? Sikilizeni! Siku itakapowajia basi haitaondolewa kwao. Na yatawazunguka yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.
HAKUNA MNYAMA YOYOTE KATIKA ARDHI
Aya 6 – 8
MAANA
Na hakuna mnyama yoyote katika ardhi ila riziki yake iko kwa Mwenyezi Mungu.
Neno Daabbah, kilugha lina maana ya kila anayetembea ardhini. Na kidesturi lina maana ya mnyama anayepandwa kama vile punda, farasi n.k.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameumba ardhi na akampa kila anayetembea ardhini mahitaji yake yote, kuanzia mdudu, mbu, ndovu, binadamu n.k. Na akampa kila mmoja uwezo wa kuhangaikia riziki yake.
Kwa hiyo maana ya Aya ni kuwa Mwenyezi Mungu amejaalia kwa kila kiumbe hai riziki yake iliyowekwa ardhini. Na wala sio kuwa Mwenyezi Mungu amekadiria riziki mahsus kwa kila kiumbe hai, ambayo haizidi kwa kuihangaikia wala kupungua kwa kuacha kuitafuta, kama wasemavyo wengine! La, Sio hivyo! Mwenye Tafsir Al-Manar anasema: “Baadhi ya watu na washairi wanadai kuwa kuchumma na kuacha kuchumma ni sawa, kama wanavyosema baaadhi ya wajinga wasiojali:
Mekwishapita kalamu bure sijihangaishe
Kuhangaikia riziki ni sawa na kujikalia
Sijitie na wazimu wala sijishughilishe
Alo tumboni mwa mama riziki hujipatia
Mshairi huyu ndiye anayestahiki kuitwa mwenda wazimu wala sio yule anayeihangaikia riziki yake.
Kwa maelezo zaidi unaweza kurudia Juz.6 (5:64) kifungu cha ‘riziki na ufisadi,’ Juz.7 (5:100) kifingu cha ‘je riziki ni bahati au majaaliwa?’ Juz.8 (7: 56) kifungu cha ‘Mwenyezi mungu ameitengeneza vizuri ardhi na binadamu akaiharibu’
Na anajua makao yake na mapitio yake. Yote yamo katika Kitabu kinachobainisha.
Makusudio ya mapitio hapa ni alipokuwa kabla ya kuwa katika tumbo la uzazi na kabla ya kutembea ardhini. Na Kitabu kinachobainisha ni fumbo la kwamba Mwenyezi Mungu anajua vizuri kila kitu. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anayesababisha sababu za kuishi na uhai wa kila mnyama, vyovyote alivyo na atakavyokuwa; Kwa sababu yeye Mwenyezi Mungu ni muweza na Mjuzi wa kila kitu.
Naye ndiye aliyeumba mbingu na ardhi katika siku sita.
Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 8 (7:54)
Na arshi yake ilikuwa juu ya maji.
Makusudio ya arshi (kiti cha enzi) ni utawala na ufalme. Aya inafahamisha kuwa maji yalikuwa kabla ya kuumbwa mbingu na ardhi. Ama yalitoka wapi au yalikuwa vipi, hakuna nukuu ya Aya wala Hadith mutawatir juu ya hilo. Akili peke yake haina ujuzi wa hilo.
Hatuna tafsiri yoyote kuhusu mada ya kwanza iliyoumbiwa ulimwengu, isipokuwa neno lake Mwenyezi Mungu. ‘kuwa ukawa’ atakayekanusha haya tutamsomeya:
لَكُمْ دِينُكُمْ وَلِيَ دِينِ ﴿٦﴾
“Mna dini yenu na mimi nina dini yangu.” (109:6)
Ili awajaribu ni nani miongoni mwenu mzuri zaidi wa vitendo?
Yaani Mwenyezi Mungu ametuleta sisi katika ardhi na akatupatia nishati zilizomo ndani yake, ili awapambanue wale wanaoishi kwa jasho lao na wanaoishi kwa jasho la wenzao. Atawaadhibu hawa kwa kuasi kwao na kuwapa thawabu wale kwa utiifu wao.
Na kama ukisema, hakika nyinyi mtafufuliwa baada ya kufa, bila shaka waliokufuru watasema hayakuwa haya ila ni uchawi ulio wazi.
Aya hii ni kama Aya nyingine miongoni mwa Aya nyingi zinazowaelezea wanaokadhibisha ufufuo; isipokuwa ina tofauti moja tu, kwamba hapa kumeelezwa kukadhibisha kwao kwa kufafanisha ufufuo na uchawi, kuwa ni kuwahadaa watu ili wavutike kumfuata Mtume Muhamad(s.a.w.w) .
Na kama tukiwacheleweshea adhabu mpaka muda uliohisabiwa bila shaka watasema: Nini kinachozuia hiyo adhabu?
Yaani watasema ni kitu gani kinachozuia adhabu isitufikia ikiwa ni kweli?
Sikilizeni! Siku itakapowajia basi haitaondolewa kwao.
Kwa sababu adhabu yake Mwenyezi Mungu haiwezi kuzuiwa na watu wenye makosa.
Na yatawazunguka yale waliyokuwa wakiyafanyia mzaha.
Yaani adhabu itawashukia, kuwa ni malipo ya dharau zao na kutohofia kwao ghadhabu za Mwenyezi Mungu.“Dhambi kubwa ni ile aliyoipuuza mwenye dhambi hiyo” kama asemavyo Imam Ali(a.s) .
Na miongoni mwa kauli zake nyingine ni: “Mtu mwenye dhana nzuri zaidi ya Mwenyezi Mungu ni yule anayemhofia zaidi Mwenyezi Mungu.”
وَلَئِنْ أَذَقْنَا الْإِنسَانَ مِنَّا رَحْمَةً ثُمَّ نَزَعْنَاهَا مِنْهُ إِنَّهُ لَيَئُوسٌ كَفُورٌ ﴿٩﴾
9. Na kama tukimwonjesha mtu rehma inayotoka kwetu, kisha tukamwondolea, hakika yeye hukata tamaa akakufuru.
وَلَئِنْ أَذَقْنَاهُ نَعْمَاءَ بَعْدَ ضَرَّاءَ مَسَّتْهُ لَيَقُولَنَّ ذَهَبَ السَّيِّئَاتُ عَنِّي إِنَّهُ لَفَرِحٌ فَخُورٌ ﴿١٠﴾
10. Na kama tukimwonjesha neema baada ya madhara yaliyompata, bila shaka husema: taabu zimeniondokea. Hakika yeye ndiye mwenye kufurahi sana akijitapa.
إِلَّا الَّذِينَ صَبَرُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَـٰئِكَ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَأَجْرٌ كَبِيرٌ ﴿١١﴾
11. Isipokuwa wale waliosubiri na wakatenda mema, hao watapata msamaha na ujira mkubwa.
KUHUSU MTU
Aya 9 – 11
MAANA
Na kama tukimwonjesha mtu rehma inayotoka kwetu, kisha tukamwondolea, hakika yeye hukata tamaa akakufuru.
Makusudio ya kuonjeshwa hapa ni kupewa. Mtu anaporuzukiwa afya njema, mali inayomtosha na familia nzuri, kisha akapatwa na jambo lolote baya, basi hukata tamaa na kuanza kukufuru na kutokuwa na shukrani hata na neema iliyobakia.
Na kama tukimwonjesha neema baada ya madhara yaliyompata, bila shaka husema, taabu zimeniondokea. Hakika yeye ndiye mwenye kufurahi sana akijitapa.
Akitoka kwenye uzito kwenda kwenye wepesi na kutoka kwenye hofu hadi amani, basi huanza kujisahau.
Tumekwishaeleza mara nyingi kwamba Mwenyezi Mungu anategemezewa yeye matukio yote kwa kuwa yeye ndiye sababu ya kwanza ya mambo, kwamba ndiye muumba wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake.
Hapana budi kudokeza kwamba Qur’ani inamwangalia mtu kulingana na itikadi yake na tabia yake. Anaamini nini na anafanya nini? Mtazamo huu unalazimiana na tabia ya Qur’ani, kama Kitabu cha dini na mwongozo. Ni kwa msingi huu ndipo anapohukumiwa mtu kuwa ni mwema au mwovu.
Na inajulikana kuwa itikadi ambayo Qur’ani inalingania ni kumwamini Mwenyezi Mungu na Mitume yake na siku ya mwisho, na matendo iliyoamrisha ni yale yaliyomo mema.
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَـٰئِكَ هُمْ خَيْرُ الْبَرِيَّةِ ﴿٧﴾
“Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema, hao ndio bora wa viumbe.” (98:7).
Kwa maneno mengine ni kuwa Uislamu unamwelekeza mtu kwenye malengo ambayo anapaswa kushikamana nayo. Kama akiyawacha malengo hayo, basi Qur’ani inamwita mtu huyo kwa majina mabaya; kama vile dhalimu, mwenye hasara, kafiri, mjinga, mwenye kupetuka mipaka, mwenye inadi n.k. Kwa hakika sifa hizi hazielezei tabia ya mtu na umbile lake, isipokuwa ni tafsiri ya tabia yake katika baadhi ya misimamo yake.
Qur’ani inatufahamisha kuwa kila sifa iliyotajwa inaambatana na tukio fulani. Imemsifu mtu kuwa ni mwenye kukata tamaa pale anapopatwa na majanga, mwenye furaha akiwa amejitosheleza na mwenye fazaa akipatwa na madhara. n.k.
Watu wengi, hawaijui hakika hii. Wanadhani kuwa sifa hizi zimekuja katika Qur’ani kuelezea umbile la mtu alivyo, na wakawa wanamsifu nazo mtu kinyume na kinavyoeleza Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Kama ingelikuwa kweli dhana yao hii, basi isingelifaa Mwenyezi Mungu kumwaadhibu kafiri na aliyepetuka mipaka, kwa sababu ni umbile lake kufanya hivyo. Pia kauli yake:
وَلَقَدْ كَرَّمْنَا بَنِي آدَمَ ﴿٧٠﴾
“Na hakika tumewatukuza binadamu.” (17:70),
ingelikuwa ni kuutukuza ukafiri na dhulma. Mwenyezi Mungu ametakata na hayo kabisa.
Kwa hiyo basi makusudio ya mtu katika kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na kama tukimwonjesha mtu”, ni yule asiyemwamini Mwenyezi Mungu au anayemwamini kinadharia tu, sio kimatendo. Kwa sababu anayemwamini kikweli kweli, humtegemea yeye tu, katika hali zote na anamshukuru wakati wa faraja na wa dhiki. Anamwogopa na kumnyenyekea akiwa tajiri na kuwa na subira akiwa fukara. Kwa sababu imani ni nusu mbili: nusu ya hofu na nusu ya kutarajia.
Linalosisitiza kuwa lengo la mtu hapa ni yule tuliyemtaja, ni kauli yake Mwenyezi Mungu moja kwa moja bila kuweko na maneno mengine:
Isipokuwa wale waliosubiri na wakatenda mema, hao watapata msamaha na ujira mkubwa.
Waliofanya subira katika masaibu na madhara kwa kumwamini Mwenyezi Mungu kutumai kupata thawabu na radhi yake na wakatenda mema katika shida na raha. Hiyo ndiyo nembo ya wenye itikadi na msimamo. Kwa sababu itikadi ikituwa kwenye moyo wa mtu, inakuwa kama roho, haimbanduki mpaka kufa.
فَلَعَلَّكَ تَارِكٌ بَعْضَ مَا يُوحَىٰ إِلَيْكَ وَضَائِقٌ بِهِ صَدْرُكَ أَن يَقُولُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ كَنزٌ أَوْ جَاءَ مَعَهُ مَلَكٌ إِنَّمَا أَنتَ نَذِيرٌ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ ﴿١٢﴾
12. Basi pengine utaacha baadhi ya yale uliyopewa wahyi. Na kifua chako kitaona dhiki kwa hayo, kwa sababu wanasema, mbona hakuteremshiwa hazina? au wakaja naye Malaika? Hakika wewe ni muonyaji tu. Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa kila kitu.
أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ قُلْ فَأْتُوا بِعَشْرِ سُوَرٍ مِّثْلِهِ مُفْتَرَيَاتٍ وَادْعُوا مَنِ اسْتَطَعْتُم مِّن دُونِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿١٣﴾
13. Au wanasema ameizua? Sema, basi leteni Sura kumi zilizozuliwa mfano wa hii na waiteni muwawezao badala ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnasema kweli.
فَإِلَّمْ يَسْتَجِيبُوا لَكُمْ فَاعْلَمُوا أَنَّمَا أُنزِلَ بِعِلْمِ اللَّـهِ وَأَن لَّا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ فَهَلْ أَنتُم مُّسْلِمُونَ ﴿١٤﴾
14. Na wasipowaitikia, basi jueni ya kwamba imeteremshwa kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kwamba hapana Mola isipokuwa Yeye, basi je, nyinyi ni Waislamu?
MBONA HAKUTEREMSHIWA HAZINA
Aya 12 – 14
MAANA
Basi pengine utaacha baadhi ya yale uliyopewa wahyi.
Mtume Muhammad(s.a.w.w) alikuwa akiwasomea washirikina Aya za Qur’anii kwa kuwalingania kwenye imani ya umoja na ufufuo. Mara nyingine wakimkejeli na mara nyingine wakitaka aina ya miujiza kwa kukaidi sio kutaka kuongoka. Hali hiyo ilikuwa ikimuuma Mtume Muhammad(s.a.w.w) na kumhuzunisha, ndipo Mola Mtukufu akamwambia, ili kumwondokea huzuni hiyo.
Endelea na mwito wako wala usijali wayasemayo na wayatakayo. Utawafanya nini hao! Je, uwaache wahyi na ufute kwenye Qur’anii yale yasiyowapendeza? Hapana! Wewe huwezi kufanya hivyo. Kwa hiyo basi kwa nini unahuzunika na kujitia jaka moyo?
Haya ndiyo maana ya kauli ya Mwenyezi Mungu. ‘Basi pengine uache baadhi ya yale tuliyokupa wahyi.’ Kwa sababu Mtume ni maasum hawezi na haiwezekani kuacha kitu katika wahyi. Aya inafuatana na kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu.
يَا أَيُّهَا الرَّسُولُ لَا يَحْزُنكَ الَّذِينَ يُسَارِعُونَ فِي الْكُفْرِ ﴿٤١﴾
“Ewe Mtume! Wasikuhuzunishe wanaofanya haraka kukufuru.” Juz.6 (5:41).
Na kifua chako kitaona dhiki kwa hayo, kwa sababu wanasema, mbona hakuteremshiwa hazina au wakaja naye Malaika?
Miongoni mwa mambo waliyoyataka washirikina, kwa Mtume Muhamamad(s.a.w.w) , ni kunyesha mvua ya dhahabu au amjie Malaika ashuhudie utume wake.
Hivi ndivyo wanavyofikiria wenye mali na utajiri tangu zamani na sasa. Wanaamini kwamba cheo ni lazima kiwe kwa wenye mali. Ama mafukara, wao ni wakufuata tu.
Majigambo yao haya yalimsababishia Mtume(s.a.w.w) huzuni, ndipo Mola akamwambia:
Hakika wewe ni muonyaji tu.
Lako ni kufikisha wahyi tu. Usifazahike na upumbavu wa wapumbavu na ujinga wa wajinga.
Na Mwenyezi Mungu ndiye Mlinzi wa kila kitu.
Kauli kwake ni yenye kuhifadhiwa na siri inafichika na kila nafsi ni rahani wa ilichokichumma. Aya hii inaambatana na tuliyo yataja Juz. 8 (6:111) kifungu cha ‘aina ya watu’.
Au wanasema ameizuia? Sema, basi leteni Sura kumi zilizozuliwa mfano wa hii na waiteni muwawezao badala ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnasema kweli.
Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz.1 (2:23).
Na wasipowaitikia, basi jueni ya kwamba imeteremshwa kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kwamba hapana Mola isipokuwa Yeye, basi je, nyinyi ni waislamu?
Wasipowaitikia ni wale wanaoikadhibisha Qur’ani na wasioitikiwa ni Mtume Muhammad(s.a.w.w) na kila mwenye kuulingania Uislam na ‘jueni’ anaambiwa kila mwenye kuikadhibisha Qur’ani wakati wowote na mahali popote alipo.
Maana ni kuwa wajue wanaokadhibisha ambao wameshindwa kuipinga Qur’ani, kwamba hiyo imeteremshwa kwa Mtume Muhammad(s.a.w.w) kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambaye hapana Mola isipokuwa yeye.
Hakuna lililobaki isipokuwa musilimu, kwani upinzani umewashinda. Inatosha kusema kuwa Qur’ani ni muujiza kule kuwa imebakia na thamani yake na utukufu wake pamoja na kuwa umepita muda mrefu.
Na itabakia hivyo ikimvutia kila mwenye kuisoma na mawenye kuisikiliza, mpaka siku ya mwisho. Na hilo ni kwa vile hakika yake ni ya kiutu inayokubaklika kwa kila mwenye akili, vyovyote alivyo.
2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI
مَن كَانَ يُرِيدُ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا وَزِينَتَهَا نُوَفِّ إِلَيْهِمْ أَعْمَالَهُمْ فِيهَا وَهُمْ فِيهَا لَا يُبْخَسُونَ ﴿١٥﴾
15. Wanaotaka maisha ya dunia na pambo lake, tutawalipa humo vitendo vyao kamili na humo hawatapunjwa.
أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَيْسَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ إِلَّا النَّارُ وَحَبِطَ مَا صَنَعُوا فِيهَا وَبَاطِلٌ مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٦﴾
16. Hao ndio ambao katika Akhera hawatakuwa na kitu ispokuwa moto. Na yataharibika waliyokuwa wakiyafanya humo na yatapotea bure waliyokuwa wakiyatenda.
أَفَمَن كَانَ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّهِ وَيَتْلُوهُ شَاهِدٌ مِّنْهُ وَمِن قَبْلِهِ كِتَابُ مُوسَىٰ إِمَامًا وَرَحْمَةً أُولَـٰئِكَ يُؤْمِنُونَ بِهِ وَمَن يَكْفُرْ بِهِ مِنَ الْأَحْزَابِ فَالنَّارُ مَوْعِدُهُ فَلَا تَكُ فِي مِرْيَةٍ مِّنْهُ إِنَّهُ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٧﴾
17. Basi je, aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola wake na anaifuata na shahidi atokaye kwake na kabla yake kulikuwa na Kitabu cha Musa kilichokuwa kiongozi na rehema (atakuwa muongo?) Hao wanamwamini yeye. Na atakayemkataa katika makundi, basi moto ndio miadi yake. Basi usiwe na shaka naye, hakika yeye ni haki itokayo kwa Mola wako. Lakini watu wengi hawaamini.
WANAOTAKA MAPAMBO YA DUNIA
YA 15-17
MAANA
Wanotaka maisha ya dunia na pambo lake, tutawalipa humo vitendo vyao kamili na humo hawatapunjwa.
Atakayepanda atavuna, mwenye kufanya biashara vizuri, atapata faida, mwenye kusoma kwa bidii, atafaulu, mwenye kujenga viwanda, kuchimba visima vya mafuta na madini bila shaka hazina yake itajaa mali na kila mwenye kulifanyia bidii jambo lolote, atapata matunda yake, awe mumin au kafiri.
Riziki huja ikiwa ni natija ya kazi; haipunguzwi na ulafi wala kuzidishwa na imani. Hayo ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Tutawalipa humo vitendo vyao kamili na humo hawatapunjwa.” Hata hivyo ufisadi nao una athari zake; kama tulivyoieleza katika Juz. 6 (5:64).
Neema za maisha ya Akhera zinashikiliwa na kazi ya hapa duniani; sawa na mapambo katika maisha haya. Ni desturi ya Mwenyezi Mungu na hutapata mabadiliko katika desturi ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema:
أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّـهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ ﴿١٤٢﴾
“Je, mnadhani mtaingia Peponi na hali Mwenyezi Mungu haja wajua wale waliofanya jihadi miongoni mwenu na kuwajua wale waliofanya subira?” Juz.4 (3:142).
Amesema tena Mwenyezi Mnungu:
وَمَنْ أَرَادَ الْآخِرَةَ وَسَعَىٰ لَهَا سَعْيَهَا وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَأُولَـٰئِكَ كَانَ سَعْيُهُم مَّشْكُورًا ﴿١٩﴾
“Na anayeitaka Akhera na akaihangaikia inavyotakikana, naye ni mumin, basi hao mahangaiko yao yatakuwa ni yenye kushukuriwa” (17:19)
Mwenye kuhangaikia riziki yake nzuri ya halali, basi atakuwa amehangaikia dunia na Akhera.
Hao ndio ambao katika Akhera hawatakuwa na kitu isipokuwa moto.
Hao ni ishara ya wale waliozama katika dunia wakawa hawajishughulishi na lolote isipokuwa dunia tu. Hawatakuwa na malipo yoyote isipokuwa adhabu.
Na yataharibika waliyokuwa wakiyafanya humo na yatapotea bure waliyokuwa wakiyatenda.
Humo ni duniani. Maana ni kuwa matendo yao si kitu mbele ya Mwenyezi Mungu; hata kama watu watanufaika nayo, maadamu lengo halikuwa la heri ya kiutu. Kwa ufupi, mwenye kutafuta heri yoyote itamfikisha pale anapopataka; mwenye akili hujichagulia njia ya uokovu bila ya kudanganyika na chochote.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumtaja yule anayejishighulisha na dunia tu, amemtaja anayetenda kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kumlin- gania yeye tu, akiwa na dalili itokayo kwa Mola wake. Ufafanuzi ni kama ufuatao:
Basi je, aliye na dalili wazi itokayo kwa Mola wake.
Makusudio ya aliye na dalili wazi ni Muhammad(s.a.w.w) na dalili wazi ni Qur’ani.
Na anaifuata na shahidi atokaye kwake.
Tabari, Razi, Abu Hayan Alaandalusi na wengineo katika wafasiri, wamesema kuwa kuna kutofautiana kuhusu shahidi huyu anayemshuhudia Muhammad na utume wake. Wengine wamesema ni Jibril, wengine ni ulimi wa Muhammad na wengine wakasema ni Ali bin Abutwalib.
Waliosema kuwa ni Ali wametoa dalili kwa Hadith aliyoipokea Bukhari katika Sahih yake, inayosema: “Alisema Mtume(s.a.w.w) kumwambia Ali:Wewe ni katika mimi na mimi ni katika wewe.” Na Umar akasema: Mtume(s.a.w.w) alikufa akiwa yuko radhi naye (Ali).
Na kabla yake kulikuwa na Kitabu cha Musa kilichokuwa kiongozi na rehema (atakuwa muongo?).
Tawrat ilimbashiria Muhammad na utume wake kabla ya kushuhudiwa na Qur’ani. Tawrat ni Kitab cha Mwenyezi Mungu alichomteremshia Musa na ni kiongozi kinachofuatwa katika mambo ya kidini na rehema kwa anayekitumia kabla ya kupotolewa.
Hao wanamwamini yeye.
Yaani yeye Muhammad(s.a.w.w) na hao ni wale wanaofuata dalili za haki na ubainifu wake; kama vile Qur’ani na Kitabu cha Musa jinsi kilivyoteremshwa. Na hao, wanaoashiriwa, hawakutajwa katika Qur’ani, isipokuwa wametajwa kwa sifa zao.
Na atakayemkataa katika makundi, basi moto ndio miadi yake.
Makusudio ya makundi ni yaliyompiga vita Mtume(s.a.w. w ) . Mwenye Tafsir Al-manar na sheikh Al-maraghi, wamesema: “Amesema Muqatil: Hao ni ni ukoo wa Ummayya, ukoo wa Mughira bin Abdallah Al-makhzumi na jamii ya Twalha bin Abdallah na mfano wao katika Mayahudi na manaswara”
Basi usiwe na shaka naye, hakika yeye ni haki itokayo kwa Mola wako.
Dhamir katika usiwe na shaka naye na hakika yeye, inaweza kuwa ni ya Muhammad au ya Qur’ani na msemo wa usiwe, unaelekezwa kwa kila aliyesikia ujumbe wa Muhammad. Maana ni kuwa haitakikani kwa mwenye akili kutia shaka kuwa Muhammad ni mtume na kwamba Qur’ani ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, baada ya kuweko na dalili zilizowazi juu ya hilo.
Ikiwa mtu anaweza kutia shaka kuwa Tawrat na Injil zimetoa bishara ya utume wa Muhammad, je anaweza kutia shaka kwamba Muhammad amewapatia watu njia za maisha na kwamba yeye ameleta ambayo hakuwahi kuwaletea nabii au kiongozi yeyote.
Lakini watu wengi hawaamini haki, kwa sababu hiyo ni adui wa dhulma yao na ufisadi wao katika nchi au kwa kuwa wao hawatilii umuhimu dini ya haki au batil madamu maisha yao hayategemei dini. Sisi tutaachana nao hawa na yale waliyojichagulia; na wao wawaache wengine na yale waliyojichagulia na wasiingilie dini wasiyoijua isipokuwa jina tu.
وَمَنْ أَظْلَمُ مِمَّنِ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا أُولَـٰئِكَ يُعْرَضُونَ عَلَىٰ رَبِّهِمْ وَيَقُولُ الْأَشْهَادُ هَـٰؤُلَاءِ الَّذِينَ كَذَبُوا عَلَىٰ رَبِّهِمْ أَلَا لَعْنَةُ اللَّـهِ عَلَى الظَّالِمِينَ ﴿١٨﴾
18. Ni nani dhalimu mkubwa zaidi kuliko yule amzuliaye Mwenyezi Mungu uongo. Hao watahudhurishwa mbele ya Mola wao. Na watasema mashahidi: Hawa ndio waliomzulia Mola wao uwongo. Sikilizeni! Laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu.
الَّذِينَ يَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَيَبْغُونَهَا عِوَجًا وَهُم بِالْآخِرَةِ هُمْ كَافِرُونَ ﴿١٩﴾
19. Ambao wanazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na wanataka ipotoke na wanaikataa Akhera.
أُولَـٰئِكَ لَمْ يَكُونُوا مُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ وَمَا كَانَ لَهُم مِّن دُونِ اللَّـهِ مِنْ أَوْلِيَاءَ يُضَاعَفُ لَهُمُ الْعَذَابُ مَا كَانُوا يَسْتَطِيعُونَ السَّمْعَ وَمَا كَانُوا يُبْصِرُونَ ﴿٢٠﴾
20. Hao hawataweza kuponyoka katika nchi na wala hawana walinzi badala ya Mwenyezi Mungu. Watazidishiwa adhabu maradufu. Hawakuwa wakiweza kusikia wala hawakuwa wakiona.
أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴿٢١﴾
21. Hao ndio ambao wamezitia hasara nafsi zao. Na yamepotea waliyokuwa wakiyazua.
لَا جَرَمَ أَنَّهُمْ فِي الْآخِرَةِ هُمُ الْأَخْسَرُونَ ﴿٢٢﴾
22. Bila shaka hao ndio wenye hasara zaidi katika Akhera.
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَأَخْبَتُوا إِلَىٰ رَبِّهِمْ أُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢٣﴾
23. Hakika wale walioamini na wakafanya matendo mema na kunyenyekea kwa Mola wao, hao ndio watu wa Peponi, wao watadumu humo.
مَثَلُ الْفَرِيقَيْنِ كَالْأَعْمَىٰ وَالْأَصَمِّ وَالْبَصِيرِ وَالسَّمِيعِ هَلْ يَسْتَوِيَانِ مَثَلًا أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٢٤﴾
24. Mfano wa makundi mawili ni kama kipofu na kiziwi na anayeona na anayesikia. Je, hawa wawili wanaweza kuwa sawa? Je, hamfikiri?
WATAHUDHURISHWA MBELE YA MOLA WAO
Aya 18-24
MAANA
Ni nani dhalimu mkubwa zaidi kuliko yule amzuliaye Mwenyezi Mungu uongo.
Ikiwa kumzulia uongo kiumbe ni kauli mbaya, itakuwaje kwa muumba? Kumzulia uongo Mwenyezi Mungu kuko aina nyingi; kama vile kumfanyia washirika, kuhalalisha na kuharamisha bila ya hoja kutoka Qur’ani au Hadith, wizi na unyang’anyi kwa kisingizio cha demokrasia n.k.
Hao watahudhurishwa mbele ya Mola wao.
Hao ni ishara ya wale wazushi, na kwamba wao kesho watasimama kuhisabiwa; kaulizao na vitendo vyao vitahudhurishwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Na watasema mashahidi: hawa ndio waliomzulia Mola wao uwongo. Sikilizeni! Laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) hahitajii mashahidi, kwa sababu yeye anajua na ni muweza wa kila kitu; anahukumu kwa ujuzi wake na uadilifu wake na kutekeleza kwa neno ‘kuwa.’
Ama ushuhuda wa Malaika na mitume na ushuhuda wa ndimi za waongo waliopotea na mikono yao na miguu yao, lengo lake ni kuzidisha majuto na kwamba wawe na yakini kuwa hawana hoja wala udhuru watakaoukimbilia; hakuna kuepuka laana ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.
Ambao wanazuilia njia ya Mwenyezi Mungu na wanataka ipotoke na wanaikataa Akhera.
Aya hii ni ubainifu na tafsiri ya madhalimu ambao Mwenyezi Mungu amewalaani; kwamba wao wanawazuia watu na tawhid na imani ya ufufuo. Vile vile wanawadanganya kwa shirki na kuikataa siku ya mwisho.
Hao hawataweza kuponyoka katika nchi.
Vipi waweze kufanya hivyo na hali lau Mwenyezi Mungu angelitaka asingeliacha yeyote kwenye ardhi
Na wala hawana walinzi badala ya Mwenyezi Mungu.
Hata masanamu waliyokuwa wakiyafanya mungu na kuyaabudu na pia watawa na wakuu wao waliowafanya waungu hawawezi kufaa kitu.
Watazidishiwa adhabu maradufu.
Hili ni jawabu la swali la kukadiriwa; kama kwamba muulizaji ameuliza wale waliozulia Mwenyezi Mungu uwongo wana hukumu gani? Basi Mwenyezi Mungu akajibu, watazidishiwa adhabu mara mbili.
Kuwa maradufu adhabu hapa ni fumbo la ukali wa adhabu. Wengine wamesema maana yake ni kuwa kila kosa lina adhabu yake: Watadhibiwa kwa uzushi na watadhibiwa kwa kuzuia njia na kupinga ufufuo.
Hawakuwa wakiweza kusikia wala hawakuwa wakiona.
Hii ni sababu ya kufanyiwa adhabu maradufu kwamba Mwenyezi Mungu akiwapa adhabu hii kwa vile walikuwa hawawezi kuisikiliza haki wala kuichunguza, kwa sababu ya kuzama kwao kwenye kufru na inadi.
Hao ndio ambao wamezitia hasara nafsi zao.
Mwenye hasara zaidi katia watu ni yule aliyejihasiri mwenyewe na adhabu isiyokwisha wala kupunguzwa.
Na yamepotea waliyokuwa wakiyazua.
Ambayo ni kumfanyia Mwenyezi Mungu washirika na watetezi, kuhalalisha na kuharamisha kwa uwongo na uzushi.
Bila shaka hao ndio wenye hasara zaidi katika Akhera.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kusema kuwa wao wamezitia hasara nafsi zao, amesisitiza kuwa hasara hii itatokea tu, haina kizuizi wala kuikimbia.
Hakika wale walioamini na wakafanya matendo mema na kun- yenyekea kwa Mola wao, hao ndio watu wa Peponi, wao watadumu humo.
Baada ya Mwenyezi Mungu(s.w.t) kuwataja makafiri, amefuatilia kwa kuwataja wauminii na malipo yao; kama ilivyo desturi ya Qur’ani – kutaja vitu na vinyume vyake.
Neno kunyenyekea hapa limetumika kutokana na neno ‘khibt’ lenye maana ya kunyenyekea na utulivu. Tabrasi anasema: Asili ya neno khibt ni usawa wenye kuenea yaani ardhi iliyo sambamba.
Mfano wa makundi mawili ni kama kipofu na kiziwi na anayeona na anayesikia.
Makundi mawili ni makafiri na waumini. Moja halinufaiki na hisia zake, ambapo kipofu hanufaiki na macho yake na kiziwi hanufaiki na masikio yake; na jingine linanufaika na hisia hizo mbili. Imama Ali (a.s.) anasema: “Mwenye kuzingatia huwa na busara na mwenye busara hufahamu na mwenye kufahamu huwa na elimu.” Ni hivyo hivyo mwenye kusikia.
Je, hawa wawili wanaweza kuwa sawa? Kwa sifa na hali.Je, hamfikiri? Hiyo tofauti?
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ إِنِّي لَكُمْ نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿٢٥﴾
25. Hakika tulimpeleka Nuh kwa watu wake. Hakika: mimi kwenu ni muonyaji abainishaye.
أَن لَّا تَعْبُدُوا إِلَّا اللَّـهَ إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ أَلِيمٍ ﴿٢٦﴾
26. Ya kwamba msiabudu isipokuwa Mwenyezi Mungu. Hakika mimi nawahofia na adhabu ya siku iumizayo.
UJUMBE WA NUH
Aya 25-26
MAANA
Aya mbili hizi zinaelezea kwa ufupi kwamba watu wa Nuh walikuwa wakiabudu masanamu. Inasemekana wao ndio wa kwanza kufanya shirki na kumfanyia Mwenyezi Mungu washirika.
Ndipo Mwenyezi Mungu akawapelekea mtume awape bishara na maonyo.
Basi Nabii Nuh(a.s) akatekeleza risala yake kwa maneno haya mafupi: Mwabuduni Mwenyezi Mungu peke yake wala msimshirikishe na kitu.
Akadhihirisha hurumma yake kwao kwa kuwahofia kupata adhabu ya Mwenyezi Mungu, kama wataendelea na shirk. Huu ndio msingi wa kwanza wa risala ya mitume wote.
فَقَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَوْمِهِ مَا نَرَاكَ إِلَّا بَشَرًا مِّثْلَنَا وَمَا نَرَاكَ اتَّبَعَكَ إِلَّا الَّذِينَ هُمْ أَرَاذِلُنَا بَادِيَ الرَّأْيِ وَمَا نَرَىٰ لَكُمْ عَلَيْنَا مِن فَضْلٍ بَلْ نَظُنُّكُمْ كَاذِبِينَ ﴿٢٧﴾
27. Wakasema wakuu wa wale waliokufuru katika kaumu yake: Hatukuoni ila ni mtu sawa na sisi. Wala hatukuoni wamekufuata ila wale wanaonekana dhahiri kwetu kuwa ni watu duni, wala hatuwaoni kuwa mnayo ziada juu yetu; bali tunawaona kuwa mu waongo.
قَالَ يَا قَوْمِ أَرَأَيْتُمْ إِن كُنتُ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّي وَآتَانِي رَحْمَةً مِّنْ عِندِهِ فَعُمِّيَتْ عَلَيْكُمْ أَنُلْزِمُكُمُوهَا وَأَنتُمْ لَهَا كَارِهُونَ ﴿٢٨﴾
28. Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninayo dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na amenipa rehema kutoka kwake, ikafichikana kwenu, Je, tuwalazimishe na hali nyinyi mnaichukia?
وَيَا قَوْمِ لَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مَالًا إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَى اللَّـهِ وَمَا أَنَا بِطَارِدِ الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّهُم مُّلَاقُو رَبِّهِمْ وَلَـٰكِنِّي أَرَاكُمْ قَوْمًا تَجْهَلُونَ ﴿٢٩﴾
29. Na enyi watu wangu! Siwaombi mali kwa hili. Sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu. Na mimi sitawafukuza wale walioamini, hakika wao watakutana na Mola wao. Lakini mimi nawaona nyinyi ni watu wajinga.
وَيَا قَوْمِ مَن يَنصُرُنِي مِنَ اللَّـهِ إِن طَرَدتُّهُمْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٣٠﴾
30. Na enyi watu wangu! Ni nani atakayenisaidia mbele za Mwenyezi Mungu nikiwafukuza? Basi je, hamfikiri?
وَلَا أَقُولُ لَكُمْ عِندِي خَزَائِنُ اللَّـهِ وَلَا أَعْلَمُ الْغَيْبَ وَلَا أَقُولُ إِنِّي مَلَكٌ وَلَا أَقُولُ لِلَّذِينَ تَزْدَرِي أَعْيُنُكُمْ لَن يُؤْتِيَهُمُ اللَّـهُ خَيْرًا اللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا فِي أَنفُسِهِمْ إِنِّي إِذًا لَّمِنَ الظَّالِمِينَ ﴿٣١﴾
31. Wala siwaambii kuwa nina hazina za Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi ninajua mambo ya ghaibu; wala sisemi kuwa mimi ni Malaika. Wala sisemi yale ambayo yanayadhuru macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri. Mwenyezi Mungu anayajua yaliyo katika nafsi zao. Hapo bila shaka nitakuwa miongoni mwa madhalimu.
NUH NA WATU WAKE
Aya 27-31
MAANA
Wakasema wakuu wa wale waliokufuru katika kaumu yake, hatukuoni ilia ni mtu sawa na sisi.
Nuh alipowalingania watu wake kwenye tawhid walikataa mwito wake, kabla ya kuchunguza uhakika wake. Wakaleta sababu mbili: Ya kwanza, kwamba vipi watamfuata na hali yeye ni mmoja wao? Wao waliangalia msemaji, hawakuangalia yanayosemwa; wakapima haki na watu badala ya kuwapima watu na haki.
Unaweza kuuliza : Hili halihusiki na watu wa Nuh tu, tumewaona watu wengi wamewatukuza wageni kuliko wenyeji; na kuna usemi mashuhuri usemao: ‘msichana wa nyumbani ana sura mbaya,’ sasa kuna ubaya gani?
Jibu : ni kweli kwamba hayo hayahusiki na watu wa Nuh tu na wala Aya haipingi hilo; isipokuwa inawashutumu kwa jambo hilo na hii haiwabakishi watu wengine, wote wanashutumiwa.
Sababu ya pili waliyoisema wapinzaini ni:
Wala hatukuoni wamekufuata ila wale wanaonekana dhahiri kwetu kuwa ni watu duni, wala hatuwaoni kuwa mnayo ziada juu yetu.
Yaani walimwambia Nuh na waumini kuwa vipi tuwafuate na nyinyi hamtuzidi na chochote kihali na kimali; sawa na walivyosema washirikina wa kiqurayash kumwambia Muhammad(s.a.w.w) :
لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ كَنزٌ ﴿١٢﴾
“Mbona hakuteremshiwa hazina” (11:12).
Na wakasema tena:
لَوْلَا نُزِّلَ هَـٰذَا الْقُرْآنُ عَلَىٰ رَجُلٍ مِّنَ الْقَرْيَتَيْنِ عَظِيمٍ ﴿٣١﴾
“Mbona hii Qur’ani haikuteremshwa kwa mtu mkubwa katika miji miwili.” (43:31)
Bali tunawaona kuwa mu waongo , kwa vile nyinyi ni mafukara mlio maskini. Haya ndiyo matamshi ya wenye utajiri kung’ang’nia mali tu, lakini maneno ya kheri na matendo mema kwao ni maneno matupu yasiyokuwa na faida.
Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ninayo dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na amenipa rehema kutoka kwake.
Hili ni jawabu la kauli yao, kuwa vipi tukuamini na wewe ni kama sisi. Maana ya jawabu ni kuwa nifanye nini ikiwa Mwenyezi Mungu amenichagua kutekeleza ujumbe wake na amenihusu mimi na rehema yake? Tena akanipa ubainifu kutoka kwake wa risla hii.
Je, nikatae; nimwambie Mwenyezi Mungu sitaki kutumwa na wewe wala sitafikisha ujumbe wako kwa waja wako. Je, yote hayo niyakatae?
Kwa vile nyinyi hamna akili ndioikafichikana kwenu risala na mmeshindwa kuifahamu.
Je, tuwalazimishe? Yaani tuwalazimishe na ujumbe wangu,na hali nyinyi mnaichukia?
Na enyi watu wangu! Siwaombi mali kwa hili la kuwaonya.
Sina ujira ila kwa Mwenyezi Mungu.
Kwa sababu mwenye kuzungumzia jina la Mwenyezi Mungu, akiwa ni mkweli katika maneno yake, basi hataki malipo kutoka kwa mwenginewe. Na wanaotafuta riziki kwa jina la dini ndio waombao watu mali na sadaka; na ndio wengi siku hizi.
Na mimi sitawafukuza wale walioamini, hakiaka wao watakutana na Mola wao.
Kwa nini niwafukuze? Kwani ufukara ni dhambi kwa Mwenyezi Mungu? Mwenyezi Mungu anajua imani yao kwa vile wao wanamwelekea yeye.
Lakini mimi nawaona ni watu wajinga . Na watu ni maadui wa wasichokijua.
Na enyi watu wangu! Ni nani atakayenisaidia mbele za Mwenyezi Mungu nikiwafukuza?
Je, mnaweza nyinyi au wengine kunikinga na adhabu ya Mwenyezi Mungu.
Basi je, hamfikiri? Vipi atafikiri ambaye haogopi mwisho?
Wala siwaambii kuwa nina hazina za Mwenyezi Mungu; wala kuwa mimi ninajua mambo ya ghaibu; wala sisemi kuwa ni Malaika.
Kauli hii ni ya Nuh(a.s) ikiwa ni ufafanuzi na tafsiri ya kauli yake: “Hakika mimi kwenu ni muonyaji abainishaye” Si lazima muonyaji amiliki mali, ili fukara aonekane mwongo; wala si lazima ajue ghaibu, ili aonekane mwongo yule asiyejua ghaibu; wala pia si lazima awe Malaika ili asiyekuwa Malaika ambiwe wewe si lolote isipokuwa ni mtu.
Wala sisemi yale ambayo yanayadhuru macho yenu kuwa Mwenyezi Mungu hatawapa kheri. Mwenyezi Mungu anayajua yaliyo katika nafsi zao.
Kuna mazoweya ya wenye mali kuona utajiri ndio kipimo cha haki na heri; bali hata wajinga na wapumbavu huona hivyo. Ama mbele ya Mwenyezi Mungu na watu wa Mwenyezi Mungu kipimo ni takua na amali njema na Nuh(a.s) anapima kwa vipimo vya Mwenyezi Mungu. Vipi awaambie waumini kuwa hamtapata heri ya Mwenyezi Mungu; kama walivyoambiwa na mataghut? Ila ikiwa yeye naye ni taghuti kama wao.
Hapo bila shaka nitakuwa miongoni mwa madhalimu.
Kama wale waliomshirikisha Mwenyezi Mungu, wakavikataa vitabu vyake na mitume yake.
3
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI
قَالُوا يَا نُوحُ قَدْ جَادَلْتَنَا فَأَكْثَرْتَ جِدَالَنَا فَأْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٣٢﴾
32. Wakasema: Ewe Nuh! Umejadiliana nasi na umezidisha kutujadili basi tuletee unayotuahidi ukiwa ni miongoni mwa wakweli.
قَالَ إِنَّمَا يَأْتِيكُم بِهِ اللَّـهُ إِن شَاءَ وَمَا أَنتُم بِمُعْجِزِينَ ﴿٣٣﴾
33. Akasema: Mwenyezi Mungu atawaletea akipenda na wala nyinyi si wenye kumshinda.
وَلَا يَنفَعُكُمْ نُصْحِي إِنْ أَرَدتُّ أَنْ أَنصَحَ لَكُمْ إِن كَانَ اللَّـهُ يُرِيدُ أَن يُغْوِيَكُمْ هُوَ رَبُّكُمْ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٣٤﴾
34. Wala nasaha yangu haitawafaa kitu nikitaka kuwapa nasaha ikiwa Mwenyezi Mungu anataka kuwapoteza. Yeye ndiye Mola wenu; na kwake mtarejeshwa.
أَمْ يَقُولُونَ افْتَرَاهُ قُلْ إِنِ افْتَرَيْتُهُ فَعَلَيَّ إِجْرَامِي وَأَنَا بَرِيءٌ مِّمَّا تُجْرِمُونَ ﴿٣٥﴾
35. Au wanasema ameizua? Sema: ikiwa nimeizua, basi kosa hilo ni juu yangu, na mimi sihusiki na makosa myatendayo.
EWE NUH UMEZIDISHA MAJADILIANO NASI
Aya 32-35
MAANA
Wakasema: Ewe Nuh! Umejadiliana nasi na umezidishi kutujadili basi tuletee unayotuahidi ukiwa ni miongoni mwa wakweli.
Nuh(a.s) alipowaziba mdomo watu wake kwa hoja na dalili, walipata dhiki na wakawa hawana pa kutokea, basi wakaona njia pekee, iliyobaki, ya upinzani ni kuomba adhabu.
Walipoiomba, Akasema: Mwenyezi Mungu atawaletea akipenda na wala nyinyi si wenye kumshinda.
Washirikina wa Makka walimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu, kama walivyosema watu wa Nuh. Tazama Juz.9 (8:32).
Wala nasaha yangu haitawafaa kitu nikitaka kuwapa nasaha.
Mwenyezi Mungu alitaka kuwanasihi bali alikithirisha kuwanasihi, lakini kuna faida gani ikiwa nyoyo zimesusuwaa na wala hazipondokei kwenye uongofu,ikiwa Mwenyezi Mungu anataka kuwapoteza.
Mwenyezi Mungu haumbi upotevu kwa mtu. Lau ingelikuwa hivyo basi angekuwa ameuondoa utu wake. Lakini desturi ya Mwenyezi Mungu, katika maumbile yake, imepitisha kuwa mwenye kufuata, njia ya upotevu, kwa matakwa yake, atakuwa katika wapotevu tu. Sawa na na aliyejinyonga kwa hiyari yake.
Ni kwa maana hii ndio ikafaa kunasibishwa upotevu kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t). Yametangulia maelezo katika Juz.11 (10:78) kifungu cha‘uongofu na upotevu’
Yeye ndiye Mola wenu; na kwake mtarejeshwa
Wala hakuna kuhepa kukutana naye, hisabu yake na malipo yake.
Au wanasema ameizua? Sema: ikiwa nimeizua, basi kosa hilo ni juu yangu, na mimi sihusiki na makosa myatendayo.
Dhahiri ya mfumo wa maneno inafahamisha kuwa dhamiri katika ‘wanasema’ inawarudia watu wa Nuh na uliozuliwa ni wahyi; kwa maana ya kuwa: Sema ewe Nuh kuwaambia watu wako: Ikiwa mimi ni mwongo wa ninayoyasema, kama mnavyodai, basi mimi peke yangu ndiye nitakayebeba majukumu na dhambi ni zangu na adhabu. Na ikiwa ninasema kweli, basi nyinyi ndio wenye majukumu, na adhabu ya kukadhibisha itawashukia peke yenu.
Insemekana kuwa Aya ii ni jumla ya maneno iliyoingia kati, katika kisa cha Nuh; na kwamba ilishuka kwa washirikina wa kiquraish, kwa sababu walimtilia shaka Muhammad(s.a.w.w) katika kuwaelezea kisa hiki. Ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha awaambie: Sio lawama lenu uzushi wangu, ni langu mimi peke yangu. Maana haya yenyewe yanafaa, lakini yako mbali na dhahiri ya maneno.
وَأُوحِيَ إِلَىٰ نُوحٍ أَنَّهُ لَن يُؤْمِنَ مِن قَوْمِكَ إِلَّا مَن قَدْ آمَنَ فَلَا تَبْتَئِسْ بِمَا كَانُوا يَفْعَلُونَ ﴿٣٦﴾
36. Akaletewa wahyi Nuh kuwa hataamini katika watu wako isipokuwa yule aliyekwishaamini. Basi usisikitike kwa waliyokuwa wakiyatenda.
وَاصْنَعِ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا وَلَا تُخَاطِبْنِي فِي الَّذِينَ ظَلَمُوا إِنَّهُم مُّغْرَقُونَ ﴿٣٧﴾
37. Na unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa wahyi wetu wala usinizungumzie kuhusu wale waliodhulumu, hakika wao watagharikishwa.
وَيَصْنَعُ الْفُلْكَ وَكُلَّمَا مَرَّ عَلَيْهِ مَلَأٌ مِّن قَوْمِهِ سَخِرُوا مِنْهُ قَالَ إِن تَسْخَرُوا مِنَّا فَإِنَّا نَسْخَرُ مِنكُمْ كَمَا تَسْخَرُونَ ﴿٣٨﴾
38. Na akawa anaunda jahazi na kila wakimpita wakuu wa kaumu yake wakimkejeli. Akasema: Ikiwa nyinyi mnatukejeli, hakika nasi tutawakejeli, kama mnavyotukejeli.
فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ مَن يَأْتِيهِ عَذَابٌ يُخْزِيهِ وَيَحِلُّ عَلَيْهِ عَذَابٌ مُّقِيمٌ ﴿٣٩﴾
39. Mtakuja jua ni nani itakayemfikia adhabu ya kumfedhehesha na itakaye mteremkia adhabu ya kudumu.
AKALETEWA WAHYI NUHU
Aya 36-39
MAANA
Akaletewa wahyi Nuh kuwa hataamini katika watu wako isipokuwa yule aliyekwi shaamini. Basi usisikitike kwa waliyokuwa wakiyatenda.
Mwenyezi Mungu alimpa habari Nuh kwamba kazi yake imekwisha, baada ya kutekeleza ujumbe kwa njia sahihi na kumpa hoja kila mpinzani; na kwamba hakuna yeyote atakayemwitikia baada ya sasa.
Mwenyezi Mungu alimpoza Nuh, kwani alikuwa anaungulika na kuwa na kuwa na huzuni, kwa sababu ya watu wake kuendelea na ushirikina.
Na unda jahazi mbele ya macho yetu na kwa wahyi wetu wala usinizungumzie kuhusu wale waliodhulumu, hakika wao watazamishwa.
Mbele ya macho yetu ni fumbo la kuhifadhi kwake na kuchunga kwake Mwenyezi Mungu. Na makusudio ya wahyi wetu ni amri na maelekezo yake. Baada ya Mwenyezi Mungu kumwamrisha kuunda jahazi, alimkataza kutawasali naye kuhusu wale waliojidhulumu, kwa sababu neno la adhabu limekwisha wathibitikia wote.
Na akawa anaunda jahazi na kila wakimpita wakuu wa kaumu yake wakimkejeli kwa vile anaitengeza kwenye nchi kavu mbali na maji. Walimkejeli na kumcheka kwa vile walikuwa na yakini kuwa hakuna chochote zaidi ya wanavyoona. Hivi ndivyo alivyo mjinga anategemea mambo ya nje tu wala hafikirii vizuri au kuzingatia.
Inasemekana kuwa watu wa Nuh walikuwa hawajui jahazi wala manufaa yake; ndio wakamkejeli na kustaajabu. Lakini ni maarufu kuwa Wafoeniki ndio watu wa mwanzo mwanzo kuunda majahazi.
Abu Hayyan Al-andalusiy, katika tafsir yake, Albahrul muhit, akimnukuu Ibn Abbas, anasema kuwa Nuh alikata mbao za kutengenezea Safina, kutoka katika msitu wa milima ya Lebanon. Hili linafahamisha kwamba, misitu ya mili- ma ya Lebanon, ilikuwa maarufu tangu zamani na kwamba Wafoniki walikuwa wakikata mbao za majahazi yao kwenye msitu huo.
WAUMINI NA WENYE KEJELI
Akasema: Ikiwa nyinyi mnatukejeli, hakika nasi tutawakejeli, kama mnavyotukejeli. Nanyi mtakuja jua ni nani itakayemfikia adhabu ya kumfedhehesha na itakaye mteremkia adhabu ya kudumu.
Hawakujua hakika ya jahazi (Safina) na lengo lake, hawakujua siku zimeficha majanga gani. Hilo likawapelekea dharau na kejeli. Lakini Nuh alikuwa na hakika na alifanyalo, kwamba yeye anafanya kwa uangalizi, kuwa ataokoka yeye na walio pamoja naye na kwamba mwisho wa wenye kejeli ni gharka tu.
Vijana wetu wa leo wanafanana sana na wale waliokufuru katika watu wa Nuh. Wale walikejeli Safina ya Nuh na hawa wanawakejli waumini, wakisema: Mpaka sasa, karne ya ishirini, bado watu wanaswali na kufunga tu; sawa na walivyosema wale makafiri: Jahazi kwenye nchi kavu kusiko na bahari wala maji? Hawakujua siri na hakika ya Safina, wakamkejeli Nuh. Na vijana wa leo hawajui siri ya saum na swala, ndio wanawadharau wafungaji na waswaliina. Je, vijana wanaokejeli dini, watasalimika kupatwa na yaliyowapata watu wa Nuh na Safina yake?
حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَمْرُنَا وَفَارَ التَّنُّورُ قُلْنَا احْمِلْ فِيهَا مِن كُلٍّ زَوْجَيْنِ اثْنَيْنِ وَأَهْلَكَ إِلَّا مَن سَبَقَ عَلَيْهِ الْقَوْلُ وَمَنْ آمَنَ وَمَا آمَنَ مَعَهُ إِلَّا قَلِيلٌ ﴿٤٠﴾
40. Ikawa inakwenda nao katika mawimbi kama milima. Na Nuh akamwita mwanawe naye alikuwa mbali: Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi wala usiwe pamoja na makafiri.
وَقَالَ ارْكَبُوا فِيهَا بِسْمِ اللَّـهِ مَجْرَاهَا وَمُرْسَاهَا إِنَّ رَبِّي لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٤١﴾
41. Na akasema: Pandeni humo kwa Bismillahi, Kwa Jina la Mwenyezi Mungu, kwenda kwake na kusimama kwake. Hakika Mola wangu Mlezi ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
وَهِيَ تَجْرِي بِهِمْ فِي مَوْجٍ كَالْجِبَالِ وَنَادَىٰ نُوحٌ ابْنَهُ وَكَانَ فِي مَعْزِلٍ يَا بُنَيَّ ارْكَب مَّعَنَا وَلَا تَكُن مَّعَ الْكَافِرِينَ ﴿٤٢﴾
42. Ikawa inakwenda nao katika mawimbi kama milima. Na Nuh akamwita mwanawe naye alikuwa mbali: Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi wala usiwe pamoja na makafiri.
قَالَ سَآوِي إِلَىٰ جَبَلٍ يَعْصِمُنِي مِنَ الْمَاءِ قَالَ لَا عَاصِمَ الْيَوْمَ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ إِلَّا مَن رَّحِمَ وَحَالَ بَيْنَهُمَا الْمَوْجُ فَكَانَ مِنَ الْمُغْرَقِينَ ﴿٤٣﴾
43. Akasema: Nitakimbilia mlimani unilinde na maji. Akasema: Leo hapana wa kulindwa na amri ya Mwenyezi Mungu. Na wimbi likaingia kati yao akawa miongoni mwa waliogharikishwa.
وَقِيلَ يَا أَرْضُ ابْلَعِي مَاءَكِ وَيَا سَمَاءُ أَقْلِعِي وَغِيضَ الْمَاءُ وَقُضِيَ الْأَمْرُ وَاسْتَوَتْ عَلَى الْجُودِيِّ وَقِيلَ بُعْدًا لِّلْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٤٤﴾
44. Na ikasemwa: Ewe ardhi! meza maji yako na ewe mbingu! Jizuie. Na maji yakadidimia chini na amri ikapitishwa, na Jahazi ikasimama juu ya Judi. Na ikasemwa: wapotelee mbali watu madhalimu!
MAFURIKO
Aya 40-44
LUGHA
Neno tannur (tanuri) katika lugha ya kiarabu lina maana nyingi; miongoni mwazo ni ardhi, na ndiyo iliyokusudiwa hapa.
MAANA
Hata ilipokuja amri yetu na ikafurika tanuri.
Maana ni kuwa, ilipokuja amri ya Mwenyezi Mungu na maji yakawa yanabubujika kutoka ardhini
Tulisema: Pakia humo wawili wawili, dume na jike kutoka kila aina.
Neno kila linategemea kile kinachoelzewa. Kwa mfano katika kaule yake Mwenyezi Mungu: Nichake kila kitu, inamaanisha kuwa vitu vyote ni vyake. Na kauli yake kuhusu Bilqis:
وَأُوتِيَتْ مِن كُلِّ شَيْءٍ ﴿٢٣﴾
Na amepewa kila kitu, (27:23),
Inahusu vitu vya wakati wake au mji wake. Kwa hiyo basi maana ya kila aina katika Aya hii tuliyonayo ni kiasi kile atakachoweza kukichukua Nuh(a.s) . Katika Safina (jahazi ) miongoni mwa viumbe na wala sio aina yote ya viumbe.
Vinginevyo ingelibidi urefu na upana wa Safina uwe mamia ya maili.
Na watu wako wa nyumbani isipokuwa yule ambaye limempitia neno.
Yaani pakia ndani ya Safina watu wa nyumbani isipokuwa wale ambao tumekukataza kuwachukua.
Wafasiri wanasema kuwa watoto wa Nuh aliowachukuwa ni: Ham, Sam na Yafith. Ama yule ambaye aliandikiwa kuangamia katika watu wake wa nyumbani ni mmoja wa watoto wake ambaye Mwenyezi Mungu amemwashiria kwa kusema: Akawa katika waliozama ambaye inasemekana jina lake ni Kanani.
Mke wa Nuh pia alikuwa ni miongoni mwa waliozama, kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu:
ضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا لِّلَّذِينَ كَفَرُوا امْرَأَتَ نُوحٍ وَامْرَأَتَ لُوطٍ ﴿١٠﴾
“Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa waliokufuru kwa mke wa Nuh na mke wa Lut” (66:10).
Na walioamini; na hawakuamini pamoja naye isipokuwa wachache tu.
Yaani chukua kikundi kidogo cha watu walioamini pamoja nawe.
Na pandeni humo kwa Jina la Mwenyezi Mungu (Bismillah) kuwa ndio kwenda kwake na kuthibiti kwake.
Nuh alifuata amri ya Mwenyezi Mungu, akwaita wauminii katika watu wake wa nyumbani na swahaba zake wapande Safina; na yeye pamoja na waliokuwa naye wasome Bismillah katika kwenda na kutua.
Nimeona baadhi ya tafsir za kisufi wakisema kuwa makusudio ya Safina hapa ni sharia na makusudio ya mawimbi ni hawa za nafsi na matamanio yake. Nikawa najiulza: wametoa wapi masheikh hawa tafsir ya kukiita Kitabu cha Mwenyezi Mungu na ujumbe wake kuwa ni Safina?
Ikawa inakwenda nao katika mawimbi kama milima.
Katika hali hii, inayofanana na kukata roho, Nuh alimwangalia mwanawe kwa masikitiko akimpa mwito wa kumwamini Mungu na kuokoka, kabla ya kuvuta pumzi za mwisho.
Na Nuh akamwita mwanawe naye alikuwa mbali: Ewe mwanangu! Panda pamoja nasi wala usiwe pamoja na makafiri.
Maskini! Hurumma za mzazi, mwanawe akiguswa na shida yoyote naye inamgusa moyoni mwake na rohoni mwake. Nuh alikuwa na uhakika kuwa mwanawe ataangamia ikiwa atang’ang’ania kumshirikisha Mwenyezi Mungu, hivyo akamtaka amwamini Mwenyezi Mungu na apande Safina pamoja nao, lakini hakuna kuokoka kwa mwenye inadi. Upuuzaji wa ujana ukampofusha kujua mwisho mbaya,akasema: Nitakimbilia mlimani unilinde na maji.
Ujinga na ghururi ulimpa picha kuwa tatizo ni maji tu na kwamba ataweza kulitatua tatizo hilo kwa kupanda mlimani; hakujua kwamba hayo ni matakwa ya Mwenyezi Mungu na hasira zake kwa washirikina.
Akasema: Leo hapana wa kulindwa na amri ya Mwenyezi Mungu.
Nuh akamjibu kuwa tatizo sio maji; isipokuwa ni matakwa ya Mwenyezi Mungu ambayo hayana kimbilio. Atakayeokoka ni yule aliyerehemiwa na Mwenyezi Mungu na atakyeangamia ni yule aliyekasirikiwa na Mwenyezi Mungu.
Na wimbi likaingia kati yao akawa miongoni mwa waliogharikishwa.
Wimbi lilikuja katikati ya mazungumzo ya mzazi na mwanawe. Yaliyomfika Nuh(a.s) na mwanawe yanawafika wazazi wengi na watoto wao wanaojifanya wajuaji; kisha mwisho wao unakuwa kama wa mtoto wa Nuh.
Na ikasemwa: Ewe ardhi! meza maji yako na ewe mbingu! Jizuie. Na maji yakadidimia chini na amri ikapitishwa, na Jahazi ikasimama juu ya Judi.
Mwenyezi Mungu aliamrisha ardhi imeze maji na akaamrisha mbingu isimamiishe kumimina na mambo yakaishia kwa kuokoka waumini na kuangamia washirikina. Safina nayo ikatua Judiy mlima uloko Muosal, Lebanon; kama inavyosemekana.
Na ikasemwa: wapotelee mbali watu madhalimu!
Ambao wameikadhibisha haki. Neno ‘potolea mbali’ ni dua ya kuwekwa mbali na rehema. Kama kauli yake Mwenyezi Mungu:
فَسُحْقًا لِّأَصْحَابِ السَّعِيرِ ﴿١١﴾
“ Kuangamia ni kwa watu wa motoni” (67:11).
وَنَادَىٰ نُوحٌ رَّبَّهُ فَقَالَ رَبِّ إِنَّ ابْنِي مِنْ أَهْلِي وَإِنَّ وَعْدَكَ الْحَقُّ وَأَنتَ أَحْكَمُ الْحَاكِمِينَ ﴿٤٥﴾
45. Na Nuh alimwomba Mola wake akasema: Ewe Mola wangu! Hakika mwanangu ni katika watu wangu, na hakika ahadi yako ni haki na wewe ni hakimu bora wa mahakimu wote.
قَالَ يَا نُوحُ إِنَّهُ لَيْسَ مِنْ أَهْلِكَ إِنَّهُ عَمَلٌ غَيْرُ صَالِحٍ فَلَا تَسْأَلْنِ مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ إِنِّي أَعِظُكَ أَن تَكُونَ مِنَ الْجَاهِلِينَ ﴿٤٦﴾
46. Akasema: Ewe Nuh! Huyo si katika watu wako. Hakika yeye ni mwendo usio mwema. Basi usiniombe usilo na ujuzi nalo mimi ninakuwaidhi usije ukawa miongoni mwa wasiojua.
قَالَ رَبِّ إِنِّي أَعُوذُ بِكَ أَنْ أَسْأَلَكَ مَا لَيْسَ لِي بِهِ عِلْمٌ وَإِلَّا تَغْفِرْ لِي وَتَرْحَمْنِي أَكُن مِّنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٤٧﴾
47. Akasema: Ewe Mola wangu! Hakika mimi ninajikinga kwako kukuomba nisilo na ujuzi nalo. Na kama hutanisamehe na kunirehemu nitakuwa katika waliohasirika.
قِيلَ يَا نُوحُ اهْبِطْ بِسَلَامٍ مِّنَّا وَبَرَكَاتٍ عَلَيْكَ وَعَلَىٰ أُمَمٍ مِّمَّن مَّعَكَ وَأُمَمٌ سَنُمَتِّعُهُمْ ثُمَّ يَمَسُّهُم مِّنَّا عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٤٨﴾
48. Ikasemwa: Ewe Nuh! Shuka kwa salama itokayo kwetu na baraka juu yako na juu ya umma zilizo pamoja nawe; na zitakuwepo umma tutakazozistarehesha kisha zishikwe na adhabu chungu itokayo kwetu.
تِلْكَ مِنْ أَنبَاءِ الْغَيْبِ نُوحِيهَا إِلَيْكَ مَا كُنتَ تَعْلَمُهَا أَنتَ وَلَا قَوْمُكَ مِن قَبْلِ هَـٰذَا فَاصْبِرْ إِنَّ الْعَاقِبَةَ لِلْمُتَّقِينَ ﴿٤٩﴾
49. Hizo ni habari za ghaibu tunazokupa wahyi. Hukuwa ukizijua wewe wala watu wako kabla ya hii. Basi subiri! Hakika mwisho ni wa wacha Mungu.
NUHU AKAMWOMBA MOLA WAKE
Aya Ya 45-49
MAANA
Na Nuh alimwomba Mola wake akasema: Ewe Mola wangu! Hakika mwanangu ni katika watu wangu, na hakika ahadi yako ni haki na wewe ni hakimu bora wa mahakimu wote.
Katika Aya ya 40 Mwenyezi Mungu alimwamrisha Nuh kuchukua watu wake wa nyumbani, isipokuwa yule aliyemkataza; na hakumkataza wala kumwamrisha kumchukua mwanawe, bali alinyamaza kwa hekima yake. Nuh akadhani kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawaokoa watu wake wote wa nyumbani, waasi na watiifu.
Ndio maana akamwomba Mola atekeleze ahadi yake kwa mwanawe, kwa sababu ni katika watu wake.
Unaweza kuuliza : Nuh ni mtume na mtume ni maasumu (aliyehifadhiwa na dhambi) itakuwaje adhanie kinyume?
Jibu : Kudhania kinyume hakuharibu isma (kuhifadhiwa na dhambi) ikiwa hakuna kitendo, kwa vile kunafanana na mawazo tu yanayopita kichwani kisha yanaondoka, kama vile hayakuwepo. Hata tukikadiria kuwa maasum amedhania kinyume na hali halisi, basi Mwenyezi Mungu atamfichulia na atamhifadhi na makosa. Hayo tumekwisha yafafanua katika Juz.5 (4:105).
Akasema: Ewe Nuh! Huyo si katika watu wako. Hakika yeye ni mwendo usio mwema.”
Yaani ana mwendo usiokuwa mwema. Mwenyezi Mungu anamwambia Nuh kuhusu mwanawe kuwa nimekuamrisha uchukue watu wako katika Safina ispkokuwa niliokukataza. na yey- ote katika wao niliyekukataza basi ni kwa hekima niliyoipitisha na matakwa yangu yametaka mwanao awe ni miongoni mwa watakaoazama, kwa vile mwendo wake si mzuari. Hakika watu wa Mtume ni wale wema hata kama wako mbali kinasaba na madui zao ni waovu hata kama wako karibu kinasaba.
Maana haya yanatiliwa mkazo na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Hakika watu wanaomkurubia zaidi Ibrahimu ni wale waliomfuata” Juz.3 (3:68).
Na hapo ndipo alipochukua Imam Ali(s.a) kauli yake: “ Hakika mpenzi wa Muhammad ni yule anayemtii Mwenyezi Mungu hata kama yuko mbali naye kidamu na adui wa Muhammad ni yule anaye muasi Mwenyezi Mungu hata kama yuko karibu naye kiudugu”.
Mshairi naye anasema: Mapenzi ya Salmani kwao, udugu walishibana, Lakini Nuh na mwanawe katu hawakuwiyana
Basi usiniombe usilo na ujuzi nalo mimi ninakuwaidhi usije ukawa miongoni mwa wajinga.”
Jambo ambalo hakuwa akilijua Nuh ni alivyopitisha Mwenyezi Mungu tangu mwanzo kuwa mwanawe atakuwa miongoni mwa watakaozama, kwa maslahi fulani; na alipomuomba Mola wake akamwambia usiniombe usilolijua, akasema:
Ewe Mola wangu! Hakika mimi ninajikinga kwako kukuombe nisilo na ujuzi nalo [1] .
Yaani sitakuomba tena kuhusu mototo wangu baada ya kunifahamisha uhakika; bali ninaridhia hukumu yako na ulivyopitisha.
Na kama hutanisamehe na kunirehemu nitakuwa katika waliohasirika.
Hii ni kiasi cha unyeneyekevu wa Nuh tu kwa Mwenyezi Mungu, sio kutubia dhambi iliyofanyika. Ndivyo walivyo Mitume na watu wema. Tumelifafanua hilo katika Juz.4 (4:18) kifungu cha ‘Toba na maumbile.’
Ikasemwa: Ewe Nuh! Shuka kwa Salama itokayo kwetu na baraka nyingi juu yako na juu ya umma zilizo pamoja nawe; na zitakuwepo umma tutakazozistarehesha kisha zishikwe na adhabu chungu itokayo kwetu.
Tufani ilipokwisha na washirikina kuangamia, Mwenyezi Mungu alimwamrisha Nuh ashuke ardhini yeye na wenzake aliokuwa nao kwa salama na baraka za maisha na riziki, waenee huku na huko kisha wazaane na upatikane umma mwingine; kama ilivyokujatokea wakapatikana Ad na Thamud, watastarehe kidogo duniani kisha wakapata adhabu kwa kufru yao na uasi wao.
KIGANO CHA MWEZI 10, MUHARRAM
Kinasema kigano kwamba Nuh alishuka kwenye Safina yake siku ya Ashura(10,Muharram) akafunga kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu. Naye alikuwa amemaliza chakula.
Akachanganya kofi moja la choroko (pojo), kofi moja la adesi na ngano hadi zikawa nafaka saba akazipika, wakala wote mpaka wakashiba. Basi kiganao hiki kikaenea katika miji na watu wakaifanya ni sunna siku ya Ashura.
Hizo ni habari za ghaibu tunazokupa wahyi. Hukuwa ukizijua wewe wala watu wako kabla ya hii. Basi subiri! Hakika mwisho ni wa wacha Mungu.
Msemo unaelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.w) Baada ya Mwenyezi Mungu kumwelezea kisa cha Nuh, alimwambia kuwa kisa hiki ni wahyi, hukukijua wewe wala maquraish. Kwa hiyo nawe vumilia kwa yatakayokupata kutoka kwa watu wako; kama alivyovumilia Nuh. Kama ambavyo mwisho ulikuwa wake na walioamini pamoja naye, basi vilevile mwisho utakuwa wako na waislam. Kwa sababu siku zote mwisho ni wa wenye kusubiri wenye kumcha Mwenyezi Mungu.
TUFANI IMETHIBITI KWA UMA NYINGINEZO
Masimulizi ya Tufani ya Nuh hayahusiki na vitabu vya dini tu. Watafiti wamegundua mabaki ya mbao zinazoashiria kisa hiki na tarehe yake inarudi kwenye mwaka 2100 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa(a.s) .
Wataalamu wengine wasiohusika na dini wamesema kuwa kisa cha Tufani kinajulikana na umma za kale za Wahindi, Wagiriki, Wajapani, Wachina, Wabrazili, watu wa Mexico na wengineo. Wanatofautiana katika masimulizi, lakini wanaafikiana katika madhumuni na kwamaba sababu ilikuwa ni kufuru ya watu na dhulma yao.
4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI
وَإِلَىٰ عَادٍ أَخَاهُمْ هُودًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا مُفْتَرُونَ ﴿٥٠﴾
50. Na kwa A’ad (tulimpeleka) ndugu yao Hud, akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenye Mungu! Nyinyi hamna Mungu isipokuwa yeye tu. Hamkuwa nyinyi isipokuwa ni wazushi.
يَا قَوْمِ لَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ أَجْرًا إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَى الَّذِي فَطَرَنِي أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿٥١﴾
51. Enyi watu wangu! Siwaombi ujira juu ya haya. Haukuwa ujira wangu ila kwa yule aliyeniumba, basi hamtumii akili?
وَيَا قَوْمِ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُم مِّدْرَارًا وَيَزِدْكُمْ قُوَّةً إِلَىٰ قُوَّتِكُمْ وَلَا تَتَوَلَّوْا مُجْرِمِينَ ﴿٥٢﴾
52. Enyi watu wangu! Muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake, atawaletea mbingu zenye mvua tele na atawazidishia nguvu juu ya nguvu zenu. Wala msigeuke kuwa waovu.
قَالُوا يَا هُودُ مَا جِئْتَنَا بِبَيِّنَةٍ وَمَا نَحْنُ بِتَارِكِي آلِهَتِنَا عَن قَوْلِكَ وَمَا نَحْنُ لَكَ بِمُؤْمِنِينَ ﴿٥٣﴾
53. Wakasema: Ewe Hud! Hujatuletea dalili wazi, wala sisi hatuiachi miungu yetu kwa kauli yako na wala sisi hatukuamini wewe.
إِن نَّقُولُ إِلَّا اعْتَرَاكَ بَعْضُ آلِهَتِنَا بِسُوءٍ قَالَ إِنِّي أُشْهِدُ اللَّـهَ وَاشْهَدُوا أَنِّي بَرِيءٌ مِّمَّا تُشْرِكُونَ ﴿٥٤﴾
54. Hatuna la kusema ila baadhi ya miungu yetu imekutia balaa. Akasema: Hakika mimi ninamshuhudisha Mwenyezi Mungu na nyinyi shuhudieni kwamba niko mbali na hao mnaowashirikisha.
مِن دُونِهِ فَكِيدُونِي جَمِيعًا ثُمَّ لَا تُنظِرُونِ ﴿٥٥﴾
55. Mkamwacha Yeye. Basi nyote nifanyieni vitimbi tena msinipe muda.
إِنِّي تَوَكَّلْتُ عَلَى اللَّـهِ رَبِّي وَرَبِّكُم مَّا مِن دَابَّةٍ إِلَّا هُوَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهَا إِنَّ رَبِّي عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٥٦﴾
56. Hakika mimi nimemtegemea Mwenyezi Mungu Mola wangu na Mola wenu. Hakuna mnyama yeyote isipokuwa Yeye amemshika utosi wake. Hakika Mola wangu yuko juu ya njia iliyonyooka.
NA KWA A’AD NDUGU YAO HUD
Aya 50-56
MAANA
Na kwa A’ad (tulimpeleka) ndugu yao Hud, akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenye Mungu! Nyinyi hamna Mungu isipokuwa yeye tu. Hamkuwa nyinyi isipokuwa ni wazushi mnaozusha ibada ya masanamu.
Hud anatokana na kabila la A’ad kinasaba na kinchi, ndio maana Mwenyezi Mungu akamsifu kuwa ni ndugu yao. Ujumbe wake huu ni ujumbe wa mitume wote.
Umetangulia mfano wa Aya hii katika kisa cha Nuh katika Aya 26 ya sura hii, na kisa cha Hud katika Juz.8 (7:65).Na tumetaja ilipo kaburi yake na kwamba yeye ndiye wa kwanza kuzungumza kiarabu; naye ndiye baba wa ya Yaman na Mudhar. Rudia huko.
Enyi watu wangu! Siwaombi ujira juu ya haya. Haukuwa ujira wangu ila kwa yule aliyeniumba, basi hamtumii akili?
Anayefanya kazi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu hataki riziki kutoka kwa mwengine na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anayedhuru na kunufaisha. Tafsiri hii imepita katika Aya 29 ya sura hii.
Enyi watu wangu! Muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake.
Tofauti kati ya kuomba maghufira na kutubia ni: Kuomba maghufira ni kutaka msamaha wa yaliyopita bila ya kuangalia yajayo. Na kutubia ni kuomba msamaha kwa yaliyopita na kuahidi kutofanya tena
Atawaletea mbingu zenye mvua tele na atawazidishi nguvu juu ya nguvu zenu. Wala msigeuke kuwa waovu.
Inaonyesha kuwa wao walikuwa ni watu wa kilimo na mifugo ndio maanaMwenyezi Mungu akawavutia kwenye mvua nyingi; kama ambavyo kauli yake: ‘Atawazidishia nguvu juuu ya nguvu zenu,’ inafahamisha kuwa walikuwa ni watu wenye nguvu za Kiundani na dhahiri (kimaana na kimaada) Hilo linaonyeshwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:
أَلَمْ تَرَ كَيْفَ فَعَلَ رَبُّكَ بِعَادٍ ﴿٦﴾ إِرَمَ ذَاتِ الْعِمَادِ ﴿٧﴾ الَّتِي لَمْ يُخْلَقْ مِثْلُهَا فِي الْبِلَادِ ﴿٨﴾
” Je, hukuona jinsi Mola wako alivyowafanya Aa’d Wairam wenye maguzo marefu. Ambao mfano wao haukuumbwa katika miji” (89:6-8).
Unaweza kuuliza kuwa : Mwenyezi Mungu ameunganisha baina ya imani na kuteremshwa mvua. Utasemaji wewe ulipofasiri Juz. 9 (8:2) ukasema kuwa dini haioteshi ngano na kwamba Mwenyezi Mungu hupitisha mambo kwa desturi ya kimaumbile?
Jibu : Ni kweli kwamba Mwenyezi Mungu anapitisha mambo kulingana na desturi ya kimaumbile, hilo halina shaka. Lakini hilo halizuwii kupatikana muujiza, au kuacha desturi kwa hekima fulani. Ukomo wa desturi zote na maumbile unaishilia kwenye matakwa ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Yeye pekee ndiye msababishaji wa sababu zote. Na matakwa haya matakatifu yanaweza kufungamana na kupatikana kitu moja kwa moja bila ya kupitia sababu yoyote iliyozoeleka; kama Tufani ya Nuh n.k. Mwenyezi Mungu Mtukufu alitaka kutoidhihirisha miujiza hii inayohalifu kawaida, isipokuwa kwa kupatikana mtume, ili kuthibitisha utume wake, kuitikiwa mwito wake au kuwaadhibu maadui zake.
Kwa maneno mengine ni kuwa kupita mambo kwa desturi ni kitu kingine na muujiza ambao unategemea matakwa ya Mwenyezi Mungu ni kitu kingine.
Wakasema: Ewe Hud! Hujatuletea dalili wazi.
Huu ni uongo na uzushi. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) hatumi mjumbe ila humsheheni na hoja za kutosha juu ya utume wake. Watu wa Hud walikataa mwito wake na hoja zake kwa vile zinapingana na hawaa zao; kama ilivyokuwa kwa kaumu nyingine za mitume. Mwenyezi Mungu anasema:
كُلَّمَا جَاءَهُمْ رَسُولٌ بِمَا لَا تَهْوَىٰ أَنفُسُهُمْ فَرِيقًا كَذَّبُوا وَفَرِيقًا يَقْتُلُونَ ﴿٧٠﴾
“Kila alipowafikia Mtume kwa yale zisiyoyapenda nafsi zao kundi moja wakalikadhibisha na kundi jengine wakaliua.”Juz.6 (5:70)
Wala sisi hatuiachi miungu yetu kwa kauli yako.
Mwenye Kitabu Al-Mughni anasema kuwa herufi a’n hapa ni ya sababu; yaani hatuwezi kuacha miungu kwa sababu tu ya kusema kwako iacheni, bila kutuonyesha dalili wala ubainifu
Na wala sisi hatukuamini wewe.
Huu ni ufafanuzi wa kauli yao ya kutoacha miungu yao. Amesema kweli yule aliyesema: Mtu ndiye aliyeumba Miungu wala sio miungu iliyoumba mtu.
Hatuna la kusema ila baadhi ya miungu yetu imekutia balaa.
Kauli yao hii inaonyesha upeo wa ujinga wao na imani yao iliyo kombo ya vigano. Mawe yaliyotulia wanayaamini kuwa yanamdhuru anayesema yasiabudiwe! Mtu akifikia kiwango hiki cha ujinga basi ni wa kuachana naye tu. Ndio maana Mwenyezi Mungu akawasifu kwa uziwi na upofu.
Akasema: Hakika mimi ninamshuhudisha Mwenyezi Mungu na nyinyi shuhudieni kwamba niko mbali na hao mnaowashirikisha. Mkamwacha Yeye basi nyote nifanyieni vitimbi tena msinipe muda.
Walipomwambia kuwa miungu yao imemdhuru, aliwapinga na kuwapa ushindani kuwa wajikusanye wao na waungu wao na wajaribu kila wawezavyo wamdhuru na yeye yuko tayari. Hii maana yake ni kwamba wao wako kwenye mghafala na ni wenye kudanganyika.
Hakika mimi nimemtegemea Mwenyezi Mungu Mola wangu na Mola wenu.
Hii ndio sababu ya kushinda kwao kumdhuru na kuwabeza wao na masanamu yao.
Hakuna mnyama yeyote isipokuwa Yeye amemshika utosi wake.
Yaani hakuna kiumbe chochote ila Mwenyezi Mungu hukiendesha vile atakavyo. Hakuna chochote kinachoweza kujikinga au kujinufahisha hicho chenyewe tu, sikwambii kunufaisha au kudhuru kingine.
Hakika Mola wangu yuko juu ya njia iliyonyooka.
Yeye ndiye anayenusuru na kutweza na anatoa thawabu na kuadhibu kwa msingi wa njia hii iliyonyooka, njia ya haki na uadilifu.
Unaweza kuuliza : Ikiwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye aliyeshika hatamu ya mja na utosi wake, kwa maana ya kumpeleka vile atakavyo; na ikiwa Yeye Mwenyezi Mungu yuko juu ya njia iliyonyooka, hapo patakuwa na mambo mawili:
1. Kuwa mja ni mwenye kuendeshwa hana hiyari; kwa sababu anakokotwa.
2. Kuwa kila mtu yuko juu ya njia iliyonyooka katika vitendo vyake vyote na kauli zake; kwa vile anamfuata; Mungu sawa na mnyama aliyefungwa hatamu anavyomfuata yule mwenye kushika hatamu akiwa kwenye njia nzuri na mnyama naye atakuwa kwenye njia nzuri?
Jibu: Makusudio ya kushika utosi sio kuwa mja hana hiyari katika cho- chote; isipokuwa ni fumbo la uweza wa Mwenyezi Mungu juu ya kila kitu na kwamba Yeye pekee ndiye mwenye kunufaisha. Hiyo ni kuwajibu washirikina ambao wameyapa masanamu uwezo wa kudhuru na kunufaisha.
فَإِن تَوَلَّوْا فَقَدْ أَبْلَغْتُكُم مَّا أُرْسِلْتُ بِهِ إِلَيْكُمْ وَيَسْتَخْلِفُ رَبِّي قَوْمًا غَيْرَكُمْ وَلَا تَضُرُّونَهُ شَيْئًا إِنَّ رَبِّي عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ حَفِيظٌ ﴿٥٧﴾
57. Wakirudi nyuma, basi mimi nimekwishawafikishia niliyotumwa kwenu. Na Mola wangu atawaleta watu wengine badala ya nyinyi. Wala hamumdhuru kitu. Hakika Mola wangu ni mwenye kuhifadhi kila kitu.
وَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا نَجَّيْنَا هُودًا وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ بِرَحْمَةٍ مِّنَّا وَنَجَّيْنَاهُم مِّنْ عَذَابٍ غَلِيظٍ ﴿٥٨﴾
58. Ilipofika amri yetu tulimwokoa Hud na walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu na tukawaokoa na adhabu ngumu.
وَتِلْكَ عَادٌ جَحَدُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ وَعَصَوْا رُسُلَهُ وَاتَّبَعُوا أَمْرَ كُلِّ جَبَّارٍ عَنِيدٍ ﴿٥٩﴾
59. Na hao ndio Aa’d, walikanusha Ishara za Mola wao na wakawaasi mitume wake na wakafuata amri ya kila jabari mwenye inadi.
وَأُتْبِعُوا فِي هَـٰذِهِ الدُّنْيَا لَعْنَةً وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ أَلَا إِنَّ عَادًا كَفَرُوا رَبَّهُمْ أَلَا بُعْدًا لِّعَادٍ قَوْمِ هُودٍ ﴿٦٠﴾
60. Na wakafuatishiwa laana katika dunia hii na siku ya kiyama. Ehee! Hakika Aa’d walimkufuru Mola wao. Ehee! Wamepotelea mbali watu wa Hud.
WAKIRUDI NYUMA
Aya 57-60
MAANA
Wakirudi nyuma, basi mimi nimekwishawafikishia niliyotumwa kwenu bila ya kuchoka wala kuzembea.
Na Mola wangu atawaleta watu wengine badala ya nyinyi baada ya kuwaletea adhabu ya dunia kabla ya Akhera.
Wala hamumdhuru kitu kwa kuacha kwenu imani
Hakika Mola wangu ni mwenye kuhifadhi kila kitu anachunga kila kitu na kukiangalia kwa ujuzi wake na hekima yake. Anasema ibn Arabi katika Futahatul Makkiyya: “Kama ambavyo Mola wako ni mwenye kuhifadhi kila kitu, basi naye ni mwenye kuhifadhika na kila kitu.” Anaashiria kauli ya aliyesema: “Kila kitu kina Aya”
Ilipofika amri yetu tulimwokoa Hud na walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu na tukawaokoa na adhabu ngumu.
Makusudio ya amri yetu ni adhabu yetu, kuokoka kwa kwanza ni kutokana na adhabu ya dunia na kuokoka kwa pili ni kutokana na adhabu ya Akhera.
Imesemekana kuwa kuokoka kwa kwanza ni kubainisha kuokoka na adhabu bila ya kuangalia aina yake na kuokoka kwa pili ni kubainisha aina ya adhabu iliyowashukia watu wa Hud ambayo ilikuwa ni ngumu. Maana zote mbili zinakubali. Yametangulia maelezo ya kuokoka Hud na waliokuwa pamoja naye katika Juz. 8 (7:72).
Na hao ndio Aa’d, walikanusha Ishara za Mola wao na wakawaasi mitume yake na wakafuata amri ya kila jabari mwenye inadi.
Baada ya kuelza kwa ufupi kisa cha Aa’d aliashiria Mwenyezi Mungu, sababu ya kuangamia kwao kwamba ni kumkufuru kwao Mwenyezi Mungu na Ishara zake, kuasi kwao mitume, kuacha kuitetea haki, kuikinga batili na kufuata kwao upotevu na utaghuti.
Mwenyezi Mungu amesema: ‘na wakawaasi mitume’ na wala hakusema na wakamuasi mtume. Kwa sabau mwenye kumwasi mtume mmoja basi ni kama amewaasi wote kwa kuangalia kuwa ujumbe ni mmoja tu, nao ni mwito wa imani ya umoja wa Mungu na ufufuo
Na wakafuatishiwa laana katika dunia hii na siku ya kiyama.
Yaani walifanya yanayowajibisha laana duniani na Akhera. Maana ya laana ni kuwa mbali na kheri. Ndio maana Mwenyezi Mungu akasema:
Ehee! Hakika Aa’d walimkufuru Mola wao. Ehee! Wamepotelea mbali watu wa Hud.
Limekaririka neno ‘Ehe!’ kwa kutilia mkazo na kusisitiza kukanya.
وَإِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ هُوَ أَنشَأَكُم مِّنَ الْأَرْضِ وَاسْتَعْمَرَكُمْ فِيهَا فَاسْتَغْفِرُوهُ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ إِنَّ رَبِّي قَرِيبٌ مُّجِيبٌ ﴿٦١﴾
61. Na kwa Thamud (tulimpeleka) ndugu yao Swaleh, akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenye Mungu! Nyinyi hamna Mungu isipokuwa yeye. Yeye ndiye aliyewaumba kutokana na ardhi na akaifanya iwe koloni lenu. Enyi watu wangu! Muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake. Hakika Mola wangu yuko karibu mwenye kuitikia maombi.
قَالُوا يَا صَالِحُ قَدْ كُنتَ فِينَا مَرْجُوًّا قَبْلَ هَـٰذَا أَتَنْهَانَا أَن نَّعْبُدَ مَا يَعْبُدُ آبَاؤُنَا وَإِنَّنَا لَفِي شَكٍّ مِّمَّا تَدْعُونَا إِلَيْهِ مُرِيبٍ ﴿٦٢﴾
62. Wakasema: Ewe Swaleh! Ulikuwa ukitarajiwa kwetu kabla ya haya. Hivi unatukataza kuabudu waliyokuwa wakiyaabudu mababa zetu? Na sisi tuna shaka na wasiwasi kwa haya unayotuitia.
قَالَ يَا قَوْمِ أَرَأَيْتُمْ إِن كُنتُ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّي وَآتَانِي مِنْهُ رَحْمَةً فَمَن يَنصُرُنِي مِنَ اللَّـهِ إِنْ عَصَيْتُهُ فَمَا تَزِيدُونَنِي غَيْرَ تَخْسِيرٍ ﴿٦٣﴾
63. Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa nina dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na akanipa rehema kutoka kwake, basi ni nani atakayenisaidia kwa Mwenyezi Mungu kama nikimwasi? Basi hapo hamtanizidishia isipokuwa hasara tu.
SWALEH
Aya 61-63
MAANA
Na kwa Thamud (tulimpeleka) ndugu yao Swaleh, akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenye Mungu! Nyinyi hamna Mungu isipokuwa yeye.
Imetangulia Aya hii kwa herufi zake katika Juz. 8 (7:73).
Yeye ndiye aliyewaumba kutokana na ardhi.
Hakuna kitu chochte chenye uhai, kiwe binadamu, mnyama au mmea, ila kitakuwa kimetokana na Ardhi moja kwa moja au kupitia kingine.
Na akaifanya iwe koloni lenu.
Qur’ani Tukufu imelitumia neno hili ukoloni (istimari) kwa maana ya kuamirisha na kuendeleza. Na hii ndiyo maana yake nzuri. Ama hivi leo neno hili linatumika katika dhulma, unyang’anyi na kuwakandamiza wanyonge; na hiyo ndiyo maana mbaya sana. Angalia kifungu cha ‘Mwenyezi Mungu ameitengeneza ardhi na binadamu akaiharibu’ katika Juz. 8 (7:56)
Enyi watu wangu! Muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake.
Hud aliwaambia watu namna hii hii katika Aya 52 ya sura hii. Huko tumeeleza tofauti kati ya kuomba maghufira na kutubia.
Hakika Mola wangu yuko karibu mwenye kuitikia maombi.
Yuko karibu na mwenye kumfanyia ikhlas na mwenye kumwitikia anayeitikia mwito wake.
Wakasema: Ewe Swaleh! Ulikuwa ukitarajiwa kwetu kabla ya haya ya kutukataza kuabudu masanamu. Lakini hivi sasa, baada ya kutukataza hatukuamini tena.
Hivi unatukataza kuabudu waliyokuwa wakiyaabudu mababa zetu?
Vizazi na vizazi wameyaabudu na wakayapelekea madhabihu na hakuna yeyote aliyewahi kuwakataza, je yeye watamkubalia kweli?
Na sisi tuna shaka na wasiwasi kwa haya unayotuitia.
Hii ndiyo mantiki ya kijinga kila mahali na kila wakati. Kila kitu ni desturi yetu na kufuata wazee wetu tu.
Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa nina dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na akanipa rehema kutoka kwake, basi ni nani atakayenisaidia kwa Mwenyezi Mungu kama nikimwasi?
Walimwambia Swaleh kuwa wanashaka naye, naye akawaambia, hebu niambieni nifanyeje ikiwa nina uhakika kwamba Mwenyezi Mungu amenituma kwenu na akaniamrisha niwalinganie kwenye Tawhid; tena akanipa dalili za kutosha juu ya ujumbe huu, je, nimuasi kwa ajili ya kuwaridhisha nyinyi? Na ni nani atakayenikinga na adhabu yake kama nikimwasi?
Basi hapo hamtanizidishia isipokuwa hasara tu.
Kundi la wafasiri wamesema kuwa maana yake ni, nikiwatii mtanifanya nipate hasara. Na wengine wakasema kuwa ni, upinzani wenu haunizidishii chochote isipokuwa ni hasara yenu.
Tuonavyo sisi ni kuwa Swaleh alitaka kuwaambia watu wake lau atawakubalia, basi watamwamini, lakini yeye hatapata radhi ya Mwenyezi Mungu.
وَيَا قَوْمِ هَـٰذِهِ نَاقَةُ اللَّـهِ لَكُمْ آيَةً فَذَرُوهَا تَأْكُلْ فِي أَرْضِ اللَّـهِ وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابٌ قَرِيبٌ ﴿٦٤﴾
64. Enyi watu wangu! Huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu, ni ishara kwenu, basi mwacheni ale katia ardhi ya Mwenyezi Mungu; wala msimguse kwa ubaya isije ikawaangamiza adhabu iliyo karibu.
فَعَقَرُوهَا فَقَالَ تَمَتَّعُوا فِي دَارِكُمْ ثَلَاثَةَ أَيَّامٍ ذَٰلِكَ وَعْدٌ غَيْرُ مَكْذُوبٍ ﴿٦٥﴾
65. Wakamchinja. Basi (Swaleh) akasema: Stareheni katika mji wenu kwa siku tatu. Hiyo ni ahadi isiyokadhibishwa.
فَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا نَجَّيْنَا صَالِحًا وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ بِرَحْمَةٍ مِّنَّا وَمِنْ خِزْيِ يَوْمِئِذٍ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ الْقَوِيُّ الْعَزِيزُ ﴿٦٦﴾
66. Ilipofika amri yetu tulimwokoa Swaleh na walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu kutokana na hizaya ya siku hiyo. Hakika Mola wako ni mwenye nguvu, mwenye kushinda.
وَأَخَذَ الَّذِينَ ظَلَمُوا الصَّيْحَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دِيَارِهِمْ جَاثِمِينَ ﴿٦٧﴾
67. Na ukelele ukawaangamiza wale waliodhulumu, wakapambaukiwa wameanguka kifudifudi katika majumba yao.
كَأَن لَّمْ يَغْنَوْا فِيهَا أَلَا إِنَّ ثَمُودَ كَفَرُوا رَبَّهُمْ أَلَا بُعْدًا لِّثَمُودَ ﴿٦٨﴾
68. Kama kwamba hawakuwemo humo. Ehee! Hakika Thamud walimkufuru Mola wao. Ehee! Thamud wamepotelea mbali.
NGAMIA WA MWENYEZI MUNGU
Aya 64-68
MAANA
Enyi watu wangu! Huyu ngamia wa Mwenyezi Mungu, ni ishara kwenu, basi mwacheni ale katia ardhi ya Mwenyezi Mungu; wala msimguse kwa ubaya isije ikawaangamiza adhabu iliyo karibu.
Imekwishatangulia tafsiri yake katika Juz.8 (7:73).
Wakamchinja. Basi Swaleh akasema: Stareheni katika mji wenu kwa siku tatu. Hiyo ni ahadi isiyokadhibishwa.
Swaleh(a.s) aliwaamrisha waachane naye ngamia, lakini wakamchinja, basi akawaonya kushukiwa na ahabu kwa muda wa siku tatu.
Ibn Abbas anasema kuwa Mungu aliwapa muda huu kuwahimiza imani na kutubia, lakini wao waling’ang’ania ukafiri wao, kwa sababu hawakumwamini Swaleh na ahadi yake.
Ilipofika amri yetu tulimwokoa Swaleh na walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu kutokana na hizaya ya siku hiyo. Hakika Mola wako ni mwenye nguvu mwenye kushinda.
Baada ya siku tatu, ilishuka adhabu, wakaokoka wauminii na wakaangamia makafiri, baada ya kuwasimamia hoja. Huu ndio mwisho wa kila mwenye kuzama katika upotevu na ufisadi.
Na ukelele ukawaangamiza wale waliodhulumu, wakapambaukiwa wameanguka kifudifudi katika majumba yao.
Hapa amesema ukulele ukawaangamiza na katika Juz.8 (7:78) amesema na mtetemeko ukawaangamiza. Maana ni kuwa ukelele ulileta mtetemeko na hofu katika nyoyo zao.
Kama kwamba hawakuwemo humo. Ehee! Hakika Thamud walimkufuru Mola wao. Ehee! Thamud wamepotelea mbali.
Yani jinsi walivyoondoka haraka ni kama kwamba hawakukaa majumbani mwao, na wala hawakuzifaidi mali zao na watoto wao.
Hawakuicheka dunia bali imewacheka wao. Mwenye akili ni yule anayepata somo kutokana na mwengine.
وَلَقَدْ جَاءَتْ رُسُلُنَا إِبْرَاهِيمَ بِالْبُشْرَىٰ قَالُوا سَلَامًا قَالَ سَلَامٌ فَمَا لَبِثَ أَن جَاءَ بِعِجْلٍ حَنِيذٍ ﴿٦٩﴾
69. Na wajumbe wetu walimjia Ibrahim na bishara, wakasema: Salaam! Naye akasema: Salaam! Hakukaa ila akaleta ndama aliyeokwa.
فَلَمَّا رَأَىٰ أَيْدِيَهُمْ لَا تَصِلُ إِلَيْهِ نَكِرَهُمْ وَأَوْجَسَ مِنْهُمْ خِيفَةً قَالُوا لَا تَخَفْ إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَىٰ قَوْمِ لُوطٍ ﴿٧٠﴾
70. Alipoona mikono yao hamfikii, aliwatilia shaka na akawahofia. Wakasem: usiogope! Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya Lut.
وَامْرَأَتُهُ قَائِمَةٌ فَضَحِكَتْ فَبَشَّرْنَاهَا بِإِسْحَاقَ وَمِن وَرَاءِ إِسْحَاقَ يَعْقُوبَ ﴿٧١﴾
71. Na mkewe kasimama wima akacheka. Tukampa bishara ya Is-haq na baada ya Is-haq, Ya’qub.
قَالَتْ يَا وَيْلَتَىٰ أَأَلِدُ وَأَنَا عَجُوزٌ وَهَـٰذَا بَعْلِي شَيْخًا إِنَّ هَـٰذَا لَشَيْءٌ عَجِيبٌ ﴿٧٢﴾
72. Akasema: Miye! Hivi nitazaa na hali mimi ni kikongwe na huyu mume wangu ni mzee? Hakika hili ni jambo la ajabu!
قَالُوا أَتَعْجَبِينَ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ رَحْمَتُ اللَّـهِ وَبَرَكَاتُهُ عَلَيْكُمْ أَهْلَ الْبَيْتِ إِنَّهُ حَمِيدٌ مَّجِيدٌ ﴿٧٣﴾
73. Wakasema: Unastajabu amri ya Mwenyezi Mungu? Rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake iko juu yenu enyi watu wa nyumba hii Hakika yeye ni Mwenye kusifiwa Mwenye kutukuzwa.
MALAIKA WANAMBASHIRIA IBRAHIM
Aya 69-73
MAANA
Na wajumbe wetu walimjia ibrahim na bishara, wakasema: Salaam! Naye akasema: Salaam!
Wajumbe walikuwa ni Mlaika waliomjia Ibrahim(a.s) kwa sura za kibinadamu, ili wampe habari njema ya kumzaa Ish-haq (a.s). Walianza kwa maakuzi, naye akawarudishia mfano wake au zaidi. Mwenyezi Mungu ameashiria ugeni huu pale aliposema:
هَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ الْمُكْرَمِينَ ﴿٢٤﴾
Je, imekufikia hadithi ya wageni waheshimiwa wa Ibrahim?” (51:24)
Hakukaa ila akaleta ndama aliyeokwa.
Ibrahim(a.s) alikuwa maarufu kwa ukarimu na kuwapenda wageni. Kwa hiyo aliharakisha kutayarisha ndama aliyechomwa kwa moto wa mbali, kwa kuangalia hali ya wageni. Ndama alikuwa amenona, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
فَرَاغَ إِلَىٰ أَهْلِهِ فَجَاءَ بِعِجْلٍ سَمِينٍ ﴿٢٦﴾
“Mara akaenda kwa watu wake akaleta ndama aliyenona” (51:26)
Alipoona mikono yao hamfikii, aliwatilia shaka na akawahofia.
Hawakuweza kula kwa sababu wao si watu. Kwahiyo Ibrahim akawahofia kwa sababu yeye aliwachukulia ni watu kumbe sivyo; na hajui wanataka nini. Mtu yeyote, awe Maasum (aliyehifadhiwa na dhambi) au la, akijiwa na jambao la ghafla asilolijua mwisho wake, lazima ahofie.
Malaika walipomuona hali yakeWakasema: Usiogope! Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya Lut, wala hatuna ubaya na wewe wala kaumu yako. Mahali pengine hofu imeelezwa:
Akasema:
إِنَّا مِنكُمْ وَجِلُونَ ﴿٥٢﴾
“Hakika sisi tunawaogopa.” (15:52).
Na mkewe kasimama wima akacheka.
Kusimama ni kusikiliza mazungumzo yanayoendelea baina ya mumewe na Malaika. Ama kicheko, Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye. Kila mazungumzo kwa wanawake ni bashasha. Wafasiri wamegawanyika kuhusu hilo.
Tukampa bishara ya Is-haq na baada ya Is-haq, Ya’qub.
Yaani tukampa habari njema ya kumzaa Is-haq na Is-haq atamzaa Ya’qub. Hiyo inafahamisha kuwa mtoto wa mtoto ni mtoto.
Akasema: Miye! Hivi nitazaa na hali mimi ni kikongwe na huyu mume wangu ni mzee? Hakika hili ni jambo la ajabu!
Alistaajabu kwa vile si desturi mwanamke aliye katika umri wake kuweza kuzaa au mwanamume aliye katika umri wa mumewe kuweza kuzaa. Katika Kitabu cha kikiristo, Kutoka, imeelezwa kuwa Ibrahim wakati huo alikuwa na umri wa Miaka mia na mkewe, Sarah alikuwa na miaka tisini. Sisi hatukikubali Kitabu hicho. Tunalolifahamu ni kuwa wote wawili walikuwa wazee sana. Ama idadi ya miaka yao anayeijua ni Mungu.
Wakasema: Unastajabu amri ya Mwenyezi Mungu?
Vipi isiwezekane na yeye amri yake ni kukiambia kitu kuwa kikawa.
Rehema ya Mwenyezi Mungu na baraka zake iko juu yenu enyi watu wa nyumba hii.
Na amewahusu na neema nyingi. Na hii ni mojawapo. Kuna ajabu zaidi ya kuufanya moto uwe baridi na salama kwa Ibrahim?
Hakika yeye ni Mwenye kusifiwa Mwenye kutukuzwa.
Ni mwenye kusifiwa kwa sababu ana sifa njema ni mwenye kutukuzwa kwa sabubu ana ukarimu. Kwa hiyo siajabu kumpa anayemuomba na asiyemuomba na mwenye kutazamia na asiyetazamia.
5
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI
فَلَمَّا ذَهَبَ عَنْ إِبْرَاهِيمَ الرَّوْعُ وَجَاءَتْهُ الْبُشْرَىٰ يُجَادِلُنَا فِي قَوْمِ لُوطٍ ﴿٧٤﴾
74. Basi hofu ilipomwondokea Ibrahim na ikawa ile bishara imemfikia, alianza kujadiliana nasi juu ya watu wa Lut.
إِنَّ إِبْرَاهِيمَ لَحَلِيمٌ أَوَّاهٌ مُّنِيبٌ ﴿٧٥﴾
75. Hakika Ibrahim alikuwa mpole, mwenye huruma, mwepesi wa kurejea (kwa Mungu).
يَا إِبْرَاهِيمُ أَعْرِضْ عَنْ هَـٰذَا إِنَّهُ قَدْ جَاءَ أَمْرُ رَبِّكَ وَإِنَّهُمْ آتِيهِمْ عَذَابٌ غَيْرُ مَرْدُودٍ ﴿٧٦﴾
76. Ewe Ibrahim! Achana nayo haya. Hakika amri ya Mola wako imekwishakuja, na hakika wao itawafikia adhabu isiyorudishwa.
IBRAHIM ANAJADILI KUHUSU WATU WA NUH
Aya 74-76
MAANA
Basi hofu ilipomwondokea Ibrahim na ikawa ile bishara imemfikia, alianza kujadiliana nasi juu ya watu wa Lut.
Baada ya kujua Ibrahim hali halisi ya wageni wake na madhumuni yao alitulia, na akajawa na furaha yeye na mkewe, Sarah, kwa habari ya kupata mtoto na mjukuu. Lakini hakufurahishwa na habari ya adhabu ya watu wa Lut. Akawa anajadiliana naao.
Kundi kubwa la wafasiri, akiwemo Arrazi na mwenye Tafsir Al-Manar, wamesema kuwa Ibrahim hakujadili kuhusu watu wa Lut; isipokuwa alijadili kuhusu Lut akihofia kupatwa na adhabu. Wafasiri hao wametoa dalili kwa kauli yake Mwenyezi Mungu:
قَالَ إِنَّ فِيهَا لُوطًا قَالُوا نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَن فِيهَا لَنُنَجِّيَنَّهُ وَأَهْلَهُ إِلَّا امْرَأَتَهُ كَانَتْ مِنَ الْغَابِرِينَ ﴿٣٢﴾
Akasema: Humo yumo Lut. Wakasema: Sisi twajua zaidi aliyemo humo, kwa hakika tutamuokoa yeye na watu wake ila mkewe aliye miongoni mwa watakaobaki nyuma. (29:32).
Lakini ilivyo, Aya hii waliyoitolea ushahidi, haina uhusiano wowote na mjadala wa wa Ibrahim; isipokuwa ni kutolea habari tu kwamba humo yumo Lut; na ndio maana wakasema tunajua sana.
Ayah hii tunayoifasiri inazungumzia mjadala kuhusu watu wa Lut sio kwa Lut peke yake. Kuongezea kauli yake Mwenyezi Mungu:
Na hakika wao itawafikia adhabu isiyorudishwa.
Dhamir katika hakika wao na itawajia inawarudia watu wa Lut ambao ibrahim amewajadili. Lakini wafasiri wakasema kuwa kuwajadili watu wa Lut ni kumkosea Adabu Mwenyezi Mungu, na Ibrahim ni Maasum, kwa hiyo hapana budi iwe ni kujadili Lut pekee.
Nasi tunasema:
Kwanza : hakuna tofauti katika kumjadili Lut peke yake au kaumu yake. Kujadili ni kujadili tu.
Pili : Mjadala ulikuwa unahusiana na kuondolewa adhabu waja wa Mungu au kuchelweshwa. Kwa hiyo hilo si dhambi; bali ni kinyume cha hivyo. Kwa sababu mjadala huu hauna kupingana wala kuzozana; isipokuwa ni kutaka hurumma kutoka kwa mwenye nguvu kwenda kwa mnyonge. Ombi hili linafahamisha upole na hurumma.
Ndio maana Mwenyezi Mungu akamsifu kuwa niMpole, mwenye hurumma mwepesi wa kurejea (kwa Mungu) baada ya kuwahurumia watu wa Lut
Tatu : Ibrahim alijadili kuhusu watu wa Lut ili awe na yakini kwamba wao wameasi kiasi ambacho hakuna tamaa ya kuongoka kwao; sawa na alivyosema:
قَالَ أَوَلَمْ تُؤْمِن قَالَ بَلَىٰ وَلَـٰكِن لِّيَطْمَئِنَّ قَلْبِي ﴿٢٦٠﴾
Akasema: Huamini? Akasema: Kwa nini! (naamini) Lakini upate kutulia moyo wangu. (2:260).
Hili linasisitizwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:
Ewe Ibrahim! Achana nayo haya. Hakika amri ya Mola wako imekwishakuja, na hakika wao itawafikia adhabu isiyorudishwa.
Yaani usiniulize ewe ibrahim katika mambo yanayohusu watu wa Lut, kwa vile wao wataangamia tu, kwa sababu ya kuendelea kwao na shirk na ufisadi na kutokuwepo tama ya kutubia.
وَلَمَّا جَاءَتْ رُسُلُنَا لُوطًا سِيءَ بِهِمْ وَضَاقَ بِهِمْ ذَرْعًا وَقَالَ هَـٰذَا يَوْمٌ عَصِيبٌ ﴿٧٧﴾
77. Na wajumbe wetu walipomfikia lut, aliwahuzunikia na akawaonea dhiki. Na akasema: Hii ni siku ngumu.
وَجَاءَهُ قَوْمُهُ يُهْرَعُونَ إِلَيْهِ وَمِن قَبْلُ كَانُوا يَعْمَلُونَ السَّيِّئَاتِ قَالَ يَا قَوْمِ هَـٰؤُلَاءِ بَنَاتِي هُنَّ أَطْهَرُ لَكُمْ فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَلَا تُخْزُونِ فِي ضَيْفِي أَلَيْسَ مِنكُمْ رَجُلٌ رَّشِيدٌ ﴿٧٨﴾
78. Na wakamjia kaumu yake mbiombio na kabla ya haya walikuwa wakifanya maovu. Akasema: Enyi kaumu yangu! Hawa binti zangu wao wametakasika zaidi kwenu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu. Wala msinifedheheshe mbele ya wageni wangu. Hivi hakuna mtu muongofu miongoni mwenu.
قَالُوا لَقَدْ عَلِمْتَ مَا لَنَا فِي بَنَاتِكَ مِنْ حَقٍّ وَإِنَّكَ لَتَعْلَمُ مَا نُرِيدُ ﴿٧٩﴾
79. Wakasema: Umekwishajua hatuna haki juu ya binti zako, na hakika unajua tunayoyataka.
قَالَ لَوْ أَنَّ لِي بِكُمْ قُوَّةً أَوْ آوِي إِلَىٰ رُكْنٍ شَدِيدٍ ﴿٨٠﴾
80. Akasema: Lau ningelikuwa na nguvu kwenu au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu!
HUZUNI YA LUT
Aya 77- 80
MAANA
Na wajumbe wetu walipomfikia Lut, aliwahuzunikia na akawaonea dhiki.
Ujumbe uliondoka kwa Ibrahim(a.s) kuelekea kwa Lut(a.s) .
Katika Juz.8 (7:80) tulitaja kuwa Lut ni mtoto wa ndugu yake Ibrahim na kwamba yeye alikuwa mashariki mwa Jordan na kaumu yake ndio watu wa kwanza kuwaingilia kimwili wanaume badala ya wanawake. Na hili walikuwa wakilifanya dhahiri bila ya uficho wowote. Mwenye kukataa walikuwa wakimshika kwa nguvu; hata kama ni mgeni mheshimiwa.
Kwa hiyo walipokuja wajumbe wa Mwenyezi Mungu kwa Lut, kwa sura za kibinadamu, alihofia watu wake wasiwakosee heshima, huku akiwa hawezi kuwazuia.
Basi akawa anaona uchunguNa akasema: Hii ni siku ngumu.
Na wakamjia kaumu yake mbiombio.
Yaani walikuja nyumbani kwa Nuh haraka wakidhani kuwa siku hii ni kama nyinginena kabla ya haya walikuwa wakifanya maovu hawakufkiria mwisho wake.
Akasema: Enyi kaumu yangu! Hawa binti zangu wao wametakasika zaidi kwenu.
Makusudi ya binti zake ni binti wa umma wake; kwa sababu mtume ni kama mzazi kwa umma wake. Maana ni kuwa oweni wanawake na mstarehe kwa halali na wema na muache ulawiti kwa sababu hiyo ni kazi ya shetani.Basi mcheni Mwenyezi Mungu.
Anawahofisha na Mungu, na hilo wanalipuuza watu wa ufuska na uovu.
Wala msinifedheheshe mbele ya wageni wangu. Ikiwa hamumuogopi Mwenyezi Mungu basi angalau muone haya, msinifedheheshe mbele ya wageni.Hivi hakuna mtu muongofu miongoni mwenu? mwenye akili atakayewazuia hayo mnayotaka?
Wakasema: Umekwishajua hatuna haki juu ya binti zako Yaani hatuwataki.Na hakika unajua tunayoyataka.
Yaani unajua kuwa sisi hatupendelei mabinti, tunataka wanaume na unajua kuwa sisi hatutishwi na huyo Mungu wako. Binadamu anafikia kiwango hiki cha kiburi akiwa amejiachia, akipinga misimamo na kukosa majukumu.
Kuna watu leo walio mfano wa kaumu Lut katika ushenzi na kiburi tena ni wengi. Miongoni mwao wamo walezi na waalimu wa mashule na vyuo vikuu.
Na sisi hatuna shaka kwamba kuna watu wa dini ambao ni waovu mara elfu kuliko hao. Lakini la kusisitiza ni kuwa lau kusingelikuweko na watu wanaolingania kwenye dini na misimamo, basi ulimwengu ungelikuwa mbaya kuliko ulivyo hivi sasa.
Akasema: Lau ningelikuwa na nguvu kwenu au nategemea kwenye nguzo yenye nguvu!
Baada ya Lut kukata tamaa na watu wake, alitamani lau angelikuwa na nguvu za kuwazuia au kupata msadizi. Alitamani hivi akiwa hajui kwamba nusura ya Mwenyezi Mungu iko nyumbani kwake na kwamba umebakia wakati mchache sana wa kuangamia wafisadi.
قَالُوا يَا لُوطُ إِنَّا رُسُلُ رَبِّكَ لَن يَصِلُوا إِلَيْكَ فَأَسْرِ بِأَهْلِكَ بِقِطْعٍ مِّنَ اللَّيْلِ وَلَا يَلْتَفِتْ مِنكُمْ أَحَدٌ إِلَّا امْرَأَتَكَ إِنَّهُ مُصِيبُهَا مَا أَصَابَهُمْ إِنَّ مَوْعِدَهُمُ الصُّبْحُ أَلَيْسَ الصُّبْحُ بِقَرِيبٍ ﴿٨١﴾
81. Wakasema: Ewe Lut! Hakika sisi ni wajumbe wa Mola wako. (Hawa) hawatakufikia. Basi ondoka pamoja na watu wako wa nyumbani katika sehemu ya usiku. Wala yeyote katika nyinyi asigeuke nyuma, isipokuwa mke wako, kwani yeye yatamsibu yatakayowasibu. Hakika miadi yao ni asubuhi, je asubuhi si karibu?
فَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا جَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهَا حِجَارَةً مِّن سِجِّيلٍ مَّنضُودٍ ﴿٨٢﴾
82. Basi ilipofika amri yetu tuliigeuza juu chini. Na tukawateremshia mvua ya mawe ya udongo mkavu yaliyopandana.
مُّسَوَّمَةً عِندَ رَبِّكَ وَمَا هِيَ مِنَ الظَّالِمِينَ بِبَعِيدٍ ﴿٨٣﴾
83. Yaliyotiwa alama kwa Mola wako. Na hayo hayako mbali na wenye kudhulumu.
HAWATAKUFIKIA
Aya 81-83
MAANA
Wakasema: Ewe Lut! Hakika sisi ni wajumbe wa Mola wako. Hawa hawatakufikia.
Arrazi anasema: Malaika walipoona wasiwasi na huzuni ya Lut walimpa bishara zifuatazo:
1. Kwamba wao ni wajumbe wa Mwenyezi Mungu.
2. Makafiri hwatafikia lile walilolikusudia.
3. Mwenyezi Mungu atawaangamiza.
4. Mwenyezi Mungu atamwokoa yeye na watu wake kutokana na adhabu.
5. Kwamba yeye Lut yuko kwenye Nguzo yenye nguvu, kwa sababu Mungu atamwokoa na watu madhalimu.
Basi ondoka pamoja na watu wako wa nyumbani katika sehemu ya usiku. Wala yeyote katika nyinyi asigeuke nyuma, isipokuwa mke wako, kwani yeye yatamsibu yatakayowasibu.
Malaika walimtaka Lut atoke na watu wake wa nyumbani na kutoangalia nyuma yeyote. Huenda hekima ya hilo ilikuwa ni kutoona muangaliaji jinsi mji wake unavyoangamia asishikwe na hurumma akahuzunika.
Ama mkewe alimwacha, kwa amri ya Mwenyezi Mungu, pamoja na makafiri kwa sababu yeye ni miongoni mwao. Kwa hiyo naye alikuwa na laana ya Mwenyezi Mungu na ghadhabu zake.
Hakika miadi yao ni asubuhi, je asubuhi si karibu?
Haya ni katika maneno ya kuashiria jibu la anayeharakisha adhabu.
Basi ilipofika amri yetu tuliigeuza juu chini.
Dhamiri ya tuliiegeuza ni ya ardhi ya vijiji vya kaumu ya Lut. Baadhi ya tafsiri zinasema kuwa umbali wake na Baytul maqdis ni mwendo wa siku tatu
Na tukawateremshia mvua ya mawe ya udongo mkavu yaliyopandana, yaliyotiwa alama kwa Mola wako.
Mahali pengine Mwenyezi Mungu anasema:
لِنُرْسِلَ عَلَيْهِمْ حِجَارَةً مِّن طِينٍ ﴿٣٣﴾
“Tuwatupie mawe ya udongo” (51:33).
Yaliyopandana inaweza kuwa ni kupandana hayo yenyewe au kupandana kwa mfululizo wa kushuka. Alama ni alama maalumu ya kumfikia yule anayestahiki. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu aliteremsha adhabu mbili kwa kaumu ya Lut: Mvua ya mawe na kuzama ardhini.
Na hayo hayako mbali na wenye kudhulumu.
Wafasiri wanasema kuwa wenye kudhulumu hapa ni makafiri wa Makka, kwamba Mwenyezi Mungu aliwaahidi kuwa wao, yatawapata yaliyowapata watu wa Lut, kama wataendelea kumkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) .
Maana haya hayako mbali, pamoja na kujua kuwa kila dhalimu aliyeko mashariki au magharibi anaweza kushukiwa na adhabu kutoka mbinguni au kuadhibiwa ardhini. Kwani mapinduzi yoyote yanayotokea au yatakayotokea, basi matokeo yake ni adhabu kwa dhulma na watu wake na kwa ufisadi na wasaidizi wake.
وَإِلَىٰ مَدْيَنَ أَخَاهُمْ شُعَيْبًا قَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ وَلَا تَنقُصُوا الْمِكْيَالَ وَالْمِيزَانَ إِنِّي أَرَاكُم بِخَيْرٍ وَإِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ مُّحِيطٍ ﴿٨٤﴾
84. Na kwa Wamadian (tulimpeleka) ndugu yao Shuaib. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, hamna Mungu mwingine zaidi yake. Wala msipunguze kipimo na mizani. Mimi ninawaona mko katika kheri; na mimi nawahofia na adhabu ya siku izungukayo.
وَيَا قَوْمِ أَوْفُوا الْمِكْيَالَ وَالْمِيزَانَ بِالْقِسْطِ وَلَا تَبْخَسُوا النَّاسَ أَشْيَاءَهُمْ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ ﴿٨٥﴾
85. Enyi watu wangu! Timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu wala msiwatilie kasoro watu vitu vyao. Wala msifanye ufisadi katika nchi mkafanya vurugu.
بَقِيَّتُ اللَّـهِ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ وَمَا أَنَا عَلَيْكُم بِحَفِيظٍ ﴿٨٦﴾
86. Alivyowabakishia Mwenyezi Mungu ni bora kwa ajili yenu ikiwa nyinyi ni waumini. Wala mimi si mlinzi wenu.
SHUAIB
Aya 84-86
MAANA
Na kwa Wamadian (tulimpeleka) ndugu yao Shuaib. Akasema: Enyi watu wangu! Mwabuduni Mwenyezi Mungu, hamna Mungu mwingine zaidi yake.
Imepita tafsiri ya Aya hii kwa herufi zake katika Juz. 8 (7:85).
Wala msipunguze kipimo na mizani.
Hili ni katazo la kupunja; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:
وَيْلٌ لِّلْمُطَفِّفِينَ ﴿١﴾ الَّذِينَ إِذَا اكْتَالُوا عَلَى النَّاسِ يَسْتَوْفُونَ ﴿٢﴾
“Ole wao wanopunja. Ambao wanapojipimia kwa watu hutaka watimiziwe. Na wanapowapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza.” (83:1-2)
Mimi ninawaona mko katika kheri.
Makusudio ya kheri hapa ni riziki nyingi.
Na mimi nawahofia na adhabu ya siku izungukayo.
Hii ni kuwaonya na adhabu, kama wataendelea na maasi
Enyi watu wangu! Timizeni kipimo na mizani kwa uadilifu.
Baada ya kuwakataza kupunguza sasa anawaamrisha kutimiza vipimo. Maana zote mbili ni sawa. Hatufahamu lengo lake zaidi ya kuwa ni kusisitiza tu.
Wala msiwatilie kasoro watu vitu vyao.
Vitu ni kila kitu; kama vile haki ya kimaada (yakuonekana) na ya kimaana (isyoonekana). Kwa hiyo ni haramu kumpunguzia mtu kitu au jambo lolote; kama ilimu yake na hulka yake.
Wala msifanye ufisadi katika nchi mkafanya vurugu.
Katika Aya hii kuna maneo mawili (ta’thaw na Mufsidin) yenye maana moja, ya ufisadi. Kwa hiyo ikawa ni lazima kufanya T’awil (tafsir inayowakilisha). Ama kutafsir Ta’athaw kwa maana ya juhudi; yaani msifanye juhudi ya kuleta ufisadi; au kutafsir Mufisidin kwa maana ya kuleta vurugu; kama vile vita na umwagaji damu, bila ya sababu inayowajibisha. Lakini vita vyenyewe vikiwa ni vya kuondoa ufisadi, basi itakuwa kuacha kupigana ndio ufisadi. Hapo Ndipo jihadi inakuwa ndio twaa bora. Taawili hii ni bora kuliko ile ya kwanza.
Alivyowabakishia Mwenyezi Mungu ni bora kwa ajili yenu ikiwa nyinyi ni waumini.
Halali ni njema na yenye kubaki hata ikiwa chache na haramu ni uovu, ni shari na inakwisha hata ikiwa nyingi. Tukichunguza sababu ya vita leo, tutaona ni kujilundikia mali wachache na kunyimwa wengi.
Imetokea sadfa kusoma magazeti ya leo 24-12-1968, kwamba jamaa huko London walifanya maandamano kuelekea makao ya mfalme, Birmingham (Birmingham Palace) wakimtaka malkia aiache ikulu yake, inayoweza kukaliwa na watu elfu, ambapo London pekee ina watu elfu sita wasio na makazi.
Wala mimi si mlinzi wenu wa kuwazuia na maasi kwa nguvu.
Umuhimu wangu ni kuwanasihi na kufikisha tu, na nimekwishatekeleza kwa ukamilifu na nimeondokana na majukumu. Shuaib (a.s.) ndiye anayesema hivyo.
قَالُوا يَا شُعَيْبُ أَصَلَاتُكَ تَأْمُرُكَ أَن نَّتْرُكَ مَا يَعْبُدُ آبَاؤُنَا أَوْ أَن نَّفْعَلَ فِي أَمْوَالِنَا مَا نَشَاءُ إِنَّكَ لَأَنتَ الْحَلِيمُ الرَّشِيدُ ﴿٨٧﴾
87. Wakasema: Ewe Shuaib! Je, Swala yako inakuamuru tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu au kufanya tupendavyo katika mali zetu? Hakika wewe ndiwe mpole, mwongofu!
قَالَ يَا قَوْمِ أَرَأَيْتُمْ إِن كُنتُ عَلَىٰ بَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّي وَرَزَقَنِي مِنْهُ رِزْقًا حَسَنًا وَمَا أُرِيدُ أَنْ أُخَالِفَكُمْ إِلَىٰ مَا أَنْهَاكُمْ عَنْهُ إِنْ أُرِيدُ إِلَّا الْإِصْلَاحَ مَا اسْتَطَعْتُ وَمَا تَوْفِيقِي إِلَّا بِاللَّـهِ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ أُنِيبُ ﴿٨٨﴾
88. Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa nina dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu na ameniruzuku riziki njema itokayo kwake? Wala sipendi kuwakhalifu nikafanya yale ninayowakataza. Sitaki ila kutengeneza kiasi ninavyoweza. Na taufiki yangu haiko ila kwa Mwenyezi Mungu. Kwake ninategemea na kwake naelekea.
وَيَا قَوْمِ لَا يَجْرِمَنَّكُمْ شِقَاقِي أَن يُصِيبَكُم مِّثْلُ مَا أَصَابَ قَوْمَ نُوحٍ أَوْ قَوْمَ هُودٍ أَوْ قَوْمَ صَالِحٍ وَمَا قَوْمُ لُوطٍ مِّنكُم بِبَعِيدٍ ﴿٨٩﴾
89. Na enyi watu wangu! Kupingana nami kusije kukawapelekea yakawasibu kama yaliyowasibu kaumu ya Nuh au kaumu ya Hud au kaumu ya Swaleh, na kaumu ya Lut si mbali nanyi.
وَاسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ ثُمَّ تُوبُوا إِلَيْهِ إِنَّ رَبِّي رَحِيمٌ وَدُودٌ ﴿٩٠﴾
90. Na muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake. Hakika Mola wangu ni Mwenye kurehemu, Mwenye upendo.
HISTORIA YA UKOMUNISTI NA UBEPARI
Aya 87-90
MAANA
Wakasema: Ewe Shuaib! Je, Swala yako inakuamuru, tuyaache waliyokuwa wakiyaabudu baba zetu au kufanya tupendavyo katika mali zetu?
Kila asiyemwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, huifanya swala ni ya kudharau na kuifanyia stizai pamoja na hao wanaoswali. Bila shaka yoyote Shuaib alikuwa ni katika wanaoswali.
Alipowaamuru watu wake kutupilia mbali masanamu, na kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake na kuwakataza chumo la haramu, ndio wakaanza kumdharau na kusema: Hivi swala yako ya kipuuzi unayoiswali ndiyo inakufanya utuamrishe tuache ada zetu tulizowakuta nazo mababa zetu na mababu zetu jadi na jadi; tena unatukataza tuache kuchumma mali vile tupendavyo?
Hakika wewe ndiwe mpole, mwongofu!
Yaani, kweli wewe una akili kwa haya uyasemayo?
Aya hii inakusanya mambo yafuatayo:-
1. Risala ya mitume haiko kwenye nembo peke yake, bali inakusanya maisha ya kijamii na kumpangia binadamu uhuru wake na matumizi yake na kumwekea mipaka ya kutomwingilia mwingine, vilevile kumzuia kufanya tendo lolote baya litakaloleta madhara kwa mtu binafsi na kwa jamii. Dalili wazi juu ya hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya 85 ya sura hii: “wala msiwatilie kasoro watu vitu vyao. Wala msifanye ufisadi katika nchi mkafanya vurugu”
2. Aya imefahamisha kuwa maadui wakubwa wa mitume na wenye kuswali ni wale wanaotafuta mali kwa hadaa na utapeli na kutumia vipato vya watu vile wanavyotaka; kama yanavyofanya mashirika mengi ya ulanguzi na unyonyaji.
3. Vilevile Aya inafahamisha kwamba ubepari una mizizi ya kihistoria.
Ushahidi wa hilo ni mwingi sana. Kwa mfano huu ubepari unaotaka kila mtu awe na uhuru wa kupata utajiri vile atakavyo, iwe ni kwa uporaji au kwa lolote lile. Hilo linafafanuliwa na kauli ya waliomdodosa Shuaib: “Au kufanya tupendavyo katika mali zetu” Makusudio sio kula na kuvaa watakavyo; isipokuwa ni kuwatumia watu katika kupata mali vile wapendavyo.
Kama ambavo historia imeonyesha kuwa siasa za Ubepari zilianza zamani, vilevile inafahimisha historia kuwa Ukomonisti nao ulianza zamani. Imeelezwa katika uchunguzi wa mwanahistoria W.L. Dewarnet kwamba watafiti walipata ubao wa Sumeria ambao tarehe yake inarudi kwenye mwaka 2100, kabla ya kuzaliwa Nabii Issa, ukisema kuwa Serikali ndiyo inayopanga mwelekeo wa kiuchumi.
Katika Babilon, mnamo mwaka wa 1750, kabla ya kuzaliwa Nabii Issa, Sheria ya Hamurabi ndiyo iliyokuwa ikipanga bei za kila kitu. Na katika zama za Batholomeo, serikali ndiyo iliyokuwa ikimiliki ardhi na kuongoza kilimo na mengimeyo.
Uislamu haukubaliani na siasa za ubepari wala za ukomonisti kwa maana yake yaliyo mashuhuri; isipokuwa unakubaliana na kila linalotatua matati- zo ya maisha bila ya kuwapunguzia watu vitu vyao. Angalia kifungu, ‘Tajiri ni wakili sio mweneyewe’ katika kufasiri Juz. 4 (3:182)
Akasema: Enyi watu wangu! Mwaonaje ikiwa ni dalili iliyo wazi itokayo kwa Mola wangu?
Imetangulia Aya kama hii katika Aya 28 ya sura hii.
Na ameniruzuku riziki njema itokayo kwake?
Baada ya Shuaib kuwaamrisha watu wake wachume kihalali na kuwakataza haramu, aliwapa hoja ya riziki aliyoruzukiwa na Mwenyezi Mungu, inayotosheleza mahitaji yake yote, pamoja nakuwa yeye yuko mbali na haramu.
Kwa hiyo basi sababu za riziki nzuri sio haramu. Ni jambo lisilowezekana kwa Mwenyezi Mungu afungue mlango wa riziki kisha awanyime waja wake. Kauli yake: Na ameniruzuku riziki njema, inaonyesha alikuwa na maisha mazuri.
Wala sipendi kuwakhalifu nikafanya yale ninayowakataza.
Lau angelifanya hivyo wao wangelikuwa na hoja juu yake. Na katika sharti za mtume ni kuwa sifa zake zote ziwe ni za kuvutia sio za kufukuza. Na ilivyo ni kuwa anayesema asiyoyafanya basi atakimbiwa.
Sitaki ila kutengeneza kiasi ninavyoweza.
Na mtengenezaji huwaonya watu kwa vitendo vyake kabla ya maneno yake. Na kuendeleza mwito wake huku akivumlia adha na mashaka. Ndio maana Shuaib na mitume wengineo walikuwa wakila kutokana na kazi ya mikono yao na walikuwa wakivumilia adha kutoka kwa makafiri na wapinzani.
Na taufiki yangu haiko ila kwa Mwenyezi Mungu. Kwake ninategemea na kwake naelekea.
Yaani kwamba yeye ataendelea kutekeleza risala yake kwa hali yoyote itakavyokuwa, akiwa anamtegemea Mwenyezi Mungu, kutaka msaada wake na kumrejea yeye katika mambo yake.
Na enyi watu wangu! Kupingana nami kusije kukawapelekea yakawasibu kama yaliyowasibu kaumu ya Nuh au kaumu ya Hud au kaumu ya Swaleh, na kaumu ya Lut si mbali nanyi.
Yaani uadui wenu kwangu usije ukawasababishia adhabu. Kwani hakuna watu waliomfanyia uadui mtume wao ila huwashukia wao adhabu. Ushahidi wa hayo ni mitume waliotajwa. Ni kama mfano wa anayeambiwa: Usimuudhi baba yako usije ukapatwa na hasira za Mwenyezi Mungu.
Na muombeni maghufira Mola wenu kisha mtubie kwake.
Umepita mfano wake pamoja na tafsir yake katika Aya ya 52 na 61 ya Sura hii.
Hakika Mola wangu ni Mwenye kurehemu Mwenye upendo.
Mwenye kurehemu anayemtaka maghufira na Mwenye upendo kwa kuwaneemesha waja wake, kuwapa nasaha na kuapa muda ili wapate kurejea.
6
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI
قَالُوا يَا شُعَيْبُ مَا نَفْقَهُ كَثِيرًا مِّمَّا تَقُولُ وَإِنَّا لَنَرَاكَ فِينَا ضَعِيفًا وَلَوْلَا رَهْطُكَ لَرَجَمْنَاكَ وَمَا أَنتَ عَلَيْنَا بِعَزِيزٍ ﴿٩١﴾
91. Wakasema: Ewe Shuaib! Hatufahamu mengi ya hayo unayoyasema; na sisi tunakuona kwetu ni mdhaifu. na lau si jamaa zako, bila shaka tungelikurujumu. Wala wewe si Mtukufu kwetu.
قَالَ يَا قَوْمِ أَرَهْطِي أَعَزُّ عَلَيْكُم مِّنَ اللَّـهِ وَاتَّخَذْتُمُوهُ وَرَاءَكُمْ ظِهْرِيًّا إِنَّ رَبِّي بِمَا تَعْمَلُونَ مُحِيطٌ ﴿٩٢﴾
92. Akasema: Enyi watu wangu! Kwani jamaa zangu ni watukufu zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu? Na Yeye mmemuweka nyuma ya migongo yenu? Hakika Mola wangu ni mwenye kuyazunguka yote mnayoyatenda.
وَيَا قَوْمِ اعْمَلُوا عَلَىٰ مَكَانَتِكُمْ إِنِّي عَامِلٌ سَوْفَ تَعْلَمُونَ مَن يَأْتِيهِ عَذَابٌ يُخْزِيهِ وَمَنْ هُوَ كَاذِبٌ وَارْتَقِبُوا إِنِّي مَعَكُمْ رَقِيبٌ ﴿٩٣﴾
93. Enyi watu wangu! Fanyeni muwezavyo, mimi ninafanya. Karibuni mtajua ni nani itakayemfika adhabu itakayomfedhehesha na nani aliye mwongo. Na ngojeni nami ninangoja pamoja nanyi.
وَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا نَجَّيْنَا شُعَيْبًا وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ بِرَحْمَةٍ مِّنَّا وَأَخَذَتِ الَّذِينَ ظَلَمُوا الصَّيْحَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دِيَارِهِمْ جَاثِمِينَ ﴿٩٤﴾
94. Ilipofika amri yetu tulimwokoa Shuaib na walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu. Na ukelele ukawaangamiza wale waliodhulumu, wakapambaukiwa wameanguka kifudifudi katika majumba yao.
كَأَن لَّمْ يَغْنَوْا فِيهَا أَلَا بُعْدًا لِّمَدْيَنَ كَمَا بَعِدَتْ ثَمُودُ ﴿٩٥﴾
95. Kama kwamba hawakuwemo humo. Ehee! (watu wa) Madyan wamepotelea mbali; kama walivyopotelea mbali (watu wa) Thamud.
LAU SI JAMAA YAKO TUNGEKURUJUMU
Aya 91-95
MAANA
Wakasema: Ewe Shuaib! Hatufahamu mengi ya hayo unayoyasema.
Walifahamu vizuri amri, makatazo makemeo na ahadi alizowaambia, isipokuwa walikusudia, kwa kauli yao hii, kwamba vitisho na ahadi walizopewa na Shuaib si lolote kwao.
Kwa vile eti wao ni wasafi. Ibada yao ya masanamu ni safi kwa sababu waaliifanya mababu zao; na kupunja katika vipimo ni kusafi kwa vile ni demokrasia. Kwa hiyo madai ya Shuaib kwao ni kuvuruga amani ya uhuru wao.
Hayo ndiyo maneno ya wanyang’anyi kila mahali na kila wakati. Wanaua na kunyang’anya mali za watu; ukiwaambia wanasema tunataka kuleta amani na demokrasia na wewe unataka kuleta vurugu, kusababisha vita na kuvuruga amani. Kwa sababu amani, wanavyotaka wao, ni kuupigia magoti uovu wao na kusujudia masanamu yao.
Na sisi tunakuona kwetu ni mdhaifu Hakuna wakutuzuia kukukamata, kwa hiyo bora unyamaze. Na lau si jamaa zako, bila shaka tungelikurujumu.
Unaweza kuuliza : imekuwaje kusema kuwa Shuaib ni mdhaifu, lakini watu wake wana nguvu; kwani nguvu za watu wa mtu si ndio nguvu zake?
Jibu : Hakuna kufanana kati ya nguvu mbili; huenda nguvu za watu wa mtu ni dhidi yake sio za kumsaidia yeye. Makuriash walikuwa ndio maadui wakubwa zaidi wa Muhammad mkuraishi.
Baadhi ya wafasiri wanasema kuwa kauli ya lau si jamaa zako, ina maana ya lau si kuwaheshimu jamaa zako. Tamko la Aya linakubaliana na maana haya.
Akasema: Enyi watu wangu! Kwani jamaa zangu ni watukufu zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu?
Ni ajabu gani ya ujinga huu na upotevu?
إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ ﴿٢٨﴾
“Hakika wanomwogopa Mwenyezi Mungu miongoni mwa waja wake ni wale tu wenye elimu” (35: 28).
Na Yeye mmemuweka nyuma ya migongo yenu?
Yaani mmemsahau na kumpuuza.
Enyi watu wangu! Fanyeni muwezavyo, mimi ninafanya niwezavyo.
Huu ni mfano wa kauli yake:
لِّي عَمَلِي وَلَكُمْ عَمَلُكُمْ أَنتُم بَرِيئُونَ مِمَّا أَعْمَلُ وَأَنَا بَرِيءٌ مِّمَّا تَعْمَلُونَ ﴿٤١﴾
“Mimi nina amali yangu na nyinyi mna amali yenu. Nyinyi hamna jukumu kwa ninayoyatenda na mimi sina jukumu kwa mnayoyatenda.” Juz. 11 (10:41).
Na pia kauli yake:
لَكُمْ دِينُكُمْ وَلِيَ دِينِ ﴿٦﴾
“Mna dini yenu nami ninadini yangu” (109:6).
Karibuni mtajua ni nanai itakayemfika adhabu itakayomfedhehesha na nani aliye mwongo. Na ngojeni nami ninangoja pamoja na nyinyi.
Hili ni karipio kutoka kwa Shuaib kwa watu wake kuwa watashukiwa na adhabu. Na hakuna dalili kubwa zaidi, inayofahamisha utume wake, kuliko kuamini ghaibu hii.
Ilipofika amri yetu tulimwokoa Shuaib na walioamini pamoja naye, kwa rehema itokayo kwetu. Na ukelele ukawaangamiza wale waliodhulumu, wakapambaukiwa wameanguka kifudifudi katika majumba yao. Kama kwamba hawakuwemo humo. Ehee! (watu wa) Madyan wamepotelea mbali; kama walivyopotelea mbali (watu wa) Thamud.
Umekwishapita mfano wa Aya hii katika Aya 66-67 ya Sura hii.
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا مُوسَىٰ بِآيَاتِنَا وَسُلْطَانٍ مُّبِينٍ ﴿٩٦﴾
96. Na hakika tulimtumma Musa pamoja na Ishara zetu na dalili zilizo wazi
إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ فَاتَّبَعُوا أَمْرَ فِرْعَوْنَ وَمَا أَمْرُ فِرْعَوْنَ بِرَشِيدٍ ﴿٩٧﴾
97. Kwa Firauni na waheshimiwa wake, lakini wao walifuata amri ya Firauni na amri ya Firauni haikuwa yenye uongofu.
يَقْدُمُ قَوْمَهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَأَوْرَدَهُمُ النَّارَ وَبِئْسَ الْوِرْدُ الْمَوْرُودُ ﴿٩٨﴾
98. Siku ya Kiyama atawatangulia watu wake na atawaingiza motoni. Ni pabaya mno mahala pa kufikiwa.
وَأُتْبِعُوا فِي هَـٰذِهِ لَعْنَةً وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ بِئْسَ الرِّفْدُ الْمَرْفُودُ ﴿٩٩﴾
99. Na wamefuatishiwa laana katika (dunia) hii na siku ya Kiyama ni kibaya mno watakachopewa.
MUSA
Aya 96-99
MAANA
Alipomaliza, Mwenyezi Mungu (s.w.t), kutaja yaliyowapata watu wa Nuh, Hud, Swaleh, Lut, Na wa Shuaib, ameashiria kwa Firaun na kaumu yake. Na lengo ni mazingatio na mawaidha.
Kwa muhtasari Aya hizi nne zinazungumzia kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimtumma Mussa(a.s) kwa Firauni na watu wake kwa hoja na dalili zilizo wazi. Miongoni mwazo ni fimbo na mkono, lakini Firauni aling’angania ukafiri na utaghuti; kama alivyowalazimisha watu wake wamfuate na wafuate amri zake.
Mwisho wa wafuasi na anyefuatwa ukawa ni laana na maangamizi hapa duniani na Akhera.
Lau Firaun asingepata wafuasi na wasaidizi, basi asingeweza kujasiri na kusema:
أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٤﴾
“Mimi ndiye Mola wenu mkubwa” (79:24) na
مَا عَلِمْتُ لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرِي ﴿٣٨﴾
“Simjiu kwa ajili yenu Mungu asiyekuwa mimi” (28:38)
Mfisadi na mpotezaji yoyote hawezi kujitokeza ila baada ya kupata wafuasi.
Tabia ya binadamu iko hivyo wakati wowote, linalobadilika ni jina na mfumo tu. Zamani kulikuwa na Firauni na Namrud, leo ni majeshi ya ushirika na mashirika kama vile ARAMCO n.k. Ama wafuasi na wasaidizi ni wale wanaokabidhiwa majukumu na kuonekana ndio watukufu baina ya watu.
ذَٰلِكَ مِنْ أَنبَاءِ الْقُرَىٰ نَقُصُّهُ عَلَيْكَ مِنْهَا قَائِمٌ وَحَصِيدٌ ﴿١٠٠﴾
100. Hizo ni habari za miji tunazokusimulia, mingine bado ipo na mingine imefyekwa.
وَمَا ظَلَمْنَاهُمْ وَلَـٰكِن ظَلَمُوا أَنفُسَهُمْ فَمَا أَغْنَتْ عَنْهُمْ آلِهَتُهُمُ الَّتِي يَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مِن شَيْءٍ لَّمَّا جَاءَ أَمْرُ رَبِّكَ وَمَا زَادُوهُمْ غَيْرَ تَتْبِيبٍ ﴿١٠١﴾
101. Nasi hatukuwadhulumu, lakini wao wamejidhulumu wenyewe. Na miungu yao waliyokuwa wakiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu, haikuwafaa kitu ilipofika amri ya Mola wako, na haikuwazidishia isipokuwa maangamizi.
وَكَذَٰلِكَ أَخْذُ رَبِّكَ إِذَا أَخَذَ الْقُرَىٰ وَهِيَ ظَالِمَةٌ إِنَّ أَخْذَهُ أَلِيمٌ شَدِيدٌ ﴿١٠٢﴾
102. Na ni kama hivyo kushika kwa Mola wako anapoishika miji inapokuwa imedhulumu. Hakika kushika kwake ni kuchungu, kukali.
HABARI ZA MIJI
Aya 100-102
MAANA
Hizo ni habari za miji tunazokusimulia, mingine bado ipo na mingine imefyekwa.
Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja sehemu ya visa katika umma zilizopita pamoja na mitume yao, alimwambia mtume mtukufu(s.a.w.w) kwamba baadhi ya umma hizo athari zake bado zipo na nyingine athari zake hazipo.
Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa ambazo athari zake zimebakia ni miji ya Aa’d na Thamud, na zile ambazo hazikubakia athari zake ni miji ya Nuh. Ama sisi tunawachia wataalamu wa mambo ya kale.
Kwa hali yoyote iwayo, ni kuwa ubainifu wa kisa hiki kwa ulimi wa Muhammad(s.a.w.w) ni dalili mkataa ya utume wake na kwamba ni wahyi wa kutoka kwa Mwenyezi Mungu sio njozi wala nukuu ya yaliyosemekana.
Nasi hatukuwadhulumu, lakini wao wamejidhulumu wenyewe kwa kumkadhibisha kwao mtume wa Mwenyezi Mungu na kung’ang’ania kwao shirki na ufisadi. Maana haya yamekaririka katika Katika Qur’ani kwa karibu Aya ishirini.
Na miungu yao waliyokuwa wakiiabudu badala ya Mwenyezi Mungu, haikuwafaa kitu ilipofika amri ya Mola wako, na haikuwazidishia isipokuwa maangamizi.
Miungu yao ni masanamu yao. Maana yanaupishwa na kauli yake:
وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُهُمْ وَلَا يَضُرُّهُمْ ﴿٥٥﴾
“Na wanaabudu kinyume cha Mwenyezi Mungu yasiyowafaa wala kuwadhuru” (25:55)
Na ni kama hivyo kushika kwa Mola wako anapoishika miji inapokuwa imedhulumu.
Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t). Atawaangamiza makafiri, madhlimu kama mfano wa tufani, tetemeko na ukelele wa adhabu.
Hakika kushika kwake ni kuchungu, kukali, lakini ni baada ya onyo na hoja kupitia mitume wakionya ana kwa ana.
Tumesema ana kwa ana, kwa sababu hivi sasa ukafiri na ufisadi ni mwingi kuliko hapo zamani, na maonyo yapo, ya kiakili, vitabu vya mbinguni na hadith za Mtume, lakini pamoja na hayo, hakuna matufani wala mitetemeko au mawe ya udongo mkavu.
Hatujui siri ya hilo, isipokuwa kudhani kuwa matakwa ya Mwenyezi Mungu yamehukumia maangamivu ya wale wanaowapinga mitume wao ana kwa ana; na sio wale wanaoasi wahyi na akili. Lakini dhana haitoshelezi kitu haki. Na Mwenyezi ndiye Mjuzi zaidi.
إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّمَنْ خَافَ عَذَابَ الْآخِرَةِ ذَٰلِكَ يَوْمٌ مَّجْمُوعٌ لَّهُ النَّاسُ وَذَٰلِكَ يَوْمٌ مَّشْهُودٌ ﴿١٠٣﴾
103. Hakika katika hayo kuna Ishara kwa yule anayeogopa adhabu ya Akhera. Hiyo ndiyo siku itakayokusanyiwa watu na hiyo ndiyo siku itakayoshuhudiwa.
وَمَا نُؤَخِّرُهُ إِلَّا لِأَجَلٍ مَّعْدُودٍ ﴿١٠٤﴾
104. Na hatuiakhirishi ila kwa muda unaohisabiwa.
يَوْمَ يَأْتِ لَا تَكَلَّمُ نَفْسٌ إِلَّا بِإِذْنِهِ فَمِنْهُمْ شَقِيٌّ وَسَعِيدٌ ﴿١٠٥﴾
105. Siku itakapofika, nafsi yoyote haitasema ila kwa kwa idhini yake. Katika wao kuna waovu na wengine ni wema.
فَأَمَّا الَّذِينَ شَقُوا فَفِي النَّارِ لَهُمْ فِيهَا زَفِيرٌ وَشَهِيقٌ ﴿١٠٦﴾
106. Ama wale waovu watakuwa motoni watachachatika na kukorama.
خَالِدِينَ فِيهَا مَا دَامَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ إِلَّا مَا شَاءَ رَبُّكَ إِنَّ رَبَّكَ فَعَّالٌ لِّمَا يُرِيدُ ﴿١٠٧﴾
107. Watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipokuwa apendavyo Mola wako. Hakika Mola wako hufanya atakavyo.
وَأَمَّا الَّذِينَ سُعِدُوا فَفِي الْجَنَّةِ خَالِدِينَ فِيهَا مَا دَامَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ إِلَّا مَا شَاءَ رَبُّكَ عَطَاءً غَيْرَ مَجْذُوذٍ ﴿١٠٨﴾
108. Ama wale wema watakuwa Peponi watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipokuwa apendavyo Mola wako. Ni kipawa kisicho na ukomo.
فَلَا تَكُ فِي مِرْيَةٍ مِّمَّا يَعْبُدُ هَـٰؤُلَاءِ مَا يَعْبُدُونَ إِلَّا كَمَا يَعْبُدُ آبَاؤُهُم مِّن قَبْلُ وَإِنَّا لَمُوَفُّوهُمْ نَصِيبَهُمْ غَيْرَ مَنقُوصٍ ﴿١٠٩﴾
109. Basi usiwe na shaka na wanayo yaabudu hao. Hawaabudu ila kama walivyoabudu baba zao zamani. Na hakika sisi tutawatimizia fungu lao bila ya kupunguzwa.
SIKU ITAKAYOSHUHUDIWA
Aya 103 – 109
MAANA
Hakika katika hayo kuna ishara kwa yule anayeogopa adhabu ya Akhera. Hiyo ndiyo siku itakayokusanyiwa watu na hiyo ndiyo siku itakayoshuhudiwa.
Hayo ni ishara ya kuadhibu kwake Mwenyezi Mungu vijiji. Yaani katika kuadhibu huku kuna mazingatio kwa mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na ni waadhi kwa anayeogopa adhabu ya siku watakayoishuhudia viumbe wote, pale atakapowakusanya kwa ajili ya hisabu na malipo.
Unaweza kuuliza kuwa : tufani au tetemeko na mfano wake mara nyingi huzuka kwa sababu za kimaumbile na maumbile hayawezi kumpambanua mwema na muovu. Je, haiwezekani kuwa yaliyowatokea kaumu za mitume ni aina hii?
Jibu : Mtume alikuwa akiwaonya watu wake kwa kuzuka adhabu na kuieleza aina ya adhabu yenyewe na wakati wa kutokea kwake.
Nayo hutokea kama ilivyoelezwa. Kwa hiyo haiwezekani kuipa tafsiri ya ugunduzi wa kielimu, kwani wakati huo hakukuwa na nyenzo zozote za kielimu, wala hatuwezi kuitafsiri kua ni kawaida ya maumbile, kwa sababu Mtume alikuwa akielezea kwa kujiamini; akisema huu ndio uhakika na mtaona.
Kama ambavyo pia haiwezekani tafsiri ya sadfa kutokana na kukaririka. Ikiwa tafsiri zote hizi haziwezekani, basi inabaki tafsiri ya wahyi na matakwa ya Mwenyezi Mungu peke yake.
Na hatuiakhirishi ila kwa muda unaohisabiwa.
Kila kitu mbele ya Mwenyezi Mungu kina muda wake, hautangulii wala kuchelewa. Miongoni mwavyo ni kuisha dunia na kuja Akhera.
Siku itakapofika, nafsi yoyote haitasema ila kwa idhini yake.
Itapewa idhini ya kujitetea kama ilivyo katika mahakama za kidunia.
Katika wao kuna waovu na wengine ni wema.
Uovu wa mtu au wema wake kesho utakuwa kwa matendo yake tu hapa duniani.
Ile kauli ya “Muovu ni muovu tangu tumboni mwa mama yake na mwema ni mwema tangu tumboni mwa mama yake,” inatiliwa mashaka. Kwa sababu dhahiri yake inapingana na uadilifu wake Mwenyezi Mungu na rehema yake; mbali ya kuwa ni hadith Ahaad ambayo ni hoja katika hukumu za kisharia tu; kama halali, haramu, twahara na najisi; sio katika misingi ya itikadi na yanayoambatana nayo.
Kisha akawaelezea wale watakaokuwa waovu kwa kusema:
Ama wale waovu watakuwa motoni watachachatika na kukoroma.
Kimsingi ni kuwa Mwenyezi Mungu humwadhibu mfisadi. Kwa hiyo basi uovu anauchumma mwenyewe mtu; sio kwa kadha na kadari.
kuchachatika na kukoroma ni kuelezea uchungu wa watu wa motoni.
Watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipokuwa apendavyo Mola wako.
Wafasiri wamerefusha maneneno sana kuhusu makusudio ya ‘apendavyo Mwenyezi Mungu,’ hapa. Wakataja njia zilizofanya Aya iwe yenye kutatiza na yenyewe siyo ya kutatiza, bali iko wazi.
Kwa ufupi ni kuwa mwenye kuingia Jahannam kwa dhambi yoyote ile, hataweza kutoka humo yeye mwenyewe, si kwa kuombewa wala kwa fidia. Kwa namna hiyo ndiyo inasemwa ni mwenye kudumu. Lakini Mungu akitaka atoke humo atatoka na ataondokewa na wasifa wa kudumu motoni. Kwa sababu matakwa ya Mwenyzi Mungu, hayazuiwi na kitu chochote.
Hakika Mola wako hufanya atakavyo.
Na kila kitu mwisho wake unarejea kwenye matakwa yake wala matakwa yake hayarejei isipokuwa kwake. Kwa hiyo sababu ya kudumu itafanyakazi madamu muumbaji anataka hivyo na asipotaka basi haiwi.
إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٨٢﴾
“Hakika amri yake anapotaka chochote ni kukiambia: Kuwa, kikawa” (36:82)
Kama alivyowaelezea walio mashakani kuwa watadumu motoni, vile vile amewaeelezea wenye furaha kuwa ni wenye kudumu Peponi.
Ama wale wema watakuwa Peponi watadumu humo muda wa kudumu mbingu na ardhi, isipokuwa apendavyo Mola wako. Ni kipawa kisicho na ukomo. Yaani hakikatiki.
Unaweza kuuliza kwamba : mwenye kuingia pepeoni hatoki, sasa kuna haja gani ya kukuwekea matakwa ya Mwnyezi Mungu?
Imesemekana kuwa Mwenyezi Mungu atawatoa kutoka pepo moja hadi nyingine mfano wake au nzuri zaidi.
Tuonavyo sisi ni kuwa hilo ni kiasi cha kuashiria uweza wa Mwenyezi Mungu na ukuu wake, na kwamba sababu zinafanya kazi ikiwa hazikugongana na matakwa ya Mwenyezi Mungu.
Kwa hiyo moto utaunguza ikiwa mwenyezi Mungu hakuuambia kuwa baridi na salama.
Basi usiwe na shaka na wanayoyaabudu hao.
Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.w) . Na hao ni ishara ya watu wake waliomkadhibisha. Muhammad hakuwa wala hatakuwa na shaka kwamba wao wako kwenye ubatilifu katika ibada yao, lakini lengo ni kuwatahayariza na kuwahadharisha.
Hawaabudu ila kama walivyoabudu baba zao zamani.
Hii ni sababu ya yakini ya kutokuwepo shaka katika kubatilika wanayoaabudu hawa. Kwa sababu ni mfano wa walivyoabudu wa kwanza ambao walipatwa na adhabu kwa sababu ya shirki yao na kuabudu kwao masanamu.
Na hakika sisi tutawatimizia fungu lao bila ya kupunguzwa.
Sawa na tulivyotimiza fungu la adhabu waliyostahaiki mababa zao bila ya kupunguza kitu.
Unaweza kuuliza : Huku sikukatisha tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu amesema:
قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ﴿٥٣﴾
“Enyi waja wangu waliojidhulumu msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu” (39:53).
Jibu : Hakika makusudio ya kauli yake, Msikate tamaa ni kuhimiza katika toba na kwamba mwenye kutubia Mwenyezi Mungu humtakabalia toba yake.
Na makusudio ya bila kupunguzwa ni kwamaba mwenye kung’ang’ania shirki na wala asitubie, Mungu atamlipa anavyostahiki.
Sisi hatuna shaka kwamba Mwenyezi Mungu anasamehe na kumhurumia anayewahurumia watu, na anayefanya kwa maslahi ya watu. Ama wale wanaoingilia uhuru na ahaki zao, hawatapunguziwa adhabu wala hawatasaidiwa.
7
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI
وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ فَاخْتُلِفَ فِيهِ وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ لَقُضِيَ بَيْنَهُمْ وَإِنَّهُمْ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ مُرِيبٍ ﴿١١٠﴾
110. Na hakika tulimpa Musa Kitabu, zikazuka khitilafu ndani yake. Na lau kama si neno lililokwisha tangulia kutoka kwa Mola wako, bila shaka ingelihukumiwa baina yao. Na hakika wao wamo katika shaka inayowahangaisha.
وَإِنَّ كُلًّا لَّمَّا لَيُوَفِّيَنَّهُمْ رَبُّكَ أَعْمَالَهُمْ إِنَّهُ بِمَا يَعْمَلُونَ خَبِيرٌ ﴿١١١﴾
111. Na hakika Mola wako atawatimizia malipo ya vitendo vyao. Hakika yeye ana khabari za wanayoyatenda.
فَاسْتَقِمْ كَمَا أُمِرْتَ وَمَن تَابَ مَعَكَ وَلَا تَطْغَوْا إِنَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿١١٢﴾
112. Basi simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa wewe na yule anayeelekea (kwa Mwenyezi Mungu) pamoja nawe wala msipetuke mipaka. Hakika yeye anayaona mnayoyafanya.
وَلَا تَرْكَنُوا إِلَى الَّذِينَ ظَلَمُوا فَتَمَسَّكُمُ النَّارُ وَمَا لَكُم مِّن دُونِ اللَّـهِ مِنْ أَوْلِيَاءَ ثُمَّ لَا تُنصَرُونَ ﴿١١٣﴾
113. Wala msiwategemee madhalimu, usije ukawagusa moto. Na hamna walinzi asiyekuwa Mwenyezi Mungu wala hamtasaidiwa.
وَأَقِمِ الصَّلَاةَ طَرَفَيِ النَّهَارِ وَزُلَفًا مِّنَ اللَّيْلِ إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ذَٰلِكَ ذِكْرَىٰ لِلذَّاكِرِينَ ﴿١١٤﴾
114. Na simamisha Swala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana. Hakika mema huondoa maovu. Hiyo ni ukumbusho kwa wanaokumbuka.
وَاصْبِرْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يُضِيعُ أَجْرَ الْمُحْسِنِينَ ﴿١١٥﴾
115. Na subiri, kwani hakika Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa wanaofanya wema.
NENO LILILOKWISHATANGULIA
Aya 110- 115
MAANA
Na hakika tulimpa Musa Kitabu, zikazuka khitilafu ndani yake.
Makusudio ya Kitabu hapa ni Tawrat. Kaumu ya Musa ilikhitalifiana kuhusiana na Tawrat, wengine waliiamini na wengine wakaikataa. Ndio ilivyo kwa umma wowote, wa zamani na wa sasa, hauafikiani kuhusu mtume wake au kiongozi wake aliyemwaminifu.
Bali wana wa israil waliwaua mitume wao. Hata wale waliomwamini Musa waliigeuza Tawrat baada yake, wakazusha mambo ya upotevu. Kwa hiyo siajabu kwako ewe Muhammad wakikuamini baadhi na wengine wakikukana.
Na lau kama si neno lililokwisha tangulia kutoka kwa Mola wako, bila shaka ingelihukumiwa baina yao.
Makusudio ya neno ni kupitisha kuakhirisha adhabu. Baina yao ni wale waliokhitalifiana katika Tawrat. Hekima yake ilitaka wasipate adhabu hapa duniani.
Na hakika wao wamo katika shaka inayowahangaisha.
Bado maneno yako kwa Musa(a.s ) , kaumu na Kitabu chake. Amekuwa mbali yule anayesema kuwa hapa maneno yametoka kwa wana wa Israil hadi kwa Muhammad(s.a.w.w) na Maquraishi.
Kwa ujumla ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameakhirisha adhabu ya waliokadhibisha Tawrat katika kaumu ya Musa, na waliokadhibisha Qur’ani katika kaumu ya Muhammad.
Na hakika Mola wako atawatimizia malipo ya vitendo vyao. Hakika Yeye ana khabari za wanayoyatenda.
Yaani kila muongo na mkweli atapata malipo ya matendo yake kesho yakiwa kamili. Ikiwa ni kheri basi ni kheri na ikiwa ni shari basi ni shari.
MSIMAMO
Basi simama sawa sawa kama ulivyoamrishwa wewe na yule anayeelekea (kwa Mwenyezi Mungu) pamoja nawe wala msipetuke mipaka. Hakika yeye anayaona mnayoyafanya.
Maana ya kusimama sawa sawa (msimamo) inatofautiana kulingana na inavyonasibiana. Kwa hiyo maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
إِنَّ رَبِّي عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٥٦﴾
“Hakika Mola wangu yuko juu ya njia iliyonyooka” (11:56), ni kuwa Yeye anaongoza kwenye njia hiyo na kuamuru ifuatwe na kwenye msingi wake analipa thawabu na adhabu na kwamba vitendo vyake vyote vinaenda na hekima na maslahi.
أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا ﴿١١٥﴾
“ Je, mlidhani kwamba tuliwaumba bure bure…?” (23:115)
وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا بَاطِلًا ذَٰلِكَ ظَنُّ الَّذِينَ كَفَرُوا ﴿٢٧﴾
“Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo kati yake bure; hiyo ni dhana ya wale waliokufuru.” (38:27).
Na kama ukisifu kusimama sawa kwenye kitu na ukasema kitu hiki kiko sawasawa maana yake umekiweka mahali panapolingana nacho. Ama mtu aliye sawasawa (msimamo) maelezo yake mazuri ni yale aliyoyasema Mwenyezi Mungu:
الَّذِينَ يَسْتَمِعُونَ الْقَوْلَ فَيَتَّبِعُونَ أَحْسَنَهُ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ هَدَاهُمُ اللَّـهُ وَأُولَـٰئِكَ هُمْ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿١٨﴾
“Ambao husikiliza kauli wakafuata zilizo nzuri zaidi. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaongoza na hao ndio wenye akili” (39:18).
Kauli nzuri zaidi kwa Mungu na mwenye kumwamini ni hii Qur’ani:
اللَّـهُ نَزَّلَ أَحْسَنَ الْحَدِيثِ كِتَابًا مُّتَشَابِهًا ﴿٢٣﴾
“Mwenyezi Mungu ameteremsha hadith nzuri kabisa, Kitabu chenye maneno yenye kufanana.” (39:23).
Na kauli nzuri zaidi kwa Mungu na kwa watu wote ni ile inayozipa raha nyoyo za walimwengu sio wezi na wamwaga damu.
Kuna Hadith ya Mtume(s.a.w.w) inayosema: “Sura ya Hud imenizeesha” Inasemekana kuwa alikusudia Aya hii ya Sura ya Hud. Kwa sababu umma wake umeamrishwa kusimama sawa (msimamo) naye hana mategemeo kama watauitikia.
Na sisi tunaona sio mbali kuwa makusudio ya umma ni viongozi wake kwa sababu hao ndio asili ya ugonjwa na chimbuko la balaa. Tumezungumza msimamo katika maelezo ya Bismillah kwenye Juzuu ya kwanza. Itikadi ya Uislamu, sharia yake na maadili yake inakuwa katika neno moja ‘Unyoofu’ (msimamo).
MAJUKUMU YA MSHIKAMANO DHIDI YA DHULMA
Wala msiwategemee madhalimu, usije ukawagusa moto. Na hamna walinzi asiyekuwa Mwenyezi Mungu wala hamtasaidiwa.
Dhulma haihusiki na wanaowafanyia uadui watu na uhuru wao tu, Imeelezwa katika Hadith na Nahju-lbalagha “Dhulma ni tatu: Dhulma isiyosamehewa, dhulma isiyoachwa na dhulma inayosamehewa.
Dhlma isiyosamehewa ni kumshirikisha Mwenyezi Mungu (ushirikina), Dhulma inayosamehewa ni kujidhulumu mja yeye mwenyewe kwa kufanya madhambi madogo; na dhulma isiyoachwa ni ya kudhulumiana waja wenyewe kwa wenyewe.”
Makusudio ya kutegemea madhalimu ni pamoja na kuwanyamazia kwa sababu ni wajibu kukataza maovu. Kuna Hadith isemayo: “Watu wakiona maovu na wasiyakanye, basi wanakurubia nao kuchanganywa kwenye adhabu. Imam Ja’far As-swadiq(a.s ) anasema: “Muumin kumsaidia mumin mwengine ni faradhi ya wajib.” Katika Kitabu Wasail katika mlango Aljihadi anil-ma’sum Imeelezwa: “Mwislamu anapigana kwa ajili ya Uislam au kuhofia miji ya waislamu.”
Kwa kutegemea Hadith hizo na nyenginezo, mafaqih wamegawanya jihadi kwenye aina mbili:
1. Jihadi ya kupigana katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuueneza Uislam.
2. Kuulinda Uislamu na miji ya Waislamu, bali ni kuitetea haki yoyote ni sawa iwe yake au ya mtu mwengine.
Mwenye Al-Jawahir amesema: “Akishambulia adui, anayehofiwa, himaya ya waislamu au kafiri akitaka kuteka miji ya waislamu, kuwachukua mateka na kupora mali zao, ikitokea hivyo, basi ni wajibu kuutetea kwa kila mtu: muungwana, mtumwa, mwanamume, mwanamke, mwenye afya, mgonjwa, kipofu, kilema na wengineo wakihitajika. Na wajibu wenyewe haungoje kuwepo Imam au idhini yake. Vile vile wajibu huo hahusiki na walioshambuliwa na kulengwa tu, bali ni wajibu kwa kila atakayejua hata kama siye aliyelengwa, ikiwa hajui kuwa walioshambuliwa wanamuweza adui yao. Na wajibu unasisitizwa kwa aliyekaribu na aliye karibu zaidi.”
Kisha akaendelea kusema mwenye A-Jjawahir “Kujitetea mtu ni wajib hata kama hadhanii usalama wake, kwa sababu tayari yuko hatarini kwa namna yoyote. Ama kupigania heshima yake na mali yake ni wajibu ikiwa anaona hakuna hatari ya nafsi yake, kwa kuhofia isiende nafsi, mali na heshima pamoja. Vile vile kutetea maisha ya mtu mwingine, mali yake au heshima yake.”
Mafaqihi wametoa fat-wa ya wajibu wa kumwokoa mwenye kuangamia na kuzima moto ikiwa unaangamiza mali ya mtu mwingine. Na kwamba ni wajibu kwa mwenye kuswali kukata swala yake ili kuzuia hatari ya nafsi yoyote muhimu au mali ambayo ana wajib kwake kuihifadhi; iwe ni yake au ya mtu mwingine. Na atakayemuona mtoto jangwani ni wajib kumwokota na kumuhifadhi ikiwa hawezi kujilinda.
Imepokewa riwaya kwamba watuhumiwa watatu, waliomuua mtu, waliletwa kwa Imam Ali(a.s) . Mmoja alimshika yule aliyeuliwa, wapili akaua na watatu akaangalia bila ya kufanya lolote. Yule aliyeua akamhukumu kuuliwa na aliyeshika, afungwe maisha na aliyeangalia, ang’olewe macho. Mafakihi wameitumia riwaya hii.
Mwenye kufuatilia utafiti wa vitabu vingi vya Fiqh ataona aina hii ya maelezo; nayo ni dalili mkataa kwamba mtu kumsaidia na kumwokoa mtu mwingine ni wajibu wa kisharia ikiwa ni umuhimu kufanya hivyo.
Na simamisha Swala katika ncha mbili za mchana na nyakati za usiku zilizo karibu na mchana.
Ncha ya kwanza ya mchana ni wakati wa swala ya asubuhi, ncha ya pili ni adhuhuri na alasiri, na usiku uliokaribu na mchana ni maghribi na isha. Aya nyingine inasema:
أَقِمِ الصَّلَاةَ لِدُلُوكِ الشَّمْسِ إِلَىٰ غَسَقِ اللَّيْلِ وَقُرْآنَ الْفَجْرِ إِنَّ قُرْآنَ الْفَجْرِ كَانَ مَشْهُودًا ﴿٧٨﴾
“Simamisha swala jua linapopinduka mpaka giza la usiku na Qur’ani ya alfajiri. Hakika Qur’ani ya alfajiri ni yenye kushuhudiwa.” (17:78).
Kupinduka jua ni wakati wa swala ya adhuhuri na alasiri na giza la usiku ni wakati wa swala ya maghrib na isha na Qur’ani ya alfajiri ni swala ya asubuhi ambayo watu wanaishuhudia. Ufafanuzi uko katika vitabu vya Fiqh, ikiwemo Juzuu ya kwanza ya Fiqhul-Imam Jaffer As-swadiq.
Hakika mema huondoa maovu.
Mwenye Majmaulbayan, akiwanukuu wafasiri wengi, anasema kuwa makusudio ya mema hapa ni swala tano na kwamba hizo zinafuta madhambi yaliyo baina yao. Wengine wakasema ni kule kusema tu: “Subhanallah walhamdulillah walailahaillaha illallah wallahu akbar”
Tafsiri zote zinakataliwa na akili. Kwani hakuna mahusiano yoyote baina yake si ya kihukumu wala sharia au akili. Vile vile si kikanuni wala kidesturi. Hukumu yoyote ya wajibu au haramu haiifungi hukumu nyingine. Ama hadith inayosema: “Kila anaposwali hufutiwa madhambi yaliyo baina ya swala mbili ni fumbo la kwamba swala ina mema mengi.
Ikiwa mwenye kuswali ana maovu huwekwa kwenye kiganja na yale mengine kwenye kiganja, hapo mazuri huondoa mabaya. Kwa sharti yasiwe makubwa wala yasiwe ni haki miongoni mwa haki za watu. Maelezo ya maudhui haya yamekwishatangulia katika Juz. 2 (2:217).
Hiyo ni ukumbusho kwa wanaokumbuka.
Hiyo ni ishara ya amri ya kusimama sawa sawa (msimamo), kusimamisha swala na kukatazwa kuwategemea madhalimu. Makusudio ya wenye kukumbuka ni wenye kuwaidhika.
Na subiri, kwani hakika Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa wanaofanya wema.
Hapo kuna ishara kwamba mwenye kufuata njia ya sawa sawa atapambana na wapotevu wenye kupotoka na kwamba subra (uvumilivu) katika jihadi yao ndio twaa bora na wema mkuu.
فَلَوْلَا كَانَ مِنَ الْقُرُونِ مِن قَبْلِكُمْ أُولُو بَقِيَّةٍ يَنْهَوْنَ عَنِ الْفَسَادِ فِي الْأَرْضِ إِلَّا قَلِيلًا مِّمَّنْ أَنجَيْنَا مِنْهُمْ وَاتَّبَعَ الَّذِينَ ظَلَمُوا مَا أُتْرِفُوا فِيهِ وَكَانُوا مُجْرِمِينَ ﴿١١٦﴾
116. Basi mbona hawakuwamo katika watu wa karne ya kabla yenu wenye akili wakakataza ufisadi katika nchi? Na wakafuata wale waliodhulumu waliyostareheshewa na wakawa ni wakosefu.
وَمَا كَانَ رَبُّكَ لِيُهْلِكَ الْقُرَىٰ بِظُلْمٍ وَأَهْلُهَا مُصْلِحُونَ ﴿١١٧﴾
117. Na hakuwa Mola wako wa kuiangamiza miji kwa dhulma na hali watu wake ni watenda mema.
وَلَوْ شَاءَ رَبُّكَ لَجَعَلَ النَّاسَ أُمَّةً وَاحِدَةً وَلَا يَزَالُونَ مُخْتَلِفِينَ ﴿١١٨﴾
118. Na lau Mola wako angelitaka angeliwafanya watu wote kuwa umma mmoja. Na hawaachi kukhitalifiana.
إِلَّا مَن رَّحِمَ رَبُّكَ وَلِذَٰلِكَ خَلَقَهُمْ وَتَمَّتْ كَلِمَةُ رَبِّكَ لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنَ الْجِنَّةِ وَالنَّاسِ أَجْمَعِينَ ﴿١١٩﴾
119. Ispokuwa wale ambao Mola wako amewarehemu. Na kwa hiyo Mwenyezi Mungu amewaumba. Na litatimia neno la Mola wako: kwa hakika nitaijaza Jahannam kwa majini na watu kwa pamoja.
WATU WA KARNE ZILIZOTANGULIA
Aya 116-119
MAANA
Basi mbona hawakuwamo katika watu wa karne ya kabla yenu wenye akili wakakataza ufisadi katika nchi?
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja maangamizi yaliyowapitia kaumu ya Nuh, ya A’d, ya Thamud na wengineo kwa sababu ya jeuri na ufisadi wao, anasema hivi hawakupatikana watu na viongozi wema kuweza kuzuia dhulama na ufisadi.
Kwa sababu ya dhulma hiyo na ufisadi na wengine wakayanyamazia, basi walistahiki adhabu na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu wote;
Isipokuwa wachache tu, tuliowaokoa miongoni mwao.
Ambao ni mitume na wale walioamini pamoja nao. Yaani kikundi kidogo alichokiokoa Mwenyezi Mungu kilikuwa kikiamrisha mema na kukataza maovu, lakini hakuna amri kwa asiyetiiwa.
Na wale waliodhulumu waliyostareheshewa na wakawa ni wakosefu wakafuata.
Makusudio ya waliyostreheshewa ni mali zao. Wale wachache waliwakataza wengine ufisadi na dhulma, lakini kwa sababu ya mali zao hawakujali kabisa. Mwenyezi Mungu anasema:
وَمَا أَرْسَلْنَا فِي قَرْيَةٍ مِّن نَّذِيرٍ إِلَّا قَالَ مُتْرَفُوهَا إِنَّا بِمَا أُرْسِلْتُم بِهِ كَافِرُونَ ﴿٣٤﴾ وَقَالُوا نَحْنُ أَكْثَرُ أَمْوَالًا وَأَوْلَادًا وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ ﴿٣٥﴾
“Na hatukutumma mwonyaji yoyote kwenye mji, ila husema wenyeji wake waliostareheshwa: Hakika sisi tunayakataa hayo mliyotumwa nayo. Na wakasema sisi tuna mali nyingi zaidi na watoto, wala sisi hatutadhibiwa.” (34:34-35)
Na hakuwa Mola wako wa kuiangamiza miji kwa dhulma na hali watu wake ni watenda mema.
Vinginevyo angelikuwa sawa kwake, mwema na muovu na mzuri na mbaya. Haiwi hivyo kwa Mwnyezi Mungu:
مَّا يَفْعَلُ اللَّـهُ بِعَذَابِكُمْ إِن شَكَرْتُمْ وَآمَنتُمْ وَكَانَ اللَّـهُ شَاكِرًا عَلِيمًا ﴿١٤٧﴾
“Mwenyezi Mungu ana haja gani ya kuwaadhibu kama mtashukuru na mtaamini na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye (kupokea) shukrani Mjuzi. Juz. 5 (4:147).
Na lau Mola wako angelitaka angeliwafanya watu wote kuwa umma mmoja.
Tangu iliposhuka Aya hii mpaka leo,watu wengi wanasema : Kwanini hakutaka Mwenyezi Mungu. Laiti Mwenyezi Mungu angelifanya hivyo miji ikawa na raha na kuepukana na balaa hili la kubaguana.
Jibu linafafanuka kwa namna ifuatayo:
1. Kabla ya kitu chochote inatakikana tuwe na yakini kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hataki waja wake wachukiane, wabughudhiane au wachinjane. Kwanini isiwe hivyo na hali yeye ndiye mwenye kusema:
وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا ﴿٤٦﴾
“Wala msizozane, msije mkafunjika moyo.” (8:46).
Haina maana kuwa kwa vile hakuwalazimisha mshikamano na maafikiano, basi anawataka wazozane na wapigane. Kwa mfano ukisema: Sitaki wanangu wawe na rai moja katika siasa. Haina maana kwamba unataka wapigane na wauane.
2. Kulazimisha kwenye dini kuna njia mbili: Kwanza, ni kutumia nguvu. Pili, ni kuumba Mwenyezi Mungu imani katika moyo wa mtu, kama alivyomba ulimi katika mdomo.
Njia ya kwanza inapingana na misingi ya dini na ya mantiki pia. Kwa sababu nguvu haitengenezi imani; bali ni kinyume. Kwa vile njia ya imani ya haki ni dalili. Ndio maana Qur’ani ikazionyesha dalili hizi kwa mifumo mbalimbali. Na ikamuhimiza mtu kuzichunguza, kuziangalia vizuri na kuzizingatia. Ni hiyari yake sasa kumwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.
Ama amri ya kupigana ni kwa ajili yakuitetea sharia ya haki na uadilifu na kuchunga usalama na amani kwa jamii.
Na njia ya pili, ya kuumba imani moyoni, itamatoa mtu kwenye utu wake, awe sawa na matunda yaliyo mtini, hana matakwa wala fikra juu ya muumbaji na hatastahiki kusifiwa wala kulaumiwa au kuwa na thawabu au adhabu. Yametangulia maelezo katika kufasiri Juz. 7 (6:35).
Kwa ufupi ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakutaka kwa namna yoyote ile kuwatumilia watu nguvu katika imani. Kwa sababu lau angelifanya hivyo angaliwaondolea sifa ya ubinadamu; wangelikuwa kama wanyama na wadudu, hawana majukumu yoyote wala hawahisabiwi chochote. Lakini Mwenyezi Mungu alitaka amtofautishe binadamu na viumbe vyote na afikie hali ambayo hakutakua na chochote juu yake isipokuwa Muumbaji tu.
Itakuwa Muhali kufikia cheo hiki bila ya juhudi na khiyari. Ndio maana Mwenyezi Mungu, amempa uwezo, utambuzi wa mambo, mhemuko na kumwonyesha njia mbili, kisha akamwachia uhuru wa hiyari, ili abebe mwenyewe lile atakalojichagulia.
Na hilo litamkamilishia ubinadamu wake kamili. Matokeo ya hayo sasa ni kutofautiana watu rai zao na itikadi zao. Angalia Juz. 2 (2:213) na Juz. 5 (4:78).
Na hawaachi kukhitalifiana.
Yaani watu waliopita walikhitalifiana na wataeendelea kukhitalifiana milele. Kwa vile hiyo ni natija ya kumfanya binadamu awe ni mwenye khiyari akielekea popote apendapo.
Ispokuwa wale ambao Mola wako amewarehemu.
Makusudio ya waliorehemiwa ni wale walioshikamana kiuhakika na kiikhlasi, hawavurugani. Ikitokea kutofautiana basi ni katika rai na mitazamo. “Kutofautiana rai hakuharibu mapenzi.” Na kuweko mitazamo tofauti kunaleta faida. Kwa sababu kauli yenye nguvu ni ile ambayo inakuwa na nguvu hata kama kuna kauli nyinginezo.
Na kwa hiyo Mwenyezi Mungu amewaumba.
Yaani Mwenyezi Mungu amewaumba kwa hiyo rehema na kwa kuhurumiana wao kwa wao. Itawapa rehema yake Mwenyezi Mungu mtukufu, ikiwa wataitafuta haki na kuitumia.
Abu Bakr almua’firiy Al-andalusi (Mhispania) anasema katika Kitabu Ahkamul Qur’ani: “Hakika Mwenyezi Mungu amewaumba watu ili watofautiane sio wahurumiane.”
Maana yake ni kwamba Mwenyezi Mungu anataka shari, kufru na maasi. Ikiwa Mwenyezi Mungu anataka shari basi kuna tofauti gani na Iblis aliyesema “Nitawapoteza wote”? Ametakata Mwenyezi Mungu na wanavyomsifu Juz. 7 (6:100).
Na litatimia neno la Mola wako: kwa hakika nitaijaza Jahannam kwa majini na watu kwa pamoja.
Yaani Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ataijaza Jahannam waasi wafuasi wa shetani miongoni mwa majini na watu. Mahali pengine Mwenyezi Mungu anasema:
قَالَ فَالْحَقُّ وَالْحَقَّ أَقُولُ ﴿٨٤﴾ لَأَمْلَأَنَّ جَهَنَّمَ مِنكَ وَمِمَّن تَبِعَكَ مِنْهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٨٥﴾
“Akasema: Haki na haki ninaisema. Hakika nitaijaza Jahannam kwa wewe na kwa wale wote wenye kukufuata miongoni mwao.” (38:84-85).
وَكُلًّا نَّقُصُّ عَلَيْكَ مِنْ أَنبَاءِ الرُّسُلِ مَا نُثَبِّتُ بِهِ فُؤَادَكَ وَجَاءَكَ فِي هَـٰذِهِ الْحَقُّ وَمَوْعِظَةٌ وَذِكْرَىٰ لِلْمُؤْمِنِينَ ﴿١٢٠﴾
120. Na yote tunayokusimulia katika habari za mitume ni ya kuufanya thabiti moyo wako. Na katika hii imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa wenye kuamini.
وَقُل لِّلَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ اعْمَلُوا عَلَىٰ مَكَانَتِكُمْ إِنَّا عَامِلُونَ ﴿١٢١﴾
121. Na waambie wale wasioamini: Fanyeni muwezavyo, nasi (pia) tunafanya.
وَانتَظِرُوا إِنَّا مُنتَظِرُونَ ﴿١٢٢﴾
122. Na ngojeni, hakika sisi tunangoja.
وَلِلَّـهِ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَإِلَيْهِ يُرْجَعُ الْأَمْرُ كُلُّهُ فَاعْبُدْهُ وَتَوَكَّلْ عَلَيْهِ وَمَا رَبُّكَ بِغَافِلٍ عَمَّا تَعْمَلُونَ ﴿١٢٣﴾
123. Na ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyofichikana katika ardhi na mbingu. Na mambo yote yatarejezwa kwake. Basi muabudu yeye na umtegemee yeye Na Mola wako si mwenye kughafilika na mnayoyafanya.
TUNAYOKUSIMULIA
Aya 120-123
MAANA
Na yote tunayokusimulia katika habari za mitume ni ya kuufanya thabiti moyo wako. Na katika hii imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa wenye kuamini.
Hii ni ishara ya sura, ukumbusho ni mazingatio na makusudio ya kuufanya thabiti moyo wa Mtume(s.a.w.w) ni subra na uvumilivu wa maudhi katika njia ya ujumbe wake na kuufikisha. Maana ni kuwa habari za mitume na watu wao tulizokusimulia ni haki hazina shaka na kwamba lengo lake ni kukupunguzia adha inayokupata.
Kwani anayeona masaibu ya mwingine, yake huyaona madogo. Vile vile katika visa hivi kuna mawaidha na mazingatio kwa mwenye kuwaidhika na kuzingatia.
Kwa hakika wanahistoria wa zamani walikuwa wakitilia umuhimu matukio ya siasa na dola na wapya wakatilia umuhimu uchumi, sayansi, sanaa, fasihi na mengineyo katika harakati za binadamu.
Lakini Qur’ani inaleta matukio kuwa ni mazingatio na mawaidha yatakayomwongoza binadamu kwenye njia iliyo sawa. Kauli yake Mwenyezi MunguMtukufu: “N mawaidha na ukumbusho” inaeleza hivyo. Aya nyingine inasema:
إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَعِبْرَةً لِّمَن يَخْشَىٰ ﴿٢٦﴾
“Hakika katika hayo mna mazingatio kwa anayemcha (Mwenyezi Mungu)” (79:26).
Na waambie wale wasioamini: Fanyeni muwezavyo, nasi (pia) tunafanya.
Umepita mfano wake katika Juz. 8 (6:135).
Na ngojeni, hakika sisi tunangoja.
Vile vile mfano wake umepita katika (6: 158).
Na ni vya Mwenyezi Mungu vyote vilivyofichikana katika ardhi na mbingu.
Kila siri kwake iko wazi na kila lililofichikana linaonekana. Katika mfano wa hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye; anajua kilichomo nchi kavu na kilichomo baharini; na halianguki jani ila analijua wala punje katika giza la ardhi; wala kibichi au kikavu, ila kimo katika Kitabu kinachobainisha.” Juz.7 (6:59).
Na mambo yote yatarejeshwa kwake.
Wala hakuna kitu kinachokimbia ufalme wake.
Basi muabudu yeye na umtegemee yeye.
Yaani ikiwa Mwenyezi Mungu yuko hivi, basi yeye ndiye mwenye kustahiki kuabudiwa na kutegemewa si mwengine. Amri ya kurukui na kusu- judi ni nyepesi, lakini kumtegemea Mwenyezi Mungu na kuachana na wengine, asiyekuwa Yeye ni jambo zito, isipokuwa kwa wanaomcha Mwenyezi Mungu.
Na Mola wako si mwenye kughafilika na mnayoyafanya.
Atawalipa wale waliofanya uovu kwa yale waliyoyafanya na atawalipa mema wale waliofanya mema. Imesemwa kwenye Nahjul balagha: “Usighafilike kwani wewe hujasahauliwa… Ee! Kuangamia kwa mwenye kughafilika kuwa umri wake ni hoja juu yake.” Tunamuomba Mwenyezi Mungu atuhifadhi na yale yanayoleta majuto na majonzi.
MWISHO WA SURA YA KUMI NA MOJA: SURAT HUD
8
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI
Surah Ya Kumi na Mbili: Surat Yusuf
Sura hii imeshuka Makka. Tabrasi akimnukuu Ibn Abbas, anasema kuwa kuna aya nne zilizoshuka Madina ambazo ni: 1,2,3,8.Ina Aya 111.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
الر تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ الْمُبِينِ ﴿١﴾
1. Alif laam raa. Hizo ni Aya za Kitabu kinachobainisha
إِنَّا أَنزَلْنَاهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لَّعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٢﴾
2. Hakika sisi Tumeiteremsha Qur’ani kwa kiarabu ili mpate kutia akilini.
نَحْنُ نَقُصُّ عَلَيْكَ أَحْسَنَ الْقَصَصِ بِمَا أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ هَـٰذَا الْقُرْآنَ وَإِن كُنتَ مِن قَبْلِهِ لَمِنَ الْغَافِلِينَ ﴿٣﴾
3. Sisi tunakusimulia simulizi nzuri sana kwa kukupa wahyi Qur’ani hii. Na hakika kabla ya haya ulikuwa miongoni mwa wasio na habari.
AYA ZA KITABU KINACHOBAINISHA
Aya 1-3
MAANA
Alif laam raa.
Umetangulia mfano wake katika mwanzo wa sura Baqara. Juz. 1 (2:1)
Hizo ni Aya za Kitabu kinachobainisha.
Hizo ni ishara ya Aya za sura hii na Kitabu kinachobainisha ni Qur’ani. Mwenyezi Mungu amekisifu kuwa ni chenye kubainisha, kwa sababu kinauweka wazi utume wa Muhammad(s.a.w.w) na kinadhihirisha uongofu
Hakika sisi Tumeiteremsha Qur’ani kwa kiarrabu ili mpate kutia akilini.
Maana yako ya wazi kwamba Mwenyezi Mungu ameiteremsha kwa lugha ya kiarabu ili watambue siri yake na utukufu wake, wayafahamua maana yake na wayatumie. Unaweza kuuliza: Muhammad ametumwa kwa watu wote kama inavyose-ma Qur’ani:
وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا ﴿٢٨﴾
“Na hatukukutumua ila kwa watu wote uwe mbashiri na muonyaji” (34:28).
Na kuteremshwa Qur’ani kwa lugha ya kiarabu kunafahamisha kuwa yeye ni wa Waarabu tu, si wa wengine. Sasa tutazioanishaje Aya mbili hizi?
Jibu :Kwanza : kuteremshwa Qur’ani kwa Lugha ya kiarabu hakummaaanishi kuwa waarabu peke yao ndio wanaokalifiwa na hukumu zake na mafunzo yake. Qura’ni yenyewe na wale wanaoiamini wanaisadikisha Tawrat iliyoteremshiwa Musa(a.s) na Injil iliyoteremshiwa Issa(a.s) na lugha ya vitabu hivyo siyo lugha ya Qur’ani wala ya wale wanayoiamini.
Pili : lugha ni nyenzo na maana ndio lengo. Haiwezekani kuwa maana yahusike na kaumu fulani tu. Kwani watu wote wanaamini ukaumu wa binadamu. Kwa maneno mengine lugha inahusika na watu fulani, lakini maana yanawaenea wote, hayana kundi fulani wala jinsi fulani.
Tatu ; ikiwa Mtume hatatumwa kwa lugha ya watu wake basi ataleta ujumbe kwa lugha gani na hakuna lugha inayozungumzwa na wote? Hapa ndipo inafichuka siri ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا بِلِسَانِ قَوْمِهِ لِيُبَيِّنَ لَهُمْ ﴿٤﴾
“Na hatukumtumma Mtume yeyote ila kwa lugha ya watu wake ili apate kuwabainishia.” (14:4).
Sisi tunakusimulia simulizi nzuri sana kwa kukupa wahyi Qur’ani hii.
Makusudio ya simulizi ni habari za mitume zilizokuja katika Qur’ani Tukufu, nazo ni habari nzuri sana kutokana na mafunzo na hekima zili- zomo ndani yake.
Na hakika kabla ya haya ulikuwa miongoni mwa wasio na habari.
Kwa sababu yalitokea karne zilizopita nayo hayajulikani kiujumla. Hii ni dalili mkataa kwamba ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
وَكَذَٰلِكَ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ رُوحًا مِّنْ أَمْرِنَا مَا كُنتَ تَدْرِي مَا الْكِتَابُ وَلَا الْإِيمَانُ ﴿٥٢﴾
“Na kama hivyo tulikupa wahyi roho (Qur’ani) kwa amri yetu. Hukuwa ukijua Kitabu ni nini wala imani.” (42:52).
Mwenye kuisoma vizuri Qur’ani, akayazingatia maana yake ataishia kuamini kwamba hakuna anayeweza kujua yote isipokuwa yule ambaye kila kitu amekizunguka kwa ujuzi wake.”
إِذْ قَالَ يُوسُفُ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ إِنِّي رَأَيْتُ أَحَدَ عَشَرَ كَوْكَبًا وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ رَأَيْتُهُمْ لِي سَاجِدِينَ ﴿٤﴾
4. Yusuf alipomwambia baba yake: Ewe baba yangu! Hakika mimi nimeota nyota kumi na moja na jua na mwezi nimeota zikinisujudia.
قَالَ يَا بُنَيَّ لَا تَقْصُصْ رُؤْيَاكَ عَلَىٰ إِخْوَتِكَ فَيَكِيدُوا لَكَ كَيْدًا إِنَّ الشَّيْطَانَ لِلْإِنسَانِ عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿٥﴾
5. Akasema: Ewe mwanagu! Usiwasimulie ndugu zako ndoto yako wasije wakakufanyia vitimbi. Hakika Shetani ni adui aliye dhahiri kwa mtu.
وَكَذَٰلِكَ يَجْتَبِيكَ رَبُّكَ وَيُعَلِّمُكَ مِن تَأْوِيلِ الْأَحَادِيثِ وَيُتِمُّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكَ وَعَلَىٰ آلِ يَعْقُوبَ كَمَا أَتَمَّهَا عَلَىٰ أَبَوَيْكَ مِن قَبْلُ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْحَاقَ إِنَّ رَبَّكَ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٦﴾
6. Na kadhalika Mola wako atakuteua na atakufundisha tafsiri ya mambo. Na atatimiza neema yake juu yako na juu ya ukoo wa Ya’qub; kama alivyowatimizia hapo zamani baba zako Ibrahim na Is-haq. Hakika Mola wako ni Mjuzi, Mwenye hekima.
NYOTA KUMI NA MBILI
Aya 4-6
MAANA
Yusuf alipomwambia baba yake: Ewe baba yangu! Hakika mimi nimeota nyota kumi na moja na jua na mwezi nimeota zikinisujudia.
Yusuf ni mtoto wa Ya’qub mtoto wa Is-haq mtoto wa Ibrahim Khalil(a.s ) . Ya’qub ndiye Israil. Maana ya Israil, wakati huo, ilikuwa ni Abdullah (Mtumishi wa Mwenyezi Mungu), lakini wakati huu ni mtumishi wa ukoloni na jeshi lake.
Siku moja Yusuf aliota ndoto aliyomsimulia baba yake Ya’qub. Nayo ni kwamba yeye aliona usingizini nyota kumi na moja na jua na mwezi zikimsujudia. Hapo baba yake akajua kuwa ndoto hii ni ya kweli, akapata bishara ya mustakbali wa mwanawe.
Kuna tafsiri zisemazo kuwa umri wa Yusuf wakati huo ulikuwa ni miaka saba; wala hatujui rejea sahii za kipimo hiki. Lakini ukweli ni kuwa yeye, wakati huo, alikuwa ni kijana mwenye haiba na mwenye sura nzuri, akipigiwa mfano kwa uzuri wake; kama itakavyobainika katika masimulizi ya kisa.
Nyota kumi na moja ni ndugu zake na jua na mwezi ni baba na mama yake. Hayo yanafahamika kutokana na kauli yake itakayokuja mbele kwenye Aya 100: “Hii ndiyo tafsir ya ile ndoto yangu” Ufafanuzi unafuatia.
Akasema ewe mwanagu! Usiwasimulie ndugu zako ndoto yako wasije wakakufanyia vitimbi. Hakika Shetani ni adui aliye dhahiri kwa mtu.
Baba yake alihofia ndugu zake wakisikia aliyomsimulia na wakafahamu alivyofahamu yeye wasije wakadhihirisha chuki yao kwake na wasighilibiwe na Shetani kwa kumfanyia vitimbi vya kumwangamiza. Kwa vile alijua wivu wao kwake kutokana na kumpenda sana na kutukuza kwake. Kwa hiyo akamnasihi asiwasimule ndoto yake. Tutaizungumzia ndoto mahali pake, inshaallah.
Na kadhalika Mola wako atakuteua na atakufundisha tafsiri ya mambo.
Kukuteua ni kukuchagua wewe si mwingine na kukujaza aina za karama. Imesemekana makusudio ya kutafsiri mambo ni kutafsiri ndoto, kwa vile Yusuf alikuwa na kiwango cha juu cha kutafsiri ndoto, lakini dhahiri ya neno inaenea zaidi ya hivyo. Linalonasibiana na utume wa Yusuf ni kuwa tafsri ya mambo ni fumbo la kujua hakika ya mambo na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) atamfundisha ambayo hakuwa akiyajua.
Na atatimiza neema yake juu yako na juu ya ukoo wa Ya’qub; kama alivyowatimizia hapo zamani baba zako Ibrahim na Is-haq.
Nema za Mwenyezi Mungu hazihisabiki na ukamilifu wake ni unabii na utume. Na amewaneemesha nao Ibrahim babu wa Ya’qub na Is-haq babu wa Yusuf na Ya’qub mwenyewe. Pia na atamneemesha nao Yusuf baada ya ndoto hii na wengineo katika wajukuu wa Ya’qub.
Hakika Mola wako ni Mjuzi Mwenye hekima.
Anamjua anayemchagua na kumteua kwa ujumbe na ana hekima katika uteuzi huo na katika mambo yote.
لَّقَدْ كَانَ فِي يُوسُفَ وَإِخْوَتِهِ آيَاتٌ لِّلسَّائِلِينَ ﴿٧﴾
7. Kwa hakika katika Yusuf na ndugu zake kuna ishara kwa wanaouliza.
إِذْ قَالُوا لَيُوسُفُ وَأَخُوهُ أَحَبُّ إِلَىٰ أَبِينَا مِنَّا وَنَحْنُ عُصْبَةٌ إِنَّ أَبَانَا لَفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٨﴾
8. Waliposema: Hakika Yusuf na nduguye wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko sisi na hali sisi ni kikundi imara. Hakika baba yetu yumo katika upotevu dhahiri.
اقْتُلُوا يُوسُفَ أَوِ اطْرَحُوهُ أَرْضًا يَخْلُ لَكُمْ وَجْهُ أَبِيكُمْ وَتَكُونُوا مِن بَعْدِهِ قَوْمًا صَالِحِينَ ﴿٩﴾
9. Muuweni Yusuf au mtupeni nchi ya mbali, uso wa baba yenu utawaelekea nyinyi. Na baada ya haya mtakuwa ni watu wema.
قَالَ قَائِلٌ مِّنْهُمْ لَا تَقْتُلُوا يُوسُفَ وَأَلْقُوهُ فِي غَيَابَتِ الْجُبِّ يَلْتَقِطْهُ بَعْضُ السَّيَّارَةِ إِن كُنتُمْ فَاعِلِينَ ﴿١٠﴾
10. Akasema msemaji kati yao: Msimuue Yusuf, lakini mtumbukizeni ndani ya kisima, watamuokota baadhi ya wasafiri, ikiwa nyinyi ni wenye kufanya.
قَالُوا يَا أَبَانَا مَا لَكَ لَا تَأْمَنَّا عَلَىٰ يُوسُفَ وَإِنَّا لَهُ لَنَاصِحُونَ ﴿١١﴾
11. Wakasema: Ewe baba yetu! Mbona hutuamini kwa Yusuf na hakika sisi ni wenye kumnasihi.
أَرْسِلْهُ مَعَنَا غَدًا يَرْتَعْ وَيَلْعَبْ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿١٢﴾
12. Mpeleke kesho pamoja nasi afaidi na acheze, na bila shaka sisi tutamhifadhi.
قَالَ إِنِّي لَيَحْزُنُنِي أَن تَذْهَبُوا بِهِ وَأَخَافُ أَن يَأْكُلَهُ الذِّئْبُ وَأَنتُمْ عَنْهُ غَافِلُونَ ﴿١٣﴾
13. Akasema: Kwa hakika inanihuzunisha kwamba nyinyi mwende naye, na ninahofia asije mbwa mwitu akamla nanyi mmeghafilika naye.
قَالُوا لَئِنْ أَكَلَهُ الذِّئْبُ وَنَحْنُ عُصْبَةٌ إِنَّا إِذًا لَّخَاسِرُونَ ﴿١٤﴾
14. Wakasema: Ikiwa mbwa mwitu atamla na sisi ni kundi imara, basi hakika sisi tutakuwa kwenye hasara.”
فَلَمَّا ذَهَبُوا بِهِ وَأَجْمَعُوا أَن يَجْعَلُوهُ فِي غَيَابَتِ الْجُبِّ وَأَوْحَيْنَا إِلَيْهِ لَتُنَبِّئَنَّهُم بِأَمْرِهِمْ هَـٰذَا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿١٥﴾
15. Basi walipokwenda naye na wakakubaliana wamtumbukize ndani ya kisima. Na tukampa wahyi bila shaka utakuja waambia jambo lao hili na hali hawatambui.
YUSUF NA NDUGUZE
Aya 7-15
MASILAHI KULIKO UDUGU
Binadamu ni mtumwa wa hisia zake, ni vigumu kuepukana nazo au kujipu- rukusha nazo. Kwa nini? Kwani inawezekana kukiepusha kitu na dhati yake? Kitu cha kwanza cha hisia hizi ni masilahi; yaani kutaka raha na kufukuza machungu. Maamuzi ya kufanya au kuacha jambo yanategemea masilahi.
Ama udugu si chochote ikiwa hauna raha au kuweka mbali machungu. Kwa hiyo kiwango cha pendo la mtu kwa jamaa zake linapimwa kwa masilahi haya. Mfano mzuri wa hilo ni kwamba huzuni na masikitiko ya kumpoteza ndugu yanakuja kutokana na kiwango cha alivyokuwa akinufaika naye wakati alipokuwa hai; kama ambavyo ndugu anaweza kuwa adui mkubwa akiwa anasababisha machungu au kuharibu raha na ladha.
Ni akina mama wangapi wamewaua watoto wao kwa sababu ya starehe tu?[2] Ni watoto wangapi wamewaua wazazi wao kwa sababu ya kuharakisha mirathi? Qabil alimuua Habil nao ni ndugu waliotokamana na tone moja la manii na wakawa katika mfuko mmoja wa uzazi.
Wana wa israil walimtupa Yusuf kwenye shimo bila ya kuwa na hurumma ya udugu na damu moja.
Ndio Ali, Amirul mumin(a.s) akasema:“ Udugu una haja kubwa zaidi ya mapenzi kuliko mapenzi kwenye udugu.” Hata mapenzi na urafiki chimbuko lake ni ladha ya roho, lakini mara nyingi mtu anjisahau na kusahau uhalisi wake, akaufanya udugu utokane na masilahi.
Kwa hiyo si dharura masilahi yawe ndiyo yanaupeleka utu. Kwani mtu safi aliye na ikhlas anaamini kwa kauli na vitendo kwamba masilahi yake ni masilahi ya jamii. Kwa hiyo anaumia ikiwa jamii inaumia na anafurahi ikiwa inafuraha. Anaona heri ni kuisimamisha haki na uadilifu.
Ama asiyekuwa hivyo basi haoni umuhimu ila umuhimu wake wala maisha isipokuwa maisha yake tu; kama walivyofanya wana wa israil kwa Yusuf ili wapate kupendwa wao na baba yao, lakini matokeo yake ni kuadhibiwa kwa kunyimwa na Mwenyezi Mungu hilo walilolitaka, wakastahiki hasira ya Mwenyezi Mungu na ya mtume wake Ya’qub na Yusuf akapata utukufu na cheo, wakasimama mbele yake wakiwa dhalili huku wakikiri makosa yao na kuomba msamaha kwa kusema: “Wallahi Mwenyezi Mungu amekufadhilisha wewe kuliko sisi na hakika sisi tulikuwa wenye makosa” Aya 91 ya sura hii.
Kwa hakika katika Yusuf na ndugu zake kuna ishara kwa wanaouliza.
Makusudio ya ishara hapa ni mazingatio na mafunzo.
Wana wa israil walimtupa Yusuf shimoni, si kwa lolote ila ni kwamba baba yao alikuwa akimpenda na kumhurumia zaidi. Maquraishi walimpiga vita Muhammad na wakafika kikomo cha kumuudhi, naye ni mquraishi mwenzao, kwa sababu tu Mwenyezi Mungu alimfanya bora kuliko wao na kuliko watu wote. Hata hivyo Mwenyezi Mungu alimnusuru Yusuf na ndugu zake na akamnusuru Muhammad na jamaa zake.
Katika hayo kuna mawaidha na mafunzo kwa wenye kutaka kujua uhakika na kufaidika nao.
Waliposema: Hakika Yusuf na nduguye wanapendwa zaidi na baba yetu kuliko sisi na hali sisi ni kikundi imara. Hakika baba yetu yumo katika upotevu dhahiri.
Maana ya Aya hii na inayoifuatia iko wazi, lakini pamoja na hayo tunaifuatilia kila Aya na yale yanayonasibiana nayo. Wana wa israil walipoona baba yao amelemea zaidi kwa Yusuf na ndugu yake, hasadi na chuki iliwachemka na wakaanza kuulizana: Kwa nini huyu mzee ameathirika na hawa watoto wawili na hali sisi ni wakubwa tena ni wengi wenye nguvu tulio na manufaana kumhudumia? Hakika huyu mzee amepotea.
Yusuf na nduguye, Benjamin, mama yao alikuwa mmoja, aliyeitwa Rachel. Mara nyingi hutokea chuki baina ya watoto kutokana na kuoa wake wengi.
Muuweni Yusuf au mtupeni nchi ya mbali uso wa baba yenu utawaelekea nyinyi.
Walikula njama ya kumuua si kwa chochote ila, ni kwa kutaka kuhodhi mapenzi ya baba yao; kama wanavyokiri wenyewe. Hii ndio mantiki ya wenye kuhodhi na kulimbikiza; ‘uwa na ufukuze’ hata kama ni ndugu wa damu, ili upate faida na chumo.
Na baada ya haya mtakua watu wema.
Wafasiri wanasema kuwa makusudi ya wema hapa ni wema wa dini; kwamba wao watatubia baada ya tendo lao hili ovu. Lakini dhahiri ya mfumo wa maneno inafahamisha kuwa makusudio ni kuwa wema kwa baba yao wao peke yao.
Akasema msemaji kati yao: Msimuue Yusuf, lakini mtumbukizeni ndani ya kisima, watamuokota baadhi ya wasafiri, ikiwa nyinyi ni wenye kufanya.
Katika Tawrat, Kitabu cha mwanzo 37:18-22, imesemwa kuwa aliyeyasema haya ni Reuben na ni ya yake ilikuwa ni kumtoa Yusuf kisimani baada ya kuondoka ndugu zake.
Wakasema: Ewe baba yetu! Mbona hutuamini kwa Yusuf na hakika sisi ni wenye kumnasihi, tunampenda na kumtakia kila la heri. Hivi ndivyo alivyo mwenye hadaa na vitimbi, kila mahali na kila wakati, ni mbwa mwitu katika ngozi ya kondoo.
Mpeleke kesho pamoja nasi afaidi na acheze, na bila shaka sisi tutamhifadhi.
Walijua kwamba baba yao anampenda Yusuf na anapenda afurahi na pia walijua jinsi alivyokuwa akimlinda sana. Kwa hiyo wakamwingilia kwa mlango huo huo. Yusuf anacheza huku wao wakimlinda na jambo lolote baya: ‘kikulacho kinguoni mwao.’
Akasema: Kwa hakika inanihuzunisha kwamba nyinyi mwende naye, na ninahofia asije mbwa mwitu akamla nanyi mmeghafilika naye.
Aliwapa udhuru kwamba yeye hawezi kuachana na Yusuf. Hilo likawazidishia chuki. Pia aliwapa udhuru kwamba anahofia asiliwe na mbwa mwitu. Razi anasema juu ya udhuru huu: Ni kama mbaye amewatafutia hoja. Mithali inasema: “Balaa iliponzwa na ulimi”
Wakasema: Ikiwa mbwa mwitu atamla na sisi ni kundi imara, basi hakika sisi tutakuwa kwenye hasara.
Mzee akaghurika na akawaachia Yusuf nao wakawa ni katika watu walio kwenye hasara.
Basi walipokwenda naye na wakakubaliana wamtumbukize ndani ya kisima, walilitekeleza hilo wakidhani kuwa wamepata yale waliyoyataka, lakini Yusuf alimkabidhi Mwenyezi Mungu mambo yake naye akamlinda na ubaya wa hila walizozifanya.
Na tukampa wahyi bila shaka utakuja waambia jambo lao hili na hali hawatambui.
Mwenyezi Mungu alimtuliza moyo Yusuf kwamba wewe utaokoka kutokana na mitihani yako hii na kwamba utawapa habari ya hili walilolifanya bila ya kukutambua.
BAINA YA WATOTO WA ISRAIL NA WATOTO WA MAULAMA
Kwa mnasaba huu mambo yanyonasibiana kati ya watoto wa maulama wa kidini na watoto wa Israil.
Watoto wa Israil walisema: “Hakika baba yetu yumo katika upotevu dhahiri.” Baadhi ya watoto wa mulama nao husema hivyo hivyo ikiwa wameambiwa na baba zao yale yasiyowapendeza hata kama ni maneno ya Mwenyezi Mungu.
Watoto wa Israil walisema: “Muuweni Yusuf au mtupeni nchi (ya mbali) uso wa baba yenu utawaelekea nyinyi”
Watoto wa maulama nao wanafanya hivyo hivyo. Wanawafanyia njama viongozi wazuri waliowaaminifu, wanawazushia mambo na kuwachafua ili nyuso za baba zao ziwaelekee wao. Wanawafanyia kazi mashetani wao kisha wanapata malipo kwa pesa za kigeni. Athari ikiwa kubwa zaidi na malipo nayo yanakuwa makubwa.
Watoto wa Israil walikuja na kanzu ya Yusuf “ina damu ya uongo” Kila siku baadhi ya watoto wa maulama wanakwenda na uzushi wanaowazushia watu wema, ili wao waonekani wazuri na waaminifu.
Watoto wa Isralil walikuja kwa baba yao “usiku wakilia” wakificha vitendo vyao kwa unafiki na machozi ya mamba.
Vile vile baadhi ya watoto wa maulama, mbele ya baba zao wanajifanya ni wacha Mungu wenye ikhlasi kwa uongo na ria.
وَجَاءُوا أَبَاهُمْ عِشَاءً يَبْكُونَ ﴿١٦﴾
16. Wakaja kwa baba yao usiku wakilia.
قَالُوا يَا أَبَانَا إِنَّا ذَهَبْنَا نَسْتَبِقُ وَتَرَكْنَا يُوسُفَ عِندَ مَتَاعِنَا فَأَكَلَهُ الذِّئْبُ وَمَا أَنتَ بِمُؤْمِنٍ لَّنَا وَلَوْ كُنَّا صَادِقِينَ ﴿١٧﴾
17. Wakasema: Ewe baba yetu! Hakika tulikwenda kushindana mbio na tukamwacha Yusuf kwenye vitu vyetu, basi mbwa mwitu akamla. Na wewe hutatuamini, ijapokuwa tunasema kweli.
وَجَاءُوا عَلَىٰ قَمِيصِهِ بِدَمٍ كَذِبٍ قَالَ بَلْ سَوَّلَتْ لَكُمْ أَنفُسُكُمْ أَمْرًا فَصَبْرٌ جَمِيلٌ وَاللَّـهُ الْمُسْتَعَانُ عَلَىٰ مَا تَصِفُونَ ﴿١٨﴾
18. Na wakaja na kanzu yake ina damu ya uongo, bali nafsi zenu zimewashawishi kutenda jambo, lakini subira ni njema. Na Mwenyezi Mungu ndiye wa kuombwa msaada kwa haya mnayoyasema.
وَجَاءَتْ سَيَّارَةٌ فَأَرْسَلُوا وَارِدَهُمْ فَأَدْلَىٰ دَلْوَهُ قَالَ يَا بُشْرَىٰ هَـٰذَا غُلَامٌ وَأَسَرُّوهُ بِضَاعَةً وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِمَا يَعْمَلُونَ ﴿١٩﴾
19. Ukaja msafara. Wakamtuma mchota maji wao. Akatumbukiza ndoo yake. Akasema: Ee habari njema! Huyu hapa mvulana! Wakamficha ili awe bidhaa. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wanayoyafanya.
وَشَرَوْهُ بِثَمَنٍ بَخْسٍ دَرَاهِمَ مَعْدُودَةٍ وَكَانُوا فِيهِ مِنَ الزَّاهِدِينَ ﴿٢٠﴾
20. Na wakamuuza kwa thamani duni kwa pesa za kuhisabiwa, na walikuwa hawana haja naye.
WAKAJA KWA BABA YAO WAKILIA
Aya 16-20
MAANA
Wakaja kwa baba yao usiku wakilia. Kwa kuvunga na kuyafinika waliyoyafanya. Wakasema: Ewe baba yetu! Hakika tulikwenda kushindana mbio na tukamwacha Yusuf kwenye vitu vyetu, basi mbwa mwitu akamla.
Kuna mithali inayosema “Damu ya Yusuf iko mbali na mbwa mwitu.” Imeelezwa kuwa msimulizi mmoja alikuwa akiwasimulia watu kisa cha Yusuf. Alipofika mahali pa mbwa mwitu, akasema mbwa mwitu aliyemla Yusuf anaitwa fulani. Wakasema waliokuwepo: Yusuf hakuliwa na mbwa mwitu! Akasema msimulizi: Basi naliwe hili ni jina la mbwa ambaye hakumla Yusuf.
Na wewe hutatuamini, ijapokuwa tunasema kweli.
Imam Ali(a.s) anasema:“Inatosha kua ni adhabu kwa muongo kuwa akisema ukweli haaminiwi
Na wakaja na kanzu yake ina damu ya uongo.
Maana yako wazi, lakini wafasiri walipokosa la kusema wakatofautiana kuhusu damu, kuwa je, ilkuwa ya paa au ya mwanakondoo. Wengine wamaesema kuwa Ya’qub alipoona kanzu ya mtoto wake ni nzima, alise- ma: Sijawahi kuona mbwa mwitu mpole kuliko huyu aliyemla mwanangu bila ya kuirarua kanzu yake.
Ama sisi tunatosheka na kuwa Ya’qub alisema:Bali nafsi zenu zimewashawishi kutenda jambo, lakini subira ni njema. Na Mwenyezi Mungu ndiye wakuombwa msaada kwa haya mnayoyasema.
Haya ndiyo yaliyoelezwa na wahyi kuhusu jawabu ya Ya’qub kuwaambia wanawe; wala hakuna dalili ya jengine.
Aya inaonyesha kuwa Ya’qub alitambua uongo wao kutokana na husuda yao kubwa kwa Yusuf. Lakini alisubiri na kumwachia mambo yake Mwenyezi Mungu.
Ukaja msafara.
Katika Tawrat Kitabu cha mwanzo imesemwa kwamba msafara wenyewe ulikuwa wa kizazi cha Ismail; yaani waarabu, kwa sababu nasabu yao inaishia kwa Ismail bin Ibrahim(a.s) .
Wakamtuma mchota maji wao. Yaani awaletee maji.Akatumbukiza ndoo yake.
Mchota maji alipomuona Yusuf alisema:Ee habari njema! Huyu hapa mvulana!
Anajipa habari yeye mwenyewe au anawapa jamaa zake. Basi wakamtoa kisimaniwakamficha ili awe bidhaa.
Walimficha na watu ili jamaa zake wasimjue, wakamfanya mtumwa aliye katika jumla ya bidhaa zao za biashara.
Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wanayoyafanya.
Yaani anajua siri yao ya kumfanya mtumwa na hali yeye ni mtu huru.
Na wakamuuza kwa thamani duni kwa pesa za kuhisabiwa.
Wafasiri wengi wamesema kuwa watu wa zama hizo wakipima pesa, kikiwa kitu thamani yake ni kubwa na wakihisabu ikiwa thamani ni ndogo. Na kwamba kusemwa pesa zenye kuhisabiwa ni ishara ya uchache wa thamani waliyouzia.
Na walikuwa hawana haja naye.
Ndio wakafanya haraka kumuuza kwa bei ya kutupa ili waondokane naye wasije wakatuhumiwa wizi.
9
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI
وَقَالَ الَّذِي اشْتَرَاهُ مِن مِّصْرَ لِامْرَأَتِهِ أَكْرِمِي مَثْوَاهُ عَسَىٰ أَن يَنفَعَنَا أَوْ نَتَّخِذَهُ وَلَدًا وَكَذَٰلِكَ مَكَّنَّا لِيُوسُفَ فِي الْأَرْضِ وَلِنُعَلِّمَهُ مِن تَأْوِيلِ الْأَحَادِيثِ وَاللَّـهُ غَالِبٌ عَلَىٰ أَمْرِهِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٢١﴾
21. Na yule aliyemnunua kule Misri alimwambia mkewe: Mtengenezee makazi ya heshima, huenda akatufaa au tukamfaya mtoto. Na kama hivyo tulimkalisha Yusuf katika nchi ili tumfundishe kufasiri mambo. Na mwenyezi Mungu ndiye mshindi katika jambo lake, lakini watu wengi hawajui.
وَلَمَّا بَلَغَ أَشُدَّهُ آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُحْسِنِينَ ﴿٢٢﴾
22. Na alipofikilia kukomaa kwake, tulimpa hukumu na elimu. Na hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.
ALIYEMNUNUA
Aya 21 -22
MAANA
Na yule aliyemnunua kule Misri alimwambia mkewe: “Mtengenezee makazi ya heshima, huenda akatufaa au tukamfaya mtoto.”
Yusuf alinadiwa sokoni na akanunuliwa na Aziz (mheshimiwa). Hii ni lakabu ya waziri mkuu wa mfalme. Linalotufahamisha kuwa yeye ndiye aliyemnunua ni kauli yake Mwenyezi Mungu kwnye Aya 30 katika sura hii: “Na wanawake wa mjini wakawa wanasema: Mke wa muheshimiwa anamtaka mtumishi wake pasipo kutakiwa naye”
Waziri alitambua werevu na akili ya Yusuf, akamwambia mkewe amuweke makazi ya kiheshima. Kwa maana ya kuwa akishakuwa mkubwa, aje asimamie mambo yao au wamfanye ni mtoto wao.
Kwa sababu mheshimiwa alikuwa mgumba, hana mtoto; kama walivyosema wafasiri wengi. Na Aya inaashiria hilo pale iliposema: “Au tumfanye mtoto”
Na kama hivyo tulimkalisha Yusuf katika nchi ili tumfundishe kufasiri mambo.
Mwenyezi Mungu alimneemesha Yusuf kwa kumwokoa na vitimbi vya ndugu zake, kumtoa kisimani, kumjaalia kuwa katika nyumba ya mheshimiwa, kumweka kwenye moyo wa mwenye nyumba na kumfundisha hakika ya mambo, ikiwa ni pamoja na kutabiri ndoto.
Neema zote hizi zilimwinua Yusuf mbele za watu na kumfanya awe ni tegemeo la watu wote na mwenye kuheshimiwa. Vile vile kuwekwa kuwa ndiye mweka hazina wa nchi ya Misr na kuambiwa na mfalme: “Hakika wewe leo kwetu ni mwenye heshima mwenye kuaminika”
Na mwenyezi Mungu ndiye mshindi katika jambo lake.
Ndugu zake Yusuf walimtakia shari na Mwenyezi Mungu alimtakia kheri.
إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٨٢﴾
“Hakika amri yake anapotaka chochote hukiambia ‘Kuwa,’ basi kinakuwa” (36:82).
Lakini watu wengi hawajui.
Kuwa amri ni ya Mwenyezi Mungu peke yake na kwamba mwenye kujifanya jeuri na kughurika na nguvu zake na uwezo wake, Mwenyezi Mungu atampatiliza kwa mashiko ya mwenye nguvu mwenye uweza.
Na alipofikilia kukomaa kwake, tulimpa hukumu na elimu.
Kukomaa hapa ni kukomaa kimwili na kiakili. Ahglab, hali hii huaanzia kwenye umri wa miaka thelathini na kuendelea hadi arobaini. Katika muda huu yanatimia maandalizi ya utume na kuanza wahyi. Makusudio ya hukumu hapa ni hekima; yaani kila kitu kukiweka mahali pake na kupatia.
Maana ni kuwa, baada ya Yusuf kukomaa, Mwenyezi Mungu alimpa elimu na kumwezesha kuitumia.
Imesemekana kuwa makusudio ya elimu hapa ni utume. Hilo haliko mbali. Kwa sababu Yusuf ni katika mitume.
Na hivyo ndivyo tunavyowalipa watendao mema.
Yusuf alitenda wema kwa uvumilivu wake na twaa yake kwa Mwenyezi Mungu, naye akamlipa mema kwa sababu yeye Mwenyezi Mungu hapotezi ujira wa yeyote mwenye kutenda jambo.
وَرَاوَدَتْهُ الَّتِي هُوَ فِي بَيْتِهَا عَن نَّفْسِهِ وَغَلَّقَتِ الْأَبْوَابَ وَقَالَتْ هَيْتَ لَكَ قَالَ مَعَاذَ اللَّـهِ إِنَّهُ رَبِّي أَحْسَنَ مَثْوَايَ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الظَّالِمُونَ ﴿٢٣﴾
23. Na bibi mwenye nyumba aliyokuwemo (Yusuf) alimshawishi kinyume cha nafsi yake. Na akafunga milango akasema: Njoo. Akasema: Najikinga kwa Mwenyezi Mungu. Hakika yeye ni Bwana wangu ameyatengeneza vizuri makazi yangu. Hakika waliodhulumu hawatengenekewi.
AKAMWAMBIA NJOO
Aya 23
MAANA
Na bibi mwenye nyumba aliyokuwemo (Yusuf) alimshawishi kinyume cha nafsi yake.
Neno alimshawishi linamaanisha kuwa alimfanyia vitimbi Yusuf ili atake vile anavyotaka yeye. Neno hili peke yake, linaonyesha kutojiheshimu. Lakini baadhi ya wafasiri wamechafua kurasa kuonyesha picha ya mke wa waziri kumvutia Yusuf kwa uzuri wake na ulimbwende wake. Na hayo hayana chimbuko lolote isipokuwa hadith za kiisrail. Amesema kweli mwenye Al-Manar: “Wapokezi wa kiisrail wamepokea riwaya zinazohusiana na Yusuf na mke wa waziri mambo ya ufedhuli ya uongo.
Mfano wa maneno hayo haujulikani kuwa unatoka kwa Mwenyezi Mungu, au kwa riwaya sahihi. Na hakuna yeyote anayedai hivyo”[3]
MTU NA MALI NA MAMBO YA KIJINSIYA NA AKAFUNGA MILANGO
Alijiuliza Mustafa Sadiq Arrafiy: kwanini ametumia neno waghallaqat, ambayo pia inakuwa kwenye mfumo wa kutilia mkazo jambo, na hakusema waaghlaqat? Na akajibu: “Hii inafahamisha kuwa yeye alipokata tamaa na kuona kuwa anataka kwenda zake, alikikuwa kama aliyepagawa akifikiria kufuli moja kama ni nyingi akakimbia kwenye mlango mmoja hadi mwingine, akiupigisha mkono wake, kama ambaye anajaribu kuziba milango sio kuufunga tu.”
Sisi hatuoni tofauti yoyote baina ya matamko hayo. Na hiyo inafahamisha tu uhodari wa Rafiy katika fasihi na uweza wake wa kutoa kitu kutoka kusiko na kitu.
Vyovyote iwavyo, ni kuwa Yusuf aliishi pamoja na mke wa waziri kwa muda mwingi akiwa ni barobaro mbichi, mwenye kuvutia. Kwa hiyo hakuna ajabu kwa mke wa waziri kuvutiwa naye wala si ajabu kwa Yusuf kuziepuka mbinu zake pamoja na kuwa matamanio mara nyingi yanashinda akali.
Kwani binadamu sio mtumwa wa matamanio yake ya kijinsia tu; kama asemavyo Freud; na wala si mtumwa wa mali na uchumi; kama asemavyo Marks. Ispokuwa anakuwa kwenye misukumo mingi, ikiwemo mambo ya kijinsia, mali, umashuhuri, utawala, dini, desturi kupenda nchi na mambo mazuri n.k. Kwa binadamu kuna misukumo miwili inayopingana:
Kheri inayomwongoza kwenye njia ya uongofu na shari inayompeleka kwenye njia ya maangamivu. Mara nyingine mvutano huu unaendelea kwa muda mfupi na mara nyingine kwa muda mrefu mpaka upande mmoja ushinde mwingine. Au hata unaweza kuendelea hadi mwisho, huku binadamu akiwa yuko huku na huku.
Mke wa waziri alipambana na mivutano miwili: Matamanio yake ya kinya- ma yaliyomfanya amtongoze Yusuf na kwa upande mwingine hadhi nakibri kinamkataza kujidhalilisha mbele ya aliyenunuliwa kwa thamani ndogo. Akabakia yuko katikati kiasi cha muda. Kisha akashindwa akanasa kwenye mtego wa matamanio ya kijinsia ambayo yanaonyeshwa na kauli yake: “Njoo.” Kauli hii si rahisi kuisema mwanamke ila yule aliyeshindwa kabisa, kiasi cha kuwa kama wazimu.
Ama Yusuf alikuwa na msukumo mmoja tu, unaomwongoza; na wala hakuna hata chembe ya msukumo mwingine katika moyo wake. Nao ni kumcha Mwenyezi Mungu na radhi yake. Hiyo peke yake ndiyo ladha yake na starehe yake, akasema:
Najikinga kwa Mwenyezi Mungu. Hakika yeye ni Bwana wangu ameyatengeneza vizuri makazi yangu. Hakika waliodhulumu hawatengenekewi.
Yaani najilinda kumwasi Mwenyezi Mungu. Vipi nimuasi na hali yeye amenipa hisani na fadhila nyingi; pale aliponitoa kisimani na akaufanya moyo wa waziri unipende na kuniweka kwenye daraja ya mwanawe. Na vipi nijidhulumu kwa kumwasi Mwenyezi Mungu na hali Mungu hawaongozi madhalimu? Hivi ndivyo ifanyavyo imani ya kweli. Inamlinda mtu na yaliyoharamu na kumpa ushindi katika kupambana na shetani na chama chake.
Wafasiri wengi wamesema kuwa dhamiri ya yeye ni bwana wangu inamrudia waziri kwa maana ya kuwa yeye ni mlezi wangu vipi nitamfanyia hiyana? Lakini mfumo wa maneno unaerejesha dhamiri kwa Mwenyezi Mungu kutokana na kuwa karibu na neno: “Najilinda kwa Mwenyezi Mungu,” kuongezea kuwa msukumo wa kujizuia Yusuf ni kumwofia Mwenyezi Mungu, sio waziri.
Kama tutakadiria kuwa dhamir inarudia kwa waziri, basi makusudio yatakuwa ni kumtahayariza kuwa anavyotakikana ni kuwa na heshima na mumewe ambaye amemfanya awe na daraja ya juu.
وَلَقَدْ هَمَّتْ بِهِ وَهَمَّ بِهَا لَوْلَا أَن رَّأَىٰ بُرْهَانَ رَبِّهِ كَذَٰلِكَ لِنَصْرِفَ عَنْهُ السُّوءَ وَالْفَحْشَاءَ إِنَّهُ مِنْ عِبَادِنَا الْمُخْلَصِينَ ﴿٢٤﴾
24. Na hakika (mke) alimtamani naye alimtamani kama asingeona dalili ya Mola wake. Hivyo ndivyo ilivyokuwa ili tumwepushie uovu na uchafu. Hakika yeye ni katika waja wetu waliotakaswa.
وَاسْتَبَقَا الْبَابَ وَقَدَّتْ قَمِيصَهُ مِن دُبُرٍ وَأَلْفَيَا سَيِّدَهَا لَدَى الْبَابِ قَالَتْ مَا جَزَاءُ مَنْ أَرَادَ بِأَهْلِكَ سُوءًا إِلَّا أَن يُسْجَنَ أَوْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٢٥﴾
25. Na wote wawili wakakimbilia mlangoni na mwanamke akairarua kanzu yake kwa nyuma. Wakamkuta bwana wake mlangoni. Akasema: Hapana malipo ya mwenye kukusudia uovu kwa mkeo isipokuwa kufungwa gerezani au kupewa adhabu iumizayo.
قَالَ هِيَ رَاوَدَتْنِي عَن نَّفْسِي وَشَهِدَ شَاهِدٌ مِّنْ أَهْلِهَا إِن كَانَ قَمِيصُهُ قُدَّ مِن قُبُلٍ فَصَدَقَتْ وَهُوَ مِنَ الْكَاذِبِينَ ﴿٢٦﴾
26. Akasema (Yusuf): Yeye ndiye aliyenitaka bila ya mimi kumtaka. Na shahidi, aliyekuwa katika jamaa za mke, akatoa ushahidi, ikiwa kanzu yake imechanwa mbele, basi mke ni mkweli na yeye (Yusuf) ni katika waongo.
وَإِن كَانَ قَمِيصُهُ قُدَّ مِن دُبُرٍ فَكَذَبَتْ وَهُوَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٢٧﴾
27. Na ikiwa kanzu yake imechanwa nyuma basi mke ni muongo na yeye Yusuf ni katika wakweli.
فَلَمَّا رَأَىٰ قَمِيصَهُ قُدَّ مِن دُبُرٍ قَالَ إِنَّهُ مِن كَيْدِكُنَّ إِنَّ كَيْدَكُنَّ عَظِيمٌ ﴿٢٨﴾
28. Basi mume alipoona kanzu imechanywa nyuma, alisema: Hii ni katika vitimbi vyenu (wanawake). Hakika vitimbi vyenu ni vikuu.
يُوسُفُ أَعْرِضْ عَنْ هَـٰذَا وَاسْتَغْفِرِي لِذَنبِكِ إِنَّكِ كُنتِ مِنَ الْخَاطِئِينَ ﴿٢٩﴾
29. Yusuf! Achana nayo haya. Na wewe mwanamke omba msamaha kwa dhambi zako, hakika wewe ni miongoni mwa wakosaji.
ALIMTAMANI NAYE AKAMTAMANI
Aya Ya 24-29
LUGHA
Amesema Tabrasi, katika Majmaul-bayan kuwa neno hamma (lililofasiriwa kwa maana ya kutamani) lina maana nyingi. Miongoni mwanzo ni kuazimia, kupitia na mawazo bila ya kuazimia, kutamani kitu nk.
Na hakika (mke) alimtamani naye alimtamani kama asingeona dalili ya Mola wake.
Tumezungumzia, katika Juz.1 (2:35-39) na 124. Vile vile Juz.5 (4:58-59), kuhusu isma (kuhifadhiwa na dhambi) ya mitume na kwamba mitume wote ni wenye kuhifadhiwa na dhambi. Hapo linakuja swali, kuwa Yusuf ni mwenye kuhifadhiwa na dhambi kwa sababu yeye ni mtume. Na kauli yake Mwenyezi Mungu:
Naye alimtamani, inaonyesha azma mbaya ya kuitikia matamanio ya mke wa waziri. Imekuwaje?
Wafasiri wamejibu kwa majibu ya kufedhehesha, wengine wakatoka nje ya dhahiri ya maneno. Jawabu lililo karibu zaidi na dhahiri ya maneno na heshima ya mitume ni lile lisemalo kuwa katika Aya kuna kutangulizwa maneno na kuja nyuma. Asili yake ni: Na hakika (mke) alimtamani naye kama asingeona dalili ya Mola wake angelimtamani. Yaani hakumtamani kabisa; kama vile kusema: alikuwa amekwisha yule kama si fulani.
Ubainifu wa pili ni: Mambo yote yalikuwa tayari. Mwanamke amejileta mwenyewe; kijana naye amekamilika kuwa mwanamume, wako peke yao, hakuna wa kuwasikia wala wa kuwaona. Lakini kulikuwa na kizuizi kimoja tu, kilichomzuia Yusuf, chenye nguvu kuliko makemeo yoyote na kikubwa zaidi ya kila anayesikia na anayeona.
Nacho ni kujua kwake halali ya Mwenyezi Mungu na haramu yake na yakini yake kwamba Mwenyezi Mungu yuko karibu naye zaidi kuliko kuliko mshipa wa shingo; na kwam- ba yeye Mungu anajua zaidi kilicho moyoni na kilichojificha.
Hiyo ndiyo dalili iliyomzuia Yusf na kufikiria haram na inayomzuia kila mwenye kumwamini kikwelikweli Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, awe mtume au sio mtume.
Kuna wengine wamesema kuwa Yusuf haikumdhihirikia dalili ya Mola wake ila alipomtamani. La hasha! Haiwi hivyo kwa mitume na wakweli. Hakika dalili ya Mwenyezi Mungu, haiondoki kwa wauminii wakweli.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa ili tumwepushie uovu na uchafu. Hakika yeye ni katika waja wetu waliotakaswa.
Uovu ni vitimbi vya mke wa waziri na uchafu ni zina. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaomcha ambao wanamkimbilia kwake wakiwa ni wenye ikhlasi; anawalinda na kuwahifadhi na kila anayewakusudia uovu au anyejaribu kuwaingiza kwenye upotevu; sawa na alivyofanya Yusuf, alikimbilia kwa Mola wake, huku akisema:
“ Na kama hutaniondolea vitimbi vyao nitawaelekea na nitakuwa miongoni mwa wajinga Basi Mola wake akamwitikia na akamuondoshea vitimbi vyao. Kama Hakika yeye ni msikizi Mjuzi”
Na wote wawili wakakimbilia mlangoni, na mwanamke akairarua kanzu yake kwa nyuma.
Yusuf alijaribu kumponyoka kwa kutoka pale nyumbani. Mwanamke naye akamfuatia nyuma, kama ngamia mkali, akamuwahi kabla ya kufika mlangoni, akamvuta kanzu yake kwa nyuma hadi ikachanika. Mara mume naye akaingia.
Wakamkuta bwana wake mlangoni.
Mwenye Tafsir Al-Manar anasema: “Wanawake wa Misri walikuwa wakiwaita waume zao bwana (sayyid) na hilo linaendela hadi leo.
Mume alipoingia nyumbani alimkuta Yusuf mlangoni alipomuona Yusuf amesimama mlangoni, huku kanzu yake ikiwa imeraruka; kabla ya kuuliza habari yoyote Akasema:
Hapana malipo ya mwenye kukusudia uovu kwa mkeo isipokuwa kufungwa gerezani au kupewa adhabu iumizayo.
Mke aliyasema haya kwa utulivu bila ya kuonyesha fadhaiko lolote. Anasema hapana malipo ya mwenye kukusudia uovu, nayeye mwenyewe ndiye muovu anayeutuhumu wema na usafi. Hii inatukumbusha wale ambao leo wameanzisha vita huko Vietnam, Mashariki ya kati, Kongo na kwengineko.
Na wanawapa silaha mabeberu ili wawamalize wanyonge huko Angola, Afrika kusini, Rhodesia (sasa ni Zimbwabwe), Latin Amerika na kwengineko. Wanaweka vituo vya kijeshi ardhini kote, mashariki na magharibi vikiwa na kila aina ya silaha za maangamizi.
Wanayafanya yote hayo kwa madai ya kuhifadhi amani na kuchunga haki za binadamu. Kwa hiyo hakuna ajabu kwa mwanamke huyo kuficha uongo wake kwa mumewe ili afiche makosa yake.
Akasema (Yusuf): Yeye ndiye aliyenitaka bila ya mimi kumtaka.
Nimejizuia naye na nikamkimbia akanipata hapa mlangoni akaifanyia hivi nguo yangu.
Na shahidi, aliyekuwa katika jamaa za mke, akatoa ushahidi.
Wafasiri wamerefusha maneno kuhusu shahidi huyu. Wengine wamesema ni binamu yake, wengine wakasema ni katika jamaa za mume na wengine wakasema alikuwa mtoto mchanga. Ama sisi tunasimama kwenye dhahiri ya wahyi amabo unafahamisha kuwa shahidi alikuwa ni katika jamaa za mke na alikuwa ni baleghe, kutokana kauli yake:
Ikiwa kanzu yake imechanwa mbele, basi mke ni mkweli na yeye Yusuf ni katika waongo na ikiwa kanzu yake imechanwa nyuma basi mke ni muongo na yeye Yusuf ni katika wakweli.
Haya ndiyo yaliyosemwa na wahyi. Ama kuwa shahidi alikuwa nani, alitoa vipi huo ushahidi, alikuja tu yeye mwenyewe au aliitwa na mengineyo, haya yamenyamaziwa na wahyi. Kuna hadith isemayo: “Mwenyezi Mungu ameyanyamazia mambo, basi msijikalifishe nayo.”
Basi mume alipoona kanzu imechanywa nyuma, alisema: Hii ni katika vitimbi vyenu (wanawake). Hakika vitimbi vyenu ni vikuu.
Mume alikinai na akawa na yakini ya ukweli wa Yusuf(a.s) na uongo wa mkewe, lakini akaona asitri aibu. Akatosheka na kusema: Hakika vitimbi vyenu ni vikuu.
Wasifu huu unawapendeza wanawake, kwa sababu unaonyesha werevu wao na kwamba wanaume hawawezi kwa kwa hila na vitimbi.
Unaweza kuuliza : Hapa imesemwa kuwa vitimbi vya wanawake ni vikuu na katika Juz.5 (4:76), imesemwa kuwa vitimbi vya shetani ni dhaifu; je maana yake ni kuwa mwanamke ana nguvu kuliko shetani?
Jibu : Vitimbi vya wanawake ni sehemu ya vitimbi vya shetani. Mkusudio ya kuwa vitimbi vya shetani ni dhaifu ni kuwa shetani hana nguvu kwa waja wa Mwenyezi Mungu; isipokuwa yule mwenye kumfuata katika wapotevu. Na makusudio ya kuwa vitimbi vya wanawake ni vikuu ni kuwa wao ndio askari wa shetani wenye nguvu zaidi. Imepokewa kutokana na iblis kwamba yeye amesema: “Ninapochachiwa na laana za watu wema huwaendea wanawake kujiliwaza…”
Kisha waziri akasema:Yusuf! Achana nayo haya. Yaani yafiche haya wala usimwambie mtu. Na akamwambia mkewe:Na wewe mwanamke omba msamaha kwa dhambi zako, hakika wewe ni miongoni mwa wakosaji.
Hii ni dalili mkataa kwamba mume alikuwa na hakika kuwa Yusuf hakuwa na makosa, na mkewe ndiye mwenye makosa. Abu Hayan Al-andalusi (mhispania) katika tafsir yake Albahrul-muhit anasema: “Waziri hakuwa na wivu mwingi na hii ni tabia ya watu wa Misr” Naye mwenye tafsir Al- Manar akamjibu: “Haya ni maneno ya kujisemea yasiyokuwa ya kielimu sahihi.” Nasi tunaongeza kuwa hiyo imesababishwa na hawa na ubinafsi.
Neno wakosaji hapa kwa kiarabu limetumika kwa khatwiin dhamiri inay- otumika kwa wote wanaume na wanawake kwa sababu makosa yanatokea kwa wote.
HUKUMU KWA USHAHIDI WA MAZINGIRA
Makusudio ya shahidi katika neno: ‘Na akashuhudia shahidi’ sio kuwa ni sharia kuchukua ushahidi wa aina hii; isipokuwa ni ujuzi wa kujua mambo yasiyojulikana. Kuchanika kanzu kunajulikana wazi na ni kawaida mtu akishikwa kwa nyuma, kanzu yake itachanika kwa nyuma, na akishikwa kwa mbele itachanika kwa mbele. Hapo anajulikana mkweli na muongo. Kwa mnasaba huu tunaashiria kuwa kuna aina tatu za kujua uhakika wa mambo:
1. Mambo yasiyokubalika kiakila; kwa mfano, mtu mwenye umri wa miaka arubaini kudai kuwa yeye ni mzazi wa mtu aliye na umri kama wake. Au kudai kuwa amerithi jengo fulani na inajulikana kwamba baba yake alikufa fukara. Madai kama haya na mfano wake, hayahitaji nukuu ya sharia katika kuyapinga.
2. Yanayotumika na kutegemewa na sharia; kama, kukiri makosa, ushahidi wa mwenyewe, ushahidi wa waadilifu wawili. Aina hii huitwa ‘ubainifu wa kisharia’ na katika sheria za kutungwa, wanaita: ‘ushahidi wa kikanuni.’ Wameafikiana wote kuwa ni wajibu kwa kadhi kuhukumu kulingana na nukuu za kisharia. Iwe ana uhakika au la.
3. Ushahidi wa kimazingira. Kutoa hukumu kwa ijtahadi yake na werevu wake kwa kulinganisha hali na mambo yanayoyazunguka madai. Kila madai yana mambo yake na hali zake na kila kadhi ana fahamu yake na ijtihadi yake. Miongoni mwa ulinganisho ni: ikiwa kanzu ime chanika kwa mble. Vile vile yale yaliyonasibishwa kwa Nabii Suleiman bin Daud(a.s) , au Imam Ali(a.s) alipohukumu baina ya wanawake wawili waliokuwa wakigombania mtoto mmoja, kila mmoja akisema ni wake; akasema nipeni kisu nimpasue katikati, mmoja akakataa na mwengine akakubali, akampa mtoto yule aliyekataa.
La kushangaza katika niliyoyasoma kuhusiana na maudhui haya ni kauli ya Shatibi katika Kitabu almuwafiqat Juzuu ya pili uk. 267 suala la 11: “Abu bakar alitekeleza wasia wa ndoto” Yaani mtu alikufa na hakuwahi kuusia katika uhai wake, kisha akaufikisha wasia wake kwa anayemtaka kwenye usingizi na Abu bakar akaupitisha wasia huo.
وَقَالَ نِسْوَةٌ فِي الْمَدِينَةِ امْرَأَتُ الْعَزِيزِ تُرَاوِدُ فَتَاهَا عَن نَّفْسِهِ قَدْ شَغَفَهَا حُبًّا إِنَّا لَنَرَاهَا فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٣٠﴾
30. Na wanawake wa mjini wakawa wanasema: Mke wa mheshimiwa anamtaka mtumishi wake pasipo kutamaniwa naye. Hakika amegubikwa na mapenzi. Sisi hakika tunamuona yuko katika upotevu uliodhahiri.
فَلَمَّا سَمِعَتْ بِمَكْرِهِنَّ أَرْسَلَتْ إِلَيْهِنَّ وَأَعْتَدَتْ لَهُنَّ مُتَّكَأً وَآتَتْ كُلَّ وَاحِدَةٍ مِّنْهُنَّ سِكِّينًا وَقَالَتِ اخْرُجْ عَلَيْهِنَّ فَلَمَّا رَأَيْنَهُ أَكْبَرْنَهُ وَقَطَّعْنَ أَيْدِيَهُنَّ وَقُلْنَ حَاشَ لِلَّـهِ مَا هَـٰذَا بَشَرًا إِنْ هَـٰذَا إِلَّا مَلَكٌ كَرِيمٌ ﴿٣١﴾
31. Aliposikia vitimbi vyao. Aliwaita na akawawekea matakia, na akampa kila mmoja wao kisu. Akasema: Tokea mbele yao. Walipomuona wakaona ni kitu kikubwa na wakakata mikono yao Na wakasema: “Hasha lillahi! Huyu si mtu, hakuwa huyu ila ni Malaika mtukufu.
قَالَتْ فَذَٰلِكُنَّ الَّذِي لُمْتُنَّنِي فِيهِ وَلَقَدْ رَاوَدتُّهُ عَن نَّفْسِهِ فَاسْتَعْصَمَ وَلَئِن لَّمْ يَفْعَلْ مَا آمُرُهُ لَيُسْجَنَنَّ وَلَيَكُونًا مِّنَ الصَّاغِرِينَ ﴿٣٢﴾
32. Akasema (yule bibi): Huyu ndiye mliyekua mkinilaumia. Hakika nilimtaka kinyume cha nafsi yake, lakini akakataa. Na akitofanya ninayomwamrisha basi hapana shaka atafungwa gerezani na atakuwa miongoni mwa madhalili.
قَالَ رَبِّ السِّجْنُ أَحَبُّ إِلَيَّ مِمَّا يَدْعُونَنِي إِلَيْهِ وَإِلَّا تَصْرِفْ عَنِّي كَيْدَهُنَّ أَصْبُ إِلَيْهِنَّ وَأَكُن مِّنَ الْجَاهِلِينَ ﴿٣٣﴾
33. Akasema: Ewe Mola wangu! Gereza linapendeza zaidi kwangu kuliko haya wanayoniitia. Na kama hutanion- dolea vitimbi vyao nitawaelekea na nitakuwa miongoni mwa wajinga.
فَاسْتَجَابَ لَهُ رَبُّهُ فَصَرَفَ عَنْهُ كَيْدَهُنَّ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٣٤﴾
34. Basi Mola wake akamwitikia na akamuondoshea vitimbi vyao; hakika yeye ni Msikizi, Mjuzi.
ثُمَّ بَدَا لَهُم مِّن بَعْدِ مَا رَأَوُا الْآيَاتِ لَيَسْجُنُنَّهُ حَتَّىٰ حِينٍ ﴿٣٥﴾
35. Kisha ikawadhihirikia baada ya kuona ishara ya kuwa wamfunge kwa muda.
MKE WA MHESHIMIWA NA WANAWAKE WA MJINI
Aya 30-35
LUGHA
Kugubikwa ni kufunikwa kabisa, yaani moyo wake ulifunikwa.
Na wanawake wa mjini wakawa wanasema: Mke wa mheshimiwa anamtaka mtumishi wake pasipo kutamaniwa naye. Hakika amegubikwa na mapenzi. Sisi hakika tunamuona yuko katika upotevu uliodhahiri.
Ilienea habari mjini, hasa kwa wanawake kwamba mke wa mheshimiwa amesalitika kimapenzi na mtumishi wake na akamtaka, lakini akakataa. Hilo ni kosa lisilosamehewa.
Aliposikia vitimbi vyao.
Yaani maneno yao. Yameeitwa vitimbi kwa vile hawakukusudia njia ya haki, bali ni kule kuenea tu. Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa pengine walimlaumu kwa kumwambia wazi wazi mwanamume, na kwamba ilitakikana watumie mbinu. Kauli hii inaweza kufaa kwa Malaya sio kwa wanaojihesimu.
Aliwaita na akawawekea matakia, na akampa kila mmoja wao kisu.
Alitaka kuwafanyia vitimbi, kama wao walivyomfanyia. Kwa hiyo akawaandalia karamu ya kukata na shoka, akawekea mito laini na chakula chenye ladha na kila mmoja akampa kisu cha kukatia nyama. Kutumia visu wakati huo kunafahamisha kuwa walikuwa wameendelea. Katika Tafsir Attabariy anasema: Kazi ya kisu katika karamu ni ya kukatia kinacholiwa tu. Kwa hiyo kikitajwa kisu ndio kimetajwa kinacholiwa.
Akasema kumwambia Yusuf:Tokea mbele yao. Walipomuona wakaona ni kitu kikubwa na wakakata mikono yao kutokana na mshangao mkubwa.
Baadhi ya wafasiri wanasema maana ya kukata hapa ni kujijeruhi. Lakini dhahiri ya neno kukata ni kukata tu, na mfano wa matukio haya hufasiriwa vingine ikiwa iko haja ya kufanya hivyo kwa sababu ya mikanganyo na sio kwa nukuu iliyo wazi.
Na wakasema: Hasha lillahi Huyu si mtu, hakuwa huyu ila ni Malaika mtukufu.
Alie katika umbo la binadamu, kutokana na haiba yake na uzuri, ambao ulimletea aina za balaa na mitihani.
Akasema yule bibi: Huyu ndiye mliyekua mkinilaumia.
Aliasema haya kwa uhuru ule wanaopigania wanawake wa sasa uhuru bila ya majukumu; hata katika kuvunja heshima na uharibifu. Sisi pia tunapigania uhuru wa wanaume na wanawake, lakini katika mipaka ya majukumu kikauli na kivitendo.
Hakika nilimtaka kinyume cha nafsi yake, lakini akakataa. Na akitofanya ninayomwamrisha basi hapana shaka atafungwa gerezani na atakuwa miongoni mwa madhalili.
Mwenye tafsir Al-Manar anasema: “Wallahi sistajabu kwa Yusuf kumkataa mwanamke aliyejileta mwenyewe; isipokuwa kustajabu kwangu ni mtazamo wake Yusuf kwa Mwenyezi Mungu haukuacha nafasi yoyote katika moyo wake wa kibinadamu wa kumwangalia mwanamke huyu aliyeshikwa na nyonda.” Nasi tunaongeza kwenye kauli hii kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) amepiga mfano kwa Yusuf wa mumin mwenye ikhlasi ili ajulikane mumin aliye kombo kombo ambaye huipeleka dini vile atakavyo yeye.
Akasema: Ewe Mola wangu! Gereza linapendeza zaidi kwangu kuliko haya wanayoniitia.
Makusudio ya kupendeza hapa sio kuwa ni zuri, isipokuwa ni hiyari tu yaani afadhali. Amesema wanayoniitia, kwa tamko la wengi. Kwa sababu wanawake waliomuona pia walimtamani, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu katka Aya 50 ya sura hii: “Rejea kwa bwana wako na umuulize habari ya wale wanawake waliokata mikono yao. Hakika Mola wangu anajua vizurivitimbi vyao”. Yusuf alihiyari gereza pamoja na uchungu wake na kuacha ladha ili apate mwisho mtamu.
Unaweza kuuliza : Ikiwa mtu atahiyarishwa baina ya zina na kufungwa gerezani na hawezi kuepuka moja ya mawili hayo, je inaruhusiwa kuzini?
Jibu : Hairuhusiwi. Kwa sababu hiyari hapo iko baina ya zina ambayo hiyo yenyewe ni haramu na kufungwa ambako ni haramu kwa dhalimu sio kwa mwenye kufungwa. Ila ikiwa kufungwa kutasababisha dhambi kubwa zaidi ya zina. Kwa hiyo mtu akihiyarishwa baina ya kuzini na kuua, basi atachagua kuzini. Lakini hiyo ni kwa asiyekuwa maasumu. Yeye an hukumu nyingine.
Na kama hutaniondolea vitimbi vyao nitawaelekea na nitakuwa miongoni mwa wajinga.
Vilipozidi vitisho na vivutio, Yusuf alihofia kudhoofika msimamo wake, kwa hiyo akamwelekea Mwenyezi Mungu akiomba kujinasua, huku akisema: Ewe Mola wangu! Yamenishukia nisiyoyaweza isipokuwa kwa msaada wako; na wewe ni muweza wa kuyaondoa. Na kama hutayaondoa nguvu zangu zitadhoofika na uwezo wangu utakuwa mchache.
Basi Mola wake akamwitikia na akamuondoshea vitimbi vyao; kama alivyomwondoshea vya ndugu zake hapo mwanzo. Mja yeyote hamfanyii ikhlasi Mwenyezi Mungu ila humjaalia matokeo na faraja.
وَكَانَ حَقًّا عَلَيْنَا نَصْرُ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٤٧﴾
“Na ililkuwa ni haki juu yetu kuwanusuru wauminii.” (30:47).
Hakika yeye ni Msikizi, Mjuzi.
Anasikia dua ya mwenye kumnyenyekea na anajua ikhlasi ya mwenye kumfanyia ikhlas.
Kisha ikawadhihirikia baada ya kuona ishara ya kuwa wamfunge kwa muda.
Dhamir ya ikawadhihirikia inamrudia mheshimiwa na mkewe na wengineo waliokuwa na maoni kama yao. Imesemekana kuwa inamrudia yeye peke yake na tamko la wengi likafaa kwa vile halikutajwa jina lake.
Makusudio ya ishara ni dalili zinazonyesha usafi wa Yusuf na kutokuwa na hatia. Hatia yake ni usafi wake na kujichunga. Kama angelikuwa mhalifu kama wao wasingempa cheo kikubwa.
Yusuf alikataa matakwa yao kwa hiyo wakamwadhibu kama mwenye hatia. Hivi ndivyo ilivyo katika historia yoyote.
Mtu mzuri anapata tabu katika mazingira ya dhulma, lakini Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wanaomcha na wakavumilia misukosuko katika njia yake si katika njia yao. Na muovu anampa muda kisha mambo humgeukia.
Na Mwenyezi Mungu humpa nguvu kwa nusra yake mwenye kuamini na akawa na subira; sawa na yaliyomtokea Yusuf pamoja na ndugu zake na mke wa mheshimiwa, pale mwisho ndugu zake walipomwambia:
“Wallahi Mwenyezi Mungu amekufadhilisha wewe kuliko sisi na hakika sisi tulikuwa wenye makosa” Aya: 90. Na mke wa mheshimiwa aliposema: “Sasa haki imedhihiri. Mimi ndiye niliyemtaka kinyume cha nafsi yake na hakika yeye ni katika wakweli” Aya: 51
10
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI
وَدَخَلَ مَعَهُ السِّجْنَ فَتَيَانِ قَالَ أَحَدُهُمَا إِنِّي أَرَانِي أَعْصِرُ خَمْرًا وَقَالَ الْآخَرُ إِنِّي أَرَانِي أَحْمِلُ فَوْقَ رَأْسِي خُبْزًا تَأْكُلُ الطَّيْرُ مِنْهُ نَبِّئْنَا بِتَأْوِيلِهِ إِنَّا نَرَاكَ مِنَ الْمُحْسِنِينَ ﴿٣٦﴾
36. Na wakaingia gerezani pamoja naye vijana wawili. Mmoja wao akasema: Hakika mimi nimeota nakamua mvinyo. Mwingine akasema: Hakika mimi nimeota nimebeba mkate juu ya kichwa changu na ndege wanaula hebu tuambie tafsiri yake. Kwani sisi tunakuona wewe ni katika watu wema.
قَالَ لَا يَأْتِيكُمَا طَعَامٌ تُرْزَقَانِهِ إِلَّا نَبَّأْتُكُمَا بِتَأْوِيلِهِ قَبْلَ أَن يَأْتِيَكُمَا ذَٰلِكُمَا مِمَّا عَلَّمَنِي رَبِّي إِنِّي تَرَكْتُ مِلَّةَ قَوْمٍ لَّا يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَهُم بِالْآخِرَةِ هُمْ كَافِرُونَ ﴿٣٧﴾
37. Akasema: Hakitawafikia chakula mtakachopewa ila nitawaambia hakika yake kabla hakijawafikia. Haya ni katika aliyonifundisha Mola wangu. Hakika mimi nimeacha mila ya watu wasiomwamini Mwenyezi Mungu na wao wanaikanusha siku ya mwisho.
وَاتَّبَعْتُ مِلَّةَ آبَائِي إِبْرَاهِيمَ وَإِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ مَا كَانَ لَنَا أَن نُّشْرِكَ بِاللَّـهِ مِن شَيْءٍ ذَٰلِكَ مِن فَضْلِ اللَّـهِ عَلَيْنَا وَعَلَى النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَشْكُرُونَ ﴿٣٨﴾
38. Na nikafuata mila ya baba zangu Ibrahim na Is-haq na Ya’qub. Haitufalii sisi kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote. Hiyo ni katika fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yetu na juu ya watu, lakini watu wengi hawashukuru.
GEREZANI PAMOJA NA VIJANA WAWILI
Aya 36-38
MAANA
Na wakaingia gerezani pamoja naye vijana wawili. Mmoja wao akasema: Hakika mimi nimeota nakamua mvinyo. Mwingine akasema: Hakika mimi nimeota nimebeba mkate juu ya kichwa changu na ndege wanaila.
Yusuf mtwaharifu aliingia gerezani na mke mchafu wa mheshimiwa akabaki kwenye jumba akiwa huru, anaamrisha na kukataza. Lakini Yusuf aliingia gerezani huku moyo umemtua akiwa na raha ya dhamiri, kuokoka na maasi na kufuzu kupata radhi ya Mwenyezi Mungu. Na mke wa mheshimiwa alikuwa katika gereza la adhabu iumizayo, adhabu ya dhamiri, fedheha na kukosa raha ya moyo.
Miongoni mwa walioingia gerezani pamoja na Yusuf ni vijana wawili kati- ka wafanyakazi wa mfalme: Anayehusika na vinywaji na mtunza vyakula kutokana na tuhumma walizobandikiwa. Yule wa vinywaji akasema nimeota ninakamua mvinyo. Na wa vyakula akasema ameota kichwani kwake kuna mkate unaoliwa na ndege na kwenda nao. Wakasema:
Hebu tuambie tafsir yake. Kwani sisi tunakuona wewe ni katika watu wema. katika sera yako.
Akasema: Hakitawafikia chakula mtakachopewa ila nitawaambia hakika yake kabla hakijawafikia.
Kuna karibu kauli sita zilizosemwa kuhusu tafsri ya Aya hii. Iliyokaribu zaidi ni ile isemayo kuwa Yusuf aliwaambia mimi na nyinyi tumezuiliwa hapa, hakuna hata mmoja anayejua kinachoendelea nje, lakini pamoja na hayo nitawaambia chakula mtakacholetewa, ni cha aina gani na lengo la kuletwa kwake.
Unaweza kuuliza : Yeye aliulizwa kuhusu ndoto naye anajibu mambo ya vyakula, kuna uhusiano gani?
Jibu : Ndio ni kweli kuwa hii si ibara ya ndoto, lakini ni utangulizi. Yusuf alitaka kuitumia nafasi hii ili kuwathibitishia wafungwa wenzake kwamba yeye ni Nabii aliyetumwa na Mwenyezi Mungu.
Akatoa dalili ya utume wake kwa kutolea habari mambo yaliyofichikana; sawa na alivyotoa dalili Nabii Issa(a.s) .
وَأُبْرِئُ الْأَكْمَهَ وَالْأَبْرَصَ وَأُحْيِي الْمَوْتَىٰ بِإِذْنِ اللَّـهِ وَأُنَبِّئُكُم بِمَا تَأْكُلُونَ وَمَا تَدَّخِرُونَ فِي بُيُوتِكُمْ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لَّكُمْ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿٤٩﴾
“Na niwaambie mnavyo vila na mtakavyoweka akiba. Hakika katika haya ipo ishara kwenu mkiwa ni wenye kuamini.” Juz.3 (3:49)
Kimsingi hasa, lengo la kwanza la Yusuf ni kuwaeleza wafungwa itikadi ya tawhid (umoja wa Mungu) na kuikubali siku ya mwisho; kama ilivyo kawaida ya mitume. Hilo linadhirika katika kauli yake:
Haya ni katika aliyonifundisha Mola wangu.
Yaani haya ya kuwaambia mambo yaliyofichikana sio ukuhani wala uchawi au utabiri; isipokuwa ni wahyi wa Mwenyezi Mungu alioniletea; kama alivyowa pelekea mitume katika mababa zangu.
Hakika mimi nimeacha mila ya watu wasiomwamini Mwenyezi Mungu na wao wanaikanusha siku ya mwisho.
Hii ni kupinga itikadi yao kwa upole, ili mafundisho yake yaingie nyoyoni mwao. Imeelezwa katika historia kwamba Wamisri wakati huo walikuwa wakiaabudu miungu, likiwemo jua na walikuwa wakiita ra na ndama wao (ibis).
Na nikafuata mila ya baba zangu Ibrahim na Is-haq na Ya’qub. Haitufalii sisi kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kitu chochote.
Majina ya wote hao yalikuwa maarufu kwa wote; hasa Ibrahim kipenzi(a.s) , ndio maana Yusuf akajinasibisha kwao kinasabu na dini.
Razi anasema: Yusuf alipodai utume na kuonyesha muujiza, wa kujua ghaibu, aliunganisha na kuwa yeye ni katika watu wa nyumba ya utume na kwamba mababa zake na mababu zake walikuwa mitume. Kwani mtu anapodai kuwa na kazi ya baba yake, basi haiwi uzito kuaminiwa nayo.
Vile vie daraja ya Ibrahim, ish-aq, na Ya’qub ilikuwa maarufu mbele za watu. ikibainika kuwa yeye ni katika watoto wao, basi wanamuadhimisha. Na kuathirika zaidi na maneno yake katika nyoyo zao.
Hiyo ni katika fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yetu na juu ya watu.
Yaani kuhusika kwetu na utume ni fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwa kutuona kua tunafaa. Vile vile ni fadhila kwa watu kwa vile wao wameongoka kwa sababu yetu sisi.
Lakini watu wengi hawashukuru.
Bali wanaendelea kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kumkana. Na kila wanavyozidi utajiri ndivyo wanavyozidi ukafiri na utaghuti.
يَا صَاحِبَيِ السِّجْنِ أَأَرْبَابٌ مُّتَفَرِّقُونَ خَيْرٌ أَمِ اللَّـهُ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿٣٩﴾
39. Enyi wafungwa wenzangu wawili! Je, waungu wengi wanaofarikiana ni bora au Mwenyezi Mungu mmoja mwenye nguvu?
مَا تَعْبُدُونَ مِن دُونِهِ إِلَّا أَسْمَاءً سَمَّيْتُمُوهَا أَنتُمْ وَآبَاؤُكُم مَّا أَنزَلَ اللَّـهُ بِهَا مِن سُلْطَانٍ إِنِ الْحُكْمُ إِلَّا لِلَّـهِ أَمَرَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ ذَٰلِكَ الدِّينُ الْقَيِّمُ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٤٠﴾
40. Hamuabudu badala yake ila majina matupu mliyoyapanga wenyewe na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuyateremshia dalili yoyote. Hapana hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu tu. Ameamrisha msimwabudu yoyote isipokuwa yeye tu. Hiyo ndiyo dini iliyonyooka, lakini watu wengi hawajui.
ENYI WAFUNGWA WENZANGU
Aya 39-40
MAANA
Enyi wafungwa wenzangu wawili! Je, waungu wengi wanaofarikiana ni bora au Mwenyezi Mungu mmoja mwenye nguvu?
Wafungwa wawili ni wale vijana wawili walioingia gerezani pamoja na Yusuf. Alijadiliana kuhusu wanaowaaabudu, ameleta majadala na hoja katika njia ya swali, kwa sababu hiyo ni njia nzuri zaidi ya kuiponda itikadi mbovu. Tumezungumzia kuhusu dalili ya Tawhid katika Juz.5 (4: 48)
Kisha Yusuf akapiga hatua ya pili katika kuelezea Tawhid na kuitupilia mbali shirk kwa kusema:
Hamuabudu badala yake ila majina matupu mliyoyapanga wenyewe na baba zenu. Mwenyezi hakuyateremshia dalili yoyote.
Nyinyi mnaabudu majina tu yasiyokuwa na maana yoyote, yaani hawako hao mnaowataja. Na kila kisichokuwapo hakina athari yoyote na ni muhali kuwasimishia dalili. Kwa hiyo mnaowaabudu ni wa kuwazia tu. Hivi ndivyo anavyofanya Mjuzi mwenye hekima. Hutumia mifumo mbalimbali kumkinaisha mjinga. Anaonyesha na kusema mpaka afikie kwenye lengo.
HAPANA HUKUMU ISPOKUWA YA MWENYEZI MUNGU
Hapana hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu tu. Ameamrisha msimwabudu yoyote isipokuwa yeye tu.
Maana ya msimwabudu ila yeye tu, iko wazi. Ama maana ya kuwa hukumu ni ya Mwenyezi Mungu, inahitaji tafsir. Kwa ufupi ni kuwa hukumu ya Mwenyezi Mungu iko mafungu mawili:
Kwanza : ni kupitisha kwake na makadirio yake ( kadha na kadar). Hii haiepukiki kwa binadamu.
Pili : ni halali ya Mwenyezi Mungu na haramu yake inayoitwa hukumu ya sharia. Inajulikana kwamba Mwenyezi Mungu hawasiliani na waja wake moja kwa moja katika maisha haya; isipokuwa anaweka sharia na kuzifikisha kupitia kwa mitume yake.
Haya ndiyo makusudio ya kuwa hukumu ni ya Mwenyezi Mungu. Kwamba yeye ndio chimbuko la sharia sio mtu mmoja wala vikundi; hakuna mwenye kuhalalisha au kuharamisha isipokuwa yeye tu.Yeyote mwenye kuhukumu hukumu yake haiwezi kuwa ya haki na uadilifu isipokuwa kama itaafikiana na aliyoyaleta Mwenyezi Mungu:
وَمَن لَّمْ يَحْكُم بِمَا أَنزَلَ اللَّـهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٤٥﴾
“Na wasiohukumu kwa yale aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu, basi hao ndio madhalimu.”
Juz.6 (5: 45).
Aya nyingine inasema hao ndio mafasiki na nyingine inasema hao ndio makafiri.
Kwa hiyo hukumu yoyote isiyofuata matakwa na radhi za Mwenyezi Mungu, basi ni ukafiri, dhula na ufasiki.
Tafsir hii tumeitoa kutokana na kauli ya Imam Ali(a.s) aliposikia kauli ya makhawarij waliposema: Hakuna hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu, alisema: “Ni neno la haki liliokusudiwa batili, ndio! Hakuna hukumu isipokuwa ya Mwenyezi Mungu, lakini hawa wanasema hakuna mamlaka ila ya Mwenyezi Mungu. Na ilivyo hasa hakuna budi aweko mwenye mamlaka aliye mwema, au muovu ambaye mamlaka yake yanatumiwa na mumin na anafurahika nayo kafiri.”
Yaani haki ya kuweka sharia ni ya Mwenyezi Mungu peke yake na nijuu ya watu kufuata aliyoyawekea sharia, na anayewachukua kwenye hilo ni mwenye mamlaka. Na makhawarij wamechanganya baina ya chimbuko la sharia na yule anayeifuata na anayeipotosha. Hawakutofautisha baina ya hawa wawili.
Hiyo ndiyo dini iliyonyooka, lakini watu wengi hawajui.
Hiyo ni ishara ya kudhibiti sharia na ibada kwa Mwenyezi Mungu tu. Maana ni kuwa dini yenye kunyooka ambayo haiko kombo kombo ni lile inayomuhusu Mwenyezi Mungu peke yake katika kuweka sharia na ibada. Binadamu yeyote haimfai kuwafanya watu wamwabudu au awawekee sharia ya hukumu, halali na haramu. Wote, hata mitume, ni waja wa Mwenyezi Mungu, wanafanya kulingana na amri yake na makatazo yake.
Maana ya yote haya ni kuwa watu wote ni ndugu waliosawa. Muumba wao amewapa haki ya ubinadamu ya milele, isiyokubali mabadilko wala marekebisho. Haki hizi zimedhihirisha maisha, uhuru na wema. Mwenye kuizuwiya haki basi huyo ni adui mkubwa wa Mwenyezi Mungu, dini yake na sharia yake.
يَا صَاحِبَيِ السِّجْنِ أَمَّا أَحَدُكُمَا فَيَسْقِي رَبَّهُ خَمْرًا وَأَمَّا الْآخَرُ فَيُصْلَبُ فَتَأْكُلُ الطَّيْرُ مِن رَّأْسِهِ قُضِيَ الْأَمْرُ الَّذِي فِيهِ تَسْتَفْتِيَانِ ﴿٤١﴾
41. Enyi wafungwa wenzangu wawili! Ama mmoja wenu atamnywesha bwana wake mvinyo. Na ama mwingine atasulubiwa na ndege watamla kichwa chake. Imekwisha katwa hukumu ya hilo jambo mlilokuwa mkiuliza.
وَقَالَ لِلَّذِي ظَنَّ أَنَّهُ نَاجٍ مِّنْهُمَا اذْكُرْنِي عِندَ رَبِّكَ فَأَنسَاهُ الشَّيْطَانُ ذِكْرَ رَبِّهِ فَلَبِثَ فِي السِّجْنِ بِضْعَ سِنِينَ ﴿٤٢﴾
42. Na akamwambia yule aliyemdhania kuwa ataokoka katika wawili hao: Unikumbuke mbele ya bwana wako. Lakini shetani akamsahaulisha kumtaja kwa bwana wake. Basi (Yusuf) akakaa gerezani miaka kadhaa.
UTABIRI WA NDOTO ZA WAFUNGWA WAWILI
Aya 41-42
Baada ya Yusuf kutekeleza wajib wa mwito wa kulingania kwa Mwenyezi Mungu, aliwafasiria ndoto zao. Yule muhusika wa vinywaji alimwambia utatoka jela na utarudia kazi yako.
Na yule wa vyakula akamwambia utasulubiwa na ndege watakula kichwa chako. Yusuf alikuwa na uhakika na utabiri wake, kwa vile ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ndio maana akawaambia kuwa mambo yamekwisha.
Yusuf akamwambia yule wa vinywaji ambaye ataokoka, kuwa amwambie mfalme kuwa yeye amefungwa bila ya hatia yoyote na hata bila ya kuhukumiwa au kuulizwa. Lakini akasahau kumkumbuka Yusuf kutokana na kazi nyingi. Kwa hiyo akamaliza miaka gerezani. Kuna riwaya inayosema alikaa miaka saba, nyingine inasema minane. Mungu ndiye ajuaye zaidi.
وَقَالَ الْمَلِكُ إِنِّي أَرَىٰ سَبْعَ بَقَرَاتٍ سِمَانٍ يَأْكُلُهُنَّ سَبْعٌ عِجَافٌ وَسَبْعَ سُنبُلَاتٍ خُضْرٍ وَأُخَرَ يَابِسَاتٍ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ أَفْتُونِي فِي رُؤْيَايَ إِن كُنتُمْ لِلرُّؤْيَا تَعْبُرُونَ ﴿٤٣﴾
43. Na akasema mfalme: Hakika mimi nimeota ng’ombe saba walionona wanaliwa na ng’ombe saba waliokonda; na mashuke saba mabichi na mengine makavu. Enyi wakubwa niambieni maana ya ndoto yangu ikiwa nyinyi mnaweza kutabiri ndoto.
قَالُوا أَضْغَاثُ أَحْلَامٍ وَمَا نَحْنُ بِتَأْوِيلِ الْأَحْلَامِ بِعَالِمِينَ ﴿٤٤﴾
44. Wakasema: Ni ndoto zilizoparaganyika wala sisi sio wenye kujua tafsir ya ndoto hizi.
وَقَالَ الَّذِي نَجَا مِنْهُمَا وَادَّكَرَ بَعْدَ أُمَّةٍ أَنَا أُنَبِّئُكُم بِتَأْوِيلِهِ فَأَرْسِلُونِ ﴿٤٥﴾
45. Na akasema yule aliyeokoka katika wale wawili, akakumbuka baada ya muda: Mimi nitawaambia tafsiri yake, basi nitumeni.
يُوسُفُ أَيُّهَا الصِّدِّيقُ أَفْتِنَا فِي سَبْعِ بَقَرَاتٍ سِمَانٍ يَأْكُلُهُنَّ سَبْعٌ عِجَافٌ وَسَبْعِ سُنبُلَاتٍ خُضْرٍ وَأُخَرَ يَابِسَاتٍ لَّعَلِّي أَرْجِعُ إِلَى النَّاسِ لَعَلَّهُمْ يَعْلَمُونَ ﴿٤٦﴾
46. Yusuf! Ewe mkweli! Tueleze nini maana ya ng’ombe saba wanene kuliwa na ng’ombe saba waliokonda na mashuke saba mabichi na mengine yaliyokauka Ili nirejee kwa watu wapate kujua.
قَالَ تَزْرَعُونَ سَبْعَ سِنِينَ دَأَبًا فَمَا حَصَدتُّمْ فَذَرُوهُ فِي سُنبُلِهِ إِلَّا قَلِيلًا مِّمَّا تَأْكُلُونَ ﴿٤٧﴾
47. Akasema: Mtalima miaka saba mfululizo. Mtakachovuna kiwacheni katika mashuke yake, isipokuwa kidogo mtakachokula.
ثُمَّ يَأْتِي مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ سَبْعٌ شِدَادٌ يَأْكُلْنَ مَا قَدَّمْتُمْ لَهُنَّ إِلَّا قَلِيلًا مِّمَّا تُحْصِنُونَ ﴿٤٨﴾
48. Kisha itakuja baadaye miaka saba ya shida itakayokula kile mlichokitanguliza, isipokuwa kidogo mtakachokihifadhi.
ثُمَّ يَأْتِي مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ عَامٌ فِيهِ يُغَاثُ النَّاسُ وَفِيهِ يَعْصِرُونَ ﴿٤٩﴾
49. Kisha baada ya haya utakuja mwaka ambao watu watapata mvua na watakamua.
NG’OMBE SABA WALIONONA
Aya 43-49
NDOTO NA NADHARIA YA FREUD
Ndoto ni dhahiri ya kinafsi. Wataalamu mbali mbali wamefanya utafiti na wakasema maneno mengi, lakini hawakuleta jambo la kutegemewa kuhusu ndoto kwa namna zake zote.
Ni kweli kwamba wamepatia katika kuelezea chanzo chake na wakagundua baadhi ya maradhi ya mishipa ya fahamu. Lakini kuna ndoto nyingine hazizungumzi lugha ya anayeiota wala nafsi au maisha yake. Wataalamu wameshindwa kuzielezea.
Freud amejaribu kukadiria tafsiri ya mamabo ya kijinsia kwenye ndoto zote; bali kwenye vitu vyote katika maisha haya au kwenye vitu vingi. Kwa hiyo ndoto zote kwake ni alama ya mambo ya kijinsia.
Mtoto mdogo wa kiume kumpenda zaidi mama yake na kumwonea wivu baba yake, kunatokana na fikra ya kinjisiya. Na vilevile msichana kumpenda zaidi baba yake na kumwonea wivu mama yake. Bali hata urafiki wa aina yoyote. Hata fikra ya dini pia, anasema, matokeo yake ni mambo ya kijinsiya; ndio maana dini ikahofia kulala pamoja maharimu.
Wataalamu wengi wameipinga fikra hii na wakasema kuwa binadamu anaendeshwa na matamanio mengi, sio mambo ya kijinsia tu. Gastro kutoka Poland, ametunga Kitabu cha kumjibu Freud katika juzuu mbili na akakiita Dream and sex na kikatarjumiwa ( kwa kiarabu) na Fauzi Shushtary.
Miongoni mwa yaliyomo katika Kitabu hicho ni kwamba maulama wamezichambua ndoto kwa maelfu kutoka kwa watu mbalimbali, wakakuta karibu asilimia hamsini za ndoto hizo haziwezekani kuzifasiri kwa nadharia ya Freud. Na nadharia hii inaacha maswali mengi yasiyokuwa na majibu.
Nadharia ya Freud haifuatwi isipokuwa na yeye mwenyewe. Yeye ni mwenye mawazo ya kuona kila kilicho mduara basi ni cha kike na kila kilicho mstatili basi ni kiume. Lakini ubinadamu uko mbali na nadharia hii. Nadharia hii ni finyu, haina ukweli. Binadamu sio mtumwa wa ngono tu; isipokuwa ni mtumwa wa starehe nyingi, ngono ikiwa moja yao. Nyingine ni mapenzi, urafiki, urembo, maarifa, utawala, nguvu na uhuru. Vizuri ni kuungana starehe zote hizi katika maisha ya pamoja yenye upeo mpana.
Tuanavyo ni kuwa ndoto ziko aina nyingi; kama ifuatavyo:-
Kuna zile zinazoakisi desturi na fikra ya mtu; kama mwanafalsafa kuota kuwa anajadiliana na Plato au Aristotle. Au Mwislamu kuswali msikitini, mkristo na msalaba wake kanisani, mkulima akilima shambani, mjenzi akijenga n.k. Aina hii ya ndoto iko wazi haihitaji ufafanuzi wala watu hawatofautiani kwayo. Kwa sababu iko pamoja na tafsiri yake.
Kuna zisizokuwa na uhusiano kabisa na maisha ya muotaji na fikra zake; kama mfalme kuota n’gombe saba na mashuke, ambapo yeye si mkulima wala mfugaji. Ndoto imekuja kuonya juu ya ukame baada ya rutuba.
Kuna ndoto nyingine ziko sawa na yale yaliyotokea mtu akiwa macho. Ndoto hii ni nadra kutokea.
Aina hizi mbili za mwisho za ndoto bado elimu haijagundua tafsir yake, pengine hivi karibuni inawezekana kujulikana. Wengine wamefasiri kuwa ni sadfa. Bila ya shaka sadfa ni kimbilio la kushindwa. Mwengine akatafsiri kuwa ni hisia za binadamu ambazo hazijulikani hakika yake. Huku ndiko kushindwa kabisa.
Mnamo mwaka 1956 nilimuota ndugu yangu, marehemu Sheikh Abdulkarim, aliyefariki miaka ishirini iliyopita. Akanipa habari ya mambo yatakayotokea na wakati wake. Ikawa kama alivyonieleza. Baadae nikaota ndoto nyingine mbaya kama ile ya mwanzo, ikatokea kama nilivyoota. Basi nikafanya utani na rafiki yangu na kumwambia kuwa ndoto mbaya huwa za kweli kinyume na ndoto za shari.
Nilipokuwa nafasiri sura Yusuf nilisoma ibara kwenye Tafsir ya Razi ikisema: “Jua kwamba wenye hekima wanasema kuwa ndoto mbaya zinajitokeza haraka” basi nikashangaa sana na kukumbuka mshairi aliyesema: Ubaya niutao uko karibu uzuri niutao uko janibu
Kwa ufupi ni kwamba hakuna udhibiti hasa wa kutegemea katika kufasiri ndoto kwa ukamilifu. Kwa sababu zinapingana. Kuna zinazotokea kwa wasiwasi wa nafsi na matatizo yake. Chimbuko la ndoto hii linajulikana, nyingine zinanukuu yale yaliyotokea kabla ya kulala. Aina hii hatuijui chimbuko lake. Nyingine ni ishara ya yatakayotokea baadae; kama vile nyota zilizomsujudia Yusuf, mkate uliochukuliwa na mfungwa na ng’ombe na mashuke aliyoyaota mfalme wa Misri. Hii pia haijulikani siri yake wala chimbuko lake.
Yule anayedai kuwa aina hizi mbili za ndoto ni bishara kutoka kwa Mwenyezi Mungu au ni hisia za binadamu, basi atakuwa amedai kuwa na elimu ya ghaibu, asiyekubali kuwa hajui hata yale aliyoyafunika Mwenyezi Mungu kwa waja wake.
MAANA
Na akasema mfalme: Hakika mimi nimeota ng’ombe saba walionona wanaliwa na ng’ombe saba waliokonda na mashuke saba mabichi na mengine makavu.
Siku moja Mfalme alota ndoto ya kushangaza kuwa ng’ombe walionona wanaliwa na waliokonda. Mfano wa ndoto kama hii haukuwahi kutokea. Vilevile mashuke saba mabichi na mengine saba makavu katika shamba moja. Akawaita wasaidizi wake na wakuu wa serkali yake na kuwaambia:
Enyi wakubwa niambieni maana ya ndoto yangu ikiwa nyinyi mnaweza kutabiri ndoto.”
Lakini walishindwa kutafsir na Wakasema:
Ni ndoto zilizoparaganyika wala sisi sio wenye kujua tafsir ya ndoto hizi.
Maana yako wazi, lakini Razi hapa ana maneno yenye faida, ambayo kwa ufupi ni kwamba Mwenyezi Mungu mtukufu alijaalia ndoto ya mfalme ni sababu ya kuokoka Yusuf(a.s) . Mwenyezi Mungu akitaka jambo huliandalia sababu zake. Mfalme ameshuhudia dhaifu akimtawala mwenye nguvu, jambo ambalo ni kinyume na maumbile.
Akaona kuwa inatoa onyo la shari, lakini ikawa hajui hakika yake. Kwa hiyo akawa na hamu sana ya kujua hakika yake. Akawakusanya watabiri na kuwauliza tafsir ya alivyoota, lakini Mwenyezi Mungu akawapofusha na hakika yake, ili iwe ni sababu ya kutoka Yusuf gerezani.
Kisha Razi akaendelea kusema: “Watabri hawakukataa kuwa na ujuzi wa kutabiri ndoto; isipokuwa waligawanya ndoto kwenye mafungu mawili: Zile zilizopangika ambazo zinakuwa nyepesi kuzijua na zile ambazo zimeparaganyika ambazo hazina tafsir isipokuwa dhana na kuwazia tu, na wakasema kuwa ndoto ya Mfalme ni katika ile isiyokuwa na tafsir au wa hawaijui; pengine yule aliyebobea kwenye ilimu ya ndoto anaweza kutafsiri”.
Na akasema yule aliyeokoka katika wale wawili, akakumbuka baada ya muda: Mimi nitawaambia tafsiri yake, basi nitumeni.
Itakumbukwa kwamba Yusuf aliingia gerezani na vijana wawili na akawatafsiria ndoto zao amabazo zilitokea kweli kama alivyowatafsiria. Mmoja aliuawa na mwingine akaokoka.
Aya hii inamuashiria yule aliyeokoka ambaye aliambiwa na Yusuf, ni kumbuke mbele ya bwana wako, lakini shetani alimsahauliza. Basi alipoona kudangana kwa mfalme kuhusu ndoto yake na hamu ya kutafsiriwa na kushindwa watabiri kuiagua, alimkumbuka Yusuf na akampa habari Mfalme za Yusuf, kuhusu wema wake na ujuzi wake wa kutafsiri ndoto, akamwambia kama ukinituma nitakuletea habari za uhakika.
Yusuf! Ewe mkweli! Tueleze nini maana ya ng’ombe saba walionona kuliwa na ng’ombe saba waliokonda na mashuke saba mabichi na mengine yaliyokauka.
Mfalme almwamrisha mtumishi wake wa vinywaji kwenda kwa huyo mtu mwema aliyemzungumizia na amwelezee hiyo ndoto kisha amletee habari atakazozisikia kwake. Yule mtumishi alikwenda kwa Yusuf, na kama kawaida akaomba msamaha kwa kusahau maagizo ya Yusuf. Baada ya kumsifu kwa ukweli alimsimulia ndoto ya Mfalme, na kumtaka amtafsirie huku akisema:
Ili nirejee kwa watu wapate kujua.
Yaani mfalme na wasaidizi wake wapate kujua hadhi yako na fadhila yako, ili waweze kukutoa gerezani.
Akasema mtalima miaka saba mfululizo. Mtakachovuna kiwacheni katika mashuke yake, isipokuwa kidogo mtakachokula.
Yusuf alimwambia kuwa watalima miaka saba mfululizo na kutakuwa na rutuba katika miaka hiyo. Hiyo inaishiriwa na ng’ombe saba walionona na mashuke ya kijani; kila ng’ombe na kila shuke likiashiria mwaka mmoja.
Kisha akawapa nasaha Yusuf kuwa kila watakachokivuna wakiweke akiba kikiwa kwenye mashuke yake, kwa sababu ngano ikiwa kwenye mashuke yake inahifadhika na wadudu waharibifu na inabaki kuwa kavu. Ama kile mnachotaka kukila basi mnaweza kukipukuchua huku mkichunga israf na kutosheka na kinachotosheleza haja tu.
Kisha itakuja baadaye miaka saba ya shida itakayokula kile mlichokitanguliza, isipokuwa kidogo mtakachokihifadhi.
Miaka imefanywa ndiyo inayokula, lakini makusudio yake ni watu, mara nyingi Waarabu wanatumia aina hii ya maneno. Maana ni kuwa miaka ya mavuno itafuatiwa na miaka ya ukame, hakitamea chochote ardhini. Hapo mtakula kile mlichokiweka akiba, na hakutabakia isipokuwa kiasi kidogo tu cha mbegu.
Kisha baada ya haya utakuja mwaka ambao watu watapata mvua na watakamua.
Yaani baada ya miaka saba ya shida utafuatia mwaka amabao utakuwa na mvua, mimea itamea na miti itanawiri, na watu watakamua matunda wapate vinywaji na mafuta.
Kwa hakika mwaka huu haukuashiriwa kwenye ndoto ya Mfalme, isipokuwa ni katika ghaibu za mwenyezi Mungu ambazo hawazijui isipokuwa wale aliowaridhia katika mitume.
وَقَالَ الْمَلِكُ ائْتُونِي بِهِ فَلَمَّا جَاءَهُ الرَّسُولُ قَالَ ارْجِعْ إِلَىٰ رَبِّكَ فَاسْأَلْهُ مَا بَالُ النِّسْوَةِ اللَّاتِي قَطَّعْنَ أَيْدِيَهُنَّ إِنَّ رَبِّي بِكَيْدِهِنَّ عَلِيمٌ ﴿٥٠﴾
50. Na mfalme akasema: Nileteeni. Basi mjumbe alipomjia Yusuf alisema: Rejea kwa bwana wako na umuulize habari ya wale wanawake waliokata mikono yao. Hakika Mola wangu anajua vizuri vitimbi vyao.
قَالَ مَا خَطْبُكُنَّ إِذْ رَاوَدتُّنَّ يُوسُفَ عَن نَّفْسِهِ قُلْنَ حَاشَ لِلَّـهِ مَا عَلِمْنَا عَلَيْهِ مِن سُوءٍ قَالَتِ امْرَأَتُ الْعَزِيزِ الْآنَ حَصْحَصَ الْحَقُّ أَنَا رَاوَدتُّهُ عَن نَّفْسِهِ وَإِنَّهُ لَمِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٥١﴾
51. Akasema: Mlikuwa mna nini nyinyi mlipomshawishi Yusuf kinyume cha nafsi yake? Wakasema: Hasha lillah! Sisi hatukujua ubaya wowote kwake. Mke wa mheshimiwa akasema: Sasa haki imedhihiri. Mimi ndiye niliyemtaka kinyume cha nafsi yake na hakika yeye ni katika wakweli.
ذَٰلِكَ لِيَعْلَمَ أَنِّي لَمْ أَخُنْهُ بِالْغَيْبِ وَأَنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي كَيْدَ الْخَائِنِينَ ﴿٥٢﴾
52. Hayo ni apate kujua kuwa mimi sikumfanyia khiyana alipokuwa hayuko. Na kwamba Mwenyezi Mungu haviongoi vitimbi vya wahaini.
MFALME AKASEMA NILETEENI
Aya 50-51
MAANA
Na mfalme akasema: Nileteeni.
Baada ya Yusuf kufasiri ndoto ya Mfalme, yule mjumbe alirudi kwa bwana wake na ule utabiri na nasaha. Na mfalme akagundua kuwa kwenye kauli ya Yusuf kuna elimu ikhlas na ukweli; akapenda awe karibu naye ili anufaike na elimu yake na ikhlasi yake, akasema aletewe huyo aliyefasiri. Qur’ani imetosheka na kauli hii ya mfalme na kumwacha msomaji aongeze mwenyewe.
Basi mjumbe alipomjia Yusuf na kumwita aende kwa Mfalme,alisema Yusuf:Rejea kwa bwana wako na umuulize habari ya wale wanawake waliokata mikono yao. Hakika Mola wangu anajua vizuri vitimbi vyao.
Yusuf alikataa kutoka gerezani na wala hakuwa na haraka ya kukimbilia mwito wa Mfalme, kama wafanyavyo wengi wanaojiita watu wa dini. Hakumharakia kwa kupima mambo yafuatayo:-
Kwamba mumin wa kweli hauoni ukubwa; isipokuwa ukubwa wa Mungu; wala hajali lolote katika njia ya kuidhihirisha haki na kuitangaza. Na kwa ajili hii, alikataa, siddiq (mkweli) kutoka gerezani hivi hivi tu, kwa msamaha wa raisi. Aliendelea kushikilia msimamo wa kuitangaza haki kabla ya chochote. Akahiyari kuvumilia kifungo maisha yote au atoke gerezani akiwa hana tuhumma yoyote.
Yusuf alipendelea upite uchunguzi akiwa yeye hayupo. Hilo litamasafisha zaidi na tuhumma na kufahamisha zaidi hadhi yake na upole wake.
Yusuf alikuwa na imani kwamba uchunguzi utakuwa kwa masilahi yake; na kutofanya haraka kutoka gerezani kutapelekea watu kuwa na imani naye na kuitikia mwito wa ujumbe wake.
Kuongezea kuwa hilo litakata njia ya atakayewasilisha tuhumma kwa Mfalme pale atakapokuwa karibu naye na kwa mwenginewe, atakapomwita kwenye haki.
Mjumbe alirudi kwa mfalme na kumpa habari kuwa Yusuf amekataa kutoka gerezani mpaka kufanywe uchunguzi wa kufungwa kwake.
Basi Mfalme akalichukulia umuhimu hilo na akawahudhurisha wanawake, akasema:
Mlikuwa mna nini nyinyi mlipomshawishi Yusuf kinyume cha nafsi yake? Wakasema: “Hasha lillah! Sisi hatukujua ubaya wowote kwake. Mke wa mheshimiwa akasema: Sasa haki imedhihiri. Mimi ndiye niliyemtaka kinyume cha nafsi yake na hakika yeye ni katika wakweli.
Huku ndiko kukiri hasa, kunakoondoa tuhumma na shakashaka zote, kwa sababu kunatoka kwa mtesi mwenyewe. Hana uovu… Yeye ni mkweli… Namna hii haki hudhihiri, hata muda ukiwa mrefu. Wanasalimu amri waovu wakiwa hawana la kufanya, hawana kimbilio wala kukana.
Hayo ni apate kujua kuwa mimi sikumfanyia khiyana alipokuwa hayuko.
Wafasiri wametofautiana kuhusu Aya hii: Kuna wanaosema kuwa haya ni maneno ya Yusuf kwa maana ya kuwa nimetaka uchunguzi pamoja na wanawake wengine ili mheshimiwa waziri ajue kuwa ikumfanyia khiyana kwa mkewe wakati hayuko.
Wengine wanasema kuwa ni maneno ya mke wa waziri. Sisi tuko pamoja na wanaosema hivi kwa kuangalia dhahiri ya mfumo wa kuungana maneno. Hapo dhamir ya sikumfanyia khiyana inamrudia Yusuf. Maana yake ni kuwa mke wa waziri hakumtaja kwa ubaya Yusuf wakati akiwa gerezani mpaka sasa. Hata pale alipomsingizia kwa mumewe mwenyewe Yusuf alikuwepo.
Na kwamba Mwenyezi Mungu haviongoi vitimbi vya wahaini.
Bali anawafedhehesha, anafichua siri yao na anawanusuru nao waumini, kama alivyowafedhehsha wanawake na kumnusuru Yusuf.
وَأَرَادُوا بِهِ كَيْدًا فَجَعَلْنَاهُمُ الْأَخْسَرِينَ ﴿٧٠﴾
“Na walimkusudia ubaya, lakini tukawafanya wao ndio wenye kupata hasara.” (21:70).
SHARTI YA KUCHAPA
Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)
Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.
MWISHO WA JUZUU YA KUMI NA MBILI
YALIYOMO
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI 1
IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA 1
IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA 1
IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED 1
IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU 1
UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI 1
MAKOSA YA CHAPA 2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI 3
HAKUNA MNYAMA YOYOTE KATIKA ARDHI 3
MAANA 3
KUHUSU MTU 5
MAANA 5
MBONA HAKUTEREMSHIWA HAZINA 7
MAANA 7
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI 9
WANAOTAKA MAPAMBO YA DUNIA 9
MAANA 9
WATAHUDHURISHWA MBELE YA MOLA WAO 12
MAANA 12
UJUMBE WA NUH 13
MAANA 13
NUH NA WATU WAKE 14
MAANA 14
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI 17
EWE NUH UMEZIDISHA MAJADILIANO NASI 17
MAANA 17
AKALETEWA WAHYI NUHU 18
MAANA 18
WAUMINI NA WENYE KEJELI 19
MAFURIKO 20
LUGHA 20
MAANA 20
NUHU AKAMWOMBA MOLA WAKE 22
MAANA 22
KIGANO CHA MWEZI 10, MUHARRAM 24
TUFANI IMETHIBITI KWA UMA NYINGINEZO 24
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI 25
NA KWA A’AD NDUGU YAO HUD 25
MAANA 25
WAKIRUDI NYUMA 28
MAANA 28
SWALEH 29
MAANA 29
NGAMIA WA MWENYEZI MUNGU 31
MAANA 31
MALAIKA WANAMBASHIRIA IBRAHIM 32
MAANA 32
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI 34
IBRAHIM ANAJADILI KUHUSU WATU WA NUH 34
MAANA 34
HUZUNI YA LUT 35
MAANA 35
HAWATAKUFIKIA 37
MAANA 37
SHUAIB 38
MAANA 38
HISTORIA YA UKOMUNISTI NA UBEPARI 40
MAANA 40
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI 43
LAU SI JAMAA YAKO TUNGEKURUJUMU 43
MAANA 43
MUSA 45
MAANA 45
HABARI ZA MIJI 46
MAANA 46
SIKU ITAKAYOSHUHUDIWA 47
MAANA 47
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI 50
NENO LILILOKWISHATANGULIA 50
MAANA 50
MSIMAMO 51
MAJUKUMU YA MSHIKAMANO DHIDI YA DHULMA 52
WATU WA KARNE ZILIZOTANGULIA 54
MAANA 54
TUNAYOKUSIMULIA 57
MAANA 57
MWISHO WA SURA YA KUMI NA MOJA: SURAT HUD 58
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI 59
AYA ZA KITABU KINACHOBAINISHA 59
MAANA 59
NYOTA KUMI NA MBILI 60
MAANA 60
YUSUF NA NDUGUZE 62
MASILAHI KULIKO UDUGU 62
BAINA YA WATOTO WA ISRAIL NA WATOTO WA MAULAMA 65
WAKAJA KWA BABA YAO WAKILIA 66
MAANA 66
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI 68
ALIYEMNUNUA 68
MAANA 68
AKAMWAMBIA NJOO 69
MAANA 69
MTU NA MALI NA MAMBO YA KIJINSIYA NA AKAFUNGA MILANGO 70
ALIMTAMANI NAYE AKAMTAMANI 71
LUGHA 71
HUKUMU KWA USHAHIDI WA MAZINGIRA 74
MKE WA MHESHIMIWA NA WANAWAKE WA MJINI 75
LUGHA 75
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA MBILI 78
GEREZANI PAMOJA NA VIJANA WAWILI 78
MAANA 78
ENYI WAFUNGWA WENZANGU 80
MAANA 80
HAPANA HUKUMU ISPOKUWA YA MWENYEZI MUNGU 80
UTABIRI WA NDOTO ZA WAFUNGWA WAWILI 82
NG’OMBE SABA WALIONONA 83
NDOTO NA NADHARIA YA FREUD 83
MAANA 84
MFALME AKASEMA NILETEENI 86
MAANA 86
SHARTI YA KUCHAPA 87
MWISHO WA JUZUU YA KUMI NA MBILI 87
YALIYOMO 88
[1] . Zimegongana kauli za wafasiri wengi walivyofahamu, kutokana na Aya, kuwa Mungu anamwambia Nuh, usiniombe na Nuh naye anamwambia Mungu sijakuomba. Wakaleta taawili zao za kuwazia tu,Tuliyoyaeleza yanabainisha kuwa Aya iko wazi haihitaji taawili.
[2] . Nimesoma kwenye gazeti kwamba mwanamke mmoja alikuwa na mpenzi wake na mtoto wake mdogo akiwa amelala naye, Mtoto alipolia yule mama akamnyonga. Vile vile nimesoma kwamba msichana mmoja alimuua baba yake kwa sumu, na alipoulizwa akasema: Nataka tubaki peke yetu nyumbani mimi na mpenzi wangu. Namna hii dini na dhamiri inaondoka yakija matamanio.
[3] . Sheikh Al-maraghi amenukuu ibara hii kwa herufi, lakini hakuashiria chimbuko lake au kuweka alama za nukuu. Amefanya hivi mara nyingi katika kauli za mwenye Al-Manar akimnukuu kwa kudhania kuwa yeye ndiye aliyesema na kumbe sheikh ana rai yake.