TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KUMI NA TISA Juzuu 19

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
Qurani tukufu

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA

IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED

IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.

Kama lilivyo jina la Tafsiri ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo.

Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.

Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea. Hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka kwa lugha ya kiswahili hivi karibuni Inshaallah).

Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasayansi kama kina Enstein, wasanii kama Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.

Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.

Mwisho: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.

MAKOSA YA CHAPA

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa, Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146), Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawamal qiyama. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu Jabal amil 'Makosa ya chapa.'

Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"

Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.

Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa.” Kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu." Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH


1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA

Mwendelezo Wa Sura Ya Ishirini Na Tano: Surat Al-Furqan.

وَقَالَ الَّذِينَ لَا يَرْجُونَ لِقَاءَنَا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْنَا الْمَلَائِكَةُ أَوْ نَرَىٰ رَبَّنَا لَقَدِ اسْتَكْبَرُوا فِي أَنفُسِهِمْ وَعَتَوْا عُتُوًّا كَبِيرًا ﴿٢١﴾

21. Na walisema wale wasiotarajia kukutana nasi: Mbona sisi hatuteremshiwi Malaika au hatumwoni Mola wetu. Hakika wametakabari katika nafsi zao na wameasi uasi mkubwa.

يَوْمَ يَرَوْنَ الْمَلَائِكَةَ لَا بُشْرَىٰ يَوْمَئِذٍ لِّلْمُجْرِمِينَ وَيَقُولُونَ حِجْرًا مَّحْجُورًا ﴿٢٢﴾

22. Siku watakayowaona Malaika, haitakuwa furaha siku hiyo kwa wakosefu, na watasema: Kuwe na kizuizi kizuiacho.

وَقَدِمْنَا إِلَىٰ مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاءً مَّنثُورًا ﴿٢٣﴾

23. Na tutayaendea yale waliyoyatenda katika matendo, kisha tutayafanya mavumbi yaliyotawanyika.

أَصْحَابُ الْجَنَّةِ يَوْمَئِذٍ خَيْرٌ مُّسْتَقَرًّا وَأَحْسَنُ مَقِيلًا ﴿٢٤﴾

24. Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makazi bora na mapumziko mazuri zaidi.

وَيَوْمَ تَشَقَّقُ السَّمَاءُ بِالْغَمَامِ وَنُزِّلَ الْمَلَائِكَةُ تَنزِيلًا ﴿٢٥﴾

25. Siku itakapopasuka mbingu kwa mawingu na watateremshwa malaika kwa wingi.

الْمُلْكُ يَوْمَئِذٍ الْحَقُّ لِلرَّحْمَـٰنِ وَكَانَ يَوْمًا عَلَى الْكَافِرِينَ عَسِيرًا ﴿٢٦﴾

26. Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Mwingi wa rehema. Na itakuwa siku ngumu kwa makafiri.

وَيَوْمَ يَعَضُّ الظَّالِمُ عَلَىٰ يَدَيْهِ يَقُولُ يَا لَيْتَنِي اتَّخَذْتُ مَعَ الرَّسُولِ سَبِيلًا ﴿٢٧﴾

27. Na siku dhalimu atajiuma mikono yake akisema: Laiti ningelishika njia pamoja na Mtume!

يَا وَيْلَتَىٰ لَيْتَنِي لَمْ أَتَّخِذْ فُلَانًا خَلِيلًا ﴿٢٨﴾

28. Ee ole wangu! Laiti nisingelimfanya fulani kuwa rafiki.

لَّقَدْ أَضَلَّنِي عَنِ الذِّكْرِ بَعْدَ إِذْ جَاءَنِي وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِلْإِنسَانِ خَذُولًا ﴿٢٩﴾

29. Kwa hakika amenipoteza nikaacha dhikri baada ya kunijia, na shetani ndiye anayemtupa mtu.

HAKUNA FURAHA KWA WAKOSEFU

Aya 21 – 29

MAANA

Na walisema wale wasiotarajia kukutana nasi: Mbona sisi hatuteremshiwi Malaika au hatumwoni Mola wetu.

Bado maneno yanaendelea kuwahusu washirikina, wasiotarajia kukutana na Mola wao, wala kuhofia adhabu yake.

Mwenyezi Mungu (s.w.t), katika Aya hii, amewazungumzia kwamba wao wamependekeza washuke Malaika ili wawape habari kuwa Muhammad ni Nabii au aje Yeye mwenyewe Mwenyezi Mungu atoe habari hiyo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (17:92)

Hakika wametakabari katika nafsi zao na wameasi uasi mkubwa.

Kuna kiburi gani kikubwa zaidi kuliko jeuri yao hii ya kutaka kumuona Mungu na kuzungumza naye ana kwa ana? Hawa hawana tofauti na wale waliosema kuwa hatumwamini Mungu mpaka tumuone, wakati huo wanaamini vitu ambavyo haviingii katika hisia yoyote.

Watu wa kimaada wanadai kuwa hakuna kitu chochote isipokuwa asili pofu ambayo ilijileta yenyewe au ilipatikana kwa sadfa, na ndiyo iliyoupangilia ulimwengu huu wa ajabu na iliyoumba usikizi na uoni. Katika mantiki yao ni kwamba asili ndiyo iliyo na uwezo wa kila kitu, lakini hiyo yenyewe haitambui kitu.

Wao wanajipinga wenyewe, kwa sababu kukubali kwao kupatikana nidhamu, ni kukiri kuweko nguvu yenye uwezo na ujuzi; na kusema kwao kuwa hakuna chochote isipokuwa asili pofu ni kuikana nguvu hiyo. Maana yake ni kuwa asili ina utambuzi na haina utambuzi, inajua na haijui.

Siku watakayowaona Malaika, haitakuwa furaha siku hiyo kwa wakosefu.

Washirikina walipendekeza washukiwe na malaika, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawajibu kuwa kutakuwa na siku ambayo watawaona malaika, Siku ya Kiyama, lakini hakutakuwa na jambo la kuwafurahisha , bali ni majanga juu ya majanga yatakayowapata:

يَوْمَ يَغْشَاهُمُ الْعَذَابُ مِن فَوْقِهِمْ وَمِن تَحْتِ أَرْجُلِهِمْ وَيَقُولُ ذُوقُوا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٥٥﴾

“Siku itakapowafunika adhabu kutoka juu yao na chini ya miguu yao, na atasema: Onjeni hayo mliyokuwa mkiyatenda” (29:55).

Na watasema: Kuwe na kizuizi kizuiacho.

Watakaosema ni malaika. Maana ni kuwa malaika watawaambia wakosefu, leo ni haramu mtazuiwa kuona mnayoyataka.

Imesemekana kuwa watakaosema ni wakosefu kuwaambia malaika kuwa haifai nyinyi leo kutuudhi na kutuadhibu.

Tafsiri zote mbili zinafaa na zinarejea kwenye maana moja ambayo ni kuhofia wakosefu shari ya siku ya Kiyama na vituko vyake.

Na tutayaendea yale waliyoyatenda katika matendo, waliyodhani kuwa yatawafaa leo,kisha tutayafanya mavumbi yaliyotawanyika.

Kwa sababu yalikuwa kwenye misingi isiyokuwa ya imani wala ikhalsi: “Mfano wa wale ambao wamemkufuru Mola wao vitendo vyao ni kama majivu yanayopeperushwa kwa nguvu za upepo katika siku ya kimbunga. Hawana uwezo wa chochote juu ya walichokichuma. Huko ndiko kupotelea mbali.” Juz. 13 (14:18).

Watu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makazi bora na mapumziko mazuri zaidi.

Makusudio ya bora na zaidi sio uzaidi wa mengine, isipokuwa makusudio ni kuwa makazi na mapumziko hayo yenyewe ni bora na mazuri; ni kama kusema Mwenyezi Mungu ni mkubwa zaidi, kwa maana ya kuwa ni mkubwa zaidi katika dhati yake na sifa zake.

Siku itakapopasuka mbingu kwa mawingu.

Makusudio ya siku hapa ni Siku ya Kiyama; na mawingu ni sayari ambazo zitakuwa chembechembe zisizoweza kuonekana hata kwa macho, zitaijaza anga, kama vile mawingu. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameashiria kuharibika kwa Siku hiyo, kwenye Aya nyingi; kama vile:

إِذَا الشَّمْسُ كُوِّرَتْ ﴿١﴾

“Jua litakapokunjwa.” (81:1),

وَإِذَا الْكَوَاكِبُ انتَثَرَتْ ﴿٢﴾

“Na nyota zitakapotawanyika.” (82:2).

Yaani jua litakapozimika na nyota zitakapoanguka.”

Na watateremshwa malaika kwa wingi, wakiwa na ya kuwafurahisha wema na kuwachukiza wakosefu.

Ufalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Mwingi wa rehema Yeye tu peke yake, hakuna atakayekuwa na lolote.

Na itakuwa siku ngumu kwa makafiri.

Hakuna siku ngumu zaidi kwa mkosefu kuliko siku ya kuhukumiwa kwake, kuhisabiwa makosa yake na kutolewa hukumu ya haki na uadilifu? Lau angelihukumiwa kunyongwa ingelikuwa mambo yamekwisha, lakini ni hukumu ya kudumu:

كُلَّمَا نَضِجَتْ جُلُودُهُم بَدَّلْنَاهُمْ جُلُودًا غَيْرَهَا لِيَذُوقُوا الْعَذَابَ ﴿٥٦﴾

“Kila zitakapoiva ngozi zao, tutawabadilishia ngozi nyingine ili waonje adhabu.” Juz.5 (4:56).

Na siku dhalimu atajiuma mikono yake akisema: Laiti ningelishika njia pamoja na Mtume!

Hiki ni kinaya cha majuto na masikitiko. Hapo ndio ukomo wa kila mwenye kughurika, mzushi na muongo. Miongoni mwa dua zilipokewa kutoka kwa Nabii(s.a.w.w) ni:“Ewe Mola wangu! Najilinda kwako na madhambi yanayoleta majuto.”

Ee ole wangu! Laiti nisingelimfanya fulani kuwa rafiki.

Makusudio ya fulani hapa ni kila mwenye kufuatwa aliyempoteza mfuasi wake na kumwongoza kwenye maangamizi. Kuna Hadith isemayo:“Mtu atafufuliwa kwenye dini ya rafiki yake.”

Jamaa katika wafasiri wamesema kuwa Aya hii ilimshukiwa Uqba bin Mu’it na Ubayya bin Khalaf. Kwamba dhalimu atakayeuma mikono yake ni huyo wa kwanza na fulani ni huyo wa pili. Hata kama tukikadiria usahihi wa riwaya, ni kuwa sababu ya kushuka Aya haizuwii kuenea kwa wengine.

Hakika amenipoteza nikaacha dhikri baada ya kunijia, na shetani ndiye anayemtupa mtu.

Makusudio ya dhikri hapa ni Qur’an, kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) amelitumia neno hili kwa kukusudia Qur’an katika Aya kadhaa; kama vile:

ص وَالْقُرْآنِ ذِي الذِّكْرِ ﴿١﴾

“Naapa kwa Qur’an yenye dhikri.” (38:1).

Aya inafahamisha kuwa wale walioisikiza Qur’an walikinai kwenye nafsi zao, lakini mashetani-watu waliwadanganya na wakawaepusha na haki, ikawa mwisho wao ni kufedheka. Na huu ndio mwisho wa kila mwenye kufanya kwa maelekezo ya watu wa hawa, si kwa maelekezo ya imani yake na dhamiri yake.

وَقَالَ الرَّسُولُ يَا رَبِّ إِنَّ قَوْمِي اتَّخَذُوا هَـٰذَا الْقُرْآنَ مَهْجُورًا ﴿٣٠﴾

30. Na Mtume alisema: Ewe Mola wangu! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur’an ni mahame.

وَكَذَٰلِكَ جَعَلْنَا لِكُلِّ نَبِيٍّ عَدُوًّا مِّنَ الْمُجْرِمِينَ وَكَفَىٰ بِرَبِّكَ هَادِيًا وَنَصِيرًا ﴿٣١﴾

31. Na hivi hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wakosefu. Na Mola wako anatosha kuwa mwenye kuongoza na mwenye kunusuru.

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا نُزِّلَ عَلَيْهِ الْقُرْآنُ جُمْلَةً وَاحِدَةً كَذَٰلِكَ لِنُثَبِّتَ بِهِ فُؤَادَكَ وَرَتَّلْنَاهُ تَرْتِيلًا ﴿٣٢﴾

32. Na walisema wale ambao wamekufuru: Mbona haikuteremshwa kwake Qur’an yote mara moja? Ndivyo hivyo, ili tuuimarishe kwayo moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu.

وَلَا يَأْتُونَكَ بِمَثَلٍ إِلَّا جِئْنَاكَ بِالْحَقِّ وَأَحْسَنَ تَفْسِيرًا ﴿٣٣﴾

33. Wala hawatakuletea mfano wowote ila nasi tutakuletea haki na tafsiri iliyonzuri.

الَّذِينَ يُحْشَرُونَ عَلَىٰ وُجُوهِهِمْ إِلَىٰ جَهَنَّمَ أُولَـٰئِكَ شَرٌّ مَّكَانًا وَأَضَلُّ سَبِيلًا ﴿٣٤﴾

34. Wale watakaokusanywa kifudifudi kwenye Jahannam, hao watakuwa mahali pabaya na ndio wenye kupotea njia sana.

وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ وَجَعَلْنَا مَعَهُ أَخَاهُ هَارُونَ وَزِيرًا ﴿٣٥﴾

35. Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamuweka pamoja naye nduguye, Harun, kuwa waziri.

فَقُلْنَا اذْهَبَا إِلَى الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا فَدَمَّرْنَاهُمْ تَدْمِيرًا ﴿٣٦﴾

36. Tukawaambia nendeni kwa watu waliozikadhibisha Ishara zetu, basi tukawaangamiza kabisa.

وَقَوْمَ نُوحٍ لَّمَّا كَذَّبُوا الرُّسُلَ أَغْرَقْنَاهُمْ وَجَعَلْنَاهُمْ لِلنَّاسِ آيَةً ۖ وَأَعْتَدْنَا لِلظَّالِمِينَ عَذَابًا أَلِيمًا ﴿٣٧﴾

37. Na watu wa Nuh walipowakadhibisha mitume, tuliwagharikisha na tukawafanya ni ishara kwa watu. Na tumewaandalia madhalimu adhabu chungu.

وَعَادًا وَثَمُودَ وَأَصْحَابَ الرَّسِّ وَقُرُونًا بَيْنَ ذَٰلِكَ كَثِيرًا ﴿٣٨﴾

38. Na kina Ad na Thamud na watu Rass na vizazi vingi vilivyokuwa baina yao.

وَكُلًّا ضَرَبْنَا لَهُ الْأَمْثَالَ وَكُلًّا تَبَّرْنَا تَتْبِيرًا ﴿٣٩﴾

39. Na wote tuliwapigia mifano na wote tuliwaangamiza kabisa kabisa.

وَلَقَدْ أَتَوْا عَلَى الْقَرْيَةِ الَّتِي أُمْطِرَتْ مَطَرَ السَّوْءِ أَفَلَمْ يَكُونُوا يَرَوْنَهَا بَلْ كَانُوا لَا يَرْجُونَ نُشُورًا ﴿٤٠﴾

40. Na kwa hakika wao walifika kwenye mji ulionyeshewa mvua mbaya, basi je hawakua wakiuona? Bali walikuwa hawatarajii kufufuliwa.

WAMEIFANYA QUR’AN NI MAHAME

Aya 30 – 40

MAANA

Na Mtume alisema: Ewe Mola wangu! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur’an ni mahame.

Yaani wameachana nayo na wakakataa kuiamini au kuipa mtazamo wa kutafuta haki ili kuwa na yakini nayo. Vigogo wa kikuraishi waliukadhibisha unabii wa Muhammad(s.a.w.w) na yaliyosemwa na Qur’an kwa kuhofia uchumi wao na kupupia vyeo vyao.

Ndipo Mtume akapeleka mashtaka yake kwa Mola wake ambaye mambo yote yako mikononi mwake. Hivi ndivyo afanyavyo mwenye akili, hashtakii haja yake isipokuwa kwa yule ambaye hukumu ya mashtaka hayo iko mikononi mwake.

Ndio, inawezekana mtu kumshtakia rafiki yake atakayemliwaza na kumpa moyo. Imam Jafar Sadiq(a.s) amesema:“Mwenye kumshtakia ndugu yake amemshitakia Mwenyezi Mungu, na mwenye kumshtakia mwingine atakuwa amemshtaki Mungu.” Anakusudia ndugu wa kiimani, na kwamba muuminii akimshtakia muuminii kama yeye humwombea Mungu ampe faraja na kumwamrisha awe na subira, kumtegemea Mwenyezi Mungu na kutokata tamaa na rehema yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, lakini akimshitakia asiyekuwa muumini humshakizia au kumshauri kuepukana na Mungu.

Na hivi hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wakosefu.

Mkombozi anaweza akamwambia taghuti, ewe mkosefu, na kumlaumu kwa ufisadi, upotevu na kuvunja haki za binadamu na mengineyo, lakini taghuti ametulia tu, wala hajali. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6:112).

Huko tumejibu swali la: Ikiwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye aliyewajaalia Manabii wawe na maadui, kama inavyoonyesha Aya, kwa nini basi awaadhibu kwa kuwafanyia uadui Mitume?

Na Mola wako anatosha kuwa mwenye kuongoza na mwenye kunusuru.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume(s.a.w.w) yakiwa na ahadi kutoka kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kumsaidia Mtume wake kutokana na maadui zake; kama alivyomsadia kumuongoza kwenye haki na kuidhihirisha dini yake kuliko dini zote, wajapochukia washirikina.

Na walisema wale ambao wamekufuru: Mbona haikuteremshwa kwake Qur’an yote mara moja?

Qur’an ilishuka kwa vipindi kulingana na haja ya watu. Mwanzo wa kushuka kwake ulikuwa pale Mtume(s.a.w.w) alipokuwa na miaka arubaini ya umri wake mtukufu. Ukaendelea wahyi kushuka polepole mpaka pale Mtume alipohama kwenda mahali pa hali ya juu akiwa na miaka 63.

Washirikina walijaribu kila mbinu kuwaepusha watu na Qur’an. Wakasema ni vigano vya watu wa kale, lakini hawakuendelea na mbinu hii, kwa sababu ilikuwa ikijipinga yenyewe. Wakatafuta propaganda nyingine, wakasema mbona Qur’an isiteremshwe mara moja, kwani Mungu anahitaji kufikiria, kama wafanyavyo watunzi?

Hata kama ingeliteremka mara moja wasingelikosa la kusema, kama kawaida ya wapinzani, kuwa mbona isingeliteremka kidogo kidogo ili tuweze kuifahamu, kuathirika nayo na kuizowea. Lakini ukweli hujitokeza, hata wakiupinga.

Ndivyo hivyo, ili tuuimarishe kwayo moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu.

Yaani tumeiteremsha Qur’an kwa mpangilio wa moja baada ya nyingine, ili moyo wake uwe na nguvu ya kuuhifadhi, kufahamu maana yake na kudhibiti hukumu zake.

Wala hawatakuletea mfano wowote ila nasi tutakuletea haki na tafsiri iliyo nzuri, wale watakaokusanywa kifudifudi kwenye Jahannam, hao watakuwa mahali pabaya na ndio wenye kupotea njia sana.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume(s.a.w.w) . Watakaoleta mfano na kufufuliwa kifudifudi ni washirikina. Makusudio ya mfano wowote ni kila wanalomtaaradhi nalo Mtume mtukufu.

Katika Aya ya 5, ya Sura hii kwenye Juzuu iliyopita, wanapinga kwa kusema kuwa ni ngano za watu wa kale, katika Aya ya 7, wanasema kwa nini anakula na kutembea sokoni, katika Aya 8, wanasema amerogwa, katika Aya ya 21, iliyo kwenye Juzuu hii, wanasema kwa nini hakuteremshiwa malaika au tumuone Mungu na katika Aya 32 wanasema kwa nini isiteremshwe mara moja.

Baada ya kuyabatilisha madai yao haya ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) hapa anamwambia Mtume wake:‘Wala hawatakuletea mfano wowote ila nasi tutakuletea haki na tafsiri iliyo bora’

Yaani washirikina watakujadili kwa batili na sisi tutakuunga mkono kwa haki iliyo wazi na hoja ambayo itavunja kauli zao na kufedhesha batili zao. Hiyo ni hapa duniani. Ama malipo yao huko akhera, ni kuwa mazabania watawavuta kwenye nyuso zao.

Ambaye atakuwa katika hali hii huyo ndiye muovu wa viumbe vya Mungu na mwenye makazi mabaya zaidi.

Na hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamuweka pamoja naye nduguye, Harun, kuwa waziri. Tukawaambia nendeni kwa watu waliozikadhibisha Ishara zetu, basi tukawaangamiza kabisa.

Kisa cha Musa na Firauni kimekwishatangulia kwenye Aya kadhaa; miongoni mwazo ni: Juz.9 (7:103 – 145). Katika Juz. 16 (20:9), tumezungumzia sababu za kukaririka kisa cha Musa(a.s) .

Na watu wa Nuh walipowakadhibisha mitume, tuliwagharikisha na tukawafanya ni Ishara kwa watu. Na tumewaandalia madhalimu adhabu chungu.

Pia kisa cha Nuh kimekwishapita mara kadhaa. Tazama Juz.12 (11:25 – 49).

Na kina Ad na Thamud na watu a Rass.

Rass ni jina la kisima na watu wake ni kaumu ya Shu’ayb. Imetangulia mifano katika Juz. 12 (11:50 – 61 na 84 – 95).

Na vizazi vingi vilivyokuwa baina yao.

Yaani, vile vile tuliangamiza kaumu nyingi zilizokuwa baina ya kina Ad na watu wa Rass, kwa sababu wao waliwakadhibisha manabii na mitume.

Na wote tuliwapigia mifano na wote tuliwaangamiza kabisa kabisa.

Tuliwaangamiza baada ya ubainifu, onyo, mawaidha ya visa na kupiga mifano, lakini wao waling’ang’ania ukafiri na upotevu. Ikawa malipo yao ni kuangamizwa.

Na kwa hakika wao walifika kwenye mji ulionyeshewa mvua mbaya, basi je hawakua wakiuona? Bali walikuwa hawatarajii kufufuliwa.

Makusudio ya mji hapa ni mji wa kaumu ya Lut kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَلُوطًا آتَيْنَاهُ حُكْمًا وَعِلْمًا وَنَجَّيْنَاهُ مِنَ الْقَرْيَةِ الَّتِي كَانَت تَّعْمَلُ الْخَبَائِثَ ﴿٧٤﴾

“Na Lut tukampa hukumu na elimu na tukamwokoa na ule mji uliokuwa ukifanya maovu.” Juz. 17 (21:74).

na pia kauli yake:

فَلَمَّا جَاءَ أَمْرُنَا جَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهَا حِجَارَةً مِّن سِجِّيلٍ مَّنضُودٍ ﴿٨٢﴾

“Basi ilipofika amri yetu tuliigeuza juu chini. Na tukawateremshia mvua ya mawe ya udongo mkavu yaliyopandana.” Juz. 12 (11:82).

Maana ni kuwa washirikina walipokuwa kwenye misafara yao wakipitia mji wa Lut na kuona athari ya maangamizi na kubomoka, walitakiwa wapate funzo na waamini utume wa Muhammad, lakini wakapinga na kuwa na inadi, kwa sababu hawana yakini na ufufuo, hisabu na malipo.


2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA

وَإِذَا رَأَوْكَ إِن يَتَّخِذُونَكَ إِلَّا هُزُوًا أَهَـٰذَا الَّذِي بَعَثَ اللَّـهُ رَسُولًا ﴿٤١﴾

41. Na wanapokuona hawakufanyii ila kejeli tu, ati huyu ndiye Mwenyezi Mungu aliyemtuma kuwa mtume?

إِن كَادَ لَيُضِلُّنَا عَنْ آلِهَتِنَا لَوْلَا أَن صَبَرْنَا عَلَيْهَا وَسَوْفَ يَعْلَمُونَ حِينَ يَرَوْنَ الْعَذَابَ مَنْ أَضَلُّ سَبِيلًا ﴿٤٢﴾

42. Kwa hakika alikuwa karibu kutupoteza kwa miungu yetu, kama tusingelikazana juu yao. Na karibu watajua watakapoiona adhabu, ni nani aliyepotea njia.

أَرَأَيْتَ مَنِ اتَّخَذَ إِلَـٰهَهُ هَوَاهُ أَفَأَنتَ تَكُونُ عَلَيْهِ وَكِيلًا ﴿٤٣﴾

43. Je, umemuona aliyeyafanya matamanio yake kuwa ndio Mungu wake? Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake?

أَمْ تَحْسَبُ أَنَّ أَكْثَرَهُمْ يَسْمَعُونَ أَوْ يَعْقِلُونَ إِنْ هُمْ إِلَّا كَالْأَنْعَامِ بَلْ هُمْ أَضَلُّ سَبِيلًا ﴿٤٤﴾

44. Au unadhani kwamba wengi wao wanasikia na wanafahamu? Hao hawakuwa ila ni kama wanyama howa; bali wao wamepotea zaidi njia.

ATI HUYU NDIYE MTUME?

Aya 41 – 44

MAANA

BAINA YA ISA NA MUHAMMAD

Na wanapokuona hawakufanyii ila kejeli tu, ati huyu ndiye Mwenyezi Mungu aliyemtuma kuwa Mtume?

Kwa muda wa miaka 13, Mtume(s.a.w.w) alikuwa akiwalingania watu wake kwenye imani ya Mungu mmoja, akiamrisha uadilifu na kukataza dhulma. Mbele yake mweusi na mweupe walikuwa sawa. Vile vile tajiri na fukara. Hakuna kuzidiana isipokuwa kwa takua.

Si ajabu kuwa hili liliwafanya vigogo wa kikuraishi kumpa dhiki Muhammad(s.a.w.w) na kumkejeli kutokana na mwito wake huo. Mada ya usawa ndiyo waliyoitumia sana kumkejelia: Bilal, mtumwa fukara anawezaje kuwa sawa na Abu Jahl, mungwana na mwenye mali; tena ati awe bora zaidi yake kwa Mungu kwa vile ni mwenye takua! Ilikuwa ni ajabu hilo kwao.

Mtume(s.a.w.w) alivumilia maudhi yao, akaendelea na mwito wake. Kwa sababu yale anayoyapigania yanamfanya asijali lolote. Hivi ndivyo anavyokuwa imara mtu adhimu kwa wapumbavu na washari walio wapotevu; anategemea kuwa Mwenyezi Mungu yuko pamoja naye na kwamba kesho ni yake, kwa sababu batili itaisha tu hata kama muda utarefuka.

Mustafa Sadiq Rafi, analinganisha baina ya Isa(a.s) alipokejeliwa na wana wa Israil na Muhammad(s.a.w.w) alipokejeliwa na makuraish. Miongoni mwa aliyoyasema ni: “Walimkejeli Bwana Masih hapo zamani, akawaambia: Hakuna Mtume asiyetukuzwa isipokuwa mjini na nyumbani kwake. Hivi ndivyo alivyowajibu wale waliomdharau.

Lakini Mtume(s.a.w.w) hakuwajibu waliomkejeli hata pale alipokuwa na nguvu za uarabuni kote. Alikuwa hasemi isipokuwa lile analolifanyia kazi. Kunyamaza kwake kulikuwa na maneno mengi katika falsafa ya utashi, uhuru na maendeleo. Na kwamba hapana budi kuweko na mageuzi ya watu.

Na mti uchipue na utoe majani mapya yatakayoendeleza maisha. Yeye hakuchukia wala hakusema kitu. Alikuwa kama mtengenezaji ambaye hachukii wala kukata tamaa kwa kosa la kifaa, bali hupeleka mkono wake kurekebisha.

Ni juu yetu sisi waislamu katika somo hili kupata funzo la uthabiti, ukakamavu na kujitolea muhanga kwenye haki. Tusikate tamaa ya haki kuishinda batili hata kama watu wake ni wengi.

Kwa sababu miongoni mwao wamo waliodanganyika na uongo ambao utafichuka na kuyeyuka siku zikipita; kuna wale walioghafilika dhamiri zao na Mola wao, kisha watarejea na kutubia dhambi zao.

Vile vile haitakikani tumwamini kila anayedai ni mtetezi wa haki, kwa sababu wadanganyifu na wafanya biashara ya dini ni wengi.

Kwa hakika alikuwa karibu kutupoteza kwa miungu yetu, kama tusingelikazana juu yao.

Haya ni maneno ya makuraishi ambao walimdharau Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Wanasema haya kwa kujipinga wenyewe bila ya kujitambua. Wanakubali kuwa Muhammad alikurubia kuwatia shaka kwenye masanamu yao kutokana na dalili, hoja na miujiza iliyodhihiri mikononi mwake.

Vilevile walikubali kuwa akili zao walizisimamisha kwa hawa na matamaanio yao. “Kwa hakika alikuwa karibu kutupoteza kwa miungu yetu, kama tusingelikazana juu yao,” hiyo ni fedheha na kupingana na kejeli zao kwa Muhammad. Walimkejeli na wakati huo huo wanakubali kuwa ana nguvu ya hoja. Hivi ndivyo alivyo kila mbatilifu; maneno yake yanagongana bila ya kujitambua. Siri katika hilo ni kuwa haki inaelea haizami.

Na karibu watajua watakapoiona adhabu, ni nani aliyepotea njia.

Walisema kuwa Muhammad anakurubia kuwapoteza, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawajibu kuwa kesho mtakapokabiliana na vituko vikubwa ndio mtajua kuwa nyinyi ndio mliopotea na mlio na hasara, sio Muhammad na waliomwamini.

Je, umemuona aliyeyafanya matamanio yake kuwa ndio Mungu wake?

Kila ambaye matamanio yake yanashinda dini yake, atakuwa ameyafanya ndio mungu wake, atake asitake. Anayekuwa hivyo, hakuna matumaini ya kuongoka kwake. Kwa sababu kila hoja kwake ni upuzi, kwa vile inapingana na matamanio na matakwa yake.

Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake?

Utakayemtetea na ufisadi na upotevu wake? Achana naye hana kheri yoyote. Umekwisha muonya. Basi ni juu yetu hisabu yake.

WAMEPOTEA ZAIDI KULIKO WANYAMA

Au unadhani kwamba wengi wao wanasikia na wanafahamu? Hao hawakuwa ila ni kama wanyama howa; bali wao wamepotea zaidi njia.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema wengi wao, kwa sababu baadhi yao walipinga mwanzoni, kisha wakarejea, wakaelekea kwenye uongofu na wakaifuata. Mwenyezi Mungu akaondoa usikizi na akili kwa wale waliong’ang’ania upinzani, kwa sababu hawakunufaikia na usikizi wao wala akili zao. Kila ambalo halitumainiwi kupatikana ni sawa na kuwa haliko.

Mwenyezi Mungu, imetukuka hekima yake, amewafananisha na wanyama, kwa sababu wao hawakuzingatia dalili wala kuwaidhika na hekima na mazingatio; bali ni afadhali wanyama kuliko wao. Kwa sababu wanyama howa (wakufugwa) wanatekelza wajibu wao kulingana na maumbile yao; wanafuata amri na makatazo ya wachungaji wao; wanajua yanayowadhuru na kuayaacha na yanayowanufaisha wakayafanya.

Lakini wao wafisadi hawamfuati Muumba wao, hawaogopi adhabu yake wala hawatarajii thawabu zake. Zaidi ya hayo, wanyama hawamdhuru yoyote aliye jinsi yake na asiyekuwa jinsi yake; bali watu wananufaika nao kwa kuwapanda, maziwa na sufu zao. Ama wafisadi na wapotevu, wao ni balaa kwa jamii yao na ndio sababu ya majanga na chimbuko la kutoendelea.

Kwa hakika wasifu huu hauhusiki na yule anayemkufuru Mwenyezi Mungu au kumshirikisha tu. Kila anayeipinga haki pamoja na kuweko dalili na hoja, huyo atakuwa amepotea zaidi kuliko mnyama; ni sawa awe amepinga kwa kiburi na inadi au kwa uzembe na kupuuza dalili za haki na rejea zake.

أَلَمْ تَرَ إِلَىٰ رَبِّكَ كَيْفَ مَدَّ الظِّلَّ وَلَوْ شَاءَ لَجَعَلَهُ سَاكِنًا ثُمَّ جَعَلْنَا الشَّمْسَ عَلَيْهِ دَلِيلًا ﴿٤٥﴾

45. Je, umeona jinsi Mola wako alivyokitandaza kivuli? Na angelitaka angelikifanya kitulie. Kisha tukalifanya jua ni dalili yake.

ثُمَّ قَبَضْنَاهُ إِلَيْنَا قَبْضًا يَسِيرًا ﴿٤٦﴾

46. Kisha tukakivutia kwetu kidogo kidogo.

وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ اللَّيْلَ لِبَاسًا وَالنَّوْمَ سُبَاتًا وَجَعَلَ النَّهَارَ نُشُورًا ﴿٤٧﴾

47. Yeye ndiye aliyewafanyia usiku kuwa ni vazi na usingizi kuwa ni mapumziko na akaufanya mchana kuwa ni wa matawanyiko.

وَهُوَ الَّذِي أَرْسَلَ الرِّيَاحَ بُشْرًا بَيْنَ يَدَيْ رَحْمَتِهِ وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً طَهُورًا ﴿٤٨﴾

48. Naye ndiye anayezituma pepo kuwa bishara kabla ya rehema yake na tunayateremsha kutoka mbinguni maji twahara.

لِّنُحْيِيَ بِهِ بَلْدَةً مَّيْتًا وَنُسْقِيَهُ مِمَّا خَلَقْنَا أَنْعَامًا وَأَنَاسِيَّ كَثِيرًا ﴿٤٩﴾

49. Ili kwayo tuihuishe nchi iliyokufa na tuwanyweshe miongoni mwa wanyama tuliowaumba na watu wengi.

وَلَقَدْ صَرَّفْنَاهُ بَيْنَهُمْ لِيَذَّكَّرُوا فَأَبَىٰ أَكْثَرُ النَّاسِ إِلَّا كُفُورًا ﴿٥٠﴾

50. Na hakika tumeisarifu kati yao wapate kukumbuka, lakini watu wengi wamekataa ila kukufuru.

وَلَوْ شِئْنَا لَبَعَثْنَا فِي كُلِّ قَرْيَةٍ نَّذِيرًا ﴿٥١﴾

51. Na kama tungetaka tungepeleka katika kila mji muonyaji.

فَلَا تُطِعِ الْكَافِرِينَ وَجَاهِدْهُم بِهِ جِهَادًا كَبِيرًا ﴿٥٢﴾

52. Basi usiwatii makafiri na pambana nao kwayo kwa jihadi kubwa.

وَهُوَ الَّذِي مَرَجَ الْبَحْرَيْنِ هَـٰذَا عَذْبٌ فُرَاتٌ وَهَـٰذَا مِلْحٌ أُجَاجٌ وَجَعَلَ بَيْنَهُمَا بَرْزَخًا وَحِجْرًا مَّحْجُورًا ﴿٥٣﴾

53. Yeye ndiye aliyezichanganya bahari mbili , hii ni tamu mno na hii ni chumvi sana, na akaweka kinga kati yake na kizuizi kizuiacho.

وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ مِنَ الْمَاءِ بَشَرًا فَجَعَلَهُ نَسَبًا وَصِهْرًا وَكَانَ رَبُّكَ قَدِيرًا ﴿٥٤﴾

54. Naye ndiye aliyemuumba mwanadamu kutokana na maji na akamjaalia kuwa na nasaba na ukwe. Na Mola wako ni mwenye uwezo.

DHAHIRI YA MAUMBILE

Aya 45 – 54

MAANA

Mwenyezi Mungu (s.w.t), katika Aya hizi, ametaja badhi ya neema alizozieneza kwa waja wake, ambazo zinafahamisha kuweko kwake na ukuu wake. Anatuzindua nazo Mungu Mtukufu ili tumwamini na tumwabudu kwa kumfanyia ikhlasi. Ufafanuzi ni kama ufuatavyo:-

Je, umeona jinsi Mola wako alivyokitandaza kivuli?

Makusudio ya kutaja kivuli, ni kukumbusha neema ya kivuli ambacho kinampatia mtu mapumziko na raha na kwamba Mwenyezi Mungu ndiye anayekiweka na kukiondoa.

Na angelitaka angelikifanya kitulie.

Yaani angeliifanya ardhi ikatulia, na kwa kutulia ardhi ndio kingetulia kivuli na kuwa katika hali moja. Kwa sababu kivuli hakina uhuru, kinamfuata mwenye kivuli hicho, akitaharaki nacho hutaharaki na akitingishika nacho hutingishika.

Kisha tukalifanya jua ni dalili yake.

Lau si kuweko jua, ardhi isingelikuwa na kivuli. Kwa hiyo kupatikana kwa jua kunajulisha kupatikana kivuli; sawa na kuweko sababu kunakofahamisha kuweko kinachosababishwa.

Kisha tukakivutia kwetu kidogo kidogo.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anakitandaza kidogo kidogo, kisha anakiondoa kidogo kidogo kulingana na harakati za ardhi.

Mwenyezi Mungu Mtukufu amenasibisha kwake kivuli na kukitandaza na kukiondoa, pamoja na kuwa hilo linategemea ardhi moja kwa moja, kwa sababu yeye Mwenyezi Mungu ndiye muathiri wa kwanza wa kupatikana kwake na dhahiri ya maumbile ni nyenzo tu.

Yeye ndiye aliyewafanyia usiku kuwa ni vazi.

Hapa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameusifu usiku kuwa ni vazi na katika Juz. 7 (6:96) ameusifu kuwa ni utulivu. Maana zote mbili zinakurubiana. Kwa sababu kivazi kinazuia macho na utulivu hauna sauti itakayofikia masikio.

Na usingizi kuwa ni mapumziko.

Neno subata liliofasiriwa mapumziko, lina maana ya kustarehe na kuacha kufanya kazi.

Na akaufanya mchana kuwa ni wa matawanyiko ya harakati na kufanya kazi. Tafsiri iliyo wazi zaidi ya Aya hii ni ile Aya isemayo: “Na katika rehema zake ni kuwafanyia usiku na mchana mpate kupumzika humo na mtafute fadhila zake na ili mpate kushukuru.” (28:73).

Naye ndiye anayezituma pepo kuwa bishara kabla ya rehema yake na tunayateremsha kutoka mbinguni maji twahara.

Makusudio ya rehema zake hapa ni mvua. Maana ni kuwa upepo unaleta habari njema ya kushuka maji kutoka mbinguni, ambayo ni twahara na yanatwaharisha; kama wasemavyo mafaqihi.

Ili kwayo tuihuishe nchi iliyokufa na tuwanyweshe miongoni mwa wanyama tuliowaumba na watu wengi.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwenye neno lililofasiriwa nchi ametumia ‘Balda’ na kwenye Juz. 8 (7:58) ametumia neno ‘Balad’ maneno yote hayo yana maana moja.

Na hakika tumeisarifu kati yao wapate kukumbuka.

Inawezekana kuwa iliyosarifiwa ni Qur’an na maana yawe kama Juz. 15 (17:41): “Hakika tumekwishasarifu katika Qur’an hii ili wapate kukumbuka, lakini haiwazidishii isipokuwa kuwa mbali.”

Pia inawezekana iliyosarifiwa ni mvua. Maana yawe ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaipeleka mvua kutoka sehemu moja hadi nyingine, kwa vile kama ingelibakia sehemu moja tu ingeleta uharibifu, pia kama ingelikatika kabisa wangelikufa na kiu.

Kila mwenye akili inampasa afikirie vizuri hekima na neema hii, ili amshukuru,lakini watu wengi wamekataa ila kukufuru. Yaani kumkana Mungu na kukufuru neema zake.

Na kama tungetaka tungepeleka katika kila mji muonyaji.

Kabla ya kutumwa Muhammad(s.a.w.w) Mwenyezi Mungu alituma Mtume kwa kila umma. Mwenyezi Mungu anasema:

وَلِكُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولٌ ﴿٤٧﴾

“Na kila Umma una Mtume.” Juz. 11 (10:47).

Kuanzia zama za Muhammad(s.a.w.w) mpaka siku ya mwisho, Mwenyezi Mungu amefunga kupeleka mitume kwa viumbe na akatosheka na Mtume mmoja kwa viumbe wote ambaye ni Muhammad bin Abdillah(s.a.w.w) . Dini yake ndiyo dini ya mwisho kwa watu wote.

Ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t) akachukua ahadi kwa kila Mtume kumtolea habari Muhammad na sifa zake:

“Na Mwenyezi Mungu alipochukua ahadi kwa manabii. Nikiwapa kitabu na hekima; kisha akawajia mtume msadikishaji wa yale yaliyo pamoja nanyi, ni juu yenu kumwamini na kumsaidia. Akasema: Je, mmekubali na mmechukua ahadi yangu kwa hayo? Wakasema: ‘Tumekubali.’ Akasema: basi shuhudieni, na mimi ni pamoja nanyi katika mashahidi.” Juz. 3 (3:81).

Hakuna aliye juu zaidi ya cheo hiki, isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake. Na amemkumbusha mwenye cheo hiki kwa kumwambia: ‘Na kama tungetaka tungepeleka katika kila mji muonyaji.’ Lakini hatukufanya; tumekuwakilisha wewe uzionye umma zote kwa kukuadhimisha, kwa sababu taadhima ina kiwango chake na uzito wake.

QUR’AN NA IDHAA

Basi usiwatii makafiri na pambana nao kwayo kwa jihadi kubwa.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Inafaa kukataza jambo, hata ikiwa inajulikana mwenye kukatazwa halifanyi kabisa; hasa ikiwa mkatazaji ni Mwenyezi Mungu Mtukufu. Kwayo ni kwa hiyo Qur’an.

Maana ni kuwa ewe Muhammad! Usiwaitikie makafiri kwa jambo lolote watakalokuitia; wala usiwache fursa yoyote ya kuitangaza Qur’an; uwasomee kwenye masikio yao, wapende wasipende. Na uvumilie maudhi yatakayokupata katika njia hii. Maudhi yao yasiwe ni kikwazo cha kui- tangaza; kwani kutangaza Aya za Mwenyezi Mungu ni jihadi kubwa katika njia ya haki na ya ubinadamu.

Lengo la msisitizo huu sio kuwanyamazisha wapinzani na mataghuti tu; isipokuwa ni kuwaamsha wanaokandamizwa na wasiofahamu na kuwaongoza kwenye uhuru wao ambao wameuchukua wenye nguvu; kwamba uadilifu na usawa ni haki ya kila mtu itokayo kwa Mungu; na kwamba hakuna mwenye nguvu wala tajiri au mtukufu isipokuwa kwa takua na amali njema.

Qur’an ndiyo inayodhamini haki hii. Hakuna dini wala sharia itakayoweza kutekeleza hilo ila ikiwa itasimamia uadilifu na usawa.

Hapa ndio tunajua siri iliyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَإِذَا قُرِئَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُوا لَهُ وَأَنصِتُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٢٠٤﴾

“Na isomwapo Qur’an isikilizeni na mnyamaze ili mpate kurehemiwa.” Juz. 9 (7:204).

Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwamrisha Mtume wake mtukufu kufanya juhudi kubwa ya kusoma Qur’an na kuitangaza, kwa sababu kwayo sauti ya haki na uadilifu itainuka na kuenea elimu na mwamko kwa watu. Hapo kila mtu atahisi heshima yake na kuilinda. Hapa inatubainikia kuwa kuisoma Qur’an katika idhaa zote za ulimwengu, sio kubainisha ufasaha kama wanavyodhani; isipokuwa umuhimu wa kwanza ni kuleta uadilifu na usawa kwa watu wote.

Yeye ndiye aliyezichanganya bahari mbili , hii ni tamu mno na hii ni chumvi sana, na akaweka kinga kati yake na kizuizi kizuiacho.

Makusudio ya bahari mbili katika Aya sio bahari mbili hasa; isipokuwa ni aina mbili za maji: moja ni tamu na nyingine ni chumvi. Neno bahari hutumiwa pia kwa maji mengi yawe chumvi au tamu.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameyajaalia maji ya chumvi kwenye ardhi iliyoinama (pwani) na akajaalia maji tamu kwenye ardhi iliyo juu ya maji-chumvi (bara); kwa namna ambayo maji-tamu ya bara, yanaminika kwenye maji-chumvi ya pwani na maji-tamu yanabaki na utamu wake na maji-chumvi yanabaki na chumvi yake. Kama ingelikuwa kinyume, pwani ikawa juu na bara ikawa chini na maji yachanganyike, basi maji yote yangelikuwa chumvi na watu kuwa na matatizo.

Haya yote hayakutokea kisadfa; bali ni kwa makadirio ya mwenye hekima mjuzi. Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:’ na akaweka kati yake kinga na kizuizi kizuiacho’ ni kuwa aina mbili hizi za maji hata zikikutana hakuna moja inayozidi nyingine, bali kila moja inabakia na athari yake. Ametukuka ambaye ameumba kila kitu na akakikadiria kipimo.

Naye ndiye aliyemuumba mwanadamu kutokana na maji na akam- jaalia kuwa na nasaba na ukwe.

Makusudio ya nasaba ni udugu wa kuzaliwa na ukwe ni udugu unaotokana na kuoana. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemumba mtu, ambaye ni kiumbe wa ajabu, kutokana na manii na akajaalia udugu na kuhurumiana baina yao. Tazama Juz. 18: (23:12-14).

Na Mola wako ni mwenye uwezo.

Miongoni mwa uweza wake ni kumfanya mke na mume kutokana na chembe moja.


3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA

وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَنفَعُهُمْ وَلَا يَضُرُّهُمْ وَكَانَ الْكَافِرُ عَلَىٰ رَبِّهِ ظَهِيرًا ﴿٥٥﴾

55. Na wanaabudu wasiowadhuru wala kuwanufaisha badala ya Mwenyezi Mungu. Na kafiri daima ni msaidizi wa mpinzani wa Mola wake.

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا مُبَشِّرًا وَنَذِيرًا ﴿٥٦﴾

56. Na hatukukutuma ila uwe mbashiri na muonyaji.

قُلْ مَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِلَّا مَن شَاءَ أَن يَتَّخِذَ إِلَىٰ رَبِّهِ سَبِيلًا ﴿٥٧﴾

57. Sema: Siwaombi ujira juu yake, isipokuwa mwenye kutaka ashike njia iendayo kwa Mola wake.

وَتَوَكَّلْ عَلَى الْحَيِّ الَّذِي لَا يَمُوتُ وَسَبِّحْ بِحَمْدِهِ وَكَفَىٰ بِهِ بِذُنُوبِ عِبَادِهِ خَبِيرًا ﴿٥٨﴾

58. Na mtegemee aliye hai ambaye hafi na umtukuze kwa sifa zake. Na yatosha kuwa yeye ni mwenye habari za dhambi za waja wake.

الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا فِي سِتَّةِ أَيَّامٍ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ الرَّحْمَـٰنُ فَاسْأَلْ بِهِ خَبِيرًا ﴿٥٩﴾

59. Ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha akastawi juu ya Arshi. Mwingi wa rehema! Uliza habari zake kwa ajuaye.

وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ اسْجُدُوا لِلرَّحْمَـٰنِ قَالُوا وَمَا الرَّحْمَـٰنُ أَنَسْجُدُ لِمَا تَأْمُرُنَا وَزَادَهُمْ نُفُورًا ﴿٦٠﴾

60. Na wanapoambiwa msujudieni Mwingi wa rehema, wanasema: Ni nani huyo mwingi wa rehema? Je, tumsujudie unayetuamrisha wewe? Na huwazidishia chuki.

تَبَارَكَ الَّذِي جَعَلَ فِي السَّمَاءِ بُرُوجًا وَجَعَلَ فِيهَا سِرَاجًا وَقَمَرًا مُّنِيرًا ﴿٦١﴾

61. Amekuwa na baraka yule aliyejaalia katika mbingu buruji na akajaalia humo taa na mwezi wenye nuru.

وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ خِلْفَةً لِّمَنْ أَرَادَ أَن يَذَّكَّرَ أَوْ أَرَادَ شُكُورًا ﴿٦٢﴾

62. Naye ndiye ambaye ameujaalia usiku na mchana kufuatana, kwa yule anayetaka kukumbuka au anayetaka kushukuru.

KAFIRI NI MSADIZI WA MPINZANI WA MOLA WAKE

Aya 55 – 62

MAANA

Na wanaabudu wasiowadhuru wala kuwanufaisha badala ya Mwenyezi Mungu.

Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 11 (10 18).

Na kafiri daima ni msaidizi wa mpinzani wa Mola wake.

Yaani anawasaidia watu wa batili dhidi ya haki. Kila mwenye kusaidia batili atakuwa amesaidia dhidi ya Mwenyezi Mungu na kuwa adui yake; hata kama atamsabihi na kumtukuza kwa ulimi wake. Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) :“Mwenye kumsaidia dhalimu na huku anajua kuwa ni dhalimu basi amejitenga na Uislamu.”

Kadiri nitakavyotia shaka, lakini siwezi kutia shaka kuwa mwenye kumtegemea dhalimu ni kafiri; bali kafiri aliye mwadilifu ni bora kuliko yeye. Aya za Qur’an kuhusu hilo ni nyingi na ziko wazi. Ama Hadith za Mtume zimepituka kiwango cha mutawatir.

Ndio! Ni wajibu wetu kuamiliana naye muamala wa kiislamu kwa vile tu ametamka: Lailaha illallah Muhammadurrasulullah (Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu.)

Na hatukukutuma ila uwe mbashiri na muonyaji.

Imetangulia kwa herufi zake katika Juz. 15 (17:105).

Sema: Siwaombi ujira juu yake, isipokuwa mwenye kutaka ashike njia iendayo kwa Mola wake.

Mimi sina tamaa ya mali yenu wala siwauzii pepo. Ninalotaka ni kutengeneza tu. Anayetaka kufanya njia ya kumwendea Mola miongoni mwenu, basi malipo yake yako kwa Mungu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:90) na Juz.12 (11:88).

Na mtegemee aliye hai ambaye hafi na umtukuze kwa sifa zake. Na yatosha kuwa yeye ni mwenye habari za dhambi za waja wake.

Ewe Muhammad! Toa bishara na onyo ukimtegemea Mwenyezi Mungu kwa kuwa na ikhlasi naye katika kauli yako na vitendo vyako na ujitakashe na kumfanyia mfano na kila lile ambalo halifanani na utukufu na ukuu wake. Yeye anamjua zaidi aliyepotea njia, na atamhisabu na kumlipa.

Ambaye ameumba mbingu na ardhi katika siku sita, kisha akastawi juu ya Arshi.

Makusudio ya kustawi ni kutawala. Lililo na nguvu ni kuwa makusudio ya siku ni mikupuo, kwa sababu hakuna siku kabla ya kupatikana ulimwengu na jua. Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:54), Juz. 11 (103), na Juz. 12 (11:7).

Mwingi wa rehema! Uliza habari zake kwa ajuaye.

Habari yake, ni habari ya huko kuumbwa mbingu na ardhi, ambako kunafahamika kutokana na mfumo wa Aya. Hapa kuna maneno yaliyotan- gulizwa na ya kukadiriwa. Maana ni: Yeye ni Mwingi wa rehema, ulizia habari za kuumbwa mbingu na ardhi kwa yule ajuaye ambaye ni Mwenyezi Mungu.

Na wanapoambiwa msujudieni Mwingi wa rehema, wanasema: ‘Ni nani huyo mwingi wa rehema? Je, tumsujudie unayetuamrisha wewe?’ Na huwazidishia chuki.

Nabii(s.a.w.w) akiwaambia washirikina: ‘Mwabuduni Mwingi wa rehema, wala msiabudu masanamu,’ wao husema kwa kujitia hamnazo, kwa madharau, ni nani huyo unayetuambia tumwabudu unayemuita Mwingi wa rehema? Unataka tukutii wewe na tuwaasi baba zetu katika yale waliyokuwa wakiyaabudu?’

Ujinga na upumbavu huu unatukumbusha ujinga wa vijana wetu wanapoambiwa swalini na mfunge, husema: “Bado kuna Swala katika karne hii ya ishirini? Jambo la kushangaza ni kuwa vijana hawa wanaimba uhuru wa bianadamu; kama kwamba uhuru ni uzandiki na utu ni kujitoa kwenye misimamo.

Hawajui kuwa aliye huru ni yule anayemwabudu Mwenyezi Mungu wala hamnyenyekei asiyekuwa yeye na kwamba utu ni dini ya Mwenyezi Mungu ambayo inakataza maovu na munkar.

Amekuwa na baraka yule aliyejaalia katika mbingu buruji na akajaalia humo taa na mwezi wenye nuru.

Makusudio ya buruji ni mashukio ya jua na mwezi. Tazama Juz.14 (15: 16). Makusudio ya taa hapa ni jua, kutokana na kuunganisha na mwezi. Mahali pengine Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema:

هُوَ الَّذِي جَعَلَ الشَّمْسَ ضِيَاءً وَالْقَمَرَ نُورًا ﴿٥﴾

“Yeye ndiye aliyefanya jua kuwa mwanga na mwezi kuwa nuru.” Juz.11 (10:5).

Wengine wametofautisha baina ya nuru na mwanga. Kwamba mwanga unategemea sayari moja kwa moja; kama vile mwanga wa jua, unatoka kwenye jua moja kwa moja.

Nuru inategemea sayari kupitia sayari nyingine; kama vile nuru ya mwezi inavyotegmea jua. Wametoa dalili wanaotofautisha, kwa Aya hiyo ya Juz. 11 (10:5) tuliyoitaja punde.

Naye ndiye ambaye ameujaalia usiku na mchana kufuatana, kwa yule anayetaka kukumbuka au anayetaka kushukuru.

Usiku unaondoka kisha unakuja mchana, nao unaondoka kisha unarudi usiku na kuendelea; wala hakuna unaobakia muda mrefu kuzidi kiasi cha haja ya viumbe.

Kufuatana kwa namna hii kunafahamisha kuweko mpangiliaji mwenye hekima. Kufuatana huku kunategemea harakati za ardhi, nazo zinategemea msababishaji wake wa kwanza.

Ama hekima ya mfuatano huu, ni kwamba lau lingelibakia giza tu, au mwangaza tu, maisha yangelikuwa magumu hapa ardhini.

Kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) ‘Kwa anayetaka kukumbuka,’ maana yake ni kuwa mwenye kutaka dalili ya kuweko Mwenyezi Mungu ataipata katika vitu vyote, vikiwemo kufuatana usiku na mchana.

Na kauli yake ‘Au anayetaka kushukuru,’ ni kuwa anayetaka kumshukuru Mweneyzi Mungu kwa neema yake naashukuru vile vile kwa kufuatana usiku na mchana, kwa sababu hilo ni katika neema kubwa.

وَعِبَادُ الرَّحْمَـٰنِ الَّذِينَ يَمْشُونَ عَلَى الْأَرْضِ هَوْنًا وَإِذَا خَاطَبَهُمُ الْجَاهِلُونَ قَالُوا سَلَامًا ﴿٦٣﴾

63. Na waja wa Mwingi wa rehema ni wale wanaotembea ardhini kwa unyenyekevu. Na wajinga wakiwasemesha, husema: ‘Salama.’

وَالَّذِينَ يَبِيتُونَ لِرَبِّهِمْ سُجَّدًا وَقِيَامًا ﴿٦٤﴾

64. Na wale wanaokesha kwa ajili ya Mola wao kusujudu na kusimama.

وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا اصْرِفْ عَنَّا عَذَابَ جَهَنَّمَ إِنَّ عَذَابَهَا كَانَ غَرَامًا ﴿٦٥﴾

65. Na wale wanaosema: ‘Mola wetu! Tuondolee adhabu ya Jahannam,’ hakika adhabu yake ni yenye kuendelea.

إِنَّهَا سَاءَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا ﴿٦٦﴾

66. Hakika hiyo ni mbaya kuwa kituo na mahali pa kukaa.

وَالَّذِينَ إِذَا أَنفَقُوا لَمْ يُسْرِفُوا وَلَمْ يَقْتُرُوا وَكَانَ بَيْنَ ذَٰلِكَ قَوَامًا ﴿٦٧﴾

67. Na wale ambao wanapotumia hawafanyi israfu wala hawafanyi uchoyo wanakuwa katikati baina ya hayo.

وَالَّذِينَ لَا يَدْعُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ وَلَا يَقْتُلُونَ النَّفْسَ الَّتِي حَرَّمَ اللَّـهُ إِلَّا بِالْحَقِّ وَلَا يَزْنُونَ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ يَلْقَ أَثَامًا ﴿٦٨﴾

68. Na wale ambao hawamwombi mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaiui nafsi aliyoiharamisha ila kwa haki, wala hawazini. Na mwenye kuyafanya hayo atapata madhambi.

يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا ﴿٦٩﴾

69. Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama na atadumu humo kwa kufedheheka.

إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلًا صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يُبَدِّلُ اللَّـهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ وَكَانَ اللَّـهُ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٧٠﴾

70. Isipokuwa atakayetubia na akatenda matendo mema, basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.

وَمَن تَابَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَإِنَّهُ يَتُوبُ إِلَى اللَّـهِ مَتَابًا ﴿٧١﴾

71. Na aliyetubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kwa Mwenyezi Mungu toba ya kweli.

وَالَّذِينَ لَا يَشْهَدُونَ الزُّورَ وَإِذَا مَرُّوا بِاللَّغْوِ مَرُّوا كِرَامًا ﴿٧٢﴾

72. Na wale ambao hawawi kwenye uzushi, na wanapopita kwenye upuzi hupita kwa heshima zao.

وَالَّذِينَ إِذَا ذُكِّرُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ لَمْ يَخِرُّوا عَلَيْهَا صُمًّا وَعُمْيَانًا ﴿٧٣﴾

73. Na wale ambao wanapokumbushwa ishara za Mola wao hawajifanyi ni viziwi nazo na vipofu.

وَالَّذِينَ يَقُولُونَ رَبَّنَا هَبْ لَنَا مِنْ أَزْوَاجِنَا وَذُرِّيَّاتِنَا قُرَّةَ أَعْيُنٍ وَاجْعَلْنَا لِلْمُتَّقِينَ إِمَامًا ﴿٧٤﴾

74. Na wale ambao wanasema: Mola wetu! Tupe katika wake zetu na wanetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wenye takua.

أُولَـٰئِكَ يُجْزَوْنَ الْغُرْفَةَ بِمَا صَبَرُوا وَيُلَقَّوْنَ فِيهَا تَحِيَّةً وَسَلَامًا ﴿٧٥﴾

75. Hao ndio watakolipwa ghorofa kwa walivyosubiri na watakuta humo maamkuzi na salaam.

خَالِدِينَ فِيهَا حَسُنَتْ مُسْتَقَرًّا وَمُقَامًا ﴿٧٦﴾

76. Watadumu humo kituo na makao mazuri.

قُلْ مَا يَعْبَأُ بِكُمْ رَبِّي لَوْلَا دُعَاؤُكُمْ فَقَدْ كَذَّبْتُمْ فَسَوْفَ يَكُونُ لِزَامًا ﴿٧٧﴾

77. Sema, Mola wangu asingewajali lau si kupewa kwenu mwito, lakini nyinyi mmewakadhibisha, basi (adhabu) ni lazima.

WAJA WA MWINGI WA REHEMA

Aya 63 – 77

MAANA

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja sifa za makafiri na kiaga chao, kama kawaida yake, anataja sifa za waumini na malipo aliyowaandalia. Zifuatazo ndizo sifa zao:

1.Na waja wa Mwingi wa rehema ni wale wanaotembea ardhini kwa unyenyekevu.

Imam Jafar Sadiq(a.s) anasema katika tafsiri ya hilo:“Ni yule mtu anayetembea kwenye asili yake aliyoumbiwa, hajikalifishi wala hajifanyi.” Ndio, anayetembea kwenye umbile lake aliloumbiwa, tena akiwa peke yake bila ya kuwa na wapambe na wafuasi wanaomfuta nyuma na wengine mbele wakiwa wamepanda farasi au pikipiki na kupiga ving’ora vinavyohanikiza watu kwa sauti zake vikitangaza kuja kwake ili aachiwe njia, kwa ajili ya kumheshimu na kumtukuza.

2.Na wajinga wakiwasemesha, husema: ‘Salama.’

Makusudio ya kusemeshwa na wajinga ni kama vile kejeli zao, shutuma zao au mijadala ya hawa na masilahi. Amani ni kinaya cha kuachana nao, kwa kuwadharau na kuchunga mtu heshima yake. Maana ni kuwa, muumini akisikia neno ovu, aachane nalo; kama kwamba hakulisikia au kama anayekusudiwa ni mwingine sio yeye. Huu ndio mwepuko mwema aliousema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَاهْجُرْهُمْ هَجْرًا جَمِيلًا ﴿١٠﴾

“Na uwaepuke mwepuko mwema.” (73:10).

Hakuna mwenye shaka kwamba kuachana na jambo ni pale ikiwa hakuna uwezo au nguvu za kulikabili. Vinginevyo itakuwa ni wajibu kulikabili. Hapana budi kuihusisha Aya na hilo.

3.Na wale wanaokesha kwa ajili ya Mola wao kusujudu na kusimama.

Waumini wanasimama usiku kwenye giza wakifanya ibada ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu hilo liko mbali na ria, wala hawaupitishi usiku mikahawani na kwenye mambo ya mchezo mchezo tu, huku wakifuja mali na kupanga njama dhidi ya waumini na wenye ikhlasi. Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

كَانُوا قَلِيلًا مِّنَ اللَّيْلِ مَا يَهْجَعُونَ ﴿١٧﴾

“Walikuwa wakilala kidogo usiku.” (51:17).

4.Na wale wanaosema: ‘Mola wetu! Tuondolee adhabu ya Jahannam, hakika adhabu yake ni yenye kuendelea. haikwepeki na ni yakudumu. Hakika hiyo ni mbaya kuwa kituo na mahali pa kukaa,

Waliamini Pepo na Moto, kutokana na waliyoyashuhudia na kuyaona; ndio wakauhofia moto wakaitumai pepo. Imam Ali(a.s ) anasema: “Wao na Pepo ni kama walioiona wakiwa ndani yake wananeemeshwa. Na wao na moto ni kama waliouona wakiwa ndani yake wanaadhibiwa.”

5.Na wale ambao wanapotumia hawafanyi israfu wala hawafanyi uchoyo wanakuwa katikati baina ya hayo, hakuna kupitisha kiasi, Si ubakhili wala ubadhirifu.

Huu ndio mwenendo wa Uislamu, wastani katika kila kitu; hakuna ulahidi wala waungu wengi, udikteta wala ukiritimba na hakuna kutaifisha mali ya mtu wala ubepari. Tazama Juz. 15 (17:29) kifungu cha ‘Uislamu na nadharia ya maadili.’

6.Na wale ambao hawamwombi mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu.

Mwenye kufanya riya au akamtii kiumbe katika kumuasi Muumba, basi huyo ni kama aliyemwomba mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu.

Wala hawaiui nafsi aliyoiharamisha ila kwa haki.

Nafsi inayouliwa kwa haki na kwa uadilifu ni ile iliyoua nafsi nyingine bila ya haki, aliyezini akiwa kwenye ndoa, kurtadi dini au kuleta ufisadi katika ardhi.

Ufafanuzi wa hayo uko katika vitabu vya Fiqh.

Wala hawazini

Kwa sababu zinaa ni katika madhambi makubwa. Ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t). Akaiweka sawa na kumshirikisha Mwenyezi Mungu na kuua nafsi na akajaalia hukumu ya haya matatu ni kuuliwa kwa masharti yaliyotajwa kwenye vitabu vya fiqh.

Na mwenye kuyafanya hayo atapata madhambi.

Hayo ni hayo ya shirk, kuua na kuzini. Na madhambi ni adhabu.

Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama na atadumu humo kwa kufedheheka.

Kuna adhabu gani kubwa na kufedheheka zaidi kuliko adhabu ya Jahannam? Si kwambii tena ikiwa itazidishwa pamoja na kudumu kusiko na mwisho.

Isipokuwa atakayetubia na akatenda matendo mema, basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe mwenye kurehemu.

Mwenye kutubia dhambi ni kama asiyekuwa na dhambi, zaidi ya hayo, Mwenyezi Mungu atampa thawabu kwa kule kutubia kwake na atampa mema kulingana na maovu ya dhambi zake; kiasi ambacho toba itafuta maovu ya dhambi.

إِنَّ الْحَسَنَاتِ يُذْهِبْنَ السَّيِّئَاتِ ﴿١١٤﴾

“Hakika mema huondoa maovu.” Juz. 12 (11:114).

Haya ndiyo maana ya ‘Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema’ kwa sababu uovu, kwa ulivyo, haustahiki kuwa wema, wala wema, kwa ulivyo, haustahiki kuwa uovu’

Na aliyetubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kwa Mwenyezi Mungu toba ya kweli.

Baada ya kubainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya iliyotangulia kwamba mwenye kutubia atampa thawabu za mwenye kufanya mema, hapa anamsifu kuwa amerejea kwa Muumba wake kurejea kuzuri.

7.Na wale ambao hawawi kwenye uzushi, na wanapopita kwenye upuzi hupita kwa heshima zao.

Neno ‘hawawi’ limefasiriwa kutokana na neno la kiarabu ‘laa yash-hadu- una’ kama ilivyotumika tafsiri hiyo katika Juz. 2 (2:185). Makusudio ya uzushi ni mambo ya batili na upuzi ni kila lisilo na kheri. Maana ni kuwa waumini hawahudhurii vikao vya ubatilifu wala hawavisaidii, sikwambii kuvifanya. Pia hawashiriki mazungumzo yasiyokuwa na kheri na wanapoyapitia hayo masiko yao huyaepuka; kama wanavyoziepusha ndimi zao kuayatamka; sawa na nyuki anavyopita haraka kwenye mzoga na harufu mbaya.

8.Na wale ambao wanapokumbushwa ishara za Mola wao hawaji- fanyi ni viziwi nazo na vipofu.

Mshairi huwa anasikiliza mashairi kwa umakini kabisa. Vile vile kila mwenye kuhusika na jambo akizungumziwa huwa anakuwa makini nalo sana anapolisikilza. Mtu unapomzungumzia jambo lililo mbali naye atakuepuka na hayo mazungumzo yako, hata kama ni ya uongofu na mwangaza.

Hapa ndipo inabainika siri ya muumini kuikubali Qur’an, na kafiri kuachana nayo. Mumin anakikubali Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa vile anakiamini na kutambua maana yake na makusudio yake. Anakikuta kwenye nafsi yake, itikadi yake, matendo yake mema na malipo aliyomuandalia Mola wake.

Kafiri anakipa mgongo Kitabu cha Mwenyezi Mungu kwa sababu anakipinga na hajui malengo yake na siri yake; wala hapati humo isipokuwa kushutumiwa na kukosolewa itikadi yake na sifa zake na pia makaripio ya ukafiri wake.

9.Na wale ambao wanasema: Mola wetu! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wenye takua.

Muovu huwa anatamaani watu wamfuate katika uovu wake, sio kwa kuwa amekinai kuwa yuko kwenye uongofu kutoka kwa Mola wake, hapana! Isipokuwa anataka kupunguza lawama na shutuma na kufunika kosa lake kwa kuwa wengi wakosefu. Lakini hataki mkewe na watoto wake wawe hivyo; kama vile mgonjwa asivyopenda watu wake wapatwe na ugonjwa alio nao.

Ama yule aliye mwema na mwenye takua ana yakini na dini yake na ana busara katika mambo yake. Kwa hivyo huwa anatamaani kwa dhati ya moyo kimsingi na kiitikadi kuwa watu wote wafuate njia yake na kwamba watoto wake wakimuiga yeye huwa anafurahi.

Kwa hiyo wenye ikhlasi humuomba Muumba wao wapate wa kuwaiga, sio kwa kuziba vitendo vyao kwa watu wala kutaka jaha duniani na kuchukua mali kwa kutumia haki za Mwenyezi Mungu; bali ni kwa kujipendekeza mbele ya Mwenyezi Mungu aliye peke yake.

Hao ndio watakaolipwa ghorofa kwa walivyosubiri na watakuta humo maamkuzi na salaam. Watadumu humo kituo na makao mazuri.

Ghorofa ni kinaya cha makao ya juu. Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kubainisha wasifu wa wenye takua na watiifu, sasa anataja malipo yao watakayoyapata kwake, ambayo ni kudumu katika raha, amani na neema pamoja na heshima.

Mwenyezi Mungu amehusisha kutaja subira hapa kuashiria kuwa kila mwenye haki hana budi kupata taabu na udhia kutoka kwa wasio na haki na kwamba thawabu za Mwenyezi Mungu hatazipata ispokuwa mwenye kuwa na uvumilivu na subira na akaendelea kuwa na msimamo kadiri hali itakavyokuwa ngumu.

Sema, Mola wangu asingewajali lau si kupewa kwenu mwito, lakini nyinyi mmewakadhibisha, basi (adhabu) ni lazima.

Makusudio ya neno ‘duakum’ hapa ni kupewa mwito kutokana na maneno yanayovutia, lakini mlikadhibisha. Ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu:

فَدَعَوْهُمْ فَلَمْ يَسْتَجِيبُوا لَهُمْ ﴿٥٢﴾

“Basi watawaita nao hawatawaitikia.” Juz. 15 (18:52)

Kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwapa mwito kwenye imani na utiifu kupitia kwa Mtume wake.

Maana ni kuwa nyinyi washirikina hamstahiki hata kutajwa pia lau si kuwa mliitwa kwenye imani na utiifu, ili kuweko na hoja siku ya hisabu na malipo, ikiwa hamtasikia na kuitikia mwito. Nanyi mmeupinga mwito na mkadhibishaji aliyetoa mwito huo, basi adhabu inawastahiki na ni lazima.


4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA

Sura Ya Ishirini Na Sita: Surat Shua’rau.

Twabrasiy amesema imeshuka Makka isipokuwa Aya 224 hadi mwisho, zimeshuka Madina. Ina Aya 227

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehma Mwenye kurehemu.

طسم ﴿١﴾

1. Twaa Siin Miim.

تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ الْمُبِينِ ﴿٢﴾

2. Hizo ni Aya za Kitabu kinachobainisha.

لَعَلَّكَ بَاخِعٌ نَّفْسَكَ أَلَّا يَكُونُوا مُؤْمِنِينَ ﴿٣﴾

3. Huenda ukaiangamiza nafsi yako kwa kuwa hawawi waumini.

إِن نَّشَأْ نُنَزِّلْ عَلَيْهِم مِّنَ السَّمَاءِ آيَةً فَظَلَّتْ أَعْنَاقُهُمْ لَهَا خَاضِعِينَ ﴿٤﴾

4. Tungelipenda tungeliwateremshia kutoka mbinguni ishara zikainyenyekea shingo zao.

وَمَا يَأْتِيهِم مِّن ذِكْرٍ مِّنَ الرَّحْمَـٰنِ مُحْدَثٍ إِلَّا كَانُوا عَنْهُ مُعْرِضِينَ ﴿٥﴾

5. Na hauwajii ukumbusho mpya kutoka kwa Mwingi wa rehema ila hujitenga nao.

فَقَدْ كَذَّبُوا فَسَيَأْتِيهِمْ أَنبَاءُ مَا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٦﴾

6. Kwa hakika wamekadhibisha, kwa hivyo zitakujawafikia habari za yale waliyokuwa wakiyafanyia stihizai.

أَوَلَمْ يَرَوْا إِلَى الْأَرْضِ كَمْ أَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ زَوْجٍ كَرِيمٍ ﴿٧﴾

7. Je hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri.

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿٨﴾

8. Hakika katika hayo kuna ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿٩﴾

9. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

HUENDA UKAANGAMIZA NAFSI YAKO

Aya 1-9

MAANA

Twaa Siin Miim.

Umetangulia mfano wake mwanzo wa Sura Baqara, Juz. 1

Hizo ni Aya za Kitabu kinachobainisha.

Hizo ni ishara ya Aya za Sura hii, kitabu ni Qur’an na chenye kubainisha ni kubainisha haki na kudhihirisha.

Huenda ukaiangamiza nafsi yako kwa kuwa hawawi waumini.

Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.w) kwamba asiikere na kuiumiza nafsi yake kwa sababu ya watu wake kuukataa uongofu na haki. Umetangulia mfano wake katika Juz.7 (6:35) na Juz. 15 (18:6).

Tungelipenda tungeliwateremshia kutoka mbinguni ishara zikainyenyekea shingo zao.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamwambia Mtume wake mtukufu: Poa moyo wako! Lau tungelitaka waamini kwa nguvu tungeliteremsha adhabu kutoka mbinguni waione kwa macho na kuwaambia chagueni imani au adhabu; bila shaka wao wangelisalimu amri kwa unyenyekevu.

Lakini je, hii itahisabiwa kuwa ni imani? Hapana! Imani ya kweli inakuwa kwa utashi na hiyari, sio kwa kulazimishwa kwa nguvu. Ndio maana tukawakadiria kheri na shari, tukawaamrisha hili na kuwakataza lile; kisha tukawaachia hiyari, waweze kustahiki thawabu kwa utiifu na adhabu kwa uasi.

Unaweza kuuliza : Mwenyezi Mungu (s.w.t) alifanya hivyo katika zama za Musa(a.s) kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na tulipoinua mlima juu yao kama kwamba ni kiwingu kilichowafunika na wakadhani kuwa utawaangukia. Tukawaambia: shikeni kwa nguvu tuliyowapa.” Juz. 9 (7: 171).

Jibu : kwa hakika Qur’an Tukufu inafahamisha waziwazi kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ana muamala maalum na Mayahudi usiofanana na waja wengine. Kwa sababu wao wana tabia za pekee zisizokuwa na mfano. Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi zaidi kwa anuani ya ‘Mayahudi hawana mfano’ katika Juz. 1: (2:63-66).

Na hauwajii ukumbusho mpya kutoka kwa Mwingi wa rehema ila hujitenga nao. Kwa hakika wamekadhibisha, kwa hivyo zitakujawafikia habari za yale waliyokuwa wakiyafanyia stihizai.

Tumewaongoza washirikina, kupitia kwako ewe Muhammad, kwenye yale yaliyo na kheri yao na masilahi yao, wakaachana nayo, wakayadharau na kuyafanyia masikhara. Basi nawe achana nao na watakumbana na adhabu waliyoahidiwa tu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:68).

Je hawakuiona ardhi, mimea mingapi tumeiotesha humo, ya kila namna nzuri. Hakika katika hayo kuna ishara, lakini wengi wao hawakuwa wenye kuamini.

Alikufuru Mungu aliyekufuru huku akiona dalili na ubainifu wa kupatikana kwake na ukuu wake. Miongoni mwa dalili hizi ni kutoa mimea ya aina na rangi mbali mbali. Kwa maelezo zaidi angalia Juz.7 (6:99) na Juz. 13 (13:3).

Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

Kwa nguvu zake anawashinda mataghuti na rehema zake anawapa muda bila ya kuwaharakishia adhabu mpaka awajie mbashiri na muonyaji na kuwapa fursa ya kufikiria vizuri na kutubia.

Imam Ali(a.s) anasema:“Hasira zake hazimfanyi kuacha huruma yake, wala huruma haimfanyi kupuuza adhabu yake.”

وَإِذْ نَادَىٰ رَبُّكَ مُوسَىٰ أَنِ ائْتِ الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ ﴿١٠﴾

10. Na Mola wako alipomwita Musa kwamba nenda kwa watu madhalimu.

قَوْمَ فِرْعَوْنَ أَلَا يَتَّقُونَ ﴿١١﴾

11. Watu wa Firauni. Hawaogopi?

قَالَ رَبِّ إِنِّي أَخَافُ أَن يُكَذِّبُونِ ﴿١٢﴾

12. Akasema: Mola wangu! Hakika mimi naogopa watanikadhibisha.

وَيَضِيقُ صَدْرِي وَلَا يَنطَلِقُ لِسَانِي فَأَرْسِلْ إِلَىٰ هَارُونَ ﴿١٣﴾

13. Na kifua changu kinadhikika, na ulimi wangu haukunjuki vyema, basi mtumie ujumbe Harun.

وَلَهُمْ عَلَيَّ ذَنبٌ فَأَخَافُ أَن يَقْتُلُونِ ﴿١٤﴾

14. Nao wanalo kosa juu yangu basi naogopa wasije wakaniua.

قَالَ كَلَّا فَاذْهَبَا بِآيَاتِنَا إِنَّا مَعَكُم مُّسْتَمِعُونَ ﴿١٥﴾

15. Akasema, sivyo kabisa! Nendeni na ishara yetu. Hakika sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza.

فَأْتِيَا فِرْعَوْنَ فَقُولَا إِنَّا رَسُولُ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦﴾

16. Basi mfikieni Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni wajumbe wa Mola wa walimwengu wote.

أَنْ أَرْسِلْ مَعَنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿١٧﴾

17. Ya kwamba uwaachilie wana wa Israil waende nasi.

قَالَ أَلَمْ نُرَبِّكَ فِينَا وَلِيدًا وَلَبِثْتَ فِينَا مِنْ عُمُرِكَ سِنِينَ ﴿١٨﴾

18. Akasema: Je, hatukukulea utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi?

وَفَعَلْتَ فَعْلَتَكَ الَّتِي فَعَلْتَ وَأَنتَ مِنَ الْكَافِرِينَ ﴿١٩﴾

19. Na ukatenda kitendo chako ulichokitenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani?

قَالَ فَعَلْتُهَا إِذًا وَأَنَا مِنَ الضَّالِّينَ ﴿٢٠﴾

20. Akasema: Nililifanya hilo nikiwa miongoni mwa wasioelewa.

فَفَرَرْتُ مِنكُمْ لَمَّا خِفْتُكُمْ فَوَهَبَ لِي رَبِّي حُكْمًا وَجَعَلَنِي مِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٢١﴾

21. Basi niliwakimbia nilipowahofia. Na Mola wangu akanitunukia hukumu na akanijaalia niwe miongoni mwa mitume.

وَتِلْكَ نِعْمَةٌ تَمُنُّهَا عَلَيَّ أَنْ عَبَّدتَّ بَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿٢٢﴾

22. Na hiyo ndiyo neema ya kunisimbulia na wewe umewatia utumwani wana wa Israil?

MUSA

Aya 10 – 22

MAANA

Aya hizi hadi kufikia Aya ya 28 ni za kisa cha Musa ambacho kimetangulia mara kadhaa. Katika Juz. 16 (20: 9) tumeleza sababu za kukaririka kisa hicho.

Na Mola wako alipomwita, Musa kwamba nenda kwa watu madhal- imu watu wa Firauni.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:24).

Hawaogopi?

Hii ni jumla nyingine, maana yake ni kuwa, umefika wakati sasa Firauni na watu wake waogope mwisho wa uovu na utaghuti.

Akasema: Mola wangu! Hakika mimi naogopa watanikadhibisha.

Katika Juz. 16 (20 45) ni: “Ewe Mola wetu! Hakika sisi tunaogopa asije akapindukia mipaka juu yetu au kufanya jeuri.”

Yaani asije akatuwahi kutuadhibu kabla kufikishia ujumbe.

Na kifua changu kinadhikika, na ulimi wangu haukunjuki vyema, basi mtumie ujumbe Harun.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimtuma Musa kupeleka ujumbe wake kwa Firauni. Na hili, kwa upande mmoja, ni jambo zito na lenye mashaka sana, kutokana na utaghuti wa Firauni na nguvu za utawala wake. Na kwa upande mwingine, ujumbe wenyewe ni mzito.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwambia Mtume wake Muhammad(s.a.w.w) :

إِنَّا سَنُلْقِي عَلَيْكَ قَوْلًا ثَقِيلًا ﴿٥﴾

“Hakika sisi tutakuteremshia kauli nzito.” (73:5).

Musa alikuwa ni mwepesi wa kughadhibika kwa ajili ya haki, na ulimi wake ulikuwa na kigugumizi kinachomzuia kutamka. Kwa hiyo akahofia kutotekeleza vizuri ujumbe mkuu. Hakuna yeyote anayehofia kutekeleza haki ya Mwenyezi Mungu kuliko mitume; hasa wale Ulul-a’zm. Hii inatokana na isma. Ndipo Musa akamtaka Mwenyezi Mungu kumtuma Jibril kwa nduguye, Harun, ili awe msaidizi wake katika jambo hili muhimu.

Nao wanalo kosa juu yangu basi naogopa wasije wakaniua.

Anaishiria lile tukio la kumuua mtu wa upande wa Firauni pale alipom- saidia mtu wa upande wake; kama ilivyoelezwa katika Aya hii:

فَوَجَدَ فِيهَا رَجُلَيْنِ يَقْتَتِلَانِ هَـٰذَا مِن شِيعَتِهِ وَهَـٰذَا مِنْ عَدُوِّهِ فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ فَوَكَزَهُ مُوسَىٰ فَقَضَىٰ عَلَيْهِ ﴿١٥﴾

“Na akakuta humo watu wawili wanapigana – mmoja ni katika wenzake na mwingine ni katika maadui zake. Yule aliye katika wenzake akamtaka msaada juu ya adui yake. Musa akampiga ngumi akammaliza.” (28:15).

Musa alihofia kuchukua risala ya Mwenyezi Mungu kwa Firauni asije akamuua kabla kukamilisha lengo, lakini akiwa na nduguye na ikatokewa kuuawa, basi atachukua nafasi yake kuendeleza malengo.

Akasema – Mwenyezi Mungu –sivyo kabisa! Nendeni na ishara yetu, Hakika sisi tu pamoja nanyi, tunasikiliza. Basi mfikieni Firauni na mwambieni: Hakika sisi ni wajumbe wa Mola wa walimwengu wote. Ya kwamba uwaachilie wana wa Israil waende nasi.

Musa alihofia dhiki ya kifua, kufungika ulimi na kuuliwa, lakini Mwenyezi Mungu akamhakikishia usalama na akamwambia kuwa hakuna kitu kitaka- chokuwa katika hayo, kwa sababu mimi nitawasaidia na kuwanusuru. Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20: 46 – 47).

Akasema: Je, hatukukulea utotoni, na ukakaa kwetu katika umri wako miaka mingi? Na ukatenda kitendo chako ulichokitenda, nawe ukawa miongoni mwa wasio na shukrani?

Musa na Harun walielekea kwa Firauni, wakaingia kwake wakiwa wamevaa deraya ya sufu, mikononi mwao wakiwa na fimbo. Wakampa mwito wa kumwamini Mungu na kumpa sharti la kusilimu na kutii ili utawala wake ubakie na kudumu enzi yake.

Firauni aliwabeza wawili hawa, waliompa masharti ya kudumu utawala na enzi yake, wakiwa hawana cheo chochote wala mali. Hakutaka kuwaua kwa kuhofia asiambiwe kuwa ameshindwa na hoja akakimbilia upanga.

Lakini Firauni anaweza kuwa na hoja gani? Ni kwa mantiki gani atakayoweza kujadili? Hana kitu isipokuwa kuvungavunga na kumtajia Musa yaliyopita.

Je, hatukukulea na ukakaa nyumbani kwetu miaka, kisha ukatuulia mtu wetu na ukakimbia? Hii ndio shukrani yako? Zaidi ya hayo unadai kuwa wewe ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwetu? Unataka tukusikize na kukutii na sisi ndio mabwana zako na wafadhili wa neema zako?

Kisha Firauni akawegeukia watu wa baraza lake na akasema: “Basi mbona hakuvikwa vikukuku vya dhahabu?” (43:53). Kwenye dhahabu tu ndio kuna kuwa na siri ya mantiki ya mataghuti. Hakuna utume wala ubwana au ubora isipokuwa kwa ajili ya dhahabu na dhahabu yenyewe.

Musa (a.s) akamjibu kuhusu kuua akasema: “Nililifanya hilo nikiwa miongoni mwa wasioelewa.”

Yaani sikuelewa kuwa ngumi yangu itamuua. Nami nilikusudia kukinga na kutia adabu, nikakosea makusudio. Basi mimi nina dhambi gani katika hilo? Kukusudia ni nguzo ya msingi ya kosa la jinai kwa watu wa sharia.

Basi niliwakimbia nilipowahofia.

Sikukimbia hukumu ya uadilifu, bali nilikimbia dhulma kwa kuhofia kunichukulia kuwa ni muuaji wa makusudi. Kuna mmoja alimwambia Musa:

إِنَّ الْمَلَأَ يَأْتَمِرُونَ بِكَ لِيَقْتُلُوكَ فَاخْرُجْ إِنِّي لَكَ مِنَ النَّاصِحِينَ ﴿٢٠﴾

“Hakika wakubwa wanashauriana kukuua. Basi toka! Hakika mimi ni katika wanaokupa nasaha.” (28:20).

Na Mola wangu akanitunukia hukumu na akanijaalia niwe miongoni mwa mitume.

Firauni alimtajia Musa ufukara na utoro; Musa naye akamwambia kuwa utukufu haupimwi kwa mali wala kwa ufalme; isipokuwa uko mikononi mwa Mwenyezi Mungu, humpatia amtakaye katika waja wake. Na mimi Mwenyezi Mungu amenitunukia elimu ya dini yake na sharia yake kwa njia ya kheri na usawa na akanitukuza kwa kunituma kwako na kwa watu wako.

Musa aliendelea kumjibu Firauni, kuhusu malezi na akasema:

Na hiyo ndiyo neema ya kunisimbulia na wewe umewatia utumwani wana wa Israil?

Yaani unanisimbulia kwa malezi yako kwangu na unajitia kutojua kuwa sababu ni uadui wako wa kuwachinja watoto wa kiume wa watu wangu na kuwatia utumwani watoto wao wa kike? Mama yangu alipohofia wewe kunichinja akanitupa baharini na matokeo yake yakawa ni kuishi mimi mbali ugenini bila ya huruma ya mama na mapenzi ya baba? Hii ndiyo fadhila yako kwangu? Firauni alizibwa mdomo, akaanza kuwatafuta wabatilifu wake; kama utakavyoona katika kifungu kifuatacho.

قَالَ فِرْعَوْنُ وَمَا رَبُّ الْعَالَمِينَ ﴿٢٣﴾

23. Akasema Firauni: Na ni nani huyo Mola wa walimwengu wote?

قَالَ رَبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا إِن كُنتُم مُّوقِنِينَ ﴿٢٤﴾

24. Akasema: Ni Mola wa mbingu na ardhi ikiwa nyinyi mna yakini.

قَالَ لِمَنْ حَوْلَهُ أَلَا تَسْتَمِعُونَ ﴿٢٥﴾

25. Akawaambia waliomzunguuka: Je, hamsikii?

قَالَ رَبُّكُمْ وَرَبُّ آبَائِكُمُ الْأَوَّلِينَ ﴿٢٦﴾

26. Akasema: Ni Mola wenu na Mola wa baba zenu wa kwanza.

قَالَ إِنَّ رَسُولَكُمُ الَّذِي أُرْسِلَ إِلَيْكُمْ لَمَجْنُونٌ ﴿٢٧﴾

27. Akasema: Hakika mtume wenu mliyetumiwa ni mwenda wazimu.

قَالَ رَبُّ الْمَشْرِقِ وَالْمَغْرِبِ وَمَا بَيْنَهُمَا إِن كُنتُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٢٨﴾

28. Akasema: Ni Mola wa mashariki na magharibi na viliomo baina yake, ikiwa nyinyi mna akili.

قَالَ لَئِنِ اتَّخَذْتَ إِلَـٰهًا غَيْرِي لَأَجْعَلَنَّكَ مِنَ الْمَسْجُونِينَ ﴿٢٩﴾

29. Akasema: Kama ukimfanya mungu mwingine asiyekuwa mimi basi bila shaka nitakufanya miongoni mwa wafungwa.

قَالَ أَوَلَوْ جِئْتُكَ بِشَيْءٍ مُّبِينٍ ﴿٣٠﴾

30. Akasema: Ijapokuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi?

قَالَ فَأْتِ بِهِ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٣١﴾

31. Akasema: Kilete basi kama wewe ni katika wakweli.

فَأَلْقَىٰ عَصَاهُ فَإِذَا هِيَ ثُعْبَانٌ مُّبِينٌ ﴿٣٢﴾

32. Akaitupa fimbo, mara ikawa nyoka dhahiri.

وَنَزَعَ يَدَهُ فَإِذَا هِيَ بَيْضَاءُ لِلنَّاظِرِينَ ﴿٣٣﴾

33. Na akautoa mkono wake. Mara ukawa mweupe kwa watazamao.

قَالَ لِلْمَلَإِ حَوْلَهُ إِنَّ هَـٰذَا لَسَاحِرٌ عَلِيمٌ ﴿٣٤﴾

34. Akasema kuwaambia wakuu waliomzunguka: Hakika huyu ni mchawi, mjuzi.

يُرِيدُ أَن يُخْرِجَكُم مِّنْ أَرْضِكُم بِسِحْرِهِ فَمَاذَا تَأْمُرُونَ ﴿٣٥﴾

35. Anataka kuwatoa katika ardhi yenu. Basi mnatoa shauri gani?

قَالُوا أَرْجِهْ وَأَخَاهُ وَابْعَثْ فِي الْمَدَائِنِ حَاشِرِينَ ﴿٣٦﴾

35. Wakasema: Mwache kidogo yeye na ndugu yake, na uwatume wakusanyao watu mijini.

يَأْتُوكَ بِكُلِّ سَحَّارٍ عَلِيمٍ ﴿٣٧﴾

37. Wakuletee kila mchawi mkubwa, mjuzi.

MAJIBIZANO BAINA YA MUSA NA FIRAUNI

Aya 23 – 37

MAANA

Akasema Firauni: Na ninani huyo Mola wa walimwengu wote?

Ewe Musa! Wewe unadai kuwa ni Mtume wa Mola wa walimwengu wote; hebu tubainishie jinsi yake na hakika yake huyo Mola?

Akasema: “Ni Mola wa mbingu na ardhi ikiwa nyinyi mna yakini.”

Musa alisema: Mwenyezi Mungu hajulikani isipokuwa kwa sifa zake na athari zake; zikiwa ni pamoja na huku kuumbwa ulimwengu huu wa ajabu katika mpangilio wake na nidhamu yake. Basi fikirini na mzingatie ikiwa mna akili zinazoweza kutambua kuwa nidhamu hii haiwezekani ila kwa uweza wa ujuzi na hekima.

Firauniakawaambia waliomzunguuka: Je, hamsikii?

Yaani mnasikia maajabu hayo. Hatujawahi kusikia haya kwa mababa zetu wa kwanza.

Akasema: Ni Mola wenu na Mola wa baba zenu wa kwanza.

Musa alisema kwa kusisitiza kwamba Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa ulimwengu, muumba wenu na muumba wa baba zenu wa mwanzo na pia ndiye muumba wa huyu Firauni mnayemfanya mungu na kumwabudu.

Akasema: Hakika mtume wenu huyu mliyetumiwa ni mwenda wazimu.

Musa ni mwendawazimu katika mantiki ya Firauni, kwa nini? Kwa sababu amesema Firauni si mungu bali ni kiumbe. Mantiki haya ya kifirauni anayo kila anayedai asichokuwa nacho. Yeyote anayedai kuwa na elimu naye ni mjinga, ikhlasi naye ni mhaini au ukweli naye ni mrongo, basi yeye yuko katika mila ya Firauni na desturi yake. Lau atapata wanaomwamini atasema: Mimi ndiye mola wenu au simjui mungu mwingine kwenu zaidi ya mimi; kama alivyosema Firauni.

Akasema: Ni Mola wa mashariki na magharibi na viliomo baina yake, ikiwa nyinyi mna akili.

Musa aliendelea kushikilia msimamo wake kuwa Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa kila kitu. Akaashiria kuchomoza jua na kuchwa kwake, ambapo Firauni hawezi kujasiri kusema kuwa yeye ndiye anayelichomoza jua mashariki na kulipeleka magharibi.

Kwa hiyo alipigwa na butwaa aliposikia maneno haya kutoka kwa Musa; sawa na alivyopigwa na butwaa Namrud kabla yake, pale Ibrahim(a.s) alipomnyamazisha kwa kusema:

فَإِنَّ اللَّـهَ يَأْتِي بِالشَّمْسِ مِنَ الْمَشْرِقِ فَأْتِ بِهَا مِنَ الْمَغْرِبِ ﴿٢٥٨﴾

“Hakika Mwenyezi Mungu hulichomoza jua mashariki, basi wewe lichomoze magharibi.”

Juz. 3 (2:258).

Firauni alipoishiwa, alikereka, akawa anatoa vitisho naakasema: Kama ukimfanya mungu mwingine asiyekuwa mimi basi bila shaka nitakufanya miongoni mwa wafungwa.

Jela na kutesa ndio silaha pekee ya utawala muovu wa mabavu dhidi ya haki uadilifu na uhuru, tangu zamani. Lakini jihadi ya wakombozi na ukakamavu wao, unaifanya silaha ya mataghuti ishindwe kwenye shingo zao na vifua vyao; kama ilivyoshindwa silaha ya Firauni.

Walisema wa kale: Mwenye kuchomoa upanga wa dhulma atauliwa nao.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:

فَكُلًّا أَخَذْنَا بِذَنبِهِ فَمِنْهُم مَّنْ أَرْسَلْنَا عَلَيْهِ حَاصِبًا وَمِنْهُم مَّنْ أَخَذَتْهُ الصَّيْحَةُ وَمِنْهُم مَّنْ خَسَفْنَا بِهِ الْأَرْضَ ﴿٤٠﴾

“Kila mmoja tulimtesa kwa makosa yake. Kati yao wapo tuliowapelekea kimbunga cha changarawe, na kati yao wapo walionyakuliwa na ukelele na kati yao wapo ambao tuliwadidimiza katika ardhi.” (29:40).

Akasema: Ijapokuwa nitakuletea kitu cha kubainisha wazi?” Akasema: Kilete basi kama wewe ni katika wakweli.

Musa hakuogopa vitisho vya Firauni na akamwambia kwa kujiamini kuwa utanifanya mfungwa hata kama ni mwenye haki, kwa kukuletea dalili isiyo na shaka kwako na kwa mwingine?

Atajibu nini Firauni? Je, amwambie ndio nitakufunga hata kama ni mwenye haki? Hawezi kumwambia hivi, kwa sababu itakuwa ni kukubali ukweli kuwa Musa ni Mtume wa Mola wa viumbe wote na kwamba yeye ni mzushi katika madai yake ya uungu. Kwa hiyo ndio akalazimika kusema lete hiyo dalili kama wewe ni mkweli.

Akaitupa fimbo mara ikawa nyoka dhahiri. Na akautoa mkono wake. Mara ukawa mweupe kwa watazamao. Akasema kuwaambia wakuu waliomzunguka: Hakika huyu ni mchawi mjuzi. Anataka kuwatoa katika ardhi yenu. Basi mnatoa shauri gani? Wakasema: Mwache kidogo yeye na ndugu yake, na uwatume wakusanyao watu mijini. Wakuletee kila mchawi mkubwa, mjuzi.

Aya hizi sita zimetangulia katika Juz. 9 (7:107 - 112) zikifanana kiutaratibu, kimpangilio na hata herufi; isipokuwa katika mambo mawili:

Hapa imesemwa: ‘mchawi mkubwa’ na kule ikasemwa ‘mchawi’ hakuna tofauti katika maneno haya isipokuwa kutilia mkazo.

Hapa imesemwa: ‘Akasema kuwaambia wakuu waliomzunguka: Hakika huyu ni mchawi mjuzi,’ na kule imesemwa: ‘Wakasema wakuu wa watu wa Firauni: Hakika huyu ni mchawi mjuzi.’ Tofauti hapa ni kubwa kama inavyojionyesha.

Kwa sababu hapa aliyesema ni Firauni kuwaambia wakuu na kule wakuu ndio waliosema kumwambia Firauni. Sasa je, kuna wajihi gani wa kuunganisha baina ya Aya mbili hizi?

Jibu : Sikupata ishara yoyote ya hilo katika tafsiri nilizonazo, wala sijui sababu yake. Kwa vyovyote iwavyo, jibu ninaloliona ni kuwa Firauni ndiye aliyeanza kuwaambia jamaa zake kuwa huyu ni mchawi; kisha jamaa zake nao wakaanza kuambiana kuwa ni kweli Musa ni mchawi; kama ilivyo kwa wanaoongozwa, wanaigiza kiongozi wao na kutolea ushahidi kauli zake.

Hapo basi hakuna kupingana baina ya Aya mbili. Firauni aliwaambia jamaa zake nao wakamwambia yeye kwa kumwigiza.


5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA

فَجُمِعَ السَّحَرَةُ لِمِيقَاتِ يَوْمٍ مَّعْلُومٍ ﴿٣٨﴾

38. Basi wakakusanywa wachawi wakati wa siku maalum.

وَقِيلَ لِلنَّاسِ هَلْ أَنتُم مُّجْتَمِعُونَ ﴿٣٩﴾

39. Na watu wakaambiwa: Je, mtakusanyika?

لَعَلَّنَا نَتَّبِعُ السَّحَرَةَ إِن كَانُوا هُمُ الْغَالِبِينَ ﴿٤٠﴾

40. Huenda tutawafuata wachawi wakiwa wao ndio watakaoshinda.

فَلَمَّا جَاءَ السَّحَرَةُ قَالُوا لِفِرْعَوْنَ أَئِنَّ لَنَا لَأَجْرًا إِن كُنَّا نَحْنُ الْغَالِبِينَ ﴿٤١﴾

41. Basi walipokuja wachawi wakamwambia Firauni: Je, tutapata ujira ikiwa tutashinda?

قَالَ نَعَمْ وَإِنَّكُمْ إِذًا لَّمِنَ الْمُقَرَّبِينَ ﴿٤٢﴾

42. Akasema: Ndio, hapo nanyi hakika mtakuwa miongoni mwa wanaokurubishwa.

قَالَ لَهُم مُّوسَىٰ أَلْقُوا مَا أَنتُم مُّلْقُونَ ﴿٤٣﴾

43. Musa akawaambia: Tupeni mnavyotaka kutupa.

فَأَلْقَوْا حِبَالَهُمْ وَعِصِيَّهُمْ وَقَالُوا بِعِزَّةِ فِرْعَوْنَ إِنَّا لَنَحْنُ الْغَالِبُونَ ﴿٤٤﴾

44. Wakatupa kamba zao na fimbo zao na wakasema: Kwa nguvu za Firauni hakika sisi bila shaka ni wenye kushinda.

فَأَلْقَىٰ مُوسَىٰ عَصَاهُ فَإِذَا هِيَ تَلْقَفُ مَا يَأْفِكُونَ ﴿٤٥﴾

45. Musa akatupa fimbo yake, mara ikavimeza walivyovibuni.

فَأُلْقِيَ السَّحَرَةُ سَاجِدِينَ ﴿٤٦﴾

46. Wachawi wakapomoka kusujudu.

قَالُوا آمَنَّا بِرَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٤٧﴾

47. Wakasema: Tumemwamini Mola wa Walimwengu.

رَبِّ مُوسَىٰ وَهَارُونَ ﴿٤٨﴾

48. Mola wa Musa na Harun.

قَالَ آمَنتُمْ لَهُ قَبْلَ أَنْ آذَنَ لَكُمْ إِنَّهُ لَكَبِيرُكُمُ الَّذِي عَلَّمَكُمُ السِّحْرَ فَلَسَوْفَ تَعْلَمُونَ لَأُقَطِّعَنَّ أَيْدِيَكُمْ وَأَرْجُلَكُم مِّنْ خِلَافٍ وَلَأُصَلِّبَنَّكُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٤٩﴾

49. Akasema Firauni: Je, mmemwamini kabla sijawaruhusu. Hakika yeye ndiye mkubwa wenu aliyewafundisha uchawi, lakini punde mtajua. Nitawakata mikono yenu na miguu yenu kwa kubadilisha, kisha nitawasulubu nyote.

قَالُوا لَا ضَيْرَ إِنَّا إِلَىٰ رَبِّنَا مُنقَلِبُونَ ﴿٥٠﴾

50. Wakasema: Haidhuru, hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu.

إِنَّا نَطْمَعُ أَن يَغْفِرَ لَنَا رَبُّنَا خَطَايَانَا أَن كُنَّا أَوَّلَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٥١﴾

51. Hakika sisi tunatumai Mola wetu atughufirie makosa yetu kwa kuwa ndio wa kwanza kuamini.

WALIFIKA WACHAWI

Aya 38 – 51

MAANA

Basi wakakusanywa wachawi wakati wa siku maalum.

Siku yenyewe ni sikukuu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

قَالَ مَوْعِدُكُمْ يَوْمُ الزِّينَةِ وَأَن يُحْشَرَ النَّاسُ ضُحًى ﴿٥٩﴾

“Akasema: Miadi yenu ni siku ya sikukuu na watu wakusanywe kabla ya adhuhuri.” Juz. 16 (20:59).

Na watu wakaambiwa: Je, mtakusanyika ili mshuhudie mapambano haya? Watu hawahitaji kuhimizwa kwenye mambo haya; hao wenyewe watashindana kufika. Na hili ndilo alilolitaka Musa, ili haki idhihirike na batili ibatilike machoni mwa watu.

Huenda tutawafuata wachawi wakiwa wao ndio watakaoshinda.

Waliosema haya kwa watu ni Firauni na wakuu wake. Dhahiri ya kauli yao hii inaashiria kuwa wana shaka na dini ya wachawi na kwamba wao wanitafuta haki ili waifuate, lakini haya sio makusudio yao. Kwa sababu wao na wachawi wako kwenye dini moja. Makusudio yao ni kuwa huenda tutabaki kwenye uthabiti wa dini yetu wala hatutamfuta Musa.

Basi walipokuja wachawi wakamwambia Firauni: Je, tutapata ujira ikiwa tutashinda? Akasema: Ndio, hapo nanyi hakika mtakuwa miongoni mwa wanaokurubishwa. Musa akawaambia: Tupeni mnavyotaka kutupa. Wakatupa kamba zao na fimbo zao na wakasema:

“Kwa nguvu za Firauni hakika sisi bila shaka ni wenye kushinda. Musa akatupa fimbo yake, mara ikavimeza walivyovibuni. Wachawi wakapomoka kusujudu.Wakasema: Tumemwamini Mola wa Walimwengu. Mola wa Musa na Harun.

Akasema Firauni: Je, mmemwamini kabla sijawaruhusu. Hakika yeye ndiye mkubwa wenu aliyewafundisha uchawi, lakini punde mtajua. Nitawakata mikono yenu na miguu yenu kwa kubadilisha, kisha nitawasulubu nyote. Wakasema: Haidhuru, hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu. Hakika sisi tunatumai Mola wetu atughufirie makosa yetu kwa kuwa ndio wa kwanza kuamini.

Aya hizi zote zimetajwa katika Juz. 9 (7: 113 – 126); wala hakuna tofauti baina ya hapa na huko, isipokuwa katika baadhi ya ibara tu; kwa mfano kule imesemwa: ‘wakaja wachawi’ na hapa ikasemwa; ‘walipokuja wachawi,’ n.k.

وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ أَنْ أَسْرِ بِعِبَادِي إِنَّكُم مُّتَّبَعُونَ ﴿٥٢﴾

52. Na tulimpelekea wahyi Musa kwamba nenda na waja wangu wakati wa usiku, kwa hakika mtafuatwa.

فَأَرْسَلَ فِرْعَوْنُ فِي الْمَدَائِنِ حَاشِرِينَ ﴿٥٣﴾

53. Basi Firauni akawatuma mjini wakusanyao.

إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ لَشِرْذِمَةٌ قَلِيلُونَ ﴿٥٤﴾

54. Hakika hawa ni kikundi kidogo.

وَإِنَّهُمْ لَنَا لَغَائِظُونَ ﴿٥٥﴾

55. Nao wanatuudhi.

وَإِنَّا لَجَمِيعٌ حَاذِرُونَ ﴿٥٦﴾

56. Na sisi ni wengi wenye kuchukua hadhari.

فَأَخْرَجْنَاهُم مِّن جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ ﴿٥٧﴾

58. Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem.

وَكُنُوزٍ وَمَقَامٍ كَرِيمٍ ﴿٥٨﴾

58. Na mahazina na vyeo vya heshima.

كَذَٰلِكَ وَأَوْرَثْنَاهَا بَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿٥٩﴾

59. Hivyo ndivyo! Na tukawarithisha wana wa Israil.

فَأَتْبَعُوهُم مُّشْرِقِينَ ﴿٦٠﴾

60. Kisha wakawafuata walipotokewa na jua.

فَلَمَّا تَرَاءَى الْجَمْعَانِ قَالَ أَصْحَابُ مُوسَىٰ إِنَّا لَمُدْرَكُونَ ﴿٦١﴾

61. Yalipoonana makundi mawili, watu wa Musa wakasema: Hakika tumepatikana.

قَالَ كَلَّا إِنَّ مَعِيَ رَبِّي سَيَهْدِينِ ﴿٦٢﴾

62. Akasema: Hapana! Hakika Mola wangu yuko pamoja nami, ataniongoza.

فَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ أَنِ اضْرِب بِّعَصَاكَ الْبَحْرَ فَانفَلَقَ فَكَانَ كُلُّ فِرْقٍ كَالطَّوْدِ الْعَظِيمِ ﴿٦٣﴾

63. Tulimpelekea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana na kila sehemu ikawa kama milima mkubwa.

وَأَزْلَفْنَا ثَمَّ الْآخَرِينَ ﴿٦٤﴾

64. Na tukawajongeza hapo wale wengine.

وَأَنجَيْنَا مُوسَىٰ وَمَن مَّعَهُ أَجْمَعِينَ ﴿٦٥﴾

65. Na tukamwokoa Musa na waliokuwa pamoja naye wote.

ثُمَّ أَغْرَقْنَا الْآخَرِينَ ﴿٦٦﴾

66. Kisha tukawazamisha hao wengine.

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿٦٧﴾

67. Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara lakini wengi wao si wenye kuamini.

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿٦٨﴾

68. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

KUGHARIKI FAIRAUNI NA WATU WAKE

Aya 52 – 68

MAANA

Na tulimpelekea wahyi Musa kwamba nenda na waja wangu wakati wa usiku, kwa hakika mtafuatwa.

Mwenyezi Mungu alimwamrisha Musa atoke na wana wa Israil kutoka ardhi ya Misri usiku na akampa habari kwamba Firauni atawafuata ili awarudishe.

Basi Firauni akawatuma mjini wakusanyao.

Firauni alipojua kuwa Musa na watu wake wametoka aliwakusanyia watu ili awarudishe kwenye utawala wake na awape adhabu ya utoro.

Akasema: Hakika hawa ni kikundi kidogo nao wanatuudhi na sisi ni wengi wenye kuchukua hadhari.

Ni nani huyo Musa na watu wake. Wao si chochote kwetu; wanajaribu kutukasirisha na kutufanyia jeuri, na sisi tunawachunga. Basi watapata adhabu ya matendo yao. Lakini juu ya mipango ya Firauni kuna mipango ya Mwenyezi Mungu. Imam(a.s) anasema:Mambo yanakuwa kwa makadirio ili maangamizi yawe kwa mpangilio.

Basi tukawatoa katika mabustani na chemchem na mahazina na vyeo vya heshima.

Firauni na jeshi lake alitoka ili amwadhibu Musa na watu wake, lakini Mungu akawaadhibu wao na akawatoa katika yale waliyokuwa wakiyamilikii na kustarehe nayo; yakiwemo makasri ya ghorofa, mito inayotiririka, miti iliyojaa matunda kochokocho, mahazina yaliyojificha, mabembea, mabwawa ya kuogelea na sehemu za kupunga upepo. Yote haya na mengineyo waliyaacha bila ya kurudi.

Hivyo ndivyo! Na tukawarithisha wana wa Israil.

Tabari anasema: “Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwarithisha wana wa Israil majumba ya Firauni na watu wake.” Abu Hayyani Al-Andalusi naye amesema katika kitabu Al-bahrul-Muhit: “Haya ndio maana ya dhahiri, kwa sababu Aya ya kurithishwa wana wa Israil, imekuja moja kwa moja baada ya Aya ya kuwatoa.”

Wengine wamesema kuwa Mwenyezi Mungu aliwarithisha wana wa Israil mfano wa alivyokuwa Firauni na watu wake. Kwa sababu Waisrail hawakurudi Misri baada ya kuitoka.

Vyovyote iwavyo Aya inaeleza kuwa Mwenyezi Mungu hawaachi madhal- imu na dhulma yao na kwamba yeye anawaadhibu mikononi mwa wenye ikhlasi au kwa sababu yoyote. Haya ndiyo tunayoyaamini na kuyakubali. Ama uchunguzi wa historia na mfano wake tunawaachia wataalamu wake, ila ikiwa tuna yakini nayo.

Kisha wakawafuata walipotokewa na jua.

Firauni alitoka na jeshi lake la wapanda farasi na wendao kwa miguu kumtafuta Musa na watu wake wakawapata lilipochomoza jua.

Yalipoonana makundi mawili, kundi la Musa na la Firauni, watu wa Musa wakasema : Hakika tumepatikana.

Walisema hivyo kwa hofu na fazaa, kuwa adui amekwishatufikia hatuna la kufanya.

Akasema: Hapana! Hakika Mola wangu yuko pamoja nami, ataniongoza. Tulimpelekea wahyi Musa tukamwambia: Piga bahari kwa fimbo yako. Basi ikatengana na kila sehemu ikawa kama milima mkubwa.

Musa aliwaambia watu wake kuwa msimuogope Firauni na nguvu zake. Hakika Mwenyezi Mungu ana nguvu zaidi na yuko pamoja nami, nanyi mtaona.

Hakumaliza maneno yake, mara Mwenyezi Mungu akamwamrisha kupiga bahari kwa fimbo yake. Alipoipiga ikapasuka njia kumi na mbili kulingana na koo za waisrail. Maji yakainuka baina ya njia moja na nyingine kama mlima. Musa na watu wake wakavuka hadi ng’ambo ya pili.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:77).

Na tukawajongeza hapo wale wengine. Na tukamwokoa Musa na waliokuwa pamoja naye wote. Kisha tukawazamisha hao wengine.

Makusudio ya wengine ni kundi la Firauni. Maana ni kuwa baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwavusha wana wa Israil upande wa pili na wakawa wameokoka, kundi la Firauni nalo liliwasili. Wakaona muuujiza mkubwa – maji ya bahari yamesimama kama jabali na kutengeneza njia. Firauni akawaambia watu wake: Tazameni bahari ilivyoitikia matakwa yangu na kunifungulia njia ya kuwafuata walionitoroka.

Kisha wakajitoma na wakaenda kwa amani na utulivu. Hawakufika katikati, bahari ikawafunika wote, baada ya kuhadharishwa na kupewa muda mrefu, lakini walizama kwenye upotevu wao.

Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara ya muujiza, mazingatio na mawaidha, lakini wengi wao si wenye kuamini. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

Wengi wao hapa wanakusudiwa wana wa Israil waliookolewa na Mwenyezi Mungu mikononi mwa Firauni, kwa kuchukilia dhahiri ya mfumo wa maneno ulivyo.

Na wala sio walioangamia, kama wasemavyo baadhi ya wafasiri. Dalili ya kuwa makusudio ni wana wa Israil ni kuwa wafuasi wa Firauni wote wlikuwa makafiri, bila ya kubaki; hasa wale aliokuwa nao. Na wana wa Israili, walipookolewa na Mungu kutoka kwa Firauni, walimwambia Musa: Tunataka sanamu tuliabudu badala ya Mwenyezi Mungu:

وَجَاوَزْنَا بِبَنِي إِسْرَائِيلَ الْبَحْرَ فَأَتَوْا عَلَىٰ قَوْمٍ يَعْكُفُونَ عَلَىٰ أَصْنَامٍ لَّهُمْ قَالُوا يَا مُوسَى اجْعَل لَّنَا إِلَـٰهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ ﴿١٣٨﴾

“Na tukawavusha bahari wana wa Israil na wakawafikia waliokuwa wakiyaabudu masanamu yao; wakasema: Ewe Musa! Hebu nasi tufanyie waungu kama hawa walivyo na waungu.” Juz. 9 (7:138).

Kwa hiyo maana yanakuwa kwamba Waisraili walishuhudia muujiza wa kupasuka bahari na miujiza mingineyo, lakini bado waliendelea kung’ang’ania ukafiri wao na jeuri yao.

وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ إِبْرَاهِيمَ ﴿٦٩﴾

69. Na wasomee habari za Ibrahim.

إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ وَقَوْمِهِ مَا تَعْبُدُونَ ﴿٧٠﴾

70. Alipomwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?

قَالُوا نَعْبُدُ أَصْنَامًا فَنَظَلُّ لَهَا عَاكِفِينَ ﴿٧١﴾

71. Wakasema: Tunaabudu masanamu nasi tutaendelea kuyanyenyekea.

قَالَ هَلْ يَسْمَعُونَكُمْ إِذْ تَدْعُونَ ﴿٧٢﴾

72. Akasema: Je yanawasikia mnapoyaita?

أَوْ يَنفَعُونَكُمْ أَوْ يَضُرُّونَ ﴿٧٣﴾

73. Au yanawafaa au yanawadhuru?

قَالُوا بَلْ وَجَدْنَا آبَاءَنَا كَذَٰلِكَ يَفْعَلُونَ ﴿٧٤﴾

Wakasema: Bali tumewakuta mababa zetu wakifanya hivyo hivyo.

قَالَ أَفَرَأَيْتُم مَّا كُنتُمْ تَعْبُدُونَ ﴿٧٥﴾

75. Akasema: Je, mmewaona mnaowaabudu?

أَنتُمْ وَآبَاؤُكُمُ الْأَقْدَمُونَ ﴿٧٦﴾

76. Nyinyi na baba zenu wa zamani?

فَإِنَّهُمْ عَدُوٌّ لِّي إِلَّا رَبَّ الْعَالَمِينَ ﴿٧٧﴾

77. Hakika hao ni maadui zangu isipokuwa Mola wa walimwengu wote.

الَّذِي خَلَقَنِي فَهُوَ يَهْدِينِ ﴿٧٨﴾

78. Ambaye ameniumba naye ananiongoza.

وَالَّذِي هُوَ يُطْعِمُنِي وَيَسْقِينِ ﴿٧٩﴾

79. Na ambaye ananilisha na kuninywesha.

وَإِذَا مَرِضْتُ فَهُوَ يَشْفِينِ ﴿٨٠﴾

80. Na ninapougua basi yeye ananiponya.

وَالَّذِي يُمِيتُنِي ثُمَّ يُحْيِينِ ﴿٨١﴾

81. Na ambaye atanifisha kisha atanihuisha.

وَالَّذِي أَطْمَعُ أَن يَغْفِرَ لِي خَطِيئَتِي يَوْمَ الدِّينِ ﴿٨٢﴾

82. Na ambaye ndiye ninayemtumai kunighufuria makosa yangu siku ya malipo.

رَبِّ هَبْ لِي حُكْمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ ﴿٨٣﴾

83. Mola wangu! Nitunukie hukumu na uniunganishe na wema.

وَاجْعَل لِّي لِسَانَ صِدْقٍ فِي الْآخِرِينَ ﴿٨٤﴾

84. Na unijaalie kutajwa kwa wema na wengine.

وَاجْعَلْنِي مِن وَرَثَةِ جَنَّةِ النَّعِيمِ ﴿٨٥﴾

85. Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema.

وَاغْفِرْ لِأَبِي إِنَّهُ كَانَ مِنَ الضَّالِّينَ ﴿٨٦﴾

86. Na umghufirie baba yangu, kwani alikuwa miongoni mwa wapotevu.

وَلَا تُخْزِنِي يَوْمَ يُبْعَثُونَ ﴿٨٧﴾

87. Wala usinihizi siku watakapofufuliwa.

يَوْمَ لَا يَنفَعُ مَالٌ وَلَا بَنُونَ ﴿٨٨﴾

88. Siku ambayo haitafaa mali wala wana.

إِلَّا مَنْ أَتَى اللَّـهَ بِقَلْبٍ سَلِيمٍ ﴿٨٩﴾

89. Isipokuwa mwenye kuja kwa Mwenyezi Mungu na moyo uliosalimika.

IBRAHIM

Aya 69 – 89

MAANA

Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekitaja kisa cha Ibrahim kwa kukigawa kulingana na mnasaba ulivyo.

Katika Aya hizi Mwenyezi Mungu (s.w.t) amerudia majibizano baina ya Ibrahim na watu wake, kwa mfumo mwingine unaotofautiana na ule ulio katika Juz. 17 (21:51).

Na wasomee habari za Ibrahim.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) kuwa awasomee makuraishi ambao wanadai kuwa ni kizazi cha Ibrahim na wako kwenye dini yake.

Alipomwambia baba yake na kaumu yake: Mnaabudu nini?

Katika Juz.7 (6:74) tumetaja tofauti za wafasiri kuhusu baba aliyeambiwa maneno haya na Ibrahim, kuwa je, ni baba yake hasa au ni baba wa kimajazi au ni ami yake?

Wakasema: Tunaabudu masanamu nasi tutaendelea kuyanyenyekea.

Tutadumu kuyaabudu na kuyatukuza. Kukubali kwao kuabudu masanamu kunajulisha kuwa neno sanamu halikuwa linamaanisha shutuma katika ufahamu wao, kama tunavyofahamu sisi; bali neno hilo lilikuwa likimaanisha utukufu na ukuu.

Akasema: Je yanawasikia mnapoyaita? Au yanawafaa au yanawadhuru?

Ni kawaida anayeabudiwa asikie, aone, adhuru na kunufaisha. Je, haya mnayoyaabudu yana sifa hizi? Swali hapa ni la kupinga.

Wakasema: Bali tumewakuta mababa zetu wakifanya hivyo hivyo.

Hii ni kukubali kuwa wao ni waigaji. Wala hilo si ajabu. Katika karne ya ishirini, zama za kutembea angani, tumeona wafuasi wakiwaiga viongozi wao na wakitoa dalili kwa kauli zao na kuzichukulia kuwa ni msingi, bila ya kuhakisha na kuchunguza.

Akasema: Je, mmewaona mnaowaabudu nyinyi na baba zenu wa zamani? Hakika hao ni maadui zangu isipokuwa Mola wa walimwengu wote.

Ikiwa nyinyi mnawaiga baba zenu, basi mimi simwigi yeyote na ninatangaza kujitenga kwangu na uadui wangu kwa hao waungu wenu; wala siabudu isipokuwa Mola wa walimwengu wote. Yeye ndiye walii wangu duniani na akhera. Yakiwa masanamu ni miungu, kama mnavyodai, basi na waniteremshie hasira zao, mimi napingana nao.

Ambaye ameniumba naye ananiongoza.

Mwenyezi Mungu amenipa akili nami naitumia kuniongoza kwenye haki. Ninaifuata na ninaitumia vizuri; wala simuigi yoyote; kama mnavyodai.

Na ambaye ananilisha na kuninywesha.

Kwa kuzifanya nyepesi sababu kwangu mimi na kwa viumbe vyake vyote.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameiumba ardhi hii na akaweka kila wanayoyahitajia na akasema: Yeye ndiye aliyeidhalisha ardhi kwa ajili yenu, basi tembeeni katika pande zake na kuleni katika riziki zake. Na kwake yeye ndio kufufuliwa.

Na ninapougua basi yeye ananiponya kutokana na madawa aliyoyaumba.

Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anasema, “Hakika kila ugonjwa una dawa, dawa ikifika kwenye ugonjwa hupona kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.” Kuna Hadithi nyingine isemayo: Hakika Mwenyezi Mungu ameteremsha ugonjwa na dawa, basi fanyeni dawa wala msifanye dawa kwa haramu.

Na ambaye atanifisha kisha atanihuisha na ambaye ndiye ninayemtumai kunighufuria makosa yangu siku ya malipo.

Uhai, mauti na maghufira yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu, hilo halina shaka. Na Ibrahim(a.s) ni mwenye kuhifadhiwa na makosa na hatia (maasumu). Katika isma ya kila maasumu ni kuikuza hofu yake kwa Mwenyezi Mungu.

Mola wangu! Nitunukie hukumu.

Makusudio ya hukumu hapa, sio utawala bali ni hekima na kukata hukumu:

وَآتَيْنَاهُ الْحِكْمَةَ وَفَصْلَ الْخِطَابِ ﴿٢٠﴾

“Na tukampa hekima na kukata hukumu.” (38:20).

Na uniunganishe na wema.

Unipe tawfiki ya kufuata nyao zao na kutenda matendo yao.

Na unijaalie kutajwa kwa wema na wengine.

Makusudio ya wengine ni umma utakaokuja baadaye. Maana ni nijaalie kutajwa kwa wema baina ya watu baada yangu. Mwenyezi Mungu aliitikia dua yake; ambapo dini zote za mbinguni zimeafikiana kumtukuza na kumwadhimisha Nabii Ibrahim(a.s) .

Na unijaalie katika warithi wa Bustani za neema.

Ni nani anayestahiki hizo zaidi kuliko Ibrahim.

Na umghufirie baba yangu, kwani alikuwa miongoni mwa wapotevu.

Angalia tafsiri ya “Na haikuwa Ibrahim kumtakia msamaha baba yake ila ni kwa sababu ya ahadi aliyofanya naye, lakini ilipopambanukia kuwa yeye ni adui wa Mwenyezi Mungu, alijiepusha naye.” Juz. 11 (9:114).

Wala usinihizi siku watakapofufuliwa.

Dua hii ni katika aina ya dua za mitume na viongozi wema.Siku ambayo haitafaa mali wala wana. Isipokuwa mwenye kuja kwa Mwenyezi Mungu na moyo uliosalimika.

Kutokana na maafa ya ukafiri, unafiki, mifundo, ria na maafa mengineyo na maradhi.

Moyo ukiwa salama na uchafu, basi viungo vyote huwa salama: ulimi utasalimika na uwongo, kusengenya, kusikiliza upuzi na ubatilifu. Vile vile mkono unasalimika na kufanya haramu na tupu kutokana na zina na uovu.


6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA

وَأُزْلِفَتِ الْجَنَّةُ لِلْمُتَّقِينَ ﴿٩٠﴾

90. Na Bustani (Pepo) itasogezwa kwa wenye takua.

وَبُرِّزَتِ الْجَحِيمُ لِلْغَاوِينَ ﴿٩١﴾

91. Na Jahannam itadhihirishwa kwa wapotofu.

وَقِيلَ لَهُمْ أَيْنَ مَا كُنتُمْ تَعْبُدُونَ ﴿٩٢﴾

92. Na wataambiwa, wako wapi mliokuwa mkiwaabudu.

مِن دُونِ اللَّـهِ هَلْ يَنصُرُونَكُمْ أَوْ يَنتَصِرُونَ ﴿٩٣﴾

93. Badala ya Mwenyezi Mungu? Je, watawasaidia au kujisaidia wenyewe?

فَكُبْكِبُوا فِيهَا هُمْ وَالْغَاوُونَ ﴿٩٤﴾

94. Basi watavurumizwa humo wao na wapotofu.

وَجُنُودُ إِبْلِيسَ أَجْمَعُونَ ﴿٩٥﴾

95. Na majeshi ya Ibilisi yote.

قَالُوا وَهُمْ فِيهَا يَخْتَصِمُونَ ﴿٩٦﴾

96. Watasema na hali ya kuwa wanazozana humo:

تَاللَّـهِ إِن كُنَّا لَفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٩٧﴾

97. Wallah! Hakika tulikuwa katika upotevu ulio wazi.

إِذْ نُسَوِّيكُم بِرَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٩٨﴾

98. Tulipowafanya sawa na Mola wa walimwengu wote.

وَمَا أَضَلَّنَا إِلَّا الْمُجْرِمُونَ ﴿٩٩﴾

99. Na hawakutupoteza ila wakosefu.

فَمَا لَنَا مِن شَافِعِينَ ﴿١٠٠﴾

100. Basi hatuna waombezi.

وَلَا صَدِيقٍ حَمِيمٍ ﴿١٠١﴾

101. Wala rafiki wa dhati.

فَلَوْ أَنَّ لَنَا كَرَّةً فَنَكُونَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٠٢﴾

102. Laiti tungepata kurejea tena tungelikuwa katika waumi- ni.

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٠٣﴾

103. Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini.

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿١٠٤﴾

104. Na hakika Mola wako ndiye mwenye nguvu mwenye kurehemu.

PEPO KWA WENYE TAKUA NA MOTO KWA WAPOTEVU

Aya 90 – 104

MAANA

Na Bustani (Pepo) itasogezwa kwa wenye takua

Bila shaka iko karibu na mwenye kuongoka na akamcha Mungu na iko mbali na mwenye kupotea.

Na Jahannam itadhihirishwa kwa wapotofu.

Ataidhihirisha Mwenyezi Mungu kwa wale walioikana na kuikadhibisha.

Na wataambiwa wako wapi mliokuwa mkiwaabudu badala ya Mwenyezi Mungu? Na mkiwatarajia kwa siku hii, huku mkisema kuwa mliwabudu ili wawakurubishe kwa Mwenyezi Mungu?

Je, watawasaidia au kujisaidia wenyewe?

Hakika wao hawawezi kuwasaidia wala kujisaidia wenyewe.

Basi watavurumizwa humo wao na wapotofu na majeshi ya Ibilisi yote.

Wao ni hao waungu wao na wapotofu ni wale walioabudu. Mwanajeshi wa Ibilisi ni kila mpotofu na mpotoshaji. Mwenyezi Mungu atawachanganya wote kisha awatupe kwenye shimo la Jahannam.

Watasema na hali ya kuwa wanazozana humo: Wallah! Hakika tulikuwa katika upotevu ulio wazi, tulipowafanya sawa na Mola wa walimwengu wote. Na hawakutupoteza ila wakosefu.

Wapotofu kesho watasema, baada ya kupitwa na wakati, kuwaambia waungu wao na mashetani wao, kwamba nyinyi ndio mliokuwa viongozi wetu wa upofu na upotevu, wakati tulipowaabudu na kuwafanya mko sawa na Mwenyezi Mungu. Na wakosefu ndio waliokuwa kikwazo, ambao ni viongozi wa manufaa na masilahi, asili ya ufisadi na balaa.

Basi hatuna waombezi wala rafiki wa dhati.

Kesho hakuna uombezi wala ugombezi. Hakuna kitakachomfaa mtu isipokuwa moyo ulio salama na amali njema. Na muovu ni yule asiyekuwa na mawili hayo.

Laiti tungepata kurejea tena tungelikuwa katika waumini.

Baada ya kukata tamaaa na kila kitu ndio wanatamani kurudi duniani ili waamiini na kutenda. Mwenyezi Mungu anasema:

وَلَوْ رُدُّوا لَعَادُوا لِمَا نُهُوا عَنْهُ وَإِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ ﴿٢٨﴾

“Na kama wangelirudishwa, bila shaka wangeyarudia yale waliyokatazwa na hakika wao ni waongo.” Juz. 7 (6:28)

Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

Imetangulia kwa herufi zake, katika Aya 67 na 68 ya sura hii.

كَذَّبَتْ قَوْمُ نُوحٍ الْمُرْسَلِينَ ﴿١٠٥﴾

105. Kaumu ya Nuh waliwakadhibisha mitume.

قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ نُوحٌ أَلَا تَتَّقُونَ ﴿١٠٦﴾

106. Alipowaambia ndugu yao Nuh: Je, hamna takua?

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ ﴿١٠٧﴾

107. Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٠٨﴾

108. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٠٩﴾

109. Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١١٠﴾

110. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

قَالُوا أَنُؤْمِنُ لَكَ وَاتَّبَعَكَ الْأَرْذَلُونَ ﴿١١١﴾

111. Wakasema: Je, tukuamini na hali wanaokufuata ni walio duni?

قَالَ وَمَا عِلْمِي بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١١٢﴾

112. Akasema: Nayajuaje waliyokuwa wakiyafanya?

إِنْ حِسَابُهُمْ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّي لَوْ تَشْعُرُونَ ﴿١١٣﴾

113. Hisabu yao haiko ila kwa Mola wangu. Lau mngelitambua.

وَمَا أَنَا بِطَارِدِ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١١٤﴾

114. Wala mimi si mwenye kuwafukuza waumini.

إِنْ أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿١١٥﴾

115. Sikuwa mimi ila ni muonyaji aliye dhahiri.

قَالُوا لَئِن لَّمْ تَنتَهِ يَا نُوحُ لَتَكُونَنَّ مِنَ الْمَرْجُومِينَ ﴿١١٦﴾

116. Wakasema: Kama hutakoma ewe Nuh bila shaka utapigwa mawe.

قَالَ رَبِّ إِنَّ قَوْمِي كَذَّبُونِ ﴿١١٧﴾

117. Akasema: Mola wangu! Hakika kaumu yangu wamenikadhibisha.

فَافْتَحْ بَيْنِي وَبَيْنَهُمْ فَتْحًا وَنَجِّنِي وَمَن مَّعِيَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١١٨﴾

118. Basi amua baina yagu mimi na wao uamuzi. Na uniokoe na walio pamoja nami katika waumini.

فَأَنجَيْنَاهُ وَمَن مَّعَهُ فِي الْفُلْكِ الْمَشْحُونِ ﴿١١٩﴾

119. Basi tukamuokoa na walio pamoja naye katika jahazi iliyosheheni.

ثُمَّ أَغْرَقْنَا بَعْدُ الْبَاقِينَ ﴿١٢٠﴾

120. Kisha tukawagharikisha baadaye waliobaki.

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٢١﴾

121. Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini.

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿١٢٢﴾

122. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

NUH

Aya 105 – 122

MAANA

Kaumu ya Nuh waliwakadhibisha mitume.

Mtume aliyetumwa kwao ni mmoja ambaye ni Nuh, lakini mwenye kumkadhibisha Mtume mmoja ni kama amewakadhibisha mitume wote, kwa vile aliyewatuma ni mmoja na ujumbe ni mmoja.

Alipowaambia ndugu yao Nuh: Je, hamna takua?

Mwenye kuishika takua atakuwa katika amani na atasalimika na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.

Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.

Alijisifu kwa uaminifu ambao waliujua kwake akiwa mdogo na mtu mzima; sawa na makuraishi walivyomjua Muhammad(s.a.w.w) kwa ukweli na uaminifu katika hali zake zote.

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii. Kwa sababu ninawaita kwenye lile ambalo lina kheri yenu ya dunia na akhera.

Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:90) na Juz. 12 (11:29).

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

Hakuna sababu ya kukaririka jambo la takua (kumcha Mungu) isipokuwa ni jambo muhimu na la msingi.

Wakasema: Je, tukuamini na hali wanaokufuata ni walio duni.

Walimtia ila Nuh, si kwa lolote ila ni kwa kuwa mafukara walimwamini na kwao, hawana thamani. Kwa hiyo utume wa Nuh hauna thamani. Kwa maneno mengine ni kuwa wapenda anasa hawaoni kuwa ufukara ni maisha. Vipi wataamini waliloliamini mafukara? Hivi ndivyo wafanyavyo wapenda anasa; wanakuwa vipofu wa haki na wanakuwa na kiburi.

Akasema: Nayajuaje waliyokuwa wakiyafanya? Hisabu yao haiko ila kwa Mola wangu.

Nuh aliwaambia wale waliomjadili kuhusu ufukara, kuwa thamani ya mtu ni matendo yake na malengo yake, sio kwa cheo na mali. Na mimi sijui kuwa wao walimfanyia ubaya mtu yoyote kwa kauli au vitendo. Siri iko kwa Mwenyezi Mungu. Yeye peke yake ndiye anayejua na kuhisabu.

Lau mngelitambua kwamba thamani ya mtu ni kwa matendo sio kwa mali na dhahiri ni ya watu na batini ni ya Mwenyezi Mungu.

Wala mimi si mwenye kuwafukuza waumini. Sikuwa mimi ila ni muonyaji aliye dhahiri.

Umetangulia mfano wake katika Juz. Juz. 12 (11: 29).

Wakasema: Kama hutakoma ewe Nuh bila shaka utapigwa mawe.

Wameshindwa kuijadili haki wakakimbilia vitisho na mabavu. Hii ndio tabia ya wasiofuta haki, kila mahali na kila wakati.

Akasema: Mola wangu! Hakika kaumu yangu wamenikadhibisha. Basi amua baina yagu mimi na wao uamuzi.

Walipompa vitisho vya kutumia nguvu, alimuomba msaada Mwenyezi Mungu na nguvu zake. Na kwa unyenyekevu akamuomba Mwenyezi Mungu ahukumu, baina yake na yao, hukumu itakayomnusuru mwenye haki na kumwadhibu mwenye batili.

Na uniokoe na walio pamoja nami katika waumini pale itakapowashukia adhabu makafiri.

Basi tukamuokoa na walio pamoja naye katika jahazi iliyosheheni walioamini katika watu wake na wengineo na viumbe wengine wa kiume na wa kike. Kisha tukawagharikisha baadaye waliobaki.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:64) na Juz. 12 (11:40).

Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini . Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu. Imetangulia kwa herufi zake, katika Aya 67 na 68 ya Sura hii.

كَذَّبَتْ عَادٌ الْمُرْسَلِينَ ﴿١٢٣﴾

123. A’d waliwakadhibisha mitume.

إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ هُودٌ أَلَا تَتَّقُونَ ﴿١٢٤﴾

124. Alipowaambia ndugu yao Hud: Je, hamna takua?

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ ﴿١٢٥﴾

125. Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٢٦﴾

126. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٢٧﴾

127. Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

أَتَبْنُونَ بِكُلِّ رِيعٍ آيَةً تَعْبَثُونَ ﴿١٢٨﴾

128. Je, mnajenga juu ya kila muinuko ishara ya kufanyia upuuzi?

وَتَتَّخِذُونَ مَصَانِعَ لَعَلَّكُمْ تَخْلُدُونَ ﴿١٢٩﴾

129. Na mnajenga ngome ili mkae milele.

وَإِذَا بَطَشْتُم بَطَشْتُمْ جَبَّارِينَ ﴿١٣٠﴾

130. Na mnaposhika kwa nguvu mnashika kwa nguvu kwa ujabari.

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٣١﴾

131. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

وَاتَّقُوا الَّذِي أَمَدَّكُم بِمَا تَعْلَمُونَ ﴿١٣٢﴾

132. Na mcheni ambaye amewapa mnayoyajua.

أَمَدَّكُم بِأَنْعَامٍ وَبَنِينَ ﴿١٣٣﴾

133. Amewapa wanyama na watoto wa kiume.

وَجَنَّاتٍ وَعُيُونٍ ﴿١٣٤﴾

134. Na mabustani na chemchemi.

إِنِّي أَخَافُ عَلَيْكُمْ عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿١٣٥﴾

135. Hakika ninawahofia adhabu ya siku kubwa.

قَالُوا سَوَاءٌ عَلَيْنَا أَوَعَظْتَ أَمْ لَمْ تَكُن مِّنَ الْوَاعِظِينَ ﴿١٣٦﴾

136. Wakasema: Ni mamoja kwetu ukitupa mawaidha au kutokuwa miongoni mwa watoao mawaidha.

إِنْ هَـٰذَا إِلَّا خُلُقُ الْأَوَّلِينَ ﴿١٣٧﴾

137. Haya si chochote ila ni hulka ya wa kale.

وَمَا نَحْنُ بِمُعَذَّبِينَ ﴿١٣٨﴾

138. Wala sisi hatutaadhibiwa.

فَكَذَّبُوهُ فَأَهْلَكْنَاهُمْ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٣٩﴾

139. Basi wakamkadhibisha na tukawahilikisha. Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini.

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿١٤٠﴾

140. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

Hud

Aya 123 – 140

MAANA

Kisa cha Hud kimetangulia katika Juz. 8 (7:65 – 72) na Juz. 12 (11:50 – 60).

A’d waliwakadhibisha mitume. Alipowaambia ndugu yao Hud: Je, hamna takua? Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii. Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

Zimetangulia Aya kwa herufi zake katika sehemu iliyopita ya Sura hii Aya 105 – 110, bila ya mabadiliko yoyote isipokuwa jina tu. Kule imesemwa kaumu ya Nuh na hapa ni Hud na A’d.

Siri ya hilo ni kuwa risala ya mitume wote ni moja, ikilingania kwenye umoja wa Mwenyezi Mungu na kutii amri yake na makatazo yake.

Je, mnajenga juu ya kila muinuko ishara ya kufanyia upuuzi?

Makusudio ya ishara hapa ni jengo. Kila jengo linalotekeleza haja ya maisha hilo ni la kheri na ni katika dini. Kwa sababu dini ya Mwenyezi Mungu ni dini ya maisha. Ama jengo lisilokuwa na faida zaidi ya kujionyesha na kujifaharisha, hilo ni shari kidini na kiakili. Aina hii ndio inayokusudiwa hapa kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu ‘ya kufanyia upuuzi’ kwa sababu upuuzi ni ule usiohitajika.

Na mnajenga ngome ili mkae milele.

Makusudio ya ngome hapa ni jengo lisilokuwa na manufaaa yoyote.

Na mnaposhika kwa nguvu mnashika kwa nguvu kwa ujabari. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

Kutumia nguvu kwa ujabari ni kudhulumu kwa hali ya juu, na inakuwa kubwa dhulma kwa kumdhulumu mnyonge. Lililothibiti katika dini ya Mwenyezi Mungu ni kuwa dhulma ni miogoni mwa madhambi makubwa; bali ni sawa na kumkufuru Mungu.

Tumelithibitisha hilo huko nyuma kwa nukuu ya Qur’an.

Aya hii ilishuka wakati ambao hakukuwa na silaha za maangamizi wala hakukuwa na matajiri wanaotoa mamilioni ya pesa ili waangamizwe wanawake kwa ujumla. Ilishuka wakati ambao kutumia nguvu kulikuwa ni kwa kutumia mkono zaidi - upanga mshale na mkuki.

Ikiwa Mwenyezi Mungu amesifu kuwa ni ubaya na uovu mkubwa kutumia nguvu kwa kiganja cha mkono, basi atawalipa nini wale wanaowanyeshea wanyonge mvua ya makombora, mabomu ya sumu na silaha za nuklia? Au wale ambao wameijaza ardhi na anga kwa vikosi vya majeshi. Wameijaza maroketi ya kijeshi; si kwa lolote ila wanataka kuhukumu roho za waja na nyenzo za nchi kulingana na hawa zao na masilahi yao tu.

Na mcheni ambaye amewapa mnayoyajua. Amewapa wanyama na watoto wa kiume na mabustani na chemchemi. Hakika ninawahofia adhabu ya siku kubwa.

Hud aliwalingania kwenye twaa ya Mwenyezi Mungu na akawakumbusha neema yake juu yao na anavyowapa muda na pia akawahadharisha na mwisho mbaya wa dhulma. Lakini hilo halikuwazidisha kitu isipokuwa kiburi nawakasema: Ni mamoja kwetu ukitupa mawaidha au kutokuwa miongoni mwa watoao mawaidha sisi hatutakuamini. Mawaidha yako hayatatuzidishia isipokuwa kuachana nawe.

Haya si chochote ila ni hulka ya wa kale wala sisi hatutaadhibiwa.

Haya ni ishara ya dini yao na masanamu yao wanayoyaabudu; na kwamba wao hawatayaacha kwa sababu wameyarithi kutoka jadi na jadi. Hiyo ndiyo hoja yao; hawana zaidi ya ‘tumewakuta nayo baba zetu na sisi tunafuata nyayo zao.’

Basi wakamkadhibisha na tukawahilikisha.

Hud aliwaonya watu wake kwa dalili na hoja, lakini hawakujali, wakawa miongoni mwa walioangamia.

Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

Imetangulia kwa herufi zake, katika Aya 67 na 68 ya Sura hii na pia sehemu iliyopita.


7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA

كَذَّبَتْ ثَمُودُ الْمُرْسَلِينَ ﴿١٤١﴾

141. Thamud waliwakadhibisha mitume.

إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ صَالِحٌ أَلَا تَتَّقُونَ ﴿١٤٢﴾

142. Alipowaambia ndugu yao Swaleh: Je, hamna takua?

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ ﴿١٤٣﴾

143. Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٤٤﴾

144. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٤٥﴾

145. Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

أَتُتْرَكُونَ فِي مَا هَاهُنَا آمِنِينَ ﴿١٤٦﴾

146. Je, mtaachwa salama katika haya yaliyopo hapa?

فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ ﴿١٤٧﴾

147. Katika mabustani na chem- chem?

وَزُرُوعٍ وَنَخْلٍ طَلْعُهَا هَضِيمٌ ﴿١٤٨﴾

148. Na mimea na mitende yenye makole yalioiva?

وَتَنْحِتُونَ مِنَ الْجِبَالِ بُيُوتًا فَارِهِينَ ﴿١٤٩﴾

149. Na mnachonga majumba mlimani kwa ustadi

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٥٠﴾

150. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

وَلَا تُطِيعُوا أَمْرَ الْمُسْرِفِينَ ﴿١٥١﴾

151. Wala msitii amri za waliopituka mipaka.

الَّذِينَ يُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ وَلَا يُصْلِحُونَ ﴿١٥٢﴾

152. Ambao wanafanya ufisadi katika ardhi wala hawaiten- genezi.

قَالُوا إِنَّمَا أَنتَ مِنَ الْمُسَحَّرِينَ ﴿١٥٣﴾

153. Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa tu.

مَا أَنتَ إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُنَا فَأْتِ بِآيَةٍ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿١٥٤﴾

154. Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi. Basi lete ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.

قَالَ هَـٰذِهِ نَاقَةٌ لَّهَا شِرْبٌ وَلَكُمْ شِرْبُ يَوْمٍ مَّعْلُومٍ ﴿١٥٥﴾

155. Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalum.

وَلَا تَمَسُّوهَا بِسُوءٍ فَيَأْخُذَكُمْ عَذَابُ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿١٥٦﴾

156. Wala msimguse kwa ubaya isije ikawashika adhabu ya siku kubwa.

فَعَقَرُوهَا فَأَصْبَحُوا نَادِمِينَ ﴿١٥٧﴾

157. Lakini wakamuua wakawa wenye kujuta.

فَأَخَذَهُمُ الْعَذَابُ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٥٨﴾

158. Basi ikawashika adhabu. Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini.

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿١٥٩﴾

159. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

SWALEH

Aya 141 – 159

MAANA

Kisa cha Swaleh kimetangulia katika Juz. 8 (7: 73 – 79) na Juz. 12 (11: 61 -68).

Thamud waliwakadhibisha mitume. Alipowaambia ndugu yao Swaleh: Je, hamna takua? Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii. Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

Zimetangulia Aya hizi kwa herufi zake katika sura hii Aya 105 – 110, na pia katika sehemu iliyopita bila ya mabadiliko yoyote isipokuwa jina tu la Thamud na Swaleh. Tumesema huko kuwa siri ya hilo ni kuwa risala ya mitume wote ni moja.

Je, mtaacha salama katika haya yaliyopo hapa katika mabustani na chemchem na mimea na mitende yenye makole yalioiva? Na mna chonga majumba mlimani kwa ustadi

Kabila la Thamud lilizama katika anasa na strehe – matunda, mito, makasri, wanyama n.k. Wakiwa wameghafilika na kila kitu isipokuwa matamanio yao na ladha zao. Ndipo ndugu yao Swaleh akawaonya na mwisho mbaya na akawaambia, Je, mmemsahau Mwenyezi Mungu na yeye hajawasahau? Je, mmejiaminisha na matukio ya ghafla?

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na nitiini wala msitii amri za waliopituka mipaka ambao wanafanya ufisadi katika ardhi wala hawaitengenezi.

Makusudio ya waliopituka mipaka, walio wafisadi, ni viongozi ambao ndio chimbuko la balaa zote; isipokuwa wachache sana. Hakuna dini wala misimamo, katika ufahamu wao, isipokuwa masilahi yao na masilahi ya jamaa zao.

Wafisadi hawa, katika kaumu ya Swaleh, walikuwa tisa; kama ilivyoelezwa katika Aya nyingine: kwenye juzuu hii. “Na walikuwako mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika ardhi wala hawafanyi la masilahi” (25:48).

Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa tu.

Umerogwa na mchawi mpaka umekuwa hujui unalolisema. Hivi ndivyo wasemavyo vijana wengi wa kileo wanapoambiwa swalini na fungeni.

Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi, unakula chakula na kutembea sokoni, sasa vipi unateremshiwa wahyi zaidi yetu sisi?

Basi lete ishara ukiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.

Walisema haya wakiwa wameazimia kuendelea na ukafiri wao na inadi yao, hata kama wataletewa dalili elfu na moja; vinginevyo maombi yao yangelikuwa ya haki na ya sawa.

Akasema: Huyu ngamia jike; awe na zamu yake ya kunywa na nyinyi muwe na zamu yenu ya kunywa katika siku maalum. Wala msimguse kwa ubaya isije ikawashika adhabu ya siku kubwa.

Walimuomba awaletee muujiza unaofahamisha utume wake, akawaletea ngamia kwa njia isiyo ya kawaida na akawawekea sharti la maji kwa zamu; siku moja yao na siku moja ya ngamia na kwamba wasimdhuru isije ikawafikia adhabu,

lakini wakamuua wakawa wenye kujuta, Basi ikawashika adhabu.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7: 77 – 78).

Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

كَذَّبَتْ قَوْمُ لُوطٍ الْمُرْسَلِينَ ﴿١٦٠﴾

160. Kaumu ya Lut waliwakadhibisha mitume.

إِذْ قَالَ لَهُمْ أَخُوهُمْ لُوطٌ أَلَا تَتَّقُونَ ﴿١٦١﴾

161. Alipowaambia ndugu yao Lut: Je, hamna takua?

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ ﴿١٦٢﴾

162. Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٦٣﴾

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٤﴾

164. Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

أَتَأْتُونَ الذُّكْرَانَ مِنَ الْعَالَمِينَ ﴿١٦٥﴾

165. Je, katika viumbe wote mnawaendea wanaume?

وَتَذَرُونَ مَا خَلَقَ لَكُمْ رَبُّكُم مِّنْ أَزْوَاجِكُم بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ عَادُونَ ﴿١٦٦﴾

166. Na mnaacha alichowaumbia Mwenyezi Mungu katika wake zenu? Bali nyinyi ni watu mnaoruka mipaka.

قَالُوا لَئِن لَّمْ تَنتَهِ يَا لُوطُ لَتَكُونَنَّ مِنَ الْمُخْرَجِينَ ﴿١٦٧﴾

167. Wakasema: Kama hutakoma ewe Lut bila shaka utakuwa miongoni mwa wanaotolewa.

قَالَ إِنِّي لِعَمَلِكُم مِّنَ الْقَالِينَ ﴿١٦٨﴾

168. Akasema: Hakika mimi ni katika wanaokichukia hiki kitendo chenu.

رَبِّ نَجِّنِي وَأَهْلِي مِمَّا يَعْمَلُونَ ﴿١٦٩﴾

Mola wangu! Niokoe na ahli zangu kwa wayatendao.

فَنَجَّيْنَاهُ وَأَهْلَهُ أَجْمَعِينَ ﴿١٧٠﴾

Basi tukamuokoa na ahli zake wote.

إِلَّا عَجُوزًا فِي الْغَابِرِينَ ﴿١٧١﴾

171. Isipokuwa kikongwe katika waliokaa nyuma.

ثُمَّ دَمَّرْنَا الْآخَرِينَ ﴿١٧٢﴾

Kisha tukwaangamiza wale wengine.

وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِم مَّطَرًا فَسَاءَ مَطَرُ الْمُنذَرِينَ ﴿١٧٣﴾

173. Na tukawanyesheza mvua, basi ni uovu mno wa mvua ya waliyoonywa.

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٧٤﴾

174. Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini.

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿١٧٥﴾

175. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

LUT

Aya 160-175

MAANA

Kisa cha Lut kimetangulia katika Juz. 8 (7:80 –84) na Juz. 12 (11:82– 87).

Kaumu ya Lut waliwakadhibisha mitume. Alipowaambia ndugu yao Lut: Je, hamna takua?

Ni ndugu yao katika kuwa pamoja na makazi; si katika dini wala nasabu. Kwa kuwa yeye alikuja hapo na ami yake, Ibrahim(a.s) kutoka Babel (Babylon) kupitia Misr hadi Palestina. Lut alikaa katika bonde la Jordan na Ibrahim akakaa katika nyanda za juu kaskazini. Hapo ilikuwa ni karne kumi na tisa kabla ya kuzaliwa Nabii Isa (19 B.C.)

Imetangulia kwa herufi zake, katika Aya 67 na 68 ya sura hii na pia sehemu iliyopita.

“Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii. Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

Lut alianza kama alivyoanza Nuh, Hud na Swaleh(a.s ) . Kwa sababu risala ya wote ni moja. Soma katika sura hii Aya zinazomzungumzia kila mmoja katika wao.

Je, katika viumbe wote mnawaendea wanaume?

Mnafanya kitendo hiki cha fedheha kwa wanaume katika wanadamu?

Na mnaacha alichowaumbia Mwenyezi Mungu katika wake zenu?

Kwa hiyo mnahalifu hukumu ya maumbile na kanuni, tabia na lengo la kumbwa mume na mke.

Tendo lenu halikubaliwi hata na wanyama na wadudu. Lakini bunge la Uingereza limeruhusu ulawiti. Hiyo ni dalili kuwa Uingereza ni duni zaidi kuliko wanyama katika hulka yake na thamani yake. Sio mbali kuwa hii ni natija ya historia yake ndefu ya ukoloni unaochukiwa. Kwa sababu utaghuti na uadui una mwisho mbaya.

Bali nyinyi ni watu mnaoruka mipaka.

Mmepituka mipaka yote kwa hawa, usafihi, uasi na ujeuri wenu.

Wakasema: Kama hutakoma ewe Lut bila shaka utakuwa miongoni mwa wanaotolewa.

Umetangulia mfano wake katika Aya 116 ya Sura hii.

Akasema: Hakika mimi ni katika wanaokichukia hiki kitendo chenu.

Katika maana yake ni; Aya 216 ya sura hii! “Na ikiwa watakuasi basi sema mimi ninajitenga mbali na hayo mnayo yatenda.”

Mola wangu! Niokoe na ahli zangu kwa wayatendao. Basi tukamuokoa na ahli zake wote. Isipokuwa kikongwe katika waliokaa nyuma. Kisha tukwaangamiza wale wengine. Na tukawanyesheza mvua, basi ni uovu mno wa mvua ya waliyoonywa.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:83 – 84) na Juz. 14 (15:59 – 60).

Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

Imetangulia kwa herufi zake, katika Aya 67 na 68 ya Sura hii na pia sehemu iliyopita.

كَذَّبَ أَصْحَابُ الْأَيْكَةِ الْمُرْسَلِينَ ﴿١٧٦﴾

176. Watu wa mwituni waliwakadhibisha mitume.

إِذْ قَالَ لَهُمْ شُعَيْبٌ أَلَا تَتَّقُونَ ﴿١٧٧﴾

177. Alipowaambia Shua’yb: Je, hamna takua?

إِنِّي لَكُمْ رَسُولٌ أَمِينٌ ﴿١٧٨﴾

178. Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu.

فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُونِ ﴿١٧٩﴾

179. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii.

وَمَا أَسْأَلُكُمْ عَلَيْهِ مِنْ أَجْرٍ إِنْ أَجْرِيَ إِلَّا عَلَىٰ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٨٠﴾

180. Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

أَوْفُوا الْكَيْلَ وَلَا تَكُونُوا مِنَ الْمُخْسِرِينَ ﴿١٨١﴾

181. Timizeni kipimo sawasawa wala msiwe miongoni mwa wanaopunja.

وَزِنُوا بِالْقِسْطَاسِ الْمُسْتَقِيمِ ﴿١٨٢﴾

182. Na pimeni kwa mizani iliyo sawa.

وَلَا تَبْخَسُوا النَّاسَ أَشْيَاءَهُمْ وَلَا تَعْثَوْا فِي الْأَرْضِ مُفْسِدِينَ ﴿١٨٣﴾

183. Wala msiwapunguzie watu vitu vyao, Wala msifanye ufisadi katika nchi mkafanya vurugu.

وَاتَّقُوا الَّذِي خَلَقَكُمْ وَالْجِبِلَّةَ الْأَوَّلِينَ ﴿١٨٤﴾

184. Na mcheni aliyewaumba nyinyi na vizazi vilivyotangulia.

قَالُوا إِنَّمَا أَنتَ مِنَ الْمُسَحَّرِينَ ﴿١٨٥﴾

185. Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa tu.

وَمَا أَنتَ إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُنَا وَإِن نَّظُنُّكَ لَمِنَ الْكَاذِبِينَ ﴿١٨٦﴾

186. Na wewe si chochote ila ni mtu kama sisi, na kwa hakika tunakuona ni katika waongo.

فَأَسْقِطْ عَلَيْنَا كِسَفًا مِّنَ السَّمَاءِ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿١٨٧﴾

187. Basi tuangushie kipande cha mbingu, ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.

قَالَ رَبِّي أَعْلَمُ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿١٨٨﴾

188. Akasema: Mola wangu anajua zaidi mnayoyatenda.

فَكَذَّبُوهُ فَأَخَذَهُمْ عَذَابُ يَوْمِ الظُّلَّةِ إِنَّهُ كَانَ عَذَابَ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿١٨٩﴾

189. Basi wakamkadhibisha, ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa.

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً وَمَا كَانَ أَكْثَرُهُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٩٠﴾

190. Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini.

وَإِنَّ رَبَّكَ لَهُوَ الْعَزِيزُ الرَّحِيمُ ﴿١٩١﴾

191. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

SHUA’YB

Aya 176 – 191

MAANA

Kisa cha Shua’yb kimetangulia katika Juz. 8 (7: 85) na Juz. 12 (11:84 – 95).

Watu wa mwituni waliwakadhibisha mitume. Alipowaambia Shua’yb: Je, hamna takua?

Wafasiri wamesema kuwa watu wa mwituni ni watu waliokuwa karibu na Madyan kwenye miti mingi.

Alipowaambia Shua’yb: Je, hamna takua?

Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakusema ndugu yao Shua’yb, kama alivyosema ndugu yao Hud, Swaleh na Lut, kwa sababu Shua’yb si mtu wa hapo kinasabu wala hana uhusiano wowote na watu wa mwituni, isipokuwa ujirani. Mwenyezi Mungu alimtuma kwao; kama alivyomtuma kwa watu wake wa Madyan.

Hakika mimi kwenu ni Mtume mwaminifu. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na mnitii. Na siwataki ujira juu yake, kwani ujira wangu hauko ila kwa Mola wa walimwengu wote.

Aya hizi zimetanguliwa kwa herufi zake kupitia mdomoni mwa Nuh, Hud, Swaleh na Lut. Hayo ni maneno ya kila Nabii.

Timizeni kipimo sawasawa wala msiwe miongoni mwa wanaopunja. Na pimeni kwa mizani iliyo sawa. Wala msiwapunguzie watu vitu vyao, Wala msifanye ufisadi katika nchi mkafanya vurugu.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7: 85) na Juz. 12 (11:84)

Na mcheni aliyewaumba nyinyi na vizazi vilivyotangulia.

Yaani mhofie adhabu ya Mwenyezi Mungu aliyewaumba nyinyi na wale waliotangulia.

Wakasema: Hakika wewe ni miongoni mwa waliorogwa tu.

Imetangulia kwa herufi zake katika Aya 153 ya sura hii.

Wewe si chochote ila ni mtu kama sisi, na kwa hakika tunakuona ni katika waongo.

Yaani wewe unakusudia uwongo katika madai yako ya utume, kwa dalili ya kuwa wewe ni mtu unayekula chakula na kutembea sokoni. Lau wahyi ungeliwashukia watu basi watu wote wangelikuwa Mitume.

Ibn Hisham katika kitabu Al-Mughni, katika kuelezea watu wasiofaliwa na maneno yoyote, anasema: “Mtu mmoja alimwambia mwengine: ‘Baba yako amemfanyaje punda wako?’ Akasema: ‘Amemuuzo’ akiwa na maana amemuuza. Yule muulizaji akasema kwa mshangao: kwa nini umeweka o kwenye herufi ya mwisho? yule akajibu: si wewe umeweka o kwenye herufi ya mwisho!” Mtu wa namna hii utamwambiaje?

Basi tuangushie kipande cha mbingu, ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli.

Aliwahadharisha na adhabu wakamdharau na wakasema iko wapi hiyo adhabu unayotutisha nayo, basi teremsha kipande cha mbingu kiwe ni adhabu, ukiwa ni mkweli wa madai yako.

Akasema: Mola wangu anajua zaidi mnayoyatenda na amri ni yake peke yake, akitaka ataileta haraka au ataicheleweshwa. Basi wakamkadhibisha, ikawashika adhabu ya siku ya kivuli. Hakika hiyo ilikuwa adhabu ya siku kubwa.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakubainisha kivuli hicho. Wafasiri wanasema ni mawingu waliyoyafanya kivuli kutokana na joto lililowapata, kisha yakawanyeshea mvua ya moto iliyowaunguza wote.

Hakika bila shaka katika hayo ipo ishara, lakini wengi wao si wenye kuamini. Na hakika Mola wako ndiye Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

Imetangulia kwa herufi zake, katika Aya 67 na 68 ya Sura hii na pia sehemu iliyopita.


8

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA

وَإِنَّهُ لَتَنزِيلُ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٩٢﴾

192. Na hakika hiyo ni uteremsho wa Mola wa walimwengu wote.

نَزَلَ بِهِ الرُّوحُ الْأَمِينُ ﴿١٩٣﴾

193. Ameiteremsha Roho mwaminifu.

عَلَىٰ قَلْبِكَ لِتَكُونَ مِنَ الْمُنذِرِينَ ﴿١٩٤﴾

194. Juu ya moyo wako, ili uwe katika waonyaji.

بِلِسَانٍ عَرَبِيٍّ مُّبِينٍ ﴿١٩٥﴾

195. Kwa ulimi wa kiarabu ulio wazi.

وَإِنَّهُ لَفِي زُبُرِ الْأَوَّلِينَ ﴿١٩٦﴾

197. Na hakika hiyo iko katika vitabu vya kale.

أَوَلَمْ يَكُن لَّهُمْ آيَةً أَن يَعْلَمَهُ عُلَمَاءُ بَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿١٩٧﴾

198. Je haikuwa kwao ni ishara kwamba wanayajua haya maulama wa wana wa Israil?

وَلَوْ نَزَّلْنَاهُ عَلَىٰ بَعْضِ الْأَعْجَمِينَ ﴿١٩٨﴾

198. Lau tungeliitermsha juu ya mmoja wa wasiokuwa waarabu.

فَقَرَأَهُ عَلَيْهِم مَّا كَانُوا بِهِ مُؤْمِنِينَ ﴿١٩٩﴾

199. Na akawasomea wasingelikuwa wenye kuiamini.

كَذَٰلِكَ سَلَكْنَاهُ فِي قُلُوبِ الْمُجْرِمِينَ ﴿٢٠٠﴾

200. Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wakosefu.

لَا يُؤْمِنُونَ بِهِ حَتَّىٰ يَرَوُا الْعَذَابَ الْأَلِيمَ ﴿٢٠١﴾

201. Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu.

فَيَأْتِيَهُم بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٢٠٢﴾

202. Basi itawafikia ghafla na hali hawaitambui.

فَيَقُولُوا هَلْ نَحْنُ مُنظَرُونَ ﴿٢٠٣﴾

203. Na watasema: Je sisi tutapewa muda?

أَفَبِعَذَابِنَا يَسْتَعْجِلُونَ ﴿٢٠٤﴾

204. Basi je wanahimiza adhabu yetu?

أَفَرَأَيْتَ إِن مَّتَّعْنَاهُمْ سِنِينَ ﴿٢٠٥﴾

205. Unaonaje, kama tukiwastarehesha kwa miaka.

ثُمَّ جَاءَهُم مَّا كَانُوا يُوعَدُونَ ﴿٢٠٦﴾

206. Kisha yawafikie waliyokuwa wakiahidiwa.

مَا أَغْنَىٰ عَنْهُم مَّا كَانُوا يُمَتَّعُونَ ﴿٢٠٧﴾

207. Hayatawafaa yale waliyostareheshewa.

وَمَا أَهْلَكْنَا مِن قَرْيَةٍ إِلَّا لَهَا مُنذِرُونَ ﴿٢٠٨﴾

208. Wala hatukuuangamiza mji wowote ila ulikuwa na waonyaji.

ذِكْرَىٰ وَمَا كُنَّا ظَالِمِينَ ﴿٢٠٩﴾

209. Kuwa ni ukumbusho wala hatukuwa sisi ni wenye kudhulumu.

وَمَا تَنَزَّلَتْ بِهِ الشَّيَاطِينُ ﴿٢١٠﴾

210. Wala mashetani hawakuteremka nayo.

وَمَا يَنبَغِي لَهُمْ وَمَا يَسْتَطِيعُونَ ﴿٢١١﴾

211. Wala haiwapasi wala hawaiwezi.

إِنَّهُمْ عَنِ السَّمْعِ لَمَعْزُولُونَ ﴿٢١٢﴾

121. Hakika wao wametengwa na kusikia.

AMEITERMSHA ROHO MWAMINIFU

Aya 192 – 212

MAANA

Na hakika hiyo ni uteremsho wa Mola wa walimwengu wote. Ameiteremsha Roho mwaminifu juu ya moyo wako, ili uwe katika waonyaji.

Hiyo ni Qur’an. Roho mwaminifu ni Jibril(a.s) na maneno yanelekezwa kwa Muhammad(s.a.w.w) .

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja visa vya mitume katika Aya zilizotangulia, sasa anamtaja Muhammad na Qur’an na kwamba Jibril ameitermsha kwa Mtume mtukufu ili apambane na makafiri na wapinzani kwa Aya zake na ubainifu wake. Jibril ameitwa roho kwa sababu ameiteremsha Qur’an ambayo ni uongofu na ponyo kwa roho:

هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ ﴿٤٤﴾

“Hiyo ni uwongofu na ponyo kwa wenye kuamini.” (41:44).

Na ameitwa mwaminifu kwa sababu ni mtiifu kwa Mwenyezi Mungu, akiwa na biidii ya kuufikisha ujumbe wake kwa mitume, kama ulivyo. Yeye vile vile anaujua huo ujumbe na malengo yake.

Kwa ulimi wa kiarabu ulio wazi.

Katika Juz. 12 (12:2) tumebainisha sababu za kushuka Qur’an kwa lugha ya kiarabu, tazama huko.

Na hakika hiyo iko katika vitabu vya kale.

Yaani vitabu vya Mwenyezi Mungu vilivyotangulia, vilimbashiria Muhammad(s.a.w.w) na Qur’an. Huko nyuma tulithibitisha dalili za kiakili na kinakili kwamba Qur’an ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Katika dalili za kiakili ni kwamba Qur’an iliwashinda wapinzani hata kuleta mfano mmoja tu wa Sura zake. Walijaribu wakashindwa. Na kwamba inatolea habari mambo ya ghaibu na yakatokea. Pia hiyo Qur’an inachukua njia nyingi za tafsiri. Wala hakuna siri ya hili ila ni kwa kuwa inatoka kwa ambaye amekizunguka kila kitu kwa ujuzi. Tazama Juz. 1 (2: 23) Juz. 5 (4:53 na 82) na Juz. 18 (24:55).

Ama dalili za kinukuu, miongoni mwazo ni Tawrat na Injili za asili, zilizoleta bishara ya Muhammad. Tazama Juz. 9 (7: 157). Vile vile vitabu vingine vya mbinguni vilitoa habari ya kuja Muhammad. Tazama Juz. 1 (2:46).

Je, Haikuwa kwao ni ishara kwamba wanayajua haya maulama wa wana wa Israil?

Maulama wa kiyahudi, kabla ya kutumwa Mtume(s.a.w.w) , walikuwa wakimbashiria Muhammad; wakiwazungumzia waarabu kuhusiana naye na kutaja sifa zake kwa makuraishi na wengineo. Alipokuja wakasilimu baadhi ya Mayahudi waliokuwa wakimzungumzia; kama vile Abdallah bin Salaam na wenzake. Vile vile wakasilimu jamaa katika waarabu na wakampinga mayahudi wengine na vigogo katika makuraishi.

Aya hii inawaambia wale waliomkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) baada ya kusikia hadith ya mayahudi kumhusu. Inawaambia, vipi mnamkadhibisha na hali mmewasikia maulama wa kiyahudi kabla, wakimtolea habari, wakikiri kuwa ametajwa katika Tawrat? Ushahidi wao huo hauwatoshi kuwa ni dalili ya ukweli wa Muhammad(s.a.w.w) ?

Hakuna mwenye shaka kwamba dalili hii ni tosha kwa mwenye kuitafuta haki kwa njia ya haki, lakini vigogo ambao walipinga utume wa Muhammad(s.a.w.w) walifanya hivyo kwa sababu ya masilahi yao; sio kwa sababu ya udhaifu wa hoja na dalili:

وَمَا تُغْنِي الْآيَاتُ وَالنُّذُرُ عَن قَوْمٍ لَّا يُؤْمِنُونَ ﴿١٠١﴾

“Na dalili na maonyo hayawafai watu wasioamini.” Juz. 11 (10:101).

Lau tungeliiteremsha juu ya mmoja wa wasiokuwa waarabu na akawasomea, wasingelikuwa wenye kuiamini.

Wao hawaiamini haki na ubainifu wake, iwe imekuja na mwarabu au asiyekuwa mwarabu. Kwa sababu haki na elimu kwao ni masilahi; vinginevyo si chochote kwao. Tumelikariri hilo mara nyingi pamoja na uwazi wake.

Namna hivi tunaingiza katika nyoyo za wakosefu.

Yaani wakosefu wanapoisikia haki au Qur’an wanaipinga na kuikanusha. Kwa maneno mengine ni kuwa mbengu inaota vizuri kwenye ardhi iliyo na rutuba, lakini ikiwa ardhi si nzuri, basi uotaji wake utakuwa hauna manufaa:

وَالْبَلَدُ الطَّيِّبُ يَخْرُجُ نَبَاتُهُ بِإِذْنِ رَبِّهِ وَالَّذِي خَبُثَ لَا يَخْرُجُ إِلَّا نَكِدًا ﴿٥٨﴾

“Na mji mzuri hutoa mimea yake kwa idhini ya Mola wake. Na ule ulio mbaya hautoi ila kwa taabu tu.” Juz. 8 (7:58).

Kadhalika haki inaleta matunda na athari ikisadifu kuwa kwenye nafsi safi na haileti chochote ikiwa kwenye nafsi chafu. Maana ni kuwa Qur’an haina athari yoyote katika nafsi zao isipokuwa upinzani na kukadhibisha.

Hawataiamini mpaka waione adhabu chungu. Basi itawafikia ghafla na hali hawaitambui.

Wakosefu hawaiamini Qur’an. Yaani wao hawaiamini haki hata ikiwa na dalili kiasi gani ila ikiwafikia adhabu kwa ghafla. Na wakionywa kabla wanaifanyia masihara. Ilivyo ni kwa kunyenyekea wakati wa kuona adhabu ni unafiki na ni kulazimishwa sio hiyari.

Na watasema: Je sisi tutapewa muda?

Waliiharakia adhabu kabla ya kuiona na wakamwambia Mtume wao ilete ukiwa ni katika wakweli. Walipoiona kwa macho walijuta na wakatamani lau wangelipewa muda ili waamini na watii. Ndivyo alivyo mpotevu; anatamani kurudi au kupewa muda baada ya kupita wakati.

Basi je wanahimiza adhabu yetu?

Haya ni maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwajibu wale waliomwambia Mtume wao. Tuangushie kipande cha mbingu na tuletee yale uliyotuahidi. Maana yake ni kuwa vipi mnaiharakia adhabu na ikiwafikia hamuiwezi wala kuikwepa.

Unaonaje, kama tukiwastarehesha kwa miaka, kisha yawafikie waliyokuwa wakiahidiwa, hayatawafaa yale waliyostareheshewa?

Wakosefu watatamaani kupewa muda watakapoiona adhabu, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawajibu kwamba kupewa muda hakufai kitu hata kama muda utakuwa mrefu kiasi gani. Bali kila muda unavyokuwa mrefu ndio madhambi yanazidi na kuongezeka na kuzidi adhabu yao.

Wala hatukuuangamiza mji wowote ila ulikuwa na waonyaji.

Aya hii iko katika maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَمَا كُنَّا مُعَذِّبِينَ حَتَّىٰ نَبْعَثَ رَسُولًا ﴿١٥﴾

“Wala sisi hatuadhibu mpaka tupeleke Mtume.” Juz. 15 (17:15).

Kuwa ni ukumbusho wala hatukuwa sisi ni wenye kudhulumu katika kuangamiza miji, wakati ambapo tulituma waonyaji wa hiyo adhabu, na wakumbushaji wa twaa ya Mwenyezi Mungu wakiwa na dalili. Wakawakadhibisha ndio ikastahiki adhabu.

Wala mashetani hawakuteremka nayo wala haiwapasi wala hawaiwezi.

Watu wa wakati wa ujahili walikuwa wakiitakidi ukuhani; kwamba kila kuhani ana shetani wake anayemletea habari za ghaibu. Iliposhuka Qur’an wakasema kuwa inatoka kwa shetani kwenda kwa makuhani ambao nao wanampelekea Muhammad(s.a.w.w) ; au yeye mwenyewe ni kuhani anayeteremkiwa na shetani.

Ndipo Mwenyezi Mungu akayajibu madai haya, kuwa Qur’an ni uongofu, mwanga na ni ubainifu ulio wazi. Ni wapi na wapi ukuhani na ushetani kulinganisha na uongofu na ubainifu? Wao ni dhaifu na ni duni zaidi. Zaidi ya hayo ni kuwa hakika wao wametengwa na kusikia.

Wamezuiliwa kusikia Qur’an pale Mwenyezi Mungu anapompa Jibril kuileta kwa Muhammad(s.a.w.w) . Ikiwa mashetani wameshindwa kuleta hata Aya moja mfano wake na pia kusikiliza japo tamko moja, basi watainukuu vipi kwa makuhani na kuitolea habari?

فَلَا تَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَتَكُونَ مِنَ الْمُعَذَّبِينَ ﴿٢١٣﴾

213. Basi usimwombe Mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakaoadhibiwa.

وَأَنذِرْ عَشِيرَتَكَ الْأَقْرَبِينَ ﴿٢١٤﴾

214. Na uwonye jamaa zako walio karibu.

وَاخْفِضْ جَنَاحَكَ لِمَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٢١٥﴾

215. Na inamisha bawa lako kwa wanokufuata katika waumini.

فَإِنْ عَصَوْكَ فَقُلْ إِنِّي بَرِيءٌ مِّمَّا تَعْمَلُونَ ﴿٢١٦﴾

216. Na ikiwa watakuasi basi sema: Mimi ninajitenga mbali na hayo mnayoyafanya.

وَتَوَكَّلْ عَلَى الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ ﴿٢١٧﴾

217. Na mtegemee Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.

الَّذِي يَرَاكَ حِينَ تَقُومُ ﴿٢١٨﴾

218. Ambaye anakuona unaposimama.

وَتَقَلُّبَكَ فِي السَّاجِدِينَ ﴿٢١٩﴾

219. Na mageuko yako katika wale wanaosujudu.

إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ ﴿٢٢٠﴾

220. Hakika yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

WAONYE JAMAA ZAKO WA KARIBU

Aya 213 – 220

MAANA

Basi usimwombe Mungu mwingine pamoja na Mwenyezi Mungu ukawa miongoni mwa watakaoadhibiwa.

Dhahiri ya mfumo wa maneno inaonyesha yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , lakini makusudio ni kutoa habari kuwa kila atakayemuomba Mungu mwingine zaidi ya Mwenyezi Mungu basi atakuwa ni mwenye kuadhibiwa kwa hali yoyote atakayokuwa.

Na uwonye jamaa zako walio karibu.

Mtume(s.a.w.w) ni mwenye kuamrishwa kuwaonya watu wote:

يَا أَيُّهَا الْمُدَّثِّرُ ﴿١﴾ قُمْ فَأَنذِرْ ﴿٢﴾

“Ewe uliyejigubika! Simama uonye.” (74:1 – 2),

عَجَبًا أَنْ أَوْحَيْنَا إِلَىٰ رَجُلٍ مِّنْهُمْ أَنْ أَنذِرِ النَّاسَ وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا ﴿٢﴾

“Kwamba tumempa wahyi mmoja wao, kuwa uwaonye watu na uwape bishara wale walioamini.” Juz. 11 (10:2).

Amehusisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja jamaa wa Mtume(s.a.w.w) , kwa sababu mwenye kutaka kutengeneza kwanza anajianza yeye mwenyewe, kisha jamaa zake, ndio wafuatie wengine. Jamaa zake wakimsadiki na kumwamini watamsaidia kueneza mwito wake.

Maneno ya Waislamu yamekuwa mengi kuhusiana na Aya hii. Jamaa katika Sunni wamesema kuwa iliposhuka Aya hii Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alisema: “Ewe Fatima bint Muhammad! Ewe Swafiya bint Abdul Muttwalib! Enyi wana wa Abdillah! Fanyeni amali, kwani mimi siwatoshelezei chochote kwa Mwenyezi Mungu.

Shia na jamaa wengie wa kisunni; akiwemo: Ahmad bin Hambal, An-Nasai, As-Suyutwi, Abu Na’im Al-Baghwi, Atha’alabi, mwenye kitabu Assiratul-halabiya, mwenye kitabu Kanzul-u’mmal na wengineo, wamesema kuwa, iliposhuka Aya hii, Mtume(s.a.w.w) aliwaita watu wa ukoo wa Abdul-Muttwalib. Wakati huo walikuwa ni watu arobaini, wakiwemo maami zake: Abu Twalib, Hamza, Abbas na Abu Lahab.

Alikuwa amewaandalia karamu. Baada ya kula na kunywa, akasema: “Enyi wana wa Abdul-Muttwalib! Nimewaletea kheri ya duniani na Akhera na Mwenyezi Mungu ameniamrisha nitoe mwito wa hilo. Basi ni nani atakayenisaidia kwenye jambo hili, awe ndugu yangu, wasii wangu na khalifa wangu kwenu?”

Wakanyamaza wote, isipokuwa Ali(a.s) akasema:“Mimi ewe Nabii wa Mwenyezi Mungu.” Basi akamshika shingoni na akasema: “Hakika huyu ni ndugu yangu, wasii wangu na khalifa wangu kwenu. Basi msikilizeni na mumtii [1]

Tukio hili alilitaja Muhammad Haykal katika kitabu chake Hayatu Muhammad, chapa ya kwanza na akaliondoa katika chapa ya pili.

Abu Hayyan Al-Andalusi katika Bahrul-muhit, anasema: “Zimepokewa Hadith kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) kuhusiana na hilo.” Anaashiria Hadith zilizomtaja Imam Ali na zile ambazo hazikumtaja. Wala hakuna kupingana baina ya Hadith hizi.

Kwa sababu kuzichanganya pamoja ni jambo linalowezekana na la karibu sana. Mtume(s.a.w.w) aliwaandalia chakula watu arobaini katika jamaa zake na kuwaambia ni nani atakayenisaidia … kisha pia akawaambia mimi siwatoshelezi lolote kwa Mwenyezi Mungu.

Na inamisha bawa lako kwa wanokufuata katika waumini.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 14 (15:88).

Na ikiwa watakuasi basi sema: Mimi ninajitenga mbali na hayo mnayoyafanya.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , awaambie wale jamaa zake aliowaonya. ‘Aliye karibu na Mwenyezi Mungu na Mtume wake ni yule aliyekurubishwa na takua. Na aliye mbali na Mwenyezi Mungu na Mtume wake ni yule aliyewekwa mbali na maasi, kwa namna yoyote atakavyokuwa’

Na mtegemee Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu na uachane nao wakikuasi; wala roho isikutoke juu yao, na uelekee kwa Mwenyezi Mungu peke yake katika mambo yako yote.

Ambaye anakuona unaposimama kwenye tahajjud (Swala za usiku wa manane)na mageuko yako katika wale wanaosujudu.

Shia Imamiyya wanasema kuwa mababa wote wa Mtume walikuwa wakimpwekesha Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa dalili zao katika hilo ni Aya hii; walipofasiri mgeuko kwa maana ya mgeuko wake katika migongo ya wanaompwekesha Mungu; yaani kupitia mifupani mwao.

Tamko la Aya linakubaliana na maana haya na pia linakubaliana na tafsiri ya anayesema kuwa Mungu anakuona ukiwa pamoja na wanaoswali. Dhahiri ya mfumo wa maneno inafahamisha tafsiri hii zaidi kuliko ile.

Hakika yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.

Anasikia kauli na anajua siri na vitendo vyote na kuvilipa. Vikiwa ni kheri basi ni kheri na vikiwa ni shari basi ni shari.

هَلْ أُنَبِّئُكُمْ عَلَىٰ مَن تَنَزَّلُ الشَّيَاطِينُ ﴿٢٢١﴾

221. Je niwaambie ambao mashetani wanawashukia?

تَنَزَّلُ عَلَىٰ كُلِّ أَفَّاكٍ أَثِيمٍ ﴿٢٢٢﴾

222. Wanamshukia kila mzushi mkubwa, mwingi wa dhambi.

يُلْقُونَ السَّمْعَ وَأَكْثَرُهُمْ كَاذِبُونَ ﴿٢٢٣﴾

223. Wanawapa masikio na wengi wao ni waongo.

وَالشُّعَرَاءُ يَتَّبِعُهُمُ الْغَاوُونَ ﴿٢٢٤﴾

224. Na washairi ni wapotofu ndio wanaowafuata.

أَلَمْ تَرَ أَنَّهُمْ فِي كُلِّ وَادٍ يَهِيمُونَ ﴿٢٢٥﴾

225. Je huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde?

وَأَنَّهُمْ يَقُولُونَ مَا لَا يَفْعَلُونَ ﴿٢٢٦﴾

226. Na kwamba wao wanasema wasiyoyatenda?

إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَذَكَرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا وَانتَصَرُوا مِن بَعْدِ مَا ظُلِمُوا وَسَيَعْلَمُ الَّذِينَ ظَلَمُوا أَيَّ مُنقَلَبٍ يَنقَلِبُونَ ﴿٢٢٧﴾

227. Isipokuwa wale ambao wameaamini na wakatenda mema na wakamtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi na wakajitetea wanapodhulumiwa. Na punde watajua waliodhulumu ni mgeuko gani watakaogeuka.

WASHAIRI WANAFUATWA NA WAPOTOFU

Aya 221 – 227

MAANA

Qur’an inawapiga vita wabatilifu, lakini kabla ya chochote, kwanza inawapiga vita kwa mantiki ya kiakili iliyo salama na inawajadili kwa njia nzuri, huku ikiwalingania kwenye haki kwa hekima na mawaidha mazuri; ikifafanua kwa kila aina ya mfumo na kuwaomba, kwa upole na ulaini kabisa, walete hoja zao:

لَّوْلَا يَأْتُونَ عَلَيْهِم بِسُلْطَانٍ بَيِّنٍ ﴿١٥﴾

“Kwa nini hawawaletei dalili bayana?” Juz. 15 (18:15).

Wanapoleta hoja dhaifu, Qur’an huibatilisha na kubainisha udhaifu uliopo. Washirikina na watu wengi wanaojali masilahi yao tu, wamesema mengi kuhusiana na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Miongoni mwa madai yao ni kuwa Qur’an inatokana na shetani na pia kudai kuwa Muhammad(s.a.w.w) ni mshairi. Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawajibu kwa haya yafuatayo:

Je niwaambie ambao mashetani wanawashukia? Wanamshukia kila mzushi mkubwa, mwingi wa dhambi.

Hili ni jibu la kauli yao kuwa Qur’an ni katika wahyi wa shetani. Njia ya kujibu ni kuwa shetani anaingiza wasiwasi na ubatilifu kwa waongo na wenye madhambi mfano wao: “Mashetani watu na majini. Baadhi yao wanawapa wenzao maneno ya kupambapamba kuwahadaa.” Juz. 8 (6:112).

Shetani hana njia kwa wa kweli na waaminifu, kama vile mitume na viongozi wema. Zaidi ya hayo ni kuwa ni kuwa Qur’an ni haki na kheri na mawazo ya shetani ni shari na uzushi.

Wanawapa masikio na wengi wao ni waongo.

Makusudio ya kuwapa masikio hapa ni kuwasikiliza. Wanaosikilizwa ni makafiri. Maana ni kuwa wale ambao wanawasikiliza mashetani na kuchukua kutoka kwao uwongo na ubatilifu ndio makafiri. Na makafiri wengi ni waongo katika mazungumzo yao na kauli zao. Muhammad(s.a.w.w) ni mkweli katika kauli zake zote na vitendo vyake vyote; vipi aambiwe amesikiliza na kupokea kutoka kwa shetani?

Na washairi ni wapotofu ndio wanaowafuata. Je huwaoni kwamba wao wanatangatanga katika kila bonde na kwamba wao wanasema wasiyoyatenda?

Hii ni kuwajibu washirikina waliosema kuwa Muhammad ni mshairi. Njia ya kubainisha ni kuwa kuna tofauti kubwa baina ya washairi na Muhammad kwa njia hizi zifuatazo:

Kwanza : wale waliomfuata Muhammad(s.a.w.w) walimfuata kwa kumwamini na kumwadhimisha. Na pia kumwamini Mwenyezi Mungu wakitarajia biashara isiyofilisika.

Ndio maana walimfidia kwa roho zao na wakapigana na mababa zao na watoto wao kwa ajili yake. Lakini washairi wao wanaishi katika njozi na kufikirika tu. Wakale walisema: “ushairi ni njozi ” wala hakuna anayewafuata hawa isipokuwa wale wanaoelekeana nao.

Pili : washairi wengi hapo zamani walikuwa wakiwasaidia viongozi madhalimu. Mshairi alikuwa akitumia kipawa chake na akili yake kutunga shairi au nyimbo itakayoimbwa mbele ya viongozi madhalimu. Sasa hili ni wapi na wapi na risala ya Muhammad(s.a.w.w) ambayo hiyo yenyewe ni mapinduzi dhidi ya dhulma na ufisadi?

Tatu, kwamba washairi wengi wanasema sana na kutenda kidogo, wala hakiwapi umuhimu kitu isipokuwa hawa na malengo yao tu ndio yanayowapa msukumo yakiwalekeza popote yanapoelekea. Lakini Muhammad(s.a.w.w) yeye hatamki kwa hawa yake wala hafuati isipokuwa wahyi kutoka kwa Mola wake. Sasa vipi ataambiwa ni mshairi:

وَمَا عَلَّمْنَاهُ الشِّعْرَ وَمَا يَنبَغِي لَهُ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ وَقُرْآنٌ مُّبِينٌ ﴿٦٩﴾

“Wala hatukumfundisha mashairi, wala hayatakikani kwake. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur’an inayobainisha.” (36:69).

Unaweza kuuliza : Je hii haifahamishi kuwa Uislamu unapiga vita mashairi, kutokana na Qur’an kuyashutumu?

Jibu : Hapana! Qur’an haikushutumu shairi kama shairi au washairi kama washairi; isipokuwa imewashutumu washairi wanaoipinga haki na kufuata kombokombo. Ama washairi wanaoelezea matumaini ya wanyonge na kuwa pamoja na wanaodhulumiwa, kuusaidia uadilifu na uhuru wa binadamu na kupinga utaghuti, ujinga na kurudi nyuma, hawa wako katika safu ya wapigania jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu.

Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) aliulizwa unasemaje kuhusu washairi? Akasema: “Hakika muumini ni mpigania jihadi kwa upanga wake na ulimi wake. Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake, wao ni kama kwamba wanarusha mikuki.”

Aina ya mashairi ambayo ni mikuki katika nyoyo za madhalimu ndiyo aliyoikusudia Mtume(s.a.w.w) katika kauli yake: “Hakika katika shairi kuna hekima.” Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Amemfundisha ubainifu.” (55:4).

Hakuna mwenye shaka kuwa ushairi ni fani ya hali ya juu ya ubainifu na fasihi, kama ambavyo ni utajiri wa lugha na hazina yake yenye thamani.

Ndio maana Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawavua washairi wema na wapigania jihadi kwa kusema:

Isipokuwa wale ambao wameaamini na wakatenda mema na wakamtaja Mwenyezi Mungu kwa wingi na wakajitetea wanapodhulumiwa.

Yaani washairi wakiitetea haki na na watu wake kutokana na wachokozi na maadui na wakautetea uhuru wa ubinadamu na heshima yake.

Hii ni nukuu iliyo wazi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwamba shairi la kimapinduzi dhidi ya dhulma na uonevu ni katika umuhimu wa dini, imani na matendo mema.

Katika maana ya Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t):

لَّا يُحِبُّ اللَّـهُ الْجَهْرَ بِالسُّوءِ مِنَ الْقَوْلِ إِلَّا مَن ظُلِمَ ﴿١٤٨﴾

“Hapendi Mwenyezi Mungu maneno ya kutangaza uovu ila kwa mwenye kudhulumiwa.”

Juz. 6 (4:148).

Na punde watajua waliodhulumu ni mgeuko gani watakaogeuka.

Huu ni ukemeo na kiaga cha mwisho mbaya kwa kila mwenye kudhlumu na kuonea.

Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu Mola wa viumbe wote na rehema na amani zimshukie Muhammad na kizazi chake kitakatifu.


9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA

Sura Ya Ishirini Na Saba: Surat An-Naml. Imeshuka Makka ina Aya 93

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

طس تِلْكَ آيَاتُ الْقُرْآنِ وَكِتَابٍ مُّبِينٍ ﴿١﴾

1. Twa siin. Hiyo ni Aya za Qur’an na Kitabu kinachobainisha.

هُدًى وَبُشْرَىٰ لِلْمُؤْمِنِينَ ﴿٢﴾

2. Mwongozo na bishara kwa waumini.

الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَهُم بِالْآخِرَةِ هُمْ يُوقِنُونَ ﴿٣﴾

3. Wale ambao wanasimamisha Swala na wakatoa Zaka na wana yakini na Akhera.

إِنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ زَيَّنَّا لَهُمْ أَعْمَالَهُمْ فَهُمْ يَعْمَهُونَ ﴿٤﴾

4. Hakika ambao hawaiamini Akhera, tumewapambia vitendo vyao, basi wao wanamanga-manga.

أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ لَهُمْ سُوءُ الْعَذَابِ وَهُمْ فِي الْآخِرَةِ هُمُ الْأَخْسَرُونَ ﴿٥﴾

5. Hao ndio watakaopata adhabu mbaya, na wao katika Akhera ni wenye kupata hasara.

MWONGOZO NA BISHARA KWA WAUMINI

Aya 1-5

MAANA

Twa siin.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:1)

Hiyo ni Aya za Qur’an na Kitabu kinachobainisha.

Hiyo ni ishara ya Sura hii. Qur’an na Kitabu ina maana moja. Tofauti ni wasifu tu, sio kwa dhati yake. Ni Qur’an kwa vile inasomwa, kutokana na neno na qiraa lenye maana ya kusoma. Na kitabu kwa vile imeandikwa, kutokana na neno kitaba lenye maana ya kuandika.

Ni chenye kubainisha kwa vile kiko wazi. Pia vilevile ni mwongozo na bishara kwa waumini.

Kinamuongoza mwenye kutafuta uongofu na kumpa habari njema ya Pepo ikiwa ataamini na kutenda mema.

Wale ambao wanasimamisha Swala na wakatoa Zaka na wana yakini na Akhera.

Imani peke yake si kitu mbele ya Mwenyezi Mungu ila zikidhihiri athari zake; miongoni mwa zile zilizo muhimu zaidi ni swala na zaka. Kwa ufupi ni kuwa kuamini haki sio fikra ya kichwani wala maneno ya mdomoni; isipokuwa ni matendo na tabia.

Unaweza kuuliza : Wenye kusimamisha Swala na kutoa Zaka tayari wana yakini na Akhera, sasa kuna wajihi gani wa kusema na wana yakini na akhera?

Jibu : Makusudio ni kuwa wanaiamini Akhera kwa imani isiyo na shaka; kama vile wameiona.

Hakika ambao hawaiamin Akhera, tumewapambia vitendo vyao, basi wao wanamangamanga.

Nyoyo zimepofuka, hazioni matendo yao. Kwa hiyo wanafanya bila ya kuhofia hisabu wala adhabu.

Unaweza kuuliza : Hapa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametegemeza kupambia kwake yeye mwenyewe na katika Aya nyingine amekutegemeza kwa shetani: “Lakini shetani aliwapambia vitendo vyao.” Juz. 14 (16:63). Sasa je, kuna wajihi gani wa kuunganisha Aya mbili hizi?

Jibu : Kule kumetegemezwa kupamba kwa shetani kwa kuangalia kuwa yeye ni mhalifu na mtia wasiwasi. Hapa kumetegemzwa kwa Mwenyezi Mungu kwa kuangalia kuwa desturi ya Mwenyezi Mungu na matakwa yake yamepitisha kupofuka na uovu wa matendo yake yule asiyeamini Siku ya Mwisho; sawa kama yalivyopitisha matakwa yake Mwenyezi Mungu kufa kwa yule anayefuata njia inayopelekea kifo.

Kwa maneno mengine ni kuwa yule asiyeamini Akhera anafanya haramu huku akiona ni halali, kwa sababu Mwenyezi Mungu amejaalia kukosa imani ni sababu ya kutojua haramu.

Kama mtu atasema, hilo si ni jambo la kawaida? Tutajibu: Vitu vyote vya kawaida ya maumbile na sababu vinakomea kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu, kwa sababu yeye ndiye aliyeleta hayo maumbile ya kawaida na ulimwengu kwa ujumla.

Hao ndio watakaopata adhabu mbaya, na wao katika Akhera ni wenye kupata hasara.

Wamepata hasara duniani kwa sababu wameiacha na wamepata hasara Akhera ya thawabu na kupata adhabu. Hiyo ndiyo hasara ya dhahiri.

وَإِنَّكَ لَتُلَقَّى الْقُرْآنَ مِن لَّدُنْ حَكِيمٍ عَلِيمٍ ﴿٦﴾

6. Na kwa hakika wewe unapewa Qur’an kutoka kwake Mwenye hekima, Mwenye ujuzi.

إِذْ قَالَ مُوسَىٰ لِأَهْلِهِ إِنِّي آنَسْتُ نَارًا سَآتِيكُم مِّنْهَا بِخَبَرٍ أَوْ آتِيكُم بِشِهَابٍ قَبَسٍ لَّعَلَّكُمْ تَصْطَلُونَ ﴿٧﴾

7. Musa alipowaambia ahli zake: Hakika nimeona moto, nitakwenda kuwaletea habari au kuwaletea kijinga kinachowaka ili mpate kuota.

فَلَمَّا جَاءَهَا نُودِيَ أَن بُورِكَ مَن فِي النَّارِ وَمَنْ حَوْلَهَا وَسُبْحَانَ اللَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٨﴾

8. Basi alipoufikia, pakanadiwa kwamba umebarikiwa uliomo katika moto huu na aliyeko pembezoni mwake na ametakasika Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote.

يَا مُوسَىٰ إِنَّهُ أَنَا اللَّـهُ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٩﴾

9. Ewe Musa! Hakika mimi ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

وَأَلْقِ عَصَاكَ فَلَمَّا رَآهَا تَهْتَزُّ كَأَنَّهَا جَانٌّ وَلَّىٰ مُدْبِرًا وَلَمْ يُعَقِّبْ يَا مُوسَىٰ لَا تَخَفْ إِنِّي لَا يَخَافُ لَدَيَّ الْمُرْسَلُونَ ﴿١٠﴾

10. Na itupe fimbo yako! Alipoiona inatingishika, kama kwamba ni nyoka, aligeuka kurudi nyuma wala hakungoja. Ewe Musa! Usihofu! Hakika mimi hawagopi mbele yangu mitume.

إِلَّا مَن ظَلَمَ ثُمَّ بَدَّلَ حُسْنًا بَعْدَ سُوءٍ فَإِنِّي غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١١﴾

11. Ila aliyedhulumu kisha akabadilisha wema baada ya ubaya, basi hakika mimi ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

وَأَدْخِلْ يَدَكَ فِي جَيْبِكَ تَخْرُجْ بَيْضَاءَ مِنْ غَيْرِ سُوءٍ فِي تِسْعِ آيَاتٍ إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَقَوْمِهِ إِنَّهُمْ كَانُوا قَوْمًا فَاسِقِينَ ﴿١٢﴾

12. Na ingiza mkono wako katika mfuko wako utatoka mweupe pasipo ubaya. Ni katika ishara tisa kwa Firauni na watu wake. Hakika wao ni watu mafasiki.

فَلَمَّا جَاءَتْهُمْ آيَاتُنَا مُبْصِرَةً قَالُوا هَـٰذَا سِحْرٌ مُّبِينٌ ﴿١٣﴾

13. Zilipowafikia ishara zetu zionyeshazo, walisema: Huu ni uchawi dhahiri.

وَجَحَدُوا بِهَا وَاسْتَيْقَنَتْهَا أَنفُسُهُمْ ظُلْمًا وَعُلُوًّا فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُفْسِدِينَ ﴿١٤﴾

14. Na wakazikataa kwa dhulma na kujivuna, na hali ya kuwa nafsi zao zina yakini nazo. Basi angalia ulikuwaje mwisho wa wafisadi.

MUSA

Aya 6 – 14

MAANA

Na kwa hakika wewe unapewa Qur’an kutoka kwake Mwenye hekima, Mwenye ujuzi.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye aliyekupa Qur’an na wala haitoki kwako, kama wanavyodai wapinzani.

Musa alipowaambia ahli zake: Hakika nimeona moto, nitakwenda kuwaletea habari au kuwaletea kijinga kinachowaka ili mpate kuota.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:10).

Basi alipoufikia, pakanadiwa kwamba umebarikiwa uliomokatika moto huu na aliyeko pembezoni mwake na ametakasika Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu wote.

Makusudio ya moto hapa ni nuru, uliomo ndani yake ni uweza wa Mwenyezi Mungu na aliyeko pembeni ni Musa.

Maana ni kuwa, ewe Musa! Kile ulichokiona ukadhania ni moto ni nuru iliyobarikiwa iliyoletwa na Mwenyezi Mungu kwa uweza wake na wewe uliyesimama pembeni mwa nuru hii pia umebarikiwa vilevile. Kwa sababu mimi nimekuchagua kwa risala yangu, upeleke bishara, kuonya na kueneza baraka ardhini. Hivi ndivyo tulivyoifahamu Aya baada ya kufuatilia na kutaamali. Ikiwa ndio makusudio ni sawa; ikiwa sivyo, lakini maelezo yenyewe ni sahihi.

Ewe Musa! Hakika mimi ndiye Mwenyezi Mungu Mwenye nguvu, Mwenye hekima.

Alimfichulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwa anayemuita na kumwambia maneno ni Mola Mwenyezi, ili asikie na kutii.

Na itupe fimbo yako! Alipoiona inatingishika, kama kwamba ni nyoka, aligeuka kurudi nyuma wala hakungoja. Ewe Musa! Usihofu! Hakika mimi hawagopi mbele yangu mitume.

Neno nyoka hapa limefasiriwa kutokana na neno la kiarabu Jann lenye maana ya Jinn. Limefasiriwa kutokana na Aya nyingine zinazotaja nyoka moja kwa moja:

فَأَلْقَاهَا فَإِذَا هِيَ حَيَّةٌ تَسْعَىٰ ﴿٢٠﴾

“Akaitupa mara ikawa nyoka anayekwenda mbio.” Juz. 16 (20:20),

فَأَلْقَىٰ عَصَاهُ فَإِذَا هِيَ ثُعْبَانٌ مُّبِينٌ ﴿١٠٧﴾

“Akaitupa fimbo yake mara ikawa nyoka dhahiri.” Juz. 9 (7:107).

Musa ni mtu, na kawaida ya mtu ni lazima ahofie. Ni nani asiyeogopa atakapoiona kanzu yake iliyo mwilini imegeuka kuwa mnyama anayeshambulia, pete iliyomo kidoleni mwake imekuwa nge au fimbo iliyo mkononi mwake imegeuka nyoka?

Musa alihofia, kwa vile yeye ni mtu, anakula chakula, anatembea sokoni n.k. Lakini Mwenyezi Mungu alimpa amani na akamwambia kuwa wewe ni mjumbe wangu na wajumbe wangu wote wako katika amani na salama.

Ila aliyedhulumu kisha akabadilisha wema baada ya ubaya, basi haki- ka mimi ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.

Mitume hawahofii, kwa sababu wao hawazidhulumu nafsi zao wala kuwadhulumu wengine; isipokuwa anayetakiwa kuwa na hofu ni yule aliyemdhulumu Mwenyezi Mungu kwa ushirikina na kufuru, kujidhulumu yeye mwenyewe kwa maasi au kuwadhulumu wengine kwa kuingilia haki zao.

Lakini aliyetubia baada ya dhulma yake basi Mwenyezi Mungu atam- takabalia toba na kumpa msamaha na rehema yake.

Na ingiza mkono wako katika mfuko wako utatoka mweupe pasipo ubaya.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7: 108), Juz. 16 (20:22) na Juzuu hii tuliyo nayo (26:33).

Ni katika ishara tisa kwa Firauni na watu wake. Hakika wao ni watu mafasiki.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (17:101).

Zilipowafikia ishara zetu zionyeshazo, walisema: Huu ni uchawi dhahiri.

Yaani zionyeshazo watu haki watakapoona hiyo miujiza tisa aliyokuja nayo Musa. Firauni na watu wake waliiona haki walipoona miujiza hii tisa, lakini walifanya kiburi na inadi, wakamkadhibisha Mwenyezi Mungu na wao wenyewe kwa kusema kuwa ni uchawi dhahiri. Ndio maana Mwenyezi Mungu Mtukufu akasema:

Na wakazikataa kwa dhulma na kujivuna, na hali yakuwa nafsi zao zina yakini nazo.

Nyoyo zao na akili zao zilikuwa na yakini na ukweli wa Musa na miujiza yake, lakini walimpinga kwa ndimi zao kuhofia manufaa yao na vyeo. Haya ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Kwa dhulma na kujivuna.

Basi angalia ulikuwaje mwisho wa wafisadi katika ardhi kwa kufuru, dhulma na ufisadi?

وَلَقَدْ آتَيْنَا دَاوُودَ وَسُلَيْمَانَ عِلْمًا وَقَالَا الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي فَضَّلَنَا عَلَىٰ كَثِيرٍ مِّنْ عِبَادِهِ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٥﴾

15. Na hakika tulimpa Daud na Suleiman elimu na wakasema: Sifa njema zote (alham-du-lillah) ni za Mwenyezi Mungu ambaye ametufadhilisha kuliko wengi katika waja wake waumini.

وَوَرِثَ سُلَيْمَانُ دَاوُودَ وَقَالَ يَا أَيُّهَا النَّاسُ عُلِّمْنَا مَنطِقَ الطَّيْرِ وَأُوتِينَا مِن كُلِّ شَيْءٍ إِنَّ هَـٰذَا لَهُوَ الْفَضْلُ الْمُبِينُ ﴿١٦﴾

16. Na Suleiman alimrithi Daud. Na akasema: “Enyi watu! Tumefunzwa usemi wa ndege. Na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo dhahiri.

وَحُشِرَ لِسُلَيْمَانَ جُنُودُهُ مِنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ وَالطَّيْرِ فَهُمْ يُوزَعُونَ ﴿١٧﴾

17. Na alikusanyiwa Suleiman majeshi yake kutokana na majini na watu na ndege nayo yakapangwa kwa nidhamu.

حَتَّىٰ إِذَا أَتَوْا عَلَىٰ وَادِ النَّمْلِ قَالَتْ نَمْلَةٌ يَا أَيُّهَا النَّمْلُ ادْخُلُوا مَسَاكِنَكُمْ لَا يَحْطِمَنَّكُمْ سُلَيْمَانُ وَجُنُودُهُ وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿١٨﴾

18. Hata walipofikia kwenye bonde la chungu, alisema chungu mmoja: Enyi chungu, ingieni maskani zenu, asije akawaponda Suleiman na jeshi lake na hali wao hawatambui.

فَتَبَسَّمَ ضَاحِكًا مِّن قَوْلِهَا وَقَالَ رَبِّ أَوْزِعْنِي أَنْ أَشْكُرَ نِعْمَتَكَ الَّتِي أَنْعَمْتَ عَلَيَّ وَعَلَىٰ وَالِدَيَّ وَأَنْ أَعْمَلَ صَالِحًا تَرْضَاهُ وَأَدْخِلْنِي بِرَحْمَتِكَ فِي عِبَادِكَ الصَّالِحِينَ ﴿١٩﴾

19. Basi akatabasamu akicheka kwa kauli yake, akasema: Ewe Mola wangu! Nizindue niishukuru neema yako uliyonineemesha na wazazi wangu na nipate kutenda mema unayoyaridhia na uni- ingize kwa rehema yako katika waja wako wema.

SULEIMAN

Aya 15 – 19

MAANA

Na hakika tulimpa Daud na Suleiman elimu, iliyowaongoza kwenye utiifu wa Mwenyezi Mungu na manufaa ya watu. Wala hawakujivuna nayo kwa waja wa Mungu au kuvumbua nayo silaha za maangamizi ili kuwakandamiza wanyonge wawanyonye nyenzo zao.

Bali hawa wawili walimtii Mwenyezi Mungu katika maamrisho yake na makatazo yake na wakamshukuru kwa neema ya elimu ambayo hailinganishwi na chochotena wakasema: Sifa njema zote (alhamdu lillah) ni za Mwenyezi Mungu ambaye ametufadhilisha kuliko wengi katika waja wake waumini.

Makusudio ya kufadhilishwa (kufanywa bora) hapa, ni kufadhilishwa kwa elimu yenye manufaa. Maana ya kuiliko wengi katika waumini ni wale wasiofikia cheo chao cha elimu.

Hapo kuna ishara kuwa katika waumini wako waliofadhilishwa zaidi yao. Na hivyo ndivyo ilivyo.

Kwa vyovyote iwavyo ni kuwa ubora mbele ya Mwenyezi Mungu haupimwi kwa elimu wala kwa kuupeleka upepo au kulainisha chuma; isipokuwa ni kwa manufaa ya watu na masilahi yao.

Na Suleiman alimrithi Daud.

Daud(a.s ) ni katika kizazi cha Ya’qub bin Is-haq bin Ibrahim. Mwenyezi Mungu alimtukuza kwa utume, akamteremshia Zabur, akamfanya ni khalifa katika ardhi, akamuhusisha kuwa na sauti nzuri zaidi na akamlainishia chuma. Yeye ni mfalme wa pili wa dola ya kiyahudi.

Alipewa jina la Mfalme Daud. Mfalme wa kwanza alikuwa ni Talut, kama alivyosema Mwenyezi Mungu:

إِنَّ اللَّـهَ قَدْ بَعَثَ لَكُمْ طَالُوتَ مَلِكًا ﴿٢٤٧﴾

Hakika Mwenyezi Mungu amewachagulia Talut kuwa mfalme. Juz.2 (2:247).

Mwanawe Suleiman(a.s ) alikuwa ni mtume vile vile. Naye Mwenyezi Mungu alimpa neema nyingi, zikiwemo kurithi ufalme wa baba yake. Historia inasema kuwa ufalme wao uliendelea kwa miaka sabini.

Baada ya kufa Suleiman, mayahudi waligawanyika dola mbili zinazopigana: Dola ya Israil na dola ya Yahudha. Alipokuja Nebuchadnezzar aliwafyeka na hakukua na dola tena ya kiyahudi, mpaka pale ukoloni wa Anglo America ulipoanzisha kambi ya kijeshi kulinda masilahi yake mashariki ya kati, ukaipa jina la dola Israil kwenye ardhi ya Palestina mnamo mwaka 1948.

Mayahudi wanamzungumza vibaya mfalme wao Daud, kwamba alikuwa akiwapora wanawake na kuwaua waume zao na mwanawe Suleman alikuwa ni jabari mkandamizaji na mwenye israfu.

Baadhi ya wafasiri wanasema kuwa makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na Suleiman alimrithi Daud” ni kuwa alirithi elimu tu kutoka kwa baba yake. Lakini ilivyo hasa ni kuwa Aya inafahamisha urithi wa ufalme; kama ilivyotokea hasa. Ama elimu haiwi kwa kurithi, bali ni kwa juhudi au kwa wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kuna tofauti katika Hadith ya “Sisi Mitume haturithiwi,” baina ya Waislamu. Kuna walioithibitisha na walioikanusha.

Na akasema: Enyi watu! Tumefunzwa usemi wa ndege.

Uislamu umethibitisha fikra ya muujiza mikononi mwa mitume. Mwenye kuikana si Mwislamu, kwa sababu ukanusho huo ni sawa na kumkadhibisha Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ni kwa muujiza pekee yake ndio tunaweza kufasiri kauli ya Nabii Suleiman: ‘Na tumefunzwa usemi wa ndege.”

Na tumepewa kila kitu. Hakika hii ni fadhila iliyo dhahiri.

Makusudio ya neno ‘kila’ hapa ni wingi sio kuenea kwenye kila kitu; ni sawa na kusema fulani ana kila kitu, kwa kuelezea kuwa ana vitu vingi.

Aya inafahamisha kuwa ndege wana utambuzi na lugha inayofahamika. Hilo linasisitizwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَمَا مِن دَابَّةٍ فِي الْأَرْضِ وَلَا طَائِرٍ يَطِيرُ بِجَنَاحَيْهِ إِلَّا أُمَمٌ أَمْثَالُكُم ﴿٣٨﴾

Na hakuna mnyama katika ardhi wala ndege arukaye kwa mbawa zake, ila ni umma kama nyinyi. Juz. 7 (6:38).

Na alikusanyiwa Suleiman majeshi yake kutokana na majini na watu na ndege, nayo yakapangwa kwa nidhamu.

Neno ‘kutokana’ ni baadhi; yaani baadhi ya majini, watu na ndege. Tumesema mara nyingi kwamba sisi tunaamini kuweko majini, kwa sababu Qur’an inathibitisha hilo na akili haikatai.

Suleiman alikuwa na jeshi la majini, watu na ndege. Kila moja ya makundi haya matatu lilikuwa na kamanda wake anayechunga nidhamu ya kutembea n.k. Hii ndio maana ya kupangwa kwa nidhamu.

SOMO NA MAZINGATIO KATIKA CHUNGU WA SULEIMAN

Hata walipofikia kwenye bonde la chungu, alisema chungu mmoja: Enyi chungu, ingieni maskani zenu, asije akawaponda Suleiman na jeshi lake na hali wao hawatambui.

Wafasiri wametofautiana kuhusu bonde hili. Kuna waliosema ni Taif na wengine wakasema ni Sham. Vyovyote iwavyo ni kuwa Aya inafahamisha kuwa wadudu chungu wana utambuzi, lugha na nidhamu. Haya yamethibitishwa na elimu. Ama Suleiman kujua lugha ya chungu, hilo halina tafsiri isipokuwa ni muujiza.

Unaweza kuliza : Vipi Suleiman aliweza kusikia maneno ya chungu na yaye alikuwa mbali nao kiasi ambacho anayejua ni Mungu tu; kama tunavyojua kuwa lau mmoja wetu ataingiwa na chungu sikioni hawezi kusikia?

Jibu : Baadhi ya riwaya zinasema kuwa upepo ulichukua maneno ya chungu kwa Suleiman. Haya yanatiliwa nguvu na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

فَسَخَّرْنَا لَهُ الرِّيحَ تَجْرِي بِأَمْرِهِ ﴿٣٦﴾

“Basi tukamtiishia upepo ukienda kwa amri yake.” (38:36).

Basi akatabasamu akicheka kwa kauli yake, akasema: Ewe Mola wangu! Nizindue niishukuru neema yako uliyonineemesha na wazazi wangu na nipate kutenda mema unayoyaridhia na uniingize kwa rehe- ma yako katika waja wako wema.

Suleiman alipoomba ufalme ambao hataupata yeyote baada yake, alikusudia kuwatumia majini, upepo, ndege n.k. Kwa sababu ni wengi waliomakinika katika ardhi.

Suleiman alipofika kwenye bonde la chungu na upepo kuchukua maneno ya chungu hadi masikioni mwake na kufahamu maana yake, alitambua kuwa haya ni katika ambayo hatakuwa nayo yeyote baada yake.

Basi aliihisi raha kwa neema hii na akatekeleza haki yake ya kumshukuru Mwenyezi Mungu. Kutambua tu, kwamba neema hii inatoka kwa Mwenyezi Mungu ni aina ya shukrani. Na shukrani kubwa zaidi ni kufanya kheri kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.

Kama ambavyo Aya inafahamisha kuwa Suleiman ana dola na jeshi lake na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) amempa elimu ya kujua lugha ya chungu; vile vile Aya inafahamisha kuwa chungu naye ana dola yake na raia zake na kwamba Mwenyezi Mungu naye amempa elimu ya kuwajua baadhi ya binadamu na majina yao. Kama si hivyo alijuaje kuwa huyu anayekuja na msafara wa jeshi ni Suleiman bin Daud?

Hakika mdudu huyo aliyewaambia wenzake, alikuwa mkubwa katika ulimwengu wake, kama alivyokuwa Suleiman katika ulimwengu wake. Na kwamba alikuwa akiwafanyia uadilifu raia wake, akiwahurumia, kujali masilahi yao na kutekelza haki kamili ya uongozi, kama anavyofanya Suleiman na viongozi wengineo waadilifu na wa haki.

Mwenye kuchunguza na kutaamali tukio la chungu na Suleiman atafikia kwenye somo na mazingatio yafuatayo:-

1. Nidhamu na mpangilio uko kwenye viumbe vyote; kuanzia kidogo, kama chunguchungu, hadi kikubwa, kama sayari. Hakuna tafisiri ya nid- hamu hii ya hali ya juu na mpangilio huu wa ajabu isipokuwa kuweko Muweza aliye Mjuzi: “Na ameumba kila kitu na akikadiria kipimo.” Juz. 18 (25:2).

2. Ushirikiano na kutambua majukumu, hakuhusuki na watu tu, bali hata kwa wanyama, ndege, wadudu n.k. Kijichembe hiki ambacho mara nyingine hata hakionekani kwa macho, kilipohisi hatari kwa jamaa zake, kilisimama kuwahadharisha kikisema: ‘ingieni maskani yenu, asije akawaponda Suleiman na jeshi lake.’ Wataalamu wameleta ushahidi mwingi wa hakika hii ya maisha ya wanyama.

3. Mtu ni lazima ashukuru anaponeemeshwa na Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa elimu, utawala au mengine. Amshukuru Mwenyezi Mungu na awanyenyekee watu; sio kujivuna na kujiona kwa wengine kwa sababu ya neema ya Mwenyezi Mungu.

Pia, mtu akineemeka, inatakikana ajue kwamba Mwenyezi Mungu amekwishaitoa neema kama hiyo au kushinda hiyo kwa kiumbe kilicho dhaifu zaidi; na binadamu sio peke yake anayeneemeshwa na Mwenyezi Mungu.

Uvumbuzi wa elimu umegundua kuwa kuna maumbile makubwa zaidi ya haya tuyaonayo; hakuna hata mmoja anayeweza kujua hakika yake isipokuwa Muumba. Binadamu si chochote katika maumbile hayo. Hayo yanaashiriwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ ﴿٥٧﴾

“Bila shaka kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa zaidi kuliko kuwaumba watu.” (40:57).

Kwa hiyo basi, Aya:

وَاللَّـهُ يَخْتَصُّ بِرَحْمَتِهِ مَن يَشَاءُ ﴿١٠٥﴾

“Na Mwenyezi Mungu humhusisha kwa rehema zake amtakaye.” Juz. 1 (2:105),

تُؤْتِي الْمُلْكَ مَن تَشَاءُ ﴿٢٦﴾

“Humpa ufalme umtakaye.” Juz. 3 (3:26)

وَإِن مِّنْ أُمَّةٍ إِلَّا خَلَا فِيهَا نَذِيرٌ ﴿٢٤﴾

“Na hapana umma wowote ila ulipata muonyaji.” (35:24)

Zote hizi, na mfano wake, zinaenea kwa binadamu na wasiokuwa binadamu.

Ikumbukwe kwamba Mwenyezi Mungu amelitumia neno umma kwa wasiokuwa binadamu; kama kauli yake: Na hakuna mnyama katika ardhi wala ndege arukaye kwa mbawa zake, ila ni umma kama nyinyi.” Juz. 7 (6:38).


10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA

وَتَفَقَّدَ الطَّيْرَ فَقَالَ مَا لِيَ لَا أَرَى الْهُدْهُدَ أَمْ كَانَ مِنَ الْغَائِبِينَ ﴿٢٠﴾

20. Na akawakagua ndege na akasema: Mbona simwoni Hud-hud au amekuwa miongoni mwa walio ghaibu.

لَأُعَذِّبَنَّهُ عَذَابًا شَدِيدًا أَوْ لَأَذْبَحَنَّهُ أَوْ لَيَأْتِيَنِّي بِسُلْطَانٍ مُّبِينٍ ﴿٢١﴾

21. Kwa yakini nitamwadhibu kwa adhabu kali au nitamchinja, au aniletee hoja iliyo wazi.

فَمَكَثَ غَيْرَ بَعِيدٍ فَقَالَ أَحَطتُ بِمَا لَمْ تُحِطْ بِهِ وَجِئْتُكَ مِن سَبَإٍ بِنَبَإٍ يَقِينٍ ﴿٢٢﴾

22. Basi hakukaa sana mara akasema: Nimegundua usiloligundua na nimekujia na habari za yakini kutoka Sabai.

إِنِّي وَجَدتُّ امْرَأَةً تَمْلِكُهُمْ وَأُوتِيَتْ مِن كُلِّ شَيْءٍ وَلَهَا عَرْشٌ عَظِيمٌ ﴿٢٣﴾

23. Hakika nimemkuta mwanamke anayewatawala na amepewa kila kitu na anacho kiti cha enzi kikubwa.

وَجَدتُّهَا وَقَوْمَهَا يَسْجُدُونَ لِلشَّمْسِ مِن دُونِ اللَّـهِ وَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَصَدَّهُمْ عَنِ السَّبِيلِ فَهُمْ لَا يَهْتَدُونَ ﴿٢٤﴾

24. Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi Mungu; na shetani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia njia. Kwa hivyo hawakuongoka.

أَلَّا يَسْجُدُوا لِلَّـهِ الَّذِي يُخْرِجُ الْخَبْءَ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَيَعْلَمُ مَا تُخْفُونَ وَمَا تُعْلِنُونَ ﴿٢٥﴾

25. Kwamba hawamsujudii Mwenyezi Mungu ambaye huyatoa yaliyofichikana katika mbingu na ardhi na huyajua mnayoyaficha na mnayoyadhihirisha.

اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ ﴿٢٦﴾

26. Mwenyezi Mungu hapana Mola ila Yeye Mola wa arshi tukufu.

MBONA SIMWONI HUD-HUD

Aya 20 – 26

MAANA

Na akawakagua ndege na akasema: Mbona simwoni Hud-hud au amekuwa miongoni mwa walio ghaibu. Kwa yakini nitamwadhibu kwa adhabu kali au nitamchinja, au aniletee hoja iliyo wazi.

Suleiman alikuwa na aina ya ndege wanaofuata amri yake, wakiwa wako huru sio ndani ya tundu. Siku moja alipokuwa anawakaguakagua, kama anavyokagua kamanda jeshi lake, akamkosa Hud-hud, na hakuwa amemruhusu kundoka. Akatishia – mbele ya ndege wengine - kumwadhibu; kama kumtia jela n.k. Au kumuua, ikiwa hatakuwa na hoja wazi ya udhuru wa kutoweka kwake.

Basi hakukaa sana mara akasema: Nimegundua usiloligundua.

Haukupita muda wa kutishia Suleiman ila alikuja Hud-hud na akasema: Nimegundua kitu muhimu usichokijua pamoja na upana wa elimu yakona nimekujia na habari za yakini kutoka Sabai.

Hakika nimemkuta mwanamke anayewatawala na amepewa kila kitu na anacho kiti cha enzi kikubwa.

Makusudio ya Sabai (Sheba) ni watu wanaonasibika na Sabai bin Yashjab bin Ya’rub bin Qahtan. Mwanamke (Malkia wa Sheba) alikuwa ni Bilqis bint Sharahil, aliyekuwa mfalme na kurithiwa na binti yake huyo, aliyekuwa akimiliki utajiri na starehe zote.

Alikuwa akikaa kwenye kiti cha hali ya juu na cha thamani, kikiwa kimepambwa na nyoyo za maskini na kupakwa jasho lao na damu zao. Ajabu ni kauli ya baadhi ya wafasiri waliosema kuwa kilikuwa kimeezekwa na kwamba upana wake ulikuwa ni futi 80 za mraba na kimo chake pia ni futi 80.

Nimemkuta yeye na watu wake wanalisujudia jua badala ya Mwenyezi Mungu; na shetani amewapambia vitendo vyao na akawazuilia njia. Kwa hivyo hawakuongoka.

Unaweza kuuliza : Ndege, wanyama na wadudu kwa maumbile yao wanajua chakula chao, kinywaji chao, kinachowadhuru na kinachowanufaisha. Wanajua hivyo na vinginevyo kwa sababu ndio nyenzo za kuishi kwao, kuhifadhi maisha yao na kuendela kuwepo.

Lakini kumtambua mume na mke katika binadamu, kujua kuwa kabila hili ni la wasabai na lile ni la Thamud, kujua hawa wanamuamini Mwenyezi Mungu na wale ni makafiri, haya yote hayalingani na maisha yao kwa umbali wala karibu.

Basi Hud-hud aliwezaje kujua jina la kabila, mwanamke anayewatawala na kwamba wao wanaabudu jua? Sisi wanadamu tu, hatuwezi kutambua baina ya mume na mke katika aina nyingi za ndege, wadudu na wanyama?

Jibu : Aya imethibitisha sifa hizi kwa Hud-hud wa Suleiman tu, jambo ambalo halilazimishi kuthibiti katika ndege wote au kwa Hud-hud wote; kama ambavyo kujua kiingereza kwa mtu fulani hakulazimishi kujua kiingereza kwa watu wote. Ama maarifa ya Hud-hud wa Suleiman kwa aliyoyatolea habari, sisi hatuna tafsiri yake isipokuwa matakwa ya Mwenyezi Mungu.

Kwamba hawamsujudii Mwenyezi Mungu ambaye huyatoa yaliyofichikana katika mbingu na ardhi na huyajua mnayoyaficha na mnayoyadhihirisha.

Makusudio ya yaliyofichikana hapa ni kheri za ulimwengu. Mwenyezi Mungu (s.w.t) huzitoa kwa waja wake kwa sababu zake za kimaumbile; kama mimea inayotoka ardhini kwa sababu ya mvua, kuzaana kwa sababu ya kupandishwa au kwa nyenzo nyingine za kielimu anazozitoa Mwenyezi Mungu kupitia mikononi mwa wataalamu na vifaa vyao.

Sababu na nyenzo zote hizi, Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameziletea ibara ya mkono wa Mungu pale aliposema:

أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا خَلَقْنَا لَهُم مِّمَّا عَمِلَتْ أَيْدِينَا أَنْعَامًا فَهُمْ لَهَا مَالِكُونَ ﴿٧١﴾

“Je, hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyofanya mikono yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki?” (36:71).

Mwenyezi Mungu hapana Mola ila Yeye Mola wa arshi tukufu, ambaye haufananishwi ufalme wake wala ukuu wake na wa yeyote.

قَالَ سَنَنظُرُ أَصَدَقْتَ أَمْ كُنتَ مِنَ الْكَاذِبِينَ ﴿٢٧﴾

27.Akasema: Tutatazama, umesema kweli au uko katika waongo.

اذْهَب بِّكِتَابِي هَـٰذَا فَأَلْقِهْ إِلَيْهِمْ ثُمَّ تَوَلَّ عَنْهُمْ فَانظُرْ مَاذَا يَرْجِعُونَ ﴿٢٨﴾

28. Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha waache na utazame watarejesha nini.”

قَالَتْ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ إِنِّي أُلْقِيَ إِلَيَّ كِتَابٌ كَرِيمٌ ﴿٢٩﴾

29. Akasema: Enyi waheshimiwa! Hakika imeletwa kwangu barua tukufu.

إِنَّهُ مِن سُلَيْمَانَ وَإِنَّهُ بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ ﴿٣٠﴾

Imetoka kwa Suleiman, nayo ni: Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.

أَلَّا تَعْلُوا عَلَيَّ وَأْتُونِي مُسْلِمِينَ ﴿٣١﴾

31. Kwamba msinifanyie jeuri na fikeni kwangu mkiwa waislamu.

قَالَتْ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ أَفْتُونِي فِي أَمْرِي مَا كُنتُ قَاطِعَةً أَمْرًا حَتَّىٰ تَشْهَدُونِ ﴿٣٢﴾

Akasema: Enyi waheshimiwa! Nipeni ushauri katika jambo langu hili, kwani mimi sikati shauri lolote mpaka muhudhurie.

قَالُوا نَحْنُ أُولُو قُوَّةٍ وَأُولُو بَأْسٍ شَدِيدٍ وَالْأَمْرُ إِلَيْكِ فَانظُرِي مَاذَا تَأْمُرِينَ ﴿٣٣﴾

33. Wakasema: Sisi ni wenye nguvu na wakali wa vita, na amri iko kwako, basi tazama nini unaamrisha.

قَالَتْ إِنَّ الْمُلُوكَ إِذَا دَخَلُوا قَرْيَةً أَفْسَدُوهَا وَجَعَلُوا أَعِزَّةَ أَهْلِهَا أَذِلَّةً وَكَذَٰلِكَ يَفْعَلُونَ ﴿٣٤﴾

34. Akasema: Hakika wafalme wanapouingia mji wanauharibu na wanawafanya wale watukufu wake kuwa wanyonge, na hivyo ndivyo watendavyo.

وَإِنِّي مُرْسِلَةٌ إِلَيْهِم بِهَدِيَّةٍ فَنَاظِرَةٌ بِمَ يَرْجِعُ الْمُرْسَلُونَ ﴿٣٥﴾

35. Na mimi ninawapelekea zawadi ningoje watakayorudi nayo wajumbe.

NENDA NA BARUA YANGU HII

Aya 27 – 35

MAANA

Akasema: Tutatazama, umesema kweli au uko katika waongo.

Hud-hud alimpa habari Suleiman kuhusu watu wa Sabai, akamwambia tutachunguza maneno yako tuone kama yana ukweli.

Nenda na barua yangu hii na uwafikishie, kisha waache na utazame watarejesha nini.

Suleiman aliwaandikia barua watu wa Sabai akiwaita kwenye twaa yake na akampatia Hud-hud akamwamabia ifikishe hii kwa njia yoyote, kisha ujitenge nao sehmu ambayo utaweza kujua au kusikia wanasema nini na wanaafikiana nini, kisha urudi uniletee habari.

Akasema: Enyi waheshimiwa! Hakika imeletwa kwangu barua tukufu, imetoka kwa Suleiman, nayo ni: Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu, kwamba msinifanyie jeuri na fikeni kwangu mkiwa waislamu.

Hud-hud alichukua barua na akaitupa mahali kwenye kasri ya malkia kwa namna ambayo inaweza kuonekana bila ya kujulikana aliyeileta, kama linavyojulisha neno ’imeletwa.’ Kisha Hud-hud akajiweka kando kuchunguza harakati za watu na mazungumzo yao; sawa na mwandishi wa habari.

Malkia alipoiona na akajua kilichoandikwa, aliwakusanya mawaziri na washauri, akawaonyesha na akaisifu kwa utukufu, kwa sababu mwenye barua hiyo ni mwenye cheo kikubwa cha heshima.

Bismillah ilikuwa ni sehemu ya barua hiyo ambayo aliifupisha kwa kutoa mwito wa utiifu bila ya utangulizi wala kuzidisha maneno. Hii ndio desturi ya mitume katika barua zao kwenda kwa wafalme. Mtume(s.a.w.w) alikuwa akifupiliza barua zake kwa wafalme kwa kusema: “Silimu utasalimika” baada ya bismillah na Alhamdu.

Akasema: Enyi waheshimiwa! Nipeni ushauri katika jambo langu hili, kwani mimi sikati shauri lolote mpaka muhudhurie.

Nipeni ushauri, maana mimi sipitishi jambo mpaka nipate rai yenu. Hii inaashiria kuwa demokrasia ya serikali ina mizizi yake katika historia ya mbali; kisha ikakua hadi ilivyo hivi sasa.

Wakasema: Sisi ni wenye nguvu na wakali wa vita, na amri iko kwako, basi tazama nini unaamrisha.

Walisema hivi kwa njia ya kujishasha, kutangaza nguvu zao na kumwachia majukumu yote malkia hata kama uamuzi wake utakuwa na mwisho mbaya.

Akasema: Hakika wafalme wanapouingia mji wanauharibu na wanawafanya wale watukufu wake kuwa wanyonge, na hivyo ndivyo watendavyo.

Mfasiri mmoja wa kisasa akifafanua Aya hii anasema: “Inajulikana kuwa ni tabia ya kimaumbile ya wafalme wanapoingia mji wanaeneza ufisadi na wanawaangusha viongozi na kuwafanya ni watu wa chini. Haya ndio mazowea yao wanayoyafanya.”

Ukweli ni kuwa ufisadi unaenea ardhini kwa kiasi cha nguvu za mfisadi, na unazidi kadiri nguvu zao zinavyozidi, wawe wafalme au si wafalme. Aya imewahusu kuwataja wafalme kwa sababu wao wanakuwa na nguvu zaidi kuliko wengine.

Uhakika wa mhalifu unajificha kwenye unyonge wake, na unajitokeza anapokuwa na guvu. Kwa hiyo ni makosa kuuweka uhakika wa mtu anapokuwa mnyonge.

Kuna badhi ya watu tunaowajua ambao walikuwa ni mashuhuri kwa takua wakati walipokuwa hohehahe, lakini mara tu walipopata madaraka wakaandamwa na tuhuma ambazo hazifutiki hata siku zikipita. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe hidaya sisi na wao.

Kwa hiyo inatubainikia kuwa sifa ya ufisadi haihusiki kwa wafalme tu wala si tabia yao ya kimaumbile, vinginevyo ingelikuwa ni muhali kupatikana uadilifu na utengeneo kwao. Isipokuwa hiyo ni tabia ya wahalifu wenye nguvu; ni sawa iwe nguvu ya mali, cheo, akili au utawala na, kidini au kidunia. Wala hakuna wa kumzuia mkosefu mwenye nguvu isipokuwa dini tu.

Imam Ali(a.s) anasema: Mwenye uzowefu wa maisha na uelewa wa mambo anaweza akaona ujanja wa kukwepa amri ya Mwenyeezi Mungu akaachana nao; lakini asiyejilinda (na dini) anaitumia fursa hiyo (Nahjul balagha khutba 41).

Na mimi ninawapelekea zawadi ningoje watakayorudi nayo wajumbe.

Mawaziri na washauri walimwachia malkia amri ya vita au usalama. Kabla ya kuamua chochote aliona kwanza ampelekee Suleiman zawadi ya thamani kubwa, kisha aangalie, je, ataikubali au ataikataa. Akiikubali basi atakuwa anatafuta dunia sio dini. Kwa hiyo ataweza kumtengeneza kwa mali na kama ataikataa na kung’ang’ania kuwa tumwendee tukiwa wanyenyekevu, basi atakua ni katika wenye misingi ya risala na misimamo ya itikadi yao wakijitolea muhanga kwa kila hali. Watu wa namna hiyo haifai kuwapiga vita.

فَلَمَّا جَاءَ سُلَيْمَانَ قَالَ أَتُمِدُّونَنِ بِمَالٍ فَمَا آتَانِيَ اللَّـهُ خَيْرٌ مِّمَّا آتَاكُم بَلْ أَنتُم بِهَدِيَّتِكُمْ تَفْرَحُونَ ﴿٣٦﴾

36. Alipokuja kwa Suleiman, alisema: Hivi nyinyi mnanisaidia kwa mali? Aliyonipa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuliko aliyowapa nyinyi, lakini nyinyi mnaifurahia zawadi yenu.

ارْجِعْ إِلَيْهِمْ فَلَنَأْتِيَنَّهُم بِجُنُودٍ لَّا قِبَلَ لَهُم بِهَا وَلَنُخْرِجَنَّهُم مِّنْهَا أَذِلَّةً وَهُمْ صَاغِرُونَ ﴿٣٧﴾

37. Rejea kwao! Kwa yakini tutawajia na majeshi wasiyoweza kuyakabili na hakika tutawatoa humo na hali wao wamekuwa madhalili na wanyonge.

قَالَ يَا أَيُّهَا الْمَلَأُ أَيُّكُمْ يَأْتِينِي بِعَرْشِهَا قَبْلَ أَن يَأْتُونِي مُسْلِمِينَ ﴿٣٨﴾

38. Akasema: Enyi wakuu wa baraza! Ni nani kati yenu atakayeniletea kiti chake cha enzi kabla hawajanijia nao wamekwisha salimu amri.

قَالَ عِفْرِيتٌ مِّنَ الْجِنِّ أَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَن تَقُومَ مِن مَّقَامِكَ وَإِنِّي عَلَيْهِ لَقَوِيٌّ أَمِينٌ ﴿٣٩﴾

39. Akasema afriti katika majini: Mimi nitakuletea kabla hujainuka mahala pako. Na mimi hakika nina nguvu, mwaminifu.

قَالَ الَّذِي عِندَهُ عِلْمٌ مِّنَ الْكِتَابِ أَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَن يَرْتَدَّ إِلَيْكَ طَرْفُكَ فَلَمَّا رَآهُ مُسْتَقِرًّا عِندَهُ قَالَ هَـٰذَا مِن فَضْلِ رَبِّي لِيَبْلُوَنِي أَأَشْكُرُ أَمْ أَكْفُرُ وَمَن شَكَرَ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ وَمَن كَفَرَ فَإِنَّ رَبِّي غَنِيٌّ كَرِيمٌ ﴿٤٠﴾

40. Akasema mwenye elimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea kabla ya kupepesa jicho lako. Basi alipokiona kimewekwa mbele yake, alisema: Haya ni katika fadhila za Mola wangu, ili anijaribu, nitashukuru au nitakufuru. Na mwenye kushukuru kwa hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake na mwenye kukufuru kwa hakika Mola wangu ni Mkwasi, Mkarimu.

KITI CHA ENZI CHA BILQIS

Aya 36 – 40

MAANA

Alipokuja mjumbe kwa Suleiman, alisema: Hivi nyinyi mnanisaidia kwa mali? Aliyonipa Mwenyezi Mungu ni bora zaidi kuliko aliyowapa nyinyi, lakini nyinyi mnaifurahia zawadi yenu.

Ujumbe wa malkia ulifika kwa Suleiman ukiwa na zawadi ya thamani kubwa. Alipoiona alimwambia yule aliyekuja nayo kuwa mimi ninawaita kwa Mwenyezi Mungu na nyinyi mnanipa mali nami nina mali nyingi kama uonavyo; bali Mwenyezi Mungu amenineemesha kwa makubwa zaidi kuliko mali, ambayo ni: utume, elimu na kuutumia upepo majini na ndege. Hivi mnanikisia kuwa ni katika waabudu mali?

Kisa hiki kinatukumbusha makuraishi, wakati walipomtaka mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) aachane na jambo lake hili, wakamwambia:“Ukiwa, kwa jambo hili, unataka mali basi sisi tutakukusanyia mali mpaka uwe ni tajiri zaidi kuliko sisi, na kama unataka ufalme tutakupa.

Waliposhindwa naye wakakimbilia kwa ami yake Abu Talib ili amkinaishe mwana wa nduguye akubali mali, vinginevyo atapigwa vita. Mtume(s.a.w. w ) akasema maneno yake mashuhuru:“Wallah! Ewe Ami yangu! Lau wataliweka jua kuumeni kwangu na mwezi kushotoni kwangu kwamba niliache jambo hili sitaliacha mpaka alidhihirishe Mwenyezi Mungu au niangamie.”

Rejea kwao! Kwa yakini tutawajia na majeshi wasiyoweza kuyakabili na hakika tutawatoa humo na hali wao wamekuwa madhalili na wanyonge.

Maneno haya anaambiwa kiongozi wa msafara uliokuja na zawadi. Maana yake ni rejea wewe na wenzako na hiyo mliyokuja nayo. Wambie watu wako kuwa mimi nitakuja na jeshi langu la watu majini na ndege ambalo hamtaliweza si nyinyi wala wengene.

Hud-hud alikuwa amemwambia walivyosema: ‘Hakika wafalme wanapouingia mji wanauharibu na wanawafanya wale watukufu wake kuwa wanyonge.’ Kwa hiyo Suleiman akasisitiza kauli ya malkia kwa kusema: ‘Tutawatoa humo na hali wao wamekuwa madhalili na wanyonge.’

Akasema: Enyi wakuu wa baraza! Ni nani kati yenu atakayeniletea kiti chake cha enzi kabla hawajanijia nao wamekwishasalimu amri.

Msafara uliporeja kutoka kwa Suleiman na wakampa habari Malkia kwa waliyoyaona na kuyasikia, aliona hapana budi isipokuwa kusikiliza na kutii. Akaelekea kwa Suleiman pamoja na wapambe wake. Akakiacha kiti cha enzi kikilindwa na askari.

Suleiman alipojua kufika Bilqis alipendelea kumuonyesha miujiza ya kufahamisha utume wake na ukuu wake; na kwamba muujiza huo uwe ni kukichukua kiti chake ambacho ndicho kinachoonyesha enzi yake na umalkia wake. Ndipo akauliza wale waliokuwapo mbele yake, ni nani atakayeniletea?

Akasema afriti katika majini: Mimi nitakuletea kabla hujainuka mahala pako. Na mimi hakika nina nguvu, mwaminifu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimtiishia Suleiman upepo ukienda kwa amri yake. Bila shaka huu ni mujiza. Akamtiisha ndege wakifuata amri yake.

Nao pia ni muujiza. Vile vile Mwenyezi Mungu alimuhusisha na baadhi ya askari binadamu na majini, wakifanya maajabu kulingana na wakati wo. Walikuwa wakiandamana na jeshi la Suleiman, wakisaidiana kumshinda adui; kama wafanyavyo wataalamu wa kiufundi hivi sasa.

Hilo linaashiriwa na matakwa ya Suleiman kwao kuwaletea kiti cha enzi cha Bilqis katika muda mchache na hali anajua kuwa kiko masafa ya mbali sana. Mmoja wa majini akamwambia nitakuletea kikiwa salama, kama kilivyo ukiwa wewe umekaa hapa.

Lakini akasema mwenye elimu ya Kitabu: Mimi nitakuletea kabla ya kupepesa jicho lako.

Ikawa ushindi ni wa huyu ambapo, kwa uweza wa elimu alio nao, aliweza kukileta kiti wakati uliotakiwa.

Haya ndiyo yaliyofahamishwa na dhahiri ya Aya. Ama maswali ya kuwa ni nani huyo aliyekuwa na elimu ya kitabu? Je, alikuwa ni Malaika, Khidhr au mja mwema katika binadamu aliyeitwa Asif bin Barkhiya Na kwamba je yeye alikuwa akijua jina kuu la Mwenyezi Mungu au ni elimu gani hiyo aliyoitumia?

Maswali yote haya na mengineyo mengi, jibu lake liko kwa Mola wangu. Kwa sababu Aya haikuweka wazi hilo, wala hakuna Hadith sahih iliyothibiti.

Uwezekano wa karibu, tunaoweza kusema ni kuwa yeye hakuwa katika majini, kwa sababu alimzidi jini Afrit, kama ilivyoweka wazi Aya, kwamba yeye alikileta kiti kabla ya kupepesa jicho. Miujiza inayodhihiri kwa mitume, pia inadhihiri kwa wale ambao wamechaguliwa na mitume kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

La muhimu kujua, katika tukio hili, ni kwamba Bilqis aliyekuwa na madaraka makubwa na neema, alimnyenyekea Suleiman.

Basi alipokiona kimewekwa mbele yake, alisema: Haya ni katika fadhila za Mola wangu, ili anijaribu, nitashukuru au nitakufuru.

Makusudio ya kukufuru hapa ni kukufuru neema, sio kumkufuru Mwenyezi Mungu. Suleiman hawezi kuzikufuru neema za Mola wake, kwa sababu yeye ni maasum. Alisema haya kama utangulizi wa kusema:

Na mwenye kushukuru kwa hakika anashukuru kwa manufaa ya nafsi yake na mwenye kukufuru kwa hakika Mola wangu ni Mkwasi, Mkarimu.

Katika maana ya Aya hii ni ile isemayo:

إِنْ أَحْسَنتُمْ أَحْسَنتُمْ لِأَنفُسِكُمْ وَإِنْ أَسَأْتُمْ فَلَهَا ﴿٧﴾

“Mkifanya uzuri mnajifanyia wenyewe na mkifanya ubaya mnajifanyia wenyewe.” Juz. 15 (17:7).


11

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA

قَالَ نَكِّرُوا لَهَا عَرْشَهَا نَنظُرْ أَتَهْتَدِي أَمْ تَكُونُ مِنَ الَّذِينَ لَا يَهْتَدُونَ ﴿٤١﴾

41. Akasema: Kibadilini kiti chake cha enzi, tuone ataongoka au atakuwa miongoni mwa wasioongoka?

فَلَمَّا جَاءَتْ قِيلَ أَهَـٰكَذَا عَرْشُكِ قَالَتْ كَأَنَّهُ هُوَ وَأُوتِينَا الْعِلْمَ مِن قَبْلِهَا وَكُنَّا مُسْلِمِينَ ﴿٤٢﴾

42. Basi alipofika akaambiwa: Je kiti chako cha enzi ni kama hiki? Akasema: Kama kwamba ndicho hicho. Nasi tulipewa ilimu kabla yake na tukawa waislamu.

وَصَدَّهَا مَا كَانَت تَّعْبُدُ مِن دُونِ اللَّـهِ إِنَّهَا كَانَتْ مِن قَوْمٍ كَافِرِينَ ﴿٤٣﴾

43. Na yale aliyokuwa akiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yalimzuilia. Hakika yeye alikuwa katika kaumu ya makafiri.

قِيلَ لَهَا ادْخُلِي الصَّرْحَ فَلَمَّا رَأَتْهُ حَسِبَتْهُ لُجَّةً وَكَشَفَتْ عَن سَاقَيْهَا قَالَ إِنَّهُ صَرْحٌ مُّمَرَّدٌ مِّن قَوَارِيرَ قَالَتْ رَبِّ إِنِّي ظَلَمْتُ نَفْسِي وَأَسْلَمْتُ مَعَ سُلَيْمَانَ لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٤٤﴾

44. Akaambiwa liingie jumba. Alipoliona alidhani ni lindi la maji, akapandisha nguo mpaka kwenye miundi yake. Akasema: Hakika limesakafiwa kwa vioo. Akasema: Mola wangu! Hakika nimedhulu- mu nafsi yangu na najisalimisha pamoja na Suleiman kwa Mola wa walimwengu.

KIBADILINI KITI CHAKE

Aya 41 – 44

MAANA

Akasema: Kibadilini kiti chake cha enzi, tuone ataongoka au atakuwa miongoni mwa wasioongoka?”

Suleiman aliwaambia baadhi ya watu wake: “Badilisheni kitu katika kiti chake cha enzi, tuone atakitambua au hatakitambua.”

Basi alipofika akaambiwa: Je kiti chako cha enzi ni kama hiki?

Walikibadilisha kiti kisha wakamuuliza.

Akasema: Kama kwamba ndicho hicho.

Hakukanusha kwa sababu ya kufanana sana nacho, wala hakukubali kwa sababu alikiacha kwenye kasri yake kikiwa na ulinzi mkali. Hivi ndivyo walivyo wanasiasa na viongozi, wanachunga sana maneno yao na majibu yao.

Nasi tulipewa ilimu kabla yake na tukawa waislamu.

Haya ni maneno ya Suleiman na watu wake. Maana ni kuwa waliijua haki kabla ya Bilqis.

Na yale aliyokuwa akiyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yalimzuilia. Hakika yeye alikuwa katika kaumu ya makafiri.

Yaani kilichomzuia Bilqis kuijua haki na imani ni ile shirki yake na kuabudu kwake jua badala ya Mwenyzi Mungu.

Akaambiwa liingie jumba. Alipoliona alidhani ni lindi la maji, akapandisha nguo mpaka kwenye miundi yake. Akasema: “Hakika limesakafiwa kwa vioo.

Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa Suleiman alikuwa na kasri lililosakafiwa kwa vioo na kwamba maji yalikuwa yakipita chini yake. Bilqis aliingia kwenye kasr, hakutambua kioo kutokana na usafi wake.

Akasema: Mola wangu! Hakika nimedhulumu nafsi yangu na najisalimisha pamoja na Suleiman kwa Mola wa walimwengu.

Alidhulumu nafsi yake kwa ukafiri, kisha akatubia, akasilimu na akaufanya vizuri uislmu wake.

وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا إِلَىٰ ثَمُودَ أَخَاهُمْ صَالِحًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ فَإِذَا هُمْ فَرِيقَانِ يَخْتَصِمُونَ ﴿٤٥﴾

45. Na hakika tuliwapelekea Thamud ndugu yao Swaleh; kwamba muabuduni Mwenyezi Mungu. Basi mara yakawa makundi mawili yakihasimiana.

قَالَ يَا قَوْمِ لِمَ تَسْتَعْجِلُونَ بِالسَّيِّئَةِ قَبْلَ الْحَسَنَةِ لَوْلَا تَسْتَغْفِرُونَ اللَّـهَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٤٦﴾

46. Akasema: Enyi watu wangu! Kwa nini mnahimiza uovu kabla ya wema? Mbona hamuombi maghufira kwa Mwenyezi Mungu mpate kurehemiwa?

قَالُوا اطَّيَّرْنَا بِكَ وَبِمَن مَّعَكَ قَالَ طَائِرُكُمْ عِندَ اللَّـهِ بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ تُفْتَنُونَ ﴿٤٧﴾

47. Wakasema: Tuna kisirani nawe na wale walio pamoja nawe. Akasema: Kisirani chenu kiko kwa Mwenyezi Mungu. Lakini nyinyi ni watu mnaojaribiwa.

وَكَانَ فِي الْمَدِينَةِ تِسْعَةُ رَهْطٍ يُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ وَلَا يُصْلِحُونَ ﴿٤٨﴾

48. Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika ardhi wala hawafanyi la maslahi.

قَالُوا تَقَاسَمُوا بِاللَّـهِ لَنُبَيِّتَنَّهُ وَأَهْلَهُ ثُمَّ لَنَقُولَنَّ لِوَلِيِّهِ مَا شَهِدْنَا مَهْلِكَ أَهْلِهِ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ ﴿٤٩﴾

49. Wakasema: Apishaneni kwa Mwenyezi Mungu, tutamshambulia usiku yeye na ahli zake, kisha tutamwambia walii wake: Sisi hatukushuhudia maangamizi ya watu wake, na sisi bila shaka tunasema kweli.

وَمَكَرُوا مَكْرًا وَمَكَرْنَا مَكْرًا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٥٠﴾

50. Na wakapanga hila nasi tukapanga hila na wao hawatambui.

فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ مَكْرِهِمْ أَنَّا دَمَّرْنَاهُمْ وَقَوْمَهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٥١﴾

51. Basi angalia ulivyokuwa mwisho wa hila yao, ya kwamba tuliwaangamiza wao na watu wao wote.

فَتِلْكَ بُيُوتُهُمْ خَاوِيَةً بِمَا ظَلَمُوا إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَعْلَمُونَ ﴿٥٢﴾

52. Basi hizo nyumba zao ni tupu kwa sababu ya walivyodhulumu. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaojua.

وَأَنجَيْنَا الَّذِينَ آمَنُوا وَكَانُوا يَتَّقُونَ ﴿٥٣﴾

Na tukawaokoa wale walioamini na waliokuwa na takua.

SWALEH

Aya 45 –53

MAANA

Na hakika tuliwapelekea Thamud ndugu yao Swaleh, kwamba muabuduni Mwenyezi Mungu.

Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:73) na Juz. 12 (11:61).

Basi mara wakawa makundi mawili wakihasimiana.

Kundi moja liliamini haki na kundi jingine likaikadhibisha, kwa sababu inagongana na manufaa yao. Na hii hasa ndio sababu ya kuhasimiana; vinginevyo wangelisema, mna dini yenu na sisi tuna dini yetu

Akasema: Enyi watu wangu! Kwa nini mnahimiza uovu kabla ya wema? Mbona hamuombi maghufira kwa Mwenyezi Mungu mpate kurehemiwa?

Makusudio ya uovu hapa ni adhabu; na wema ni rehema.

Swaleh aliwaonya na adhabu wakadhibishaji kama watang’ang’ania upotevu na inadi yao. Wakasema kwa dharau kuwa tuletee unayotuahidi ikiwa wewe ni mkweli; kama ilivyoelezwa katika Juz. 8 (7:77).

Lakini bado akawajibu kwa upole, kuwa kwa nini mnaharakisha nakama ya Mwenyezi Mungu na hali Yeye amewapa muda mrefu ili mrejee kutoka kwenye upotevu wenu? Basi heri yenu ni kutubia na kutaka rehema kutoka kwake kwani Yeye ni mkarimu mwingi wa maghufira na mwenye kurehemu.

Wakasema: Tuna kisirani nawe na wale walio pamoja nawe.

Bada ya Swaleh kuwalingania kwa Mola wao na wakapinga, walipatwa na maradhi na wakaanza kumwambia kuwa umetutia dege wewe na wale walio pamoja nawe.

Akasema: Kisirani chenu kiko kwa Mwenyezi Mungu.

Hakika balaa liliowashukia ni kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu ambaye kwake zinakomea sababu zote. Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7:131). Mtume(s.a.w.w) alikuwa akipenda mdomo wa kheri, kwa sababu ndani yake mna kumtegemea Mwenyezi Mungu na alikuwa akichukia kisirani, kwa sababu ndani yake mna kutarajia balaa.

Kuna Hadith ise- mayo: “Ukiona kisirani endelea, ukiwa na hasadi usiifanye na ukidhania usitafute uhakika.” Yaani ukiona jambo lina kisirani endelea nalo, na ukiona kijicho basi kibakie moyoni tu usidhihirishe na ukiwa na dhana mbaya basi usitafute uhakika.

Lakini nyinyi ni watu mnaojaribiwa.

Manajribiwa kwa mazuri na mabaya, ili vifichuke vitendo vyenu ambavyo mtastahikia thawabu na adhabu.

Na walikuwamo mjini watu tisa wakifanya ufisadi katika ardhi wala hawafanyi la maslahi.

Walikuwako wapenda anasa wakijifakharisha kwa watu kwa utajiri wao na wakiufanya ni nyenzo ya kuwakandamiza na kufanya ufisadi katika nchi; wakimzuia kila kiongozi mwenye kutaka kuleta maslahi ya watu na anayependa heri.

Na hakukuwa na nafuu yoyote, bali kila jambo lao lilikuwa ni baya. Haya ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Wala hawafanyi maslahi.

Wakasema: Apishaneni kwa Mwenyezi Mungu, tutamshambulia usiku yeye na ahli zake, kisha tutamwambia walii wake: Sisi hatukushuhudia maangamizi ya watu wake na sisi bila shaka tunasema kweli.

Waliosema hivyo ni wale watu tisa wakimkusudia Nabii Swaleh. Waliambiana kuwa waape kumshambulia Swaleh na watu wake usiku, kisha wawaambie ndugu zake kuwa wao sio waliomuua na wala hawamjui aliyemuua.

Na wakapanga hila nasi tukapanga hila na wao hawatambui.

Mipango ya wale tisa ni njama za kumshambulia Swaleh na watu wake usiku; na mipango ya Mwenyezi Mungu ni kuwawahi kuwaangamiza kabla ya kumfikia Swaleh bila ya wao kutambua. Tazama Juz. 3 (3: 54) kifungu “Mwenyezi Mungu ni mbora wa wapanga hila.”

Basi angalia ulivyokuwa mwisho wa hila yao, ya kwamba tuliwaangamiza wao na watu wao wote.

Walitaka kumwangamiza Swaleh, lakini Mwenyezi Mungu akawaangamiza wao. Katika hilo kuna mazingatio kwa kila mwenye kumpangia njama mwingine.

Basi hizo nyumba zao ni tupu kwa sababu ya walivyodhulumu nafsi zao.

Mwenyezi Mungu aliwahadharisha akawapa muda, lakini wakang’ang’ania ufisadi na upotevu.

Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaojua.

Makusudio ya kujua hapa ni kule kunakokwenda pamoja na matendo na mazingatio. Ama kujua tu bila ya matendo basi ni afadhali ujinga. Kwa sababu kutaleta maangamizi na balaa.

Na tukawaokoa wale walioamini na waliokuwa na takua.

Hii ni desturi ya Qur’an; inapowataja madhalimu na adhabu yao inafuatishia kuwataja wenye takua na thawabu zao. Makusudio ni kuhadharisha na kupendekeza.

وَلُوطًا إِذْ قَالَ لِقَوْمِهِ أَتَأْتُونَ الْفَاحِشَةَ وَأَنتُمْ تُبْصِرُونَ ﴿٥٤﴾

54. Na Lut alipowaambia watu wake: Je mnafanya uchafu nanyi mnaona?

أَئِنَّكُمْ لَتَأْتُونَ الرِّجَالَ شَهْوَةً مِّن دُونِ النِّسَاءِ بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ تَجْهَلُونَ ﴿٥٥﴾

55. Hakika nyinyi mnawaendea wanaume kwa matamanio badala ya wanawake! Bali nyinyi ni watu mnaofanya ujinga.

فَمَا كَانَ جَوَابَ قَوْمِهِ إِلَّا أَن قَالُوا أَخْرِجُوا آلَ لُوطٍ مِّن قَرْيَتِكُمْ إِنَّهُمْ أُنَاسٌ يَتَطَهَّرُونَ ﴿٥٦﴾

56. Na halikuwa jibu la watu wake isipokuwa kusema: Watoeni mjini mwenu, maana hao ni watu wanaojitakasa.

فَأَنجَيْنَاهُ وَأَهْلَهُ إِلَّا امْرَأَتَهُ قَدَّرْنَاهَا مِنَ الْغَابِرِينَ ﴿٥٧﴾

57. Tukamwokoa yeye na ahli zake isipokuwa mkewe, alikuwa miongoni mwa waliobakia nyuma.

وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِم مَّطَرًا فَسَاءَ مَطَرُ الْمُنذَرِينَ ﴿٥٨﴾

58. Na tukawamiminia mvua, ni mbaya mno mvua hiyo ya wale walioonywa.

LUT

Aya 54 – 58

MAANA

Umetangulia mfano wa Aya 54 - 58 katika Juz. 8 (7:80 – 84). Wala hakuna tofauti isipokuwa katika baadhi ya ibara zifuatazo:

Kule Mwenyezi Mungu amesema: Je, mnafanya uchafu ambao hajawatangulia yeyote kwa hilo katika walimwengu? Na hapa anasema:

Je, mnafanya uchafu nanyi mnaona?

Maneno yote hayo ni ya kutahayariza. Kule amesema: “Bali nyinyi ni watu warukao mipaka” na hapa akasema:

Bali nyinyi ni watu mnaofanya ujinga.

Ujinga pi ni katika aina ya kuruka mipaka. Kule amesema: “Na tukawamiminia mvua,basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa waovu.” Na hapa amesema:

Na tukawamiminia mvua, ni mbaya mno mvua hiyo ya wale walioonywa.

Mifano hii ni mingi katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Anasimulia maneno ya mitume kwa matamshi mengine katika Aya ya pili na pia katika Aya ya tatu anasimulia kwa matamshi mengine. Hii inafahamisha kuwa mtu anaweza kunukuu maneno ya watu wengine neno kwa neno au kwa maneno mengine yenye maana sawa, lakini kwa sharti la kutopunguza au kuongeza chumvi.

قُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ وَسَلَامٌ عَلَىٰ عِبَادِهِ الَّذِينَ اصْطَفَىٰ آللَّـهُ خَيْرٌ أَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٥٩﴾

59. Sema: Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu (alhamdu-lillah) na amani ishuke juu ya waja wake aliowateua. Je Mwenyezi Mungu ni bora au wale wanaowashirikisha naye?

AMANI JUU YA WAJA ALIOWATEUA

Aya 59

REHEMA NA AMANI KWA WENYE TAKUA

Sema: Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu (Alhamdu lillah) na amani ishuke juu ya waja wake aliowateua.

Aya hii imetangulia mwisho wa Juzuu iliyopita. Tumeileta hapa kwa vile maelezo yake yanaungana na hapa.

Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja baadhi ya Mitume na baadhi ya miujiza aliyowahusisha nayo, sasa anamwamrisha Mtume wake Muhammad(s.a.w.w) kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema alizomhusisha nazo na kuwatakia amani mitume wote ambao amewateua kwa ujumbe wake. Amekutanisha kuwatakia amani pamoja na sifa njema kwake, kutanabahisha daraja yao na ukuu wa vyeo vyao.

Kila mwenye kumcha Mwenyezi Mungu na akazifanyia kazi Sunna za Mtume wa Mweneyzi Mungu inafaa kumuombe rehema na amani, awe hai au maiti, Mtume au asiyekuwa Mtume; hasa akiwa ni katika watu wa nyumba ya Muhammad(s.a.w.w) na akapigana jihadi kwa ajili ya Uisalmu na kuenea mwito wake. Mweneyezi Mungu (s.w.t) anasema: malaika wake ndio wanaowarehemu.” (33:43).

“Yeye na Katika Sahih Bukhari na vinginevyo, imeelezwa: “Waliuliza: “Vipi tukutakie rehema ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu?” Akasema: “Semeni, Allahumma swalli ala Muhammadi wwa ala ali Muhammad. Kama swal-layta ala Ibrahima wa ala ali Ibrahima. Wa barik ala Muhammadi wwa ala ali Muhammad. Kama barakta ala Ibrahima wa ala ali Ibrahim. Innaka hamidu mmajid

(Ewe Mwenyezi Mungu, mrehemu Muhammad na kizazi cha Muhammad, kama ulivyomrehemu Ibrahim na kizazi cha Ibrahim; na umbariki Muhammad na kizazi cha Muhammad, kama ulivyombariki Ibrahim na kizazi cha Ibrahim. Hakika wewe ni Mwenye kusifiwa Mwenye kutukuzwa.

Imekuwa ni desturi ya Waislamu, tangu wakati wa Mtume mtukufu(s.a.w.w) , kufungua vitabu vyao na khutba zao kwa Bismillah, kumshukuru Mwenyezi Mungu na kumtakia rehema Muhammad na wanaokwenda mwenendo wake katika ahli baiti wake na swahaba zake. Chimbuko la hilo ni Aya hii.

Je Mwenyezi Mungu ni bora au wale wanaowashirikisha naye?

Maelezo ya sehemu hii yatakuja kwenye juzuu inayofuatia, kwa vile yanaungana na huko.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA JUZUU YA KUMI NA TISA


YALIYOMO

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA 1

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA 1

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA 1

IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED 1

IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU 1

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI 1

MAKOSA YA CHAPA 2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA 3

HAKUNA FURAHA KWA WAKOSEFU 3

MAANA 3

WAMEIFANYA QUR’AN NI MAHAME 7

MAANA 7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA 10

ATI HUYU NDIYE MTUME? 10

MAANA 10

BAINA YA ISA NA MUHAMMAD 10

WAMEPOTEA ZAIDI KULIKO WANYAMA 12

DHAHIRI YA MAUMBILE 13

MAANA 13

QUR’AN NA IDHAA 15

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA 17

KAFIRI NI MSADIZI WA MPINZANI WA MOLA WAKE 17

MAANA 17

WAJA WA MWINGI WA REHEMA 20

MAANA 21

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA 25

HUENDA UKAANGAMIZA NAFSI YAKO 25

MAANA 25

MUSA 27

MAANA 27

MAJIBIZANO BAINA YA MUSA NA FIRAUNI 30

MAANA 30

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA 33

WALIFIKA WACHAWI 34

MAANA 34

KUGHARIKI FAIRAUNI NA WATU WAKE 35

MAANA 35

IBRAHIM 38

MAANA 39

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA 41

PEPO KWA WENYE TAKUA NA MOTO KWA WAPOTEVU 41

MAANA 42

NUH 43

MAANA 43

Hud 46

MAANA 46

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA 48

SWALEH 49

MAANA 49

LUT 51

MAANA 51

SHUA’YB 53

MAANA 53

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA 55

AMEITERMSHA ROHO MWAMINIFU 56

MAANA 56

WAONYE JAMAA ZAKO WA KARIBU 59

MAANA 59

WASHAIRI WANAFUATWA NA WAPOTOFU 61

MAANA 61

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA 64

MWONGOZO NA BISHARA KWA WAUMINI 64

MAANA 64

MUSA 66

MAANA 66

SULEIMAN 68

MAANA 68

SOMO NA MAZINGATIO KATIKA CHUNGU WA SULEIMAN 70

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA 73

MBONA SIMWONI HUD-HUD 73

MAANA 73

NENDA NA BARUA YANGU HII 75

MAANA 75

KITI CHA ENZI CHA BILQIS 77

MAANA 78

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA TISA 80

KIBADILINI KITI CHAKE 80

MAANA 80

SWALEH 82

MAANA 82

LUT 83

MAANA 84

AMANI JUU YA WAJA ALIOWATEUA 84

REHEMA NA AMANI KWA WENYE TAKUA 84

SHARTI YA KUCHAPA 85

MWISHO WA JUZUU YA KUMI NA TISA 85

YALIYOMO 86



[1] . Tazama A’yanushia cha Amin Juz,3 uk. 110 chapa ya 1960 na Dalailu-sswidq cha Mudhwaffar Juz. 2 Uk: 232 chapa ya 1954.

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KUMI NA TISA Juzuu ١٩

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASIF JUZUU YA KUMI NA TISA

Mwandishi: Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
: HASANI MWALUPA
Kundi: Qurani tukufu
Kurasa: 14