TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA- Juzuu 9
Kuweka vikundi Qurani tukufu
mwandishi Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya
Lugha ya kitabu سواحیلی
mwaka wa kuchapisha 1404

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA

IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED

IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI

Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.

Kama lilivyo jina la Tafsiri yenyewe ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo. Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.

Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.

Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea, hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho 'Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah' (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka hivi karibuni Inshaallah).

Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.

Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasyansi kama kina Enstein, Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.

Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.

Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.

Mwisho: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.

MAKOSA YA CHAPA

Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa, Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.

Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146). Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua), Mfano wa makosa haya hausameheki.

Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa "Fawqahum ila yawmil qiyama” badala ya “Fawqahum yawamal qiyama",Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.

Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu jabal amail 'Makosa ya chapa.'

Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: " Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"

Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.

Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa, kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.

Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu."

Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubali- ayale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).

MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH


1

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

Mwendelezo Wa Sura Ya Saba: Surat Al-A’raf

قَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ اسْتَكْبَرُوا مِن قَوْمِهِ لَنُخْرِجَنَّكَ يَا شُعَيْبُ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَكَ مِن قَرْيَتِنَا أَوْ لَتَعُودُنَّ فِي مِلَّتِنَا قَالَ أَوَلَوْ كُنَّا كَارِهِينَ ﴿٨٨﴾

88. Wakuu waliotakabari katika kaumu yake wakasema: Ewe Shuaib! Tutakutoa wewe na wale walioamini pamoja nawe katika mji wetu au mrejee katika mila yetu. Akasema: Je, ingawa tunaichukia?

قَدِ افْتَرَيْنَا عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا إِنْ عُدْنَا فِي مِلَّتِكُم بَعْدَ إِذْ نَجَّانَا اللَّـهُ مِنْهَا وَمَا يَكُونُ لَنَا أَن نَّعُودَ فِيهَا إِلَّا أَن يَشَاءَ اللَّـهُ رَبُّنَا وَسِعَ رَبُّنَا كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا عَلَى اللَّـهِ تَوَكَّلْنَا رَبَّنَا افْتَحْ بَيْنَنَا وَبَيْنَ قَوْمِنَا بِالْحَقِّ وَأَنتَ خَيْرُ الْفَاتِحِينَ ﴿٨٩﴾

89. Hakika tutakuwa tumemzulia Mwenyezi Mungu uwongo ikiwa tutarudi katika mila yenu baada ya kwisha kutuokoa nayo Mwenyezi Mungu, Wala haiwi kwetu kuirudia mpaka akipenda Mwenyezi Mola wetu. Ujuzi wa Mola wetu umeenea katika kila kitu, Kwa Mwenyezi Mungu tunategemea. Mola wetu! Hukumu baina yetu na baina ya kaumu yetu kwa haki, nawe ndiwe bora wa wenye kuhukumu.

TUTAKUTOA EWE SHUAIB

Aya 88 – 89

MAANA

Wakuu waliotakabari katika kaumu yake wakasema: Ewe Shuaib! Tutakutoa wewe na wale walioamini pamoja nawe katika mji wetu au mrejee katika mila yetu.

Tumetangulia kueleza katika Juz.8, kwamba Shuaib aliwataka makafiri kuishi kwa amani na wale walioamini na kumwachia hiyari anayetaka kuingia dini anayotaka. Lakini makafiri wakakataa mwito wake na wakamuhiyarisha mambo mawili tu: Ama atoke yeye na wale walioamini mjini mwao, au wale walioamini warudie ukafiri, na yeye arudie msimamo wake wa kwanza, kabla ya utume, asiwe wa kuunga mkono dini yao wala kuipinga. Kwa maneno mengine ni kuwa hali irudie kama ilivyokuwa kabla ya Utume.

Akasema: Je, ingawa tunaichukia?

Hiyo ndiyo mantiki ya mwenye kuchunga haki mwenye ikhlasi, hamchukii yeyote kwa analolichukia, wala hataki yeyote amchukue kwenye lile asilolitaka. Kisha je, inawezekana imani kwa kulazimishwa? Je, Mu’min wa kweli dini yake na itikadi yake inaathirika kwa kukaa katika mji?

Hakika tutakuwa tumemzulia Mwenyezi Mungu uwongo ikiwa tutarudi katika mila yenu baada ya kwisha kutuokoa nayo Mwenyezi Mungu.

Washirikina walimtaka Shuaib(a.s) artadi awe kwenye shirk. Akawaambia, kurtadi ni kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo; na mwisho wa kumzulia Mwenyezi Mungu ni balaa na adhabu; na Mwenyezi Mungu amekwisha tuokoa nayo, sasa vipi tumzulie? Ama kuwa murtadi ni kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo ni wazi, kwa sababu maana yake ni kuwa kumshirikisha Mwenyezi Mungu ni bora kwake kuliko kumwamini.

Wala haiwi kwetu kuirudia mpaka akipenda Mwenyezi Mola wetu.

Dhamir ya ‘kuirudia’ ni ya mila ya ukafiri na shirk. Sharti la kupenda kwa Mwenyezi Mungu hapa ni sharti la muhali (lisilowezekana). Kwa sababu Mwenyezi Mungu hapendi shirki na ukafiri, ni sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya ya 40 ya Sura hii:“Wala hawataingia peponi mpaka ngamia apite kwenye tundu ya sindano.”

Ujuzi wa Mola wetu umeenea katika kila kitu.

Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz 7 (6:80).

Kwa Mwenyezi Mungu tunategemea.

Na mwenye kumtegemea Mwenyezi Mungu haogopi vitisho wala makamiano; Kwa sababu anajua kwa yakini kwamba kiumbe hadhuru wala kunufaisha.

Mola wetu! Hukumu baina yetu na baina ya kaumu yetu kwa haki, nawe ndiye bora wa wenye kuhukumu.

Baada ya Shuaib kukata tamaa nao na kuona kung’ang’ania kwao ukafiri, alikimbia kwa Mwenyezi Mungu na akanyenyekea kwake ahukumu baina yake na waliokufuru katika watu wake. Kwa sababu Yeye Mwenyezi Mungu ndio rejea ya nguvu na uadilifu.

وَقَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَوْمِهِ لَئِنِ اتَّبَعْتُمْ شُعَيْبًا إِنَّكُمْ إِذًا لَّخَاسِرُونَ ﴿٩٠﴾

90. Na wakuu waliokufuru katika kaumu yake wakasema: Kama nyinyi mkimfuata Shuaib, hapo hakika mtakuwa wenye hasara.

فَأَخَذَتْهُمُ الرَّجْفَةُ فَأَصْبَحُوا فِي دَارِهِمْ جَاثِمِينَ ﴿٩١﴾

91. Ukawanyakua mtetemeko wakaamkia majumbani mwao wamejifudikiza.

الَّذِينَ كَذَّبُوا شُعَيْبًا كَأَن لَّمْ يَغْنَوْا فِيهَا الَّذِينَ كَذَّبُوا شُعَيْبًا كَانُوا هُمُ الْخَاسِرِينَ ﴿٩٢﴾

92. Wale waliomkadhibisha Shuaib wakawa kama kwamba hawakuwako. Wale waliomkadhibisha Shuaib ndiyo wenye hasara.

فَتَوَلَّىٰ عَنْهُمْ وَقَالَ يَا قَوْمِ لَقَدْ أَبْلَغْتُكُمْ رِسَالَاتِ رَبِّي وَنَصَحْتُ لَكُمْ فَكَيْفَ آسَىٰ عَلَىٰ قَوْمٍ كَافِرِينَ ﴿٩٣﴾

93. Basi (Shuaib) akaachana nao na akasema: Enyi watu wangu! Kwa hakika nimewafikishia ujumbe wa Mola wangu na nikawanasihi, basi vipi nihuzunike juu ya watu makafiri.

MKIMFUATA SHUAIB

Aya 90 – 93

MAANA

Na wakuu waliokufuru katika kaumu yake wakasema: Kama nyinyi mkimfuata Shuaib, hapo hakika mtakuwa wenye hasara.

Washirikina kwanza walimkabili Shuaib, mwenye mwito, walimtisha na kumkamia. Walipokata tamaa naye waliwageukia wale waliomuamini wakijaribu kuwafitini na dini yao, wakasema miongoni mwa waliyoyasema: “Nyinyi mtakuwa wenye hasara mkifuata Shuaib.” Hii ndiyo desturi ya asiye na hoja ila kupoteza tu.

Ukawanyakua mtetemeko wakaamkia majumbani mwao wamejifudikiza.

Hili ndilo jibu sahihi kwa mpinzani na akakataa ila upotevu. Imetangulia Aya hii kwa herufi. Aya ya 78, ya Sura hii.

Wale waliomkadhibisha Shuaib wakawa kama kwamba hawakuwako.

Iliwajia adhabu kwao na kwenye majumba yao na athari zao zote, kama kwamba maisha haya hawakuyajua nayo yamewajua, Kila mtu atalipwa alilofanya sasa au baadaye.

Wale waliomkadhibisha Shuaib ndiyo wenye hasara.

Washirikina waliwaambia wale walioamini: nyinyi mtakuwa kwenye hasara, lakini wao mwisho ndio waliokuwa wenye hasara na maangamizi na waumini wakafaidika na kuokoka.

Mwenye akili hawezi kumwambia mwenye kiburi ‘Pongezi’ na kumwambia mnyonge ‘Ole wako’ kwa sababu zama zinaficha na kuleta mambo ghafla. Na mambo huzingatiwa kwa mwisho wake.

Imekaririka jumla “wale waliomkadhibisha Shuaib” kwa kutilia mkazo hasara yao na maangamizi yao.

Basi (Shuaib) akaachana nao na akasema: Enyi watu wangu! Kwa hakika nimewafikishia ujumbe wa Mola wangu na nikawanasihi, basi vipi nihuzunike juu ya watu makafiri.

Vipi nihuzunike na yule aliyejiangamiza mwenyewe kwa kung’ang’ania kumkufuru Mwenyezi Mungu, vitabu vyake na Mitume yake; na kumfanyia stizai aliyemwamini na kufuata njia yake ya sawa. Umetangulia mfano wake katika Aya 79 katika Sura hii.

وَمَا أَرْسَلْنَا فِي قَرْيَةٍ مِّن نَّبِيٍّ إِلَّا أَخَذْنَا أَهْلَهَا بِالْبَأْسَاءِ وَالضَّرَّاءِ لَعَلَّهُمْ يَضَّرَّعُونَ ﴿٩٤﴾

94. Na hatukumtuma Nabii yeyote katika mji wowote isipokuwa huwapatiliza watu wake kwa tabu na mashaka ili wapate kunyenyekea.

ثُمَّ بَدَّلْنَا مَكَانَ السَّيِّئَةِ الْحَسَنَةَ حَتَّىٰ عَفَوا وَّقَالُوا قَدْ مَسَّ آبَاءَنَا الضَّرَّاءُ وَالسَّرَّاءُ فَأَخَذْنَاهُم بَغْتَةً وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٩٥﴾

95. Kisha tukabadilisha mahali pa ubaya kwa wema, hata wakazidi na wakasema: Tabu na raha ziliwafikia baba zetu. Basi tuliwaadhibu kwa ghafla hali hawatambui.

HATUKUMLETA NABII YOYOTE KATIKA MJI

Aya 94 – 95

MAANA

Na hatukumtuma Nabii yeyote katika mji wowote isipokuwa huwap- atiliza watu wake kwa tabu na mashaka ili wapate kunyenyekea.

Makusudio ya mji ni ule ambao aghlabu hukaliwa na viongozi.

Katika Aya zilizotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) maangamivu yaliyowafikia wakadhibishaji katika watu wa Nuh, Hud, Swaleh, Lut, na Shuaib na mwisho wao ulio na mazingatio na mawaidha; na kwamba kheri ndio mwisho wa wenye kumcha Mwenyezi Mungu, na uovu uliwarudia wabatilifu.

Katika Aya hii anabainisha kuwa yaliyowapitia watu wa Mitume hiyo hayahusiki na wao tu peke yao, lakini ni desturi ya Mwenyezi Mungu, inawapitia kila watu wanaomkadhibisha Mtume wao. Anawaadhibu Mwenyezi Mungu kwa shida na mashaka katika nafsi zao, miili yao na mali zao. Si kwa lolote ila ni kwa ajili wawaidhike na wazingatie wao na watakaokuja baada yao.

Kisha tukabadilisha mahali pa ubaya kwa wema, hata wakazidi na wakasema: Tabu na raha ziliwafikia baba zetu.

Makusudio ya ubaya hapa ni dhiki na uzito na wema ni wasaa na wepesi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwajaribu kwa dhiki na shida ili wawaidhike na kwa wasaa na afya ili washukuru lakini ni wachache wanao waidhika na ni wachache zaidi wanaoshukuru.

Neema ilipowazidi na kizazi kuwa kingi, waliidharau haki na kuwafanyia stihizai watu wake; wakawa wanafasiri desturi ya Mwenyezi Mungu kwa ujinga wao na hawaa zao, wakisema: taabu waliyoipata baba zetu haikuwa ni mateso kutokana upotevu na uharibifu wao; wala raha waliyoipata haikuwa na malipo ya wema wao na uongofu wao, isipokuwa ni sadfa tu iliyokuja shaghala-baghala.

Ikiwa hawa wanaghafilika na kuhukumiwa na Mwenyezi Mungu na hekima yake, basi Mwenyezi Mungu mtukufu hakughalifika nao na vitendo vyao.

Basi tuliwaadhibu kwa ghafla hali hawatambui.

Yakiwa ni malipo ya kughurika kwao na kuwa huru na hawa na malengo yao. Namna hii Qur’an inawahadharisha wale ambao hawachungi haki na kutojali chochote wasiadhibiwe ghafla hali hawatambui.

وَلَوْ أَنَّ أَهْلَ الْقُرَىٰ آمَنُوا وَاتَّقَوْا لَفَتَحْنَا عَلَيْهِم بَرَكَاتٍ مِّنَ السَّمَاءِ وَالْأَرْضِ وَلَـٰكِن كَذَّبُوا فَأَخَذْنَاهُم بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٩٦﴾

96. Na lau kama watu wa mji wangeliamini na kuogopa, kwa hakika tungewafungulia baraka za mbingu na ardhi. Lakini walikadhibisha, kwa hiyo tukawapatiliza kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

أَفَأَمِنَ أَهْلُ الْقُرَىٰ أَن يَأْتِيَهُم بَأْسُنَا بَيَاتًا وَهُمْ نَائِمُونَ ﴿٩٧﴾

97. Je, watu wa miji wameaminisha ya kuwa adhabu yetu haitawafikia usiku, hali wamelala?

أَوَأَمِنَ أَهْلُ الْقُرَىٰ أَن يَأْتِيَهُم بَأْسُنَا ضُحًى وَهُمْ يَلْعَبُونَ ﴿٩٨﴾

98. Au watu wa miji wameaminisha kuwa adhabu yetu haitawafikia mchana, hali wanacheza?

أَفَأَمِنُوا مَكْرَ اللَّـهِ فَلَا يَأْمَنُ مَكْرَ اللَّـهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْخَاسِرُونَ ﴿٩٩﴾

99. Je, wamejiaminisha na hila ya Mwenyezi Mungu? Hawaaminishi hila ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye hasara.

أَوَلَمْ يَهْدِ لِلَّذِينَ يَرِثُونَ الْأَرْضَ مِن بَعْدِ أَهْلِهَا أَن لَّوْ نَشَاءُ أَصَبْنَاهُم بِذُنُوبِهِمْ وَنَطْبَعُ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ فَهُمْ لَا يَسْمَعُونَ ﴿١٠٠﴾

100. Je, hawaongoki ambao wamerithi ardhi baada ya wenyeji wake kwamba tukitaka tutawasibu kwa dhambi zao?

NA LAU KAMA WATU WA MJI

Aya 96 – 100

MAANA

Na lau kama watu wa mji wangeliamini na kuogopa, kwa hakika tungewafungulia baraka za mbingu na ardhi.

Baraka ya mbingu iliyodhahiri zaidi ni mvua na baraka ya ardhi, iliyo dhahiri zaidi, ni mimea mifugo na aina kadhaa za madini.

Tumebainisha katika kufasiri Juz, 7, (5:100) kifungu: ‘Je riziki ni sadfa au majaaliwa, kwamba kumwamini Mwenyezi Mungu peke yake hakuwezi kuotesha ngano.

Vilevile tumebainisha katika kufasiri Juz.6 (5:66) kifungu ‘Riziki na ufisadi’ kwamba makusudio ya imani yenye kuwajibisha riziki ni kumwamini Mwenyezi Mungu pamoja na kufanya amali kwa hukumu zote za Mwenyezi Mungu na misingi yake. Vilevile kufanya uadilifu katika kila kitu, na kwamba utakapoenea uadilifu na kutawala, basi hali itakuwa nzuri, na kutoweka ubaya na uovu.

Lakini walikadhibisha, kwa hiyo tukawapatiliza kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyachuma.

Yaani hawakujua hukumu za Mwenyezi Mungu, bali walihangaika katika ardhi kueneza ufisadi, dhulma, unyang’anyi na kulimbikizaa mali ya jasho la wanyonge. Mwenyezi Mungu amewapatiliza kwa maangamizi. Kwa sababu wao wamekufuru na kujilimbikiza vyote.

Je, watu wa miji wameaminisha ya kuwa adhabu yetu haitawafikia usiku, hali wamelala?

Huu ni uhofisho na tahadhari kutoka kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa waasi na wenye kujilimbikizia mali kuwa Mwenyezi Mungu atawashtukizia na adhabu yake wakiwa wameghafilika; kama alivyofanya kwa waliokuwa kabla yao.

Je, mtu ataweza kuizuia hukumu ya Mwenyezi Mungu? Vipi ataweza naye atakuwa kama aliyekufa?

Au watu wa miji wameaminisha kuwa adhabu yetu haitawafikia mchana, hali wanacheza?

Wanacheza, hapa ni fumbo la kughafilika kwao na mshtukizo na kujisahau.

Utauliza : hakuna tofauti kabisa baina ya kuwa macho mtu na kughafilika kwake mbele ya adhabu ya Mwenyezi Mungu. Sasa je, kuna makusudio gani ya kutaja usingizi na mchezo?

Jibu : Ni kuwa binadamu atambue udhaifu wake, ili awaidhike au aogope.

Je, wamejiaminisha na hila ya Mwenyezi Mungu? Hawaaminishi hila ya Mwenyezi Mungu ila watu wenye hasara.

Makusudio ya hila ya Mwenyezi Mungu hapa ni adhabu ambayo inawajia ghafla bila ya kutangulia hadhari yoyote.

Yametangulia maelezo kuhusu hila ya Mwenyezi Mungu katika kufasiri Juz.3 (3:54); kwamba yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t) anajisifu kuwa ni mwenye hila, kwa vile yeye anapangua hila za wenye hila; na anajisifu kuwa ni mwingi wa shukrani kwa vile anawapa thawabu wenye kushukuru.

Ama kuwa wao ni wenye hasara ni kwamba wao wamejingiza katika hasara kwa sababu ya inadi yao na kutojali kwao.

Je, hawaongoki ambao wamerithi ardhi baada ya wenyeji wake kwamba tukitaka tutawasibu kwa dhambi zao?

Yaani hawa washirikina waliorithi ardhi ya wale tuliyowaangamiza kwa dhambi zao, nao walikuwa na nguvu kuliko wao hawabainishi kwamba hali yetu kwao ni sawa na hali yetu kwa waliokuwa kabla yao? Lau tunataka itawapata adhabu yetu, kama ilivyowapata wengineo kabla yao? Hakika desturi ya Mwenyezi Mungu ni moja kwa viumbe vyake vyote.

Lengo la kuendelea sana huku katika nasaha na tahadhari ni kuwa mtu ajichunge wala asighafilike, na awaidhike na mwengine wala asidan- ganyike na mambo ya dhahiri yasiyo na chochote, “Watu wasioamini, haziwafai kitu ishara na maonyo” (10:101).

Na tutapiga muhuri juu ya nyoyo zao, kwa hiyo hawasikii.

Yametangulia maelezo yake katika Juz.1 (2:53).


2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

تِلْكَ الْقُرَىٰ نَقُصُّ عَلَيْكَ مِنْ أَنبَائِهَا وَلَقَدْ جَاءَتْهُمْ رُسُلُهُم بِالْبَيِّنَاتِ فَمَا كَانُوا لِيُؤْمِنُوا بِمَا كَذَّبُوا مِن قَبْلُ كَذَٰلِكَ يَطْبَعُ اللَّـهُ عَلَىٰ قُلُوبِ الْكَافِرِينَ ﴿١٠١﴾

101. Miji Hiyo tunakusimulia baadhi ya habari zake, Hakika waliwajia Mitume wao kwa ishara zilizo wazi-wazi, lakini hawakuwa wenye kuamini waliyoyakadhibisha zamani, Namna hii Mwenyezi Mungu anazipiga muhuri nyoyo za makafiri.

وَمَا وَجَدْنَا لِأَكْثَرِهِم مِّنْ عَهْدٍ وَإِن وَجَدْنَا أَكْثَرَهُمْ لَفَاسِقِينَ ﴿١٠٢﴾

102. Na hatukuona kwa wengi wao ahadi yoyote. Na hakika tuliwakuta wengi wao ni mafasiki.

MIJI HIYO TUNAKUSIMULIA

Aya 101 – 102

MAANA

Miji hiyo tunakusimulia baadhi ya habari zake.

Miji hiyo ni ishara ya watu wa miji hiyo ambao ni aina tano: Watu wa Nuh, wa Hud, wa Swaleh, wa Lut na wa Shuaib.

Maneno yanaelekezwa kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, Nabii Muhammad(s.a.w.w) wakikusudiwa waislamu kupewa habari ya hali za waliopita, ili wazingatie na watahadhari.

Hakika waliwajia Mitume wao kwa ishara zilizo waziwazi, lakini hawakuwa wenye kuamini waliyoyakadhibisha zamani.

Ametaja Razi njia tatu za kutafsiri kipande hiki cha Aya, na Tabrasi naye akazidisha ya nne. Hakuna hata moja waliyoitilia nguvu, na wakamwacha msomaji wa kawaida kwenye mataa; ambapo maana yako wazi yasiyokuwa na undani wowote.

Kwa ufupi ni kuwa watu wa miji hiyo kabla ya kupelekewa Mitume wa Mwenyezi Mungu, walikuwa kwenye shirki na upotevu; na kwamba wao waliendelea katika shirki yao na upotevu baada ya kuwafikia Mitume kwa dalili na miujiza. Na hawakuathirika na chochote, wakawa kama ambao hawakupelekewa mjumbe anayetoa bishara na maonyo. Haya yanafahamishwa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

Namna hii Mwenyezi Mungu anazipiga muhuri nyoyo za makafiri.

Muhuri hapa ni fumbo la kususuwaa kwa nyoyo zao na kwamba hazijali kupotea kwake wala haitarajiwi kheri yake.

Na hatukuona kwa wengi wao ahadi yoyote.

Hawaamini dini ya Mwenyezi Mungu wala hawalazimiani na chochote kinachohusiana na ubinadamu. Hata hivyo wanayo ahadi moja tu wanayolazimiana nayo wala hawapingani nayo, nayo ni kufuata masilahi na hawaa.

Na hakika tuliwakuta wengi wao ni mafasiki.

Yaani wamepotea kufuata njia.

ثُمَّ بَعَثْنَا مِن بَعْدِهِم مُّوسَىٰ بِآيَاتِنَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ فَظَلَمُوا بِهَا فَانظُرْ كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُفْسِدِينَ ﴿١٠٣﴾

103. Kisha baada yao tukamtuma Musa na ishara zetu kwa Firauni na wakuu wake lakini wakazikanusha. Basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa wafisadi.

وَقَالَ مُوسَىٰ يَا فِرْعَوْنُ إِنِّي رَسُولٌ مِّن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٠٤﴾

104. Akasema Musa: Ewe Firauni! Hakika mimi ni Mtume nitokaye kwa Mola wa walimwengu.

حَقِيقٌ عَلَىٰ أَن لَّا أَقُولَ عَلَى اللَّـهِ إِلَّا الْحَقَّ قَدْ جِئْتُكُم بِبَيِّنَةٍ مِّن رَّبِّكُمْ فَأَرْسِلْ مَعِيَ بَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿١٠٥﴾

105. Yanipasa nisiseme juu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa haki. Nimewajia na dalili wazi itokayo kwa Mola wenu. Basi waache wana wa Israel waende nami.

قَالَ إِن كُنتَ جِئْتَ بِآيَةٍ فَأْتِ بِهَا إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿١٠٦﴾

106. Akasema: Ikiwa umekuja na ishara, basi ilete ukiwa ni miongoni mwa wasemao kweli.

فَأَلْقَىٰ عَصَاهُ فَإِذَا هِيَ ثُعْبَانٌ مُّبِينٌ ﴿١٠٧﴾

107. Akaitupa fimbo mara ikawa nyoka dhahiri.

وَنَزَعَ يَدَهُ فَإِذَا هِيَ بَيْضَاءُ لِلنَّاظِرِينَ ﴿١٠٨﴾

108. Na akautoa mkono wake. Mara ukawa mweupe kwa watazamao.

قَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِ فِرْعَوْنَ إِنَّ هَـٰذَا لَسَاحِرٌ عَلِيمٌ ﴿١٠٩﴾

109. Wakasema wakuu wa watu wa Firauni: Hakika huyu ni mchawi mjuzi.

يُرِيدُ أَن يُخْرِجَكُم مِّنْ أَرْضِكُمْ فَمَاذَا تَأْمُرُونَ ﴿١١٠﴾

110. Anataka kuwatoa katika ardhi yenu. Basi mnatoa shauri gani?

قَالُوا أَرْجِهْ وَأَخَاهُ وَأَرْسِلْ فِي الْمَدَائِنِ حَاشِرِينَ ﴿١١١﴾

111. Wakasema: Mwache kidogo yeye na ndugu yake, na uwatume wakusanyao watu mijini.

يَأْتُوكَ بِكُلِّ سَاحِرٍ عَلِيمٍ ﴿١١٢﴾

112. Wakuletee kila mchawi, mjuzi.

MUSA NA FIRAUNI

Aya 103 – 112

MUHTASARI WA KISA

Tumepitia Aya kadhaa zinazoeleza kisa cha Nabii Musa(a.s) na wa Israel. Sasa tunaeleza kisa cha Nabii Musa(a.s) na Firauni katika Aya hizi tunazofasiri.

Neno ‘Firauni’ ni msimbo wa wafalme wa Misri wa zamani; kama vile msimbo wa Kaizari kwa wafalme wa Roma, Kisra kwa wafalme wa Fursi (Iran ya sasa) na Najashi kwa wafalme wa Uhabeshi (Ethiopia ya sasa).

Imenukuliwa kutoka kwa wale wanaojishughulisha sana na Historia ya Misri ya zamani, kwamba jina la Firauni aliyekuwa wakati wa Nabii Musa ni Munfitah.

JINA LA MAMAKE MUSA NA VIGANO

Ama Nabii Musa(a.s) ni mtoto wa Imran ambaye watu wa Kitab wanamwita Imram. Katika Juz.1 (2:51), tumeeleza kwamba jina la Nabii Musa ni maneno mawili yaliyochanganywa: neno ‘Mu’ lenye maana ya maji na ‘Sa ‘ lenye maana ya mti. Kwa sababu mama yake alimweka katika sanduku, akalifunga kufuli na akalitupa katika mto Nile kwa kumhofia Fir’aun.

La kushangaza ni uzushi wa mgunduzi wa kufuli hii, aliyotumia mama yake Nabii Musa kumfungia mwanawe, kuzusha kigano kilichoenea na kutangaa karne kwa karne na ambacho wamekiamini wapuzi wengi.

Nacho ni kuwa hakuna kufuli yoyote ila hufunguka ikisomewa jina la mama yake Nabii Musa. Kwa ajili hii hawalijui jina hilo isipokuwa watu maalum wenye siri.

Siku moja nilikwenda kwa mtu mmoja katika watu wa dini mwenye jina kubwa kati ya watu wake. Nikamkuta anapekua kwa hima sana mijalada ya kitabu Biharul-Anwar cha Allama Majlisi. Nikamwuliza: “Kwani una nini?” Akajibu: “Ninataka kujua jina la mama yake Nabii Musa.”

Miaka miwili iliyopita, bwana mmoja alinifuata akidhani mimi ni katika watu wa siri na kuniuliza jina la mama yake Nabii Musa. Nikamwambia: “Wewe wajua zaidi kuliko mimi,” lakini hakukubali. Nikamwambia: “Lakini huu ni upuuzi.” Akaona kuwa mimi namuhepa tu, sitaki kumfichulia siri hii. Nilipokata tamaa kabisa ya kumtuliza nikamwambia: “Haifai nikufichulie, kwa sababu sikuamini, utaiba mali za watu.” Basi akaapa kwa kiapo kizito kwamba yeye hataiba lakini mimi nikajifanya simwamini.

Siku zikapita nikaingilia kufasiri Qur’an Tukufu, nilipofika Aya hii nikawa narudia rejea mbalimbali, miongoni mwazo ni kitabu Qasasul–Quran kili- choandikwa na waandishi wane wa Kimisri: Muhammad Ahmad Jadul-Maula, Ali Muhammad Al-Bajawi, Muhamad Abul-Fadhl na Sayyid Shahatih, mara nikaona jina la mama yake Nabii Musa Yukabid (Jochebed) lakini watungaji hawakulinasibisha kwenye chimbuko lake.

Baada ya kutoka nje kidogo, turudie kisa cha Musa na Firauni; kama kilivyokuja katika Aya tulizo nazo. Kwa ufupi maana yake ni kwamba Firauni alikuwa akidai uungu badala ya Mwenyezi Mungu na alikuwa akiwakandamiza WaIsrael.

Mwenyezi Mungu akamtuma Nabii Musa na Harun kwa Firauni. Wakaenda na kujitosa kwenye kikao chake bila ya kuhofia usultani na utaghuti wake. Nabii Musa akamkabili na kumwambia: “Ewe Firauni! Mimi ni Mtume kutoka kwa Mola wa viumbe vyote nimetumwa kwako na kwa kila mpizani; na ninayo yanayothibitisha ujumbe wangu, Sasa waache waisrael na uwape uhuru waende watakapo”

Firauni akadharau akasema: “Lete hayo yanayothibitisha utume wako.” Nabii Musa akaitupa fimbo yake mara ikawa nyoka. Akaweka mkono wake kwenye mfuko wa kanzu yake alipoutoa ukawa unameremeta kwa weupe, na Nabii Musa hakuwa mweupe bali maji ya kunde.

Watu wa Firauni na halmashauri yake wakasema huyu ni mchawi bingwa, Basi Firauni akawakusanya wachawi. Kabla ya kuanza mazingaombwe yao walimwambia Firauni, “Je, tutapata malipo tukimshinda Musa?” Akasema: “Mtakuwa na malipo na kuwa karibu yangu.”

Wachawi wakaanza kutupa kamba na fimbo zao; mara watazamaji wakaona ni kama nyoka wanaotembea, Nabii Musa akatupa fimbo yake, ikameza yote waliyoyabuni. Wale wachawi wakasilimu na kuamini utume wa Nabii Musa. Firauni akawatishia kuwaadhibu na kuwatesa, lakini hawakurudi nyuma na wakathibiti kwenye imani yao, Riwaya nyingi zimeeleza kuwa Firauni alitekeleza vitisho vyake. Na hali ilivyo inalitilia nguvu hilo.

Firauni akawa anampa Nabii Musa na waliokuwa pamoja naye aina kwa aina za adhabu, lakini Nabii Musa aliendelea na mwito wake kwa Mwenyezi Mungu. waisrael wakampigia kelele Nabii Musa: “Tumeudhiwa kabla ya wewe kutujia na baada ya kutujia pia.” Nabii Musa akawaamuru kuvumilia na kuwapa tamaa ya kufaulu.

Mwenyezi Mungu akawaadhibu watu wa Firauni kwa kahati na dhiki. Akawapelekea mvua ya kuharibu mimea na mazao yao, nzinge waliokula vilivyobakishwa na athari ya mafuriko, chawa waliouma miili yao na vyura walioharibu maisha yao. Zaidi ya haya yote, maji yao yaligeuka na kuwa damu.

Hapo walifazaika kwa Nabii Musa. Wakamwambia: “Mola wako akituondolea adhabu tutakuwa miongoni mwa walioamini.” Mwenyezi Mungu akawaondoloea adhabu ili nao warejee, lakini wakavunja ahadi na wakaendelea na ukafiri. Mwenyezi Mungu akawaangamiza kwenye bahari na ikakatwa mizizi ya makafiri. Huu ndio muhtasari wa haraka haraka unaoelezwa na Aya tulizo nazo kuanzia Aya (103) mpaka mwisho wa Aya (137).

Sasa tufafanue yanayofahamishwa na Aya hizo.

MAANA

Kisha baada yao tukamtuma Musa na ishara zetu kwa Fir’aun na wakuu wake lakini wakazikanusha.

Dhamir ya baada yao inawarudia Mitume watano. Nuh, Hud, Swaleh, Lut na Shuaib. Ishara alizotumwa nazo Nabii Musa ni miujiza inayofahamisha utume wake. Wakuu wa Fir’aun, ni wale watukufu wa watu wake ambao mambo yote yako mikononi mwao, wengine ni kufuata na kunyenyekea tu.

Basi tazama jinsi ulivyokuwa mwisho wa wafisadi.

Ambao ni Fir’aun na wasaidizi wake waliozikalia shingo za watu. Mwisho huu utaelezwa katika mfumo mzima wa maelezo.

Akasema Musa: Ewe Firauni! Hakika mimi ni Mtume nitokaye kwa

Mola wa walimwengu.

Hivi ndivyo alivyomwita, “Ewe Firauni” bila ya kumtukuza na kumwadhimisha. Kwa sababu Nabii Musa alikuwa akizungumza lugha ya Mwenyezi Mungu na akafiksha ujumbe wa Mwenyezi Mungu ambao unamfanya mdogo mkubwa yeyote.

Kutokana na hivi ndio tunajua siri ya sera ya watu wema, wakijitukuza kwa mafasiki na kuwanyenyekea kwa udhalili na huruma waumin.

Yanipasa nisiseme juu ya Mwenyezi Mungu isipokuwa haki.

Hivi ndivyo ilivyo kwa kila Mtume aliyeaminiwa na Mwenyezi Mungu juu ya wahyi na kumchaguwa kuwa ni mjumbe wake.

Nimewajia na dalili wazi itokayo kwa Mola wenu.

Inayofahamisha kuwa mimi ni Mtume kutoka kwa Mola wa walimwengu.

Basi waache wana wa Israel waende nami.

Firauni alikuwa amewafanya waisraili watumwa na kuwatumia katika kazi ngumu, Ndipo Nabii Musa akataka waachiwe huru waende popote watakapo.

Akasema: Ikiwa umekuja na ishara, basi ilete ukiwa ni miongoni mwa wasemao kweli.

Inaonyesha kuwa Firauni alikuwa akidhani kuwa Nabii Musa ni mwongo katika madai yake, akataka kumfedhesha mbele ya wakuu, akamwambia: “Ilete hiyo hoja kama ni mkweli.” Nabii Musa akamziba mdomo wake kwa hoja mkataa.

Akatupa fimbo yake, mara ikawa nyoka dhahir . yaani nyoka halisi. Hapo Firauni akafazaika, lakini akajikaza kwa vile alikuwa akidai kuwa yeye ni Mungu Mkuu.

Nabii Musa tena akamshutukizia na muujiza wa pili.Na akautoa mkono wake. Mara ukawa mweupe kwa watazamao na mkono wa Nabii Musa ulikuwa rangi ya kahawia, sasa umekuwaje mweupe bila ya ugonjwa wowote?

Fir’aun akahisi unyonge na udhalili, akajiona yuko chini kabisa. Wale waliokaa naye wakatambua hilo kwamba Nabii Musa amewangusha kutoka juu.

Wakasema wakuu wa watu wa Firauni: Hakika huyu ni mchawi mjuzi.

Hiyo ndiyo hoja ya mwenye kushindwa nayo ni kutuhumu watu wema. Kisha wakuu wakaendelea kusema:

Anataka kuwatoa katika ardhi yenu .

Yaani Nabii Musa anataka kuwaondoa kwenye ufalme. Fir’aun aliposikia hivi akasema:

Basi mnatoa shauri gani? Wakasema: Mwache kidogo yeye na ndugu yake kwa sababu ukiwaua, watu watakasirika na utawala wako utakuwa hatarini.

Na uwatume mijini wakusanyao Yaani askariWakuletee kila mchawi mjuzi.

Watu wa Historia wanasema kuwa nchi ya Misri wakati wa Mafir’aun ilikuwa ikichemka na uchawi. Makuhani na waangalizi wa miungu ndio waliokuwa wakiendeleza kazi ya Uchawi. Anasema Aqqad katika Kitabu Iblisi kwenye kifungu cha Maendeleo ya Kimisr:

“Mafirauni wenyewe walikuwa wakikimbilia wachawi kwa kushindana na roho zilizojifiicha. Na tunayo mabaki ya visa vya uchawi ambayo hawakuyachagua wanaokusanya athari, lakini waliafikiana kuwa ni kazi za kichawi.

Walikuwa wakiugawanya uchawi kwenye mafungu: Kuna ule unaosaidiwa na uwezo wa mungu wa kheri dhidi ya mungu wa shari na ule unaosaidiwa na uwezo wa shetani mkubwa dhidi ya shetani mdogo.”

Kuenea uchawi wakati wa Firauni kunatufasiria sisi fimbo ya Nabii Musa na unatilia nguvu msingi unasema kuwa kila mwujiza wa Mtume ulikuja kulingana na aina iliiyoenea wakati wake, ili ushindi uwe mkubwa katika hoja na kukata kila udhuru – hoja mkataa.

Kwa hiyo Nabii Musa alivunja uchawi kwa vile ulienea zama zake.

Nabii Isa akafufua wafu, na Nabii Muhammad akawanyamazisha wanafasihi, kwa lengo hilo hilo.

وَجَاءَ السَّحَرَةُ فِرْعَوْنَ قَالُوا إِنَّ لَنَا لَأَجْرًا إِن كُنَّا نَحْنُ الْغَالِبِينَ ﴿١١٣﴾

113. Wakaja wachawi wa Firauni, wakasema: Tutapata ujira ikiwa tutashinda?

قَالَ نَعَمْ وَإِنَّكُمْ لَمِنَ الْمُقَرَّبِينَ ﴿١١٤﴾

114. Akasema: Ndio, nanyi hakika mtakuwa miongoni mwa wanaokurubishwa.

قَالُوا يَا مُوسَىٰ إِمَّا أَن تُلْقِيَ وَإِمَّا أَن نَّكُونَ نَحْنُ الْمُلْقِينَ ﴿١١٥﴾

115. Wakasema: Ewe Musa utatupa wewe au tutupe sisi?

قَالَ أَلْقُوا فَلَمَّا أَلْقَوْا سَحَرُوا أَعْيُنَ النَّاسِ وَاسْتَرْهَبُوهُمْ وَجَاءُوا بِسِحْرٍ عَظِيمٍ ﴿١١٦﴾

116. Akasema: Tupeni. Walipotupa waliyazuga macho ya watu na wakawaogopesha, wakaleta uchawi mkubwa.

وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ أَنْ أَلْقِ عَصَاكَ فَإِذَا هِيَ تَلْقَفُ مَا يَأْفِكُونَ ﴿١١٧﴾

117. Tukampelekea wahyi Musa kwamba tupa fimbo yako, mara ikavimeza walivyovibuni.

فَوَقَعَ الْحَقُّ وَبَطَلَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١١٨﴾

118. Ukweli ukasimama na yakabatilika waliyokuwa wakiyatenda.

فَغُلِبُوا هُنَالِكَ وَانقَلَبُوا صَاغِرِينَ ﴿١١٩﴾

119. Kwa hiyo hapo walishindwa wakageuka wakawa wadogo.

وَأُلْقِيَ السَّحَرَةُ سَاجِدِينَ ﴿١٢٠﴾

120. Wachawi wakapomoka kusujudu.

قَالُوا آمَنَّا بِرَبِّ الْعَالَمِينَ ﴿١٢١﴾

121. Wakasema: Tumemwamini Mola wa Walimwengu.

رَبِّ مُوسَىٰ وَهَارُونَ ﴿١٢٢﴾

122. Mola wa Musa na Harun.

قَالَ فِرْعَوْنُ آمَنتُم بِهِ قَبْلَ أَنْ آذَنَ لَكُمْ إِنَّ هَـٰذَا لَمَكْرٌ مَّكَرْتُمُوهُ فِي الْمَدِينَةِ لِتُخْرِجُوا مِنْهَا أَهْلَهَا فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ ﴿١٢٣﴾

123. Akasema Firauni: Je, mmemwamini kabla sijawaruhusu. Hakika hizi ni njama mlizozipanga mjini ili muwatoe wenyewe lakini punde mtajua.

لَأُقَطِّعَنَّ أَيْدِيَكُمْ وَأَرْجُلَكُم مِّنْ خِلَافٍ ثُمَّ لَأُصَلِّبَنَّكُمْ أَجْمَعِينَ ﴿١٢٤﴾

124. Nitawakata mikono yenu na miguu yenu kwa kubadilisha, kisha nitawasulubu nyote.

قَالُوا إِنَّا إِلَىٰ رَبِّنَا مُنقَلِبُونَ ﴿١٢٥﴾

125. Wakasema: Hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu.

وَمَا تَنقِمُ مِنَّا إِلَّا أَنْ آمَنَّا بِآيَاتِ رَبِّنَا لَمَّا جَاءَتْنَا رَبَّنَا أَفْرِغْ عَلَيْنَا صَبْرًا وَتَوَفَّنَا مُسْلِمِينَ ﴿١٢٦﴾

126. Na wewe hutufanyii kisasi ila kwa sababu tumeziamini ishara za Mola wetu zilipotujia. Ewe Mola, tumiminie subira na utufishe hali ya kuwa waislamu.

WAKAJA WACHAWI

Aya 113 – 126

MAANA

Wakaja wachawi kwa Firauni, wakasema: Tutapata ujira ikiwa tutashinda? Akasema, ndiyo, nanyi hakika mtakuwa miongoni mwa wanaokurubishwa.

Wachawi hawa waliojiuza kwa Firauni dhidi ya Nabii Musa walikuwa wanawakilisha dini katika zama zao, Nao wana mifano kila wakati. Wanauza dini yao na dhamiri kwa kila mwenye kutoa pesa. Siku hizi Wazayuni na Wakoloni wamewanunua wengi wenye kofia na vilemba wakawalipa na kuwashika sawasawa wasaidie ukoloni na unyonyaji kwa kuwavunga watu na kuwapoteza. Wakaanzisha jumuia mbalimbali na vitengo kwa jina la dini kwa lengo hilo. Lakini ni haraka mno kufedheka na kuwa kwenye midomo ya dharau ya kila mwenye mwamko mwenye ikhlasi.

Wakasema: Ewe Musa! Utatupa wewe au tutatupa sisi?

Walimuhiyarisha kuanza au waanze wao kwa kutegemea uchawi wao kuwa watashinda na kutomjali Nabii Musa(a.s) . La kushangaza ni kauli ya Razi, kwamba wachawi walimuhiyarisha Nabii Musa kwa kumheshimu.

Akasema: Tupeni ! Akiwadharau wao na uchawi wao.

Walipotupa waliyazuga macho ya watu na wakawaogopesha, na wakaleta uchawi mkubwa.

Kunasibisha kuzuga kwenye macho ya watu ni dalili kwamba uchawi wao si tukio la kweli, isipokuwa ni kuwavunga watu tu.

Kuwaogopesha, ni kwamba wachawi waliwatisha watazamaji na wakaleta uchawi mkubwa katika kuzuga na kupoteza si katika uhakika au hali halisi.

Tukampelekea wahyi Musa kwamba tupa fimbo yako, Mara ikavimeza walivyovibuni, Ukweli ukasimama na yakabatilika waliyokuwa wakiyabuni.

Nabii Musa alihofia wajinga wasihadaike na mizungu ya wachawi na upotevu wao. Mwenyezi Mungu akamfunga mkanda na kumpa wahyi kwamba yuko pamoja naye; na kwamba waliyoyaleta si chochote ni mizungu tu.

Akamwamrisha atupe fimbo, Alipoitupa ikameza yale waliyoyabuni kukabatilika kujifanya kwao ikadhihiri haki machoni kwa wote.

Firauni akaduwaa kwa mshtuko uliompata mbele ya umma wa watu. Amewaleta wachawi kutoka kila pembe ili wakilinde kiti chake na awathibitishie watu uwongo wa Nabii Musa na uzushi wake, Leo mambo yamebadilika kichwa chini miguu juu. Wote wakiwemo wachawi wameamini ukweli wa Nabii Musa na uaminifu wake na kukadhibisha uwongo wa Firauni na hiyana yake.

Kwa hiyo hapo walishindwa wakageuka wakawa wadogo baada ya kiburi kile.

Lau mambo yangeishia hivyo hivyo, kidogo Firauni angelipumua, lakini alishtukiziwa kwa jambo zito na chungu.

Na wachawi wakapomoka wakasujudu, Wakasema: Tumemwamini Mola wa waliimwengu (wote), Mola wa Musa na Harun si Firauni aliyewaleta kubatilisha mwito wa Mwenyezi Mungu na wa haki.

Utauliza : kuna makusudio gani ya kauli ya Wachawi ‘Mola wa Musa na Harun’ ambapo ingelitosha tu kusema ‘Mola wa walimwengu’?

Jibu : Firauni alikuwa akiwaambia watu:

فَقَالَ أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٤﴾

“Mimi ndiye Mola wenu mkubwa (79: 24)

مَا عَلِمْتُ لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرِي ﴿٣٨﴾

“Simjui kwa ajili yenu Mungu asiyekuwa mimi” (28: 38).

Lau wachawi wangelitosheka na kusema Mola wa walimwengu, basi Firauni angeligeuza na kujisifu yeye na kusema wananikusudia mimi Mola wa walimwengu. Ndipo wakaikata njia ya majisifu yake na kubadilisha kwake mambo.

UCHAWI

Katika Juz.1 (2:103) Tulizungumzia kuhusu uchawi kwa anuani ya ‘Uchawi na hukumu yake’, Tukasema katika tuliyoyasema, kwamba sisi tuko pamoja na wale waonao kuwa uchawi hauna chochote na tukatoa dalili ya hilo. Kuunganisha yaliyopita hapa tunaongezea haya yafuatayo:

Kauli yake Mwenyezi Mungu Wakayazuga macho ya watu ni dalili wazi kwamba uchawi hauna kitu chochote, na kwamba ni ujanja na kiini macho.

Ama kauli yake Mwenyezi Mungu: wakaleta uchawi mkubwa maana yake ni kwamba walifika kikomo cha ujanja na kubadilisha mambo. Maana haya yafafanuliwa na kusisitizwa na kauli yake Mwenyezi Mungu.

فَإِذَا حِبَالُهُمْ وَعِصِيُّهُمْ يُخَيَّلُ إِلَيْهِ مِن سِحْرِهِمْ أَنَّهَا تَسْعَىٰ ﴿٦٦﴾

“Mara kamba zao na fimbo zao zikadhaniwa mbele yake, kwa uchawi wao, kuwa zinapiga mbio”(20:66).

Hazikuwa zikienda hasa, bali ni dhana na mawazo tu. Mtume mtukufu(s.a.w.w) amesema: “Mwenye kumwendea mchawi au kuhani na mwongo akamsadiki, basi amekufuru aliyoyateremsha Mwenyezi Mungu.”

Wafasiri wengi wamesema kuwa wachawi wa Firauni walifanya hila ya kutingisha kamba na fimbo kwa kuziwekea Zebaki ili zitingishike na joto la jua.

Vyovyote iwavyo tunaamini kwa imani isiyo na shaka kwamba mchawi ni mwongo hakuna anayemsadiki ila mpuzi; na kwamba waliyoyafanya wachawi wa Firauni na wanayofanya wahindi na wengineo ambayo yanashangaza, yana sababu bila ya shaka yoyote.

Na sisi ijapokuwa hatujui sababu yenyewe, tunaamini kwa yakini kabisa kwamba uchawi hauwezi kubadilisha kitu, vinginevyo basi mchawi angeliweza kujizuia yeye na madhara na kujinufaisha na kutawala ulimwengu wote kwa kutaka kwake na matabano yake; na angelikuwa mshirika wa Mwenyezi Mungu katika milki yake Mwenyezi Mungu. Ametukuka kabisa na hayo Mwenyezi Mungu.

Akasema Firauni: Je, mmemwamini kabla sijawaruhusu?

Unaona mantiki hii? Anawataka wamwombe ruhusa katika mambo ya nyonyo zao imani, mapenzi na chuki. Hata mtu ulimwenguni asiutawale moyo wake mwenyewe! Lakini hiyo ni mantiki ya kitaghuti.

Hakika hizi ni njama mlizozipanga mjini ili muwatoe wenyewe, lakini punde mtajua.

Firauni anawaelekezea wachawi tuhuma hizi kuwa kumwamini kwao Nabii Musa hakukuwa kwa hoja na kukinaika, isipokuwa ni hila na hadaa tu walizozipanga pamoja kabla na kwamba lengo la njama hizi ni kuwatoa watawala na kuwavua utawala wao katika Misri.

Firauni alisema maneno haya akiwa anajua kwamba yeye ni mwongo katika kauli yake, lakini alitaka kuwababaisha watu akihofia wasimwache yeye wakamwamini Nabii Musa, lakini watu wanajua kwamba wachawi hawakuamini isipokuwa kwa kuona na kukinai. Vilevile watu wanajua kwamba Nabii Musa hakuwa pamoja na wachawi. Kwa sababu Firauni aliwakusanya huku na huko.

Nitawakata mikono yenu na miguu yenu kwa kubadilisha, kisha nitawasulubu nyote.

Kukata kwa kubadilisha ni kukata mkono wa kuume na mguu wa kushoto, na kinyume.

Hiyo ndiyo silaha ya mataghuti katika kuikabili haki, Anasema Masud katika kitabu Muruju-dhahab: “Katika mwaka 59 (A.H.) Muawiya ali- wakusanya watu ili wambai mwanawe Yazid. Akasimama kuhutubu mtu mmoja kutoka Azdi akasema:

“Akifa huyu akimwonyesha Muawiya basi ni huyu,akimwonyesha Yazid. Na atakayekataa basi ni huu, akautingisha upanga. Muawiya akamwambia: “Kaa, wewe ni hatibu bora kuliko watu wote.”

Wakasema: Hakika sisi ni wenye kurejea kwa Mola wetu.

Fanya utakavyo hatukujali wewe wala kuua kwako, Sisi tuna yakini ya kukutana na Mola wetu na uadilifu wake.

Kila mwenye kuamini kukutana na Mwenyezi Mungu anakuwa na msimamo huu bali anaona kufa shahidi ni kheri na nyenzo ya kupata radhi ya Mwenyezi Mungu na thawabu zake, Ama wale ambao wanaoogopa mauti katika njia ya Mwenyezi Mungu, wanaamini kinadharia tu; ama kimatendo wao wanakanusha.

Na wewe hutufanyii kisasi ila kwa sababu tumeziamini ishara za Mola wetu zilipotujia.

Kauli yao hii ina madhumuni ya kumtisha Firauni. Kwa sababu maana yake ni kwamba wewe hutuchukulii kisasi isipokuwa unamchukulia kisasi Mwenyezi Mungu na Mtume Muhammad(s.a.w.w) wake hasa. Kwa sababu hatuna kosa sisi ila kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake Nabii Musa:

أَلَمْ يَعْلَمُوا أَنَّهُ مَن يُحَادِدِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَأَنَّ لَهُ نَارَ جَهَنَّمَ ﴿٦٣﴾

“Je hawajui kwamba anayeshindana na Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi yeye atapata moto wa Jahanam.” (9:63).

Ewe Mola wetu tumiminie subira . Katika msimamo huu.

Unasifiwa uvumilivu (subira) kwa kuuliwa na kuadhibiwa katika njia ya Mwenyezi Mungu (s.w.t). Walimuomba Mungu awaruzuku fadhila hii kwa kuhofia wasilegeze mkanda na kurudi nyuma watakapohisi upanga ukipenya milini mwao.

Na utufishe hali ya kuwa ni waislamu, wanyenyekevu kwako na kwa Mtume wako tukiwa radhi na adhabu na mateso katika njia yako.


3

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

وَقَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِ فِرْعَوْنَ أَتَذَرُ مُوسَىٰ وَقَوْمَهُ لِيُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ وَيَذَرَكَ وَآلِهَتَكَ قَالَ سَنُقَتِّلُ أَبْنَاءَهُمْ وَنَسْتَحْيِي نِسَاءَهُمْ وَإِنَّا فَوْقَهُمْ قَاهِرُونَ ﴿١٢٧﴾

127. Na wakasema wakuu wa kaumu ya Firauni: Je, utamwacha Musa na watu wake walete uharibifu katika nchi na kukuacha wewe na waungu wako. Akasema: Tutawauwa watoto wao wa kiume na tutawaacha hai wanawake wao. Na hakika sisi ni wenye nguvu juu yao.

قَالَ مُوسَىٰ لِقَوْمِهِ اسْتَعِينُوا بِاللَّـهِ وَاصْبِرُوا إِنَّ الْأَرْضَ لِلَّـهِ يُورِثُهَا مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ وَالْعَاقِبَةُ لِلْمُتَّقِينَ ﴿١٢٨﴾

128. Musa akawaambia watu wake: Ombeni msaada kwa Mwenyezi Mungu na subirini. Ardhi ni ya Mwenyezi Mungu atamrithisha amtakaye katika waja wake na mwisho ni wa wenye takuwa.

قَالُوا أُوذِينَا مِن قَبْلِ أَن تَأْتِيَنَا وَمِن بَعْدِ مَا جِئْتَنَا قَالَ عَسَىٰ رَبُّكُمْ أَن يُهْلِكَ عَدُوَّكُمْ وَيَسْتَخْلِفَكُمْ فِي الْأَرْضِ فَيَنظُرَ كَيْفَ تَعْمَلُونَ ﴿١٢٩﴾

129. Wakasema: Tumeudhiwa kabla hujatufikia na baada ya kutujia. Akasema: Huenda Mola wenu atamwangamiza adui yenu na kuwafanya makhalifa katika ardhi aone jinsi mtakavyokuja fanya.

UTAMWACHA MUSA?

Aya 127 – 129

MAANA

Na wakasema wakuu wa kaumu ya Fir’aun: Je, utamwacha Musa na watu wake walete uharibifu katika nchi.”

Baada ya kwisha tukio hilo la kutisha ambalo Nabii Musa alipata ushindi na kufedheheka Firauni. Nabii Musa aliendelea kuwalingania kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake, na dalili yake ni yaliyotukia jana tu kati yake na wachawi, Watu wengi wakamkusanyikia.

Wakuu wa Firauni wakahofia hali isibadilike na mambo yakawageukia wao na bwana wao, hapo wakamchochea Firauni na kumwambia: “Mpaka lini utamnyamazia Musa na kumwacha akiharibu nchi?” Kuharibu nchi, wanamaanisha watu kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake.

Na wakuache wewe na waungu wako.

Kauli hii ya wakuu wa Firauni inafahamisha kuwa alikuwa nao waungu anaowaabudu; nayo inapingana, kwa dhahiri yake, na kauli ya Firauni kuwa Mimi ndiye mola wenu mkubwa na simjui kwa ajili yenu Mungu asiyekuwa mimi.

Wafasiri wamelijibu hilo kwa majibu kadhaa. Lenye nguvu zaidi ni kuwa Firauni alikuwa na miungu akidai kuwa yeye ni mwana kipenzi wa hiyo miungu na kwamba yeye anaitegemeza hukumu yake na utawala wake kwenye hiyo miungu. Kwa hiyo kauli yake simjui kwa ajili yenu Mungu na Mola isipokuwa yeye peke yake inamaanisha kuwa hakuna yeyote mwenye kuhukumu kwa jina la mungu isipokuwa yeye. Maana haya yanatiliwa nguvu na kauli yake:

أَلَيْسَ لِي مُلْكُ مِصْرَ وَهَـٰذِهِ الْأَنْهَارُ تَجْرِي مِن تَحْتِي ﴿٥١﴾

“Kwani ufalme wa Misri si wangu na hii mito inapita chini yangu?” (43:51).

Akasema: Tutawaua watoto wao wakiume na tutawaacha hai wanawake wao.

Kabla ya kuzaliwa Nabii Musa, Fir’aun alikua akwaiua watoto wa kiume wa Bani Israel waliposisitizia wakuu katika watu wake apambane na Nabii Musa, aliwajibu atarudisha mpango huo wa mwanzo.

Na hakika sisi ni wenye nguvu juu yao.

Yaani tuna nguvu juu yao kama ilivyokuwa kabla ya Musa.

Musa akawaambia watu wake: Ombeni msaada kwa Mwenyezi Mungu na subirini. Ardhi ni ya Mwenyezi Mungu atamrithisha amtakaye katika waja wake na mwisho ni wa wenye takuwa.”

Waisrael waliposikia vitisho vya Firauni na kiaga chake waliogopa. Nabii Musa(a.s) akawatuliza na kuwaamrisha kuwa na subira (uvumilivu) na kumtegemea Mwenyezi Mungu; na akawapa tumaini la ushindi ikiwa wao watasubiri na kumwogopa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu ardhi ni ya Mwenyezi Mungu si ya Firauni, na Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye kumcha.

Wakasema: Tumeudhiwa kabla hujatufikia na baada ya kutujia!

Firauni alikuwa akiwakandamiza waisrael kabla ya kuja Nabii Musa na akawashtua kuwakandamiza zaidi baada ya kuja kwake. Walipomwambia Nabii Musa hivyo akasema:

Huenda Mola wenu akamwangamiza adui yenu na kuwafanya makhalifa katika nchi aone jinsi mtakavyokujafanya.

Nabii Musa(a.s) alikuwa anajua wazi kuwa Firauni ataangamia na kwamba Mungu atawaokoa wana wa Israil na kuwamakinisha katika ardhi, lakini alitoa ibara ya huenda ili wasibweteke na ahadi yake.

Kisha akaishiria Nabii Musa kwamba, si muhimu kuwa adui ataangamia na wao kuwa makhalifa katika ardhi, lakini muhimu zaidi ni kumcha Mungu na kuutumia vizuri huo ukhalifa katika ardhi yake; na kwamba Mungu atawaangalia je, watatengeza au wataharibu?

Na wamefanya mengi sana katika ardhi; hapo mwanzo waliwaua mitume na viongozi wema, baadae wakaunda dola isiyokuwa na sharia isipokuwa matamanio ya kuua na kufukuza watu makwao.

Mwaka huu wa 1968, kimetoka kitabu huko Israil kinaitwa Siyakh lokhamim yaani simulizi za wanajeshi. Gazeti la Al-ahram la Misr toleo la tarehe 23-8-1968, limefasiri baadhi ya yaliyomo katika kitabu hicho:

“Ambaye hawezi kuvunja nyumba na kuwafurusha waliomo katika nyumba hiyo, basi bora akae nyumbani kwake tu. Sisi tulipokuja kwenye nchi ya Palestina kulikuwa na watu wengine wanaoishi humo; hatukuwa na matumaini kuwa wataweza kukubali kutuachia mashamba yao na majumba yao. Kwa hiyo ikawa hakuna budi tuwaue au kuwatishia kuwaua ili wakimbie watuachie majumba na mashamba”

Hii ndiyo sharia na lengo la Israil: kuua na kufukuza. Hii sio dola kama dola nyinginezo; isipokuwa ni kikosi cha kizayuni cha mauaji chenye lengo la kuwafukuza wenyeji na kukalia nchi zao kuanzia mto Nail hadi Furat.

Je Waarabu wamejiandaa na nini? Hakuna njia wala mbinu yoyote isipokuwa misimamo ya kivietnam inayosema: ‘Kufa na kupona’ ama kusiweko na Israil au kusiweko na Mwarabu.

وَلَقَدْ أَخَذْنَا آلَ فِرْعَوْنَ بِالسِّنِينَ وَنَقْصٍ مِّنَ الثَّمَرَاتِ لَعَلَّهُمْ يَذَّكَّرُونَ ﴿١٣٠﴾

130. Na hakika tuliwaadhibu watu wa Firauni kwa ukame na kwa kupungukiwa na mazao, ili wapate kukumbuka.

فَإِذَا جَاءَتْهُمُ الْحَسَنَةُ قَالُوا لَنَا هَـٰذِهِ وَإِن تُصِبْهُمْ سَيِّئَةٌ يَطَّيَّرُوا بِمُوسَىٰ وَمَن مَّعَهُ أَلَا إِنَّمَا طَائِرُهُمْ عِندَ اللَّـهِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿١٣١﴾

131. Ulipowafikia wema, walisema: Huu ni kwa ajili yetu na ulipowafikia ubaya walimnasibishia mkosi Musa na walio pamoja naye. Sikilizeni! Hakika mkosi wao unatoka kwa Mwenyezi Mungu lakini wengi wao hawajui.

وَقَالُوا مَهْمَا تَأْتِنَا بِهِ مِنْ آيَةٍ لِّتَسْحَرَنَا بِهَا فَمَا نَحْنُ لَكَ بِمُؤْمِنِينَ ﴿١٣٢﴾

132. Na wakasema: Hata ukituletea ishara yoyote kutur- oga hatutakuamini.

فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمُ الطُّوفَانَ وَالْجَرَادَ وَالْقُمَّلَ وَالضَّفَادِعَ وَالدَّمَ آيَاتٍ مُّفَصَّلَاتٍ فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا مُّجْرِمِينَ ﴿١٣٣﴾

133. Basi tukawapelekea tufani na nzige na chawa na vyura na damu kuwa ishara mbalimbali, lakini wakatakabari na wakawa watu wakosefu.

TULIWAADHIBU WATU WA FIRAUNI

Aya 130-133

MAANA

Na hakika tuliwaadhibu watu wa Firauni kwa ukame na kwa kupungukiwa na mazao, ili wapate kukumbuka.

Misri ilikuwa ikibubujika rutuba na mazao. Firauni akajifaharusha kwa rutuba hii na kusema:

وَهَـٰذِهِ الْأَنْهَارُ تَجْرِي مِن تَحْتِي ﴿٥١﴾

"Na pia mito hii ipitayo chini yangu" (43:51)

Mwenyezi Mungu alitia balaa ya kahati na dhiki ya maisha wakati wa Firauni wa Musa ili ajutie upotevu wake na aitikie mwito wa haki. Kuna Hadith isemayo: "Wakiwa waovu watawala hufungwa mvua."

Ni sawa iwe kulikuwako na uhusiano baina ya dhuluma ya mtawala na kahati kwa njia ya ujumla au isiweko, lakini Mwenyezi Mungu aliwaadhibu watu wa Firauni kwa dhulma yao ili wao wakumbuke kabla ya kuwaingiza ndani kwenye uchungu.

Ulipowafikia wema, walisema: Huu ni kwa ajili yetu na ulipowafikia ubaya walimnasibishia mkosi Musa na walio pamoja naye.

Wanafasiri matukio kwa mantiki haya, Kila heri inayowapata basi wanaistahiki wao. Kwa sababu wao wanatawala watu, na kila ubaya unaowapa- ta, basi sababu yake ni yule anayewalingania kwenye haki. Ama rutuba na ukame wanautenga na Mwenyezi Mungu na maumbile aliyo yaumba.

Ndipo Mwenyezi Mungu akawajibu kwa kusema: Sikilizeni! Hakika mkosi wao unatoka kwa Mwenyezi Mungu lakini wengi wao hawajui. Mkosi wao ni fumbo la ukame uliowapata na huo ni kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu ambayo sababu zote huishia kwake, na kumnasibishia Musa na ujinga na upumbavu tu.

Utauliza : Kwa nini Mwenyezi Mungu ametumia neno wema kwa ibara yenye al (Al-Hasana) ambayo katika sarufi ya Kiarabu inaitwa ma'rifa, na neno ubaya aktumia bila ya al ambyo ni nakira?

Jibu : Sio mbali kuwa ni ishara ya kwamba maumbile ya heri, kama vile rutuba n.k, ni mengi, na kwamba ubaya, kama vile matetemeko na tufani na ukame ni machache.

Na wakasema: Hata ukituletea ishara yoyote kuturoga hatutakuamini

Huku ni kukiri wazi, kwamba wao wanaikataa haki, wakati huo huo wanakiri kushindwa kwao kwa hoja na dalili. Yakawa malipo ya inadi yao hii ni kuwapata balaa ya aina tano za adhabu:

1.Tukawapelekea tufani ya mvua ikaharibu mimea na mifugo.

2.Na nzige waliokuja baada ya tufani,kama kawaida, wakala mimea yao iliyobakia.

3.Na chawa.

4.Na vyura waliowaghasi maisha yao.

5.Na damu. Inasemekana maji yao yaligeuka kuwa damu na wasi weze kupata maji matamu. Na inasemekana walipatwa na maradhi ya kutokwa na damu za pua.

وَلَمَّا وَقَعَ عَلَيْهِمُ الرِّجْزُ قَالُوا يَا مُوسَى ادْعُ لَنَا رَبَّكَ بِمَا عَهِدَ عِندَكَ لَئِن كَشَفْتَ عَنَّا الرِّجْزَ لَنُؤْمِنَنَّ لَكَ وَلَنُرْسِلَنَّ مَعَكَ بَنِي إِسْرَائِيلَ ﴿١٣٤﴾

134. Na ilipowaangukia adhabu wakasema: Ewe Musa Tuombee kwa Mola wako kwa yale aliyokuahidi. Kama ukituondolea adhabu bilashaka tutakuamini na hakika tutawaacha wana wa Israil waende nawe.

فَلَمَّا كَشَفْنَا عَنْهُمُ الرِّجْزَ إِلَىٰ أَجَلٍ هُم بَالِغُوهُ إِذَا هُمْ يَنكُثُونَ ﴿١٣٥﴾

135. Lakini tulipowaondolea adhabu kwa muda watakaoufikia, mara wakavunja ahadi.

فَانتَقَمْنَا مِنْهُمْ فَأَغْرَقْنَاهُمْ فِي الْيَمِّ بِأَنَّهُمْ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا عَنْهَا غَافِلِينَ ﴿١٣٦﴾

136. Basi tuliwapatiliza na tukawazamisha baharini kwa sababu walizikadhibisha ishara zetu na wakaghafilika nazo

وَأَوْرَثْنَا الْقَوْمَ الَّذِينَ كَانُوا يُسْتَضْعَفُونَ مَشَارِقَ الْأَرْضِ وَمَغَارِبَهَا الَّتِي بَارَكْنَا فِيهَا وَتَمَّتْ كَلِمَتُ رَبِّكَ الْحُسْنَىٰ عَلَىٰ بَنِي إِسْرَائِيلَ بِمَا صَبَرُوا وَدَمَّرْنَا مَا كَانَ يَصْنَعُ فِرْعَوْنُ وَقَوْمُهُ وَمَا كَانُوا يَعْرِشُونَ ﴿١٣٧﴾

137. Tukawarithisha watu walionekana wadhaifu mashariki na magharibi ya ardhi tuliyoibariki. Na likatimia neno jema la Mola wako kwa wana wa Israil, kwa sababu walikuwa na subira; na tukayaangamiza yale aliyokuwa akiyafanya Firauni na kaumu yake na yale waliyokuwa wakiyajenga.

ILIPOWAANGUKIA ADHABU

Aya 134-137

MAANA

Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja aina tano za adhabu alizowaadhibu watu wa Firauni. Na walikuwa kila inapowapata adhabu hutawasali kwa Musa kutaka kuondolewa adhabu hiyo kwa karamu yake mbele ya Mwenyezi Mungu.

Walikuwa wakijiwekea ahadi wao wenyewe kwa Musa kuwa akifanya, basi wataitikia mwito wa haki. Mwenyezi Mungu naye alikuwa akiwaondolea adhabu kwa muda fulani ili wajiandae na toba na kuwasimamishia hoja, Lakini walikuwa wakivunja ahadi, hawakutekeleza wanayoyasema.

Hapo Mwenyezi Mungu huwateremshia mara ya pili, Tena wanarudia kunyenyekea na kutawasali, na Mwenyezi Mungu huwaondolea. Ikawa namna hii mpaka adhabu ya tano, au jaribio la tano, ndipo akawatesa na kuwatupa ndani ya bahari.

Baada ya muda mrefu kupita tangu kufamaji Firauni na kufariki Musa na Harun, alitokea katika waisrail, Daudi na Suleiman wakafanya dola yenye mipaka mashariki na magharibi.

Lakini haraka sana dola iliyeyuka na Waisrail wakatawaliwa na Ebuchadnezer, wafursi na makhalifa wa Alexandria kisha wa Roma.

وَجَاوَزْنَا بِبَنِي إِسْرَائِيلَ الْبَحْرَ فَأَتَوْا عَلَىٰ قَوْمٍ يَعْكُفُونَ عَلَىٰ أَصْنَامٍ لَّهُمْ قَالُوا يَا مُوسَى اجْعَل لَّنَا إِلَـٰهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ قَالَ إِنَّكُمْ قَوْمٌ تَجْهَلُونَ ﴿١٣٨﴾

138. Na tukawavusha bahari wana wa Israil na wakawafikia waliokuwa wakiyaabudu masanamu yao; wakaema: Ewe Musa! Hebu nasi tufanyie waungu kama hawa walivyo na waungu. Akasema Hakika nyinyi ni watu wafanyao ujinga.

إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ مُتَبَّرٌ مَّا هُمْ فِيهِ وَبَاطِلٌ مَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٣٩﴾

139. Hakika waliyona hawa yatawangamiza na ni bure waliyokuwa wakiyafanya.

قَالَ أَغَيْرَ اللَّـهِ أَبْغِيكُمْ إِلَـٰهًا وَهُوَ فَضَّلَكُمْ عَلَى الْعَالَمِينَ ﴿١٤٠﴾

140. Akasema je, niwatafutie mungu badala ya Mwenyezi Mungu, hali yeye ameweafadhilisha juu ya walimwengu?

وَإِذْ أَنجَيْنَاكُم مِّنْ آلِ فِرْعَوْنَ يَسُومُونَكُمْ سُوءَ الْعَذَابِ يُقَتِّلُونَ أَبْنَاءَكُمْ وَيَسْتَحْيُونَ نِسَاءَكُمْ وَفِي ذَٰلِكُم بَلَاءٌ مِّن رَّبِّكُمْ عَظِيمٌ ﴿١٤١﴾

141. Na Tulipowaokoa kwa kaumu ya Firaun waliowapa adhabu mbaya wakiwaua watoto wenu wa kiume na kuwaacha hai wanawake wenu. Na katika hayo ulikuwa mtihani mkubwa uliotokea kwa Mola wenu.

TULIWAVUSHA WANA WA ISRAIL

Aya 138-141

MAANA

Na tukawavusha bahari wana wa Israil na wakawafikia waliokuwa wakiyaabudu masanamu yao; wakaema: Ewe Musa! Hebu nasi tufanyie waungu kama hawa walivyo na waungu. Akasema: Hakika nyinyi ni watu wafanyao ujinga.

Baadhi ya riwaya zinaeleza kuwa Musa aliendelea miaka ishirini na tatu akipigana jihadi na Firauni kwa ajili ya Tawhid na kuwakomboa wana wa Israil kutokana ukandamizaji, Wakashuhudia miujiza ya kushangaza iliyodhihiri mikononi mwa Musa.

Mwisho wakaona kupasuka bahari kwa fimbo ya Musa, na jinsi zilivyotokea njia kavu kumi na mbili. Kila ukoo ukawa na njia yake. Vile vile waliona jinsi bahari ilivyofungika kwa Firauni na askari wake.

Yote hayo waliyashuhudia, lakini kabla ya kupita muda walisahau miujiza waliyoiona na macho yao yakawa kwa watu wanaoabudu masanamu, wakamtaka Musa awafanyie sanamu la kuabudu. Walitaka haya wakiwa wanajua kwamba Musa ni mtu wa Mwenyezi Mungu na kwamba umuhimu wake wa kwanza ni mwito wa Tawhid na kupiga vita ushirikina. Vile vile walikuwa wakijua kuwa Mwenyezi Mungu alimwangamiza Firauni na jeshi lake, kwa sababu ya ushirikina wake. Baadhi ya wafisri wanasema; "Lau wao wenyewe wangejifanyia mungu, mshangao ungelikuwa mdogo kuliko kumtaka Mtume wa Mola wa walimwengu wote kuwafanyia mungu. Lakini hao ndio Waisrail!

Hakika yaliyo na hawa yatawangamiza na ni bure waliyokuwa wakiyafanya.

Musa(a.s) alianza kuwajibu watu wake kuwa wao ni wajinga na wapumbavu; kisha akawapa habari kwamba mwisho wa washirikina na waabudu masanamu ni hasara na maangamizi.

Akasema je, niwatafutie mungu badala ya Mwenyezi Mungu, hali yeye ameweafadhilisha juu ya walimwengu?

Imepita tafsiri yake katika Juz.1 (2:47)

Kwa vyovyote kufadhilishwa kwao juu ya Firauni na watu wake hakuhisabiwi kuwa ni fadhila kubwa.

Na Tulipowaokoa kwa kaumu ya Firaun waliowapa adhabu mbaya wakiwaua watoto wenu wa kiume na kuwaacha hai wanawake wenu. Na kati- ka hayo ulikuwa mtihani mkubwa uliotokea kwa Mola wenu.

Umepita mfano wake katika Juz.1(2:49)


4

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

وَوَاعَدْنَا مُوسَىٰ ثَلَاثِينَ لَيْلَةً وَأَتْمَمْنَاهَا بِعَشْرٍ فَتَمَّ مِيقَاتُ رَبِّهِ أَرْبَعِينَ لَيْلَةً وَقَالَ مُوسَىٰ لِأَخِيهِ هَارُونَ اخْلُفْنِي فِي قَوْمِي وَأَصْلِحْ وَلَا تَتَّبِعْ سَبِيلَ الْمُفْسِدِينَ ﴿١٤٢﴾

142. Na tulimwahidi Musa masiku thalathini na tukayazitimiza kwa kumi; ndipo ikatimia miadi ya Mola wake siku arubaini. Na Nabii Musa akamwambia ndugu yake Harun: Shika mahali pangu katika watu wangu na utengeneze wala usifu- ate njia ya waharibifu.

وَلَمَّا جَاءَ مُوسَىٰ لِمِيقَاتِنَا وَكَلَّمَهُ رَبُّهُ قَالَ رَبِّ أَرِنِي أَنظُرْ إِلَيْكَ قَالَ لَن تَرَانِي وَلَـٰكِنِ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي فَلَمَّا تَجَلَّىٰ رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكًّا وَخَرَّ مُوسَىٰ صَعِقًا فَلَمَّا أَفَاقَ قَالَ سُبْحَانَكَ تُبْتُ إِلَيْكَ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٤٣﴾

143. Na alipofika Musa kwenye miadi yetu Na Mola wake akamsemeza, alisema: Mola wangu nionyeshe nikutazame. Akasema: Hutaniona, lakini tazama jabali, kama litakaa pahali pake ndipo utaniona. Basi Mola wake alipojionyesha kwa jabali alilifanya lenye kuvunjika vunjika, na Musa akaanguka hali amezimia. Alipozinduka alisema: kutakasika ni kwako! Natubu kwako na mimi ni wa kwanza wa wanaoamini.

قَالَ يَا مُوسَىٰ إِنِّي اصْطَفَيْتُكَ عَلَى النَّاسِ بِرِسَالَاتِي وَبِكَلَامِي فَخُذْ مَا آتَيْتُكَ وَكُن مِّنَ الشَّاكِرِينَ ﴿١٤٤﴾

144. Akasema: Ewe Musa! Mimi nimekuteua kwa watu kwa ujumbe wangu na kwa kusema nawe kwangu; basi yashike ninayokupa, na uwe miongoni mwa wanaoshukuru.

وَكَتَبْنَا لَهُ فِي الْأَلْوَاحِ مِن كُلِّ شَيْءٍ مَّوْعِظَةً وَتَفْصِيلًا لِّكُلِّ شَيْءٍ فَخُذْهَا بِقُوَّةٍ وَأْمُرْ قَوْمَكَ يَأْخُذُوا بِأَحْسَنِهَا سَأُرِيكُمْ دَارَ الْفَاسِقِينَ ﴿١٤٥﴾

145. Na tukamwandikia katika mbao kila kitu mawaidha na ufafanuzi wa kila jambo. Basi yashike kwa imara na uwaamrishe watu wako washike mazuri yake zaidi, Nitawaonyesha makao ya wafasiki.

Aya 142 – 145

MAANA

Na tulimwahidi Musa masiku thalathini na tukayazitimiza kwa kumi; ndipo ikatimia miadi ya Mola wake siku arubaini.

Nabii Musa(a.s) alimtaka Mola wake amteremshie Kitab atakachowaongozea watu kwenye yale wanayoyahitajia katika mambo ya dini yao. Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamwahidi kuteremshia Kitab baada ya siku thalathini, na utaendelea ushukaji wake kwa siku kumi. Kwa ujumla itakuwa muda wa miadi na wa kushuka ni siku arubaini.

Hapa tumefafanua baada ya kueleza kwa ujumla kwenye Juz. 1 (2:51).

Na Musa akamwambia ndugu yake Harun: Shika mahali pangu katika watu wangu na utengeneze wala usifuate njia ya waharibifu.

Nabii Musa alipoondoka alimwachia mahali pake ndugu yake Harun kwa Wana wa Israel; akampa nasaha kusimamia mambo yao na kuyatengeneza. Akamhadharisha na tabia zao zinazopondokea zaidi kwenye ufisadi. Ni jana tu walipokodolea macho ibada ya masanamu mpaka Nabii Musa akawaambia kuwa ni watu wajinga.

Harun akakubali nasaha kwa moyo mkunjufu, kama anavyokubali nasaha kaimu kiongozi mwenye ikhlasi kutoka kwa kiongozi wake mwaminifu.

Na alipofika Nabii Musa kwenye miadi yetu ambayo aliiweka Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumpa Tawrat,

Na Mola wake akamsemeza bila ya kumwona kwa sababu:

وَمَا كَانَ لِبَشَرٍ أَن يُكَلِّمَهُ اللَّـهُ إِلَّا وَحْيًا أَوْ مِن وَرَاءِ حِجَابٍ أَوْ يُرْسِلَ رَسُولًا ﴿٥١﴾

“Haikuwa kwa mtu aseme na Mwenyezi Mungu ila kwa wahyi au kwa nyuma ya pazia au kumtuma mjumbe” (42:51)

Nabii Musa alisema:Mola wangu nionyeshe nikutazame.

Baadhi ya maulamaa wanasema kuwa Nabii Musa hakumwomba Mola wake kumwona kwa ajili yake isipokuwa ni kwa ajili ya watu wake. Lakini hii inapingwa na kauli yake Nabii Musa pale aliposema:

Kutakasika ni kwako, na natubu kwako.

Vyovyote iwavyo ni kwamba Nabii Musa alitaka kuona, ni sawa iwe ni kwa ajili yake au kwa ajili ya wengine, sisi hatuoni ubaya wowote katika ombi hili, kwa sababu nafsi ya mtu ina hamu ya kutaka kujua yanayokuwa na yasiyokuwa hasa kuona kile ambacho kitazidisha utulivu wa nafsi.

Ibrahim(a.s) alitaka mfano wa hayo. Angalia Juz.3 (2:260).

Akasema: Hutaniona.

Kwa sababu kumwona Mwenyezi Mungu ni muhali. Tumeyazungumza hayo kwa ufafanuzi katika kufasiri Juz. 1(2:51).

Lakini tazama jabali, kama litakaa mahali pake utaniona.

Nabii Musa aligeuka kwenye jabali ili amwone Mwenyezi Mungu, mara akaanguka chini na hakuona chochote. Mwenyezi Mungu (s.w.t) alifanya hivi ili kumfahamisha Nabii Musa(a.s) kwamba kumwona Mwenyezi Mungu hakuwezekani kwake wala kwa mwingine.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliuwekea sharti uwezekano wa kuonekana kwake kwa kutulia mahali jabali na jabali halikutulia, Kwa hiyo kumwona Mwenyezi Mungu hakuwezekani.

Mfumo huu alioutumia Mwenyezi Mungu hapa ni kama ule wa kusema: Nitafanya hivi kunguru akiota mvi, Au akipita ngamia kwenye tundu ya sindano.

Basi Mola wake alipojionyesha kwenye jabali alilifanya lenye kuvunjika vunjika.

Yaani ilipodhihiri amri ya Mola wake; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَجَاءَ رَبُّكَ وَالْمَلَكُ صَفًّا صَفًّا ﴿٢٢﴾

“Akaja Mola wako na Malaika (wamejipanga) safu kwa safu.” (89:22).

Yaani ikaja amri ya Mola wako.

Na Musa akaanguka chini amezimia.

Akawa hana fahamu kwa kishindo cha ghafla, Mwenyezi Mungu akamhurumia akazinduka.

Alipozinduka alisema: Kutakasika ni kwako! Natubu kwako. Kwa kukuomba kukuonana mimi ni wa kwanza wa wanaoamini.

Kwa sababu wewe ni mtukufu zaidi ya kuonekana kwa jicho.

Makusudio ya wa mwanzo sio kulingana na hisabu ya wakati; isipokuwa makusudio yake ni uthabiti na kutilia mkazo.

Akasema: Ewe Musa! Mimi nimekuteua kwa watu kwa ujumbe wangu na kwa kusema nawe kwangu; basi yashike ninayokupa, na uwe miongoni mwa wanaoshukuru.”

Baada ya Nabii Musa kunyenyekea kwa muumba wake, Mwenyezi Mungu alimkumbusha neema yake, kubwa zaidi ni Utume na kuzungumza na Mwenyezi Mungu. Makusudio ya watu ni watu wa zama zake, kwa dalili ya kauli yake: Kwa ujumbe wangu. Kwani Mwenyezi Mungu aliwachagua Mitume wengi kabla ya Nabii Musa na baada yake.

Ama kuhusika kwake na kuzungumza naye hakuna dalili ya ubora zaidi. Ikiwa kunafahamisha ubora wowote basi kupelekewa roho mwaminifu kwa mwisho wa Mitume na bwana wa Mitume ndio daraja ya juu na bora zaidi.

Na tukamwandikia katika mbao kila kitu mawaidaha na ufafanuzi wa kila jambo.

Makusudio ya mbao ni Tawrat kwa sababu ndiyo aliyoteremshiwa Nabii Musa, ndani yake mna mawaidha na upambanuzi wa hukumu.

“Kila jambo ni neno la kiujumla, lakini limekusudia mahsusi; yaani kila linalofungamana na maudhui ya risala miongoni mwa mawaidha, hukumu, misingi ya itikadi, kama vile kumwamini Mwenyezi Mungu, Mitume yake na siku ya mwisho, na hukumu za sharia, kama halali na haramu. Kwa hiyo kauli yake: Mawaidha na maelezo ni ubainifu wa tafsiri ya kauli yake kila jambo. Kwa sababu makusudio ya maelezo ni kubainisha hukumu za kisharia.

Basi yashike kwa imara.

Yaani ichunge Tawrat na uitumie kwa ukweli wa nia.

Na uwaamrishe watu wako washike mazuri yake zaidi.

Kila aliloliteremsha Mwenyezi Mungu ni zuri, lakini kuna yaliyo mazuri zaidi. Mwenyezi Mungu mtukufu anasema: “Na fanyeni wema, Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema.”

Nitawaonyesha makao ya wafasiki.

Yaani fasiki na dhalimu atafikwa na majanga. Haya ndiyo niliyoyafahamu kutokana na jumla hii kabla ya kupitia tafsir, Baada ya kuzipita nikakuta kauli kadhaa. Miongoni mwazo ni kwamba Mwenyezi Mungu atawaonyesha makao ya Firauni na watu wake baada ya kuangamizwa kwao. Nyingine inasema kuwa atawaonyesha ardhi ya Sham iliyokuwa mikononi mwa waabudu mizimu wakati huo.

سَأَصْرِفُ عَنْ آيَاتِيَ الَّذِينَ يَتَكَبَّرُونَ فِي الْأَرْضِ بِغَيْرِ الْحَقِّ وَإِن يَرَوْا كُلَّ آيَةٍ لَّا يُؤْمِنُوا بِهَا وَإِن يَرَوْا سَبِيلَ الرُّشْدِ لَا يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا وَإِن يَرَوْا سَبِيلَ الْغَيِّ يَتَّخِذُوهُ سَبِيلًا ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا عَنْهَا غَافِلِينَ ﴿١٤٦﴾

146. Nitawatenga na ishara zangu wale wanaofanya kiburi katika ardhi pasipo haki. Na wakiona kila ishara hawaiamini; na wakiona njia ya uongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wao wamezikadhibisha ishara zetu na wameghafilika nazo.

وَالَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَلِقَاءِ الْآخِرَةِ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ هَلْ يُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٤٧﴾

147. Na wale waliozikadhibisha ishara zetu na mkutano wa akhera, amali zao zime- poromoka. Kwani watalipwa isipokuwa yale waliyokuwa wakiyatenda?

وَاتَّخَذَ قَوْمُ مُوسَىٰ مِن بَعْدِهِ مِنْ حُلِيِّهِمْ عِجْلًا جَسَدًا لَّهُ خُوَارٌ أَلَمْ يَرَوْا أَنَّهُ لَا يُكَلِّمُهُمْ وَلَا يَهْدِيهِمْ سَبِيلًا اتَّخَذُوهُ وَكَانُوا ظَالِمِينَ ﴿١٤٨﴾

148. Na baada yake watu wa Musa walimfanya ndama kutokana na mapambo yao, kiwiliwili kilichokuwa na sauti, Je, hawakuona kwamba huyo hasemi nao wala hawaongozi njia? Walimfanya na wakawa wenye kudhulumu.

وَلَمَّا سُقِطَ فِي أَيْدِيهِمْ وَرَأَوْا أَنَّهُمْ قَدْ ضَلُّوا قَالُوا لَئِن لَّمْ يَرْحَمْنَا رَبُّنَا وَيَغْفِرْ لَنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿١٤٩﴾

149. Na walipojuta na wakaona kwamba wamekwishapotea walisema: Kama Mola wetu hataturehemu na kutusamehe bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliopata hasara.

NITAWAEPUSHIA AYA ZANGU

Aya 146 – 149

MAANA

Nitawatenga na ishara zangu wale wanaofanya kiburi katika ardhi pasipo haki.

Wenye kufanya kiburi katika ardhi ni wale wanaopinga haki na wasiotaka kutawaliwa nayo. Kusema kwake bila ya haki ni kwa ufafanuzi, sio kwa kuvua; sawa na kusema: “Na wakiwaua mitume bila ya haki.”

Neno Aya katika Qur’an mara nyingine hutumia kuwa ni Aya zenye misingi ya itikadi na hukumu ya sharia na mfano wake. Mara nyingine hutumi- ka kuwa ishara yaani hoja na dalili zenye kuthibitisha uungu na utume.

Ikiwa makusudio ni maana ya kwanza katika Aya hii tunayoifasiri, basi maana yatakuwa kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) anazihifadhi Aya na kuzilinda zisipotolewe; sawa na kauli yake: “Hakika sisi ndio tuliouteremsha ukumbusho huu na hakika ndio tutakaoulinda”

Na ikiwa makusudio ni maana ya pili, yaani ishara kwa maana ya dalili na hoja, basi maana ni kwamba baada ya wapinzani kujiepusha nazo na kuacha kuzisikiliza, basi Mwenyezi Mungu ataachana nao, wala hatawategemeza kwenye imani. Tumekwisha elezea hilo mara kadhaa; kama vile katika kufasiri Juz.5 (4:88).

Na wakiona kila ishara hawaiamini; na wakiona njia ya uongofu hawaishiki kuwa ndiyo njia; lakini wakiona njia ya upotofu wanaishika kuwa ndiyo njia. Hayo ni kwa sababu wao wamezikadhibisha ishara zetu na wameghafilika nazo.

Huu ni ubainifu wa hakika ya wenye kiburi na sababu inayowajibisha kiburi chao vilevile. Ama hakika yao ni kuwa wao hawajizuilii na uovu wala hawapondokei kwenye uongofu.

Sababu inayowajibisha hilo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaletea hoja na dalili; akawataka wazichunguze, wazizingatie na wazitumie vile inavyotakikana, wakakataa na wakaendelea kuzipinga tena bila ya kuzichunguza. Lau kwamba wao wangeliziitikia na kuzichunguza dalili hizo kungeliwapelekea kuamini na kuikubali haki; wala wasingelikua na kiburi na kufanya ufisadi katika nchi.

Na wale waliozikadhibisha ishara zetu na mkutano wa akhera, amali zao zimeporomoka. Kwani watalipwa isipokuwa yale waliyokuwa wakiyatenda?

Kila asiyemwamini Mwenyezi Mungu na kukutana na Mola wake, basi yeye ni katika wale watakaoangamia kesho na yote yale aliyokuwa akijifaharisha nayo yatakuwa si lolote. Hayo ni malipo ya ukafiri wake na inadi yake.

Yamenipendeza yale aliyoyasema mfasiri mmoja Mwenyezi Mungu amughufirie na amrehemu, namnukuu: “Kuporomoka amali kunachukuliwa kama wanavyosema: ‘Ameporomokaa ngamia.’ ikiwa amekula mmea wenye sumu na tumbo lake likafura kisha akafa.

Hiyo ndiyo sifa ilivyo kwa batili inayowatokea wenye kukadhibisha ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana na akhera, Mwongo hufura mpaka watu wanamdhania kuwa ni mkubwa mwenye nguvu, kisha huporomoka, kama alivyoporomoka yule ngamia, aliyekula mmea wa sumu.”

Na baada yake watu wa Musa walimfanya ndama kutokana na mapambo yao, kiwiliwili kilichokuwa na sauti.

Imetangulia kuelezwa katika Aya 142 kuwa Nabii Musa(a.s) alikwenda kwa miadi ya Mola wake, na kwamba yeye alimpa ukaimu nduguye Harun kwa watu wake. Vilevile imeelezwa katika Aya 138 kwamba Wana wa Israel baada ya kupita bahari walimtaka Nabii Musa awafanyie sanamu watakayoiabudu; si kwa lolote isipokuwa tu wameona ni vizuri waabudu masanamu.

Kwa hivyo mara tu Nabii Musa alipokuwa mbali nao waliitumia nafasi hiyo; Msamaria (Samiri): akakusanya mapambo ya wanawake akaten- geneza ndama; akatengeneza katika umbo ambalo liliweza kutoa sauti ya ndama.

Akawaambia huyu ni Mola wenu na Mola wa Musa; wakaingilia kumwabudu. Harun aliwakataza, lakini hakuweza kuwazuia, na hawakum- sikiliza isipokuwa wachache, Yametangulia kudokezwa hayo katika kufasiri Juz, 1 (2: 51), Pia yatakuja tena maelezo.

Aya hii tuliyo nayo, inatilia nguvu yale tuliyoyakariri katika Juzuu ya kwanza na ya pili, kuwa Israeli haithibiti ila kwenye misingi ya matamanio na hawaa; ikiwa ni kweli kuwa matamanio ni misingi.

Je, hawakuona kwamba huyo hasemi nao wala hawaongozi njia? Walimfanya na wakawa wenye kudhulumu.

Haya ndiyo mantiki ya kimaumbile na akili ambayo inakataa mtu amwabudu Mungu aliyemtengeneza kwa mkono wake, lakini waisraili hawana akili wala maumbile au dini.

Na walipojuta na wakaona kwamba wamekwishapotoea walisema: Kama Mola wetu hataturehemu na kutusamehe bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliopata hasara.

Hii ndiyo sifa nzuri pekee na ndiyo ya kwanza na ya mwisho, iliyosajiliwa na Qur’an kwa waisrael kwa ujumla, bila ya kuangalia uchache wa wachache waliomwamini Nabii Musa hadi mwisho.

Baadhi ya Wafasiri wamechukulia dhahiri toba ya Bani Israel kwamba wakati huo ilikuwa ni masalia ya maandalizi ya wema, kisha masalia hayo yakaenda; wala haikubaki athari yoyote kwao ya kuonyesha kujiandaa kwa kheri. Kuchukulia huku hakuko mbali na ukweli na kunaashiriwa na Aya isemayo:

ثُمَّ قَسَتْ قُلُوبُكُم مِّن بَعْدِ ذَٰلِكَ فَهِيَ كَالْحِجَارَةِ أَوْ أَشَدُّ قَسْوَةً ﴿٧٤﴾

“Kisha nyoyo zenu zikawa ngumu baada ya hayo, zikawa kama mawe au ngumu zaidi” Juz.1(2: 74)

Aya hii ni baada ya kisa cha ng’ombe ambacho kilitokea baada ya kuabudu ndama.


5

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

وَلَمَّا رَجَعَ مُوسَىٰ إِلَىٰ قَوْمِهِ غَضْبَانَ أَسِفًا قَالَ بِئْسَمَا خَلَفْتُمُونِي مِن بَعْدِي أَعَجِلْتُمْ أَمْرَ رَبِّكُمْ وَأَلْقَى الْأَلْوَاحَ وَأَخَذَ بِرَأْسِ أَخِيهِ يَجُرُّهُ إِلَيْهِ قَالَ ابْنَ أُمَّ إِنَّ الْقَوْمَ اسْتَضْعَفُونِي وَكَادُوا يَقْتُلُونَنِي فَلَا تُشْمِتْ بِيَ الْأَعْدَاءَ وَلَا تَجْعَلْنِي مَعَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿١٥٠﴾

150. Aliporudi Musa kwa watu wake naye ameghadhibika na kuhuzunika. Akasema: Ni uovu ulioje mlionifanyia nyuma yangu! Je, mmeitangulia amri ya Mola wenu na akazitupa mbao na akamkata kichwa ndugu yake akimvuta kwake. Akasema: Ewe mtoto wa mama yangu! Hakika watu hawa wamenidharau na wakakaribia kuniua. Basi usiwafurahishe maadui juu yangu wala usinifanye pamoja na watu madhalimu.

قَالَ رَبِّ اغْفِرْ لِي وَلِأَخِي وَأَدْخِلْنَا فِي رَحْمَتِكَ وَأَنتَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ ﴿١٥١﴾

151. Akasema: Mola wangu! Nisamehe mimi na ndugu yangu na utuingize katika rehema yako na wewe ni mwenye kurehemu kushinda wote wenye kurehemu.

إِنَّ الَّذِينَ اتَّخَذُوا الْعِجْلَ سَيَنَالُهُمْ غَضَبٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَذِلَّةٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي الْمُفْتَرِينَ ﴿١٥٢﴾

152. Hakika wale walioabudu ndama, itawapata ghadhabu kutoka kwa Mola wao na madhila katika maisha ya dunia, Na hivyo ndivyo tunavyowalipa wazushi.

وَالَّذِينَ عَمِلُوا السَّيِّئَاتِ ثُمَّ تَابُوا مِن بَعْدِهَا وَآمَنُوا إِنَّ رَبَّكَ مِن بَعْدِهَا لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٥٣﴾

153. Na wale waliotenda maovu, kisha wakatubia baada yake na wakaamini, hakika Mola wako baada ya hayo ni mwenye kusamehe mwenye kurehemu.

وَلَمَّا سَكَتَ عَن مُّوسَى الْغَضَبُ أَخَذَ الْأَلْوَاحَ وَفِي نُسْخَتِهَا هُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلَّذِينَ هُمْ لِرَبِّهِمْ يَرْهَبُونَ ﴿١٥٤﴾

154. Na ilipomtulia ghadhabu Musa, aliziokota zile mbao na katika maandiko yake mna uongozi na rehema kwa wanaomwogopa Mola wao.

ALIPORUDI MUSA KWA WATU WAKE

Aya 150-154

MAANA

Aliporudi Musa kwa watu wake naye ameghadhibika na kuhuzunika.

Nabii Musa(a.s) alipokuwa mlimani akizungumza na Mola wake mtuku- fu, alipewa habari na Mola wake kuwa watu wake wameabudu ndama baada yako; kama inavyofahamisha Aya isemayo:

قَالَ فَإِنَّا قَدْ فَتَنَّا قَوْمَكَ مِن بَعْدِكَ وَأَضَلَّهُمُ السَّامِرِيُّ ﴿٨٥﴾ فَرَجَعَ مُوسَىٰ إِلَىٰ قَوْمِهِ غَضْبَانَ أَسِفًا ﴿٨٦﴾

“Akasema: Sisi tumewatia mtihani watu wako bada yako na Msamaria amewapoteza. Nabii Musa akarudi kwa watu wake kwa ghadhabu na kusikitika.” (20:85-86).

Ghadhabu ilidhihiri kwa kusema:Ni uovu ulioje mlionifanyia nyuma yangu! Je, mmeitangulia amri ya Mola wenu.

Aliwaacha kwenye Tawhid, lakini aliporudi aliwakuta kwenye shirk.

Ama amri ya Mola wao ambayo hawakuingoja ni kumngoja Nabii Musa siku arubaini.

Hii inafahamishwa na Aya isemayo:

أَفَطَالَ عَلَيْكُمُ ﴿٨٦﴾

“Je, umekuwa muda mrefu kwenu?” (20:86).

Kama ambavyo ghadhabu yake ilidhihiri kwa kauli, Vilevile ilidhihiri kwa vitendo:

Na akazitupa mbao na akamkamata kichwa ndugu yake akimvuta kwake.

Wamesema baadhi ya maulama kuwa Nabii Musa alitupa Tawrat nayo ina jina la Mwenyezi Mungu na akamvuta nduguye Harun naye ni mja mwema. Imekuwaje na Nabii Musa ni ma’sum? Baada ya kujiuliza huku wakaanza kuleta taawili na kutafuta sababu.

Ama sisi hatu hatuleti taawili wala kutafuta sababu, bali tunayaacha maneno na dhahiri yake. Kwa sababu isma haibadilishi tabia ya maumbile ya binadamu na kumfanya ni kitu kingine wala haimuondolei sifa ya kuridhia na kukasirika hasa ikiwa ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu; tena ikiwa ni ghafla kama ilivyomjia Nabii Musa(a.s) .

Amekaa na watu siku nyingi akiwafundisha tawhid na dini ya Mwenyezi Mungu, kiasi cha kutulia imani yao; halafu ghafla tu waache yote na waingie kwenye shirki bila ya sababu yoyote ya maana.

Wengine wamesema kuwa Nabii Musa alikuwa mkali na Haruna alikuwa mpole. Sisi tunasemaNabii Musa alikuwa mwenye azma kubwa, mwenye nguvu ya alitakalo na mwenye kujiamini; na Haruna naye alikuwa chini kidogo ya Nabii Musa kulingana na masilahi.

Akasema: Ewe mtoto wa mama yangu! Hakika watu hawa wamenidharau na wakakaribia kuniua. Basi usiwafurahishe maadui juu yangu wala usinifanye pamoja na watu madhalimu.

Anakusudia madui ni wale walioabudu ndama; kama kwamba anamwambia nduguye: unachinganya mimi na maadui zangu na maadui zako, tena unanivuta mbele yao wanicheke. Vipi unanichanganya nao kwenye hasira zako na mimi niko mbali nao na vitendo vyao? Tena nimewapinga na wala sikuzembea kuwapa nasaha na tahadhari!

Hapo Nabii Musa akarudi chini na kumuonea huruma nduguye, akasema: Mola wangu! Nisamehe mimi na ndugu yangu na utuingize katika rehema yako na wewe ni mwenye kurehemu kushinda wote wenye kurehemu.

Alijiombea maghufira yeye mwenyewe kwa ukali wake kwa nduguye, kisha akamuombea maghufira nduguye kwa kuhofia kuwa hakufanya bidii ya kuwazuia na shirk. Bila shaka Mwenyezi Mungu, aliitikia maombi ya Nabii Musa kwa sababu yeye ni mwenye kurehemu kushinda wenye kurehemu; na pia kujua kwake ikhlasi ya Nabii Musa na nduguye Harun.

Hakiaka wale walioabudu ndama, itawapata ghadhabu kutoka kwa Mola wao na madhila katika maisha ya dunia. Na hivyo ndivyo tunavyowalipa wazushi

Unaweza kuuliza kuwa : dhahiri ya Aya hii nikuwa wale walioabudu ndama wamekasirikiwa na Mwenyezi Mungu na hali wao walitubia na kuomba maghufira; kama ilivyoeleza Aya ya 149 ya Sura hii na Aya nyingine inasema:

ثُمَّ إِنَّ رَبَّكَ لِلَّذِينَ عَمِلُوا السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ تَابُوا مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ وَأَصْلَحُوا إِنَّ رَبَّكَ مِن بَعْدِهَا لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١١٩﴾

“Kisha hakika Mola wako kwa waliotenda uovu kwa ujinga; kisha wakatubia baada ya hayo na wakatenda mema; bila shaka Mola wako ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu” (16:119).

Kwa hiyo vipi walazimiane na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu ya milele na laana ya daima?

Baadhi wamejibu kuwa : waabudu ndama waligawanyika mafungu mawili baada ya kurudi Nabii Musa, Kundi moja lilitubia toba sahihi. Hao ndio waliosamhewa na Mwenyezi Mungu. Na wengine waling’ang’ania ushirikina; kama vile Msamaria na wafuasi wake. Hawa ndio waliokasirikiwa na Mwenyezi Mungu na akawadhalilisha katika maisha ya duniani.

Ilivyo ni kwamba kwenye Aya hakuna ufahamisho wowote wa makundi haya. Jibu linalonasibu zaidi ni kuwa Mwenyezi Mungu alijua kuwa Mayahudi milele hawatubii wala hawatatubia toba ya kiuhakika ambayo hawatarudia. Hakia hii inafahamishwa na tabia yao na sera yao. Kwani wao walikuwa na wanaendelea kuwa ni watu wasiokatazika wala kukanyika na ufisadi na upotevu ila kwa kutumia nguvu peke yake.

Swali la pili : Mayahudi leo wanayo dola inayoitwa Israil, kwa hiyo hawana udhalili; je hili si jambo linalopingana na dhahiri ya Aya?

Jibu : Hapana! Tena hapana! Hakuna dola wala haitakuwa dola ya Mayahudi milele; kama kilivyosajili kitabu cha Mwenyezi Mungu. Israil sio dola, kama dola nyingine; isipokuwa ni kambi ya jeshi; kama vile askari wa kukodiwa waliowekwa na wakoloni kulinda masilahi yao na kuvunja nguvu za wazalendo. Tumeyathibitisha hayo katika kufasiri Juz.4 (3:112) na Juzuu nyenginezo.

Vilevile katika kitabu Min huna wa hunaka (Huku na huko) mlango wa man baa’ dinahu li shaitan (Mwenye kumuuzia dini yake shetani)

Na wale waliotenda maovu, kisha wakatubia baada yake na wakaami- ni, hakika Mola wako baada ya hayo ni mwenye kusamehe mwenye kurehemu.

Maana ya Aya yako wazi, na mfano wake umekwishapita mara nyingi. Lengo la kutajwa kwake baada ya Aya iliyotangulia ni kutilia mkazo kwamba mwenye kutubia na akarudi kwa Mola wake kwa ikhlasi na asirudie maasi, kama walivyofanya waisrail, basi Mwenyezi Mungu (s.w.t) atamrehemu, awe ni mwisraili au Mkuraysh n.k.

Na ilipomtulia ghadhabu Musa, aliziokota zile mbao na katika maandiko yake mna uongozi na rehema kwa wanaomwogopa Mola wao.

Nabii Musa ni Mtume aliye ma’sum, hilo halina shaka, lakini yeye ni binadamu, anahuzunika na kufurahi, anridhia na kukasirika. Hasira zilimpanda alipoona watu wake wamertadi dini ya Mwenyezi Mungu. Hasira aliiacha alipombwa na ndugu yake, Harun; na Mungu akamwahidi kuwaadhibu walortadi.

Baada ya Nabii Musa kurudia hali yake ya kawaida, alizirudia zile mbao alizokuwa amezitupa alipokuwa amekasirika na akatulizana kutokana na yaliyomo ndani yake katika uongofu kwa yule ambaye moyo wake utaifungukia kheri na rehema zilizomo kwa yule anayeogopa adhabu ya Mwenyezi Mungu. Hekima ya Mwenyezi Mungu imepitisha kumpa radhi na rehema kila mwenye kumtii kwa kuogopa adhabu yake, na kumletea adhabu na mateso kila mwenye kuasi kwa kubweteka na rehema yake.

وَاخْتَارَ مُوسَىٰ قَوْمَهُ سَبْعِينَ رَجُلًا لِّمِيقَاتِنَا فَلَمَّا أَخَذَتْهُمُ الرَّجْفَةُ قَالَ رَبِّ لَوْ شِئْتَ أَهْلَكْتَهُم مِّن قَبْلُ وَإِيَّايَ أَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ السُّفَهَاءُ مِنَّا إِنْ هِيَ إِلَّا فِتْنَتُكَ تُضِلُّ بِهَا مَن تَشَاءُ وَتَهْدِي مَن تَشَاءُ أَنتَ وَلِيُّنَا فَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا وَأَنتَ خَيْرُ الْغَافِرِينَ ﴿١٥٥﴾

155. Na Musa akachagua watu sabini katika kaumu yake kwa miadi yetu. Lilipowashika tetemeko alisema: Mola wangu! Lau ungetaka ungeliwaangamiza wao na mimi zamani. Unatuangamiza kwa sababu ya yale waliyoyafanya wajinga katika sisi? Halikuwa hilo ila ni adhabu yako, humpoteza kwayo umtakaye na kumwongoza umtakaye, Wewe ndiye mlinzi wetu. Basi tughufurie na uturehemu nawe ndiye bora wa kughufiria.

وَاكْتُبْ لَنَا فِي هَـٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الْآخِرَةِ إِنَّا هُدْنَا إِلَيْكَ قَالَ عَذَابِي أُصِيبُ بِهِ مَنْ أَشَاءُ وَرَحْمَتِي وَسِعَتْ كُلَّ شَيْءٍ فَسَأَكْتُبُهَا لِلَّذِينَ يَتَّقُونَ وَيُؤْتُونَ الزَّكَاةَ وَالَّذِينَ هُم بِآيَاتِنَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٥٦﴾

156. Na utuandikie mema katika dunia hii na katika akhera, Sisi tunarejea kwako. Akasema: Adhabu yangu nitamsibu nayo nimtakaye; na rehema yangu imekienea kila kitu. Nitaiandika kwa ajili ya wale wanaoogopa, na wanaotoa Zaka na wanaoziamini ishara zetu.

الَّذِينَ يَتَّبِعُونَ الرَّسُولَ النَّبِيَّ الْأُمِّيَّ الَّذِي يَجِدُونَهُ مَكْتُوبًا عِندَهُمْ فِي التَّوْرَاةِ وَالْإِنجِيلِ يَأْمُرُهُم بِالْمَعْرُوفِ وَيَنْهَاهُمْ عَنِ الْمُنكَرِ وَيُحِلُّ لَهُمُ الطَّيِّبَاتِ وَيُحَرِّمُ عَلَيْهِمُ الْخَبَائِثَ وَيَضَعُ عَنْهُمْ إِصْرَهُمْ وَالْأَغْلَالَ الَّتِي كَانَتْ عَلَيْهِمْ فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿١٥٧﴾

157. Ambao wanamfuata Nabii asiyesoma wala kuandika ambaye wanamkuta ameandikwa kwao katika Tawrat na Injili ambaye anawaamrisha mema na anawakataza maovu, na anawaahalalishia vizuri na kuwaharamishia vibaya, na kuwaondolea mizigo yao na minyororo iliyokuwa juu yao. Basi wale walioamini na wakamheshimu na wakamsaidia na wakafuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye, Hao ndio wenye kufaulu.

HAIKUWA ILA NI ADHABU YAKO

Aya 155 – 157

MAANA

Na Musa akawachagua watu sabini katika kaumu yake kwa miadi yetu.

Wafasiri wamerefusha maneno kuhusu Aya hii na zikagongana kauli zao katika kuifasiri. Wakatofautiana katika kubainisha miadi, kuwa je, ni miadi ya kuteremshwa Tawrat au mingine?

Vilevile wametofautiana kuwa ni kwa nini Nabii Musa aliwachagua watu sabini katika watu wake, Je, ni kwa kuwa wao walimtuhumu Nabii Musa na kumwambia hatutakuamini mpaka tusikie maneno ya Mwenyezi Mungu kama unavyosikia wewe; ndipo akasuhubiana nao ili asikie, kama alivyosikia; au ni kwa sababu nyingine?

Vilevile wametofautiana wafasiri katika sababu ambayo aliwaadhibu Mwenyezi Mungu, Hatimae wakahitalifiana kuwa je, mtetemeko uliwaua au ulikurubia tu kuvunja migongo yao, lakini hawakufa?

Katika Aya hakuna kidokezo chochote cha yale waliyoyachagua kikundi katika wafasiri. Linalofahamika ni kuwa tu, Nabii Musa aliwachagua watu sabini ili aende nao kwa miadi ya Mola wake. Kwa hali ilivyo ni kuwa uchaguzi huo ulikuwa ni kwa amri ya Mwenyezi Mungu, kwa sababu Nabii Musa hafanyi ila aliloamrishwa; na kwamba Mwenyezi Mungu ali- wateremshia hao sabini aina ya adhabu kulingana na hekima ilivyoka.

Basi hatuna cha kuthibitisha miadi ilivyo kuwa wala sababu ya kuchagua au ya adhabu.

Ni kweli kwamba kauli ya Nabii Musa kumwambia Mwenyezi Mungu:Unatuangamiza kwa sababu ya yale waliyoyafanya wapumbavu katika sisi? inafahamisha kwamba wao walifanya yaliyowajibisha maangamizi, lakini halikubainishwa walilolifanya; nasi hatuna haki ya kusema tusiyoyajua.

Lilipowashika tetemeko alisema: Mola wangu! Lau ungetaka ungeli- waangamiza wao na mimi zamani!

Nabii Musa alichagua watu sabini walio bora katika watu wake akaenda nao kwenye miadi ya Mola wake, walipofika huko wakaangamia wote akabakia, peke yake. Hilo ni tatizo la kukatisha tamaa hakuna la kufanya tena. Je, arudi peke yake kwa wa Israel? Atawajibu nini wakimuuliza watu wao?

Hakuna kimbilio kabisa isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu. Basi akanyenyekea kwa Mwenyezi Mungu amwondolee tatizo hilo na akatamani lau Mwenyezi Mungu angelimwangamiza pamoja nao kabla ya kuja nao hapa.

Kisha akasema kumwambia mtukufu aliye zaidi:

Unatuangamiza kwa sababu ya yale waliyoyafanya wajinga katika sisi?

Yaani wewe ni mtukufu na mkuu kuliko kufanya hivyo. Kwa sababu wewe ni Mpole na Mkarimu.

Halikuwa hilo ila ni adhabu yako, humpoteza kwayo umtakaye na humwongoza umtakaye.”

Neno Fitna lililofasiriwa adhabu hapa, lina maana nyingi; ikiwemo upote- vu na ufisadi; kama ilivyo katika Aya ya 26 ya Sura hii. Maana nyingine ni kupigana na majaribu, mara nyingi hutumiwa kwa maana ya adhabu; kama anavyosema Mwenyezi Mungu:

وَاتَّقُوا فِتْنَةً لَّا تُصِيبَنَّ الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنكُمْ خَاصَّةً ﴿٢٥﴾

“Na jikingeni na adhabu ambayo haitawasibu waliodhulumu peke yao” (8:25).

Haya ndiyo makusudio yake katika Aya hii tuliyonayo, Dhamir ya hilo inarudia tetemeko ambalo limekwishatajwa. Maana ya kumpoteza amtakaye, ni kuwa Mwenyezi Mungu humpelekea tetemeko, ambalo ndio adhabu, yule amtakaye katika waja wake, na maana ya kumwongoza ni kumwepushia tetemeko amtakaye.

Maana ya kijumla ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) huteremsha adhabu kwa amtakaye anayestahiki na kumwondolea asiyestahiki. Kwa hiyo inatubainikia kuwa kauli yake halikuwa hilo ila ni adhabu yako, maana yake yanafungamana na yaliyotangulia na yaliyo baada yake; na kwamba haijuzu kuitolea dalili kuwa upotevu unatokana na Mwenyezi Mungu.

Vipi Mwenyezi Mungu ampoteze mtu kisha amwaadhibu kwa upotevu huo? Na hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kutaka kuwadhulumu waja. Hakika Shetani ni adui mwenye kupoteza na inatosha kuwa Mola wako ni mwongozi na mwenye kunusuru.

Kwa maelezo zaidi rudia Juz.1 (2:26).

Wewe ndiye mlinzi wetu, Basi tughufurie na uturehemu nawe ndiwe bora wa kughufuria. Na utuandikie mema katika dunia hii na katika akhera. Sisi tunarejea kwako”

Hakuna tafsir bora ya Munajat huu, kama kauli ya bwana wa mashahidi, Imam Husein bin Ali(a.s) wakati alipozungukwa na maelfu kila upande akiwa peke yake. Akakimbilia kwa Mola wake na kumtaka hifadhi dhidi ya maadui zake akisema:

“Ewe Mola wangu wewe ndiye matarajio yangu katika kila shida, Kila jambo lililonishukia wewe ni tegemeo, Ni matatizo mangapi ya kukatisha tamaa, ya kuondokewa na marafiki na kufuatwa na maadui, uliyoniteremshia, kisha nikakushitakia wewe, kwa kuwa sina mwingine zaidi yako, nawe ukanitatulia na kunifariji! Basi wewe ndiye mtawalia kila neema,mwenye kila hisani na mwisho wa matakwa yote!”

Akasema: Adhabu yangu nitamsibu nayo nimtakaye katika wananostahiki adhabu.

Kwa sababu matakwa ya Mwenyezi Mungu yanapitia kwenye haki na uadilifu tu, hakuna mchezo wala dhulma mbele ya Mwenyezi Mungu.

Razi anasema: “Amesoma Hasan: Usibu bihi man Asaa kwa sin (nitam- sibu nayo mwenyewe kufanya uovu), na Shafii amechagua kisomo hiki.”

REHMA YA MWENYEZI MUNGU INAMFIKIA IBLISII

Qur’an hutumia neno Rehma ya Mwenyezi Mungu kwa maana ya msaada wake na kwa thawabu zake. Maana ya usaidizi kutoka kwake Mwenyezi Mungu ni kwamba vitu vyote vilivyoko, hata Iblisi, vinamhitajia Mwenyezi Mungu katika kubakia kwake na kuendelea kwake; kama ambavyo vinamhitajia yeye katika asili ya kupatikana kwake, na kwamba yeye ndiye anayevisaidia kubaki wakati wote, kiasi ambacho lau msaada wake huo utakiepuka kitu kitambo kidogo cha mpepeso wa jicho, basi kitu hicho hakitakuwako tena.

Ufafanuzi zaidi wa rehma hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّـهُ النَّاسَ بِمَا كَسَبُوا مَا تَرَكَ عَلَىٰ ظَهْرِهَا مِن دَابَّةٍ وَلَـٰكِن يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ﴿٤٥﴾

“Lau Mwenyezi Mungu angeliwachukulia watu kwa waliyoyachuma, asin- geliacha juu ya ardhi hata mnyama mmoja” (35:45).

Rehma hiyo ndiyo iliyokusudiwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu:Na rehma yangu imekienea kila kitu hata Iblisi aliyelaaniwa. Ama rehma kwa maana ya thawabu, Mwenyezi Mungu (s.w.t) humpa anayemwamini na kumcha. Ndiyo aliyoiashiria kwa kusema kwake. Nitaiandika kwa ajili ya wale wanaoogopa maasi na wakafuata amri ya Mwenyezi Mungu na kuacha makatazo yake.

Na wanaotoa Zaka.

Ametaja Zaka badala ya Swala. Kwa sababu mtu hupituka mpaka kwa kujiona amejitoshea.

Na wanaoziamini ishara zetu ambao wanamfuata Nabii asiyesoma wala kuandika.

Rehma ya Mwenyezi Mungu ambayo ni kwa maana ya thawabu haipati isipokuwa mwenye kumwogopa Mwenyezi Mungu, akatoa mali kwa kupenda kwake na akauamini utume wa Nabii Muhammad(s.a.w.w) kama utamfikia ujumbe wake.

Amehusisha kutaja mali kutokana na tulivyoyadokezea, na pia kuwa mazungumzo ni ya Mayahudi ambao mali ndio Mola wao hakuna mwingine isipokuwa yeye. Mwenyezi Mungu amemsifu Nabii Muhammad(s.a.w.w) , katika Aya hii kwa sifa hizi zifuatazo:-

1.Nabii Asiyesoma Wala Kuandika.

Hiyo ni sifa inayomhusu yeye tu, kinyume cha Mitume wengine, kutambulisha kuwa licha ya kuwa hivyo lakini amewatoa watu kutoka katika giza mpaka kwenye mwangaza, akaathiri maisha ya umma wote wakati wote na mahali kote.

2.Ambaye Wanamkuta Ameandikwa Kwao Katika Tawrat Na Injil.

Rudia Juz.1 (2:136) na Juz.6 (4:163).

3.Ambaye Anawaamrisha Mema Na Anawakataza Maovu.

Rudia Juz, 4 (3:104 - 110).

4.Na Anawahalalishia Vizuri Na Kuwaharamishia Vibaya.

5.Na Kuwaondolea Mizigo Na Minyororo Iliyokuwa Juu Yao.

Makusudio ya minyororo ni mashaka. Mwenyezi Mungu aliwaharamishia waisrail baadhi ya vitu vizuri, vilivyodokezwa kwenye Juz.8 (6:146); kama ambavyo sharia ya Nabii Musa ilikuwa ngumu na yenye mashaka; kiasi kwamba mwenye kutubia katika waisrael hakubaliwi toba yake ila kwa kujiua:

فَتُوبُوا إِلَىٰ بَارِئِكُمْ فَاقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ ﴿٥٤﴾

“Basi tubuni kwa Muumba wenu na jiueni” Juz.1 (2:54).

Kwa hiyo Mwenyezi Mungu amewaambia waisrael ambao wamemkuta Nabii Muhammad(s.a.w.w) kwamba wao wakisilimu watahalalishiwa vizuri vilivyokuwa haramu, na atawaondolea mashaka katika taklifa. Kwa sababu Nabii Muhammad ametumwa na sharia nyepesi isiyo na mikazo.

Basi wale waliomwamini.

Makusudio ni waliomwamini Nabii Muhammad(s.a.w.w) miongoni mwa Mayahudi na wengine.

Na wakamheshimu.

Yaani kumsaidia katika mwito wake na kumheshimu kwa cheo chake.

Na wakamsaidia juu ya maadui zake.

Na wakafuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye.

Yaani wakafanya matendo kwa mujibu wa Qur’an.Hao ndio wenye kufaulu duniani na akhera.


6

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

قُلْ يَا أَيُّهَا النَّاسُ إِنِّي رَسُولُ اللَّـهِ إِلَيْكُمْ جَمِيعًا الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ يُحْيِي وَيُمِيتُ فَآمِنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ النَّبِيِّ الْأُمِّيِّ الَّذِي يُؤْمِنُ بِاللَّـهِ وَكَلِمَاتِهِ وَاتَّبِعُوهُ لَعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ ﴿١٥٨﴾

158. Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi nyote, ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, hapana Mola ila yeye, ndiye ahuyishaye na ndiye afishaye, basi mwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake asiyesoma wala kuandika ambaye humuamini Mwenyezi Mungu na maneno yake. Na mfuateni ili mpate kuongoka.

وَمِن قَوْمِ مُوسَىٰ أُمَّةٌ يَهْدُونَ بِالْحَقِّ وَبِهِ يَعْدِلُونَ ﴿١٥٩﴾

159. Na katika kaumu ya Musa kuna umma unaoongoza kwa haki, na kwayo hufanya uadilifu.

MTUME WA MWENYEZI MUNGU KWENU NYOTE

Aya 158 – 159

MAANA

Sema: Enyi watu! Hakika mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi nyote.

Aya hii imeshuka Makka katika Sura ya Makka, Inakadhibisha wale waliosema kuwa Nabii Muhammad(s.a.w.w) alipokuwa dhaifu, alisema mimi ni Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya watu wa Makka na walio viungani mwake, na baada ya kuwa na nguvu, eti ndio akasema mimi ni Mtume wa watu wote. Tumewajibu hao kwa jibu mkataa katika kufasiri Juz.7 (6:92).

Amabaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, hapana Mola ila yeye, ndiye ahuyishaye na ndiye afishaye.

Aya hii na nyingine nyingi inatilia makazo na kusisitiza kuwa hakuna wa katikati baina ya Mwenyezi Mungu na waja wake, na kwamba milki na amri ni ya Mwenyezi Mungu peke yake.

Kwa hiyo Nabii Muhammad(s.a.w.w) , ingawaje ni Mtume wa watu wote, wakati wote na mahali popote na ni mtukufu wa viumbe na mwisho wa Mitume na bwana wao, lakini yeye mwenyewe hajimiliki chochote, sikwambii mwingine tena.

Mwenyezi Mungu anasema:

قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي ضَرًّا وَلَا نَفْعًا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ ﴿٤٩﴾

“Sema sijimilikii nafsi yangu madhara wala kwa manufaa ila apendavyo Mwenyezi Mungu” (10: 49)

Maana haya yamekaririka katika Aya kadhaa, na makusudio yake ni kuwafahamisha waislamu hakika ya Nabii Muhammad(s.a.w.w) na kwamba yeye ni mtu kama wao, ili wasijingize sana kwake waislamu kama walivyojingiza Wakristo kwa Bwana Masih(a.s) .

Tamko Lailaha illallah nabii Muhammadu-rasulullah (Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, Nabii Muhammad ni Mtume wa mwenyezi Mungu) wanalolikariri Waislamu usiku na mchana, linatosha kuwa ni dalili ya kuepukana Waislamu na kujingiza sana, na vilevile kuamini kwao kuwa Nabii Muhammad(s.a.w.w) hamiliki jambo lolote zaidi ya Utume na kufikisha (tabligh).

Basi mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake asiyesoma wala kuandika ambaye anamwamini Mwenyezi Mungu na maneno yake. Na mfuateni ili mpate kuongoka.

Kusema kwake mfuateni baada ya kusema kwake basi mwaminini, ni dalili kwamba imani tu haitoshi kitu bila ya kuwa na vitendo vinavyofuata Kitab cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake, Rudia Juz.2 (2:212) kifungu ‘hakuna imani bila ya takuwa.’

UZAYUNI NA UYAHUDI

Na katika kaumu ya Musa kuna umma unaoongoza kwa haki, na kwayo hufanya uadilifu.

Razi anasema: “Wametofautiana kuhusu umma huo, ulipatikana lini, na wapi? Ikasememkana kuwa ni Mayahudi waliomwamini Nabii Muhammad(s.a.w.w) , kama vile Abdallah bin Salam na bin Suria. Na imesemekana kuwa ni watu waliothibiti kwenye dini ya Nabii Musa bila ya kugeuza, kama walivyofanya wengineo waliozusha mambo.”

Sisi tuko katika upande wa hao wasemao kuwa ni waliokuwa katika wakati wa Nabii Musa, kisha wakaisha, kama linavyodokeza neno lake Mwenyezi Mungu: Na katika kaumu ya Nabii Musa. Ama bin Salam na bin Suria hao wawili wala kumi mfano wao hawawezi kuitwa umma au kundi.

Kwa vyovyote iwavyo, Qur’an katika Aya kadhaa imewapa Mayahudi kila sifa mbaya, na kuiambatanisha historia yao kuwa ya aibu. Kwa hiyo linalofahamika kutokana na kauli, katika kaumu ya Nabii Musa ni kuwa katika desturi yoyote kunapatikana nadra; na nadra haibadilishi kawaida, baliinatilia nguvu.

Hata kama tutaifungia macho Qur’an Tukufu yenye hekima, kwani ufisadi na upotevu uko mbali na tabia na sera ya Mayahudi? Je, Mayahudi wametakata na upotevu na kujifanya? Bali historia ya Mayahudi ina kitu hata kimoja kinachotambulisha kheri? Pengine mtu anaweza kusema kuwa ufisadi ni sifa inayolazimiana na uzayuni kwa vile ni harakati za siasa za ubaguzi na ufashisti zenye lengo la kuhudumia na kueneza ukoloni. Lakini Uyahudi ni dini tu, kama dini nyingine.

Jibu :Kwanza , kwani hatujui kuwa chimbuko la tofauti hii ni Mayahudi wenyewe ili wajikinge na historia yao ya zamani na sasa, ya aibu, inayoambatana nao. Rudia Juz.6 (5:64).

Pili , kukadiria kuweko na tofauti baina ya Uyahudi na Uzayuni, ni jambo ambalo haliwezekani. Je, Mayahudi kwa ujumla wanauridhia au wanachuikia Uzayuni ambao umejisheheneza silaha, kwa jina la Israel, wenye lengo la kuuhami ukoloni na kupinga ukombozi?

Kwa nini basi Mayahudi wameusaidia Uzayuni kwa hali na mali na kujitolea wake kwa waume, baada ya kujifundisha silaha kali, katika vita vya tarehe 5 Juni 1967?

Tena je, si Mayahudi wanaoamini kidini na kiitikadi kwamba wao ni taifa teule la Mwenyezi Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu yuko upande wao dhidi ya watu wote, na kwamba Mwenyezi Mungu ameharamisha damu zao na kuwahalalalishia wao damu za watu wengine wote, na kwamba wao wameweka kanuni zao na nidhamu zao juu ya misingi hii na watekelezaji ni Israel?

Baada ya hayo, Uyahudi ni dini kama dini nyingine, iliyoteremshwa kwa Nabii Musa(a.s) , lakini imekwisha na wamekwisha watu wake, hakuna aliyebakia; kama zilivyokwisha dini nyingine. Uyahudi wa leo ni Uzayuni isipokuwa nadra sana, na kama tulivyotangulia kusema kuwa nadra sio kipimo.

وَقَطَّعْنَاهُمُ اثْنَتَيْ عَشْرَةَ أَسْبَاطًا أُمَمًا وَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ إِذِ اسْتَسْقَاهُ قَوْمُهُ أَنِ اضْرِب بِّعَصَاكَ الْحَجَرَ فَانبَجَسَتْ مِنْهُ اثْنَتَا عَشْرَةَ عَيْنًا قَدْ عَلِمَ كُلُّ أُنَاسٍ مَّشْرَبَهُمْ وَظَلَّلْنَا عَلَيْهِمُ الْغَمَامَ وَأَنزَلْنَا عَلَيْهِمُ الْمَنَّ وَالسَّلْوَىٰ كُلُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ وَمَا ظَلَمُونَا وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿١٦٠﴾

160. Na tukawagawanya katika koo kumi na mbili, mataifa mbalimbali. Na tukampa wahyi Musa walipomuomba maji watu wake kuwa lipige jiwe kwa fimbo yako. Mara zikabubujika chem-chemi kumi na mbili, na kila watu wakajua mahali pao pa kunywea. Na tukawatilia kivuli kwa mawingu na tukawateremshia manna na salwa, Kuleni katika vizuri tulivyowaruzuku. Wala hawakutudhulumu bali, wamejidhulumu wenyewe.

وَإِذْ قِيلَ لَهُمُ اسْكُنُوا هَـٰذِهِ الْقَرْيَةَ وَكُلُوا مِنْهَا حَيْثُ شِئْتُمْ وَقُولُوا حِطَّةٌ وَادْخُلُوا الْبَابَ سُجَّدًا نَّغْفِرْ لَكُمْ خَطِيئَاتِكُمْ سَنَزِيدُ الْمُحْسِنِينَ ﴿١٦١﴾

161. Na walipoambiwa kaeni katika mji huu na kuleni humo maridhawa popote mpendapo na ingieni katika mlango (wake) kwa kunyenyekea na semeni: Tusamehe. Tutawasamehe makosa yenu na tutawazidishia wale wafanyao mazuri.

فَبَدَّلَ الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنْهُمْ قَوْلًا غَيْرَ الَّذِي قِيلَ لَهُمْ فَأَرْسَلْنَا عَلَيْهِمْ رِجْزًا مِّنَ السَّمَاءِ بِمَا كَانُوا يَظْلِمُونَ ﴿١٦٢﴾

162. Wakabadilisha wale walio dhulumu kauli isiyokuwa ile waliyoambiwa. Na ndipo tukaiteremsha juu ya wale waliodhulumu adhabu kubwa kutoka mbinguni kwa vile walivyokuwa.

TULIWAGAWANYA KOO KUMI NA MBILI

Aya 160 – 162

MAANA

Na tukawagawanya katika koo kumi na mbili, mataifa mbalimbali.

Yaani tuliwagawanya waisrael makundi kumi na mawili, kila kundi likiishia kwa wajukuu kumi na wawili wa Yaqub bin Is-Haq bin Ibrahim. Alikuwa na watoto kumi na wawili na kila mtoto alikuwa na kizazi chake.

Na tukampa wahyi Musa walipomuomba maji watu wake kuwa lipige jiwe kwa fimbo yako. Mara zikabubujika chemchem kumi na mbili, na kila watu wakajua mahali pao pa kunywea.

Umetangulia mfano wake katika Juz.1 (2:60).

Na tukawatilia kivuli kwa mawingu na tukawateremshia manna na salwa. Kuleni katika vitu vizuri tulivyowaruzuku, Wala hawakutudhulumu bali, wamejidhulumu wenyewe.

Umetangulia mfano wake katika Juz.1 (2:57), Pia zinazofuatia mfano wake uko katika Juz,1 (2: 58 - 59).

وَاسْأَلْهُمْ عَنِ الْقَرْيَةِ الَّتِي كَانَتْ حَاضِرَةَ الْبَحْرِ إِذْ يَعْدُونَ فِي السَّبْتِ إِذْ تَأْتِيهِمْ حِيتَانُهُمْ يَوْمَ سَبْتِهِمْ شُرَّعًا وَيَوْمَ لَا يَسْبِتُونَ لَا تَأْتِيهِمْ كَذَٰلِكَ نَبْلُوهُم بِمَا كَانُوا يَفْسُقُونَ ﴿١٦٣﴾

163. Na waulize habari za mji uliokuwa kando ya bahari walipokuwa wakivunja Sabato, samaki wao walipowajia juu juu siku ya Sabato na siku wasiyofanya Sabato hawakuwajia. Kama hivyo tuliwajaribu kwa sababu walikuwa wakifanya ufuska.

وَإِذْ قَالَتْ أُمَّةٌ مِّنْهُمْ لِمَ تَعِظُونَ قَوْمًا اللَّـهُ مُهْلِكُهُمْ أَوْ مُعَذِّبُهُمْ عَذَابًا شَدِيدًا قَالُوا مَعْذِرَةً إِلَىٰ رَبِّكُمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ ﴿١٦٤﴾

164. Na kikundi katika wao waliposema: Kwa nini mnawaonya watu ambao Mwenyezi Mungu atawaangamiza au atawaadhibu kwa adhabu kali? Wakasema: Ili uwe ni udhuru mbele ya Mola wenu na huenda wakawa na takua.

فَلَمَّا نَسُوا مَا ذُكِّرُوا بِهِ أَنجَيْنَا الَّذِينَ يَنْهَوْنَ عَنِ السُّوءِ وَأَخَذْنَا الَّذِينَ ظَلَمُوا بِعَذَابٍ بَئِيسٍ بِمَا كَانُوا يَفْسُقُونَ ﴿١٦٥﴾

165. Basi walipoyasahau waliyokumbushwa tuliwaokoa waliokuwa wakikataza maovu na tukawapatiliza walio dhulumu kwa adhabu kali kwa sababu walikuwa wakifanya ufuska.

فَلَمَّا عَتَوْا عَن مَّا نُهُوا عَنْهُ قُلْنَا لَهُمْ كُونُوا قِرَدَةً خَاسِئِينَ ﴿١٦٦﴾

166. Walipoasi waliyokatazwa tuliwaambia kuweni manyani wadhalilifu.

WAULIZE HABARI ZA MJI

Aya 163 – 166

MAANA

Na waulize habari za mji uliokuwa kando ya bahari.

Maneno anaambiwa Nabii Muhammad(s.a.w.w) , na mji maana yake ni watu wa mji. Dhamir ya waulize ni ya mayahudi wa Madina ambao waliishi na Mtume Nabii Muhammad(s.a.w.w) . Kwa sababu Aya hii ilishuka Madina kutokana na inavyowakabili mayahudi wa huko, imeingizwa katika Sura ya Makka kwa kukamilisha mazungumzo kuhusu mayahudi. Mwenyezi Mungu hakutaja jina la mji, Inasemekana ulikuwa kando kando ya bahari ya Sham.

Kwa vyovote iwavyo mji wenyewe unajulikana kwa Mayahudi walioulizwa na Mtume Nabii Muhammad(s.a.w.w) .

Kuna mambo mawili yaliyoyopelekea swali hili: Kwanza, ni kuwasuta mayahudi wa Madina kwamba wao wamepinga utume wake wakiwa na yakini katika nafsi zao.

Kwa vile yeye amewapa masimulizi mengi katika historia ya wakale wao, ikiwa ni pamoja na kisa hiki cha watu wa mji uiliokuwa kando ya bahari, ingawaje yeye hakusoma katika Kitab wala kusikia kwa yoyote. Ila ni wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Jambo la pili, ni kuwazindua kuwa wao wana kiburi na ni wapinzani wa haki na kwamba inadi yao hii si jambo la kushangaza, kwani ndio mazoweya yao tangu zamani.

Dalili ni kisa cha watu wa mji huo ambacho kimedokezwa na kauli yake Mwenyezi Mungu.

Walipokuwa wakivunja Sabato, samaki wao walipowajia juu juu siku ya Sabato yao na siku wasiyofanya Sabato hawakuwajia. Namna hiyo tuliwajaribu kwa sababu walikuwa wakifanya ufuska.

Ufupi wa kisa hiki ni kwamba: Mwenyezi Mungu aliwaharamishia Mayahudi kufanya kazi siku ya Sabato (Jumamosi) ikiwa ni pamoja na kuvua samaki, kwa ajili ya kuwajaribu hali yao na kuwadhihirishia watu hakika yao.

Mwenyezi Mungu alikuwa akiwapelekea samaki kwa wingi wakionekana juu juu ya maji siku ya Jumamosi na kuwazuia siku nyingine, wakafanya hila ya kuhalalisha aliyowaharamishia Mwenyezi Mungu, wakachimba mfuo unaoungana na maji na kuwavuta samaki mpaka kwenye mfuo kisha hawawezi kutoka. Wakawa wanawachukua siku ya Jumapili huku wakisema: “Tunavua siku ya Jumapili.

Wenzao wakawakataza na kuwakemea kutokana na hila hii na kuchezea dini, na wakawahadharisha na adhabu ya Mwenyezi Mungu, lakini hawakusikia.

Na kikundi katika wao waliposema: Kwa nini mnawaonya watu ambao Mwenyezi Mungu atawaangamiza au atawaadhibu kwa adhabu kali?

Yaani, kikundi katika waisrael kiliwaambia wenzao waliowakataza mambo mabaya: Kuna faida gani kuwakataza waasi na kuwahadharisha maadam hawataacha wala kuwa na hadhari? Waacheni, kwani Mwenyezi Mungu atawango’a hadi wa mwisho wao kutoka katika ardhi hii, au awabakishe na kuwaadhibu adhabu kali.

Wakasema wale wa kundi la kuamrisha mema:

Ili uwe ni udhuru mbele ya Mola wenu na huenda wakawa na takuwa.

Yaani tumewakataza maovu ili Mwenyezi Mungu ajue kuwa hatuko pamoja nao na kwamba tunachukia matendo yao; wakati huohuo tukitaraji kuwa huenda wakunufaika na makatazo na mawaidha yetu.

Basi walipoyasahau waliyokumbushwa tuliwaokoa waliokuwa wakikataza maovu na tukawapatiliza waliodhulumu kwa adhabu kali kwa vile walivokuwa wakifanya ufuska.

Mwenyezi Mungu amewasifu na ufuska, kwa vile waliasi amri yake, na waliodhulumu, kwa sababu kila anayeasi amri ya Mola wake basi huyo ameidhulumu nafsi yake. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu aliwaadhibu wakosaji kwa sababu ya madhambi yao na aliwaokoa watiifu kwa sababu ya utiifu yao.

Walipoasi waliyokatazwa, tuliwaambia: Kuweni manyani wadhalilifu.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaadhibu waasi hao kwa kuwageuza manyani. Kuna Hadith inayosema kuwa wao walibakia siku tatu, kisha wakaangamia kwa sababu mwenye kugeuzwa haishi zaidi ya muda huu wala hazai chochote jinsi yake.

Utauliza : Desturi ya Mwenyezi Mungu imepita kutomwadhibu mwenye dhambi kwa dhambi zake katika dunia, kwa ushahidi ulivyoonekana, kuongezea kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّـهُ النَّاسَ بِمَا كَسَبُوا مَا تَرَكَ عَلَىٰ ظَهْرِهَا مِن دَابَّةٍ وَلَـٰكِن يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى ﴿٤٥﴾

“Lau Mwenyezi Mungu angeliwachukulia watu kwa waliyoyachuma, asingeliacha juu ya ardhi hata mnyama mmoja” (35:45).

Kwa nini aliwaadhibu hao waliotoka kwenye twaa yake katika kuvua samaki, na kuwaacha wale waliomwaga damu za watu wasiokuwa na hatia katika Palestina na Vietnam, na kabla yake Congo, Japan na wengineo wengi wasiokuwa na idadi?

Jibu : ndio imepita desturi yake Mwenyezi Mungu mtukufu kutomuadhibu mwenye dhambi kwa dhambi zake katika maisha haya kadiri itakavyokuwa kubwa.

Na kama angefanya hivyo basi asingelipambanuka mwovu na mwema, na mwenye kuacha uovu asingelikuwa na fadhila yoyote.

Kwa sababu kuacha kutakuwa ni kwa msukumo wa hofu. Sio kupenda kheri na kuchukia shari, lakini hekima yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) imepitisha kuivua desturi hii kwa miujiza ya Mitume na kuitikia dua zao kwa waasi na wafisadi kwa vyeo vyao mbele ya Mwenyezi Mungu na kuthibitisha utume wao. Wafasiri wanasema katika kufasiri:

لُعِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن بَنِي إِسْرَائِيلَ عَلَىٰ لِسَانِ دَاوُودَ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ ذَٰلِكَ بِمَا عَصَوا وَّكَانُوا يَعْتَدُونَ ﴿٧٨﴾

“Walilaaniwa wale waliokufuru miongoni mwa wana wa Israil kwa ulimi wa Daud na wa Isa mwana wa Maryam, Hayo ni kwa sababu waliasi, nao walikuwa wakiruka mipaka.” (5:78)

Kwamba Daud(a.s) aliwalaani watu wa Ayla katika waisrael walipoasi kwa kuvua siku ya Sabato na kusema: “Ewe Mwenyezi Mungu wavishe laana mfano wa nguo” Mwenyezi Mungu akawageuza manyani.

Kwa hiyo sababu ya kugeuzwa wavuvi kuwa manyani ni dua ya Mtume Daud wala hakuna Mtume wakati huu atakayewaombea wamwagaji damu na waporaji wa mali za wananchi.

Vyovyote iwavyo, sisi tunaamini uadilifu wa Mwenyezi Mungu na kuwa haki haiendi bure, na mtu atalipwa kwa matendo yake.

وَإِذْ تَأَذَّنَ رَبُّكَ لَيَبْعَثَنَّ عَلَيْهِمْ إِلَىٰ يَوْمِ الْقِيَامَةِ مَن يَسُومُهُمْ سُوءَ الْعَذَابِ إِنَّ رَبَّكَ لَسَرِيعُ الْعِقَابِ وَإِنَّهُ لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٦٧﴾

167. Na alipotangaza Mola wako (kwamba) hakika atawaleta watu ambao watawaadhibu kwa adhabu mbaya mpaka siku ya Kiyama. Hakika Mola wako ni mwepesi wa kuadhibu na hakika yeye ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

MAYAHUDI NA ADHABU MBAYA

Aya 167

MAANA

Qur’an imezungumzia kwa urefu kuhusu waisrael, imezungumzia kufuru yao, na ufisadi wao katika ardhi, kuasi kwao haki. Nasi, kwa kufuatilia Aya tukufu, tumewazungumzia sana, tukataja mifano kadhaa ya sera yao, ikiwa ni ufafanuzi wa Qur’an kuwahusu. Lakini hapa kuna swali ambalo linapelekea shaka na kudangana kuhusu Aya hii na ile isemayo:

ضُرِبَتْ عَلَيْهِمُ الذِّلَّةُ أَيْنَ مَا ثُقِفُوا ﴿١١٢﴾

“Wamepigwa na udhalili popote wanapokutikana” Juz, 4 (3:112).

Tumelijibu swali hili katika Juz,7 (5:112). Vilevile tumelijibu kwa mfumo mwingine hivi karibuni katika kufasiri Aya 153 ya Sura hii. Hata hivyo hapa tutadokeza kwa ufupi.

Mwenyezi Mungu aliwasalitia waisrael, Mafirauni, kisha wababilon, wafursi, makhalifa wa Alexander kisha manaswara (wakristo).

Imeelezwa katika Tafsir Bahrul-Muhit kuwa kundi la manaswara walifukarika wakawauza wayahudi walio katika mji wao kwa mji ulio jirani yao.

Mwisho mayahudi wakakimbia udhalili na mateso kutaka hifadhi katika miji ya Kiarabu. Wakaishi huko kwa amani. Lakini wao wakavunja ahadi waliyopewa na Mtume(s.a.w.w) .

Baadhi wakauawa, na Umar bin Al-Khattab akawafukuza waliobaki, wakatawanyika duniani, Mashariki na Magharibi wakiwa ni wenye kufuata tu, bila ya kuwa huru, wakisikiliza amri na kuzitii wakiwa dhalili.

Hatimaye mayahudi wakaona kuwa hawatakuwa na jina isipokuwa wajitoe kwa wakoloni. Kwa ajili hii wakajiuza kwa kila mkoloni mwenye nguvu wamtekelezee njama zake.

Hivi sasa, tukiwa katika majira ya Kusi ya mwaka 1968, imegunduliwa kuwa dola moja ya kikoloni imewashauri mayahudi wa Ulaya Mashariki wafanye mageuzi ya kuendesha miji hiyo chini ya wakoloni, Mayahudi wakaanza kutekeleza njama, lakini njama zao zikafichuka kabla ya kutimia, walikaribia kuuingiza ulimwengu kwenye vita vya tatu.

Kwa ajili ya njama hizo, ndio wakoloni wakatengeneza kikosi cha silaha cha mayahudi katika ardhi ya wapalestine na kukipa jina ya dola la Israel.

Kila mwenye akili anajiuliza, Je, inafaa Israel kuitwa dola kwa maana yake sahihi, ambapo inajuliakana wazi kuwa lau wakoloni watajiepusha nayo siku moja tu, basi haitakuwako.

Je, duniani kuna dola yoyote ambayo haitambuliwi na hata dola moja inayopakana nayo? Ikiwa kweli Israel ni dola kwa nini inaishi kiuadui na kujipanua kwenye nchi jirani?

Dola hasa sio uhaini na silaha; isipokuwa kabla ya chochote, ni kuwa na tabia inayosimamia misingi ya amani, nidhamu inayotilia mkazo haki na msimamo ulio mbali na ubaguzi.

Na tabia ya Israel ni tabia ya kiaskari inayosimama kwa misingi ya vita, nidhamu yake ni kuendeleza uchokozi na msimamo wake ni uzayuni, ubaguzi, chuki, vitimbi na uhaini.

Mwandishi mmoja Mwingereza, Christopher Marlo, anasema katika tamthilia ya Kiyahudi. “Hakika mawazo ya uwezekano wa kuishi pamoja na mayahudi ni aina ya wazimu, wala hawana dawa isipokuwa upanga wenye kukata.”

Je, baada ya yote hayo waarabu wataambiwa ishini kwa amani na mayahudi au mayahudi wataambiwa ni watukufu kwa vile ni kikosi cha silaha kinachoitwa Taifa la Israel kinachoua na kuwafukuza maelfu kwa kusaidiwa na wakoloni? Ikiwa uovu ni ukarimu, basi mayahudi wako katika kilele cha utukufu na ukarimu.

Hatimaye ni Mwenyezi Mungu peke yake ndiye anayejua hatua itakayofuatia, na mwenye akili hahadaiki na mambo ya dhahiri wala hatapitwa na matukio.

Hakika Mola wako ni mwepesi wa kuadhibu wale waliothibitikiwa na adhabu.

Na hakika yeye ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu.

Yule atakayejing’oa na dhambi zake na akatubia.


7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

وَقَطَّعْنَاهُمْ فِي الْأَرْضِ أُمَمًا مِّنْهُمُ الصَّالِحُونَ وَمِنْهُمْ دُونَ ذَٰلِكَ وَبَلَوْنَاهُم بِالْحَسَنَاتِ وَالسَّيِّئَاتِ لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿١٦٨﴾

168. Na tukawafarikisha katika ardhi makundi makundi, Miongoni mwao wako walio wema na wengine kinyume cha hivyo. Na tukawajaribu kwa mema na mabaya ili wapate kurejea.

فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ وَرِثُوا الْكِتَابَ يَأْخُذُونَ عَرَضَ هَـٰذَا الْأَدْنَىٰ وَيَقُولُونَ سَيُغْفَرُ لَنَا وَإِن يَأْتِهِمْ عَرَضٌ مِّثْلُهُ يَأْخُذُوهُ أَلَمْ يُؤْخَذْ عَلَيْهِم مِّيثَاقُ الْكِتَابِ أَن لَّا يَقُولُوا عَلَى اللَّـهِ إِلَّا الْحَقَّ وَدَرَسُوا مَا فِيهِ وَالدَّارُ الْآخِرَةُ خَيْرٌ لِّلَّذِينَ يَتَّقُونَ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿١٦٩﴾

169. Na wakafuatia baada yao wabaya waliorithi Kitab wanachukua vitu vya maisha haya duni na wakasema: Tutasamehewa! Na vikiwajia vingine mfano wake, watavichukua, Je, hawakuchukua ahadi katika Kitab kuwa hawatasema juu ya Mwenyezi Mungu ila haki? Nao wamekwishasoma yaliyomo humo, Na nyumba ya Akhera ni bora kwa wale wenye takuwa Basi je, hamtii akilini?

وَالَّذِينَ يُمَسِّكُونَ بِالْكِتَابِ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ إِنَّا لَا نُضِيعُ أَجْرَ الْمُصْلِحِينَ ﴿١٧٠﴾

170. Na wale wanaoshikamana na Kitab na wakasimamisha Swala, hakika sisi hatupotezi ujira wa watendao mema.

وَإِذْ نَتَقْنَا الْجَبَلَ فَوْقَهُمْ كَأَنَّهُ ظُلَّةٌ وَظَنُّوا أَنَّهُ وَاقِعٌ بِهِمْ خُذُوا مَا آتَيْنَاكُم بِقُوَّةٍ وَاذْكُرُوا مَا فِيهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٧١﴾

171. Na tulipouinua mlima ukawa juu yao kama kwamba ni kiwingu kilichowafunika na wakadhani kuwa utawaangukia. Tukawaambia: shikeni kwa nguvu tuliyowapa na yakumbukeni yaliyomo ndani yake ili mpate kuwa na takua.

TUKAWAJARIBU KWA MEMA NA MABAYA

Aya 168-171

MAANA

Na tukawafarikisha katika ardhi makundi makundi.

Mwenyezi Mwenye aliwatawanya Waisraili makundi na vipote mbalimbali, hawana nchi inayowaweka pamoja wala dola inayowalinda.

Uzayuni umejaribu kuwawekea dola kutoka mto Naili hadi Furat kwa kunyang’anya kimabavu. Wanafikiria kuwa uadui wa Israil utapata unayoyataka, wakisahau kuwa dola ya Israili ni ya kupandikizwa tu na kwamba iko siku litawatokea la kuwatokea na mambo yote ya viumbe yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu, sio mikononi mwa uzayuni na ukoloni.

Miongini mwao wako walio wema na wengine kinyume cha hivyo.

Kwa dhahir ni kuwa makusudio ya wema hapa ni imani na kinyume cha hivyo ni wasiokuwa waumini. Umetangulia mfano wake katika Aya 159 ya Sura hii.

Na tukawajaribu kwa mema na mabaya ili wapate kurejea.

Makusudio ya mema ni afya na raha, na mabaya ni kinyume chake. Lengo la kupewa mema na mabaya ni kulipwa uongofu wao na kutubia kwa Mola wao.

Na wakafuatia baada yao wabaya waliorithi Kitab wanachukua vitu vya maisha haya duni na wakasema: Tutasamehewa! Na vikiwajia vingine mfano wake, watavichukua.

Makusudio ya maisha haya duni, ni dunia na vitu vya maisha duni; kama riba na rushwa.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja kwamba wakati wa Nabii Musa(a.s) kulikuwa na watu wema miongoni mwa wana wa Israil na wengine wasiokuwa wema, aliendelea kusema kuwa wote hao wameacha kizazi kilichojua halali ya Tawrat na haramu yake, lakini wakawa wanahalalisha haramu na wakiharamisha halali, huku wakisema: Mwenyezi Mungu atatughufria wala hatatuadhibu na kitu chochote. Kwa sababu sisi ni watoto wake wapenzi na ni taifa lake teule.

Unaweza kuuliza : Kwanini Mwenyezi Mungu amesema: “Wanachukua vitu vya maisha haya” tena akasema: “Vikiwajia mfano wake, wanachukua?” pamoja na kuwa kauli mbili ziko kwenye maana moja? Je, kuna lengo gani la kukaririka huku?

Lengo ni kuwakanya kwa vile wao wanang’ang’ania madhambi makubwa na kuyarudia mara kwa mara bila ya kujali na huku wakisema kuwa Mungu atatusamehe. Ikiwa kuendelea na madhambi madogo yanageuka kuwa makubwa, je kuendelea na makubwa itakuwaje?

Je, hawakuchukua ahadi katika Kitab kuwa hawatasema juu ya Mwenyezi Mungu ila haki? Nao wamekwishasoma yaliyomo humo.

Hili ni kemeo la pili kwao. Anawakemea kwa madai yao kuwa wao wana- iamini Tawrat na kwamba wameisoma na kuyafahamu yaliyomo. Na katika yaliyokuja katika Tawrat ni kwamba Mwenyezi Mungu anamsamehe mwenye kutubia na akayang’oa madhambi yake. Ama mwenye kung’ang’ania basi yeye ni katika walioangamia.

Vilevile Tawrat imechukua ahadi kuwa kila mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na hiyo Tawrat, basi asimzulie Mungu uwongo. Na waasi hao wanajua hakika hii, lakini bado wanaendelea na madhambi makubwa huku wakisema: “Mungu atatusamehe.” Huku ni kuvunja ahadi na kumzulia Mungu.

Na nyumba ya Akhera ni bora kwa wale wenye takua hawarukii maisha ya dunia hii wala hawasemi uwongo na uzushi kuwa Mungu atatusamehe.

Basi je, hamtii akilini?

Vipi atatia akilini ambaye akili yake imetekwa na matamanio yake na moyo wake ukatiwa maradhi na hawaa yake?

Na wale wanaoshikamana na Kitab na wakasimamisha Swala, hakika sisi hatupotezi ujira wa watendao mema.

Wanoshikamana na kitabu ni wale wanaotenda kulingana nacho. Anayeshikamana na kitu hasa ni yule anayetenda, kwa sababu anahisi uthabiti na azma ya kufanya.

Ameunganisha kushikamana na Kitab na kusimamisha Swala katika hali ya kuungania mahsus kwenye ujumla, kwa sababu ya siri iliyowajibisha mahsus.

Aya inawataaradhi Mayahudi ambao wameamini Tawrat na wasitumie hukumu zake. Vilevile kumtaaradhi kila mwenye kunasibika kwenye dini na akapuuza hukumu zake; hasa Swala ambayo ndiyo nguzo ya dini, lakini vijana wa sasa wameiweka pembeni.

Na tulipouinua mlima ukawa juu yao kama kwamba ni kiwingu kilichowafunika na wakadhani kuwa utawangukia. Tukawaambia: Shikeni kwa nguvu tuliyowapa na yakumbukeni yaliyomo ndani yake ili mpate kuwa na takua.

Mwenyezi Mungu aliwainulia wana wa Israil mlima ukawa kama kiwingu kilichowafunika, kuwahofisha ili wamche Mungu, lakini Waisraili ni Waisraili tu… Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:63).

وَإِذْ أَخَذَ رَبُّكَ مِن بَنِي آدَمَ مِن ظُهُورِهِمْ ذُرِّيَّتَهُمْ وَأَشْهَدَهُمْ عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ أَلَسْتُ بِرَبِّكُمْ قَالُوا بَلَىٰ شَهِدْنَا أَن تَقُولُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّا كُنَّا عَنْ هَـٰذَا غَافِلِينَ ﴿١٧٢﴾

172. Na Mola wako alipowaleta katika wanadamu kutoka miongoni mwa kizazi chao, na akawashuhudiza juu ya nafsi zao. Je, mimi si Mola wenu? Wakasema: Kwa nini! Tumeshuhudia, Msije mkasema siku ya Kiyama kuwa sisi tulikuwa tumeghafilika na haya.

أَوْ تَقُولُوا إِنَّمَا أَشْرَكَ آبَاؤُنَا مِن قَبْلُ وَكُنَّا ذُرِّيَّةً مِّن بَعْدِهِمْ أَفَتُهْلِكُنَا بِمَا فَعَلَ الْمُبْطِلُونَ ﴿١٧٣﴾

173. Au mkasema, baba zetu ndio walioshirikisha zamani, nasi tulikuwa kizazi nyuma yao, basi utatuangamiza kwa waliyofanya wabatilifu.

وَكَذَٰلِكَ نُفَصِّلُ الْآيَاتِ وَلَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿١٧٤﴾

174. Na kama hivyo tunazipambanua ishara, kwa kutaraji kuwa watarejea.

JE MIMI SI MOLA WENU?

Aya 172 –174

MAANA

ULIMWENGU WA CHEMBE CHEMBE

Na Mola wako walipowaleta katika wanadamu kutoka migongoni mwa kizazi chao, na akawashuhudiza juu ya nafsi zao. Je, mimi si Mola wenu? Wakasema: Kwanini! Tunashuhudia” Msije mkasema siku ya Kiyama kuwa sisi tulikuwa tumeghafilika na haya.

Katika Waislamu kuna kikundi kinachoamini ulimwengu wa chembe chembe. Maana yake, kinasema, ni kuwa baada ya Mwenyezi Mungu kumuumba Adam, alitoa mgongoni kwake kila mwanaume na mwanamke watakaozaliwa baadaye kuanzia Adam wa kwanza mpaka mwisho wa ulimwengu. Akawakusanya wote pamoja wakiwa na umbo la chembe chembe, kisha akawaambia. Je, mimi si Mola wenu? Wakasema ndiye Mola wetu. Baada ya kukiri hivi akawarudishia mgongoni mwa Adam.

Sisi tuko tayari kuwaunga mkono wale wanaoamini ulimwengui wa chem- be iwapo watatujibu maswali haya yafuatayo:

Je, ni wapi alikusanya Mwenyezi Mungu chembe chembe hizi, Ni katika ardhi hii au nyingine? Je, ardhi hii iliwatosha kwa sababu walikuwa kwenye umbo la chembe. Je, Adam alikuwa mkubwa kiasi cha kuweza kuchukua kila atakayetoka kwake moja kwa moja na kupitia wengine mpaka siku ya ufufuo?

Kisha je, katika rundo hilo linalozidi idadi ya mchanga anaweza kukum-buka mmoja tu maneno hayo na ahadi hiyo aliyompa Mwenyezi Mungu kwa mdomo? Ikiwa ameisahau kwa sababu ya muda mrefu. Je, Mwenyezi Mungu atakuwa na hoja kwake kwa kitu asichokikumbuka?

Haya ni katika upande wa akili, yaani baadhi ya yanayozunguka akilini. Ama katika upande wa

Aya, ni kwamba inafahamisha kinyume na ulimwengu wa chembe chembe, uliochukuliwa kutoka katika mgongo wa Adam wa kwanza. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema: Mola wako alipowaleta katika wanadamu, na wala hakusema katika Adam. Na ilivyo ni kuwa mwanadamu anaweza kuitwa Adam, lakini Nabii Adam wa kwanza hawezi kuitwa mwanadamu.

Vilevile Mwenyezi Mungu anasema kutoka migongoni mwao na hakuse- ma kutoka mgongoni mwake. Akasema , kizazi chao na hakusaema kizazi chake. Zaidi ya haya ni kwamba Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya pili kwamba amefanya hivi ili asiwe na hoja yeyote ya shirk ya mababa, ambapo mshirikina wa kwanza hawezi kutoa hoja ya ushirikina wa baba yake.

Ikiwa haya yote yanafahamisha kitu, basi kitu chenyewe ni kwamba ahadi ilichukuliwa kwa kila mmoja peke yake baada ya kupatikana kwake, bali na baada ya kuongoka na kutambua kwake.

Sisi hatujui maana nyingine ya ahadi hii, inayochukuliwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu kutuoka kwa mwanadamu, zaidi ya maumbile na silika ya maandalizi ambayo Mwenyezi Mungu ameipa kila akili, na ambayo lau mtu anakusudia kufahamu, hupambanua baina ya uongofu na upotevu na baina ya haki na batili. Na kwa silika hiyo huongoka kwenye imani ya Mwenyezi Mungu na dini yake ya haki.

Kwa maneno mengine ni kwamba kila mtu ni lazima afikirie ishara za Mwenyezi Mungu na dalili zake.

Wameafikiana Waislamu wote kwa kauli moja kwamba Hadith za Mtume ni tafsir na ubainifu wa Aya za Qur’an. Imethibiti Hadith Mutawatir inayosema: “Kila anayezaliwa huzaliwa katika umbile (safi). Wazazi wake ndio watakaomfanya Myahudi au Mnaswara (Mkristo) au Mmajusi.” Na ile isemayo: “Mwenyezi Mungu anasema: Hakika mimi nimewaumba waja wangu wakiwa wameachana na upotofu, kisha huwajia mashetani na kuwaepusha na dini yao.”

Na akawashuhudiza juu ya nafsi zao, Je, mimi sio Mola wenu? Wakasema: Kwanini! Tumeshuhudia.

Swali na jawabu yako mpaka leo ni hayo hayo mpaka siku ya mwisho. Kwa sababu ni lugha ya hali na matukio, sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

فَقَالَ لَهَا وَلِلْأَرْضِ ائْتِيَا طَوْعًا أَوْ كَرْهًا قَالَتَا أَتَيْنَا طَائِعِينَ ﴿١١﴾

“Akaiambia (mbingu) na ardhi: Njooni kwa hiyari au kwa nguvu! Zikasema: Tumekujia hali ya kuwa watiifu” (41:11).

Msije mkasema siku ya Kiyama kuwa sisi tulikuwa tumeghafilika na haya.

Haya, ni Tawhid inayofahamishwa na kauli yake: “Je, mimi si Mola wenu?” Hakuna sababu wala udhuru, si katika maisha haya wala ya akhera, kwa aliyepewa na Mwenyezi Mungu maanadalizi kamili ya kufahamu dalili na hoja juu ya umoja wa Mwenyezi Mungu na ukuu wake, kisha akakufuru na akashirikisha.

Au mkasema: Hakika baba zetu ndio walioshirikisha zamani, nasi tulikuwa kizazi nyuma yao, basi utatuangamiza kwa waliofanya wabatilifu?

Mtu hufuata vitu ambavyo anahitaji kujihusisha navyo na kumaliza miaka kadhaa ya kusoma; kama vile udaktari, uhandisi n.k. Ama utambuzi wa kimaumbile ambao haukalifishi mtu zaidi ya kuzinduka na kuamka, kama vile kuwako Mwenyezi Mungu na umoja wake, yote hayo yako sawa.

Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesimamisha dalili zenye kutosheleza juu ya umoja wake, na akaipa kila akili maandalizi ya kuufahamu kwa wepesi.

Kwa hiyo haikubaki udhuru wa mwenye kusema kuwa yeye amekanusha au kushirikisha kwa kuwafuata wengine wabatilifu. Wala hakuna tofauti kabisa katika mtazamo wa akili baina ya anayefanya bila elimu yake kwa makusudi na yule anayefuata batili kwa ujinga bila ya kukusudia, lakini ana uwezo wa kujua na kupambanua.

Na kama hivyo tunazipambanua ishara, kwa kutaraji kuwa watarejea kwenye akili zao ambazo, kwa vyovyote zikisaidiwa na dalili, zitawapeleka kwenye itikadi ya Tawhid.

Angalia Juz, 7 (6:41) kifungu ‘Mwenyezi Mungu na maumbile.

وَاتْلُ عَلَيْهِمْ نَبَأَ الَّذِي آتَيْنَاهُ آيَاتِنَا فَانسَلَخَ مِنْهَا فَأَتْبَعَهُ الشَّيْطَانُ فَكَانَ مِنَ الْغَاوِينَ ﴿١٧٥﴾

175. Na wasomee habari za yule tuliyempa ishara zetu, kisha akajivua nazo na shetani akamwandama akawa miongoni mwa waliopotea.

وَلَوْ شِئْنَا لَرَفَعْنَاهُ بِهَا وَلَـٰكِنَّهُ أَخْلَدَ إِلَى الْأَرْضِ وَاتَّبَعَ هَوَاهُ فَمَثَلُهُ كَمَثَلِ الْكَلْبِ إِن تَحْمِلْ عَلَيْهِ يَلْهَثْ أَوْ تَتْرُكْهُ يَلْهَث ذَّٰلِكَ مَثَلُ الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا فَاقْصُصِ الْقَصَصَ لَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ ﴿١٧٦﴾

176. Na kama tungelitaka tungelimuinua kwazo. Lakini yeye akashikilia ardhi na akafuata hawaa yake. Basi mfano wake ni kama wa mbwa, ukimhujumu hutweta na ukimwacha pia hutweta. Huo ni mfano wa watu waliozikadhibisha ishara zetu, Basi simulia visa, huenda wakatafakari.

سَاءَ مَثَلًا الْقَوْمُ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا وَأَنفُسَهُمْ كَانُوا يَظْلِمُونَ ﴿١٧٧﴾

177. Huu ni mfano muovu kabisa wa watu wanaokadhibisha ishara zetu na wakajidhulumu nafsi zao.

TUMEMPA AYA ZETU AKAJIVUA

Aya 175 – 177

MAANA

Na wasomee habari za yule tuliyempa ishara zetu, kisha akajivua nazo na shetani akamwandama akawa miongoni mwa waliopotea.

Maneno hapa anaambiwa Mtume Muhammad(s.a.w.w) , Wanaosomewa ni Mayahudi. Ama yule ambaye Mwenyezi Mungu amempa ishara akajivua nazo, hatumjui ni nani, nasi hatujiingizi katika kitu kisichokuwa katika Qur’an wala Hadith Mutawatir, lakini wasimulizi wa visa na wafasiri wengi wanasema kuwa mtu huyo alikuwa akiitwa Balam Bin Baur, na kwamba yeye alikuwa kwenye dini ya Nabii Musa na mjuzi wa hukumu zake, kisha akartadi.

Sisi tunaangalia nukuu hii na nyingine kwa hadhari, wala hautulii moyo ila kwa nukuu ya Qur’an. Na nukuu hii inafahamisha tu, kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwamrisha Mtume awape habari Mayahudi juu ya Kisa cha mtu ambaye alikuwa akijua dini ya Mwenyezi Mungu na ishara zake, kisha akahadaliwa na shetani akaacha ilimu yake na dini, akashikamana na upotevu, akawa miongoni mwa wapotevu walioangamia. Kama kawaida maulama wa kiyahudi walikuwa wakimjua mtu huyu.

Na kama tungelitaka tungelimuinua kwazo.

Yaani kwa aliyompa Mwenyezi Mungu kujua ishara zake, Lakini Mwenyezi Mungu hakutaka kumlazimisha kuzitumia ishara zake. Kwa sababu Mwenyezi Mungu mtukufu hawapeleki watu kwa matakwa ya kuumba ambayo ni kukiambia kitu kuwa kikawa. Isipokuwa huwapeleka kwa matakwa ya nasaha na mwongozo yanayoitwa amri zake na makatazo yake. Kwa hiyo akamwachia yule aliyejivua na ishara zake, uhuru na hiyari, akachagua dunia kuliko akhera.

Lakini yeye akashikilia ardhi na akafuata hawaa yake.

Makusudio ya ardhi hapa ni starehe za maisha ya dunia, kwa sababu ardhi ndio chimbuko lake. Maisha yenyewe ni pamoja na starehe na anasa. Maaana ni kuwa huyu aliyejivua amemwasi Mola wake akatii hawaa yake akiwa ameishikilia haiachi.

Razi anasema kuwa Aya hii ni kali zaidi kwa mwenye elimu. Mtume wa Mwenyezi Mungu anasema: “Mwenye kuzidi elimu, lakini asizidi uongofu hatazidi kwa Mwenyezi Mungu ila kuwa umbali.”

Basi mfano wake ni kama wa mbwa, ukimhujumu hutweta na ukimwacha pia hutweta.

Mbwa anayepumua kwa nguvu na kutoa ulimi kwa kiu au kuchoka (kuhaha) anaendelea tu, ukimkemea au ukimwacha yeye ataendelea hivyo hivyo.

Vilevile mwenye kushikilia hawaa yake huendelea katika upotevu wake umwonye au umwache yeye hupotea tu.

Huo ni mfano wa watu waliozikadhibisha ishara zetu.

Yaani hiyo ndiyo hali ya kila mwenye kuendelea na maasi, daima hanufaiki na ishara wala hazingatii mawaidha. Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mwenye kupumua na kutoa ulimi na mwasi mwenye kuendelea kwa kuishiria uduni wake.

Basi simulia visa, huenda wakatafakari.

Yaani “Ewe Nabii Muhammad(s.a.w.w) wasimulie mayahudi kuhusu wakale wao na yaliyowafikia, kama watu wa kijiji kilichokuwa ufukweni mwa bahari na huyu aliyejivua ili yawe ni mazingatio kwao na kuwakanya kukadhibisha utume wako.

Huu ni mfano muovu kabisa wa watu wanaokadhibisha ishara zetu na wakajidhulumu nafsi zao.

Kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo na kuzikadhibisha ishara zake, yote hayo ni uzushi, Hali ya kwanza inathibitisha katika dini yasiyokuwamo.

Ya pili inakanusha yaliyomo, na huo ndio uzushi (bid’a) hasa, na kila uzushi ni upotevu, na kila upotevu ni katika moto. Kwa hiyo mwenye kuzua ameidhulumu nafsi yake kuiingiza kwenye adhabu na maangamizi.

Utauliza : mwenye kuipindua haki kwa kuhofia nafsi yake na dhalimu, je, anahisabiwa kuwa mzushi?

Jibu : Ndio, ni mzushi anayestahiki adhabu, hilo halina shaka. Kwa sababu ni juu yake kuhofia ghadhabu ya Mwenyezi Mungu kwa kuipindua haki sio ghadhabu ya dhalimu kwa kuithibitisha haki.

Inawezekana mtu kuacha kufanya haki kwa kujikinga na madhara, lakini kuipindua dini kwa kumzulia Mwenyezi Mungu uwongo, hakuna sababu yoyote, vyovyote itakavyokuwa.

مَن يَهْدِ اللَّـهُ فَهُوَ الْمُهْتَدِي وَمَن يُضْلِلْ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿١٧٨﴾

178. Atakayeongozwa na Mwenyezi Mungu ndiye aongokaye, na atakayepotezwa, basi hao ndio watakaopata hasara.

وَلَقَدْ ذَرَأْنَا لِجَهَنَّمَ كَثِيرًا مِّنَ الْجِنِّ وَالْإِنسِ لَهُمْ قُلُوبٌ لَّا يَفْقَهُونَ بِهَا وَلَهُمْ أَعْيُنٌ لَّا يُبْصِرُونَ بِهَا وَلَهُمْ آذَانٌ لَّا يَسْمَعُونَ بِهَا أُولَـٰئِكَ كَالْأَنْعَامِ بَلْ هُمْ أَضَلُّ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْغَافِلُونَ ﴿١٧٩﴾

179. Na hakika tumewaumbia Jahannam majini wengi na watu. Wana nyonyo, lakini hawafahamu kwazo, na wana macho, lakini hawaoni kwayo, na wanayo masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama bali wao ni wapotevu zaidi, Hao ndio walioghafilika.

وَلِلَّـهِ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ فَادْعُوهُ بِهَا وَذَرُوا الَّذِينَ يُلْحِدُونَ فِي أَسْمَائِهِ سَيُجْزَوْنَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٨٠﴾

180. Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri, Basi mwombeni kwayo, Na waacheni wale wanaoharibu utakatifu wa majina yake, watalipwa waliyokuwa wakiyatenda.

وَمِمَّنْ خَلَقْنَا أُمَّةٌ يَهْدُونَ بِالْحَقِّ وَبِهِ يَعْدِلُونَ ﴿١٨١﴾

181. Na miongoni mwa tuliowaumba wako watu wanaoongoza kwa haki na kwayo wafanya uadilifu.

ATAKAOWAONGOZA MUNGU NDIO WATAKAOONGOKA

Aya 178 – 181

MAANA

Atakayeongozwa na Mwenyezi Mungu ndiye aongokaye, na atakayepotezwa, basi hao ndio watakaopata hasara.

Makusudio sio kuwa yule aliyeumbiwa kuongoka ndiye atakayeongoka na kwamba aliyeumbiwa kupotea ndiye mpotevu. Hapana si hivyo! Maana haya yanakataliwa na maumbile na hali ilivyo; Kwa sababu Mwenyezi Mungu si mwenye kuwadhulumu waja.

Vilevile inakataliwa na nukuu ya Qur’an:

فَمَنِ اهْتَدَىٰ فَإِنَّمَا يَهْتَدِي لِنَفْسِهِ وَمَن ضَلَّ فَإِنَّمَا يَضِلُّ عَلَيْهَا ﴿١٠٨﴾

“…Basi anayeongoka anaongoka yeye mwenyewe na anayepotea hupotea yeye mwenyewe…” (10:108).

Vipi Mwenyezi Mungu awe na sifa ya uadilifu na wakati huo huo awe ni mpotezaji. Mpotezaji ni shetani:

قَالَ هَـٰذَا مِنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ إِنَّهُ عَدُوٌّ مُّضِلٌّ مُّبِينٌ ﴿١٥﴾

“Akasema hii ni kazi ya shetani, hakika yeye ni adui mpotezaji aliye wazi” (28:15).

Tuanavyo sisi ni kuwa makusudio ya Aya ni kuwa mwenye kuongoka hasa ni yule aliyeongoka mbele ya Mwenyezi Mungu, hata kama mbele ya watu ni mpotevu.

Hakuna mwenye shaka kwamba mtu hawezi kuwa ni muongofu katika mizani ya Mungu ila akiamini na kutenda mema:

إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ يَهْدِيهِمْ رَبُّهُم بِإِيمَانِهِمْ ﴿٩﴾

“Hakika wale walioamini na wakatenda mema, Mola wao atawaongoa kwa sababu ya imani yao” (10:9).

وَالَّذِينَ جَاهَدُوا فِينَا لَنَهْدِيَنَّهُمْ سُبُلَنَا ﴿٦٩﴾

“Na wanaofanya juhudi kwa ajili yetu, tutawaongoa kwenye njia yetu” (29:69)

Vilevile mpotevu ni yule aliyepotea kwa Mwenyezi Mungu sio kwa watu. Kwa maneno mengine ni kwamba Aya inapinga maana ya kuwa basi amefanywa hivyo na Mwenyezi Mungu; kama alivyosema Imam Ali(a.s) :“Utajiri na ufukara ni baada ya kuonekana kwa Mwenyezi Mungu.”

Na hakika tumewauumbia Jahannam majini wengi na watu.

Mwenyezi Mungu hakuumba wala hataumba yeyote kwa ajili ya kumwadhibu. Vipi iwe hivyo? Kwani Mwenyezi Mungu anaona raha kuwaadhibu wanyonge ambao hawana hila yoyote na wala hawanyookewi.

Katika baadhi ya mambo niliyoyasoma, ni kwamba wamarekani walikuwa wanapotaka kujistarehesha, humleta mmoja asiyekuwa mweupe, wanamzunguka na kumiminia mvua ya risasi za bastola zao. Anapoanguka chini akiwa amelowa damu, wao hucheka sana.

Na kwamba Mwenyezi Mungu hatamwunguza mtu katika moto wake akiwa ana jinsia ya kimarekani au Kizayuni, Ametakata Mwenyezi Mungu na wanavyomsifu.

Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemuumba mwanadamu kwa ajili ya kupata elimu yenye manufaa amali njema, na akampa maandalizi yote ya hayo.

Akampa akili yenye kupambanua baina ya uongofu na upotevu, akampelekea Mitume wa kumzindua na kumwongoza, na akamwachia hiyari ya kufuata njia anayoitaka. Kwa sababu uhuru ndio msimamo wa hakika ya mtu. Lau asingempa uhuru angelikuwa sawa na mawe.

Kwa hiyo basi, akichagua njia ya uongofu itampeleka kwenye radhi ya Mwenyezi Mungu na thawabu zake; na akifuata njia ya upotevu basi mwisho wake ni Jahannam, ni marejeo mabaya. Kwa hali hiyo herufi Laam ni ya umwisho; kama ilivyo katika kauli yake Mwenyezi Mungu:

فَالْتَقَطَهُ آلُ فِرْعَوْنَ لِيَكُونَ لَهُمْ عَدُوًّا وَحَزَنًا ﴿٨﴾

“Basi wakamwokota watu na Firauni ili awe adui kwao na huzuni.” (28:8).

Yaani mwisho wake alikuwa adui yao. Utauliza: Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema:

وَمَا خَلَقْتُ الْجِنَّ وَالْإِنسَ إِلَّا لِيَعْبُدُونِ ﴿٥٦﴾

“Sikuumba majini na watu ila waniabudu” (51:56)

Na wewe unasema kuwa mtu ameumbwa kwa ajili ya elimu yenye manufaa na amali njema, sasa ni vipi?

Jibu : Elimu yenye manufaa na amali njema ni katika twa’a bora zaidi. Imekuja riwaya isemayo: “Mwanachuoni mmoja ni bora kuliko wenye kuabudu elfu na wenye zuhudi elfu.” Riwaya nyingine inasema: “Mwanachuoni anayepatiwa manufaa kwa elimu yake ni bora kuliko wenye kuabudu elfu sabini.”

Wana nyonyo, lakini hawafahamu kwazo, na wana macho, lakini hawaoni kwayo, na wanayo masikio, lakini hawasikii kwayo.

Kitu chochote ambacho hakitekelezi lengo linalotakiwa basi kuweko kwake na kutokuwepo ni sawa. Na katika malengo yaliyokusudiwa moyo ni kufungukia dalili za haki, macho yaone dalili hizi na masikio yasikie. Kama vifaa hivi vitatu ukiviepusha na hayo na wala visinufaike kwa chochote katika dalili ya haki, basi kuweko kwake ni sawa na kutokuwepo. Mwenyezi Mungu anasema:

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَذِكْرَىٰ لِمَن كَانَ لَهُ قَلْبٌ أَوْ أَلْقَى السَّمْعَ وَهُوَ شَهِيدٌ ﴿٣٧﴾

“Kwa hakika katika hayo upo ukumbusho kwa mwenye moyo au ategaye sikio naye yupo” (50:37)

Moyo upo na masikio yapo, lakini inafaa kusema haupo ikiwa umeghafilika na haki na dalili zake.

Hao ni kama wanyama

Wana nyoyo, macho na masikio, lakini nyoyo zao hazifungukii haki, macho yao hayaoni dalili za haki na masikio yao hayasikii, basi wakawa kama wanyama.

Bali wao ni wapotevu zaidi.

Kwa sababu wanyama wanatekeleza lengo wanalotakiwa kwa njia ya ukamilifu kwa vile wanashindwa kufikia ukamilifu, na wala hawahisabiwi au kuadhibiwa; na tena mnyama hulijua umbile lake la asili. Makafiri hawatekelezi wanayotakiwa kuyafanya, wanaweza kufikia ukamilifu laki- ni hawafanyi, nao watahisabiwa na kuadhibiwa.

Hao ndio walioghafilika na dalili za Mwenyezi Mungu zilimo katika nafsi zao na pambizoni mwao. Pia wameghafilika na mwisho wao na yale yatakayowapata huko akhera katika hizaya na adhabu.

JE, MAJINA YA MWENYEZI MUNGU NI HAYOHAYO AU YANA KIASI

Na Mwenyezi Mungu ana majina mazuri.

Majina yote ya Mwenyezi Mungu ni mazuri, kwa sababu yana maana mazuri na makamilifu, na yote yako sawa katika uzuri. Kwani Mwenyezi Mungu hana hali mbalimbali wala sifa zenye kugeuka; hata kwa wale wasemao kuwa sifa yake sio dhati yake, wala pia hana vitendo vinavyotofautiana. Kuumba bawa la mbu na kuumba ulimwengu wote ni sawa kwake. Vyote hupatikana kwa neno “Kuwa na Ikawa.”

Basi mwombeni kwayo.

Yaani mtajeni Mwenyezi Mungu na mwombeni kwa jina lolote mnalolita- ka katika majina yake. Yote hayo ni matamko yanaelezea utakatifu wake na ukuu wake kwa kipimo kimoja; wala Mwenyezi Mungu hana jina kubwa na jina lisilokuwa kubwa.

Kwa ajili hiyo, sisi hatusemi kama wale wanaosema kuwa Mwenyezi Mungu ana jina mahsus ambalo ni katika majina matukufu (Ism A’dham), na kwamba mwenye kulijua atamiminikiwa na kheri nyingi na kuwa na miujiza.

Pia imesemekana kuwa Mwenyezi Mungu ana majina tisini na tisa, na kwamba mwenye kuyajua ataingia peponi; kama kwamba pepo imeumbi- wa watungaji kamusi za lugha na sio wacha Mungu.

Na waacheni wale wanaoharibu utakatifu wa majina yake, watalipwa waliyokuwa wakiyatenda.

Kuharibu ni kuacha lengo lililokusudiwa. Maana ya ujumla ni kukataza kabisa tamko lolote linalotambulisha Uungu kwa mwingne; awe Mtume, nyota, sanamu au kitu chochote kingine. Vilevile haijuzu kabisa kutumia tamko litakalofahamisha usiokuwa Ungu, kama vile baba na mwana.

Wametofautiana maulamaa wa Tawhid kuhusu majina ya Mwenyezi Mungu mtukufu, kuwa je, ni hayo hayo au yana kiasi. Maana ya kuwa ni hayo hayo ni kusimama katika majina yake yaliyotajwa kwenye Qur’an na Hadith; kiasi ambacho haijuzu kabisa jina lolote isipokuwa liwe limetokana na nukuu ya Aya au Hadith.

Maana ya kuwa yana kiasi ni kuwa jina loloate ambalo maana yake yanathibiti katika haki yake Mwenyezi Mungu, basi inajuzu kulitumia, ni sawa liwe limenukuliwa au la.

Maulama wengi wamesema kuwa majina ya Mwenyezi Mungu ni hayo hayo tu. Ama sisi tunaona kuwa inafaa kumwita au kumwomba MwenyeziMungu kwa jina lolote linalofahamisha utukatifu na utukufu wake; ni sawa liwe limenukuliwa kwenye Qur’an na Hadith au la.

Hatujizui ila lile lilozuiwa na Mwenyezi. Tunasema hivyo kwa kutegemea msingi wa: “Kila kitu ni halali mpaka kielezwe kukatazwa kwake.”

Haya ndiyo yanayopitishwa na elimu ya misingi ya kidini; kuongezea kongamano (Ijma’i) la umma, zamani na sasa, kuwa wasiokuwa waarabu wanaweza kuitaja dhati ya Mwenyezi Mungu, sifa zake na vitendo vyake kwa lugha zao.

Na miongoni mwa tuliowaumba wako watu wanaoongoza kwa haki na wafanyao uadilifu.

Katika watu kuna Muumin na kafiri na mwema na mwovu, wote wanajua hakika hii, sasa kuna makusudio gani kubainisha?

Jibu : Katika Aya iliyotangulia, Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema kuwa wengi katika majini na watu mwisho wao ni Jahannam, kwa hiyo ikanasi- bu hapa kusema kuwa miongoni mwao mwisho wake ni pepo, hata ingawaje ni wachache kuliko wale; kama lilivyofahamisha neno miongoni. Amewaita watu wa peponi kwa ibara ya wanaoongoza kwa haki na kufanya uadilifu kuishiria kuwa sababu inayowajibisha kuingia kwao peponi ni uongofu na uadilifu.


8

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

وَالَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا سَنَسْتَدْرِجُهُم مِّنْ حَيْثُ لَا يَعْلَمُونَ ﴿١٨٢﴾

182. Na wale waliokadhibisha ishara zetu, tutawavuta kidogo kidogo kidogo kwa namna wasiyoijua.

وَأُمْلِي لَهُمْ إِنَّ كَيْدِي مَتِينٌ ﴿١٨٣﴾

183. Nami nitawapa muda, hakika hila yangu ni madhubuti.

أَوَلَمْ يَتَفَكَّرُوا مَا بِصَاحِبِهِم مِّن جِنَّةٍ إِنْ هُوَ إِلَّا نَذِيرٌ مُّبِينٌ ﴿١٨٤﴾

184. Je,hawafikiri kuwa mwenzao hana wazimu? Hakuwa yeye ila ni mwonyaji aliye dhahiri.

أَوَلَمْ يَنظُرُوا فِي مَلَكُوتِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا خَلَقَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ وَأَنْ عَسَىٰ أَن يَكُونَ قَدِ اقْتَرَبَ أَجَلُهُمْ فَبِأَيِّ حَدِيثٍ بَعْدَهُ يُؤْمِنُونَ ﴿١٨٥﴾

185. Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi na alivyoviumba Mwenyezi Mungu. Na kuwa pengine ajali yao imekwisha karibia. Basi ni mazungumzo gani baada yake watakayoyaamini?

مَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَلَا هَادِيَ لَهُ وَيَذَرُهُمْ فِي طُغْيَانِهِمْ يَعْمَهُونَ ﴿١٨٦﴾

186. Ambaye Mwenyezi Mungu humpoteza hana wa kumwongoza, Na anawaacha katika upotofu wao wakimangamanga.

WALIOKADHIBISHA AYA ZETU

Aya 182 – 186

MAANA

Na wale waliokadhibisha ishara zetu, tutawavuta kidogo kidogo kwa namna wasiyojua.

Huwa zikafululiza neema kwa mtu, naye akaendelea kupetuka mipaka kwa kuhadalika na wingi wake na utajiri huku akisahau yaliyofichikana na yajayo ghafla, mpaka watu wakisema kheri zote ni zake, basi humjia ghafla kuharibikiwa.

Abu Sufyan alihadaika siku ya Uhud akasema: “Leo tumewalipizia siku ya Badr”, lakini ulipokuja msaada wa Mwenyezi Mungu na ushindi, alisilimu akiwa mnyonge.

Imam Ali(a.s) anasema:“Ni wangapi wanachukuliwa kidogo kidogo kufanyiwa hisani, na wanaohadaliwa kwa kusitiriwa, na wanaofitiniwa kwa kuambiwa maneno mazuri. Na hakujaribiwa yeyote na Mwenyezi Mungu mfano wa kupewa muda.”

Nami nitawapa muda, hakika hila yangu ni madhubuti.

Makusudio ya hila ya Mwenyezi Mungu ni kwamba yeye atawaacha wahadaike na hisani yake ya dhahir, mpaka wakielemea, basi huwachukua bila ya kujua.

أَيَحْسَبُونَ أَنَّمَا نُمِدُّهُم بِهِ مِن مَّالٍ وَبَنِينَ ﴿٥٥﴾ نُسَارِعُ لَهُمْ فِي الْخَيْرَاتِ بَل لَّا يَشْعُرُونَ ﴿٥٦﴾

“Je, wanadhani ya kuwa kwa vile tunavyowapa mali na watoto ndio tunawahimizia kheri? Bali hawatambui” (23:55 – 56).

Je,hawafikiri kuwa mwenzao hana wazimu? Hakuwa yeye ila ni mwonyaji aliye dhahiri.

Hivi ndivyo wezi, wauaji wanavyoeneza propaganda zao dhidi ya kila mwenye ikhlas, kila wakati na kila mahali. Nabii Muhammad(s.a.w.w) ni mwenda wazimu, mchawi na mwongo, Kwa nini? Kwa vile tu yeye anakataa uongo na upotevu na kuupiga vita wizi na unyang’anyi.

Makureish walimzulia Nabii Muhammad(s.a.w.w) wakiwa wanamjua tangu utoto wake mpaka kufikia miaka arubaini katika umri wake mtukufu. Wanamjua akili aliyo nayo, ukweli na uaminifu. Lakini Vilevile wanajua kuwa ujumbe wa Nabii Muhammad(s.a.w.w) ndio hatari kubwa juu ya utawala wa Kikuraish. Ni kwa ajili hii pekee ndio wakasema yeye ni mwenda wazimu, ili angalau wahadaike wale wanaowatawala na kuwanyonya.

Ndipo Qur’an ikawalingania kwenye kufikiri na kuzingatia jambo la Nabii Muhammad(s.a.w.w) , naye ni mwenzao na jamaa yao waliyempima, wafikiri, je, wamempata na lawama yoyote au wamepata katika akili yake na hulka yake tuhuma yeyote?

Hakuwa yeye ila ni muonyaji aliye dhahiri anayebainisha haki na kumwonya anayemhalifu, Hili ndilo kosa pekee kwao.

Je, hawatazami ufalme wa mbingu na ardhi na alivyoviumba Mwenyezi Mungu.

Yaani mbingu na ardhi na vyote vilivyomo vinanyenyekea ufalme wake na kufahamisha umoja wake, na kwamba hakuna yeyote mwenye akili atakayeangalia vitu hivi vilivyopo, bila ya kuwa na lengo jingine lolote, ila atamwamini Mwenyezi Mungu, vitabu vyake na Mitume yake.

Ama ambaye hafikirii isipokuwa maslahi yake tu, haongoki wala hataongoka kwa Mwenyezi Mungu wala kwa kitu chochote cha kheri.

Na kuwa pengine ajali yao imekwisha karibia.

Baada ya Mwenyezi Mungu kuwataka wafikiri kuzingatia maumbile ya ulimwengu na vitu vyake sasa, anawazindua kwenye mauti, mvunja starehe na mtawanyaji makundi, na kwamba hayo mauti huenda yakawajia ghafla hivi karibuni na wao wakiwa wanaendelea katika upotevu wao. Amezindua hivi, huenda wao wakatubu na kuelekea kwenye uongofu.

Basi ni mazungumzo gani baada yake watakayoyaamini?

Dhamir ya yake inarudia Qur’an, Hakuna ubainifu wa kutosheleza baada ya Qur’an wala dalili yenye nguvu zaidi yake. Ambaye hakinaishwi na dalili za Mwenyezi Mungu basi hakinaishwi na chochote.

Ambaye Mwenyezi Mungu humpoteza hana wa kumwongoza.

Tumetaja maana yake punde tu katika kufasiri Aya 178 ya Sura hii.

Na anawaacha katika upotofu wao wakimangamanga.

Yaani Mwenyezi Mungu atawaacha wakitangatanga ovyo katika upotevu na kuwapa muda kisha awalipe yale waliyoyafanya nyuma, Wala kuwapuuza huko sio dhulma. Kwa sababu kumekuja baada ya ubainifu na hadhari, na baada ya kukata tamaa ya kuwakemea na kuwaongoza.

يَسْأَلُونَكَ عَنِ السَّاعَةِ أَيَّانَ مُرْسَاهَا قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ رَبِّي لَا يُجَلِّيهَا لِوَقْتِهَا إِلَّا هُوَ ثَقُلَتْ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ لَا تَأْتِيكُمْ إِلَّا بَغْتَةً يَسْأَلُونَكَ كَأَنَّكَ حَفِيٌّ عَنْهَا قُلْ إِنَّمَا عِلْمُهَا عِندَ اللَّـهِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿١٨٧﴾

187. Wanauliza hiyo saa (Kiyama) kutokea kwake kutakuwa lini? Sema: Ujuzi wake uko kwa Mola wangu. Hakuna wa kuidhihirisha kwa wakati wake ila yeye tu. Ni nzito katika mbingu na ardhi. Haitawafikia ila kwa ghafla tu. Wanakuuliza kama kwamba unaidadisi. Sema, Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu tu, Lakini watu wengi hawajui.

قُل لَّا أَمْلِكُ لِنَفْسِي نَفْعًا وَلَا ضَرًّا إِلَّا مَا شَاءَ اللَّـهُ وَلَوْ كُنتُ أَعْلَمُ الْغَيْبَ لَاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ إِنْ أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿١٨٨﴾

188. Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara ila apendavyo Mwenyezi Mungu. Na lau kama ningelijua ghaibu ningelijizidishia kheri nyingi, wala isingelinigusa dhara. Mimi si chochote ila ni mwonyaji na mtoaji bishara kwa watu wanaoamini.

WANAKUULIZA SAA (KIYAMA)

Aya 187 – 188

MAANA

Wanauliza hiyo saa (Kiyama) kutokea kwake kutakuwa lini? Sema: Ujuzi wake uko kwa Mola wangu. Hakuna wa kuidhihirisha kwa wakati wake ila yeye tu.

Makusudio ya saa ni utakapokwisha ulimwengu na kufa viumbe.

Dhahiri ya Aya inafahamisha kwamba, jamaa walimwuliza Mtume Muhammad(s.a.w.w) : “Kiyama kitakuwa lini.” Mwenyezi Mungu akamwamrisha awaambie kwamba hiyo ni katika mambo ambayo hayako chini ya uwezo wa mtu katika kuyajua, na kwamba ujuzi wake unahusika na Mwenyezi Mungu tu peke yake, yeye ndiye atakayeidhihirisha wakati wake uliopangwa.

Ni nzito katika mbingu na ardhi.

Yaani ni nzito kutokea kwake kwa watu wa mbingu na ardhi kwa ukuu wake na ukali wake.

Haitawafikia ila kwa ghafla tu, bila ya kutangaza mapema.

Wanakuuliza kama kwamba unaidadisi.

Yaani kama kwamba wewe unapupa sana kujua saa itakuwa lini. Mtume (s.a.w.) hakuwa akijishighulisha na kujua Kiyama kitakuwa lini; isipokuwa alikuwa akijishughulisha na kuifanyia amali saa hiyo ya kiyama, kuonya watu na kuunganisha kati ya kuokoka na vituko vyake na kufanya amali njema. Kwa ajili hii ndio hakumuliza Mola wake kuhusu saa hiyo.

Imesemekana kuwa bedui mmoja alimwuliza Mtume(s.a.w.w) : “Ni lini itakuwa hiyo saa? Akamjibu: “Umeiandalia nini?” Kwa jibu hili anakusudia kumfahamisha kuwa ubora kwako ni kuuliza kitakachokuokoa wakati huo itakapofika na si kujua wakati wake na picha yake. Mwenye akili akipatwa na ugonjwa haulizi namna ya kufa na ugonjwa huo, isipokuwa anauliza ni lipi litakalomponesha na ugonjwa huo.

Tena amerudia Mwenyezi Mungu kusema:Sema, Ujuzi wake uko kwa Mwenyezi Mungu tu, kwa kutilia mkazo kuwa ujuzi wa hiyo saa uko kwa Mwenyezi Mungu peke yake, na pia ni utangulizi wa kauli yake,Lakini watu wengi hawajui kwamba ujuzi wa saa uko kwa aliyeiumba wala hajui mwengine yoyote.

MTUME NA ELIMU YA GHAIB

Sema: Siimilikii nafsi yangu manufaa wala madhara ila apendavyo Mwenyezi Mungu.

Hii ndiyo itikadi ya Waislamu kwa Mtume wao Muhammad(s.a.w.w) mtukufu wa viumbe vyote vya Mwenyezi Mungu, Yeye mwenyewe hajimilikii nafsi yake sikwambii kummilikia mwingine. Na itikadi hii kwa Nabii Muhammad ni natija ya itikadi ya Tawhid.

Na lau kama ningelijua ghaibu ningelijizidishia kheri nyingi, wala isingelinigusa dhara.

Neno ghaibu halifahamishi maana yake tu, bali vilevile linafahamisha kuwa ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu peke yake.

Zaidi ya dalili hii ni kwamba aliye karibu zaidi na Mola wake kuliko yey ote, anawatangazia watu kuwa yeye mbele ya ghaibu ni mtu wa kawaida tu, hana tofauti na watu wengine. Kisha hatosheki na tangazo hili, bali analitolea dalili hilo kwa hisia na dhamiri, kuwa lau kama yeye angelijua ghaibu basi angelijua mwisho wa mambo, hapo angefanya lile ambalo mwisho wake ni wema na kuliacha lile ambalo mwisho wake ni shari na yasingempata yale anayoyachukia kumpata katika maisha haya.

Na ili mtu asije akasema: Itakuwaje Nabii Muhammad(s.a.w.w) hajui ghaibu naye ni Mtume mwenye kukurubishwa kwa Mwenyezi Mungu, ndio Nabii Muhammad akasema:

Mimi si chochote ila ni mwonyaji na mtoaji bishara kwa watu wanaoamini.

Yeye ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, hilo halina shaka, lakini umuhimu wa Mtume unathibitika kwa kufikishia watu ujumbe wa Mola wao na kumwonya kwa adhabu yule mwenye kutii. Ama elimu ya ghaibu, kunufaisha na kudhuru, hayo yako mikononi mwa Mwenyezi Mungu peke yake.

Amewahusisha waumini kwa bishara na maonyo, pamoja na kuwa yanawahusu watu wote, kuishiria kwamba anayenufaika na hayo ni yule tu anayeitaka haki na imani, ama mwenye kiburi halimfai yeye jambo lolote.

Utauliza : Yamekuja maelezo katika sera ya Mtume na vitabu vya Hadith kwamba Nabii Muhammad(s.a.w.w) ametolea habari mambo mengi ya ghaibu, kama vile kuwa waislamu baadaye watawashinda warumi na wafursi, na kwamba Salman Farsy atavishwa taji la Kisra kichwani kwake, na ikawa.

Vilevile alitoa habari ya mauti ya Najash, na kufa shahid Zaid bin Harith, Jafar bin Abu Talib na Abdallah bin Rawaha, na pia kuhusu mbweko wa mbwa wa Hawab kwa Aisha kupigana na Ali bin Abu Twalib na wavunja ahadi waliokengeuka, na Khawarij, kufa shahid kwa mjukuu wake, Husein bin Ali na mengine mengi. Sasa itakuwaje hayo na kauli yake, Lau ningelijua ghaibu.

Jibu : Ghaib za Mwenyezi Mungu hazina mpaka wala idadi, Na ghaibu ziko aina nyingi.

Kuna aina anayoificha Mwenyezi Mungu na wala hamfichulii yeyote katika waja wake vyovyote walivyo, kama vile kuja saa ya Kiyama.

Aina nyingine humfichulia anayemridhia katika waja wake, Hayo ameyashiria katika Aya isemayo:

عَالِمُ الْغَيْبِ فَلَا يُظْهِرُ عَلَىٰ غَيْبِهِ أَحَدًا ﴿٢٦﴾ إِلَّا مَنِ ارْتَضَىٰ مِن رَّسُولٍ ﴿٢٧﴾

“Yeye ndiye mjuzi wa ghaibu wala hamdhihirishii ghaibu yake yoyote, isipokuwa Mtume wake aliyemridhia.” (72: 26 – 27).

Na pia Aya isemayo:

وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُطْلِعَكُمْ عَلَى الْغَيْبِ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يَجْتَبِي مِن رُّسُلِهِ مَن يَشَاءُ فَآمِنُوا بِاللَّـهِ وَرُسُلِهِ وَإِن تُؤْمِنُوا وَتَتَّقُوا فَلَكُمْ أَجْرٌ عَظِيمٌ ﴿١٧٩﴾

“Na hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwafunulia mambo ya ghaibu, lakini Mwenyezi Mungu humchagua amtakaye katika Mitume yake. Basi mwaminini Mwenyezi Mungu na Mitume Yake.” Juz.4 (3:179).

Na kuna aina nyingine anawafichulia watu wote, kama vile ufufuo, pepo na moto.

Makusudio ya kuwa ghaibu ni ya Mwenyezi Mungu na iko kwa Mwenyezi Mungu, ni kuwa hakuna njia ya kuijua kwa majaribio, akili wala kwa kitu chochote isipokuwa kwa wahyi kutoka kwa Mwenyezi Mungu mtukufu.

Naye humpa wahyi kwa sehemu ndogo ya ghaibu yake kulingana na heki- ma inavyotaka na haja ya watu. Na Mtume naye kwa nafasi yake hii huwapa watu habari ya ghaibu hiyo; kama alivyoipokea kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kwa hiyo basi hakuwi kutolea habari kwa Mtume kuwa ni kujua ghaibu, bali ni kunakili kutoka kwa mwenye ujuzi wa ghaibu. Na tofauti ni kubwa baina ya chimbuko la ujuzi na yule anayenukuu kutoka kwenye chimbuko hilo. Kwa sababu, wa kwanza ni shina na wapili ni tawi. Vilevile kuna tofauti baina ya anayenukuu kutoka kwenye shina moja kwa moja na yule anaye nukuu kwa mnukuu huyu.

قَالُوا سُبْحَانَكَ لَا عِلْمَ لَنَا إِلَّا مَا عَلَّمْتَنَا إِنَّكَ أَنتَ الْعَلِيمُ الْحَكِيمُ ﴿٣٢﴾

“Wakasema: Utakatifu ni wako hatuna elimu isipokuwa ile uliyotufundisha; hakika wewe ndiwe mjuzi, mwenye hekima.” Juz.1 (2:32)

Aya hizi ni dalili mkataa juu ya kubatilika wanayoyasema masufi kwamba nafsi ya mtu kwa upande wa mazoezi ya kiroho inageukea kwenye mambo ya ghaibu na mgeuko huu wameuita elimu ya kimungu.

Sijui masufi wanachanganya vipi itikadi hii ya elimu ya kimungu na kumwamini Mwenyezi Mungu na Utume wa Nabii Muhammad(s.a.w.w) ?

Ya kushangaza zaidi ni yale aliyoyasema Ibn Al-Araby, katika Kitab Futuhatil – Makkiyya Juz.3 mlango wa 311, kwamba mwenye kumpenda Mwenyezi Mungu kwa mapenzi halisi anaweza kuigeuza nafsi yake kwenye kitu chochote anachotaka, iwe mnyama, mti, jiwe au maji.

Na kuwa hayo yametokea; Kwamba mmoja wa wapenzi wa Twariqa hii, yaani ya kisufi aliingia kwa Sheikh akajigeuza mbele yake kuwa ukufi wa maji. Sheikh alipoulizwa, fulani ameingia kwako na hakutoka, yuko wapi? Akawaambia: “Haya maji ndiye yeye!”

هُوَ الَّذِي خَلَقَكُم مِّن نَّفْسٍ وَاحِدَةٍ وَجَعَلَ مِنْهَا زَوْجَهَا لِيَسْكُنَ إِلَيْهَا فَلَمَّا تَغَشَّاهَا حَمَلَتْ حَمْلًا خَفِيفًا فَمَرَّتْ بِهِ فَلَمَّا أَثْقَلَت دَّعَوَا اللَّـهَ رَبَّهُمَا لَئِنْ آتَيْتَنَا صَالِحًا لَّنَكُونَنَّ مِنَ الشَّاكِرِينَ ﴿١٨٩﴾

189. Yeye ndiye aliyewaumba katika nafsi moja, na katika hiyo akamjaalia mkewe ili apate utulivu kwake Alipomkurubia alishika mimba nyepesi na kutembea nayo. Hata alipokuwa mzito, wote wawili walimwomba Mola wao, kama ukitupa mwema tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.

فَلَمَّا آتَاهُمَا صَالِحًا جَعَلَا لَهُ شُرَكَاءَ فِيمَا آتَاهُمَا فَتَعَالَى اللَّـهُ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿١٩٠﴾

190. Basi alipowapa mwema walimfanyia washirika katika kile alichowapa. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu na hao wanaowashirikisha.

ALIYEWAUMBA KATIKA NAFSI MOJA

Aya 189 – 190

MAANA

Aya mbili hizi sio masimulizi ya tukio lililotokea baina ya mtu na mkewe, kama inavyoonyesha dhahiri ya matamshi, isipokuwa ni kuzungumzia hali ya mtu alivyo, bila ya kuangalia mtu maalum.

Kwa ufupi masimulizi ya hali hiyo au tamthilia hiyo ni kuwa mtu akipatwa na machukivu au akitaka kupata ayatakayo hukimbilia kwa Mwenyezi Mungu akimwomba na kunyenyekea huku akiweka ahadi kwamba Mwenyezi Mungu akimpatia anayoyataka basi atamshukuru na kumtii, lakini akimpatia yale anayoyataka, hana habari tena na ahadi zake.

Baada ya utangulizi huu, inatakikana kufahamiwa misingi ya Aya hizi tunayoifafanua kama ifuatavyo.

Yeye ndiye aliyewaumba katika nafsi moja, na katika hiyo akamjaalia mkewe ili apate utulivu kwake.

Maneno katika ‘Aliyewaumba’ yanaelekezwa kwa watu wote. Maana ni kuwa. Enyi watu wote nyinyi ni kitu kimoja, kwa kwa jinsia, maumbile na rangi. Hakuna tofauti kabisa baina ya wa mashariki na wa magharibi, mwarabu na mwajemi, mweusi na mweupe wala baina ya mwanamume na mwanamke.

Suala la jinsia linahusu vitu vyote, Mwenyezi Mungu anasema:

وَمِن كُلِّ شَيْءٍ خَلَقْنَا زَوْجَيْنِ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿٤٩﴾

“Na katika kila kitu tumeumba dume na jike ili mpate kujua” (51:49)

Lengo katika hilo linajulikana, nalo ni kuchunga aina. Kuongezea lengo hilo ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemuumba mtu mke katika jinsi yake ili kila mmoja kati ya wawili hao apate utulivu kwa mwenzake na kuweko mapenzi na kuhurumiana baina ya wawili hao.

Alipomkurubia alishika mimba nyepesi na kutembea nayo. Hata alipokuwa mzito, wote wawili walimwomba Mola wao, kama ukitupa mwema tutakuwa miongoni mwa wanaoshukuru.

Kumkurubia, ni kumwingilia, kutembea nayo, ni kuendelea mimba bila ya kutoka, na kuwa mzito, ni kukaribia wakati wa kuzaa. Wakati huu ndipo baba na mama huelekea kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) na kumnyenyekea awaruzuku mtoto mwema; yaani aliye sawa kimaumbile na kihulka. Na kama Mwenyezi Mungu akiwatakabalia basi watashukuru neema hii kwa ukamilifu.

Basi alipowapa mwema walimfanyia washirika katika kile alichowapa.

Dhamir ya walifanya, ni ya mume na mke. Makusudio ya alichowapa ni mtoto waliyemtaka. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu alipowapa mtoto, walisema, kuwa fadhila na baraka ni za masanamu na wakamsahau Mwenyezi Mungu na yale waliyomwahidi.

Basi ametukuka Mwenyezi Mungu na hao wanaowashirikisha.

Yaani wanashirikisha makafiri wakiwemo hawa wawili mke na mume. Kwa mara nyingine tena tunasema kuwa lengo la masimulizi ni hali ya mtu alivyo, sio tukio maalum.


9

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

أَيُشْرِكُونَ مَا لَا يَخْلُقُ شَيْئًا وَهُمْ يُخْلَقُونَ ﴿١٩١﴾

191. Je, wanawashirikisha wale ambao hawaumbi kitu, hali wao wameumbwa?

وَلَا يَسْتَطِيعُونَ لَهُمْ نَصْرًا وَلَا أَنفُسَهُمْ يَنصُرُونَ ﴿١٩٢﴾

192. Wala hawawezi kuwasaidia wala kujisaidia wenyewe.

وَإِن تَدْعُوهُمْ إِلَى الْهُدَىٰ لَا يَتَّبِعُوكُمْ سَوَاءٌ عَلَيْكُمْ أَدَعَوْتُمُوهُمْ أَمْ أَنتُمْ صَامِتُونَ ﴿١٩٣﴾

193. Na kama mkiwaita kwenye uwongofu hawatawafuata, Ni sawa ikiwa mtawaita au mtanyamaza.

إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ عِبَادٌ أَمْثَالُكُمْ فَادْعُوهُمْ فَلْيَسْتَجِيبُوا لَكُمْ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿١٩٤﴾

194. Hakika hao mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni waja mfano wenu, Hebu waombeni nao wawaitikie ikiwa nyinyi mnasema kweli.

أَلَهُمْ أَرْجُلٌ يَمْشُونَ بِهَا أَمْ لَهُمْ أَيْدٍ يَبْطِشُونَ بِهَا أَمْ لَهُمْ أَعْيُنٌ يُبْصِرُونَ بِهَا أَمْ لَهُمْ آذَانٌ يَسْمَعُونَ بِهَا قُلِ ادْعُوا شُرَكَاءَكُمْ ثُمَّ كِيدُونِ فَلَا تُنظِرُونِ ﴿١٩٥﴾

195. Je, wao wanayo miguu ya kuendea? Au wanayo mikono ya kushika? Au wanayo macho ya kuonea? Au wanayo masikio ya kusikiliza? Sema: Waiteni hao mnaowashirikisha kisha nifanyieni vitimbi wala msinipe muda.

إِنَّ وَلِيِّيَ اللَّـهُ الَّذِي نَزَّلَ الْكِتَابَ وَهُوَ يَتَوَلَّى الصَّالِحِينَ ﴿١٩٦﴾

196. Hakika mlinzi wangu ni Mwenyezi Mungu aliyeteremsha Kitab naye ndiye awalindaye wafanyao mema.

وَالَّذِينَ تَدْعُونَ مِن دُونِهِ لَا يَسْتَطِيعُونَ نَصْرَكُمْ وَلَا أَنفُسَهُمْ يَنصُرُونَ ﴿١٩٧﴾

197. Na wale mnaowaabudu badala yake hawawezi kuwasaidia wala kujisaidia wenyewe.

وَإِن تَدْعُوهُمْ إِلَى الْهُدَىٰ لَا يَسْمَعُوا وَتَرَاهُمْ يَنظُرُونَ إِلَيْكَ وَهُمْ لَا يُبْصِرُونَ ﴿١٩٨﴾

198. Na kama mkiwaita kwenye uongofu hawatasikia, Na unawaona wanakutizama, nao hawaoni.

JE, WANAWASHIRIKISHA WASIOUMBA KITU?

Aya 191 – 198

MAANA

Je, wanawashirikisha wale ambao hawaumbi kitu, hali wao wameumbwa?

Kuumba na amri ni ya Mwenyezi Mungu tu ndiye ambaye kukiambia kitu kuwa kikawa. Yoyote asiyekuwa Yeye, yakiwemo masanamu, anamhitajia Yeye katika asili ya kupatikana kwake na katika kuendelea kuweko kwake.

Wala hawawezi kuwasaidia wala kujisaidia wenyewe.

Usaidizi, ushindi, utukuzaji na udhalilishaji, yote hayo yako chini ya uwezo wa Mwenyezi Mungu. Masanamu yanayokojolewa na paka na mbwa hayawezi kusaidia wala kujisaidia.

Na kama mkiwaita kwenye uwongofu hawatawafuata, Ni sawa ikiwa mtawaita au mtanyamaza.

Haya masanamu hayaumbi, hayasaidii wala hayajisaidii, hayaongoki wala hayaongozi, hayamwiti yeyote wala hayaitikii mwito wa yeyote. Pamoja na yote haya yanaabudiwa!

Hakika hao mnaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni waja mfano wenu, Hebu waombeni nao wawaitikie ikiwa nyinyi mnasema kweli.

Mmedai nyinyi washirikina kwamba masanamu ni miungu; na Mungu hunufaisha na kudhuru, hutoa na kuzuia, basi waombeni ili tuone kuwa je, wataitikia maombi yenu?

Je, wao wanayo miguu ya kuendea? Au wanayo mikono ya kushika? Au wanayo macho ya kuonea? Au wanayo masikio ya kusikiliza?.

Huku ni kuamshwa na kuzinduliwa washirikina kwamba wao ni bora kuliko masanamu wanayoyaabudu. Kwa sababu wao wana akili za utambuzi, macho ya kuona, masikio ya kusikia, miguu ya kutembelea, mikono ya kushika na ndimi za kutamka.

Lakini masanamu hayana chochote katika hayo, Sasa imekuaje aliye duni ndiye anayeabudiwa badala ya aliye mkamilifu?

Sema: Waiteni hao mnaowashirikisha kisha nifanyieni vitimbi wala msinipe muda.

Anaambiwa Nabii Muhammad(s.a.w.w) awaambie washirikina, ikiwa masanamu yenu yana kitu, kama mnavyodai, basi mimi ninayadharau pamoja na nyinyi, basi kama mnaweza shindaneni wala msingoje.

Hakika mtawala wangu ni Mwenyezi Mungu aliyeteremsha Kitab naye ndiye awalindaye wafanyao mema.

Baada ya Mtume(s.a.w.w) kuwakana washirikina na miungu yao aliwaam- bia kuwa nyinyi mnawatawalisha masanamu na mimi ninatawalisha Mungu aliyeniteremshia Qur’an iliyo na ubainifu wa kila kitu yake, Yeye vilevile anasimamia hifadhi yangu nani mlinzi wangu.

Je, masananu yenu yana kitabu? Je,yanawalinda? Natija ikawa, kama wanavyojua wote, ni kudhalilika washirikina na kutukuka Uislam na waislamu.

Na wale mnaowaabudu badala yake hawawezi kuwasaidia wala kuji- saidia wenyewe.

Imetangulia punde katika Aya 192. Kumekuja kukaririka kwa sababu Mtume(s.a.w.w) alishindana na masanamu, kuwa yampe madhara, ndipo ikanasibu kuishiria kwamba hayo hayawezi hata kujisaidia yenyewe.

Na kama mkiwaita kwenye uongofu hawatasikia.

Vilevile imetangulia katika Aya 193, kukiwa kukaririka ni kwa lengo hilo hilo.

Na unawaona wanakutizama,nao hawaoni.

Inafahamisha nasi hii kwamba masanamu yalikuwa sawa na masanamu haya yaliyomo makanisani. Na kwamba Waarabu walikuwa ni wasanii wa kuchonga. Kwani wao waliyafanya masanamu yao yaonekane kama yanaona ukiyatazama haraka haraka.

Utauliza : Kwa nini Mwenyezi Mungu amerudiarudia katika Aya zinazo fanana kwamba masanamu hayadhuru wala hayanufaishi, hayasaidii wala hayajisaidii na kwamba hayana mikono wala miguu wala macho, mpaka kufikia Aya tisa ambapo ingeotosha tu kusema hayo ni mawe?

Jibu : Fikra ya kuabudu mizimu na masanamu ilitawala sana katika akili za waarabu na ikachanganyika na roho zao na damu zao kwa vizazi na karne. Imani yao hii ilikuwa na nguvu kuliko kumwamini Mwenyezi Mungu waliyemfanya ni mshirika wa masanamu.

Kwa hiyo haikuwa rahisi kubadili itikadi yao hii. Wao walikuwa wakijitolea kwa pumzi zao zote, kama ikitajwa kwa ubaya imani yao hiyo.

Ndipo ikalazimika kukaririka huko na kusisitiza na kufananua. Hebu tufaradhie mtu mmoja wa kanisa ajaribu kuondoa picha na sanamu ndani ya kanisa. Je, itatosha aseme tu, hizi ni karatasi na mawe au itabidi atoe hotuba ndefu na pana?

خُذِ الْعَفْوَ وَأْمُرْ بِالْعُرْفِ وَأَعْرِضْ عَنِ الْجَاهِلِينَ ﴿١٩٩﴾

199. Shika usamehevu na amrisha mema na achana na wajinga.

وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ إِنَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٢٠٠﴾

200. Na kama uchochezi wa shetani ukikuchochea, basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu; hakika yeye ndiye asikiaye na ajuaye.

إِنَّ الَّذِينَ اتَّقَوْا إِذَا مَسَّهُمْ طَائِفٌ مِّنَ الشَّيْطَانِ تَذَكَّرُوا فَإِذَا هُم مُّبْصِرُونَ ﴿٢٠١﴾

201. Hakika wale wanye takuwa zinapowagusa pepesi za shetani huzinduka.

وَإِخْوَانُهُمْ يَمُدُّونَهُمْ فِي الْغَيِّ ثُمَّ لَا يُقْصِرُونَ ﴿٢٠٢﴾

202. Na ndugu zao wanawavutia katika upotofu kisha wao hawaachi.

وَإِذَا لَمْ تَأْتِهِم بِآيَةٍ قَالُوا لَوْلَا اجْتَبَيْتَهَا قُلْ إِنَّمَا أَتَّبِعُ مَا يُوحَىٰ إِلَيَّ مِن رَّبِّي هَـٰذَا بَصَائِرُ مِن رَّبِّكُمْ وَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٢٠٣﴾

203. Na usipowaletea ishara, husema: "Kwa nini hukuibuni?" Sema: Hakika nafuata niliyopewa wahyi kutoka kwa Mola wangu tu. Hizi ni busara zitokazo kwa Mola wenu na ni uwongofu na rehema kwa watu wanaoamini.

SHIKA USAMEHEVU

Aya 199 – 203

MAANA

Shika usamehevu na amrisha mema na achana na wajinga.

Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimfunza tabia njema Mtume wake Nabii Muhammad(s.a.w.w) , naye alikuwa akisema katika dua yake: “Ewe Mwenyezi mungu nifanye mzuri wa maumbile na tabia na niepushe na tabia mbaya.” Alimwitikia dua yake na akamtimizia tabia njema kisha akamtuma kutimiza tabia njema kwa watu wote.

Aya hii ni miongoni mwa mafunzo ya Mwenyezi Mungu kwa Mtume wake mtukufu(s.a.w.w) . nayo imekusanya misingi mitatu ya sharia na adabu.

USAMEHEVU

Nao ni kuchukulia upole bila uzito wala mashaka. Nako kunakua katika vitendo na hulka. Na katika mali ni ile iliyozidi haja.

Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake kutowatia kwenye uzito na mashaka katika anayowaamrisha na kuwakataza. Na kuchukua Zaka ya mali yao katika kinachozidi haja zao. Huu ni msingi katika misingi ya sharia.

وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ ﴿٧٨﴾

“Wala hakuweka juu yenu uzito katika dini” (22:78)

Na pia alimwamrisha kutowakalifisha hulka; kama kumwamrisha mmoja wao asamehe deni lake au asichukue kisasi.

KUAMRISHA MEMA

Ni kheri inayojulikana na iliyo wazi anayoijua mtu kwa umbile lake.

NA ACHANA NA WAJINGA

Wale ambao hakutarajiwi kuongoka kwao kwa hoja na dalili wala kwa mawaidha na uongozi. Huenda ikawa kuwapuuza na kuachana nao ni vizuri kuliko kuwaongoza.

Amesema Sheikh Maraghi katika tafsir ya Aya hii: “Imepokewa kutoka kwa Jafar As-Sadiq (r.a) kwamba yeye amesema: “Hakuna katika Qur’an Aya inayokusanya maadili mema kama hii.”

Na kama uchochezi wa shetani ukikuchochea, basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu; hakika yeye ndiye asikiaye na ajuaye.

Mtume hukasirika, hilo halina shaka, lakini yeye anakasirika kwa ajili ya Mwenyezi Mungu; hata kukasirika kwa nafsi yake ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Huenda akakasirikia ujinga wa mjinga katika alioamrishwa kuachana nao na kutaka kumkabili kwa neno litakalomstahiki.

Ndipo Mwenyezi Mungu mtukufu akamwambia kwa kumfundisha: Ikisadifu kukutokea mfano wa hali hii, basi ghadhabu isiondoe upole wako, vumilia na mtake hifadhi Mwenyezi Mungu, kwani yeye anakusikia na kukuitikia na anajua yanayokupata kutoka kwa wajinga.

Hapana budi kuishiria kuwa kauli yake hii Mwenyezi Mungu ni kiasi cha kukadiria tu, kutokana na neno ‘kama’ sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu:

لَئِنْ أَشْرَكْتَ لَيَحْبَطَنَّ عَمَلُكَ وَلَتَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ ﴿٦٥﴾

”Kama ukishirikisha, hakika amali zako zitapomoka na utakuwa miongoni mwa wenye hasara. (39:65).

Kimsingi ni kwamba kukadiri muhali sio muhali. Katika Juz.3 (3:60) kifungu ‘Mtume na Isma’, tumebainisha kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaweza kuwakataza maasi Mitume wake walio maasum; Kwa sababu kukataza kwake kunatoka juu kuja chini; na wala haijuzu kwa yeyote, asiyekuwa Mwenyezi Mungu, kuwaamrisha au kuwakataza.

Hakika wale wenye takuwa zinapowagusa pepesi za shetani huzinduka.

Hakuna mtu asiyeshindana na misukumo ya kibinafsi, baadhi yake ni ya tamaa ya moyo, mingine ni ya akili na pia ya kidini.

Mara nyingi dini na akili hushindwa na msukumo wa moyo. Kwa sababu unachimbuka katika dhati ya mtu, na unakuwa naye tangu yuko tumboni mwa mama yake.

Na akili inakuja baadae, nayo hukua kwa mafunzo na majaribio. Ama dini imeletwa kuuzoeza msukumo wa moyo na kuufunga hatamu.

Nayo utendaji kazi wake ni dhaifu, isipokuwa tu kwa mtu aliyekinai kwa nafsi yake na dhati yake, kwa namna ambayo haoni wema, isipokuwa wa dini na kufanya amali kulingana na hukumu zake.

Aina hii ya wanadini ndio wale ambao dini yao inashinda mapondokeo yao. Ndio wanokusudiwa na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Zinapowagusa pepesi za shetani huzinduka” Yaani shetani akiwahadaa kwa maasia ya Mwenyezi Mungu au akiwapa wasiwasi wa nafsi inayoamrisha uovu, basi hukumbuka aliyowaamrisha Mwenyezi Mungu na aliyowakataza. Mara wao hutambua vitimbi vya shetani na wasiwasi wa nafsi, basi hujizuia na maasi na dini yao hushinda hawa zao.

Na ndugu zao wanawavutia katika upotofu kisha wao hawaachi.

Makusudio ya ndugu hapa ni mashetani. Dhamir ya ndugu zao inarudia kwa washirikina ambao wametajwa. Makusudio ya hawaachi, ni kuwa shetani haachi kuwapoteza washirikina na kuwaharibu. Kwa ufupi ni kwamba mashetani ndio ndugu wa washirikina hawaachi kuwapoteza.

Na usipowaletea ishara, husema: Kwa nini hukuibuni?

Washirikina walikuwa wamemtaka Mtume miujiza maalum kwa njia ya inadi. Kama hakuwaletea muujiza huo husema: Kwani huwezi kuufanya mwenyewe, kwani wewe si ni Mtume?

Sema: Hakika nafuata niliyopewa wahyi kutoka kwa Mola wangu tu.

Yaani sema ewe Muhammad kuwaambia hawa wenye inadi: Ndio mimi ni Mtume, lakini Mtume hatengenezi muujiza wala haonyeshi ishara yoyote au kuipendekeza kwa Mwenyezi Mungu; bali anangoja wahyi na kuufik- isha kwa waja wake.

Hii ni busara zitokazo kwa Mola wenu na ni uwongofu na rehema kwa watu wanaoamini.

Hii ni ishara ya Qur’an na busara ni hoja na dalili ambazo mwenye akili anapata busara kwazo.

Baada ya Mtume(s.a.w.w) kuwaambia washirikina kuwa nafuata niliyope- wa wahyi kutoka kwa Mola wangu, aliwaambia, na Mwenyezi Mungu amenipa wahyi hii Qur’an ambayo ina dalili wazi za utume wangu. Nayo ni uwongofu na rehema kwa anayetaka kuamini haki kwa njia ya haki.

Mkiwa mwaitafuta haki, kama mnavyodai, basi acheni shirk na msilimu. Vinginevyo basi nyinyi ni watafutaji manufaa na watu wa malengo yenu tu.

وَإِذَا قُرِئَ الْقُرْآنُ فَاسْتَمِعُوا لَهُ وَأَنصِتُوا لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٢٠٤﴾

204. Na isomwapo Qur’an isikilizeni na mnyamaze ili mpate kurehemiwa.

وَاذْكُر رَّبَّكَ فِي نَفْسِكَ تَضَرُّعًا وَخِيفَةً وَدُونَ الْجَهْرِ مِنَ الْقَوْلِ بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ وَلَا تَكُن مِّنَ الْغَافِلِينَ ﴿٢٠٥﴾

205. Na mtaje Mola wako nafsini mwako kwa unyenyekevu na hofu na bila ya kupiga kelele kwa kauli, asubuhi na jioni, Wala usiwe miongoni mwa walioghafilika.

إِنَّ الَّذِينَ عِندَ رَبِّكَ لَا يَسْتَكْبِرُونَ عَنْ عِبَادَتِهِ وَيُسَبِّحُونَهُ وَلَهُ يَسْجُدُونَ ۩﴿٢٠٦﴾

Hakika wale walioko kwa Mola wako hawajivuni wakaacha kumwabudu na wanamtakasa na wanaumsujudia.

ISOMWAPO QUR’AN ISIKILIZENI

Aya 204 – 206

MAANA

Na isomwapo Quar’an isikilizeni na mnyamaze ili mpate kurehemiwa.

Alipotaja Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya iliyotangulia kwamba hii Qur’an ni busara na uwongofu na rehema, anaamrisha katika, Aya hii, kuisikiliza na kunyamaza ili kuzingatia uwongofu na dalili zilizomo. Hapana shaka kwamba mwenye kuizingatia vyema Qur’an na akawaidhika nayo, basi yeye anastahiki rehema ya Mwenyezi Mungu na radhi zake.

Wameafikiana mafakihi, isipokuwa wa madhebu ya Dhahiriya, kwamba kuinyamazia Qur’an ni sunna na wala sio wajibu kwa asiyekuwa Maamuma anayeswali nyuma ya Imam.

Wamehitalifiana kuhusu Maamuma, kuwa je, ni wajibu asikilize na amnyamazie Imam akiwa anasoma Qur’an? Kuna kundi lililosema kuwa ni wajibu na wengine wakasema si wajibu.

Kwa hali yoyote iwavyo, ni kwamba amri katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:

‘Isikilizeni’ na nyamazeni’ ni ya kupendekeza sio ya wajibu. Kwa sababu amri hii hukumu yake ni kama hukumu ya Aya inyofuatia (Na mtaje Mola wako moyoni mwako…) Kwa sababu, zote mbili zimekuja katika mfumo mmoja. Na amri ya kutaja ni ya sunna, kwa hiyo pia amri ya kusikiliza na kunyamaza.

Zaidi ya hayo ni kwamba kumnyamazia kila msomaji ni jambo zito na lenye mashaka; hasa hivi sasa ambapo kusomwa Qur’an katika vipaza sauti ni kama mchezo na nyimbo; watu hupaaza sauti kukiwa na tukio na hata kama hakuna.

Na mtaje Mola wako nafsini mwako kwa unyenyekevu na hofu na bila ya kupiga kelele kwa kauli, asubuhi na jioni.

Msemo katika ‘Mtaje’ unaelekezwa kwa Nabii Muhammad na makusudio ni kwa wote. ‘Bila ya kupiga kelele’ maana yake ni mtaje Mola wako kwa sauti ya katikati baina ya sauti kubwa na ndogo. Na asubuhi na jioni ni fumbo la kudumu kumtaja na kumkumbuka.

Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘Bila ya kupiga kelele’ inafahamisha wazi kwamba mtu anayeinua sauti yake kwa kusoma Qur’an basi ameacha mapendekezo na kufanya kinyume; hasa ikiwa ni kwa kuwasumbua wali- olala.

Wala usiwe miongoni mwa walioghafilika na kumtaja Mwenyezi Mungu katika nafsi yako.

Kwa sababu kumtaja kwa ulimi tu, kunafanana na maneno matupu yasiyo kuwa na maana. Maana ya kumtaja Mwenyezi Mungu mtukufu katika nafsi ni kujua kwamba Mwenyezi Mungu peke yake ndiye muumba mwenye kuruzuku mwenye kutoa uhai na mwenye kufisha na mwenye kuanzisha na kurud- isha.

Kumtaja kuliko bora ni kuogopa mtu kumfanyia ubaya ndugu yake binadamu kwa kuhofia mateso ya Mwenyezi Mungu; na bora zaidi kwake ni kumfanyia wema kwa kutaraji thawabu za Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Tunasema bila ya kusita kuwa; haya ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu:

وَلَذِكْرُ اللَّـهِ أَكْبَرُ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تَصْنَعُونَ ﴿٤٥﴾

“Na kwa hakika kumbuko la Mwenyezi Mungu ni (jambo) kubwa kabisa, Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda” (29:45)

Kauli yake: “anajua mnayoyatenda” baada ya kusema “na kumbuko la Mwenyezi Mungu ni kubwa”, kunatilia nguvu kuwa kumtaja na kumkumbuka Mwenyezi Mungu ni kuwafanyia wema waja wa Mwenyezi Mungu.

Na mwenye hasara zaidi katika watu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule anayefanya Tahlili na takbira, na huku anafanya ufisadi katika nchi kwa kudanganya na hadaa na kuwasaidia mataghuti na wakoloni dhidi ya waja wanyonge wa Mwenyezi Mungu wasio na hatia.

Hakika wale walioko kwa Mola wako hawajivuni wakaacha kumwabudu na wanamtakasa na wanamsujudia.

Wafasiri wanasema kuwa Mwenyezi Mungu amewakusudia Malaika,Wametoa dalili ya neno walioko kwa Mola wako. Kwa sababu walioko kwa Mwenyezi Mungu ni Malaika.

Lakini inawezekana kwamba makusudio ni kila mwenye nafasi na jaha mbele ya Mwenyezi Mungu; ni sawa awe ni Malaika au mwanadamu.

Wametofautiana mafakihi, kuwa je ni wajibu, kusujudu wakati wa kusomwa Aya iliyo na neno

‘Wanasujudi’, kama hii?

Amenukuu Tabrasi kauli kutoka kwa Hanafi kuwa ni wajib na kutoka kwa Shafii na Shia Imamiya kuwa ni sunna yenye kutiliwa mkazo.

Ikumbukwe kuwa Shia Imamia wamewajibisha kusujudi msomaji na msikilizaji zinaposomwa Aya zilizo katika Sura nne: 32, 41, 53 na 96.

MWISHO WA SURA YA SABA


10

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

Sura Ya Nane: Surat Al-Anfal

Ina Aya 75. Imeshuka Madina, isipokuwa Aya 30 hadi 36, hizo zimeshuka Makka.

بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu

يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْأَنفَالِ قُلِ الْأَنفَالُ لِلَّـهِ وَالرَّسُولِ فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَصْلِحُوا ذَاتَ بَيْنِكُمْ وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١﴾

1. Wanakuuliza juu ya Anfal. Sema Anfal ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume. Basi mcheni Mwenyezi Mungu na msuluhishe mambo baina yenu, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni waumini.

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٢﴾

2. Hakika waumini ni wale ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa hofu, Na wanaposomewa Aya zake huwazidisha imani, Na wanamtegemea Mola wao.

الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ ﴿٣﴾

3. Ambao wanasimamisha Swala. Na wanatoa katika yale tuliyowaruzuku.

أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا لَّهُمْ دَرَجَاتٌ عِندَ رَبِّهِمْ وَمَغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ ﴿٤﴾

4. Hao kweli ndio waumini. Wao wana vyeo kwa Mola wao, na maghufira na riziki bora.

ANFAL NI YA MWENYEZI MUNGU NA MTUME

Aya 1 – 4

MAANA

Wanakuuliza juu ya Anfal

Katika Aya hii Mwenye Mungu (s.w.t) ametaja kwamba: watu walimuuliza Mtume(s.a.w.w) kuhusu Anfal, wala hakubainisha makusudio yake.

Wameifikiana watu wa elimu ya dini kwamba neno lolote litakalokuja katika kitabu cha Mwenyezi Mungu na Hadith za Mtume bila ya kuelezwa maana yake, basi litachukuliwa kwenye maana wanayoifahamu watu, Ikiwa watu hawalijui maana yake, zitarudiwa kamusi za lugha.

Kamusi zinasema: Anfal ni ngawira na ziada kwa ujumla bila ya kuyafunga maana yake na ngawira au ziada maalum.

Kwa ajili hiyo ndipo wafasiri wakatofautiana katika makusudio ya Anfal, Je, ni ngawira zote au ni ngawira za Badr tu au ni ngawira nyingine.

Shia Imamia wamesema: “Hakuna sababu ya kutofautiana huku. Kwa sababu imethibiti katika Hadith za Mtume kwa riwaya za Ahlul-bait wa Mtume Muhammad(s.a.w.w) kwamba makusudio ya Anfal ni ardhi iliyochukuliwa kwa wasiokuwa waislamu bila vita na ardhi iliyokufa, ni sawa iwe ilikuwa ikimilikiwa kisha akatoweka mmiliki au la. Pia vilele vya milima, mabonde, misitu minene na kila kinachohusika na vita, kwa sharti ya kuwa kisiwe kimechukuliwa kwa mwislamu au mwenye mkataba. Vilevile na mirathi ya asiyekuwa na mrithi.

Haya yanaafikiana na madhehebu ya Malik, kwa sababu wao wamefasiri Anfal kuwa ni kilichochukulia bila ya vita. Hayo yanapatikana katika Kitab Ahkamul Qur’an cha Abu Bakar, maaruf kwa jina la Ibn Arabi Al-Muafiri. Abu Is-haq Al-fairuzbadi, wa madhehebu ya Shafi, anasema:

Anfal ni kutoa ziada Amiri jeshi kwa aliyefanya tendo lililopelekea kushindwa adui; kama vile uchunguzi, kuonyesha njia au ngome n.k.

Naye Al-Jisas wa madhehebu ya Hanafi anasema: “Ni kusema Amiri jeshi: Atakayemuuwa mtu basi vitu vyake ni vyake na atakayepata kitu ni chake.”

Sema Anfal ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume.

Huu ni ubainifu wa mahali pa Anfal, na kwamba ni ya Mwenyezi Mungu, na cha Mwenyezi Mungu ni cha Mtume wake, na cha Mtume wake hutolewa kwa kuinua tamko la Uislam na maslahi ya waislamu, Atachukua kila mwenye haja kiasi cha haja yake, Ufafanuzi umo katika vitabu vya Fiqh, kikiwemo kitabu chetu Fiqhul-Imam Jafar As-Sadiq Juz. 2.

Basi mcheni Mwenyezi Mungu na msuluhishe mambo baina yenu, na mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikiwa nyinyi ni waumini.

Hii inatambulisha kuwa swahaba walizozana juu ya Anfal, na walipomuuliza Mtume(s.a.w.w) aliwaambia, kwa amri itokayo kwa Mwenyezi Mungu, kuwa hiyo ni ya Mwenyezi Mungu na Mtume, na kwamba ni juu yao kuitoa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake wala wasigombane juu ya Anfal na mengineyo, waungane wapendane kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kama ilivyo kwa waumini wa kweli.

Kisha Mwenyezi Mungu mtukufu akawafafanulia kwamba waumini wa kweli ni wale wanaosifika na sifa zifuatazo:

1.Hakika waumini ni wale ambao anapotajwa Mwenyezi Mungu nyoyo zao hujaa hofu.

Hofu inakuwa kwa waumini, kwa sababu ya kukutana kwao na Mwenyezi Mungu, hisabu yake na malipo yake, Lakini wao wakati huo huo wanataraji rehema ya Mwenyezi Mungu. Kwa sababu wao vilevile wanaamini kauli yake Mwenyezi Mungu:

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا إِنَّهُ هُوَ الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿٥٣﴾

“Enyi waja wangu mliojidhulumu nafsi zenu msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika yeye ni Mwingi wa kusamehe mwingi wa kurehemu” (39:53).

Na pia kauli ya Mwenyezi Mungu:

كَتَبَ رَبُّكُمْ عَلَىٰ نَفْسِهِ الرَّحْمَةَ ﴿٥٤﴾

Mola wenu amejilazimisha rehema. (6:54)

Miongoni mwa aliyoyasema Imam Ali(a.s) katika kuwasifu waumini:“Wao na pepo ni kama waliyoiona wakiwa ndani wananeemeshwa. Na wao na moto ni kama waliouona, wakiwa ndani wanaadhibiwa”

Anasema mshairi katika kuwasifu: Yalingana hofu na matarajio si kwa kuogopa wala tamanio

2.Na wanaposemewa Aya zake huwazidisha Imani.

Kwa sababu wao na dini yao ni kama vile wameiona ghaibu kwa macho. Bali wanaweza kutilia shaka wanaloliona kwa jicho. Kwa sababu macho mara nyingine hudanganya mtu akadhani mangati ni maji na uvimbe ni shahamu, Lakini kauli yake Mwenyezi Mungu haina shaka hata chembe.

DINI HAIOTESHI NGANO

3.Na wanamtegemea Mola wao.

Maana ya kutegemea sio tu kusema kwa midomo yetu: Tumemtegemea Mungu, pia sio kuacha visababishi na kuacha kufanya kazi kwa kutegemea mambo yaje yenyewe tu, na sisi tumekaa. Isipokuwa kutegemea ni kuhangaika, kama alivyotuamrisha Mwenyezi Mungu, tukitaraji tawfik kutoka kwake katika kuhangaika kwetu tukiamini kuwa kazi ni sharti la msingi la kutegemea. Na kwamba hiyo ni ibada, na kutii kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِن رِّزْقِهِ ُ ﴿١٥﴾

Basi tembeeni katika pande zake zote na kuleni katika riziki zake. (67:15).

Hakika kuamini na kumtegemea Mwenyezi Mungu bila ya kazi hakuwezi kuotesha ngano wala kuponesha mgonjwa; vinginevyo Mwenyezi Mungu asingetuumbia mikono na miguu kwa ajili ya kufanya kazi.

Ndio! Dini ya kweli inaotesha upendo, ikhlas na msimamo, lakini sio mkate na dawa, hata elimu haitupatii chakula wala haitupozi magonjwa; isipokuwa inatufundisha jinsi ya kulima chakula na kutengeneza dawa; kisha haitushughulikii kuwa tutakufa na njaa na magonjwa au hatutakufa.

Dini inatuhimiza kushghulikia maisha yetu, Ndiyo maana inatuhimiza elimu na kufuata njia zake, na inazingatia kuwa kuipuuza ni kosa, kwani kutasababisha madhara na ufisadi.

Elimu nayo inapanga mkakati wa maisha mazuri. Na hayo ndiyo yanayolengwa na Uislamu. Kwa ajili hiyo Uislamu umeamrisha na kuhimiza elimu; sawa na Swaumu na Swala, na ataadhbiwa atakayeitumia elimu kwa unyang’anyi na uchokozi; kama ambavyo ataadhibiwa atakayeiharibu dini kwa manufaa yake ya kiutu.

Kwa ufupi ni kwamba, ikiwa ni sawa kuwa mtu hawezi kuishi kwa mkate peke yake, Vilevile hawezi kuishi kwa Swala peke yake.

4.Ambao wanasimamisha Swala. Na wanatoa katika yale tuliy- owaruzuku.

Sifa zilizotangulia ni za hali ya moyo, na Swala na Zaka ni katika vitendo vya mwili, vyote viwili ni natija ya kumwamini Mwenyezi Mungu na kumhofia na kumtegemea. Mwenye kuacha Swala hahisabiwi kuwa ni katika waumini wa kweli, na dalili ni kauli yake Mwenyezi Mungu:

Hao kweli ndio waumini, Wao wana vyeo kwa Mola wao, na maghufira na riziki bora.

Hao, ni ishara ya wale waliokusanya sifa tano; waumini wa kweli, ni wale ambao imani yao inaonekana katika vitendo vyao, si katika kauli zao tu. Vyeo mbele ya Mwenyezi Mungu vinatofautiana kufuatana na juhudi na kujitolea mhanga, mwenye cheo cha juu zaidi ni yule ambaye watu wamenufaika naye na akavumilia mengi ili waja wa Mwenyezi Mungu wote waishi katika kivuli cha amani na uadilifu. Maghufira ni kukiuka utelezi; na riziki bora ni pepo.

كَمَا أَخْرَجَكَ رَبُّكَ مِن بَيْتِكَ بِالْحَقِّ وَإِنَّ فَرِيقًا مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ لَكَارِهُونَ ﴿٥﴾

5. Kama alivyokutoa Mola wako nyumbani kwako kwa haki, na hakika kundi moja la waumini linachukia.

يُجَادِلُونَكَ فِي الْحَقِّ بَعْدَ مَا تَبَيَّنَ كَأَنَّمَا يُسَاقُونَ إِلَى الْمَوْتِ وَهُمْ يَنظُرُونَ ﴿٦﴾

6. Wanajadiliana nawe katika haki baada ya kubainika. Kama kwamba wanasukumwa katika mauti na huku wanaona.

وَإِذْ يَعِدُكُمُ اللَّـهُ إِحْدَى الطَّائِفَتَيْنِ أَنَّهَا لَكُمْ وَتَوَدُّونَ أَنَّ غَيْرَ ذَاتِ الشَّوْكَةِ تَكُونُ لَكُمْ وَيُرِيدُ اللَّـهُ أَن يُحِقَّ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ وَيَقْطَعَ دَابِرَ الْكَافِرِينَ ﴿٧﴾

7. Na alipowaahidi moja ya makundi mawili kuwa ni lenu. Nanyi mkapenda lile lisilo na nguvu ndio liwe lenu. Na Mwenyezi Mungu anataka kuihakikisha haki kwa maneno yake na kuikata mizizi ya makafiri.

لِيُحِقَّ الْحَقَّ وَيُبْطِلَ الْبَاطِلَ وَلَوْ كَرِهَ الْمُجْرِمُونَ ﴿٨﴾

8. Ili kuihakikisha haki na kuivunja batili; ijapokuwa watachukia wafanyao makosa.

KAMA ALIVYOKUTOA MOLA WAKO

Aya 5 – 8

KWENDA BADR

Mtume(s.a.w.w) alitumwa kufikisha ujumbe akiwa na umri wa miaka arubaini na akakaa Makka, miaka kumi na tatu, Kisha akahamia Madina ambako aliingia siku ya Jumatatu tarehe 12 Rabiul-Awwal (Mfungo sita).

Akaishi hapo kwa muda wa mika kumi, na kufariki Jumatatu, tarehe 12 Rabiul-Awwal akiwa na umri wa miaka Sitini na tatu[1] .

Alipotulia Madina akawa anatuma vikosi kwenye misafara ya washirikina kuchunguza habari zao na kuwashtua. Al-Mas’udi anasema: Vita alivyoviongoza Mtume mwenyewe ni 26, katika hivyo alipigana tisa.

Hapa tunaeleza kutoka kwake kwenda Baadr kwa sababu ni maudhiu ya Aya tulizo nazo sasa, vita hii ilidhihirisha mwanzo wa nguvu za waislamu dhidi ya washirikina ambao walikuwa wakiwanyanyasa na kuwaudhi waislamu zaidi ya miaka kumi na tatu, huku waislamu wakipata mateso hayo na maudhi kwa kuvumilia kwa kustahmili. Kwa sababu kushindana nao na udhaifu waliokuwa nao ni sawa na kujichinja.

Kwa ufupi kisa cha Badr ni kwamba Mtume(s.a.w.w) alisikia kuwa Abu Sufyan anarudi kutoka Sham na msafara ulio na mali nyingi. Katika jumla ya mali hizo ni zile walizozitaifisha kutoka kwa Muhajirin (Wahamiaji) walizoziacha Makka.

Basi Mtume akawakusanya maswahaba akawahimiza kutoka kuchukua mali za msafara. Baadhi wakaingia uvivu na kuchukia kutoka kwa kuhofia Maquraish. Kisha wakaenda pamoja na Mtume.

Hapo ilikuwa ni tarehe 17 Ramadhan mwaka wa pili wa Hijra. maswahaba walikuwa hawajui kuwa sasa wanakwenda kwenye mojawapo ya vita kuu ya waislamu na yenye athari kubwa katika maisha ya Kiislamu na waislamu.

Mayahudi wakamtuma mtu wa kumwonya Abu Sufyan akiwa njiani. Naye akatuma ujumbe kwa maquraish akiwataka waende wakawaokoe. Kukatokwa huko Makka, hakubaki hata mtu mmoja awezaye kushika silaha,Waislamu wakati huo bado wako njiani kuelekea Badr. Lakini Abu Sufyan akabadisha njia akapitia mwambao wa Bahari nyekundu.

Mtume alipopata habari hiyo akawashauri Maswahaba kuwa je, waaendelee na vita au watarudi Madina? Wakati huo huo akawaambia kuwa Mungu amewaahidi mojawapo ya makundi mawili kama wakienda kupigana.

Makundi mawili hayo, ni masfara uliobeba mali, na jeshi la maquraish waliotoka kuja kuhami mali. Wengi wakashauri kuendelea na vita, na baadhi wakachukia, kama walivyochukia tangu mwanzo.

Hatimaye wakaungana kuwakabili maquraish, Hapo Mtume(s.a.w.w) akawaambia: “Nendeni kwa baraka ya Mwenyezi Mungu. Wallah kana kwamba mimi ninaona vifo vya watu, basi jiandaeni na vita.”

Idadi ya maquraish walikuwa wapiganaji elfu moja wakiwemo wapanda farasi mia moja, Waislamu walikuwa mia tatu wakiwa na mpanda farasi mmoja tu, wengine wanasema walikuwa wawili. Wakawaua washirikina sabini na kuteka sabini waliobaki wakakimbia. Kwa upande wa Waislamu walikufa mashahidi watu 14 na hakuna aliyetekwa.

Vita hii ilikuwa ushindi wa kwanza wa waislamu uliobadilisha hali zao, na kupata watu wengi, wakawa wanakabili nguvu kwa nguvu na ukali kwa ukali sio tena kunyamaza au kukimbia nchi.

Baada ya utangullizi huuu, sasa tunaingilia kufasiri Aya:

MAANA

Kama alivyokutoa Mola wako nyumbani kwako kwa haki, na hakika kundi moja la Waumini linachukia.

Makusudio ya nyumba ni Madina. Wakati Mtume alipotaka kutoka Madina kwenda kuukamata msafara, baadhi ya jamaa walikuwa wazito na wakasema: “Hatuwawezi Maquraish.” Wakatoka kwa kuchukia pamoja na waliotoka kwa kupenda.

Huko njiani Mtume akawapa habari ya maquraish kuwa wanakuja kutoka Makka, Akawataka ushauri kuwa wataendelea na vita au watarudi Madina? Baadhi wakachukia na kusema kuwa sisi tumetoka kwa ajili ya msafara tu. Lakini wengi wakasema: “Tutakwenda nawe kupigana.” Kisha wakaenda wote kwa baraka ya Mwenyezi Mungu.

Aya hii inaashiria misismamo miwili ya baadhi ya Swahaba: Kuchukia kutoka Madina kwenda kwenye msafara na wapili ni kuchukia kuendelea na vita, baada ya kutoka kwa ajili ya msafara tu.

Hayo ndiyo maana ya Aya hiyo, yako wazi na hayana ugumu wowote. Lakini baadhi ya wafasiri wamedangana katika kuifasiri kwake, Mwenye Al-bahrul Muhit ametaja kauli kumi na tano.

Ajabu ni yale aliyoyasema mfasiri huyu katika Kitab kingine kwamba yeye ametaja kauli 15 katika Bahrul-muhit. Lakini hakukinaika na kitu chochote katika kauli hizo, mpaka akaota usingizini kwamba yeye anatembea kwenye njia iliyotandikwa mawe mapana akiwa na mtu mwingine akifanya naye utafiti kuhusu kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu: “Kama alivyokutoa Mola wako nyumbani kwako.”

Akamwambia: “Haujanipitia mushkeli katika Qur’an mfano wa huu.” Pengine kuna maneno yaliyokadiriwa yanayotengeneza maana ambayo hakuyaeleza mfasiri yeyote, Kisha nikamwambia yule mtu: “Nimejua sasa, kuwa yale maneno yaliyokadiriwa ni ‘Nusura yako.’

Ninachotaka kusema, sio kumdharau mfasiri huyu mkubwa; isipokuwa ninataka kutoa dalili kuwa hata ulamaa, mwenye akili, mara nyingine akili yake inafungika; mpaka akawa anafasiri Qur’an kwa ndoto, na yeye katika hali halisi yuko kwenye makosa naye hajijui, Ni ajabu, lakini ndivyo ilivyo. Dalili ya kuwa yeye yuko kwenye makosa ni kwamba lau ataona jengine, basi lile angelilipinga.

Wanajadiliana nawe katika haki baada ya kubainika.

Kundi moja la waumini walibishana katika kupigana na kikosi cha waliotoka Makka ingawaje kupigana huku ni haki na kheri. Wakaathirika na msafara wa ngamia, kwa vile ulikuwa na mali nyingi na watu wachache.

Kauli yake Mwenyezi Mungu: “Baada ya kubainika” inaashiria kwamba wao walibishana baada ya Mtume(s.a.w.w) kuwapa habari ya ushindi.

Kama kwamba wanasukumwa katika mauti na huku wanaona wazi sababu za mauti.

Hii ni Sura inayochorwa na Qur’an ya kuwogopa kwao Maquraish sana. Kwa sababu wamejiandaa kwa nguvu na wako wengi.

Utauliza : Waislamu wanawatukuza sana watu wa Badr na kuwaweka kwenye cheo cha juu; na hapa Qur’an inawadunisha waziwazi. Na kwamba wao walibishana na Mtume pamoja na kubainishiwa haki na kuwekewa wazi, kwa sababu wahyi umemshukia.

Jibu : Hili haliwagusi na wala haligusi imani yao kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Wao ni wanadamu, nafsi zao hutetema zionapo mauti japo wana imani na utulivu. Zaidi ya hivyo, hayo yalikuwa ni mawingu ya Kaskazi tu, yalifunga kisha yakaondoka. Wakaenda pamoja na Mtume wakayakabili mauti kwa azma na uthabiti.

Na alipowaahidi moja ya makundi mawili kuwa ni lenu.

Ama ushindi katika vita bila ya mali ya msafara; au mali ya msafara bila ushindi.

Nanyi mkapenda lile lisilo na nguvu ndio liwe lenu.

Lisilo na nguvu ni msafara wa mali zao, ambalo ndilo waliloathirika nalo kuliko jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Lakini Mwenyezi Mungu aliwatakia kheri wao na Uislamu kwa kuvunja ushirikina na utaghuti.

Na Mwenyezi Mungu anataka kuihakikisha haki kwa maneno yake na kuikata mizizi ya makafiri.

Makusudio ya haki hapa ni ushindi wa waislamu dhidi ya washirikina. Na makusudio ya maneno yake, kuwa ni ahadi yake kuwa mojawapo ya makundi mawili ni ya waislamu.

Maana ni kuwa: “Enyi waislamu! Nyinyi mmetaka mali inayokwisha, na Mwenyezi Mungu ametaka kuwanusuru juu ya mamwinyi wa Kiquraish, maadui wa Mweneyzi Mungu na maadui zenu; awaangamize kwa mikono yenu, aing’oe mizizi ya makafiri na ahakikishe ahadi yake kwa kuwanusuru. Basi ni nini bora katika haya? Utukufu huu, au ngamia na shehena zao?

Ili kuihakikisha haki na kuivunja batili; ijapokuwa watachukia wafanyao makosa.

Makusudio ya haki katika Aya iliyotangulia, ni ushindi wa waislamu dhidi ya washirikina. Na makusudio ya haki hapa ni Uislamu, na wenye makosa ni maadui wa Uislamu. Makusudio ya batili ni shirki.

Kuihakikisha haki na kuitangaza na kuidhihirisha kwa watu au kwa kuwanusuru watu wake, au yote mawili. Na kuivunja batili ni kwa kui- tangaza au kuwadhalilisha wabatilifu, au yote pamoja. Ufafanuzi zaidi wa tafsir ya Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu mtukufu:

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ ﴿٣٣﴾

“Yeye ndiye aliyemtuma Mtume wake kwa uongofu na dini ya haki ili ipate kushinda dini zote, ijapokuwa watachukia washirikina.” (9:33).

إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ أَنِّي مُمِدُّكُم بِأَلْفٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُرْدِفِينَ ﴿٩﴾

9. Mlipokuwa mkimwomba msaada Mola wenu. Naye akawajibu kuwa: Hakika mimi nitawasaidia kwa Malaika elfu moja wanaofuatana mfululizo.

وَمَا جَعَلَهُ اللَّـهُ إِلَّا بُشْرَىٰ وَلِتَطْمَئِنَّ بِهِ قُلُوبُكُمْ وَمَا النَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِندِ اللَّـهِ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ ﴿١٠﴾

10. Na Mwenyezi Mungu hakuyafanya haya ila ni bishara na ili nyoyo zenu zitue kwayo. Na hakuna msaada ila utokao kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye hekima.

إِذْ يُغَشِّيكُمُ النُّعَاسَ أَمَنَةً مِّنْهُ وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّنَ السَّمَاءِ مَاءً لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ وَيُذْهِبَ عَنكُمْ رِجْزَ الشَّيْطَانِ وَلِيَرْبِطَ عَلَىٰ قُلُوبِكُمْ وَيُثَبِّتَ بِهِ الْأَقْدَامَ ﴿١١﴾

11. Alipowafunika kwa usingizi uliokuwa amani itokayo kwake, na akawateremshia maji kutoka mawinguni ili awatwaharishe kwayo, na kuwaondolea uchafu wa shetani na kuzikazanisha nyoyo zenu na kuimarisha nyayo zenu kwayo.

إِذْ يُوحِي رَبُّكَ إِلَى الْمَلَائِكَةِ أَنِّي مَعَكُمْ فَثَبِّتُوا الَّذِينَ آمَنُوا سَأُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُوا الرُّعْبَ فَاضْرِبُوا فَوْقَ الْأَعْنَاقِ وَاضْرِبُوا مِنْهُمْ كُلَّ بَنَانٍ ﴿١٢﴾

12. Mola wako alipowapa wahyi Malaika: Hakika mimi niko pamoja nanyi, basi watieni nguvu wale walioamini; nitatia woga katika nyoyo za makafiri, basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole.

ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ شَاقُّوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَمَن يُشَاقِقِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿١٣﴾

13. Hayo ni kwa kuwa wamemwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

ذَٰلِكُمْ فَذُوقُوهُ وَأَنَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابَ النَّارِ ﴿١٤﴾

14. Ndiyo hivyo! Basi onjeni! Na hakika makafiri wana adhabu ya moto.

MLIPOKUWA MKIMWOMBA MSAADA MOLA WENU

Aya 9 – 14

MAANA

Mlipokuwa mkimwomba msaada Mola wenu, Naye akawajibu kuwa: Hakika mimi nitawasaidia kwa Malaika elfu moja wanaofuatana mfululizo.

Waislamu walipohakikisha kwamba kupigana na adui mwenye nguvu na idadi kubwa ya wapiganaji, kutakuwa tu, basi walikimbilia kwa Mwenyezi Mungu wakitaka kuokoka na ugumu huu. Naye Mwenyezi Mungu alipoona ukweli wa nia na azma yao, aliwapa habari kupitia kwa Mtume wake(s.a.w.w) , kwamba yeye amewatikia dua yao kwa Malaika elfu moja wanaofuatana.

Utauliza : hapa Mwenyezi Mungu amesema: Nitawasaidia kwa Malaika elfu moja wanaofuatana, mahali pengine akasema: “Je, haiwatoshi kuwasaidia Mola wenu kwa Malaika elfu tatu wenye kuteremshwa?”

Tena akasema: “Atawasaidia Mola wenu kwa Malaika elfu tano wenye alama” Juz.4 (3:124-125).

Jibu la swali hili tumelijibu huko Juz,4 (3:124-125).

Na Mwenyezi Mungu hakuyafanya haya ila ni bishara na ili nyoyo zenu zitue kwayo. Na hakuna msaada ila utokao kwa Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu mwenye hakima.

Mwenyezi Mungu anasema lengo la msaada huu ni kutua nyoyo zenu na mvumilie katika kupigana na adui sio, kutegemea Malaika. Bali ni juu yenu kumaliza juhudi zenu zote. Ama ushindi hauwi wala hautakuwa ila kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, si kwa juhudi zenu na wala kwa msaada wa Malaika. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz.4. (3:126).

Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t.) akataja njia sita za neema yake kwa Waislamu:

1.Alipowafunika usingizi uliokuwa amani itokayo kwake.

Waislamu waliwahofia Washirikina kwa wingi wao, Mwenyezi Mungu akaipoza hofu yao kwa usingizi; Hawakuamka ila nafsi zao zimejawa na uutulivu.

Sote tunajua, kwa majaribio, kwamba usingizi unapunguza sehemu ya huzuni na hofu. Imam Ali(a.s) anasema:“Ni kuvunja kulikoje kwa usingizi, kwa tatizo la siku.” Yaani mtu anaweza kufikiria tatizo fulani akilala, mpaka atakapoamka hulikuta limetatuka.

2.Na akawateremshia maji kutoka mawinguni ili awatwaharishe kwayo.

Baada ya waislamu kupumzika kwa usingizi walijikuta wana haja ya maji; Kwa sababu walikuwa hawajafika Badr wakati huo. Ndipo Mwenyezi Mungu akawateremshia mvua, wakanywa na wakajisafisha. Hii ni neema ya pili baada ya usingizi.

3.Na kuwaondolea uchafu wa shetani.

Shetani alikuwa akiwatia wasiwasi waislamu na kuwahofisha na washirikina. Mwenyezi Mungu akawaondolea hofu hii, ambayo ameiita uchafu wa shetani, kwa usingizi na kusaidiwa na Malaika.

4.Na kuzikazanisha nyoyo zenu kwa kuondoa hofu na fazaa.

5.Na kuimarisha nyayo zenu kwayo.

Wafasiri wengi wanasema kuwa dhamir ya kwayo inarudi kwenye maji, na nyayo ni miguu. Kwamba waislamu walikuwa katika tifu tifu, miguu yao haina uimara, mvua iliponyesha mchanga ukashikana na miguu ya waislamu ikawa imara.

Hayo ndiyo yalioelezwa katika tafsir nyingi, Ama sisi tunaona kuwa dhamir ya kwayo inarudia kwenye kukazana nyoyo, Kwamba makusudio ya kuimarika nyayo ni uimara katika uwanja wa vita, na kuacha kukimbia. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amewapa uimara katika uwanja wa vita kama alivyowapa utulivu na uimara wa moyo.

6.Mola wako alipowapa wahyi Malaika: Hakika mimi niko pamoja nanyi, basi watieni nguvu wale walioamini; nitatia woga katika nyoyo za makafiri.

Msemo katika ‘Mola wako’ unaelekezwa kwa Mtume Muhammad(s.a.w.w) na katika ‘pamoja nanyi’ na ‘watieni nguvu’ ni kwa Malaika. Hiyo ni kwa kuangalia dhahir ya mfumo wa maneno.

Utauliza : Malaika walishiriki kinamna gani katika kuwasaidia waislamu siku ya Badr? Je, ilikuwa ni kwa kupiga na kuua au ni kwa kushajiisha; kwamba wao walikuwa wanakwenda mbele ya safu kwa sura za watu wanaopigana na wala hawapigani, isipokuwa kuwaambia waislamu: Furahini, hakika Mwenyezi Mungu atawanusuru; kama walivyosema baadhi ya wafasiri?

Jibu : Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaamrisha Malaika kuwapa uimara waumini. Hakuna mwenye shaka kwamba wao walifanya, kwa sababu wao wanafanya yale wanayoamrishwa, Vilevile hakuna mwenye shaka kwamba washirikina waliwaogopa waislamu.

Kwa sababu Mwenyezi Mungu aliwaahidi na ahadi yake ni kweli na kwamba waumini wali- washinda washirikina.

Haya ndiyo yanayofahamishwa na dhahiri ya Aya. Ama ufafanuzi na vipi walivyofanya, hayo ni katika mambo ya ghaibu yaliyonyamaziwa na wahyi. Na sisi ni bora kuyanyamazia.

Kunyamaza kwa wahyi ni dalili mkataa kwamba kuamini ufafanuzi si chochote katika itikadi, vinginevyo ingelikuwa wajibu kubainisha.

Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kwenye kila ncha za vidole.

Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa msemo ‘Pigeni’ unaelekezwa kwa Malaika, Wengine wakasema wanaambiwa waislamu, Kisha wakatofautiana katika makusudio ya juu ya shingo.

Kuna waliosema makusudio ni shingo zenyewe na kwamba maana ya juu ni kwenye; na wengine wakasema ni vichwa. La kushangaza ni kauli ya baadhi ya masufi kwamba makusudio ni nafsi chafu.

Tuonavyoona sisi ni kwamba maneno hayo wanaambiwa waislamu, kwa sababu ndio waliokusudiwa kupigana. Na kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Juu ya shingo na kila ncha ya vidole’ ni fumbo la kuwahimiza waislamu kukazana kuwaua; wasiwape nafasi ila wawapige kiungo chochote katika viungo vyao.

Aya hii inafanana na Aya isemayo:

وَلَا تَأْخُذْكُم بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ﴿٢﴾

“Wala isiwashike huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho” (24:2).

Hayo ni kwa kuwa wamemwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

Hayo ni ishara ya ulazima wa kuwatumilia ukali washirikina, kwa vile wao wamekuwa katika msimamo wa upinzani na uhalifu.

Ndiyo hivyo! Basi onjeni! Na hakika makafiri wana adhabu ya moto mbali na yale yaliyowapata duniani, miongoni mwa kuuawa, kutekwa na kushindwa, na hayo si chochote kulinganisha na moto mkubwa.


11

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا زَحْفًا فَلَا تُوَلُّوهُمُ الْأَدْبَارَ ﴿١٥﴾

15. Enyi mlioamini! Mnapokutana vitani na wale waliokufuru, basi msiwageuzie migongo.

وَمَن يُوَلِّهِمْ يَوْمَئِذٍ دُبُرَهُ إِلَّا مُتَحَرِّفًا لِّقِتَالٍ أَوْ مُتَحَيِّزًا إِلَىٰ فِئَةٍ فَقَدْ بَاءَ بِغَضَبٍ مِّنَ اللَّـهِ وَمَأْوَاهُ جَهَنَّمُ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿١٦﴾

16. Na atakayewageuzia mgongo wake siku hiyo – isipokuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi - hakika amestahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu; na makazi yake ni Jahannam, napo ni mwishilio muovu.

فَلَمْ تَقْتُلُوهُمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ قَتَلَهُمْ وَمَا رَمَيْتَ إِذْ رَمَيْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ رَمَىٰ وَلِيُبْلِيَ الْمُؤْمِنِينَ مِنْهُ بَلَاءً حَسَنًا إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿١٧﴾

17. Hamkuwaua nyinyi, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaua, Na hukutupa wewe ulipotupa, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyetupa, Ili awajaribu waumini majaribu mazuri, Hakika Mweyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.

ذَٰلِكُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ مُوهِنُ كَيْدِ الْكَافِرِينَ ﴿١٨﴾

18. Ndiyo hivyo! Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye adhoofishaye vitimbi vyamakafiri.

إِن تَسْتَفْتِحُوا فَقَدْ جَاءَكُمُ الْفَتْحُ وَإِن تَنتَهُوا فَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ وَإِن تَعُودُوا نَعُدْ وَلَن تُغْنِيَ عَنكُمْ فِئَتُكُمْ شَيْئًا وَلَوْ كَثُرَتْ وَأَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿١٩﴾

19. Kama mnataka ushindi, basi ushindi umekwishawajia, na kama mkiacha, basi itakuwa kheri kwenu; na kama mtarudia sisi pia tutarudia; na jeshi lenu halitawafaa chochote hata likiwa kubwa. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na waumini.

KUKIMBIA VITA

Aya 15 – 19

MAANA

Enyi mlioamini! Mnapokutana vitani na wale waliokufuru, basi msi- wageuzie migongo.

Yametangulia maelezo kuwa washirikina walitoka Makka kuja kupambana na waislamu. Aya hii ni katika mafunzo ya vita, Inamaanisha waislamu wawe imara kumkabili adui wala wasikimbie wanapokutana vitani. Kwa sababu kukimbia ni unyonge katika dini na udhalili kwa waislamu.

Na atayewageuzia mgongo wake siku hiyo - isipokuwa kwa mbinu za vita au kuungana na kikosi - hakika amestahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu; na kimbilio lake ni Jahannam, napo ni mwisho muovu.

Mbinu za vita, ni kama kuacha mahali pake na kwenda mahali pazuri zaidi. Na kuungana na kikosi, ni kuungana na kikosi kingine kinachomhitajia au anachokihitajia.

Maana ni kuwa: Enyi waislamu! Mjizatiti na adui yenu katika vita wala msimkimbie ila ikiwa ni kuchagua sehemu nzuri au kupanga mpango mzuri kwa kuungana; na kwamba mwenye kukimbia adui bila ya sababu za msingi basi amestahiki ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na marejeo yake ni Jahannam.

Mafakihi wametoa fatwa kuwa ni haramu kukimbia vita ila ikiwa idadi ya jeshi la adui ni kubwa kuliko jeshi la waislamu.

Tuanavyo sisi ni kuwa mafakihi hawawezi kuwa na fatwa hapa ya wajibu wa kubaki au kujuzu kukimbia; isipokuwa amri katika hilo ni lazima aachiwe kamanda mwaminifu mwenye majukumu ya vita na wala sio mafakihi. Kwa hiyo ni wajibu yeye aachiwe kupanga wajibu wa kubaki au kukimbia.

Anaweza akaonelea kuwa wabakie licha ya kuzidi idadi ya adui mara tatu zaidi, na anaweza akaona lazima wakimbie na kujiondoa vitani hata kama idadi ya waislamu ni maradufu ya maradufu. Kwa sababu kubaki ni tendo la kujiua. Na, katika hali zote ni wajibu kuchukua kauli yake sio kauli ya mafakihi wanayofutu wenyewe wakiwa wamelalia mito.

Zaidi ya hayo ni kwamba kauli ya mafakihi imepitwa na wakati, ambapo nguvu zilikuwa zikipimwa na idadi sio kwa aina, na kwa idadi ya jeshi sio kwa maandalizi yake ya silaha za kisasa.

Hamkuwaua nyinyi, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaua.

Waislamu waliwashinda washirikina Badr; wakawauwa na kuwateka. Sababu ya ushindi huu ni uimara wa waislamu na uvumilivu. Ama sababu ya uimara huu na uvumilivu ni ile iliyoashiriwa na Aya iliyotangulia kuwa Mwenyezi Mungu alizikazanisha nyoyo za waislamu, akaimarisha nyayo zao, akawasaidia kwa Malaika na akaondoa hofu katika nyoyo zao na kuitia katika nyoyo za washirikina.

Kwa hali hiyo inafaa kunasibisha kwa waislamu kuuwa washirikina, kwa sababu ilikuwa ni kwa mikono yao na ni kwa sababu ya uimara na subira yao. Vilevile itafaa kunasibisha kwa Mwenyezi Mungu mtukufu kwa sababu yeye ndiye aliyewaandalia uimara na subira hiyo, Zaidi ya hayo yeye ndiye sababu ya sababu zote.

Imesimuliwa kwamba baadhi ya waislamu walisema siku ya Badr: “Mimi nimemuuwa fulani”, mwengine naye akasema, Ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha kauli yake hiyo.

Na hukutupa wewe ulipotupa, lakini Mwenyezi Mungu ndiye aliyetupa.

Ndio Mwenyezi Mungu ndiye aliyetupa, lakini yeye alichagua kiganja cha kutupa cha Nabii Muhammad(s.a.w.w) ambaye amemfadhilisha juu ya viumbe vyote; akamhusisha na ujumbe wake ambao rehma yake imewaenea walimwengu wote.

Imepokewa kuwa Mtume alichukua gao la changarawe au mchanga, akawatupia washirikina, akasema: “Na zihizike nyuso”, hilo likafuatiwa na kushindwa kwao. Sio mbali kuwa riwaya hii ni sahih. Vilevile sio mbali kuwa makusudio ya kutupa ni kupanga mambo.

Vyovyote itakavyokuwa ni kwamba matakwa ya Mwenyezi Mungu ndiyo sababu ya sababu. Kwani sababu yoyote ya tukio lolote iwe ya moja kwa moja au si ya moja kwa moja, basi itaishia kwenye nguvu kuu iliyopatikana bila ya mpatishaji. Vinginevyo basi neno kupatikana lisingekuwa na maana.

Ili awajaribu waumini majaribu mazuri.

Majaribu (mtihani) yanaweza kuwa ya neema ili kudhihirisha shukrani na yanaweza kuwa ni misukosuko ili kudhihirisha uvumilivu. Pia maana yake yanakuwa ni kupewa, Hayo ndio maana yaliyokusudiwa katika Aya hii.

Ama makusudio ya mazur ni ushindi na ngawira; yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaamrisha waislamu kuwa imara, wavumilivu na kuacha kukimbia vita; na akawaandalia wao njia ya hilo, ili awatimizie neema yake ya ushindi na ngawira.

Hakika Mweyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.

Amesikia maombi ya msaada na akawaitikia, kwa vile alijua usafi wao wa nia na usahihi wa azma.

Ndiyo hivyo! Na hakika Mwenyezi Mungu ndiye adhoofishaye hila za Makafiri.

Hakuna neema kubwa na adhimu kuliko kudhoofishwa adui na kubatilishwa hila zake.

Kama mnataka ushindi, basi ushindi umekwishawajia, na kama mkiacha, basi itakuwa kheri kwenu; na kama mtarudia sisi pia tutarudia; na jeshi lenu halitawafa chochote hata likiwa kubwa. Na kwa hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na waumini.

Maneno yote wanaambiwa washirikina kwa kuangalia mfumo wa maneno na kutimia maana.

Imepokewa kuwa Washirikina walipotoka Makka kuelekea Badr waliishika nguo inayofunika Al-Kaaba, wakamtaka nusura ya ushindi Mwenyezi Mungu, wakasema: “Ewe Mwenyezi Mungu lipe ushindi jeshi lililo juu na lililo tukufu kati ya majeshi mawili.”

Ndipo Mwenyezi Mungu akawajibu: Kama mnataka ushindi; yaani mkitaka ushindi kwa jeshi lililo juu na lililo na uongofu basi amekwisha lipa ushindi. Na kama mkiacha kupigana na waislamu na kumpinga Mwenyezi Mungu na Mtume, basi itakuwa ni bora kwenu baada ya kuonja kipigo cha kuuawa na kutekwa. Na kama mkirudia vita yatawafika tena yale yaliyowafika mwanzo.

Ama wingi ambao mnajitukuza nao, mmeuona haufai kitu, hauwazuilii kuuliwa, kutekwa na kushindwa. Kwani Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kutoa ushindi, naye yuko pamoja na waumini.

Ikiwa mnataka ushindi wa kweli basi acheni shirk na mumuami Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَوَلَّوْا عَنْهُ وَأَنتُمْ تَسْمَعُونَ ﴿٢٠﴾

20. Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msijiepushe naye hali mnasikia.

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ قَالُوا سَمِعْنَا وَهُمْ لَا يَسْمَعُونَ ﴿٢١﴾

21. Wala msiwe kama wale wanaosema: Tumesikia; na kumbe hawasikii.

إِنَّ شَرَّ الدَّوَابِّ عِندَ اللَّـهِ الصُّمُّ الْبُكْمُ الَّذِينَ لَا يَعْقِلُونَ ﴿٢٢﴾

22. Hakika wanyama waovu mbele ya Mwenyezi Mungu ni viziwi, mabubu ambao hawatumii akili.

وَلَوْ عَلِمَ اللَّـهُ فِيهِمْ خَيْرًا لَّأَسْمَعَهُمْ وَلَوْ أَسْمَعَهُمْ لَتَوَلَّوا وَّهُم مُّعْرِضُونَ ﴿٢٣﴾

23. Na kama Mwenyezi Mungu angelijua wema wowote kwao angeliwasikilizisha;na kama angeliwasikilizisha, wangeligeuka wakipuuza.

KUMTII MWENYEZI MUNGU NA MTUME

Aya 20 – 23

MAANA

Enyi mlioamini! Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wala msi- jiepushe naye hali mnasikia.

Mwito huu umekuja baada ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na kwa hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na waumin.” Lengo lake ni kumuelezea Mumini ambaye atapewa ushindi na Mwenyezi Mungu na atakayekuwa naye Mwenyezi Mungu popote alipo.

Huyo ni yule ambaye anamtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake katika wanayomwamrisha na wanayomkataza na kwamba mwenye kumhalifu na kuasi; basi amestahiki adhabu na hizaya kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Wala msiwe kama wale wanaosema: Tumesikia; na kumbe hawasikii.

Mara nyingi kusikia kutumiwa kwa maana ya kukubali; kama vile mtu kusema: Mimi sikuzikilizi; yaani sikukubalii. Au kama vile kusema: Wenye kusikia sana uwongo; yaani wenye kuukubali

Haya ndiyo maana yaliyokusudiwa katika Aya hii, Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawakataza waumini kuwa kama wanafiki wakidhihirisha kumkubalia Mtume na kutii amri yake na huku wakificha uhalifu na uasi.

Hakika wanyama waovu mbele ya Mwenyezi Mungu ni viziwi, mabubu ambao hawatumii akili.

Kiziwi hasikii na bubu hasemi. Wanyama wana masikio ya kusikia, lakini hawafahamu maneno wanayoyasikia na wana ndimi lakini hawasemi, Kwa hiyo hawafahamu wala hawafahamiwi.

Mwenye kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu na Mtume kisha asiongoke kwayo, basi mfano wake ni kama mfano wa mnyama kiziwi aliye bubu, husikia maneno, lakini hanufaiki nayo.

MWENYE KUTAFUTA HAKI NA MWENYE KUTAFUTA WINDO

Na kama Mwenyezi Mungu angelijua wema wowote kwao angeliwasikilizisha; na kama angeliwasikilizisha wangeligeuka wakipuuza.

Watu ni aina mbili:

1. Ni yule mwenye kuitafuta akiwa hana lengo lolote. Huyu hawezi kuamini msingi wala kuona rai yoyote ila baada ya utafiti na kutilia manani dalili kisha hujenga rai yake juu ya dalili hizo.

2. Ni mwenye kutafuta windo fulani. Haamini isipokuwa dhati yake na maslahi yake. Hukaribisha yale yanayoafikiana na maslahi yake, hata kama ni batili na hukataa yale yanayopingana nayo, hata kama ni haki.

Mwenyezi Mungu huwasikilizisha mwito wa haki wote wawili kwa njia ya sawa sawa, kuweka hoja. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu:

وَمَا كُنَّا مُعَذِّبِينَ حَتَّىٰ نَبْعَثَ رَسُولًا ﴿١٥﴾

Na hatukuwa ni wenye kuadhibu mpaka tumpeleke Mtume. (17:15).

Baada ya ubainifu unaotumiza hoja kwa wote, Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anazidisha nasaha na mwongozo kwa wale wanaoitikia na kunufaika nao

وَالَّذِينَ اهْتَدَوْا زَادَهُمْ هُدًى وَآتَاهُمْ تَقْوَاهُمْ ﴿١٧﴾

“Na wale wanaokubali kuongoka huwazidishia uongofu.” (47:17).

Ama wale ambao hawaitikii isipokuwa manufaa yao ya kidhati, basi Mwenyezi Mungu huachana nao, maadamu nasiha haziwafai chochote. Haya ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na kama angejua wema wowote angeliwasikilizisha.”

Hilo linafahamika kutokana na kauli yake moja kwa moja bila ya kuingia kati kitu kingine: “Na kama angewasikilizisha wangeligeuka wakipuuza.” Yaani lau angeliwasikilizisha haki, wangeliachana nayo, kwani haikubaliani na hawaa zao.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ يَحُولُ بَيْنَ الْمَرْءِ وَقَلْبِهِ وَأَنَّهُ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ ﴿٢٤﴾

24. Enyi mlioamini! Mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapowaita kwenye lile litakalowapa uhai. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake, na kwamba mtakusanywa kwake.

DINI NA MAISHA

Aya 24

MAANA

Mwenye kuujua vilivyo Uislamu atakuta kila asili ya itikadi yake na kila tawi la sharia yake inasimamia kwa uwazi au kuwa na madhumuni ya kufanya kazi kwa ajili ya uhai (maisha).

Kumwamini Mungu ni imani iliyo na mwito wa kujikomboa na utumwa, isipokuwa kwa Mwenyezi Mungu mmoja peke yake, na kwamba hakuna utawala kwa sababu ya mali wala jaha au jinsi au kitu chochote kile isipokuwa kwa haki na uadilifu.

Kimsingi ni kwamba maisha mema yenye nguvu hayapatikani na ni muhali kupatikana ila kwa kushikamana na msingi huu na kuufuatilia.

Ama kuamini Utume wa Muhammad(s.a.w.w) kwenyewe ni kuamini sharia ya udugu na usawa, uhuru wa mtu na himaya yake na kila msingi ambao unampa binadamu kheri njema. Hilo ni kwa vile utume wa Muhammad unalenga kwenye uongofu wa mtu na wema wake na kueneza uadilifu baina ya watu.

Kuamini siku ya mwisho ni kuamini kuwa mtu hataachwa bure na kwamba yeye ataulizwa kila dogo na kubwa katika amali zake. Atahisabiwa na kulipwa; ikiwa ni kheri basi atalipwa kheri, na ikiwa ni shari basi atalipwa shari. Imani hii, kama unavyoona, inafanana na serikali kuu, au mhimizaji wa matendo yanayowajibisha kumwamini Mwenyezi Mungu na Mtume.

Hayo ni katika yale yanayohusiana na misingi ya itikadi. Ama matawi ya dini, yaani yale yanayofaa kufanywa na yasiyofaa katika sharia ya kiislamu, huwa yanasimamia misingi ya binadamu, iliyoashiriwa na kauli yake Imam Jafar As-Sadiq(a.s) :“Kila lililo na masilahi kwa watu kwa upande fulani basi linajuzu, na kila lililo na ufisadi kwa upande fulani basi halijuzu.

Huu ndio mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume ulioelezwa na Qur’an waziwazi:

Mwitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapowaita kwenye lile litakalowapa uhai.

Tukiinganisha Aya hii na ile isemayo:

قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْكَافِرِينَ ﴿٣٢﴾

“Sema mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume. Na kama wakikata, basi hakika Mwenyezi Mungu hawapendi Makafiri” Juz.3 (3:32),

Tutapata picha hii ya makisio ya kimantiki kuwa: Mungu na Mtume wametoa mwito kwa ajili ya maisha na akahukumu ukafiri wa kila anayepinga mwito huu. Kwa hiyo natija ni kuwa asiyetenda kwa ajili ya maisha basi ni kafiri[2] .

Kwa hali hiyo basi inatubainikia kuwa Uislamu unakwenda sambamba na maisha, na kwamba kila ambalo liko mbali na maisha basi si Uislamu chochote.

Kila mtu, vyovyote awavyo, akilingania kwenye maisha yasiyokuwa na unyanyasaji, dhulma au matatizo, basi mwito wake huo unakutana na mwito wa Mwenyezi Mungu na Mtume, apende asipende.

Na yule anayeikingamia njia ya maisha na maendeleo yake, basi huyo ni adui wa Mwenyezi Mungu na Mtume, hata akiswali usiku na kufunga mchana.

Ama vikundi vilivyojitokeza siku hizi ambavyo vimeiuza dini yake kwa uzayuni na ukoloni, huku vikijificha kwa jina la dini, tumevielezea kaatika Juz. 4 (3:142).

Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake na kwamba mtakusanywa kwake.

Moyo ndio mahali pa imani, ukafiri, ikhlas na unafiki. Pia ni mahali pa pendo na chuki. Kwenye moyo hutokea matendo mema na mbaya, Lau si moyo mtu asingekuwa mtu.

Inatosha kuwa moyo ni kitu kikubwa, kauli yake Mwenyezi Mungu katika Hadith Qudsi: “Haikunipanua ardhi yangu wala mbingu yangu, lakini umenipanua moyo wa mja wangu muu’min.” Hakuna mwenye shaka kwamba kinachompanua aliyeshindwa kupanuliwa na mbingu na ardhi, kuwa ni kikubwa zaidi ya ardhi na mbingu.

Utauliza : vipi kiungo hiki kidogo kiweze kupanua aliyeshindikana na ardhi na mbingu? Tena, kwa nini Mwenyezi Mungu mtukufu amehusisha moyo wa Mumini na wala sio wa kafiri?

Jibu : Makusudio ya upana katika Hadith Qudsi hii, sio upana wa mahali. Kwa sababu Mwenyezi Mungu hana mahali isipokuwa makusudio ni kumfahamu Mwenyezi Mungu, na kwamba moyo wa mumini unamfahamu Mwenyezi Mungu mtukufu kwa namna isiyoweza mbingu na ardhi kufahamu.

Vilevile moyo wa kafiri, haufahamu chochote kuhusu Mwenyezi Mungu, kwa vile uko katika kifuniko cha upotevu na ufisadi. Mwenyezi Mungu mtukufu, anasema:

وَقَالُوا قُلُوبُنَا فِي أَكِنَّةٍ مِّمَّا تَدْعُونَا إِلَيْهِ وَفِي آذَانِنَا وَقْرٌ وَمِن بَيْنِنَا وَبَيْنِكَ حِجَابٌ ﴿٥﴾

“Na wakasema: Nyoyo zetu ziko katika vifuniko kwa yale unayotulingania, na katika masikio yetu mna uzito, na baina yetu na baina yako kuna pazia” (41:5).

Kwa hivyo basi inatubainikia kuwa makusudio ya mtu ambaye Mwenyezi Mungu huingia kati yake na moyo wake, ni yule ambaye amepofushwa na hawaa zake na upotevu. Hivyo Aya hii inakuwa na maana ya Aya isemayo: “Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao; na juu ya macho yao pana kifuniko,”

Yaani hawanufaiki kwa nyoyo zao kwa sababu ya kutu za upotevu zilizo juu yake, mpaka ikawa kama kwamba Mwenyezi Mungu amepiga sili au amekaa kati yake na mwenye moyo huo.

Hivyo anakuwa kunasibisha muhuri na kuzuia kwake Mwenyezi Mungu mtukufu ni kimajazi sio kihakika.

Kundi la wafasirii wamesema kuwa maana ya kuingia kati ya mtu na moyo wake ni kwamba moyo unashikwa na Mwenyezi Mungu akiugeuza vile anavyotaka, hubadilisha ukumbusho ukawa usahaulivu na usahaulivu ukawa ukumbusho, hofu kuwa amani na amani kuwa hofu. Lakini tafsiri zote hizo ni za kudhania tu.


12

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA

وَاتَّقُوا فِتْنَةً لَّا تُصِيبَنَّ الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنكُمْ خَاصَّةً وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٢٥﴾

25. Na jikingeni na fitna ambayo haitawasibu wale waliodhulumu miongoni mwenu peke yao, na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

وَاذْكُرُوا إِذْ أَنتُمْ قَلِيلٌ مُّسْتَضْعَفُونَ فِي الْأَرْضِ تَخَافُونَ أَن يَتَخَطَّفَكُمُ النَّاسُ فَآوَاكُمْ وَأَيَّدَكُم بِنَصْرِهِ وَرَزَقَكُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٢٦﴾

26. Nakumbukeni mlipokuwa wachache, mkionekana wadhaifu katika nchi; mkawa mnaogopa watu wasiwanyakue; akawapa makao na akawatia nguvu kwa nusura yake na akawapa riziki njema ili mpate kushukuru.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَخُونُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ وَتَخُونُوا أَمَانَاتِكُمْ وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٢٧﴾

27. Enyi mlioamini! Msimfanyie hiyana Mwenyezi Mungu na Mtume na mkahini amana zenu na hali mnajua.

وَاعْلَمُوا أَنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ وَأَنَّ اللَّـهَ عِندَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ ﴿٢٨﴾

28. Na jueni kwamba mali zenu na watoto wenu ni fitna. Na hakika kwa Mwenyezi Mungu yako malipo makubwa.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَتَّقُوا اللَّـهَ يَجْعَل لَّكُمْ فُرْقَانًا وَيُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ وَاللَّـهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ ﴿٢٩﴾

29. Enyi mlioamini! Mkimcha Mwenyezi Mungu atawajaalia upaambanuzi, na atawafutia makosa yenu na atawasamehe; na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kuu.

OGOPENI ADHABU

Aya 25 – 29

LUGHA

Neno Fitna lina maana nyingi, miongoni mwa maana hizo ni adhabu ambayo ndiyo makusudio yake katika Aya hii ya 25. Ama katika Aya 28, makusudio yake ni mapenzi na hawaa zinazozuia haki. Makusudio ya upambanuzi ni mwongozo.

MAANA

Na jikingeni na fitna ambayo haitawasibu wale waliodhulumu mion- goni mwenu peke yao, na jueni kuwa Mwenyezi Mungu ni mkali wa kuadhibu.

Ni tahadhari inayotoka kwake Mwenyezi Mungu mtukufu kwa kila mfitini anayeharibu nchi; hasa wale wanaoeneza farakano na kuvuruga amani na kuwachokoza wanyonge. Hadhari ni kwamba ubaya wa adhabu hautaishia kwa madhalimu tu, bali utaenea katika jamii yote na kumwenea mwema na mwovu.

Imeelezwa katika Tafsir Tabari akimnukuu Sadiy, ambaye ni mfasiri mkubwa, kwamba Aya hii inafungamana na watu wa (Vita vya Jamal) ngamia ambao walimpiga vita Ali bin Abu Talib.

Ametaja Razi katika kufasiri Aya hii: “Zubeir siku moja alikuwa akibarizi na Mtume(s.a.w.w) mara akatokea Ali (r.a), Zubeir akamcheka. Mtume wa Mwenyezi Mungu akamwambia: “Vipi unavyompenda Ali?” Akajibu “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ninapenda kama ninavyompenda mwanangu au zaidi. Mtume akamwambia:‘’Utakuwaje ukienda kupigana naye?

Vilevile imeelezwa katika Tafsiru Tabari: “Zubeir bin Al-a’wam alisema: “Tumesoma Aya hii zama zilizopita, lakini hatukuwaona wanaohusika nayo, mara sisi ndio tunahusika nayo”.

Na kumbukeni mlipokuwa wachache, mkionekana wadhaifu katika nchi; mkawa mnaogopa watu wasiwanyakue; akawapa makao na akawatia nguvu kwa nusura yake na akawapa riziki njema ili mpate kushukuru.

Maneno wanaambiwa Maswahaba wa Mtume(s.a.w.w) . Mwenyezi Mungu mtukufu anawakumbusha udhaifu na hofu waliyokuwa nayo kabla ya Uislamu. Vilevile udhalili na ufukara, na jinsi alivyowapa amani utajiri na utukufu baada ya Uislamu, kwa vile wao wameitikia mwito wa maisha waliyopewa na Mwenyezi Mungu na Mtume wake.

Lengo la ukumbusho huu ni kuwa waendelee na utiifu na kuitikia mwito wa uhai, ili waishi wakiwa wenye nguvu na heshima. Na kwamba wao pindi tu wakikengeuka na kuasi watarudia unyonge na udhalili waliokuwa nao wenzao, kama ilivyo hali ya waislamu leo, hasa waarabu.

Enyi mlioamini! Msimfanyie hiyana Mwenyezi Mungu na Mtume.

Kumfanyia hiyana Mwenyezi Mungu sio kuacha kufunga na kuswali tu; isipokuwa hiyana kubwa ni kuufanyia hiyana umma na nchi, kwa kuwatawalisha mataghuti kwenye sehemu za uongozi wakatawala nchi na huku tunawavumilia na kuwanyamazia bila ya kuwapiga vita.

Na mkahini amana zenu.

Yaani wala msihini amana zenu, Wafasiri wengi wamesema kuwa ukatazo huu ni wa hiyana ya amana ya mangiliano ya kimali baina ya watu. Hakuna mwenye shaka kwamba kurudisha amana ni wajibu na kuifanyia hiyana ni haramu, lakini hiyana kubwa ni kuacha kusaidiana na wanyonge kurudisha haki zao kutoka kwa wenye nguvu walio madhalimu.

Na hali mnajua.

Hakuna mjeuri zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko yule anayemuasi Mwenyezi Mungu kwa makusudi hali anajua.

Jueni kwamba mali zenu na watoto wenu ni fitna.

Imekuja Aya hii baada ya makatazo ya hiyana ili kumzindua Mumini kwamba haitakikani mali na watoto wamzuie kutekeleza wajibu wake kwa umma na nchi mbele ya Mungu. Makusudio ya fitna hapa ni mapenzi yanayozuia haki na kheri.

Imepokewa Hadith kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) amesema: “Mtoto ni tunda la moyo. Na yeye ni mahali pa woga, ubahili na huzuni” Sawa na mali ambayo ni matunda ya jasho na mkono.

Ni woga kwa sababu, mwenye nayo huhofia kusema haki na kufanya kwa kuihofia; kama ambavyo anahofia juu ya mtoto wake.

Ni ubahili, kwa sababu mwenye kuimiliki anakuwa na pupa nayo na uchoyo; kama anavyokuwa na pupa na mtoto wake.

Nayo ni huzuni kwa sababu mwenye kuikusanya huhuzunika ikipatwa na jambo; kama anavyohuzunika likipatwa na jambo tunda la moyo wake.

Maneno mazuri niliyosoma kuhusu maudhui haya ni shairi la bedui mmoja akisema:

• Alikuwa fukara

• Akatajirika akapenda mali uchu ukamshika

• Akitaka kutumia huhuzunika

Na hakika kwa Mwenyezi Mungu yako malipo makubwa.

Mwenye akili hupendelea malipo haya na kuyahangaikia kwa juhudi na amali njema; wala haathiriki na mali inayokwisha na mtoto asiyebakia.

Enyi mlioamini! Mkimcha Mwenyezi Mungu atawajalia upaambanuzi.

Mara nyingi sana mtu anakuwa mateka wa matamanio. Humgeuzia zuri likawa baya na baya likawa zuri. Mara nyingi hilo huwa katika mambo yanayohusiana na mali na watoto ambapo matamanio hufikia kilele chake.

Kwa ajili hii ameamrisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) takuwa baada ya kuhadharisha fitna ya mali na watoto. Ama upambanzi, yaani mwongozo, anaowapa Mwenyezi Mungu wenye kumcha ili wapambanue haki na batili, ni natija ya kujikomboa na hawa na matamanio.

Kwa sababu, matamanio hupofusha na hutia uziwi.

Kunasibisha mwongozo kwa Mwenyezi Mungu ni kuwa yeye ndiye aliyeuwekea dalili. Mwenye kuzichunguza vizuri, akiwa hana malengo mengine yoyote isipokuwa kutafuta mwongozo wa haki, basi ataifikia tu.

Na atawafutia makosa yenu na atawasamehe; na Mwenyezi Mungu ni mwenye fadhila kuu.

Wafasiri wanasema kuwa makusudio ya kufutiwa makosa ni kusitiriwa duniani; na kusamehewa ni kusamehewa akhera, Wamesema hivi kukimbia kukaririka.

Ama sisi hatukimbii kukarika Qur’an na tumebainisha njia yake katika Juz.1 Maana ya Aya yote ni kuwa mwenye kumcha Mwenyezi Mungu atampa mwongozo, msamaha na thawabu.

Hilo kwa Mwenyezi Mungu si kubwa. Kwa sababu ni mkuu wa fadhila na kutoa kwake ni sahali kunamfikia kila mwenye kutafuta na kutaka radhi zake.

وَإِذْ يَمْكُرُ بِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِيُثْبِتُوكَ أَوْ يَقْتُلُوكَ أَوْ يُخْرِجُوكَ وَيَمْكُرُونَ وَيَمْكُرُ اللَّـهُ وَاللَّـهُ خَيْرُ الْمَاكِرِينَ ﴿٣٠﴾

30. Na walipokupangia njama wale waliokufuru ili wakufunge au wakuue au wakutoe. Na wakapanga njama na Mwenyezi Mungu akapanga njama. Na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kupanga njama.

وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا قَالُوا قَدْ سَمِعْنَا لَوْ نَشَاءُ لَقُلْنَا مِثْلَ هَـٰذَا إِنْ هَـٰذَا إِلَّا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ ﴿٣١﴾

31. Na wanaposomewa Aya zetu, husema: Tumekwishasikia, na lau tungependa tungelisema kama haya. Haya si chochote ila ni ngano tu za watu wa kale.

وَإِذْ قَالُوا اللَّـهُمَّ إِن كَانَ هَـٰذَا هُوَ الْحَقَّ مِنْ عِندِكَ فَأَمْطِرْ عَلَيْنَا حِجَارَةً مِّنَ السَّمَاءِ أَوِ ائْتِنَا بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٣٢﴾

32. Na waliposema: Ewe Mwenyezi Mungu! Ikiwa haya ni haki itokayo kwako, basi tupige mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu iumizayo.

وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُعَذِّبَهُمْ وَأَنتَ فِيهِمْ وَمَا كَانَ اللَّـهُ مُعَذِّبَهُمْ وَهُمْ يَسْتَغْفِرُونَ ﴿٣٣﴾

33. Na Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwaadhibu maadamu wewe umo pamoja nao. Wala hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaadhibu hali wanaomba msamaha.

وَمَا لَهُمْ أَلَّا يُعَذِّبَهُمُ اللَّـهُ وَهُمْ يَصُدُّونَ عَنِ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَمَا كَانُوا أَوْلِيَاءَهُ إِنْ أَوْلِيَاؤُهُ إِلَّا الْمُتَّقُونَ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٤﴾

34. Na wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu; hali wao wanazuilia (watu) msikiti mtakatifu? Wala wao hawakuwa ndio walinzi wake. Hawakuwa walinzi wake isipokuwa wenye takuwa tu, lakini wengi wao hawajui.

وَمَا كَانَ صَلَاتُهُمْ عِندَ الْبَيْتِ إِلَّا مُكَاءً وَتَصْدِيَةً فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ ﴿٣٥﴾

35. Na haikuwa Swala yao kwenye hiyo nyumba ila miluzi (kupiga mbinja) na makofi. Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkikufuru.

WALIPOKUFANYIA VITIMBI

Aya 30 – 35

LUGHA

Njama ikinasibishwa kwa mtu maana yake ni hila na hadaa. Na ikinasibishwa kwa Mwenyezi Mungu maana yake ni kuvunja njama.

MAANA

Na walipokupangia njama wale waliokufuru ili wakufunge au wakuue au wakutoe.

Katika Aya iliyotangulia (26) Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewakumbusha Waislamu neema yake juu yao. Katika Aya hii anamkumbusha Mtume(s.a.w.w) neema yake juu yake ambapo Washirikina wa Kiquraish walikubaliana kummaliza Nabii Muhammad(s.a.w.w) , Wakatofautiana katika njia ya kummaliza, Mmoja akasema tumfunge, mwingine akasema tumtoe Makka.

Kisha wakaafikiana wachague mtu katika kila ukoo na waivamie nyumba yake akiwa amelala kitandani wampige kwa panga zao pigo moja. Hapo damu yake itakuwa kwa koo zote, na Bani Hashim watashindwa kupigana na waarabu wote.

Wafasiri wanasema, akiwemo Tabari, Razi, na Abul Hayaan Al-Andalusi, kwamba; Mwenyezi Mungu alimpa wahyi Mtume wake kumjulisha hilo. Akamwamrisha atoke kuelekea Madina na akamwamrisha Ali bin Abu Talib alale kitandani kwake. Ali akalala kitandani kwake na kujifinika shuka yake. Walipovamia kitanda chake walimwona Ali, wakapigwa na mshangao. Pia Mtume alimwusia Ali kurudisha amana za watu walizoziweka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Na wakapanga njama na Mwenyezi Mungu akapanga njama na Mwenyezi Mungu ndiye mbora wa kupanga njama.

Njama ya Maquraish ni ile mipango yao ya kumuua Nabii Muhammad kwa namna ambayo ukoo wa Hashim utashindwa kulipizia kisasi. Ama njama ya Mwenyezi Mungu ni kupangua njama yao kwa kupanga Mwenyezi Mungu (s.w.t) Mtume atoke, na Ali alale kitandani kwake, Yametangulia maelezo kuhusu hayo katika kufasiri Juz.3 (3:54).

Na wanaposomewa Aya zetu, husema: Tumekwishasikia. Na lau tungependa tungelisema kama haya. Haya si chochote ila ni ngano tu za watu wa kale.

Maquraish walisema kuwa Qur’an ni ngano za watu wa kale, na kwamba wao wakitaka wanaweza kusema mfano wake. Walisema hivi wakiwa wanajua fika kwamba hiyo inatoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu wao na watu wote walishindwa kuleta mfano wa hata Sura moja tu.

Maquraish wameshindwa ndio maana wanakimbilia uzushi, kuficha kushindwa kwao na upotevu wao; sawa na kila anayeshindwa kuikabili haki kwa hoja na mantiki.

Na waliposema: Ewe Mwenyezi Mungu! Ikiwa haya ni haki itokayo kwako, basi tupige mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu iumizayo.

Baadhi ya watu wanaweza kung’angania dhambi kwa kiburi chao; sawa na wanavong’ang’ania dini au zaidi; mpaka wanafikia kuwa tayari kufa kuliko kukubali kushindwa, hata kama upande wa pili ni haki.

Wako tayari kuangamia na kuadhibiwa kuliko kuacha mafunzo yao na mila zao. Historia imetaja mifano mingi ya watu wa aina hiyo. Qur’an imetaja Firauni, watu wa Nuh, n.k.

Maquraish walipoitwa na Mtume kwenye Uislamu walisema: “Kama Muhammad ni mkweli basi itupige mvua ya mawe.” Yaani wanaona afadhali kuangamia kwa kupigwa mawe kuliko kumfuata Muhammad, hata kama ni Nabii.

Basi Mwenyezi Mungu akawajibu kwamba adhabu bado iko mbele yao na kwamba mlango bado uko wazi; na aliwapa muda kwa sababu moja aliy oiashiria kwa kauli yake:

Na Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwaadhibu maadamu wewe umo ndani yao.

Yaani Mwenyezi Mungu mtukufu hawaadhibu watu wa Makka maadamu Nabii Muhammad yuko. Hii ikiwa ni kumtukuza na kumwadhimisha.

Wala hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaadhibu hali wanaomba msamaha.

Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kusema kuwa hatawaadhibu Maquraish maadam Nabii Muhammad yuko kwao, anasema kuwa, vilevile, hatawaadhibu wakiamini, ni sawa Nabii Muhammad awe nao au asiwe nao. Kauli yake hii Mwenyezi Mungu ni sawa na kauli yake nyingine:

مَّا يَفْعَلُ اللَّـهُ بِعَذَابِكُمْ إِن شَكَرْتُمْ وَآمَنتُمْ ﴿١٤٧﴾

“Mwenyezi Mungu ana haja gani ya kuwaadhibu kama mtashukuru na mtaamini” Juz.5 (4:147).

Makusudio ya maana haya yanafahamika kutokana na kusema kwake moja kwa moja.

Na wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu?

Na pia kauli yake akiwaambia Maquraish:

Basi onjeni adhabu kwa sababu ya yale mliyokuwa mkikufuru.

Kwa ufasaha zaidi ni kuwa maana ya Aya ni kwamba, Yeye Mwenyezi Mungu hatawadhibu ikiwa Nabii Muhammad yuko kwao, Vilevile hatawaadhibu wakisilimu.

Ametumia neno msamaha kwa maana ya kusilimu, kwa sababu msamaha ni katika mambo yanayolazimiana na Uislamu, Kwa ufafanuzi huu, inatubainikia kuwa hakuna haja ya taawili walizozitaja wafasiri, tena zinamwacha msomaji gizani.

Na wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu: hali wao wanazuilia (watu) msikiti mtakatifu?

Hilo ni swali lenye maana ya kukanusha; yaani hakuna chochote katika dini au tabia kitakachowazuia kuadhibiwa kwao. Kwani wao kwa upande wa ushirikina wao wanazuia waislamu kumwabudu Mwenyezi Mungu katika nyumba yake takatifu.

Mwislamu yeyote, hata Mtume(s.a.w.w) alipokuwa Makka, hakuwa akiweza kuswali ndani ya Masjudil-Haram bila ya kupata udhia na mateso. Waliafikiana wamzuie Mtume kwa nguvu asifanye umra mwaka wa Hudaybiya.

Wala wao hawakuwa ndio walinzi wake.

Yaani washirikina si walinzi wa Masjidul Haram wala si watu wa nyumba hiyo, bali ni maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui wa nyumba yake. Kwa hiyo ni wajibu kuwafukuza na kuwazuia, kwa vile wanauchafua kwa najisi zao na uchafu wao. Kwa ajili hii, Uislamu ulipopata nguvu, walizuiliwa kuukurubia:

إِنَّمَا الْمُشْرِكُونَ نَجَسٌ فَلَا يَقْرَبُوا الْمَسْجِدَ الْحَرَامَ بَعْدَ عَامِهِمْ هَـٰذَا ﴿٢٨﴾

“Hakika washirikina ni najisi, kwa hiyo wasiukaribie Msikiti mtakatifu baada ya mwaka wao huu” (9:28).

Hawakuwa walinzi wake isipokuwa wenye takuwa tu.

Yaani hatastahiki yeyote, vyovyote alivyo; kuusimamia Msikiti mtakatifu (Masjidul Haram) ila akiwa ni mwema mwenye kumcha Mungu akiwa Mwislamu aliyepiga shahada, Je, itakuwaje mshirikina na mwenye kupinga?

Ingawaje maudhui ya Aya yanahusika na msikiti mtakatifu, lakini takuwa ni sharti ya kila anayesimamia misikiti au sehemu za kidini. Kwa vile sababu ya hilo ni utwahara wa mahali na utakatifu wake. La kushangaza ni kwamba wengi wanaosimamia mambo haya ni wale viumbe waovu ambao ni mabingwa wa fani ya hila na wizi.

Lakini wengi wao hawajui kwamba mwenye kusimamia msikiti na sehemu takatifu ni lazima awe mwema, mcha Mungu; na kwamba hakuna usimamizi kwa fasiki.

Utauliza : kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na wana jambo gani hata Mwenyezi Mungu asiwaadhibu” inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu aliwaadhibu Maquraish, ambapo inajulikana kuwa hayakuwapitia kama yaliyowapitia watu wa Mitume waliotangulia, kama vile Ad, Thamud, watu wa Nuh, wa Lut n.k.?

Jibu : Wale waliomuudhi Mtume na waislamu, Mwenyezi Mungu aliwaua siku ya Badr kwa mikono ya waislamu wenyewe. Miongoni mwa waliouwawa ni Abu Jahl, Uqba bin Abu Mui’t, Nadhr bin Al-Harith, Umayya bin Khalaf na wengineo katika vigogo vya Maquraish ambao walikuwa wamezidi mno kuwaudhi waislamu.

Kwa mfano Umayya bin Khalaf alikuwa akimmiliki Bilal mwadhini wa Mtume(s.a.w.w) . Alikuwa akimwadhibu kwenye mchanga ulio moto sana na kumpa adhabu za kila aina. Siku ya Badr Umayya alitoka pamoja na washirikina, na Bilal naye akatoka pamoja na Mtume wa Mwenyezi Mungu.

Mara tu, Bilal alipomwona Umayya alipiga ukelele: “Huyu kiongozi wa ukafiri, ama zake ama zangu.” Wakakusanyika baadhi ya wanyonge waliokuwa wakiteswa na huyu Umayya wakamshika; Bilal naye akampiga Umayya kwa upanga mpaka akamuua.

Akakichukua kichwa chake akakitungika kwenye upanga wake na huku akicheza kwa furaha.

Na haikuwa swala yao kwenye hiyo nyumba ila miluzi (kupiga mbinja) na makofi.

Kama kwamba mwulizaji anauliza: Maquraish walikuwa wakiswali katika msikiti mtukufu, sasa vipi wamestahiki adhabu? Akajibu Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwa swala yao ilikuwa ni vurugu tu, haina unyenyekevu.

Kwa sababu ilikuwa ni miluzi (mbinja) ya mdomoni na makofi ya mikononi.

Basi onjeni adhabu iliyowafikia siku ya Badr.

Na adhabu ya akhera ni kali zaidi.

Kwa sababu ya yale mliyokuwa mkikufuru.

Lau mngesilimu mngelisalimika na adhabu ya duniani na akhera.

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ لِيَصُدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ فَسَيُنفِقُونَهَا ثُمَّ تَكُونُ عَلَيْهِمْ حَسْرَةً ثُمَّ يُغْلَبُونَ وَالَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ يُحْشَرُونَ ﴿٣٦﴾

36. Hakika wale waliokufuru hutoa mali zao ili kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu. Basi watazitoa, kisha zitakuwa majuto juu yao, kisha watashindwa. Na wale waliokufuru watakusanywa kwenye Jahanamu.

لِيَمِيزَ اللَّـهُ الْخَبِيثَ مِنَ الطَّيِّبِ وَيَجْعَلَ الْخَبِيثَ بَعْضَهُ عَلَىٰ بَعْضٍ فَيَرْكُمَهُ جَمِيعًا فَيَجْعَلَهُ فِي جَهَنَّمَ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿٣٧﴾

37. Ili Mwenyezi Mungu apate kuwapambanua walio wabaya na walio wazuri na kuwaweka wabaya juu ya wabaya wengine na kuwarundika wote pamoja na kuwatupa katika Jahanamu, Hao ndio waliohasirika.

قُل لِّلَّذِينَ كَفَرُوا إِن يَنتَهُوا يُغْفَرْ لَهُم مَّا قَدْ سَلَفَ وَإِن يَعُودُوا فَقَدْ مَضَتْ سُنَّتُ الْأَوَّلِينَ ﴿٣٨﴾

38. Waambie wale waliokufuru, kama watakoma, watasamehewa yaliyopita. Na wakirudia basi imekwishapita desturi ya watu wa zamani.

وَقَاتِلُوهُمْ حَتَّىٰ لَا تَكُونَ فِتْنَةٌ وَيَكُونَ الدِّينُ كُلُّهُ لِلَّـهِ فَإِنِ انتَهَوْا فَإِنَّ اللَّـهَ بِمَا يَعْمَلُونَ بَصِيرٌ ﴿٣٩﴾

39. Na piganeni nao mpaka kusiwe na fitna na dini yote iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Wakikoma, basi hakika Mwenyezi Mungu anayaona wanayotenda.

وَإِن تَوَلَّوْا فَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَوْلَاكُمْ نِعْمَ الْمَوْلَىٰ وَنِعْمَ النَّصِيرُ ﴿٤٠﴾

40. Na wakigeuka, basi jueni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mola wenu, ni Mola mwema na msaidizi mwema.

WALIOKUFURU HUTOA MALI ZAO

Aya 36 – 40

MAANA

Hakika wale waliokufuru hutoa mali zao ili kuzuilia njia ya Mwenyezi Mungu. Basi watazitoa, kisha zitakuwa majuto juu yao, kisha watashindwa. Na wale waliokufuru watakusanywa kwenye Jahanamu.

Washirikina walikuwa wakitoa mali zao katika kupigana na waislamu na kuzuilia watu Uslamu.

Ndipo Mwenyezi Mungu akabainisha, katika Aya hii, kwamba mali hizo zitawarudishia majuto, udhalili duniani na adhabu kali huko akhera. Kwa sababu mwisho ushindi utakuwa wa dini ya Mwenyezi Mungu na watu wake.

Ili Mwenyezi Mungu apate kuwapambanua walio wabaya na walio wazuri.

Hii ni sababu na kubainisha sababu yenye kuwajibisha majuto ya Washirikina na udhalili wao. Nayo ni kuwa Mwenyezi Mungu ni Mwadilifu na mwenye hekima.

Miongoni mwa uadilifu wake ni kutokuwa sawa mbele yake mwema na mwovu na Mu’min na kafiri, bali atampambanua kila mmoja na kumfanyia anayostahiki.

Kwa ajili hii, atampa thawabu mwema na kumwinua huko akhera. Na pengine humchanganyia malipo ya dunia na akhera. Na atamdhalilisha mwovu na kumwadhibu huko akhera kwenye nyumba ya hisabu na malipo. Pengine humpa aina fulani ya adhabu katika dunia kwa kadiri hekima yake inavyotaka.

Na kuwaweka wabaya juu ya wabaya wengine na kuwarundika wote pamoja na kuwatupa katika Jahanamu.

Makusudio ni jinsi ya wabaya; yaani wanaofungamana na jina hilo. Kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu.

Hao ndio waliohasirika.

Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu kesho atawakusanya wabaya wakiwa mrundo kisha awatupe katika Jahanamu, kama anavyofanya mtafuta kuni akizikusanya pamoja na kuzitia motoni. Mwenyezi Mungu anasema:

وَأَمَّا الْقَاسِطُونَ فَكَانُوا لِجَهَنَّمَ حَطَبًا ﴿١٥﴾

“Na ama wanaokengeuka (kuiacha haki) watakuwa kuni za Jahanamu.” (72:15).

Hao ndio waliohasirika.

Kuna hasara gani kubwa zaidi ya kuwa mtu na nyama zake na damu yake ni kuni za moto alioukoka Mwenyezi Mungu kwa ghadhabu yake juu ya aliyemfanyia hiyana Mola wake na dhamir yake!

“Ewe Mwenyezi Mungu! Hakika sisi tunaihofia adhabu yako, Na tunakimbilia kwako, Wewe ni mkarimu humfukuzi mwenye kutaka hifadhi ya ukarimu wako na kukimbilia rehema yako.”

Waambie wale waliokufuru, kama watakoma, watasamehewa yaliyopita.

Maneno haya anaambiwa Mtume(s.a.w.w) . Mwenyezi Mungu anamwamrisha kuwapa mawaidha makafiri na kuwaambia mlango wa toba uko wazi mbele yao, na kwamba wamepewa fursa ya kuacha ukafiri na uadui kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, wakitubia basi Mwenyezi Mungu atawakubalia toba.

Kwa sababu Uislamu unakata yaliyokuwa kabla yake; kama ilivyoelezwa katika Hadith.

Na wakirudia basi imekwishapita desturi ya watu wa zamani.

Mfano wale waliokadhibisha Mitume na kuwapiga vita. Makusudio ya desturi ya Mwenyezi Mungu kwa waliopita – ni kuangamizwa makafiri, na Mitume kuwa washindi.

Mwenyezi Mungu amekwishandika: Hakika nitashinda mimi na Mitume wangu.

إِنَّ اللَّـهَ قَوِيٌّ عَزِيزٌ ﴿٢١﴾

“Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye nguvu, mwenye kushinda.” (58:21).

Na piganeni nao mpaka kusiwe na fitna na dini yote iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, Wakikoma, basi hakika Mwenyezi Mungu anayaona wanayotenda.

Makusudio ya Fitna hapa ni ukafiri. Aya imetangulia na tafsiri yake katika Juz.2 (2:193).

Na wakigeuka, basi jueni kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mola wenu, ni Mola mwema na msaidizi mwema.

Yaani kama washirikina wakipingana na ubainifu wa Mtume na amani yake, basi mjiizatiti enyi Waislamu wala msiwaogope. Kwani Mwenyezi Mungu atawasaidia na atawalinda; naye ni mbora wa walinzi na wasaidizi.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA JUZUU YA TISA


YALIYOMO

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA 1

IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA 1

IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA 1

IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED 1

IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU 1

UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI 1

MAKOSA YA CHAPA 2

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA 3

TUTAKUTOA EWE SHUAIB 3

MAANA 3

MKIMFUATA SHUAIB 4

MAANA 4

HATUKUMLETA NABII YOYOTE KATIKA MJI 5

MAANA 5

NA LAU KAMA WATU WA MJI 6

MAANA 7

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA 9

MIJI HIYO TUNAKUSIMULIA 9

MAANA 9

MUSA NA FIRAUNI 10

MUHTASARI WA KISA 10

JINA LA MAMAKE MUSA NA VIGANO 11

MAANA 12

WAKAJA WACHAWI 15

MAANA 15

UCHAWI 16

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA 19

UTAMWACHA MUSA? 19

MAANA 19

TULIWAADHIBU WATU WA FIRAUNI 21

MAANA 21

ILIPOWAANGUKIA ADHABU 23

MAANA 23

TULIWAVUSHA WANA WA ISRAIL 23

MAANA 23

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA 25

MAANA 25

NITAWAEPUSHIA AYA ZANGU 28

MAANA 28

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA 31

ALIPORUDI MUSA KWA WATU WAKE 31

MAANA 31

HAIKUWA ILA NI ADHABU YAKO 34

MAANA 34

REHMA YA MWENYEZI MUNGU INAMFIKIA IBLISII 36

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA 39

MTUME WA MWENYEZI MUNGU KWENU NYOTE 39

MAANA 39

UZAYUNI NA UYAHUDI 40

TULIWAGAWANYA KOO KUMI NA MBILI 41

MAANA 41

WAULIZE HABARI ZA MJI 42

MAANA 42

MAYAHUDI NA ADHABU MBAYA 44

MAANA 45

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA 47

TUKAWAJARIBU KWA MEMA NA MABAYA 47

MAANA 47

JE MIMI SI MOLA WENU? 49

MAANA 49

ULIMWENGU WA CHEMBE CHEMBE 49

TUMEMPA AYA ZETU AKAJIVUA 51

MAANA 52

ATAKAOWAONGOZA MUNGU NDIO WATAKAOONGOKA 53

MAANA 53

JE, MAJINA YA MWENYEZI MUNGU NI HAYOHAYO AU YANA KIASI 55

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA 58

WALIOKADHIBISHA AYA ZETU 58

MAANA 58

WANAKUULIZA SAA (KIYAMA) 60

MAANA 60

MTUME NA ELIMU YA GHAIB 61

ALIYEWAUMBA KATIKA NAFSI MOJA 63

MAANA 63

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA 65

JE, WANAWASHIRIKISHA WASIOUMBA KITU? 65

MAANA 65

SHIKA USAMEHEVU 67

MAANA 67

USAMEHEVU 68

KUAMRISHA MEMA 68

NA ACHANA NA WAJINGA 68

ISOMWAPO QUR’AN ISIKILIZENI 70

MAANA 70

MWISHO WA SURA YA SABA 71

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA 72

ANFAL NI YA MWENYEZI MUNGU NA MTUME 72

MAANA 72

DINI HAIOTESHI NGANO 74

KAMA ALIVYOKUTOA MOLA WAKO 75

KWENDA BADR 75

MAANA 76

MLIPOKUWA MKIMWOMBA MSAADA MOLA WENU 79

MAANA 79

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA 82

KUKIMBIA VITA 82

MAANA 82

KUMTII MWENYEZI MUNGU NA MTUME 85

MAANA 85

MWENYE KUTAFUTA HAKI NA MWENYE KUTAFUTA WINDO 85

DINI NA MAISHA 86

MAANA 86

TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA TISA 89

OGOPENI ADHABU 89

LUGHA 89

MAANA 89

WALIPOKUFANYIA VITIMBI 92

LUGHA 92

MAANA 92

WALIOKUFURU HUTOA MALI ZAO 96

MAANA 96

SHARTI YA KUCHAPA 97

MWISHO WA JUZUU YA TISA 97

YALIYOMO 98



[1] Hata hivyo kauli yenye nguvu kwa upande wa shia ni kuwa alifariki 28 Safar (mfunguo tano)

[2] Tulipofasiri Juz.6 (5:47) tulisema kuwa ukafiri ukitegemezwa kwenye kitendo, makusudio yake yanakuwa ufasiki, na ufasiki ukitegemezewa kwenye itikadi, basi makusudio yake ni ukafiri. Kwa hivyo makusudio ya ukafiri wa kuacha kutenda kwa ajili ya maisha ni ukafiri wa kimatendo, sio wa kiitikadi.