TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA
IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU
Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.
Kama lilivyo jina la Tafsiri ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo.
Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.
Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.
Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea. Hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka kwa lugha ya kiswahili hivi karibuni Inshaallah).
Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.
Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasayansi kama kina Enstein, wasanii kama Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.
Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.
Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.
Mwisho : Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.
Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa. Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.
Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146), Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.
Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawamal qiyama. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.
Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu Jabal amil 'Makosa ya chapa.'
Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"
Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.
Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa.” Kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.
Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu." Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).
MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH
1
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
Surah Ya Kumi na Tano: Surat Al-Hijri. Ina Aya 99, immeshuka Makka.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, Mwenye kurehemu.
الر تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ وَقُرْآنٍ مُّبِينٍ ﴿١﴾
1. Alif Laam Raa. Hiyo ni Aya za Kitabu na Qur’an inayobainisha.
رُّبَمَا يَوَدُّ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْ كَانُوا مُسْلِمِينَ ﴿٢﴾
2. Huenda waliokufuru wakatamani wangekuwa Waislamu.
ذَرْهُمْ يَأْكُلُوا وَيَتَمَتَّعُوا وَيُلْهِهِمُ الْأَمَلُ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ ﴿٣﴾
3. Waache wale (chakula), na wastarehe na iwazuge tamaa; watakuja jua.
وَمَا أَهْلَكْنَا مِن قَرْيَةٍ إِلَّا وَلَهَا كِتَابٌ مَّعْلُومٌ ﴿٤﴾
4. Na hatukuangamiza mji wowote ule ila una muda maalum.
مَّا تَسْبِقُ مِنْ أُمَّةٍ أَجَلَهَا وَمَا يَسْتَأْخِرُونَ ﴿٥﴾
5. Hauwezi umma wowote kuitangulia ajali yake wala kuchelewa.
Aya 1-5
Alif laam Raa.
Umetangulia mfano wake na maelezo yake katika Juz. 1, mwanzo wa Sura ya Baqara.
Hiyo ni Aya za Kitabu na Qur’an inayobainisha.
Hiyo, ni ishara ya hiyo Sura yenyewe tunayoifasiri. Makusudio ni kueleza kuwa hiyo ni miongoni mwa Aya za Kitabu cha Mwenyezi Mungu na ni Qur’an inayopambanua baina ya haki na batili.
Huenda waliokufuru wakatamani wangekuwa Waislamu.
Neno ‘Huenda’ hapa lina maana ya maana ya wingi; yaani kila mmoja kati ya wenye makosa, kesho atafunukiwa na pazia na atatamani lau angelikuwa hapa duniani ni miongoni mwa wenye takua ambao wameisalimisha haki na wakaitumia. Angalia kifungu cha maneno ‘Hakika dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu’ katika Juz. 3. (3:19).
Waache wale (chakula), na wastarehe na iwazuge tamaa; watakuja jua.
Waliathirika na starehe za duniani, Mwenyezi Mungu akawahadharisha na yatakayowapata kesho miongoni mwa adhabu kali.
Na hatukuangamiza mji wowote ule ila una Kitabu maalum.
Kana kwamba muulizaji ameuliza: Kwa nini Mwenyezi Mungu haharakishi adhabu ya wale waliomuasi Yeye na mitume yake? Ndio akajibu Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwa kila adhabu ina muda wake na kwamba Yeye, ambaye imetukuka hekima yake, hakuangamiza umma wowote hapo nyuma ila baada ya kufikia muda wake. Mjinga ni yule anayedanganyika na muda.
Hauwezi umma wowote kuitangulia ajali yake wala kuchelewa.
Angalia kifungu cha ‘Ajali haina kinga’ Juz; 4. (3:145).
وَقَالُوا يَا أَيُّهَا الَّذِي نُزِّلَ عَلَيْهِ الذِّكْرُ إِنَّكَ لَمَجْنُونٌ ﴿٦﴾
6. Na walisema: “Ewe uliyeteremshiwa ukumbusho! Wewe ni mwendawazimu.
لَّوْ مَا تَأْتِينَا بِالْمَلَائِكَةِ إِن كُنتَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٧﴾
7. Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli?.
مَا نُنَزِّلُ الْمَلَائِكَةَ إِلَّا بِالْحَقِّ وَمَا كَانُوا إِذًا مُّنظَرِينَ ﴿٨﴾
8. Hatuteremshi Malaika ila kwa haki na hapo hawatapewa muda.
إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ ﴿٩﴾
9. Hakika sisi tumeuteremsha ukumbusho huu na hakika sisi ndio tuulindao.
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ فِي شِيَعِ الْأَوَّلِينَ ﴿١٠﴾
10. Na hakika tulikwishawatuma Mitume kabla yako katika mataifa ya mwanzo.
وَمَا يَأْتِيهِم مِّن رَّسُولٍ إِلَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿١١﴾
11. Na hakuwajia Mtume ila walikuwa wakimfanyia stihzai.
كَذَٰلِكَ نَسْلُكُهُ فِي قُلُوبِ الْمُجْرِمِينَ ﴿١٢﴾
12. Hivyo ndivyo tunavyouingiza katika nyoyo za wakosefu.
لَا يُؤْمِنُونَ بِهِ وَقَدْ خَلَتْ سُنَّةُ الْأَوَّلِينَ ﴿١٣﴾
13. Hawauamini na hali umewapitia mfano wa wa kwanza.
وَلَوْ فَتَحْنَا عَلَيْهِم بَابًا مِّنَ السَّمَاءِ فَظَلُّوا فِيهِ يَعْرُجُونَ ﴿١٤﴾
14. Na lau tungeliwafungulia mlango wa mbingu wakawa wanapanda.
لَقَالُوا إِنَّمَا سُكِّرَتْ أَبْصَارُنَا بَلْ نَحْنُ قَوْمٌ مَّسْحُورُونَ ﴿١٥﴾
15. Basi wangelisema: Macho yetu yamelevywa; bali sisi ni watu waliorogwa.
وَلَقَدْ جَعَلْنَا فِي السَّمَاءِ بُرُوجًا وَزَيَّنَّاهَا لِلنَّاظِرِينَ ﴿١٦﴾
16. Hakika tumeweka katika mbingu buruji na tumezipamba kwa wenye kuangalia.
وَحَفِظْنَاهَا مِن كُلِّ شَيْطَانٍ رَّجِيمٍ ﴿١٧﴾
17. Na tukazilinda na kila shetani afukuzwaye.
إِلَّا مَنِ اسْتَرَقَ السَّمْعَ فَأَتْبَعَهُ شِهَابٌ مُّبِينٌ ﴿١٨﴾
18. Isipokuwa asikilizaye kwa kuiba, naye hufuatwa na kijinga kinachoonekana.
Aya 6-18
Na walisema: Ewe uliyeteremshiwa ukumbusho! Wewe ni mwendawazimu.
Waliosema ni maquraysh wakimwambia Muhammad aliyeteremshiwa Qur’an, kwa kumdharau. Kwa vile katika mantiki yao na vipimo vyao ni kwamba yeye ni mkichaa kwa kuwa anawaambia mambo yasiyowaingia; hata kama ni rehema kwa walimwengu na muujiza ulioshinda kwa elimu yake na mafunzo yake.
Mantiki haya hayahusiki na waabudu masanamu pekee yao wala wazandiki au walahidi; isipokuwa yanamkusanya kila anyeifanya dhati yake na manufaa yake ndio kipimo cha haki na mizani ya uadilifu, hata kama atasema: Lailaha illallah Muhammadur-rasulullah (Hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu).
Kabisa! Hakuna tofauti baina ya Mwislamu huyu wa masilahi, ambaye amekubali utume wa Muhammad na mshirikina ambaye anapinga utume wa Muhammad; isipokuwa Mwislamu huyu amemwamini Muhammad kinadharia na akamakana kimatendo; na mshirikina amemkana kikauli na kimatendo. Kwa hiyo natija kwa upande wa kimatendo ni moja tu.
Mbona hutuletei Malaika ikiwa wewe ni miongoni mwa wasemao kweli?
Hii ni kauli ya washirikina kwa Mtume(s.a.w.w) . Walitoa sharti la kuamini kwao kuwa Malaika wateremshwe kutoka mbinguni na washuhudie utume wa Muhammad, ndio akawajibu kwa kusema:
Hatuteremshi Malaika ila kwa haki na hapo hawatapewa muda.
Ufupisho wa jibu ni kuwa Mwenyezi Mungu huwateremsha Malaika kwa ajili ya kufikisha ujumbe na hawateremshi kwa waongo wenye inadi, isipokuwa kwa adhabu na maangamizi; kama alivyofanya kwa umma zilizopita. Lau kama Mwenyezi Mungu angeliwajibu washirikina kwa kuwateremshia Malaika, wangeliangamia wote. Umetangulia mfano wa Aya hii kwa swali na jawabu katika Juz. 7 (6:8).
Hakika sisi tumeuteremsha ukumbusho huu na hakika sisi ndio tuulindao.
Makusudio ya ukumbusho ni Qur’an. Imesemekana kuwa dhamir katika neno kulinda inamrudia Mtume kwamba yeye ndiye alindwaye kukingwa na maadui zake, lakini hilo ni kinyume na dhahiri ya Aya. Kwa hiyo inarudia kwenye ukumbusho ambao ni Qur’an, kama tulivyofasiri.
Unaweza kuuliza kuwa : Mwenyezi Mungu anailinda na nini? Ikiwa ni kuilinda na kupotolewa, kama walivyosema wafasiri wengi, basi juzi juzi[1] tu Israil ilichapisha maelfu ya nakala za Qur’an na wakaipotosha Aya hii: Na mwenye kutaka dini isiyokuwa Uislam haitakubaliwa kwake, Juz. 3 (3:85), ambayo kwenye Qur’an ya Israil inasomeka hivi: Na mwenye kutaka dini isiyokuwa Uislam itakubaliwa kwake.
Na kama ukisema kuwa makusudio ni kuwa hakuna yeyote atakayeitia ila, itakuwa ni kinyume na hali halisi ilivyo. Sasa ni kulindwa vipi?
Razi na Tabrasi wameleta majibu mengi yasiyokinaisha. Tuonavyo sisi ni kuwa makusudio ya kulindwa Qur’an ni kuwa kila liliomo ndani yake ni haki inayothibiti kila wakati, isiyowezwa kupingwa wala kutiwa ila kwa hoja; bali kila akili na elimu zinaavyozidi kupanuka, hujitokeza dalili mpya za ukweli wa Qur’an na utukufu wake.
Maana haya ya kulindwa Qur’an tunayapata katika kauli yake Mwenyezi Mungu:
لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ ﴿٤٢﴾
“Hautakifikia upotofu mbele yake wala nyuma yake, kimeteremshwa na Mwenye hekima, Msifiwa” (41:42).
Na hakika tulikwisha watuma Mitume kabla yako katika mataifa ya mwanzo, Na hakuwajia Mtume ila walikuwa wakimfanyia istihzai.
Maneno haya anaambiwa Muhammad, Mataifa ya mwanzo ni umma uliokwishapita. Maana ni kuwa hali ya washirikina - kukukadhibisha wewe na kukuita kuwa ni mwendawazimu - ni kama hali ya washirikina wa zamani. Hakuwajia Mtume ila walimkadhibisha. Pamoja na hivyo walikuwa na subira na kuvumilia upumbavu wao. Lengo ni kumtuliza Mtume mtukufu(s.a.w.w) . Umepita mfano wake katika Juz. 7 (6:34).
Hivyo ndivyo tunavyouingiza katika nyoyo za wakosefu hawauamini na hali umewapitia mfano wa wa kwanza.
Dhamir ya tunavyouingiza na hawauamini inarudia kwenye ukumbusho (Qur’an). Maana ni kuwa Qur’an haiingii katika nyoyo za wakosefu kiukweli na kiimani; isipokuwa inaingia kidharau na kikejeli.
Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘hawauamini’ ni tafsiri ya ‘tunavyouingiza.’ Maana ya ‘umepita mfano wa wa kwanza ni kuwa wakadhibishaji wa sasa ni kama wakadhibishaji wa zamani. Nyoyo zao zinaingia batili badala ya imani na upotevu badala ya uongofu.
Kusema kuwa Mungu anawaingiza ni kunasibisha kitu kwa sababu yake ya mbali moja kwa moja, Yamekwishapita maelezo ya hayo mara kadhaa.
Na lau tungeliwafungulia mlango wa mbingu wakawa wanapanda, basi wangelisema: “Macho yetu yamelevywa; bali sisi ni watu waliorogwa.”
Katika Aya ilyotangulia, wapinzani walimtaka Muhammad(s.a.w.w) kuwateremshia Malaika, Mwenyezi Mungu akwajibu kwamba Malaika hushuka na adhabu ya mangamizi kwa wapinzani na wakadhibishaji.
Kisha katika Aya hii akafuatishia jibu hilo kwa kusema kuwa lau atawafungulia milango ya mbinguni, kisha wapande kwa mili yao na wawaone Malaika na maajabu mengi, wangelisema: hakika Muhammad ameturoga na ametuonyesha njozi kuwa hali halisi na halisi kuwa njozi. Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:7).
Hakika tumeweka katika mbingu buruji na tumezipamba kwa wenye kuangalia.
Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa makusudio ya buruji ni nyota. Wengine wakasema ni vituo vya sayari ya Jua na Mwezi.
Vyovyote iwavyo, lengo la Aya sio kutufundisha elimu ya falaki ili tujue hiyo buruji hasa ni nini; isipokuwa lengo la kwanza kabisa ni kuzingatia na kutilia manani (tadabbur) uwezo wa Mwenyezi Mungu na hekima yake katika kuumba mbingu na ardhi na kwamba undani, nidhamu na uzuri aliouumba ni dalili wazi ya kuweko Mwenyezi Mungu na umoja wake, kuliko kuteremsha Malaika na kuliko miujiza yote wanayoitaka
Na tukazilinda na kila shetani afukuzwaye; isipokuwa asikilizaye kwa kuiba, naye hufuatwa na kijinga kinachoonekana.
Watu wa wakati wa jahilia walikuwa wakiamini kuwa kila kuhani ana shetani wake apandae mbinguni na kusikiliza mazungumzo ya Malaika kuhusu watu wa ardhini, kisha anashuka ardhini kwa kuhani wake kumpa habari. Aya mbili hizi zinapinga na kukana ngano hizi na kwamba mashetani hawawezi kabisa kupanda mbinguni. Na kusema kwake kijinga kinachoonekana ni fumbo la kuwa shetani hawezi kabisa hata kukurubia kuwasikilza Malaika; kama walivodai watu wa zama za jahiliya.
وَالْأَرْضَ مَدَدْنَاهَا وَأَلْقَيْنَا فِيهَا رَوَاسِيَ وَأَنبَتْنَا فِيهَا مِن كُلِّ شَيْءٍ مَّوْزُونٍ ﴿١٩﴾
19. Na ardhi tumeitandaza na tumeweka humo milima na tumeotesha kila kitu kwa wizani.
وَجَعَلْنَا لَكُمْ فِيهَا مَعَايِشَ وَمَن لَّسْتُمْ لَهُ بِرَازِقِينَ ﴿٢٠﴾
20. Na tumejaalia humo maisha, Na ya ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku.
وَإِن مِّن شَيْءٍ إِلَّا عِندَنَا خَزَائِنُهُ وَمَا نُنَزِّلُهُ إِلَّا بِقَدَرٍ مَّعْلُومٍ ﴿٢١﴾
21. Na hakuna chochote ila hazina yake iko kwetu na wala hatukiteremshi isipokuwa kwa kipimo maalum.
وَأَرْسَلْنَا الرِّيَاحَ لَوَاقِحَ فَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَسْقَيْنَاكُمُوهُ وَمَا أَنتُمْ لَهُ بِخَازِنِينَ ﴿٢٢﴾
22. Na tukazipeleka pepo za kupandishia na tukateremsha kutoka mbinguni maji tukawanywesha hayo wala nyinyi sio mnaoyaweka akiba.
وَإِنَّا لَنَحْنُ نُحْيِي وَنُمِيتُ وَنَحْنُ الْوَارِثُونَ ﴿٢٣﴾
Na hakika sisi ndio tunaohuyisha na tunaofisha, Na sisi ndio warithi.
وَلَقَدْ عَلِمْنَا الْمُسْتَقْدِمِينَ مِنكُمْ وَلَقَدْ عَلِمْنَا الْمُسْتَأْخِرِينَ ﴿٢٤﴾
24. Na hakika tunawajua watanguliao katika nyinyi na hakika tunawajua wachelewao.
وَإِنَّ رَبَّكَ هُوَ يَحْشُرُهُمْ إِنَّهُ حَكِيمٌ عَلِيمٌ ﴿٢٥﴾
25. Na hakika Mola wako ndiye atakayewakusanya. Hakika Yeye ni Mwenye hekima, Mjuzi.
Aya 19 -25
Na ardhi tumeitandaza na tumeweka humo milima na tumeotesha kila kitu kwa wizani.
Umetangulia ufafanuzi wake katika Juz. 13 (13:3).
Kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Kila kitu kwa wizani’ ina maana moja na kauli yake:
وَكُلُّ شَيْءٍ عِندَهُ بِمِقْدَارٍ ﴿٨﴾
“Na kila kitu kwake, ni kwa kipimo” Juz.13 (13:8),
Pia kauli yake:
وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا ﴿٢﴾
“Na akaumba kila kitu na akakikadiria kipimo” (25:2).
Yaani anachunga kiwango, aina, sura na lengo la kupatikana kitu hicho. Kama ingelikuwa ni sadfa basi kusingelikuwa na mpangilio huu.
Na tumejaalia humo maisha.
Yaani humo ardhini, Maana ya maisha ni zile sababu za maisha; kama vile kilimo, biashara na viwanda. Lakini maisha ya unyonyaji na uporaji hivyo ni viwanda vya shetani, sivyo alivyovijaalia Mwenyezi Mungu.
Na ya ambao nyinyi sio wenye kuwaruzuku.
Kila kiumbe hai ardhini sisi hatukiruzuku wala hatukalifiwi na riziki yake, hilo liko wazi; isipokuwa lengo la ishara hii ni kuwa sisi tujue kuwa viumbe vyote hai vinaishi kwa riziki ya Mwenyezi Mungu, hakuna aliye hai anayeweza kumruzuku aliye hai; hata watoto tuwaleao na wanyama tuwafugao, riziki zao zote zinaatoka kwa Mungu, si kwa mwengine.
Na hakuna chochote ila hazina yake iko kwetu na wala hatukiteremshi isipokuwa kwa kipimo maalum.
Razi anasema: “Wameafikiana wafasiri kuwa makusudio ya chochote ni mvua, kwa vile hiyo ndiyo sababu ya riziki na maisha.” Lakini ukweli ni kuwa makusudio ya chochote ni mvua na mengineo. Kwa sababu neno chochote linaenea kwenye kila kitu; kama kusema sikumuona yeyote. Makusudo ya kuteremsha ni kutoa. Kiwango maalum ni sababu ya riziki. Maana ni kuwa heri yote iko kwa Mungu, Yeye ndiye anayewapa wenye kujitahidi, sio wavivu na wazembe. Mwenyezi Mungu ansema:
هُوَ الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ ذَلُولًا فَامْشُوا فِي مَنَاكِبِهَا وَكُلُوا مِن رِّزْقِهِ ﴿١٥﴾
Yeye ndiye aliyewafanyia ardhi iwe laini basi nendeni katika pande zake na kuleni katika riziki zake (67:15).
Kwa maelezo zaidi angalia kifungu ‘Je riziki ni bahati au majaaliwa?’ Juz.7 (5:100).
Na tukazipeleka pepo za kupandishia na tukateremsha kutoka mbinguni maji tukawanywesha hayo wala nyinyi sio mnaoyaweka akiba.
Pepo zimesifiwa kuwa za kupandishia mbegu kwa vile zinaabeba mawingu ya mvua na kufanya miti iwe inamea kutokana na mvua. Kwenye hali hii Mwenyezi Mungu ameishria mahali pengine kwa kusema: “Na yeye ndiye azipelekaye pepo kuwa ni bishara kabla ya kufika rehema yake. Hata zinapobeba mawingu mazito tunayasukuma kwa ajili ya mji uliokufa, Juz. 8 (7:57).
Vilevile zimesifiwa kuwa ni za kupandishia kwa vile zinahamisha mbegu za maua ya kiume na kuzipeleka kwenye maua ya kike ili yaweze kutoa mazao na matunda.
Makusdio ya kusema: ‘wala nyinyi sio mnaoyaweka akiba’, sio kuwa maji yote yako kwenye tangi kubwa lililoko kwa Mwenyezi Mungu, hapana; isipokuwa makusudio ni kuwa Mwenyezi Mungu anayateremsha maji kwa sababu zake za kimaumbile, kuayahifadhi ardhini na kuyatoa kidogo kidogo, kupitia mito, kulingana na mahitaji.
Na hakika sisi ndio tunaohuyisha na tunaofisha, Na sisi ndio warithi.
Sisi ndio warithi ni fumbo la kuwa kila aliyeko ataondoka, hatabaki yoyote isipokuwa dhati ya Mola mwenye utukufu na kutukuka.
Na hakika tunawajua watanguliao katika nyinyi na hakika tunawajua wachelewao.
Razi na Tabrasi wametaja njia sita katika maana ya watanguliao na wachelewao. Usahihi ni kuwa makusudio ni kwamba hakifichiki kitu chochote mbele ya Mwenyezi Mungu katika hali ya waliotangulia na watakaokuja nyuma.
Na hakika Mola wako ndiye atakayewakusanya, Hakika Yeye ni Mwenye hekima, Mjuzi.
Atawakusanya wote siku ya hisabu na malipo na ni Mwenye hekima katika kuwakusanya kwao huko, ambapo mtenda mema atapata thawabu za mema yake na mtenda maovu atapata adhabu ya movu yake. Vilievile Yeye anamjua aliyefanya mema na aliyefanya maovu.
2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ ﴿٢٦﴾
26. Na hakika tulimuumba mtu kutokana udongo mkavu kwa matope meusi yenye kufinyangwa.
وَالْجَانَّ خَلَقْنَاهُ مِن قَبْلُ مِن نَّارِ السَّمُومِ ﴿٢٧﴾
27. Na majini tumewaumba kwa moto wenye joto kali.
وَإِذْ قَالَ رَبُّكَ لِلْمَلَائِكَةِ إِنِّي خَالِقٌ بَشَرًا مِّن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ ﴿٢٨﴾
28. Na Mola wako alipowaambia Malaika: “Hakika mimi nitamuumba mtu kutokana na udongo mkavu kwa matope meusi yenye kufinyangwa.
فَإِذَا سَوَّيْتُهُ وَنَفَخْتُ فِيهِ مِن رُّوحِي فَقَعُوا لَهُ سَاجِدِينَ ﴿٢٩﴾
29. Basi nitakapomkamilisha na nikampulizia roho yangu, basi muangukieni kumsujudia.
فَسَجَدَ الْمَلَائِكَةُ كُلُّهُمْ أَجْمَعُونَ ﴿٣٠﴾
30. Wakasujudu Malaika wote pamoja.
إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ أَن يَكُونَ مَعَ السَّاجِدِينَ ﴿٣١﴾
31. Isipokuwa Ibilisi alikataa kuwa pamoja na waliosujudi.
Aya 26 – 31
Na hakika tulimuumba mtu kutokana na udongo mkavu kwa matope meusi yenye kufinyangwa.
Watu wamezungumza mengi sana kuhusu asili ya mtu. Darwin amesema kuwa asili ya mtu ni nyani. Tumefafanua kuhusu dhana ya Darwin na asili ya mtu katika Juz. 8. (7: 11). Hapa tunayarudia maudhui hayo kwa mfumo mwingine:
Maarifa ya kujua mambo yanakuwa tu katika hali zifuatazo:- Majaribio, kushuhudia, akili na wahyi. Ni wazi kwamba, kutokana na utafiti, tunaweza kumjua mtu alivyo. Ama kujua alipatikana vipi na alikuwa katika hali gani, swali hili haliwezi kujibiwa na majaribio.
Tukija kwenye kushuhudia, hakuna mtu aliyeshuhudia uumbwaji wa mtu, wala hakuna kitu, katika vinavyofukuliwa, kinachofahamisha asili ya mtu, Hilo tumelifafanua katika Juz. 8: (7:11–18). Ama tukiuliza akili kuhusu asili ya mtu, ni sawa na kuiuliza hiyo akili, ni nani baba yake fulani, je alikuwa ni mrefu au mfupi? Kwa hiyo basi hakuna kilichobakia katika kuja asili ya kuumbwa mtu isipokuwa ni kwa wahyi tu.
Mwenye kufuatilia Aya za Qur’an yenye hekima, atakuta baadhi ya Aya zinaasema:
وَهُوَ الَّذِي خَلَقَ مِنَ الْمَاءِ بَشَرًا ﴿٥٤﴾
Yeye ndiye aliyemuumba binadamu kutokana na maji (25:54).
Nyingine inasema:
كَمَثَلِ آدَمَ خَلَقَهُ مِن تُرَابٍ ثُمَّ قَالَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٥٩﴾
“...ni kama mfano wa Adam; alimuumba kutokana na udongo, kisha akamwambia kuwa akawa.” Juz.3 (3:59)
Pia kuna ile isemayo: “Yeye ndiye aliyewaumba kwa udongo.” Juz, 7 (6:2) udongo uliokusudiwa hapa, kutokanana neno la kiarabu twin ni udongo mbichi – machanganyiko wa mchanga na maji.
Aya tuliyo nayo inasema kuwa mtu ameumbwa kutokana na udongo mkavu kwa tope nyeusi zinazoweza kufinyangwa, bila shaka hapo itakuwa ni mchanganyiko wa udongo na maji.
Kwa hiyo basi asili ya mtu ni maji na mchanga alioumbia Mwenyezi Mungu baba wa watu.
Na majini tumewaumba kwa moto wenye joto kali.
Jamaa wamekanusha kuweko majini, Baadhi ya waumini wamefasri majini waliotajwa katika Qur’an kuwa ni viini (microbe) visivyoonekana kwa macho. Wamechukulia neno Jinn kilugha, lenye maana ya kitu kililichofichikana na macho.
Wengine wakasema kuwa majini wapo, Wakatunga vitabu kuhusu idadi yao, miji yao, desturi zao, nembo zao na hata viongozi wao. Pia wakaelezea uwezekano wa jini kumuoa mtu au mtu kumuoa jini.
Sisi tunaamini kuweko majini, si kwa jingine isipokuwa tu wahyi umethibitisha hilo na inakubalika kiakili, Hatumwamini yeyote anayedai kuwa ana mawasiliano au kumuona jini. Hatukubali masimulizi yoyote yanayohusiana nao isipokuwa kwa kutamkwa wazi na wahyi.
Aya hii tuliyonayo imeweka wazi kuwa jini ameumbwa kutokana na moto na pia ile isemayo:
وَخَلَقَ الْجَانَّ مِن مَّارِجٍ مِّن نَّارٍ ﴿١٥﴾
Na akawaumba majini kwa ulimi wa moto (55:15).
Kwa hiyo sisi tunaamini kuwa asili ya majini ni moto. Lakini ni aina gani ya moto na je, umbile lenyewe lilikuwaje, Mwenyezi Mungu ndiye ajuaye zaidi.
Katika baadhi ya niliyoyasoma ni kuwa wataalamu wamegundua aina ya vidudu ambavyo haviwezi kupata uhai isipokuwa kwenye hewa ya sumu na vingine uhai wake uko kwenye visima vya mafuta na kwenye mwako.
Kwa hiyo kuna uwezekano kuwa kwenye sayari ya Jua kuna viumbe hai vinavyoafikiana na joto la Jua; kama samaki anavyoishi kwenye maji na kipepeo anavyopata rangi ya waridi na kobe kuwa na rangi ya jangwani.
Na Mola wako alipowaambia Malaika: Hakika mimi nitamuumba mtu kutokana udongo mkavu kwa matope meusi yenye kufinyangwa.
Mwenyezi Mungu aliwaambia hivi Malaika, lakini Malaika nao wakamawambia Mungu:
Je utaweka humo watakaofanya ufisadi humo na kumwaga damu? Juz,1 (2:30).
Tumeeleza huko kuhusu Malaika kujibizana na Mungu na kwamba aliwa- pa nafasi ya maswali na majibizano yaliyofanana na kupinga; kisha akawafahamisha uhakika kwa njia ya upole. Pengine anaweza kupata funzo yule anayejiona ni zaidi ya wote.
Basi nitakapomkamilisha na nikampulizia roho yangu.
Yaani nitakapompa uhai, Angalia Juz, 6 (4: 171 – 173), huko tumefafanua zaidi kuhusu neno roho
Basi muangukieni kumsujudia, Wakasujudu Malaika wote pamoja isipokuwa Ibilisi alikataa kuwa pamoja na waliosujudu.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 1 (2:34).
قَالَ يَا إِبْلِيسُ مَا لَكَ أَلَّا تَكُونَ مَعَ السَّاجِدِينَ ﴿٣٢﴾
32. Akasema (Mwenyezi Mungu): Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na waliosujudu?
قَالَ لَمْ أَكُن لِّأَسْجُدَ لِبَشَرٍ خَلَقْتَهُ مِن صَلْصَالٍ مِّنْ حَمَإٍ مَّسْنُونٍ ﴿٣٣﴾
33. Akasema (Iblis): “Haiwi mimi kumsujudia uliyemuumba kutokana na udongo mkavu kwa matope meusi yenye kufinyangwa.”
قَالَ فَاخْرُجْ مِنْهَا فَإِنَّكَ رَجِيمٌ ﴿٣٤﴾
34. Akasema (Mwenyezi Mungu): Basi toka humo, kwani hakika wewe ni mwenye kufukuzwa.
وَإِنَّ عَلَيْكَ اللَّعْنَةَ إِلَىٰ يَوْمِ الدِّينِ ﴿٣٥﴾
35. Na hakika itakuwa juu yako laana mpaka siku ya malipo.
قَالَ رَبِّ فَأَنظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ ﴿٣٦﴾
36. Akasema (Iblisi): “Mola wangu! Nipe muda mpaka siku watakapofufuliwa.
قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنظَرِينَ ﴿٣٧﴾
37. (Mwenyezi Mungu) akasema: Basi hakika wewe ni katika waliopewa muda.
إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ ﴿٣٨﴾
38. Mpaka siku ya wakati maalum.
قَالَ رَبِّ بِمَا أَغْوَيْتَنِي لَأُزَيِّنَنَّ لَهُمْ فِي الْأَرْضِ وَلَأُغْوِيَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٣٩﴾
39. Akasema (Iblisi): Kwa ulivyonipoteza, basi nitahakikisha ninawazaini hapa ardhini na nitawapoteza wote.
إِلَّا عِبَادَكَ مِنْهُمُ الْمُخْلَصِينَ ﴿٤٠﴾
40. Isipokuwa waja wako waliosafishwa.
قَالَ هَـٰذَا صِرَاطٌ عَلَيَّ مُسْتَقِيمٌ ﴿٤١﴾
41. Akasema (Mwenyezi Mungu): Hii ni njia juu yangu mimi iliyonyooka.
إِنَّ عِبَادِي لَيْسَ لَكَ عَلَيْهِمْ سُلْطَانٌ إِلَّا مَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْغَاوِينَ ﴿٤٢﴾
42. Hakika waja wangu hutakuwa na mamlaka nao, isipokuwa wale wapotofu waliokufuata.
وَإِنَّ جَهَنَّمَ لَمَوْعِدُهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٤٣﴾
43. Na hakika Jahannam ndipo mahali pao walipoahidiwa wote.
لَهَا سَبْعَةُ أَبْوَابٍ لِّكُلِّ بَابٍ مِّنْهُمْ جُزْءٌ مَّقْسُومٌ ﴿٤٤﴾
44. Ina milango saba, kila mlango una sehemu waliyotengewa.
Aya 32 – 44
Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliwaamuru Malaika kumsujudia Adam kwa sijda ya kimaamkuzi sio ya kiibada, Wakatii wote, lakini Ibilisi akaasi. Maulamaa wamehitilafiana kuhusu jinsia ya Iblisi, kuwa je, alikuwa Malaika kisha akafukuzwa au alikuwa shetani tangu mwanzo?
Mzozo huu ni tasa. Maadam Ibilisi kwa hali yoyote ni mwenye kulaumiwa na mwenye kufurushwa. Alpojizuia kusujudu Mola Mtukufu alimuuliza:
Akasema (Mwenyezi Mungu): Ewe Iblisi! Una nini hata hukuwa pamoja na waliosujudu?
Je, wewe una cheo zaidi au ni mtukufu sana kuliko waliomsujudia Adam?
Akasema (Iblis): Haiwi mimi kumsujudia uliyemuumba kutokana na udongo mkavu kwa matope meusi yenye kufinyangwa.
Iblisi aliasi na kufanya jeuri, sio kwa kitu kingine isipokuwa ni ubaguzi wa rangi tu. Na kila mwenye kufanya ubaguzi kwa sababu ya asili yake na jinsia yake, basi ni mwenye kulaaniwa, kufukuzwa na kulaumiwa; sawa na Iblisi.
Akasema (Mwenyezi Mungu): Basi toka humo, kwani hakika wewe ni mwenye kufukuzwa na hakika itakuwa juu yako laana mpaka siku ya malipo.
Humo, ni humo mwenye daraja ya juu. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu alimfukuza Iblisi kutoka kwenye rehema yake hadi kwenye adhabu yake na akamfanya ni maluuni kwa ndimi zote mpaka siku ya Kiyama, ikiwa ni malipo ya kiburi chake na kuacha kwake kumtii Mwenyezi Mungu.
Akasema (Iblisi): “Mola wangu! Nipe muda mpaka siku watakapofufuliwa.
Alitaka muda huu kwa haja yake aliyoikusudia, tutakayoifafanua mbele(Mwenyezi Mungu) akasema: Basi hakika wewe ni katika waliopewa muda mpaka siku ya wakati maalum.
Hiyo ni siku ya kupuliziwa parapanda ambayo inafahamishwa na Aya isemayo:
وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَصَعِقَ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَمَن فِي الْأَرْضِ ﴿٦٨﴾
“Na itakapopuziwa parapanda wazimie waliomo mbinguni na waliomo ardhini” (39:68)
Akasema (Iblisi): Kwa ulivyonipoteza,
Yaani kwa sababu ya kunitia mtihani wa amri ya kumsujudia Adam ambayo imeniingiza katika upotevu na uasi,basi nitahakikisha ninawazaini hapa ardhini na nitawapoteza wote, isipokuwa waja wako waliosafishwa.
Iblisi alichukua ahadi ya kuchukua kisasi cha maafa yake kwa kiumbe hiki kilichokuwa ni sababu ya kufukuzwa kwake kutoka rehema ya Mola wake hadi kwenye laana yake.
Akasema (Mwenyezi Mungu): Hii ni njia juu yangu mimi iliyonyooka.
Hii ni ishara ya kujichunga wale wenye ikhlasi kutokana na shetani na upotevu wake.
Juu yangu mimi, yaani ni yenye kuthibiti kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu; mfano kauli yake Mwenyezi Mungu: “Mola wenu amejilazimisha rehema, Juz, 7 (6:54).
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amejilazimishia kwamba ikhlasi ndiyo njia ya kunyooka. Mwenye kuifuata ataokoka na mwenye kukengeuka nayo ameangamia.
Hakika waja wangu hutakuwa na mamlaka nao, isipokuwa wale wapotofu waliokufuata.
Wale wanaoabudu pesa wakiuza dini na nchi kwa kila atakayetoa pesa. Ama wale wema wenye ikhlasi, hawawezi hata kusogelewa na Iblisi, sikwambii kuwa na mamlaka nao. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz, 8 (7:11- 18).
Na hakika Jahannam ndipo mahali pao walipoahidiwa wote.
Huko kwenye shimo la Jahannam watakutana wote, Iblisi na wafuasi wake. Kila mmoja atamlaani mwenzake na kumkana; mfuaswa atamkana mfuasi, Kwa maelezo zaidi angalia kifungu cha ‘Hotuba ya shetani’ katika Juz. 13 (14:22)
Ina milango saba, kila mlango una sehemu waliyotengewa.
Imesemekana kuwa makusudio ya milango ni milango hasa kwa maana ya tamko lenyewe. Wengine wakasema makusudio ni tabaka na kwamba baadhi ya moto uko juu ya baadhi ya mwingine; na kuwa kila tabaka ina jina lake inalolihusu; kama vile Jahnnam, Jahim, Ladhaa, Saqar, Hutama n.k.
Vyovyote yatakavyokuwa makusudio, hali halisi inajulikana; kwamba maovu yana daraja; kuna yaliyo makubwa ya hatari, yaliyo madogo yasiyo na hatari na yale ya katikati, Kila ovu lina adhabu yake inayolistahili bila ya kuzidi, Tumefafanua katika Juz, 13 (46 – 52), Kifungu cha ‘Jahannam na silaha za maangamizi.
إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ ﴿٤٥﴾
45. Hakika wenye takua watakuwa katika Bustani (Pepo) na chemchemi.
ادْخُلُوهَا بِسَلَامٍ آمِنِينَ ﴿٤٦﴾
46. (Wataambiwa): Ingieni kwa salama mkiwa na amani.
وَنَزَعْنَا مَا فِي صُدُورِهِم مِّنْ غِلٍّ إِخْوَانًا عَلَىٰ سُرُرٍ مُّتَقَابِلِينَ ﴿٤٧﴾
47. Na tutaondoa chuki iliyokuwamo vifuani mwao wawe ndugu, juu ya viti wakielekeana.
لَا يَمَسُّهُمْ فِيهَا نَصَبٌ وَمَا هُم مِّنْهَا بِمُخْرَجِينَ ﴿٤٨﴾
48. Humo hayatawagusa machovu wala hawatatolewa humo.
نَبِّئْ عِبَادِي أَنِّي أَنَا الْغَفُورُ الرَّحِيمُ ﴿٤٩﴾
49. Watanabahishe waja wangu ya kwamba mimi ndiye Mwenye kughufiria, mwenye kurehemu.
وَأَنَّ عَذَابِي هُوَ الْعَذَابُ الْأَلِيمُ ﴿٥٠﴾
50. Na kwamba adhabu yangu ndiyo adhabu iliyo chungu.
Aya 45 – 50
Bada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja adhabu ya wakosefu na wale waliopotea, na kwamba wao watafufuliwa kesho huku nyuso zao zikiwa zimegubikwa na moto tena wakiwa na nguo za moto, amefuatishia kwa kutaja malipo ya wenye takua, wacha Mungu. Kwamba wao watalipwa raha starehe amani na usafi wa kila aina, kwa ufafanuzi ufuatao:
1.Hakika wenye takua watakuwa katika Bustani (Pepo) na chemchemi.
Maisha ni mazuri katika kila kitu, kuanzia vyakula hadi vinywaji na mandhari hadi Hurulaini.
وَفِيهَا مَا تَشْتَهِيهِ الْأَنفُسُ وَتَلَذُّ الْأَعْيُنُ ﴿٧١﴾
Kuna vinavyopendwa na nafsi na kufurahiwa na macho (43:71).
2.(Wataambiwa): Ingieni kwa salama mkiwa na amani.
Maisha mazuri ya amani yasiyokuwa na hofu wala huzuni
Na tutaondoa chuki iliyokuwamo vifuani mwao wawe ndugu, juu ya viti wakielekeana.
Hata starehe pia ni safi, hakuna chuki zinazochemka nyoyoni; kama ilivyo kwa watu wa motoni, alipowasifu Mwenyezi Mungu kwa kauli yake: “Kila utakapoingia umma utalaani ndugu zake. Juz.8 (7:38).
3.Humo hayatawagusa machovu wala hawatatolewa humo.
Hakuna ufukara, maradhi, hofu wala chuki, Pia hakuna tabu wala kuchoka, Sifa zote hizi ni za kudumu, haziondoki wala kupungua.
Watanabahishe waja wangu ya kwamba mimi ndiye Mwenye kughufiria, mwenye kurehemu, na kwamba adhabu yangu ndiyo adhabu iliyo chungu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekutanisha, katika Aya mbili hizi, bishara na hadhari, ili muasi asikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu na maghufira yake, bali arejee na atubie kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu na ili awe na hadhari mtiifu kutokana na makosa na ufisadi, na awe mnyenyekevu; wala asijitie majivuno na ghururi. Razi anasema: “Mwenyezi Mungu alipotaja maghufira na rehema alilisisitiza sana kwa matamshi matatu: ‘Hakika mimi, mimi na kuingiza alif na lam katika neno la kiarabu al-ghafur (mwenye kughufiria). Lakini alipotaja adhabu hakusema hakika mimi wala mimi; bali amesema: hakika adhabu yangu.
3
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
وَنَبِّئْهُمْ عَن ضَيْفِ إِبْرَاهِيمَ ﴿٥١﴾
51. Na watanabahishe kuhusu wageni wa Ibrahim.
إِذْ دَخَلُوا عَلَيْهِ فَقَالُوا سَلَامًا قَالَ إِنَّا مِنكُمْ وَجِلُونَ ﴿٥٢﴾
52. Walipoingia kwake wakasema: “Salaam.” Akasema: “Hakika sisi tunawaogopa.”
قَالُوا لَا تَوْجَلْ إِنَّا نُبَشِّرُكَ بِغُلَامٍ عَلِيمٍ ﴿٥٣﴾
53. Wakasema: Usiogope, Sisi tunakubashiria (kupata) kijana mwenye ujuzi.
قَالَ أَبَشَّرْتُمُونِي عَلَىٰ أَن مَّسَّنِيَ الْكِبَرُ فَبِمَ تُبَشِّرُونَ ﴿٥٤﴾
54. Akasema: “Mnanibashira na uzee umenishika! Basi mnanibashiria kwa lipi?
قَالُوا بَشَّرْنَاكَ بِالْحَقِّ فَلَا تَكُن مِّنَ الْقَانِطِينَ ﴿٥٥﴾
55. Wakasema: “Tunakubashiria kwa haki, basi usiwe miongoni mwa wanaokata tamaa.”
قَالَ وَمَن يَقْنَطُ مِن رَّحْمَةِ رَبِّهِ إِلَّا الضَّالُّونَ ﴿٥٦﴾
56. Akasema: “Na ni nani anayekata tamaa na rehema ya Mola wake isipokuwa wale waliopotea.”
قَالَ فَمَا خَطْبُكُمْ أَيُّهَا الْمُرْسَلُونَ ﴿٥٧﴾
57. Akasema: “Nini kusudio lenu enyi wajumbe?”
قَالُوا إِنَّا أُرْسِلْنَا إِلَىٰ قَوْمٍ مُّجْرِمِينَ ﴿٥٨﴾
58. Wakasema: “Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu.
إِلَّا آلَ لُوطٍ إِنَّا لَمُنَجُّوهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٥٩﴾
59. Isipokuwa familia ya Lut, hakika tutawaokoa wote.
إِلَّا امْرَأَتَهُ قَدَّرْنَا إِنَّهَا لَمِنَ الْغَابِرِينَ ﴿٦٠﴾
60. Isipokuwa mkewe tumekadiria kuwa miongoni mwa watakaobakia nyuma.
Aya 51 – 60
Na watanabahishe kuhusu wageni wa Ibrahim.
Maneno haya anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) na wanotanabahishwa ni waja wa Mwenyezi Mungu waliotajwa katika Aya iliyotangulia. Wageni wa Ibrahim ni Malaika waliokuja kwake.
Walipoingia kwake wakasema: Salaam.
Waliingia kwake wakamsalimia naye akawarudishia salaam; kama ilivy- oelezwa katika Juz. 12: (11:69).
Akasema: Hakika sisi tunawaogopa.
Kwa sababu aliwaletea chakula wakakikataa.
Wakasema: “Usiogope. Sisi tunakubashiria (kupata) kijana mwenye ujuzi, ambaye atakuwa na shani.
وَبَشَّرْنَاهُ بِإِسْحَاقَ نَبِيًّا مِّنَ الصَّالِحِينَ ﴿١١٢﴾
Na tukamabashiria Is-haq, nabii miongoni mwa watu wema, (37:112).
Akasema: “Mnanibashira na uzee umenishika! Basi mnanibashiria kwa lipi?
Ibrahim hakuyasema haya kwa kutilia mashaka uwezo wa Mwenyezi Mungu wala kukata tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu; bali ni kwa kusisitiza ili atulie.
Wakasema: Tunakubashiria kwa haki, basi usiwe miongoni mwa wanaokata tamaa.
Malaika walidhani kuwa Ibrahim ni katika wanokata tamaa kutokana na swali lake. Ilifaa wadhanie hivyo, lakini Nabii Ibrahim aliikana dhana yao hiyo Akasema:
Na ni nani anayekata tamaa na rehema ya Mola wake isipokuwa wale waliopotea.
Kauli yake hii ni dalili mkataa kuwa yeye hakuuliza kwa kutilia shaka wala kukata tamaa; bali ni kusisitiza na kuthibitisha. Mahali pengine alisema: “Lakini upate kutulia moyo wangu. Juz.3 (2:260).
Akasema: Nini kusudio lenu enyi wajumbe?
Yaani ni jambo gani muhimu mlilotumiwa zaidi ya bishara mliyonipa.
Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwa kaumu ya wakosefu ambayo ni watu wa Lutisipokuwa familia ya Lut hakika tutawaokoa wote ambao ni watu wake wanomuhusu na wafuasi wake waumini.
Isipokuwa mkewe tumekadiria kuwa miononi mwa watakaobakia nyuma.
Mwenyezi Mungu alimwangamiza pamoja na walioangamia, kwa sababu alikuwa mnafiki akimpangia njama mumewe Lut pamoja na maadui zake washirikina. Umetangulia mfano wa Aya hizi katika Juz .12 (11: 69 – 74)
فَلَمَّا جَاءَ آلَ لُوطٍ الْمُرْسَلُونَ ﴿٦١﴾
61. Basi wajumbe walipokuja kwa familia ya Lut.
قَالَ إِنَّكُمْ قَوْمٌ مُّنكَرُونَ ﴿٦٢﴾
62. Alisema: Nyinyi ni watu msiojulikana.
قَالُوا بَلْ جِئْنَاكَ بِمَا كَانُوا فِيهِ يَمْتَرُونَ ﴿٦٣﴾
63. Wakasema: “Bali tumekuletea yale waliyokuwa wakiyafanyia shaka.
وَأَتَيْنَاكَ بِالْحَقِّ وَإِنَّا لَصَادِقُونَ ﴿٦٤﴾
64. Na tumefika kwako kwa haki na hakika tunasema kweli.
فَأَسْرِ بِأَهْلِكَ بِقِطْعٍ مِّنَ اللَّيْلِ وَاتَّبِعْ أَدْبَارَهُمْ وَلَا يَلْتَفِتْ مِنكُمْ أَحَدٌ وَامْضُوا حَيْثُ تُؤْمَرُونَ ﴿٦٥﴾
65. Ondoka na Ahali zako na usiku ungalipo nawe ufuate nyuma yao, wala yeyote kati yenu asigeuke nyuma, Na mwende mnapoamrishwa.
وَقَضَيْنَا إِلَيْهِ ذَٰلِكَ الْأَمْرَ أَنَّ دَابِرَ هَـٰؤُلَاءِ مَقْطُوعٌ مُّصْبِحِينَ ﴿٦٦﴾
66. Na tukampa wahyi hukumu hiyo, ya kwamba wa mwisho wao ikifika asubuhi atakuwa amekatiliwa mbali.
وَجَاءَ أَهْلُ الْمَدِينَةِ يَسْتَبْشِرُونَ ﴿٦٧﴾
67. Wakaja watu wa mji huo wakifurahi.
قَالَ إِنَّ هَـٰؤُلَاءِ ضَيْفِي فَلَا تَفْضَحُونِ ﴿٦٨﴾
68. Akasema: “Hakika hawa ni wageni wangu, basi msinifedheheshe.
وَاتَّقُوا اللَّـهَ وَلَا تُخْزُونِ ﴿٦٩﴾
Na mcheni Mwenyezi Mungu, wala msinihizi.
قَالُوا أَوَلَمْ نَنْهَكَ عَنِ الْعَالَمِينَ ﴿٧٠﴾
70. Wakasema: Je hatukukataza na watu.
قَالَ هَـٰؤُلَاءِ بَنَاتِي إِن كُنتُمْ فَاعِلِينَ ﴿٧١﴾
71. Akasema: “Hawa binti zangu ikiwa nyinyi ni watendaji.”
لَعَمْرُكَ إِنَّهُمْ لَفِي سَكْرَتِهِمْ يَعْمَهُونَ ﴿٧٢﴾
72. Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao wakimangamanga.
Aya 61 – 72
Mwenyezi Mungu (s.w.t) hukariri visa vya mitume na upinzani uliowa- tokea na jinsi walivyoweza kusimama imara na ujumbe wao, ili watu wapate funzo na mawaidha kutokana na mwisho wa wakadhibishaji ulivyokuwa. Kila lililoelezwa katika Aya hizi tulizo nazo litakuwa limeelezwa kwa ufafanuzi katika sura ya Hud iliyoko katika Juz. 12. Vilevile maelezo ya Nabii Ibrahim(a.s) yaliyopita punde tu. Kwa ajili hii tutafupiliza kufasiri Aya hizi; kama tulivyofupiliza Aya zilizotangulia.
Basi wajumbe walipokuja kwa familia ya Lut.
Malaika walitoka kwa Ibrahim na wakaelekea kwa Lut. Walipofika kwake kwa kuwafikiria kuwa ni wageni, aliona dhiki sana kutokana na uovu wa kaumu yake.
Alisema: “Nyinyi ni watu msiojulikana siwajui wala sijui mnataka nini. Mmeingiaje mjii huu na wenyeji wake wanajulikana wanayoyafanya?
Wakasema: Bali tumekuletea yale waliyokuwa wakiyafanyia shaka na tumefika kwako kwa haki na hakika tunasema kweli.
Malaika walimfichulia Lut hakika yao na umuhimu waliokuja nao ambo ni kuwaangamiza kaumu ya Lut.Walikuwa wakiwaendea wanaume kwa matamanio badala ya wanawake. Mtume wao Lut alikuwa akiwahadharisha na kuwaonya na adhabu itakayotokea mbinguni.
Malaika wakamwambia Lut: Tumekuja na adhabu uliyokuwa ukiwahadharisha nayo na kukukadhibisha na kwamba hiyo adhabu itatokea tu.
Ondoka na watu wako na usiku ungalipo nawe ufuate nyuma yao, wala yeyote kati yenu asigeuke nyuma, Na mwende mnapoamrishwa.
Baada ya kumpa habari ya kutokea adhabu, alimwamrisha kujiokoa yeye na watu wake. Kwa kutoka usiku kabla ya asubuhi na yeye awe nyuma yao akiwaangalia na kuwatunza na kwamba asigeuke nyuma yeyote asije akaona adhabu akafazaika.
Na tukampa wahyi hukumu hiyo, ya kwamba wa mwisho wao ikifika asubuhi atakuwa amekatiliwa mbali.
Mwenyezi Mungu alimpa wahyi Lut kwamba kufkia asubuhi atakuwa amewafyeka makafiri hadi wa mwisho wao, hakutabakia hata chembe.
Wakaja watu wa mji huo wakifurahi.
Wale mafasiki walikuja kwa wageni wa Lut wakipeana habari ya furaha kuwa wamepata nyara mpya. Uso wa Lut ukasawijika kwa kuwa hajawajua hasa wageni wake. Akawakabili kwa upole,Akasema: Hakika hawa ni wageni wangu, basi msinifedheheshe na mumche Mwenyezi Mungu wala msinihizi.
Aliwahofisha na Mwenyezi Mungu ingawaje kwao si chochote na akawataka wawe na murua kwa kutomfedhehesha na wageni wake ingawaje walikuwa ni watu wasiokuwa na murua wala utu kabisa.
Wakasema: Je hatukukukataza na watu?
Yaani hatukukukataza kukaribisha watu wa nje? Angalia upuzi na ushenzi huu. Eti wao ndio wasiokuwa na kosa na Lut ndiye mwenye kosa, kwa vile wao walimkataza asikaribishe wageni na hakukoma! Je hatukukukataza!
Mantiki haya ya watu wa Lut ndio mantiki ya kila wachokozi. Sikuzote, hawana kipimo isipokuwa matakwa yao na manufaa yao. Wavietnam wamegeuka kuwa ndio wamwaga damu na wavunja amani kwa Wamarikani kwa vile tu wamekataa kutawaliwa na USA.
Waarabu wamekuwa magaidi na wanyama kwa Marekani na Uingereza kwa vile tu wanasema Palestina ni ya Wapalestina sio ya Wazayuni. Dola za kikoloni zinadai usalama na amani wakati zikiwapiga makombora na mabomu ya sumu wanyonge kwenye nchi zao.
Akasema: Hawa binti zangu, ikiwa nyinyi ni watendaji.
Alileta ibara ya binti zangu, akiwakusudia wanawake wa kaumu yake, kwa sababu Mtume wa umma ni kama baba kwa wanachi wote waume kwa wake.
Lut aliwaambia watu wake waache kuwaendea wanaume na waoe wanawake walio halali, lakini nafsi zao hazioni raha isipokuwa kwa haramu na kupendelea dhambi na uchafu.
Naapa kwa umri wako! Hakika hao walikuwa katika ulevi wao wakimangamanga.
Wafasiri wengi wamesema kuwa msemo wa ‘naapa kwa umri wako’ unatoka kwa Mwenyezi Mungu kuelekea kwa Muhammad(s.a.w.w) . Wengine wakasema unatoka kwa Malaika kuelekea kwa Lut(a.s) . Huenda hii iko karibu zaidi na dhahiri ya mfumo wa maneno. Maana yoyote yatakayokuwa ni kuwa kaumu Lut walizama kwenye upotevu wala hawakuwa na mwelekeo wa kuongoka kwa namna yoyote atakayokuwa muongozaji.
فَأَخَذَتْهُمُ الصَّيْحَةُ مُشْرِقِينَ ﴿٧٣﴾
73. Ukelele ukawanyakuwa wakipambaukiwa.
فَجَعَلْنَا عَالِيَهَا سَافِلَهَا وَأَمْطَرْنَا عَلَيْهِمْ حِجَارَةً مِّن سِجِّيلٍ ﴿٧٤﴾
74. Tukaugeuza (mji) juu chini na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo.
إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّلْمُتَوَسِّمِينَ ﴿٧٥﴾
75. Hakika katika hayo kuna ishara kwa waaguzi.
وَإِنَّهَا لَبِسَبِيلٍ مُّقِيمٍ ﴿٧٦﴾
76. Na hakika mji huo uko kwenye njia, bado iko.
إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٧٧﴾
77. Hakika katika hayo kuna ishara kwa waumini.
وَإِن كَانَ أَصْحَابُ الْأَيْكَةِ لَظَالِمِينَ ﴿٧٨﴾
78. Na hakika watu wa kichakani walikuwa madhalimu.
فَانتَقَمْنَا مِنْهُمْ وَإِنَّهُمَا لَبِإِمَامٍ مُّبِينٍ ﴿٧٩﴾
79. Kwa hiyo tukawaadhibu, Na miwili hiyo iko katika njia iliyo wazi.
وَلَقَدْ كَذَّبَ أَصْحَابُ الْحِجْرِ الْمُرْسَلِينَ ﴿٨٠﴾
80. Na hakika watu wa Hijr waliwakadhibisha Mitume.
وَآتَيْنَاهُمْ آيَاتِنَا فَكَانُوا عَنْهَا مُعْرِضِينَ ﴿٨١﴾
81. Na tuliwapa ishaa zetu nao wakazipuuza.
وَكَانُوا يَنْحِتُونَ مِنَ الْجِبَالِ بُيُوتًا آمِنِينَ ﴿٨٢﴾
82. Na walikuwa wakichonga majumba katika majabali kwa amani.
فَأَخَذَتْهُمُ الصَّيْحَةُ مُصْبِحِينَ ﴿٨٣﴾
83. Ukelele ukawanyakuwa asubuhi.
فَمَا أَغْنَىٰ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٨٤﴾
84. Hayakuwafaa waliyokuwa wakiyachuma.
وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا إِلَّا بِالْحَقِّ وَإِنَّ السَّاعَةَ لَآتِيَةٌ فَاصْفَحِ الصَّفْحَ الْجَمِيلَ ﴿٨٥﴾
85. Na hatukuiumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake ila kwa haki, Na hakika saa itafika, Basi samehe msamaha mzuri.
إِنَّ رَبَّكَ هُوَ الْخَلَّاقُ الْعَلِيمُ ﴿٨٦﴾
86. Hakika Mola wako ndiye Muumbaji, Mjuzi.
Aya 73 – 86
Ukelele ukawanyakuwa wakipambaukiwa.
Yaani adhabu iliwashukia wakati wa mapambazuko. (mawiyo).
Tukaugeuza (mji) juu chini na tukawanyeshea mvua ya mawe ya udongo.
Aya hii imetangulia kwa herufi zake hizi hizi katika Juz. 12. (11:92).
Hakika katika hayo kuna ishara kwa waaguzi.
Makusudio ya waaguzi hapa ni wenye akili ambao wanazingatia na kupata mawaidha.
Na hakika mji huo uko kwenye njia, bado iko.
Yaani athari za mji huo zilikuwako mpaka wakati wa Muhammad(s.a.w.w) na njia ya kwenda huko ilikuwako na kuweza kupitika kwa kila mwenye kutaka kwenda na kushuhudia athari za maangamizi. Wafasiri wanasema mji huo unajulikana kwa jina la Sodom[2] .
Hakika katika hayo kuna ishara kwa waumini.
Yaani wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, wanaitakidi kwamba adhabu waliyoipata kaumu ya Lut ni malipo ya kufuru yao na upotevu wao.
Lakini walahidi wanasema ni matukio ya kawaida tu ya maumbile.
Na hakika watu wa kichakani walikuwa madhalimu.
Makusudio ya watu wa kichakani ni watu wa Shua’yb(a.s) . Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja maangamizi ya kaumu ya Lut, anadokeza kuhusu kaumu ya Shua’yb; kwamba Yeye pia aliwaangamiza kwa sababu ya kufru yao na kuipinga kwao haki, Yametangulia maneno kuhusu Shua’yb katika Juz, 8 (7:85), Vile vile yatakuja maelezo katika Juz 16 kwenye Sura ya Shua’rau.
Kwa hiyo tukawaadhibu. Na miwili hiyo iko katika njia iliyo wazi.
Yaani waliadhibiwa wote kaumu ya Lut na ya Shua’yb na miwili hiyo ni miji ya kaumu ya Lut na Shua’yb. Kwa maana ya kuwa dalili na athari za kuangamia miji miwili hiyo bado ziko na hata njia ya kuendea huko kujionea pia iko tena wazi wazi.
Na hakika watu wa Hijr waliwakadhibisha Mitume.
Watu wa Hijr ni watu wa Nabii Swaleh, mwenye ngamia, Hijr ni jina la mji waliokuwa wakikaa. Mtume waliyemkadhibisha ni mmoja tu, Mtume wao, lakini limekuja neno la wengi, Mitume, kwa vile mwenye kumkadhibisha Mtume mmoja ni kama amekadhibisha Mitume yote.
Na tuliwapa ishara zetu nao wakazipuuza ingawaje zilikuwa na dalili za kutosha kuhusu haki, lakini kwa vile zilikuwa haziafikiani na hawa zao na kuigiza kwao ufisadi.
Na walikuwa wakichonga majumba katika majabali kwa amani.
Walikuwa wakikaa katika majumba ya mawe wakiwa na amani ya vita, kuonyesha kuwa walikuwa kwenye maendeleo wakati huo. Miongoni mwa ishara alizowaletea Mwenyezi Mungu mikononi mwa Mtume ni ngamia waliyemchinja huku wakijigamba kwa kusema:
يَا صَالِحُ ائْتِنَا بِمَا تَعِدُنَا إِن كُنتَ مِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٧٧﴾
“Ee Swaleh! Tuletee unayotuahidi ikiwa wewe ni miongoni mwa Mitume. Jz. 8 (7:77).
Ukelele ukawanyakuwa asubuhi Yaani adhabu iliwafikia wakati wa asubuhi.
Hayakuwafaa waliyokuwa wakiyachuma.
Adhabu iliwafikia, lakini utajiri wao, majengo na makasri waliyoyajenga kwa mawe hayakuweza kuizuia. Umetangulia ufafanuzi wa Swaleh(a.s) na kaumu yake katika Juz.8 (7: 73).
Na hatukuiumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake ila kwa haki.
Hakuna kitu chochote kilichopo ila kina hekima yake; kukiwemo kuangamia kwa makafiri katika umma uliotangulia. Katika maana ya Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t):
وَمَا خَلَقْنَا السَّمَاءَ وَالْأَرْضَ وَمَا بَيْنَهُمَا بَاطِلًا ﴿٢٧﴾
Hatukuiumba mbingu na ardhi na vilvyomo baina yake bure (38: 27).
Na hakika saa itafika.
Makusudio ya saa hapa ni Kiyama, wakati huo atalipwa kila mmoja stahiki yake.
Basi samehe msamaha mzuri.
Maneno yanaelekezwa kwa Muhammad, akiamrishwa kuachana na washirikina na wajinga na kutojishughulisha nao. Katika maana ya Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu (s.w.t): “Na vumilia na wayasemayo na jitenge nao kwa uzuri” (73: 10).
وَلَقَدْ آتَيْنَاكَ سَبْعًا مِّنَ الْمَثَانِي وَالْقُرْآنَ الْعَظِيمَ ﴿٨٧﴾
87. Na hakika tumekupa Aya saba zinaazorudiwa rudiwa na Qur’an Tukufu.
لَا تَمُدَّنَّ عَيْنَيْكَ إِلَىٰ مَا مَتَّعْنَا بِهِ أَزْوَاجًا مِّنْهُمْ وَلَا تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَاخْفِضْ جَنَاحَكَ لِلْمُؤْمِنِينَ ﴿٨٨﴾
88. Usikodolee macho yako yale tuliyowastareheshea makundi mbalimbali, Wala usiwahuzunikie. Na inamisha bawa lako kwa Waumini.
وَقُلْ إِنِّي أَنَا النَّذِيرُ الْمُبِينُ ﴿٨٩﴾
89. Na sema: Hakika mimi ni muonyaji niliye dhahiri.
كَمَا أَنزَلْنَا عَلَى الْمُقْتَسِمِينَ ﴿٩٠﴾
90. Kama tulivyowateremshia waliojigawanya.
الَّذِينَ جَعَلُوا الْقُرْآنَ عِضِينَ ﴿٩١﴾
91. Ambao wameipiga pande Qur’an.
فَوَرَبِّكَ لَنَسْأَلَنَّهُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٩٢﴾
92. Naapa kwa Mola wako wataulizwa wote.
عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٩٣﴾
93. Yale waliyokuwa wakiyatenda.
فَاصْدَعْ بِمَا تُؤْمَرُ وَأَعْرِضْ عَنِ الْمُشْرِكِينَ ﴿٩٤﴾
94. Basi yatangaze uliyoamrishwa na achana na washirikina.
إِنَّا كَفَيْنَاكَ الْمُسْتَهْزِئِينَ ﴿٩٥﴾
95. Hakika sisi tunakutosha na wafanyao isthizai.
الَّذِينَ يَجْعَلُونَ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ فَسَوْفَ يَعْلَمُونَ ﴿٩٦﴾
96. Wale wanaofanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu yuko Mungu mwingine, basi watajua.
وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّكَ يَضِيقُ صَدْرُكَ بِمَا يَقُولُونَ ﴿٩٧﴾
97. Na kwa hakika sisi tunajua kuwa kifua chako kinadhikika na yale wanayoyasema.
فَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ وَكُن مِّنَ السَّاجِدِينَ ﴿٩٨﴾
98. Basi msabihi Mola wako kwa sifa njema na uwe miongoni mwa wanaosujudi.
وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ ﴿٩٩﴾
99. Na mwabudu Mola wako mpaka ikufikie yakini.
Aya 87 – 99
Saba zinazorudiwa, ni Sura ya Fatiha, kwa vile ina Aya saba na inarudiwa kusomwa katika Swala. Imesemekana kuwa imeitwa saba kwa vile inazianzia Sura saba ndefu za mwanzo katika Qur’an ambazo ni: Al-baqara, Al-imran, An-nisaa, Al-maidah, Al-an’am, Al-a’raf na Yunus (2, 3, 4, 5, 6, 7, 8); kama ilivyoelezwa katika Tafsir At-tabari. Au Al-anfal pamoja na At-tawba; kama ilivyoelezwa katika tafsiri nyingine.
Na hakika tumekupa Aya saba zinaazorudiwa rudiwa na Qur’an Tukufu.
Wametofautiana katika makusudio ya saba zinaazorudiwa. Wafasiri wametaja kauli tano, lakini yenye nguvu zaidi ni ile inayosema kuwa ni Sura ya Fatiha. Kwani ina Aya saba na kwenye swala inarudiwa na imeku- sanya mambo mawili ya Mungu na Ibada.
Usikodolee macho yako yale tuliyowastareheshea makundi mbalimbali.
Makusudio ya makundi mbalimbali hapa ni makafiri, washirikina na watu wa kitabu. Kwa maneno mengine ni aina zote za makafiri. Maana ni kuwa usiangalie au usishughulike na starehe wanazokuwa nazo makafiri katika washirikina na watu wa kitabu.
Wala usiwahuzunikie.
Mtume(s.a.w.w) alikuwa akihuzunika na kuona uchungu sana kutokana na washirikina kukosa kuamini. Ndipo Mola Mtukufu akamwamrisha Mtume, lisimshghulishe hilo wala kumpa majonzi:
فَلَا تَذْهَبْ نَفْسُكَ عَلَيْهِمْ حَسَرَاتٍ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِمَا يَصْنَعُونَ ﴿٨﴾
“Basi roho yako isitoke kwa majonzi juu yao; hakika Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyafanya.” (35:8).
Na inamisha bawa lako kwa waumini.
Wanyenyekee waumini, kwani kuwanyenyekea hao ni kumnyenyekea Mwenyezi Mungu. Na kuwafanyia kiburi wahaini waliowafisadi ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu:
أَذِلَّةٍ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ أَعِزَّةٍ عَلَى الْكَافِرِينَ ﴿٥٤﴾
“Wanyenyekevu kwa waumini, wenye nguvu juu ya makafiri” Juz. 6: (5:54).
Na sema: Hakika mimi ni muonyaji niliye dhahiri.
Muhammad(s.a.w.w) aliwalingania watu kwa hoja na ubainifu, na bado mwito wake pamoja na hoja na dalili zake ziko mpaka leo na mpaka siku ya mwisho. Kwa hiyo kila mwenye akili anapaswa kuziangalia na kuzichunguza.
Akiziamini atakuwa ameziamini kwa hoja na akizikataa atakuwa ameziakataa kwa hoja, Ama yule mwenye kuzikimbia bila ya kuziangalia basi huyo ana lawama.
Kama tulivyowateremshia waliojigawanya ambao wameipiga pande Qur’an.
Makusudio ya waliojigawanya ni Mayahudi, kwani hao ndio walioigawa Qur’an vipande kwa kuamini baadhi na kupinga baadhi. Wanapinga yale yanayogongana na masilahi yao na maigizo yao na wakaamini yasiyokuwa hayo.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu ameteremsha Qur’an kwa Muhammad(s.a.w.w) , kama alivyoiteremsha Tawrat kwa Mayahudi na Injili kwa manaswara ambao waliamini sehemu ya Qur’an na wakaipinga sehemu nyingine. Basi kuna ajabu gani kwa Muhammad kuteremshiwa kitabu kutoka kwa Mola wake ambaye alikwishateremsha vitabu kabla yake?
Naapa kwa Mola wako wataulizwa wote yale waliyokuwa wakiyatenda.
Qur’an hapa imethibitisha majukumu ya mtu kwenye matendo yake; kama ambavyo katika Aya nyingine imethibitisha majukumu katika kauli na nyingine ikathibitisha majukumu katika makusudio na maazimio:
مَّا يَلْفِظُ مِن قَوْلٍ إِلَّا لَدَيْهِ رَقِيبٌ عَتِيدٌ ﴿١٨﴾
Hatamki kauli yoyote isipokuwa karibu yake yuko mngojeaji aliye tayari (50:18).
يَعْلَمُ خَائِنَةَ الْأَعْيُنِ وَمَا تُخْفِي الصُّدُورُ ﴿١٩﴾
“Anajua hiyana ya macho na yanayoficha vifua” (40:19).
Kwa hiyo mtu atakapojua kuwa kuna anayemfuatilia, aliye na uwezo na mwadilifu, basi ataogopa na kuwa na takua. Ni vigumu kuweko nidhamu ya kibinadamu bila ya mtu kutambua majukumu na uwajibikaji wake.
Basi yatangaze uliyoamrishwa na achana na washirikina.
Lingania Mola wako kwa hoja na dalili wala usimjali anayekupinga na akakupa mgongo.
Hakika sisi tunakutosha na wafanyao isthizai, wale wanaofanya kuwa pamoja na Mwenyezi Mungu yuko Mungu mwingine, basi watajua.
Wafasiri, akiwemo Tabari, Razi na Tabrasi, wamesema kuwa jamaa wa kiqurayshi waliokuwa na nguvu walikuwa wakimdharau na kumcheza shere Mtume(s.a.w.w) , Mwenyezi Mungu akawaangamiza kwa sababu ndogo na nyepesi. Miongoni mwao ni Walid bin Al-mughira, Asi bin Wail, Uday bin Qays na As-wad bin Abd yaghuth.
Na kwa hakika sisi tunajua kuwa kifua chako kinadhikika kwa yale wanayoyasema. Basi msabihi Mola wako kwa sifa njema na uwe miongoni mwa wanaosujudi.
Ni kawaida Mtume kuhuzunika na kuona uchungu pale Washirikina wanapomdharau na kumwambia ni mwendawazimu au anamzulia Mungu. Vile vile ni kawaida kifua chake kidhikike na yale wayasemayo makafiri kwa sababu yeye ni binadamu kwa nyama na damu. Anafurahi kwa yale wanayoyafurahia watu na anahuzunika kwa yale wayahuzinikiayo watu.
Lakini kuna uhusiano gani baina ya huzuni na ibada ambayo Mwenyezi Mungu amemwamrisha kuikimbilia anapohuzunika na kudhikika kifua chake?
Jibu : Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakumwamrisha Mtume wake ibada hapa ili ambainishie kuwa kudhikika kifua ndio sababu ya amri ya ibada, hapana! Hakika amri ya ibada ya Mwenyezi Mungu haifungamani na furaha wala huzuni; isipokuwa amri ya ibada hapa ni fumbo la kumtegemea Mwenyezi Mungu peke yake, pale anapopata machungu na kuhuzunika; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
وَإِمَّا يَنزَغَنَّكَ مِنَ الشَّيْطَانِ نَزْغٌ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ إِنَّهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٢٠٠﴾
Na kama uchochezi wa shetani ukikuchochea, basi jikinge kwa Mwenyezi Mungu, Hakika yeye ndiye asikiaye na ajuaye. Juz; 9 (7:200).
Angalia huko utapata ufafanuzi zaidi.
Na mwabudu Mola wako mpaka ikufkie yakini.
Makusudio ya yakini hapa ni mauti kwa sababu hayana budi kutokea. Kwa maana ya kuwa mtu aendelee na ibada ya Mwenyezi Mungu na kumfanyia ikhlasi maisha yake yote:
وَأَوْصَانِي بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ مَا دُمْتُ حَيًّا ﴿٣١﴾
Na ameniusia Swala na Zaka maadamu ningali hai (19:31).
4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
Sura Ya Kumi na Sita: Surat An Nahl.
Sura Annahl (Nyuki) Ina Aya 128.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu.
أَتَىٰ أَمْرُ اللَّـهِ فَلَا تَسْتَعْجِلُوهُ سُبْحَانَهُ وَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿١﴾
1. Imefika amri ya Mwenyezi Mungu msiifanyie haraka. Ametakata na kutukuka kuliko vile wanavyovishirkisha.
يُنَزِّلُ الْمَلَائِكَةَ بِالرُّوحِ مِنْ أَمْرِهِ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ أَنْ أَنذِرُوا أَنَّهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاتَّقُونِ ﴿٢﴾
2. Huwateremsha Malaika na roho kwa amri yake juu ya anayemtaka katika waja wake; kwamba onyeni kuwa hakuna Mola aabudiwaye isipokuwa mimi tu, basi niogopeni.
خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِالْحَقِّ تَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٣﴾
3. Ameumba mbingu na ardhi kwa haki, ametukuka kuliko vile wanavyovishirkisha.
خَلَقَ الْإِنسَانَ مِن نُّطْفَةٍ فَإِذَا هُوَ خَصِيمٌ مُّبِينٌ ﴿٤﴾
4. Amemuumba mtu kwa tone la manii, mara amekuwa hasimu aliye dhahiri.
Aya 1 – 4
Badhi ya Aya za sura hii zimeshuka Makka na nyingine zimeshuka Madina. Wametofautiana katika idadi ya Aya za Makka na zile za Madina. Ikasemekana kuwa kuanzia ya kwanza hadi ya arobaini ni za Makka na zilizobaki ni za Madina, Pia ikasemekana kuwa zote zilishuka Makka isipokuwa tatu za mwisho.
Imefika amri ya Mwenyezi Mungu msiifanyie haraka, Ametakata na kutukuka kuliko vile wanavyovishirkisha.
Mtume alikuwa akiwaonya washirikina na kuwahofisha na adhabu kali, lakini wao walikuwa wakimjibu kwa dharau huku wakisema:
فَأَمْطِرْ عَلَيْنَا حِجَارَةً مِّنَ السَّمَاءِ أَوِ ائْتِنَا بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٣٢﴾
“Basi tupige mvua ya mawe kutoka mbinguni au tuletee adhabu iumizayo, ” Juzl 9 (8:32).
Basi Mwenyezi Mungu akawajibu kuwa adhabu itakuja na kila lijalo liko karibu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameleta ibara ya kitendo kilichopita ‘imefika’ kwa maana ya kuwa itafika, kwa kufahamisha kuwa hakuna budi kutokea kwake. Kila ambalo linawajibika kutokea basi ibara yoyote itakayoelezewa iwe ya kupita ya sasa au ya muda ujao itakuwa sawa tu. Kesho wataambiwa:
هَـٰذَا الَّذِي كُنتُم بِهِ تَسْتَعْجِلُونَ ﴿١٤﴾
“Haya ndiyo yale mliyokuwa mkiyaharakishia” (51:14).
Hawatakuwa na jibu isipokuwa kusema:
يَا وَيْلَنَا قَدْ كُنَّا فِي غَفْلَةٍ مِّنْ هَـٰذَا بَلْ كُنَّا ظَالِمِينَ ﴿٩٧﴾
“Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa tumeghafilika na haya; bali tulikuwa wenye kudhulumu.” (21:97).
Huwateremsha Malaika na roho kwa amri yake juu ya anayemtaka katika waja wake; kwamba onyeni kuwa hakuna Mola aabudiwaye isipokuwa mimi tu, basi niogopeni.
Makusudio ya roho hapa ni wahyi, kwa sababu wenyewe ni kwa ajili ya nafsi, sawa na roho kwa ajili ya mwili. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu anachagua anayestahiki risala yake.
Na risala yenyewe kwa ufupi ni Tawhid kiitikadi na msimamo kimatendo. Kwa sababu kila mwenye kumcha Mwenyezi Mungu basi yuko katika njia ya amani iliyo na msimamo na kila mwenye kumwasi yuko katika njia ya maangamivu na upotevu.
Ameumba mbingu na ardhi kwa haki, ametukuka kuliko vile wanavyovishirkisha.
Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja, katika Aya iliyotangulia, kuwa hakuna mola isipokuwa Yeye, katika Aya hii, ameishiria dalili ya hilo; kuwa Mwenyezi Mungu ameziumba mbingu na ardhi na akazipangilia bila ya kuwa na msaidizi yeyote. Kuumba bila ya kutumia nyenzo yoyote ni dalili ya uungu; kama ambavyo kuwa Peke Yake katika kuumba ni dalili ya umoja. Tazama Juz. 5 (4:48) kifungu cha ‘Dalili ya umoja na utatu’
Amemuumba mtu kwa tone la manii, mara amekuwa hasimu aliye dhahiri.
Baada ya Mwenyezi Mungu kuashiria dalili ya umoja anasema, lakini binadamu huyu dhaifu tuliyemuumba kwa tone anakufuru neema ya aliyemneemesha na anapinga kuweko aliyemleta; huku akiabudu yale yasiyodhuru wala kunufaisha.
Yametangulia maelezo mara nyingi sana kwamba mtu hawi kombo ila kwa ujinga na ugizaji au kwa manufaa binafsi. Tazama Juz, 13 (14: 34) Kifungu ‘je mtu ana maumbile ya hatia?.
وَالْأَنْعَامَ خَلَقَهَا لَكُمْ فِيهَا دِفْءٌ وَمَنَافِعُ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ ﴿٥﴾
5. Na wanyama amewaumba, katika hao mnapata joto na manufaa na wengine mnakula.
وَلَكُمْ فِيهَا جَمَالٌ حِينَ تُرِيحُونَ وَحِينَ تَسْرَحُونَ ﴿٦﴾
6. Na mnaona raha mnapowarudisha jioni na mnapowapeleka asubuhi.
وَتَحْمِلُ أَثْقَالَكُمْ إِلَىٰ بَلَدٍ لَّمْ تَكُونُوا بَالِغِيهِ إِلَّا بِشِقِّ الْأَنفُسِ إِنَّ رَبَّكُمْ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٧﴾
7. Na hubeba mizigo kupeleka kwenye mji msiyoweza kuifikia ila kwa mashaka ya nafsi. Hakika Mola wenu ni Mpole sana, Mwenye kurehemu.
وَالْخَيْلَ وَالْبِغَالَ وَالْحَمِيرَ لِتَرْكَبُوهَا وَزِينَةً وَيَخْلُقُ مَا لَا تَعْلَمُونَ ﴿٨﴾
8. Na farasi na nyumbu na punda ili muwapande na pambo, Na anaumba msivyovijua.
وَعَلَى اللَّـهِ قَصْدُ السَّبِيلِ وَمِنْهَا جَائِرٌ وَلَوْ شَاءَ لَهَدَاكُمْ أَجْمَعِينَ ﴿٩﴾
9. Na nijuu ya Mwenyezi Mungu njia iliyo sawa. Na nyingine ni kombo, Lau angelitaka angeliwaongoza nyote.
Aya 5-9
Na wanyama amewaumba, katika hao mnapata joto na manufaa na wengine mnakula.
Wanyama waliokusudiwa ni wale wa kufugwa amabo ni ngamia, ngombe, mbuzi na kondoo.
Qur’an ilishuka wakati ambao maisha ya kilimo na mengineyo yalikuwa hayapangiki bila wanyama. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja aina mbalimbali za wanyama na faida zake katika Aya kadhaa, kwa makusudio ya kumkumbuka Mwenyezi Mungu na neema zake kwa waja wake ili waweze kumcha Yeye katika matendo yao na kauli zao. Miongoni mwa Aya hizo ni: Juz, 8 (6: 143-144).
Katika Aya hii tuliyo nayo Mwenyezi Mungu ametaja faida tatu za wanyama; Joto kwa maana ya mavazi ya kuzuia baridi yanayotokana na ngozi za wanyama, sufu, manyoya yake n.k. Ametaja manufaa, yakiwa ni pamoja na maziwa, samli na kulima. Ama kauli yake ‘mnakula’ ni nyama pamoja na bidhaa za maziwa ambazo pia ni miongoni mwa manufaa.
Na mnaona raha mnapowarudisha jioni na mnapowapeleka asubuhi.
Makusudio ya kuona raha hapa ni kuona raha ya mandhari ya wanyama hasa wakiwa wamenona. Makusudio ya kuwarudisha jioni ni kuwarudisha zizini kutoka malishoni na kuwapeleka asubuhi ni kuwatoa zizini kwenda malishoni. Mandhari haya kwa hakika ni mazuri yanayoleta raha kwenye nafsi.
Na hubeba mizigo kupeleka kwenye mji msiyoweza kuifikia ila kwa mashaka ya nafsi.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja faida ya wanyama kwa chakula na kivazi, hapa anataja kuwa pia wanyama ni nyenzo ya mawasiliano na uchukuzi kutoka mji mmoja hadi mwengine; na lau si hao basi binadamu angelipata tabu.
Hakika Mola wenu ni Mpole sana Mwenye kurehemu.
Miongoni mwa huruma zake ni kuwatumikisha wanyama kwa masilahi ya watu ilikuweza kurahisisha mambo na kupunguza tabu
Na farasi na nyumbu na punda ili muwapande na pambo.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja manufaa matatu ya wanyama, sasa anataja manufaa ya farasi, nyumbu na punda, ambayo muhimu zaidi ni kupanda na vipambo, katika wakati huo.
Na anaumba msivyovijua.
Kila mwanachuoni ameifasiri jumla hii kulingana na wakati wake na maisha yake. Baadhi ya wakale wamesema kuwa makusudio ni kuwa Mwenyezi Mungu anaumba aina ya wanyama, mimea na vitu vingine vingi sana ambavyo watu hawavijui.
Tabari anasema: Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu atawaumbia watu wa Peponi aina kadha za neema na atawaumbia watu wa motoni aina kadhaa za adhabu ambazo hakuna jicho lililoziona wala sikio lililozisikia au moyo ulioziwazia. Baadhi ya wafasiri wapya, akiwemo Sheikh Al-maraghi, wamesema:
“Hii ni ishara ya ndege, magari n.k.”
Maana yanayonasibiana na mfumo wa maneno – tuonavyo sisi – ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya kutaja manufaa kwa waja wake, anasema kuwa haya ni machache miongoni mwa manufaa mengi msiyoyajua wala kujua idadi yake.
Kwa maneno mengine jumla hii inafanana na kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya ya 18 ya Sura hii: “Na mkizihisabu neema za Mwenyezi Mungu hamuwezi kuzidhibiti.
Sha’rani amenukuu katika kitabu chake Al-mizani kutoka kwa Abu Hanifa, uharamu wa nyama ya farasi. Na kutoka kwa Shafii, Malik, na Ibn Hambal wamesema ni halali.
Ama nyama ya nyumbu na punda, amenukuu kutoka kwa Shafi, Abu Hanifa na Ibn Hambal kuwa ni haramu. Shia Imamiya wamesema kuwa nyama ya farasi, nyumbu na punda ni halali, lakini ni makruh.
Na ni juu ya Mwenyezi Mungu njia iliyo sawa.
Juu hapa, ni kwa maana ya wajibu. Aya hii inafanana na ile isemayo: “Hakika ni juu yetu kuonyesha uwongofu” (92:12). Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amejilazimisha kuwabainishia watu, kupitia Mitume, njia ya haki na ya uongofu.
Na nyingine ni kombo.
Yaani kuna njia zilizo sawa, kama vile Uislamu, na nyingine ziko kombo kombo, kama dini nyinginezo.
Lau angelipenda angeliwaongoza nyote.
Yaani kama Mwenyezi Mungu angelitaka angeliwaelekeza watu wote kwenye imani kwa nguvu na asingelikufuru yeyote.
Lakini Yeye Mwenyezi Mungu amemwachia mtu hiyari, baada ya kumbainishia njia mbili, kwa kuchukulia utu wake. Angalia Juz. 12 (12: 118).
هُوَ الَّذِي أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً لَّكُم مِّنْهُ شَرَابٌ وَمِنْهُ شَجَرٌ فِيهِ تُسِيمُونَ ﴿١٠﴾
10. Yeye ndiye aliyewateremshia maji kutoka mbinguni. Katika hayo nyinyi mnapata ya kunywa na miti ya kulishia.
يُنبِتُ لَكُم بِهِ الزَّرْعَ وَالزَّيْتُونَ وَالنَّخِيلَ وَالْأَعْنَابَ وَمِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿١١﴾
11. Kwayo anazalisha mimea kwa ajili yenu na mizaituni na mitende na mizabibu na kila matunda. Hakika katika hayo zipo ishara kwa watu wanaofikiri.
وَسَخَّرَ لَكُمُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ وَالشَّمْسَ وَالْقَمَرَ وَالنُّجُومُ مُسَخَّرَاتٌ بِأَمْرِهِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴿١٢﴾
12. Na amefanya uwatumikie usiku na mchana na jua na mwezi na nyota ziwatumikie kwa amri yake. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu walio na akili.
وَمَا ذَرَأَ لَكُمْ فِي الْأَرْضِ مُخْتَلِفًا أَلْوَانُهُ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَذَّكَّرُونَ ﴿١٣﴾
13. Na alivyovieneza katika ardhi vya rangi mbali mbali. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaowaidhikia.
وَهُوَ الَّذِي سَخَّرَ الْبَحْرَ لِتَأْكُلُوا مِنْهُ لَحْمًا طَرِيًّا وَتَسْتَخْرِجُوا مِنْهُ حِلْيَةً تَلْبَسُونَهَا وَتَرَى الْفُلْكَ مَوَاخِرَ فِيهِ وَلِتَبْتَغُوا مِن فَضْلِهِ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿١٤﴾
14. Yeye ndiye aliyeifanya bahari iwatumikie ili kutoka humo mpate kula nyama freshi na mtoe humo mapambo mnayoyavaa. Na unaona vyombo vikikata maji humo, ili mtafute fadhila yake na mpate kushukuru.
وَأَلْقَىٰ فِي الْأَرْضِ رَوَاسِيَ أَن تَمِيدَ بِكُمْ وَأَنْهَارًا وَسُبُلًا لَّعَلَّكُمْ تَهْتَدُونَ ﴿١٥﴾
15. Na akaweka katika ardhi milima ili isiyumbe nanyi. Na mito na njia ili mpate kuon- goka.
وَعَلَامَاتٍ وَبِالنَّجْمِ هُمْ يَهْتَدُونَ ﴿١٦﴾
16. Na alama nyingine. Na kwa nyota wao wanajiongoza.
أَفَمَن يَخْلُقُ كَمَن لَّا يَخْلُقُ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿١٧﴾
17. Je, anayeumba ni kama asiyeumba? Hivi hamkumbuki?
وَإِن تَعُدُّوا نِعْمَةَ اللَّـهِ لَا تُحْصُوهَا إِنَّ اللَّـهَ لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١٨﴾
17. Na mkizihisabu neema za Mwenyezi Mungu hamuwezi kuzidhibiti. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تُسِرُّونَ وَمَا تُعْلِنُونَ ﴿١٩﴾
19. Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyafanya siri na mnaoyoyatangaza.
Aya 10 – 19
Yeye ndiye aliyewateremshia maji kutoka mbinguni, Katika hayo nyinyi mnapata ya kunywa na miti ya kulishia.
Kila kinachomea katika ardhi ni mti. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amewaneemesha waja wake kwa maji akayafanya kinywaji chao na akaotesha mimea ambayo wanalishia wanyama wao.
Kwayo anazalisha mimea kwa ajili yenu na mizaituni na mitende na mizabibu na kila matunda. Hakika katika hayo zipo ishara kwa watu wanaofikiri.
Vilevile Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa maji haya ameotesha vitu kwa masilahi yetu na manufaa yetu. Basi na tufikiri na kuzingatia kwa makini uweza wa Mwenyezi Mungu na ukuu wake na tumshukuru kwa kumtii na kutenda kulingana na radhi yake. Huko nyuma tumewahi kudokeza kuwa maji yanatokana na sababu za kimaumbile alizoziweka Mwenyezi Mungu katika ulimwengu huu; na kwamba inategemezwa kwake moja kwa moja kwa kuwa Yeye ndiye msababishi wa kwanza.
Mfano wa Aya hii umetangulia katika Juz. 13 (14:32) na katika Juz. hii tuliyo nayo (15:22).
Na amefanya uwatumikie usiku na mchana na Jua na Mwezi na nyota ziwatumikie kwa amri yake. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu walio na akili.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:2) na (14: 33). Kusema ‘kwa amri yake’ kunaishiria majibu ya wamaada wanaodai kuwa matukio yote ya ulimwengu yanatokana na sababu zake za kimaumbile tu.
Unaweza kuuliza : Kwani haitoshi kutaja usiku mpaka utajwe mwezi na mchana mpaka litajwe jua?
Jibu : Hapana! Usiku unaweza kuweko bila ya mwezi, Na mchana ni baadhi tu ya athari na faida za Jua, lakini kuna athari na faida nyinginezo zinazoletwa na Jua.
Na alivyovieneza katika ardhi vya rangi mbali mbali, Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaowaidhikia.
Makusudio ya kueneza ni kuumba, na rangi ni aina. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametupatia vitu alivyoviumba duniani, vikiwemo vitu vikavu kama madini na vya majimaji, tuvitumie, ili aweze kuwaid- hika mwenye kuwaidhika na ashukuru mwenye kushukuru.
Yeye ndiye aliyeifanya bahari iwatumikie ili kutoka humo mpate kula nyama freshi[3] na mtoe humo mapambo mnayoyavaa. Na unaona vyombo vikikata maji humo, ili mtafute fadhila yake na mpate kushukuru.
Ametaja Mwenyezi Mungu faida tatu za bahari:
1. Samaki
2. Vipambo; kama vile lulu na marijani. Mwenyezi Mungu anasema: “Hutoka humo lulu na marijani” (55: 22). Al-Maraghi katika kufasiri Aya hii anasema: “Yanapatikana mashamba ya lulu na marijani ndani ya bahari ya kati (Mediterranean sea) baina ya Tunisia na Algeria. Serikali ya Ufaransa ndiyo inayovuna mashamba haya kisha huwauzia wenyewe; kama kwamba wao hawakusoma Qur’an, kama kwamba wao hawakuumbiwa dunia hii na kama kwamba wao hawakuamrishwa kufanya kazi na kuitoa.”
3. Safari ya baharini kibiashara na mengineyo.
Na akaweka katika ardhi milima ili isiyumbe nanyi.
Ameweka mlima katika ardhi ili iwe imara kusipatikane mgongano. Umepita mafano wake katika Juz. hii (15:19).
Na mito na njia ili mpate kuongoka.
Amepitisha mito pia amefanya njia ili muweze kufika kule mnakotaka kwa njia hizo.
Na alama nyingine.
Makusudio ya alama hapa ni dalili zinaazomsadia msafiri kufuata njia; mfano mlima, mabonde n.k.
Na kwa nyota wao wanjiongoza wanaposafiri bara na baharini.
Umepita mfano wake katika Juz. 7 (6:97).
Je, anayeumba ni kama asiyeumba? Hivi hamkumbuki?
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja kuwa Yeye ndiye muumbaji wa mbingu na ardhi, binadamu, wanyama, maji, miti, Jua, Mwezi n.k. Sasa anasema kuwa je, aliyeumba vyote hivi anakuwa sawa na jiwe na sanamu?
Swali hili liko pamoja na jawabu lake.
Na mkizihisabu neema za Mwenyezi Mungu hamuwezi kuzidhibiti.
Umepita mfano wake katika Juz, 13 (14:34).
Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Anamsamehe mwenye kuzembea kumshukuru bila ya kumnyang’anya neema, kwa sababu ya kumuonea huruma.
Na Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyafanya siri na mnaoyoyatangaza.
Ikiwa anayajua mnayoyafanya siri na mnayoyafanya dhahiri ni wajibu kumtii Yeye kwa kuhofia hasira zake na adhabu yake.
وَالَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ لَا يَخْلُقُونَ شَيْئًا وَهُمْ يُخْلَقُونَ ﴿٢٠﴾
20. Na wale wanaowaomba wasiokuwa Mwenyezi Mungu hawaumbi kitu, bali wao wameumbwa.
أَمْوَاتٌ غَيْرُ أَحْيَاءٍ وَمَا يَشْعُرُونَ أَيَّانَ يُبْعَثُونَ ﴿٢١﴾
Ni wafu si hai. Na wala hawatambui watafufuliwa lini.
إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَالَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ قُلُوبُهُم مُّنكِرَةٌ وَهُم مُّسْتَكْبِرُونَ ﴿٢٢﴾
22. Mungu wenu ni Mungu mmoja, Lakini wasioamini Akhera nyoyo zao zinakataa, nao wana kiburi.
لَا جَرَمَ أَنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا يُسِرُّونَ وَمَا يُعْلِنُونَ إِنَّهُ لَا يُحِبُّ الْمُسْتَكْبِرِينَ ﴿٢٣﴾
23. Hapana shaka kuwa Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyafanya siri na wanayoyatangaza, Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi.
Aya 20 – 23
Na wale wanaowaomba wasiokuwa Mwenyezi Mungu hawaumbi kitu, bali wao wameumbwa.
Yametangulia mazungumzo kuhsu ushirikina na mjadala pamoja na washirikina, katika Aya kadhaa. Sasa baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kuelezea aina kadhaa za neema zake kwa waja wake, anadokeza, kwenye Aya hizi na zinaazofuatia, kuhusu wale wanaomkufuru Mwenyezi Mungu na wanaomfanyia washirika katika kuumba kwake.
Akawaambia wazi na kwa hoja fasaha, kwamba Mungu anayefaa kuabudiwa ni yule anayekuwa muumbaji sio aliyeumbwa, Na nyinyi washirikina mnaabudu aliyeumbwa sio aliyeumba.
Ni wafu si hai.
Vile vile miongoni mwa masharti ya mwenye kuabudiwa ni kuwa hai; na mnayemwabudu ameganda tu hana uhai.
Na wala hawatambui watafufuliwa lini.
Jumla hii maana yake yatafahamika kutokana na maswali mawili yafutayo pamoja na majibu yake:
Swali la kwanza : Neno hawatambui linatumika kwa wenye akili na washirikina wanaabudu masanamu, sasa imekuwaje kutumia dhamiri ya wenye akili kwa visivyo na akili?
Jibu : matumizi haya yamekuja kulingana na wanavyoitakidi washirikina kwamba masanamu yanaakili na utambuzi. Kwani kuna ubaya gani wa matumizi haya na mfano wake maadamu ni masuala ya tamko tumko tu na ibara?
Swali a pili : Masanamu hayatafufuliwa, vipi Mwenyezi Mungu (s.w.t) akasema: ‘Na wala hawatambui watafufuliwa lini’
Jibu : baadhi ya wafasiri wamejibu kwamba dhamir katika ‘hawatambui’ ni ya masanamu na ‘watafuliwa’ ni ya washirikina; Kwa hiyo maana yanakuwa masanamu hayatambui lini watafufuliwa washirikina kutoka makubirini mwao, Ikiwa masanamu hayatambui hayo, basi inakuwaje kuwa yanastahiki kuabudiwa?
Mungu wenu ni Mungu mmoja, Lakini wasioamini Akhera nyoyo zao zinakataa, nao wana kiburi.
Mwenyezi Mungu (s.w.t), katika Aya hii, ametaja sifa mbili za wanaopinga Akhera:
Sifa ya kwanza: kwamba nyoyo zao zimepinga na kuikana Akhera. Kwa hiyo wao hawafanyi chochote kwa kutummai thawabu au kuhofia adhabu; isipokuwa wanafanya kwa misingi ya faida na manufaa ya maisha haya ya dunia. Sifa ya pili: kwamba wao wanaikimbia haki na wala hawaifuati kwa sababu ya kujiona wakubwa na kuwa na kiburi.
Hapana shaka kuwa Mwenyezi Mungu anayajua wanayoyafanya siri na wanyoyatangaza, Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi.
Hakika Yeye Mwenyezi Mungu anajua kupinga kwao kulikuwa ni kwa kujipa uluwa na kiburi, naye anawachukia wanaoinyenyekea haki na atawaadhibu yale wanayostahiki.
5
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
وَإِذَا قِيلَ لَهُم مَّاذَا أَنزَلَ رَبُّكُمْ قَالُوا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ ﴿٢٤﴾
24. Wanapoambiwa: Ameteremsha nini Mola wenu? Husema: ngano za watu wa kale.
لِيَحْمِلُوا أَوْزَارَهُمْ كَامِلَةً يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَمِنْ أَوْزَارِ الَّذِينَ يُضِلُّونَهُم بِغَيْرِ عِلْمٍ أَلَا سَاءَ مَا يَزِرُونَ ﴿٢٥﴾
25. Ili wabebe mizigo yao kwa ukamilifu siku ya Kiyama na sehemu ya mizigo ya wale wanaowapoteza bila ya kujua. Ehe! Ni maovu hayo wanayoyabeba.
قَدْ مَكَرَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَأَتَى اللَّـهُ بُنْيَانَهُم مِّنَ الْقَوَاعِدِ فَخَرَّ عَلَيْهِمُ السَّقْفُ مِن فَوْقِهِمْ وَأَتَاهُمُ الْعَذَابُ مِنْ حَيْثُ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٢٦﴾
26. Walipanga vitimbi waliokuwa kabla yao. Mwenyezi Mungu akazifikia nyumba zao kwenye misingi akayasekua majengo yao kwenye misingi, dari zikawaporomokea juu yao na adhabu ikawajia kutoka wasipotambua.
ثُمَّ يَوْمَ الْقِيَامَةِ يُخْزِيهِمْ وَيَقُولُ أَيْنَ شُرَكَائِيَ الَّذِينَ كُنتُمْ تُشَاقُّونَ فِيهِمْ قَالَ الَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ إِنَّ الْخِزْيَ الْيَوْمَ وَالسُّوءَ عَلَى الْكَافِرِينَ ﴿٢٧﴾
27. Kisha siku ya Kiyama atawahizi. Na atasema: Wako wapi hapo hao washirika wangu ambao kwao mlikuwa mkipatisha mashaka. Watasema waliopewa: Hakika leo hizaya na uovu utawashukia makafiri.
الَّذِينَ تَتَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ ظَالِمِي أَنفُسِهِمْ فَأَلْقَوُا السَّلَمَ مَا كُنَّا نَعْمَلُ مِن سُوءٍ بَلَىٰ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٢٨﴾
28. Wale ambao Malaika wamewafisha hali ya kuwa wamejidhulumu. Basi watasalimu amri (waseme): Hatukuwa tukifanya uovu: Ndiyo! Hakika Mwenyezi Mungu anajua sana mliyokuwa mkiyatenda.
فَادْخُلُوا أَبْوَابَ جَهَنَّمَ خَالِدِينَ فِيهَا فَلَبِئْسَ مَثْوَى الْمُتَكَبِّرِينَ ﴿٢٩﴾
29. Basi ingieni milango ya Jahannam, humo mdumu, Ni maovu mno makazi ya wafanyao kiburi.
Aya 24 – 29
Wanapoambiwa: Ameteremsha nini Mola wenu? Husema: ngano za watu wa kale.
Katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja kuwa wanaopinga Akhera wamefanya hivyo kwa kujifanya wakubwa na kiburi cha kutoinyenyekea haki. Katika Aya hii anawasimulia kuwa wao wanaipa Qur’an sifa ya kuwa ni uzushi na ni vigano.
Katika Aya nyingine Muhammad(s.a.w.w) wamembandika uwendawazimu na mara ningine wanasema ni mshairi au kuhani. Pia wanadiriki kusema kuwa ni mchawi.
Lengo lao la kwanza ni kuwapoteza watu wasiijue haki ambayo inafichua aibu zao na hakika yao. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewataja hawa wanowazuia watu na na haki katika Aya nyingi. Mara nyingine amewapa sifa ya wanaotaka kupotosha na pia akawataja kuwa wanataka kuizima nuru ya Mwenyezi Mungu kwa vinywa vyao. Na Mwenyezi Mungu akawahadharisha kwa kusema: Na kwa hakika watabeba mizigo yao na mizigo mingine pamoja na mizigo yao. Na kwa yakini wataulizwa siku ya kiyama yale waliyokuwa wakiyazua (29:13). Maana ya Aya hii yanafanana na Aya ifuatayo:
Ili wabebe mizigo yao kwa ukamilifu siku ya Kiyama na sehemu ya mizigo ya wale wanaowapoteza bila ya kujua. Ehe! Ni maovu hayo wanayoyabeba.
Hakika wamepotea na wakapoteza wengine. Kwa sababu ya upotevu wao basi wao watabeba madhambi yao kwa ukamailifu; yaani Mwenyezi Mungu hatawasamehe kitu. Na kwa sababu ya kuwapoteza wengine basi watabeba dhambi nyingine za wale waliowapoteza na kuwaharibu. Kuna hadithi isemayo: “Yeyote atakayetoa mwito wa upotevu na wakafuata- yaani wakifuata watubasi atakuwa na malipo sawa na yale ya waliomfu- ata bila ya kupungua kitu katika madhambi yao.”
Walipanga vitimbi waliokuwa kabla yao. Mwenyezi Mungu akazifikia nyumba zao kwenye misingi akayasekua majengo yao kwenye misingi, dari zikawaporomokea juu yao na adhabu ikawajia kutoka wasipotambua.
Makusudio ya majengo, misingi na dari ni kufananisha matendo yao na hayo majengo. Maana ni kuwa washirikina wa mwanzo walipanga njama na hila dhidi ya mitume na manabii wa Mwenyezi Mungu, lakini Mwenyezi Mungu akazitibua zote na ikawa ndiyo sababu ya kuangamia kwao; sawa na aliyejenga nyumba akaipangilia vizuri pamoja na msingi wake; na alipoanza kufanya maskani hapo na kutulia ikaporomoka kuanzia msingi, ikawa chini juu. Huu hasa ndio mwisho wa kila mwenye kuipinga haki na akaeneza uzushi na propaganda. Ni sawa haki ije kupitia kwa Muhammad(s.a.w.w) au mwenginewe.
Kisha siku ya kiyama atawahizi.
Makusudio ya kuhizi hapa ni adhabu ya moto: “Mola wetu! Hakika wewe, ambaye utamwingiza motoni utakuwa umemuhizi, Juz, 4 (3:192).
Na atasema: Wako wapi hapo hao washirika wangu ambao kwao mlikuwa mkipatisha mashaka.
Anayesema ni Mwenyezi Mungu, wanaoambiwa ni washirikina na maana ya kupatisha mashaka ni kule kugombana nao kuhusu masanamu. Kwa sababu washirikina walikuwa wakiyaabudu na kuyatetea na kugombana na kila mwenye kuyashutumu na kuyasema kwa ubaya. Walikuwa wakisema: haya yanatuombea na kutuweka karibu na Mwenyezi Mungu.
Kwa hiyo watakaposimama kesho mbele ya Mwenyezi Mungu atauliza kuhusu hayo kwa kuwatahayariza: wakowapi hao washirika wangu mliokuwa mkidai? Hata ikiwa hakuna adhabu basi swali hili peke yake, kutoka kwa Mwenye nguvu, linatosha.
Watasema waliopewa elimu ya haki na wakaitumia:Hakika leo hizaya na uovu utawashukia makafiri.
Makusudio ya makafiri hapa ni kila wanaopinga haki na wakaacha kuinyenyekea, wawe walahidi au la. Kwa sababu wote hao wataingia Jahannam na ni mahali pabaya.
Wale ambao Malaika wamewafisha hali ya kuwa wamejidhulumu.
Wamejidhulumu kwa vile wamekufa wakiwa ni makafiri na wapotevu.
Basi watasalimu amri.
Wanasalimu amri siku ambayo hakufai kitu kusalimu kwao wala kunyenyekea(waseme): Hatukuwa tukifanya uovu na hapo Mwenyezi Mungu atajibu kwa kusema:
Ndiyo! Hakika Mwenyezi Mungu anajua sana mliyokuwa mkiyatenda. Miongoni mwa dhulma na madhambi, na leo mtalipwa adhabu kwa yale mliyokuwa mkiyazua
Basi ingieni milango ya Jahannam, humo mdumu. Ni maovu mno makazi ya wafanyao kiburi.
Kila mwenye kuikataa haki basi huyo mbele ya Mwenyezi Mungu ni mwenye kiburi, ni sawa awe amenasibika na Uislamu au kunasibika na dini nyingine. Mwisho wake ni kudumu katika Jahannam, Ama kuhusu milango yake, yametangulia maelezo katika Juz hii (15: 44).
وَقِيلَ لِلَّذِينَ اتَّقَوْا مَاذَا أَنزَلَ رَبُّكُمْ قَالُوا خَيْرًا لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا فِي هَـٰذِهِ الدُّنْيَا حَسَنَةٌ وَلَدَارُ الْآخِرَةِ خَيْرٌ وَلَنِعْمَ دَارُ الْمُتَّقِينَ ﴿٣٠﴾
30. Na wataambiwa wale waliofanya takua: Mola wenu ameteremsha nini? Watasema: Kheri, Waliofanya wema katika dunia hii watapata wema. Na nyumba ya Akhera ni bora zaidi. Na ni bora mno nyumba ya wenye takua.
جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ لَهُمْ فِيهَا مَا يَشَاءُونَ كَذَٰلِكَ يَجْزِي اللَّـهُ الْمُتَّقِينَ ﴿٣١﴾
31. Bustani za milele wataziingia, hupita chini yake mito, Humo watapata watakacho, Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu awalipavyo wenye takua.
الَّذِينَ تَتَوَفَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ طَيِّبِينَ يَقُولُونَ سَلَامٌ عَلَيْكُمُ ادْخُلُوا الْجَنَّةَ بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٣٢﴾
Wale ambao Malaika huwafisha katika hali njema. Wanawaambia, amani iwe juu yenu (Salamun alaykum) kwa yale mliyokuwa mkiyatenda.
هَلْ يَنظُرُونَ إِلَّا أَن تَأْتِيَهُمُ الْمَلَائِكَةُ أَوْ يَأْتِيَ أَمْرُ رَبِّكَ كَذَٰلِكَ فَعَلَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَمَا ظَلَمَهُمُ اللَّـهُ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿٣٣﴾
33. Je, wanangojea jengine isipokuwa Malaika wawafikie au iwafikie amri ya Mola wako? Kama hivyo walitenda waliokuwa kabla yao, Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu, Lakini wamejidhulumu wenyewe.
فَأَصَابَهُمْ سَيِّئَاتُ مَا عَمِلُوا وَحَاقَ بِهِم مَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٣٤﴾
34. Basi ukawasibu uovu wa waliyoyatenda na yakawazunguka waliyokuwa wakiyafanyia stihzai.
Aya 30 – 34
Na watambiwa wale waliofanya takua: Mola wenu ameteremsha nini? Watasema: kheri.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwataja washirikina ambao waliitaja Qur’an kuwa ni potofu na ni ngano za watu wa kale, sasa anawataja waumini katika Aya hii, na kwamba wao watakapo ulizwa kuhusu Qur’an wataitaja kwa utukufu na taadhima na kuisifu kama alivyoisifu Imam Aliy(a.s) katika Nahjul- balagha:“Dhahiri yake ni safi na undani wake ni wakina. maajabu yake hayatoweki na mshangazo wake hauishi, wala giza halitanzuki ila kwayo”
Waliofanya wema katika dunia hii watapata wema.
Hii ni jumla inayoanza upya, haina uhusiano na maneno yaliyo kabla yake. Imesemekana kuwa ni katika maneno ya wenye takua. Hata hivyo maana ni moja tu katika makadirio yote mawili, nayo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawalipa heri watenda mema hapa duniani ijapokuwa ni kwa kutajwa vizuri
Na nyumba ya Akhera ni bora zaidi kuliko neema ya duniani iliyojaa ghasia na wasiwasi na iliyo na kipimo na kiasi.Na ni bora mno nyumba ya wenye takua, kwa sababu ni nyumba ya raha ya daima ambayo haina tashwishi yoyote ya wasiwasi wala kutaabika.
Bustani za milele wataziingia, hupita chini yake mito, Humo watapata watakacho, Hivi ndivyo Mwenyezi Mungu awalipavyo wenye takua.
Hawaaingii Pepo hii adhimu isipokuwa wenye takua, nao ni wale waliofanya juhudi ya kuinusuru haki, wakavumilia adha kwa ajili yake. Qur’an imenukuu wazi aina hii ya wenye takua watakaoingia peponi, pale iliposema:
أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَعْلَمِ اللَّـهُ الَّذِينَ جَاهَدُوا مِنكُمْ وَيَعْلَمَ الصَّابِرِينَ ﴿١٤٢﴾
Je, mwadhani mtaingia peponi na hali Mwenyezi Mungu hajawajua wale waliofanya jihadi miongoni mwenu na kuwajua wale waliofanya subira? Juz, 4 (3:142).
Wale ambao Malaika huwafisha katika hali njema kwenye makusudio yao na kwenye vitendo na kauli zao. Mtu hupimwa kwa mwisho wake na mwema ni yule mwenye kuiacha dunia hii na Mungu yuko radhi naye na kumshuhudia kuwa yeye ni katika watu wema.
Wanawaambia amani iwe juu yenu (Salamun alaykum) kwa yale mliyokuwa mkiyatenda.
Yaani Malaika wanawasalimu watu wema wakati wa kufa kwa rehema, huku wakiwabashiria Pepo, ili zitulie nyoyo zao na wapate furaha ya karama na vyeo walivyoahidiwa na Mwenyezi Mungu.
Je, wanangojea jengine isipokuwa Malaika wawafikie au iwafikie amri ya Mola wako?
Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (6: 159).
Kama hivyo walitenda waliokuwa kabla yao.
Huu ni ukumbusho na onyo kwa wale ambao wamemkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) kwamba yatawapata yaliyowapata waliotangulia.
Na Mwenyezi Mungu hakuwadhulumu.
Vipi iwe hivyo na hali Yeye mwenyewe ameikataza dhulma na kuiita kuwa ni upotofu tena akawalaani madhalimu?
بَلِ الظَّالِمُونَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿١١﴾
“Bali madhalimu wako katika upotovu ulio wazi” (31:11)
“Basi mtangazaji atatangaza kati yao kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iko juu ya madhalimu”
Juz. 8 (7:44)
Lakini wamejidhulumu wenyewe.
Maana haya yamekaririka katika Aya kadha, Iliyo wazi zaidi ni ile isemayo: “Hakika Mwenyezi Mungu hadhulumu watu chochote, lakini watu wanajidhulumu wenyewe.” Juz,11 (10:44).
Mwenyezi Mungu amekariri neno watu ili kuondoa tashwishi. Lau si Ashaira (Sunni) kusema kuwa mtu hana hiyari bali ni mwenye kuendeshwa, basi tusingelikuwa na haja ya kurefusha maneno au misisitizo hii ambayo inafanana na kufafanua ufafanuzi.
Basi ukawasibu uovu wa waliyoyatenda na yakawazunguka waliyokuwa wakiyafanyia stihzai.
Washirikina walipinga risala ya Muhammad(s.a.w.w) , wakaidharau na wakawazuia watu nayo, basi nao watapata matunda ya matendo yao, wala hawatadhulumiwa, Bali wengi katika wao watapata malipo yaohapa duniani kabla ya akhera.
وَقَالَ الَّذِينَ أَشْرَكُوا لَوْ شَاءَ اللَّـهُ مَا عَبَدْنَا مِن دُونِهِ مِن شَيْءٍ نَّحْنُ وَلَا آبَاؤُنَا وَلَا حَرَّمْنَا مِن دُونِهِ مِن شَيْءٍ كَذَٰلِكَ فَعَلَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَهَلْ عَلَى الرُّسُلِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿٣٥﴾
35. Na wale ambao wameshirikisha wanasema: “Lau Mwenyezi Mungu angelitaka, tusingeliabudu chochote badala yake, sisi wala baba zetu, wala tusingeliharamisha chochote bila ya Yeye. Kama hivyo walifanya waliokuwa kabla yao. Basi kuna lolote juu ya mitume isipokuwa kufikisha kwa uwazi?
وَلَقَدْ بَعَثْنَا فِي كُلِّ أُمَّةٍ رَّسُولًا أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ وَاجْتَنِبُوا الطَّاغُوتَ فَمِنْهُم مَّنْ هَدَى اللَّـهُ وَمِنْهُم مَّنْ حَقَّتْ عَلَيْهِ الضَّلَالَةُ فَسِيرُوا فِي الْأَرْضِ فَانظُرُوا كَيْفَ كَانَ عَاقِبَةُ الْمُكَذِّبِينَ ﴿٣٦﴾
36. Na kwa hakika tulimtuma Mtume kwa kila umma kwamba muabuduni Mwenyezi Mungu na mumwepuke taghuti. Basi miongoni mwao wapo aliowaongoa Mwenyezi Mungu na miongoni mwao wapo ambao uliwathibitikia upotovu. Basi tembeeni katika ardhi muone ulikuwaje mwisho wa wale waliokadhibisha.
إِن تَحْرِصْ عَلَىٰ هُدَاهُمْ فَإِنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي مَن يُضِلُّ وَمَا لَهُم مِّن نَّاصِرِينَ ﴿٣٧﴾
37. Hata ukipupia kuwaongoza, lakini Mwenyezi Mungu hamuongoi yule aliyempoteza, wala hawatapata wa kuwanusuru.
Aya 35 – 37
Na wale ambao wameshirikisha wanasema: Lau Mwenyezi Mungu angelitaka tusingeliabudu chochote badala yake, sisi wala baba zetu, wala tusingeliharamisha chochote bila ya Yeye.
Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 8 (6:149).
Kama hivyo walifanya waliokuwa kabla yao.
Huu ndio msingi wa mataghuti kila wakati na kila mahali. Wanaipinga haki na kuwapiga vita wenye haki, kisha wanalibadilisha hilo kwenye matakwa ya Mwenyezi Mungu.
Basi kuna lolote juu ya mitume isipokuwa kufikisha kwa uwazi?
Huu ndio umuhimu wa kufikisha amri na makatazo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu. Ama kuyatenda wanayoyafikisha hiyo si kazi yao kidogo wala sana, Maana ya Aya hii yametangulia katika Aya nyingi.
Na kwa hakika tulimtuma Mtume kwa kila umma kwamba muabuduni Mwenyezi Mungu na mumwepuke taghuti.
Aya hii inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu ametuma Mtume, kwa kila umma katika kila karne na kila mahali, awaamrishe ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake na kuwakataza ibada ya asiyekuwa Mwenyezi Mungu; iwe ni sanamu, nyota, binadamu au kitu chochote. Si lazima Mtume huyu awe ni mtu, inaweza kuwa akili. Kwani akili ni mtume wa ndani na Nabii ni mtume wa nje, Angalia kifungu ‘Mwenyezi Mungu na maumbile’ katika Juz, 7 (6: 41).
Basi miongoni mwao wapo aliowaongoa Mwenyezi Mungu na miongoni mwao wapo ambao uliwathibitikia upotovu.
Makusudio ya upotovu hapa ni adhabu; mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu:
فَرِيقًا هَدَىٰ وَفَرِيقًا حَقَّ عَلَيْهِمُ الضَّلَالَةُ ﴿٣٠﴾
“Kundi moja ameliongoa na kundi jingine limethibitikiwa na upotofu” Juz, 8 (7: 30)
Mwenyezi Mungu (s.w.t) alituma Mitume kuleta bishara na kuonya. Wakaamini baadhi ya watu, wakawa ni katika walioongoka wenye kukurubishwa kwa Mwenyezi Mungu. Na wengine wakakufuru, wakawa ni wenye kuwekwa mbali wenye kuadhibiwa.
Basi tembeeni katika ardhi muone ulikuwaje mwisho wa wale waliokadhibisha.
Yamekaririka maana ya Aya hii katika Aya nyingi, ikiwemo ile iliyo katika Juz, 4 (93:137)
Hata ukipupia kuwaongoza, lakini Mwenyezi Mungu hamuongoi yule aliyempoteza, wala hawatapata wa kuwanusuru.
Hakuna mwenye shaka kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anapupia watu wote waongoke; hasa watu wake Maquraishi, lakini kupupia tu kwa mtume sio sababu ya kupatikana uongofu; isipokuwa sababu ni matakwa ya mtu kuongoka kama ambavyo sababu ya kupotea ni matakwa ya mtu mwenyewe.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amezithibitisha sababu zote hizi mbili; kwa maana ya kuwa Yeye ambaye hekima yake imetukuka, amejaalia matakwa ya mtu katika uongofu ndiyo natija ya uongofu wake na matakwa ya mtu katika upotevu ndio natija ya upotevu wake; sawa na mwenye kunywa sumu itakayomuua na yule mwenye kujiepusha na hatari atakavyookoka.
Haya ndio makusudio ya kunasibisha uongofu na upotevu kwa Mwenyezi Mungu, katika Aya hii na mfano wake. Mwenye kusema kuwa Mwenyezi Mungu ndiye anayeungiza uongofu au upotevu ndani ya binadamu, huyo atakuwa ni katika washirikina ambao Mwenyezi Mungu amewasimulia katika Aya iliyotangulia: “Lau Mwenyezi Mungu angelitaka tusingeliabudu chochote badala yake, sisi wala baba zetu, wala tusingeliharamisha chochote bila ya Yeye.”
Mwenyezi Mungu ametakata na wayasemayo madhalimu kabisa.
6
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
وَأَقْسَمُوا بِاللَّـهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ لَا يَبْعَثُ اللَّـهُ مَن يَمُوتُ بَلَىٰ وَعْدًا عَلَيْهِ حَقًّا وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٨﴾
38. Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwa viapo vyao vya nguvu (kwamba) Mwenyezi Mungu hatawafufua wafu. Ndio! Ni ahadi iliyo lazima kwake, lakini watu wengi hawajui
لِيُبَيِّنَ لَهُمُ الَّذِي يَخْتَلِفُونَ فِيهِ وَلِيَعْلَمَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَنَّهُمْ كَانُوا كَاذِبِينَ ﴿٣٩﴾
39. Ili awabainishie yale walioyokhitalifiana na ili wajue waliokufuru kwamba wao walikuwa waongo.
إِنَّمَا قَوْلُنَا لِشَيْءٍ إِذَا أَرَدْنَاهُ أَن نَّقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٤٠﴾
40. Kauli yetu kwa kitu tunachokitaka kiwe, ni kukiambia: Kuwa tu! Basi kinakuwa.
وَالَّذِينَ هَاجَرُوا فِي اللَّـهِ مِن بَعْدِ مَا ظُلِمُوا لَنُبَوِّئَنَّهُمْ فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَلَأَجْرُ الْآخِرَةِ أَكْبَرُ لَوْ كَانُوا يَعْلَمُونَ ﴿٤١﴾
41. Na wale waliohama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu baada ya kudhulumiwa, hakika tutawaweka katika dunia kwa wema. Na ujira wa Akhera ni mkubwa zaidi, lau wangelikuwa wanajua.
الَّذِينَ صَبَرُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٤٢﴾
42. Wale wanosubiri na wakamtegemea Mola wao.
Aya 38 – 42
Na wanaapa kwa Mwenyezi Mungu kwa viapo vyao vya nguvu.
Katika Aya ya 20 ya Sura hii, Mwenyezi Mungu aliwaambia washirikina kuwa nyinyi mnaabudu aliyeumbwa badala ya kumwabudu muumbaji, Katika Aya ya 24, amewasimulia kuwa wameibandaka jina Qur’an kuwa ni ngano za watu wa kale. Katika Aya ya 35 ametaja Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwa wao wanategemeza shirki yao na shirki ya mababa zao kwa Mwenyezi Mungu.
Katika Aya hii tuliyonayo Mwenyezi Mungu anasema kuwa wao wanapinga ufufuo, wakiapa viapo vya nguvu na kufanya juhudi kueleza kuwa mwenye kufa yake yamekwisha, kwa sababu kitu kikitawanyika hakiwezi kujirudia mara ya pili.
Hayo tumeyazungumzia katika Juz, 13 (13:5).
(Kwamba) Mwenyezi Mungu hatawafufua wafu, Ndio! Ni ahadi iliyo lazima kwake, lakini watu wengi hawajui.
Washirikina walikuwa wakiaamini kuweko Mwenyezi Mungu na kuweko washirika wake na walikuwa wakipinga ufufuo. Kwa vile wao wanaamini kuweko Mwenyezi Mungu, ndio likaja jibu kuwa ufufuo uko tu. Kwa sababu Mwenyezi Mungu wanayemwamini kuwa yuko, ndiye aliyetoa ahadi ya ufufuo na ahadi yake ni kweli. Ama kuvikusanya viungo baada ya kutawanyika kwake, hilo ni jepesi zaidi kuliko kuviumba. Kwa sababu ambaye amefanya kitu kilichokuwa hakipo basi ni rahisi zaidi kwake kuki kusanya baada ya kutawanyika.
Ili awabainishie yale walioyokhitalifiana na ili wajue waliokufuru kwamba wao walikuwa waongo.
Ufufuo una hekima nyingi sana; mingoni mwazo ni hizi zifuatazo:- Kujulikana mzuri na mbaya, mwema na muovu na malipo wanayostahiki. Hekima nyingine ni Mwenyezi Mungu kuwabainishia viumbe haki waliyokuwa wakihitalifiana; kama vile Tawhid, utume, halali na haramu.
Wale walioapa kuwa hakuna ufufuo wajue na wahakikishe kuwa wao walikuwa waongo katika viapo vyao.
Kauli yetu kwa kitu tunachokitaka kiwe, ni kukukiambia: Kuwa tu! Basi kinakuwa.
Mwenyezi Mungu alianza kuumba kwa neno ‘kuwa’ na atarudisha kwa neno hilohilo, “Na hili ni jepesi zaidi kwake. Naye ndiye mwenye mfano bora katika mbingu na ardhi na Yeye ndiye mwenye nguvu mwenye hekima.
Na wale waliohama kwa ajili ya Mwenyezi Mungu baada ya kudhu- lumiwa, hakika tutawaweka katika dunia kwa wema.
Aya hii inawahusu moja kwa moja waliohama (wahajiri) katika maswahaba wa mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) ambao walipata mtihani mwema kwa kumsaidia Mtume; wakacha dunia, watu wao na mali zao kwa kukimbia na dini yao na kumfuata Mtume wao kwa ajili ya kutafuta radhi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Ama wema ambao Mwenyezi Mungu amewapa duniani kabla ya Akhera ni majumba yao na milki zao mpya hapo Madina, kwani zilikuwa ni bora kuliko zile za Makka.
Na ujira wa Akhera ni mkubwa zaidi kuliko dunia na vilivyomo lau wangelikuwa wanajua!
Maneno hapa, wanaambiwa washirikina ambao walipinga ufufuo, Ama waumini, hasa maswahaba, wao wanajua kwa yakini kuwa thawabu za Akhera ni kubwa na adhimu zaidi. Tumezungumzia kuhusu Hijra na wahajiri katika Juz. 5 (4: 97 – 100) na kuhusu Wahajiri na Answari katika Juz. 10 (72 – 75).
Wale wanosubiri na wakamtegemea Mola wao.
Hakika Mumini wa kweli ana sifa na alama. Zilizo muhimu zaidi ni hizi zifuatazo:-Kuacha ubinafsi, kujitoa mhanga katika njia ya Mwenyezi Mungu, kuvumilia maudhi na mashaka kwa ajili ya kuihakikisha haki na kuibatilisha batili na kumtegemea Mwenyezi Mungu peke yake, sio mali wala cheo au ukoo; sawa na walivyokuwa maswahaba wa Mtume mtukufu(s.a.w.w) .
وَمَا أَرْسَلْنَا مِن قَبْلِكَ إِلَّا رِجَالًا نُّوحِي إِلَيْهِمْ فَاسْأَلُوا أَهْلَ الذِّكْرِ إِن كُنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٤٣﴾
43. Na hatukutuma kabla yako ila wanaume tuliowapa wahyi, Basi waulizeni wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui.
بِالْبَيِّنَاتِ وَالزُّبُرِ وَأَنزَلْنَا إِلَيْكَ الذِّكْرَ لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ وَلَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٤٤﴾
44. Kwa hoja zilizo wazi na kwa Vitabu. Na tumekuteremshia ukumbusho ili uwabainishie watu yale waliyoteremshiwa wapate kufikiri.
أَفَأَمِنَ الَّذِينَ مَكَرُوا السَّيِّئَاتِ أَن يَخْسِفَ اللَّـهُ بِهِمُ الْأَرْضَ أَوْ يَأْتِيَهُمُ الْعَذَابُ مِنْ حَيْثُ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٤٥﴾
45. Je, wameaminisha waliofanya vitimbi vya uovu kwamba Mwenyezi Mungu awadidimize katika ardhi au iwafikie adhabu kutoka wasipopajua?
أَوْ يَأْخُذَهُمْ فِي تَقَلُّبِهِمْ فَمَا هُم بِمُعْجِزِينَ ﴿٤٦﴾
46. Au Awakamate katika nyendo zao na wasiweze kuponyoka?
أَوْ يَأْخُذَهُمْ عَلَىٰ تَخَوُّفٍ فَإِنَّ رَبَّكُمْ لَرَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٤٧﴾
47. Au awakamate kidogo kidogo? Kwani hakika Mola wenu ni Mpole, Mwenye huruma.
أَوَلَمْ يَرَوْا إِلَىٰ مَا خَلَقَ اللَّـهُ مِن شَيْءٍ يَتَفَيَّأُ ظِلَالُهُ عَنِ الْيَمِينِ وَالشَّمَائِلِ سُجَّدًا لِّلَّـهِ وَهُمْ دَاخِرُونَ ﴿٤٨﴾
48. Je hawavioni vitu alivyoviumba Mwenyezi Mungu vivuli vyao vinaelekea kuliani na kushotoni vikimsujudia Mwenyezi Mungu na vikimnyenyekea?
وَلِلَّـهِ يَسْجُدُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ مِن دَابَّةٍ وَالْمَلَائِكَةُ وَهُمْ لَا يَسْتَكْبِرُونَ ﴿٤٩﴾
49. Na vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini katika wanyama na Malaika, nao hawatakabari.
يَخَافُونَ رَبَّهُم مِّن فَوْقِهِمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ ﴿٥٠﴾
50. Wanamhofia Mola wao aliye juu yao na wanafanya wanayoamriwa.
Aya 43 – 50
Na hatukutuma kabla yako ila wanaume tuliowapa wahyi.
Washirikina waliukana utume wa Muhammad na wakasema kuwa Mwenyezi Mungu hakutuma mtu kuwa mjumbe. Ndio Mwenyezi Mungu akabatilisha madai yao kwamba mitume na Manabii wote waliotangulia walikuwa ni watu wanaume wakiletewa wahyi; kama vile: Nuh, Ismail, Musa na wengineo. Kwa sababu lengo la kutumwa Mtume haliwezi kutimia ila ikiwa aliyetumwa ni jinsi ya wale waliotumiwa:
وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا بِلِسَانِ قَوْمِهِ لِيُبَيِّنَ لَهُمْ ﴿٤﴾
“Na hatukumtumma Mtume ila kwa ulimi wa watu wake ili apate kuwabainishia.” Juz. 13 (14:4)
قُل لَّوْ كَانَ فِي الْأَرْضِ مَلَائِكَةٌ يَمْشُونَ مُطْمَئِنِّينَ لَنَزَّلْنَا عَلَيْهِم مِّنَ السَّمَاءِ مَلَكًا رَّسُولًا ﴿٩٥﴾
“Sema: Ingelikuwa katika Ardhi kuna malaika wanotembea katika ardhi kwa utulivu, basi hakika tungeliwateremshia Malaika kuwa ni mitume wao” (17:95).
Basi waulizeni wenye ukumbusho ikiwa nyinyi hamjui.
Makusudio ya wenye ukumbusho hapa ni wenye elimu wanaochunga haki; ni sawa wawe ni katika Watu wa kitab au wengineo. Maana ni kuwa enyi washirikina! Mkiwa na shaka na maneno yetu, basi waulizeni wajuzi wawambie kuwa mitume wote walikuwa ni watu.
Kwa hoja zilizo wazi na kwa Vitabu.
Yaani Mwenyezi Mungu aliwatuma Mitume wakiwa na hoja zilizowazi ambazo ni dalili na ishara. Na kwa vitabu ambavyo vina ubainifu wa dini, itikadi na sharia.
Na tumekuteremshia ukumbusho ili uwabainishie watu yale waliyoteremshiwa wapate kufikiri.
Maneno anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) , Makusudio ya ukumbusho hapa ni Qur’an. Ilivyo hasa ni kuwa lengo la kutumwa Mitume na kuteremshwa vitabu ni kuwaongoza watu kwenye haki na uadilifu na maisha ya amani na raha.
Kauli yake Mwenyezi Mungu ‘wapate kufikiri’ ni kuwa wapate kuizingatia vizuri Qur’an na kugundua siri zake na malengo yake wapate kujua kuwa imeteremshwa kwa maslahi yao.
Je, wameaminisha waliofanya vitimbi vya uovu.
Wafasiri wamesema kuwa makusudio ya waliofanya vitimbi hapa ni washirikina wa kiquraish, kwa vile wao ndio waliomfanyia uovu Mtume(s.a.w.w) na wakamfanyia njama. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewahofisha na aina nne za adhabu:
1.Kwamba Mwenyezi Mungu awadidimize katika ardhi; kama alivyomfanyia Qarun:
فَخَسَفْنَا بِهِ وَبِدَارِهِ الْأَرْضَ فَمَا كَانَ لَهُ مِن فِئَةٍ يَنصُرُونَهُ مِن دُونِ اللَّـهِ وَمَا كَانَ مِنَ الْمُنتَصِرِينَ ﴿٨١﴾
“Na tukamadidimiza yeye na nyumba yake, wala hapakuwa na kundi lolote la kumsaidia zaidi ya Mwenyezi Mungu” (28:81)
2.Au iwafikie adhabu kutoka wasipopajua , awaangamize ghafla, kama alivyofanya kwa watu wa Lut.
3.Au awakamate katika nyendo zao na wasiweze kuponyoka , Yaani awaangamize wakiwa wanashughulika kutafuta riziki.
4.Au awakamate kidogo kidogo.
Neno kidogo kidogo, limefasiriwa kutokana na neno takhawwuf; kama walivyosema wafasiri wengi wakiongozwa na Tabrasi. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hatawaangamiza mara moja bali atawapa balaa ya kupungukiwa na watu na mali kidogo kidogo mpaka wa mwisho wao.
Kwani hakika Mola wenu ni Mpole, Mwenye huruma.
Miongoni mwa huruma zake ni kutowaharakishia adhabu wanayostahiki waasi, kwa kutumai kuwa watatubia na kuongoka.
Je hawavioni vitu alivyoviumba Mwenyezi Mungu vivuli vyao vinaelekea kuliani na kushotoni vikimsujudia Mwenyezi Mungu na vikimnyenyekea.
Wanaoambiwa hapa ni wale waliofanya vitimbi vya uovu, waliotajwa katika Aya iliyotangulia na pia inawezekana wanaambiwa watu wote. Kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema kwa kuwatahayariza wapinzani wenye inadi.
Makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Vivuli vinaelekea’ ni kuwa kila kitu kina kivuli; kama vile milima, miti, wanyama, majengo n.k. Na kauli yake: ‘kuliani na kushotoni’ ni ishara ya upande wa kitu kilicho na kivuli. Kwa sababu kivuli cha kitu kinakuwa upande mmoja kuanzia mawiyo hadi Adhuhuri na kinageuka upande wa pili kuanzia adhuhri hadi machweo.
Kwa hiyo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akaleta ibara ya kulia kwa upande mmoja na ibara ya kushoto kwa upande wa pili. Ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu: “ Na vivuli vyao asubuhi na jioni” Juz. 13 (13: 15) Ama kauli yake vikimsujudia Mwenyezi Mungu ni fumbo la utiifu. Unaweza kuuliza: Kwa nini Mwenyezi Mungu alipotaja kulia ametaja kwa tamko la umoja na alipotaja kushoto akatumia tamko la wingi (yamin wa shamail)[4] ?
Wafasiri wamelijibu hilo kwa majibu ambayo la karibu zaidi ni kuwa mfumo wa fasihi ya kiarabu wakitaja vitu viwili vyenye maana mbili tofauti kimoja kinatajwa kwa umoja na kingine kwa wingi; kama kusema kwake Mwenyezi Mungu: “Amejaalia viza na mwanga.”
Kwa ufupi ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) baada ya kuwahadharisha washirikina na wenye inadi, anasema katika Aya hii, kwamba kila kilicho ulimwenguni – isipokuwa washirikina na wenye inadi – vinamnyenyekea na kufuata amri yake.
Na vinamsujudia Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini katika wanyama na Malaika nao hawatakabari.
Viumbe vyote vya juu na chini vinafahamisha waziwazi kuweko aliyevifanya na kufahamisha uweza wake, elimu yake na hekima yake na dalili hii ndio tasbihi, tahmid, sujudi na rukui kwa muumbaji.
Pia haya ndio makusudio ya kusujudi kwa viumbe visivyo na akili; kama ambavyo ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na hakuna kitu chochote ila kinamtakasa kwa sifa zake” (17: 44). Lengo la kutaja wanyama na Malaika, baada ya kutaja vilivyo katika mbingu na ardhi, ni ubainifu wa kuchanganya aina zote za viumbe, Yametangulia maelezo yake katika Juz, 13 (13:13-25).
Wanamhofia Mola wao aliye juu yao na wanafanya wanayoamriwa.
Aya hii inafahamisha waziwazi kwamba mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu humhofia na hutii amri yake na makatazo yake, na inafahamisha katika madhumuni yake kwamba mwenye kumwasi Mwenyezi Mungu kisha akadai kuwa anamwamini na anamhofia, basi huyo ni mwongo katika madai yake.
وَقَالَ اللَّـهُ لَا تَتَّخِذُوا إِلَـٰهَيْنِ اثْنَيْنِ إِنَّمَا هُوَ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَإِيَّايَ فَارْهَبُونِ ﴿٥١﴾
51. Na amesema Mwenyezi Mungu: Msiabudu miungu wawili! Hakika Yeye ni Mungu mmoja tu. Basi niogopeni mimi tu.
وَلَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلَهُ الدِّينُ وَاصِبًا أَفَغَيْرَ اللَّـهِ تَتَّقُونَ ﴿٥٢﴾
52. Ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini, na dini ni yake Yeye daima, Je, mtamcha mwingine asiyekuwa Mwenyezi Mungu?
وَمَا بِكُم مِّن نِّعْمَةٍ فَمِنَ اللَّـهِ ثُمَّ إِذَا مَسَّكُمُ الضُّرُّ فَإِلَيْهِ تَجْأَرُونَ ﴿٥٣﴾
53. Na neema yoyote mliyo nayo inatoka kwa Mwenyezi Mungu, Kisha ikiwagusa dhara mnamlilia yeye.
ثُمَّ إِذَا كَشَفَ الضُّرَّ عَنكُمْ إِذَا فَرِيقٌ مِّنكُم بِرَبِّهِمْ يُشْرِكُونَ ﴿٥٤﴾
54. Kisha anapowaondolea dhara, kundi moja miongoni mwenu linamshirikisha Mola wao.
لِيَكْفُرُوا بِمَا آتَيْنَاهُمْ فَتَمَتَّعُوا فَسَوْفَ تَعْلَمُونَ ﴿٥٥﴾
55. Ili wakufuru tuliyowapa, Basi stareheni mtakujajua.
Aya 51 – 55
Na amesema Mwenyezi Mungu: Msiabudu miungu wawili! Hakika Yeye ni Mungu mmoja tu. Basi niogopeni mimi tu.
Kuna desturi maarufu kwa wanafiqhi isemayo: Hakika dharura hupimwa kwa kiasi chake na kwamba kinachozidi haja na dharura basi ni upuzi.
Desturi hii tunaweza kuitumia kwa yule anayemshirikisha Muumba, kwamba kuchukulia kuwa kuna Muumba mwenye kupanga vizuri mambo na mwenye hekima ni jambo la lazima halikimbiliki katika mtazamo wa kiakili, ambapo haiwezekani kuufasiri ulimwengu na vilivyomo ndani yake kuanzia nidhamu na mfumo isipokuwa lazima awepo mpangaji wa hayo Mwenye hekima.
Kwa hiyo baada ya kuchukulia huku haiwezekani kubakia madai yoyote ya kuchukulia kuwa kuna Mungu mwingine, katika mtazamo wa kiakili; bali akili inalikataa hilo, Angalia katika Juz. 5 (4:48-50) kifungu ‘Dalili ya umoja na utatu’.
Kisha umoja wa Mwenyezi Mungu una athari na mambo yanayolazimiana nao, ameyadokeza Mwenyezi Mungu kwa kauli yake kama yafuatavyo:-
1.Ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini.
Hilo halina upinzani wala ubishi, kwa sababu yeye ndiye aliyeiumba mbin- gu na ardhi na viliyvomo ndani yake.
2.Na dini ni yake Yeye daima.
Makusudio ya dini hapa ni kufuatwa na utiifu. Ikiwa Mwenyezi Mungu ni muumba na mmiliki wa kila kitu basi imethibitika kuendelea kutiiwa Yeye tu si mwenginewe.
3.Na neema yoyote mliyo nayo inatoka kwa Mwenyezi Mungu,
Kwa sababu Yeye ni Muumba wa kila kitu moja kwa moja kwa neno ‘kuwa na kikawa’ au kupitia kitu kingine.
Kisha ikiwagusa dhara mnamlilia Yeye; kisha anapowaondolea dhara, kundi moja miongoni mwenu linamshirikisha Mola wao.
Muumin wa kweli anamtegemea Mwenyezi Mungu katika hali zote, lakini mfanyabiashara humkimbilia Mwenyezi Mungu wakati wa dhiki na anajipurukusha naye wakati wa raha. Umepita mfano wa Aya hii katika Juz, 11 (10: 12).
Ili wakufuru tuliyowapa.
Makusudio ya kukufuru hapa ni kukufuru neema; zikiwemo kuondolewa madhara. Maana ya ‘ili’ ni natija; kama kusema amejitia kwenye hatari ili afe.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu amewaneemesha lakini natija ya neema yake ikawa ni kukufuriwa neema zake.
Basi stareheni mtakujajua mwisho wenu mbaya na mtajuta, ambapo hakutafaa chochote kujuta kwenu.
وَيَجْعَلُونَ لِمَا لَا يَعْلَمُونَ نَصِيبًا مِّمَّا رَزَقْنَاهُمْ تَاللَّـهِ لَتُسْأَلُنَّ عَمَّا كُنتُمْ تَفْتَرُونَ ﴿٥٦﴾
56. Na ambao hawajui wanawawekea sehemu ya tunavyowaruzuku. Wallahi! Hakika mtaulizwa hayo mliyokuwa mkiyazua.
وَيَجْعَلُونَ لِلَّـهِ الْبَنَاتِ سُبْحَانَهُ وَلَهُم مَّا يَشْتَهُونَ ﴿٥٧﴾
57. Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu mabinti. Ametakata na hayo! Na hali wao hupata wanavyovitamani.
وَإِذَا بُشِّرَ أَحَدُهُم بِالْأُنثَىٰ ظَلَّ وَجْهُهُ مُسْوَدًّا وَهُوَ كَظِيمٌ ﴿٥٨﴾
58. Na mmoja wao akibashiriwa msichana uso wake unasawijika naye amejaa chuki.
يَتَوَارَىٰ مِنَ الْقَوْمِ مِن سُوءِ مَا بُشِّرَ بِهِ أَيُمْسِكُهُ عَلَىٰ هُونٍ أَمْ يَدُسُّهُ فِي التُّرَابِ أَلَا سَاءَ مَا يَحْكُمُونَ ﴿٥٩﴾
59. Anajificha na watu kwa ubaya wa aliyobashiriwa. Je, akae naye juu ya fedheha au amfukie mchangani, Ehe! Yamekuwa maovu wanayoyahukumu.
لِلَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ مَثَلُ السَّوْءِ وَلِلَّـهِ الْمَثَلُ الْأَعْلَىٰ وَهُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ ﴿٦٠﴾
60. Sifa ya wale wasioamini Akhera ni uovu na Mwenyezi Mungu ana sifa tukufu na Yeye ni Mwenye nguvu Mwenye hekima.
Aya 56 – 60
Na ambao hawajui wanawawekea sehemu ya tunavyowaruzuku, Wallahi! Hakika mtaulizwa hayo mliyokuwa mkiyazua.
Wanaoweka ni washirikina na wanaowawekea ni masanamu. Imesemwa ‘hawajui’ kwa masanamu badala ya ‘hayajui’ kwa vile wao wameyaweka daraja ya wenye akili; kama vile ilivyosemwa katika Aya ya 20 ya Sura hii: “Na wale ambao wanawaomba wasiokuwa Mwenyezi Mungu hawaumbi kitu, bali wao wameumbwa.” Kwa hiyo Qur’an imelitumia neno hilo kulingana na itikadi ya washirikina.
Maana ni kuwa washirikina waliyawekea, fungu katika mali zao, masana- mu ambayo yameganda hayana chochote yajualo wala hisia zozote.
Inawezekana kuwa ‘ambao hawajui’ ni washirikina. Kwa maana ya kuwa washirikina waliyawekea fungu masanamu wakiwa hawajui kuwa masanamu hayana fungu lolote katika mali zao wala katika zisizokuwa mali zao. Lakini kufasiri kwa maana haya kunakalifisha kukadiria maneno yasiyokuwepo. Umepita mfano wake katika Juz. 8 (6: 136).
Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu mabinti, Ametakata na hayo! Na hali wao hupata wanavyovitamani
Waliposikia kuwa Mwenyezi Mungu ana Malaika wakafikiria ni wanawake tena ati ni mabinti wa Mungu. Ametakata Mwenyezi Mungu na wanayomsifu. Wakamabandikiza yale wanayoyachukia wao, huku wenyewe wakiwa na wavulana wanaowapenda. Mwenyezi Mungu anasema: “Je, Mola wenu amewachagulia wavulana na Yeye akawafanya Malaika ni wanawake? Kwa hakika nyinyi mnasema kauli kubwa (17: 40).
Baadhi ya tafsiri zinasema kuwa walioitakidi hivi ni Bani Khuza’a na Kinana.
Na mmoja wao akibashiriwa msichana uso wake unasawijika naye amejaa chuki.
Qur’an hutumia neno ‘bishara’ kwa habari njema na mbaya; kwa mfano:
وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ﴿٢٥﴾
“Na wabashirie walioamini na wakafanya vitendo vizuri, kwamba watapata mabustani”
Juz,1 (2:25).
وَبَشِّرِ الَّذِينَ كَفَرُوا بِعَذَابٍ أَلِيمٍ ﴿٣﴾
Na wabashirie waliokufuru adhabu iumizayo, Juz, 10 (9:3).
Kusawijika uso ni fumbo la kuhuzunika sana. Waarabu hulitumia neno hilo kwa mtu aliyepatwa na mambo ya kuchukiza.
Ingawaje hii ni desturi ya kijahili na Qur’an ikaikemia na kuwasafihi watu wake, lakini kuna Waislamu wengi wanachukia kupata watoto wasichana, na wanasawijika nyuso wakipewa habari za kuzaliwa msichana.
Anajificha na watu kwa ubaya wa aliyobashiriwa.
Wakati wa jahiliya, mtu akiwa mkewe anaanza uchungu wa kuzaa anajificha mpaka ajuea atakayezaliwa, akiwa ni mwanamume anajitokeza na kufurahi na akiwa ni mwanamke huhuzunika na kufikiria afanye nini.
Je, akae naye juu ya fedheha abakie na udhaliliau amfukie mchangani akiwa hai? Imesimuliwa kuwa baadhi ya waarabu walikuwa wakiwazika hai watoto wao wa kike, wengine wakiwatupa, wengine wakiwachinja na hata wengine walikuwa wakiwatosa.
Walikuwa wakifanya hivyo ama kwa hasira au kwa kuogopa ukata; kama alivyodokeza Mwenyezi Mungu kwa kusema: “Wala msiwaue watoto wenu kwa kuogopa kuishiwa, sisi tutawaruzuku nyinyi na wao.” Juz. 8 (6:151).
Imesimuliwa kuwa mtu mmoja alisema: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: mimi sina raha tangu nisilimu. Kwani nilikuwa na binti wakati wa ujahili, nikamwaamrisha mke wangu ampambe kisha nikatoka naye hadi kwenye bonde lenye kina nikamtupa huko, akaniambia: ‘Baba yangu unaniua! Kila ninapokumbuka kauli yake hiyo sioni kitu chochote kinachonifaa.
Inaweza kudhania kuwa ukatili huu unatokana na ujinga na kutoendela, lakini sisi hivi sasa tuko kwenye zama za kutembea angani, bado wakoloni na wazayuni wanatupa makombora kwa vikongwe, wanawake na watoto huko Vietnam na Palestina.
Wanayatupa sio kwa hasira za kijinga wala kuhofia ukata; isipokuwa ni kwa sababu ya kuzidisha faida na kurundika utajiri. Sasa ni nani kati ya makundi mawili haya ndio walio waovu zaidi. Je, watu wa jahilia au ni wakoloni na wazayuni walio katika wakati wa elimu na mwanga?
Ehe! Yamekuwa maovu wanayoyahukumu na wanayoyazua na kuyafanya, Sisi tuna hakika kabisa kuwa kila mwenye kuzama kwenye uovu mwisho utamrudia mwenyewe.
Sifa ya wale wasioamini Akhera ni uovu na Mwenyezi Mungu ana sifa tukufu na Yeye ni Mwenye nguvu, Mwenye hekima.
Mataghuti wana sifa mbaya ambayo ni dhulma, unyang’anyi, ufisadi na kuua watoto na wasio na hatia. Na Mwenyezi Mungu ana sifa tukufu ambazo ni umoja, uadilifu, utukufu na sifa zote nzuri za ukamilifu.
Ilivyo ni kuwa lengo la kutaja sifa za Mwenyezi Mungu pamoja na kuwataja wao ni kujibu kauli yao kuwa Mungu ana wasichana na wao wana wavulana.
7
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
وَلَوْ يُؤَاخِذُ اللَّـهُ النَّاسَ بِظُلْمِهِم مَّا تَرَكَ عَلَيْهَا مِن دَابَّةٍ وَلَـٰكِن يُؤَخِّرُهُمْ إِلَىٰ أَجَلٍ مُّسَمًّى فَإِذَا جَاءَ أَجَلُهُمْ لَا يَسْتَأْخِرُونَ سَاعَةً وَلَا يَسْتَقْدِمُونَ ﴿٦١﴾
61. Lau Mwenyezi Mungu angeliwachukulia watu kwa dhulma yao asingeliacha juu yake hata mnyama mmoja, lakini anawaakhirisha mpaka muda uliowekwa, Utakapofika muda wao hawatakawia hata saa moja wala hawatatangulia.
وَيَجْعَلُونَ لِلَّـهِ مَا يَكْرَهُونَ وَتَصِفُ أَلْسِنَتُهُمُ الْكَذِبَ أَنَّ لَهُمُ الْحُسْنَىٰ لَا جَرَمَ أَنَّ لَهُمُ النَّارَ وَأَنَّهُم مُّفْرَطُونَ ﴿٦٢﴾
62. Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu yale wanayoyachukia, Na ndimi zao zitasifia uwongo kwamba wao watapata mema, Hapana shaka hakika wamewekewa moto nao watatangulizwa.
تَاللَّـهِ لَقَدْ أَرْسَلْنَا إِلَىٰ أُمَمٍ مِّن قَبْلِكَ فَزَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ فَهُوَ وَلِيُّهُمُ الْيَوْمَ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٦٣﴾
63. Wallahi! Tulituma kwa umma zilizokuwa kabla yako, Lakini shetani aliwapambia vitendo vyao. Kwa hiyo leo huyo ndiye msimamizi wao na wana wao adhabu chungu.
وَمَا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ إِلَّا لِتُبَيِّنَ لَهُمُ الَّذِي اخْتَلَفُوا فِيهِ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٦٤﴾
64. Na hatukukuteremshia Kitabu isipokuwa uwabainishie yale ambayo wanakhitalifiana na kiwe ni uongofu na rehema kwa watu wanaoamini.
Aya 61 -64
Lau Mwenyezi Mungu angeliwachukulia watu kwa dhulma yao asingeliacha juu yake hata mnyama mmoja, lakini anawakhirisha mpaka muda uliowekwa
Juu yake hapa ni juu ya Ardhi, kutokana, mfumo wa maneno ulivyo na pia neno mnyama linafahamisha hivyo. Mtu amemdhulumu Muumba wake kwa kumkana, kumfanyia washirika na kuwa ana mtoto. Vile vile mtu mwenye nguvu amemdhulumu ndugu yake mdhaifu, akamafanya mtumwa na akampora nguvu yake na nyenzo za maisha yake.
Pia mwenye kiburi amejidhulumu kwa kupetuka mipaka na ghururi. Lakini pamoja na yote hayo Mungu hakumharakishia adhabu; Kwani ana haraka ya nini? Anaogopa wakati usimpite au anahofia waasi wasitubie; na yeye ndiye aliyewahimiza kufanya hivyo?
Imesemekana kuwa anawacheleweshea ili waweze kurejea kwenye toba. Hilo haliko mbali kutokana na upole, huruma na ukarimu wake.
Aya hii inafanana na ile isemayo: “Na Mola wako ni mwenye maghufira, mwenye rehema. Lau angeliwachukulia kwa yale waliyoyachuma angeliwaharakishia adhabu, lakini wanayo miadi ambayo hawatapata makimbilio yoyote ya kuepukana nayo” (18: 58).
Utakapofika muda wao hawatakawia hata saa moja wala hawatatangulia.
Imetangulia tafsiri yake katika Juz; 4 (3: 144 -148) kifungu cha ‘Ajali haina kinga’ Pia imetajwa neno kwa neno katika Juz; 8 (7:34).
Na wamemfanyia Mwenyezi Mungu yale wanayoyachukia wao ya kuwa na mabinti na kushirikiana uongozi.
Na ndimi zao zitasifia uwongo kwa kusema kwaokwamba wao watapata mema; yaani Pepo.
Wamemzulia Mwenyezi Mungu kwamba Yeye ana washirika na ana mabinti; kisha wakasema uwongo kwamba wao watapata Pepo; ndio Mwenyezi Mungu akawakadhibisha kwa kusema:Hapana shaka hakika wamewekewa moto nao watatangulizwa; yaani wataharakishwa.
Wallahi! Tulituma – Mitume –kwa umma zilizokuwa kabla yako ewe Muhammad, lakini hawakuwaitikia mitume wao, bali waliachana nao na wakawaudhi; kama walivyokufanyia wewe washrikina wa kiqurayishi, basi poa moyo wala usihuzunike.
Lakini shetani aliwapambia vitendo vyao ambavyo ni kufru, upotevu, ukiukaji mipaka na ufisadi.
Kwa hiyo leo huyo ndiye msimamizi wao leo na wana wao adhabu chungu.
Shetani alitawala mambo ya mataghuti katika maisha ya dunia baada ya kumpa hatamu za uongozi, kwa hiyo akawaongoza kwenye madhambi na maangamizi. Basi malipo yake na yao kwa Mwenyezi Mungu ni Jahannam, ni mahali pabaya kabisa.
Imam Aliy anasema: “Ajali ya mtu imefichwa, tamaa yake imemhadaa, na shetani ni wakala wake, anampambia maasi ili ayafanye, na anamdhoofisha na toba ili aipe muda. Mpaka ukifika muda anaghafilika na aliyokuwa nayo” yaani anakufa kwenye upotevu na maasi, nayo ni mauti mabaya.
Na hatukukuteremshia Kitabu isipokuwa uwabainishie yale ambayo wanakhitalifiana na kiwe ni uwongofu na rehema kwa watu wanaoamini
Maneno haya anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) na Kitabu ni Qur’an nayo ni uwongofu na rehema kwa mwenye kutaka. Pia ndiyo hukumu inayofafanua kila itikadi na kila sharia na ni kauli na vitendo, “Ewe Mola utujaalie ni wenye kushikamana na kamba yake na kuongoka na uongozi wake”.
وَاللَّـهُ أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَحْيَا بِهِ الْأَرْضَ بَعْدَ مَوْتِهَا إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَسْمَعُونَ ﴿٦٥﴾
65. Na Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni na kwayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaosikia.
وَإِنَّ لَكُمْ فِي الْأَنْعَامِ لَعِبْرَةً نُّسْقِيكُم مِّمَّا فِي بُطُونِهِ مِن بَيْنِ فَرْثٍ وَدَمٍ لَّبَنًا خَالِصًا سَائِغًا لِّلشَّارِبِينَ ﴿٦٦﴾
66. Na katika wanyama mna mazingatio. Tunawanywesha katika vile vilivyomo matumboni mwao, vikatoka, baina ya kinyesi na damu, maziwa safi, mazuri kwa wanywao.
وَمِن ثَمَرَاتِ النَّخِيلِ وَالْأَعْنَابِ تَتَّخِذُونَ مِنْهُ سَكَرًا وَرِزْقًا حَسَنًا إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴿٦٧﴾
67. Na kutokana na matunda ya mitende na mizabibu mnatengeneza kileo na riziki nzuri. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaotumia akili.
وَأَوْحَىٰ رَبُّكَ إِلَى النَّحْلِ أَنِ اتَّخِذِي مِنَ الْجِبَالِ بُيُوتًا وَمِنَ الشَّجَرِ وَمِمَّا يَعْرِشُونَ ﴿٦٨﴾
68. Na Mola wako akampa wahyi nyuki kwamba, tengeneza nyumba katika milima, na katika miti, na katika wanaoyajenga.
ثُمَّ كُلِي مِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ فَاسْلُكِي سُبُلَ رَبِّكِ ذُلُلًا يَخْرُجُ مِن بُطُونِهَا شَرَابٌ مُّخْتَلِفٌ أَلْوَانُهُ فِيهِ شِفَاءٌ لِّلنَّاسِ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَةً لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٦٩﴾
69. Kisha kula katika kila matunda na ufuate njia za Mola wako zilizo dhalili. Na katika matumbo yao kinatoka kinywaji chenye rangi mbalimbali, ndani yake kina matibabu kwa watu. Hakika katika haya kuna ishara kwa watu wanaofikiri.
MWENYEZI MUNGU AMETERMSHA MAJI KUTOKA MBINGUNI
Aya 65 – 69
Katika Juz. 7 (6: 134) Mwenyezi Mungu amerudisha dhamir ya wanyama kwa muannath ( ya kike) na hapa ameirudisha kwa dhamir ya mudhakkar (ya kiume). Wamejibu kwamba dhamir hapa inarudia kwenye baadhi; yaani baadhi ya wanyama ambao ni wakike, na kule inarudia kwa wanyama wote.
Na Mwenyezi Mungu ameteremsha maji kutoka mbinguni na kwayo akaihuisha ardhi baada ya kufa kwake. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaosikia kwa kuzingatio na kutilia manani maji na faida zake.
Aya hii na inayofuatia ni katika Aya za mambo ya ulimwengu ambazo Qur’an inazikariri kwa lengo la kuleta uzinduzi kwenye dalili za Tawhid na ufufuo, Aya hii imekwishapita katika Juz.1 (2:22, 164), Juz. 7: (6:99), Juz. 13 (13: 17), (14: 32) na sura hii tunayoifasiri Aya ya 6.
Na katika wanyama mna mazingatio, Tunawanywesha katika vile vilivyomo matumboni mwao, vikatoka, baina ya kinyesi na damu, maziwa safi, mazuri kwa wanywao.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja baadhi ya faida za wanyama katika Juz; 8 (6:142) aliposema: “Na katika wanyama wale wabebao na wa kutoa matandiko.”
Katika sura hii tuliyo nayo, mbele, kwenye Aya 80, amesema: “Na akawafanyia kutokana na ngozi za wanyama wenu nyumba mnazoziona nyepesi siku ya kusafiri kwenu na siku ya kutulia kwenu.
Na katika sufu zao na manyoya yao na nywele zao mnatengeneza vyombo na vifaa vya kutumia kwa muda.” Mwanzoni mwa sura hii amekusanya faida za wanyama kwa kuhusisha maziwa akasema kuwa yanatoka katika matumbo ya baadhi ya wanyama; yaani wa kike, Angalia kifungu cha Nahw.
Wataalamu wanasema kuwa wanyama wanakula mimea, baada ya kutafuna matumbo yanatoa nje kinyesi chenye madhara na kufyonza majimaji yenye manufaa ambayo yanageuka damu inayotembea kwenye mishipa. Baadhi ya damu hii inapofika kwenye viwele inageuka na kuwa maziwa safi ya kunywa.
Na kutokana na matunda ya mitende na mizabibu mnatengeneza kileo na riziki nzuri. Hakika katika hayo kuna ishara kwa watu wanaotumia akili
Dhahiri ya neno kileo hapa ni kinywaji chochote kinacholevya, kiwe ni pombe au kitu kingine. Lakini Aya haidokezi hukumu ya ulevi kwa umbali wala karibu; kwamba wakati huo iliposhuka ulevi ulikuwa halali au haramu; isipokuwa inaelezea desturi ya watu kwamba wao wanatengeneza kinywaji na ulevi kutokana na matunda ya mitende na mizabibu. Ama riziki nzuri makusudio yake ni tende mbichi na za kuiva, zabibu mbichi na kavu, siki, jamu n.k.
Yamekuja maelezo kutoka baadhi ya mapokezi kwamba makusudio ya kileo katika Aya, ni kilicho haramu na riziki nzuri ni kilicho halali.
Tumefafanua dalili za uharamu wa pombe katika Juz. 2 (2: 219) na pia katika kitabu Fiqhul-imam Ja’far asswadiq Mlango wa Al-at’ima wa wal Ashriba (Vyakula na vinywaji)
Na Mola wako akampa wahyi nyuki.
Makusudio ya wahyi hapa ni maumbile ya akili ambayo Mwenyezi Mungu alimpa nyuki.
Kwamba tengeneza nyumba katika milima na katika miti na katika wanaoyajenga.
Yaani wanayoyajenga watu.
Razi anasema: “Kuna aina mbili za nyuki: Ile inayokaa milimani na kwenye misitu, hawashughulikiwi na mtu yoyote. Ndio makusudio ya kusema kwake Mwenyezi Mungu: ‘Kwamba tengeneza nyumba katika milima na katika miti’ na aina nyingine inakaa katika majumba ya watu na wanashughulikiwa na watu. Ndio makusudio ya kauli yake: ‘katika wanaoyajenga’.
Kisha kula katika kila matunda maua na mimea unayoipenda,Na ufuate njia za Mola wako zilizo dhalili. Yaani ni dhalili kwa kwa ajili yako wewe nyuki ili upate wepesi wa kupita
Na katika matumbo yao kinatoka kinywaji amabacho ni asali wanayoitema kama mate.Chenye rangi mbali mbali nyeupe, nyekundu na yanjano, kulingana na mimea waliyokula.
Ndani yake kina matibabu kwa watu; kama vile ukosefu wa damu, kutosagika vizuri chakula tumboni, vidonda vya mdomoni, matatizo ya mapafu na kibofu cha mkojo. Pia maradhi ya figo na mengineyo waliyoyataja watabibu.
Hakika katika haya kuna ishara kwa watu wanaofikiri katika alivyoviumba Mwenyezi Mungu na maajabu yake yanayofahamisha kuweko mpangiliaji hodari Mwenye hekima.
Wataalamu wameandika mengi kuhusu mipangilio ya hali ya juu ya nyuki, nidhamu yake na jinsi wanavyosaidiana katika maisha yao, kujenga nyumba na usalam, Huko nyuma tumeashiria kwamba hatimae imegunduliwa kuwa linapozidi joto nyuki huanza kazi ya kuchukua maji kwenye visiku vyao.
Wengine wanayanyunyiza ndani ya masega na wengine wanatingisha mbawa zao ili wafanye tiyara ya hewa. Kwa hiyo maji yananyunyizika kwa haraka jambo ambalo linafanya joto lipungue.
Mfano huu pekee unatosheleza yote yaliyoandikwa kuhusiana na mpangilio wa nyuki.
وَاللَّـهُ خَلَقَكُمْ ثُمَّ يَتَوَفَّاكُمْ وَمِنكُم مَّن يُرَدُّ إِلَىٰ أَرْذَلِ الْعُمُرِ لِكَيْ لَا يَعْلَمَ بَعْدَ عِلْمٍ شَيْئًا إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ قَدِيرٌ ﴿٧٠﴾
70. Na Mwenyezi Mungu amewaumba kisha anawafisha, na miongoni mwenu wapo wanaorudishwa kwenye umri dhaifu kabisa ili asijue kitu baada ya kujua. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye uweza.
وَاللَّـهُ فَضَّلَ بَعْضَكُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ فِي الرِّزْقِ فَمَا الَّذِينَ فُضِّلُوا بِرَادِّي رِزْقِهِمْ عَلَىٰ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَهُمْ فِيهِ سَوَاءٌ أَفَبِنِعْمَةِ اللَّـهِ يَجْحَدُونَ ﴿٧١﴾
71. Na Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika riziki, Na wale waliofadhilishwa hawarudishi riziki zao kwa wale ambao imewamiliki mikono yao ya kulia ili wawe sawa katika riziki hiyo, Basi je, wanazikataa neema za Mwenyezi Mungu?
وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَجَعَلَ لَكُم مِّنْ أَزْوَاجِكُم بَنِينَ وَحَفَدَةً وَرَزَقَكُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ أَفَبِالْبَاطِلِ يُؤْمِنُونَ وَبِنِعْمَتِ اللَّـهِ هُمْ يَكْفُرُونَ ﴿٧٢﴾
72. Na Mwenyezi Mungu amewafanyia wake kutokana na nyinyi wenyewe. Na amewafanyia kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu na akawaruzuku vitu vizuri. Basi je, wanaamini upotofu na wanazikufuru neema za Mwenyezi Mungu?
وَيَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ مَا لَا يَمْلِكُ لَهُمْ رِزْقًا مِّنَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ شَيْئًا وَلَا يَسْتَطِيعُونَ ﴿٧٣﴾
73. Na badala ya Mwenyezi Mungu wanaabudu wasiowamilikia riziki yoyote kutoka mbinguni na ardhini wala hawana uwezo.
فَلَا تَضْرِبُوا لِلَّـهِ الْأَمْثَالَ إِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿٧٤﴾
74. Basi msimpigie Mwenyezi Mungu mifano. Hakika Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.
MUNGU AMEFADHILISHA BAADHI YENU KATIKA RIZKI
Aya 70 – 74
Na Mwenyezi Mungu amewaumba kisha anawafisha na miongoni mwenu wapo wanaorudishwa kwenye umri dhaifu kabisa ili asijue kitu baada ya kujua. Hakika Mwenyezi Mungu ni mjuzi mwenye uweza.
Mtu anapitia hatua nyingi, kuanzia utoto hadi ubarobaro na ujana. Na kuanzia ujana hadi uzee na ukongwe. Kila hatua ina sababu zake za kimaumbile. Zinategemezwa kwake Mwenyezi Mungu kwa vile Yeye ndiye aliyeyaumba maumbile.
Umri dhaifu ni ukongwe ambapo mwili, akili, kumbukumbu na hisia nyingine za ndani na nje zote zinaadhoofika. Na zikishadhoofika hivyo basi hapo ndio mwisho wake, hazitarajiwi kurudia hali yake ya kwanza; bali zinazidi kudhoofika kila siku zinaavyozidi kupita; hasa kumbukumbu, ndio zinaakosekana kabisa na kurudia hali ya utoto; kama kwamba hakuwahi kujifundisha chochote wala kufanya majaribio yoyote.
Na Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika riziki, Na wale waliofadhilishwa hawarudishi riziki zao kwa wale ambao imewamiliki mikono yao ya kulia ili wawe sawa katika riziki hiyo, Basi je, wanazikataa neema za Mwenyezi Mungu?
Baadhi wamefikiri dhahiri ya Aya hii inafahamisha kuwa riziki ni kwa qadha na qadari ya Mungu. Kwamba Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu ndiye aliyemfanya huyu kuwa tajiri na yule kuwa fukara.
Lakini Aya iko mbali tena mbali, sana na maana haya, kwa sababu imeku- ja kuwarudi washirikina. Ufafanuzi wa hilo ni kwamba washirikina walimfanyia Mwenyezi Mungu washirika, Mwenyezi Mungu akawarudi kwa kuwambia kuwa nyinyi washirikina hamridhii watumwa wenu washirikiane nanyi kwenye mali zenu na kuwa wao ni sawa na nyinyi katika riziki zenu na milki zenu.
Ikiwa nyinyi hamkubali hivyo, imekuwaje fahamu zenu zione kuwa ni sawa watumwa wa Mwenyezi Mungu wawe washirika wake katika kuumba kwake?
Kwa maneno mengine ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewapa hoja ya mantiki yao na makisio yao kwa kuwaambia: Nyinyi mnajifanya ni mabwana na mna watumwa wasiokuwa na chochote, basi ni kwa mantiki gani mkasema kuwa masanamu au wengineo katika watumwa wa Mungu wasiokuwa na chochote wawe wana chochote?
Unaweza kuuliza : Kauli ya Mwenyezi Mungu ‘Na Mwenyezi Mungu amewafadhilisha baadhi yenu kuliko wengine katika riziki’ si inafahamisha kuwa kuzidiana riziki ni kwa qadha ya Mwenyezi Mungu na qadari yake?
Jibu : Tumekariri mara kwa mara kuwa kuitegemeza riziki kwa Mungu ni kwa upande wa kutegemeza kitu kwenye sababu yake ya kwanza na kwa kuizindua akili kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Muumba wa ulimwengu na vilivyomo. Tumezungumzia kwa ufafanuzi suala hilo kwa anuani ya ‘Riziki na ufisadi’ kwenye Juz. 6 (5: 64-66) na kwa anuani ya ‘Je, riziki ni bahati au majaliwa?’ katika Juz, 7 (7:100), Pia ‘Mtu na riziki’ katika Juz, 13 (13: 26).
Na Mwenyezi Mungu amewafanyia wake kutokana na nyinyi wenyewe.
Yaani katika jinsi yenu, sio duni wala ya hali ya juu, ili ukamailike utu kwa pande mbili, zisadiane na zishirikiane katika maisha kwa pande zote.
Tafsiri iliyo wazi zaidi ya jumla hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِّتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُم مَّوَدَّةً وَرَحْمَةً ﴿٢١﴾
Na katika ishara zake ni kuwa amewaumbia wake zenu kutokana na nyinyi wenyewe ili mpate utulivu kwao na amejalia baina yenu mapenzi na huruma”(30:21).
Na amewafanyia kutoka kwa wake zenu wana na wajukuu.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja neema ya wake, sasa anataja neema ya watoto nao ni kipambo cha dunia kama mali.
Na akawaruzuku vitu vizuri : vyakula, vinywaji, kivazi, maskani na vipando kuongezea wake na watoto, Baada ya neema zote hiziBasi je, wanaamini upotofu?
Makusudio ya upotofu hapa ni wale wanaowashirikisha na Mungu kwa kuamini kuwa ndio wanaowapa neema wao au kwa kushirikiana na Mwenyezi Mungu.
Na wanazikufuru neema za Mwenyezi Mungu? kwa kula riziki yake na kumwabudu mwingine
Na badala ya Mwenyezi Mungu wanaabudu wasiowamilikia riziki yoyote kutoka mbinguni na ardhini wala hawana uwezo.
Riziki ya mbinguni ni mvua na riziki ya ardhini ni mimea na madini. Wasiowamilikia riziki ni masanamu. Maana ya kuwa hawana uwezo ni kuwa masanamu hayana uwezo kabisa wala kuweza kumiliki.
Basi msimpigie Mwenyezi Mungu mifano kwa kumfanya kuwa ana wanoshabihiana naye: “Hapana kitu kama mfano wake, Na Yeye ni mwenye kusikia Mwenye kuona” (42:11).
Hakika Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.
Kutokana na elimu yake Mwenyezi Mungu Mtukufu na ujinga wenu, basi ni wajibu kwenu kutofanya au kusema jambo lolote isipokuwa yale aliyowafundisha Mwenyezi Mungu kupitia kwa manabii na mitume yake.
8
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
ضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا عَبْدًا مَّمْلُوكًا لَّا يَقْدِرُ عَلَىٰ شَيْءٍ وَمَن رَّزَقْنَاهُ مِنَّا رِزْقًا حَسَنًا فَهُوَ يُنفِقُ مِنْهُ سِرًّا وَجَهْرًا هَلْ يَسْتَوُونَ الْحَمْدُ لِلَّـهِ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٧٥﴾
75. Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mtumwa mwenye kumilikiwa asiyeweza kitu, na mwengine tuliyemruzuku riziki njema inayotoka kwetu, naye anatoa katika riziki hiyo kwa siri na kwa dhahiri, Je, wanalingana sawa? Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu; bali wengi wao hawajui.
وَضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا رَّجُلَيْنِ أَحَدُهُمَا أَبْكَمُ لَا يَقْدِرُ عَلَىٰ شَيْءٍ وَهُوَ كَلٌّ عَلَىٰ مَوْلَاهُ أَيْنَمَا يُوَجِّههُّ لَا يَأْتِ بِخَيْرٍ هَلْ يَسْتَوِي هُوَ وَمَن يَأْمُرُ بِالْعَدْلِ وَهُوَ عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٧٦﴾
76. Na Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa watu wawili. Mmoja wao ni bubu hawezi chochote, naye ni mzigo kwa bwana wake, Popote anapomuelekeza haleti kheri. Je, huyo anaweza kuwa sawa na yule anayeamrisha uadilifu, naye yuko juu ya njia iliyonyooka?
وَلِلَّـهِ غَيْبُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا أَمْرُ السَّاعَةِ إِلَّا كَلَمْحِ الْبَصَرِ أَوْ هُوَ أَقْرَبُ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٧٧﴾
77. Mwenyezi Mungu ana siri zote za mbingu na ardhi. Wala halikuwa jambo la saa (ya kiyama) ila kama kupepesa kwa jicho au karibu zaidi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Aya 75 – 77
Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mtumwa mwenye kumilikiwa asiyeweza kitu, na mwengine tuliyemruzuku riziki njema inayotoka kwetu, naye anatoa katika riziki hiyo kwa siri na kwa dhahiri, Je, wanalingana sawa?
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja, katika Aya iliyotangulia, kwamba washirikina wamemfanyia Mungu mfano, hapa anataja mifano miwili ya kuwafahamisha washirikina kwamba Mwenyezi Mungu hana wa kufanana naye.
Kwa ufupi mfano wa kwanza unaoelezwa na Aya hii, ni kuwa mfano wenu enyi washirikina katika kumfanya Mungu kuwa ni sawa na masanamu unafanana na anayemfanya mtumwa asiyemiliki chochote na kushindwa kufanya chochote kuwa ni sawa na aliye huru ambaye ni tajiri tena mkarimu anatoa kwa siri na kwa dhahiri bila ya kumwogopa yeyote.
Ikiwa akili na maumbile zinaakataa usawa huu, basi imekuwaje nyinyi kumfanya sawa Mwenyezi Mungu Mwenye uweza wa kila kitu na masana- mu yasiyioweza chochote?
Sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu.
Hii ni jumla iliyoingia kati, ikiwa na maana kuwa hakuna yeyote anayestahiki sifa, shukrani na kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu peke yake.
Bali wengi wao hawajui kuwa sifa njema zinaamstahiki Mungu tu sio mwengine.
Na Mwenyezi Mungu anapiga mfano wa watu wawili. Mmoja wao ni bubu hawezi chochote, naye ni mzigo kwa bwana wake, Popote anapomuelekeza haleti kheri. Je, huyo anaweza kuwa sawa na yule anayeamrisha uadilifu, naye yuko juu ya njia iliyonyooka?
Huu ni mfano wa pili. Kwa ufupi ni kuwa bubu anayeshindwa na kila kitu hawezi kuwa sawa na anayetamka. Kwa hiyo vipi nyinyi washirikina mnafanya ni sawa katika ibada baina ya mwenye kuwa na sifa zote za ukamailifu na ambaye si chochote?
Mwenyezi Mungu ana siri zote za mbingu na rdhi.
Kila siri mbele ya Mwenyezi Mungu inajulikana na kila ghaibu kwake inaonekana. Punde tu imetangulia Aya ya 73 ya sura hii isemayo: ‘Hakika Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.’
Wala halikuwa jambo la saa (ya kiyama) ila ni kama kupepesa kwa jicho au karibu zaidi.
Hii ni ibara nyingine ya: “Hakika amri yake anapotaka kitu ni kukiambia kuwa na kikawa”. Ndani yake mna makemeo na kumuhofisha yule anayehalifu na akawa na inadi.
Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Wala hakuna yeyote anayeweza kumzuia akitaka kuwaangamiza washirikina na viumbe wote
وَاللَّـهُ أَخْرَجَكُم مِّن بُطُونِ أُمَّهَاتِكُمْ لَا تَعْلَمُونَ شَيْئًا وَجَعَلَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ ﴿٧٨﴾
Na Mwenyezi Mungu amewatoa matumboni mwa mama zenu hamjui kitu, na amewajaalia usikizi na uoni na nyoyo ili mpate kushukuru.
أَلَمْ يَرَوْا إِلَى الطَّيْرِ مُسَخَّرَاتٍ فِي جَوِّ السَّمَاءِ مَا يُمْسِكُهُنَّ إِلَّا اللَّـهُ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٧٩﴾
79. Je, hawaoni ndege waliowezeshwa katika anga ya mbingu? Hawazuii isipokuwa Mwenyezi Mungu, Hakika katika haya kuna ishara kwa watu wanaoamini.
وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُم مِّن بُيُوتِكُمْ سَكَنًا وَجَعَلَ لَكُم مِّن جُلُودِ الْأَنْعَامِ بُيُوتًا تَسْتَخِفُّونَهَا يَوْمَ ظَعْنِكُمْ وَيَوْمَ إِقَامَتِكُمْ وَمِنْ أَصْوَافِهَا وَأَوْبَارِهَا وَأَشْعَارِهَا أَثَاثًا وَمَتَاعًا إِلَىٰ حِينٍ ﴿٨٠﴾
80. Na Mwenyezi Mungu amewafanyia majumba yenu yawe ni maskani. Na akawafanyia kutokana na ngozi za wanyama wenu nyumba mnazoziona nyepesi siku ya kusafiri kwenu na siku ya kutulia kwenu. Na katika sufu zao na manyoya yao na nywele zao mnatengeneza vyombo na vifaa vya kutumia kwa muda.
وَاللَّـهُ جَعَلَ لَكُم مِّمَّا خَلَقَ ظِلَالًا وَجَعَلَ لَكُم مِّنَ الْجِبَالِ أَكْنَانًا وَجَعَلَ لَكُمْ سَرَابِيلَ تَقِيكُمُ الْحَرَّ وَسَرَابِيلَ تَقِيكُم بَأْسَكُمْ كَذَٰلِكَ يُتِمُّ نِعْمَتَهُ عَلَيْكُمْ لَعَلَّكُمْ تُسْلِمُونَ ﴿٨١﴾
81. Mwenyezi Mungu amewafanyia vivuli katika alivyoviumba na amewafanyia makazi katika milima na amewafanyia nguo za kuwakinga na joto na nguo za kuwakinga na vita vyenu. Ndio hivyo anatimiza neema zake kwenu ili mpate kusilimu.
فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿٨٢﴾
82. Na kama wakikengeuka, basi juu yako ni kufikisha tu ujumbe ulio wazi.
يَعْرِفُونَ نِعْمَتَ اللَّـهِ ثُمَّ يُنكِرُونَهَا وَأَكْثَرُهُمُ الْكَافِرُونَ ﴿٨٣﴾
Wanazijua neema za Mwenyezi Mungu kisha wanazikanusha, Na wengi wao ni makafiri.
MWENYEZI MUNGU AMEWATOA MATUMBONI MWA MAMA ZENU HAMJUI KITU
Aya 78 – 83
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja katika Aya hizi baadhi ya dalili za kuweko Muumbaji mwenye kupangilia mambo vizuri, Wakati huo huo dalili hizo ni katika neema za Mwenyezi Mungu kwa waja wake. Dalili hizo ni hizi zifuatazo:
Na Mwenyezi Mungu amewatoa matumboni mwa mama zenu hamjui kitu na amewajaalia usikizi na uoni na nyoyo ili mpate kushukuru.
Mtu anatoka tumboni mwa mama yake hajui chochote, lakini Mwenyezi Mungu ana zana za maarifa za hisia ambazo ni usikizi na uoni na zana za maarifa ya kiakili ambazo ni akili na maumbile.
Wanaoamini maada wanasema kuwa maada pofu na kiziwi imejianzishia hiyo yenyewe usikizi, uoni na akili. Sisi tunawajibu hivi: Kwanza, asiye nacho hawezi kutoa kitu. Pili, ikiwa maisha na utambuzi unahusika na maada tu basi itabidi usikizi, uoni na moyo uwe ni maada; Kwa sababu kuenea sababu kunapeleka kuenea msababishaji.
Wakisema kuwa kwenye maada kuna aina maalum inayohusika nayo; Kwa namna ambayo inakuwa ni lazima mwili usikie uone na utambue, nasi tutawaambia: ama mseme kwamba maada hiyo yenyewe ndiyo iliyoleta uhai na utambuzi au mseme hapana. Mkisema ndio, itakuwa ni lazima maada iwe na uhai na utambuzi. Mkisema hapana, itakuwa ni lazima maada yote isiwe na uhai kabisa.
Yote mawili hayawezekani; Kwa sababu imeshuhudiwa waziwazi kwamba baadhi ya maada zimeganda na nyingine ziko hai na utambuzi. Na mgawanyiko huu unajulisha kuwa nyuma ya maada kuna nguvu yenye ujuzi na hekima; ndiyo ambayo imeleta uhai, na utambuzi kwenye baadhi ya maada na kuleta kutofautiana kwenye hizo maada.
Je, hawaoni ndege waliowezeshwa katika anga ya mbingu? Hawazuii isipokuwa Mwenyezi Mungu, Hakika katika haya kuna ishara kwa watu wanaoamini.
Makusudio ya kuwezeshwa hapa ni kuwezeshwa kuruka angani; na kuzuwiya ni kuzuiwa wasianguke; mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu:
أَوَلَمْ يَرَوْا إِلَى الطَّيْرِ فَوْقَهُمْ صَافَّاتٍ وَيَقْبِضْنَ مَا يُمْسِكُهُنَّ إِلَّا الرَّحْمَـٰنُ ﴿١٩﴾
“Kwani hawaoni ndege walioko juu yao wanavyozikunjua mbawa na kuzikunja, hawazuii isipokuwa Mwingi wa rehema” (67:19).
Ni wazi kuwa Mwenyezi Mungu anapitisha mambo kwenye sababu zake, Inaeleweka kwamba Mwenyezi Mungu akilitaka jambo huliandalia sababu.
Kwa hiyo maana ya kauli yake Mungu: ‘Hawazuii isipokuwa Mwingi wa rehema’ ni kwamba Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaumbia ndege mbawa mbili na akaziwekea vitu vinavyowezesha kuruka angani baina ya mbingu na ardhi:
فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا ﴿٢﴾
“Na ameumba kila kitu akakikadiria kwa kipimo (chake)”, (25:2).
إِنَّا كُلَّ شَيْءٍ خَلَقْنَاهُ بِقَدَرٍ ﴿٤٩﴾
“Hakika sisi kila kitu tumekiumba kwa kipimo,” (54:49).
Kwa hiyo kuumba, kukadiria na mpangilio ni dalili wazi kuwa kuna Muumbaji mwenye kupangilia vizuri.
Kuna wanouliza, kuwa : binadamu amevumbua ndege inayokwenda kwa kasi zaidi ya sauti, akatengeneza roketi inayokata maelfu ya maili kwa muda wa saa, ikaweza kufika hadi mwezini. Tena binadamu huyo akatengeneza satelaiti inazozunguuka ardhini na mwezini na kuzungumza na wataalamu kwa lugha zao kutoka huko iliko. Sasa ndege wanoruka angani ni kitu gani mbele ya uvumbuzi huu?
Jibu : Ajabu ya mtu na akili zake kuuliza swali kama hili. Anashangazwa na ugunduzi huu akisahau yule aliyeifanya akili iliyoweza kugundua vitu hivyo? Lau mtu atafanya insafu akajiangalia yeye mwenyewe na akili yake, ataiona ni kubwa zaidi kuliko kuvumbua maroketi, madege n.k.
Bali lau atafanya insafu akaangalia ulimwengu, atauona ni mkubwa kuliko kuumbwa binadamu aliyevumbua maroketi na masatalaiti. Mwenyezi Mungu anasema:
لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٥٧﴾
“Hakika kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa zaidi kuliko kuwaumba watu, lakini watu wengi hawajui” (40:57)
na kuumba mtu ni kukubwa mara nyingi zaidi kuliko kutengeneza maroketi.
Zaidi ya hayo mazungumzo tangu mwanzo yalikuwa juu ya mnyama ndege aliye hai. Ama ndege za kutengeneza, roketi na satalaiti ni katika vitu visivyo na uhai. Kwa hiyo kuvilinganisha na vyenye uhai si mahali pake. Ni wazi kuwa wataalamu wa maroketi wakichanganyika na wataalamu wa kijini hawawezi kuumba nzi hata ubawa wake:
لَن يَخْلُقُوا ذُبَابًا وَلَوِ اجْتَمَعُوا لَهُ وَإِن يَسْلُبْهُمُ الذُّبَابُ شَيْئًا لَّا يَسْتَنقِذُوهُ مِنْهُ ﴿٧٣﴾
“Hawataumba hata nzi ijapokuwa watajumuika kwa hilo, Na nzi akiwapokonya kitu hawawezi kukipata kwake” (22:73).
Kwa hakika Mwenyezi Mungu ametegemeza kuzuiya ndege angani kwake moja kwa moja kwa vile yeye ndiye sababu ya kwanza na akamapa viungo vya kurukia.
Ashaira wamekana kuweko sababu za kimaumbile kwa aina zote na wakasema, kila vitendo vinategemezwa kwa Mwenyezi Mungu moja kwa moja bila ya kuingia kati kitu chochote kwa namna yoyote ile; ni sawa vitendo hivyo vijitokeze kwenye ndege au wadudu, wanyama au binadamu, au hata kwenye maumbile mengine.
Kwa hiyo, kwa upande wao, hakuna uhusiano wowote baina ya kuungua na moto, au kuondoka kiu na kunywa maji, wala baina ya kushiba na kula. Mwenyezi Mungu ndiye anayeunguza wakati wa kugusa moto, ndiye anayeondoa kiu wakati wa kunywa maji na pia ndiye anayeshibisha wakati wa kula, sio kuwa moto wenyewe ndio uliounguza, au maji kuondoa kiu au kuwa chakula ndio kilichoondoa njaa.
Kujibu hoja hiyo inatosha tu kusema kuwa hilo linapingana na hisia na dhamira. Na kwamba linapelekea kuwa mtu ni sawa na mnyama na vitu visiyo na harakati; hawezi kusifika kwa wema wala ubaya na kuwa ni mwenye hatia au asiye na hatia.
Kwa hiyo hatastahiki sifa wala lawama au thawabu wala adhabu; Kwa sababu Mungu ndiye mtendaji na mtu ni chombo tu; sawa na chombo cha kuwekea maji
Na Mwenyezi Mungu amewafanyia majumba yenu yawe ni maskani.
Makusudio ya maskani hapa ni utulivu kutokana na neno la kiarabu sakan; yaani kutulia majumbani, majumba haya ni yale yanayojengwa kwa miti, mawe simiti n.k.
Na akawafanyia kutokana na ngozi za wanyama wenu nyumba mnazoziona nyepesi siku ya kusafiri kwenu na siku ya kutulia kwenu.
Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja majumba yaliyojengwa, sasa anataja majumba ya kutembea nayo; kama vile mahema. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametaja ngozi na wala hakuaja katani n.k., kwa sababu ngozi ndiyo iliyokuwa ikitumika zaidi katika nchi za uarabuni. Vyovyote itakavyokuwa nyumba, itakuwa inafahamisha kupatikana aliyeiumba na kuitengeneza.
Imenipendeza ibara ya mwanafasihi mmoja na fasaihi yake, ninamnukuu: “kila kilicho juu yako kikakufunika basi ni paa, kila kilicho chini yako basi ni sakafu na kila kinachokusitiri katika pembe nne basi ni kuta, Vyote hivyo ukivipangilia na ukavishikanisha basi hiyo ni nyumba.”
Aina zote za nyumba ni katika neema za Mwenyezi Mungu. Haijui thamani yake ila yule asiyekuwa nayo. Nyumba ina heshima zake katika sharia ya kiislamu; miongoni mwazo ni kutoingia mtu bila ya hodi na kukaribishwa. Mwenyezi Mungu anasema:
فَلَا تَدْخُلُوهَا حَتَّىٰ يُؤْذَنَ لَكُمْ وَإِن قِيلَ لَكُمُ ارْجِعُوا فَارْجِعُوا ﴿٢٨﴾
“Basi msiyaingie mpaka mpewe idhini na mkiambiwa rudini basi rudini” (24:28).
Wanafiqh wanasema kuwa mwenye kuchungulia nyumba ya mtu kutoka tunduni au kwenye mwanya wa mlango n.k., mwenye nyumba anayo haki ya kumkemea, akiendela anayo haki ya kumpiga au kumrushia jiwe n.k., akipata madhara mchunguliaji basi ni shauri yake, mwenye nyumba hana lawama yoyote.
Kuna Hadith ya Mtume(s.a.w.w) isemayo:“Mwenye kukuchungulia ukimtupia jiwe na jicho lake likapofuka basi huna lawama.” Imam Jafar As- swadiq(a.s) amesema:“Tupu ya muumini ni haramu kwa muumini Mwenye kumchungulia muumini katika nyumba yake, basi macho yake ni halali yake katika hali hiyo.”
Na katika sufu zao na manyoya yao na nywele zao mnatengeneza vyombo na vifaa vya kutumia kwa muda.
Makusudio ya vyombo hapa ni mahitaji ya mtu, kama vile matandiko, mavazi n.k. Vifaa ni kila kinachomnufaisha mtu katika mahitaji yake. Kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘kwa muda’ ni ishara ya kuwa vitu vyote vya maisha ya hapa duniani ni vya muda sio vya kudumu.
Mwenyezi Mungu amewafanyia vivuli katika alivyoviumba.
Kivuli ni kile anachojikinga mtu na joto la Jua.
Na amewafanyia makazi katika milima.
Chochote anachokihitajia mtu ni katika neema akikipata; hata wingu litakalomkinga na jua, bali hata pango katika milima.
Na amewafanyia nguo za kuwakinga na joto.
Vilevle za kuwakinga na baridi. Hazikutajwa kwa sababu ya kujulikana kwa kutajwa moja.
Na nguo za kuwakinga na vita vyenu . Hizi ni deraya n.k.
Ndio hivyo anatimiza neema zake kwenu ili mpate kusilimu.
Makusudio ya kusilimu hapa ni kutii na kuinyenyekea haki kwa kuifuata na kuitumia.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amewapa watu neema ya majumba, vifaa, mavazi ya kawaida, mavazi ya vita, vivuli na mapango, ili waweze kumshukuru na kumcha Yeye na wasilete ufisadi katika nchi.
Ikiwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewapa waarabu wa wakati wa giza, vivuli, miti, mawingu na mapango ya milima na akazingatia kuwa hizo zote ni katika kutimiza neema zake, na akawataka washukuru kwa hayo na wainyenyekee haki tena akawahadharisha wale watakaoasi.
Ikiwa ni hivyo, itakuwaje kwa neema hii ya dhahabu nyeusi inayotiririka katika miji ya Waarabu? Itakuwaje majumba yanayopasua mawingu wanayoyajenga kwayo? Vipi vifaa wanavyomiliki, zikiwemo ndege gari n.k.?
Mwenyezi Mungu aliwaneemesha waliopita kwa wanyama; kama ngamia, nyumbu baghala na punda. Vilevile kwa majumba ya mawe, ngozi, vifaa vya sufu na manyoya ya wanyama na nguo za kuwakinga na joto na baridi; bali hata mapango. Pia naye amewataka washukuru na wakumbuke.
Je, vipi wale wenye kustarehe hivi leo wakikaa kwenye majumba ya ghorofa wakiibadilisha hewa vile watakavyo – baridi au joto na pembeni mwao kuna mahema ya wakimbizi na huku wanadai kuwa wao wanamwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho?
Na kama wakikengeuka, basi juu yako ni kufikisha tu ujumbe ulio wazi na hisabu ni juu yetu sisi. Wewe umekwishamaliza kazi yako kwa ukamilifu na sisi tutawalipa hisabu yao na malipo yao.
Imetangulia Aya hii katika Juz.3 (3:20) na Juz.13 (13:40),Wanazijua neema za Mwenyezi Mungu kisha wanazikanusha . Makusudio ya kuzijua ni kwamba wao wanazitumia. Na kuzikanusha ni kwamba wao wanazitegemeza neema hizo kwa asiyestahiki. Yaani wanakula riziki ya Mwenyezi Mungu na wanamwabudu mwingine.
Na wengi wao ni makafiri.
Inafaa kulitumia neno wengi kwa maana yake ya dhahiri na inafaa pia kulitumia kwa maana ya wote. Makusudio hapa ni kila ambaye imemfikia risala ya Muhammad(s.a.w.w) na akaikanusha kwa inadi.
9
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
وَيَوْمَ نَبْعَثُ مِن كُلِّ أُمَّةٍ شَهِيدًا ثُمَّ لَا يُؤْذَنُ لِلَّذِينَ كَفَرُوا وَلَا هُمْ يُسْتَعْتَبُونَ ﴿٨٤﴾
84. Siku tutakapomwinua shahidi kwa kila umma, kisha hawataruhusiwa wale ambao wamekufuru wala hawataachiliwa kutaka radhi.
وَإِذَا رَأَى الَّذِينَ ظَلَمُوا الْعَذَابَ فَلَا يُخَفَّفُ عَنْهُمْ وَلَا هُمْ يُنظَرُونَ ﴿٨٥﴾
85. Na wale ambao wamedhulumu watakapoiona adhabu hawatapunguziwa wala hawatangojewa.
وَإِذَا رَأَى الَّذِينَ أَشْرَكُوا شُرَكَاءَهُمْ قَالُوا رَبَّنَا هَـٰؤُلَاءِ شُرَكَاؤُنَا الَّذِينَ كُنَّا نَدْعُو مِن دُونِكَ فَأَلْقَوْا إِلَيْهِمُ الْقَوْلَ إِنَّكُمْ لَكَاذِبُونَ ﴿٨٦﴾
86. Na wale ambao wameshirikisha watakapowaona wale ambao wamewashirikisha watasema: Mola wetu! Hawa ndio washirikishwa wetu ambao tulikuwa tukiwaomba badala yako, Ndipo wale watakapowatupia kauli: Hakika nyinyi ni waongo.
وَأَلْقَوْا إِلَى اللَّـهِ يَوْمَئِذٍ السَّلَمَ وَضَلَّ عَنْهُم مَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ ﴿٨٧﴾
87. Na siku hiyo watasalimu amri mbele ya Mwenyezi Mungu na yatapotea waliyokuwa wakiyazua.
الَّذِينَ كَفَرُوا وَصَدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ زِدْنَاهُمْ عَذَابًا فَوْقَ الْعَذَابِ بِمَا كَانُوا يُفْسِدُونَ ﴿٨٨﴾
88. Wale ambao wamekufuru na kuzuilia watu njia ya Mwenyezi Mungu tutawazidishia adhabu juu ya adhabu kwa walivyokuwa wafisadi.
وَيَوْمَ نَبْعَثُ فِي كُلِّ أُمَّةٍ شَهِيدًا عَلَيْهِم مِّنْ أَنفُسِهِمْ وَجِئْنَا بِكَ شَهِيدًا عَلَىٰ هَـٰؤُلَاءِ وَنَزَّلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ تِبْيَانًا لِّكُلِّ شَيْءٍ وَهُدًى وَرَحْمَةً وَبُشْرَىٰ لِلْمُسْلِمِينَ ﴿٨٩﴾
89. Na siku tutakapomwinua katika kila umma akiwashudia kutokana na wao na tukakuleta wewe uwe shahidi juu ya hawa na tumekuteremshia Kitabu hiki kubainisha kila kitu na uongofu na bishara kwa Waislamu.
Aya 84 -89
Siku tutakapomwinua shahidi kwa kila umma, kisha hawataruhusiwa wale ambao wamekufuru wala hawatachiliwa kutaka radhi.
Haya ni makemeo na kiaga kwa wale aliowaashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya iliyotangulia kwa kusema kwake: “Wanazijua neema za Mwenyezi Mungu kisha wanazikanusha”
Njia ya makemeo hayo ni kuwa Mwenyezi Mungu atawakusanya watu kesho na atamleta kila mtume ashuhudie au awe shahidi wa umma wake. Atakpotoa ushahidi Mwenyezi Mungu ataichukua kauli yake na wala hawataruhusiwa kuipinga kauli hiyo na kutoa udhuru. Mwenyezi Mungu anasema:
هَـٰذَا يَوْمُ لَا يَنطِقُونَ ﴿٣٥﴾ وَلَا يُؤْذَنُ لَهُمْ فَيَعْتَذِرُونَ ﴿٣٦﴾
Hii ni siku ambayo hawtazungumza, Wala hawatapewa ruhusa kutoa udhuru, (77:35-36).
Makusudio ya kutoachiliwa kutaka radhi ni kuwa hawatatakiwa kuomba msamaha kwa kauli wala vitendo. Kwa sababu Akhera ni nyumba ya hisabu na malipo, sio nyumba ya matendo na kuomba msamaha.
Na wale ambao wamedhulumu watakapoiona adhabu hawatapunguziwa wala hawatangojewa.
Makusudio ya wale ambao wameadhulumu ni kila dhalimu; ni sawa awe amemdhulumu Muumba wake kwa kumkanusha au amemdhulumu mwingine kwa kumfanyia ubaya; au awe amejidhulumu yeye mwenyewe kwa kujiingiza kwenye majanga. Yeye ataadhibiwa tu kwa sababu ya dhul- ma. Atapata malipo yanayolingana na kosa, hatapunguziwa wala kuzidishiwa tena bila ya kuchelewa.
Na wale ambao wameshirikisha watakapowaona wale ambao wamewashirikisha watasema: Mola wetu! Hawa ndio washirikishwa wetu ambao tulikuwa tukiwaomba badala yako, Ndipo wale watakapowatupia kauli: Hakika nyinyi ni waongo.
Watakaotupa kauli ni wale walioshirikishwa, wakiwatupia washirikina. Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa Mwenyezi Mungu atawafufua wale waliokuwa wakiabudiwa, wawe ni masanamu au kitu kingine, ili awape hoja wale waliokuwa wakiwafanya wengine kuwa ni waungu. Na kwamba washirikina watakapowaona hao waungu wao waliokuwa wakiwaabudu, watamwambia Mwenyezi Mungu: hawa ndio tuliokuwa tukiwashirikisha nawe. Na hao waungu wajibu kwa maneno au kwa kihali kuwa, nyinyi washirikina ni waongo na wazushi kwa kutufanya sisi ni washirika wa Mwenyezi Mungu.
Sio mbali kuwa masimulizi haya ya kauli ya washirikina ni fumbo la kufichuka uhakika kesho na kwamba hakutakuwa na nafasi ya uwongo wala kudanganya.
Na siku hiyo watasalimu amri mbele ya Mwenyezi Mungu.
Yaani washirikina na waungu wao watasalimu amri na kunyenyekea amri ya Mwenyezi Munguna yatapotea waliyokuwa wakiyazua. Kila mzushi katika maisha haya utamrudia uzushi wake kwa hizaya na adhabu siku hiyo ngumu.
Wale ambao wamekufuru na kuzuilia watu njia ya Mwenyezi Mungu tutawazidishia adhabu juu ya adhabu kwa walivyokuwa wafisadi.
Walifanya ufisadi kwa kukufuru kwao haki na wakafanya ufisadi kwa kuizuilia haki kwa hiyo wanastahiki adhabu mara mbili. Moja kwa ajili ya ufisadi na nyingine kwa ajili ya kufisidisha:
وَمَا هُم بِحَامِلِينَ مِنْ خَطَايَاهُم مِّن شَيْءٍ ﴿١٢﴾
“Na hakika wataibeba mizigo yao pamoja na mizigo mingine” (29:12)
Na siku tutakapomwinua katika kila umma akiwashudia kutokana na wao.
Yametangulia maana ya Aya hii katika Aya 84 ya sura hii, Hapa imerudia kuwakema wale waliomkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) .
Na tukakuleta wewe uwe shahidi juu ya hawa.
Neno ‘wewe’ hapa ni Muhammad(s.a.w.w) na ‘hawa’ ni umma wake.Unaweza kuuliza kwamba : Muhammad(s.a.w.w) ni Mtume wa Mwenyezi
Mungu kwa watu wote kwa nukuu ya Aya hii:
وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا كَافَّةً لِّلنَّاسِ بَشِيرًا وَنَذِيرًا وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٢٨﴾
Na hatukukutumma ila kwa watu wote uwe mbashiri na muonyaji, lakini watu wengi hawajui (34:28).
Kwa hiyo ikiwa risala ya Muhammad ni kwa watu wote, inatakikana ushahidi wake pia uwe kwa watu wote huko akhera, lakini kama ikiwa ushahidi wake huko akhera ni kwa umma wake tu, basi itabidi risala yake hapa duniani iwe kwa umma wake tu?
Jibu : hakuna uhusiano wa ushahidi wake kwa umma wote huko akhera na kuenea risala yake hapa duniani. Kwa sababu risala ya Uislamu inafikishwa na umma wa Muhammad(s.a.w.w) baada yake kwa umma zote wakati wote na mahali pote. Mtume anatoa ushahidi juu ya umma wake kwamba hawakufikisha risala kwa vizazi vingne.
Na tumekuteremshia Kitabu hiki kubainisha kila kitu.
Maneno anaambiwa Muhammad, Makusudio ya kitabu hiki ni Qur’an, ndani yake mna ubainifu wa kila kitu unaoamabatana na itikadi, sharia, maadili, mazingatio na mawaidha.na uongofu kwa anayeutakana bishara kwa Waislamu.
Makusudio ya bishara hapa ni Pepo na Mwislamu ni kila mwenye kusalimu amri ya haki na akaitumia.
إِنَّ اللَّـهَ يَأْمُرُ بِالْعَدْلِ وَالْإِحْسَانِ وَإِيتَاءِ ذِي الْقُرْبَىٰ وَيَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ وَالْبَغْيِ يَعِظُكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿٩٠﴾
90. Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha uadilifu na hisani na kuwapa jamaa na anakataza uchafu na uovu na dhulma. Anawapa mawaidha ili mpate kukumbuka.
وَأَوْفُوا بِعَهْدِ اللَّـهِ إِذَا عَاهَدتُّمْ وَلَا تَنقُضُوا الْأَيْمَانَ بَعْدَ تَوْكِيدِهَا وَقَدْ جَعَلْتُمُ اللَّـهَ عَلَيْكُمْ كَفِيلًا إِنَّ اللَّـهَ يَعْلَمُ مَا تَفْعَلُونَ ﴿٩١﴾
91. Na tekelezeni ahadi ya Mwenyezi Mungu mnapoahidi; wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha, ilhali mmekwishamfanya Mwenyezi Mungu ndiye mdhamini wenu, Hakika Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyafanya.
وَلَا تَكُونُوا كَالَّتِي نَقَضَتْ غَزْلَهَا مِن بَعْدِ قُوَّةٍ أَنكَاثًا تَتَّخِذُونَ أَيْمَانَكُمْ دَخَلًا بَيْنَكُمْ أَن تَكُونَ أُمَّةٌ هِيَ أَرْبَىٰ مِنْ أُمَّةٍ إِنَّمَا يَبْلُوكُمُ اللَّـهُ بِهِ وَلَيُبَيِّنَنَّ لَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ مَا كُنتُمْ فِيهِ تَخْتَلِفُونَ ﴿٩٢﴾
92. Wala msiwe kama mwanamke ambaye ameufumua uzi wake baada ya kuusokota na kuwa mgumu. Mnavifanya viapo vyenu kuwa ni njia ya kudanganyana baina yenu kwa kuwa kundi moja lina nguvu zaidi kuliko jengine. Hakika Mwenyezi Mungu anawajaribu kwayo na hakika atawabainishia siku ya kiyama yale mliyokuwa mkihitalifiana.
وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَجَعَلَكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَلَـٰكِن يُضِلُّ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي مَن يَشَاءُ وَلَتُسْأَلُنَّ عَمَّا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٩٣﴾
93. Na lau Mwenyezi Mungu angelitaka bila shaka angeliwafanya umma mmoja, lakini humpoteza anayemtaka na humwongoa anayemtaka. Hakika mtaulizwa kuhusu yale mliyokuwa mkiyafanya.
MWENYEZI MUNGU ANAAMRISHA UADILIFU NA HISANI
Aya 90 – 93
Kwa kawaida kila analojilazimisha nalo mtu kwa hiyari yake ni Ahadi. Ahadi inakuwa ni wajib kuitekeleza ikiwa ni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na kuambatanishwa na jina lake; mfano kusema: ‘Nimemwahidi Mwenyezi Mungu kufanya jambo fulani’ au ‘Nimejilazimisha ahadi ya Mwenyezi Mungu kufanya jambo fualani’ Kuvunja ahadi hii ni kama kuvunja kiapo, inabidi kutoa kafara; kama ilivyoelezwa katika vitabu vya Fiqh.
Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha uadilifu na hisani na kuwapa jamaa na anakataza uchafu na uovu na dhulma.
Aya imeamrisha mambo matatu mazuri na kukataza matatu maovu. Ama matatu mazuri ni haya yafuatayo:
1. Uadilifu: Mtu mwadilifu ni yule anayewafanyia insafu watu yeye mwenyewe na kuwafanyia yale yaliyo wajibu kuwafanyia.
2. Hisani: Inakusanya kila jambo la kheri. Watu wanafahamu kuwa hisani ni kujitolea mtu kwa mali yake au juhudi yake katika njia ya kheri.
3. Kuwapa jamaa: Huko pia ni kufanya hisani. Mwenyezi Mungu amekuhusisha kukutaja peke yake kwa kukukweza kutokana na ubora wake.
Ama matatu mabaya ni:
1. Uchafu; kama zinaa, ulawiti, pombe, kamari, uwongo na uzushi. Uchafu ulio dhahiri zaidi ni zinaa. Mwenyezi Mungu (s.w.t.) anasema:
وَلَا تَقْرَبُوا الزِّنَىٰ إِنَّهُ كَانَ فَاحِشَةً وَسَاءَ سَبِيلًا ﴿٣٢﴾
“Wala msiikurubie zinaa; hakika hiyo ni uchafu na njia mbaya.” (17:32).
2. Uovu: Ni kila linalopingana na akili na sharia.
3. Dhulma: Ni kuwafanyia uadui watu kwa kauli au vitendo. Hukumu yake kesho mbele ya Mwenyezi Mungu ni sawa na shirki, bali dhulma ni zaidi. Kwa sababu shrki ni kuifanyia uadui haki ya Mwenyezi Mungu ambaye anaweza kuisamehe. Lakini dhulma ni kuifanyia uadui haki ya Mwenyezi Mungu na haki ya watu.
Mara nyingine uchafu unaitwa uovu na uovu unaitwa uchafu. Yote hayo mawili ni dhulma.
Anawapa mawaidha ili mpate kukumbuka.
Makusudio ya mawaidha yake Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni kuamrisha kwake mambo mazuri na kukataza kwake mambo mabaya. Lengo la mawaidha ni kuwa tuwe waumini wenye takua, wema na wasafi. Wapokezi wa Hadith wamepokea kutoka kwa Ibn Mas’ud kwamba Aya hii ndiyo iliyokusanya zaidi mambo ya kheri na ya shari katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu.
Amesema Uthman Bin Madh’un: “Nilisilimu kwa kumstahi Mtume wa Mwenyezi Mungu, Na haukuingia Uisalmu moyoni mwangu mpaka iliposhuka Aya hii. Kwa hiyo nikamwamini Muhammad(s.a.w.w) na nikamwendea ami yake, Abu Twalib, nikampa habari ya jambo langu hilo, akasema: ‘Enyi maquraish! Mfuateni Muhammad mtaongoka; Kwa sababu yeye hawaamuru isipokuwa tabia nejema.
Na tekelezeni ahadi ya Mwenyezi Mungu mnapoahidi.
Kumwahidi Mwenyezi Mungu kunaweza kuwa kwa mambo mawili: Kwanza, kukata mtu katika nafsi yake kumwahidi Mwenyezi Mungu kufanya jambo fulani au kuliacha; kama kusema: ‘Namwahidi Mwenyezi Mungu kuwa nitafanya jambo kadhaa au kuacha jambo kadhaa’
Aina ya pili ni kumwamini Mwenyezi Mungu. Kwa sababu mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu anakuwa amempa ahadi Mwenyezi Mungu kufuata amri yake na kukatazika na makatazo yake.
Ahadi zote hizi mbili ni wajibu kuzitekeleza. Makusudio ya ahadi kwenye Aya hii ni aina ya kwanza ya ahadi tuliyoieleza.
Wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha.
Makusudio ya kuvidhibitisha hapa ni kuvifunga hivyo viapo, yaani kuapa. Kwa sababu kiapo kinafungika ikiwa si kwa kumwasi Mwenyezi Mungu na wala hakifungiki, kivyovyote, ikiwa ni kwa jili ya kumwasi.
Imesemekana kuwa makusudio ya kuvithibisha hapa ni kuvitilia mkazo na kuvisisitiza. Lakini maelezo haya ni kutatizika. Ambapo maana yake yatakuwa viapo visivyosisitizwa havina wajibu wa kuvitekeleza na inajulikana kuwa kiapo kikitimia basi ni wajibu kukitekeleza, kiwe kimesisitizwa au la.
Ilhali mmekwishamfanya Mwenyezi Mungu ndiye mdhamini wenu.
Kila aliyeapa kwa jina la Mwenyezi Mungu amemfanya Mwenyezi Mungu ni mdhamini kiutekelezaji. Akivunja kiapo basi atakuwa amemfanyia hiyana Mwenyezi Mungu hasa, na atastahiki adhabu.
Hakika Mwenyezi Mungu anayajua mnayoyafanya.
Mwenye kutekeleza ahadi yake na kiapo chake, Mwenyezi Mungu atamlipa thawabu za watiifu na mwenye kuvunja na akafanya hiyana atamwadhibu adhabu ya waasi.
Kwa hakika ilivyo ni kwamba ahadi na kiapo vinafunguka ikiwa kuacha ni bora kuliko kutekeleza. Kwa mfano, mtu akiapa au kumwahidi Mungu kuwa hatakula nyama na ikawa kuacha kula nyama kuna manufaa ya afya yake, basi kiapo au ahadi itafungika.
Na kama baadae, ukimtokea ulazima wa kula nyama, atakula na kiapo au ahadi itafunguka na hatakuwa na chochote. Kuna hadith isemayo: “Ukiona heri yoyote katika kiapo chako basi kiache”
Wala msiwe kama mwanamke ambaye ameufumua uzi wake baada ya kuusokota na kuwa mgumu.
Kila kitu kinachovunjwa baada ya kufungwa basi kimefumuka, kiwe uzi, kamba au kitu chochote.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amepiga mfano wa kuvunja ahadi na uzi uliofumuliwa baada ya kusokotwa.
Inasemekana kuwa huko Makka kulikuwa na mwanamke mmoja mpum- bavu aliyekuwa akisokota sufu yake asubuhi na ikifika jioni anaifumua, na Mwenyezi Mungu akamfananisha na mvunja ahadi.
Vyovyote iwavyo ni kuwa Aya inatilia mkazo kauli yake Mwenyezi Mungu: ”Wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha.”
Mnavifanya viapo vyenu kuwa ni njia ya kudanganyana baina yenu kwa kuwa kundi moja lina nguvu zaidi kuliko jengine.
Yaani msijaalie viapo vyenu kuwa ni nyenzo ya kudanganya na hiyana; kwa kuapa mbele ya wale walio wengi na wenyenguvu zaidi kuliko nyinyi ili wawaamini, wakati nyinyi mnadhamiria kuvunja viapo hivyo na muwaache wale ambao mliapa mbele yao pale mtakapojiona nyinyi mna nguvu zaidi kuliko wao.
Hakika Mwenyezi Mungu anawajaribu kwayo
Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawakalifisha waja ili atii mtiifu kwa hiyari yake na aasi muasi kwa hiyari yake; kisha kila mmoja amlipe malipo yake anayostahiki. Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi katika Juz. 7 (5:94)
Na hakika atawabainishia siku ya Kiyama yale mliyokuwa mkihitali- fiana.
Mwenyezi Mungu atawarudisha waja siku ya kiyama ili ajulikane mtiifu na mbatilifu na amlipe kila mmoja stahiki yake.
Na Mwenyezi Mungu angelitaka bila shaka angeliwafanya umma mmoja.
Yaani kama Mwenyezi Mungu angelitaka kumlazimisha mtu kuamini watu wote wangelikuwa umma mmoja, lakini amemwachia mtu na hiyari yake. Kwani lau angelimnyang’anya uhuru huu na hiyari, angelikuwa sawa na mnyama Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi katika Juz. 7 (6: 35) na katika Juz. 12 (11:118).
Lakini humpoteza anayemtaka na humwongoa anayemtaka.
Hakuna shaka kwa mwenye akili kwamba Mwenyezi Mungu hapotezi wala kumwongoza yeyote kwa lazima. Lau ingelikuwa hivyo isingelikuwa sawa kumuuliza na kumchukulia hisabu. Naye amesema mara tu baada ya maneno hayo:
Hakika mtaulizwa kuhusu yale mliyokuwa mkiyafanya.
Maana ya Aya ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamzingatia mtu kuwa ni mpotevu baada ya yeye mwenyewe kufuata njia ya upotevu, na anamzingatia ni mwongofu baada ya kufuata njia ya uwongofu; sawa na anavyomuua anayeamua kujinyonga.
Yametangulia maelezo kuhusu uongofu na upotevu katika Juz; 1 (2:26), Juz. 3 (2: 272) na Juz; 5 (4:88).
10
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
وَلَا تَتَّخِذُوا أَيْمَانَكُمْ دَخَلًا بَيْنَكُمْ فَتَزِلَّ قَدَمٌ بَعْدَ ثُبُوتِهَا وَتَذُوقُوا السُّوءَ بِمَا صَدَدتُّمْ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ وَلَكُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿٩٤﴾
94. Wala msivifanye viapo vyenu ni njia ya kudanganyana baina yenu. Na mkaonja maovu kwa sababu ya kuzuilia kwenu njia ya Mwenyezi Mungu na mkapata adhabu kubwa.
وَلَا تَشْتَرُوا بِعَهْدِ اللَّـهِ ثَمَنًا قَلِيلًا إِنَّمَا عِندَ اللَّـهِ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٩٥﴾
95. Wala msinunue ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa thamani ndogo. Hakika kilicho kwa Mwenyezi Mungu ndio bora kwenu ikiwa mnajua.
مَا عِندَكُمْ يَنفَدُ وَمَا عِندَ اللَّـهِ بَاقٍ وَلَنَجْزِيَنَّ الَّذِينَ صَبَرُوا أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٩٦﴾
96. Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu ndivyo vitakavyobaki. Na kwa hakika tutawalipa waliosubiri ujira wao kwa mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya.
مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٩٧﴾
97. Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya.
فَإِذَا قَرَأْتَ الْقُرْآنَ فَاسْتَعِذْ بِاللَّـهِ مِنَ الشَّيْطَانِ الرَّجِيمِ ﴿٩٨﴾
98. Unaposoma Qur’an muombe Mwenyezi Mungu akulinde na shetani mwenye kufukuzwa.
إِنَّهُ لَيْسَ لَهُ سُلْطَانٌ عَلَى الَّذِينَ آمَنُوا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ ﴿٩٩﴾
99. Hakika yeye hana madaraka juu ya walioamnini na wakamtegemea Mola wao.
إِنَّمَا سُلْطَانُهُ عَلَى الَّذِينَ يَتَوَلَّوْنَهُ وَالَّذِينَ هُم بِهِ مُشْرِكُونَ ﴿١٠٠﴾
100. Hakika madaraka yake yako juu ya wale tu wanaomtawalisha na wale ambao kwaye wanashirikisha.
Aya 94 – 100
Katika Aya ya 91, ya sura hii, Mwenyezi Mungu amesema: “Wala msivunje viapo baada ya kuvithibitisha,” katika Aya 92 akasema: Wala msiwe kama mwanamke ambaye ameufumua uzi wake baada ya kuusokota na kuwa mgumu Mnavifanya viapo vyenu kuwa ni njia ya kudanganyana baina yenu kwa kuwa kundi moja lina nguvu zaidi kuliko jengine?” na katika Aya hii tunayoifasiri anasema:
Wala msivifanye viapo vyenu ni njia ya kudanganyana baina yenu , Je, nini lengo la kukaririka huku?
Razi, akiwanukuu wafasiri, anasema kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwanza amewakataza watu wote kutovunja viapo na ahadi, kisha akawahusu watu maalum ambao ni wale waliombai Muhammad(s.a.w.w) kwa Uislamu.
Ufafanuzi huu uko mbali na ufahamisho wa Aya. Kwa sababu kukataza kuvunja ahadi na kiapo kumekuja kiujumla bila ya kufungwa na baia au jambo jenginelo.
Jawabu bora ni kuwa kukaririka kukataza hapa kumekuja kwa sababu zake ambazo zinatajwa, akasema Mwenyezi Mungu baada ya katazo la kwan- za:” Ilhali mmekwishamfanya Mwenyezi Mungu ndiye mdhamini wenu.´ Hapo anawakumbusha kuwa wao wamekwishamfanya Mwenyezi Mungu ni mdhamini, kwa hiyo ni lazima watekeleze; vinginevyo watakuwa wamemfanyia hiyana Mwenyezi Mungu hasa.
Baada ya kutaja katazo la pili akasema: “Hakika Mwenyezi Mungu anawajaribu kwayo.” Hii ni kuwakumbusha walioapa kwamba Mwenyezi Mungu anawapa mtihani ili wastahiki kile watakacholipwa.
Baada ya katazo la tatu akasema:Usije mguu ukateleza baada ya kuimarika kwake. Hili ni kemeo na kiaga kwa yule mwenye kuiacha haki akafuata batili na uwongofu kwa upotevu.
Na mkaonja maovu kwa sababu ya kuzuilia kwenu njia ya Mwenyezi Mungu na mkapata adhabu kubwa.
Kila mwenye kuizuilia njia ya Mwenyezi Mungu na haki ni wajibu kumzuia kwa mawaidha na mwongozo. Akitubia na kurejea nyuma, ndio sawa. Vinginevyo itakuwa ni wajibu kumpiga jihadi na inafaa kumchukua mateka au kumuua. Hii ni katika dunia. Ama huko Akhera atakuwa na adhabu kuu.
Wala msinunue ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa thamani ndogo.
Ahadi ya Mwenyezi Mungu ni kulazimiana na haki na kuitumia; ikiwa ni pamoja na kutekeleza ahadi na kiapo. Makusudio ya thamani ndogo ni manufaa ya kidunia hata kama yatakuwa mengi. Maana ni kuwa manufaa yenu ya kibinafsi yasiathiri haki mkaiuza kwa mali na cheo au kwa starehe yoyote katika dunia hii. Kwani hakika dunia na vilivyomo si chochote kulinganisha na yale ambayo Mwenyezi Mungu amewaandalia watiifu na wahisani.
Hakika kilicho kwa Mwenyezi Mungu ndio bora kwenu kuliko manufaa ya dunia, kwa vyovyote yakavyofikia na yatakavyokuwa,ikiwa mnajua.
Tofauti ni kubwa baina ya manufaa ya Akhera na ya kidunia; kisha Mwenyezi Mungu akabainisha wajihi wa tofauti hiyo kwa kusema:
Mlivyo navyo vitakwisha na vilivyoko kwa Mwenyezi Mungu ndivyo vitakavyobaki.
Hakuna mwenye shaka kwamba vinavyodumu ni bora kuliko vinavyokwisha. Zaidi ya hayo ni kuwa manufaa ya dunia yanaambatana na tabu na shida. Yakiwa matamu upande fulani yanakuwa machungu kwa upande mwengine. Lakini manufaa ya Akhera ni safi kabisa hayambatani na chochote.
Na kwa hakika tutawalipa waliosubiri ujira wao kwa mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya.
Ilivyo ni kuwa mwito wa haki na uimara wake unaleta maudhi kutoka kwa wapinzani. Kwa hiyo mwenye kuvumilia misukosuko atakayoipata katika njia ya haki na akawa imara katika jihadi na maadui wa haki mpaka mwisho, basi Mwenyezi Mungu atamlipa malipo ya wavumilivu walio na juhudi.
Unaweza kuuliza : kauli yake hii Mwenyezi Mungu inaashiria kwamba Mwenyezi Mungu atawalipa kwa yale mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya, ama yale mazuri ya kawaida hayatalipwa kitu. Je, maana haya ndiyo yaliyokusudiwa na Aya?
Jibu : Hakika matendo ya mtu yanagawanyika kwenye utiifu, wajibu na sunna. Vile vile kwenye maasi na halali. Hakuna mwenye shaka kwamba yaliyo mazuri zaidi ni utiifu na yaliyo mabaya zaidi ni uasi.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawalipa thawabu wale wenye kuwa na subira kutokana na yote ya utiifu waliyoyafanya, ikiwemo subira na uvumilivu katika kumtii Mwenyezi Mungu ambako ndiko bora na kutukufu zaidi, Ama mwenye kutenda yaliyo halali hastahiki adhabu wala thawabu.
Kwa hiyo makusudio ya mazuri zaidi waliyoyafanya ni yale ya utiifu waliyoyafanya kwa namna zake zote na sio makusudio kuwa ni subira tu.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameweka wazi kwambaYeye atawalipa waliosubiri kutoka na mema yao, na akanyamazia maovu yao. Katika unyamazo huu kuna ahadi au mfano wa ahadi kwamba Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawasamehe kwa rehema yake na fadhila zake.
Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni muumini, tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya.
Katika Aya hii kuna njia zifuatazo:-
Aya imefahamisha kwamba kila mmoja kati ya mwanamume na mwanamke anapimwa kwa vitendo vyake mbele ya Mwenyezi Mungu; na kwamba hakuna mbora zaidi kati yao isipokuwa kwa takua. Ikiwa mwan- mke atakuwa mcha Mungu zaidi ya mwanamume basi atakuwa ni bora na mtukufu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko mwanamume na ikiwa mwanamume atakuwa anamcha Mungu zaidi ya mwanamke basi atakuwa ni bora na mtukufu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko mwanamke.
Tumelizungumzia hilo kwa ufafanuzi katika Juz. 2 (2:228) kifungu cha ‘Mwanamume na mwanamke katika sharia ya Kiislamu.
Aya imefahamisha vilevile kuwa imani na matendo mema ndio sababu ya malipo na thawabu za akhera, Ama moja pekee haitoshelezi. Lakini tukichanganya Aya hii na ile isemayo: Atakayefanya wema uzani wa chembe atauona, (99:7), inakuwa kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) anambadilishia kafiri mwenye kufanya wema kwa siha, mali, jaha au kurefuka umri katika maisha ya dunia, au kupunguziwa adhabu huko akhera, Yametangulia maelezo haya katika, Juz. 7 (3:178) kwa anuani ya Kafiri na amali ya kheri.
Wametofautiana katika uhai mwema uliotajwa katika Aya hii, kuwa je, utapatikana duniani au Akhera?
Ni jambo la kushangaza kwa wafasiri kutofautiana katika hilo, na wao wenyewe wanashuhudia kwa hisia na macho kwamba dunia ni pepo ya makafiri na jela ya muumini! Pia wanasoma na kuifafanua Aya isemayo:
وَلَوْلَا أَن يَكُونَ النَّاسُ أُمَّةً وَاحِدَةً لَّجَعَلْنَا لِمَن يَكْفُرُ بِالرَّحْمَـٰنِ لِبُيُوتِهِمْ سُقُفًا مِّن فِضَّةٍ وَمَعَارِجَ عَلَيْهَا يَظْهَرُونَ ﴿٣٣﴾وَلِبُيُوتِهِمْ أَبْوَابًا وَسُرُرًا عَلَيْهَا يَتَّكِئُونَ ﴿٣٤﴾ وَزُخْرُفًا وَإِن كُلُّ ذَٰلِكَ لَمَّا مَتَاعُ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةُ عِندَ رَبِّكَ لِلْمُتَّقِينَ ﴿٣٥﴾
“Na lau isingekuwa watu watakuwa umma mmoja, bila shaka tungelifanya nyumba za wanaomkufuru Mwingi wa rehema zina dari ya fedha na ngazi wanazopandia na milango ya nyumba zao na vitanda wanavyoviegemea na mapambo, lakini yote si chochote ila ni starehe ya maisha ya dunia. Na Akhera iliyoko kwa Mola wako ni ya wenye takua” (43:33 – 35).
Kwa hiyo basi tunaipa nguvu kauli ya kuwa makusudio ya Aya ni maisha mema Peponi na kwamba kaulia yake Mwenyezi Mungu: ‘tutawapa ujira wao...’ inaungana kitafisiri na kuli hii:”tutamhuisha maisha mema” Ni mfano wa kauli yake Mwenyezi Mungu, katika Aya ya 105 ya sura hii: “. Hakika wanaozua uwongo ni wale tu wasioziamini Aya za Mwenyezi Mungu, na hao ndio waongo “ (16:105).
Unaposoma Qur’an muombe Mwenyezi Mungu akulinde na shetani mwenye kufukuzwa.
Maneno anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) na hukumu inawaenea wote. Maana ni kuwa mwenye kutaka kusoma Qur’an aseme kabla ya kusoma “Audhu billahi minashhaytwnir-rajim” (Najilinda kwa Mwenyezi Mungu na shetani mwenye kufukuzwa).
Katika tafsir ya Razi kuna maelezo kwamba Malik na Daud Dhahiri wanasema kuwa kusoma Audhu ni baada ya kusoma Qur’an sio kabla yake. Wamesema hivyo kwa kuganda kwenye dhahiri ya tamko. Vyovyote iwavyo, kusoma Audhu ni sunna wala sio wajib kwa maafikiano ya wote.
Hakika yeye hana madaraka juu ya walioamnini na wakamtegemea Mola wao mlezi. Hakika madaraka yake yako juu ya wale tu wanaomtawalisha na wale ambao kwaye wanashirikisha.
Neno ‘yeye’ linamrudia shetani na neno ‘kwaye’ inawezekana kuwa linamrudia Mwenyezi Mungu, kwa maana ya kuwa wanamshrikisha Mungu au likamarudia shetani kwa maana ya kuwa wanamshirikisha Mungu kwa sababu ya kumtii shetani.
Maana ni kuwa shetani hana njia yoyote ya kumfanya binadamu afanye haramu isipokuwa kwa wasiwasi na hadaa, na hawamuitikii kwa hilo isipokuwa wenye nyoyo na imani dhaifu. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 13 (14:22) na Juz, 14 (15: 39 – 42).
وَإِذَا بَدَّلْنَا آيَةً مَّكَانَ آيَةٍ وَاللَّـهُ أَعْلَمُ بِمَا يُنَزِّلُ قَالُوا إِنَّمَا أَنتَ مُفْتَرٍ بَلْ أَكْثَرُهُمْ لَا يَعْلَمُونَ ﴿١٠١﴾
101. Na tunapoibadilisha Aya mahali pa Aya nyingine, na Mwenyezi Mungu anajua anayoteremsha, wao husema: Hakika wewe ni mzushi, Bali wengi wao hawajui.
قُلْ نَزَّلَهُ رُوحُ الْقُدُسِ مِن رَّبِّكَ بِالْحَقِّ لِيُثَبِّتَ الَّذِينَ آمَنُوا وَهُدًى وَبُشْرَىٰ لِلْمُسْلِمِينَ ﴿١٠٢﴾
102. Sema, ameiteremsha Roho takatifu kutoka kwa Mola wako, ili awathibitishe wale walioamini na kuwa ni uwongofu na bishara kwa Waislamu.
وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّهُمْ يَقُولُونَ إِنَّمَا يُعَلِّمُهُ بَشَرٌ لِّسَانُ الَّذِي يُلْحِدُونَ إِلَيْهِ أَعْجَمِيٌّ وَهَـٰذَا لِسَانٌ عَرَبِيٌّ مُّبِينٌ ﴿١٠٣﴾
103. Na hakika tunajua kwamba wao wanasema yuko mtu anayemfundisha, Lugha ya huyo wanayemuelekezea sio fasaha na hii ni lugha ya kiarabu bayana.
إِنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ لَا يَهْدِيهِمُ اللَّـهُ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿١٠٤﴾
104. Hakika wale ambao hawaziamini Aya za Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu hawaongoi, nao watapata adhabu chungu.
إِنَّمَا يَفْتَرِي الْكَذِبَ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِآيَاتِ اللَّـهِ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْكَاذِبُونَ ﴿١٠٥﴾
105. Hakika wanaozua uwongo ni wale tu wasioziamini Aya za Mwenyezi Mungu, na hao ndio waongo.
Aya 101 – 105
Tofauti kati ya neno Aa’jamiyy na A’jamiyy ni kuwa la kwanza lina maana ya mtu asiyekuwa fasaha katika Kiarabu, hata kama ni mwarabu, Na lapili lina maana ya lugha nyingine isiyokuwa Kiarabu.
Na tunapobadilisha Aya mahali pa Aya nyingine, na Mwenyezi Mungu anajua anayoteremsha. Wao husema: “Hakika wewe ni mzushi, Bali wengi wao hawajui.
Wanaosema hapa ni washirikina waliomkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) . Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewaumba viumbe na Yeye ni mwenye hekima, Mjuzi wa kujua masilahi yao na uharibifu wao. Mara nyingine hekima inaona kuwa ni masilahi kuweka kwa waja wake sharia ya hukumu kwa muda fulani, wakafanya.
Kisha ukiisha ule muda, sharia ile inaondolewa na Yule ambaye imetukuka hekima yake huweka hukumu nyingine mahali pa ile hukumu ya kwanza kulingana na masilahi vilevile.
Haya ndiyo makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu: Tunapobadilisha Aya mahali pa Aya nyingine’
Washirikina walipokuwa wakiona hivi humwambia Muhammad(s.a.w.w) kuwa wewe unajifanyia mwenyewe tu haya kisha unayanasibisha kwa Mwenyezi Mungu kwa uwongo na uzushi. Mwenyezi Mungu (s.w.t) anajua kuwa Yeye ndiye aliyeteremsha mabadiliko haya kwa Mtume wake mkweli, mwaminifu na anajua kuwa wao ndio wazushi kwa kusema kwao kuwa Mtume ni mzushi.
Tafsiri wazi zaidi niliyosoma kuhusu Aya hii ni ile iliyopokewa kutoka kwa Ibn Abbas, kwamba inapoteremshwa Aya ya ugumu kisha ikateremshwa Aya ya laini, maquraishi husema kuwa Muhammad anawachezea maswahaba zake; leo anawaamrisha hivi na kesho anawakataza na kwamba yeye hayasemi haya ila yeye mwenyewe tu, ndipo Mwenyezi Mungu akateremsha Aya hii, tumezungumzia kuhusu kufuta hukumu katika Juz. 1 (2:106).
Sema ameiteremsha Roho takatifu kutoka kwa Mola wako, ili awathibitishe wale walioamini na kuwa ni uwongofu na bishara kwa Waislamu.
Roho takatifu ni Jibril. Ameitwa hivyo kwa sababu ameteremsha Qur’an ambayo ni takatifu kutoka kwa Mwenyezi Mungu hadi kwa Muhammad(s.a.w.w) . Umetangulia mfano wa Aya hii katika Aya ya 89 ya sura hii.
Hapa imetajwa kwa kuwarudi washirikina walionasibisha kubadilisha kwa Mtume. Kule imetajwa kwa mnasaba wa kuwa Mwenyezi Mungu amesema atamleta shahidi kwa kila umma na Muhammad atakuwa shahidi wa umma wake kwamba yeye amiefikisha Qur’an ambayo ni ubainifu wa kila kitu.
Na hakika tunajua kwamba wao wanasema yuko mtu anayemfundisha.
Washirikina walimtuhumu Muhammad(s.a.w.w) kwamba yeye anafundishwa Qur’an na mtu mwingine. Hakuna mwenye shaka kwamba hii ni aina ya vita vya propaganda za uwongo wanazozitangaza wafisadi duniani kwa masilahi yao. Leo watu wameendelea na mfumo wa aina yake katika propaganda dhidi ya wenye ikhlasi na viongozi wema. Wamekuwa na ufundi ambao unawahadaa watu wema wengi walio wasafi.
Lugha ya huyo wanayemuelekezea sio fasaha na hii ni lugha ya kiarabu bayana.
Yaani lugha ya huyo mtu wanayemsema ni kiarabu cha mtaani.
Hii ni kuwarudi washirikina na kauli yao kuhusu Muhammad(s.a.w.w) kwamba anafundiswa na mtu mwingine. Hapa inaonyesha kwamba huyo mtu waliyemsema kuwa anamfundisha, lugha yake ni ya mtaani na lugha ya Qur’an ni kiarabu fasihi, Sasa itawezekana vipi asiyejua fasihi amfundishe mwengine fasihi.
Walirudiarudia uzushi huu maadui wa Uislamu baadae na mpaka leo wahubiri wengi wa Kikiristo wanathubutu kusema, kwa kutojua au kujitia kutojua, kwamba kwenye Qur’an kuna fani na hekima ambazo wakati huo hazikuwa na athari yoyote.
Kama tukichukulia kuwa zilikuweko, basi isingewezekana yeyote kuzikusanya na kuzijua na kama angelizijua basi umashuhuri wake ungelizidi ule wa Aristatle ambaye Waarabu wanamwita mwalimu wa kwanza. Licha ya wao kujua kwamba hakuwa na yeyote aliyekuwa wakati wa Mtume aliyedaiwa kujua hizo elimu zilizomo ndani ya Qur’an.
Hakika wale ambao hawaziamini Aya za Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu hawaongoi, nao watapata adhabu chungu.
Makusudio ya Aya za Mwenyezi Mungu ni dalili zinazosema kuhusu kuweko kwake, miujiza inayoshuhudia utume wa Mitume na hukumu zilizoteremshwa kwao. Ama makusudo ya uongofu hapa ni thawabu; yaani Mwenyezi Mungu hatampa thawabu, bali atamwadhibu kwa aina za adhabu
Hakika wanaozua uwongo ni wale tu wasioziamini Aya za Mwenyezi Mungu wala ufufuo, hisabu na malipo; kama washirikina waliomwambia Muhammad(s.a.w.w) yale waliyomwambia.
Na hao ndio waongo.
Wanajasiri kusema uwongo na kufanya ufisadi na dhambi kwa vile wao hawaogopi adhabu ya uwongo na wala hawatarajii thawabu.
Unaweza kuuliza : Kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Hakika wanaozua uwongo ni wale tu wasioziamini Aya za Mwenyezi Mungu’ si inatosha, sasa kuna haja gani tena ya kusema: Na hao ndio waongo? Je, kuna makusudio gani ya kukaririka huku?
Wafasiri wamejibu kuwa : lengo ni kutanabahisha kuwa sifa ya uwongo kwao imethibiti; sawa na kumwambia mtu: ‘Wewe ni mwongo tena mwongo sana’ yaani hali yako na mazoweya yako ni uwongo tu.
Swali la pili ni : Mwenyezi Mungu anasema “Hakika wanaozua uwongo ni wale tu wasioziamini Aya za Mwenyezi Mungu” Hii si ni kuwafanya makafiri kuwa ndio waongo tu; na inajulikana kuwa kuna makafiri walio wakweli sana na wakutegemewa zaidi, katika mazungumzo yao, kuliko wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho?
Jibu : Hakika Mwislamu muongo anamwamini Mwenyezi Mungu kinad- hariya na ni kafiri kimatendo. Kwa hiyo yeye kwa wasifu wake ni muumini kinadhariya na kifikra, atachukuliwa duniani kuwa ni Mwislamu. Na kafiri kwa wasifu wake atachukuliwa kuwa ni kafiri kulingana na Aya hii na yaliyopokewa kutoka kwa Mtume, alipoulizwa: Je, Mumin anasema uwongo? Akajibu: La; kisha akasoma Aya hii.
11
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ وَلَـٰكِن مَّن شَرَحَ بِالْكُفْرِ صَدْرًا فَعَلَيْهِمْ غَضَبٌ مِّنَ اللَّـهِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١٠٦﴾
106. Anayemkufuru Mwenyezi Mungu baada ya imani yake, Isipokuwa aliyelazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetua juu ya imani. Lakini aliyekifungulia kifua chake ukafiri, basi hao ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yao na watapata adhabu kubwa.
ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمُ اسْتَحَبُّوا الْحَيَاةَ الدُّنْيَا عَلَى الْآخِرَةِ وَأَنَّ اللَّـهَ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الْكَافِرِينَ ﴿١٠٧﴾
107. Hiyo ni kwa sababu wao wamestahabu maisha ya dunia kuliko ya akhera, Na kwamba Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ طَبَعَ اللَّـهُ عَلَىٰ قُلُوبِهِمْ وَسَمْعِهِمْ وَأَبْصَارِهِمْ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْغَافِلُونَ ﴿١٠٨﴾
108. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amepiga chapa juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao; na hao ndio wenye kughafilika.
لَا جَرَمَ أَنَّهُمْ فِي الْآخِرَةِ هُمُ الْخَاسِرُونَ ﴿١٠٩﴾
109. Hapana shaka kwamba wao ndio wenye kuhasirika Akhera.
ثُمَّ إِنَّ رَبَّكَ لِلَّذِينَ هَاجَرُوا مِن بَعْدِ مَا فُتِنُوا ثُمَّ جَاهَدُوا وَصَبَرُوا إِنَّ رَبَّكَ مِن بَعْدِهَا لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١١٠﴾
110. Kisha hakika Mola wako kwa wale waliohajiri baada ya kusumbuliwa kisha wakafanya jihadi na wakasubiri, bila shaka Mola wako baada ya hayo ni Mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.
يَوْمَ تَأْتِي كُلُّ نَفْسٍ تُجَادِلُ عَن نَّفْسِهَا وَتُوَفَّىٰ كُلُّ نَفْسٍ مَّا عَمِلَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿١١١﴾
111. Siku ambayo kila nafsi itakuja jitetea, Na kila nafsi italipwa sawa na yale iliyoyafanya, nao hawatadhulumiwa.
Aya 106 –111
Anayemkufuru Mwenyezi Mungu baada ya imani yake.
Tabari ametaja njia nne za irab ya jumla hii. Razi ametaja njia nne na akachagua moja kuwa iko mahali pa maf ’ul; kwa maana ya kukadiriwa kuwa, ninamkusudia kumtaja anayemkufuru...
Ama sisi tumechagua kuwa iko mahali pa mubdata (jumla ya kuanzia maneno) na Khabar yake (ukamailisho wake) ni jumla inayokadirwa kuwa, anayemkufuru Mwenyezi Mungu baada ya imani yake basi ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yake. Jumla hii inafahamika kutokana na jumla iliyo mwishoni mwa Aya hiyo hiyo: ‘Basi ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yao.
Isipokuwa aliyelazimishwa na hali ya kuwa moyo wake umetua juu ya imani.
Hii inafahamisha kuwa iko ruhusa ya kutamka neno la kufuru kwa ajili ya kujiokoa na kuuuliwa ikiwa mwenye kutamka ni muumini wa kweli.
Imeelezwa katika tafsiri ya Razi: Watu walilazimishwa neno la kufuru. Miongoni mwao ni Ammar na wazazi wake Yasir na Summayya. Vilevile Suhayb, Bilal, Khabbab na Salim, Wote hao waliaadhibiwa.
Summayya alifungwa baina ya ngamia wawili na akachomwa mkuki moyoni mwake na Yasir naye pia akauawa, lakini Ammar aliwapatia kile walichotaka kwa ulimi wake, akiwa amelazimika kufanya hivyo. Baadhi ya watu wakasema: ‘Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hakika Ammar amekufuru.
Mtume(s.a.w.w) akasema: Hapana! Hakika Ammar imani imemmjaa kuanzia utosini mwake hadi nyayoni mwake.
Ammar akamajia Mtume huku akilia, Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) akawa anampangusa machozi na kumwambia: Kwani una nini? Wakikurudia, rudia uliyosema, Yametangulia maelezo ya Taqiya katika Juz, 3 (3:28).
Lakini aliyekifungulia kifua chake ukafiri, basi hao ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iko juu yao na watapata adhabu kubwa.
Baada ya Mwenyezi Mungu kumtaja muumini halisi aliyedhihirisha kufu- ru, kuwa yeye anakubaliwa udhuru mbele ya Mwenyezi Mungu; sasa anamtaja yule kafiri wa kweli asiyekuwa na jengine zaidi ya kupendelea ukafiri. Hakuna malipo kwa huyu isipokuwa ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake kali.
Hiyo ni kwa sababu wao wamestahabu maisha ya dunia kuliko ya Akhera.
Hiyo ni ishara ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake. Wamestahabu, yaani wameathirika zaidi, Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawaondolea makafiri rehema yake na atawaadhibu kwa moto wake, kwa sababu wao wameathirika zaidi na maisha ya dunia na starehe zake.
Maana ya yote haya ni kuwa kila mwenye kuathirika na matamanio kuliko haki na mambo ya sasa kuliko yajayo, basi huyo mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama kafiri na mshirikina katika kustahiki ghadhabu na adhabu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Na kwamba Mwenyezi Mungu hawaongoi watu makafiri.
Kwa maana ya kuwa Mwenyezi Mungu hawazingatii kuwa ni wenye kuongoka baada ya kustahabu ukafiri kuliko imani. Vilevile hawaongozi kwa maana ya kuwa hawalipi thawabu. Hakuna mwenye shaka kwamba Mwenyezi Mungu amewaongoa kwa maana ya kuwa amewawekea dalili za kutosha juu ya kuweko kwake Mwenyezi Mungu na utume wa mitume yake. Mwenyezi Mungu anasema:
وَأَمَّا ثَمُودُ فَهَدَيْنَاهُمْ فَاسْتَحَبُّوا الْعَمَىٰ ﴿١٧﴾
Na ama Thamud tuliwaongoa, wakastahabu upofu kuliko uongofu” (41:17).
Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amepiga chapa juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao; na hao ndio wenye kughafilika.
Umetangulia mfano wa Aya hii pamoja na tafsiri yake katika Juz. 1 (2:2).
Hapana shaka kwamba wao ndio wenye kuhasirika Akhera.
Wala hapana hasara kubwa zaidi kuliko ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake.
Kisha hakika Mola wako kwa wale waliohajiri baada ya kusumbuliwa kisha wakafanya jihadi na wakasubiri, bila shaka Mola wako baada ya hayo ni Mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.
Baada ya Mwenyezi Mungu kutaja waumini halisi na makafiri dhahiri, hapa sasa anataja wale waliokuwa wamemwamini Mtume, lakini wakabakia Makka na wasihame naye kwenye Hijra, Wakawapa washirikina baadhi ya waliyoyataka. Kisha wakatubia, wakahama kwa Mtume na wakasubiri kwa kupigania jihadi dhidi ya washirikina na wafisadi. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amebainisha hukumu ya ya hawa kwa kusema: “Bila shaka Mola wako baada ya hayo ni Mwingi wa maghufira, mwenye kurehemu.”
Makusudio ya baada ya hayo ni hayo waliyoyatenda; kama unavyofahamisha mfumo wa maneno. Inawezekana pia ni kwa maana ya baada ya kutubia kwao pamoja na kuhama, jihadi na subira.
Katika tafsiri nyingi imeeelezwa kuwa Aya hii ilishuka kwa sababu ya jamaa fulani katika maswahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) waliokuwa wamebaki nyuma Makka na wasihame pamoja na Mtume. Washirikina wakawapa shida sana mpaka baadhi yao wakafitinishwa na dini yao; kisha wakajuta, lakini wakahofia kuwa toba yao haitatakabaliwa; ndipo ikashuka Aya hii.
Siku ambayo kila nafsi itakuja jitetea.
Yaani kila mtu siku ya Kiyama atajitetea mwenyewe, wala hatajishuguhulisha na mwingine:
لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُمْ يَوْمَئِذٍ شَأْنٌ يُغْنِيهِ ﴿٣٧﴾
Kila mtu siku hiyo atakuwa na jambo linalomshughulisha, (80:37).
Na kila nafsi italipwa sawa na yale iliyoyafanya, nao hawatadhulumiwa.
Mfano wa Aya hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
كُلُّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٢٢﴾
“Na ili ilipwe kila nafsi kwa yale iliyoyachuma, nao hawatadhulumiwa” (45:22)
na pia kauli yake:
كُلُّ نَفْسٍ بِمَا تَسْعَىٰ ﴿١٥﴾
Ili kila nafsi ilipwe kwa iliyoyahangaikia, (20:15).
Yamekaririka maana ya Aya hii katika Aya nyingi.
وَضَرَبَ اللَّـهُ مَثَلًا قَرْيَةً كَانَتْ آمِنَةً مُّطْمَئِنَّةً يَأْتِيهَا رِزْقُهَا رَغَدًا مِّن كُلِّ مَكَانٍ فَكَفَرَتْ بِأَنْعُمِ اللَّـهِ فَأَذَاقَهَا اللَّـهُ لِبَاسَ الْجُوعِ وَالْخَوْفِ بِمَا كَانُوا يَصْنَعُونَ ﴿١١٢﴾
112. Na Mwenyezi Mungu amepiga mfano wa mji uliokuwa na amani na utulivu, riziki yake ikiufikia kwa nafasi kutoka kila mahali. Lakini ukazikufuru neema za Mwenyezi Mungu; kwa hiyo Mwenyezi Mungu akauvika vazi la njaa na hofu kwa sababu ya yale waliyokuwa wakiyafanya.
وَلَقَدْ جَاءَهُمْ رَسُولٌ مِّنْهُمْ فَكَذَّبُوهُ فَأَخَذَهُمُ الْعَذَابُ وَهُمْ ظَالِمُونَ ﴿١١٣﴾
113. Na alikwishawajia Mtume kutoka miongoni mwao, lakini wakamkadhibisha, basi ikawafikia adhabu hali ya kuwa wamedhulumu.
Aya 112 – 113
Wafasiri wametofautiana kuhusu mji uliotajwa kuwa, je, ni mji hasa au ni kiasi cha kukadiria tu kwa ajili ya kupigia mfano? Razi amenukuu kutoka kwa wafasiri wengi kuwa makusidio ya mji huo ni Makka.
Vyovyote iwavyo, sifa hizi zinafanana na Makka na watu wake. Kwa sababu watu walikuwa na amani ya nafsi na mali zao; hawakuwa na hofu ya vita wala ujambazi; kama ilivyokuwa kwa miji mingine ya waarabu.
Pia wakazi wa hapo hawakuwa na haja ya kuhemea chakula, kwa sababu riziki ilkuwa ikiwajia kutoka kila mahali, kutokana na kuitikiwa dua ya Ibrahim(a.s) :
رَبَّنَا لِيُقِيمُوا الصَّلَاةَ فَاجْعَلْ أَفْئِدَةً مِّنَ النَّاسِ تَهْوِي إِلَيْهِمْ وَارْزُقْهُم مِّنَ الثَّمَرَاتِ ﴿٣٧﴾
Basi zijaalie nyoyo za watu zielekee kwao na uwaruzuku matunda. Juz; 13: (14:37).
Lakini watu wa Makka walizikufuru neema za Mwenyezi Mungu kwa kumkadhibisha Muhammad(s.a.w.w) na wakaazimia kumuua mpaka akalazimika kuuhama mji wake.
Watu wa Makka walipatwa na njaa kwa dua ya Mtume(s.a.w.w) , pale aliposema: “Ewe Mola wangu! Wadhikishe kwa madhara na uajaalie miaka (ya shida) kama miaka ya Yusuf, Basi Mwenyezi Mungu akaitikia maombi yake. Wakapatwa na shida mpaka wakawa wanakula mizoga, majibwa, mifupa iliyochomwa, manyani na ngozi iliyochanganywa na damu.
Mtu alikuwa akiangalia mbinguni na kuona moshi kutokana na njaa. Ama hofu iliyowapata ni pale nchi ilipowatingisha wakaanguka ni mateka wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) .
فَكُلُوا مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّهُ حَلَالًا طَيِّبًا وَاشْكُرُوا نِعْمَتَ اللَّهِ إِنْ كُنْتُمْ إِيَّاهُ تَعْبُدُونَ {114 }
114. Basi kuleni katika vile alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu vilivyo halali na vizuri. Na shukuruni neema ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnamwabudu Yeye tu.
إِنَّمَا حَرَّمَ عَلَيْكُمُ الْمَيْتَةَ وَالدَّمَ وَلَحْمَ الْخِنزِيرِ وَمَا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللَّـهِ بِهِ فَمَنِ اضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلَا عَادٍ فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١١٥﴾
115. Hakika amewaharamishia mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilichosomewa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Basi aliyefikwa na dharura bila kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwengi maghufira, Mwenye kurehemu.
وَلَا تَقُولُوا لِمَا تَصِفُ أَلْسِنَتُكُمُ الْكَذِبَ هَـٰذَا حَلَالٌ وَهَـٰذَا حَرَامٌ لِّتَفْتَرُوا عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ إِنَّ الَّذِينَ يَفْتَرُونَ عَلَى اللَّـهِ الْكَذِبَ لَا يُفْلِحُونَ ﴿١١٦﴾
116. Wala msiseme uwongo kwa kuropokwa na ndimi zenu: Hiki ni halali na hiki ni haramu, mkimzulia uwongo Mwenyezi Mungu, Hakika wanaomzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafaulu.
مَتَاعٌ قَلِيلٌ وَلَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿١١٧﴾
117. Ni starehe ndogo nao watapata adhabu chungu.
وَعَلَى الَّذِينَ هَادُوا حَرَّمْنَا مَا قَصَصْنَا عَلَيْكَ مِن قَبْلُ وَمَا ظَلَمْنَاهُمْ وَلَـٰكِن كَانُوا أَنفُسَهُمْ يَظْلِمُونَ ﴿١١٨﴾
118. Na wale waliokuwa mayahudi tuliwaharamishia tuliyokusimulia kabla, Na hatukuwadhulumu, laikini walijidhulumu wenyewe.
ثُمَّ إِنَّ رَبَّكَ لِلَّذِينَ عَمِلُوا السُّوءَ بِجَهَالَةٍ ثُمَّ تَابُوا مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ وَأَصْلَحُوا إِنَّ رَبَّكَ مِن بَعْدِهَا لَغَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿١١٩﴾
119. Kisha hakika Mola wako kwa waliotenda uovu kwa ujinga kisha wakatubu baada ya hayo na wakatengenea, hakika Mola wako ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Aya 114 – 119
Basi kuleni katika vile alivyowaruzuku Mwenyezi Mungu vilivyo halali na vizuri. Na shukuruni neema ya Mwenyezi Mungu ikiwa mnamwabudu Yeye tu. Hakika amewaharamishia mzoga tu na damu na nyama ya nguruwe na kilichosomewa jina la asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Basi aliyefikwa na dharura bila kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwengi maghufira, Mwenye kurehemu.
Umetangulia mfano wa Aya hizi na tafsiri zake katika Juz. 2 (2:173) na katika Juz. 6 (5: 3)
Wala msiseme uwongo kwa kuropokwa na ndimi zenu: Hiki ni halali na hiki ni haramu.
Watu wa jahilia walikuwa wakijihalalalishia na kujiharamishia wao wenyewe tu; kisha wananasibisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu; kama kuhalalisha nyamafu, damu, nyama ya nguruwe na mnyama aliyechinjwa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Vilevile kusema kuwa aliye tumboni mwa mnyama huyu ni wa wanaume tu na ni haramu kwa wanawake na mengineyo yaliyotajwa katika Juz, 8 (6: 139 – 139).
Ndipo Mwenyezi Mungu akawakataza hayo na kusema kuwa ni uwongo na uzushi:Mkimzulia uwongo Mwenyezi Mungu.
Kila mwenye kumtegemezea Mwenyezi Mungu hukumu, kauli au jambo lolote bila dalili mkataa basi atakuwa amemzulia Mwenyezi Mungu uwongo.
Hakika wanaomzulia uwongo Mwenyezi Mungu hawatafaulu. Vipi watafaulu na Mwenyezi Mungu amewakasirikia na amewaandalia adhabu chungu?
Ni starehe ndogo nao watapata adhabu chungu.
Manufaa yoyote katika dunia hayalingani hata na ile adhabu ndogo ya akhera, sikwambi tena ikiwa ni ahabu kubwa:
نُمَتِّعُهُمْ قَلِيلًا ثُمَّ نَضْطَرُّهُمْ إِلَىٰ عَذَابٍ غَلِيظٍ ﴿٢٤﴾
Tunawastarehesha kidogo kisha tutawasukuma kwenye adhabu ngumu. (31:24).
Na wale waliokuwa mayahudi tuliwaharamishia tuliyokusimulia kabla.
Maneno haya anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) , Mwenyezi Mungu anamkumbusha yale aliyomwambia hapo nyuma: “Na kwa wale walio mayahudi tuliharamisha kila mwenye kucha. Na katika ng’ombe na mbuzi na kondoo tukawaharamishia mafuta yao; isipokuwa yale iliyobeba migongo yao, au matumbo, au iliyochanganyika na mifupa, Juz. 8 (6:146).
Na hatukuwadhulumu, laikini walijidhulumu wenyewe.
Kwa sababu wao walimwasi Mwenyezi Mungu na wakapetuka mipaka, ndipo akawaadhibu kwa uharamisho huu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu:
فَبِظُلْمٍ مِّنَ الَّذِينَ هَادُوا حَرَّمْنَا عَلَيْهِمْ طَيِّبَاتٍ أُحِلَّتْ ﴿١٦٠﴾
“Basi kwa dhuluma ya ambao ni mayahudi tuliwaharamishia vitu vizuri walivyohalalishiwa,” Juz.6 (4:160).
Kisha hakika Mola wako kwa waliotenda uovu kwa ujinga kisha wakatubu baada ya hayo na wakatengenea, hakika Mola wako ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Umepita mfano wa Aya hii pamoja na tafsiri yake katika Juz.7 (6: 54).
12
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE
إِنَّ إِبْرَاهِيمَ كَانَ أُمَّةً قَانِتًا لِّلَّـهِ حَنِيفًا وَلَمْ يَكُ مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿١٢٠﴾
120. Hakika Ibrahim alikuwa ni umma, mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu, mnyoofu, wala hakuwa katika washirikina.
شَاكِرًا لِّأَنْعُمِهِ اجْتَبَاهُ وَهَدَاهُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿١٢١﴾
121. Mwenye kuzishukuru neema zake, alimteua na akamwongoza kwenye njia iliyonyooka.
وَآتَيْنَاهُ فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَإِنَّهُ فِي الْآخِرَةِ لَمِنَ الصَّالِحِينَ ﴿١٢٢﴾
122. Na tukampa wema duniani na hakika yeye Akhera atakuwa miongoni mwa watu wema.
ثُمَّ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ أَنِ اتَّبِعْ مِلَّةَ إِبْرَاهِيمَ حَنِيفًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿١٢٣﴾
123. Kisha tukakupa wahyi kwamba ufuate mila ya Ibrahim mnyoofu na hakuwa katika washirikina.
إِنَّمَا جُعِلَ السَّبْتُ عَلَى الَّذِينَ اخْتَلَفُوا فِيهِ وَإِنَّ رَبَّكَ لَيَحْكُمُ بَيْنَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فِيمَا كَانُوا فِيهِ يَخْتَلِفُونَ ﴿١٢٤﴾
124. Hakika Sabato iliwekwa kwa wale waliohitafiliana tu kwenye hiyo. na hakika Mola wako bila shaka atahukumu katika lile walilohitalifiana siku ya Kiyama.
Aya 120 – 124
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuashiria washirikina, katika Aya zilizotangulia, kwamba wao wamehalalisha haramu na kuharamisha halali, sasa anawatolea hoja kwa Ibrahim(a.s) ambaye wanamtakasa na wanalazimisha kumfuata.
Mwenyezi Mungu amemsifu Ibrahim kwa sifa zifuatazo:
1.Hakika Ibrahim alikuwa ni umma . Wametofautiana katika kufasiri umma katika Aya hii, Razi amenukuu kauli nne, zenye nguvu zaidi ni kauli mbili: Kwanza kwamba Ibrahim alikuwa ni mwadilifu kwenye umma aliokuwa nao, Pili kwamba yeye alikuwa ni Imam. Vyovyote iwavyo ni kuwa makusudio ya umma hapa ni kuwa yeye alikuwa ni mkuu aliye adhimu.[5]
2.Mnyenyekevu kwa Mwenyezi Mungu . Yaani mtiifu kwa Mungu.
3.Mnyoofu. Yaani mwenye kuachana na dini potofu, na kushikamana na haki.
4.Wala hakuwa katika washirikina . Hii ni kuwarudi washirikina ambao wanadai kuwa wao wako katika mila ya Ibrahim.
5.Mwenye kuzishukuru neema zake . Shukrani yake kwa Mwenyezi Mungu, kwa yale aliyomneemesha, alikuwa na ikhlasi.
6.Alimteua , Yaani alimchagua kuwa Mtume.
7.Na akamawongoza kwenye njia iliyonyooka , ambayo ni Uislamu sio Uyahudi wala Ukiristo:
مَا كَانَ إِبْرَاهِيمُ يَهُودِيًّا وَلَا نَصْرَانِيًّا وَلَـٰكِن كَانَ حَنِيفًا مُّسْلِمًا وَمَا كَانَ مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٦٧﴾
Ibrahimu hakuwa myahudi wala mnaswara (mkristo), lakini alikuwa Mwislamu, mnyoofu na hakuwa katika washirikina, Juz, 3 (3:67).
8.Na tukampa wema duniani ambao ni kuadhimishwa na watu wa dini zote na kukubali kuwa yeye ni Mtume
9.Na hakika Akhera yeye atakuwa miongoni mwa watu wema . Hii ni kuitikiwa dua yake pale alisema:
رَبِّ هَبْ لِي حُكْمًا وَأَلْحِقْنِي بِالصَّالِحِينَ ﴿٨٣﴾
“Mola wangu nitunukie hukumu na uniunganishe na watu wema” (26:83)
Kisha tukakupa wahyi kwamba ufuate mila ya Ibrahim mnyoofu na hakuwa katika washirikina.
Hii ni dalili kwamba Uislamu na dini ya Ibrahim ni moja katika itikadi na kuukana ushirikina. Basi mwenye kudai kuwa yuko katika dini ya Ibrahim na huku anaukana utume wa Muhammad atakuwa amejipinga yeye mweyewe, atake asitake.
Unaweza kuuliza kuwa : Muhammad(s.a.w.w) ni bwana wa Mitume, itakuwaje aamrishwe kumfuata Mtume mwengine?
Jibu : Lengo la kufuata hapa ni kuwarudi washirikina amabao wanaikubali dini ya Ibrahim na kuipinga dini ya Muhammad(s.a.w.w) na hali ni kitu kimoja. Zaidi ya hayo ni kuwa amri ya kufuata hapa ni kwa kutangulia; yaani amfuate aliyemtangulia, Na kutangulia hakumaanishi ubora zaidi katika jamabo lolote.
Hakika Sabato iliwekwa kwa wale waliohitalifiana tu kwenye hiyo.
Makusudio ya kuwekwa ni kuwa ni wajibu; yaani Mwenyezi Mungu alilazimisha kuadhimishwa sabato (Jumamosi) na kuacha kufanyakazi kwa mayahudi peke yao wala haikuwekewa yeyote kabla yao wala baada yao.
Inasemekana kuwa jamaa miongoni mwao waliikataa Ijumaa; wakawa hawataki siku nyigine isipokuwa Jummamosi tu. Ndipo Mwenyezi Mungu akawakubalia, lakini kwa sharti la kuwa wasivue siku hiyo. Basi wakakubali sharti, lakini hawakulitekeleza; kama ilivyo desturi ya mayahudi siku zote na sehemu zote.
Mwenyezi Mungu hakubainisha sababu ya kutofautiana katika Sabato, kuwa je, walitofautiana katika ruhusa ya kufanya kazi siku hiyo, au walitofautiana kuhusu Sabato yenyewe kwamba wengine walisema ni sikukuu na wengine wakasema si sikuu?
Lililo na nguvu ni kuwa wao waliotofautiana katika uharamu wa kuvua siku hiyo; kama tulivyodokeza katika Juz.9 (7:163–166). Kwa sababu wote waliafikiana kuwa sabato ni sikukuu.
Na hakika Mola wako bila shaka atahukumu katika lile walilohitalifiana siku ya Kiyama.
Na hukumu yake siku hiyo itakuwa ni kuwapa thawabu watiifu na kuwaadhibu waasi.
ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ إِنَّ رَبَّكَ هُوَ أَعْلَمُ بِمَن ضَلَّ عَن سَبِيلِهِ وَهُوَ أَعْلَمُ بِالْمُهْتَدِينَ ﴿١٢٥﴾
125. Waite kwenye njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako ndiye anayemjua zaidi aliyepotea njia yake na Yeye ndiye anayewajua zaidi walioongoka.
وَإِنْ عَاقَبْتُمْ فَعَاقِبُوا بِمِثْلِ مَا عُوقِبْتُم بِهِ وَلَئِن صَبَرْتُمْ لَهُوَ خَيْرٌ لِّلصَّابِرِينَ ﴿١٢٦﴾
126. Na kama mkilipiza basi lipizeni kama mlivyofanyiwa. Na kama mtasubiri, basi hakika hivyo ni bora zaidi kwa wanaosubiri.
وَاصْبِرْ وَمَا صَبْرُكَ إِلَّا بِاللَّـهِ وَلَا تَحْزَنْ عَلَيْهِمْ وَلَا تَكُ فِي ضَيْقٍ مِّمَّا يَمْكُرُونَ ﴿١٢٧﴾
127. Na subiri na subira yako haikuwa ila kwa Mwenyezi Mungu, wala usihuzunike wala usiwe katika dhiki kwa hila wanazozifanya.
إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الَّذِينَ اتَّقَوا وَّالَّذِينَ هُم مُّحْسِنُونَ ﴿١٢٨﴾
128. Na wale ambao wanatenda mema Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye kucha.
Aya 125 -128
Waite kwenye njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora.
Aya hii inatupa mwongozo wa mambo yafuatayo:-
1. Mwito unapasa uwe wa haki usiokuwa na lengo jingine lolote. Mtu yeyote anayetoa mwito usiokuwa wa haki, basi mwito wake utakuwa ni ufisadi na upotofu. Kosa kubwa zaidi ni la yule anayeufanya mwito wa kumwendea Mungu na kwenye haki kuwa ni nyenzo za kufikia kwenye mambo yake na jaha yake; kama wafanyavyo viongozi na maraisi wa dini na dunia.
2. Mwito uwe kwa hekima na mawaidha mazuri. Ni wazi kuwa vitenda kazi vya hekima ni elimu na akili. Akili ndiyo itakayoweza kutofautisha anayetoa mwito wa haki na wa batili na wa heri na wa sahari. Hali za wahutubiaji hujulikana kulingana na ukali na upole.
3. Mawaidha mazuri zaidi ni kuhutubia yule anayemuongoza aliyekosea kwa mfumo unaotambulisha kuwa amekosea, sio kurukia kwa lawama. Walishasema wa kale: “Kubembeleza ni ufasaha zaidi kuliko kuweka wazi” Kwa maneno mengine ni kuwa mwaidha mazuri ndiyo yanayopelekea kufikia malengo; kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Pinga kwa lililo zuri. Hapo yule ambaye baina yako na yeye pana uadui atakuwa kama rafiki mkubwa” (42: 34).
Kujadiliana kwa namna iliyo bora. Hilo litakuwa ikiwa lengo ni kuidhi- hirisha haki na kukinaisha, sio kwa lengo la ushindi na kuziba mdomo wa mwengine.
Hakika Mola wako ndiye anayemjua zaidi aliyepotea njia yake na Yeye ndiye anayewajua zaidi walioongoka.
Baada ya Mwenyezi Mungu kumwamuru Mtume wake kufikisha (tabligh) kwa hekima na kujadiliana vizuri, sasa anamwambia kuwa hilo tu ndio lililo wajibu juu yake, Ama uwongofu hana jukumu nao. Hii ni kuonyesha kuwa hamasa katika mwito (da’wa) haifai katika mambo yote na hali zote. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: Sema hii ni haki itokayo kwa Mola wenu, anayetaka na aiamini na anayetaka aikatae, (18: 29).
Na kama mkilipiza basi lipizeni kama mlivyofanyiwa.
Aya hii ni sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Basi wanaowachokoza, pia nanyi wachokozeni kwa kadiri walivyowachokoza.” Juz.2 (2:193).
Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa Aya hii ilishuka Madina, iliyoingizwa kwenye Sura ya Makka na kwamba sababu ya kushuka kwake ni kuwa washirikina walizikatakata maiti za Waislamu katika vita vya Uhudi; hasa Hamza bin Abdul-Mutwalib, walimpasua tumbo lake, na Hind akachukua ini lake akalitafuna. Wakamakata pua na masikio na wakamkata mkono wake wa kuume. Waislamu wakasema: Tukiwapata, wachilia mbali waliokufa; hata walio hai tutawakatakata, Ndipo ikashuka Aya hii.
Na kama mtasubiri, basi hakika hivyo ni bora zaidi kwa wanaosubiri.
Baada ya Mwenyezi Mungu kuashiria kuwa kisasi kizidi mfano wake, sasa anasema kuwa kusamehe na kuvunja ghadhabu ni bora zaidi; kama alivyosema mahali pengine: “Na anayesubiri na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa” (42:43).
Na subiri na subira yako haikuwa ila kwa Mwenyezi Mungu.
Yaani kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na tawfiki yake, Maneno haya anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) , lakini wanakusudiwa wote, Tumezungumzia kuhusu subira katika Juz, 2 (2:153–155).
Wala usihuzunike wala usiwe katika dhiki kwa hila wanazozifanya.
Hakuna yeyote anayetoa mwito wa heri ila atapambana na maudhi na kero za watu wa shari. Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemuusia kila anayelingania kwenye njia yake kutohuzunika kwa kufanywa mwongo na upinzani wa mwenye kupinga mwito wake. Kwa sababu mwisho siku zote ni wa mwenye kumcha Mungu:
Hakika Mwenyezi Mungu yuko pamoja na wenye kucha yale aliyowayaharamisha kwa kumuogopa Yeyena wale ambao wanatenda mema kwa kuipiga vita batili na watu wake na kuwasamehe watu katika haki binafsi sio haki za umma.
Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s) Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.
YALIYOMO
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE 1
IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA 1
IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA 1
IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED 1
IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU 1
UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI 1
MAKOSA YA CHAPA 2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE 3
HIYO NI AYA ZA KITABU 3
MAANA 3
WEWE NI MWENDAWAZIMU 4
MAANA 4
NA ARDHI TUMEITANDAZA 7
MAANA 7
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE 10
MTU KUTOKANA NA UDONGO 10
MAANA 10
MUNGU ANAULIZA NA IBLISI ANAJIBU 13
MAANA 13
WENYE TAKUA PEPONI 14
MAANA 15
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE 16
WAGENI WA IBRAHIM 16
MAANA 16
KAUMU YA LUT 18
MAANA 18
UKELELE UKAWANYAKUA 20
MAANA 20
SABA ZINAZORUDIWA 23
LUGHA 23
MAANA 23
MWISHO WA SURA YA KUMI NA TANO 25
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE 26
IMEFIKA AMRI YA MWENYEZI MUNGU 26
MAANA 26
WANYAMA, FARASI, NYUMBU NA PUNDA 28
MAANA 28
KUKUMBUSHA NEEMA ZA MWENYEZI MUNGU 30
MAANA 30
WANAOOMBA ASIYEKUWA MWENYEZI MUNGU 32
MAANA 32
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE 34
HUSEMA NGANO ZA WATU WA KALE 34
MAANA 34
WATASEMA KHERI 37
MAANA 37
WAKASEMA WALIOSHIRIKISHA 38
MAANA 39
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE 41
WANAAPA KWA MWENYEZI MUNGU 41
MAANA 41
WAULIZENI WENYE UKUMBUSHO 43
MAANA 43
HAKIKA YEYE NI MUNGU MMOJA TU 46
MAANA 46
WANAMFANYIA MWENYEZI MUNGU MABINTI 47
MAANA 47
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE 50
MWENYE KUHOFIA MAUTI HUHARAKISHWA 50
MAANA 50
MWENYEZI MUNGU AMETERMSHA MAJI KUTOKA MBINGUNI 52
NAHAW (SARUFI) 52
MAANA 52
MUNGU AMEFADHILISHA BAADHI YENU KATIKA RIZKI 54
MAANA 54
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE 57
MWENYE UWEZA NA MWENYE KUSHINDWA 57
MAANA 57
MWENYEZI MUNGU AMEWATOA MATUMBONI MWA MAMA ZENU HAMJUI KITU 59
MAANA 59
PAMOJA NA WENYE MAADA 59
ULIMWENGU NI MKUBWA KULIKO MAROKETI 59
HESHIMA YA NYUMBA KATIKA SHARIA 61
VIPI NEEMA YA DHAHABU NYEUSI 62
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE 64
TUTAPOMWINUA SHAHIDI 64
MAANA 64
MWENYEZI MUNGU ANAAMRISHA UADILIFU NA HISANI 67
LUGHA 67
MAANA 67
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE 70
KILICHO KWA MUNGU NI BORA 70
MAANA 71
AYA MAHALI PA AYA NYINGINE 74
LUGHA 74
MAANA 74
MWONGO KAFIRI 75
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE 77
MOYO WAKE UMETUA JUU YA IMANI 77
MAANA 77
MJI ULIOKUWA NA AMANI 79
MAANA 80
KULENI NA MSHUKURU 81
MAANA 81
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NNE 83
IBRAHIM ALIKUWA UMMA 83
MAANA 83
HEKIMA NA MAWAIDHA MAZURI 85
MAANA 85
SHARTI YA KUCHAPA 86
MWISHO WA JUZUU YA KUMI NA NNE 87
YALIYOMO 88
[1] . Kumbuka juzijuzi hiyo, ilikuwa ni katika mwaka wa 1969 - Mtarjumu.
[2] . Hata Waingereza wamechukua msamiati wa neno la kuingiliana wanume kwa kunasibisha kwenye mji huo, wakasema: Sodomy - Mtarjumu.
[3] . Nimeshindwa kupata neno moja la kiswahili kufasiri neno Twariyya, ndio nikalitohoa neno hilo la kingerza Fresh ambalo linatumika sana kwenya kiswahili cha mitaani; kama walivyotohoa kwenye kiswahili sanifu wakapata neno fremu n.k.-Mtarjumu.
[4] . Katika Kiswahili hakuna wingi wa kulia wala kushoto, lakini kwenye kiarabu uko-Mtarjumu.
[5] . Mwenye tafsir Rawhil bayan alipofasiri Aya hii, alisema: “Imeelezwa katika Hadith ‘Hassein ni mjukuu katika vitukuu” yaani umma katika ummati. Kwa maana ya kuwa vitukuu ambao ni masharifu wanatokana na kizazi cha Zaynul’abidin, mtoto wa Husseni, Kwa hiyo ameeneza umma. Kisha akaendelea kusema mwenye Rawhil-bayan: “Baadhi ya jamaa wakati wake walisema kuwa Hussein ni mtume”, Na sisi hatujawahi kusikia hili. Hakuna shaka kwamba hilo ni ukafiri na ulahidi.