TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA
IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU
Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.
Kama lilivyo jina la Tafsiri ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo.
Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.
Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.
Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea. Hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka kwa lugha ya kiswahili hivi karibuni Inshaallah).
Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.
Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasayansi kama kina Enstein, wasanii kama Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.
Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.
Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.
Mwisho: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.
Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa, Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.
Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146), Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.
Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawamal qiyama. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.
Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu Jabal amil 'Makosa ya chapa.'
Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"
Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.
Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa.” Kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.
Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu." Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).
MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH
1
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
قَالَ أَلَمْ أَقُل لَّكَ إِنَّكَ لَن تَسْتَطِيعَ مَعِيَ صَبْرًا ﴿٧٥﴾
75. Akasema: Sikukuambia kuwa wewe hutaweza kuvumilia kuwa pamoja nami?
قَالَ إِن سَأَلْتُكَ عَن شَيْءٍ بَعْدَهَا فَلَا تُصَاحِبْنِي قَدْ بَلَغْتَ مِن لَّدُنِّي عُذْرًا ﴿٧٦﴾
76. Akasema: Nikikuuliza tena kitu baada ya haya usifuatane nami kwani umekwishapata udhuru kwangu
فَانطَلَقَا حَتَّىٰ إِذَا أَتَيَا أَهْلَ قَرْيَةٍ اسْتَطْعَمَا أَهْلَهَا فَأَبَوْا أَن يُضَيِّفُوهُمَا فَوَجَدَا فِيهَا جِدَارًا يُرِيدُ أَن يَنقَضَّ فَأَقَامَهُ قَالَ لَوْ شِئْتَ لَاتَّخَذْتَ عَلَيْهِ أَجْرًا ﴿٧٧﴾
77. Basi wawili hao wakaondoka, mpaka wakawafikia watu wa mji mmoja, wakawaomba watu wake wawape chakula, nao wakakataa kuwakaribisha. Hapo wakakuta ukuta unataka kuanguka akausimamisha, Akasema (Musa): Ungelitaka ungelichukua ujira kwa haya.
قَالَ هَـٰذَا فِرَاقُ بَيْنِي وَبَيْنِكَ سَأُنَبِّئُكَ بِتَأْوِيلِ مَا لَمْ تَسْتَطِع عَّلَيْهِ صَبْرًا ﴿٧٨﴾
78. Akasema: “Huku ndio kufarikiana baina yangu na wewe. Nitakueleza taawili ya yale uliyokuwa huwezi kuyavumilia.
أَمَّا السَّفِينَةُ فَكَانَتْ لِمَسَاكِينَ يَعْمَلُونَ فِي الْبَحْرِ فَأَرَدتُّ أَنْ أَعِيبَهَا وَكَانَ وَرَاءَهُم مَّلِكٌ يَأْخُذُ كُلَّ سَفِينَةٍ غَصْبًا ﴿٧٩﴾
79. Ama ile jahazi iikuwa ni ya maskini wafanyao kazi baharini. Nilitaka kuitia kasoro, kwani nyuma yao kulikuwa na mfalme anayenyang’anya majahazi yote.
وَأَمَّا الْغُلَامُ فَكَانَ أَبَوَاهُ مُؤْمِنَيْنِ فَخَشِينَا أَن يُرْهِقَهُمَا طُغْيَانًا وَكُفْرًا ﴿٨٠﴾
80. Ama yule kijana wazazi wake walikuwa waumini, tukahofia asiwahangaishe kwa uasi na kufuru.
فَأَرَدْنَا أَن يُبْدِلَهُمَا رَبُّهُمَا خَيْرًا مِّنْهُ زَكَاةً وَأَقْرَبَ رُحْمًا ﴿٨١﴾
81. Basi tulitaka Mola wao awabadilishie aliye bora zaidi kuliko huyo kwa kutakasika na aliye karibu zaidi kwa huruma.
وَأَمَّا الْجِدَارُ فَكَانَ لِغُلَامَيْنِ يَتِيمَيْنِ فِي الْمَدِينَةِ وَكَانَ تَحْتَهُ كَنزٌ لَّهُمَا وَكَانَ أَبُوهُمَا صَالِحًا فَأَرَادَ رَبُّكَ أَن يَبْلُغَا أَشُدَّهُمَا وَيَسْتَخْرِجَا كَنزَهُمَا رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ وَمَا فَعَلْتُهُ عَنْ أَمْرِي ذَٰلِكَ تَأْوِيلُ مَا لَمْ تَسْطِع عَّلَيْهِ صَبْرًا ﴿٨٢﴾
82. Na ama ukuta ulikuwa ni wa vijana wawili mayatima kule mjini, na chini yake ilikuwako hazina yao, na baba yao alikuwa ni mtu mwema. Basi Mola wako alitaka wafikie kukomaa na wajitolee hazina yao. Nirehema itokayo kwa Mola wako. Hayo sikuyatenda kwa amri yangu, Hiyo ndiyo tafsiri ya ambayo hukaweza kuyavu milia.
Aya 75 – 82
Juzuu ya 15, imeishia na Aya ya kuuliwa kijana na mshangao wa Musa kwa tendo hilo. Kwenye Aya hii swahibu wa Musa anamkumbusha kuhusu walivyoahidiana:
Akasema: “Sikukuambia kuwa wewe hutaweza kuvumilia kuwa pamoja nami?
Anamkumbusha tena lile sharti na Musa naye anaomba tena msamaha akasema:Nikikuuliza tena kitu baada ya haya usifuatane nami.
Hapo mwanzo yule mtu alimuwekea sharti Musa, hivi sasa Musa anajiwekea mwenyewe sharti kwamba asisuhubiane naye tena kama atamuuliza, na waumini wanalazimiana na masharti yao; sikwambii tena mitume.
Kwani umekwishapata udhuru kwangu; Sababu zote zitakuwa zimekwisha.
Basi wawili hao wakaondoka, mpaka wakawafikia watu wa mji mmoja.
Huu ni ushahidi wa tatu wa kuwa ni wachache wanaovumilia. Ushahidi wa kwanza na wa pili umekwishapita kwenye Juzuu ya 15. Inasemekana mji huo walioufikia ni Antioch. Katika riwaya iliyopokewa kwa Imam Jafar As-Swadiq, inasema kuwa ni Nazarethi[1] .
Wakawaomba watu wake wawape chakula, lakini nao wakakataa kuwakaribisha.
Wafasiri wanasema kuwa Mwenyezi Mungu amesema walikataa kuwakaribisha, badala ya walikataa kuwapa chakula, kwa vile watu wa mji ule walikuwa wabaya sana. Kwani hakuna anayemkataa mgeni ila mtu mbaya, hasa ikiwa mgeni ni wa mbali.
Hapo wakakuta ukuta unataka kuanguka, akausimamisha.
Hapo, ni hapo kwenye mji. Aliyeusimamisha, ni yule mja mwema. Kutaka kuanguka, ni kukurubia kuanguka. Maana ni kuwa Musa na mwenzake walikuta ukuta unakaribia kuanguka, yule mwenzake akautengeneza bila ya malipo yoyote.
Ndipo Musa akastaajabu na akasema: Ungelitaka ungelichukua ujira kwa haya.
Unafanya kazi ya bure tu kwa watu waliokataa hata kutukaribisha tukiwa na shida. Kutoboa jahazi na kuua kijana ni mifano miwili yenye dhahiri ya ubaya na kusimamisha ukuta ni kinyume cha mifano hiyo miwili.
Akasema: Huku ndio kufarikiana baina yangu na wewe. Nitakueleza taawili ya yale uliyokuwa huwezi kuyavumilia.
Mja mwema alitoa sharti kwa Musa la kutoulizwa, Musa akakubali, lakini pamoja na hayo akauliza, Alipokumbushwa akaomba msamaha, Tena akauliza baada ya msamaha. Alipokumbushwa mara ya pili akajiwekea sharti yeye mwenyewe la kutofuatana naye kama atauliza tena. Lakini bado akauliza, ingawaje alikuwa na hamu sana ya kufuatana naye.
Musa hana lawama yoyote katika yote aliyoyauliza; Kwa sababu nafsi yake inaweza kuvumilia mambo ya kheri na mazuri, lakini yale anayoyaona ni mabaya, hakuweza wala hataweza kuvumilia; hata kama hilo litapelekea kuvunja masharti na maelewano. Ni kipimo gani cha masharti kinachoweza kupimwa kuacha mema na kukataza mabaya.
Imani sahihi haiwezi kuzuiwa na kitu chochote, si msukumo wa nafsi wala mengineyo. Hakuna kitu kigumu zaidi kuliko imani sahihi; na atakayeshindwa na kitu chochote katika hivyo basi hana imani sahihi; hata akiswali, kufunga na kuhiji Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu.
Huku ndio kufarikiana baina yangu na wewe , ushike njia yako nami nishike yangu, Hivyo ndivyo alivyomwambia Musa. Lakini kabla ya kutengana, yule mja mwema alimwambia Musa hekima ya yale aliyoyapinga, kama ifuatavyo:
Ama lile jahazi lilikuwa ni la maskini wafanyao kazi baharini. Nilitaka kulitia kasoro, kwani nyuma yao kulikuwa na mfalme anayenyang’anya majahazi yote.
Mwenye akili anavumilia madhara kwa ajili ya kuondoa madhara makubwa; kama anavyosema mshairi: “Nimevumilia nusu shari kihofia shari yote.”
Kuanzia hapa ndio mafaqihi wakaafikiana kuwa dhara kubwa inakingwa na dhara hafifu na yakiingiliana maovu mawili litaangaliwa lile lenye madhara zaidi kwa lile lililo na machache. Kutokana na kawaida hii wametoa hukumu nyingi, kama vile kuruhusiwa kukata kiungo ikiwa kitamletea mtu maangamizi.
Ama yule kijana wazazi wake walikuwa waumini, tukahofia asiwahangaishe kwa uasi na kufuru. Basi tulitaka Mola wao awabadilishie aliye bora zaidi kuliko huyo kwa kutakasika na aliye karibu zaidi kwa huruma.
Imepokewa riwaya kutoka kwa Imam Jafar As-Swadiq(a.s) kuwa huyo kijana aliuawa katika rika la balehe na alikuwa kafiri. Akifanya juhudi kuwaingiza wazazi wake kwenye ukafiri, sawa na wanavyofanya baadhi ya vijana wa kileo.
Tumewahi kuwona maulama wengi wa kidini waliokuwa ni tegemeo kubwa la watu, lakini mara tu walipobalehe vijana wao, wakabomoa yote waliyojenga baba zao kwa muda mrefu.
Kuna kauli mashuhuri ya Imam Ali(a.s) :“Zubeir aliendelea kuwa nasi mpaka alipokuwa na kijana wake Abdullah”
Ahmad Amin wa Misr, katika kitabu Hayati (maisha yangu), anasema: “Hivi sasa mimi na uzee wangu ninakubali kila ambalo nilikuwa nikilikataa na huwa ninaacha misimamo niliyokuwa nayo kwa sababu ya watu na mazungumzo yao na wingi wa watoto.”
• Udogo sikutaka Hawa nafsi yangu
• Zama zikakatika kawa na mvi zangu
• Hawa zikanishika kinyume matakwa yangu
• Laitani ngezalika nao ukubwa wangu
• Udogo wa marika kupinga nafsi yangu
Na ama ukuta ulikuwa ni wa vijana wawili mayatima kule mjini, na chini yake ilikuwako hazina yao, na baba yao alikuwa ni mtu mwema. Basi Mola wako alitaka wafikie kukomaa na wajitolee hazina yao. Ni rehema itokayo kwa Mola wako. Hayo sikuyatenda kwa amri yangu, Hiyo ndiyo tafsiri ya ambayo hukaweza kuyavumilia.”
Kwa ufupi ni kuwa ukuta ulikua wa watoto wawili na chini yake kulikuwa na dafina yao. Mwenyezi Mungu akataka kuilinda mali hiyo isipotee, kwa kubakia ukuta, mpaka wawe wakubwa au wawe na akili, kisha wajitolee mali yao wao wenyewe; na mzazi wao alikuwa mtu mwema “Na wema wa mtu mumini, Mwenyezi Mungu huufanya kwa mtoto wake na mtoto wa mtoto wake.”
Funzo la kisa hiki ni kwamba mtu asijione ni yeye tu na asifanye haraka kujiamulia jambo kwa kuangalia upande mmoja, bali ni lazima aangalie pande zote kwa undani na kulinganisha kisha aangalie ulio bora zaidi; kwani masilahi huwa yanasigana na madhara.
Hakuna jambo lolote la manufaa isipokuwa lina baadhi ya madhara ndani yake; kama ambavyo hakuna jambo lolote ila lina baadhi ya manufaa. Siku zote mazingatio ni kwa lililo na wingi.
وَيَسْأَلُونَكَ عَن ذِي الْقَرْنَيْنِ قُلْ سَأَتْلُو عَلَيْكُم مِّنْهُ ذِكْرًا ﴿٨٣﴾
83. Na wanakuuliza kuhusu Dhul-qarnain, Waambie nitawasimulia baadhi ya habari zake.
إِنَّا مَكَّنَّا لَهُ فِي الْأَرْضِ وَآتَيْنَاهُ مِن كُلِّ شَيْءٍ سَبَبًا ﴿٨٤﴾
84. Hakika sisi tulimmakinisha katika ardhi na tukampa sababu ya kila kitu.
فَأَتْبَعَ سَبَبًا ﴿٨٥﴾
85. Basi akafuata sababu.
حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ مَغْرِبَ الشَّمْسِ وَجَدَهَا تَغْرُبُ فِي عَيْنٍ حَمِئَةٍ وَوَجَدَ عِندَهَا قَوْمًا قُلْنَا يَا ذَا الْقَرْنَيْنِ إِمَّا أَن تُعَذِّبَ وَإِمَّا أَن تَتَّخِذَ فِيهِمْ حُسْنًا ﴿٨٦﴾
86. Hata alipofika machweo ya jua aliona linatua kwenye chemchem yenye matope meusi, Na hapo akawakuta watu, tukasema: Ewe Dhul-qarnain! Ama uwaadhibu au watwae kwa wema.
قَالَ أَمَّا مَن ظَلَمَ فَسَوْفَ نُعَذِّبُهُ ثُمَّ يُرَدُّ إِلَىٰ رَبِّهِ فَيُعَذِّبُهُ عَذَابًا نُّكْرًا ﴿٨٧﴾
87. Akasema: “Ama aliyedhulumu, basi tutamwadhibu adhabu na kisha atarudishwa kwa Mola wake amuadhibu adhabu isiyojulikana.
وَأَمَّا مَنْ آمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَلَهُ جَزَاءً الْحُسْنَىٰ وَسَنَقُولُ لَهُ مِنْ أَمْرِنَا يُسْرًا ﴿٨٨﴾
88. Na ama mwenye kuamini na akatenda mema tutamlipa malipo mazuri na tutamwambia lililo jepesi katika amri yetu.
ثُمَّ أَتْبَعَ سَبَبًا ﴿٨٩﴾
89. Kisha akafuata sababu.
حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ مَطْلِعَ الشَّمْسِ وَجَدَهَا تَطْلُعُ عَلَىٰ قَوْمٍ لَّمْ نَجْعَل لَّهُم مِّن دُونِهَا سِتْرًا ﴿٩٠﴾
90. Mpaka alipofika mawiyo ya jua aliona linawachomozea watu tusiowawekea sitara ya kuwakinga nalo.
كَذَٰلِكَ وَقَدْ أَحَطْنَا بِمَا لَدَيْهِ خُبْرًا ﴿٩١﴾
91. Kama hivyo tulizijua vizuri habari zake.
ثُمَّ أَتْبَعَ سَبَبًا ﴿٩٢﴾
92. Kisha akafuata sababu.
Aya 83 – 92
Na wanakuuliza kuhusu Dhul- qarnain, Waambie nitawasimulia baadhi ya habari zake.
Wametofautiana kuhusu Dhul-qarnaini huyu kuwa ni nani? Ikasemekana kuwa alikuwa miongoni mwa Malaika, lakini hili ni jambo la kushangaza, Ikasemekana alikuwa Mtume.
Imepokewa kutoka kwa Imam Ali(a.s) kwamba yeye alikuwa ni mja mwema. Hakuna shaka ya wema wake, kwani vitendo vyake na kauli zake, alizozisajili Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika kitabu chake, zinatoa ushahidi wa ubora wake na wema wake.
Pia imesemekana kuwa ni Alexandre wa Macedonia (The great Alexandre), mwanafunzi wa Aristotle. Lakini hili nalo ni la kushangaza zaidi, kwa sababu Alexandre alikuwa ni mwabudu masanamu na Dhul-qar-nain alikuwa akimwamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Amenukuu Razi na Abu Hayyani Al-Andalusi (Mhispania), kutoka kwa Abu Rayhan Al-Biruni, kuwa Dhul-qarnaini alikuwa ni mwarabu wa Yemen kutoka kabila la Himayr na jina ake ni Abu Bakr.
Vilevile wametofautiana, kuwa kwa nini aliitwa Dhul-qarnain (mwenye pembe mbii)? Ikasemekana ni kwa kuwa yeye aikuwa ni mtukufu wa wazazi wawili.
Ikasemekana kuwa ni kwa vile alikuwa na misokoto miwili ya nywele. Pia ikasemekana ni kwa vile yeye alimiliki mashariki na magharibi na mengineyo katika kauli za kutofautiana.
Ni ajabu kwa wafasiri kujishughulisha na kuwashughulisha watu kwa jambo lisilokuwa na faida yoyote ya kidunia wala akhera. Tangu lini Qur’an ikajishughulisha na majina na sababu zake? Kama hilo lingekuwa na faida basi Qur’an isingelinyamazia.
Ni kwa ajili hii ndio sisi tukatosheka na dhahiri ya Qur’an na tunasema: watu walimuuliza Mtume mtukufu(s.a.w.w) kuhusu mtu aliyeitwa Dhul-qarnain, Mwenyezi Mungu akamwamrisha awaambie waulizaji kuwa nitawaambia baadhi ya habari zake.
Hakika sisi tulimmakinisha katika ardhi na tumpa sababu ya kila kitu
Makusudio ya kummakinisha hapa ni nguvu na utawala. Na sababu ni nyenzo zinazomfikisha mtu kwenye yale anayoyataka; kama vile elimu, uwezo, afya, mali, watu na zana. Zaidi ya hayo ni tawfiki ya Mungu na msaada wake, Nyenzo zote hizi alikuwa nazo Dhul-qarnain. Kwa hiyo akawa ni mwenye nguvu, Hii ndiyo maana ya kummakinisha katika ardhi. Aya inafahamisha waziwazi kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) analeta vitu kwa sababu zake.
Basi akafuata sababu
Mwenyezi Mungu alimwandalia njia naye akazitumia katika kheri na matendo mema. Miongoni mwazo ni kwenda kwake magharibi ambako amekuashiria Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika kauli yake:
Hata alipofika machweo ya jua aliona linatua kwenye chemchem yenye matope meusi.
Makusudio ya machweo ya jua ni miji ya magharibi, Ni wazi kuwa jua haliwezi kuingia kwenye chemchem. Kwa hio makusudio ni chemchem yenye matope meusi ya bahari ambayo yanaonekana na watu kama Jua linatua ndani yake. Bahari hii ni miongoni mwa bahari za miji ya magharibi, lakini ni bahari gani hiyo? Mwenyezi Mungu ndiye mjuzi zaidi wa hilo. Sheikh Maraghi anasema ni bahari ya Atlantic.
Na hapo akawakuta watu, tukasema: Ewe Dhul-qarnain! Ama uwaadhibu au watwae kwa wema.
Makusudio ya hapo ni hapo kwenye chemchem. Dhahiri ya Aya, ikiwa peke yake, inafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimwachia Dhul-qarnain afanye atakavyo kwa watu wa mji huo, akitaka atawaadhibu na akitaka awafanyie hisani.
Na ilivyo hasa ni kuwa jambo hilo haliafikiani na uadilifu wake Mwenyezi Mungu Mtukufu, kafiri na washirikina, ikiwa watang’ang’ania kufru na shirk, tutapata kuwa watu aliowakuta Dhul-qar-nain huko magharibi walikuwa ni makafiri na kwamba yeye aliwelezea imani wakaikataa.
Unaweza kuuliza : kuwa je, inafaa kuwafanyia wema makafiri?
Jibu : Inafaa ikiwa hawakutupiga vita kwenye dini yetu wala hawakututoa majumbani mwetu. Mwenyezi Mungu anasema:
لَّا يَنْهَاكُمُ اللَّـهُ عَنِ الَّذِينَ لَمْ يُقَاتِلُوكُمْ فِي الدِّينِ وَلَمْ يُخْرِجُوكُم مِّن دِيَارِكُمْ أَن تَبَرُّوهُمْ وَتُقْسِطُوا إِلَيْهِمْ إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ الْمُقْسِطِينَ ﴿٨﴾
“Mwenyezi Mungu hawakatazi kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakupigana nanyi kwa ajili ya dini wala hawakuwafukuza katika miji yenu; Hakika Mwenyezi Mungu anawapenda wafanya uadilifu.” (60:8).
Akasema (Dhul-qarnain): Ama aliyedhulumu, basi tutamwadhibu adhabu na kisha atarudishwa kwa Mola wake amuadhibu adhabu isiyojulikana. Na ama mwenye kuamnini na akatenda mema tutamli- pa malipo mazuri na tutamwambia lililo jepesi katika amri yetu.
Hii ndio desturi ya hukumu Dhul-qarnain na utawala wake. Kwa ufupi ni kuwa, upanga ni kwa mwenye kuasi na wema ni kwa mtiifu. Hakika mali, elimu, na utawala ni neema kubwa anayowapa mtihani Mwenyezi Mungu kwayo waja wake.
Basi neema hiyo huwazidisha washari ukafiri na kupitua mipaka, lakini watu wazuri huifanya neema hiyo kuwa ni nyenzo ya kumtii Mwenyezi Mungu na kumridhisha, kama alivyofanya Dhul-qar- nain.
Kisha akafuata sababu, Yaani akafuata njia, Dhul-qarnain alirejea kutoka magharibi na akaelekea mashariki ambako Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekuashria kwa kauli yake:
Mpaka alipofika mawiyo ya jua aliona linawachomozea watu tusiowawekea sitara ya kuwakinga nalo.
Makusudio ya mawiyo ya jua hapa ni upande wa mashariki, na sitara ni jengo na mfano wake, kama hema, vibanda na mapango. Maana ni kuwa Dhul-qarnain alipowasili miji ya mashariki aliwakuta watu wanaishi kwenye nchi iliyo wazi ikifikiwa na jua, wakiishi maisha ya kiporini, kama wanyama.
Baadhi ya wafasiri wamesema kuwa nchi hiyo ilikuwa ufuoni mwa Afrika mashariki, Mwenyezi Mungu (s.w.t) hakutaja alichofanya Dhul-qarnain huko; kuwa je alimfanyia wema mwenye kuamini na aka- tenda mema na kumwadhibu mwenye kunga’ang’ania ukafiri na inadi au aliwaacha kama walivyo? Mwenyezi Mungu ni mjuzi zaidi.
Kama hivyo tulizijua vizuri habari zake.
Yaani hii ndiyo habari ya Dhul-qarnain, tunaijua yote.
2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
حَتَّىٰ إِذَا بَلَغَ بَيْنَ السَّدَّيْنِ وَجَدَ مِن دُونِهِمَا قَوْمًا لَّا يَكَادُونَ يَفْقَهُونَ قَوْلًا ﴿٩٣﴾
93. Hata alipofikia baina ya milima miwili, alikuta nyuma yake watu ambao takriban hawakuwa wakifahamu kauli.
قَالُوا يَا ذَا الْقَرْنَيْنِ إِنَّ يَأْجُوجَ وَمَأْجُوجَ مُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ فَهَلْ نَجْعَلُ لَكَ خَرْجًا عَلَىٰ أَن تَجْعَلَ بَيْنَنَا وَبَيْنَهُمْ سَدًّا ﴿٩٤﴾
94. Wakasema: Ewe Dhul-qar-nain! Hakika Juju na Majuju wanafanya ufisadi katika nchi. Basi je, tukulipe ujira ili utujengee baina yetu na wao ngome?
قَالَ مَا مَكَّنِّي فِيهِ رَبِّي خَيْرٌ فَأَعِينُونِي بِقُوَّةٍ أَجْعَلْ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُمْ رَدْمًا ﴿٩٥﴾
95. Akasema: Yale Mola wangu aliyoniwezesha ni bora. Lakini nisaidieni kwa nguvu nijenge kizuizi baina yenu na wao.
آتُونِي زُبَرَ الْحَدِيدِ حَتَّىٰ إِذَا سَاوَىٰ بَيْنَ الصَّدَفَيْنِ قَالَ انفُخُوا حَتَّىٰ إِذَا جَعَلَهُ نَارًا قَالَ آتُونِي أُفْرِغْ عَلَيْهِ قِطْرًا ﴿٩٦﴾
96. Nileteeni vipande vya chuma, Hata alipojaza baina ya nafasi iliyo kati ya milima miwili, akasema: Vuvieni. Hata alipokifanya moto akasema: Nileteeni shaba iliyoyeyuka niimwagie.
فَمَا اسْطَاعُوا أَن يَظْهَرُوهُ وَمَا اسْتَطَاعُوا لَهُ نَقْبًا ﴿٩٧﴾
97. Hawakuweza kuukwea wala hawakuweza kuutoboa.
قَالَ هَـٰذَا رَحْمَةٌ مِّن رَّبِّي فَإِذَا جَاءَ وَعْدُ رَبِّي جَعَلَهُ دَكَّاءَ وَكَانَ وَعْدُ رَبِّي حَقًّا ﴿٩٨﴾
98. Akasema: Hii ni rehema itokayo kwa Mola wangu, Itakapofika ahadi ya Mola wangu atauvunja vunja. Na ahadi ya Mola wangu ni ya kweli.
وَتَرَكْنَا بَعْضَهُمْ يَوْمَئِذٍ يَمُوجُ فِي بَعْضٍ وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَجَمَعْنَاهُمْ جَمْعًا ﴿٩٩﴾
99. Na siku hiyo tutawaacha wakisongana. Na parapanda itapuziwa na wote watakusanywa pamoja.
وَعَرَضْنَا جَهَنَّمَ يَوْمَئِذٍ لِّلْكَافِرِينَ عَرْضًا ﴿١٠٠﴾
100. Na siku hiyo tutawaonyesha wazi makafiri Jahannam waione.
Aya 93 – 100
Kisha akafuata sababu.
Dhul-qarnaini alirejea mji wa tatu ulioko katika Bahari nyeusi, unaokaliwa na Slaves[2] -kama ilivyosemekana - ambao Mwenyezi Mungu ameuashiria kwa kauli yake:
Hata alipofikia baina ya milima miwili, alikuta nyuma yake watu ambao takriban hawakuwa wakifahamu kauli.
Watu aliowakuta huko walikuwa hawafahamu lugha yake wala hakufaamu lugha yao, lakini walielewana kwa ishara au kwa mkalimani; kama anavyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Wakasema: “Ewe Dhul-qar-nain! Hakika Juju na Majuju wanafanya ufisadi katika nchi. Basi je, tukulipe ujira ili utujengee baina yetu na wao ngome?
Sheikh Maraghi anasema katika Tafsir yake: “Juju ni wa Tatars, na Majuju ni wa Mongoli. Asili yao wanatokana na baba mmoja anayeitwa Turk. Miji yao inaanzia Tibet na China hadi kwenye Bahri iliyoganda. Miongoni mwao ni Changez Khan na Halako.
Kisha akanukuu Maraghi Jarida la Al-Muqtatif la mwaka 1888, kwamba jengo la ukuta wa Dhul-qarnain liko nyuma ya Amou–Daria sehemu za Balkh. Jina lake hivi sasa ni mlango wa chuma na liko karibu na mji wa Tirmidh.
Mtaalamu mmoja wa kijerumani Cyllid Burger, amelitaja katika safari zake zilizokuwa mwanzoni mwa karne ya 15. Vilevile amelitaja mwana historia wa Kihispania Clavijo katika safari zake za mwaka 1402 A.D.
Vyovyote iwavyo ni kwamba watu walimtaka Dhul-qarnain awajengee ngome itakayowakinga na Juju na Majuju waliokuwa wakiishambulia nchi yao, wakiwapa adhabu mbaya ya kuwaua, kuwateka na kupora. Wakajiwekea sharti la kumlipa katika mali zao ikiwa atawajenega ngome.
Akasema: Yale Mola wangu aliyoniwezesha na akanipa utawala na malini bora kuliko yale aliyowapa Mwenyezi Mungu. Nyinyi wenyewe mna haja kubwa ya mali yenu, basi itumieni kwenye masilahi yenu.
Lakini nisaidieni kwa nguvu nijenge kizuizi baina yenu na wao.
Makusudio ya nguvu hapa ni wafanyikazi na vifaa vya ujenzi.
Nileteeni vipande vya chuma. Hata alipojaza baina ya nafasi iliyo kati ya milima miwili.
Yaani alipoletewa vyuma alivipanga mpaka vikajaza nafasi iliyo baina ya milima miwili, kisha wakamletea kuni akawasha moto akaweka mifuoakasema: Vuvieni. Hata alipokifanya (chuma)moto akasema: Nileteeni shaba iliyoyeyuka niimwagie.
Wakamletea, akamwagia kwenye vyuma vilivyo moto, vikashikana, ukawa mlima wa chuma.
Hawakuweza kuukwea hao Juju na Majuju, kutokana na urefu na kutelezawala hawakuweza kuutoboa kutokana na ugumu wake na maki yake.
Akasema: Hii ni rehema itokayo kwa Mola wangu.
Aliyesema ni Dhul-qarnain, akimshukuru Mola wake (s.w.t) kwa rehema na neema hii aliyoitimiza mikononi mwake, Hivi ndivyo anavyokuwa mumin mwenye ikhlasi. Anamnyenyekea Mwenyezi Mungu na kushukuru kila zinapokuwa neema za Mwenyezi Mungu kupitia kwake.
Kujengwa kwa ngome hii ni usadikisho wa mfano kuwa katika historia ya binadamu kulikuwa na kusaidiana baina ya mataifa makubwa na yale madogo yanayoendelea; baina ya taifa lililo na nyenzo za maendeleo na lile lisilokuwa nazo.
Nguvu za Amerika zinafanana sana na nguvu za Dhul-qarnaini, kwa vile haziwezi kukabiliwa na yoyote, lakini kuna tofauti kubwa ya matokeo na natija. Wakati nguvu zote za Dhul-qarnain zilkuwa ni utawala wa kheri ya ubinadamu na ufanisi wake, lakini nguvu za Amerika ni za kuhami uovu wa uzayuni na kutawala nyenzo zote, masoko yote kwa masilahi ya ukoloni na kuwadumaza watu kwa kila namna.
Ushahidi wa hayo hauna idadi. Kuanzia kuusaidia uzayuni dhidi ya waarabu na ubaguzi wa rangi ndani ya Amerika hadi Rhodesia,[3] mapinduzi ya kijeshi katika nchi za kiafrika[4] na kuwapiga vita wapigania ukombozi huko Kongo na kila mahali, Ama huko Vietnam ndio haisemeki. Wamekusanya majeshi na kutumia kila walicho nacho, lakini ukakamavu wa wananchi wa Vietnam umetoa somo kwa Amerika, ambalo hawatalisahau maisha.
Kwa hiyo kila ushindi wanaoupata Amerika wajue huo ni wa muda tu, utaondoka kwa upinzani wa wananchi ambao unazidi siku baada ya siku.
Itakapofika ahadi ya Mola wangu atauvunja vunja.
Yaani huo mlima atauvunja vunja, Maana ni kuwa utakapokurubia wakati wa kutokea Juju na Mjuju nyuma ya ukuta, Mwenyezi Mungu ataleta sababu za kuvunjika kwake.
Na ahadi ya Mola wangu ni kweli haina shaka.
Shekh Maraghi anasema: “Ahadi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu ilifika kwa kutoka Changez Khan wakafanya ufisadi katika ardhi”.
Katika Tafsir Ar-Razi imeelezwa kuwa maana ya ahadi hapa ni siku ya Kiyama. Katika Tafsir At-Twabariy imeelezwa ni baada ya kuuliwa Dajjal.
Ama sisi tunapondokea kwenye kauli ya Maraghi, kwa sababu iko karibu na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Na siku hiyo tutawaacha wakisongana wao kwa wao.
Kwani tunafahamu kuwa Juju na Majuju wataenea katika ardhi baada ya kuharibika ngome na wataharibu maisha ya watu. Mwenyezi Mungu anasema:
حَتَّىٰ إِذَا فُتِحَتْ يَأْجُوجُ وَمَأْجُوجُ وَهُم مِّن كُلِّ حَدَبٍ يَنسِلُونَ ﴿٩٦﴾
“Mpaka watakapofunguliwa Juju na Majuju wakawa wanateremka kutoka kila mlima.” (21:96).
Zaidi ya hayo ni kwamba lau ingelikuwa makusudio ya ahadi yake ni Kiyama au baada ya kufa Dajjal, ingelikuwa ngome bado ipo; na kama ipo basi ingelionekana, hasa kwa kuzingatia kuwa elimu imefanya dunia hivi sasa, pamoja na wakazi wake, ni kama familia moja inayoishi kwenye nyumba moja.
Na parapanda itapuziwa na wote watakusanywa pamoja.
Hii ndiyo siku ya mwisho kwa wale wa mwanzo na wa mwisho. Katika Tafsir Attwabariy imeelezwa kuwa Mtume(s.a.w.w) aliulizwa kuhusu Parapanda, akasema ni pembe itakayopuziwa.
Baada ya hayo yote, tunapenda kujulisha kuwa tuliyoyaeleza au kuyanukuu kutoka kwa wengine kuhusiana na Juju na Majuju, ni kwa njia ya kuleta karibu ufahamisho sio uhakika hasa.
Kwa vile hatukupata rejea za kutegemewa; Kwa sababu hiyo basi tutuatosheka na dhahiri ya Qur’an Tukufu na kuwaachia ufafanuzi wenzetu wengine.
الَّذِينَ كَانَتْ أَعْيُنُهُمْ فِي غِطَاءٍ عَن ذِكْرِي وَكَانُوا لَا يَسْتَطِيعُونَ سَمْعًا ﴿١٠١﴾
101. Wale ambao macho yao yalikuwa kwenye pazia ya kunitaja, Na wakawa hawawezi kusikia.
أَفَحَسِبَ الَّذِينَ كَفَرُوا أَن يَتَّخِذُوا عِبَادِي مِن دُونِي أَوْلِيَاءَ إِنَّا أَعْتَدْنَا جَهَنَّمَ لِلْكَافِرِينَ نُزُلًا ﴿١٠٢﴾
102. Je, wanadhani waliokufuru kuwafanya waja wangu ndio walinzi badala yangu? Hakika sisi tumeiandaa Jahannamu iwe ni mashukio ya makafiri.
قُلْ هَلْ نُنَبِّئُكُم بِالْأَخْسَرِينَ أَعْمَالًا ﴿١٠٣﴾
103. Sema: je, tuwaambie wale wenye hasara mno ya vitendo?
الَّذِينَ ضَلَّ سَعْيُهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَهُمْ يَحْسَبُونَ أَنَّهُمْ يُحْسِنُونَ صُنْعًا ﴿١٠٤﴾
104. Ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kuwa wanafanya kazi nzuri?
أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ وَلِقَائِهِ فَحَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فَلَا نُقِيمُ لَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَزْنًا ﴿١٠٥﴾
105. Hao ndio ambao wamezikanusha ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana naye; Kwa hiyo vitendo vyao vimepomoka; nawala siku ya Kiyama hatutawapa uzito wowote.
ذَٰلِكَ جَزَاؤُهُمْ جَهَنَّمُ بِمَا كَفَرُوا وَاتَّخَذُوا آيَاتِي وَرُسُلِي هُزُوًا ﴿١٠٦﴾
106. Hiyo Jahanamu ndiyo malipo yao kwa walivyokufuru na wakazifanyia kejeli ishara zangu na Mitume wangu.
Aya 101 – 106
Na siku hiyo tutawaonyesha wazi Jahannam makafiri waione.
Wenye makosa, kesho, watashuhudia kwa macho yao Jahannam kabla ya kuingizwa humo, ili wachomeke kwa aina mbili za moto: Moto wa hofu na moto wa kuungua.
Wale ambao macho yao yalikuwa kwenye pazia ya kunitaja.
Kutajwa huwa kunasikiwa na masikio. Kwa hiyo hapa maana ya pazia ya macho ni mfundo wa makafiri kwa Mtume na waumini, na kwamba wao walikuwa hawawezi kumwangalia Mtume(s.a.w.w) wala waumini.
Na wakawa hawawezi kusikia utajo wa Mungu kutoka kwa Mtume wake Mtukufu.
Kwa maneno mengine ni kuwa wakosefu hawawezi kusikiza haki wala kuwatazama watu wa haki. Haya ndiyo tunayoyashuhudia kwa macho, ikiwa ni matokeo ya mzozo baina ya haki na batili na kheri na shari.
Je wanadhani waliokufuru kuwafanya waja wangu ndio walinzi badala yangu?
Makusudio ya waja wangu hapa ni viumbe ambao washirikina wali- wafanya ndio walinzi wao badala ya Mwenyezi Mungu. Hapa kuna maneno yanayokadiriwa kuwa: Je, wana dhani hawa kuwa tumeghafilika nao?Hapana! Hakika sisi tumeiandaa Jahannamu iwe ni mashukio ya makafiri.
Mashukio ni mahali anapoandaliwa mgeni, vile vile linatumika neno hilo kwa maana ya nyumba. Maana ni kuwa tumewaandalia Jahannam kuwa ndio tosha yao. Hii ni sawa na kumwambia yule unayemdharau: unadhani mimi sikuwezi wewe nawe ni kama hiki kiatu?
Sema je, tuwaambie wale wenye hasara mno ya vitendo? Ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure, nao wanadhani kuwa wanafanya kazi nzuri?
Ufupi wa maana ni kuwa mwenye hasara zaidi katika watu na mwenye kuhangaika bure, ni yule mjinga sana anayeuona ujinga wake kuwa ni elimu, shari yake kuwa ni kheri na uovu wake kuwa ni wema.
Hapana mwenye shaka kuwa huyo ni mwenye hasara duniani, kwa vile yeye anaishi asivyokuwa. Vile vile huko akhera, kwa vile atakutana na Mola wake akiwa na ujinga, ghururi na matendo maovu. Aya inaashiria kuwa thamani ya mtu haiwezi kupimwa kwa kuiona yeye mwenyewe; Kwa sababu mgomvi hawezi kujihukumu. Wala pia haiwezi kupimwa kwa mtazamo wa watu.
Ispokuwa mtu hupimwa kwa kipimo cha Qur’an na misingi yake na kushikamana na mafunzo yake na hukumu zake. Hupimwa kwa ukweli na uadilifu, kuinusuru haki na watu wake na kujitolea kwa hali na mali. Qur’an imejaa aina nyingi za mafunzo haya; kama vile kauli zake Mwenyezi Mungu Mtukufu zifuatazo: “...Na kuweni pamoja na wa kweli” Juz; 11 (9:119)
قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ ﴿١٣٥﴾
“....Kuweni Imara kwa uadilifu” Juz;. 5 (4:135)
كُونُوا أَنصَارَ اللَّـهِ ﴿١٤﴾
“...Kuweni wasaidizi wa Mwenyezi Mungu (61:14)
كُونُوا رَبَّانِيِّينَ ﴿٧٩﴾
“...Kuweni watumishi wa Mwenyezi Mungu”Juz.3 (3:79)
وَجَاهِدُوا بِأَمْوَالِكُمْ وَأَنفُسِكُمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٤١﴾
“...Na mpiganie jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali zenu na nafsi zenu Juz.10 (9:41)
إِنَّ أَكْرَمَكُمْ عِندَ اللَّـهِ أَتْقَاكُمْ ﴿١٣﴾
“Hakika mtukufu wenu zaidi, kwa Mwenyezi Mungu, ni yule mwenye takua zaidi katika nyinyi” (49:13)
Unaweza kuuliza : Mkosaji anaweza kujiona kuwa amepatia na kwamba amefanya vizuri. Je atakuwa ni miongoni mwa waliohasirika; pamoja na kujua kuwa hakuna mwenye isma (kuhifadhiwa na madhambi) isipokuwa yule mwenye isma?
Jibu : Wenye kukosea wako aina mbili: Wa kwanza ni yule mwenye kukosea baada ya kutafiti na kuhakikisha; sawa na wanavyofanya wale wanaojitahidi, kiasi ambacho natija inayopatikana inaweza kuwa sawa na ya mtaalmu.
Hapana mwenye shaka kuwa mkoseaji huyu hawezi kuwa ni katika wale ambao juhudi zao zimepotea bure, au kuwa ni aibu ukoseaji wake; bali huyu analipwa thawabu kutokana na juhudi yake; kama ilivyoelezwa katika Hadith. Lakini kwa sharti awe na nia ya kujikosoa, yatakapofichuka makosa.
Aina ya pili, ni kukosea kulikotokana na kujiamini kwa juujuu, kulikotokana na mawazo, bila ya kufanya utafiti, kwa vile hajui misingi ya utafiti na elimu, Au anaweza kuwa anaijua, lakini asiitumie au aitumie nusunusu, aitumie kabla ya kuikamilisha. Huyu ndiye aliye miongoni mwa wale waliopata hasara katika kazi zao, hilo halina shaka. Kwa sababu Mwenyezi Mungu ameamrisha kuwa na mazingatio na uthabiti na akakataza pupa na kusema bila ya ujuzi.
Baada ya hayo somo tunalolipata kutokana na Aya hii, ni kuwa tusijidanganye, tukajipa sifa tusizo nazo wala kujidanganya kwa maneno.
Vile vile ni wajibu tujihisabu nafsi zetu zinapokuwa na ghururi na kujitukuza, kabla hajatuhisabu Mwenyezi Mungu na watu. Pia rai zetu na kauli zetu tusizione kuwa ndio sawa mia kwa mia. Makosa yanatokea kwa yeyote.
Hao ndio ambao wamezikanusha ishara za Mwenyezi Mungu na kukutana naye.
Mfumo wa maneno unafahamisha kuwa makusudio ya wale waliokanusha ishara za Mola wao na kukutana naye ndio wale ambao juhudi yao katika maisha ya dunia imepotea bure; ni sawa wawe wameamini ufufuo au wameukanusha. Linalozingatiwa ni imani na matendo kwa pamoja; sio imani peke yake.
Kwa hiyo vitendo vyao vimepomoka na wala siku ya kiyama hatutawapa uzito wowote.
Yaani hatutawathamini, kwa sababu hakuna heshima mbele ya Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa yule mwenye takua.
Hiyo Jahanamu ndiyo malipo yao kwa walivyokufuru na wakazifanyia kejeli ishara zangu na Mitume wangu.
Walimkufuru Mwenyezi Mungu na wakaifanyia masikhara haki na watu wake. Moto ndio mwisho na ukomo wa ufisadi na upotevu.
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ كَانَتْ لَهُمْ جَنَّاتُ الْفِرْدَوْسِ نُزُلًا ﴿١٠٧﴾
107. Hakika wale ambao wameamini wakatenda mema, mashukio yao yatakuwa kwenye Pepo za Firdausi.
خَالِدِينَ فِيهَا لَا يَبْغُونَ عَنْهَا حِوَلًا ﴿١٠٨﴾
108. watadumu humo; hawatataka kuondoka.
قُل لَّوْ كَانَ الْبَحْرُ مِدَادًا لِّكَلِمَاتِ رَبِّي لَنَفِدَ الْبَحْرُ قَبْلَ أَن تَنفَدَ كَلِمَاتُ رَبِّي وَلَوْ جِئْنَا بِمِثْلِهِ مَدَدًا ﴿١٠٩﴾
109. Sema: Lau bahari ingelikuwa ndio wino kwa maneno ya Mola wangu, basi bahari ingemalizika kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu, hata tungeleta mfano wake kuongezea.
قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَىٰ إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَـٰهُكُمْ إِلَـٰهٌ وَاحِدٌ فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاءَ رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا ﴿١١٠﴾
110. Sema: hakika mimi ni binadamu kama nyinyi tu, nimeletewa wahyi kwamba Mungu wenu ni Mungu mmoja. Mwenye kutarajia kukutana na Mola wake, basi na atende matendo mema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake.
Aya 108 – 110
Hakika wale ambao wameamini wakatenda mema, mashukio yao yatakuwa kwenye Pepo za Firdausi.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwahidi makafiri moto, sasa anatoa ahadi ya Pepo kwa waumini. Firdausi ni katika Pepo ya daraja ya juu. Mtume Mtukufu(s.a.w.w) amesema: “Mkimuomba Mwenyezi Mungu muombeni Firdausi.”
Watadumu humo; hawatataka kuondoka.
Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawalipa wema yale ambayo hawatataka mengine, tosha kabisa! Yanatosheleza yote wanayoyataka. Aya inaashiria kuwa hakuna tamaa huko Akhera; vinginevyo ingelikuwa hakuna kutosheka. Kwani mwenye tamaa hatosheki.
Sema: Lau bahari ingelikuwa ndio wino kwa maneno ya Mola wangu, basi bahari ingemalizika kabla ya kumalizika maneno ya Mola wangu, hata tungeleta mfano wake kuongezea.
Bahari ni jina la jinsi, linaenea kwenye bahari zote. Makusudio ya kabla ya kumalizika maneno, ni kuwa hayamaliziki na mfano wake ni mfano wa bahari. Maana ni kuwa lau tuchukulie kuwa bahari zote ni wino wa kuandika maneno ya Mwenyezi Mungu zisingetosha na maneno ya Mwenyezi Mungu yangelibakia bila ya kikomo.
Aya nyingine yenye maana hii ni kauli yake Mwenyezi Mungu: “Na lau miti yote iliyomo ardhini ikawa ni kalamu na bahari (ikawa wino) na ikaongezewa bahari nyingine saba, maneno ya Mwenyezi Mungu yasingelimalizika.” (31:27).
Makusudio ya maneno ya Mwenyezi Mungu hapa sio matamshi yanayotokana na herufi wala si amri ya kitendo inayotokana na ibara ya ‘kuwa na kikawa,’ kwa sababu amri hii haiingii kwenye mahisabu: “Na amri haikuwa ila ni moja tu, kama kupepesa jicho.” (54:51).
Isipokuwa makusudio ya maneno yake hapa, ni kuweza kuvileta vitu vyote, wakati wowote atakao; ni sawa iwe ni kwa kuviambia kuwa na vikawa au aviambie muda ujao, wa karibu au mbali. Uwezo huu hauna kikomo wala mwisho, lakini bahari, miti na mifano yake ina kikomo; na kila chenye kikomo kinakwisha.
Kwa maneno mengine ni kuwa kila kitu kilichopo kitakwisha na kukoma, isipokuwa uwezo wa Mwenyezi Mungu wa kukifanya hicho kitu utabakia.
Tutaifafanua zaidi fikra hii kwa mfano huu: Mtu akiwa na maarifa ya kilimo, maarifa yake haya atakuwa nayo tu wakati wote atakaokuwa hai, lakini kile atakochokilima kitaisha. Uweza wa Mwenyezi Mungu (s.w.t) hauishi kwa vile hauna kikomo ni wa milele, lakini viumbe vyake vimepatikana na kila chenye kupatikana kina mwisho.
Sema: Hakika mimi ni binadamu kama nyinyi tu, sina tofauti na nyinyi isipokuwanimeletewa wahyi kwamba Mungu wenu ni Mungu mmoja.
Ibn Abbas anasema: “Mwenyezi Mungu, kwa Aya hii, amemfundisha Mtume wake unyenyekevu, akamwamrisha aseme yeye mwenyewe kuwa ni binadamu kama wengine, isipokuwa Mwenyezi Mungu amemtukuza kwa wahyi.”
Nasi tunaongezea kauli ya Ibn Abbas: Na ili waislamu wasimfanye Muhammad(s.a.w.w) kama wanaswara (wakristo) walivyomfanya Isa(a.s) .
Mwenye kutarajia kukutana na Mola wake, kwa hisabu, thawabu na adhabu,basi na atende matendo mema, wala asimshirikishe yeyote katika ibada ya Mola wake.
Kila mwenye kufanya amali kwa ajili ya mwengine atakuwa amemshirikisha Mwenyezi Mungu kwenye ibada; ni sawa aseme waungu ni wengi au asiseme.
Tofauti ni kuwa kauli ni shirki ya waziwazi na riya ni shirki ya kificho. Kuna Hadith inayosema:
“Mwenye kuswali kwa riya amefanya shirki na mwenye kufunga kwa riya amefanya shirk”
Fananisha mengine kwenye swala na saumu.
3
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
Sura ya Kumi na Tisa: Surat Maryam. Imeshuka Makka ina Aya 98.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye Kurehemu.
كهيعص ﴿١﴾
1. Kaaf Haa Yaa A’yn Swaad.
ذِكْرُ رَحْمَتِ رَبِّكَ عَبْدَهُ زَكَرِيَّا ﴿٢﴾
2. Huu ni ukumbusho wa rehema ya Mola wako kwa mja wake Zakariya.
إِذْ نَادَىٰ رَبَّهُ نِدَاءً خَفِيًّا ﴿٣﴾
3. Alipomuomba Mola wake kwa siri.
قَالَ رَبِّ إِنِّي وَهَنَ الْعَظْمُ مِنِّي وَاشْتَعَلَ الرَّأْسُ شَيْبًا وَلَمْ أَكُن بِدُعَائِكَ رَبِّ شَقِيًّا ﴿٤﴾
4. Akasema: Mola wangu! Mfupa wangu umedhoofika, na kichwa kiname remeta kwa mvi. Mola wangu! Sikuwa mwenye bahati mbaya kwa kukuomba wewe.
وَإِنِّي خِفْتُ الْمَوَالِيَ مِن وَرَائِي وَكَانَتِ امْرَأَتِي عَاقِرًا فَهَبْ لِي مِن لَّدُنكَ وَلِيًّا ﴿٥﴾
5. Na Mimi nahofia jamaa zangu baada yangu na mke wangu ni tasa, Basi nipe mrithi kutoka kwako.
يَرِثُنِي وَيَرِثُ مِنْ آلِ يَعْقُوبَ وَاجْعَلْهُ رَبِّ رَضِيًّا ﴿٦﴾
6. Atakayenirithi mimi na arithi ukoo wa Ya’qub, Ewe Mola wangu mjaaliye mwenye kuridhisha.
Aya 1-6
Kaaf Haa Yaa A’yn Swaad.
Umetangulia mfano wake pamoja na tafsiri katika Juz. 1, mwanzo wa Sura Baqara
Huu ni ukumbusho wa rehema ya Mola wako kwa mja wake Zakariya.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamsimulia Mtume wake mtukufu, katika Aya hizi, jinsi alivyompa rehema Zakariya na akamneemesha kwa mtoto wake Yahya. Zakariya anatokana na kizazi cha Suleiman bin Daud. Alimuoa khalat (mama mdogo) wa Maryam. Naye alikuwa ni mlezi wa Maryam, Yametangulia maelezo ya hayo katika Juz; 3 (3:38), Inasemekana kuwa Zakriya alikuwa seremala.
Alipomuomba Mola wake kwa siri Alimuomba Mola wake akiwa peke yake na akasema: Mola wangu! Mfupa wangu umedhoofika, na kichwa kinameremeta kwa mvi. Mola wangu! Sikuwa mwenye bahati mbaya kwa kukuomba wewe.
Zakariya alizeeka bila ya kuwa na mtoto, kwa hiyo akamnyenyekea Mola wake, akimshtakia udhaifu wake na uzee wake. Miongoni mwa aliyoyasema ni: “Mola wangu usiniache peke yangu na Wewe ndiye mbora wa wanaorithi” (21:89). Ninakuomba ewe Mola wangu, nikiwa na matarajio ya rehema yako bila ya kukata tamaa. Vipi nikate tamaa na hali hujawahi kuyaangusha matarajio yangu kwako.
Na mimi nahofia jamaa zangu baada yangu na mke wangu ni tasa. Basi nipe mrithi kutoka kwako atakayenirithi mimi na arithi ukoo wa Ya’qub, Ewe Mola wangu mjaaliye mwenye kuridhisha.
Neno la kiarabu ‘mawalii’ lililofasiriwa jamaa, lina maana ya ndugu wa upande wa baba. Kwa hiyo Zakariya akiwa mzee na mkewe akiwa tasa, alihofia kurithiwa na binamu zake ambao ni wana wa Israil. Inasemekena walikuwa ni waovu.
Na hilo si mbali kwa Waisrail, kuwa wakirithi watawafanyia uovu watu na kuwafanyia ufisadi kwenye dini yao na dunia yao. Pamoja na uzee wake Zakariya na utasa wa mke wake, bado alikuwa na mategemeo makubwa kwa muumba wake, ndio maana akamuomba amtimizie haja yake.
يَا زَكَرِيَّا إِنَّا نُبَشِّرُكَ بِغُلَامٍ اسْمُهُ يَحْيَىٰ لَمْ نَجْعَل لَّهُ مِن قَبْلُ سَمِيًّا ﴿٧﴾
7. Ewe Zakariya! Hakika sisi tunakubashiria mwana, jina lake ni Yahya, hatujapata kumpa jina hilo yeyote kabla yake.
قَالَ رَبِّ أَنَّىٰ يَكُونُ لِي غُلَامٌ وَكَانَتِ امْرَأَتِي عَاقِرًا وَقَدْ بَلَغْتُ مِنَ الْكِبَرِ عِتِيًّا ﴿٨﴾
8. Akasema: Ewe Mola wangu! Vipi nitakuwa na mwana na hali mke wangu ni tasa, na mimi nimekwishafikia ukongwe katika uzee?
قَالَ كَذَٰلِكَ قَالَ رَبُّكَ هُوَ عَلَيَّ هَيِّنٌ وَقَدْ خَلَقْتُكَ مِن قَبْلُ وَلَمْ تَكُ شَيْئًا ﴿٩﴾
9. Akasema, ndio hivyo hivyo Mola wako amesema, haya kwangu ni mepesi. Na hakika nilikuumba wewe zamani na hukuwa kitu.
قَالَ رَبِّ اجْعَل لِّي آيَةً قَالَ آيَتُكَ أَلَّا تُكَلِّمَ النَّاسَ ثَلَاثَ لَيَالٍ سَوِيًّا ﴿١٠﴾
10. Akasema: Mola wangu nijaalie ishara. Akasema, ishara yako ni kuwa hutasema na watu kwa masiku matatu, na hali ni mzima.
فَخَرَجَ عَلَىٰ قَوْمِهِ مِنَ الْمِحْرَابِ فَأَوْحَىٰ إِلَيْهِمْ أَن سَبِّحُوا بُكْرَةً وَعَشِيًّا ﴿١١﴾
11. Akawatokea watu wake kutoka mihirabuni, akawaashiria kuwa mumsabihi asubuhi na jioni.
Aya 7 – 11
Ewe Zakariya! Hakika sisi tunakubashiria mwana, jina lake ni Yahya, hatujapata kumpa jina hilo yeyote kabla yake.
Mwenyezi Mungu aliitikia dua ya Zakariya na akampa habari njema ya kuzaliwa mtoto wa kiume, na kwamba Mwenyezi Mungu amemuita Yahya akiwa bado yuko kwenye uti wa mgongo wa baba yake. Na hakuna aliyewahi kuitwa jina hilo kabla yake. Inasemekana Yahya ndiye Yohana amabye ni maarufu kwa wakiristo kwa jina la Yohana mbatizaji).
Akasema: “Ewe Mola wangu! Vipi nitakuwa na mwana na hali mke wangu ni tasa, na mimi nimekwishafikia ukongwe katika uzee?
Kusema hivi sio kuona kuwa haiwezekani, bali ni kuadhimisha na kushukuru neema za Mwenyezi Mungu na uweza wake ambao umekiuka desturi na mazoweya. Yeye ni mzee na mkewe ni tasa tena ni mzee, lakini pamoja na yote hayo Mwenyezi Mungu amemneemesha kupata mtoto.
Akasema: ndio hivyo hivyo Mola wako amesema, haya kwangu ni mepesi. Na hakika nilikuumba wewe zamani na hukuwa kitu.
Anayesema kauli zote mbili ni mmoja, naye ni Mwenyezi Mungu. yaani Mwenyezi Mungu anamwambia Zakariya kuwa Mola wako amesema. Desturi hii wanaitumia watungaji wengi wa kiislamu.
Mtu anaweza kusema: “Amesema Muhammad yeye ni Bin Malik” akijikusudia yeye Mwenyewe. Mfano mwingine ni wa Tabariy akijizungumzia yeye mwenyewe: “Amesema Abu Jafar Muhammad bin Jarir At-Tabariy”
Aliposema Mwenyezi Mungu haya kwangu ni mepesi, ni kuwa kwa Mungu hakuna kitu chochote kilicho kigumu. Vitu vyote kwake ni sawa tu; hahitajii isipokuwa neno ‘Kuwa’
Akasema: Mola wangu nijaalie ishara. Akasema, ishara yako ni kuwa hutasema na watu kwa masiku matatu, na hali ni mzima. Akawatokea watu wake kutoka mihirabuni, akawaashiria kuwa mumsabihi asub- uhi na jioni.
Makusudio ya kuwaashiria ni kuwaashiria kwa mkono wake au kwa maandishi, kwa sababu yeye amezuiliwa kuzungumza, Umetangulia ufafanuzi wake katika Juz; 3 (3:41).
يَا يَحْيَىٰ خُذِ الْكِتَابَ بِقُوَّةٍ وَآتَيْنَاهُ الْحُكْمَ صَبِيًّا ﴿١٢﴾
12. Ewe Yahya! Kishike kitabu kwa nguvu, Na tulimpa hukumu angali mtoto.
وَحَنَانًا مِّن لَّدُنَّا وَزَكَاةً وَكَانَ تَقِيًّا ﴿١٣﴾
13. Na tukampa huruma itokayo kwetu na utakaso na alikuwa ni mwenye takua.
وَبَرًّا بِوَالِدَيْهِ وَلَمْ يَكُن جَبَّارًا عَصِيًّا ﴿١٤﴾
14. Na mwema kwa wazazi wake wala hakuwa jeuri muasi.
وَسَلَامٌ عَلَيْهِ يَوْمَ وُلِدَ وَيَوْمَ يَمُوتُ وَيَوْمَ يُبْعَثُ حَيًّا ﴿١٥﴾
15. Na amani iwe juu yake, siku alipozaliwa na siku atakapokufa na siku atakapofufuliwa.
AYA 12 – 15
Ewe Yahya!
Kauli hii inaelezea moja kwa moja kuwa Yahya amekwishazaliwa, amekuwa na akili ya kufahamu na kutia maanani na ana uwezo wa kutumia Tawrat ambayo ndiyo aliyoikusudia Mwenyezi Mungu aliposema:
Kishike kitabu kwa nguvu.
Maana ya kukishika kwa nguvu ni kukitumia kwa bidii na ikhlasi. Kisha akamsifu Yahya kwa sifa zifuatazo:
Na tulimpa hukumu angali mtoto na tukampa huruma itokayo kwetu na utakaso na alikuwa ni mwenye takua na mwema kwa wazazi wake wala hakuwa jeuri muasi.
Makusudio ya kupewa hukumu udogoni ni kujua dini mapema udogoni. Hii ni neema Mwenyezi Mungu aliyomhusisha nayo Yahya; kama alivyomhusisha kwa kuzaliwa na wazazi wazee. Mwenyezi Mungu humhusisha kwa rehema yake amtakaye. Baadhi ya riwaya zinasema kuwa siku moja watoto walimwambia Yahya: “Twendeni tukacheze.” Yahya akasema: “Hatukuumbwa kwa ajili ya kucheza, twendeni tukaswali.”
Makusudio ya upole ni upole kwa waja. Utakaso ni utwahara na utakatifu. Takua ni kumtii Mwenyezi Mungu. Kuwatendea wema wazazi wawili ni kinyume cha kuwaudhi.
Kauli yake Mwenyezi Mungu:Wala hakuwa ni jeuri muasi ni kuunganisha kwa kufafanua. Kwa sababu Mwenye utakaso na takua hawezi kuwa jeuri muasi.
Na amani iwe juu yake, siku alipozaliwa na siku atakapokufa na siku atakapofufuliwa
Hili ni fumbo la kuwa Yahya ni Mwenye kuridhiwa mbele ya Mwenyezi Mungu duniani na Akhera. Ilivyo ni kuwa kumridhia kwake Yahya (a.s.) ni matokeo ya sifa alizomsifu nazo Mwenyezi Mungu.
Unaweza kuuliza : Kwanini Mwenyezi Mungu amemuhusisha Yahya na sifa hizi tele akiwa bado angali mdogo?
Jibu : Hakika Mwenyezi Mungu ana mambo yake kwa viumbe vyake. Anaweza akampa fadhila mdogo na akamnyima mkubwa. Na kila kutoa kwake na kuzuia kwake kuna hekima ambayo akili inaweza kujua na isiweze kujua. Lakini akili huwa inajaribu; kama ifuatavyo:
Sio mbali kuwa makusudio ya kusifika Yahya na sifa hizi katika rika hilo ni kutoa hoja kwa Wana wa Israil, watakapohitilafiana naye na wasikilize nasaha zake na mwito wake, Alimuumba Isa bila ya baba, “ili tumfanye kuwa ni ishara kwa watu na rehema itokayo kwetu” Itakuja Aya hii sehemu inayofuatia hii.
Pamoja na hoja hii ya kunyamazisha, lakini bado walimuasi Yahya na wakamfanyia uadui; mwisho wakamuua yeye na baba yake, si kwa lolote isipokuwa ni kwa kuwakataza mabaya. Hili si ajabu kwa yule aliyesema kuwa mikono ya Mwenyezi Mungu imefunga au Mungu ni fukara na sisi ni matajiri. Rudia Juz. 6 (5:64).
Katika kitabu Qasasul-anbiya (Visa vya mitume) imeelezwa kuwa Herod mfalme wa Palestina, wakati huo, alimpenda Herodias, binti wa kaka yake, kutokana na uzuri wake, na akataka kumuoa. Yahya alipopinga hilo
Herodias alichukia na akatoa sharti kwa ami yake kuwa mahari yake yawe kichwa cha Yahya. Kwa hiyo Mfalme akamchinja Yahya na akampelekea mpenzi wake zawadi hiyo ya kichwa.
Kuna riwaya mashuhuri iliyopokewa kutoka kwa Ali bin Husein bin Ali(a.s) kwamba baba yake, alipokuwa akielekea Iraq, alikuwa akimkumbuka sana Yahya na akisema: “Ni katika utwevu wa dunia kwa Mwenyezi Mungu, kwamba kichwa cha Yahya bin Zakariya kitolewe zawadi kwa kahaba miongoni mwa makahaba wa ki bani Israil.”
وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ مَرْيَمَ إِذِ انتَبَذَتْ مِنْ أَهْلِهَا مَكَانًا شَرْقِيًّا ﴿١٦﴾
16. Na mtaje Maryam katika Kitabu, alipojitenga na watu wake mahali upande wa mashariki.
فَاتَّخَذَتْ مِن دُونِهِمْ حِجَابًا فَأَرْسَلْنَا إِلَيْهَا رُوحَنَا فَتَمَثَّلَ لَهَا بَشَرًا سَوِيًّا ﴿١٧﴾
17. Na akaweka pazia kujikinganao, Tukampelekea roho wetu, Akajifananisha kwake sawa na mtu.
قَالَتْ إِنِّي أَعُوذُ بِالرَّحْمَـٰنِ مِنكَ إِن كُنتَ تَقِيًّا ﴿١٨﴾
18. Akasema: Hakika mimi najilinda kwa Mwingi wa rehema aniepushe nawe, ukiwa ni mwenye takua.
قَالَ إِنَّمَا أَنَا رَسُولُ رَبِّكِ لِأَهَبَ لَكِ غُلَامًا زَكِيًّا ﴿١٩﴾
19. Akasema: Mimi ni mjumbe wa Mola wako ili nikupe mwana mtakatifu.
قَالَتْ أَنَّىٰ يَكُونُ لِي غُلَامٌ وَلَمْ يَمْسَسْنِي بَشَرٌ وَلَمْ أَكُ بَغِيًّا ﴿٢٠﴾
20. Akasema: Nitakuwaje na mwana hali hajanigusa mtu yoyote wala mimi si malaya.”
قَالَ كَذَٰلِكِ قَالَ رَبُّكِ هُوَ عَلَيَّ هَيِّنٌ وَلِنَجْعَلَهُ آيَةً لِّلنَّاسِ وَرَحْمَةً مِّنَّا وَكَانَ أَمْرًا مَّقْضِيًّا ﴿٢١﴾
21. Akasema; Ndivyo hivyo hivyo, Mola wako amesema, haya kwangu ni mepesi! Na ili tumfanye kuwa ni ishara kwa watu na rehema itokayo kwa kwetu. Nahilo ni jambo lililokwishapitishwa.
Aya 16-21
Na mtaje Maryam katika Kitabu, alipojitenga na watu wake mahali upande wa mashariki, Na akaweka pazia kujikinga nao.
Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa Maryamu alijitenga na watu na akawa peke yake upande wa mashariki na kaweka sitara baina yake na wao, kiasi ambacho hawamuoni wala yeye hawaoni wao.
Kwa nini Maryamu alijitenga? Je, ni kwa kuwa aliona mambo yanayomchukiza au ni kwa kujitenga kwa ajili ya kufanya ibada au ni kwa ajili ya jambo jengine? Je, makusudio ya mahali upande wa mashariki ni kunakotokea jua au ni mashariki ya Baytul-maqdis au ni upande wa mashariki wa nyumba ya watu wake. Pia je, ni aina gani ya pazia aliyoweka, ni ukuta au kibanda?
Hakuna kitu, katika Aya, kinachoashiria majibu ya maswali haya; Kwa sababu hayahusiani na itikadi wala maisha. Sio mbali kuwa Mwenyezi Mungu alimpa ilhamu ya kujitenga huko ili apewe habari na Jibril kuhusu kuzaliwa Isa(a.s) akiwa kando na watu.
Tukampelekea roho wetu, akajifananisha kwake sawa na mtu
Makusudio ya roho wetu, ni Jibril. Alijifananisha na mtu kamili. Imeelezwa katika baadhi ya Tafsiri kwamba alikuja na umbo la mtu ili asimwogopeshe. Tafsiri nyingine inasema kuwa aliogopa na akafadhaika, kwa mshtukizo huu.
Mgeni ajitome ndani bila ya hodi na yeye yuko peke yake! Jambo la kushangaza, Kauli hii, ya pili, ina nguvu na usahihi zaidi ya ile nyingine, kwa dalili ya kuwa yeye alifazaika na akasema:
Hakika mimi najilinda kwa Mwingi wa rehema aniepushe nawe, ukiwa ni Mwenye takua.”
Yaani nataka hifadhi kwa Mwenyezi Mungu na shari yako ikiwa wewe unamwamini Yeye na hisabu yake na adhabu yake. Alimuhofisha na Mwenyezi Mungu, kwa sababu hakuwa na nyenzo nyingine yoyote ya kumzuia hapo alipo, isipokuwa hiyo. Vinginevyo yeye ana hifadhi ya Mwenyezi Mungu akiwa anamtegemea Yeye; ni sawa huyo anayemuhofisha ni mwenye takua au muovu.
Akasema: Mimi ni mjumbe wa Mola wako ili nikupe mwana mtakatifu.” Akasema: Nitakuwaje na mwana hali hajanigusa mtu yoyote wala mimi si malaya?
Unanipa habari ya mtoto, vipi na kutoka wapi? Sina mume wala sijafanya uasharati.
Akasema: Ndivyo hivyo hivyo Mola wako amesema, haya kwangu ni mepesi! Na ili tumfanye kuwa ni ishara kwa watu na rehema itokayo kwetu. Na hilo ni jambao lililokwishapitishwa.
Roho mwaminifu alimwambia kuwa sababu za kuzaa, kwa Mungu, sio kuonana na mtu tu. Kama ambavyo Mwenyezi Mungu anafanya vitu kwa sababu zake zilizozoeleka, vile vile anafanya vitu kwa neno ‘kuwa’ sawa na alivyofanya ulimwengu bila ya kitu chochote na Adamu bila ya baba wala mama.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) alitaka azaliwe mtoto kuonyesha dalili wazi ya ukuu wa muumba na utume wa atakayezaliwa, awe ni rehema kwa ubi- nadamu na hoja ya kunyamazisha wana wa Issrail ambao walijaribu kumuua. Tumeyaeleza hayo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 3 (3: 45)
فَحَمَلَتْهُ فَانتَبَذَتْ بِهِ مَكَانًا قَصِيًّا ﴿٢٢﴾
22. Basi akachukua mimba yake akaondoka nayo mahali mbali.
فَأَجَاءَهَا الْمَخَاضُ إِلَىٰ جِذْعِ النَّخْلَةِ قَالَتْ يَا لَيْتَنِي مِتُّ قَبْلَ هَـٰذَا وَكُنتُ نَسْيًا مَّنسِيًّا ﴿٢٣﴾
23. Uchungu ukampeleka kwenye shina la mtende; akasema: Laiti ningelikufa kabla ya haya nikawa mwenye kusahaulika kabisa.
فَنَادَاهَا مِن تَحْتِهَا أَلَّا تَحْزَنِي قَدْ جَعَلَ رَبُّكِ تَحْتَكِ سَرِيًّا ﴿٢٤﴾
24. Pakanadiwa kutoka chini yake kwamba usihuzunike; hakika Mola wako amejaalia chini yako kijito cha maji.
وَهُزِّي إِلَيْكِ بِجِذْعِ النَّخْلَةِ تُسَاقِطْ عَلَيْكِ رُطَبًا جَنِيًّا ﴿٢٥﴾
25. Na litikise kwako shina la mtende utakuangushia tende freshi zilizo mbivu.
فَكُلِي وَاشْرَبِي وَقَرِّي عَيْنًا فَإِمَّا تَرَيِنَّ مِنَ الْبَشَرِ أَحَدًا فَقُولِي إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَـٰنِ صَوْمًا فَلَنْ أُكَلِّمَ الْيَوْمَ إِنسِيًّا ﴿٢٦﴾
26. Basi kula na kunywa na uburudishe jicho. Na pindi ukimuona mtu yeyote basi sema hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa rehema ya kufunga. Kwa hiyo leo sitasema na mtu.
Aya 22 – 26
Basi akachukua mimba yake akaondoka nayo mahali mbali
Inasemekana kuwa Jibril alimpulizia kwenye gauni lake, ikawa ndiyo sababu ya kushika mimba; Rejea ya kauli hii ni dhahiri ya Aya hii:
وَالَّتِي أَحْصَنَتْ فَرْجَهَا فَنَفَخْنَا فِيهَا مِن رُّوحِنَا ﴿٩١﴾
“Na (mwanamke) aliyelinda tupu yake na tukampulizia katika roho yetu” (21:91)
وَمَرْيَمَ ابْنَتَ عِمْرَانَ الَّتِي أَحْصَنَتْ فَرْجَهَا فَنَفَخْنَا فِيهِ مِن رُّوحِنَا ﴿١٢﴾
“Na Maryam Binti Imrani aliyelinda tupu yake na tukampulizia humo kutoka roho yetu,” (66:12).
Mara kwa mara tumeishiria kuwa Qur’an inajifasiri yenyewe; yaani Aya zinafasiri Aya nyingine. Kwa sababu chimbuko lake ni moja. Tukiangalia msingi huu tutafahamu, kwa ujumla wake wote kuwa makusudio ya kupulizia ni kuumba na kutengenezwa mimba, na makusudio ya Roho ni Isa mwenyewe; kama inavyofahamisha Aya hii: “Masih Isa bin Maryam ni Mtume wa Mwenyezi Mungu na neno lake tu alilompelekea Maryam, na ni roho iliyotoka kwake.” Juz.6 (4:171)
Maana ya ‘neno lake’ ni neno ‘kuwa,’ambalo anaumbia nalo vitu. Na maana ya ‘alilompelekea Maryam’ ni kuwa Maryam au tumbo lake ndio mahali pa kuumbwa; Kwa ufafanuzi zaidi angalia huko. Kwa vyovyote ilivyo ni kwamba Maryam alipojihisi ana mimba alijitenga kando na watu wake kwa kuona haya.
Uchungu ukampeleka kwenye shina la mtende; akasema: Laiti ningelikufa kabla ya haya nikawa mwenye kusahaulika kabisa.
Haya ni maneno anayoyasema mtu yeyote anapozongwa na matatizo makubwa, anatamka kupunguza msongo wa moyo na huzuni yake.
Pakanadiwa kutoka chini yake kwamba usihuzunike; hakika Mola wako amejaalia chini yako kijito cha maji.
Yanayokuja akilini mwanzo, kutokana na mfumo wa maneno, ni kuwa aliyenadi ni Isa(a.s) na wala sio Jibril, kama wanavyodai wafasiri wengi. Kunadi huku ni miongoni mwa miujiza ya Isa; sawa na kuzaliwa na kufufua kwake wafu.
Isa aliendelea kumwambia mama yake:
Na litikise kwako shina la mtende utakuangushia tende freshi zilizo mbivu.
Inasemekana huo haukuwa msimu wa tende. Kwa hiyo kupatikana tende ilikuwa ni muujiza. Hili haliko mbali, kwa sababu kila kitu hapa ni muujiza tu na tamko lenyewe pia linafahamisha hivyo.
Basi kula tende na kunywa kutoka kwenye kijito na uburudishe jicho.
Yaani poa moyo kwa kupata mtoto mwenye kubarikiwa.
Na pindi ukimuona mtu yeyote na akakuuliza kuhusu mtoto,basi sema kwa ishara kuwahakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa rehema ya kufunga kwa kunyamaza, Hiyo ndiyo iliyokuwa Swaumu ya waisrail wakati huo.
Kwa hiyo leo sitasema na mtu.
Hapana haja ya ufafanuzi hapa, isipokuwa kufasiri matamshi, kwa sababu akili haina nafasi katika maudhui haya maadamu dhahiri ya maneno haigongani na hukumu ya kiakili katika maudhui haya; Tazama Juz; 3 (3:45–51) kifungu cha ‘Lisilowezekana kiakili na kidesturi.
4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
فَأَتَتْ بِهِ قَوْمَهَا تَحْمِلُهُ قَالُوا يَا مَرْيَمُ لَقَدْ جِئْتِ شَيْئًا فَرِيًّا ﴿٢٧﴾
27. Akaenda naye kwa jamaa zake amembeba. Wakasema: Ewe Maryamu! Hakika umeleta kitu cha ajabu.
يَا أُخْتَ هَارُونَ مَا كَانَ أَبُوكِ امْرَأَ سَوْءٍ وَمَا كَانَتْ أُمُّكِ بَغِيًّا ﴿٢٨﴾
28. Ewe dada wa Harun! Baba yako hakuwa mtu muovu wala mama yako hakuwa kahaba.
فَأَشَارَتْ إِلَيْهِ قَالُوا كَيْفَ نُكَلِّمُ مَن كَانَ فِي الْمَهْدِ صَبِيًّا ﴿٢٩﴾
29. Ndipo Akashiria kwake, Wakasema: Tutamsemezaje aliye bado mdogo susuni?
قَالَ إِنِّي عَبْدُ اللَّـهِ آتَانِيَ الْكِتَابَ وَجَعَلَنِي نَبِيًّا ﴿٣٠﴾
30. Akasema: Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu amenipa Kitabu na amenifanya nabii.
وَجَعَلَنِي مُبَارَكًا أَيْنَ مَا كُنتُ وَأَوْصَانِي بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ مَا دُمْتُ حَيًّا ﴿٣١﴾
31. Na amenijaalia ni mwenye popote pale niwapo. Na ameniusia Swala na Zaka muda wa kuwa niko hai.
وَبَرًّا بِوَالِدَتِي وَلَمْ يَجْعَلْنِي جَبَّارًا شَقِيًّا ﴿٣٢﴾
32. Na kumtendea mema mama yangu, Wala hakunifanya niwe jeuri muovu.
وَالسَّلَامُ عَلَيَّ يَوْمَ وُلِدتُّ وَيَوْمَ أَمُوتُ وَيَوْمَ أُبْعَثُ حَيًّا ﴿٣٣﴾
33. Na amani iwe juu yangu, siku niliyozaliwa na siku nitakayokufa na siku nitakay- ofufuliwa.
ذَٰلِكَ عِيسَى ابْنُ مَرْيَمَ قَوْلَ الْحَقِّ الَّذِي فِيهِ يَمْتَرُونَ ﴿٣٤﴾
34. Huyo ndiye Isa Mwana wa Maryam, kauli ya haki ambayo wanaifanyia shaka.
مَا كَانَ لِلَّـهِ أَن يَتَّخِذَ مِن وَلَدٍ سُبْحَانَهُ إِذَا قَضَىٰ أَمْرًا فَإِنَّمَا يَقُولُ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٣٥﴾
35. Haiwi kwa Mwenyezi Mungu Kuwa na mwana, Yeye ametakasika! Anapolipitisha jambo basi huliambia tu: Kuwa! Likawa.
Aya 27 – 35
Akaenda naye kwa jamaa zake amembeba.
Baada ya Maryam kuzaa, alimbeba mwanawe kwenda naye kwa watu wake, akiwa na utulivu bila ya kuwa na wasiwasi; kwani mimba ambayo ilikuwa ni sababu ya kutuhumiwa kwake, sasa ndiyo yenye ushahidi wa kweli wa usafi wake.
Wakasema: Ewe Maryamu! Hakika umeleta kitu cha ajabu kwa kudai kupata mimba bila ya kuguswa na mtu, huo ni uzushi.
Ewe dada wa Harun ! Huyu ni nduguye Musa, na yeye Maryam ni katika kizazi chao. Makusudio ya kumtaja ni kuwa asili yake ni watu wema na kwamba shina likiwa zuri matawi pia yanatakiwa yawe mazuri, sasa imekuwaje kutokewa na yaliyomtokea ambayo hakuna mfano aliyetokewa na hayo?
Baba yako hakuwa mtu muovu wala mama yako hakuwa kahaba.
Unafanana na nani wewe kwa kitendo chako hiki? Hawezi kufanya hivi ila binti wa muovu au wa mama muovu.
Ndipo akaishiria kwake
Yaani kwa mtoto aweze kushuhudia usafi wake naye ni mkweli zaidi ya wanaoshuhudia, kwa sababu anatamka kwa lugha ya Mwenyezi Mungu.
Wakasema kwa mshangao; Tutamsemezaje aliye bado mdogo susuni?
Lakini yule aliye susuni alianza kuwasemesha kabla wao hawajaanza na akasema:
Hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu amenipa Kitabu na amenifanya ni nabii.
Yaani atanifanya ni nabii baadaye, kwa sababu kitoto kichanga hakiwezi kuongoza watu na kuwa ni hoja kwao. Ikiwa yeye mwenyewe hana majukumu kwa kauli yake wala vitendo vyake. Atawezaje kuwa na majukumu ya kufikisha risala ya Mwenyezi Mungu kwa waja wa Mwenyezi Mungu?
Huko nyuma tumesema kuwa alitumwa kuwa Mtume akiwa na miaka 30; na kwamba alizungumza utotoni ili kumsafisha mama yake na tuhuma ya zina na uchafu; si kwa kuwa alikuwa ni nabii aliyetumwa, Angalia kifungu ‘Isa na utume wa utoto’ katika Juz.7 (5:109 –111).
Na amenijaalia ni mwenye kubarikiwa popote pale niwapo.
Kila anayewanufaisha watu kwa namna moja au nyingine basi ni mweye kubarikiwa na kila mwenye kumdhuru mtu mmoja - sikwambii watu wengi- basi huyo ni muovu na mfisadi.
Na ameniusia Swala na Zaka muda wakuwa niko hai na kumtendea mema mama yangu.
Yeye mwenyewe anakiri utumishi na utiifu kwa Mungu na kukana kuwa ni Mungu, mwana wa Mungu au mshirika wake; kama wanavyodai wanaswara (wakristo).
Wala hakunifanya niwe jeuri muovu; kama wanavyodai mayahudi. Bali ni mja mwema na Mtume; kama wanvyoitakidi waislamu.
Na amani iwe juu yangu, siku niliyozaliwa na siku nitakayokufa na siku nitakayofufuliwa.
Umepita punde mfano wake katika Aya 15 ya sura hii.
Huyo ndiye Isa mwana wa Maryam, kauli ya haki ambayo wanaifanyia shaka.
Hili ndilo neno la kweli, la kielimu na la kiadilifu, kuhusu Bwana Masih.
Sio mjeuri kama wanavyosema mayahudi; wala si Mungu, mwanawe au mshirika wake; kama wasemavyo wanaswara. Yeye ni Nabii anayefikisha risala ya Mola wake na ni mja miongoni mwa waja wake, anaswali na kutoa Zaka. Vile vile yeye ni mwenye kubarikia anayewanufaisha watu. Pia ni mnyenyekevu anayemfanyia wema mama yake.
Haiwi kwa Mwenyezi Mungu kuwa na mwana, Yeye ametakasika! Anapolipitisha jambo basi huliambia tu: Kuwa! Likawa
Lau Mwenyezi Mungu angelikuwa na watoto wangelijifichia kheri zote na baraka na kuzizuia wengine wasizipate. Pia wangeharibu yale aliyoten- geneza vizuri baba na ulimwengu wangeliujaza shari na upotevu; sawa na wanavyofanya baadhi ya watoto wa viongozi siku hizi. Umepita mfano wake katika Juz. 3 (3:59) na katika Juz.15 (18: 111).
وَإِنَّ اللَّـهَ رَبِّي وَرَبُّكُمْ فَاعْبُدُوهُ هَـٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ ﴿٣٦﴾
36. Na Hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu na Mola Wenu, Basi muabuduni, Hii ndio njia iliyonyooka.
فَاخْتَلَفَ الْأَحْزَابُ مِن بَيْنِهِمْ فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ كَفَرُوا مِن مَّشْهَدِ يَوْمٍ عَظِيمٍ ﴿٣٧﴾
37. Lakini Makundi yakahitilafiana baina yao, Basi ole wao waliokufuru kuhudhuria siku iliyo kuu.
أَسْمِعْ بِهِمْ وَأَبْصِرْ يَوْمَ يَأْتُونَنَا لَـٰكِنِ الظَّالِمُونَ الْيَوْمَ فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٣٨﴾
38. Watasikia na wataona vizuri vilioje siku watakayotufikia! Lakini madhalimu leo wako katika upotofu uliodhahiri.
وَأَنذِرْهُمْ يَوْمَ الْحَسْرَةِ إِذْ قُضِيَ الْأَمْرُ وَهُمْ فِي غَفْلَةٍ وَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿٣٩﴾
39. Na waonye siku ya majuto itakapopitishwa amri nao wamo katika ghafla wala hawaamini.
إِنَّا نَحْنُ نَرِثُ الْأَرْضَ وَمَنْ عَلَيْهَا وَإِلَيْنَا يُرْجَعُونَ ﴿٤٠﴾
40. Hakika sisi tutairithi ardhi na walio juu yake na kwetu sisi wata rejeshwa.
Aya 36 – 40
Na hakika Mwenyezi Mungu ni Mola wangu na Mola wenu, basi muabuduni, Hii ndio njia iliyonyooka.
Aya hii inaungana na kauli ya Isa (hakika mimi ni mja wa Mwenyezi Mungu...) anawaamuru, kwenye kauli hii, wamwabudu Mungu mmoja wala wasimshirikishe na kitu chochote na kwamaba dini ya tawhid (kumpwekesha Mungu) ndio njia iliyo sawa; mwenye kuifuata ataokoka na mwenye kuiacha atapotea.
Lakini makundi yakahitilafiana baina yao.
Makundi hayo ni kaumu ya Isa. Kuna kundi lililosema kuwa Isa ni Mungu alishuka ardhini kisha akapanda mbinguni, kundi la pili likasema kuwa ni mwana wa Mungu na kundi la tatu likasema ni mja wa Mwenyezi Mungu. Tofauti ilikuwepo hapo zamani, lakini hivi sasa makundi yote yameafikiana kuwa Isa ni Mungu.
Basi ole wao waliokufuru kuhudhuria siku iliyo kuu
Makusudio ya waliokufuru hapa ni kundi la kwanza na la pili. Aya hii ni ibara nyingine ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
ذَٰلِكَ ظَنُّ الَّذِينَ كَفَرُوا فَوَيْلٌ لِّلَّذِينَ كَفَرُوا مِنَ النَّارِ ﴿٢٧﴾
“Hiyo ni dhana ya waliokufuru ole wao waliokufuru na moto.”(38:27).
Watasikia na wataona vizuri vilioje siku watakayotufikia!
Makafiri watakapoiona adhabu siku ya Kiyama watasema:
رَبَّنَا أَبْصَرْنَا وَسَمِعْنَا فَارْجِعْنَا نَعْمَلْ صَالِحًا إِنَّا مُوقِنُونَ ﴿١٢﴾
“Mola wetu! Tumeshaona na tumeshasikia, Turejeshe tukatende mema, kwani hakika sisi tumekwishakuwa na yakini”(32:12).
Walipokuwa wakilinganiwa kwenye haki walikuwa wakisema:
قُلُوبُنَا فِي أَكِنَّةٍ مِّمَّا تَدْعُونَا إِلَيْهِ وَفِي آذَانِنَا وَقْرٌ ﴿٥﴾
“Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa hayo unayotuitia na masikio yetu yana uziwi” (41:5)
Lakini madhalimu leo wako katika upotofu ulio dhahiri.
Makusudio ya leo hapa, ni siku ya Kiyama; na upotofu ni adhabu, kwa vile siku hiyo hakutakuwa na njia ya uongofu wala upotofu; bali ni hisabu na malipo, hakuna zaidi ya hivyo.
Na waonye siku ya majuto itakapopitishwa amri nao wamo katika ghafla wala hawaamini
Anaaambiwa Mtume(s.a.w.w) awaonye, Siku ya majuto ni Kiyama. Imeitwa hivyo kwa sababu nafsi yenye hatia siku hiyo itasema:
يَا حَسْرَتَىٰ عَلَىٰ مَا فَرَّطتُ فِي جَنبِ اللَّـهِ وَإِن كُنتُ لَمِنَ السَّاخِرِينَ ﴿٥٦﴾
“Ee majuto yangu kwa yale niliyoyapoteza upande wa Mwenyezi Mungu na hakika nilikuwa miongoni mwa wanofanya maskhara.”(39:56).
Amri itapitishwa siku hiyo ambapo hakutakuwa na kubatilika wala kurejea. Wao hivi sasa wameghafilika, kwani wanaweza kujirudi kufuru yao na upotevu wao, wamuombe Mwenyezi Mungu msamaha, lakini wao hawafanyi, na wameendelea na uasi wao.
Kauli yake Mwenyezi Mungu:wala hawaamini, ni kuwa wao hawaisadiki kauli yetu, kwamba wao watafufuliwa, bali wanapeta vichwa vyao huku wakifanya maskhara.
Hakika sisi tutairithi ardhi na walio juu yake na kwetu sisi watarejeshwa.
Ardhi na vilivyomo ni vya Mwenyezi Mungu, hakuna yeyote mwenye kumiliki kitu. Binadamu ni mpita njia tu. Na kila kilicho mikononi mwa mtu ni cha kuazimwa tu, ana majukumu na kuwajibika nacho ili ahisabiwe kwacho.
Kwa ufupi Aya hii inarudufu neno: “Hakika sisi ni wa Mwenyezi Mungu, na Kwake Yeye tutarejea.” Juz. 2 (2:156). Makusudio yake ni kumhadharisha muasi, kumkemea na kupunguza huzuni ya Mtume(s.a.w.w) na uchungu wake kwa kupingwa mwito wake.
وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ إِبْرَاهِيمَ إِنَّهُ كَانَ صِدِّيقًا نَّبِيًّا ﴿٤١﴾
41. Na mtaje Ibrahi mkatika Kitabu hakika yeye alikuwa mkweli sana, Nabii.
إِذْ قَالَ لِأَبِيهِ يَا أَبَتِ لِمَ تَعْبُدُ مَا لَا يَسْمَعُ وَلَا يُبْصِرُ وَلَا يُغْنِي عَنكَ شَيْئًا ﴿٤٢﴾
42. Alipomwambia baba yake: Ewe baba yangu! Kwa nini Unaabudu visivyosikia na visivyoona na visivyokufaa na chochote.
يَا أَبَتِ إِنِّي قَدْ جَاءَنِي مِنَ الْعِلْمِ مَا لَمْ يَأْتِكَ فَاتَّبِعْنِي أَهْدِكَ صِرَاطًا سَوِيًّا ﴿٤٣﴾
43. Ewe baba yangu! Hakika imenifikia elimu isyokufikia wewe, Basi nifuate mimi nitakuongoza njia iliyo sawa.
يَا أَبَتِ لَا تَعْبُدِ الشَّيْطَانَ إِنَّ الشَّيْطَانَ كَانَ لِلرَّحْمَـٰنِ عَصِيًّا ﴿٤٤﴾
44. Ewe baba yangu! Usiabudu Shetani. Hakika shetani ni Mwenye kumuasi Mwingi wa rehema.
يَا أَبَتِ إِنِّي أَخَافُ أَن يَمَسَّكَ عَذَابٌ مِّنَ الرَّحْمَـٰنِ فَتَكُونَ لِلشَّيْطَانِ وَلِيًّا ﴿٤٥﴾
45. Ewe baba yangu! Mimi nakuhofia isikupate adhabu ya Mwingi wa rehema ukawa ni walii washetani.
قَالَ أَرَاغِبٌ أَنتَ عَنْ آلِهَتِي يَا إِبْرَاهِيمُ لَئِن لَّمْ تَنتَهِ لَأَرْجُمَنَّكَ وَاهْجُرْنِي مَلِيًّا ﴿٤٦﴾
46. Akasema: Unaichukia miungu yangu ewe Ibrahim! Kama hutakoma, Basi lazima nitakupiga mawe na niondokelee mbali kwa muda.
قَالَ سَلَامٌ عَلَيْكَ سَأَسْتَغْفِرُ لَكَ رَبِّي إِنَّهُ كَانَ بِي حَفِيًّا ﴿٤٧﴾
47. Akasema Ibrahim: Amani iwe juu yako (salamun alayka)! Nitakuombea msamaha kwa Mola wangu Hakika yeye ananihurumia sana.
وَأَعْتَزِلُكُمْ وَمَا تَدْعُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَأَدْعُو رَبِّي عَسَىٰ أَلَّا أَكُونَ بِدُعَاءِ رَبِّي شَقِيًّا ﴿٤٨﴾
48. Nami na ajitenga nanyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyez Mungu na ninamuomba Mola wangu asaa nisiwe na bahati mbaya.
فَلَمَّا اعْتَزَلَهُمْ وَمَا يَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ وَهَبْنَا لَهُ إِسْحَاقَ وَيَعْقُوبَ وَكُلًّا جَعَلْنَا نَبِيًّا ﴿٤٩﴾
49. Alipojitenga nao na yale wanayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, tulimpa Is-haq na Ya’qub na kila mmoja tukamfanya nabii.
وَوَهَبْنَا لَهُم مِّن رَّحْمَتِنَا وَجَعَلْنَا لَهُمْ لِسَانَ صِدْقٍ عَلِيًّا ﴿٥٠﴾
50. Na tukawapa katika rehema zetu na tukawajaalia kuwa na sifa za kweli tukufu.
Aya 41-50
MAANA
Na mtaje Ibrahim katika Kitabu hakika yeye alikuwa mkweli sana, Nabii.
Makusudio ya Kitabu hapa ni Qur’an. Ukweli ni sifa bora na ya ukamilifu zaidi. Tunalolifahamu kutokana na wasifu wa utume baada ya ukweli, ni kuwa yeye kwa maumbile yake ni mkweli hata kama si mtume.
Katika Juz; 7: (6:74) tumetaja tofauti za maulama katika makusudio ya baba wa Ibrahim, aliyetajwa katika Qur’an, kuwa je, ni baba yake wa hakika au ni baba wa kimajazi au ni ndugu wa baba? Tukasema huko, kuwa hakuna faida ya mzozo huu na kwamba lililo wajib kwa mwislamu ni kuamini utume wa Ibrahim(a.s) . Ama kuitakidi uislamu wa baba yake hilo halihusiani na dini; hasa kwa kuwa dhahiri ya Qur’an inafahamisha ukafiri wake.
Kwa vyovyote iwavyo, ni kuwa Ibrahim alimpa mwito baba yake, awe wa kimajazi au wa kihakika, wa uislamu na akamwambia katika yale aliyomwambia:
Ewe baba yangu! Kwa nini unaabudu visivyosikia na visivyoona na visivyokufaa na chochote?
Baba yake alikuwa akiabudu masanamu, kwa hiyo akamuhoji kwa manti- ki ya kiakili na kimaumbile. Mawe yaliyonyamaza, hayadhuru wala kunufaisha, unayaabudu na kuyasujudia? Iko wapi akili yako na fahamu yako?
Ewe baba yangu! Hakika imenifikia elimu isiyokufikia wewe, Basi nifuate mimi nitakuongoza njia iliyo sawa.
Kila anayekataa ibada ya masanamu anakuwa na ufahamu na akili zaidi kuliko wanayoyaabudu; sikwambii tena mitume wanaopata elimu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ikiwa kutojua kunakuwa ni udhuru kwa yule asiyejua, lakini masanamu hayo yenyewe hayawezi kuacha udhuru kwa anayeyaabudu.
Ewe baba yangu! Usiabudu shetani. Hakika shetani ni Mwenye kumuasi Mwingi wa rehema.
Makusudio ya kumwabudu shetani ni kumtii, kwa sababu Mwenye kukitii kitu atakuwa amekiabudu; Kwa hiyo basi kila anayemuasi Mwenyezi Mungu atakuwa amemuabudu shetani.
Ewe baba yangu! Mimi nakuhofia isikupate adhabu ya Mwingi wa rehema ukawa ni walii wa shetani.
Walii wa shetani inaweza kuwa kwa maana ya kutawaliwa na shetani au kwa maana ya kuwa mtawala wa shetani katika kuabudu masanamu; sawa na kusema: watu wanajilinda na shetani na shetani anajilinda na watu. Katika makadirio yote, ni kuwa lengo ni kuhofisha na kuhadharisha kumtii shetani na kumfuata.
Akasema: Unaichukia miungu yangu ewe Ibrahim! kama hutakoma, basi lazima nitakupiga mawe na niondokelee mbali kwa muda.
Tulipokuwa tukisoma huko Najaf, siku moja tukiwa tumemzunguka mwal- imu wetu akifafanua maswala muhimu ya elimu ya misingi ya fiqh (Usuulul-fiqh) baada ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wake wote wamefahamu, alihitimisha darasa, lakini ghafla mmoja wa wanafunzi akamuuliza swali ambalo lilikuwa mbali kabisa na maudhui ya darasa. Basi mwalimu akaachana naye akawaangalia wanafunzi wengine na akasema:
“Hapo zamani palikuwa na mwanafunzi mmoja aliyejifundisha masuala ya Swaumu kwa mwalimu kwa muda wa zaidi ya mwezi. Baada ya kumaliza darasa yake mwalimu akadhania kuwa mwanafunzi wake ameelewa kila kitu kinachohusiana na Swaumu, lakini mwanafunzi akamwambia umeeleza sana na ukafafanua masuala ya Swaumu, lakini hatukufahamu kuwa Swaumu inakuwa usiku au mchana?!”
Haya hasa ndiyo yaliyompata Ibrahim pamoja na baba yake. Baada ya kumpa dalili zote na kumbembeleza kwa kumwambia ‘ewe baba yangu’ mara nne, lakini alimjibu kwa kumwambia kuwa kweli umeazimia kutowaabudu miungu pamoja nami? Ikiwa ni kweli umeazimia hivi, basi mimi sina jengine ila nikurujumu na kukuua au uniondokelee mbali nisikuone machoni mwangu.
Akasema Ibrahim: Amani iwe juu yako (salamun alayka)! Nitakuombea msamaha kwa Mola wangu, Hakika yeye ananihurumia sana”
Yaani Mwenyezi Mungu anamwitikia maombi yake, Umetangulia mfano wake katika Juz:11 (9:114).
Nami najitenga nanyi na hayo mnayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu na ninamuomba Mola wangu asaa nisiwe na bahati mbaya.
Ibrahim aliwabughudhi watu wake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na akawaondokea kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu akambadilisha familia bora kuliko wao, pale alipompa Is-haq na baada yake Ya’qub bin Is-haq na akawatukuza kwa utume.
Hayo ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
Alipojitenga nao na yale wanayoyaabudu badala ya Mwenyezi Mungu, tulimpa Is-haq na baada ya Is-haq ni Ya’qub na kila mmoja tukamfanya Nabii.
Hakuna aliyeacha kitu katika mambo ya dunia kwa kutengeneza dini yake ila humbadilishia bora zaidi yake.
Na tukawapa katika rehema zetu
Mwenyezi Mungu hakubainisha aina ya alichowapa, kwa sababu neno rehema zetu linaashiria hilo. Inatosha kuwa ni zawadi radhi za Mwenyezi Mungu na neema zake.
Na tukawajaalia kuwa na sifa za kweli tukufu.
Makusudio ya sifa za kweli ni sifa wanazozikariri watu kizazi baada ya kizazi kusifia Ibrahim, Is-haq, Ismail na Ya’qub.
Aya hizi zinatia mkazo kwamba mwenye kumfanyia ikhlasi Mungu naye Mungu humsafisha na anakuwa pamoja naye popote alipo; sawa na alivyomfanyia Ibrahim(a.s) .
5
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ مُوسَىٰ إِنَّهُ كَانَ مُخْلَصًا وَكَانَ رَسُولًا نَّبِيًّا ﴿٥١﴾
51. Na mtaje Musa katika Kitabu, hakika yeye alikuwa ni Mwenye kutakaswa na alikuwa Mtume Nabii
وَنَادَيْنَاهُ مِن جَانِبِ الطُّورِ الْأَيْمَنِ وَقَرَّبْنَاهُ نَجِيًّا ﴿٥٢﴾
52. Na tulimwita upande wa kuume wa Tur na tukamkurubisha kunong’ona naye.
وَوَهَبْنَا لَهُ مِن رَّحْمَتِنَا أَخَاهُ هَارُونَ نَبِيًّا ﴿٥٣﴾
53. Na tukampa kutokana na rehema zetu nduguye, Haruna, awe Nabii
وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ إِسْمَاعِيلَ إِنَّهُ كَانَ صَادِقَ الْوَعْدِ وَكَانَ رَسُولًا نَّبِيًّا ﴿٥٤﴾
54. Na mtaje katika Kitabu, Ismail, Hakika yeye alikuwa mkweli wa ahadi na alikuwa Mtume, Nabii.
وَكَانَ يَأْمُرُ أَهْلَهُ بِالصَّلَاةِ وَالزَّكَاةِ وَكَانَ عِندَ رَبِّهِ مَرْضِيًّا ﴿٥٥﴾
55. Na alikuwa akiwaamrisha watu wake swala na zaka na alikuwa mbele ya Mola wake mwenye kuridhiwa.
وَاذْكُرْ فِي الْكِتَابِ إِدْرِيسَ إِنَّهُ كَانَ صِدِّيقًا نَّبِيًّا ﴿٥٦﴾
56. Na mtaje katika Kitabu, Idris, Hakika yeye alikuwa mkweli wa ahadi na alikuwa Mtume, Nabii
وَرَفَعْنَاهُ مَكَانًا عَلِيًّا ﴿٥٧﴾
57. Na akamwinua mahali pa juu
أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ مِن ذُرِّيَّةِ آدَمَ وَمِمَّنْ حَمَلْنَا مَعَ نُوحٍ وَمِن ذُرِّيَّةِ إِبْرَاهِيمَ وَإِسْرَائِيلَ وَمِمَّنْ هَدَيْنَا وَاجْتَبَيْنَا إِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُ الرَّحْمَـٰنِ خَرُّوا سُجَّدًا وَبُكِيًّا ﴿٥٨﴾
58. Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaneemesha miongoni mwa manabii katika uzao wa Adam na katika wale tuliowapandisha pamoja na Nuh na katika uzao wa Ibrahim na Israil na katika wale tuliowaongoa na tukawateua. Wanaposomewa Aya za Mwingi wa rehema huanguka kusujudu na kulia.
Aya 51-58
Na mtaje Musa katika Kitabu, hakika yeye alikuwa ni Mwenye kutakaswa na alikuwa Mtume Nabii.
Neno kutakaswa limefasiriwa kutokana na neno mukhlaswa kwa maana ya kuwa Mwenyezi Mungu amemtakasa na kila lisilopendeza na akamteua Yeye Mwenyewe. Ikiwa litasomwa, Mukhliswa, litakuwa na maana yakuwa kauli za Musa na vitendo vyake vyote ni vya ikhlasi.
Maana ya Mtume na Nabii ni moja, tofauti iko katika matamshi. Mtume au Mjumbe kwa kuwa anachukua ujumbe wa Mungu na Nabii (lenye maana ya kuzindua na kutoa habari), kwa maana ya kuwa anawazindua na kuwapa habari wale anaowapelekea ujumbe.
Wengine wamesema kuwa Mtume ni yule anayepokea wahyi na kuufikisha na Nabii ni yule anayepokea wahyi tu, lakini haufikishi, Utafiti huu hauna faida yoyote.
Na tulimwita upande wa kuume wa Tur na tukamkurubisha kunong’ona naye.
Tur ni mlima ambao Mwenyezi Mungu alizungumza na Musa. Makusudio ya kuumeni ni kuumeni kwa Musa; Kwa sababu mlima hauna kuume wala kushoto.
Makusudio ya kuumkurubisha kunong’na naye, ni kumkurubisha kihadhi sio ukaribu wa mahali. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu alimtukuza Musa kwa unabii na utume na kuzungumza naye moja kwa moja bila ya kuweko mjumbe mwengine.
Maneno yalikuwa yakimjia Musa kuumeni kwake; kama vile watu walivyo na mazoweya ya kusema: Nimesikia sauti kuumeni kwangu au kushotoni mwangu.
Na tukampa kutokana na rehema zetu nduguye, Haruna, awe Nabii
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaashiria, kwa Aya hii, jambo lilokwishapita, nalo ni kuwa Mwenyezi Mungu alipomwamrisha Musa kwenda kwa Firauni, Musa alimuomba Mwenyezi Mungu kwa kusema: Na nipe waziri katika watu wangu, Harun ndugu yangu, niongeze nguvu zangu kwaye (20:30)
Na mtaje katika Kitabu, Ismail, Hakika yeye alikuwa mkweli wa ahadi na alikuwa Mtume, Nabii. Na alikuwa akiwaamrisha watu wake swala na zaka na alikuwa mbele ya Mola wake mwenye kuridhiwa.
Maana yako wazi haihitajiki tafsiri, Ni jambo zuri tukizungumzia ahadi kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Alikuwa ni mkweli wa ahadi” Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemsifu Ismail kwamba yeye anapoahidi kitu hutekeleza.
Wafasiri wamesema kuwa Ismail siku moja aliahidiana na sahibu yake amngojee mahali, Yule mtu akachelewa, akamngoja siku tatu au zaidi.
Ni sawa riwaya hii iwe sahihi au la, lakini inaonyesha kwamba ni juu ya mtu kufanya bidii, kadiri atakavyoweza kutekeleza ahadi yake.
Na kwamba atakayeacha ahadi, haifai kumwamini na kitu chochote; bali inafaa tumpe sifa ya urongo na udanganyifu; hata kama kutekeleza ahadi kuna hasara ya kimaada, kwa sababu hasara ya kidini ni kubwa zaidi.
Kuna riwaya inayosema kuwa kutekeleza ahadi ni katika alama ya dini na kwamba dini ni maingiliano. Kuna kauli mashuhuri inayosema: ‘Asiyekuwa na ahadi hana dini’
Nimesoma maneno kuhusu ahadi nikaokota baadhi yake kama ifuatavyo:-
• “Mwenye kuacha ahadi kwa sababu ya matatizo atakuwa anajaribu kukikmbia kujituhumu, lakini hali halisi itamtuhumu.
• Kutekeleza ahadi ni tamko zuri katika masikio na ni zuri katika maisha.
• Makusudio ya kutekeleza ahadi nikuwatekelezea ahadi watu wa nyum- bani na marafiki na kuitumikia nchi na mwisho kwa watu wote.
• Utekelezaji ahadi unakufanya upende maisha na kuhalifu kunakufanya uchukie maisha.
• Maana ya kutekeleza ahadi kwa ajili ya watu wa nyumbani na marafiki ni kufanya kazi kwa ajili yao bila ya malipo na kutekeleza ahadi kwa ajili ya nchi ni kujitolea muhanga”
Na mtaje katika Kitabu, Idris, Hakika yeye alikuwa mkweli wa ahadi na alikuwa Mtume, Nabii Mwenyezi Mungu amemsifu kwa ukweli na utume na akamwinua mahali pa juu.
Makusudio ya mahali hapa ni cheo. Imesekana kuwa Mwenyezi Mungu alimwinua mpaka mbingu ya nne, wengine wakasema ni ya saba, kwa kudhania tu. Katika tafsiri imeelezwa kuwa Idris ni babu wa baba yake Nuh, na kwam- ba yeye ndiye wa kwanza kushona nguo, kuandika kwa kalamu, kuangalia nyota na taaluma ya hisabu, Hatujui wafasiri wameyatoa wapi haya.
Mwanafasihi mashuhuri aitwayeTawfiki amandika tamthilia aliyoiita Izyis, Akasema kuwa Izyis huyu ndiye mke wa Ozyrys ambaye aliteswa na mfalme Typhoon. Ikasemekana kuwa Ozyrys huyu ndiye Idris aliyeashiri- wa na Qur’an. Lakini kauli zote hizi ni mawazo na hisia tu.
Hao ndio ambao Mwenyezi Mungu amewaneemesha miongoni mwa manabii katika uzao wa Adam na katika wale tuliowapandisha pamoja na Nuh na katika uzao wa Ibrahim na Israil na katika wale tuliowaongoa na tukawateua. Wanaposomewa Aya za Mwingi wa rehema huanguka kusujudu na kulia.
Amesema Razi na Tabrasiy: makusudio ya kizazi cha Adam ni Idris, kwa sababu yeye ndiye aliyewatangulia wote na yuko karibu zaidi na Adam kuliko Nuh.
Makusudio ya kizazi cha waliopandishwa pamoja na Nuh ni Ibrahim, kwa sababu yeye ni katika kizazi cha Sam. Makusudio ya kizazi cha Ibrahim ni Is-haq, Ismail, na Ya’qub, Israil ndiye Ya’qub. Miongoni mwa kizazi chake ni Musa, Harun, Zakariya, Yahya na Isa kwa upande wa mama.
Wote hao na wengineo ni wale aliwaongoza Mwenyezi Mungu na kuwateua kwa utume, wanamnyenyekea Mwenyezi Mungu na kuhofia ghadhabu yake na adhabu yake pamoja na kuwa wao wanamfanyia ikhlasi Mwenyezi Mungu na kutenda kwa amri yake. Basi inatakikana yule mwenye kujasiri kumuasi Mungu atubie na ahisi hofu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلَاةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا ﴿٥٩﴾
59. Wakafuata baadae wazawa wabaya walioiacha swala na wakafuata matamanio. Basi watakujakuta malipo ya ubaya
إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَأُولَـٰئِكَ يَدْخُلُونَ الْجَنَّةَ وَلَا يُظْلَمُونَ شَيْئًا ﴿٦٠﴾
60. Ispokuwa waliotubu, wakaamini na wakatenda mema, Hapo basi wataingia (Bustani) Peponi wala hawatadhulumiwa chochote.
جَنَّاتِ عَدْنٍ الَّتِي وَعَدَ الرَّحْمَـٰنُ عِبَادَهُ بِالْغَيْبِ إِنَّهُ كَانَ وَعْدُهُ مَأْتِيًّا ﴿٦١﴾
61. Bustani za milele ambazo Mwingi wa rehema aliwaahidi waja wake kwa ghaibu, Hakika Yeye ahadi yake itafika.
لَّا يَسْمَعُونَ فِيهَا لَغْوًا إِلَّا سَلَامًا وَلَهُمْ رِزْقُهُمْ فِيهَا بُكْرَةً وَعَشِيًّا ﴿٦٢﴾
62. Hawatasiki humo upuuzi isipokuwa salama tu na watapata humo riziki zao asubuhi na jioni
تِلْكَ الْجَنَّةُ الَّتِي نُورِثُ مِنْ عِبَادِنَا مَن كَانَ تَقِيًّا ﴿٦٣﴾
63. Hiyo ndiyo Bustani (Pepo) tutakayowarithisha katika waja wetu waliokuwa na takua
وَمَا نَتَنَزَّلُ إِلَّا بِأَمْرِ رَبِّكَ لَهُ مَا بَيْنَ أَيْدِينَا وَمَا خَلْفَنَا وَمَا بَيْنَ ذَٰلِكَ وَمَا كَانَ رَبُّكَ نَسِيًّا ﴿٦٤﴾
64. Wala hatuteremki ila kwa amri ya Mola wako. Ni yake Yeye yaliyoko mbele yetu na yaliyoko nyuma yetu na yaliyoko baina ya hayo, Na Mola wako si mwenye kusahau.
رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا فَاعْبُدْهُ وَاصْطَبِرْ لِعِبَادَتِهِ هَلْ تَعْلَمُ لَهُ سَمِيًّا ﴿٦٥﴾
Mola wa mbingu na ardhi na vilivyo baina yake. Basi muabudu Yeye na uwe na subira kwa ibada yake, Je, unamjua somo yake?
Aya 59 – 65
Wakafuata baadae wazawa wabaya walioiacha swala na wakafuata matamanio.
Baada ya Mwenyezi Mungu kuwataja Mitume watakatifu, anaashiria waovu waliowafuatilia, akawapa wasifu wa kuwacha ibada ya mwingi wa rehema na kumfuata shetani. Maana haya yanafupika kwenye ibara hii: ‘Bora ni waliopita, wabaya ni waliokuja’
Basi watakujakuta malipo ya ubaya, Shari na adhabu ikiwa ni malipo ya maasi yao na inadi yao.
Ispokuwa waliotubu, wakaamini na wakatenda mema, Hapo basi wataingia Bustani (Peponi) wala hawatadhulumiwa chochote.
Tafsiri nzuri ya Aya hii ni kauli ya Mtume mtukufu(s.a.w.w) :“Mwenye kutubia dhambi ni kama asiye na dhambi” , Umetangulia mfano wake katika Juz; 7 (6:54).
Bustani za milele, Zipo daima, neema yake haikatiki wala hakimwi mkaaji wake.
Ambazo Mwingi wa rehema aliwaahidi waja wake kwa ghaibu.
Makusudio ya waja wake hapa ni waumini wenye ikhlasi. Kwa ghaibu ni kuwa wao waliamini Pepo ikiwa iko ughaibuni, Mwenyezi Mungu ame- wasifu waumini kuwa wanaoamini ghaibu katika Aya kadhaa.
Hakika Yeye ahadi yake itafika.
Yaani Mwenyezi Mungu havunji ahadi.
Hawatasikia humo upuuzi isipokuwa salama tu na watapata humo riziki zao asubuhi na jioni.
Katika maisha ya dunia ni upuuzi uwongo na matusi, lakini Peponi ni kauli njema na riziki isiyokoma. Asubuhi na jioni ni fumbo la kudumu, kwa sababu Peponi hakuna asubuhi wala jioni.
Hiyo ndiyo Pepo tutakayowarithisha katika waja wetu waliokuwa na takua.
Neni ‘tutawarithisha’ linatambulisha kuwa Pepo ni ya wenye takua. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: “Hao ndio warithi ambao watarithi Firdausi. Humo watadumu” (23: 11)
Wala hatuteremki ila kwa amri ya Mola wako. Ni yake Yeye yaliyoko mbele yetu na yaliyoko nyuma yetu na yaliyoko baina ya hayo.
Katika Tafsiri Tabariy na Tabrasi, imeelezwa kwamba wahyi ulichelewa kushuka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Aliposhuka Jibril, Mtume akamuuliza ni lipi lililokuzuia hata usitutembelee mara kwa mara, kama ulivyokuwa ukifanya? Ikashuka Aya hii, dhahiri yake inaafikiana na Aya hii, hasa kauli yake Mwenyezi Mungu:
Na Mola wako si mwenye kusahau.
Maana ni kuwa amri ya kuteremshwa wahyi ni ya Mwenyezi Mungu peke yake. Yeye ndiye mmiliki wa kila kitu na ujuzi wake umekizunguka kila kitu na kila mahali, kilipokuwa na kitakapokuwa.
Kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘yaliyoko mbele yetu’ ni ishara ya yatakayokuja, na ‘yaliyoko nyuma yetu’ ni yaliyopita na ‘yaliyoko baina ya hayo’ ni yaliyoko sasa.
Mola wa mbingu na Ardhi na vilivyo baina yake.
Ambaye ni Mola wa ulimwengu itakuwa muhali kwake kusahahu.
Basi muabudu Yeye na uwe na subira kwa ibada yake.
Hii ni amri kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa Mtume wake kwamba aendelee na na umuhimu wake wa kufikisha (tabligh) mwito, kwa sababu hiyo ni katika ibada kubwa, na kuvumilia maudhi katika njia yake.
Je, unamjua somo yake?
Mwenyezi Mungu (s.w.t) hana kifani na chochote, katika sifa zake za utukufu na ukamilifu. Basi anayekuwa hivyo anawajibikiwa na kuabudiwa na kutiiwa.
وَيَقُولُ الْإِنسَانُ أَإِذَا مَا مِتُّ لَسَوْفَ أُخْرَجُ حَيًّا ﴿٦٦﴾
66. Na mtu husema: Hivi nitakapokufa, ni kweli nitatolewa niwe hai?
أَوَلَا يَذْكُرُ الْإِنسَانُ أَنَّا خَلَقْنَاهُ مِن قَبْلُ وَلَمْ يَكُ شَيْئًا ﴿٦٧﴾
67. Je, hakumbuki mtu ya kwamba tulimuumba kabla na hali hakuwa chochote?
فَوَرَبِّكَ لَنَحْشُرَنَّهُمْ وَالشَّيَاطِينَ ثُمَّ لَنُحْضِرَنَّهُمْ حَوْلَ جَهَنَّمَ جِثِيًّا ﴿٦٨﴾
68. Basi naapa kwa Mola wako! Hakika tutawakusanya na mashetani. Kisha tutawahud hurisha kandokando ya Jahanna mnao wamepiga magoti
ثُمَّ لَنَنزِعَنَّ مِن كُلِّ شِيعَةٍ أَيُّهُمْ أَشَدُّ عَلَى الرَّحْمَـٰنِ عِتِيًّا ﴿٦٩﴾
69. Kisha Kwa hakika tutawatoa katika kila kundi wale miongoni mwao waliozidi kumwasi Mwingi wa rehema
ثُمَّ لَنَحْنُ أَعْلَمُ بِالَّذِينَ هُمْ أَوْلَىٰ بِهَا صِلِيًّا ﴿٧٠﴾
70. Tena hakika sisi tunawajua vizuri wanaostahiki kuunguzwa humo.
وَإِن مِّنكُمْ إِلَّا وَارِدُهَا كَانَ عَلَىٰ رَبِّكَ حَتْمًا مَّقْضِيًّا ﴿٧١﴾
71. Hakuna Miongoni mwenu ila ni mwenye kuifikia. Ni hukumu ya Mola wako, ni lazima itimizwe.
ثُمَّ نُنَجِّي الَّذِينَ اتَّقَوا وَّنَذَرُ الظَّالِمِينَ فِيهَا جِثِيًّا ﴿٧٢﴾
72. Kisha tutawaokoa wale wenye takua na tutawaacha madhalimu hapo wamepiga magoti.
Aya 66 –72
Na mtu husema: hivi nitakapokufa, ni kweli nitatolewa niwe hai? Je hakumbuki mtu ya kwamba tulimuumba kabla na hali hakuwa chochote?
Kwa ufupi ni kuwa, hakuna kitu mbele ya mwenye kupinga ufufuo anachopima nacho isipokuwa kustaajabu; vipi utarudi uhai baada ya kumuondokea binadamu? Jibu ni kuwa ataurudisha mara ya pili yule aliyeuleta kwanza: ‘tulimuumba kabla na hali hakuwa chochote’. Maana ya Aya hii yamekaririka katika Aya kadhaa, Angalia Juz; 1 (2:28-29), Juz; 2 (4:87) na Juz. 13 (13:5).
Basi naapa kwa Mola wako! Hakika tutawakusanya na mashetani.
Tutawakusanya hao wanaopinga ufufuo, Makusudio ya kukusanywa ni kutolewa kwao makaburini mwao wakiwa madhalili, wamedharaulika pamoja na wale waliowapoteza
Kisha tutawahudhurisha kandokando ya Jahannam nao wamepiga magoti.
Baada ya kutoka makaburini mwao na hali mbaya hiyo, Malaika watawakalisha wakiwa wamepiga magoti, kandokando ya Jahannam ili waiangalie, wazidi machungu na masikitiko.
Kisha kwa hakika tutawatoa katika kila kundi wale miongoni mwao waliozidi kumwasi Mwingi wa rehema.
Baada ya kuizunguka Jahannam wakiwa wamepiga magoti, wakiwa ni makundi mbali mabali, Mwenyezi Mungu kwanza atachukua kiongozi kutoka kila kundi na kuwatupa katika Jahannam, kisha wanaowafuatia. Kila mmoja atawekwa mahali pake panapomstahiki katika adhabu ya kuungua
Tena hakika sisi tunawajua vizuri wanaostahiki kuunguzwa humo
Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) anajua maovu anayoyafanya kisiri na kidhahiri na atamlipa anavyostahili.
Mwenye madhambi makubwa adhabu yake ni kubwa, kisha anayefuatia na mwingine anayefuatia “Na watakuta waliyoyafanya yamehudhurishwa” Juz; 15 (18: 49).
Hakuna miongoni mwenu ila ni mwenye kuifikia. Ni hukumu ya Mola wako, ni lazima itimizwe. Kisha tutuwaokoa wale wenye takua na tutawaacha madhalimu hapo wamepiga magoti.
Makusudio ya kufikia hapa ni kuona na kushuhudia, kwa sababu waumini wataepushwa na moto; kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu:
إِنَّ الَّذِينَ سَبَقَتْ لَهُم مِّنَّا الْحُسْنَىٰ أُولَـٰئِكَ عَنْهَا مُبْعَدُونَ ﴿١٠١﴾
“Hakika wale ambao wema wetu umewatangulia wataepushwa nao” (21:101).
Pia kwamba kuadhibiwa mtiifu kunapingana na uadilifu wa Mungu. Maana ni kuwa hakuna yeyote kati ya mwema na muovu ila atauona waziwazi. Muovu atauona kisha aungie hali amepiga magoti na mwema atauona na aupite hali ya kushukuru neema ya kuokoka na mwako wake:
فَمَن زُحْزِحَ عَنِ النَّارِ وَأُدْخِلَ الْجَنَّةَ فَقَدْ فَازَ ﴿١٨٥﴾
“Mwenye kuepushwa na moto akatiwa Peponi, basi huyo amefuzu” Juz, 4 (3:185)
6
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا بَيِّنَاتٍ قَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلَّذِينَ آمَنُوا أَيُّ الْفَرِيقَيْنِ خَيْرٌ مَّقَامًا وَأَحْسَنُ نَدِيًّا ﴿٧٣﴾
73. Na wanaposomewa Aya zetu zilizowazi, waliokufuru huwaambia walioamini: lipi katika makundi mawili lenye cheo kizuri na lililo bora barazani
وَكَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّن قَرْنٍ هُمْ أَحْسَنُ أَثَاثًا وَرِئْيًا ﴿٧٤﴾
74. Na karne ngapi tuliziangamiza zilizokuwa na mapambo mazuri zaidi na wazuri zaidi kwa mandhari?
قُلْ مَن كَانَ فِي الضَّلَالَةِ فَلْيَمْدُدْ لَهُ الرَّحْمَـٰنُ مَدًّا حَتَّىٰ إِذَا رَأَوْا مَا يُوعَدُونَ إِمَّا الْعَذَابَ وَإِمَّا السَّاعَةَ فَسَيَعْلَمُونَ مَنْ هُوَ شَرٌّ مَّكَانًا وَأَضْعَفُ جُندًا ﴿٧٥﴾
75. Sema: aliye katika upotofu basi Mwingi wa rehema atampa muda mpaka ayaone aliyoahidiwa –Ama ni adhabu au ni saa. Hapo ndipo watajua ni nani mwenye makao mabaya na mwenye askari dhaifu
وَيَزِيدُ اللَّـهُ الَّذِينَ اهْتَدَوْا هُدًى وَالْبَاقِيَاتُ الصَّالِحَاتُ خَيْرٌ عِندَ رَبِّكَ ثَوَابًا وَخَيْرٌ مَّرَدًّا ﴿٧٦﴾
76. Na Mwenyezi Mungu huwazidishia uwongofu wale walioongoka, Na mema yenye kubaki ni bora katika malipo mbele ya Mola wako na yana mwisho mwema.
Aya 73-76
Na wanaposomewa Aya zetu zilizowazi, waliokufuru huwaambia walioamini: lipi katika makundi mawili lenye cheo kizuri na lililo bora barazani?
Aya za Mwenyezi Mungu zilizo wazi ni dalili, makundi mawili ni waumi- ni na washirikina. Maana ni kuwa Mtume na maswahaba wanawapa washirikina hoja ya mantiki, kiakili na kimaumbile na wao wanajibu kwa mantiki ya tumbo na falsafa yake.
Epikouros alikuwa ni mwanafalsafa wa kiyunani (ugiriki) katika wanafunzi wa Aristatle, alikuwa na madhehebu yake peke yake yaliyotofautiana na wenzake na pia wale waliomtangulia.
Kwa ufupi anasema ladha ndio kheri kuu na machungu ndio shari kuu na kwamba thamani ya fadhila inategemea ladha za kimaana; kama ukweli, maisha ya utulivu na raha na pia ladha za kihisia; kama chakula na kinywaji...
Katika mwongozo wa falsafa hii anasema: Mtu asisukumwe na hawa yake na upendeleo wake kwenye ladha fupi itakayofuatiwa na machungu marefu.
Kwa maneno mengine ni kuwa, kwake yeye Epikouros – akiwa haamini ufufuo- ni kwamba kheri yote inakuwa kwenye ladha ya kidunia; ni sawa iwe kwenye tumbo au kwengineko. Kama itakutana na machungu basi linalozingatiwa ni wingi, lile lenye ladha nyingi litakuwa ni kheri na lenye machungu mengi basi ni shari.
Kuna falsafa ya kale inayoaifikiana na Epikouros kwamba kheri yote iko kwenye ladha ya dunia. Yeye anasema kheri iko kwenye ladha ya kimaana na kihisia pamoja nayo anasema kheri iko kwenye ladha ya tumbo na mengineyo ya hisia.
Miongoni mwa wenye falsafa hii ni Firauni na washirikina wa kiquraysh. Firauni alipinga utume wa Musa(a.s) , akaleta sababu ya kupinga kwake kwa kusema:
“Au mimi si bora kulio huyu aliye mnyonge wala hawezi kusema wazi. Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu...” (43: 52 – 53)
Akasema tena:
فَقَالَ أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٤﴾
“Mimi Ndiye Mola wenu Mkubwa” (79:24).
Kisha akaendela:
أَلَيْسَ لِي مُلْكُ مِصْرَ وَهَـٰذِهِ الْأَنْهَارُ تَجْرِي مِن تَحْتِي ﴿٥١﴾
“Kwani ufalme wa Misri si wangu na hii mito inapita chini yangu?” (43:51).
Makurishi nao, kama Firauni, walikanusha utume wa Muhmmad (s.a.w.) na wakatoa hoja kwa kusema:
لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ كَنزٌ ﴿١٢﴾
“Mbona hakuteremshiwa hazina?” Juz;12 (11:12)
Falsafa hii haihusiki na Firauni na washirikina wa Makka tu, wala na watanuzi na wenye utajiri; isipokuwa inahusika na kila anayemuheshimu mtu na akampima kwa mali yake, basi yeye ni katika walioamini falsafa ya tumbo.
Miongoni mwa niliyoyasoma ni maneno ya kibaraka mmoja aliyesema: “Hawa wanaoilaumu Marekani na majeshi yake na wanavyowapiga wakombozi kila mahali na vile wanavyopora mali za wanyonge kila mahali, wamesahau au wanajitia kusahahu kuwa Marekani ina nguvu za kielimu na mali; na kwamba mwenye nguvu mpishe.”
Nilikuwa nikidhania kuwa falsafa ya tumbo ilikwisha kwenye zama za dhulma, lakini makala haya nilyoyasoma yamenifanya nitambue kuwa falsafa hii imekita mizizi kwenye nafsi za wapiga debe wa ukoloni na vibaraka wake.
Na karne ngapi tuliziangamiza zilizokuwa na mapambo mazuri zaidi na wazuri zaidi kwa mandhari?
Umetangulia mfano wake katika Juz.7 (6:6)
Sema: aliye katika upotofu basi Mwingi wa rehema atampa muda mpaka ayaone aliyoahidiwa – ama ni adhabu au ni saa. Hapo ndipo watajua ni nani mwenye makao mabaya na mwenye askari dhaifu.
Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake awaambie wale wanaoona kheri iko kwenye tumbo tu, kwamba hayo wanayojifaharisha nayo katika nafasi ya maisha waliyo nayo, kuwa ni mtihani wa Mwenyezi Mungu anowajaribu nao waja wake na anawapa muda mwingi.
Wakishukuru Mwenyezi Mungu atawapa thawabu na marejeo mazuri na wakizidi ukafiri na uasi basi atawasalitia ambaye atawatesa katika maisha haya ya duniani au atawaadhibu Mwenyezi Mungu huko Akhera. Huko watajua ni nani wenye hali mbaya, waumini walio mafukara au makafiri walio matajiri?
Lau mtu atamiliki kila kinacho chomozewa na jua, miliki hiyo si chochote kulinganisha na adhabu ya chini ya Jahannam. Amesema Amirul-mu’min, Aliy(a.s) : “Heri siyo kheri ikiwa baada yake ni moto; na shari si shari ikiwa baada yake ni Pepo, Na kila neema isiyokuwa Pepo ni kazi bure na kila balaa isiyokuwa moto ni nafuu.”
Na Mwenyezi Mungu huwazidishia uwongofu wale walioongoka
Hilo ni kwa kuwafahamisha hakika yao na sehemu za makosa na za sawa. Hii ni hidaya na neema kubwa.
Na mema yenye kubaki ni bora katika malipo mbele ya Mola wako na yana mwisho mwema.
Mema yanayobakia ni elimu na mambo ya manufaa. Hayo mawili ni bora kuliko mali na jaha. Kwa sababu yanadumu na kubakia manufaa yake na thawabu zake hazikatiki, lakini jaha na mali zinaisha na kuangamia.
أَفَرَأَيْتَ الَّذِي كَفَرَ بِآيَاتِنَا وَقَالَ لَأُوتَيَنَّ مَالًا وَوَلَدًا ﴿٧٧﴾
77. Je, umemuona aliyezikana ishara zetu na akasema: Hakika mimi nitapewa mali na watoto.
أَطَّلَعَ الْغَيْبَ أَمِ اتَّخَذَ عِندَ الرَّحْمَـٰنِ عَهْدًا ﴿٧٨﴾
78. Kwani yeye amepata habari za ghaibu au amechukua ahadi kwa Mwingi wa rehema.
كَلَّا سَنَكْتُبُ مَا يَقُولُ وَنَمُدُّ لَهُ مِنَ الْعَذَابِ مَدًّا ﴿٧٩﴾
79. Hapana! Tutaandika anayoyo asema na tutamkunjulia muda wa adhabu.
وَنَرِثُهُ مَا يَقُولُ وَيَأْتِينَا فَرْدًا ﴿٨٠﴾
80. Na tutamrithi hayo anayoyasema na atatufikia akiwa peke yake.
وَاتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ آلِهَةً لِّيَكُونُوا لَهُمْ عِزًّا ﴿٨١﴾
81. Na wamechukua miungu mingine ili iwape nguvu.
كَلَّا سَيَكْفُرُونَ بِعِبَادَتِهِمْ وَيَكُونُونَ عَلَيْهِمْ ضِدًّا ﴿٨٢﴾
82. Sivyo kabisa! Wataikataa ibada yao na watakuwa ndio dhidiyao.
أَلَمْ تَرَ أَنَّا أَرْسَلْنَا الشَّيَاطِينَ عَلَى الْكَافِرِينَ تَؤُزُّهُمْ أَزًّا ﴿٨٣﴾
83. Kwani huoni kwamba tume-watuma mashetani kwa makafiri wawachochee kwa uchochezi.
فَلَا تَعْجَلْ عَلَيْهِمْ إِنَّمَا نَعُدُّ لَهُمْ عَدًّا ﴿٨٤﴾
84. Basi usiwafanyie haraka, Sisi tunawahisabia siku.
يَوْمَ نَحْشُرُ الْمُتَّقِينَ إِلَى الرَّحْمَـٰنِ وَفْدًا ﴿٨٥﴾
85. Siku tutakayowakusanya wenye takua kuwa ni wageni wa Mwingi wa rehema.
وَنَسُوقُ الْمُجْرِمِينَ إِلَىٰ جَهَنَّمَ وِرْدًا ﴿٨٦﴾
86. Na tutawachunga wahalifu kuwapeleka Jahannam hali ya kuwa na kiu
لَّا يَمْلِكُونَ الشَّفَاعَةَ إِلَّا مَنِ اتَّخَذَ عِندَ الرَّحْمَـٰنِ عَهْدًا ﴿٨٧﴾
87. Hawatakuwa na mamlaka ya uombezi ila wale waliochukua ahadi kwa Mwingi wa rehema.
Aya 77 – 87
Je, umemuona aliyezikana ishara zetu na akasema: Hakika mimi nitapewa mali na watoto.
Imeelezwa katika Hadith na tafsiri kwamaba A’si bin Wail, mzazi wa Amru bin Al’as, aliposikia kuhusu utume, alisema kwa stihzai: Bila shaka mimi huko akhera nitapewa mali na watoto.
Lakini dhahiri ya tamko la Aya linaonyesha kuwa kuna mzandiki fulani aliyesema hivi; ama kuwataja watu majina, hiyo si katika njia ya Qur’an. Mfano wa Aya hii ni kauli ya yule mwenye kitalu aliyesema:
وَلَئِن رُّدِدتُّ إِلَىٰ رَبِّي لَأَجِدَنَّ خَيْرًا مِّنْهَا مُنقَلَبًا ﴿٣٦﴾
“Na kama nitarudishwa kwa Mola wangu bila shaka nitapata marejeo bora zaidi Kuliko haya”Juz;15 (18:36).
Ameirudi Mwenyezi Mungu kauli hii kwa kusema:
Kwani yeye amepata habari za ghaibu au amechukua ahadi kwa Mwingi wa rehema.
Amepata wapi habari hizi? Au yeye ana funguo za siri au amechukua ahadi na Mwenyezi Mungu katika hilo?
Hapana ! si hivi wala hivyo; isipokuwa yeye ni kafiri muovu.Tutaandika anayoyasema na tutamkunjulia muda wa adhabu Tumezihifadhi kauli zake na tutamzidishia adhabu zaidi ya kufuru yake na uzushi wake.
Na tutamrithi hayo anayoyasema na atatufikia akiwa peke yake, akiwa mtupu na pia tutamnyng’anya mali na watoto alio nao, pale anapokufa na kuangamia na tutamfufua siku ya kiyama akiwa peke yake mtupu; sawa na tulivyomuumba mara ya kwanza.
Na wamechukua miungu mingine ili iwape nguvu. Sivyo kabisa! Kwa sababu mwenye kutaka nguvu kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, basi Mungu humvisha vazi la udhalili.
Wataikataa ibada yao na watakuwa ndio dhidi yao
Yaani hao wanawaabudu wataikataa ibada yao na watakuwa dhidi yao. Tafsiri inayofafanua zaidi Aya hii ni kauli ya Imam Ali(a.s), katika Nahjulbalagha: Sio mbali anayefuatwa atajitenga na mfuasi na kiongozi na anayeongozwa watafarikiana kwa chuki na watalaaniana watakapokutana.
Mwenyezi Mungu naye amesema:
تَبَرَّأْنَا إِلَيْكَ مَا كَانُوا إِيَّانَا يَعْبُدُونَ ﴿٦٣﴾
“Tunajitenga nao mbele yako, Hawakuwa wakituabudu sisi” (28:63);bali walikuwa wakiabudu hawa zao na malengo yao.
Kwani huoni kwamba tumewatuma mashetani kwa makafiri wawa- chochee kwa uchochezi.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) haingilii kati baina yao na mashetani wanowapa wasiwasi na kuwahadaa na maasi, wala hajiingizi, kwa uweza wake wa kufanya, kumzuia shetani; isipokuwa amewabainishia njia ya kheri na shari na kuwapa uwezo kamili wa kutenda na kuwaacha; anawakataza hili na kuwaamrisha lile; kisha anawaachia hiyari katika watakayoyatenda na kuyaacha.
Kama angeliwanyanyag’anya utashi, basi wangelikuwa wao na miti ni sawa.
Basi usiwafanyie haraka. Sisi tunawahisabia siku.
Yaani, ewe Muhammad, usiwe na haraka ya kuangamia makafiri, kwani maangamizi yao yatakuja tu, lakini Mwenyezi Mungu anawangoja mpaka muda uliotajwa, ili avidhibiti vitendo vyao, kisha aje awalipe, wanayostahili. Kwani hakuna kheri ya kurefuka maisha isipokuwa kwa yule anayeamini na akatenda amali njema, lakini mwenye kukufuru na akafanya maovu, basi maisha yake ni balaa:
وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا أَنَّمَا نُمْلِي لَهُمْ خَيْرٌ لِّأَنفُسِهِمْ إِنَّمَا نُمْلِي لَهُمْ لِيَزْدَادُوا إِثْمًا وَلَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿١٧٨﴾
“Wala wasidhanie kabisa wale waliokufuru kwamba muda tunaowapa ni kheri kwa nafsi zao, Hakika tunawapa muda na wanazidi tu katika dhambi na wana adhabu idhalilishayo.”Juz.4 (3:178).
Siku tutakyowakusanya wenye takua kuwa ni wageni wa Mwingi wa rehema.
Neno lililotumika katika kufasiri wageni limetokana na neno la kiarabu wafd lenye maana ya wageni wa heshima. Maana ni kuwa wale wanaomtii Mwenyezi Mungu, kesho watakuwa ni wageni wenye kutukuzwa.
Na tutawachunga wahalifu kuwapeleka Jahannam halia ya kuwa na kiu
Waumini watapata makaribisho ya heshima na wahalifu watapata makaribisho ya dharau, kuchungwa kama wanyama wanavyochungwa kwenda kunywa maji; ndivyo wahalifu nao watachungwa kupelekwa kwenye Jahannam.
Hawatakuwa na mamlaka ya uombezi ila wale waliochukua ahadi kwa Mwingi wa rehema.
Kila mwenye kutekeleza ahadi ya Mwenyeezi Mungu na wala asimfanyie hiyana kwenye dogo wala kubwa, basi Mwenyezi Mungu amempa ahadi ya kufuzu na kuokoka na uombezi:
وَأَوْفُوا بِعَهْدِي أُوفِ بِعَهْدِكُمْ وَإِيَّايَ فَارْهَبُونِ ﴿٤٠﴾
“Na tekelezeni ahadi yangu nitatekeleza ahadi yenu”Juz;1(2:40)
وَقَالُوا اتَّخَذَ الرَّحْمَـٰنُ وَلَدًا ﴿٨٨﴾
88. Na wanasema Mwingi wa rehema anamwana.
لَّقَدْ جِئْتُمْ شَيْئًا إِدًّا ﴿٨٩﴾
89. Hakika mmeleta Jambo la kuchusha.
تَكَادُ السَّمَاوَاتُ يَتَفَطَّرْنَ مِنْهُ وَتَنشَقُّ الْأَرْضُ وَتَخِرُّ الْجِبَالُ هَدًّا ﴿٩٠﴾
90. Zinakurubia mbingu kutatuka kwa hilo na ardhi kupasuka na milima kuanguka vipande vipande
أَن دَعَوْا لِلرَّحْمَـٰنِ وَلَدًا ﴿٩١﴾
91. Kwa kudai kwao kuwa Mwingi wa rehema ana mwana.
وَمَا يَنبَغِي لِلرَّحْمَـٰنِ أَن يَتَّخِذَ وَلَدًا ﴿٩٢﴾
92. Hahitajii Mwingi wa rehema kuwa na mwana.
إِن كُلُّ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ إِلَّا آتِي الرَّحْمَـٰنِ عَبْدًا ﴿٩٣﴾
93. Hakuna yeyote aliyemo mbinguni na ardhini ila atafika kwa Mwingi wa rehema kuwa ni mtumwa.
لَّقَدْ أَحْصَاهُمْ وَعَدَّهُمْ عَدًّا ﴿٩٤﴾
94. Hakika amewadhibiti na amewahisabu sawa sawa.
وَكُلُّهُمْ آتِيهِ يَوْمَ الْقِيَامَةِ فَرْدًا ﴿٩٥﴾
95. Na kila mmoja kati yao atam fikia siku ya Kiyama peke yake
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ سَيَجْعَلُ لَهُمُ الرَّحْمَـٰنُ وُدًّا ﴿٩٦﴾
96. Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema Mwingi wa rehema atawajaalia mapenzi.
فَإِنَّمَا يَسَّرْنَاهُ بِلِسَانِكَ لِتُبَشِّرَ بِهِ الْمُتَّقِينَ وَتُنذِرَ بِهِ قَوْمًا لُّدًّا ﴿٩٧﴾
97. Hakika tumeifanya nyepesi, kwa ulimi wako ili uwabashirie kwayo wenye takua na uwaonye kwayo wabishi
وَكَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّن قَرْنٍ هَلْ تُحِسُّ مِنْهُم مِّنْ أَحَدٍ أَوْ تَسْمَعُ لَهُمْ رِكْزًا ﴿٩٨﴾
98. Na karne ngapi tumeziangamiza kabla yao, Je, unawaona hata mmoja katika wao au unasikia hata mchakato wao?
WANASEMA MWINGI WA REHEMA AMEJIFANYIA MWANA
Aya 88 – 98
Na wao wanasema Mwingi wa rehema ana mwana. Hakika mmeleta jambo la kuchusha, Zinakurubia mbingu kutatuka kwa hilo na ardhi kupasuka na milima kuanguka vipande vipande kwa kudai kwao kuwa Mwingi wa rehema ana mwana.
Mwenyezi Mungu amewakemea sana wale waliomfanya Mwenyezi Mungu kuwa ana watoto wa kiume na mabinti na akawapa kiaga kwenye Aya kadhaa; miongoni mwazo ni: Juz.1 (2:116), Juz.5 (4:48), Juz. 6 (4:171) na Juz. 7 (6:101).
Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akataja hapa kauli yao hii kwa mfumo huu wa kutisha. Nao unafahamisha kuwa mtu anamchezea ambaye hachezewi na yeyote aliye mbinguni wala ardhini.
Binadamu anamchezea Muumba wake naye anaishi kwenye himaya yake, na anamnasibisha mambo ambayo kuyasikia tu yanaweza yakaipasua mbingu na ardhi na kuangusha milima.
Unaweza kuuliza : kwanini hasira yote hii ya kilimwengu kwa sababu tu ya maneno ya kijinga na ya udhaifu wa akili?
Jibu : Hasira yote hii, haiko kwa mtu au kikundi cha watu maalum; isipokuwa imetokana na shirki hii ambayo sasa imekuwa ni dini na itikadi wanayoifuata mamilioni, kizazi baada ya kizazi na mifano hii ya mungu mwan na mungu mama.
مَّا الْمَسِيحُ ابْنُ مَرْيَمَ إِلَّا رَسُولٌ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِ الرُّسُلُ وَأُمُّهُ صِدِّيقَةٌ كَانَا يَأْكُلَانِ الطَّعَامَ ﴿٧٥﴾
“Masih mwana wa Maryam hakuwa ila ni Mtume, Wamepita kabla yake Mitume, Na mama yake ni mkweli, Wote wawili walikuwa wakila chaku- la”Juz; 6 (5:75).
Hahitajii Mwingi wa rehema kuwa na mwana.
Kwa sababu mwana anafanana na mzazi wake, na Mwenyezi Mungu hana aliyefanana naye. Na kwa sababu kuwa na mtoto ni kumuhitajia, na Mwenyezi Mungu amejitosheleza na walimwengu wote
Hakuna yeyote aliyomo mbinguni na ardhini ila atafika kwa Mwingi wa rehema kuwa ni mtumwa.
Hakuna yeyote aliyeko chini au juu ila huwa ni mja wa Mwenyezi Mungu anayemilikiwa. Kimsingi ni kwamba mwenye kumilikiwa sio mtoto na mmliki sio baba.
Hakika amewadhibiti na amewahisabu sawa sawa na kila mmoja kati yao atamfikia siku ya Kiyama peke yake.
Waliodhibitiwa ni walio mbinguni na ardhini na atakyefikiwa ni Mwenyezi Mungu. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu hapotewi na kujua kitu chochote katika ardhi wala katika mbingu na kwamba kila mmoja atakwenda kwa Mwenyezi Mungu siku ya kiyama akiwa peke yake, hana wa kumnusuru wala kumsaidia au kujisaidia yeye mwenyewe kwa wingi au uchache, sikwambii tena kumsadia mwenginewe. Ambaye atamjia Mwenyezi Mungu katika hali kama hiyo, anawezaje kuwa mtoto wake?
Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema Mwingi wa rehema atawajaalia mapenzi.
Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anatia mapenzi katika nyoyo za waja wake kwa watu wenye imani na ikhlasi, si kwa chochote ila kwa kuthamini fadhila na hulka njema.
Muhammad bin Ahmad Alkalabiy, mwenye kitabu Attas-hil anasema: Inasemekana kuwa Aya hii ilishukwa kwa Aliy bin Abi Twalib. Sheikh Almaraghi, mmoja wapo wa masheikh wa Al-Azhar, anasema: ‘Ibin Mardaywyh na Dilamiy wamepokea kutoka kwa Baraa, kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alimwambia Aliy: Sema ewe Mola wangu nijalie ahadi kwako na unijaalie mapenzi katika nyoyo za waumini’ ndipo ikashuka Aya hii”.
Amesema Abu Hayani Al-andalusi katika tafsir yake Albahrul-Muhit: “Aya hii ilishuka kwa Aliy bin Abi Twalib na amesema Muhammad Alhanafiya: huwezi kumpata mumin ila anampenda Aliy. Maajabu ni yale aliyotueleza Imam wa lugha Ridhad Din, Abu Abdillah Muhammad bin Aliy bin Yusuf Al-Answariy Ashatibiy kuhusu aliyosema, ibn Is-haq Mnaswara:
• Uday na Taym kwa ubaya kamwe sitothubutu kuwataja
• Lakini naona ni vibaya Ali kulaumiwa na waja
• Mimi ni mpenzi wa dhuriya ya Hashimu na wanawe pamoja
• Naswira watukufu kupambiya kwa nini imekuwa ni kioja
• Tawaambiya huku kiusiya moyo wangu umekwisha wachuja
• Kupenda nifuraha nawambiya hata wanyama pia wangoja.
Hakika tumeifanya nyepesi, kwa ulimi wako ili uwabashirie kwayo wenye takua na uwaonye kwayo wabishi.
Yaani Mwenyezi Mungu ameteremsha Qur’an kwa lugha ya kiarabu ili iwe wepesi kuijua na kufahamu maana yake na iwe ni habari njema kwa mwenye kumcha Mwenyezi Mungu na onyo kwa mwenye kukufuru na akafanya uovu. Umepita mfano wake katika Juz. 12 (12:2)
Na karne ngapi tumeziangamiza kabla yao, Je, unawaona hata mmoja katika wao au unasikia hata mchakato wao?
Yaani Mwenyezi Mungu amewaangamiza mpaka wa mwisho wao. Umetangulia mfano wake katika Aya ya 84 ya sura hii; na Juz, 15 (17:17).
MWISHO WA SURA YA KUMI NA TISA
7
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
Sura Ya Ishirini: Surat Twaha. Imeshuka Makka, ina Aya 135
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
طه ﴿١﴾
1. Twaha
مَا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لِتَشْقَىٰ ﴿٢﴾
2. Hatukukuteremshia Qur’an ili upate mashaka.
إِلَّا تَذْكِرَةً لِّمَن يَخْشَىٰ ﴿٣﴾
3. Ispokuwa ni mawaidha kwa wenye kunyenyekea.
تَنزِيلًا مِّمَّنْ خَلَقَ الْأَرْضَ وَالسَّمَاوَاتِ الْعُلَى ﴿٤﴾
4. Uteremsho utokao kwa aliyeumba ardhi na mbing zilizo juu.
الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ ﴿٥﴾
5. Mwenyezi Mungu ametawala juu ya Arshi.
لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الْأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا وَمَا تَحْتَ الثَّرَىٰ ﴿٦﴾
6. Ni vyake vilivyo katika mbingu na katika ardhi na vilivyo baina yao na vilivyo chini ya mchanga.
وَإِن تَجْهَرْ بِالْقَوْلِ فَإِنَّهُ يَعْلَمُ السِّرَّ وَأَخْفَى ﴿٧﴾
7. Na ukiinua sauti kwa kusema, basi yeye anajua siri na yanayofichika. zaidi.
اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ لَهُ الْأَسْمَاءُ الْحُسْنَىٰ ﴿٨﴾
8. Mwenyezi Mungu hapana Mola ila Yeye, Anamajina mazuri.
Aya 1 – 8
wametofautiana katika makusudio ya Twaha. Ikasemekana ni jina katika majina ya Mwenyezi Mungu. Kauli hiyo ameichagua Tabariy, pale aliposema: hii ndio maana ya sawa; kwa sababu maana ya Twaha katika Lugha ya Akka ni Ewe mtu!
Wafasiri wengi wamesema kuwa tamko la Twaha ni herufi za kuendeleza, kama ilivyo Alif Lam Mim na Kaf Ha Ya Ayn Swad.
Katika Tafsir Arraziy imeelezwa kuwa Imam Jaffer As-swadiq(a.s) amesema: herufi twa ni twahara ya watu wa nyumba ya Mtume (Ahlu bayt) na herufi Ha ni hidaya (uongofu) yao.
Si mbali kuwa tafsiri hii inayonasibishwa kwa Imam Jaffer Asswadiq ndio sababu ya wale wanaosema kuwa Twaha ni miongoni mwa majina ya Mtume(s.a.w.w) . Kwa sababu yeye ndio chimbuko la kwanza la utwahara wa watu wa nyumba yake na hidaya yao.
Hatukukuteremshia Qur’an ili upate mashaka; isipokuwa ni mawaidha kwa wenye kunyenyekea.
Mtume(s.a.w.w) alikuwa akijituma na kufuatisha na ibada na pia alikuwa akifanya juhudi na kutaabika huku akiwasikitikia makafiri na ukafiri wao. Mwenyezi Mungu akampoza na kujitaabisha huku na akamwambia:
Kwa nini unajitia mashaka na kujibebsha mzigo mzito wa ibada nyingi na kusononeka na upinzani wa anayepinga mwito wako? Mimi sikukuteua wala kuiteremsha Qur’an kwa hili la kupata tabu; isipokuwa nimekuteremshia ili uongoke nayo wewe na wanaokufuata katika waumini na uwaawidhie kwayo makafiri iwe ni hoja juu yao.
فَلَا تَذْهَبْ نَفْسُكَ عَلَيْهِمْ حَسَرَاتٍ ﴿٨﴾
“Basi roho yako isitoke kwa kuwasikitikia” (35:8)
Kwa hiyo ni neema na rehema kutoka kwa wanaoamini na balaa kwa wenye kupinga na kuasi.
Uteremsho utokao kwa aliyeumba ardhi na mbingu zilizo juu
Aliyeitermsha Qur’an ndiye aliyeumba ulimwengu; ulimwengu ni kitabu cha Mwenyezi Mungu kinachozongumza kwa lugha ya hali na Qur’an ni Kitabu chake kinachozungumza kwa lugha ya makala. Vyote hivyo viwili vina kheri ya watu na wema wao, basi ni kwa nini kushuka Qur’an kuwe ni nyenzo ya kukutaabisha ewe Muhammad?
Unaweza kuuliza : Qur’an ilishuka kwa Mtume(s.a.w.w) ili aweze kuitumia na kuwaongozea watu, imeelezwa katika hiyo Qur’an:
وَمَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فِي الدِّينِ مِنْ حَرَجٍ ﴿٧٨﴾
“Wala hakuwawekea mambo mazito katika dini ” (22:78).
Vile vile imesema:
أَوْ نَتَوَفَّيَنَّكَ فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ وَعَلَيْنَا الْحِسَابُ ﴿٤٠﴾
“Basi ni juu yako kufikisha na juu yetu ni hisabu”Juz ;13(13:40)?
Ilikuwaje kwa Mtume kujitaabisha kwa ibada na masononeko?
Jibu : yule aliye mtukufu huiona ndogo kheri anayoifanya hata kama ni kubwa, huifanya kubwa dhambi yake hata kama ni ndogo na hujituhumu kwa uzembe kadiri anavyojitahidi.
Na Mtume(s.a.w.w) ni mtukufu zaidi ya viumbe wote. Utukufu wake unategemea na kumjua kwake Mungu, kumtii na kufanya juhudi ya kulingania mwito wa njia yake.
Kwa ajili hii anaji- tuhumu na anajiona bado hajatimiza haki ya Mungu kadiri atakavyofanya ibada na kutoa mwito wa haki; hasa pale inapokuwa haujatoa matunda ya kuwaongoza makuraish.
Mwenyezi Mungu ametawala juu ya Arshi.
Hili ni fumbo la kutawalia mambo na kuyapangilia vizuri, Umetangulia mfano wake, katika Juz; 8 (7:54).
Ni vyake vilivyo katika mbingu na katika ardhi na vilivyo baina yao na vilivyo chini ya mchanga
Makusudio ya mchanga hapa ni ardhi. Aya hii ni ubainfu na tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu, ameumba ardhi na mbingu na ametawala kwenye Arsh.
Kwa sababu mwenye kuumba na kupangilia ndiye mmiliki. Hakuna yeyote anayemiliki kitu isipokuwa ni katika milki yake.
Na ukiinua sauti kwa kusema, basi yeye anajua siri na yanayofichika zaidi.
Yanayofichika zaidi ni yale yanayopita moyoni bila ya kuyatamka. Ufafanuzi zaidi wa tafisri ya yanayofichika ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ ﴿١٥٤﴾
“Na Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo vifuani”Juz; 4(3:154)
Mwenyezi Mungu hapana Mola ila Yeye, Ana majina mazuri.
Majina yote ya Mwenyezi Mungu ni mazuri, kwa sababu yanaleta ibara ya maana nzuri na sifa nzuri. Angalia kifungu cha: ‘Je, majina ya Mwenyezi Mungu ni hayo hayo au yana kiasi’ Juz. 9 (7: 178 – 181)
وَهَلْ أَتَاكَ حَدِيثُ مُوسَىٰ ﴿٩﴾
9. Je, imekujia hadith ya Musa?
إِذْ رَأَىٰ نَارًا فَقَالَ لِأَهْلِهِ امْكُثُوا إِنِّي آنَسْتُ نَارًا لَّعَلِّي آتِيكُم مِّنْهَا بِقَبَسٍ أَوْ أَجِدُ عَلَى النَّارِ هُدًى ﴿١٠﴾
10. Pale alipoona moto, akawaambia watu wake: ngojeni! Mimi nimeona moto, huenda nikawaletea kijinga kutoka huko au nikapata uongofu.
فَلَمَّا أَتَاهَا نُودِيَ يَا مُوسَىٰ ﴿١١﴾
11. Basi alipoufikia akaitwa: Ewe Musa!
إِنِّي أَنَا رَبُّكَ فَاخْلَعْ نَعْلَيْكَ إِنَّكَ بِالْوَادِ الْمُقَدَّسِ طُوًى ﴿١٢﴾
12. Hakika Mimi ndiye Mola wako, basi vua viatu vyako; kwani hakika wewe uko katika bonde takatifu la Tuwa
وَأَنَا اخْتَرْتُكَ فَاسْتَمِعْ لِمَا يُوحَىٰ ﴿١٣﴾
13. Nami nimekuteua, basi sikiliza unayopewa wahyi
إِنَّنِي أَنَا اللَّـهُ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا أَنَا فَاعْبُدْنِي وَأَقِمِ الصَّلَاةَ لِذِكْرِي ﴿١٤﴾
14. Hakika Mimi ndiye Mwenyezi Mungu, Hapana Mungu isipokuwa mimi, Basi niabudu mimi na usimamishe swala kwa ajili ya kunikumbuka
إِنَّ السَّاعَةَ آتِيَةٌ أَكَادُ أُخْفِيهَا لِتُجْزَىٰ كُلُّ نَفْسٍ بِمَا تَسْعَىٰ ﴿١٥﴾
15. Hakika Saa (kiyama) itakuja, nimekaribia kuificha, ili kila nafsi ilipwe kwa iliyoyafanya
فَلَا يَصُدَّنَّكَ عَنْهَا مَن لَّا يُؤْمِنُ بِهَا وَاتَّبَعَ هَوَاهُ فَتَرْدَىٰ ﴿١٦﴾
16. Kwa hiyo asikukengeushe nayo yule asiyeiamni na akafuata hawa yake ukaangamia.
Aya 9-16
Mwenyezi Mungu amekitaja kisa cha Musa, katika Kitabu chake, mara nyingi, Siri - kama tulivyogundua tukifasiri Aya za Dhikr Tukufu – ni kwamba Mwenyezi Mungu ametaja maovu mengi ya Wana wa Israil na Musa akiwakataza na kuwahadharisha, ndio ikawa kutajwa kwao ndio kutajwa kwake. Hii ni kuongezea kisa chake na Shuaib na Firauni, kusuhubiana kwake na mja mwema ambaye aliitoboa safina, kumuua kijana na kujenga ukuta. Vilelele kuzaliwa kwake na kuwekwa kwenye kisanduku katika maji hadi kumua kwake Firaun nk.
Badhi ya wafasiri wamesema: “Mwenyezi Mungu alikariri kisa cha Musa pamoja na Firauni, kwa sababu hikaya ya Musa tangu kuanza kutungwa mimba yake mpaka mwisho wa uhai wake, ni somo, nasaha, onyo, bishara na maliwazo kwa Mtume na waumini.
Ndani yake mna ishara zinazofahamisha elimu ya Mwenyezi Mungu, uweza wake, hekima yake na jinsi Musa alivyowachukua watu wake waliokuwa wapumbavu kuliko watu wote.”
Hii ndio dunia ya Musa: wakati wa kuzaliwa kwake aliwekwa kwenye kisanduku na akatupwa majini, akalelewa yatima katika nyumba ya Firaun, akafukuzwa akawa hana kitu akila mimea ya ardhi, akawa mchungaji kon- doo kisha akawa mtume akipata ugumu kutoka kwa watu wake.
Kwa hiyo si nyongeza kisa chake kikikaririka kutajwa na kuzungumziwa katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, maadamu maisha yake yote na kisa chake ni somo na mawaidha. Aya hizi tulizo nazo hivi sasa zinazungumzia kuanza kushuka wahyi kwa Musa na kuzungumza na Mwenyeezi Mungu.
Je imekujia hadith ya Musa?
Huu ni mfano wa kusema: ‘unayo habari?’ au ‘una habari gani?’ Makusudio ni kutanabahi msikilizaji asikilize vizuri simulizi. Na hii ifuatayo ndio hadith ya kuanza wahyi kwa Musapale alipoona moto, akawaambia watu wake: ngojeni! Mimi nimeona moto, huenda nikawaletea kijinga kutoka huko au nikapata uongofu.
Katika Aya 14 na zilizo baada yake Mwenyezi Mungu amekieleza kisa cha Musa. Anaelezea kwamba Musa alipofikia umri wa kukomaa aliwaona watu wawili wakipigana, mmoja ni wa upande wa Firaun na mwingine upande wa mayahudi. Huyu wa upande wa mayahaudi alitaka msaada kwa Musa. Musa akampiga ngumi ikamuua.
Musa akakimbia kutoka Misr kwenda Madyan ambako Shuayb alimuoza mmoja wa mabinti zake kwa kuchunga wanyama wake kwa muda wa miaka minane au miaka kumi:
فَلَمَّا قَضَىٰ مُوسَى الْأَجَلَ وَسَارَ بِأَهْلِهِ آنَسَ مِن جَانِبِ الطُّورِ نَارًا قَالَ لِأَهْلِهِ امْكُثُوا إِنِّي آنَسْتُ نَارًا لَّعَلِّي آتِيكُم مِّنْهَا بِخَبَرٍ أَوْ جَذْوَةٍ مِّنَ النَّارِ لَعَلَّكُمْ تَصْطَلُونَ ﴿٢٩﴾
“Basi alipotimiza muda wake na akasafiri na ahali zake, aliona moto upande wa Mlima Tur. Akwaambia ahali zake: ngojeni! Mimi nimeona moto, labda nitawaletea kutoka habari au kijinga cha moto ili mpate kuota” (28:29)
Musa alitokea Madyan kuelekea Misr akiwa na mkewe. Njiani alihitajia moto. Wapokezi wanasema: Musa alipotea njia katika usiku wa kusi kukiwa na baridi na giza. Mkono ukashindwa kupekecha moto na huku mkewe akiwa na uchungu wa kuzaa.
Wakati akiwa amedangana hana la kufanya mara akaona moto kwa mbali, akafurahi na akawaambia watu wake, huenda faraja inakuja katikati ya dhiki, kaeni niende kwenye moto nitawaletea moto muote au nipate habari za faraja.
Basi alipoufikia akaitwa: Ewe Musa! Hakika Mimi ndiye Mola wako Musa(a.s) alikurubia kile alichofikiria kuwa ni moto; mara ukawa ni nuru adhimu inayoangaza zaidi ya jua; huku sauti ya kuogofya ikisema:
Hakika mimi ndiye Mola wako, basi vua viatu vyako kwa adabu na kun- yenyekea. Kwanihakika wewe uko katika bonde takatifu la Tuwa, mahali palipotwahara palipobarikiwa, ilipojionyesha nuru ya Mungu na katika anga yake ikainuka sauti ya utukufu na ukamilifu.
Musa aliona nuru na akasikia sauti; hakuna kitu kingine zaidi ya hivyo. Imam Aliy(a.s) anasema:
“Hakika Mwenyezi Mungu (s.w.t) haidirikiwi na hisia wala kukisiwa na watu…ambaye alizungumza na Musa na akamuonyesha ishara zake tukufu bila ya viungo wala zana yoyote.
Nami nimekuteua, basi sikiliza unayopewa wahyi.
Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) hawateui kwa wahyi wake isipokuwa wale wasafi walio na uaminifu nao. Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7:144). Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) akabainisha kuwa dini aliyompia wahyi Musa inasimamia kwenye misingi mitatu:
Umoja wa Mungu:Hakika mimi ndiye Mwenyezi Mungu, hapana Mungu isipokuwa mimi.
Ikhalsi ya Mungu katika ibada:Basi niabudu mimi na usimamishe swala kwa ajili ya kunikumbuka Ufufuo:Hakika saa (kiyama) itakuja, nimekaribia kuificha, ili kila nafsi ilipwe kwa iliyoyafanya.
Makusudio ya kukurubia kuificha ni kuificha. Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameficha kujulikana saa ya kiyama kwa waja wake, ili watarajie kufika kwake wakati wowote, waweze kuwa na hofu nayo na waifanyie kazi, kisha walipwe malipo yao bila ya kudhulumiwa kitu.
Kwa hiyo asikukengeushe nayo yule asiyeiamni na akafuata hawa yake ukaangamia.
Dhamiri ya ‘nayo’ inarudia kwenye hiyo saa, sio swala, kwa sababu ndiyo iliyo karibu na jumla hiyo, Inawezekana kurudia kwenye zote mbili. Maana ni kuwa ewe Musa, shikilia kuamini ufufuo, hisabu na malipo na uyayafanyie kazi wala usifuate hawaa za wapinzani usije ukaangamia kama watavyoangamia wao. Tumeshawahi kudokeza kuwa inafaa kwa mkuu kumkataza aliye chini yake, hata kama ni maasumu; kuongezea kuwa kukataza kitu hakufahamishi kuwa kuna uwezekanao wa aliyekatazwa kukifanya.
وَمَا تِلْكَ بِيَمِينِكَ يَا مُوسَىٰ ﴿١٧﴾
17. Nnini hicho kilicho mkononi mwako wa kuume ewe Musa?
قَالَ هِيَ عَصَايَ أَتَوَكَّأُ عَلَيْهَا وَأَهُشُّ بِهَا عَلَىٰ غَنَمِي وَلِيَ فِيهَا مَآرِبُ أُخْرَىٰ ﴿١٨﴾
18. Akasema: Hii ni fimbo yangu; ninaiegemea na ninawaangushia majani mbuzi na kondoo wangu; tena inanifaa kwa matumizi mengine.
قَالَ أَلْقِهَا يَا مُوسَىٰ ﴿١٩﴾
19. Akasema: Itupe ewe Musa!
فَأَلْقَاهَا فَإِذَا هِيَ حَيَّةٌ تَسْعَىٰ ﴿٢٠﴾
20. Akaitupa mara ikawa nyoka anayekwenda mbio.
قَالَ خُذْهَا وَلَا تَخَفْ سَنُعِيدُهَا سِيرَتَهَا الْأُولَىٰ ﴿٢١﴾
21. Akasema: ichukue wala usihofu! Tutairudisha hali yake ya kwanza
وَاضْمُمْ يَدَكَ إِلَىٰ جَنَاحِكَ تَخْرُجْ بَيْضَاءَ مِنْ غَيْرِ سُوءٍ آيَةً أُخْرَىٰ ﴿٢٢﴾
22. Na uambatanishe mkono wako na ubavu wako, utatoka mweupe pasipokuwa na ubaya wowote. Hiyo ni ishara nyingine.
لِنُرِيَكَ مِنْ آيَاتِنَا الْكُبْرَى ﴿٢٣﴾
23. Ili tukuonyeshe baadhi ya ishara zetu kubwa.
اذْهَبْ إِلَىٰ فِرْعَوْنَ إِنَّهُ طَغَىٰ ﴿٢٤﴾
24. Nenda kwa Firauni; kwani hakika yeye amepetuka mpaka.
قَالَ رَبِّ اشْرَحْ لِي صَدْرِي ﴿٢٥﴾
25. Aksema: Ewe Mola wangu! Nikunjulie kifua changu
وَيَسِّرْ لِي أَمْرِي ﴿٢٦﴾
26. Na unifanyie wepesi jambo langu.
وَاحْلُلْ عُقْدَةً مِّن لِّسَانِي ﴿٢٧﴾
27. Na ulifungue fundo lilo katika ulimi wangu.
يَفْقَهُوا قَوْلِي ﴿٢٨﴾
28. Wapate kufahamu kauli yangu.
وَاجْعَل لِّي وَزِيرًا مِّنْ أَهْلِي ﴿٢٩﴾
29. Na nipe waziri katika watu wangu
هَارُونَ أَخِي ﴿٣٠﴾
30. Harun Ndugu yangu.
اشْدُدْ بِهِ أَزْرِي ﴿٣١﴾
31. Niongeze nguvu zangu kwaye
وَأَشْرِكْهُ فِي أَمْرِي ﴿٣٢﴾
32. Na umshirikishe katika jambo langu.
كَيْ نُسَبِّحَكَ كَثِيرًا ﴿٣٣﴾
33. Ili tukutakase sana
وَنَذْكُرَكَ كَثِيرًا ﴿٣٤﴾
34. Na tukukumbuke sana
إِنَّكَ كُنتَ بِنَا بَصِيرًا ﴿٣٥﴾
35. Hakika wewe unatuona.
NA NINI HICHO KILICHO MKONONI MWAKO WA KUUME EWE MUSA?
Aya 17 – 35
Na nini hicho kilicho mkononi mwako wa kuume ewe Musa?
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamuuliza Musa amueleze kilicho mkononi mwake, huku akiwa anajua zaidi kuliko huyo Musa mwenyewe, Kwa hiyo hapo kuna siri, Ndio kuna siri kubwa kwenye fimbo hii, aliyotaka kuidhi- hirisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa Musa, ambayo ni kugeuka fimbo kuwa nyoka.
Ikiwa tone la manii lina viini vya binadamu, yai lina viini vya kuku na mbengu kuwa na viini vya mimea, lakini mti huu mkavu hauna viini vyovyote vya nyoka, hata hivyo umegeuka nyoka! Hii ndio siri ya muujiza; na hapa ndio tunapata tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
يُخْرِجُ الْحَيَّ مِنَ الْمَيِّتِ ﴿٩٥﴾
“Humtoa aliye hai katika maiti” Juz; 7 (6:95)
Razi anasema: Anayetaka kutoa kitu kikuu kutokana na kidogo, kwanza hukionyesha hadharani kile kidogo huku akiseam: nini hiki? Nao waseme: ni kadha, Hapo ndio anaanza kazi yake. Ndio hivi alivyofanya Mwenyezi Mungu (s.w.t) na Musa.
Alimuuliza kuhusu fimbo, alipokiri kuwa ni mti tu mkavu, Mwenyezi Mungu akaugeuza nyoka mkubwa, akaipigia bahari ikapasuka na jiwe likatoka chemchem.
Jambo la kushangaza ni kwamba Sheikh Maraghi alinukuu ibara hii ya Razi bila ya kuashiria chimbuko lake; kama ilivyo kawaida yake, katika tafsiri yake kuanzia mwanzo hadi kwenye Aya hii. Na ninadhani inayofu- atia pia ni hivi hivi; sawa na mpangilio wa Nidhamuddin Naysabury, katika tafsiri yake Gharaibulqur’an wa raghaibulfurqan.
Akasema: Hii ni fimbo yangu; ninaiegemea na ninawaangushia majani mbuzi na kondoo wangu; tena inanifaa kwa matumizi mengine.
Tumesoma elimu ya maani na bayan, katika kitabu Al-mutawwal cha Taftazaniy. Tulipofika kwenye mlango wa kufupisha, kurefusha na kulinganisha sawa, mwenye kitabu alitaja faida za kurefusha; zikiwa ni pamoja na: kufafanua, kusisitiza kwa kukaririka na ladha ya elimu. Kisha Ustadh akapiga mfano wa mazungumzo pamoja na mpendwa, kutokana na riwaya ya baadhi ya wategemezi.
Kwa ufupi ni kwmba mpokezi aliota ndoto ya kuonana na Muhammad(s.a.w.w) na Musa bin Imran(a.s) . Akamsikia Musa akimlaumu Muhammad huku akimwambia: miongoni mwa mambo uliyasema ni: Ulama wa uma wangu ni kama manabii wa Bani Israil. Hii ndio hadhi yetu kwako ewe Abulqasim sawa na ulama wa uma wako?
Muhammad akataka kumthibitishia, akamwambia: hivi sasa nitakukutan- isha na mmoja wa ulama wa uma wangu ili umjaribu uone usahihi wa niliyoyasema, Musa akamwambia sawa. Akamkutanisha na mwanachuoni Ardabeliy. Musa akamuuliza: waitwaje? Akajibu: Mimi ni Ahmad na baba yangu jina lake ni Muhammad, ninatoka Ardabeliy, nimesoma Najaf na mwalimu wangu ni Shahiduthani.
Musa akamwambia: ni yanini yote hayo? Nimekuuliza jina lako tu, wewe waniambia jina lako, la baba yako, mji wako na mwalimu wako! Ardabeliy akamwambia: wewe si uliulizwa na Mwenyezi Mungu kuhusu kilicho mikononi mwako na ukasema:“Hii ni fimbo yangu; ninaiegemea na ninawaangushia majani mbuzi na kondoo wangu; tena inanifaa kwa matumizi mengine na ingetosha kusema hii ni fimbo yangu tu.”
Hapo Musa akamgeukia Muhammad na kumwambia huku akiomba msamaha: wewe unajua zaidi uliyoyasema.
Ustadh aliongezea riwaya hii kwa kusema: namna hii mtu hurefusha maneno pamoja na yule anayempenda si kwa lolote ila ni kwa kumfungulia moyo na bashasha. Miongoni mwa hayo ni kauli ya malenga mashuhuri anayeitwa Mutanabbi: Maswali mengi hutokana na shauku na mengi majibu ni kwa kutunuku
Akasema: itupe ewe Musa! Akiatupa mara ikawa nyoka anayekwenda mbio, Akasema: ichukue wala usihofu! Tutairudisha hali yake ya kwanza.
Musa alipatwa na hofu kutokana na mandhari haya yakutisha na akarudi nyuma; kama inavyofahamisha Aya isemayo:
فَلَمَّا رَآهَا تَهْتَزُّ كَأَنَّهَا جَانٌّ وَلَّىٰ مُدْبِرًا وَلَمْ يُعَقِّبْ يَا مُوسَىٰ لَا تَخَفْ إِنِّي لَا يَخَافُ لَدَيَّ الْمُرْسَلُونَ ﴿١٠﴾
“Alipoiona inayumba kama nyoka akageuka kurudi nyuma wala hakungoja. Ewe Musa! Usikhofu hakika hawakhofu mbele yangu mitume (27:10).
Yaani Mitume hawaogopi kwa yale ninayowaamrisha, kwa vile wanajua kuwa siwaamrishi isipokuwa kheri wala siwakatazi isipokuwa shari, Mara tu, Musa alipoweka mkono wake kwenye nyoka iligeuka fimbo.
Na uambatanishe mkono wako na ubavu wako, utatoka mweupe pasipokuwa na ubaya wowote. Hiyo ni ishara nyingine, Ili tukuonyeshe baadhi ya ishara zetu kubwa.
Katika Aya hii Mwenyezi Mungu (s.w.t) Amesema uambatanishe mkono na ubavu wako. Na mahali pengine akasema:
وَأَدْخِلْ يَدَكَ فِي جَيْبِكَ ﴿١٢﴾
“Na ingiza mkono wako kwenye uwazi wa vazi lako” (27:12).
Pasipokuwa na ubaya wowote ni kutokuwako madhara.
Mkono wa Musa ulikuwa wa rangi ya kahawiya, kwa sbabu yeye alikuwa wa rangi hiyo. Alipouingiza mkono wake na akautoa, ulitoa mwanga kama wa jua. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 9 (7:108).
Nenda kwa Firauni; kwani hakika yeye amepetuka mpaka.
Mwenyezi Mungu alimwamrisha Musa kumkemea Firauni na dhulma yake, akiwa ni mwenye nguvu na uwezo; kiasi cha kujigamba na kusema:
أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٤﴾
“Mimi ndiye Mola wenu Mkuu” (79:24),
مَا عَلِمْتُ لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرِي ﴿٣٨﴾
“Simjui kwa ajili yenu Mungu asiyekuwa mimi” (28: 38) tena akmwambia Musa:
قَالَ أَلَمْ نُرَبِّكَ فِينَا وَلِيدًا وَلَبِثْتَ فِينَا مِنْ عُمُرِكَ سِنِينَ ﴿١٨﴾
“Je hatukukulea kwetu ukiwa mtoto na ukakaa kwetu miaka ya umri wako?” (26:18).
Musa alikulia katika kasri ya Firauni kama yatima; kisha akawa mkimbizi akila majani. Imam Aliy(a.s) anasema katika Nahjulbalagha: Rangi ya kijani ya majani ilikuwa ikionekana kwenye ngozi ya tumbo lake kwa wembamba wake na kutenga na nyama yake.
رَبِّ إِنِّي لِمَا أَنزَلْتَ إِلَيَّ مِنْ خَيْرٍ فَقِيرٌ ﴿٢٤﴾
Mola wangu! Hakika mimi ni muhitaji wa kheri utakayonitermshia” (28:24).
Imam anasema:“Wallah hakumuomba isipokuwa mkate wa kula tu” na Mungu alimwitikia maombi yake, akapata mkate kwa Shuayb kwa kufanya kazi ya kuchunga wanyama wake.
Hii ndiyo dunia ya Musa bin Imran: Wakati wa kuzaliwa kwake aliwekwa kwenye sanduku, akatupwa majini. Akakulia kwenye nyumba ya Firauni akiwa yatima; akawa mkimbizi akila mimea ya ardhi, kisha akawa mchunga mbuzi na kondoo.
Mtu huyu oheahe asiye na chochote anaenda kumkabili kigogo mwenye kila kitu, itawezekana kweli? Ndio iliwezekana! Alikwenda Musa kwa Firauni na wakuu wake na fimbo yake ikameza vyote walivyovizua na mkono wake ulioonyesha ukweli wake na usafi wake. Mbali ya fimbo na mkono Musa aliomba mambo mengine zaidi, kama ifuatavyo:-
Ewe Mola wangu! Nikunjulie kifua changu.
Inajulikana kuwa Musa alikuwa ni mwepesi wa kukasirika kwa jambo linalomchukiza. Haya yametamkwa na Qur’an. Imeeleza kuwa alishika ndevu za nduguye Haruna na kichwa chake, pale wana wa Israil walipoabudu ndama. Akampiga ngumi mtu wa upande wa Firauni na kum- maliza na akahalifu amri ya mja mwema baada ya kumwambia kuwa nitavumilia.
Hakuna mwenye shaka kwamba matatizo aliyopamabana nayo Musa katika maisha yake yameacha athari ya hasira hizi za harakaharka; Kwa kuwa Utume unahitajia uvumilivu wa machukivu na tabu, ndio akamuomba Mola wake awe mpole na mkunjufu.
Na unifanyie wepesi jambo langu.
Yaani unisaidie, ewe Mola wangu, kwa masaada na tawfiki ya kuweza kutekekeleza yale uliyonikalifisha na unifanye niweze kuyabeba. Hakuna kitu cha kheri kinachotimia kwa mtu, isipokuwa kwa tawfiki na msaada wa Mwenyezi Mungu; hata akiwa na nyenzo zote.
Na ulifungue fundo lilo katika ulimi wangu; Wapate kufahamu kauli yangu
Aya hii tukiunganisha na ile isemayo:
وَأَخِي هَارُونُ هُوَ أَفْصَحُ مِنِّي لِسَانًا ﴿٣٤﴾
“Na ndugu yangu Harun ni fasaha zaidi kuliko mimi kwa ulimi” (28:34).
Na pia:
وَلَا يَكَادُ يُبِينُ ﴿٥٢﴾
“Wala hawezi kusema waziwazi” (43:52).
Tukiunganisha Aya zote hizi tatu, tunapata ushahidi wa yule asemaye kwamba Musa alikuwa na kigugumizi. Ama kuwa kigugumizi hiki ni cha maumbile au kilitokana na kaa la moto alilolitia mdomoni, pale alipojaribiwa na Firauni utotoni, ujuzi wake uko kwa Mola wangu.
Kwa hakika Aya hii inaonyesha kuwa ufasaha wa ulimi na kubainisha maneno ni katika sifa kuu na neeema kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa mtu:
خَلَقَ الْإِنسَانَ ﴿٣﴾ عَلَّمَهُ الْبَيَانَ ﴿٤﴾
“Amemuumba mtu akamfundisha kusema” (55:3-4).
Imam Aliy(a.s) anasema:“Mtu si mtu lau si ulimi (kuzungumza); isipokuwa mnyama mwenye kupuuzwa au picha”
Na nipe waziri katika watu wangu, Harun ndugu yangu, niongeze nguvu zangu kwaye na umshirikishe katika jambo langu, ili tukutakase sana na tukukumbuke sana, Hakika wewe unatuona.
Katika Majmaul-bayan imeelezwa kuwa Harun alikuwa ni nduguye Musa kwa baba na mama, na alikuwa ni mkubwa wake kwa miaka mitatu. Alikuwa mwenye kimo, mwenye mwili mwangavu, mwenye nyama nyingi na mfasaha wa kuzungumza. Ni kutokana na sifa hizi ndio Musa akamuomba Mola wake amfanye nduguye Harun ni mshirika wake katika utume. Mwenye Majmaul-bayan anasema kuwa alikufa kabla ya kufa nduguye Musa kwa miaka mitatu.
Kwa vyovyote ilivyo ni kuwa mwenye ujumbe hana budi kuwa na mwen- za msaidizi mwenye ikhlasi na atakayejitolea muhanga. Kwani unabii, katika hakika yake, ni habari inayotoka kwa Mungu anayoinukuu mtu; sio nguvu tekelezi au kusema ‘kuwa’ na ikawa.
Nabii ni mtu asiyeweza kujizuia na madhara wala kujiletea manufaa. Utekelezaji wake unatumia nyenzo zilezile anazozitumia mumin na asiyekuwa mumin.
Hakuna tofauti isipokuwa ni habari za kutoka kwa Mungu na kwamba Mwenyezi Mungu anamchukua mtu aliye mtukufu zaidi na kumteua mwenye sifa nzuri zaidi. Lakini sifa takatifu hazifanyi mwenye nazo asiwe na haja na desturi ya maumbile. Hapana! Manabii na wasiokuwa manabii, wote wanahitaji nyenzo.
Nabii anahitajia tabibu akiwa mgonjwa; sawa na asiyeamini Mungu na siku ya mwisho anavyohitajia. Vile vile anahitaji nguvu; kama anavyohitajia mtu mwingine. Mitume wote waliudhiwa na wengi wao wakuawa.
Hapa inatubainikia kujiingiza sana hadi kupotea kwa yule anayesema kuwa Muhammad(s.a.w.w) ndiyo hakika ambayo Mwenyezi Mungu ameiumbia viumbe na ni roho ambayo imeenea kwenye viumbe vyote vya juu na vya chini:
وَلَوْ كُنتُ أَعْلَمُ الْغَيْبَ لَاسْتَكْثَرْتُ مِنَ الْخَيْرِ وَمَا مَسَّنِيَ السُّوءُ إِنْ أَنَا إِلَّا نَذِيرٌ وَبَشِيرٌ لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿١٨٨﴾
“Na lau kama ningelijua ghaibu ningelijizidishia kheri nyingi, wala isingelinigusa dhara. Mimi si chochote ila ni mwonyaji na mtoaji bishara kwa watu wanaoamini.” Juz: 9 (7:188)
Hii ndio hakika ya utume: kuonya na kuleta bishara. Anapopatikana muonyaji na mbashiri akiwa pamoja na msaidizi, basi kuongoza kutakuwa na nguvu ya hoja. Ni kwa ajili hii ndio maana Musa akamuomba Mola wake ampe nguuvu kwa ndugu yake.
Kwa mnasaba huu itakuwa ni vizuri tutaje aliyoyasema W.L. Dewarnet kuhusu Muhammad katika ensaiklopidia yake ya Historia ‘Kisa cha maendeleo katika ulimwengu:’ “Maskani zote alizowahi kuishi Muhammad zilikuwa na upana usiozidi hatua 12 na kwenda juu hatua zisizozidi 8. Dari yake ilikuwa ya miti ya mitende, milango yake ikitokana na manyoya ya mbuzi au ya ngamia. Tandiko lake lilitandikwa ardhini na mto wake ulikwa wa ndifu.
Alikuwa akirekebisha mwenyewe viatu vyake na nguo zake, akiwasha moto, kufagia nyumba, kukama maziwa ya mbuzi, kununua chakula chake sokoni na akila kwa mkono na kuramba vidole vyake. Chakula chake kikuu kilikuwa ni tende na mkate wa shairi. Maziwa na asali ndio ilikuwa anasa yake baadhi ya wakati”
Hivyohivyo ilimtokea Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) . Suyuti, katika Durrilmanthur anasema wakati wa kufasiri: ‘Ewe Mola wangu! Nikunjulie kifua changu “Ametoa Hadith Ibn Mardawyh, Khatib na Ibn Asakir kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alisema:
Ewe Mola wangu! Hakika mimi ninakuomba aliyokuomba ndugu yangu Musa kuwa unikunjulie kifua changu, ufanye wepesi jambo langu na unifungue fundo lilo katika ulimi wangu na nipe waziri katika watu wangu, Aliy ndugu yangu, niongeze nguvu zangu kwaye na umshirikishe katika kazi yangu, ili tukutakase sana na tukukumbuke sana, Hakika wewe unatuona.
Amesema Muslim katika Sahihi yake Juz: 2 uk. 108, chapa ya 1348 AH: Hakika Mtume alimwambia Aliy: Je, huridhii kuwa wewe kwangu uko katika daraja ya Harun na Musa? Katika Juz. 1 ya Musnad Ahmad bin Hambal: Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) aliwaita Hassan wawili (Hassan na Hussein) kwa kumfuata Harun katika kuwaita wanawe Shubbar na Shabir, yenye maana ya Hassan na Hussein.
8
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
قَالَ قَدْ أُوتِيتَ سُؤْلَكَ يَا مُوسَىٰ ﴿٣٦﴾
36. Akasema: Hakika umepewa maombi yako ewe Musa
وَلَقَدْ مَنَنَّا عَلَيْكَ مَرَّةً أُخْرَىٰ ﴿٣٧﴾
37. Na hakika tulikwisha kuneemesha mara nyingine
إِذْ أَوْحَيْنَا إِلَىٰ أُمِّكَ مَا يُوحَىٰ ﴿٣٨﴾
38. Pale tulipompa wahyi mama yako yale yaliyotolewa wahyi
أَنِ اقْذِفِيهِ فِي التَّابُوتِ فَاقْذِفِيهِ فِي الْيَمِّ فَلْيُلْقِهِ الْيَمُّ بِالسَّاحِلِ يَأْخُذْهُ عَدُوٌّ لِّي وَعَدُوٌّ لَّهُ وَأَلْقَيْتُ عَلَيْكَ مَحَبَّةً مِّنِّي وَلِتُصْنَعَ عَلَىٰ عَيْنِي ﴿٣٩﴾
39. Kwamba mtie katika kisanduku kisha kitupe mtoni na mto utamfikisha ufukweni. Atamchukua adui yangu na adui yake. Na nimekutilia mapenzi kutoka kwangu na ili ulelewe machoni mwangu
إِذْ تَمْشِي أُخْتُكَ فَتَقُولُ هَلْ أَدُلُّكُمْ عَلَىٰ مَن يَكْفُلُهُ فَرَجَعْنَاكَ إِلَىٰ أُمِّكَ كَيْ تَقَرَّ عَيْنُهَا وَلَا تَحْزَنَ وَقَتَلْتَ نَفْسًا فَنَجَّيْنَاكَ مِنَ الْغَمِّ وَفَتَنَّاكَ فُتُونًا فَلَبِثْتَ سِنِينَ فِي أَهْلِ مَدْيَنَ ثُمَّ جِئْتَ عَلَىٰ قَدَرٍ يَا مُوسَىٰ ﴿٤٠﴾
40. Dada yako alipokwenda na akasema: Je, niwajulishe mtu wa kuweza kumlea? Basi tukakurujesha kwa mama yako, ili macho yake yaburudike wala asihuzunike, Na ulimuua mtu nasi tukakuokoa katika dhiki. Na tukakujaribu kwa majaribio. Ukakaa miaka kwa watu Madyana. Kisha ukaja kama ilivyokadiriwa ewe Musa
وَاصْطَنَعْتُكَ لِنَفْسِي ﴿٤١﴾
41. Na nimekuchagua kwa ajili yangu.
Aya 36 – 41
Akasema: Hakika umepewa maombi yako ewe Musa, ya kukunjuliwa kifua, kufanyiwa wepesi kazi, kufunguka ulimi, kuongezewa nguvu kwa nduguyo na kushirikishwa kwenye utume pamoja nawe. Imam Aliy(a.s) anasema: “Kuwa kwenye lile usilolitaraji kuwa unalitarajia zaidi kuliko lile unalolitaraji. Kwani Musa Bin Imran alitoka akitafuta moto, akazungumza na Mwenyezi Mungu akarejea akiwa ni Mtume”
Na hakika tulikwisha kuneemesha mara nyingine.
Neema za Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwa Musa zilkuwa nyingi; miongoni mwazo ni hizi zifuatazo:-
Pale tulipompa wahyi mama yako yale yaliyotolewa wahyi. Kwamba mtie katika kisanduku kisha kitupe mtoni na mto utamfikisha ufukweni. Atamchukua adui yangu na adui yake. Na nimekutilia mapenzi kutoka kwangu na ili ulelewe machoni mwangu
Makusudio ya wahyi hapa ni ilham – msukumo wa kufanya jambo. Macho ya Mwenyezi Mungu ni ulinzi wake.
Firauni alikuwa akimchinja kila anayezaliwa wa kiume katika waisrail na akizaliwa wa kike humfanya mjakazi. Mke wa Imran alipomzaa Musa alihofia Firauni, ndipo Mwenyezi Mungu akampa ilhamu ya kumweka kwenye sanduku kisha alitupe kwenye mto Nile, naye akafanya. Mungu akampa uthabiti wa moyo, Mto Nile ukalibebea sanduku hadi ufukweni. Inasemekana kuwa wajakazi wa Asiya, Mke wa Firaun, walitoka kwenda kuoga, wakakuta sanduku, wakalichukua. Mara tu mke wa Firauni alipolifungua na kuona mtoto, Mungu alimtia mahaba katika moyo wake:
وَقَالَتِ امْرَأَتُ فِرْعَوْنَ قُرَّتُ عَيْنٍ لِّي وَلَكَ لَا تَقْتُلُوهُ عَسَىٰ أَن يَنفَعَنَا أَوْ نَتَّخِذَهُ وَلَدًا وَهُمْ لَا يَشْعُرُونَ ﴿٩﴾
“Na mkewe Firauni akasema: Atakuwa kibirudisho cha macho kwangu na kwako. Msimuuwe! Huenda akatufaa au tumpange kuwa mtoto wetu” (28:9).
Kwa hiyo Faruni akambakisha na akalelewa katika kasri yake akilindwa na Mwenyezi Mungu.
Dada yako alipokwenda na akasema: Je, niwajulishe mtu wa kuweza kumlea? Basi tukakurujesha kwa mama yako, ili macho yake yaburudike wala asihuzunike.
Mwenyezi Mungu alitaka Musa arejee kwa mama yake, ili asiwe mbali naye na asiwe na wasiwasi, Mungu akitaka jambo, huliandalia sababu zake, Alizuwiya matiti yote yasiweze kumnyonyesha Musa, kiasi ambacho Firauni alihangaika.
Akaenda dada yake kwenye kasri ya Firauni na kusema mimi nitawafahamisha atakayemnyonyesha. Ndio akaenda na mama yake akakubali matiti yake, Firauni akamkabidhi na akampa ujira wake.
Na ulimuua mtu nasi tukakuokoa katika dhiki.
Siku moja Musa alikuwa akipita njiani, akawaona watu wawili wakipigana; mmoja ni wa upande wa Firaun na mmoja ni wa upande wake. Huyu wa upande wake akataka usaidizi kwa Musa, Akampiga ngumi yule mpin- zani, bila ya kukusudia kumuua, lakini akamuua, Musa akahofia kulipiziwa kisasi; Mwenyezi Mungu akamuondolea dhiki hiyo ya kisasi.
Haya yameashiriwa na Aya isemayo:
فَوَجَدَ فِيهَا رَجُلَيْنِ يَقْتَتِلَانِ هَـٰذَا مِن شِيعَتِهِ وَهَـٰذَا مِنْ عَدُوِّهِ فَاسْتَغَاثَهُ الَّذِي مِن شِيعَتِهِ عَلَى الَّذِي مِنْ عَدُوِّهِ فَوَكَزَهُ مُوسَىٰ فَقَضَىٰ عَلَيْهِ ﴿١٥﴾
“Akakuta humo watu wawili wanapigana – mmoja ni katika kundi lake na mwengine ni katika maadui zake, Yule mwenzake akamtaka msaada dhidi ya adui, Musa akampiga ngumi akammaliza.” (28:15).
Na tukakujaribu kwa majaribio.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) humjaribu mja wake kwa furaha na dhiki. Mwenye kushukuru hayo na akavumilia haya, humkurubisha na kumpa thawabu. Na ambaye hazijali neema na akakufuru wakati wa shida, Mwenyezi Mungu humweka mabali na rehema yake. Mwenyezi Mungu (s.w.t) Alimjaribu Musa kwa aina nyingi ya shida na misukosuko, akampata ni mwenye kuvumilia na mwenye kumkumbuka Mungu, ndipo Mwenyezi Mungu akamtukuza kwa utume na kamuinua daraja ya juu.
Ukakaa miaka kwa watu Madyana
Hapo ni baada ya kuchunga wanyama wa Shuayb, kama ilivyoashiria kauli yake Mwenyezi Mungu:
فَإِنْ أَتْمَمْتَ عَشْرًا فَمِنْ عِندِكَ ﴿٢٧﴾
“Kama ukitimiza kumi ni hiyari yako” (28:27)
Na aliitimiza kumi, kama inavyoelezwa katika baadhi ya riwaya.
Kisha ukaja kama ilivyokadiriwa ewe Musa.
Umekuja mahali hapa, kwenye jangwa takatifu la Tuwa; umekuja wakati ule alioukadiria Mwenyezi Mungu kukutuma wewe kwa utume.
Na nimekuchagua kwa ajili yangu.
Yaani nimekuchagua kwa ajili ya wahyi wangu na risala yangu. Kutegemezwa Musa kwa Mwenyezi Mungu ni ukomo wa utukufu na hes- hima; ambapo inaashiria kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amemjalia ni katika watu wake mahususi.
اذْهَبْ أَنتَ وَأَخُوكَ بِآيَاتِي وَلَا تَنِيَا فِي ذِكْرِي ﴿٤٢﴾
42. Nenda wewe na nduguyo pamoja na ishara zangu, wala msichoke kunikumbuka.
اذْهَبَا إِلَىٰ فِرْعَوْنَ إِنَّهُ طَغَىٰ ﴿٤٣﴾
43. Nendeni kwa Firauni, hakika yeye amepituka mipaka.
فَقُولَا لَهُ قَوْلًا لَّيِّنًا لَّعَلَّهُ يَتَذَكَّرُ أَوْ يَخْشَىٰ ﴿٤٤﴾
44. Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa.
قَالَا رَبَّنَا إِنَّنَا نَخَافُ أَن يَفْرُطَ عَلَيْنَا أَوْ أَن يَطْغَىٰ ﴿٤٥﴾
45. Wakasema: ewe Mola wetu! Hakika sisi tunaogopa asije akapindukia mipaka juu yetu au kufanya jeuri.
قَالَ لَا تَخَافَا إِنَّنِي مَعَكُمَا أَسْمَعُ وَأَرَىٰ ﴿٤٦﴾
46. Akasema: msiogope! Hakika mimi niko pamoja nanyi. Nasikia na ninaona.
فَأْتِيَاهُ فَقُولَا إِنَّا رَسُولَا رَبِّكَ فَأَرْسِلْ مَعَنَا بَنِي إِسْرَائِيلَ وَلَا تُعَذِّبْهُمْ قَدْ جِئْنَاكَ بِآيَةٍ مِّن رَّبِّكَ وَالسَّلَامُ عَلَىٰ مَنِ اتَّبَعَ الْهُدَىٰ ﴿٤٧﴾
47. Basi mwendeeni na mumwambie: hakika sisi ni wajumbe wa Mola wako, basi tuachie wana wa israil wala usiwaadhibu. Tumekuletea ishara itokayo kwa Mola wako, Na amani itakuwa juu ya aliyefuata uongofu.
إِنَّا قَدْ أُوحِيَ إِلَيْنَا أَنَّ الْعَذَابَ عَلَىٰ مَن كَذَّبَ وَتَوَلَّىٰ ﴿٤٨﴾
48. Hakika tumepewa wahyi kwamba adhabu itampata anayekadhibisha na akapu- uza.
Aya 42-48
Nenda wewe na nduguyo pamoja na ishara zangu, wala msichoke kunikumbuka.
Makusudio ya ishara hapa ni miujiza, amabayo ni fimbo, mkono mweupe na miujiza mingineyo, tuliyoiashiria katika Juz. 15 (17:101). Maana ya msichoke kunikumbuka ni msipuuze risala yangu na kukumbusha amri yangu na makatazo yangu.
Nendeni kwa Firauni, hakika yeye amepituka mipaka.
Nendeni ni kusisitiza ile kauli ya ‘nenda wewe na nduguyo.’ Umetangulia mfano wa Aya hii katika Aya ya 23 ya sura hii tuliyo nayo.
Mwambieni maneno laini, huenda akazingatia au akaogopa.
Kama wenye mashirika ya ukandamizaji watazingatia na kuogopa, basi Firauni angelizingatia na kuogopa.
Aya hii inapangilia mfumo wa kutoa mwito wa dini ya Mwenyezi Mungu. Kwa usahihi zaidi; inapanga mfumo wa kukinaisha haki. Mfano wake ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ ﴿١٢٥﴾
“Waite kwenye njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora.” Juz. 14(16:125).
Mawaidha mazuri ni kujua mwenye hatia, makosa yake na mpotevu kujua ubaya wake na kujiona kuwa yuko mbali na haki na hali halisi ya mambo:
وَقَالُوا لَوْ كُنَّا نَسْمَعُ أَوْ نَعْقِلُ مَا كُنَّا فِي أَصْحَابِ السَّعِيرِ ﴿١٠﴾
“Na watasema: lau tungelikuwa tunasikia au kuwa na akili, tusingelikuwa katika watu wa motoni” (67:10)
Sharti la kwanza la mawaidha mazuri ni kutotaka lolote anayetoa mwaid- ha, zaidi ya kutengeneza. Kwamba lengo la kwanza na la mwisho liwe ni kuongoza na kurekebisha.
Sharti la pili ni kuwa mawaidha kwa kauli laini. Miongoni mwa aliyoyasema Musa kwa Firauni ni: Je, unapenda kujitakasa? Nami nitakuongoza kwa Mola wako upate kumcha.(79:19).
Wakasema: Ewe Mola wetu! Hakika sisi tunaogopa asije akapindukia mipaka juu yetu au kufanya jeuri.
Ewe Mola wetu unajua ubabe wa Firauni na kwamba hakuna anayeweza kumzuia akiamrisha tuuawe kabla hata hajasikia dalili na hoja tutaka- zomwambia, Je unaweza kutuongeza kitu kitakachohakikisha usalama wetu?
Akasema: msiogope! Hakika mimi niko pamoja nanyi. Nasikia na ninaona.
Mimi ninadhamini usalama wenu, ‘Mwenyezi Mungu ni tosha wa kuhi- fadhi na kunusuru’ Unaweza kuuliza kuwa dhamiri ya wakasema: ni ya wawili, Musa na Harun, na inajulikana kuwa Harun hakuwa na Musa katika majibizano, sasa je, kuna wajihi gani wa hilo?
Baadhi ya wafasiri wamejibu kuwa kauli hii ilikuwa ni ya Musa kwa kusema na ya Harun kwa kihali; Kwa sababu Harun anamfuata Musa. Inawezekana kauli hii inatokana na wote wawili pamoja baada ya kuondoka Musa kwenda Misr na kuungana na nduguye, kabla hawajakwenda kwa Firani. Ni kawaida ya Qur’an kuacha maneno ambayo yatafahamika kutokana na mazingira au na maneno mengine.
Basi mwendeeni na mumwambie: hakika sisi ni wajumbe wa Mola wako, basi tuachie wana wa israil wala usiwaadhibu kwa kuwachukua mateka, kuwadhalilisha, kuwachinja watoto wao wa kiume na kuwatumia watoto wao wa kike. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz.9 (7:104 –105).
Tumekuletea ishara itokayo kuwa Mola wako, kwa dalili za kutosha na hoja mkataa juu ya ukweli wetu.
Na amani itakuwa juu ya aliyefuata uongofu.
Uingofu ni dini ya Mwenyezi Mungu na amani ni kusalimika na adhabu yake. Yaani mwenye kuingia dini ya Mwenyezi Mungu amesalimika na adhabu ya kuungua.
Hakika tumepewa wahyi kwamba adhabu itampata anayekadhibisha na akapuuza.
Ni makemeo na maonyo kwa Firauni kuwa ataangamia na kubomoka kama atampuuz Musa na Harun kwa kuukana utume wao na kuenedelea kwenye upotevu wake na jeuri yake.
قَالَ فَمَن رَّبُّكُمَا يَا مُوسَىٰ ﴿٤٩﴾
49. Akasema: Basi Mola wenu ni nani ewe Musa?
قَالَ رَبُّنَا الَّذِي أَعْطَىٰ كُلَّ شَيْءٍ خَلْقَهُ ثُمَّ هَدَىٰ ﴿٥٠﴾
50. Akasema: Mola wetu ni yule aliyekipa kila kitu umbo lake kisha akakiongoza
قَالَ فَمَا بَالُ الْقُرُونِ الْأُولَىٰ ﴿٥١﴾
51. Akasema Nini hali ya karne za mwanzo?
قَالَ عِلْمُهَا عِندَ رَبِّي فِي كِتَابٍ لَّا يَضِلُّ رَبِّي وَلَا يَنسَى ﴿٥٢﴾
52. Akasema: Elimu yake iko kwa Mola wangu katika Kitabu, Mola wangu hapotei wala hasahau.
الَّذِي جَعَلَ لَكُمُ الْأَرْضَ مَهْدًا وَسَلَكَ لَكُمْ فِيهَا سُبُلًا وَأَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَأَخْرَجْنَا بِهِ أَزْوَاجًا مِّن نَّبَاتٍ شَتَّىٰ ﴿٥٣﴾
53. Ambaye amewafanyia ardhi kuwa tandiko, Na akawapitishia humo njia, Na akateremsha kutoka mbinguni maji, Na kwayo tukatoa namna mbali mbali za mimea.
كُلُوا وَارْعَوْا أَنْعَامَكُمْ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّأُولِي النُّهَىٰ ﴿٥٤﴾
54. Kuleni na mchunge wanyama wenu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa wenye akili
مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ ﴿٥٥﴾
55. Kutokana nayo tumewaumba na humo tumewarudisha na kutoka humo tutawatoa mara nyingine.
وَلَقَدْ أَرَيْنَاهُ آيَاتِنَا كُلَّهَا فَكَذَّبَ وَأَبَىٰ ﴿٥٦﴾
56. Hakika tulimwonyesha ishara zetu zote, lakini alikadhibisha na akakataa.
Aya 49 -56
Akasema: Basi Mola wenu ni nani ewe Musa?
Musa na Harun walikwenda kwa Firauni kama walivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu, wakamwambia kuwa sisi ni mitume wa Mola wako, tumekujia na hoja na dalili kuthibitisha ukweli wetu. Basi ukiingia kwenye dini ya Mwenyezi Mungu utasalimika na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu na adhabu yake; vinginevyo, utakuwa miongoni mwa watakaoangamia.
Hii ilikuwa mara ya kwanza Firauni kusikia neno ‘Mola wako’ kwa sababu yeye hakubali kuwa kuna mola; kama anavyodai kuwa yeye ndiye Mola Mtukufu. Ndio maana akauliza: Ni nani huyo Mola aliyekutuma kwangu?
Akasema: Mola wetu ni yule aliyekipa kila kitu umbo lake kisha akakiongoza
Musa alimjibu Firauni swali lake, kuwa Mola wetu ni yule aliyeumba viumbe akavipa sura na akazifanya nzuri sura zake bila ya kuwa na msaidizi kwenye hilo. Ndiye ambaye amekifanya kila kiumbe kibakie na hali yake. Amesema Imam Aliy(a.s) : “Je, hamuangalii kile kidogo jinsi Mungu alivyokiumba na akapingilia vizuri umbile lake, akakiumbia usikizi na uoni na akakifanyia mifupa na nyama.
Ni kama kwamba Musa anamwambia Firauni: Hakika Mola ni yule aliyeumba vitu kutokana na kutokuwa na chochote. Sasa wewe ni wapi na wapi na huyu? Ni kama ilivyomtokea Ibrahim na Namrud:
قَالَ إِبْرَاهِيمُ فَإِنَّ اللَّـهَ يَأْتِي بِالشَّمْسِ مِنَ الْمَشْرِقِ فَأْتِ بِهَا مِنَ الْمَغْرِبِ فَبُهِتَ الَّذِي كَفَرَ ﴿٢٥٨﴾
“Ibrahim akasema: Hakika Mwenyezi Mungu hulichomoza jua mashariki, basi wewe lichomoze magharibi, Akafedheheka yule aliyekufuru” Juz; 3 (2:258)
Akasema – Firauni – Nini hali ya karne za mwanzo?
Karne za mwanzo anakusudia watu wa Nuh, A’d, Thamud na wengineo ambao walikuwa wakiabudu masanamu badala ya Mwenyezi Mungu. Firauni alitaka, kwa jawabu hili, kumrudi Musa, kwamba lau kungelikuwa na Mungu kwa sifa amabazo umezitaja, basi wangelimwabudu watu waliopita, na tunajua kuwa wao walikuwa wakiabudu masanamu.
Jawabu hili linajipinga lenyewe; Kwa sababu kutoa dalili ya kutokuweko Mungu kwa ibada ya masanamu, ni sawa na poponundu, na upofu wake, kupinga kuweko jua.
Akasema: Elimu yake iko kwa Mola wangu katika Kitabu; Mola wangu hapotei wala hasahau.
Musa alimjibu Firauni kuwa mimi sina ujuzi wa ghaibu mpaka nikupe habari za uma zilizopita. Mwenyezi Mungu peke yake ndiye mwenye ujuzi wa kila kitu na ujuzi wake daima hauingiliwi na mabadiliko wala kugeuka:
يَوْمَ يَبْعَثُهُمُ اللَّـهُ جَمِيعًا فَيُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا أَحْصَاهُ اللَّـهُ وَنَسُوهُ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ شَهِيدٌ ﴿٦﴾
“Siku atakapowafufua Mwenyezi Mungu awaambie yale waliyokuwa wakaiyatenda, Mwenyezi Mungu ameyadhibiti na wao wameyasahau, Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kushuhudia kila kitu” (58:6).
Unaweza kuuliza kuwa : Musa alikuwa na uhakika kuwa waabudu masanamu walikuwa katika upotevu, kwanini hakumwambia Firauni kuwa walikuwa kwenye upotevu na badala yake akamwambia Mwenyezi Mungu ndiye ajuye hali yao?
Jibu : Lau angelisema kuwa watu wa karne za kwanza walikuwa wapotevu, Firauni angelimtaka dalili ya kuwakinaisha waliopo au awe na hoja ambayo wasingeweza kuipinga na wakati huo Musa hakuwa nayo. Ndio maana akamjibu Firauni yale ambayo asingeyatakia dalili.
Ambaye amewafanyia ardhi kuwa tandiko.
Umekwishatangulia ufafanuzi wa kutandikwa ardhi na kufanywa kwake tandiko katika Juz.13 (13:3)
Na akawapitishia humo njia ya kufuatia matumizi yenu, Na akateremsha kutoka mbinguni maji; Na kwayo tukatoa namna mbali mbali za mimea
Umetangulia mfano wake katika Juz. 7 (6:99).
Kuleni na mchunge wanyama wenu. Hakika katika hayo zipo ishara kwa wenye akili
Makusudio ya ishara ni dalili za kuweko Mwenyezi Mungu Mtukufu. Wenye akili ni wale wenye busara. Mwenyezi Mungu amewahusisha kuwataja hapa kwa sababu wao wanaipata haki wakiwa wamejiepusha na hawa na matamanio.
Kuna Hadith ya Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.), kwamba yeye amesema: “Hakika wabora wenu ni wale wenye akili. Wakasema: Ninani hao wenye akili ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema ni wale wenye khulka njema, walio makini, wenye kuwapatiliza mafukara, mayatima na majirani, wanawalisha chakula na wanadhihirisha maamkuzi kwa watu”
Kutokana nayo tumewaumba na humo tumewarudisha na kutoka humo tutawatoa mara nyingine.
Mtu ni mtoto wa ardhi kwa mwili wake. Ndiyo mada ya kuumbwa kwake na humo mnatoka chakula chake na kinywaji chake na juu yake anakwenda na kurudi. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anasema:“Ardhi ni mama yenu na ni mlezi wenu.”
Ni mama yetu kwa vile tumetokana nayo na ni mlezi wetu kwa vile inatulisha, kama anavyonyonyesha mama mtoto wake. Kisha tutarudi ardhini baada ya kufa, tuwe mchanga kama ilivyokuwa mwanzo, tena tuwe hai mara ya pili kwa ajili ya hisabu na malipo.
Hakika tulimwonyesha ishara zetu zote, lakini alikadhibisha na akakataa.
Aliyeonyeshwa ni Firauni. Makusudio ya ishara ni miujiza aliyoidhihirisha Mwenyezi Mungu mikononi mwa Musa na ikafahamisha waziwazi juu ya ukweli wa utume wake. Lakini itafaa wapi miujiza na maonyo yakigongana na masilahi na manufaa?
9
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
قَالَ أَجِئْتَنَا لِتُخْرِجَنَا مِنْ أَرْضِنَا بِسِحْرِكَ يَا مُوسَىٰ ﴿٥٧﴾
57. Akasema: Ewe Musa! Hivi umetujia kututoa katika nchi yetu kwa uchawi wako?
فَلَنَأْتِيَنَّكَ بِسِحْرٍ مِّثْلِهِ فَاجْعَلْ بَيْنَنَا وَبَيْنَكَ مَوْعِدًا لَّا نُخْلِفُهُ نَحْنُ وَلَا أَنتَ مَكَانًا سُوًى ﴿٥٨﴾
58. Basi hakika tutakuletea uchawi kama huo. Basi weka miadi baina yetu na wewe ambayo hatutaivunja sisi wala wewe, mahali patakapokuwa sawa.
قَالَ مَوْعِدُكُمْ يَوْمُ الزِّينَةِ وَأَن يُحْشَرَ النَّاسُ ضُحًى ﴿٥٩﴾
59. Akasema: Miadi yenu ni siku ya sikukuu na watu wakusanywe kabla ya adhuhuri
فَتَوَلَّىٰ فِرْعَوْنُ فَجَمَعَ كَيْدَهُ ثُمَّ أَتَىٰ ﴿٦٠﴾
60. Basi Firauni akarudi na akatengeneza hila yake, kisha akaja.
قَالَ لَهُم مُّوسَىٰ وَيْلَكُمْ لَا تَفْتَرُوا عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا فَيُسْحِتَكُم بِعَذَابٍ وَقَدْ خَابَ مَنِ افْتَرَىٰ ﴿٦١﴾
61. Musa akawaambia: Ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu uwongo, asije akawafutilia mbali kwa adhabu, hakika ameshindwa mwenye kuzua.
فَتَنَازَعُوا أَمْرَهُم بَيْنَهُمْ وَأَسَرُّوا النَّجْوَىٰ ﴿٦٢﴾
62. Basi wakazozana kwa shauri yao wenyewe kwa wenyewe na wakanon’gona kwa siri.
قَالُوا إِنْ هَـٰذَانِ لَسَاحِرَانِ يُرِيدَانِ أَن يُخْرِجَاكُم مِّنْ أَرْضِكُم بِسِحْرِهِمَا وَيَذْهَبَا بِطَرِيقَتِكُمُ الْمُثْلَىٰ ﴿٦٣﴾
63. Wakasema: Hakika hawa wawili ni wachawi, wanataka kuwatoa katika nchi yenu kwa uchawi wao na waondoe njia yenu iliyo bora.
فَأَجْمِعُوا كَيْدَكُمْ ثُمَّ ائْتُوا صَفًّا وَقَدْ أَفْلَحَ الْيَوْمَ مَنِ اسْتَعْلَىٰ ﴿٦٤﴾
64. Kwa hiyo kusanyeni hila zenu zote, kisha mfike kwa kujipanga safu, na kwa hakika leo atafuzu atakayeshinda.
Aya 57 – 64
Akasema: Ewe Musa! Hivi umetujia kututoa katika nchi yetu kwa uchawi wako?
Firauni aligongwa na hoja asizoweza kuzijibu alipokabiliana na Musa. Vipi ataweza kuzijibu nazo ni katika ishara za Mwenyezi Mungu? Firauni alikuwa akijua wazi kuwa Musa na Harun si wachawi na kwamba uchawi hauwezi kumtoa mtu nchini mwake na kwenye ufalme wake.
Kama wachawi wangelikuwa na uwezo huu basi wangelikuwa ndio watawala kila wakati na kila mahali. Lakini Firauni aliposhindwa kujibu mapigo, alikimbila hila, ujanja ujanja, uwongo na uzushi; sawa wanavyofanya leo wakoloni na vibaraka wao, wanapowaita wakombozi kuwa ni waharibifu na wenye nia safi kuwa ni wafanya fujo.
Basi hakika tutakuletea uchawi kama huo. Weka miadi baina yetu na wewe ambayo hatutaivunja sisi wala wewe, mahali patakapokuwa sawa.
Firauni alimtaka Musa apange siku ya mapambano baina yake na wachawi, yawe mahali palipo wazi kila mtu aweze kuona mapambano hayo na kuyafuatilia.
Akasema: Miadi yenu ni siku ya sikukuu na watu wakusanywe kabla ya adhuhuri.
Musa alichagua siku ya sikukuu ndio iwe mapambano baina yake na wachawi, ambapo watu hawatakuwa na kazi waweze kukusanyika na akachaguwa wakati baina ya asubuhi na mchana, kwa vile ndio wakati mzuri wa kukusanyika watu; huku akiwa anataka kuidhihirisha haki na kuivunja batili.
Basi Firauni akarudi na akatengeneza hila yake, kisha akaja.
Aya hii pamoja na ufupi wake ina ubainifu mkubwana na inachukua maana nyingi. ‘Akarudi, akatengeneza, akaja’ Neno akarudi, linaelezea kuondoka Firauni kwenda kwa wasaidizi wake na kushauriana kupanga mipango.
Neno akatengeneza linaelezea kutuma wajumbe katika pembe zote za nchi kutafuta wachawi na kuwaleta. Mshauri wake alimshauri afanye hivyo; kama inavyoashiria Aya katika Juz. 9 (7:112). Na neno akaja, linaelezea kuja kwake na majigambo yake kwenye uwanja wa mapambano.
Musa akawaambia: Ole wenu! Msimzulie Mwenyezi Mungu uwongo, asije akawafutilia mbali kwa adhabu, hakika ameshindwa mwenye kuzua.
Musa alitanguliza nasaha na onyo kwa wachawi kabla ya kuanza kazi yoyote ya uchawi na akawahadharisha na kuondolewa mbali na adhabu kama wataendele kuwadanganya watu na kuwavunga; kisha akawafahamisha kuwa kadiri Firauni alivyo na nguvu ya utawala, lakini ni mdhaifu sana wa kuweza kuwadhuru au kuwanufaisha.
Basi wakazozana kwa shauri yao wenyewe kwa wenyewe na wakanon’gona kwa siri.
Waliozozana ni wachawi. Aya hii inaashiria kuwa baadhi ya wachawi waliathirika na maneno ya Musa au angalau waliingia shaka. Katika Tafsir Aya hii inaashiria kwamba baadhi ya wachawi waliathirika na maneno ya Musa(a.s) , Au angalau yalitia shaka katika nafsi zao. Katika Attabariy imeelezwa kuwa wachawi walisema kutokana na tahadhari ya Musa kuwa maneno haya siyo ya mchawi.
Ni kweli kwamba maneno yakitoka kwenye moyo wa mwenye ikhlasi huchukua mkondo kuelekea kwenye moyo wa mwenye ikhlasi. Waliathirika baadhi ya wachawi kwa mawaidha ya Musa, wakaanza kupingana wenyewe, Kama kawaida yalipita majadiliano kuwa je, waendelee au wasiendelee.
Majadiliano haya yalipita kwa siri asisikie Musa wala Firauni. Lakini mwisho walioshinda ni wale waliong’ang’ania kuendelea na upinzani, kwa dalili ya alivyowasimulia Mwenyezi Mungu:
Wakasema: Hakika hawa wawili ni wachawi, wanataka kuwatoa katika nchi yenu kwa uchawi wao na waondoe njia yenu iliyo bora. Kwa hiyo kusanyeni hila zenu zote, kisha mfike kwa kujipanga safu, na kwa hakika leo atafuzu atakayeshinda.
Maneno yote haya ni ya wachawi na hawa wawili wanawakusudia Musa na Harun. Makusudio ya njia iliyo bora ni dini, kwa dalili ya Aya nyingine isemayo:
“Na Firauni akaema: Niacheni nimuuwe Musa naye amwite Mola wake, mimi nahofia asije kuwabadilishia dini yenu” (40:26).
Maana ni kuwa baadhi ya wachawi walisema kuwa Musa na Haruna ni mahodari katika fani ya uchawi kwa hiyo wanataka watushinde ili waimalize dini yetu wabakie wao ndio mabwana katika miji na wawatawale watu wawe watumwa wao.
Kwa hiyo basi hatuna budi tuwe na mshikamano dhidi yao na tutoe juhudi zetu zote ili tuwashinde, tuwe na cheo siku hii ya leo inayoshuhudiwa.
قَالُوا يَا مُوسَىٰ إِمَّا أَن تُلْقِيَ وَإِمَّا أَن نَّكُونَ أَوَّلَ مَنْ أَلْقَىٰ ﴿٦٥﴾
65. Wakasema: Ewe Musa! Je, utatupa wewe au tutakuwa sisi wa kwanza kutupa?
قَالَ بَلْ أَلْقُوا فَإِذَا حِبَالُهُمْ وَعِصِيُّهُمْ يُخَيَّلُ إِلَيْهِ مِن سِحْرِهِمْ أَنَّهَا تَسْعَىٰ ﴿٦٦﴾
66. Akasema; bali tupeni nyinyi! Mara kamba zao na fimbo zao zikaonekana, kwa uchawi, kuwa zinakwenda mbio.
فَأَوْجَسَ فِي نَفْسِهِ خِيفَةً مُّوسَىٰ ﴿٦٧﴾
67. Basi Musa akaingia hofu katika nafsi yake.
قُلْنَا لَا تَخَفْ إِنَّكَ أَنتَ الْأَعْلَىٰ ﴿٦٨﴾
68. Tukasema; usihofu hakika wewe ndiye utakayeshinda.
وَأَلْقِ مَا فِي يَمِينِكَ تَلْقَفْ مَا صَنَعُوا إِنَّمَا صَنَعُوا كَيْدُ سَاحِرٍ وَلَا يُفْلِحُ السَّاحِرُ حَيْثُ أَتَىٰ ﴿٦٩﴾
69. Na kitupe kilicho kuumeni kwako, kitavimeza walivyovitengeneza, hakika walivyovitengeneza ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote aendapo.
فَأُلْقِيَ السَّحَرَةُ سُجَّدًا قَالُوا آمَنَّا بِرَبِّ هَارُونَ وَمُوسَىٰ ﴿٧٠﴾
70. Basi wachawi wakaangushwa kusujudi. Wakasema:tumemwamini Mola wa Haruna na Musa!
قَالَ آمَنتُمْ لَهُ قَبْلَ أَنْ آذَنَ لَكُمْ إِنَّهُ لَكَبِيرُكُمُ الَّذِي عَلَّمَكُمُ السِّحْرَ فَلَأُقَطِّعَنَّ أَيْدِيَكُمْ وَأَرْجُلَكُم مِّنْ خِلَافٍ وَلَأُصَلِّبَنَّكُمْ فِي جُذُوعِ النَّخْلِ وَلَتَعْلَمُنَّ أَيُّنَا أَشَدُّ عَذَابًا وَأَبْقَىٰ ﴿٧١﴾
71. Akasema: Mumemwamini kabla sijawapa ruhusa! Hakika huyo ni mkubwa wenu aliyewafundisha uchawi. Nitawakata mikono yenu na miguu yenu kwa kubadilisha, kisha nitawasu- lubu kwenye vigogo vya mitende. Na hapo kwa yakini mtajua ni nani katika sisi ni mkali wa adhabu na kuiendeleza?
قَالُوا لَن نُّؤْثِرَكَ عَلَىٰ مَا جَاءَنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالَّذِي فَطَرَنَا فَاقْضِ مَا أَنتَ قَاضٍ إِنَّمَا تَقْضِي هَـٰذِهِ الْحَيَاةَ الدُّنْيَا ﴿٧٢﴾
72. Wakasema: Hatutaathirika nawe katika ishara waziwazi zilizotujia na yule aliyetuumba. Basi hukumu utakavyohukumu; kwani wewe unahukumu maisha haya ya duniani tu
إِنَّا آمَنَّا بِرَبِّنَا لِيَغْفِرَ لَنَا خَطَايَانَا وَمَا أَكْرَهْتَنَا عَلَيْهِ مِنَ السِّحْرِ وَاللَّـهُ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ﴿٧٣﴾
73. Hakika sisi tumemwamini Mola wetu ili atusamehe makosa yetu na uchawi uliotulazimisha kuufanya na Mwenyezi Mungu ndiye Mbora na mwenye kudumu zaidi.
إِنَّهُ مَن يَأْتِ رَبَّهُ مُجْرِمًا فَإِنَّ لَهُ جَهَنَّمَ لَا يَمُوتُ فِيهَا وَلَا يَحْيَىٰ ﴿٧٤﴾
74. Hakika atakayemjia Mola wake naye ni mhalifu, basi kwa hakika yake ni Jahannamu, Hafi humo wala haishi.
وَمَن يَأْتِهِ مُؤْمِنًا قَدْ عَمِلَ الصَّالِحَاتِ فَأُولَـٰئِكَ لَهُمُ الدَّرَجَاتُ الْعُلَىٰ ﴿٧٥﴾
75. Na atakayemjia naye ni mumin aliyetenda mema basi hao ndio wenye daraja za juu
جَنَّاتُ عَدْنٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا وَذَٰلِكَ جَزَاءُ مَن تَزَكَّىٰ ﴿٧٦﴾
76. Bustani za milele zipitazo mito chini yake, watadumu humo milele na hayo ni malipo ya mwenye kujitakasa.
Aya 65 – 76
Wakasema: Ewe Musa! Je, utatupa wewe au tutakuwa sisi wa kwanza kutupa? Akasema; bali tupeni nyinyi! Mara kamba zao na fimbo zao zikaonekana, kwa uchawi, kuwa zinakwenda mbio.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7:113).
Basi Musa akaingia hofu katika nafsi yake.
Wafasiri wengi wamesema kuwa Musa alihofia nafsi yake, kama ilivyo kawaida ya maumbile, lakini ilivyo hasa hakuhofia nafsi yake. Vipi iwe hivyo naye anajua kuwa wachawi ni wazushi na kwamba Mwenyezi Mungu alimwambia yeye na nduguye kuwa mimi niko pamoja nanyi! Ispokuwa alihofiwa mambo yasivurugike na watu wakachanganyikiwa wakadanganyika na uchawi.
Tukasema; usihofu hakika wewe ndiye utakayeshinda.
Usihofu kuwa watu watachanganyikiwa, hapana! Macho na akili zitafunukiwa kuwa wewe uko katika haki na wao ni wabatilifu; hata wachawi wenyewe watakiri kuwa wewe ni mkweli mwaminifu na kwamba wao ni wazushi, wenye vitimbi na hadaa; na Firauni ndiye aliyewalazimisha.
Na kitupe kilicho kuumeni kwako, kitavimeza walivyovitengeneza, hakika walivyovitengeneza ni hila za mchawi tu, na mchawi hafanikiwi popote aendapo, Basi wachawi wakaangushwa kusujudi. Wakasema: tumemwamini Mola wa Haruna na Musa! Akasema: mumemwamini kabla sijawapa ruhusa! Hakika huyo ni mkubwa wenu aliyewafundisha uchawi. Nitawakata mikono yenu na miguu yenu kwa kubadilisha, kisha nitawasulubu kwenye vigogo vya mitende. Na hapo kwa yakini mtajua ni nani katika sisi ni mkali wa adhabu na kuiendeleza?
Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7:117)
Wakasema: Hatutaathirika nawe katika ishara waziwazi zilizotujia na yule aliyetuumba.
Firauni alitaka wachawi wamwache Mwenyezi Mungu wamfuate yeye baada ya kufunukiwa na upotevu wake. Wakasema ni kitu gani basi kinaweza kutuathiri! Je, ni hiyo dunia yako, ambayo hata wewe mwenyewe utaiacha, au ni vitisho vyako na adhabu yako, na hali adhabu ya Mwenyezi Mungu ni kubwa na kali?
Basi hukumu utakavyohukumu : Sisi hatuogopi vitisho vyako na mateso yako maadamu tuna yakini na Mola wetu;kwani wewe unahukumu maisha haya ya duniani tu, yawe tamu au chungu. Na sisi si watoto wa dunia isipokuwa ni wa Akhera, ambayo itabaki na wala wewe huna mamlaka huko hata ya kujitetea wewe mwenyewe.
Hivi ndivyo anavyokuwa kila mwenye ikhlasi, haogopi upanga wa wachinjaji kwa ajili ya dini yake na misimamo yake. Ni muhali kabisa kuishi dini au misimamo yoyote ikiwa hakuna watu wa aina hii.
Hakika sisi tumemwamini Mola wetu ili atusamehe makosa yetu na uchawi uliotulazimisha kuufanya na Mwenyezi Mungu ndiye Mbora na mwenye kudumu zaidi kuliko wewe Firauni.
Mapambano yalikuwa yanaonyesha kuwa ni baina Musa na wachawi, lakini kiuhakika hasa yalikuwa ni baina ya chama cha Mwenyezi Mungu na cha shetani.
Katika raundi ya kwanza tu walishuhudia watazamaji, akiwe- mo Firauni na wachawi, kuwa chama cha Mwenyezi Mungu ndio mshindi. Wachawi wakatangaza kuwa wao wamehakikisha haya kwa ujuzi usio na shaka. Na kwamba wao walikuwa kwenye upotevu kwa kumpinga Musa; na Firauni ndiye aliyewaelekeza hayo na kuwalazimisha, Wakamwomba msamaha Mwenyezi Mungu.
Kuomba msamaha kwa wachawi ni dalili wazi kuwa mchawi hana nguvu yoyote; isipokuwa ni kuvungavunga na upotevu; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: ‘zikaonekana, kwa uchawi, kuwa zinakwenda mbio.’
Hakika atakayemjia Mola wake naye ni mhalifu, basi kwa hakika, yake ni Jahannamu. Hafi humo wala haishi.
Hili ni fumbo la kudumu na adhabu. Mfano wake ni Aya isemayo: “Hawatamalizwa wakafa wala hawatapunguziwa adhabu yake. (35:36).
Neno mhalifu linatumika kwa kila mwenye kufanya ufisadi na uovu katika kauli au vitendo; awe kafiri au asiwe kafiri. Dalili ya kuwa makusudio ya mhalifu yanaenea ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Na atakayemjia naye ni mumin aliyetenda mema basi hao ndio wenye daraja za juu ambapo amekutanisha imani na matendo mema. Maana yake ni kuwa imani bila ya matendo haimnufaishi mwenye nayo.
Kwa maneno mengine ni kuwa waumini ni wale walio wema katika makusudio yao na matendo yao. Ama wale wanaohangaika katika ardhi kufanya ufisadi wao wako katika kundi la wahalifu; hata kama wataijaza ardhi kwa tahlili na takbir.
Bustani za milele zipitazo mito chini yake, watadumu humo milele na hayo ni malipo ya mwenye kujitakasa
Bustani (Pepo) na daraja za juu mbele ya Mwenyezi Mungu ni za wale waliozitakasa nafsi zao kwa mapenzi na ikhlasi kwa watu wote na kuzitwaharisha na kila aina ya khiyana tamaa na karaha. Kuna mamia ya Aya zenye maana hii kwa uwazi na kwa ishara.
وَلَقَدْ أَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ أَنْ أَسْرِ بِعِبَادِي فَاضْرِبْ لَهُمْ طَرِيقًا فِي الْبَحْرِ يَبَسًا لَّا تَخَافُ دَرَكًا وَلَا تَخْشَىٰ ﴿٧٧﴾
77. Na tulimpa wahyi Musa: Toka usiku na waja wangu na uwapigie njia kavu baharini, usikhofu kukamatwa wala usiogope.
فَأَتْبَعَهُمْ فِرْعَوْنُ بِجُنُودِهِ فَغَشِيَهُم مِّنَ الْيَمِّ مَا غَشِيَهُمْ ﴿٧٨﴾
78. Firauni akawafuata pamoja na majeshi yake, Basi kiliwafudikiza baharini kilichowafudikiza.
وَأَضَلَّ فِرْعَوْنُ قَوْمَهُ وَمَا هَدَىٰ ﴿٧٩﴾
79. Na Firauni aliwapoteza watu wake na hakuwaongoza.
يَا بَنِي إِسْرَائِيلَ قَدْ أَنجَيْنَاكُم مِّنْ عَدُوِّكُمْ وَوَاعَدْنَاكُمْ جَانِبَ الطُّورِ الْأَيْمَنَ وَنَزَّلْنَا عَلَيْكُمُ الْمَنَّ وَالسَّلْوَىٰ ﴿٨٠﴾
80. Enyi wana wa israil! Hakika tuliwaokoa na adui yenu! Na tukawaahidi upande wa kuume wa mlima. Na tukawateremshia Manna na Salwa
كُلُوا مِن طَيِّبَاتِ مَا رَزَقْنَاكُمْ وَلَا تَطْغَوْا فِيهِ فَيَحِلَّ عَلَيْكُمْ غَضَبِي وَمَن يَحْلِلْ عَلَيْهِ غَضَبِي فَقَدْ هَوَىٰ ﴿٨١﴾
81. Kuleni katika vizuri tulivyowaruzuku, wala msipituke mipaka katika hayo isije ikawashukia ghadahabu yangu, Na inayemshukia ghadahabu yangu basi huyo amepotea.
وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ ﴿٨٢﴾
82. Hakika mimi ni mwingi wa maghufira kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema tena akaongoka.
Aya 77 – 82
Na tulimpa wahyi Musa: Toka usiku na waja wangu na uwapigie njia kavu baharini, usikhofu kukamatwa wala usiogope.
Firauni aling’ang’ania inadi yake na akataa kila kitu isipokuwa kiburi na ujabari na kumpa sifa Musa kuwa ametoka nje na ni mchawi. Akapata wa kumuunga mkono katika hilo:
وَقَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِ فِرْعَوْنَ أَتَذَرُ مُوسَىٰ وَقَوْمَهُ لِيُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ ﴿١٢٧﴾
“Na wakasema wakuu wa kaumu ya Fir’aun: Je, utamwacha Musa na watu wake walete uharibifu katika nchi.” Juz. 9 (7:127)
Firauni alishikilia kutaka kumuua Musa, ndipo Mwenyezi Mungu akampa wahyi atoke Misr usiku pamoja na wana waisrail na apige bahari kwa fimbo yake ipasuke itokee njia waifuate waisrail hadi upande mwengine wasalimike na maangamizi na Firauni na shari yake:
فَأَوْحَيْنَا إِلَىٰ مُوسَىٰ أَنِ اضْرِب بِّعَصَاكَ الْبَحْرَ فَانفَلَقَ فَكَانَ كُلُّ فِرْقٍ كَالطَّوْدِ الْعَظِيمِ ﴿٦٣﴾ وَأَزْلَفْنَا ثَمَّ الْآخَرِينَ ﴿٦٤﴾ وَأَنجَيْنَا مُوسَىٰ وَمَن مَّعَهُ أَجْمَعِينَ ﴿٦٥﴾ ثُمَّ أَغْرَقْنَا الْآخَرِينَ ﴿٦٦﴾
“Tulimletea wahyi Musa tukamwambia piga bahari kwa fimbo yako, Basi ikatengana, na kila seemu ikawa kama mlima mkubwa, Na tukawajongeza hapo wale wengine, Na tukamwokoa Musa na waliokuwa pamoja naye, Kisha tukawazamisha hao wengine” (26: 63 – 66).
Firauni akawafuata pamoja na majeshi yake; Basi kiliwafudikiza baharini kilichowafudikiza.
Kusema kiliwafudikiza kilichowafudikiza ni kulikuza jambo. Hapo kuna maneno mengi ya kukadiriwa; kama ilivyo kawaida ya Qur’an. Kwa sababu mfumo wa maneno unafahamisha hivyo.
Kukadirwa kwake ni: Musa alitoka na watu wake usiku. Alipofika baharini akapiga kwa fimbo yake na bahari ikapasuka kukawa na njia isiyokuwa na maji, wakaifuata waisrail. Firauni na jeshi lake wakawaandama. Walipofika waisrail upande wa pili na mjeshiya Firauni kuingia yote, bahari ilirudi wakafamaji wote na waisraili wakasalimika wote.
Na Firauni aliwapoteza watu wake na hakuwaongoza.
Aliwapoteza na haki na akawapoteza baharini vilevile. Hapo mwanzo alikuwa akiwaambia:
وَمَا أَهْدِيكُمْ إِلَّا سَبِيلَ الرَّشَادِ ﴿٢٩﴾
“Wala siwaongozi ila kwenye njia ya uongofu” (40:29)
Enyi wana wa israil! Hakika tuliwaokoa na adui yenu!
Firauni aliyekuwa akiwapa adhabu mbaya ya kuwachinja watoto wenu wa kiume na kuwaacha wanawake.
Na tukawaahidi upande wa kuume wa mlima.
Anaishiria Mwenyezi Mungu (s.w.t) ahadi aliyomwahidi Musa baada ya kufa maji Firauni, Ahadi yenyewe ni kwenda Musa upande wa mlimani, ateremshiwe Tawrat, amabayo ndani yake mna ubainifu wa sharia na hukumu.
Na tukawateremshia Manna na Salwa: Kuleni katika vizuri tulivyowaruzuku
Umetangulia mfano wake, kwa herufi zake, katika Juz. 1 (2:57)
Wala msipituke mipaka katika hayo isije ikawashukia ghadahabu yangu. Na inayemshukia ghadahabu yangu basi huyo amepotea.
Katika hayo ni hayo tuliyowaruzuku. Kupetuka mpaka katika hayo, ni kuchukua au kutoa kwa njia isiyokuwa yake ya kisharia.
Maana ni kuwa mwenye kuchuma mali kwa njia isiyokuwa ya halali au kuitumia kwa njia isiyokuwa ya halali, basi malipo yake mbele ya Mwenyezi Mungu ni maangamizi na adhabu ya kuunguza; sawa na Firauni na wengineo katika waasi walio mataghuti.
Hakika mimi ni mwingi wa maghufira kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema tena akaongoka.
Mwenyezi Mungu husamehe madhambi kwa masharti mane:
1. Kwanza: kutubia nako ni kujuta kwa maasi yaliyokuwa pamoja na kuomba msamaha.
2. Pili: kuiamini haki, popote itakapokuwa na itakavyokuwa; ni sawa iafikiane na malengo yake au yahalifiane.
3. Tatu: kuitumia haki. Kwani imani bila ya matendo ni kama matamshi bila ya maana.
4. Nne: ni kuongoka. Makusudio yake ni kuendelea kuifuata haki mpaka kufa. Na hapa ndio tunapata jibu la mwenye kuuliza kuwa, kuna haja gani ya kuunganisha mwenye kuongoka na mwenye kuamini na akatenda mema.
10
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
وَمَا أَعْجَلَكَ عَن قَوْمِكَ يَا مُوسَىٰ ﴿٨٣﴾
83. Ni lipi lililokuharakisha ukaawaacha watu wako ewe Musa?
قَالَ هُمْ أُولَاءِ عَلَىٰ أَثَرِي وَعَجِلْتُ إِلَيْكَ رَبِّ لِتَرْضَىٰ ﴿٨٤﴾
84. Akasema: Hao hapo nyuma yangu wananifuatia. Na nimefanya haraka kukujia, Mola wangu, ili uridhie.
قَالَ فَإِنَّا قَدْ فَتَنَّا قَوْمَكَ مِن بَعْدِكَ وَأَضَلَّهُمُ السَّامِرِيُّ ﴿٨٥﴾
85. Akasema: Hakika sisi tumewatia mtihani watu wako baada yako na msamaria amewapoteza.
فَرَجَعَ مُوسَىٰ إِلَىٰ قَوْمِهِ غَضْبَانَ أَسِفًا قَالَ يَا قَوْمِ أَلَمْ يَعِدْكُمْ رَبُّكُمْ وَعْدًا حَسَنًا أَفَطَالَ عَلَيْكُمُ الْعَهْدُ أَمْ أَرَدتُّمْ أَن يَحِلَّ عَلَيْكُمْ غَضَبٌ مِّن رَّبِّكُمْ فَأَخْلَفْتُم مَّوْعِدِي ﴿٨٦﴾
86. Musa akarudi kwa watu wake kwa ghadhabu na kusikitika. Akasema: “Enyi watu wangu! Kwani Mola wenu hakuwaahidi ahadi nzuri? Je ahadi imerefuka? Au mmetaka iwafikie ghadhabu kutoka kwa Mola wenu, ndio maana mkavunja ahadi yangu?
قَالُوا مَا أَخْلَفْنَا مَوْعِدَكَ بِمَلْكِنَا وَلَـٰكِنَّا حُمِّلْنَا أَوْزَارًا مِّن زِينَةِ الْقَوْمِ فَقَذَفْنَاهَا فَكَذَٰلِكَ أَلْقَى السَّامِرِيُّ ﴿٨٧﴾
87. Wakasema: “Hatukuvunja ahadi yako kwa hiyari yetu, lakini tulibebeshwa mizigo ya vipambo vya watu. Basi tukaitupa na kadhalika Msamaria akatupa.
فَأَخْرَجَ لَهُمْ عِجْلًا جَسَدًا لَّهُ خُوَارٌ فَقَالُوا هَـٰذَا إِلَـٰهُكُمْ وَإِلَـٰهُ مُوسَىٰ فَنَسِيَ ﴿٨٨﴾
88. Akawaundia ndama, kiwiliwili chenye sauti, Wakasema: Huyu ndiye Mungu wenu na Mungu wa Musa, lakini amemsahau.
أَفَلَا يَرَوْنَ أَلَّا يَرْجِعُ إِلَيْهِمْ قَوْلًا وَلَا يَمْلِكُ لَهُمْ ضَرًّا وَلَا نَفْعًا ﴿٨٩﴾
89. Je, hawakuona kuwa hakuwarudishia neno, wala hakuweza kuwadhuru wala kuwafaa?.
Aya 83 – 89
Baada ya kuangamia Firauni na Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumwahidi Musa kuwa atamteremshia Tawrat na kumpa muda wake, Musa alikwenda kwa Mola wake kuichukua na kumwachia uongozi nduguye Haruna kwa Wana wa Israil, Hapo waliitumia fursa ya kuondoka Nabii wao Musa, wakaabudu ndama. Yakahakikika yale Aliokuwa wakiyawazia hapo mwanzo, pale walipowaona watu:
يَعْكُفُونَ عَلَىٰ أَصْنَامٍ لَّهُمْ قَالُوا يَا مُوسَى اجْعَل لَّنَا إِلَـٰهًا كَمَا لَهُمْ آلِهَةٌ قَالَ إِنَّكُمْ قَوْمٌ تَجْهَلُونَ ﴿١٣٨﴾
“Waliokuwa wakiyaabudu masanamu yao; wakaema: “Ewe Musa! Hebu nasi tufanyie waungu kama hawa walivyo na waungu.” Akasema: “Hakika nyinyi ni watu wafanyao ujinga.” Juz.9 (7:138).
Yametangulia maelezo ya hayo katika Juz; 1 (2:51) na Juz 9 (7: 148). Aya hii tuliyo nayo na zinazofuatia hadi ya 98, zote zinazungumzia maudhui haya na yanayoambatana nayo.
Ni lipi lililokuharakisha ukaawaacha watu wako ewe Musa?
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anamuuliza kuhusu haraka yake huku akijua sababu, Anataka kumfahamisha yaliyoowatokea watu wake-kuabudu ndama.
Akasema: Hao hapo nyuma yangu wananifuatia. Na nimefanya haraka kukujia, Mola wangu, ili uridhie.
Dhahiri ya maneno inafahamisha kuwa Musa alitakiwa aje na watu wake, lakini akaja peke yake, ndio akajibu kuwa wao wanakuja bila ya kuchelewa, nimewatangulia ili kukuridhisha. Alisema haya akiwa hajui waliyoyazua watu wake baada yake.
Akasema Mwenyezi Mungu: Hakika sisi tumewatia mtihani watu wako baada yako na msamaria amewapoteza.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewatia mtihani ili idhihirike hakika yao Waisrail. Namna ya mtihani ni kuwa Mwenyezi Mungu amewakataza kuabudu ndama kupitia kwenye ulimi wa Musa na shetani akawaamrisha kuabudu ndama kupitia ulimi wa Msamaria; wakamwasi Mungu na wakatii shetani. Ikadhihiri hakika yao ya udhaifu wa imani na ukafiri wao; sawa na afanyavyo muovu anapopata nafasi.
Musa akarudi kwa watu wake kwa ghadhabu na kusikitika.
Umetangulia mfano wake katika Juz. Juz.9 (7:150).
Akasema: Enyi watu wangu! Kwani Mola wenu hakuwaahidi ahadi nzuri?”
Anaashira kwa hili, kwamba Mwenyezi Mungu amewaahidi kuteremshiwa Tawrat kwa Mtume wao, ndani yake mna upambanuzi wa kila wanayoyahitajia katika kujua halali na haramu na kwamba Yeye Mwenyezi Mungu (s.w.t.) atawamilikisha makao ya wafasiki; kama ilivyoelezwa katika Juz. 9 (7:145):
وَكَتَبْنَا لَهُ فِي الْأَلْوَاحِ مِن كُلِّ شَيْءٍ مَّوْعِظَةً وَتَفْصِيلًا لِّكُلِّ شَيْءٍ فَخُذْهَا بِقُوَّةٍ وَأْمُرْ قَوْمَكَ يَأْخُذُوا بِأَحْسَنِهَا سَأُرِيكُمْ دَارَ الْفَاسِقِينَ ﴿١٤٥﴾
“Na tukamwandikia katika mbao kila kitu mawaidha na ufafanuzi wa kila jambo, Basi yashike kwa imara na uwaamrishe watu wako washike mazuri yake zaidi, Nitawaonyesha makao ya wafasiki.”
Je ahadi imerefuka?
Yaani muda wa kutokuwepo Musa umekuwa mrefu?
Au mmetaka iwafikie ghadhabu kutoka kwa Mola wenu.
Yaani mimi sikuwa mbali nanyi kwa muda mrefu, kwa nini basi mkamshirikisha Mwenyezi Mungu? Au mlitaka iwafikie ghadhabu yake na adhabu yake?.
Hii inaonyesha kuwa wao wanaamini maadamu Musa amewasimamia kwenye vichwa vyao, akiondoka wanageuka na kuipotoa dini kwa hawa zao, kama ilivyotokea.
Ndio maana mkavunja ahadi yangu.
Mmegeuka kwenye dini ya Mwenyezi Mungu baada ya kuniahidi kuwa mtakuwa thabiti.
Wakasema: Hatukuvunja ahadi yako kwa hiyari yetu.
Huku ni kukubali wazi kwamba wao walikufuru, kurtadi na kuvunja ahadi. Udhuru wao pekee ni kwamba wao ni kama wanoendeshwa hawawezi kujizuia na kufuru na hiyana; ni kama kwamba wao wametengenezwa hivyo, Hivi ndivyo inavyodhihiri hakika ya waisraili kwenye ndimi zao kuongezea vitendo vyao.
Lakini tulibebeshwa mizigo ya vipambo vya watu.
Vipambo vya watu ni vipambo vya wanawake wa watu wa Firauni. Wafasiri wamesema kuwa Waisraili walipojua kuwa wataipituka bahari na kwamba Mwenyezi Mungu atamwangamiza Firauni majini, waliwafanyia hila wanawake wa watu wa Firauni; wakawaazima vipambo vyao kwa kutoa visingizio vya harusi na mengineyo. Hili haliko mbali na tabia za kiisraili na hila zao za kuchuma mali kwa mbinu yoyote.
Basi tukaitupa na kadhalika Msamaria akatupa.
Tabari anasema katika Tafsiri yake: “Bani Israil walitupa vipambo walivyokuwa navyo ndani ya shimo, naye Msamaria akatupa alivyokuwa navyo, Vyote akavifua kwenye umbo la ndama” akawaundia ndama, kiwiliwili chenye sauti.
Umepita mfano wake katika Juz. 9 (7:148).
Wakasema: Huyu ndiye Mungu wenu na Mungu wa Musa, lakini amemsahau.
Waliosema ni Msamaria na wenzake wakikusudia kuwa huyo ni Mungu wa wa viumbe vyote akiwemo Musa lakini amemsahu na kwenda kumtafua milimani, hajui kuwa ni mgeni wetu na tunaye majumbani mwetu.
Hii inaashiria kuwa kila anayesema kuwa Mungu ana kiwiliwili yuko pamoja na waabudu ndama atake asitake.
Je, hawakuona kuwa hakuwarudishia neno, wala hakuweza kuwad- huru wala kuwafaa.
Vipi atakuwa ndama ni Mola wao na wamemtengeneza kwa mikono yao? Hasikii maneno yao wala harudishi jawabu; hawawaletei manufaa wala hawazuii na madhara. Baadhi ya wafasiri wamesema: Zaidi ya hayo hawezi kupiga pembe wala teke.
Katika Tafsir Razi, imelezwa kuwa Myahudi mmoja alimwambia Imam Ali(a.s) :“Hamkuzika Mtume wenu mpaka mlipohitalifiana.”
Imam akasema:“Hatukuhitalifiana naye, bali tulihitalifiana kuhusiana naye, nanyi hata maji ya bahari hayajakauka miguuni mkaanza kumwambia Nabii wenu, tutengenezee mungu kama walivyo na mungu wao.”
Kama ingelifaa kufasiri Qur’an kwa rai na taawili ya hisia basi tungesema kuwa kutengeneza ndama kutokana na dhahabu na kumfanya ni mungu wao ni nembo ya kwamba wao tangu zamani wana maumbile ya kuabudu mali na kwamba hiyo ndio mungu wao wa pekee asiyekuwa na mshirika.
Historia yao ya zamani na ya sasa inafahamisha hilo waziwazi. Wao wanahalalisha kila kitu kwa ajili ya mali, hata kumwaga damu na umalaya.
وَلَقَدْ قَالَ لَهُمْ هَارُونُ مِن قَبْلُ يَا قَوْمِ إِنَّمَا فُتِنتُم بِهِ وَإِنَّ رَبَّكُمُ الرَّحْمَـٰنُ فَاتَّبِعُونِي وَأَطِيعُوا أَمْرِي ﴿٩٠﴾
90. Na hakika Harun alikwisha waambia kabla yake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mmetiwa mtihani tu kwa kitu hiki. Na kwa hakika Mola wenu ni Mwingi wa rehema. Basi nifuateni na mtii amri yangu.
قَالُوا لَن نَّبْرَحَ عَلَيْهِ عَاكِفِينَ حَتَّىٰ يَرْجِعَ إِلَيْنَا مُوسَىٰ ﴿٩١﴾
91. Wakasema: Hatutaacha kumwabudu mpaka Musa atakaporejea kwetu.
قَالَ يَا هَارُونُ مَا مَنَعَكَ إِذْ رَأَيْتَهُمْ ضَلُّوا ﴿٩٢﴾
92. Akasema (Musa): Ewe Harun! Ni nini kilichokuzuia ulipowaona wamepotea.
أَلَّا تَتَّبِعَنِ أَفَعَصَيْتَ أَمْرِي ﴿٩٣﴾
93. Hata usinifute? Je,umeasi amri yangu?
قَالَ يَا ابْنَ أُمَّ لَا تَأْخُذْ بِلِحْيَتِي وَلَا بِرَأْسِي إِنِّي خَشِيتُ أَن تَقُولَ فَرَّقْتَ بَيْنَ بَنِي إِسْرَائِيلَ وَلَمْ تَرْقُبْ قَوْلِي ﴿٩٤﴾
94. Akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Usinishike ndevu zangu, wala kichwa change; Kwa hakika niliogopa usije ukasema umewafarikisha Wana wa Israil na hukungojea kauli yangu.
قَالَ فَمَا خَطْبُكَ يَا سَامِرِيُّ ﴿٩٥﴾
95. Akasema: Una nini wewe Msamaria?
قَالَ بَصُرْتُ بِمَا لَمْ يَبْصُرُوا بِهِ فَقَبَضْتُ قَبْضَةً مِّنْ أَثَرِ الرَّسُولِ فَنَبَذْتُهَا وَكَذَٰلِكَ سَوَّلَتْ لِي نَفْسِي ﴿٩٦﴾
96. Akasema: Nimeyaona wasiyoyaona wao na nikashika sehemu chache ya mwendo wa Mtume kisha nikaitupa, na hivyo ndivyo ilivyonielekeza nafsi yangu.
قَالَ فَاذْهَبْ فَإِنَّ لَكَ فِي الْحَيَاةِ أَن تَقُولَ لَا مِسَاسَ وَإِنَّ لَكَ مَوْعِدًا لَّن تُخْلَفَهُ وَانظُرْ إِلَىٰ إِلَـٰهِكَ الَّذِي ظَلْتَ عَلَيْهِ عَاكِفًا لَّنُحَرِّقَنَّهُ ثُمَّ لَنَنسِفَنَّهُ فِي الْيَمِّ نَسْفًا ﴿٩٧﴾
97. Akasema (Musa): Basi ondoka na kwa hakika utakuwa katika maisha ukisema: ‘Usiniguse’ Na hakika una miadi kwako isiyovunjwa, Na mtazame huyo mungu wako uliyeendelea kumwabudu; hakika tutamuunguza kisha tutamtawanya baharini atawanyike.
إِنَّمَا إِلَـٰهُكُمُ اللَّـهُ الَّذِي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ وَسِعَ كُلَّ شَيْءٍ عِلْمًا ﴿٩٨﴾
98. Hakika Mungu wenu ni Mwenyezi Mungu tu, hapana mungu mwingine ispokuwa Yeye, ujuzi wake umeenea kila kitu.
Aya 90 – 98
Na hakika Harun alikwisha waambia kabla yake: Enyi watu wangu! Hakika nyinyi mmetiwa mtihani tu kwa kitu hiki. Na kwa hakika Mola wenu ni Mwingi wa rehema. Basi nifuateni na mtii amri yangu.
Musa alipokwenda mlimani, alimwambia ndugu yake Harun: “Shika mahali pangu katika watu wangu na utengeneze wala usifuate njia ya wafisadi.” Juz; 9 (7:142). Harun akatengeneza, kama alivyoamrishwa na ndugu yake; akatoa nasaha na kuwahadharisha wana wa Israil kutokana na Msamaria na ndama wake. Miongoni mwa maneno Aliowaambia ni: ‘Ni jambo gani lililowahadaa na ndama huyu mpaka mkashindwa na mtihani wake, mkamwelekea badala ya Muumba wa mbingu na ardhi? Basi nifu- ateni nitawaongoza njia ya uwongofu.
Basi halikuwa jawabu la watu wake ispokuwawakasema: Hatutaacha kumwabudu mpaka Musa atakaporejea kwetu, tuone rai yake kwenye hili. Kama kwamba wanamgonja amlaumu Harun kwenye hilo na awaunge mkono wao.
Kila mwenye kuathirika na mali kuliko dini yake na dhamiri yake, au akamfuata mpotezaji kwenye upotevu wake, basi yeye ni katika wafuasi wa Msamaria na chama chake. Mwenyezi Mungu amewatia mtihani waja wake kila wakati kwa ndama mwenye kutoa sauti Aliyetengenezwa kwa dhahabu au kuwa bendera inayofuta upepo.
Akasema (Musa): Ewe Harun! Ni nini kilichokuzuia ulipowaona wamepotea, hata usinifute? Je, umeasi amri yangu?
Hii kwa dhahiri inaonyesha ni lawama kwa Harun, lakini kiuhakika ni lawama na kuwatahariza wale walioabudu ndama. Kwa sababu Musa alijua fika kwamba ndugu yake Harun hakumukhalifu wala hatamkhalifu kwenye jambo lolote; na kwamba yeye alitekeleza wajibu wake kwa ukamilifu, kwa sabu yeye ni mshirika wake katika utume na kuwa ni maasumu.
Akasema: Ewe mwana wa mama yangu! Usinishike ndevu zangu, wala kichwa changu.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 9 (7:150).
Kwa hakika niliogopa usije ukasema umewafarikisha Wana wa Israil na hukungojea kauli yangu.
Musa alimwambia Harun: “Kwa nini hukuwaacha wana wa Israil na kuun- gana nami ulipowaona wanakuasi wewe na kumfuata Msamaria?” Harun akamjibu: “Niliona nikiwaaacha itatokea fitna ya umwagikaji damu baina ya makundi mawili, lililo na imani na lile lilioritadi, hapo ndio utakuwa unaweza kunilaumu na ukaniambaia: umewaacha ili yatokee yaliotokea? Kwa ufupi ni kuwa aliyepo ndiye anayeona hali ilivyo.Musa akakinai na akasema:
“Mola wangu! Nisamehe mimi na ndugu yangu na utuingize katika rehe- ma yako na wewe ni mwenye kurehemu kushinda wote wenye kurehemu.” Juz; 9 (7:151).
Kisha akamwelekea Msamaria na akasema: Una nini wewe Msamaria?
Yaani, ni jambo gani lililokuacha ukafanya uliyoyafanya?
Akasema:Nimeyaona wasiyoyaona wao na nikashika sehemu chache ya mwendo wa Mtume kisha nikaitupa, na hivyo ndivyo ilivyonielekeza nafsi yangu.
Imesemekana kuwa makusudio ya mtume hapa ni mjumbe Jibril; na sehe- mu chache ya mwendo ni mchanga alioukanyaga kwa unyayo wake au kwa kwato za farasi wake. Pia imesemekana kuwa makusudio ya mtume ni Musa na sehemu ya mwendo wake ni desturi yake.
Vile vile imesemekana kuwa Msamria ni muongo na kwamba yeye hakuona chochote katika sehemu ya mwendo wa Mtume; ispokuwa alitaka kujitoa kwa alioyafanya.
Kauli hii ina nguvu kuliko ile ya mguu wa Jibril au farasi wake. Mwenye kutengeneza ndama kwa mkono wake na akataka aabudiwe badala ya Mwenyezi Mungu kusema uongo na uzushi kwake ni jambo jepesi. Ama sauti inawezekana kutengenezwa kwa ndama kwa namna ambayo upepo ukiingia unatoa sauti; kama tulivyoeleza katika Juz. 9 (7: 148).
Vyovyote iwavyo, dhahiri ya maana inayofahamishwa na Qur’an ni kwamba Msamaria ndiye aliyefanya ufisadi, akawapoteza wana wa Israil katika kuabudu ndama. Ama jinsi alivyofanya, hatuna lazima nako kukujua wala hakuna uhusiano wowote na itikadi yetu na maisha yetu.
Akasema (Musa): Basi ondoka na kwa hakika utakuwa katika maisha ukisema: Usiniguse.
Haya ndiyo malipo yako duniani – kutengwa na watu wote, hutachanganyika na watu wala hakuna atakayetaka kuchanganyika na wewe kwa kauli wala vitendo, Ama adhabu yako huko Akhera, itakuwa chungu zaidi. Inasemekana kuwa Msamaria aliishi mwituni na wanyama.
Na hakika una miadi kwako isiyovunjwa.
Hakuna kukimbia wala kuihepa nayo ni kukutana na Mungu na kuhisabi- wa yale uliyoyazua na malipo yako ni adhabu na kuungua na moto.
Na mtazame huyo Mungu wako uliyeendelea kumwabudu; hakika tutamuunguza kisha tutamtawanya baharini atawanyike.
Huu ndio mwisho wa kila mzushi mwenye vitimbi, kuhizika na utwevu.
Hakika Mungu wenu ni Mwenyezi Mungu tu, hapana mungu mwingine ispokuwa Yeye, ujuzi wake umeenea kila kitu.
Yeye peke yake ndiye Mungu wa haki, hakuna muabudiwa ispokuwa Yeye, rehema yake imeenea kwenye kila kitu; na hakuna kitu chochote ispokuwa kinamwabudu na kumsabihi kwa kusifu.
Ni vizuri tumalizie Aya hii kwa yale yalioelezwa katika Tafsir ya Razi. Ninamnukuu: “Ameseam Abul-Qasim Al-Ansariy, amesema: “Wachawi walikuwa ni washirikina, lakini walipoona muujiza mmoja tu wa fimbo kugeuka nyoka, walimwamini Mwenyezi Mungu na Musa, wakavumilia adhabu kali kwa ajili ya imani yao hiyo, wala hawakurudi nyuma. Lakini Wana wa israil waliiona fimbo ilivyovunjilia mbali uchawi, wakawaona wachawi walivyokubali kushindwa; kisha wakaona miujiza mingine tisa, zaidi ya hayo wakaona bahari ilivyopasuka njia kumi na mbili. Pamoja na yote hayo, baada ya kutoka baharini na kuona watu wengine wakiabudu ng’ombe nao wakamwambia Musa tufanyie Mungu kama wao na waliposikia sauti ya ndama tu wakaanza kumwabudu.”
Wakati nikifasiri Aya zinazohusianan na wana wa israil, nimekuwa nikitamani sana, kuundwe kamati ya wataalamu wa maumbile ya binadamu wafanye utafiti juu ya waisral na tabia zao. Wachunguze historia yao na:
11
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
كَذَٰلِكَ نَقُصُّ عَلَيْكَ مِنْ أَنبَاءِ مَا قَدْ سَبَقَ وَقَدْ آتَيْنَاكَ مِن لَّدُنَّا ذِكْرًا ﴿٩٩﴾
99. Namna hivi tunakuhadithia katika habari za yaliotangulia, Na hakika tumekuletea kutoka kwetu mawaidha.
مَّنْ أَعْرَضَ عَنْهُ فَإِنَّهُ يَحْمِلُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وِزْرًا ﴿١٠٠﴾
100. Atakayejitenga nayo basi hakika siku ya Kiyama atabeba mzigo.
خَالِدِينَ فِيهِ وَسَاءَ لَهُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ حِمْلًا ﴿١٠١﴾
101. Watadumu humo. Ni mzigo muovu kwao kuubeba siku ya Kiyama!
يَوْمَ يُنفَخُ فِي الصُّورِ وَنَحْشُرُ الْمُجْرِمِينَ يَوْمَئِذٍ زُرْقًا ﴿١٠٢﴾
102. Siku itakayopulizwa parapanda na tutawakusanya wahalifu siku hiyo wakiwa buluu.
يَتَخَافَتُونَ بَيْنَهُمْ إِن لَّبِثْتُمْ إِلَّا عَشْرًا ﴿١٠٣﴾
103. Watanong’onezana wao kwa wao: ‘Hamkukaa ila siku kumi tu.
نَّحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَقُولُونَ إِذْ يَقُولُ أَمْثَلُهُمْ طَرِيقَةً إِن لَّبِثْتُمْ إِلَّا يَوْمًا ﴿١٠٤﴾
104. Sisi tunayajua zaidi watakayoyasema, atakaposema mbora wao kwa mwendo: ‘Nyinyi hamkukaa ila siku moja tu.’
وَيَسْأَلُونَكَ عَنِ الْجِبَالِ فَقُلْ يَنسِفُهَا رَبِّي نَسْفًا ﴿١٠٥﴾
105. Wanakuuliza kuhusu milima. Sema: Mola wangu ataivurugavuruga.
فَيَذَرُهَا قَاعًا صَفْصَفًا ﴿١٠٦﴾
106. Ataiwacha tambarare iliyo sawa sawa.
لَّا تَرَىٰ فِيهَا عِوَجًا وَلَا أَمْتًا ﴿١٠٧﴾
107. Hutaona humo mabonde wala miinuko.
يَوْمَئِذٍ يَتَّبِعُونَ الدَّاعِيَ لَا عِوَجَ لَهُ وَخَشَعَتِ الْأَصْوَاتُ لِلرَّحْمَـٰنِ فَلَا تَسْمَعُ إِلَّا هَمْسًا ﴿١٠٨﴾
108. Siku hiyo watamfuata muitaji asiye na upotofu, na sauti zote zitamnyenyekea Mwingi wa rehma. Basi hutasikia ila mnong’ono.
يَوْمَئِذٍ لَّا تَنفَعُ الشَّفَاعَةُ إِلَّا مَنْ أَذِنَ لَهُ الرَّحْمَـٰنُ وَرَضِيَ لَهُ قَوْلًا ﴿١٠٩﴾
109. Siku hiyo uombezi hautafaa ila wa aliyemruhusu Mwingi wa rehema na akamridhia kusema.
يَعْلَمُ مَا بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَمَا خَلْفَهُمْ وَلَا يُحِيطُونَ بِهِ عِلْمًا ﴿١١٠﴾
110. Anayajua yalio mbele yao na yalio nyuma yao, wala wao hawawezi kumjua Yeye vilivyo.
وَعَنَتِ الْوُجُوهُ لِلْحَيِّ الْقَيُّومِ وَقَدْ خَابَ مَنْ حَمَلَ ظُلْمًا ﴿١١١﴾
111. Zitanyenyenyekea nyuso kwa Aliye hai, Mwangalizi Mkuu, Na hakika ameharibikiwa mwenye kubeba dhulma.
وَمَن يَعْمَلْ مِنَ الصَّالِحَاتِ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَا يَخَافُ ظُلْمًا وَلَا هَضْمًا ﴿١١٢﴾
112. Na mwenye kutenda mema naye ni mumin, hatahofu dhulma wala kupunjwa.
Aya 99 – 112
Namna hivi tunakuhadithia katika habari za yaliotangulia.
Mwenyezi Mungu anaashiria kisa cha Musa(a.s) na habari zake, Maneno hayo anaambiwa Muhammad(s.a.w.w) . Neno ‘katika’ ni kuelezea baadhi; yaani tunakusimulia baadhi ya habari za umma uliotangulia, kama ulivyosikia. Nazo ni mazingatio na mawaidha kwa watu. Wakati huo huo zinafahamisha ukweli wako na utume wako. Kwa sababu ni habari za ghaibu.
Na hakika tumekuletea kutoka kwetu mawaidha.
Makusudio ya mawaidha hapa ni Qur’an. Imeitwa hivyo kwa sababu ndani yake kuna utajo wa Mwenyezi Mungu na sifa zake, mitume na habari zao, akhera na mambo yake, imani na ukafiri, kheri na shari, halali na haramu, kuumbwa mbingu na ardhi na mengineyo.
Atakayejitenga nayo basi hakika siku ya Kiyama atabeba mzigo.
Kila mwenye kuipinga Qur’an kwa kauli na vitendo au kwa vitendo bila ya kauli, basi atakuwa amejitenga nayo na atakuwa ameibebesha nafsi yake mzigo mzito. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) amesema: “Hakuiamini Qur’an yule anayehalalisha yaliyo haramu” Yatakuja maelezo zaidi kwenye Aya ya 124 ya Sura hii, inshaallah.
Watadumu humo.
Yaani humo mwenye mizigo, Adhabu kuiita mizigo ni katika kutumia sababu kwa msabibishi.
Ni mzigo muovu kwao kuubeba siku ya Kiyama!
Yaani mzigo wa madhambi walioubebesha nafsi zao kwa sababu ya kujtenga kwao na Qur’an.
Siku itakayopulizwa parapanda.
Hiki ni kinaya cha kufufuliwa walioko makaburini.
Na tutawakusanya wahalifu siku hiyo wakiwa buluu.
Hii pia ni kinaya cha kufazaika kwao na hali mbaya watakayokuwa nayo. Ya kushangaza ni yale niliyoyasoma katika Tafsir Al-Bahru-Muhit ya Abu Hayan Al-Andalusi, akisema: “Makusudio ya ubuluu ni ubuluu wa macho, na macho ya buluu yanachukiza sana kwa waarabu kwa sababu maadui zao waroma wana macho ya buluu.” Mfasiri huyu alikuwa karibu na wakati wa vita vya msalaba (Crusade).
Watanong’onezana wao kwa wao: Hamkukaa ila siku kumi tu.
Miongoni mwa sifa za wahalifu siku ya Kiyama nikuwa wao kutokana na vituko watakavyopambana navyo, watasahau muda wa kukaa kwao katika maisha ya dunia.
Kwa hiyo wataambiana kwa lugha ya maneno au kwa lugha ya hali kwa sauti ya chini: Hatukukaa ispokuwa siku kumi au masaa kadhaa au kitambo kidogo tu.
Unaweza kuuliza : Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya hii, amewazungumzia kuwa watasema tumekaa siku kumi, katika Sura Kahf, Aya 19 amesema, siku moja au sehemu ya siku; na katika Sura Rum, Aya 55, watasema kuwa hawakukaa ispokuwa saa moja. Je, kuna wajihi gani wa kuchanganya Aya zote hizo?
Razi amejibu kuwa baadhi ya wahalifu wataona ni siku moja wengine kumi. Tuonavyo sisi ni kuwa neno kumi, siku au saa katika Aya sio kuzungumzia kauli halisi ya wahalifu; ispokuwa ni kinaya cha vile watakavyowazia uchache wa muda na kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) hayo ameyaletea ibara ya kumi, mara nyingine siku na hata saa. Mwenyezi Mungu ameyaashiria haya kwa kauli yake: “Siku atakayowaita nanyi mkamwitikia kwa kumsifu. Na mkadhani kuwa hamkukaa ila muda mchache tu.” Juz.15 (17:52).
Sisi tunayajua zaidi watakayoyasema, atakaposema mbora wao kwa mwendo: Nyinyi hamkukaa ila siku moja tu.
Mbora wao kwa mwendo ni yule mwenye sera nzuri na mwenye kujua hakika ya mambo. Maana ni kuwa wakati wanapoambiana kuwa tumekaa siku kumi tu, huyo mbora wao atawaambia: Maisha mliyokuwa nayo mkishindana, si chochote ispokuwa ni kama ndoto tu, hayawezi kuhisabiwa kwa wakati wala kwa siku. Maisha ya uhakika hasa ni haya tuliyo nayo hivi sasa, ambayo hayana muda wala mwisho.
Wanakuuliza kuhusu milima, Sema: Mola wangu ataivurugavuruga. Ataiwacha tambarare iliyo sawasawa, Hutaona humo mabonde wala miinuko.
Muulizaji alimuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) kuwa vipi milima itakavyokuwa siku ya kiyama? Mwenyezi Mungu akamwambia mtume wake Mtukufu: mjibu Aliyeuliza sawali hili kuwa Mwenyezi Mungu ataing’oa na ataigeuza kuwa ni mavumbi yatakayotawanyika angani na pale ilipokuwa patakuwa tambarare bila ya mabonde wala miinuko.
Siku hiyo watamfuata muitaji asiye na upotofu.
Siku hiyo ni siku ya Kiyama, watakofuata ni viumbe na muitaji ni yule atakayewaita viumbe kwenye mkusanyiko, hisabu na malipo. Maana ni kuwa mwito utakuwa wa haki na utaitikiwa na wote, hakuna atakayeweza kuuhalifu: “Siku atakapoita muitaji kuliendea jambo linalochusha; macho yao yatainama; watatoka makaburini kama nzige waliotawanyika; wanamkimbilia muitaji na makafiri watasema: Hii ni siku ngumu. (54:6-9).
Na sauti zote zitamnyenyekea Mwingi wa rehma. Basi hutasikia ila mnong’ono.
Makusudio ya sauti ni wenye sauti hizo, Na mnong’ono unafahamisha unyenyekevu.
Siku hiyo uombezi hautafaa ila wa aliyemruhusu Mwingi wa rehema na akamridhia kusema.
Hii iko katika maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu: “Wala hawaombei ila yule Aliemridhia” (21:28). Tumeazungumzia shafaa kwa urefu katika Juz; 1 (2:97).
Anayajua yalio mbele yao na yalio nyuma yao wala wao hawawezi kumjua Yeye vilivyo.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 3 (2:255).
Zitanyenyenyekea nyuso kwa Aliye hai, Mwangalizi Mkuu.
Makusudio ya nyuso ni walio na nyuso hizo. Maana ni kuwa viumbe wote kesho watasalimu amri mbele ya Aliye hai, asiyekufa na Msimamizi wa kila jambo wala hakuna kinachosimamiwa ila kwa ajili yake.
Na hakika ameharibikiwa mwenye kubeba dhulma.
Mwenye hasara zaidi katika watu kesho ni yule mwenye kuwadhulumu watu na akaingilia heshima na uhuru wao. Na mwenye faida mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule mwenye kufanya kwa ajili ya kheri ya binadamu na masilahi kwa njia ya kheri na ya ubinadamu.
Na mwenye kutenda mema naye ni mumin, hatahofu dhulma wala kupunjwa.
Hii ni sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu: “Mwenye kutenda mema, mwanamume au mwanamke, naye akawa ni mumin tutamhuisha maisha mema; na tutawapa ujira wao kwa mazuri zaidi waliyokuwa wakiyafanya.” Juz; 14 (16: 97).
وَكَذَٰلِكَ أَنزَلْنَاهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا وَصَرَّفْنَا فِيهِ مِنَ الْوَعِيدِ لَعَلَّهُمْ يَتَّقُونَ أَوْ يُحْدِثُ لَهُمْ ذِكْرًا ﴿١١٣﴾
113. Namna hiyo tumeiteremsha Qur’an kwa lugha ya kiarabu na tumekariri humo maonyo ili wawe na takua au iwaletee makumbusho.
فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ وَلَا تَعْجَلْ بِالْقُرْآنِ مِن قَبْلِ أَن يُقْضَىٰ إِلَيْكَ وَحْيُهُ وَقُل رَّبِّ زِدْنِي عِلْمًا ﴿١١٤﴾
114. Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa haki, Wala usiifanyie haraka hii Qur’an kabla haujamalizika wahyi wake, Na sema: Mola wangu! Nizidishie elimu.
وَلَقَدْ عَهِدْنَا إِلَىٰ آدَمَ مِن قَبْلُ فَنَسِيَ وَلَمْ نَجِدْ لَهُ عَزْمًا ﴿١١٥﴾
115. Na hapo zamani tuliagana na Adam, lakini alisahau wala hatukuona kwake azma.
وَإِذْ قُلْنَا لِلْمَلَائِكَةِ اسْجُدُوا لِآدَمَ فَسَجَدُوا إِلَّا إِبْلِيسَ أَبَىٰ ﴿١١٦﴾
116. Na tulipowaambia Malaika: Msujudieni Adam! Wakasujudu wote ispokuwa Iblisi alikataa.
فَقُلْنَا يَا آدَمُ إِنَّ هَـٰذَا عَدُوٌّ لَّكَ وَلِزَوْجِكَ فَلَا يُخْرِجَنَّكُمَا مِنَ الْجَنَّةِ فَتَشْقَىٰ ﴿١١٧﴾
117. Tukasema: Ewe Adam! Hakika huyu ni adui yako na wa mkeo, Basi asiwatoe katika Bustani (Pepo) hii, mkaingia mashakani.
إِنَّ لَكَ أَلَّا تَجُوعَ فِيهَا وَلَا تَعْرَىٰ ﴿١١٨﴾
118. Hakika humo hutakuwa na njaa wala hutakuwa uchi.
وَأَنَّكَ لَا تَظْمَأُ فِيهَا وَلَا تَضْحَىٰ ﴿١١٩﴾
Na kwamba wewe hutapata kiu humo wala hutapata joto.
فَوَسْوَسَ إِلَيْهِ الشَّيْطَانُ قَالَ يَا آدَمُ هَلْ أَدُلُّكَ عَلَىٰ شَجَرَةِ الْخُلْدِ وَمُلْكٍ لَّا يَبْلَىٰ ﴿١٢٠﴾
120. Lakini shetani alimtia wasi- wasi, akamwambia: Ewe Adam! Nikujulishe mti wa kuishi milele na ufalme usiokoma?
فَأَكَلَا مِنْهَا فَبَدَتْ لَهُمَا سَوْآتُهُمَا وَطَفِقَا يَخْصِفَانِ عَلَيْهِمَا مِن وَرَقِ الْجَنَّةِ وَعَصَىٰ آدَمُ رَبَّهُ فَغَوَىٰ ﴿١٢١﴾
121. Basi wakaula wote na uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Bustani. Na Adam akamuasi Mola wake na akapotea njia.
ثُمَّ اجْتَبَاهُ رَبُّهُ فَتَابَ عَلَيْهِ وَهَدَىٰ ﴿١٢٢﴾
122. Kisha Mola wake akamteua na akamkubalia toba yake naakamwongoa.
TUMEITERMSHA QUR’AN KWA LUGHA YA KIARABU
Aya 113 – 122
Namna hiyo tumeiteremsha Qur’an kwa lugha ya kiarabu na tumekariri humo maonyo ili wawe na takua au iwaletee makumbusho.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameteremsha Qur’an kwa mja wake Muhammad(s.a.w.w) kwa lugha ya kiarabu na akawahadharisha waja na hisabu yake na adhabu yake, kwa mifumo mbalimbali, ili wapate kumcha na kumtii kwenye hukumu zake zote au awamkumbuke yeye wanapofanya madhambi ili watubu na wamwombe msamaha. Au hapa, ni kwa maana ya na; kama mfano ukisema: “Kuwa mwana wa chuoni au mwenye zuhudi.” Kwa sababu kukumbuka kuko pamoja na takua; kama ambavyo zuhudi iko pamoja na elimu.
Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 12 (12:2). Huko tumejibu kwa ufafanuzi swali la mwenye kuuliza, kwa nini Qur’an imeteremshwa kwa lugha ya kiarabu pamoja na kuwa Muhammad (s.a.w.) ametumwa kwa watu wote?
Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameitaja Qur’an, katika kitabu chake kitukufu, kwa sifa nyingi, zikiwemo hizi zifuatazo:
1. Ya kiarabu; kama ilivyo katika Aya hii na ile ya Juz. 12 (12:2).
2. Ukumbusho:
إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ ﴿٩﴾
“Na hakika sisi tumeuteremsha ukumbusho huu” Juz; 14 : (15:9).
3. Nuru:
قَدْ جَاءَكُم مِّنَ اللَّـهِ نُورٌ وَكِتَابٌ مُّبِينٌ ﴿١٥﴾
“Hakika imekwishawafikia nuru kutoka kwa Mwenyezi Mungu” Juz. 6: (5:15).
4. Upambanuzi:
إِنَّهُ لَقَوْلٌ فَصْلٌ ﴿١٣﴾
“Hakika hiyo ni kauli ya upambanuzi” (86:13).
5. Uongofu: “Hicho ni kitabu, hakina shaka ndani yake, ni uongofu kwa wenye takua.” Juz; 1 (2:2).
6. Hekima:
وَالْقُرْآنِ الْحَكِيمِ ﴿٢﴾
“Naapa kwa Qur’an yenye hekima” (36:2).
وَالْقُرْآنِ الْمَجِيدِ ﴿١﴾
“Naapa kwa Qur’an Tukufu” (50:1).
7. Roho:
رَفِيعُ الدَّرَجَاتِ ذُو الْعَرْشِ يُلْقِي الرُّوحَ مِنْ أَمْرِهِ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ مِنْ عِبَادِهِ لِيُنذِرَ يَوْمَ التَّلَاقِ ﴿١٥﴾
“Hupeleka Roho kwa amri yake juu ya amtakaye katika waja wake, ili kuonya kwa siku ya makutano” (40:15).
8. Haki:
إِنَّهُ الْحَقُّ مِن رَّبِّكَ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٧﴾
Hakika hiyo ni haki itokayo kwa Mola wako, Lakini watu wengi hawaamini, Juz; 12 (11:17).
9. Habari kubwa:
قُلْ هُوَ نَبَأٌ عَظِيمٌ ﴿٦٧﴾ أَنتُمْ عَنْهُ مُعْرِضُونَ ﴿٦٨﴾
“Sema: Hiyo ni habari kubwa ambayo nyinyi mnaipuuza.” (38:67–68).
10. Ponyo:
قُلْ هُوَ لِلَّذِينَ آمَنُوا هُدًى وَشِفَاءٌ ﴿٤٤﴾
“Sema: hiyo ni uongofu na ponyo kwa wenye kuamini” (41:44).
11. Rehema:
وَإِنَّهُ لَهُدًى وَرَحْمَةٌ لِّلْمُؤْمِنِينَ ﴿٧٧﴾
Na hakika hiyo ni uwongofu na rehema kwa waumini, (27:77).
12. Uteremsho:
تَنزِيلٌ مِّن رَّبِّ الْعَالَمِينَ ﴿٨٠﴾
Ni uteremsho utokao kwa Mola wa walimwengu wote (56:80).
13. Bishara na onyo:
قُرْآنًا عَرَبِيًّا لِّقَوْمٍ يَعْلَمُونَ ﴿٣﴾ بَشِيرًا وَنَذِيرًا ﴿٤﴾
Ni Kitabu kilichopambanuliwa Aya zake, cha kusomwa kwa kiarabu kwa watu wanaojua, kinachotoa bishara na kuonya (41:3 – 4).
14. Nguvu na utukufu:
وَإِنَّهُ لَكِتَابٌ عَزِيزٌ ﴿٤١﴾
“Na hakika ni Kitabu chenye nguvu na utukufu.” (41:41).
15. Adhimu:
وَلَقَدْ آتَيْنَاكَ سَبْعًا مِّنَ الْمَثَانِي وَالْقُرْآنَ الْعَظِيمَ ﴿٨٧﴾
Na hakika tumekupa Aya saba zinazorudiwa rudiwa na Qur’an Adhimu, Juz; 14 (15:87).
16. Ubainifu:
وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ ﴿٢﴾
Naapa kwa Kitabu kinachobainisha (43:2).
Hakika bora zaidi inayofahamisha sifa hizi ni kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ameteremsha Qur’an kwa Mtume wake, kwa ajili tu ya kuwaongoza watu kwenye wema, amani na utulivu wao.
Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa haki.
Imam Ali(a.s) anasema, akilingania Mola wake:“Kutakata ni kwako! Ni utukufu ulioje wa tunayoyaona katika uumbaji wako! Na udogo ulioje wa hayo katika uweza wako! Na ni vituko vilioje wa tuvionavyo katika ufalme wako! Na ni uduni ulioje wa tusivyoviona katika ufalme wako! Na ueneaji ulioje wa neema zako katika dunia! Na ni udogo ulioje wa neema hizo kulinganisha na neema za Akhera!”
Wala usiifanyie haraka hii Qur’an kabla haujamalizika wahyi wake
Kuna Hadith isemayo kuwa Nabii wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alikuwa anapoletewa Qur’an na Jibril hufuatilia kuisoma kwa kuhofia kisimpite kitu, ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha asikilize tu wala asifuatishe na kwamba atulie tu wala asiogope kusahau. Usahihi wa Hadith hii unafahamishwa na ile Aya isemayo:
“Usiutikisie, huu wahyi, ulimi wako kwa kuufanyia haraka, Hakika ni juu yetu kuukusanya na kuusomesha, kisha ni juu yetu kuubainisha” (75: 16 – 19).
Na sema: Mola wangu! Nizidishie elimu
Elimu aliyomwamrisha Mwenyezi Mungu Mtume wake, kuomba kuzidishiwa ni ile inayomnufaisha mwenye nayo na mwenginewe. Hakuna itikadi wala misimamo, falsafa wala sharia au fasihi na sanaa, zote hizi si lolote mbele ya Mwenyezi Mungu ispokuwa kama zitakuwa ni nyenzo za maisha bora yasiyokuwa na matatizo wala vikwazo vyovyote.
Hata maisha ya Akhera yanafungamana moja kwa moja na kazi itakayon- ufaisha katika maisha ya duniani. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anasema: “Mbora zaidi wa watu mbele ya Mwenyezi Mungu ni yule anayewafaa zaidi watu.” Hakuna mwenye shaka kwamba anayewafaa zaidi watu ni yule anayefanya kwa ajili ya maisha bora na jamii.
Kila kitu, wakati huu, kinafahamisha waziwazi kuwa hakuna maisha bora ispokuwa kwa elimu; bila ya kutofautisha baina ya maisha ya kimaada, kijamii na kiutamaduni.
Kama ambavyo jamii yoyote haiwezi kuishi maisha bora bila ya mitambo ya kuchapisha, viwanda vya nguo, nyenzo za mawasiliano, vifaa vya nyumbani na maengineyo ya lazima; basi vile vile haiwezekani kuishi huru na heshima bila ya elimu ya siasa, uchumi, ya kijamii na elimu nyinginezo zinazofanya kazi ya kumtumikia mtu kwa ajili ya utu.
Hii ndiyo elimu sahihi na ndiyo iliyokusudiwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: ‘Na sema: Mola wangu! Nizidishie elimu’ na kauli ya Mtume: “Mwenye kufuata njia ya kutafuta elimu, amefuata njia ya kwenda peponi.”
Yeyote mwenye kufasiri neno elimu kwa maana ya kuhifadhi maandishi na maelezo, basi huyo ni katika wale wanaoamini kuwa elimu ni matamshi na maandishi tu; na dini ni kupiga takbira na kusoma tasbih tu.
Na hapo zamani tuliagana na Adam, lakini alisahau wala hatukuona kwake azma.
Maagano Alioagana Mwenyezi Mungu na Adam ni kutoukurubuia mti na kwamba asisikilize mwito wa Iblis. Makusudio ya kusahau ni kuacha na azma ni uthabiti.
Na tulipowaambia Malaika: Msujudieni Adam! Wakasujudu wote ispokuwa Iblisi alikataa.
Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz; 1 (2:34), Juz; 8 (7:11), Juz. 14 (15: 30 – 31), na katika Juz. 15 ( 17: 61) na (18:50).
Tukasema: Ewe Adam! Hakika huyu ni adui yako na wa mkeo, Basi asiwatoe katika Bustani (Pepo) hii, mkaingia mashakani. Hakika humo hutakuwa na njaa wala hutakuwa uchi, Na kwamba wewe hutapata kiu humo wala hutapata joto.
Yaani hutatabika kwenye joto la jua, Neno joto tumelifasiri kutoka neno Dhuha lenye maana ya mchana, Umetumika mchana kwa maana ya joto kwa vile mchana kunakuwa na joto kali.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) alimuhadharisha Adam kutokana na wasiwasi wa Ibilisi na akamwambia, wewe una hiyari ya mambo mawili; ama unitii mimi na umuasi Ibilisi upate hii Pepo (Bustani) – kama uinavyo – safi na nzuri. Humo hamna njaa, kiu, kukaa uchi wala maradhi, Hamna maumivu wala huzuni, hamna mauti, damu wala machozi, hamna kuhangaika kwenye joto wala baridi, Hamna chochote ispokuwa amani, utulivu na raha.
Au uniasi mimi na kumtii Ibilisi, utoke Peponi uende duniani kwenye taabu, balaa zote, magonjwa na majanga.
Lakini Adam alisahau hadhari hizi; akaandamwa na misukosuko yeye na kizazi chake, kuanzia na kuuliwa Habil hadi uhalifu wa Israil na mengineyo yasiyokuwa na kikomo.
Sio mbali kuwa kutolewa Adam Peponi ni somo na fundisho kwa yule anayefuata matamanio na kwamba malipo yake mbele ya Mwenyezi Mungu ni adhabu, Angalia kifungu ‘Mtaka yote hukosa yote’ Juz; 1 (2: 35–39).
Lakini shetani alimtia wasiwasi, akamwambia: Ewe Adam! Nikujulishe mti wa kuishi milele na ufalme usiokoma? Basi wakaula wote na uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Bustani.
Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz; 8 (7:19 – 22).
Na Adam akamuasi Mola wake na akapotea njia.
Unaweza kuuliza : Adam ni nabii na nabii ni maasumu wa makosa, imekuwaje Mwenyezi Mungu (s.w.t) kumnasibishia uasi na upotevu?
Wamelijibu hilo kwa majibu kadhaa; miongoni mwayo ni kuwa makusudio ya kuasi ni kuacha mapendekezo sio wajibu, jambo ambalo halipingani na isma.
Jibu jingine ni kuwa Adam alipokuwa Peponi alikuwa Akhera ambako hakuna tabligh wala taklifa yoyote ya kuhitajia mitume, na kwamba utume wa Adam ulikuwa wa duniani sio wa Akhera.
Kwa hali yoyote iwayo ni kwamba Adam alitubia na akamuomba msamaha Mola wake;kisha Mola wake akamteua na akamkubalia toba yake na akamwongoa.
Tumeuazungumzia hayo kwa ufafanuzi zaidi katika Juz; 1 (2:35–39) kifungu cha ‘isma ya mitume.
12
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA
قَالَ اهْبِطَا مِنْهَا جَمِيعًا بَعْضُكُمْ لِبَعْضٍ عَدُوٌّ فَإِمَّا يَأْتِيَنَّكُم مِّنِّي هُدًى فَمَنِ اتَّبَعَ هُدَايَ فَلَا يَضِلُّ وَلَا يَشْقَىٰ ﴿١٢٣﴾
123. Akasema: Ondokeni humu nyote; hali ya kuwa ni maadui nyinyi kwa nyinyi, Na ukiwafikia uongofu kutoka kwangu, basi atakayefuata uongofu wangu, hatapotea wala hatataabika.
وَمَنْ أَعْرَضَ عَن ذِكْرِي فَإِنَّ لَهُ مَعِيشَةً ضَنكًا وَنَحْشُرُهُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ أَعْمَىٰ ﴿١٢٤﴾
124. Na atakayejiepusha na mawaidha yangu, basi hakika atapata maisha yenye dhiki, Na tutamfufua siku ya Kiyama hali ya kuwa kipofu.
قَالَ رَبِّ لِمَ حَشَرْتَنِي أَعْمَىٰ وَقَدْ كُنتُ بَصِيرًا ﴿١٢٥﴾
125. Aseme: Ewe Mola wangu! Mbona umenifufua kipofu, nami nilikuwa nikiona?.
قَالَ كَذَٰلِكَ أَتَتْكَ آيَاتُنَا فَنَسِيتَهَا وَكَذَٰلِكَ الْيَوْمَ تُنسَىٰ ﴿١٢٦﴾
126. Atasema (Allah): Ndivyo hivyo hivyo. Zilikufikia ishara zetu, nawe ukazisahahu na kadhalika leo unasahauliwa.
وَكَذَٰلِكَ نَجْزِي مَنْ أَسْرَفَ وَلَمْ يُؤْمِن بِآيَاتِ رَبِّهِ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَشَدُّ وَأَبْقَىٰ ﴿١٢٧﴾
127. Na hivyo ndivyo tutakavy- omlipa kila apitaye kiasi na asiyeamini ishara za Mola wake. Na Hakika adhabu ya Akhera ni kali zaidi na inadumu.
أَفَلَمْ يَهْدِ لَهُمْ كَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّنَ الْقُرُونِ يَمْشُونَ فِي مَسَاكِنِهِمْ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّأُولِي النُّهَىٰ ﴿١٢٨﴾
128. Je, haikuwabainikia, ni vizazi vingapi tuliviangamiza kabla yao nao wanatembea katika maskani zao. Hakika katika hayo kuna Ishara kwa kwa wenye akili.
وَلَوْلَا كَلِمَةٌ سَبَقَتْ مِن رَّبِّكَ لَكَانَ لِزَامًا وَأَجَلٌ مُّسَمًّى ﴿١٢٩﴾
129. Na lau si neno la Mola wako lililokwishatangulia kutoka kwa Mola wako na muda uliotajwa, bila shaka ingelikuwa lazima.
Aya 123 – 129
Akasema: ‘Ondokeni humu nyote; hali ya kuwa ni maadui nyinyi kwa nyinyi, Na ukiwafikia uongofu kutoka kwangu, basi atakayefuata uon- gofu wangu, hatapotea wala hatataabika.
Aliyesema ni Mwenyezi Mungu na wanaoambiwa watoke ni Adam na mkewe Hawa. Makusudio ya nyinyi kwa nyinyi ni kizazi cha Adam na Iblisi. Uongofu ni maamrisho ya Mwenyezi Mungu na makatazo yake.
Mwenye kumtii Mwenyezi Mungu katika amri yake na makatazo yake, basi yeye ni katika walioongokoka duniani na wenye kupata mema Akhera. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz, 1 (2:36).
Na atakayejiepusha na mawaidha yangu, basi hakika atapata maisha yenye dhiki.
Unaweza kuuliza : dhahiri ya Aya inafahamisha kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t) amepitisha na amekadiria kuwa waasi walio mataghuti waishi katika maisha ya tabu na dhiki, lakini tuyaonayo ni kinyume na hivyo; kila wanavyozidi kuwa na uasi na utaghuti ndivyo wanavyozidi kuwa na jaha na mali?
Wafasiri wamejibu kuwa makusudio ya dhiki, hapa, ni jakamoyo walilon- alo na hadhari ya mwisho mbaya wa ghafla pamoja na tabu baada ya raha.
Lakini inavyoonekana ni kuwa hali hii anayo kila mwenye nacho; awe mtiifu au muasi. Kwa sababu tabia ya hali haipambanui baina ya mwema na muovu, majanga yake hayamuhurumii mdogo wala myonge, wala haijali mawalii au watu wema.
Jawabu lilo na nguvu zaidi ni yale tuliyoyataja katika Juz; 6 (5:64 – 66) kifungu cha ‘Riziki na ufisadi, Vile vile katika Juz; 7 (5: 100) kifungu cha ‘Je, riziki ni bahati au majaaliwa.
Kwa ujumla ni kuwa ufukara unahukumiwa ardhini si mbinguni; ni katika mambo walioyafanya watu kwa mikono yao, wale ambao wameua haki na uadilifu. Lau wangeliisimamisha sharia ya Mungu, asingalipatikana ardhi- ni hata fukara mmoja.
Na tutamfufua siku ya Kiyama hali ya kuwa kipofu.
Baadhi ya wafasiri wanasema kuwa makusudio ya upofu hapa ni upofu wa hoja na dalili; wengine wakasema ni upofu wa Pepo. Lakini ilivyo hasa ni kuwa makusudio ni kwa maana yake yalio dhahiri, ya kutoona, bila ya kuweko haja ya taawili; kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
Aseme: Ewe Mola wangu! Mbona umenifufua kipofu, nami nilikuwa nikiona? Atasema: Ndivyo hivyo hivyo. Zilikufikia ishara zetu, nawe ukazisahahu na kadhalika leo unasahauliwa.
Yaani, leo wewe unapuuzwa, kama ulivyopuuza hapo mwanzo. Kwa ufupi ni kuwa mwenye kuwa na matendo mabaya hapa duniani atakuwa na mwisho mbaya huko akhera.
Aya hii ni dalili iliyowazi zaidi kwamba matendo ya duniani ndio asili na malipo ya akhera ni tanzu, na kwamba hakuna njia nyingine ya kupata neema yake ispokuwa kwa amali njema.
Pamoja na kuwa Qur’an tukufu inaunganisha Uislamu na maisha na matendo na malipo, lakini vijana wetu wengi wanasema kuwa dini ni upotofu na vigano. Sababu yao katika hilo ni kutoujua Uislamu na kuwa mbali na maarifa ya uhakika wake na siri zake.
Na hivyo ndivyo tutakavyomlipa kila apitaye kiasi katika kuitafuta duniana asiyeamini ishara za Mola wake zinazofahamisha kuweko kwake na utume wa mitume yake na kuteremshwa vitabu vyake. Au anayeamini yote hayo, lakini hafanyi kwa matendo.
Na Hakika adhabu ya Akhera, ikiwemo nguo za lami, chakula cha Zaqum, kinywaji cha moto na makomeo ya chuma, ni kali zaidi na inadumu, kuliko kutokea upofu na kusahau.
Je, haikuwabainikia, ni vizazi vingapi tuliviangamiza kabla yao nao wanatembea katika maskani zao.
Wanaambiwa washirikina kuwa vipi wanendelea na kung’ania ushirikina baada ya kupewa mwito wa tawhid na hali Mwenyezi Mungu amewabain- ishia njia za uongofu kwenye tawhid; zikiwemo kuangamizwa uma zilizopita; kama vile kaumu ya Nuh, A’d na Thamud waliokuwa na nguvu, mali na watu wengi.
Mwenyezi Mungu akawapelekea Mitume, watoa bishara na maonyo, kama alivyomtuma Muhammad kwa washirikina wa kikuraishi, wakaasi na Mwenyezi Mungu akawaangamiza kwa kufuru yao na uasi wao, wakiwa wametulia kwa amani. Je washirikiana wa kikuraishi wameaminisha kuji- wa na adhabu ya ghafla, kama ilivyowajia walikowa kabla yao?
Hakika katika hayo kuna ishara kwa kwa wenye akili, kwamba yaliowapitia waliopita ni mazingatio na mawaidha kwa watu wenye akili walioko sasa.
Na lau si neno la Mola wako lililokwishatangulia kutoka kwa Mola wako na muda uliotajwa, bila shaka ingelikuwa lazima, kuwafikia adhabu.
Makusudio ya neno na muda uliotajwa ni kupitisha kwake Mwenyezi Mungu. Yaani lau si kupitisha kwake na hekima yake Mwenyezi Mungu ya kuahirisha adhabu hadi muda uliowekwa kwa washirikina wa kikuraishi, basi bila shaka ingeliwafikia tu.
فَاصْبِرْ عَلَىٰ مَا يَقُولُونَ وَسَبِّحْ بِحَمْدِ رَبِّكَ قَبْلَ طُلُوعِ الشَّمْسِ وَقَبْلَ غُرُوبِهَا وَمِنْ آنَاءِ اللَّيْلِ فَسَبِّحْ وَأَطْرَافَ النَّهَارِ لَعَلَّكَ تَرْضَىٰ ﴿١٣٠﴾
130. Fanya subra na wayasemayo. Na umsabihi Mola wako kwa kumsifu kabla ya mawiyo jua na kabla ya machweo yake. Na nyakati za usiku pia umsabihi, na ncha za mchana, ili uridhike.
وَلَا تَمُدَّنَّ عَيْنَيْكَ إِلَىٰ مَا مَتَّعْنَا بِهِ أَزْوَاجًا مِّنْهُمْ زَهْرَةَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا لِنَفْتِنَهُمْ فِيهِ وَرِزْقُ رَبِّكَ خَيْرٌ وَأَبْقَىٰ ﴿١٣١﴾
131. Wala usivikodolee macho tulivyowastarehesha aina ya watu miongoni mwao, kwa mapambo ya duniani ili tuwajaribu. Na riziki ya Mola wako ni bora na yenye kudumu zaidi.
وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا لَا نَسْأَلُكَ رِزْقًا نَّحْنُ نَرْزُقُكَ وَالْعَاقِبَةُ لِلتَّقْوَىٰ ﴿١٣٢﴾
132. Na uwaamrishe watu wako kuswali na uwe na subira nayo. Hatukuombi riziki, Sisi tunakuruzuku wewe, Na mwisho mwema ni kwa mwenye takua.
Aya 130-132
Fanya subra na wayasemayo.
Washirikina walimkadhibisha Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , wakamwambia ni mchawi, mshairi, mzushi na hata mwenda wazimu; ndipo Mwenyezi Mungu akamwamrisha awe na subira kwa sababu subira huvuta kheri.
Na umsabihi Mola wako kwa kumsifu.
Makusudio ya kumsabihi hapa sio kusoma tasbihi tu, bali ni pamoja na kumwelekea na kumtegemea Yeye tu.
Kabla ya mawiyo jua ni kuashiria swala ya Alfajirina kabla ya mach- weo yake ni swala ya Alasirina nyakati za usiku pia umsabihi ni swala ya Maghrib na Ishana ncha za mchana ni Swala ya Adhuhuri.
Limetumika neno ncha ya mchana kwa maana ya katikati ya mchana, kwa kuangalia kuwa ni ncha ya mwisho ya nusu ya kwanza ya mchana na ncha ya mwanzo ya nusu ya pili yake.
Sio mbali kuwa makusudio ya nyakati hizi ni amri ya kumkumbuka Mwenyezi Mungu kila wakati; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Ambao wanamataja Mwenyezi Mungu katika hali ya kusimama na kukaa na kulala” Juz. 4 (3:191).
Ili uridhike.
Kila anayemridhisha Mwenyezi Mungu duniani, humridhia Mwenyezi Mungu Akhera, Mwenyezi Mungu yuko radhi nao na wao wako radhi naye (98:9).
Wala usivikodolee macho tulivyowastarehesha aina ya watu miongoni mwao, kwa mapambo ya duniani ili tuwajaribu. Na riziki ya Mola wako ni bora na yenye kudumu zaidi.
Makusudio ya usikodolee ni usitilie umuhimu; baadhi ni aina ya makafiri, wawe washirikina au watu wa kitabu.
Maana ni kuwa usijishughulishe ewe Muhammad na utajiri na unayoyaona kwa makafiri wa aina yoyote; wawe washirikina, wanaswara au mayahudi. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaka kuwapa mali ili idhihiri hakika yao na awalipe kwa kupituka kwao mipaka.
Imam Ali(a.s) anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu anawajaribu kwa mali na watoto, ili abainike anayeichukia riziki ya Mwenyezi Mungu na anayeiridhia; ingawaje Mwenyezi Mungu (s.w.t) anajua zaidi hakika yao, lakini ni kudhihirisha vitendo ambavyo vinastahiki thawabu na adhabu.”
Katika Tafsir At-Twabariy imeelezwa kwamba Mtume(s.a.w.w) alituma kwa Myahudi akopeshwe, lakini yule myahudi akakataa ispokuwa kwa rahani Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) akahuzunika, ndipo ikashuka Aya hii. Ni sawa riwaya hii iwe sahihi au la, lakini ni mfano wazi wa kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Wala usivikodolee macho tulivyowastarehesha aina ya watu miongoni mwao, kwa mapambo ya duniani’
Sisi hivi sasa tuko katika mwaka 1969; kiasi cha miaka 35, aliaandika mwandishi mashuhuri, Aliyeitwa Mustafa Sadiq Arrafi’y, makala mbili kuhusu ufukara wa Mtume(s.a.w.w) yenye kichwa cha maneno: Ufukara mtukufu.
Tutanukuu kutoka katika makala hizo jumla zifutazo pamoja na nyongeza kidogo katika baadhi ya matamko, ili kuleta ufafanuzi:
Ni jambo la kushangaza katika maisha kwa mtu fukara kuendelea na ufukara naye anajua kuwa kazi yake katika mji ni kufanya watu wawe matajiri, Na kuwa mtu tajiri anaendelea na utajiri na anajua kuwa kazi yake ni kuwafanya watu wawe mafukara.
Muhammad(s.a.w.w) aliishi fukara, lakini ufukara wake ulikuwa ukihisabi- ka kuwa ni katika muujiza wake mikubwa ambao hakuugundua yeyote hadi sasa. Muhammad(s.a.w.w) alikuwa akimiliki mali, lakini alikuwa akiitoa kwa haraka kuliko upepo, hakutaka izaliane kwake; bali haikuwa ikitulia kwake.
Alikuwa – naye ndiye bwana mkubwa wa uma wake na mwenye sharia – ni mtu fukara akijitaabisha kutafuta maisha yake, siku nyingine anabaki na njaa na siku nyingine anashiba. Lengo lake la kwanza katika hilo ni kuuthibisha umoja wa ubinadamu na kuleta uuwiano baina ya watu na ajue kila mtu kwamba tatizo lake ni tatizo la jamii na kwamba mafanikio yake yawe mafanikio ya wote, sio kula mafanikio ya wengine ili waangamie.”
Na uwaamrishe watu wako kuswali na uwe na subira nayo.
Kuwa na subira na swala ni kutoathiriwa na jambo lolote. Katika Tafsir Arrazi, imeelezwa kuwa baada ya kushuka Aya hii Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alikuwa akienda kwa Fatima(a.s) kila asubuhi na kusema: Swala! Swala! Alifanya hivyo kwa miezi kadhaa.
Hatukuombi riziki.
Yaani wewe huuombwi riziki ya yoyote, si chakula chake wala kinywaji chakeSisi tunakuruzuku wewe na familia yako.
Haya yametajwa baada ya Swala; kuashiria kuwa Swala haizuii kitu chochote katika kazi ya kutafuta riziki na kwamba kuyachanganya yote mawili ni jambo jepesi. Kwa sababu Swala ina wakati maalumu ambao haumalizi ispokuwa dakika chache tu.
Na mwisho mwema ni kwa mwenye takua mwenye kucha kumwasi Mungu na alioyaharamisha kwa siri na kwa dhahiri.
Imam Ali(a.s) anasema: “Hakuna utukufu zaidi kuliko Uislamu, wala enzi kuliko takua, wala ngome kuliko kuchunga haki, wala muombezi mwenye kufaulu kuliko toba, wala hazina kubwa kuliko kukinai... na mwenye kutosheka na kiasi cha haja atakuwa na raha.”
وَقَالُوا لَوْلَا يَأْتِينَا بِآيَةٍ مِّن رَّبِّهِ أَوَلَمْ تَأْتِهِم بَيِّنَةُ مَا فِي الصُّحُفِ الْأُولَىٰ ﴿١٣٣﴾
133. Na walisema: “Kwa nini hakutuletea ishara kutoka kwa Mola wake? Je, haikuwajia dalili wazi ya yaliomo katika vitabu vya mwanzo?.
وَلَوْ أَنَّا أَهْلَكْنَاهُم بِعَذَابٍ مِّن قَبْلِهِ لَقَالُوا رَبَّنَا لَوْلَا أَرْسَلْتَ إِلَيْنَا رَسُولًا فَنَتَّبِعَ آيَاتِكَ مِن قَبْلِ أَن نَّذِلَّ وَنَخْزَىٰ ﴿١٣٤﴾
134. Na lau tungeliwaangamiza kwa adhabu kabla yake, wangelisema: Ewe Mola wetu! Kwa nini usituletee mtume tukazifuata ishara zako kabla hatujadhalilika na tukahizika?
قُلْ كُلٌّ مُّتَرَبِّصٌ فَتَرَبَّصُوا فَسَتَعْلَمُونَ مَنْ أَصْحَابُ الصِّرَاطِ السَّوِيِّ وَمَنِ اهْتَدَىٰ ﴿١٣٥﴾
135. Sema: Kila mmoja anangoja; basi ngojeni punde mtajua nani mwenye njia sawa na nani aliyeongoka.
Aya 133 – 135
Na walisema: Kwa nini hakutuletea ishara kutoka kwa Mola wake?
Umetangulia mfano wa Aya hii pamoja na tafsiri yake katika Juz. 1 (2:118). Juz; 7 (6:37) na Juz; 11 (10:20).
Je, haikuwajia dalili wazi ya yaliyomo katika vitabu vya mwanzo?
Ikiwa mnataka muujiza kweli enyi washirikina na wala sio kwa inadi, basi hii hapa Qur’an. Kwani hakika hiyo ni muujiza wa miujiza kwa namna kadhaa; miongoni mwazo ni kuwa inabainisha walioyaleta mitume na vitabu vilivyoshuka. Hapana; nyinyi hamtafuti uhakika na uongofu, wala nyinyi si watu wa kweli na wa kheri. Haya mnayoyataka ni kwa ajili ya inadi, ubabaishaji na kuvunga.
Na lau tungeliwaangamiza kwa adhabu kabla yake, wangelisema: Ewe Mola wetu! Kwa nini usituletee mtume tukazifuata ishara zako kabla hatujadhalilika na tukahizika?
Hao ni washirikina na kabla yake ni kabla ya Mtume au kabla ya Qur’an. Maana ni kuwa lau tungeliwaadhibu washirikina duniani au akhera bila ya kuwapa hoja ya kumtuma Muhammad na kuteremsha Qur’an, wangelileta hoja na kumwambia Mwenyezi Mungu: Mbona unatuadhibu kabla ya kutuletea Mtume wa kututoa kwenye ujinga na kutuzindua kwenye mghafala huu na kutuamrisha lile unalolipenda na kutukataza unalolichukia?
Lakini Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekata nyudhuru zote baada ya kumtuma Muhammad(s.a.w.w) kwa ishara zilizo waziwazi.
Sema: Kila mmoja anangoja; basi ngojeni punde mtajua nani mwenye njia sawa na nani aliyeongoka.
Hili ni onyo kwamba wao wanafuata njia ya upotevu na ya maangamizi, makemeo na kiaga cha adhabu inayowangoja, lakini maonyo hayawafai watu wasioamini isipokuwa chumo lao na manufaa yao.
Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)
Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.
MWISHO WA JUZUU YA KUMI NA SITA
YALIYOMO
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA 1
IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA 1
IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA 1
IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED 1
IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU 1
UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI 1
MAKOSA YA CHAPA 2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA 3
HUWEZI KUVUMILIA 3
MAANA 4
DHUL-QARNAIN 7
MAANA 7
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA 10
JUJU NA MAJUJU 10
MAANA 10
JAHANNAMU NA WALIOHASIRIKA 13
MAANA 13
THAMANI YA MTU 14
WALIOAMNI NA WAKATENDA MEMA 16
MAANA 16
MWISHO WA SURA YA KUMI NA NANE 17
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA 18
ZAKARIYA 18
MAANA 18
BISHARA YA YAHYA 19
MAANA 19
YAHYA 20
MAANA 20
MARYAM 22
MAANA 22
MIMBA YA ISA 23
MAANA 23
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA 25
UMELETA KITU CHA AJABU 25
MAANA 25
NJIA ILIYONYOOKA 27
MAANA 27
IBRAHIM 29
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA 32
MUSA, ISMAIL NA IDRIS 32
MAANA 32
KUTEKELEZA AHADI 33
WAKAJA BAADA YAO WALIO WABAYA 35
MAANA 35
KWELI NITATOLEWA HAI? 37
MAANA 37
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA 39
LIPI KATI YA MAKUNDI MAWILI 39
MAANA 39
FALSAFA YA TUMBO 39
JE, UMEMUONA ALIYEZIKANA ISHARA ZETU 42
MAANA 42
WANASEMA MWINGI WA REHEMA AMEJIFANYIA MWANA 44
MAANA 44
WANASWARA NA BANI HASHIM 45
MWISHO WA SURA YA KUMI NA TISA 46
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA 47
Twaha 47
Twaha 47
HADITHI YA MUSA 49
KUKARIRIKA KISA 49
NA NINI HICHO KILICHO MKONONI MWAKO WA KUUME EWE MUSA? 52
MAANA 52
HAKIKA YA UTUME 56
ALIY NA HARUN 57
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA 58
UMEPEWA MAOMBI YAKO EWE MUSA 58
MAANA 58
NENDA WEWE NA NDUGUYO 60
MAANA 60
NI YUPI HUYO MOLA WENU? 62
MAANA 63
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA 65
FIRAUNI ANAWAKUSANYA WACHAWI 65
MAANA 65
BAINA YA MUSA NA WACHAWI 68
MAANA 68
WAPIGIE NJIA 70
MAANA 70
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA 73
MSAMARIA NA NDAMA 73
MAANA 73
MUSA AMLAUMU HARUN 76
MAANA 76
WAISRAIL WANASHANGAZA 78
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA 79
KAMA HIVYO TUNAKUSIMULIA 80
MAANA 80
TUMEITERMSHA QUR’AN KWA LUGHA YA KIARABU 83
MAANA 83
WASIFU WA QUR’AN 83
NIZIDISHE ELIMU 85
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA SITA 87
AKASEMA: ONDOKENI HUMU NYOTE 87
MAANA 87
FANYA SUBRA NA WAYASEMAYO 89
MAANA 89
UFUKARA WA MTUME NI MUUJIZA MKUBWA 90
KWA NINI HAKULETEA ISHARA 91
MAANA 91
SHARTI YA KUCHAPA 92
MWISHO WA JUZUU YA KUMI NA SITA 92
YALIYOMO 93
[1] . Antioch ni mji ulioko Syria na Nazareth (kwa kiarabu Naswira) uko kaskazini mwa Palestina, mji wa Bikira Maryam. Aliishi hapo Bwana Masih ndio akaitwa Mnazareth (kwa kiarabu Mnaswara) na wakristo wakawa wanaitwa Wanaswara -Mtarjumu.
[2] . Wakazi wa Ulaya ya mashariki, ikiwemo Sarbia, Croatia, Slovakia na Bulgaria - Mtarjumu.
[3] . Jina la zamani la Zimbabwe
[4] . Wakati huo wa mwisho mwisho wa mika ya sitini na mwanzo wa miaka ya sabini, mapin- duzi ya kijeshi yalikuwa yamechachamaa sana katika nchi za kiafrika – mtarjumu.