TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA
IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED
IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU
Kitabu hiki kilichoko mikononi mwako hivi sasa ni juhudi ya miaka mingi sana ya watu waliojitolea kuona kazi hii imefanikiwa bila ya kumsahau Marhum Abu Muhammad wa London.
Kama lilivyo jina la Tafsiri ndivyo ilivyo Tafsiri yenyewe ambayo mwanachuoni huyu mahiri kabisa aliyeifafanua ni mtu aliyebobea katika fani zote ambazo mfasiri (Mfafanuzi) anatakiwa awe nazo.
Sheikh Muhammad Jawad Mughniyya ameonesha cheche zake katika vitabu vingi alivyoviandika katika maudhui mbali mbalimbali na hivyo kujipatia wasomaji wengi sana.
Msomi huyu, mwenye fikra huru na anayetetea kile anachokiamini, ni mtu mwenye mawazo mapana na kuyaangalia mambo kwa undani sana, kipaumbele chake ni katika maslahi ya umma huu na amejaribu sana kwenda na wakati.
Sifa kubwa pekee ya mwanachuoni huyu ni kuwa yeye hakujihusisha sana na kung'ang'ania madhehebu fulani tu, labda hii yatokana na wadhifa wake wa ukadhi aliokuwa nao katika nchi ya Lebanon ambayo ina madhehebu mengi, ambapo sula la madhehebu ni nyeti nchini humo, hata hivyo yeye aliweza kuamua matatizo ya watu kwenye ofisi yake kulingana na madhehebu yao pale walipomwendea. Hiyo ilimsaidia sana hata kuweza kutoa kitabu kitwacho Al-Fiqh a'laa madhaahabil-khamsah (Fikhi ya madhehebu matano) yaani ya Hanafi, Maaliki, Shafi, Hambali na Shia (ambacho twataraji kitatoka kwa lugha ya kiswahili hivi karibuni Inshaallah).
Jambo lililotupa msukumo wa kukifasiri kitabu hiki kwa lugha ya Kiswahili ni zile faida nyingi atakazozipata msomaji na kujua mambo mengi na ya ajabu yaliyo mapya kwake ambayo si rahisi kuyapata kwa wafasiri wengine.
Msomaji atapata faida katika fani za Sayansi, Siasa, Historia, Mashairi, visa vizuri, na Saikolojia miongoni mwa mengine; ndiyo maana msomaji atashangaa kidogo anapoisoma Tafsiri hii atakapoona mwandishi amewataja na kuwanukuu watu kama kina Mfalme Edward, wanasayansi kama kina Enstein, wasanii kama Charlie Champlin (Mchekeshaji maarufu), na wengineo, hali inayoifanya tafsiri hii kuwa ni ya kipekee kabisa.
Mtindo alioutumia mwandishi ni sahali uliokusudiwa watu wa tabaka mbalimbali, wanavyuoni na watu wa kawaida.
Nia yetu ni kukigawanya kitabu hiki bure lakini tumelazimika kukiuza kwa bei nafuu ili kurudisha gharama za uchapishaji.
Mwisho: Shukrani kubwa iwaendee bila ya kuwataja watu waliojitolea usiku na mchana, jopo la wafasiri, wahariri, wachapaji, waliotupa moyo na kutoa maoni yao na walioisimamia ili kuhakikisha kwamba kitabu kimemfikia msomaji.
Sikumbuki kama nimewahi kusoma kitabu kilichotoka kupigwa chapa, cha zamani au cha sasa, bila ya kukuta makosa ya chapa, Nafikiri sitasoma kitabu kisichokuwa hivyo. Nimejaribu sana kuliepuka hilo katika tungo zangu, lakini sikufanikiwa.
Nilikuwa sifikirii kama ninaweza kuona makosa haya katika maandishi ya msahafu mtukufu, kama yale yaliyo katika baadhi ya chapa; kwa mfano neno yabswutu kwa swad, badala ya yabsutu kwa sin, na katika chapa ya Tafsir Arrazi ya Misr ya mwaka 1935, Sura ya (2:146), Imeandikwa La Ya'alamuun, (hawajui) badala ya Ya'alamuun (wanajua). Mfano wa makosa haya hausameheki.
Katika Tafsir Al-Manar, chapa ya Pili, sura (5:212), imeandikwa Fawqahum ila yawmil qiyama badala ya Fawqahum yawamal qiyama. Hatuwezi kusema kosa hili ni kubwa zaidi kuliko lile.
Lakini mkosaji atatuletea udhuru kwa msemo mashuhuri huko kwetu Jabal amil 'Makosa ya chapa.'
Katika Tafsiri Majmau chapa ya Urfan, Sura (46:15), imeandikwa: Hatta idha balagha arbai' na sanah badala ya: Hattaidha balagha ashuddahu arbai ' na sanah"
Kusema hivi sio kama ninajitetea kutokana na makosa ya chapa atakayoyakuta msomaji katika kitabu hiki, ijapokuwa naomba msamaha kama litatokea hili, lakini makusudio yangu hasa ni kumwambia yule atakayefungua macho yake kwenye makosa ya matamko na kuufungia macho uzuri wa maana.
Vilevile ninamwambia yule ambaye siku moja aliniambia: "Vitabu vyako vimejaa makosa ya chapa.” Kama kwamba hakuna kitu chochote katika vitabu hivyo isipokuwa makosa ya chapa tu. Wote hao ninawaambia: Mungu awasamehe na aniongoze mimi na nyinyi.
Vyovyote iwavyo, mimi ninaomba msamaha kutokana na makosa ya kifikra na ya chapa. Anasema Amirul Muminiin(a.s) :"Watu wote ni wapungufu wenye kuchanganyikiwa, isipokuwa yule aliyehifadhiwa na Mwenyezi Mungu." Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) ndiye mwenye jukumu la kunikubalia yale niliyoyapatia na kunisamehe niliyakosea, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, ziwashukie rehema na amani (Amin).
1
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
Sura Ya Ishirini Na Tatu: Al-Mu’minun. Imeshuka Makka ina Aya 118.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾
1. Hakika wamefaulu waumini.
الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿٢﴾
2. Ambao ni wanyenyekevu katika Swala zao.
وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ ﴿٣﴾
3. Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi.
وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ ﴿٤﴾
4. Na ambao kwa Zaka ni watendaji.
وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٥﴾
5. Na ambao wanazilinda tupu zao.
إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿٦﴾
6. Isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume. Kwani si wenye kulaumiwa.
فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿٧﴾
7. Lakini anayetaka kinyume cha hayo basi hao ndio wapetukao mipaka.
وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ ﴿٨﴾
8. Na wale ambao wanachunga amana zao na ahadi zao.
وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ ﴿٩﴾
9. Na ambao Swala zao wanazihifadhi.
أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾
10. Hao ndio warithi.
الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١﴾
11. Watakaorithi Firdausi, wadumu humo.
Aya 1-11
Kila mwenye kusema: Lailaha illa llah Muhammadur rasulullah (Hapana mola isipokuwa Mwenyezi Mungu, Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu) atastahiki yale yanayowastahiki waislamu, naye atawapatia wanayostahiki waislamu kutoka kwake. Hiyo ni katika maisha ya hapa duniani. Ama maisha ya akhera, hiyo peke yake haitatosha kumpatia thawabu za Mwenyezi Mungu na radhi zake mpaka awe amekusanya mambo yafutayo:-
1.Hakika wamefaulu waumini ambao ni wanyenyekevu katika Swala zao.
Kunyenyekea ni kinyume cha kiburi na kujikweza. Mwenyezi Mungu anasema: "Wananyeyekea kwa udhalili." (42:45). Kunyenyekea katika Swala ni natija ya kuwa na yakini na Mwenyezi Mungu na kuhofia adhabu yake. Swala bila ya yakini si chochote wala lolote. Imam Ali(a.s ) anasema: "Kulala na yakini ni bora kuliko kuswali na shaka."
2. Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi.
Mumin wa kweli upuuzi na batili haimfanyi aache Mwenyezi Mungu. Imam Ali(a.s) anasema:"Hakika mawalii wa Mungu ni wale ambao wanaangalia ndani ya dunia wakati watu wanapoangalia nje yake na wanajishugulisha na ya baadaye wakati watu wakijishughulisha na ya sasa." Akasema tena:"Mwenye kuangalia kasoro zake hatajishugulisha na kasoro za wengine."
3.Na ambao kwa Zaka ni watendaji.
Angalia tuliyoyaandika kuhusu Zaka katika Juz. 3 (2:272-274).
4.Na ambao wanazilinda tupu zao isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume. Kwani si wenye kulaumiwa.
Makusudio ya iliyowamiliki mikono yao ya kuume ni wajakazi. Hivi sasa hawako tena. Zina ni miongoni mwa madhambi makubwa na uchafu katika sharia ya kiislamu. Kwenye jamii yoyote zina ikienea basi inabomoka.
Lakini anayetaka kinyume cha hayo basi hao ndio wapetukao mipaka.
Yaani atakayetaka kumwingilia asiyekuwa mkewe au mjakazi, basi atakuwa amepituka mipaka ya Mwenyez Mungu na anastahiki ghadhabu yake na adhabu yake.
Unaweza kuuliza kuwa : je, kauli yake Mwenyezi Mungu:"Lakini anayetaka kinyume cha haya" inachanganya kujitoa manii kwa mkono kunakojulikana kwa jina la punyeto (Kujipuli)?
Jibu : ndio. Kwa sababu Mwenyezi Mungu amehalalisha mke na mjakazi na akaharamisha kinyume cha hivyo kwa namna yoyote ile itakayokuwa. Ndio maana mafakihi wote wakaharamisha, isipokuwa Hanafi na Hambali wamesema inaruhusiwa kwa yule anayehofia kuingia kwenye haramu. Tazama Ruhulbayan cha Ismail Haqqiy.
Imam Jafar Sadiq(a.s) aliulizwa kuhusu punyeto (Kujipuli). Akasema:ni dhambi kubwa. Muulizaji akamuuliza iko wapi kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu ewe mtoto wa Mtume wa Mwenyezi Mungu? Imam akasoma:Lakini anayetaka kinyume cha hayo … Kisha akasema:Ponyeto ni kinyume cha hayo.
5.Na wale ambao wanachunga amana zao na ahadi zao.
Tumezungumzia kwa ufafanuzi kuhusu amana na wajibu wa utekelezaji wake katika Juz. 5 (4:58). Ahadi ni kila aliloliamrisha Mwenyezi Mungu na kulikataza. Mwenyezi Mungu anasema: "Na tekelezeni ahadi yangu. Nitatekeleza ahadi yenu" Juz. 1(2: 40).
6.Na ambao Swala zao wanazihifadhi wakidumu nazo kwa wakati wake.
Tumefafanua kuhusu Swala katika Juz. 1 (2:3, 110).
Hao ndio warithi, watakaorithi Firdausi, wadumu humo.
Mumin yoyote atakayekuwa na mambo hayo yaliyotajwa, basi atastahiki Pepo, kama anavyostahiki mrithi mirathi kutoka kwa jamaa yake wa karibu. Wapi na wapi urithi wa dunia unaoisha na mabalaa yake na urithi wa akhera na neema zake za kudumu!
وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن سُلَالَةٍ مِّن طِينٍ ﴿١٢﴾
12. Na hakika tumemuumba mtu kutokana na asili ya udongo.
ثُمَّ جَعَلْنَاهُ نُطْفَةً فِي قَرَارٍ مَّكِينٍ ﴿١٣﴾
13. Kisha tukamjaalia awe tone katika makao yaliyo makini.
ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ عِظَامًا فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْمًا ثُمَّ أَنشَأْنَاهُ خَلْقًا آخَرَ فَتَبَارَكَ اللَّـهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ ﴿١٤﴾
14. Kisha tukaumba tone kuwa pande la damu na tukaliumba pande la damu kuwa pande la nyama, na pande la nyama tukaliumba kuwa mifupa na mifupa tukaivika nyama. Basi ametukuka Mwenyezi Mungu mbora wa waumbaji.
ثُمَّ إِنَّكُم بَعْدَ ذَٰلِكَ لَمَيِّتُونَ ﴿١٥﴾
15. Kisha hakika nyinyi baada ya hayo ni maiti.
ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ تُبْعَثُونَ ﴿١٦﴾
16. Kisha hakika nyinyi siku ya Kiyama mtafufuliwa.
وَلَقَدْ خَلَقْنَا فَوْقَكُمْ سَبْعَ طَرَائِقَ وَمَا كُنَّا عَنِ الْخَلْقِ غَافِلِينَ ﴿١٧﴾
17. Hakika tumeumba juu yenu tabaka saba. Nasi katika kuumba si wenye kughafilika.
Aya 12 -17
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameashiria kwenye Aya nyingi kuhusu kuumbwa mtu; sio kwa kuwa tujue tumetoka wapi, tumepatikana vipi na tuko vipi tu, iwe ni basi. Hapana! Bali ni tuuatumbue ukuu wa muumbaji katika kutuumba kwetu, kama tunavyoutambua katika kuumba mbingu na ardhi.
Tunapaswa tumwamini na tuende na mwongozo wake kwa kutumai kupata thawabu zake na kuepukana na adhabu yake.
Miongoni mwa Aya hizo ni ile isemayo:
هَلْ أَتَىٰ عَلَى الْإِنسَانِ حِينٌ مِّنَ الدَّهْرِ لَمْ يَكُن شَيْئًا مَّذْكُورًا ﴿١﴾
"Hivi ulimfikia mtu wakati fulani hakuwa kitu kinachotajwa?" (76:1).
Ndio! Hakuwa kitu kinachotajwa kisha akawa kitu. Ama yule ambaye amemfanya aweko kutoka asikokuwako, anatutanabahisha pale aliposema:
'Na hakika tumemuumba mtu kutokana na asili ya udongo.'
Katika Aya hii Mwenyezi Mungu Mtukufu ameonyesha chimbuko la mtu, vipi alivyomgurisha kutoka hali moja hadi nyingine. Lengo la kwanza katika hilo ni kujua dalili za kuweko muumba na utukufu wake, tufikirie na tumwangalie kiumbe huyu wa ajabu katika sura yake, umbile lake, akili yake na utambuzi wake.
Mtu huyu Mwenye historia na maendeleo, kiumbe huyu ambaye ana nguvu na uwezo kuliko kiumbe yeyote mwengine, ambaye wajuzi wameileza taadhima yake hii kwa neno: "Na kwako wewe umekunjwa ulimwengu mkubwa," ametokea wapi na ameumbwa kutokana na nini?
Aya inatujibu kwamba yeye ameumbwa kutokana na udongo uliotokana na mchanga na maji, katika asili ambayo imeumbiwa wadudu na mimea. Hapa ndio pana dalili na hoja. Kwani inavyojulikana ni kuwa kitu kimoja hakiwezi kutoa vitu viwili vinavyopingana, utambuzi na kutotambua; upofu na kuona. Kwa hiyo hapa kuna siri wala hakuna tafsiri ya siri hii isipokuwa kwa nguvu yenye uwezo na yenye ujuzi wa kitu hicho.
Ni nguvu hii ambayo imefarikisha na kupamabanua baina ya vitu viwili vinavyopingana ambavyo vimeumbwa kwa asili moja. Baada ya kuashiria malengo ya Aya zinazozungumzia kuumbwa kwa mtu, sasa tunabainisha makusudio ya Aya tulizonazo.
Na hakika tumemuumba mtu kutokana na asili ya udongo.
Makusudio ya mtu hapa ni mwanadamu, sio Adam mwenyewe. Kauli yake Mwenyezi Mungu inayofuatia: 'Kisha tukamjaalia awe tone' inafahamisha hivyo. Adamu na wanawe wote wanatokana na udongo uliotokana na mchanga na maji. Tofauti ni kuwa Adam ameumbwa kutokana na mchanga na maji, moja kwa moja; na wanawe ni kupitia chakula kinachozalikana kutokana na ardhi na maji.
Kisha tukamjaalia awe tone katika makao yaliyo makini katika uti wa mgongo wa baba hadi kwenye mfuko wa uzazi wa mama.
Kisha tukaumba tone kuwa pande la damu na tukaliumba pande la damu kuwa pande la nyama.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 17 (22:5).
Na pande la nyama tukaliumba kuwa mifupa na mifupa tukaivika nyama.
Pande la nyama akaligawanya mifupa, mishipa na nyama, kisha kwenye mkusanyiko huo akaumba aina mbali mbali. Ufafanuzi uko katika elimu ya upasuaji.
Kisha tukamfanya kiumbe mwengine mtu aliye kamili kama siye yule aliyekuwa tone damu nyama n.k.
Basi ametukuka Mwenyezi Mungu mbora wa waumbaji.
Wala hakuna kitu kinachofahamisha hakika hii kuliko kuumbwa ulimwengu na nidhamu yake na kuumbwa mtu na ubainifu wake, moyo wake, akili yake n.k. Tunakariri tuliyoyasema mara kwa mara, kwamba imekuwa ni desturi ya Qur'an Tukufu kutegemeza mabadiliko ya ulimwengu kwa Mwenyezi Mungu. Kwa sababu Yeye, ambaye umetukuka utukufu wake, ndiye sababu ya kuumbwa ulimwengu.
Kisha hakika nyinyi baada ya hayo ni maiti.
Na anayekufa marejeo yake ni kwa muumba wake.
Kisha hakika nyinyi siku ya Kiyama mtafufuliwa muulizwe mliyokuwa mkiyafanya.
Hakika tumeumba juu yenu tabaka saba. Nasi katika kuumba si wenye kughafilika.
Wakati wa kufasiri Juz. 1 (2: 29), nilisema kuwa kutajwa mbingu saba hakufahamishi kuwa ni hizo hizo tu, na kwamba sababu ya kutajwa kwake huenda ikawa ni kwa mambo yanayohusika hapo. Nilitosheka na kauli hiyo wakati huo, kwa sababu mimi si mjuzi zaidi wa hilo, kwani si mtaalamu wa elimu ya falaki.
Nilipofikia kufasiri Aya hii tuliyo nayo nikasoma makala ya kisayansi katika jarida la Misr liitwalo Akhbar la tarehe 17 Julai 1969, yenye kichwa cha maneno 'Mwenyezi Mungu na mtu na mwezi,' kama ifutavyo:-
"Imethibitishwa kisayansi kwamba katika anga za mbali kuna aina za ulimwengu zaidi ya ulimwengu huu tunaoishi - yaani mkusanyiko wa sayari tunazoziona kwa macho makavu au kwa darubini - na kwamba kila ulimwengu katika aina hizo una jua lililo na nguvu zaidi ya hili jua letu linaongaza kila siku kwenye ardhi; na pembezoni mwake kunazunguka nyota kadhaa.
Haiwezekani kufikia kwenye sayari yoyote katika sayari hizo pamoja na kwamba tuna vyombo vilivyoweza kugundua sehemu hizo, kutokana na umbali wa kasi ya mwanga kufikia huko. Jua na nyota za sehemu hizo ziko mbali nasi kwa mwendo wa kasi ya mwanga ya mamilioni ya miaka. Lau kama tutakadiria mtu kusafiri kufikia huko, basi itamchukua mamilioni ya miaka kwa kasi ya mwanga kuweza kuifikia sayari iliyo karibu zaidi ya ulimwengu huo. Hii ndio hakika iliyothibitishwa na sayansi na wamekubaliana nayo wataalam wa kisasa."
Kwa hiyo basi makusudio ya mbingu saba ni ulimwengu (dunia) wa aina saba na sio sayari saba, kwamba kila ulimwengu una sayari na nyota zake zisizokuwa na idadi na kwamba mtu hawezi kuzifikia kwa sababu hawezi kuishi mamiloni ya miaka. Ama ardhi saba zilizoashiriwa katika (65:12) ni kuwa katika ulimwengu huo wa aina saba kila mmoja una sayari ya ardhi.
وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً بِقَدَرٍ فَأَسْكَنَّاهُ فِي الْأَرْضِ وَإِنَّا عَلَىٰ ذَهَابٍ بِهِ لَقَادِرُونَ ﴿١٨﴾
18. Na tumewateremshia kutoka mbinguni maji kwa kiasi na tukayatuliza ardhini. Na hakika sisi ni wenye uwezo wa kuyaondoa.
فَأَنشَأْنَا لَكُم بِهِ جَنَّاتٍ مِّن نَّخِيلٍ وَأَعْنَابٍ لَّكُمْ فِيهَا فَوَاكِهُ كَثِيرَةٌ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ ﴿١٩﴾
19. Basi kwa maji hayo tukawafanyia bustani za mitende na mizabibu, mnapata humo matunda mengi na katika hayo mnakula.
وَشَجَرَةً تَخْرُجُ مِن طُورِ سَيْنَاءَ تَنبُتُ بِالدُّهْنِ وَصِبْغٍ لِّلْآكِلِينَ ﴿٢٠﴾
20. Na mti utokao katika Mlima Sinai unaotoa mafuta na kitoweo kwa walaji.
وَإِنَّ لَكُمْ فِي الْأَنْعَامِ لَعِبْرَةً نُّسْقِيكُم مِّمَّا فِي بُطُونِهَا وَلَكُمْ فِيهَا مَنَافِعُ كَثِيرَةٌ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ ﴿٢١﴾
21. Na hakika katika wanyama howa mna mazingatio. Tunawanywesha katika vile vilivyomo matumboni, na mnapata katika hao manufaa mengi, Na katika hao mnawala.
وَعَلَيْهَا وَعَلَى الْفُلْكِ تُحْمَلُونَ ﴿٢٢﴾
22. Na juu yao na juu ya majahazi mnabebwa.
Aya 18 – 22
Na tumewateremshia kutoka mbinguni maji kwa kiasi.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kusema kuwa hatukughafilika na viumbe, alipigia mfano wa hilo kwa kuteremsha maji kutoka mbinguni kwa kiasi kile kinachowafaa watu; si kingi cha kuwadhuru wala kichache cha kudhuru mimea.
Na tukayatuliza ardhini katika chemchemi, visima, mabawa na mito, ili yawafae watu wakati wa kiangazi.
Na hakika sisi ni wenye uwezo wa kuyaondoa.
Yule aliyeweza kuyaleta bila shaka anaweza kuyaondoa kwa kuyazuia au kuyakausha yasiweze kuwafaa, lakini hakufanya hivyo kwa kuwahurumia.
Basi kwa maji hayo tukawafanyia bustani za mitende na mizabibu, mnapata humo matunda mengi na katika hayo mnakula.
Imehusishwa kutajwa mitende na mizabibu kwa sababu waarabu wakati huo walikuwa hawajui kingine zaidi yake.
Na mti utokao katika Mlima Sinai unaotoa mafuta na kitoweo kwa walaji.
Makusudio ya mti utokao Mlima Sinai ni mzaituni. Mlima Sinai ni ule mlima aliozungumza Musa na Mola wake na kitoweo ni mafuta ambayo hutengenezwa siagi ya kutowelea mkate.
Wafasiri wengi wamesema kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehusisha kutaja aina hizi tatu kwa sababu ni miti mitukufu zaidi na ina manufaa mengi, lakini ukweli ni kuwa ilikuwa ndio iliyoenea zaidi kwa waarabu.
Umetangulia mfano wake mara nyingi. Angalia kwenye Juz. 14 (16:10).
Na hakika katika wanyama howa; ngamia ng'ombe, mbuzi na kondoo,mna mazingatio mtakayoyazingatia.
Tunawanywesha katika vile viliomo matumboni, maziwa na mnapata katika hao manufaaa mengi, yakiwa ni pamoja sufu, manyoya na ngozi zake. Na katika hao mnawala nyama yake.
Na juu yao na juu ya majahazi mnabebwa kutoka sehemu moja hadi nyingine.
Umetangulia mfano wake katika Aya nyingi. Angalia Juz. !4 (16:5).
2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٢٣﴾
23. Na hakika tulimtuma Nuh kwa watu wake, akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu asiyekuwa Yeye. Basi je, hamna takua?
فَقَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَوْمِهِ مَا هَـٰذَا إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُرِيدُ أَن يَتَفَضَّلَ عَلَيْكُمْ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَأَنزَلَ مَلَائِكَةً مَّا سَمِعْنَا بِهَـٰذَا فِي آبَائِنَا الْأَوَّلِينَ ﴿٢٤﴾
24. Wakasema wale wakuu waliokufuru: Huyu si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi, anataka kujipatia ubora juu yenu. Na lau Mwenyezi Mungu angelipenda, hakika angeliteremsha Malaika. Hatukuyasikia haya kwa mababa zetu wa kwanza.
إِنْ هُوَ إِلَّا رَجُلٌ بِهِ جِنَّةٌ فَتَرَبَّصُوا بِهِ حَتَّىٰ حِينٍ ﴿٢٥﴾
25. Huyo si lolote ila ni mtu mwenye wazimu. Basi ngojeni kwa muda.
قَالَ رَبِّ انصُرْنِي بِمَا كَذَّبُونِ ﴿٢٦﴾
26. Akasema: "Mola wangu! Nisaidie kwa kuwa wamenikadhibisha.
فَأَوْحَيْنَا إِلَيْهِ أَنِ اصْنَعِ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا فَإِذَا جَاءَ أَمْرُنَا وَفَارَ التَّنُّورُ فَاسْلُكْ فِيهَا مِن كُلٍّ زَوْجَيْنِ اثْنَيْنِ وَأَهْلَكَ إِلَّا مَن سَبَقَ عَلَيْهِ الْقَوْلُ مِنْهُمْ وَلَا تُخَاطِبْنِي فِي الَّذِينَ ظَلَمُوا إِنَّهُم مُّغْرَقُونَ ﴿٢٧﴾
27. Tukampa wahyi: Tengeneza jahazi mbele ya macho yetu. Basi itakapokuja amri yetu na ikafurika tanuri, hapo waingize wa kila namna dume na jike, wawili na ahli zako, isipokuwa ambaye kauli imekwishatangulia juu yake katika wao. Wala usinitajie hao waliodhulumu, Hakika wao watagharikishwa.
فَإِذَا اسْتَوَيْتَ أَنتَ وَمَن مَّعَكَ عَلَى الْفُلْكِ فَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي نَجَّانَا مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٢٨﴾
28. Na utakapotulia wewe na walio pamoja nawe jahazini, sema, sifa njema (Alhamdulillah) ni za aliyetuokoa na watu madhalimu.
وَقُل رَّبِّ أَنزِلْنِي مُنزَلًا مُّبَارَكًا وَأَنتَ خَيْرُ الْمُنزِلِينَ ﴿٢٩﴾
29. Na sema, Mola wangu! niteremshe mteremsho wenye baraka na wewe ndiwe mbora wa wateremshaji.
إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ وَإِن كُنَّا لَمُبْتَلِينَ ﴿٣٠﴾
30. Hakika katika hilo kuna ishara na kwa hakika sisi ni wenye kuwafanyia mtihani.
Aya 23-30
Kila yaliyokuja kwenye Aya hizi yametangulia kutajwa katika Juz. 12 (11: 25-49) yamemaliza zaidi ya kurasa 22, kwa hiyo hapa tutazipitia juu juu tu.
Na hakika tulimtuma Nuh kwa watu wake, akasema: Enyi watu wangu! Muabuduni Mwenyezi Mungu. Hamna mungu asiyekuwa Yeye. Basi je, hamna takua?
Aliwalingania kwenye ibada ya Mwenyezi Mungu peke yake na kuwahadharisha na shirki. Wale wapenda anasa wakahofia vyeo vyao na chumo lao. Wakaanzisha kampeni za uongo na kuwatatiza watu kwa shubha za ubatilifu. Mwenyezi Mungu amezitaja tatu miongoni mwazo:
1.Wakasema wale wakuu waliokufuru: Huyu si chochote ila ni mtu tu kama nyinyi, anataka kujipatia ubora juu yenu.
Walisema, vipi Nuh awe ni nabii naye ni mtu kama nyinyi. Yeye hana lengo la utume katika mwito wake isipokuwa anataka kuwa raisi na nyinyi muwe raia wake. Hii ndio lugha ya wafanyi biashara, wanafasiri faida katika kila kitu.
2.Na lau Mwenyezi Mungu angelipenda, hakika angeliteremsha Malaika. Hatukuyasikia haya kwa mababa zetu wa kwanza.
Hawakusikia kuwa Mwenyezi Mungu alituma mitume, vilevile hawakusikia kuwa Mungu wa ulimwengu wote ni mmoja. Kwa hiyo Nuh si Mtume na miungu ni mingi, yakiwemo masanamu yao. Hakuna tofauti baina ya mantiki haya na mantiki ya anayesema: mimi siamini kuweko kwa sayari ya Mars kwa sababu sijafika huko.
3.Huyo si lolote ila ni mtu mwenye wazimu.
Walileta uongo huu wakijua fika kuwa ni uongo; kama walivyokuwa maquraishi na uhakika wa wa uzushi wao pale waliposema kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) amerogwa na ni mwendawazimu.
Basi ngojeni kwa muda. Yaani mngojeni Nuh afe au awache mwito wake.
Akasema: "Mola wangu! Nisaidie kwa kuwa wamenikadhibisha.
Alikimbilia kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu na akamtaka msaada baada ya kukata tamaa na kuongoka kwao.
Tukampa wahyi: Tengeneza jahazi mbele ya macho yetu.
Ni kinaya cha kuichunga kwake Mwenyezi Mungu safina. Na wahyi wetu yaani na amri yetu.
Basi itakapokuja amri yetu na ikafurika tanuri; yaani maji yatakapochimbuka kutoka ardhini.
Hapo waingize wa kila namna dume na jike, wawili na ahli zako, isipokuwa ambaye kauli imekwishatangulia juu yake katika wao.
Yaani isipokuwa mke wake Nuh na mwanawe ambaye inasemekana jina lake ni Kanani.
Wala usinitajie hao waliodhulumu, Hakika wao watagharikishwa.
Yaani usiniombe kuokoka wale ambao neno la adhabu limekwishahakika kwao; hata mkeo na mwanao pia.
Na utakapotulia wewe na walio pamoja nawe jahazini, sema, sifa njema (Alhamdulillah) ni za aliyetuokoa na watu madhalimu.
Katika Aya hii kuna somo muhimu sana, nalo ni kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) anapomwangamiza taghuti haitakikani kunyamaza yule aliyedhulumiwa; bali amuhimidi Mwenyezi Mungu kwa kuokoka kwake na kuangalia kuangamia kwake kuwa ni nyenzo tu sio lengo.
Na sema: Mola wangu! Niteremshe mteremsho wenye baraka na wewe ndiye mbora wa wateremshaji.
Niteremshe kutoka jahazini kwa namna ambayo utanihifadhi na uovu mimi na watu wangu na aliyeamini, kwani wewe ni mtermshaji na muhifadhi bora.
Hakika katika hilo kuna ishara na kwa hakika sisi ni wenye kuwafanyia mtihani.
Yaani sisi tumewafanyia mtihani waja kwa kuwapelekea mitume na kuteremsha vitabu, ili kupambanua muovu na mwema na aonekane wazi wazi kila mmoja wao alipwe thawabu au adhabu, kiasi anachostahiki.
ثُمَّ أَنشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قَرْنًا آخَرِينَ ﴿٣١﴾
31. Kisha baada yao tukaanzisha karne nyingine.
فَأَرْسَلْنَا فِيهِمْ رَسُولًا مِّنْهُمْ أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٣٢﴾
32. Tukawapelekea Mtume miongoni mwao, kwamba mumwabudu Mwenyezi Mungu! Hamna Mungu asiyekuwa Yeye, je hamuogopi?
وَقَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِهِ الَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِلِقَاءِ الْآخِرَةِ وَأَتْرَفْنَاهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا مَا هَـٰذَا إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يَأْكُلُ مِمَّا تَأْكُلُونَ مِنْهُ وَيَشْرَبُ مِمَّا تَشْرَبُونَ ﴿٣٣﴾
33. Na wakuu katika watu wake waliokufuru na wakakanusha mkutano wa Akhera na tukawadekeza kwa starehe katika maisha ya dunia, walisema: Huyu si chochote ila ni binadamu kama nyinyi, anakula mlacho na anakunywa mnywacho.
وَلَئِنْ أَطَعْتُم بَشَرًا مِّثْلَكُمْ إِنَّكُمْ إِذًا لَّخَاسِرُونَ ﴿٣٤﴾
34. Na nyinyi mkimtii mtu kama nyinyi basi hakika mtakuwa hasarani.
أَيَعِدُكُمْ أَنَّكُمْ إِذَا مِتُّمْ وَكُنتُمْ تُرَابًا وَعِظَامًا أَنَّكُم مُّخْرَجُونَ ﴿٣٥﴾
35. Je, anawaahidi ati mtakapokufa na mkawa mchanga na mifupa kwamba mtatolewa?
هَيْهَاتَ هَيْهَاتَ لِمَا تُوعَدُونَ ﴿٣٦﴾
36. Hayawi! Hayawi hayo mnayoahidiwa.
إِنْ هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا نَحْنُ بِمَبْعُوثِينَ ﴿٣٧﴾
37. Hakuna ila maisha yetu ya dunia tu, tunakufa na tunaishi. Wala sisi si wenye kufufuliwa.
إِنْ هُوَ إِلَّا رَجُلٌ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا وَمَا نَحْنُ لَهُ بِمُؤْمِنِينَ ﴿٣٨﴾
38. Huyo si lolote ila ni mtu anayemzulia Mwenyezi Mungu uongo, wala sisi si wenye kumwamini.
قَالَ رَبِّ انصُرْنِي بِمَا كَذَّبُونِ ﴿٣٩﴾
39. Akasema: Mola wangu, ninusuru kwa wanavyonikanusha.
قَالَ عَمَّا قَلِيلٍ لَّيُصْبِحُنَّ نَادِمِينَ ﴿٤٠﴾
40. Akasema: Baada ya muda mchache hakika watakuwa ni wenye kujuta.
فَأَخَذَتْهُمُ الصَّيْحَةُ بِالْحَقِّ فَجَعَلْنَاهُمْ غُثَاءً فَبُعْدًا لِّلْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٤١﴾
41. Basi ukawanyakua ukelele kwa haki. Tukawafanya takataka zinazoelea juu ya maji, ikapotelea mbali kaumu ya madhalimu.
AYA 31-41
Makusudio ya karne hapa ni watu. Mwenyezi Mungu hakuweka wazi ni akina nani hao. Wafasiri wamesema hao ni A'd, kaumu ya Hud. Na hii ni sawa kwa dalili ya yaliyokuja katika Juz.8 (7:65). Yametangulia maelezo katika Juz. 12 (11: 50 - 65). Kwa hiyo tutapita juu juu, kwenye Aya hizi, kama tulivyopita kwenye Aya zilizotangulia hizi.
Tukawapelekea Mtume mingoni mwao.
Mwenyezi Mungu alimtuma Hud kwa A'd naye ni miongoni mwao.
Kwamba mumwabudu Mwenyezi Mungu! Hamna Mungu asiyekuwa Yeye, je hamuogopi?
Aliwapa watu wake mwito wa tawhid na kuacha shirk kwa kutoa bishara ya radhi za Mwenyezi Mungu na thawabu zake na kutoa onyo la hasira za Mweyezi Mungu na adhabu yake.
Na wakuu katika watu wake waliokufuru na wakakanusha mkutano wa Akhera na tukawadekeza kwa starehe katika maisha ya dunia, walisema: Huyu si chochote ila ni binadamu kama nyinyi, anakula mlacho na anakunywa mnywacho.
Maadamu yuko hivyo hivyo basi hana tofauti wala ubora, basi vipi mnamtii.
Na nyinyi mkimtii mtu kama nyinyi basi hakika mtakuwa hasarani.
Wao ndio wako hasarani kiiudhahiri na kiuhalisi kutokana na kumuasi kwao Nabii. Lakini wamepindua na wakaufinika uhakika. Haya ndiyo mazoweya ya matwaghuti na wanaodeka kila mahali na kila wakati.
Je, anawaahidi ati mtakapokufa na mkawa mchanga na mifupa kwamba mtatolewa?
Makaburini kuwa hai kama mlivyo sasa. Hiki ni kitu cha ajabu.
Hayawi! Hayawi hayo mnayoahidiwa kuwa kuna ufufuo baada ya mauti. Hakuna ila maisha yetu ya dunia tu, tunakufa na tunaishi. Wala sisi si wenye kufufuliwa.
Kwa sababu aliyekufa na yake yamekwisha. Huu ni ubainifu wa yaliyotangulia, ya kuona kwao muhali kufufuliwa baada ya mauti, wakiwa wameghafilika kwamba aliyewaumba kwanza ndiye huyo huyo atakayewarudisha; na kwamba hilo ni rahisi zaidi kuliko kuanzisha, kama ni sawa ibara yao.
Huyo si lolote ila ni mtu anayemzulia Mwenyezi Mungu uongo, wala sisi si wenye kumwamini.
Hawamwamini Hud kwa sababu anasema uongo juu ya Mwenyezi Mungu, lakini kuabudu kwao masanmu ndio ikhlasi ya kweli kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na takua!! Aliye mtupu zaidi katika watu ni yule anayefanya uovu kisha akajiona amefanya wema.
Akasema: Mola wangu, ninusuru kwa wanavyonikanusha.
Alisema hivi baada ya kukata tamaa na kuongoka kwao.
Akasema - Mwenyezi Mungu -baada ya muda mchache hakika watakuwa ni wenye kujuta, kutokana na shirki yao na uasi wao ambapo Mwenyezi Mungu atawapatiliza kwa mpatilizo wa mwenye nguvu mwenye uwezo.
Basi ukawanyakua ukelele kwa haki.
Makusudio ya ukelele ni adhabu. Kusema kwake kwa haki ni ishara ya kuwa wanastahili adhabu kutokana na waliyoyafanya.
Tukawafanya takataka zinazoelea juu ya maji.
Yaani wako sawasawa na vitu duni vinavyoelea kwenye maji.
Ikapotelea mbali kaumu ya madhalimu.
Wamepotelea mbali na Mwenyezi Mungu na twaa yake naye akawaweka mbali na fadhila zake na rehema zake.
ثُمَّ أَنشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قُرُونًا آخَرِينَ ﴿٤٢﴾
42. Kisha baada yao tukaanzisha karne niyingine.
مَا تَسْبِقُ مِنْ أُمَّةٍ أَجَلَهَا وَمَا يَسْتَأْخِرُونَ ﴿٤٣﴾
43. Hapana umma unaoweza kutanguliza ajali yake wala kuikawiza.
ثُمَّ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا تَتْرَىٰ كُلَّ مَا جَاءَ أُمَّةً رَّسُولُهَا كَذَّبُوهُ فَأَتْبَعْنَا بَعْضَهُم بَعْضًا وَجَعَلْنَاهُمْ أَحَادِيثَ فَبُعْدًا لِّقَوْمٍ لَّا يُؤْمِنُونَ ﴿٤٤﴾
44. Kisha tukawapeleka mitume wetu mmoja baada ya mmoja. Kila umma alipowafikia Mtume wao walimkanusha. Tukawafuatishia baadhi yao wengine, ikapotelea mbali kaumu isiyoamini.
ثُمَّ أَرْسَلْنَا مُوسَىٰ وَأَخَاهُ هَارُونَ بِآيَاتِنَا وَسُلْطَانٍ مُّبِينٍ ﴿٤٥﴾
45. Kisha tukamtuma Musa na nduguye Harun pamoja na ishara zetu, na hoja zilizo wazi.
إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا عَالِينَ ﴿٤٦﴾
46. Kwenda kwa Firaun na wakuu wake, lakini wakajivu- na na walikuwa ni kaumu waliojikweza.
فَقَالُوا أَنُؤْمِنُ لِبَشَرَيْنِ مِثْلِنَا وَقَوْمُهُمَا لَنَا عَابِدُونَ ﴿٤٧﴾
47. Wakasema: Je, tuwaamini watu wawili hawa kama sisi, na ambao watu wao ni watumwa wetu?
فَكَذَّبُوهُمَا فَكَانُوا مِنَ الْمُهْلَكِينَ ﴿٤٨﴾
48. Basi wakawakadhibisha wakawa miongoni mwa walioangamizwa.
وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ لَعَلَّهُمْ يَهْتَدُونَ ﴿٤٩﴾
49. Na hakika tulimpa Musa Kitabu ili wapate kuongoka.
وَجَعَلْنَا ابْنَ مَرْيَمَ وَأُمَّهُ آيَةً وَآوَيْنَاهُمَا إِلَىٰ رَبْوَةٍ ذَاتِ قَرَارٍ وَمَعِينٍ ﴿٥٠﴾
50. Tukamfanya mwana wa Maryam na mama yake kuwa ni ishara. Na tukawapa kimbilio kwenda mahali palipoinuka, penye utulivu na chemchem za maji.
KILA UMMA ULIKANUSHA MTUME WAKE ALIPOWAFIKIA
Aya 42-50
Kisha baada yao tukaanzisha karne niyingine.
Baada yao ni baada ya A'd na karne ni watu. Watu wa kwanza kuja baada ya A'd ni Thamud, kwa dalili ya yaliyoelezwa katika Juz. 8 (7:74)
Hapana umma unaoweza kutanguliza ajali yake wala kuikawiza.
Kila kitu isipokuwa, Mwenyezi Mungu (s.w.t), kina muda wake hauchelewi wala kuja haraka. Miongoni mwa hayo ni kuangamia wale waliokadhibisha mitume yao. Adhabu ilikuwa ikawajia ghafla bila ya kutambua wala kuhisi.
Kisha tukawapeleka mitume wetu mmoja baada ya mmoja.
Mitume walikuwa wakija mmoja baada ya mwingine. Kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) alijaalia kila umma uwe na mtume.
Kila umma alipowafikia Mtume wao walimkanusha au kumuua. Si kwa lolote ila ni kwa kuwa amekuja na ambayo matamanio yao yanayakataa; kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Kila alipowajia Mtume kwa yale yasiyoyapenda nafsi zenu, mlijivuna, kundi moja mkalikadhibisha na kundi jingine mkaliua." Juz. 1 (2:87)
Tukawafuatishia baadhi yao wengine.
Yaani Mwenyezi Mungu aliangamiza umma uliomkadhibisha Mtume wake mmoja baada ya mwingine na akajaalia ni mazingatio kwa mwenye kuzingatia na habari watayoinukuu kizazi baada ya kizazi kingine.
Ikapotelea mbali kaumu isiyoamini haki wala kuitumia.
Kisha tukamtuma Musa na nduguye Harun pamoja na ishara zetu, kama vile fimbo kugeuka nyoka na kumeremeta mkono, na hoja zilizo wazi za kunyamazisha.
Kwenda kwa Firaun na wakuu wake, lakini wakajivuna na walikuwa ni kaumu waliojikweza.
Kuna kujikweza gani na majivuno makubwa zaidi ya kauli ya Firaun:
فَقَالَ أَنَا رَبُّكُمُ الْأَعْلَىٰ ﴿٢٤﴾
"Mimi ni Mola wenu mkuu." (79:24)
Au pale aliposema:
مَا عَلِمْتُ لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرِي ﴿٣٨﴾
"Simjui kwa ajili yenu mungu asiyekuwa mimi." (28:38).
Watu wengi wana moyo kama wa Firaun, wanaweza kudai uungu kama watakuwa na nyenzo na kupata watakaomwitikia kama alivyopata Firaun.
Wakasema: "Je, tuwaamini watu wawili hawa kama sisi, na ambao watu wao ni watumwa wetu?"
Firauni alidai uungu na akawaadhibu waisrail kwa kuwachinja watoto wao wa kiume na kuwaacha wa kike. Na Musa na Harun ni katika waisrail; vipi watawafuata?
Basi wakawakadhibisha wakawa miongoni mwa walioangamizwa. Kila anayepituka mipaka mwisho wake ni maangamizi tu. Na hakika tulimpa Musa Kitabu ili wapate kuongoka.
Makusudio ya Kitabu hapa ni Tawrat na wanaotakiwa kuongoka ni wana wa Israil, lakini hawakuongoka na wala hawataongoka kamwe baada ya kuipotoa Tawrat, wakafuata matamanio yao na wakaijaza dunia ufisadi na upotevu.
Kisa cha Musa kimekaririka mara nyingi kwenye Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Tumebainisha sababu ya kukaririka kisa katika Juz. 16 (20:9) Kifungu cha 'Kukaririka kisa cha Musa.'
Tukamfanya mwana wa Maryam na mama yake kuwa ni ishara.
Yaani muujiza. Isa ni muujiza kwa sababu amezaliwa bila ya Baba na Mama yake ni mujiza kwa vile amezaa bila ya mume. Tazama Juz. 3 (3:45-51).
Na tukawapa kimbilio kwenda mahali palipoinuka. Makusudio ni Palestina, kwa sababu Bwana Masih alizaliwa hapo, napo ni penye utulivu na chemchem za maji.
3
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ ﴿٥١﴾
51. Enyi Mitume! Kuleni katika vitu vizuri na fanyeni mema. Hakika mimi ni Mjuzi wa mnayoyatenda.
وَإِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاتَّقُونِ ﴿٥٢﴾
52. Na hakika umma wenu huu ni umma mmoja na mimi ni Mola wenu, basi nicheni.
فَتَقَطَّعُوا أَمْرَهُم بَيْنَهُمْ زُبُرًا كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ ﴿٥٣﴾
53. Lakini walikatiana jambo lao kwa vitabu mbali mbali. Kila kundi linafurahia kwa waliyo nayo.
فَذَرْهُمْ فِي غَمْرَتِهِمْ حَتَّىٰ حِينٍ ﴿٥٤﴾
54. Basi waache katika upotevu wao kwa muda.
أَيَحْسَبُونَ أَنَّمَا نُمِدُّهُم بِهِ مِن مَّالٍ وَبَنِينَ ﴿٥٥﴾
Je wanadhani kuwa vile tunavyowapa mali na watoto.
نُسَارِعُ لَهُمْ فِي الْخَيْرَاتِ بَل لَّا يَشْعُرُونَ ﴿٥٦﴾
56. Ndio tunawahimizia kheri? Lakini hawatambui.
MOLA MMOJA NA DINI MOJA
Aya 51 – 56
Katika Juz. 2 (2:172) Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawaambia waumini: "Kuleni vizuri tulivyowaruzuku na mumshukuru Mwenyezi Mungu." Katika Aya hii anawaambia Mitume: Kuleni katika vitu vizuri na fanyeni mema. Hakika mimi ni Mjuzi wa mnayoyatenda.
Lengo la kauli zote hizo ni kubainisha kuwa dini ya haki ni takua na matendo mema sio kujinyima raha. Kila utakalolifurahia na kuburudika nalo basi hilo ni jema mbele ya Mwenyezi Mungu, ikiwa hakulikataza; sawa na lilivyo jema kwako. Kuna Hadith isemayo:"Hakika Mwenyezi Mungu ni Mzuri na hupenda uzuri."
Na kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) alikuwa akivaa kila ali- chokimudu katika sufu, pamba (cotton) na vitambaa vinginevyo. Hakuwa akikataa vitu vizuri, lakini hakujikalifisha navyo.
Alikuwa akila haluwa na asali na akizipenda. Akila nyama ya ngamia, kondoo na kuku. Pia alikuwa akila matango na maboga kwa tende mbichi, na akipenda kula tende kwa siagi, mkate kwa nyama na maini ya kuchoma na mkate wa kuchanganywa na mchuzi.
Kwa ujumla Mtume(s.a.w.w) alikuwa akila na kuvaa kile anachokimudu, akikosa huvumilia na kuwa na subira. Na kitu kizuri zaidi ni kula kwa jasho. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) anasema: "Ni katika uzuri zaidi mtu kula kutokana na chumo lake."
Na hakika umma wenu huu ni umma mmoja na mimi ni Mola wenu, basi nicheni.
Neno umma lina maana nyingi; miongoni mwazo ni hizi:-
1. Kundi la watu: Kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Ingieni motoni pamoja na umma zilizopita." Juz. 8 (7:38).
2. Muda: Mwenyezi Mungu anasema: "Na akakumbuka baada ya muda." Juz. 12 (12:45).
Neno muda limefasiriwa kutokana na neno umma.
3. Mila: Kama ilivyo katika Aya hii tuliyo nayo.
Aya hii inaashiria mila za Mitume wote. Msemo katika neno umma wenu, unaelekezwa kwa watu wote, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu iliyokuja moja kwa moja 'lakini walikatiana jambo lao ...' ambapo maana ni kwa nini watu wanachukiana na kuwa vikundi mbali mbali, kukawa na kikundi cha Musa, cha Isa na cha Muhammad na hali Mungu wao ni mmoja, dini yao ni moja na lengo lao ni moja? Kuna Hadith isemayo: "Mitume wote ni ndugu, mama zao ni mbali mbali na dini yao ni moja."
Unaweza kuuliza : kwanini sharia za mitume ni tofauti na dini yao ni moja?
Jibu : Kutofautiana sharia hakusababishi kutofautiana dini maadamu msingi ni mmoja; kwa mfano serikali za kikiristo zinatofautiana kikanuni na kisheria, lakini zinakuwa pamoja kiitikadi na kidini.
Lakini walikatiana jambo lao kwa vitabu mbali mbali. Kila kundi linafurahia kwa waliyo nayo.
Hapa wanazungumziwa wafuasi wa Mitume; yaani mitume wako kwenye dini moja, lakini wafuasi wao wako kwenye dini mbali mbali. Kila kundi likafuata Kitabu wanachokiamini na kukikana kingine. Mayahudi waliamini Tawrat baada ya kuipotoa na kuikana Injil na Qur'an. Wanaswara nao waliipotoa Injil na wakiamini pamoja na Tawrt iliyopotolewa na wakaikana Qur'an.
Tazama tuliyoyaandika kwa anuani ya 'Kila mmoja avutia dini yake' Juz. 1 (2: 111-113).
Basi waache katika upotevu wao kwa muda.
Baada ya Mtume(s.a.w.w) kuwafikishia risala ya Mola wake na akawaondolea nyudhuru zote kwa jinsi alivyowahadharisha, Mwenyezi Mungu alimwamrisha kuachana nao na awaache na upotevu wao.
Hili ni karipio na kiaga kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu iliyokuja moja kwa moja Je wanadhani kuwa vile tunavyowapa mali na watoto ndio tunawahimizia kheri? Lakini hawatambui.
Wamedanganyika na watoto na mali wakadhani kuwa watadumu nazo, lakini hakujua kuwa Mungu amewawekea muda maalum, kisha awanyakue kwa mnyakuo wa Mwenye nguvu na ushindi.
إِنَّ الَّذِينَ هُم مِّنْ خَشْيَةِ رَبِّهِم مُّشْفِقُونَ ﴿٥٧﴾
57. Hakika wale ambao humwogopa Mola wao wanamnyenyekea.
وَالَّذِينَ هُم بِآيَاتِ رَبِّهِمْ يُؤْمِنُونَ ﴿٥٨﴾
58. Na wale ambao wanaamini ishara za Mola wao.
وَالَّذِينَ هُم بِرَبِّهِمْ لَا يُشْرِكُونَ ﴿٥٩﴾
59. Na wale ambao hawamshirikishi Mola wao.
وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَىٰ رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ ﴿٦٠﴾
60. Na wale ambao wanatoa walichopewa na hali nyoyo zao zinaogopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao.
أُولَـٰئِكَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ ﴿٦١﴾
61. Hao ndio wanokimbilia kwenye kheri na ndio watakaotangulia kuzifikia.
وَلَا نُكَلِّفُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا وَلَدَيْنَا كِتَابٌ يَنطِقُ بِالْحَقِّ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٦٢﴾
62. Na hatuikalifishi nafsi ila kwa uwezo wake. Na tuna kitabu kisemacho kweli. Nao hawatadhulumiwa.
Aya 57 – 62
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja wale wanaoishi kwenye mghafala wa upotevu, huku wenyewe wakiona kuwa wanaharakishiwa kheri, sasa anawataja waumini, kwamba ni wale wanaosifika na mambo yafuatayo:
1.Hakika wale ambao humwogopa Mola wao wanamnyenyekea.
Unaweza kuuliza kuwa : kunyenyenyekea pia ni kuogopa, sasa itakuwaje wao wawe 'wanaogopa kuogopa'?
Jibu : Makusudio ya kunyenyekea hapa ni kupupia kumtii Mwenyezi Mungu. Makadirio ya maneno ni, wao wanapupia kumtii Mwenyezi Mungu kwa kuhofia adhabu yake.
2.Na wale ambao wanaamini ishara za Mola wao.
Yaani wanaamini dalili za kuweko Mungu na ukuu wake, utume wa Mitume yake na ukweli wa vitabu vyake.
3.Na wale ambao hawamshirikishi Mola wao.
Unaweza kuuliza : Wale ambao wanaziamini ishara zake bila shaka hawawezi kumshirikisha, sasa kuna haja gani ya kurudia maneno? Razi amejibu kuwa makusudio ya shirki hapa ni ile shirki iliyojificha; kama vile ria na kukosa ikhlasi katika matendo. Makusudio ya imani katika Aya iliyotangulia ni kule kuamini tu.
4.Na wale ambao wanatoa walichopewa na hali nyoyo zao zinaogopa kwa kuwa watarejea kwa Mola wao.
Wanatoa katika vile alivyowapa Mwenyezi Mungu na kutekeleza haki yake na haki za watu kwa ukamilifu, lakini pamoja na hayo wanahofia kuwa Mwenyezi Mungu hatawatakabalia.
Hao ndio wanaokimbilia kwenye kheri na ndio watakaotangulia kuzifikia.
Yaani wale ambao wametimiza masharti haya yaliyotajwa ndio wanaoharakia twaa ya Mwenyezi Mungu na wala hawangojingoji. Kwa ajili hiyo basi wao watawatangulia watu kuingia peponi kesho.
Na hatuikalifishi nafsi ila kwa uwezo wake.
Kwa sababu kukalifisha lisilowezekana ni dhulma, na Mwenyezi Mungu ambaye ameikataza dhulma hawezi kuifanya.
Na tuna kitabu kisemacho kweli.
Kinasajili dogo na kubwa na Mwenyezi Mungu atalipa kwacho; ikiwa ni kheri basi ni kheri na ikiwa ni shari basi ni shari.
Nao hawatadhulumiwa kwa kupunguziwa thawabu mwenye kufanya wema wala kuzidishiwa adhabu mwenye kufanya uovu.
بَلْ قُلُوبُهُمْ فِي غَمْرَةٍ مِّنْ هَـٰذَا وَلَهُمْ أَعْمَالٌ مِّن دُونِ ذَٰلِكَ هُمْ لَهَا عَامِلُونَ ﴿٦٣﴾
63. Bali nyoyo zao zimo ujingani na haya na wana vitendo vingine wanavyovitenda.
حَتَّىٰ إِذَا أَخَذْنَا مُتْرَفِيهِم بِالْعَذَابِ إِذَا هُمْ يَجْأَرُونَ ﴿٦٤﴾
64. Mpaka tutakapowatia katika adhabu wale waliodekezwa na starehe kati yao, hapo ndipo watakapoyayatika.
لَا تَجْأَرُوا الْيَوْمَ إِنَّكُم مِّنَّا لَا تُنصَرُونَ ﴿٦٥﴾
65. Msiyayatike leo! Hakika nyinyi hamtanusurika nasi.
قَدْ كَانَتْ آيَاتِي تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَكُنتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ تَنكِصُونَ ﴿٦٦﴾
66. Hakika zilikuwa Aya zangu mkisomewa nanyi mkirudi nyuma juu ya visigino vyenu.
مُسْتَكْبِرِينَ بِهِ سَامِرًا تَهْجُرُونَ ﴿٦٧﴾
67. Na huku mkiifanyia kiburi na mkiizungumza usiku kwa dharau.
أَفَلَمْ يَدَّبَّرُوا الْقَوْلَ أَمْ جَاءَهُم مَّا لَمْ يَأْتِ آبَاءَهُمُ الْأَوَّلِينَ ﴿٦٨﴾
68. Je, hawakuifikiri kauli au yamewafikia yasiyowafikia baba zao wa zamani?
أَمْ لَمْ يَعْرِفُوا رَسُولَهُمْ فَهُمْ لَهُ مُنكِرُونَ ﴿٦٩﴾
69. Au hawakumjua Mtume wao ndio maana wanamkataa?
أَمْ يَقُولُونَ بِهِ جِنَّةٌ بَلْ جَاءَهُم بِالْحَقِّ وَأَكْثَرُهُمْ لِلْحَقِّ كَارِهُونَ ﴿٧٠﴾
70. Au wanasema ana wazimu? Bali amewajia na haki na wengi wao wanaichukia haki.
وَلَوِ اتَّبَعَ الْحَقُّ أَهْوَاءَهُمْ لَفَسَدَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ بَلْ أَتَيْنَاهُم بِذِكْرِهِمْ فَهُمْ عَن ذِكْرِهِم مُّعْرِضُونَ ﴿٧١﴾
71. Na lau haki ingelifuata matamanio yao basi zingeliharibika mbingu na ardhi na waliomo ndani yake. Bali tumewaletea utajo wao na wanajitenga mbali na utajo wao.
أَمْ تَسْأَلُهُمْ خَرْجًا فَخَرَاجُ رَبِّكَ خَيْرٌ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴿٧٢﴾
72. Au unawaomba ujira? Lakini ujira wa Mola wako ni bora na Yeye ndio mbora wa wanaoruzuku.
Aya 63 – 72
Bali nyoyo zao zimo ujingani na haya na wana vitendo vingine.
Wanaelezewa washirikina. Neno 'haya' ni haya aliyoyataja Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya zilizotangulia kuhusu sifa za waumini ambazo ni kumwamini Mwenyezi Mungu, kumhofia na kukimbilia kheri.
Maana ni kuwa waashirikina wamo kwenye mghafala na sifa hizi pia wana maovu mengine zaidi ya ushirikina; kwamba wao wanaifanyia maskhara Qur'an na kumzulia Mtume wa Mwenyezi Mungu huku wakisema kuwa yeye ni mchawi mwendawazimu.
Wanavyovitenda.
Unaweza kuuliza : maana ya kutenda si ndio hivyo vitendo, sasa itakuwaje watende vitendo?
Jibu : Makusudio ya vitendo hapa ni vitendo viovu; ni kama Mwenyezi Mungu (s.w.t) amesema wao wanatenda maovu.
Mpaka tutakapowatia katika adhabu wale waliodekezwa na starehe kati yao, hapo ndipo watakapoyayatika.
Hayo ndio mazoweya ya wanaodeka, wanazama kwenye upotevu. Kwa maelezo zaidi tazama Juz. 15 (17:16).
Wao wameghafilika kabisa na mambo ya ghafla yaliyojificha wala hawazingatii mifano ya waliowatangulia, mpaka itakapowafikia siku ya Kiyama na ikafika saa ya hisabu na malipo ndipo watainua sauti zao kwa kulia na kuomboleza, huku wakinyenyeka, wakati ambao hakuna msaada wowote wala maneno yoyote ya kutuliza isipokuwa kauli ya Mwenyezi Mungu, Mwenye nguvu:
Msiyayatike leo! Hakika nyinyi hamtanusurika nasi.
Yaani msitafute msaada wala kunyenyekea, kwani leo ni siku ya hisabu na malipo tu, na wala hataokoka na adhabu yake isipokwa yule aliyefanya matendo kwa ajili ya siku hii.
Hakika zilikuwa Aya zangu mkisomewa nanyi mkirudi nyuma juu ya visigino vyenu.
Mwenyezi Mungu amewahadharisha na siku hii kupitia kwa mitume wake, mara nyingi na kwa mifumo tofauti tofauti, lakini wakakataa isipokuwa kukadhibisha na kufanya inadi. Ndio akawalipa kwa yale waliyoyafanya; wala Mola wako hatamdhulumu yeyote.
Na huku mkiifanyia kiburi na mkiizungumza usiku kwa dharau.
Dhamiri katika neno mkiifanyia inarudia Qur'an na kuifanyia kiburi ni kuikadhibisha. Maana yanakuwa wao wameikadhibisha Qur'an na wakafanya hiyo Qur'an na yule aliyeteremshiwa kuwa ni gumzo lao la usiku kwa dharau
Je, hawakuifikiri kauli ambayo ni Qur'an na dalili iliyo nazo juu ya tawhidi na ukweli wa Muhammad(s.a.w.w) . Au yamewafikia yasiyowafikia baba zao wa zamani?
Vipi iwe hivyo na hali Qur'an inasadikisha wale waliotangulia katika mitume na habari ya yaliyowatokea pamoja na watu wao.
Zaidi ya hayo, washirikina wa kiarabu wanamjua Ibrahim, Hud, Swaleh na Shua'yb. Mitume wote hawa watatu ni waarabu. Kwa hiyo basi kuna kioja gani katika utume wa Muhammad?
Au hawakumjua Mtume wao ndio maana wanamkataa?
Au Makuraishi wataleta udhuru kuwa hawamjui Muhammad naye ni miongoni mwao tena walikuwa wakimwita mkweli mwaminifu? Au wanasema ana wazimu? Na hali wanajua kuwa yeye ndiye mwenye akili na mkamilifu wao zaidi? Kwa hiyo hapa kuna mengine sio haya. Kwa muhtasari ni haya yafuatayo:
Bali amewajia na haki na wengi wao wanaichukia haki.
Muhammad alikuja na haki. Hilo peke yake ni kosa kwa wabatilifu. Ni haki gani hiyo aliyokuja nayo Muhammad? Je, ni kutamka shahada mbili tu basi? Ingelikuwa hivyo ingelikuwa wepesi kwa wanompiga vita na viongozi na waanojidekeza na starehe kusema: "Hapana Mola isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu."
Lakini Muhammad hakutosheka na matamshi haya, bali alitaka kuweka ustawi wa jamii kwa misingi ya uadilifu na usawa, usiokuwa na dhalimu wala mdhulumiwa na kila mtu aishi kama sehemu ya mwingine na kiungo cha jamii; astahiki wanayostahiki wengine na wengine nao wastahiki yale anayostahiki yeye, asimwogope yeyote isipokuwa Mwenyezi Mungu mmoja tu peke yake, wala kusiwe na ubora wa kiumbe kwa kiumbe mwingine isipokuwa kwa takua na matendo mema.
Kuanzia hapa ndio ukajitokeza ukali na uadui dhidi ya Mjumbe wa uadilifu na huruma; wakampiga vita kwa kila silaha. Lakini Mtume(s.a.w.w) alikuwa na yakini na jambo lake na kwamba mwisho utakuwa ni wa msin- gi wake na risala yake. Kwa ajili hii alikuwa akiwatazama mahasimu wake, kama anavyotazama mawingu ya kaskazi au kivuli kinachoondoka.
Na lau haki ingelifuata matamanio yao basi zingeliharibika mbingu na ardhi na waliomo ndani yake.
Makusudio ya haki hapa ni Mwenyezi Mungu na matamanio yao ni batili, upotevu, vurugu na ufisadi. Nidhamu ya ulimwengu pamoja na ardhi yake na mbingu yake inasimama kwa misingi ya uadilifu na haki. Kwa hiyo kuharibika ulimwengu hakuna budi ikiwa haki itafuata matamanio yao.
Hapana shaka kwamba lau Mwenyezi Mungu (s.w.t) ataitikia matakwa yao na wanayoyatamani, basi wangelizuia mwanga wa jua kuwafikia wanyonge na wangeliuzia ulimwengu na yaliyomo ndani yake kwa jili yao wenyewe, watoto wao na wakwe zao.
Bali tumewaletea utajo wao nao wanajitenga mbali na utajo wao.
Muhammad(s.a.w.w) aliwaletea waarabu kwa ujumla na hasa makuraishi, utajo wao; yaani utawala wao sifa zao na historia yao, lakini wakamkana bali wakamuwekea vikwazo na kumpiga vita.
Lau si yeye wasingelikuwa chochote cha kutajwa. Mwenyezi Mungu anasema:
وَإِنَّهُ لَذِكْرٌ لَّكَ وَلِقَوْمِكَ ﴿٤٤﴾
"Na hakika hiyo (Qur'an) ni utajo kwako na kwa kaumu yako' (43:44).
Au unawaomba ujira? Lakini ujira wa Mola wako ni bora na Yeye ndio mbora wa wanaoruzuku.
Mtume aliwaletea utukufu wa dunia na akhera, lakini wakaukataa pamoja na kujua kwamba yeye hakuwataka malipo wala shukrani, kwa sababu Mwenyezi Mungu anamtosha kwenye dunia yake na akhera.
4
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
وَإِنَّكَ لَتَدْعُوهُمْ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٧٣﴾
73. Na hakika wewe unawaita kwenye njia iliyonyooka.
وَإِنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ عَنِ الصِّرَاطِ لَنَاكِبُونَ ﴿٧٤﴾
74. Na hakika wale ambao hawaiamini akhera wanajitenga na njia hiyo.
وَلَوْ رَحِمْنَاهُمْ وَكَشَفْنَا مَا بِهِم مِّن ضُرٍّ لَّلَجُّوا فِي طُغْيَانِهِمْ يَعْمَهُونَ ﴿٧٥﴾
75. Lau tungeliwarehemu tukawaondolea shida waliyo nayo, bila shaka wangeliendelea na upotevu wao wakimangamanga.
وَلَقَدْ أَخَذْنَاهُم بِالْعَذَابِ فَمَا اسْتَكَانُوا لِرَبِّهِمْ وَمَا يَتَضَرَّعُونَ ﴿٧٦﴾
76. Na hakika tuliwatia katika adhabu, lakini hawakuelekea kwa Mola wao wala hawakunyenyekea.
حَتَّىٰ إِذَا فَتَحْنَا عَلَيْهِم بَابًا ذَا عَذَابٍ شَدِيدٍ إِذَا هُمْ فِيهِ مُبْلِسُونَ ﴿٧٧﴾
77. Mpaka tulipowafungulia mlango wa adhabu kali, hapo ndipo wakawa ni wenye kukata tamaa.
وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ قَلِيلًا مَّا تَشْكُرُونَ ﴿٧٨﴾
78. Yeye ndiye aliyewaumbia kusikia na kuona na nyoyo. Ni kuchache mno kushukuru kwenu.
وَهُوَ الَّذِي ذَرَأَكُمْ فِي الْأَرْضِ وَإِلَيْهِ تُحْشَرُونَ ﴿٧٩﴾
79. Yeye ndiye aliyewaumba katika ardhi na kwake mtakusanywa.
وَهُوَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ وَلَهُ اخْتِلَافُ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿٨٠﴾
80. Yeye ndiye anayehuisha na kufisha na Yeye ndiye mwenye mabadiliko ya usiku na mchana. Basi je, hamfahamu?
Aya 73 – 80
Na hakika wewe unawaita kwenye njia iliyonyooka. Na hakika wale ambao hawaiamini akhera wanajitenga na njia hiyo.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuelezea upotevu wa washirikina na kwamba wao hawana udhuru wowote wa kumkanusha kwao Muhammad(s.a.w.w) , sasa anamwambia Mtume wake Mtukufu kwamba yeye anazo hoja za kutosha kuwa yeye ni mkweli katika mwito wake na kwamba washirikina ambao wamemkanusha yeye na siku ya mwisho wameiacha haki na wakapotea njia ya kheri na uongofu. Nao, katika hilo, wanajidhu- ru wenyewe na hawatakudhuru wewe na chochote.
Lau tungeliwarehemu tukawaondolea shida waliyo nayo, bila shaka wangeliendelea na upotevu wao wakimangamanga.
Baada ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) kuhamia Madina kutoka Makka aliwapa dhiki makuraishi kwa kutuma vikosi kuwazuilia njia, mara nyingine alikuwa akiviongoza mwenyewe, na akaamrisha kuwakatia uhu- siano. Basi wakaingia kwenye dhiki, lakini bado waliendelea na upotevu wao na kufuru yao. Lau kama Mwenyezi Mungu (s.w.t) angeliwaondolea shida waliyo nayo, wasingelizingatia kuachana na upotevu wao.
Na hakika tuliwatia katika adhabu, lakini hawakuelekea kwa Mola wao wala hawakunyenyekea.
Ukiwahadharisha wanapinga, ukiwatia adabu hawazingatii na ukiwaondolea wanakuwa jeuri. Watakuwa hivi mpaka siku watakapofufuliwa, watakpoondolewa pazia washuhudie malipo ya mghafala wao na jeuri yao. Hapo watakata tamaa ya kuokoka na kujutia yaliyopita.
Mpaka tulipowafungulia mlango wa adhabu kali, hapo ndipo wakawa wenye kukata tamaa na hali Mwenyezi Mungu (s.w.t) alikwishawahadharisha na adhabu hii kali na kuwapa kiaga, lakini wakapuuza nafsi zao wakazipeleka kwenye maangamizi.
Yeye ndiye aliyewaumbia kusikia na kuona na nyoyo za kufahamu, ili mnufaike kwa mtakyoyasikia na kuyaona muweze kujua ya kheri na masilahi.
Neema za Mwenyezi Mungu kwa mtu hazina idadi, kubwa yake ni akili kisha usikizi na uoni. Ametangulia kutaja usikizi kwa sababu mtoto anayezaliwa huanza kusikia tangu kuzaliwa kwake, wala haoni mpaka siku ya nne; kama wanavyosema. Ama kuchelewa akili hilo liko wazi.
Ni kuchache mno kushukuru kwenu; yaani kutii kwenu.
Yeye ndiye aliyewaumba katika ardhi na kwake mtakusanywa.
Alituuumba katika ardhi hii kisha atatufufua kwake baada ya mauti. Yeye ndiye anayehuisha na kufisha na Yeye ndiye mwenye mabadiliko ya usiku na mchana. Basi je, hamfahamu? Hakika huu ni utengenezaji wa Mwenye uweza aliye Mjuzi. Tazama Juz. 1 (2:28 -29) na Juz. 3: (3:26-27).
بَلْ قَالُوا مِثْلَ مَا قَالَ الْأَوَّلُونَ ﴿٨١﴾
81. Bali walisema kama walivyosema wa mwanzo.
قَالُوا أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ ﴿٨٢﴾
82. Je, tukishakufa tukawa mchanga na mifupa ndio tutafufuliwa?
لَقَدْ وُعِدْنَا نَحْنُ وَآبَاؤُنَا هَـٰذَا مِن قَبْلُ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ ﴿٨٣﴾
83. Tuliahidiwa haya sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni vigano vya wa kale.
قُل لِّمَنِ الْأَرْضُ وَمَن فِيهَا إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٨٤﴾
84. Sema, ni ya nani ardhi na vilivyomo ndani yake, kama nyinyi mnajua?
سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ قُلْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٨٥﴾
85. Watasema, ni vya Mwenyzi Mungu. Basi je, hamkumbuki?
قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ ﴿٨٦﴾
86. Sema, ni nani Mola wa mbingu saba na Mola wa arshi tukufu?
سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ قُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٨٧﴾
87. Watasema, ni vya Mwenyezi Mungu. Sema, basi je, hamuogopi?
قُلْ مَن بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ يُجِيرُ وَلَا يُجَارُ عَلَيْهِ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٨٨﴾
88. Sema, ni nani mkononi mwake umo ufalme wa kila kitu? Na yeye ni mlinzi wala hapalindwi kwake, kama mnajua.
سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ قُلْ فَأَنَّىٰ تُسْحَرُونَ ﴿٨٩﴾
89. Watasema, ni wa Mwenyezi Mungu. Sema, basi vipi mnadanganyika?
بَلْ أَتَيْنَاهُم بِالْحَقِّ وَإِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ ﴿٩٠﴾
90. Bali tumewaletea haki. Na kwa hakika wao ni waongo.
Aya 81 – 90
Bali walisema kama walivyosema wa mwanzo.
Waliosema ni washirikina waliokuwa zama za Mtume(s.a.w. w ) . Walikanusha ufufuo, wakatoa sababu mbili:
Kwanza : ni kustaajabu walikokuleta kwa ibara hii:
Je, tukishakufa tukawa mchanga na mifupa ndio tutafufuliwa?
Pili : kwamba wao hawajamuona aliyekufa kisha akarudi kuwa hai. Maana haya yamekusudiwa katika kauli yao:
Tuliahidiwa haya sisi na baba zetu zamani. Hayakuwa haya ila ni vigano vya wa kale.
Yaani tumeyasikia kabla yako ewe Muhammad, pia tuliyasikia kwa wazee wetu, lakini hakujatokea athari yoyote. Ni nani aliyekufa kisha akarudi kutoa habari?
Lau wangelitaamali uumbaji wa kwanza wasingelipinga uumbaji wa pili. Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13:5) na Juz. 15 (17:49).
Mwenyezi Mungu (s.w.t) amewajadili wapinzani hawa, kwa mfumo wa kielimu wenye hekima, katika Aya tatu zifuatazo:-
1.Sema, ni ya nani ardhi na vilivyomo ndani yake, kama nyinyi mnajua?
Alimwamrisha Mtume wake kuwakabili na swali hili. Kwa sababu wao wanakiri na kukubali kwamba Mwenyezi Mungu ndiye muumba wa ulimwengu, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu:
Watasema, ni vya Mwenyezi Mungu.
Yaani ardhi na vilivyomo ndani yake ni vya Mwenyezi Mungu; wala hakuna maana ya kuwa ni vyake ila ni kwakuwa ameviumba na kuvianzisha. Ikiwa Mwenyezi Mungu ni muweza wa kuumba ardhi basi vilevile Yeye anaweza kufufua wafu.
Basi je, hamkumbuki na kufikiria hakika hii ambayo ni aliyeweza kuanzisha mara ya kwanza pia anaweza kurudisha mara ya pili? Kila anayeweza kitu, asiyekuwa Mwenyezi Mungu, anashindwa na vingine, anajua vichache na hajui vingi. Lakini Yeye Mwenyezi Mungu ni Muweza na Mjuzi wa kila kitu.
2.Sema, ni nani Mola wa mbingu saba na Mola wa arshi tukufu? Watasema, ni vya Mwenyezi Mungu.
Arshi ni kinaya cha ufalme wake Mwenyezi Mungu Mtukufu na utawala wake. Ambaye mbingu na ardhi ni yake basi ni wepesi kwake kumrudisha aliyekufa humo.
Sema, basi je, hamuogopi ghadhabu za Mwenyezi Mungu na adhabu yake?
Tumezungumzia kuhusu mbingu saba katika Aya 17 ya sura hii
3.Sema, ni nani mkononi mwake umo ufalme wa kila kitu?
Makusudio ya ufalme wa kila kitu ni kuwa kila kitu kinamnyenyekea na kumhitajia Yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwamba hahitajii chochote.
Na yeye ni mlinzi wala hapalindwi kwake, kama mnajua.
Yeye ni rehema kwa mwenye kutaka rehema na ni uokovu kwa anayetaka kuokoka; wala hapana mwenye kuweza kumrehemu au kumuokoa yule ambaye anastahiki ghadhabu na adhabu yake.
Watasema: ni wa Mwenyezi Mungu.
Ufalme wa mbingu na ardhi ni wake.
Sema: basi vipi mnadanganyika?
Maadamu mnakubali hayo, basi vipi mnaukana ufufuo na kuhadika na haki?
Bali tumewaletea haki.
Hapana! Hawakudanganyika na haki wala hawakutatizika na batili, baada ya kuwasimamia hoja na dalili zilizo wazi. Na kwa hakika wao ni waongo. Hawakuhadaika isipokuwa wamejitia kuhadaika na kudhihirisha uongo na uzushi. Wao hawakutosheka na ufufuo kwa hoja kwamba dalili zake zimejificha.
Unaweza kuuliza : Imejulikana vipi kwamba wao walikana ufufuo wakiwa na imani nao, na kuna Aya nyingi zimeonyesha mshangao wao na kutojua kwao kukisia uumbaji wa kwanza na ufufuo?
Jibu : Ndio ni kweli, lakini kila ambaye amepatiwa hoja za kutosha zilizo wazi na akaendelea kukataa, ni sawa na yule anayekataa makusudi.
مَا اتَّخَذَ اللَّـهُ مِن وَلَدٍ وَمَا كَانَ مَعَهُ مِنْ إِلَـٰهٍ إِذًا لَّذَهَبَ كُلُّ إِلَـٰهٍ بِمَا خَلَقَ وَلَعَلَا بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿٩١﴾
91. Mwenyezi Mungu hakujifanyia mwana, wala hanaye mungu mwingine. Ingelikuwa hivyo basi kila Mungu angelichukua alivyoviumba. Na baadhi yao wangeliwashinda wengine. Ametakata Mwenyezi Mungu na wanavyomsifu.
عَالِمِ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ فَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٩٢﴾
92. Mjuzi wa ghaibu na dhahiri. Ametukuka juu ya hayo wanayomshirikisha nayo.
قُل رَّبِّ إِمَّا تُرِيَنِّي مَا يُوعَدُونَ ﴿٩٣﴾
93. Sema, Mola wangu! Ukinionyesha waliyoahidiwa.
رَبِّ فَلَا تَجْعَلْنِي فِي الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٩٤﴾
94. Mola wangu usinijaalie katika watu madhalimu.
وَإِنَّا عَلَىٰ أَن نُّرِيَكَ مَا نَعِدُهُمْ لَقَادِرُونَ ﴿٩٥﴾
95. Na hakika sisi ni wenye kuweza kukuonyesha tuliyowaahidi
ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ السَّيِّئَةَ نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَصِفُونَ ﴿٩٦﴾
96. Kinga maovu kwa yaliyo mema zaidi. Sisi tunayajua wanayoyasifia.
وَقُل رَّبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ ﴿٩٧﴾
97. Na sema, Mola wangu! Najikinga kwako na wasiwasi wa shetani.
وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَن يَحْضُرُونِ ﴿٩٨﴾
98. Na ninajilinda kwako wasinikaribie.
حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ ﴿٩٩﴾
99. Mpaka yanapomfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu nirudishe.
لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ كَلَّا إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ ﴿١٠٠﴾
100. Ili nitende mema badala ya yale niliyoyaacha. Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu. Na nyuma yao kuna kizuizi mpaka siku watakapofufuliwa.
Aya 91 -100
Mwenyezi Mungu hakujifanyia mwana.
Hana mshirika wala mtoto. Lau angelikuwa na mtoto angelifanana naye. Na Mwenyezi Mungu (s.w.t) hana mfano na chochote.
Wala hanaye mungu mwingine. Ingelikuwa hivyo basi kila Mungu angelichukua alivyoviumba.
Lau ulimwengu ungelikuwa na waumbaji wawili, basi kila mmoja angelihusika na sehemu fulani ya ulimwengu; angelikuwa na mipaka yake nidhamu yake na mambo yake yasiyoafikiana na sehemu nyingine. Kwa kuwa nidhamu ya ulimwengu ni moja na mambo yake ni mamoja, basi muumba wake ni mmoja.
Na baadhi yao wangeliwashinda wengine.
Vile vile lau waumbaji wangelikuwa wengi, hilo lingesababisha kila mmoja kuwa mshindi juu ya mwingine kwa wakati mmoja. Kwa sababu sifa ya Mungu ni kuwa juu ya kila kitu. Yaani kama waungu wangelikuwa wengi basi kungelikuwa na mashindano; kama inavyokuwa kwa watawala. Na huo ndio ufisadi hasa.
Ametakata Mwenyezi Mungu na wanavyomsifu kuwa ana mwana au washirika. Umetangulia ufafanuzi wake katika Juz. 5 (4:50).
Mjuzi wa ghaibu na dhahiri.
Makusudio ya ghaibu ni yale ambayo viumbe hawawezi kuyajua. Na ya dhahiri ni yale ambayo viumbe wanaweza kuyajua. Kwa hakika ilivyo hasa ni kuwa ugawanyo huu unafaa kwa viumbe, sio kwa muumba. Kwa sababu kwake yeye vitu vyote ni sawa kiujuzi na kiuwezo.
Ametukuka juu ya hayo wanayomshirikisha nayo, kutokana na kutowatambua hao washirika. Ikiwa kitu hakitambui muumba maana yake ni kuwa hakiko.
Sema, Mola wangu! Ukinionyesha waliyoahidiwa, Mola wangu usinijaalie katika watu madhalimu.
Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake aombe dua ya kuokoka na ghadhabu na adhabu yake itakayowapata wenye hatia na madhalimu, pamoja na kujua kuwa Mtume(s.a.w. w ) yuko katika amani na salama. Lakini lengo la dua hii ni kuhadharisha watu wa shirk na madhalimu. Mara nyingi waongozaji wanatumia mfumo huu kuonyesha kupingana na yule aliyeghadhibikiwa na Mwenyezi Mungu.
Na hakika sisi ni wenye kuweza kukuonyesha tuliyowaahidi.
Mtume(s.a.w. w ) aliwaonya makuraishi kwa adhabu kama watamkadhibisha na kupinga utume wake, wakacheka na wakafanya masikhara; ndio Mwenyezi Mungu akamwambia Mtume wake Mtukufu kuwa usihuzunike! Sisi tunaweza kukuonyesha maangamizi, lakini tunaahirisha kwa hekima na maslahi yako na ya Uislamu.
Pengine hekima hiyo ni kuwa Mwenyezi Mungu anajua kuwa baadhi yao au baadhi ya watoto wao watamwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, wawe ni nguvu ya kuusaidia Uislamu na waislamu; kama ilivyotokea hivyo hasa.
Kinga maovu kwa yaliyo mema zaidi. Sisi tunayajua wanyoyasifia.
Ni nini kukinga kwa kutenda yaliyo mema zaidi? Je, ni kuvumilia maudhi na kumnyamazia anayekuudhi, kama wasemavyo wafasiri wengi?
Kinga inatofautiana kulingana na hali. Inaweza ikawa kutumia nguvu dhidi ya adui ndio kukinga kwa yaliyo mema zaidi. Hapo ni ikiwa aliyechokozwa ana uwezo na ikawa kumnyamazia mchokozi kunamtia mori wa kufanya uovu na uadui. Imam Ali(a.s) anasema: "Kutekeleza ahadi kwa wasio na ahadi ni kuvunja ahadi na kuvunja ahadi kwa wasio na ahadi ni kutekeleza ahadi"
Na inawezekana kuwa kumnyamzia mchokozi ni kinga ya kufanya mema zaidi, ikiwa huko kumnyamazia kutamfanya ajute na atubie au ikiwa aliyechokozwa hana nguvu za kutosha kumzuia mchokozi. Kwani hapo itakuwa ni kujiingiza katika mambo ambayo hayana mwisho mzuri.
Kwa ajili hii Mtume alivumilia maudhi akiwa Makka kwa kutokuwa na uwezo, lakini aliwatia adabu wachokozi baada ya kuhamia Madina na kupata nguvu.
Na sema, Mola wangu! Najikinga kwako na wasiwasi wa shetani, na ninajilinda kwako wasinikaribie.
Ni wazi kuwa shetani hana uwezo wowote kwa Mitume, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "Hakika waja wangu huna mamlaka nao isipokuwa wale wapotofu waliokufuata." Juz. 14 (15:42).
Unaweza kuuliza : Ikiwa shetani hana uwezo wowote kwa Mitume, basi kwa nini Mwenyezi Mungu amemwamrisha Mtume wake kujikinga nao?
Jibu : Kujikinga na kitu hakumaanishi kutowezekana kutokea kwake. Kwani maasumu wanajikinga na ghadhabu na adhabu ya Mwenyezi Mungu zaidi kuliko wengine, pamoja na kuwa wao wako katika amani na salama. Kwa maneno mengine ni kuwa kumkimbilia Mwenyezi Mungu ni dua, na dua inafaa kuwa ni kinga ya uovu na balaa hata kama haiko. Huko nyuma tumeashiria kwamba wacha Mungu mara nyingi wanaonyesha uovu katika dua zao kwa unyenyekevu.
Mpaka yanapomfikia mmoja wao mauti, husema: Mola wangu nirud- ishe ili nitende mema badala ya yale niliyoyaacha.
Wakati alipokuwa na fursa ya kufanya matendo mema aliipoteza na kuipuuza. Baada ya kumfikia mauti ndio anataka kurudia uhai ili afanye amali njema. Hivi ndivyo alivyo kila mzembe, anaipoteza nafasi anapokuwa nayo na inapomtoka huanza kuijutia.
Wapi! Hii ni kauli aisemayo yeye tu.
Hakuna kurejea kabisa! Hata kama mzembe huyu atakubaliwa kurudi mara ya pili atarudia uasi wake. Ama kusema kwake 'ili nitende mema' ni maneno matupu tu yasiyokuwa na maana wala utekelezaji. Hilo amelifafanua Mwenyezi Mungu aliposema: "Na kama wangelirudishwa bila shaka wangeliyarudia yale waliyokatazwa na hakika wao ni waongo" Juz.7 (6:28).
Na nyuma yao kuna kizuizi mpaka siku watakapofufuliwa.
Nyuma yao ni kinaya cha kila upande. Maana ni kuwa wao wametaka kurejea duniani na baina yao na maisha ya dunia kuna kizuizi kitaka-chobaki mpaka siku ya kiyama. Hapo ndio kitaondoka kizuizi, lakini itakuwa ni wakati wa viumbe kusimama mbele ya Mola wao kwa ajili ya hisabu na malipo.
5
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
فَإِذَا نُفِخَ فِي الصُّورِ فَلَا أَنسَابَ بَيْنَهُمْ يَوْمَئِذٍ وَلَا يَتَسَاءَلُونَ ﴿١٠١﴾
101. Basi itakapopuziwa para-panda, hapo hakutakuwa na nasaba baina yao siku hiyo, wala hawataulizana.
فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿١٠٢﴾
102. Basi ambao mizani zao zitakua nzito hao ndio wenye kufanikiwa.
وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ فِي جَهَنَّمَ خَالِدُونَ ﴿١٠٣﴾
103. Na wale ambao mizani zao zitakuwa nyepesi, hao ndio waliozitia hasara nafsi zao na watadumu katika Jahannam.
تَلْفَحُ وُجُوهَهُمُ النَّارُ وَهُمْ فِيهَا كَالِحُونَ ﴿١٠٤﴾
104. Moto utababua nyuso zao nao humo watakuwa wenye kukunjana.
أَلَمْ تَكُنْ آيَاتِي تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَكُنتُم بِهَا تُكَذِّبُونَ ﴿١٠٥﴾
105. Je, hazikuwa Aya zangu mkisomewa na nyinyi mkizikadhibisha?
قَالُوا رَبَّنَا غَلَبَتْ عَلَيْنَا شِقْوَتُنَا وَكُنَّا قَوْمًا ضَالِّينَ ﴿١٠٦﴾
106. Watasema: Mola wetu! Tulizidiwa na uovu wetu na tukawa watu tuliopotea.
رَبَّنَا أَخْرِجْنَا مِنْهَا فَإِنْ عُدْنَا فَإِنَّا ظَالِمُونَ ﴿١٠٧﴾
107. Mola wetu! Tutoe humu motoni. Na tutakaporudia, basi kweli sisi ni wenye kudhulumu.
قَالَ اخْسَئُوا فِيهَا وَلَا تُكَلِّمُونِ ﴿١٠٨﴾
108. Atasema: Tokomeeni humo, wala msinisemeshe.
فَاتَّخَذْتُمُوهُمْ سِخْرِيًّا حَتَّىٰ أَنسَوْكُمْ ذِكْرِي وَكُنتُم مِّنْهُمْ تَضْحَكُونَ ﴿١١٠﴾
110. Hakika lilikuwapo kundi katika waja wangu likisema: Mola wetu tusamehe na uturehemu, na wewe ndiwe mbora wa wanaorehemu.
إِنِّي جَزَيْتُهُمُ الْيَوْمَ بِمَا صَبَرُوا أَنَّهُمْ هُمُ الْفَائِزُونَ ﴿١١١﴾
111. Lakini ninyi mliwafanyia maskhara mpaka wakawasahahulisha kunitaja na mlikuwa mkiwacheka.
قَالَ كَمْ لَبِثْتُمْ فِي الْأَرْضِ عَدَدَ سِنِينَ ﴿١١٢﴾
112. Hakika mimi leo nimewalipa kwa vile walivyosubiri. Hakika hao ndio wenye kufuzu.
Aya 101 – 111
Basi itakapopuziwa parapanda, hapo hakutakuwa na nasaba baina yao siku hiyo, wala hawataulizana.
Kupuziwa parapanda ni kinaya cha kufufuliwa walio katika makaburi. Kutokuweko nasabu maana yake ni kutokuwako kuhurumiana baina ya jamaa na ndugu: "Siku mtakapoiona, kila mwenye kunyonyesha atamsahau amnyonyeshae." Juz. 17 (22: 2).
Siku hiyo hakutakuwa na kitu chochote isipokuwa imani na matendo mema: "Na kila mmoja kati yao atamfikia siku ya Kiyama peke yake. Hakika wale ambao wameamini na wakatenda mema Mwingi wa rehema atawajaalia mapenzi." Juz.16 (19:95-96).
Kuna Hadith isemayo kuwa Mwenyezi Mungu siku ya Kiyama atasema: "Leo ninaziondoa nasaba zenu na ninaweka nasaba yangu, wako wapi wenye takua?
Neno nasaba limetokana na kunasibiana. Neno udugu linafasiriwa kutoka neno la kiarabu Qaraba, lenye maana ya ukaribu. Hakuna ukaribu na Mungu isipokuwa kwa takua. Tazama Juz. 4 (3:199 - 200) kifungu cha 'Takua' Vile vile Juz. 11 (10:5-10) Kifungu 'Wako wapi wacha Mungu.'
Basi ambao mizani zao zitakua nzito hao ndio wenye kufanikiwa. Na wale ambao mizani zao zitakuwa nyepesi, hao ndio waliozitia hasara nafsi zao na watadumu katika Jahannam.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 8 (7:8) kifungu 'Mizani ya matendo.' Vilevile tumeizungumzia mara ya pili mizani hii katika Juz. 17 (21:47) kifungu 'mizani siku ya Kiyama.'
Moto utababua nyuso zao nao humo watakuwa wenye kukunjana.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameleta ibara ya uso kwa niaba ya mwili wote, kwa sababu uso ndio kiungo kizuri zaidi.
Imepokewa Hadith kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba yeye amesema: "Moto utababua nyuso zao, ni mbabuo utakaoenea hadi kwenye visigino vyao.
Je, hazikuwa Aya zangu mkisomewa na nyinyi mkizikadhibisha?
Huku ni kusutwa, kwa kukadhibisha kwao hoja za Mwenyezi Mungu na ubainifu wake.
Watasema: Mola wetu! Tulizidiwa na uovu wetu na tukawa watu tuliopotea.
Wanakiri dhambi zao baada ya kukatikiwa na kufungwa mlango wa toba! Umetangulia mfano wake katika Juz. Juz. 8 (7:5) na Juz. 17 (21:14).
Mola wetu! Tutoe humu motoni. Na tutakaporudia, basi kweli sisi ni wenye kudhulumu.
Watayasema haya baada ya kudhihiri hukumu na baada ya kuwathibitikia uhakika. Hapo mwanzo walikuwa wamezama katika uasi wao. Ndio maana Mwenyezi Mungu atasema:
Tokomeeni humo, wala msinisemeshe.
Ni maneno yakukemewa mbwa hayo ambayo yamedhihirisha ghadhabu za Mwenyezi Mungu.
Hakika lilikuwapo kundi katika waja wangu likisema: Mola wetu tusamehe na uturehemu, na wewe ndiwe mbora wa wanaorehemu. Lakini ninyi mliwafanyia maskhara mpaka wakawasahahulisha kunitaja na mlikuwa mkiwacheka.
Baada ya kuwasuta wakosefu na kuwakemea, hapa anawabainishia kwamba wao walikuwa wakiwafanyia kejeli na kuwacheka waja wema wa Mwenyezi Mungu ambao wanataka maghufira na rehema kutoka kwa Mola wao, kiasi ambacho kejeli ziliwafanya wamsahau Mungu.
Hakika mimi leo nimewalipa kwa vile walivyosubiri. Hakika hao ndio wenye kufuzu.
Waumini walivumilia maudhi ya wakosefu, ndio Mwenyezi Mungu akawaneemesha hawa na akawaadhibu hao.
فَالْيَوْمَ الَّذِينَ آمَنُوا مِنَ الْكُفَّارِ يَضْحَكُونَ ﴿٣٤﴾
"Basi hivi leo wale ambao wameamini wanawacheka makafiri." (83:34).
قَالَ كَمْ لَبِثْتُمْ فِي الْأَرْضِ عَدَدَ سِنِينَ ﴿١١٢﴾
112. Atasema: Mlikaa muda gani katika ardhi kwa idadi ya miaka?
قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ فَاسْأَلِ الْعَادِّينَ ﴿١١٣﴾
Watasema: Tumekaa siku moja au sehemu ya siku, basi waulize wanaoweka hisabu.
قَالَ إِن لَّبِثْتُمْ إِلَّا قَلِيلًا لَّوْ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿١١٤﴾
114. Atasema: Hamkukaa ila kidogo, laiti mngelikuwa mnajua.
أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لَا تُرْجَعُونَ ﴿١١٥﴾
115. Je, mnadhani kuwa tuliwaumba bure na kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?
فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْكَرِيمِ ﴿١١٦﴾
116. Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa haki. Hapana mungu ila Yeye, Mola wa Arshi tukufu.
وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ ﴿١١٧﴾
117. Na anayemuomba - pamoja na Mwenyezi Mungu - mungu mwingine, hana dalili ya hilo. Basi hakika hisabu yake iko kwa Mola wake. Kwa hakika makafiri hawafanikiwi.
وَقُل رَّبِّ اغْفِرْ وَارْحَمْ وَأَنتَ خَيْرُ الرَّاحِمِينَ ﴿١١٨﴾
118. Na sema: Mola wangu! Ghufiria na rehemu nawe ni Mbora wa wanaorehemu.
Aya 112 – 118
Atasema: Mlikaa muda gani katika ardhi kwa idadi ya miaka?
Atakayesema ni Mwenyezi Mungu au malaika atakayeamriwa kuuliza kesho, wanaombiwa ni wale waliokana ufufuo na muda wanoulizwa ni ule walioumaliza katika kufuru duniani. Lengo la swali hili ni kuwasuta na kuwatahayariza kutokana na kuipinga kwao siku hiyo na kuwakejeli wale waliokuwa wakiwaonya na vituko vya siku hiyo na adhabu yake.
Watasema: tumekaa siku moja au sehemu ya siku, basi waulize wanaoweka hisabu.
Wapi sisi na swali hili? Tuliyonayo yanatutosha. Ikiwa hakuna budi na kujibu basi tumekaa masaa tu. Wanaojua zaidi ni wale waliokuwa wakiudhibiti umri wetu na matendo yetu ambao hawaachi dogo wala kubwa, lakini sisi hatuna tujualo. Umetangulia mfano wake katika Juz. 16 (20:103).
Atasema: Hamkukaa ila kidogo, laiti mngelikuwa mnajua.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anawaambia mmekaa miaka, sio siku moja kama mnavyosema, lakini miaka ni michache kwa vile inaisha, na kila chenye kuisha ni kichache hata kama kitakaa muda mrefu. Laiti mngelijua hakika hii mlipokuwa duniani, mkaiamini siku hii na mkajiandaa nayo, basi leo mngelikuwa kwenye amani na salama, lakini mlikufuru, ikawathibitia adhabu.
Je, mnadhani kuwa tuliwaumba bure na kwamba nyinyi kwetu hamtarudishwa?
Kwa dhahiri maneno yanaelekezwa kwa wale wanaokana ufufuo, lakini kwa uhalisi yanaelekezwa kwa kila muasi na mfisadi; ni sawa awe amepinga ufufuo tangu mwanzo au aliuamini na asiufanyie kazi.
Bure ni kisicho na faida wala hekima ya kuwako kwake. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameepukana na kufanya mambo bure.
Lau mtu asingefufuliwa baada ya mauti, akajulikana mwema na muovu na kulipwa kila mmoja anavyostahiki, ingelikuwa kuumbwa mtu ni bure tu kusiko na faida yoyote.
Ametukuka Mwenyezi Mungu, Mfalme wa haki.
Mfalme ina maana ya muweza mwenye nguvu. Na haki inaondoa batili na bure. Ikiwa haki ndio iliomuumba mtu, itakuwaje kumbwa kwake kuwe bure? Au vipi imuwache bure bila ya taklifa yoyote na hisabu au bila ya swali na jawabu la wema au uovu alioufanya?
Hapana mungu ila Yeye, Mola wa Arshi tukufu.
Yeye ni mmoja katika ufalme wa ulimwengu bila ya mshirika katika kuumba kwake, kupangilia kwake, elimu yake na hekima yake. Basi kuumbwa mtu na asiyekuwa mtu burebure na ufisadi utatoka wapi?
Na anayemuomba - pamoja na Mwenyezi Mungu - mungu mwingine, hana dalili ya hilo.
Ataitoa wapi dalili ya ushirika na kila kitu kinafahamisha kuwa Mungu ni mmoja. Inatosha kuwa ni dalili ya umoja wake nidhamu ya ulimwengu huu ambayo haina kombo wala kuharibika, hakuna anayeweza kupinga hakika hii isipokuwa yule anayepinga misingi ya dhahiri na akakataa dalili zote. Mfano wa mtu huyu ni ni kupuuzwa wala hajadiliwi.
Basi hakika hisabu yake iko kwa Mola wake, naye ndiye atakayemlipa anayostahiki. Kwa hakika makafiri hawafanikiwi, kwa sababu wameiacha njia.
Kama alivyoifungua Mwenyezi Mungu (s.w.t) sura hii kwa kusema: "Hakika wamefaulu waumini." basi anaiishilizia hivyo hivyo.
Na sema: Mola wangu! Ghufiria na rehemu nawe ni Mbora wa wanaorehemu.
Yeye peke yake ndiye anayeombwa kutukunjulia kwa rehema zake na maghufira yake, wala asikate matarajio yetu ya kuneemeshwa na neema zake na ukarimu wake, kwa jaha ya Mtume na kizazi chake, rehema za Mwenyezi Mungu zimshukie yeye na kila mwenye kufuata mwenendo wake.
Mwisho Wa Sura Ya Ishirini Na Tatu
6
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
Sura Ya Ishirini Na Nne: Surat Nuru.
Razi amesema yote imeshuka Madina, na Tabrasi akasema bila ya kutofautiana. Ina Aya 64
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
سُورَةٌ أَنزَلْنَاهَا وَفَرَضْنَاهَا وَأَنزَلْنَا فِيهَا آيَاتٍ بَيِّنَاتٍ لَّعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿١﴾
1. Ni Sura tuliyoiteremsha na tukailazimisha na tukateremsha ndani yake Aya zilizo wazi, ili mkumbuke.
الزَّانِيَةُ وَالزَّانِي فَاجْلِدُوا كُلَّ وَاحِدٍ مِّنْهُمَا مِائَةَ جَلْدَةٍ وَلَا تَأْخُذْكُم بِهِمَا رَأْفَةٌ فِي دِينِ اللَّـهِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ وَلْيَشْهَدْ عَذَابَهُمَا طَائِفَةٌ مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ ﴿٢﴾
2. Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume mtandikeni kila mmoja wao viboko mia. Wala isiwashike huruma kwa ajili yao katika dini ya Mwenyezi Mungu, ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la waumini.
الزَّانِي لَا يَنكِحُ إِلَّا زَانِيَةً أَوْ مُشْرِكَةً وَالزَّانِيَةُ لَا يَنكِحُهَا إِلَّا زَانٍ أَوْ مُشْرِكٌ وَحُرِّمَ ذَٰلِكَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ ﴿٣﴾
3. Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina. Na mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mwanamume mshirikina. Na hayo yameharamishwa kwa waumini.
وَالَّذِينَ يَرْمُونَ الْمُحْصَنَاتِ ثُمَّ لَمْ يَأْتُوا بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاءَ فَاجْلِدُوهُمْ ثَمَانِينَ جَلْدَةً وَلَا تَقْبَلُوا لَهُمْ شَهَادَةً أَبَدًا وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿٤﴾
4. Na wale ambao wanawasingizia wanawake wanaoheshimika kisha wasilete mashahidi wane, basi watandikeni viboko thamanini. Na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio mafasiki.
إِلَّا الَّذِينَ تَابُوا مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ وَأَصْلَحُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٥﴾
5. Isipokuwa wale waliotubia baada ya hayo na wakatengenea; kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kughufiria, Mwenye kurehemu.
Aya 1 – 5
Ni Sura tuliyoiteremsha na tukailazimisha na tukateremsha ndani yake Aya zilizo wazi.
Mwenyezi Mungu alimtereshia Mtume wake mtukufu sura hii, ndani yake mkiwa na mafunzo aliyowajibisha kuyatumia kila mukallaf. Kwa sababu yanalenga kujenga jamii ya binadamu kwa ukamilifu kwa manufaa yake na maendeleo yake.
Mafunzo haya yako waziwazi yasiyohitajia ubishi wala mjadala katika malengo yake ya kumlinda mtu na ufisadi na upotevu. Kwa ajili hii au nyingine ndio ikaitwa Sura ya nuru. Na Qur'an yote ni uongofu na nuru.
Ili mkumbuke.
Mwenyezi Mungu ameteremsha Sura hii iliyo wazi wazi ili mjue na muitumie.
Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume mtandikeni kila mmoja wao viboko mia.
Maneno yanaelekezwa kwa yule atakayetekeleza adhabu (hadd), ambaye ni Imam au naibu wake mwenye ujuzi na mwadilifu.
Dhahiri ya Aya inaonyesha kuwa mwenye kuzini atapigwa vibogo awe muhsan au asiyekuwa muhsan. Kwa sababu herufi lam ya jinsiya ikiingia katika nomino pekee, inafahamisha kuenea aina zote.
Muhsan ni yule aliye baleghe na akili timamu akiwa na mke anayemtosheleza wakati wowote akitaka kumjamii. Ikiwa atajamii akiwa ni mtoto au mwenda wazimu, au akiwa ni mseja au ana mke, lakini yuko mbali naye au yuko karibu naye lakini ana maradhi ya kushindwa kumjamii, basi huyo siye muhsan. Vile vile mwanamke.
Imam Abu Jafar Swadiq(a.s ) aliulizwa kuhusu muhsan,akasema: ambaye ana tupu anayoweza kuiendea basi huyo ni muhsan.
Hivi ndivyo ilivyofahamisha dhahiri ya Aya, kwamba mzinifu muhasn na asiyekuwa muhsan watandikwe viboko mia. Lakini imethibiti kwa Hadith mutawatir na kongamano la madhehbu zote za kiislamu kwamba hukumu ya muhsan ni kupigwa mpaka kufa. Kwa hiyo hukumu ya viboko ni ya asiyekuwa muhsan.
Bali imekuja Hadith katika Sahih Bukhari kwamba Umar bin Al-khattwab alisema: "Hakika Mwenyezi Mungu alimtuma Muhammad kwa haki na akamteremshia Kitabu kwa haki, katika aliyoyateremsha ni Aya ya kurujumu (kupiga mawe) tukaisoma na tukaitia akilini na tukaihifadhi."
Rejea Bukhari Juz. 8 Uk. 209 chapa ya kiarabu ya mwaka 1377 A.H. Na Muslim Juz. 2, sehemu ya kwanza Uk. 107 chapa ya kiarabu ya mwaka 1348 A.H. Katika riwaya nyingine ya Bukhari Juz. 9 Uk. 86, Umar alisema: "Lau si kuwa watu watasema Umar amezidisha katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, ningeliiandika kwa mkono wangu Aya ya kurujumu."
Unaweza kuuliza : Mwenyezi Mungu mahali pengine anasema: " Juz. 4 (15:4). Katika Aya hii Mwenyezi Mungu amewajibisha mzinifu mwanamke afungiwe nyumbani wala asitoke mpaka afe au Mwenyezi Mungu amjaalie njia nyingine; kisha katika Aya tuliyo nayo Mwenyezi Mungu amewajibisha viboko. Sasa kuna njia gani ya kuchanganya Aya mbili hizi?
Jibu : Kwenye Juz.4 tulisema kwamba makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu au 'awajaalie njia' ni kwamba yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu hakujaalia adhabu ya kufungiwa nyumbani ni ya daima, bali ni kwa muda fulani, kisha alete hukumu ya kudumu. Ndivyo ilivyokuwa, ambapo iliondolewa adhabu ya kufungwa nyumbani na mahali pake pakachukuliwa na adhabu ya viboko au kurujumiwa.
Baadhi ya ulama wanasema kuwa hatuwezi kukimbilia kufutwa hukumu mpaka kupatikane nukuu ya kufuta hukumu hiyo au iwe haiwezekani kutumia nukuu mbili. Inavyochukuliwa ni kuwa sharia haikuleta nukuu ya kufuta hukumu hiyo na kwamba kuzichanganya nukuu mbili ni jambo lisilo na uzito, basi inafaa kuzitumia Aya zote mbili, kwamba mzinifu apigwe viboko na pia afungiwe nyumbani vile vile.
Sisi tunaweza kukubaliana na anayesema hivi ikiwa atatukinaisha kuwa makusudio ya 'njia' ni kitu kingine kisichokuwa hukumu ya kudumu ambayo ndiyo inayofahamika mwanzo. Ama kufasiri njia kwa maana ya ndoa, kama alivyosema mwenye fikra hii, hiyo iko mbali na ufahamu.
Wala isiwashike huruma kwa ajili yao katika dini ya Mwenyezi Mungu.
Msicheleweshe hukumu ya mzinifu mwanamume na mzinifu mwanamke, bali mutekeleze wala isiwazuie huruma. Kwa sababu hakuna kuhurumiana katika dini ya Mwenyezi Mungu. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) amesema:"Lau Fatima ataiba nitamkata mkono wake." Katika Nahjul-bal- agha, imeelezwa: "Mwenyezi Mungu amefaradhisha kisasi kuhifadhi damu na ameweka adhabu kuheshimu miko."
Ikiwa nyinyi mnamuamini Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho.
Huu ni msisitizo na himizo la kutekeleza adhabu na kwamba kuipuuza ni kudharau dini.
Na lishuhudie adhabu yao kundi la waumini.
Lengo la hilo ni kuenea tukio la adhabu kwa watu ili wapate kuonyeka na wakome. Imesemekana kuwa uchache wa kuitwa kundi ni watu watatu, wengine wakasema hata mmoja pia, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu: "Na ikiwa makundi mawili katika waumini.." (49:9).
Tumezungumzia kwa ufafanuzi kuhusu maelezo ya zina, masharti yake, mafungu yake, njia za kuithibitisha, adhabu na utekelezaji wake, toba yamzinifu na mengineyo waliyoyaeleza mafaqihi, katika kitabu Fiqhul-Imam Ja'farus swadiq(a.s) Juz. 6.
Mwanamume mzinifu hamwoi ila mwanamke mzinifu au mwanamke mshirikina. Na mwanamke mzinifu haolewi ila na mwanamume mzinifu au mwanamume mshirikina.
Imesemkana kuwa Aya hii ni miongoni mwa zenye kutatiza. Kwa sababu dhahiri yake inaonyesha kuwa mwanamume mzinifu haoi ila mzinifu au mshirikina. Vile vile mwanamke; pamoja na kwamba mzinifu huwa anamuoa mwanamke msafi aliye mtukufu.
Vile vile mwanamke mzinifu huwa anaolewa na mwanamume msafi aliye mtukufu. Sasa imekuwaje dhahiri ya Aya ikawa kinyume na hali halisi ya mambo?
Tuonavyo sisi Aya hii iko wazi kabisa. Kwa sababu yenyewe sio kuwa inaleta habari ya hali halisi ya mambo ilivyo, wala sio hukumu ya sharia ya kumlazimisha mzinifu aoe mzinifu mwenzake au mshirikina; kama walivyodai wafasiri wengi. Hapana sivyo kabisa! Kwa sababu Mwislamu haruhusiwi kumuoa mshirikina hata kama imethibiti zina juu yake. Vile vile mwanamke Mwislamu haruhusiwi kuolewa na mshirikina hata kama amezini.
Kwa hiyo hayo siyo makusudio yake; isipokuwa maana yake - bila ya kuangalia sababu iliyoshukia - ni kuwa zina ni jambo ovu na la fedheha kabisa, haifanyi ila malaya muovu.
Akitaka kuzini mtu basi atapata aliye mfano wake katika uovu. Malaya ni wa malaya. Kwa ufupi ni kuwa maana ya Aya yanafanana na kusema: Hakuna anayekubaliana na kosa lako ila mkosa kama wewe ambaye hana dini wala dhamiri. Sasa ni wapi na wapi haya na kuleta hukumu ya sharia?
Kauli yake Mwenyezi Mungu 'Au mshirkina' ni kuashiria kwamba zina iko kwenye daraja ya ushirikina. Mwenyezi Mugu amelinganisha sawa hukumu ya shirk, kuua na kuzini, pale aliposema: "Na wale wasiomwomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu ila kwa haki, wala hawazini na mwenye kufanya hivyo atapata madhambi' (25:68). Mtume(s.a.w .w ) aliulizwa kuhusu madhambi makubwa, akataja haya matatu.
Na hayo yameharamishwa kwa waumini. Hayo ni hayo ya Kuzini. Na wale ambao wanawasingizia wanawake wanaoheshimika, kisha wasilete mashahidi wane, basi watandikeni viboko thamanini.
Makusudio ya kusingizia hapa ni kusingizia zina. Neno la kiarabu, lililofasiriwa 'ambao,' lina dhamiri ya wanaume, lakini wanakusudiwa wote. Makusudio ya wanaoheshimika hapa ni wale wanawake wasafi wanaojichunga na zina; ni sawa wawe wameolewa au la. Ulama wamelinganisha hukumu ya mwanamume sawa na mwanamke. Kwa maneno mengine ni kuwa hukumu ya kutandika viboko inamuhusu mwanamume na mwanamke.
Msingiziaji mwanamume au mwanamke atatandikwa ikiwa hakuleta mashahidi wane walioshuhudia uingiaji wa tupu na utokaji wake, kama kinavyoingia kijiti cha wanja kwenye kichupa chake. Lengo la mkazo huu na mashahidi wengi ni kulinda familia zisitawanyike kwa kusingiziana.
Na msiwakubalie ushahidi wao tena. Na hao ndio mafasiki. Isipokuwa wale waliotubia baada ya hayo na wakatengenea; kwani hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kughufiria, Mwenye kurehemu.
Wanaelzewa wale wenye kuisingizia. Maana ni kuwa mwenye kumsingizia mwenye kujichunga na asithibishe kwa ushahidi, basi huyo ni fasiki, ushahidi wake haukubaliwi kabisa kwenye jambo lolote, ila baada ya kutubia na kufanya mambo mema. Akishatubia na akawa na sera nzuri, basi ushahidi wake utakubaliwa; ni sawa awe ametubia baada ya adhabu au kabla.
Abu Hanifa anasema: "Ushahidi wake haukubaliki kabisa hata akitubia, kwa sababu kukataliwa kwake ni miongoni mwa adhabu na kutiwa adabu..." Lakini huku ni kutatizika.
Kwa sababu kauli yake Mwnyezi Mungu, 'Hakika Mwenyezi Mungu ni mwenye kughufiria Mwenye kurehemu,' iliyokuja moja kwa moja inaashiria kukubaliwa kwake hata kama ametubia baada ya adhabu. Inayofafanua zaidi Aya hii ni kauli ya Mtume(s.a.w. w ) :"Mwenye kutubia dhambi ni kama asiye na dhambi."
وَالَّذِينَ يَرْمُونَ أَزْوَاجَهُمْ وَلَمْ يَكُن لَّهُمْ شُهَدَاءُ إِلَّا أَنفُسُهُمْ فَشَهَادَةُ أَحَدِهِمْ أَرْبَعُ شَهَادَاتٍ بِاللَّـهِ إِنَّهُ لَمِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٦﴾
6. Na wale wanaowasingizia wake zao na hawana mashahidi ila nafsi zao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudia mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba hakika yeye ni katika wasema kweli.
وَالْخَامِسَةُ أَنَّ لَعْنَتَ اللَّـهِ عَلَيْهِ إِن كَانَ مِنَ الْكَاذِبِينَ ﴿٧﴾
7. Na mara ya tano kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake ikiwa ni miongoni mwa waongo.
وَيَدْرَأُ عَنْهَا الْعَذَابَ أَن تَشْهَدَ أَرْبَعَ شَهَادَاتٍ بِاللَّـهِ إِنَّهُ لَمِنَ الْكَاذِبِينَ ﴿٨﴾
8. Na mke itamwondokea adhabu kwa kutoa shahada mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu, kwamba huyo mume ni miongoni mwa waongo.
وَالْخَامِسَةَ أَنَّ غَضَبَ اللَّـهِ عَلَيْهَا إِن كَانَ مِنَ الصَّادِقِينَ ﴿٩﴾
9. Na mara ya tano kwamba ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake, kama mume ni miongoni mwa wasemao kweli.
وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ وَأَنَّ اللَّـهَ تَوَّابٌ حَكِيمٌ ﴿١٠﴾
10. Na lau kuwa si fadhila za Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kutakabali toba, Mwenye hekima.
Aya 6-10
Katika vitabu vya Fiqh kuna mlango unaoitwa Lian, ambao chimbuko lake ni Aya hizi. Inafanana na kuapizana baina ya mume anayemtuhumu mkewe na zina bila ya kuwa na ushahidi wa madai yake, na mke kuikana tuhuma ya zina yeye mwenyewe. Lengo la kulaniana huku ni kuondoka adhabu ya kutuhumu au kumkana mtoto. Liani haiwi ila katika hali mbili:
Kwanza : Mtu kumtuhumu na zina mkewe wa kisharia aliyemuoa kwa ndoa ya daima. Ni lazima mke awe si kiziwi wala bubu, mume adai kushuhudia na asiwe na ubainifu wa kisharia juu ya hiyo zina, zikikosekana sharti hizi basi haijuzu kulaniana.
Pili : Kumkana mume mtoto wa kitanda chake, ikiwa mimba haikupungua miezi sita au kuzidi mwaka. Vinginevyo anaweza kumkana mtoto bila ya kulaniana.
Basi ikiwa mume atamtuhumu mkewe na zina au kumkana mtoto,anatakikana apate adhabu (had) ya kutukana, ila akileta ushahidi au kulaniana.
Sura ya kulaniana ni kusema mbele ya hakimu wa sharia: Ninashuduia kuwa mimi ni mkweli kwa ninayoyasema kuhusu mke wangu fulani. Atasema hivyo mara nne; kisha atasema mara ya tano baada ya kuonywa na hakimu wa sharia: Laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yangu ikiwa ni muongo.
Mke naye atashuhudia mara nne kwamba huyo mume ni muongo kwa aliyomtuhumu nayo. Mara ya tano atasema ghadhabu za Mwenyezi Mungu zimshukie ikiwa huyo mume ni mkweli.
Ni lazima wote wawili wawe wamekaa wakati wa kulaniana. Kukishatimia kulaniana kwa masharti yake, matokeo yatakuwa ni mambo yafuatayo:-
1. Ndoa itavunjika.
2. Uharamu wa milele baina ya mume na mke (hawawezi kurudiana tena).
3. Adhabu ya kutuhumu itaondoka kwa mume.
4. Mtoto hatakuwa wa mume. Hawatarithiana wala halazimiki kumtunza. Lakini atakuwa ni wa mama kisharia.
Tukijua kulaniana baina ya mume na mke, itakuwa tumejua makusudio ya Aya hizi. Kwa hiyo basi tutafupiliza kufasiri kwa kutaja matamko yanayoashiriwa na mfumo wa maneno.
Na wale wanaowasingizia wake zao kwa zina na hawana mashahidi ila nafsi zao kutokana na madai yao, basi ushahidi wa mmoja wao utakuwa kushuhudia mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu ya kwamba hakika yeye ni katika wasema kweli.
Atayasema hayo mbele ya hakimu wa sharia.
Na mara ya tano kwamba laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake ikiwa ni miongoni mwa waongo.
Yaani ikiwa ni muongo katika madai yake. Na mke itamwondokea adhabu kwa kutoa shahada mara nne kwa kiapo cha Mwenyezi Mungu, kwamba huyo mume ni miongoni mwa waongo. Mke naye atatoa ushahidi wake mbele ya hakimu wa sharia kama alivyofanya mume.
Na mara ya tano kwamba ghadhabu ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake, kama mume ni miongoni mwa wasemao kweli katika haya madai yake kwangu. Na lau kuwa si fadhila za Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake mngeliangamia. Na kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye kutakabali, toba Mwenye hekima.
Hii ni kuashria hekima ya sharia ya kuapizana, kwamba lengo ni kusitiri na kuondoa adhabu kwa mume na kutoa nafasi kwa mke kujitetea na tuhumu za mume.
7
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
إِنَّ الَّذِينَ جَاءُوا بِالْإِفْكِ عُصْبَةٌ مِّنكُمْ لَا تَحْسَبُوهُ شَرًّا لَّكُم بَلْ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُم مَّا اكْتَسَبَ مِنَ الْإِثْمِ وَالَّذِي تَوَلَّىٰ كِبْرَهُ مِنْهُمْ لَهُ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١١﴾
11. Hakika wale walioleta uzushi ni kundi miongoni mwenu. Msiufikirie ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu. Kila mmoja katika wao atapata aliyoyachuma katika madhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao atapata adhabu kubwa.
لَّوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْرًا وَقَالُوا هَـٰذَا إِفْكٌ مُّبِينٌ ﴿١٢﴾
12. Mbona mlipousikia, waumini wanaume na waumini wanawake hawakujidhania mema na kusema huu ni uzushi dhahiri?
لَّوْلَا جَاءُوا عَلَيْهِ بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاءَ فَإِذْ لَمْ يَأْتُوا بِالشُّهَدَاءِ فَأُولَـٰئِكَ عِندَ اللَّـهِ هُمُ الْكَاذِبُونَ ﴿١٣﴾
13. Mbona hawakuleta mashahidi wane. Na kwa kutoleta mashahidi, basi hao mbele ya Mwenyezi Mungu ni waongo
وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ لَمَسَّكُمْ فِي مَا أَفَضْتُمْ فِيهِ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١٤﴾
14. Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake katika dunia na akhera, bila shaka ingeliwapata adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyojiingiza.
إِذْ تَلَقَّوْنَهُ بِأَلْسِنَتِكُمْ وَتَقُولُونَ بِأَفْوَاهِكُم مَّا لَيْسَ لَكُم بِهِ عِلْمٌ وَتَحْسَبُونَهُ هَيِّنًا وَهُوَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمٌ ﴿١٥﴾
15. Mlipoyapokea kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyoyajua, na mkifikiri ni dogo kumbe kwa Mwenyezi Mungu ni kubwa.
وَلَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ قُلْتُم مَّا يَكُونُ لَنَا أَن نَّتَكَلَّمَ بِهَـٰذَا سُبْحَانَكَ هَـٰذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ ﴿١٦﴾
16. Na mbona mliposikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya; utakatifu ni wako! Huu ni uzushi mkubwa.
يَعِظُكُمُ اللَّـهُ أَن تَعُودُوا لِمِثْلِهِ أَبَدًا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٧﴾
17. Mwenyezi Mungu anawaonya msirudie kufanya kama haya kabisa ikiwa nyinyi ni waumini.
وَيُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿١٨﴾
18. Na Mwenyezi Mungu anawabainishia Aya na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿١٩﴾
19. Hakika wale ambao wanapenda kueneza uchafu kwa waliaomini watapata adhabu chungu duniani na akhera. Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.
وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ وَأَنَّ اللَّـهَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٠﴾
20. Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake na kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni Mpole, Mwenye kurehemu.
Aya 11 – 20
Wameafikiana wafasri na wapokezi wa makundi yote na madhehebu ya kiislamu, isipokuwa waliotoka nje ya kundi, kwamba Aya hizi zilishuka kumuondolea tuhuma ya zina Bibi Aisha.
Sababu ya tuhuma ni kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) alikuwa akitaka kusafiri, hupiga kura baina ya wake zake. Yule atakayepa- ta kura huongozana naye.
Mnamo mwaka wa tano wa Hijra, Mtume alipigana vita na Bani Mustalaq. Kura ikamwangukia Aisha, akaongozana naye. Mwenyezi Mungu akampa ushindi Mtume wake na akamuoa binti wa kiongozi wao Harith, baada ya kusilimu huyo binti. Jina lake lilikuwa Barra, Mtume akamgeuza jina na kumwita Juwayriya. Baba yake alisilimu pamoja na watu wengi wa kabila lake.
Mtume akarudi Madina pamoja na msafara wake wa ushindi, akisafiri usiku na mchana. Mpaka ilipofikia usiku wa pili akashuka na jeshi lake kupumzika kidogo.
Alipotangaza kuondoka msafara, Aisha alikwenda haja, aliporudi akapoteza mkufu wake. Akarudi kuutafuta. Aliporudi akakuta msafara wa jeshi umekwishaondoka. Akangoja palepale kuwa pengine wakimkosa kwenye msafara wanaweza kumrudia.
Swafwan bin Mua'ttwal alikuwa nyuma ya msafara, akampitia Aisha na akamjua, kwa sababu ilikuwa ni kabla ya kuteremshwa hukumu ya hijabu. Akampeleka mnyama wake naye akajitenga kidogo, mpaka alipopanda. Akamfikisha kwenye msafara au Madina.
Hapo wazushi wakapata nafasi, wakaanza kueneza uongo na kumtuhumu Aisha kufanya hiyana na Safwan. Wa kwanza aliyeuachia ulimi wake na uongo huu ni raisi wa wanfiki, Abdallah bin Ubayya, akaudakia Hassan bin Thabit, na Misatah na wanafiki wengineo. Ndipo Mwenyezi Mungu akatermsha Aya hizi kumuondolea tuhuma Aisha.
Kwa mansaba huu tunaashiria mambo mawili:
Kwanza : kwamba Shia Imamiya wanaitakidi na kuamini kwamba wake wa mitume wote ni wasafi walio twahara na kwamba Mtume yoyote haweki maji yake ila kwenye tumbo lililo twahara.
Na mke wa Mtume anaweza kukufuru, lakini hawezi kuwa mzinifu. Kwa sababu mtume ni mtukufu zaidi kwa Mola wake, hawezi kumjaalia chini yake muasharati.
Anasema mwanachuoni, Imam Tabrasi (mshia) katika Tafsiri yake Majmau'labayan: "Hakika wake wa mitume ni lazima wawe safi na hali hii, kwa sababu ni aibu.
Mwenyezi Mungu amewatakasa Mitume wake na hilo kwa kuwapa heshima na kawaadhimisha na kuwaepusha na jambo ambalo litasababisha kukataliwa kauli zao na miito yao."
Ibn Abbas anasema: "Hakuzini mke wa Mtume kabisa. Khiyana ya mke wa Nuh ilikuwa ni kumfanya Nabii kuwa mwendawazimu na khiyana ya mke wa Lut ilikuwa ni kuwajulisha wale mahabithi kuhusu wageni wake."
Jambo la pili: Kuna baadhi wamesema kwamba Mtume(s.a.w. w) alimtaka shauri Imam Ali(a.s ) miongoni mwa aliowataka shauri, akamshauri ampe talaka, na kwamba hilo eti ndio lilomfanya Aisha kupigana na Imam katika vita vya Jamal (ngamia). Waliosema kauli hii wameitegemeza kwenye riwaya ambayo hatuijui usahihi wake; mbali ya kuwa Mtume hahitajii ushauri wa yeyote katika maamuzi yake, kwa kuzingatia kuwa yeye ni mjuzi na mbora zaidi ya viumbe wengine wote.
Vipi Mtume anaweza kumtilia shaka mkewe na hali anajua kwamba yeye ni mtukufu zaidi kwa Mwenyezi Mungu kuliko kujaaliwa chini yake kahaba? Lau Mtume angelimtilia shaka Aisha angelikuwa ndiye aliyekusudiwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Mbona mlipousikia, wau- mini wanaume na waumini wanawake hawakujidhania mema na kusema huu ni uzushi dhahiri?"
Hapana! Muhammad(s.a.w. w ) hakumtilia shaka Aisha. Na mwenye kumnasibishia shaka hii atakuwa ameleta uzushi mkubwa.
Zaidi ya hayo, kuna riwaya nyingine inayosema kwamba Imam Ali(a.s ) alimwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu:"Hakika viatu vyako havina najisi je mkeo."
Na kwamba Mtume alifurahi kwa hilo. Ismail Haqiy katika Ruuhl-bayan anasema: "Mtume alimtaka ushauri Ali kuhusu Aisha, akasema kuwa ni msafi na nimeuchukua usafi huo kutokana na tukio lililotutokea siku moja tulipokuwa tunaswali nyuma yako ukiwa na viatu vyako; kisha ukavua kiatu kimoja. Tukasema tuifanye ni sunna hiyo? Ukasema: Hapana Jibril ameniambia kuwa kiatu chako hicho kina najisi.
Basi ikiwa kiatu tu hakiwezi kuwa na najisi, vipi ahli yako? Basi Mtume akafurahi kwa hilo.
Sisi hatutaji riwaya hizi kwa kuwa tunaziamini, isipokuwa ni kuonyesha riwaya zinazopinga ushauri wa talaka.
Hakika wale walioleta uzushi ni kundi miongoni mwenu. Msiufikirie ni shari kwenu, bali hiyo ni kheri kwenu.
Wale ambao walimzulia khiyana Aisha ni kundi lililodhihirisha kuwa ni waongo na wazushi; kwamba wao wako kwenye mila ya kiislamu na kumbe hawamo kabisa.
Hilo lilimkera Nabii na maswahaba, ndio Mwenyezi Mungu Mtukufu akawambia msidhanie ni shari na madhara, hapana! Bali kuna manufaa mengi katika hili; ikiwemo kujulikana mumin aliye mwema na yule mnafiki habith ambaye anapenda kueneza uovu kwa wasiokuwa na hatia. Manufaa mengine ni majaribio ambayo yatawazidisha uongofu walioongoka na kuwazidishia wanafiki hasara.
Kila mmoja katika wao atapata aliyoyachuma katika madhambi.
Katika wao hapa ni wale waliozusha uongo. Maana ni kuwa kila mmoja katika hawa ana adhabu kwa kiasi alivyeeneza na kutangaza uongo na uzushi. Kwa kuwa tuhuma ya kutusi iliwathibitikia Hassan Bin Thabit, Mistah na mwanamke mmoja wa kikuraishi, Mtume aliwapa adhabu (hadd) ya viboko thamanini. Lakini Abdallah bin Ubayya alitafuta mbinu za kuhepa na kuponyoka adhabu kutokana na hadhari yake na kuwatosa wenzake. Yeye ndiye aliyekusudiwa katika kauli yake Mwenyezi Mungu:
Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao atapata adhabu kubwa duniani kwa kumfedhesha kwake na kumdhihirisha vitim- bi vyake kwa watu, kiasi ambacho mmoja wa vigogo wa kabila la Khazraj alikitafuta kichwa. Vilevile kigogo wa kabila la Ausi; kama ambavyo vijana wengi wa kiansari akiwemo mwanawe walimtafuta kumuua. Ama adhabu yake katika akhera ni chungu na kubwa.
Mbona mlipousikia, waumini wanaume na waumini wanawake hawakujidhania mema na kusema huu ni uzushi dhahiri?
Mlipousikia, ni huo uzushi. Makusudio ya kujidhania ni kuwadhania wenzao wengine, kwa sababu binadamu wamejengwa kwa mshikamano mmoja; hasa waumini. Kwani imani ni ahadi na kulindana. Kuna Hadith isemayo: "Waumini ni kama nafsi moja" na Qur'an nayo inasema: "Hakika waumini wote ni ndugu" (49:10).
Matumizi haya kwenye Qur'an ni mengi; kama vile: "Wala msijiue." Juz.5 (4:29) pia katika Aya 61 ya Sura hii tuliyo nayo: 'Mjitolee salaam.'
Aya inaashiria kwamba mumin wa kweli, haijuzu kwake kunyamaza kama akisikia maneno ya uzushi na ya ubatilifu. Ama kauli mashuhuri inayosema: 'Ikiwa maneno ni fedha basi kunyamaza ni dhahabu' inakusudia kusema bila ya elimu na maneno ya upuzi na ubatilifu, kama uongo, kusengenya na fitina.
Unaweza kuuliza : Kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:"Na kusema huu ni uzushi." inafahamisha kuwa ni wajibu kuukadhibisha na kuukana uovu na zina kwa kiasi cha kuisikia tu, bila ya kuthibitisha; jambo ambalo haliafikiani na misingi ya kiakili na kiislamu inayosema: 'Mwenye kukana kwa ulimi ni sawa na mwenye kuthibitisha, kila mmoja wao anahitaji dalili mkataa?'
Jibu : Ndio ni kweli; hakuna shaka kabisa na msingi huu na kwamba unaenea katika kila kitu, lakini makusudio ya kukana hapa sio kuikana hiyo zina yenyewe na kuijua kwake Mwenyezi Mungu, hapana! Bali makusudio hapa ni kukana hukumu yake na matokeo yake, kama kutekeleza adhabu. Kwa hiyo inatakikana izingatiwe kama vile haikutendeka mpaka ithibitike kisharia.
Ndio maana ikawa mwenye kutuhumu anatandikwa viboko thamanini, ikiwa hakuthibitisha. Kwa maneno mengine ni kuwa kukosekana dalili ya kisharia kwenye zina ni dalili ya kukosekana hukumu na matokeo. Ushahidi mkubwa katika hilo ni kauli yake Mwenyezi Mungu:
Mbona hawakuleta mashahidi wane. Na kwa kutoleta mashahidi basi hao mbele ya Mwenyezi Mungu ni waongo; yaani ni wongo katika hukumu ya Mwenyezi Mungu duniani. Ama elimu yake Mwenyezi Mungu Mtukufu ambayo inafungamana na uhakika wa mambo itabakia akhera.
Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake katika dunia na akhera, bila shaka ingeliwapata adhabu kubwa kwa sababu ya yale mliyojiingiza.
Mliyojiingiza ni yale ya uzushi. Rehema ya Mwenyezi Mungu kwa muasi duniani ni kule kumsitiri na kumpa muda ili aweze kutubia. Na katika akhera ni kusamehewa akitubia na kurejea.
Kisha akabainisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) sababu ya kustahiki kwake adhabu kubwa duniani na akhera, kwa kusema:
Mlipoyapokea kwa ndimi zenu na mkasema kwa vinywa vyenu msiyoyajua, na mkifikiri ni dogo kumbe kwa Mwenyezi Mungu ni kubwa.
Mnayazungusha maneno ya uzushi kwenye ndimi zenu na wengine wanayachukua bila ya dalili, huku mkidhani kuwa jambo hilo ni dogo, lakini mbele ya Mwenyezi Mungu ni kubwa na lenye dhambi.
Miongoni mwa kauli za Imam Ali(a.s ) ni"Ulimi ni mnyma mkali ukiachiwa unauma"
Na mbona mliposikia msiseme: Haitufalii kuzungumza haya kabisa, sikwambii kuyatilia shaka tena. Bali inatakikana kuuepusha ulimi na kuizungumza zina hata kama itathibitika kisharia isipokuwa katika hali ya kukemea na kukataza. Wale wanojiburudisha kwa kuizungumzia zina na uovu ni wale wapumbavu na waovu zaidi katika watu.
Utakatifu ni wako! Huu ni uzushi mkubwa.
Ni kitu gani kikubwa zaidi kuliko kuwazulia wasiokuwa na hatia? Mumin wa kweli ni yule anayemtetea ndugu yake wala hamtuhumu kwa uovu na shari.
Mwenyezi Mungu anawaonya msirudie kufanya kama haya kabisa ikiwa nyinyi ni waumini.
Anawaonya na anawakataza. Kama haya ni haya ya uzushi. Haijuzu kufanya upuzi na kusikiliza. Kuufunga utiifu na imani ni ishara kuwa mumin akikatazwa na Mwenyezi Mungu kitu au akiamrishwa basi anafuata na kutii
Na Mwenyezi Mungu anawabainishia Aya na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
Anawafafanulia halali na haramu katika Kitabu chake na katika ulimi wa Mtume wake, anamjua kila mmoja aliye muasi na aliye mtiifu na kuamil- iana naye kwa ujuzi wake, uadilifu wake na hekima yake.
Hakika wale ambao wanapenda kueneza uchafu kwa waliaomini watapata adhabu chungu duniani na akhera.
Uchafu ni mazugumzo machafu. Hakuna tofauti baina ya mwenye kutenda uchafu na mwenye kuutangaza. Kila mmoja ataadhibiwa ikithibitika kuwa amefanya au ametuhumu na akhera atakuwa na adhabu ya kuungua. Kila mwenye kasoro anapenda awe na wanaofanana naye. Kwa sababu mwenye kasoro huwa hawezi kuona ukamilifu kwa mwenzake.
Na Mwenyezi Mungu anajua na nyinyi hamjui.
Mumin hasemi wala hafanyi bila ya kujua, bali anayarudisha asiyoyajua kwa anayejua.
Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, ingeliwapata adhabu kubwa.
Na kwa kuwa Mwenyezi Mungu ni Mpole Mwenye kurehemu waja wake akiwatakia kheri hata kama wanajitakia shari.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَتَّبِعُوا خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ وَمَن يَتَّبِعْ خُطُوَاتِ الشَّيْطَانِ فَإِنَّهُ يَأْمُرُ بِالْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ مَا زَكَىٰ مِنكُم مِّنْ أَحَدٍ أَبَدًا وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ يُزَكِّي مَن يَشَاءُ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٢١﴾
21. Enyi ambao mmeamini! Msifuate nyao za shetani. Na atakayefuata nyayo za shetani, basi yeye huamrisha machafu na maovu. Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, asingelitakasika miongoni mwenu yoyote kabisa. Lakini humtakasa amtakaye na Mwenyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.
وَلَا يَأْتَلِ أُولُو الْفَضْلِ مِنكُمْ وَالسَّعَةِ أَن يُؤْتُوا أُولِي الْقُرْبَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَلْيَعْفُوا وَلْيَصْفَحُوا أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَكُمْ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٢﴾
22. Na wale katika nyinyi wenye wasaa wasiape kutowapa walio jamaa na maskini na waliohama katika njia ya Mwenyezi Mungu. Na wasamehe na wachilie mbali. Je, nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu awasamehe? Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
إِنَّ الَّذِينَ يَرْمُونَ الْمُحْصَنَاتِ الْغَافِلَاتِ الْمُؤْمِنَاتِ لُعِنُوا فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ وَلَهُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿٢٣﴾
23. Hakika wanaowasingizia wanawake wanaoheshimika, walioghafilika walio waumini, wamelaaniwa duniani na akhera na watapata adhabu kubwa.
يَوْمَ تَشْهَدُ عَلَيْهِمْ أَلْسِنَتُهُمْ وَأَيْدِيهِمْ وَأَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿٢٤﴾
24. Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao kwa waliyokuwa wakiyatenda.
يَوْمَئِذٍ يُوَفِّيهِمُ اللَّـهُ دِينَهُمُ الْحَقَّ وَيَعْلَمُونَ أَنَّ اللَّـهَ هُوَ الْحَقُّ الْمُبِينُ ﴿٢٥﴾
25. Siku hiyo atawatekelezea sawa malipo yao ya haki na watajua kwamba hakika Mwenyezi Mungu ndiye haki iliyo wazi.
Aya 21 -25
E nyi am b a o mmeamini! Msifuate nyao za shetani kwa kutangaza uovu kwa wale ambao wameamini, wala kwa jambo linalotia wasiwasi na kuwavutia kwake.
Na atakayefuata nyayo za shetani, basi yeye huamrisha machafu na maovu.
Anayewezwa na shetani nafsini mwake, humuongoza kwenye mabaya na machafu.
Na lau si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake, asingelitakasika miongoni mwenu yoyote kabisa.
Mwenyezi Mungu ametufahamisha njia ya kheri na njia ya shari, akatukataza hili na akatuamrisha lile, akatupa uwezo wa kutenda na kuacha na akaufungua mlango wa toba kwa mwenye kuasi. Hii ndiyo fadhila yake. Ama utakaso wake huwa hampi isipokuwa mwenye kusikia na akatii.
Lakini humtakasa amtakaye na Mwenyezi Mungu ni Msikizi ,Mjuzi na mwenye hekima pia. Hawatakasi isipokuwa wenye amali na nyoyo safi.
Na wale katika nyinyi wenye wasaa wasiape kutowapa walio jamaa na maskini na waliohama katika njia ya Mwenyezi Mungu.
Imepokewa kuwa Aya hii ilishuka kwa ajili ya Abu Bakri alipoapa kutomsaidia Mistah Bin Athatha baada ya kushiriki pamoja na aliyeshiriki kueneza uvumi wa uovu kumhusu Ummul-mu'min (Mama wa waumin). Sifa hizi tatu zote anazo Mistah: Ni mtoto wa mama mdogo wa Abu bakr, ni maskini asiyekuwa na mali naye ni katika wahajiri na waliopigana Badri.
Na wasamehe na waachilie mbali. Je, nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu awasamehe? Na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufira Mwenye kurehemu.
Hii ni ahadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t), kumsamehe na kumre- hemu atakayemsamehe aliyemfanyia ubaya. Imam Zaynul'abidin(a.s ) alikuwa akimsamehe anayemfanyia ubaya, kisha anamwambia Mwenyezi Mungu: Ewe Mola wetu! Hakika wewe umeamrisha tumsamehe atakayetudhulumu, nasi tumesamehe, kama ulivyoamrisha, basi tusamehe; kwani hakika wewe ndiwe mbora zaidi wa hilo kuliko sisi.
Hakika wanaowasingizia wanawake wanaoheshimika, walioghafilika walio waumini, wamelaaniwa duniani na akhera na watapata adhabu kubwa.
Katika Aya ya 4 ya Sura hii Mwenyezi Mungu (s.w.t) alibainisha kwamba mwenye kumtuhumu mwanamke kwa zina na asilete mashahidi wane basi adhabu yake duniani ni kuchapwa viboko thamanini vyovyote vile atakavyokuwa na hakutaja adhabu yake akhera.
Katika Aya hii tuliyo nayo, anabainisha malipo yake huko akhera, ambayo ni adhabu kubwa, ikiwa aliyetuhumiwa ni ni msafi mwenye kujiheshimu na hayo aliyotuhumiwa. Ndio makusudio ya wenye kughafilika; yaani wenye kughafilika na zina, hawaifanyi wala hawaifikirii.
Siku ambayo zitawashuhudia ndimi zao na mikono yao na miguu yao kwa waliyokuwa wakiyatenda.
Duniani inahitajika ushahidi ikiwa mwanamke anadai kuwa ametuhumiwa na mdaiwa akikataa. Akishindwa kuthibitisha basi madai yake yatakataliwa. Lakini huko akhera hakuhitajiki ushahidi, kwa sababu mtendaji hana njia ya kukana. Lau tukikadiria kuwa atakana au kujaribu kukana, basi viungo vyake vitamshuhudia. Kila kiungo kitashuhudia kile kilichofanya. Ulimi wake utashuhudia ulichozungumza, mkono na ulichokishika na mguu na ulichokiendea n.k.
Siku hiyo atawatekelezea sawa malipo yao ya haki na watajua kwam- ba hakika Mwenyezi Mungu ndiye haki iliyo wazi.
Yaani Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawahisabu kesho na kuwalipa malipo ya haki na ya uadilifu. Hapo ndio watajua kwamba ufufo, hisabu na malipo walioahidiwa ni kweli, hakuna kuyakimbia.
8
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
الْخَبِيثَاتُ لِلْخَبِيثِينَ وَالْخَبِيثُونَ لِلْخَبِيثَاتِ وَالطَّيِّبَاتُ لِلطَّيِّبِينَ وَالطَّيِّبُونَ لِلطَّيِّبَاتِ أُولَـٰئِكَ مُبَرَّءُونَ مِمَّا يَقُولُونَ لَهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ ﴿٢٦﴾
27. Mambo ya uhabithi ni ya mahabithi na mahabithi ni wa mambo ya uhabithi. Na mema ni ya walio wema na walio wema ni wa mema. Hao wameepushwa na wanayoyasema; wao watapata msamaha na riziki ya ukarimu.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ بُيُوتِكُمْ حَتَّىٰ تَسْتَأْنِسُوا وَتُسَلِّمُوا عَلَىٰ أَهْلِهَا ذَٰلِكُمْ خَيْرٌ لَّكُمْ لَعَلَّكُمْ تَذَكَّرُونَ ﴿٢٧﴾
27. Enyi ambao mmeamini! Msiingie nyumba zisizo nyumba zenu mpaka muombe ruhusa na muwatolee salaam wenyewe. Hayo ni bora kwenu ili mpate kukumbuka.
فَإِن لَّمْ تَجِدُوا فِيهَا أَحَدًا فَلَا تَدْخُلُوهَا حَتَّىٰ يُؤْذَنَ لَكُمْ وَإِن قِيلَ لَكُمُ ارْجِعُوا فَارْجِعُوا هُوَ أَزْكَىٰ لَكُمْ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ ﴿٢٨﴾
28. Na msipomkuta yoyote humo basi msiingie mpaka mruhusiwe. Na mkiambiwa rudini, basi rudini. Hivyo ni usafi zaidi kwenu na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda.
لَّيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَدْخُلُوا بُيُوتًا غَيْرَ مَسْكُونَةٍ فِيهَا مَتَاعٌ لَّكُمْ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تُبْدُونَ وَمَا تَكْتُمُونَ ﴿٢٩﴾
29. Si vibaya kwenu kuingia nyumba zisizokaliwa amabazo ndani yake mna bidhaa zenu. Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyadhirisha na mnayoyaficha.
Aya 26 – 29
Mambo ya uhabithi ni ya mahabithi na mahabithi ni wa mambo ya uhabithi. Na mema ni ya walio wema na walio wema ni wa mema.
Neno uhabithi limefasiriwa kutoka na neno la kiarabu Khabith lenye maana ya uovu na ubaya katika kila jambo, ikiwemo ubaya katika itikadi, nia, sifa, kauli na vitendo vya aina mbali mbali, wala hauhusiki na zina.
Na neno wema limefasiriwa kutokana na neno Twayyib lenye maana ya uzuri katika kila jambo.
Qur'an imelitumia neno uhabithi katika ubaya wa ardhi, mali, maneno na vyakula vilivyoharamu na kila anayestahiki machukivu na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu katika majini na watu.
Jamaa katika wafasiri wamesema kuwa makusudio ya neno Khabithat ni wanawake mahabithi na Khabithun ni wanaume mahabith. Vilevile katika wema. Kauli hii haiafikiani na hali halisi ilivyo.
Tumewaona wanawake mahabithi wakiolewa na wanume wema na wanawake wema wakiolewa na wanume mahabithi. Bali hata haiafikiani na Qur'an; Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema:
"Mwenyezi Mungu amewapigia mfano waliokufuru - mke wa Nuh na mke wa Lut walikuwa chini ya waja wetu wema wawili miongoni mwa waja wetu, lakini wakakhini … Na Mwenyezi Mungu amewapigia mfano walioaminimke wa Firauni, aliposema: Mola wangu nijengee kwako nyumba Peponi na uniokoe na Firauni na vitendo vyake" (66:11). Inajulikana kwamba Nuh na Lut walikuwa Manabii, maasumu na Firauni ndiye yule aliyesema: "Mimi ndiye Mola wenu mkuu."
Tuonavyo sisi ni kuwa neno Khabithat lina maana ya mambo ya uhabithi, na neno khabithun lina maana ya walio mahabithi wote wanaume na wanawake. Limekuja kwa dhamiri ya kiume kwa kuchanganya wote. Vile vile Twayyibat na Twayyibun.
Kwa hiyo maana yatakuwa, kauli na vitendo vya uhabithi vinatokana na yule aliye habithi katika wanaume na wanawake. Na kauli na vitendo vyema vinatokana na yule aliye mwema; kama alivyosema mshairi: "Kila kilicho ndani ya chombo kitaiva."
Hao wameepushwa na wanayoyasema; wao watapata msamaha na riziki ya ukarimu.
Hao ni ishara ya walio wema; wanosema ni wale mahabithi. Mwenyezi Mungu (s.w.t) atawaneemaesha na maghufira na pepo hao walioepushwa.
Enyi ambao mmeamini! Msiingie nyumba zisizo nyumba zenu mpaka muombe ruhusa na muwatolee salaam wenyewe. Hayo ni bora kwenu ili mpate kukumbuka.
Mpaka muombe ruhusa ni amri ya kubisha hodi kabla ya kuingia; sawa na kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya 59 ya Sura hii tuliyo nayo: "Na watoto wanapofikia kubaleghe basi nawatake ruhusa."
Kila anayetaka kuingia nyumba ya mwingine ni lazima aombe idhini kwa mwenyewe kwanza. Kwa sababu kuingia ni kutumia mali ya mwenyewe, ambayo haiwezi kuwa halali ila kwa ruhusa yake. Kuanzia hapa ndio mafaqihi wakasema kuwa kuomba ruhusa ni wajibu na salaam ni Sunna. Inatosha kuwa ni kuomba ruhusa kwa jambo lolote lile; kama vile kugonga mlango, kusema hodi! Au wenyewe humo! Baada ya kupewa idhii ndio aiingie atoe salaam!
Na msipomkuta yoyote humo basi msiingie mpaka mruhusiwe.
Unaweza kuuliza : hapa, ikiwa nyumbani hakuna mtu, ni nani atakayetoa ruhusa?
Sheikh Maraghi amejibu kuwa makusudio ni ikiwa hakuna anayeweza kutoa ruhusa; kama mtoto mdogo au mtumishi. Jawabu lilo na nguvu ni ikiwa nyumba haina mtu, basi hairuhusiwi kuingia mpaka amuone mwenyewe kwanza na ampe idhini; kwa mfano kumwambia nenda nyumbani kwangu ukaniletee kitu fulani au tangulia nyumbani kwangu nami naja.
Na mkiambiwa rudini, basi rudini. Hivyo ni usafi zaidi kwenu.
Wala msing'ang'anie kutaka kuingia na msiwe na chuki nyoyoni kwa mwenye nyumba mchukue uzuri tu na kusema ana udhuru wa kisharia. Angalia kifungu cha 'Kuchukulia usahihi' katika Juz.1 (2:83).
Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyatenda.
Hii ni hadhari na kiaga kwa yule anayemshtumu na kumsema ambaye hakumpa idhini ya kuingia nyumbani kwake.
Si vibaya kwenu kuingia nyumba zisizokaliwa ambazo ndani yake mna bidhaa zenu.
Makusudio ya nyumba hizi ni zile sehemu za watu wengi, kama vile mahoteli na maduka.
Kwa hiyo ambaye ana bidhaa zake hotelini au dukani, basi anaweza kuingia na kuchukua bidhaa zake bila ya kmuomba ruhusa mwenyewe, kwa sababu amekwisha fungua mlango kwa wote. Pia hakuna siri kwa mwenye hoteli kwa hilo.
Na Mwenyezi Mungu anajua mnayoyadhirisha na mnayoyaficha.
Hii inaashiria kuwa si halali kwa mtu kuingia nyumba ya mwingine kwa kusudia kufanya khiyana na kuwadhuru wenyewe, na kwamba mwenye kukusudia hivyo, basi Mwenyezi Mungu anajua malengo yake na atamwadhibu nayo.
قُل لِّلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ وَيَحْفَظُوا فُرُوجَهُمْ ذَٰلِكَ أَزْكَىٰ لَهُمْ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا يَصْنَعُونَ ﴿٣٠﴾
30. Na waambie waumini wanaume wainamishe katika macho yao na wazilinde tupu zao. Hilo ni usafi zaidi kwao. Hakika Mwenyezi Mungu ana habari za wanayoyafanya.
وَقُل لِّلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ وَيَحْفَظْنَ فُرُوجَهُنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَلْيَضْرِبْنَ بِخُمُرِهِنَّ عَلَىٰ جُيُوبِهِنَّ وَلَا يُبْدِينَ زِينَتَهُنَّ إِلَّا لِبُعُولَتِهِنَّ أَوْ آبَائِهِنَّ أَوْ آبَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ أَبْنَائِهِنَّ أَوْ أَبْنَاءِ بُعُولَتِهِنَّ أَوْ إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي إِخْوَانِهِنَّ أَوْ بَنِي أَخَوَاتِهِنَّ أَوْ نِسَائِهِنَّ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُنَّ أَوِ التَّابِعِينَ غَيْرِ أُولِي الْإِرْبَةِ مِنَ الرِّجَالِ أَوِ الطِّفْلِ الَّذِينَ لَمْ يَظْهَرُوا عَلَىٰ عَوْرَاتِ النِّسَاءِ وَلَا يَضْرِبْنَ بِأَرْجُلِهِنَّ لِيُعْلَمَ مَا يُخْفِينَ مِن زِينَتِهِنَّ وَتُوبُوا إِلَى اللَّـهِ جَمِيعًا أَيُّهَ الْمُؤْمِنُونَ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٣١﴾
31. Na waambie waumini wanawake wainamishe katika macho yao na wazilinde tupu zao, wala wasionyeshe uzuri wao, isipokuwa unaodhihirika. Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao, wala wasidhihirishe uzuri wao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba wa waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au ndugu zao, au watoto wa kaka zao, au watoto wa dada zao, au iliyowamiliki mikono yao ya kuume, au wafuasi wanaume wasio na matamanio, au watoto wadogo ambao hawajajua uchi wa wanawake. Wala wasipige miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha. Na tubieni kwa Mwenyezi Mungu nyote enyi waumini ili mpate kufanikiwa.
Aya 30 – 31
Aya mbili hizi ni miongoni mwa Aya za hukmu, na zimeeleza wajibu wa kuinamisha jicho kwa wanawake na wanaume, kuhifadhi tupu na zina na hijabu. Ufafanuzi ni huu ufuatao:
1.Na waambie waumini wanaume wainamishe katika macho yao.
Mwenyezi Mungu amewaamrisha wanaume wazuie macho yao, lakini hakubainisha wayazuie macho yao kwenye nini. Ameyanyamazia hayo kwa kutaka yafahamike kutokana na mfumo wa maneno. Kwani lilio dhahiri ni kuharamishwa kuwaangalia watu kando.
Wameafikiana mafaqihi wengi kwamba haijuzu kwa mwanamume kuangalia kitu katika mwili wa mtu kando mwanamke, isipokuwa uso wake na viganja kwa sharti ya kuangalia bila ya kujiburudisha na kutohofia kuingia katika haramu. Hii ni kwa mwanamke Mwislamu ambaye dini yake inamkataza kujiweka wazi. Ama yule ambaye dini yake haimkatazi kujiweka wazi, wametofautiana mafaqihi katika kujuzu kuwangalia bila ya kujiburudisha. Wengine wakasema inajuzu kuangalia nywele za wanawake waislamu mabedui wasiokatazika.
2.Na wazilinde tupu zao na zina.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameingiza neno 'katika' kwenye macho, lakini hakuingiza kwenye tupu. Kwa sabu ni wajibu kusitiri tupu wakati wote isipokuwa katika faragha ya mume na mke, lakini kuangalia si haramu katika hali zote isipokuwa katika baadhi ya hali.
Hilo ni usafi zaidi kwao. Hakika Mwenyezi Mungu ana habari za wanayoyafanya.
Hilo ni hilo la kuinamisha macho na walio haramu kuwaangalia, jambo ambalo ni twahara zaidi kwa nafsi na karibu zaidi kwa takua na linaweka mbali dhambi.
3.Na waambie waumini wanawake wainamishe katika macho yao na wazilinde tupu zao.
Mafaqihi wa kishia wamesema kuwa ni haramu kwa mwanamke kumtazama mwanamume aliye mtu kando, vile ilivyo haramu kwa mwanamume juu ya mwanamke. Kwa hiyo haijuzu kwa mwanamke kuangalia nywele za mwanamume n.k. Lakini wengine wamesema kuwa inajuzu kwa mwanamke kumwangalia mwanamume sehemu zote isipokuwa sehemu iliyo baina ya kitovu na magoti. Ufafanuzi uko kwenye kitabu chetu cha Fiqh ala madhahibul-khamsa (Fiqh katika madhebu tano) sehemu ya yaliyo wajibu kuangalia na yaliyo haramu.
4.Wala wasionyeshe uzuri wao, isipokuwa unaodhihirika.
Makusudio ya uzuri hapa ni sehemu zao. Kwa sababu si haramu kuangalia uzuri. Makusudio ya unaodhihirika ni sehemu za uso na viganja viwili tu. Mafaqihi wametoa dalili kwa Aya hii, juu ya wajibu wa hijabu na kwamba mwili wote wa mwanamke ni uchi isipokuwa uso na viganja viwili vya mikono.
Imam Ja'far Swadiq(a.s ) . Aliulizwa kuhusu mikono miwilli kuwa je, ni katika uzuri aliouzungumzia Mwenyezi Mungu? Akasema: ndio na sehemu yoyote isiyokuwa uso na viganja viwili ni katika uzuri ulioharamishwa. Katika kitabu Ahkamul-Ayat cha Aljasas, mmoja wa maimamu wa kihanfi anasema:"Makusudio ya unaodhihiri ni uso na viganja viwili" .
Katika Tafsir ya Razi ambaye ni wa madhehebu ya Shafi anasema: "Wameafikiana kuwa uso na viganja viwili si sehemu ya tupu."
Na waangushe shungi zao juu ya vifua vyao.
Neno vifua, limefasiriwa kutokana na neno juyub lenye maana ya uwazi wa magauni. Yaani ni wajibu kwa wanawake kuangusha mitandio yao kwa mbele ili isitiri, shingo na vifua.
Wanawake wa wakati wa jahilia, walikuwa wakifunika vichwa vyao kisha wanangusha shungi zao kwa nyuma, shingo zao na vifua vyao vinakuwa wazi. Wakaendela kuwa hivyo hata wakati wa Uislamu, mpaka iliposhuka Aya hii wakawa wanaangusha kwa mbele na kusitiri shingo na vifua.
Uislamu umeruhusu mwanamke afunue uso wake na viganja vyake; kwa sababu kuna dharura ya kimaisha. Sehemu nyinginezo zisizokuwa hizo, zimezingatiwa kuwa ni uchi, kwa sababu ni hatari. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) amesema:"Mwenye kuchunga kondoo wake kandokando ya ugo nafsi yake inamvuta kuchunga ndani yake."
Hivi ndivyo ilivyo hasa. Popote uendapo utajionea maajabu. Mwanamke alianza kufunua kichwa chake baada ya kwenda saloni, akendela kufunua kifua na mabega hadi kufikia minisketi na mavazi mengine ya maajabu yanaonyesha umbile zima la mwanamke; huku akijitembeza barabarani kama kwamba ni nyama inayouzwa sokoni. Siri ya hilo ni kwamba wanawake wengi hawaendi mbali zaidi ya kujionyesha na kuonyesha urembo wao tu.
Maajabu zaidi niliyoyasoma kuhusu mambo haya ni kwamba huko mjini Humburg, Ujerumani ya magharibi, kuna barabara ya kutisha ambayo pambizoni mwake mna sehemu zilizo na wanawake wakiwa uchi, katika hali isiyokuwa ya kawaida ambayo haingiliki akilini. Kila ambalo unaliona kuwa haliwezi kufanyika basi hapo linafanyika kiuhakika. Huu ndio upeo wa uhuru.
Nimesoma makala hii nikiwa natetema, na kufikiria kwamba barabara hii iliyo uchi, kama sio hivi karibuni basi baadae itafika kwenye miji yetu; sawa na ilivyofika minisketi na mengineyo; maadamu tunaigiza magharibi. Mungu apishe mbali na yatakayokuja kesho.
Kwa mnasaba huu tunadokeza kwamba, ikiwa mwanamke anapenda sana kuonyesha urembo wake na uzuri wake na kutengeneza shepu yake kwa kila njia, basi kuna wanaume wengi wanaopenda kuonyesha umashuhuri wao, hata kama ni kwa njia ya uongo na kudanganya. Ikiwa mwanamke anamfanyia chuki anayeshindana naye kwa uzuri na urembo, basi wanaume wanaopenda kujionyesha wana hasadi zaidi hasa kwa yule ambaye jina lake linatajwa.
Mnamo mwaka 1957, mwandishi mmoja wa Kimisri, alitoa makala ambayo ndani yake aliibeza fat-wa ya masheikh wa Al-azhar kuharamisha mwanamke kuvaa nguo ya kuogelea. Miongoni mwa aliyoyasema ni: Uislamu uko mbali na fatwa hii.
Mimi nilitoa makala kupinga maelezo yake haya, na nikathibitisha kuwa masheikh wa Al-Azhar wametamka neno la Uislamu na Qur'an, na nikatoa ushahidi wa Aya:'Wala wasidhihirishe uzuri wao.'
Baada ya kupita siku, ikasadifu mimi na mwenzangu mmoja kumtembelea sheikh mmoja. Tulipotulia yule sheikh akanikabili na kusema: "Vipi wewe unahalalisha kuvaa nguo ya kuogelea na kuwarudi masheikh wa Al-azhar ambao wametoa fatwa ya kuharamisha?
Nikamwambia: Hapana ni kinyume na hivyo. Mimi nimewaunga mkono masheikh na nikaiponda rai ya mwenye kuwarudi.
Akasema: "Hapana! Mimi ninalo gazeti lilo na makala hiyo, ngoja nikuonyeshe."
Nikamwambia ailete.
Basi akaenda haraka na akaja na gazeti mkononi mwake, akaanza kulisoma kwa hamasa kubwa.
Nikamwambia: Je, umeona nini?
Akapigwa na butwaa, gazeti likamponyoka mikononi. Alhamdulillah, hapo pia alikuwako rafiki wa sheikh na sheikh mmoja miongoni mwa jamaa zake. Hao wawili bado wako hai hivi sasa tukiwa katika wakati wa kusi mwaka 1969.
Siwezi kupata tafsiri ya sheikh huyu ambaye alijiumbua mwenyewe isipokuwa Mungu amsamehe. Yeye alitaka anitie aibu na kuniumbua, akawa anatafuta taa na utambi, kama wasemavyo watu wa Amol, ili aanze kueneza na kutangaza.
Na pale aliposoma jina langu kwenye gazeti chuki yake iliyojificha ililipuka na kupenda kwake umashuhuri kukampofusha, weupe akauona ni weusi na haki kuwa ni batili. Sio siri kwamba chuki ni sawa na mapenzi, inapofusha na kufanya uziwi. "Wana nyonyo, lakini hawafahamu kwazo, na wana macho, lakini hawaoni kwayo, na wanayo masikio, lakini hawasikii kwayo. Hao ni kama wanyama bali wao ni wapotevu zaidi. Hao ndio walioghafilika." Juz. 9 (7:179).
Sikutaja kisa hiki kwa kulalamika au kushtakia, hapana! Uzoefu umenifundisha kutowajali waongo, lakini kalamu yangu imenizidia na haikunipa hiyari. Hivi ndivyo nilivyo mimi na kalamu yangu.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwakataza wanawake Waislamu kutofunua sehemu zao isipokuwa uso na viganja, sasa anabainisha wale ambao inafaa kuwadhihirishia ambao ni aina kumi na mbili:
1.Wala wasidhihirishe uzuri wao ila kwa waume zao . Kila mmoja kati ya mume na mke anaweza kumwangalia mwenzake popote atakapo.
2.Au baba zao . Hapa wanaingia mababu wa upande wa baba na mama.
3.Au baba wa waume zao . Wanaingia mababa wa waume na mababu zao wa upande wa baba na mama
4.Au watoto wao. Mtoto wa mtoto, mwanamume au mwanamke, pia ni mtoto.
5.Au watoto wa waume zao na kuendelea chini.
6.Au ndugu zao wa baba mmoja tu au mama mmoja tu au wote.
7.Au watoto wa kaka zao na kuendelea chini.
8.Au watoto wa dada zao vilevile kuendelea chini.
9.Au wanawake wao . Ieleweke kuwa ni haramu kuwa uchi kabisa mwanamke mbele ya mwanamke mwenzake hata kama ni mama yake au binti yake, kama ambavyo ni haramu kwake yeye pia kuwaangalia uchi. Ni halali kuangaliana sehemu zisizokuwa hizo, ikiwa ni Mwislamu. Ama mwanamke asiyekuwa Mwislamu haifai kuwa wazi mbele yake. Hivi ndivyo ilivyofahamisha Aya. Linalokhalifu hilo liachwe. Baadhi ya mapokezi yanasema kuwa wanawake wasiokuwa waislamu wakijifunua mbele ya wanawake wasiokuwa waislamu wanaenda kuwasifia waume zao.
10.Au iliyowamiliki mikono yao ya kuume, katika wajakazi tu . Ama mtumwa wa kiume haijuzu kumwangalia isipokuwa uso na viganja viwili; hata kama ni hasi. Kauli na riwaya zinazokhalifu hayo basi zinaachwa. Kwa vyovyote, ni kuwa maudhui haya hayapo siku hizi, ambapo hakuna utumwa.
11.Au wafuasi wanaume wasio na matamanio. Hao ni wale wanaochanganyika na familia na kuwa nao mara nyingi, waki- wa hawana matamanio ya wanawake, kwa sababu za kimwili; kama uzee na uhanithi au za kuathirika kisaikolojia.
12.Au watoto wadogo ambao hawajajua uchi wa wanawake . Yaani watoto wadogo ambao hawawezi kupambanua baina ya uchi na kiungo kingine.
Wala wasipige miguu yao ili yajulikane mapambo waliyoyaficha.
Wanawake walikuwa wakivaa vikuku miguuni, mpaka sasa desturi hii inaendelea katika miji mingi ya waarabu. Baadhi walikuwa wakipiga miguu yao chini ili vigongane vikuku vyao kuwavutia wanaume au wajue kuwa wamevaaa vikuku. Ndipo Mwenyezi Mungu akawakataza hilo. Hapo inaashiria kwamba haifai kwa mwanamke kufanya jambo lolote litakalomvutia mwanamume.
Na tubieni kwa Mwenyezi Mungu nyote enyi waumini, ili mpate kufanikiwa.
Acheni yale aliyowakataza Mwenyezi Mungu, na ambaye atateleza kufanya makosa basi afanye haraka kutubia.
9
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
وَأَنكِحُوا الْأَيَامَىٰ مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُمْ إِن يَكُونُوا فُقَرَاءَ يُغْنِهِمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴿٣٢﴾
32. Na waozeni wajane miongoni mwenu na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu. Wakiwa mafukara Mwenyezi Mungu atawa tajirisha katika fadhila zake; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.
وَلْيَسْتَعْفِفِ الَّذِينَ لَا يَجِدُونَ نِكَاحًا حَتَّىٰ يُغْنِيَهُمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ وَالَّذِينَ يَبْتَغُونَ الْكِتَابَ مِمَّا مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ فَكَاتِبُوهُمْ إِنْ عَلِمْتُمْ فِيهِمْ خَيْرًا وَآتُوهُم مِّن مَّالِ اللَّـهِ الَّذِي آتَاكُمْ وَلَا تُكْرِهُوا فَتَيَاتِكُمْ عَلَى الْبِغَاءِ إِنْ أَرَدْنَ تَحَصُّنًا لِّتَبْتَغُوا عَرَضَ الْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَن يُكْرِههُّنَّ فَإِنَّ اللَّـهَ مِن بَعْدِ إِكْرَاهِهِنَّ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٣٣﴾
33. Na wajizuilie na machafu wale wasiopata cha kuolea, mpaka Mwenyezi Mungu awatajirishe katika fadhila zake. Na wale ambao wanataka kuandika katika wale ambao imewamiliki mikono yenu ya kuume, basi waandikieni kama mkiona wema kwao. Na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu aliyowapa. Wala msiwalazimishe vijana wenu wa kike kufanya umalaya kwa ajili ya kutafuta pato la maisha, ikiwa wanataka kujichunga. Na atakaye walazimisha basi Mwenyezi Mungu baada ya kulazimishwa kwao huko ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
وَلَقَدْ أَنزَلْنَا إِلَيْكُمْ آيَاتٍ مُّبَيِّنَاتٍ وَمَثَلًا مِّنَ الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلِكُمْ وَمَوْعِظَةً لِّلْمُتَّقِينَ ﴿٣٤﴾
34. Na hakika tumewateremshia Aya zinazobainisha na mifano kutokana na waliopita kabla yenu na mawaidha kwa wenye takua.
Aya 32 – 34
Na waozeni wajane miongoni mwenu.
Maneno yanaelekezwa kwa Waislamu wote. Wajane ni wale wasiokuwa na wake au wasiokuwa na waume. Amri hii hapa ni ya Sunna sio ya wajibu. Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwaamrisha wanaume na wanawake wahifadhi tupu zao na kujizuia na mambo yaliyo haramu na pia kuwakataza wanawake kujipamba na kudhihirisha kipambo mbele ya watu kando.
Sasa anaamrisha kusaidiana kwa kila anayehitajia ndoa baina ya wanaume na wanawake. Kwa sababu ujane ndio chimbuko la uchafu na uovu; kama zina na ulawiti. Na ndoa ni kinga ya hayo. Ndio maana Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) akasema:"Waovu wenu ni wajane wenu…"
"Ndoa ni katika sunna yangu, atakayejiepusha na sunna yangu basi si katika mimi."
Na wema katika watumwa wenu na wajakazi wenu.
Makusudio ya wema hapa ni waumini. Yaani waozeni watumwa wakiwa ni waumini, maudhui haya hayapo, kwa kutokuwepo utumwa.
Wakiwa mafukara Mwenyezi Mungu atawatajirisha katika fadhila zake
Watu wengi hawaangalii maadili ya mchumba, bali wanaangalia cheo chake au mali yake. Ndipo Mwenyezi Mungu akalaumu fikra hii na akasema kuwa yeye ni muweza wa kila kitu. Kuna Hadith isemayo:"Akiwajia ambaye mnairidhia hulka yake na dini yake, basi muozeni; kama hamtafanya itakuwa fitna katika ardhi na uharibifu mkubwa."
Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa, Mwenye kujua.
Anatoa wasaa kwa anaemuomba na asiyemuomba kwa fadhila zake.
Na wajizuilie na machafu wale wasiopata cha kuolea, mpaka Mwenyezi Mungu awatajirishe.
Unaweza kuuliza : katika Aya iliyotangulia Mwenyezi Mungu amesema kuwa watu waoe tu, wakiwa mafukara atawatajirisha; kisha hapa anasema, tena moja kwa moja baada ya kauli ya kwanza, kuwa mtu asiyepata mahari wala posho asiingie kwenye uovu na kwamba avumilie mpaka Mwenyezi Mungu ampe wasaa, basi kuna wajihi gani baina ya Aya mbili?
Jibu : Hakuna haja ya kuchanganya Aya mbili hizi, kwa sababu kila moja ina makusudio yake. Ya kwanza inawakusudia mawalii, kwamba akija mchumba msimkatae kwa sababu ya ufukara wake. Aya ya pili inamuhusu fukara mwenyewe, kwamba akinyimwa kuoa kwa sababu ya ufukara wake, basi avumilie na afanye bidii mpaka Mungu atakapompa wasaa wa kuweza kuoa.
Na wale ambao wanataka kuandika katika wale amabao imewamiliki mikono yenu ya kuume, basi waandikieni kama mkiona wema kwao.
Ambaye ana mtumwa wa kike au wa kiume anayeweza kuchuma, anaweza kuandikiana naye mkataba kuwa akitoa kiasi fulani cha pesa mara moja au pole pole, awe huru.
Akitekeleza yote basi anakuwa huru au akitoa baadhi atakuwa ana uhuru wa kiasi kile alichotoa, ikiwa hakuna sharti la kutoa chote; vinginevyo hatakuwa na uhuru wowote.
Imesekana kuwa mtumwa hawezi kugawika; ama awe huru kamili au awe mtumwa kamili. Ni Sunna kwa mwenye mtumwa kumwachia kiasi fulani cha mali waliyoelewana. Hayo ndio makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: Na wapeni katika mali ya Mwenyezi Mungu aliyowapa.
Mafaqihi wameweka istilahai ya neno mkataba kwa makubaliano haya, kutokana na Mwenyezi Mungu kutumia neno kitab.
Wala msiwalazimishe vijana wenu wa kike kufanya umalaya kwa ajili ya kutafuta pato la maisha, ikiwa wanataka kujichunga.
Makusudio ya vijana wa kike hapa ni wajakazi, ambao hivi sasa hawako. Watu wa wakati wa ujahiliya walikuwa wakiwalazimisha wajakazi wao kufanya zina kwa kutaka mali, ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akalikataza hilo.
Unaweza kuuliza kuwa : dhahiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu 'wakitaka kujichunga,' inaonyesha kuwa kama hawataki kujichunga basi wanaweza kulazimishwa kufanya zina, na hali tunajua kuwa zina ni hara- mu kwa nyanja zake zote?
Jibu : maana ya neno 'ikiwa' yanatofautiana kwa kutofautiana makusudio na maneno yalivyo. Inaweza ikawa kwa maana ya sharti hasa, ilivyo. Kwa mfano kumwambia mtu: Ikiwa utafanya hivi na mimi nitafanya kama utakavyofanya. Hapa utakuwa umeweka sharti kwamba hutafanya mpaka afanye yeye.
Mara nyingine inakuwa bila ya kukusudia sharti; kwa mfano kumwambia sahibu yako: "Ikiwa utaruzukiwa mtoto basi usimnunulie baskeli" hapa haina maana kama hataruzukiwa mtoto basi anaweza kumnunulia baskeli; jambo ambalo litakuwa kama kuchanganyikiwa. Isipokuwa unataka kumweleza maoni yako ya kutotaka watoto wapande baskeli.
Maana haya ndiyo yaliyokusudiwa hapa 'ikiwa' limekuja kubainisha hali halisi; kwamba ikiwa wajakazi wanataka kujichunga basi nyinyi itakuwa ni zaidi mjichunge.
Kama tukiliweka neno 'ikiwa' kwa maana ya sharti, itakuwa maana yake ni: walazimisheni wajakazi wenu ikiwa wanataka zina. Na inavyojulikana ni kuwa hakuna kulazimisha ikiwa mtu anataka.
Kwa maneno mengine ni kuwa neno 'ikiwa' au 'iwapo' au 'kama' na mengineyo mfano wake, huwa linafahamisha vitu viwili kwa wakati mmoja: Maana yake kimatamshi na maana yake kiufahamu na kiuelewa ambayo hayakutamkwa lakini yanafahamika kwa ishara. Kwa istlahi ya watu wa elimu ya usul, wanaita mantuq na mafhum
Mantuq ni kwa mfano kumwambia sahibu yako; ikiwa utanikirimu na mimi nitakukirimu. Kwa hiyo kimatamshi hapa imeeleweka kuwa kumkirimu kwako kutategema yeye ikiwa atakukirimu.
Ama kiufahamu, katika mfano huu ni kuwa, ikiwa hukunikirimu basi nami sikukukirimu. Maana haya hayakutajwa, lakini yamefahamika kutokana na jumla ya kwanza.
Aya tuliyo nayo iko katika aina ya kwanza tu, ya kimatamshi; haiwezi kuingia kwenye aina ya pili.
Yaani kutofaa kutolazimisha zina pamoja na kutaka kujisitiri. Hapo ufahamu hauingii, kwa sababu tukileta ufahamu maana itakuwa ni: kujuzu kulazimisha pamoja na kuitaka hiyo zina. Hapo kutakuwa na mgongano, wa kuwalazimisha na wenyewe wanataka, jambo haliwezekani kwa wakati mmoja. Itakuwaje mtu alazimishwe na wakati huo huo mwenyewe anataka. Pia ni muhali kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, kulazimisha uovu kwa namna yoyote ile.
Na atakayewalazimisha basi Mwenyezi Mungu baada ya kulazimishwa kwao huko ni Mwingi wa maghufira, Mwenye kurehemu.
Wale waliolazimishwa kufanya zina. Kwa sababu kosa ni la yule aliyelazimisha, sio aliyelazimishwa. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) amesema:"Umma wangu umeondolewa yale waliyolazishwa…" Mwenye kumlazimisha mwingine kufanya makosa, Mwenyezi Mungu atamghufiria akitubia na kurejea.
Na hakika tumekuteremshia Aya zinazobainisha na mifano kutokana na waliopita kabla yenu na mawaidha kwa wenye takua.
Makusudio ya Aya ni hukumu za Qur'an na mafundisho yake nazo ziko wazi. Mifano ni habari za waliopita na visa vyao. Mawaidha kwa wenye takua ni uongofu kwa mwenye kutaka kuongoka.
Maana ni kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu ameteremsha Qur'an kubainisha na kuweka wazi hukumu tunazozihitajia, habari za waliopita, uongofu kwa mwenye kuutaka, na nguvu kwa mwenye kumtawalisha Mungu.
اللَّـهُ نُورُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ مَثَلُ نُورِهِ كَمِشْكَاةٍ فِيهَا مِصْبَاحٌ الْمِصْبَاحُ فِي زُجَاجَةٍ الزُّجَاجَةُ كَأَنَّهَا كَوْكَبٌ دُرِّيٌّ يُوقَدُ مِن شَجَرَةٍ مُّبَارَكَةٍ زَيْتُونَةٍ لَّا شَرْقِيَّةٍ وَلَا غَرْبِيَّةٍ يَكَادُ زَيْتُهَا يُضِيءُ وَلَوْ لَمْ تَمْسَسْهُ نَارٌ نُّورٌ عَلَىٰ نُورٍ يَهْدِي اللَّـهُ لِنُورِهِ مَن يَشَاءُ وَيَضْرِبُ اللَّـهُ الْأَمْثَالَ لِلنَّاسِ وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٣٥﴾
35. Mwenyezi Mungu ni nuru ya mbingu na ardhi. Mfano wa nuru yake ni kama shubaka ndani yake mna taa. Taa hiyo imo katika tungi. Tungi hilo ni kama nyota inayomeremeta, inayowashwa kwa mafuta yanayotokana na mti uliobarikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakurubia mafuta yake kung'aa ingawa hayajaguswa na moto - Nuru juu ya nuru. Mwenyezi Mungu humuongoza kwenye nuru yake amtakaye. Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano; na Mwenyezi Mungu ni mwenye kujua kila kitu.
فِي بُيُوتٍ أَذِنَ اللَّـهُ أَن تُرْفَعَ وَيُذْكَرَ فِيهَا اسْمُهُ يُسَبِّحُ لَهُ فِيهَا بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ ﴿٣٦﴾
36. Katika nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameruhusu ziinuliwe na kutajwa humo jina lake, wanamtakasa humo asubuhi na jioni.
رِجَالٌ لَّا تُلْهِيهِمْ تِجَارَةٌ وَلَا بَيْعٌ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ وَإِقَامِ الصَّلَاةِ وَإِيتَاءِ الزَّكَاةِ يَخَافُونَ يَوْمًا تَتَقَلَّبُ فِيهِ الْقُلُوبُ وَالْأَبْصَارُ ﴿٣٧﴾
37. Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kuisimamisha Swala na kutoa Zaka. Wanaihofu siku ambayo nyoyo na macho yatageuka.
لِيَجْزِيَهُمُ اللَّـهُ أَحْسَنَ مَا عَمِلُوا وَيَزِيدَهُم مِّن فَضْلِهِ وَاللَّـهُ يَرْزُقُ مَن يَشَاءُ بِغَيْرِ حِسَابٍ ﴿٣٨﴾
38. Ili Mwenyezi Mungu awalipe mazuri ya yale waliyoyatenda, na awazidishie katika fadhila zake. Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu.
MWENYEZI MUNGU NI NURU YA MBINGU NA ARDHI
Aya 35 – 38
Mwenyezi Mungu (s.w.t) kwenye Kitabu chake kitukufu, mara nyingi ameashiria kwenye ukuu wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake. Lengo la kumfahamisha mtu ukuu wa ulimwengu ni kumfahamisha ukuu wa huyo aliyeufanya huo ulimwengu na awe na yakini ya Mola wake na Muumba wake. Mwenyezi Mungu (s.w.t) ametaja katika baadhi ya Aya kwamba kuumba ulimwengu ni kukubwa zaidi kuliko kuumba mtu.
Hilo Mwenyezi Mungu (s.w.t) amelitaja katika Aya kadhaa; kama:
أَأَنتُمْ أَشَدُّ خَلْقًا أَمِ السَّمَاءُ بَنَاهَا ﴿٢٧﴾
"Je, nyinyi ni wenye umbo gumu zaidi au mbingu alizozijenga?" (79:27)
لَخَلْقُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ أَكْبَرُ مِنْ خَلْقِ النَّاسِ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يَعْلَمُونَ ﴿٥٧﴾
"Bila shaka kuumba mbingu na ardhi ni kukubwa zaidi kuliko kuumba watu, lakini watu wengi hawajui" (40:57).
Mbingu na ardhi kwa mpangilio wake, nidhamu yake na utaratibu wake ni dalili kubwa na iliyo wazi zaidi ya ukuu wa muumba katika uweza wake, ujuzi wake na hekima yake.
Kwa kuwa kuumba ulimwengu ni dalili wazi zaidi ya kuweko Mwenyezi Mungu na kwa kuwa nuru ndiyo iliyo wazi zaidi ya uwazi wote, ndio Mwenyezi Mungu (s.w.t) akasema:
Mwenyezi Mungu ni nuru ya mbingu na ardhi.
Makusudio ya nuru ya Mwenyezi Mungu ni ukuu wake katika uweza wake, ujuzi wake na hekima yake. Ukuu huu unajitokeza katika kuumba ulimwengu. Kila kitu katika ardhi yake mbingu yake na kinafahamisha kwa mfahamisho ulio wazi juu ya kuweko kwake Mwenyezi Mungu na ukuu wake.
Hapa inatubainikia kuwa hakuna tofauti baina ya kusema: Mbingu na ardhi ni nuru ya Mwenyezi Mungu na kusema kuwa Mwenyezi Mungu ni nuru ya mbingu na ardhi.
Kwa sababu maana ya jumla ya kwanza ni kuwa ukuu wa ulimwengu unafahamisha ukuu wa Mwenyezi Mungu na maana ya jumla ya pili ni kuwa ukuu wa Mwenyezi Mungu unajitokeza kwenye ukuu wa ulimwengu. Ni sawa na kusema; Mpangilio mzuri wa jengo hili unafahamisha umahiri wa mjengaji au umahiri wa mjengaji unajitokeza katika mpangilio mzuri wa jengo hili.
Mfano wa nuru yake ni kama shubaka ndani yake mna taa, taa hiyo imo katika tungi, tungi hilo ni kama nyota inayomeremeta, inayowashwa kwa mafuta yanayotokana na mti uliobarikiwa, mzaituni. Si wa mashariki wala magharibi. Yanakurubia mafuta yake kun'gaa ingawa hayajaguswa na moto.
Huu ni mfano alioutoa Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuweka wazi dalili za kuweko kwake Mwenyezi Mungu; kwamba dalili hizo ziko kwenye kila sehemu ya ulimwengu.
Muhtasari wa mfano huu ni taa iliyowekwa kwenye ukuta wa nyumba ikiwa na mwanga wala haifikiwi na upepo kwa vile iko kwenye kandili ya kioo ambacho ni safi kikimeremeta kama nyota inayoangaza.
Mafuta yenyewe yametokana na mzaituni ambao sio kuwa unapata jua linapochomoza tu au linapotua bali unapata jua wakati wote kwa sababu unaelekea jua, wala haupatwi na kivuli cha mti wala mlima. Ndio maana mafuta yake ni safi yanayotoa mwanga yenyewe kabla ya kuunguzwa, na yanapochomwa ndio yanatoa mwanga zaidi.
Nuru juu ya nuru. Nuru ya mafuta safi na nuru ya taa. Yaani Taa ime- ongeza mwangaza kutokana na usafi wa mafuta, usafi wa kioo, uthibiti wa shubaka ukutani na kutopata mvumo wa upepo.
Mwenyezi Mungu humuongoza kwenye nuru yake amtakaye.
Ikiwa watafuata njia aliyoiweka kwa ajili ya uongofu, kwa sababu Mwenyezi Mungu (s.w.t) ni mwenye hekima, hafanyi mambo hovyo hovyo. Wale ambao anawaongoza na kuwathibitisha ni wale ambao wanaona dalili zake Mwenyezi Mungu na kuzifanyia kazi.
Mwenyezi Mungu amewaashiria katika Aya zinazofuatia kwa kusema: 'Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu.'
Na Mwenyezi Mungu huwapigia watu mifano ikiwemo hiyo iliyotajwa, "Ili aangamie wa kuangami kwa dalili dhahiri na awe hai wa kuwa hai kwa dalili dhahiri" Juz. 10 (8:42).
Na Mwenyezi Mungu ni mwenye kujua kila kitu.
Anajua wenye kukana na kuzifanyia inadi dalili zake zenye kuenea na awalipe Jahannam ambayo ni makazi mabaya.
Katika nyumba ambazo Mwenyezi Mungu ameruhusu ziinuliwe na kutajwa humo jina lake.
Makusudio ya nyumba hapa ni misikiti, na kuinuliwa ni kujengwa. Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja kwamba Yeye humuongoza kwenye nuru yake amtakaye, sasa anataja misikiti na kwamba yeye ameruhusu ijengwe kwa sababu waumini wanaswali humo.
Wanamtakasa humo asubuhi na jioni. Watu ambao biashara wala kuuza hakuwashughulishi na kumdhukuru Mwenyezi Mungu, na kuisimamisha Swala na kutoa Zaka.
Makusudio ya biashara hapa ni kinaya cha kazi yoyote ambayo ni kwa ajili ya dunia. Imetajwa biashara kwa sababu ndio yenye faida sana na yenye matumizi mengi.
Maana ni kuwa waumini wanafanya kazi kwenye masoko, mashambani, viwandani n.k., na wakati huo wakifanya kwa ajili ya akhera.
Wanaswali, wanafunga wanatoa Zaka na kuhiji. Kwa hiyo sio dunia inayowashughulisha kuicha akhera wala akhera, haiwafanyi waiache dunia. Kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu:
وَابْتَغِ فِيمَا آتَاكَ اللَّـهُ الدَّارَ الْآخِرَةَ وَلَا تَنسَ نَصِيبَكَ مِنَ الدُّنْيَا ﴿٧٧﴾
" Na utafute kwa aliyokupa Mwenyezi Mungu makazi ya akhera wala usisahu fungu lako katika dunia." (28:77).
Wanaihofu siku ambayo nyoyo na macho yatageuka.
Hiki ni kinaya cha fazaa watakayoipata wakosefu. Ama wale wema watakuwa katika amani ili Mwenyezi Mungu awalipe mazuri ya yale waliyoyatenda, katika matendo mema. Imam Ali(a.s ) anasema:"Hatafuzu kwa kheri ila aliyeifanya na wala hatalipwa malipo ya shari ila aliyeifanya."
Na awazidishie katika fadhila zake zaidi na zaidi.
Na Mwenyezi Mungu humruzuku amtakaye bila ya hisabu; yaani bila ya kustahiki, bali kwa fadhila zake na ukarimu. Amesema mwenye kitabu Al- asfar:
"Ambaye kitabu chake hakina maovu, ataingia Peponi bila ya hisabu. Na yule ambaye kitabu chake hakina mema ataingia motoni bila ya hisabu. Watakaohisabiwa ni wale ambao wamechanganya mema na maovu."
10
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
وَالَّذِينَ كَفَرُوا أَعْمَالُهُمْ كَسَرَابٍ بِقِيعَةٍ يَحْسَبُهُ الظَّمْآنُ مَاءً حَتَّىٰ إِذَا جَاءَهُ لَمْ يَجِدْهُ شَيْئًا وَوَجَدَ اللَّـهَ عِندَهُ فَوَفَّاهُ حِسَابَهُ وَاللَّـهُ سَرِيعُ الْحِسَابِ ﴿٣٩﴾
39. Na wale ambao wamekufuru vitendo vyao ni kama sarabi jangwani, mwenye kiu huyadhania ni maji, hata akiyaendea hapati chochote. Na atamkuta Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawasawa. Na Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu.
أَوْ كَظُلُمَاتٍ فِي بَحْرٍ لُّجِّيٍّ يَغْشَاهُ مَوْجٌ مِّن فَوْقِهِ مَوْجٌ مِّن فَوْقِهِ سَحَابٌ ظُلُمَاتٌ بَعْضُهَا فَوْقَ بَعْضٍ إِذَا أَخْرَجَ يَدَهُ لَمْ يَكَدْ يَرَاهَا وَمَن لَّمْ يَجْعَلِ اللَّـهُ لَهُ نُورًا فَمَا لَهُ مِن نُّورٍ ﴿٤٠﴾
40. Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyofunikwa na mawimbi juu ya mawimbi na juu yake yapo mawingu-Giza juu ya giza. Akiutoa mkono wake anakurubia asiuone. Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru, basi hawi na nuru.
أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يُسَبِّحُ لَهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَالطَّيْرُ صَافَّاتٍ كُلٌّ قَدْ عَلِمَ صَلَاتَهُ وَتَسْبِيحَهُ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ بِمَا يَفْعَلُونَ ﴿٤١﴾
41. Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtaksa vilivyomo mbinguni na ardhini na ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwishajua Swala yake na tasbihi yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wayatendayo.
وَلِلَّـهِ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَإِلَى اللَّـهِ الْمَصِيرُ ﴿٤٢﴾
42. Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi, na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo.
Aya 39 – 42
Na wale ambao wamekufuru vitendo vyao ni kama sarabi jangwani, mwenye kiu huyadhania ni maji, hata akiyaendea hapati chochote.
Makusudio ya makafiri hapa ni wale wanaokana utume wa Muhammad, kwa sababu ya inadi, ubaguzi, kupuuza au uzembe; yaani hakuutafuta uhakika akiwa ana uwezo wa kufanya utafiti na kuchunguza.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kuwataja wale ambao mambo ya dunia hayawafanyi wakaacha akhera na kwamba yeye atawalipa kwa yale mema waliyoyafanya, sasa anawataja hawa wapinzani wakanushaji, kwamba wao wametegemea batili na wakaitakidi kuwa ni haki itakayowafaa mbele ya Mwenyezi Mungu; sawa na mwenye kiu anavyotegemea mazigazi. Akitaka kuyafikia basi anakuta ni jua kali linalomzidishia kiu.
Wala hakuhusika na wasifa huu yule anayemkufuru Mwenyezi Mungu au utume wa Muhammad(s.a.w. w ) tu. Isipokuwa wanahusika wengi katika umma wa Muhammad(s.a.w. w ) ambao wanajidhania kuwa ni watu wa heri na takua, huku wakiwafanyia chuki na hasadi waja wa Mwenyezi Mungu na wakiipupia dunia na majanga yake.
Na atamkuta Mwenyezi Mungu hapo naye amlipe hisabu yake sawa-sawa. Na Mwenyezi Mungu ni mwepesi wa kuhisabu.
Kumkuta Mwenyezi Mungu ni kukuta hisabu yake na malipo yake. Maana ni kuwa kafiri anaitakidi akiwa duniani kwamba yeye ataokoka na adhabu ya Mwenyezi Mungu kutokana na amali njema aliyoifanya, lakini atakaposimama mbele ya Mwenyezi Mungu ili aangalie hisabu, hatapata kitu katika vile alivyoviwazia; bali atakuta dhambi, hisabu na adhabu. Matumaini yote yatayeyuka, kama yalivyoyeyuka ya yule aliyetegemea mangati.
Au ni kama giza katika bahari kuu, iliyofunikwa na mawimbi juu ya mawimbi na juu yake yapo mawingu. Giza juu ya giza. Akiutoa mkono wake anakurubia asiuone.
Bahari kuu ni bahari yenye maji mengi, mawimbi yamepandana na juu yake kuna mawingu mazito. Huu ni mfano fasaha zaidi wa watu wenye matamanio ambao wamezama katika bahari ya maovu na machafu: uongo, riya, mifundo, majisifu, kiburi, tamaa, pupa na mengineyo yasiyokuwa na kikomo. Mwenye kuishi katika giza hili ambalo haoni kitu, ataona vipi hakika na kuielewa.
Na ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia kuwa na nuru, basi huyo hana nuru.
Tabrasi amesema: "Makusudio ni ambaye Mwenyezi Mungu hakumjaalia wokovu katika akhera, basi hana uokovu." Tuonavyo sisi ni kuwa wale ambao hawaongoki kwenye njia ya haki aliyowapa muongozo Mwenyezi Mungu, basi wao wataishi katika kuzubaa, ujinga na upotevu.
Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu vinamtaksa vilivyomo mbinguni na ardhini na ndege wakikunjua mbawa zao? Kila mmoja amekwishajua Swala yake na tasbihi yake. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa wayatendayo.
Umepita mfano wake katika Juz. 15 (17:44).
Na ni wa Mwenyezi Mungu ufalme wa mbingu na ardhi, kwa sababu ndiye aliyeziumba na muumba ni mfalme wa kweli.
Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya hisabu na malipo.
أَلَمْ تَرَ أَنَّ اللَّـهَ يُزْجِي سَحَابًا ثُمَّ يُؤَلِّفُ بَيْنَهُ ثُمَّ يَجْعَلُهُ رُكَامًا فَتَرَى الْوَدْقَ يَخْرُجُ مِنْ خِلَالِهِ وَيُنَزِّلُ مِنَ السَّمَاءِ مِن جِبَالٍ فِيهَا مِن بَرَدٍ فَيُصِيبُ بِهِ مَن يَشَاءُ وَيَصْرِفُهُ عَن مَّن يَشَاءُ يَكَادُ سَنَا بَرْقِهِ يَذْهَبُ بِالْأَبْصَارِ ﴿٤٣﴾
43. Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatanisha pamoja, kisha huyafanya mrundo? Basi utaona mvua ikitokea kati yake. Na huteremsha kutoka mbinguni, kwenye milima ya mawingu, mvua ya mawe, akamsibu nayo amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye. Hukurubia mmemetuko wa umeme wake kupofua macho.
يُقَلِّبُ اللَّـهُ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَعِبْرَةً لِّأُولِي الْأَبْصَارِ ﴿٤٤﴾
44. Mwenyezi Mungu hubadilisha usiku na mchana. Hakika katika hilo kuna mazingatio kwa wenye busara.
وَاللَّـهُ خَلَقَ كُلَّ دَابَّةٍ مِّن مَّاءٍ فَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَىٰ بَطْنِهِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَىٰ رِجْلَيْنِ وَمِنْهُم مَّن يَمْشِي عَلَىٰ أَرْبَعٍ يَخْلُقُ اللَّـهُ مَا يَشَاءُ إِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ ﴿٤٥﴾
45. Na Mwenyezi Mungu amemuumba kila mnyama kutokana na maji. Wengine katika wao huenda kwa matumbo, na wengine huenda kwa miguu miwili na wengine huenda kwa minne. Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
لَّقَدْ أَنزَلْنَا آيَاتٍ مُّبَيِّنَاتٍ وَاللَّـهُ يَهْدِي مَن يَشَاءُ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٤٦﴾
46. Hakika tumeteremsha Ishara zinazobainisha. Na Mwenyezi Mungu humuongoza atakaye kwenye njia iliyonyooka.
Aya 43 – 46
Je, huoni kwamba Mwenyezi Mungu huyasukuma mawingu, kisha huyaambatanisha pamoja, kisha huyafanya mrundo. Basi utaona mvua ikitokea kati yake. Na huteremsha kutoka mbinguni, kwenye milima ya mawingu, mvua ya mawe.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) hupeleka upepo unoasukuma mawingu kutoka mji mmoja hadi mwingine, kisha huyakusanya pamoja yakiwa mrundo kwa umbo la mlima. Kwenye mawingu haya kunakuwa na maji yanayomiminika na yanayoganda katika vipande vya theluji ambavyo ndivo vinavyoitwa mvua ya mawe.
Akamsibu nayo amtakaye na akamuepusha nayo amtakaye.
Mwenyezi Mungu kutumia mvua ya mawe kwa mujibu wa hekima. Ikiwa hekima imepitisha kuangamia mimea au kitu chochote, basi huipelekea mvua; vinginevyo huiepusha.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 13 (13: 12 -13). Huko na sehemu nyingine zinazonasibiana nazo tumeeleza kuwa dhahiri ya ulimwengu inategemea sababu zake za kimaumbile moja kwa moja na zinakomea kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kuwa ndiye muumba wa ulimwengu na vilivyomo ndani yake.
Hukurubia mmemetuko wa umeme wake kupofua macho.
Umeme wake ni wa hayo mawingu. Mahali pengine Mwenyezi Mungu anasema: "Unakurubia umeme kunyakua macho yao." Juz. 1 (2:20).
Mwenyezi Mungu hubadilisha usiku na mchana, kwa urefu na ufupi.
Hakika katika hilo la kubadilishakuna mazingatio kwa wenye busara, ambao hawagandi tu kwenye sababu za maumbile, bali wanamtafuta aliyezifanya na kuzitengeneza na kumtambua.
Na Mwenyezi Mungu amemuumba kila mnyama kutokana na maji. Wengine katika wo huenda kwa matumbo, na wengine huenda kwa miguu miwili na wengine huenda kwa minne.
Hakika uweza wa Mwenyezi Mungu na umoja una ushahidi mwingi usiokuwa na idadi. Miongoni mwao ni ule unajitokeza katika kuumba vitu vilivyoganda, tunayoyashuhudia katika uumbaji mimea, wanyama na wanaotembea ardhini.
Hayo ndiyo yaliyoashiriwa katika Aya hii. Tukiangalia mfungamano wa maji katika kutengenezwa mnyama ni kuwa hakika ya maji ni moja, lakini wanyama walioumbwa kutokana na maji hayo wanatofautiana, wengine wanatembea kwa tumbo, kama wale wanaotambaa, wengine wanatembea kwa miguu miwili, kama binadamu na wengine kwa miguu mine, kama ngamia nyumbu wanyama mwitu na wengineo ambao Mwenyezi Mungu amewaashiria kwa kauli yake:
Mwenyezi Mungu huumba ayatakayo. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu.
Wanyama wote, kuanzia aina ndogo hadi kubwa, wako kwenye nidhamu kamili, ambapo kila mmoja anafanya kuliangana na inavyoafikiana na maslahi yake. Hii ni dalili mkataa kwamba nyuma ya yote hayo kuna mpangaji aliye hodari na mwenye hekima.
Hakika tumeteremsha Ishara zinazobainisha.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) ameleta dalili za kuweko kwake, ukuu wake na umoja wake; kama hizi za kuumba aina mbalimbali za wanyama. Hakuacha udhuru wowote kwa mwenye kutafuta sababu. Imam Ali(a.s) anasema:"Amewabunia umbile la ajabu katika vyenye uhai na visivyokuwa na uhai na vilivyotulia na vyenye harakati, akaweka ushahidi na ubainifu katika utovu wa utengenezaji wake na ukuu wa cheo chake, kiasi cha akili kuweza kumfuata na kumkubali na kusalimu amri kwake."
Na Mwenyezi Mungu humuongoza atakaye kwenye njia iliyonyooka.
Hakuna shaka kwamba mwenye kufuata njia iliyonyooka ambayo Mwenyezi Mungu ameiamrisha basi huyo ameongoka mbele ya Mwenyezi Mungu. Lakini mwenye kuasi amri yake Mwenyezi Mungu Mtukufu, huyo amepotea kwa Mungu na kwa watu wote, hilo halina shaka.
وَيَقُولُونَ آمَنَّا بِاللَّـهِ وَبِالرَّسُولِ وَأَطَعْنَا ثُمَّ يَتَوَلَّىٰ فَرِيقٌ مِّنْهُم مِّن بَعْدِ ذَٰلِكَ وَمَا أُولَـٰئِكَ بِالْمُؤْمِنِينَ ﴿٤٧﴾
47. Na wanasema tumeamini Mwenyezi Mungu na Mtume na tumetii. Kisha kikundi katika hao hugeuka baada ya hayo. Wala wao si wenye kuamini.
وَإِذَا دُعُوا إِلَى اللَّـهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ إِذَا فَرِيقٌ مِّنْهُم مُّعْرِضُونَ ﴿٤٨﴾
48. Na wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili awahukumu baina yao, ndipo kikundi kimoja kinakataa.
وَإِن يَكُن لَّهُمُ الْحَقُّ يَأْتُوا إِلَيْهِ مُذْعِنِينَ ﴿٤٩﴾
49. Na ikiwa haki ni yao wanamjia kwa kutii.
أَفِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ أَمِ ارْتَابُوا أَمْ يَخَافُونَ أَن يَحِيفَ اللَّـهُ عَلَيْهِمْ وَرَسُولُهُ بَلْ أُولَـٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ ﴿٥٠﴾
50. Je, wana maradhi katika nyoyo zao au wanaona shaka au wanahofia kuwa atawadhulumu Mwenyezi Mungu na Mtume wake? Bali wao ndio madhalimu.
إِنَّمَا كَانَ قَوْلَ الْمُؤْمِنِينَ إِذَا دُعُوا إِلَى اللَّـهِ وَرَسُولِهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ أَن يَقُولُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿٥١﴾
51. Haiwi kauli ya waumini wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ila ni kusema: Tumesikia na tumetii. Na hao ndio wenye kufaulu.
وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَيَخْشَ اللَّـهَ وَيَتَّقْهِ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَائِزُونَ ﴿٥٢﴾
52. Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakamwogopa Mwenyezi Mungu na wakamcha, basi hao ndio wenye kufuzu.
وَأَقْسَمُوا بِاللَّـهِ جَهْدَ أَيْمَانِهِمْ لَئِنْ أَمَرْتَهُمْ لَيَخْرُجُنَّ قُل لَّا تُقْسِمُوا طَاعَةٌ مَّعْرُوفَةٌ إِنَّ اللَّـهَ خَبِيرٌ بِمَا تَعْمَلُونَ ﴿٥٣﴾
53. Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwa ukomo wa viapo vyao ya kwamba ukiwaamrisha, hakika watatoka. Sema: msiape! Utiifu unajulikana. Hakika Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.
قُلْ أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ فَإِن تَوَلَّوْا فَإِنَّمَا عَلَيْهِ مَا حُمِّلَ وَعَلَيْكُم مَّا حُمِّلْتُمْ وَإِن تُطِيعُوهُ تَهْتَدُوا وَمَا عَلَى الرَّسُولِ إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿٥٤﴾
54. Sema: mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Kama mkikengeuka basi yaliyo juu yake ni aliyobebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyobebeshwa. Na mkimtii yeye mtaongoka na hapana juu ya mtume ila kufikisha (ujumbe) wazi wazi.
Aya 47 – 54
Na wanasema tumeamini Mwenyezi Mungu na Mtume na tumetii. Kisha kikundi katika hao hugeuka baada ya hayo. Wala wao si wenye kuamini.
Ambao husema tumeamini na tumetii, wako aina tatu: Ya kwanza, ni wale wanaosema kwa ulimi yale wanayoyaamini, kuyakubali moyoni na kufanya kwa mujibu wake. Hawa sio waliokusudiwa kwenye Aya tuliyo nayo.
Aina ya pili, ni wale wanaosema na kuamini, lakini wanaasi wala hawatendi kwa mujibu wake; yaani wanamini kinadharia sio kimatendo.
Aina ya tatu, ni wale wanaosema kwa ndimi zao yale ambayo hayamo nyoyoni mwao kabisa. Hawa ndio wanafiki.
Aya tuliyo nayo inahusu aina ya pili na ya tatu; wala haihusiki na wanafiki tu; kama ilivyosemekana. Kwa sababu imani bila matendo haina faida yoyote, kwa dalili ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Basi mtu haitamfaa imani yake ambaye hakuamini zamani au hakuchuma kheri kwa imani yake" Ju. 8 (6:158).
Na wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake ili awahukumu baina yao, ndipo kikundi kimoja kinakataa.
Wafasiri wengi wanasema kuwa kulitokea ugomvi wa ardhi baina ya mnafiki mmoja na Yahudi. Mnafiki akasema tukaamuliwe kwa Ka'bul-akhbar, Myahudi, kwa kujua kuwa anakubali rushwa. Myahudi akamwambia tukahukumiwe kwa Muhammad kwa kujua kuwa hakubali rushwa. Lakini mnafiki alikataa. Ndio ikashuka Aya hii. Ni sawa iwe riwaya ni sahihi au la, lakini inafafanua zaidi tafisiri ya Aya.
Na ikiwa haki ni yao wanamjia kwa kutii.
Wao hawaijui haki ila ikiafikiana na matamanio yao; kama ikihalifiana nayo basi wanaikana. Huu ndio ubinafsi ambao hauhusiki na wanafiki tu; isipokuwa uko katika maisha ya baadhi ya waumini au wale wanaojiita waumin. Wanadai kuwa wanaidhihirisha haki na wanipinga batili. Lakini ni haki gani hiyo wanayoidhihirisha na batili gani hiyo wanayoipinga?
Katika ufahamu wao na imani yao, haki ni ile inayoafikiana na masilahi yao na batili ni ile inayohalifiana na masilahi yao. Wao wamejisahau.
Wanaamini kuwa hawatendi isipokuwa haki na hawatamki isipokuwa ukweli, lakini hawapati msukumo wa hilo, isipokuwa kwa msukumo wa hawaa na masilahi yao.
Hawa wana hali mbaya zaidi kuliko wanafiki ambao wanawadanganya watu na hawajidanganyi wao wenyewe. Kwa sababu wana uhakika na uongo wao na riya yao.
Lakini hawa wanafanya uovu wenyewe wakijiona wanafanya wema. Sio siri kusema kuwa wao hawana sifa ya imani. Kwa sababu mumin wa kweli hahadaiki na hila za shetani na ubatilifu wake; bali anajituhumu ikiwa kitendo chake kitampambia sifa. Kwani kazi muhimu ya shetani ni kuwapambia watu matendo yao maovu, kuwaonyesha batili kuwa ni haki na upotevu kuwa ni unyoofu.
Inasemekana kuwa mtu mmoja alimwambia Iblisi: "Wewe huwawezi waumini mfano wangu." Ibilisi akacheka na kumwambia maneno yako haya tayari yanaonyesha umekwishaingia kwenye mtego. Ghururi yako hii ni mtekelezaji aliyeingia moyoni mwako, akauharibu na akaupofusha mpaka ukawa hauna hisia.
Baada ya hayo! Mwenye kutaka kuijaribu imani na dini yake, inatakikana aangalie kuwa je, anaituhumu nafsi yake au anaiona ni safi isiyokuwa na kasoro? Je, anaikubali haki hata kama ni dhidi yake? Ikiwa atajituhumu na kuikubali haki kwa namna yoyote itakayokuwa basi yeye ni katika waumini, vinginevyo atakuwa katika walioangamia.
Je, wana maradhi katika nyoyo zao au wanaona shaka au wanahofia kuwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake watawadhulumu? Bali wao ndio madhalimu.
Walikataa kuhukumiwa kwa Mtume; wala hakuna lililopelekea hilo ila chuki yao kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu au kuutilia shaka utume wake au kuhofia kuwa atawadhulumu. Sababu yoyote itakayokuwa, lakini hakatai hukumu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) isipokuwa kafiri au aliyeidhulumu nafsi yake na ya mwingine.
Haiwi kauli ya waumini wanapoitwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ila ni kusema: Tumesikia na tumetii. Na hao ndio wenye kufaulu.
Baada ya Mwenyezi Mungu (s.w.t) kutaja wanafiki na kwamba wao wana- jizuia kuiendea mahakama ya Mtume wanapoitwa huko, sasa anataja waumini, kwamba ni wale wanaomwitikia kila atakayewapa mwito wa kwenda kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wanaitikia mwito wake kwa unyenyekevu na utiifu. Hawa ndio wanachama wa Mwenyezi Mungu"Hakika wanachama wa Mwenyezi Mungu ndio wenye kufanikiwa." (58:22)
Na wenye kumtii Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakamwogopa Mwenyezi Mungu na wakamcha, basi hao ndio wenye kufuzu kwa kupata radhi za Mwenyezi Mungu na pepo yake.
Kuunganisha hofu na uchaji kwenye utiifu, ni kwa upande wa kuunganisha kitafsiri. Kwa sababu mwenye kumtii Mwenyezi Mungu atakuwa amemuhofia na kumcha. Lakini wafasiri hawakukubali ila kutafoutisha baina ya matendo haya. Wakasema: kumtii Mwenyezi Mungu kunakuwa katika aliyoyaamrisha na kuyakataza, kumhofia kunakuwa katika maasi na kumcha kunakuwa katika yatakayokuja.
Na waliapa kwa Mwenyezi Mungu kwa ukomo wa viapo vyao ya kwamba ukiwaamrisha, hakika watatoka.
Walioapa ni wanafiki. Wao waliaapa kwa kiapo cha nguvu kwamba Mtume akiwaamrisha waache majumba yao na mali zao basi watamsikiliza na kumtii, ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawakemea na imani yao hiyo ya uongo kwa kusema:
Sema: msiape! Utiifu unajulikana. Hakika Mwenyezi Mungu ana habari za mnayoyatenda.
Yaani ewe Muhammad! Waambie wanafiki, msiape kwani Mwenyezi Mungu anajua kuwa utiifu wenu huu ni wa uongo na wa kujionyesha (ria) na kwamba nyinyi ni maadui wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na amewaandalia adhabu chungu mnayostahiki.
Sema: Mtiini Mwenyezi Mungu na Mtume wake kwa dhahiri na batini, sio kwa unafiki na ria. Kama mkikengeuka basi yaliyo juu yake ni aliyobebeshwa, na yaliyo juu yenu ni mliyobebeshwa.
Wanaambiwa wanafiki, na yaliyo juu yake ni juu yake Mtume. Maana ni kuwa Mtume ni mwenye kukalifiwa kufikisha na nyinyi ni wenye kukalifiwa kutii. Atakayepuuza basi hisabu ya kupuuza itakuwa ni yake; ni sawa awe ni Mtume au yule aliyetumiwa Mtume.
Na mkimtii yeye mtaongoka na hapana juu ya mtume ila kufikisha (ujumbe) wazi wazi. Mwenye kutekeleza aliyokalifishwa, basi malipo yake yako kwa Mwenyezi Mungu.
Mtume amekwishafikisha na kutekeleza wajibu wake, yaliyobaki, kazi kwenu.
11
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
وَعَدَ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَيَسْتَخْلِفَنَّهُمْ فِي الْأَرْضِ كَمَا اسْتَخْلَفَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ وَلَيُمَكِّنَنَّ لَهُمْ دِينَهُمُ الَّذِي ارْتَضَىٰ لَهُمْ وَلَيُبَدِّلَنَّهُم مِّن بَعْدِ خَوْفِهِمْ أَمْنًا يَعْبُدُونَنِي لَا يُشْرِكُونَ بِي شَيْئًا وَمَن كَفَرَ بَعْدَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْفَاسِقُونَ ﴿٥٥﴾
55. Mwenyezi Mungu amewaahidi wale ambao wameamini na wakatenda mema kuwa hakika atawafanya makhalifa katika ardhi, kama alivyowafanya waliokuwa kabla yao. Na kwa yakini atawaimarishia dini yao aliyowapendelea na hakika atawabadilishia amani baada ya hofu yao. Wawe wananiabudu, hawanishirikishi. Na mwenye kukufuru baada ya hayo, basi hao ndio mafasiki.
وَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ وَآتُوا الزَّكَاةَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٥٦﴾
56. Na simamisheni Swala na toeni Zaka na mtiini Mtume ili mpate kurehemiwa.
لَا تَحْسَبَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا مُعْجِزِينَ فِي الْأَرْضِ وَمَأْوَاهُمُ النَّارُ وَلَبِئْسَ الْمَصِيرُ ﴿٥٧﴾
57. Usiwadhanie waliokufuru kwamba watashinda na makazi yao ni motoni na hakika ni marejeo maovu.
Aya 55 – 57
Mwenyezi Mungu amewaahidi wale ambao wameamini na wakatenda mema kuwa hakika atawafanya makhalifa katika ardhi, kama alivyowafanya waliokuwa kabla yao.
Dhahiri ya Aya inafahamisha kuwa umma wowote utakaomwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, ukashikana na sharia yake, basi Mwenyezi Mungu atawafanya makhalifa na kuwaimarisha ardhini. Hilo ni hakika.
Baadhi ya wafasiri wamechukua hakika hii, kisha wakafafanua na kufasiri maana ya imani na matendo mema. Wakayawekea mipaka yake na maelezo yake. Ama sisi tuko pamoja na wale waliosema kuwa makusudio ya Aya ni Mtume na maswahaba. Kwani wao walipata tabu na udhia mwingi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kabla na baada ya Hijra. Washirikina na mayahudi kwa pamoja waliwalenga kwa mishale yao.
Hadi kufikia mwaka wa ushindi, walikuwa huko Madina hawawezi kupambazukiwa au kuchwelewa na jua bila ya kushika silaha. Mpaka mmoja wao akasema, kama ilivyo katika tafsir At-Tabari: Hakuna siku tutakayokuwa na amani na kuweka chini silaha yetu. Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) akamwambia: 'Hamtakuwa na wepesi (mpaka ikifika ile siku) atakapokuwa mtu anakaa bila ya silaha. Ahadi ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake ikathibitika.
Hazikupita siku, ikawa wanaishi katika amani ya nafsi zao na mali zao, wakatawala nchi zote za urabuni na kuchukua miji mingi ya Ulaya ya mashariki na magaharibi.
Na kwa yakini atawaimarishia dini yao aliyowapendelea.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) anaishiria kuenea Uislamu na utawala wake mashariki mwa ardhi na magharibi yake.
Na hakika atawabadilishia amani baada ya hofu yao.
Hii ndio natija ya kuvumila, kuwa na subira na kumtegemea Mwenyezi Mungu. Yamepita maelezo yake kwa ufafanuzi zaidi katika Juz. 9 (8:26)
Wawe wananiabudu, hawanishirikishi.
Shirki haihusiki na kuabudu masanamu peke yake. Atakayemtii kiumbe katika kumuasi Mungu basi huyo yuko katika hukumu ya shirki.
Na mwenye kukufuru baada ya hayo ya kuwa khalifa, kuimarishwa kati- ka ardhi na kuwa na amani baada hofu,basi hao ndio mafasiki na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu mafasiki.
Na simamisheni Swala na toeni Zaka na mtiini Mtume ili mpate kurehemiwa.
Huu ni ubainifu na tafsiri ya kauli yake Mwenyezi Mungu katika Aya iliyopita. 'Wale ambao wameamini na wakatenda mema.
Usiwadhanie waliokufuru kwamba watashinda na makazi yao ni motoni na hakika ni marejeo maovu.
Anaambiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) kwa lengo la kumhadharisha anayeuhalifu ujumbe wake na akaupinga. Vile vile yeye ni tishio kwa kila mwenye kubadili neema ya Mwenyezi Mungu kuwa kufuru. Katika Nahjul-balagha imeelezwa: "Uchache wa kulazimiana kwenu na Mwenyezi Mungu ni kutotumia neema zake kwa kumuasi."
Katika Juz.1 (2:23 - 25) kifungu cha 'Siri ya muujiza wa Qur'an,' tulieleza kauli za maulama kuhusu muujiza wa Qur'an. Katika Juz. 3 (3:61) tulisema kwamba kuwa tayari Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) na maapizano kwa kutegemea ushindi ambao umeelezewa na Qur'an na ukawa, ni dalili kubwa ya ukweli wa Qur'an na yule aliyeletewa.
Katika Juz. 6 (5:53) tulieleza kwamba Qur'an ilivyofichua tabia ya mayahudi kwamba wao lau watakuwa na utawala wangefanya kama wafanyavyo leo huko Palestin, ni dalili mkataa ya muujiza wa Qur'an; ambapo yamethibitika hayo baada ya kuyatolea habari kwa zaidi ya miaka elfu moja na mia tatu iliyopita.
Hivi sasa sisi tunapofasiri Aya hii tuliyo nayo 'Mwenyezi Mungu amewaahidi…' tumegundua njia nyingine ya muujiza wa Qur'an. Nayo ni kuwa matamshi ya Qur'an ni ya kiarabu ambayo wameyatumia waarabu katika mazungumzo na maandishi, kabla ya Qur'an na baada yake, bila ya tofau- ti ya herufi au mfumo wa jumla, lakini pamoja na hayo, jumla kwenye Qur'an inabeba maana nyingi, jambo ambalo halipatikani pengine pasipokuwa kwenye Qur'an; hata Hadith pia.
Ndio maana Imam Ali(a.s ) akamwambia Ibn Abbas:"Usigombane na makhawarij kwa Qur'an, kwa sababu Qur'an inachukua sana njia mbalimbali, utasema na wao watasema, lakini wahoji kwa Hadith, hawatakuwa na njia ya kutokea"
Siri katika hilo inakuwa katika upeo wa mwenye kunena sio wa maneno yenyewe. Vinginevyo mfumo wa Qur'an na isiyokuwa Qur'an ungekuwa mmoja tu. Hakika maneno yameganda hayana uhai. Msemaji ndiye anayeyapa uhai. Ndio maana kukawa na tofauti ya uhai wa maneno kulingana na msemaji mwenyewe.
Atakavyozungumza mataalamu ni tofauti na atakavyozungumza mtu wa kawaida, hata kama maneno na jumla zitakuwa sawa. Hata Qur'an pia ufahamu wake unatofautiana kulingana na anayeisoma. Vile vile maneno yoyote yanatofautiana kulingana na anayesema akiwa mnafiki au mwenye ikhlasi.
Kwa hiyo upeo mkubwa wa Qur'an kwa njia mbalimbali ni dalili mkataa kuwa inatokana na ambaye elimu yake imeenea kwenye kila kitu.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِيَسْتَأْذِنكُمُ الَّذِينَ مَلَكَتْ أَيْمَانُكُمْ وَالَّذِينَ لَمْ يَبْلُغُوا الْحُلُمَ مِنكُمْ ثَلَاثَ مَرَّاتٍ مِّن قَبْلِ صَلَاةِ الْفَجْرِ وَحِينَ تَضَعُونَ ثِيَابَكُم مِّنَ الظَّهِيرَةِ وَمِن بَعْدِ صَلَاةِ الْعِشَاءِ ثَلَاثُ عَوْرَاتٍ لَّكُمْ لَيْسَ عَلَيْكُمْ وَلَا عَلَيْهِمْ جُنَاحٌ بَعْدَهُنَّ طَوَّافُونَ عَلَيْكُم بَعْضُكُمْ عَلَىٰ بَعْضٍ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٥٨﴾
58. Enyi ambao mmeamini! Na wawatake ruhusa, wale ambao imewamiliki mikono yenu ya kuume na wale ambao hawajafikia baleghe miongoni mwenu, mara tatu kabla ya Swala ya Alfajiri na wakati mnapovua nguo zenu adhuhuri, na baada ya Swala ya Isha. Ni nyakati tatu za faragha kwenu. Si vibaya kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi, kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowabainishia Aya; na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
وَإِذَا بَلَغَ الْأَطْفَالُ مِنكُمُ الْحُلُمَ فَلْيَسْتَأْذِنُوا كَمَا اسْتَأْذَنَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمْ آيَاتِهِ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿٥٩﴾
59. Na watoto wanapofikia kubaleghe basi na watake ruhusa, kama walivyotaka ruhusa wa kabla yao. Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowabainishia Aya; na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
وَالْقَوَاعِدُ مِنَ النِّسَاءِ اللَّاتِي لَا يَرْجُونَ نِكَاحًا فَلَيْسَ عَلَيْهِنَّ جُنَاحٌ أَن يَضَعْنَ ثِيَابَهُنَّ غَيْرَ مُتَبَرِّجَاتٍ بِزِينَةٍ وَأَن يَسْتَعْفِفْنَ خَيْرٌ لَّهُنَّ وَاللَّـهُ سَمِيعٌ عَلِيمٌ ﴿٦٠﴾
60. Na wanawake wakongwe ambao hawatarajii kuolewa, si vibaya kwao kupunguza nguo zao bila ya kuonyesha mapambo. Na kama wakistahi ni bora kwao. Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.
Aya 58 – 60
Enyi ambao mmeamini! Na wawatake ruhusa, wale ambao imewamiliki mikono yenu ya kuume na wale ambao haijafikia baleghe miongoni mwenu, mara tatu.
Iliyowamiliki mikono ni watumwa.
Kwenye Sura hii katika Aya ya 27, Mwenyezi Mungu (s.w.t) amekataza kuingia nyumba za wengine bila ya kubisha hodi. Katika Aya ya 28, akaamrisha kurudi ikiwa mtu hakuitikiwa hodi. Katika Aya 31 akawakataza wanawake kujiweka wazi; isipokuwa kwa baadhi ya ndugu, watumwa, wasiokuwa na matamanio na waototo wadogo wasiopambanua uchi na kitu kingine.
Katika Aya hii tuliyo nayo Mwenyezi Mungu (s.w.t) anasema waamrisheni watumwa wenu na watoto wadogo ambao hawajafikia baleghe, wabishe hodi, kabla ya kuingia kwenu, katika nyakati tatu. Kwa sababu ni nyakati za faragha ya mtu kujiweka uchi. Hizo nyakati tatu ni:
1.Kabla ya Swala ya Alfajiri, ambapo mtu anaamka kutoka usingini akiwa na nguo za kulalia.
2.Na wakati mnapovua nguo zenu adhuhuri; yaani wakati wa kulala kidogo mchana (qaylula) na kupumzika kwa sababu mtu anapunguza nguo zake.
3.Na baada ya Swala ya Isha, ambapo watu wanaelekea kwenye mambo yao mahususi.
Ni nyakati tatu za faragha kwenu.
Huu ni ubainfu wa kutofautisha nyakati hizo tatu na nyingine na kubainisha sababu za kupiga hodi, kwamba ni wakati wa faragha wa mtu kuvua nguo.
Si vibaya kwenu wala kwao baada ya nyakati hizi.
Hakuna dhambi kwenu enyi waumini wala kwa watumwa na watoto baada ya nyakati hizi kuingia bila ya idhini, katika nyakati zisizokuwa hizi.
Kuzungukiana nyinyi kwa nyinyi.
Yaani kuwazunguikia wao, na wao kuwazungukia nyinyi. Kila mmoja anamuhitajia mwingine.
Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowabainishia Aya, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
Amewabainishia hukumu hizi na akawaamrisha kulazimiana nazo ili muwe na adabu kwa elimu yake na hekima yake.
Na watoto wanapofikia kubaleghe basi na watake ruhusa, katika nyakati zote, sio katika nyakati tatu. Kwa sababu ruhusa hii ya nyakati tatu ni kwa wale ambao hawajafikia kubaleghe. Ama wale ambao wame- baleghe hawana tofauti na wengine walio wakubwa. Haya ndio maana ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
Kama walivyotaka ruhusa wa kabla yao.
Yaani kama ilivyo wajibu kuomba ruhusa kwa wakubwa wakati wote, vile vile ni wajibu kwa aliyefikia baleghe bila ya kutofautisha. Mvulana anakuwa baleghe kwa kutoa mbegu za uzazi au kufikisha miaka 15. Msichana anakuwa baleghe kwa kutoka hedhi au kushika mimba au kufik- isha miaka 9 kwa uchache. Wengine wanasema ni miaka 15.
Hivyo ndivyo Mwenyezi Mungu anavyowabainishia Aya, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi, Mwenye hekima.
Sisi hatujui wajihi wa kukaririka huku, kulikokuja moja kwa moja bila ya kuingia kati Aya nyingine, isipokuwa kutilia mkazo na kuhimiza amri ya kupiga hodi.
Na wanawake wakongwe ambao hawatarajii kuolewa.
Hawa ni wanawake waliokoma kutoka hedhi na kuzaa wakawa ni wazee wasiokuwa na matamanio ya wanaume wala wanaume pia hawawatamani.
Si vibaya kwao kupunguza nguo zao bila ya kuonyesha mapambo.
Hakuna ubaya kwa bibi kikongwe kuvua nguo zake za nje ambazo anazi- vaa barabarani na sokoni, lakini asikusudie kwa hilo kujionyesha kwa wanaume ili wamwangalie, hata kama yeye si wa wanaume, lakini huenda akatokea atakayesema: Huyu enzi zake!
Na kama wakistahi ni bora kwao.
Ni bora kwa bibi kikongwe, kutopunguza nguo zake kwa watu kando, hata kama ameruhusiwa kufanya hivyo. Kwa sababu hilo liko mbali na tuhuma. Kuna Hadith isemayo: "Acha lisilo na ubaya kwa kuhadhari lilo na ubaya."
Na Mwenyezi Mungu ni Msikizi, Mjuzi.
Anasikia kauli na anajua yanayotia wasiwasi katika nyoyo.
لَّيْسَ عَلَى الْأَعْمَىٰ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْأَعْرَجِ حَرَجٌ وَلَا عَلَى الْمَرِيضِ حَرَجٌ وَلَا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ أَن تَأْكُلُوا مِن بُيُوتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ آبَائِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أُمَّهَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ إِخْوَانِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخَوَاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَعْمَامِكُمْ أَوْ بُيُوتِ عَمَّاتِكُمْ أَوْ بُيُوتِ أَخْوَالِكُمْ أَوْ بُيُوتِ خَالَاتِكُمْ أَوْ مَا مَلَكْتُم مَّفَاتِحَهُ أَوْ صَدِيقِكُمْ لَيْسَ عَلَيْكُمْ جُنَاحٌ أَن تَأْكُلُوا جَمِيعًا أَوْ أَشْتَاتًا فَإِذَا دَخَلْتُم بُيُوتًا فَسَلِّمُوا عَلَىٰ أَنفُسِكُمْ تَحِيَّةً مِّنْ عِندِ اللَّـهِ مُبَارَكَةً طَيِّبَةً كَذَٰلِكَ يُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ ﴿٦١﴾
61. Si vibaya kwa kipofu, wala kwa kiguru, wala kwa mgonjwa, wala kwenu nyinyi, mkila kwenye nyumba zenu, au nyumba za baba zenu au nyumba za mama zenu au nyumba za kaka zenu, au nyumba za dada zenu, au nyumba za ami zenu, au nyumba za shangazi zenu, au nyumba za wajomba zenu, au nyumba za khalati zenu, au za mliowashikia funguo zao au rafiki yenu. Si vibaya kwenu mkila pamoja au mbali mbali. Na mkiingia katika nyumba mjitolee salaam. Ni maamkuzi kutoka kwa Mwenyezi Mungu yenye baraka yaliyo mema. Hivyo ndivyo anavyowabainishia Mwenyezi Mungu Aya zake mpate kutia akilini.
Aya 61
Wanaombiwa katika neno 'Mliowashikia' ni walio na utawala kwenye mali kwa usimamizi, wasiya au wakala. Maana ya dhairi ya Aya ni kuwa hakuna ubaya kwa kipofu, kiguru, mgonjwa na wengineo kula bila ya kuomba ruhusa, kwenye majumba ya ndugu zao waliotajwa, wakiwa pamoja na wenye nyumba au peke yao. Vile vile si vibaya kwa wakili kula kwa wema mali aliyowakilishwa; kama ambavyo si vibaya kwa rafiki kula nyumbani kwa rafiki yake.
Wote hawa wanaweza kula katika majumba haya kwa sharti la kutojua kuwa wenyewe hawataki. Mafakihi wengi wanasema anayoruhusa ya kula matunda, saladi au chakula kilichokwishaandaliwa, lakini sio kile ambacho kimewekwa akiba.
Unaweza kuuliza kuwa : neno 'Wala kwenu nyinyi mkila kwenye nyumba zenu' inafahamisha kuwa mtu anaweza kula nyumbani kwake bila ya kujiomba ruhusa yeye mwenyewe. Maneno hayaendi sawa hapa, itakuwaje?
Jibu : Makusudio yake ni nyumba ya mke na ya mtoto, kutokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu:
جَعَلَ لَكُم مِّنْ أَنفُسِكُمْ أَزْوَاجًا وَمِنَ الْأَنْعَامِ أَزْوَاجًا ﴿١١﴾
"Na amewajaalia mke na mume kutokana na nyinyi wenyewe." (42:11).
Kuna Hadith isemayo:"Chema zaidi anachokula mtu ni chumo lake." Na mtoto ni chumo lake, kutokana na Hadith nyingine isemayo:"Wewe na mali yako ni wa baba yako."
Swali la pili : Kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t) amehusisha kuwataja vipofu walemavu na wagonjwa, na wao wanaingia kwenye neno 'nyinyi wenyewe.' Kwa sababu wanambiwa watu wote. Sasa kwani kuna mtu atakayetia wasiwasi kwa walemavu hao waliotajwa na wagonjwa, kuwa hawafai kula kwenye hizo nyumba?
Kuna kauli nyingi za majibu ya swali hili. Wafasiri wengine wametaja tano. Iliyo karibu zaidi ni ile isemayo kuwa maswahaba walikuwa wakiona uzito kula na vipofu kwa kuwa hawatoweza kuona chakula kinachofaa, wasije wakala mapumba. Na kiguru waliona kuwa atapata tabu ya kukaa na wengine kwa vile chakula kilikuwa kinawekwa chini na mgonjwa naye hawezi kushiriki vizuri kula na wengine, ambapo wenzake watamaliza haraka naye ataona haya kubaki peke yake.
Kwa kuwa maswahaba walikuwa hawali katika majumba haya yaliyotajwa kutokana na Aya isemayo: "Wala msile mali zenu baina yenu kwa batili." Juz.1 (2:88). Ndipo Mwenyezi Mungu akawahalalishia kula kwenye majumba hayo, pamoja na kula na walemavu hao na wagonjwa.
إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ آمَنُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَإِذَا كَانُوا مَعَهُ عَلَىٰ أَمْرٍ جَامِعٍ لَّمْ يَذْهَبُوا حَتَّىٰ يَسْتَأْذِنُوهُ إِنَّ الَّذِينَ يَسْتَأْذِنُونَكَ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ يُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ فَإِذَا اسْتَأْذَنُوكَ لِبَعْضِ شَأْنِهِمْ فَأْذَن لِّمَن شِئْتَ مِنْهُمْ وَاسْتَغْفِرْ لَهُمُ اللَّـهَ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٦٢﴾
62. Hakika waumini ni wale tu ambao wamemwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakiwa pamoja naye kwa jambo la wote, hawaondoki mpaka wamtake ruhusa. Hakika wale wanaokuomba ruhusa, hao ndio wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake. Na watakapokuomba ruhusa kwa baadhi ya mambo yao, mruhusu umtakaye miongoni mwao na uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu; hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa msamaha, Mwenye kurehemu.
لَّا تَجْعَلُوا دُعَاءَ الرَّسُولِ بَيْنَكُمْ كَدُعَاءِ بَعْضِكُم بَعْضًا قَدْ يَعْلَمُ اللَّـهُ الَّذِينَ يَتَسَلَّلُونَ مِنكُمْ لِوَاذًا فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿٦٣﴾
63. Msifanye kumwita Mtume baina yenu kama mnavyoitana nyinyi kwa nyinyi. Hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wale wanoondoka kwa kujificha. Basi na watahadhari wale ambao wanahalifu amri yake, isije ikawapata fitna au ikawapata adhabu chungu.
أَلَا إِنَّ لِلَّـهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ قَدْ يَعْلَمُ مَا أَنتُمْ عَلَيْهِ وَيَوْمَ يُرْجَعُونَ إِلَيْهِ فَيُنَبِّئُهُم بِمَا عَمِلُوا وَاللَّـهُ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ ﴿٦٤﴾
64. Ehee! Hakika ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Hakika yeye anajua mliyo nayo. Na siku watakaporudishwa kwake atawaeleza waliyoyafanya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
Aya 62 – 64
Hakika waumini ni wale tu ambao wamemwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakiwa pamoja naye kwa jambo la wote, hawaondoki mpaka wamtake ruhusa.
Wanafiki walikuwa wakitoroka kwa kujificha kila wanapoitwa kwenye jambo muhimu katika kikao pamoja na Mtume. Ndipo ikashuka Aya hii kubainisha wajibu wa kutiiwa Mtume na umma wake, wajibu wa kusaidiana waislamu ili kuuinua Uislamu na kwamba Mwislamu wa kweli ni yule anayeitikia mwito wa Mtume na kusaidiana kwa pamoja, jambo ambalo lina kheri na masilahi, kwa juhudi zake zote. Wala asikimbie wajibu huu kwa kutafuta visababu.
Akiwa ni mkweli katika udhuru basi auleze kwa Mtume(s.a.w. w ) na amuombe ruhusa. Hali hii ni wajibu kwa kila kiongozi anayetekelea haki za raia kwa ikhlasi.
Hakika wale wanaokuomba ruhusa , wakiwa ni wa kweli katika kauli zao na wana haja ya dharura,hao ndio wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Mtume wake, kikwelikweli. Ama wale ambao wanatafuta visababu vya uongo, basi hao ndio wanafiki wanaosema kwa midomo yale ambayo hayako nyoyoni mwao. Muimin ni kama askari, anangojea amri tu ya kiongozi wake wala haiachi ila kama ana udhuru wa kweli, hapo huomba ruhusa.
Na watakapokuomba ruhusa kwa baadhi ya mambo yao, mruhusu umtakaye miongoni mwao na uwaombee msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa maghufia, Mwenye kurehemu.
Mwenyezi Mungu amemwachia amri Mtume(s.a.w. w ) akitaka atoe ruhusa au akatae, na akamwamrisha kumuombea Mungu yule mkweli mwenye ikhlasi.
Unaweza kuuliza kuwa : Mwenyezi Mungu mahali pengine amesema: "Mwenyezi Mungu amekusamehe! Kwa nini umewapa ruhusa kabla ya kubainika kwako wanaosema kweli na ukawajua waongo?" Juz. 10 (9:43) na kwenye Aya hii amemruhusu kutoa ruhusa, zitaungana vipi Aya hizi?
Jibu : Kule Mwenyezi Mungu alimwamrisha Mtume wake kuthibitisha kuweza kumjua mkweli na muongo. Katika sura hii tuliyo nayo, amem- ruhusu kutoa ruhusa baada ya kujua uhakika wa mwenye kutaka ruhusa, malengo yake na natija ya kutaka idhini awe mumin au mnafiki. Kwa hiyo atatoa ruhusa kwa misingi hii.
Inawezekana ni masilahi kumpa ruhusa mnafiki, ikiwa kubakia kwake kundini kunaleta madhara na pia inawezekana kumnyima ruhusa kukawa na manufaa kwa kuhitajika kwake kundini.
Msifanye kumwita Mtume baina yenu kama mnavyoitana nyinyi kwa nyinyi.
Maneno wanelekezewa wale waliokuwa na Mtume, wakifundishwa adabu wakiwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) ambapo waliamrishwa wanapotaka ruhusu wasimwite kwa majina yake au lakabu yake; mfano kusema: ewe Muhammad au Ewe Abul-Qasim; kama wanavyoitana wao kwa wao.
Bali wamwite kwa sifa zake tukufu, za unabii au utume; kwa mfano kusema: Ewe Nabii wa Mungu au Ewe Mtume wa Mungu! Kwani kumheshimu yeye ndio kumheshimu Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu amekutanisha twaa yake na ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) katika Aya kadha zikiwemo hizi:
فَالَّذِينَ آمَنُوا بِهِ وَعَزَّرُوهُ وَنَصَرُوهُ وَاتَّبَعُوا النُّورَ الَّذِي أُنزِلَ مَعَهُ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿١٥٧﴾
"Basi wale waliomuamini na wakamheshimu na wakamsaidia na wakafuata nuru iliyoteremshwa pamoja naye. Hao ndio wenye kufaulu. Juz.9 (7:157).
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَرْفَعُوا أَصْوَاتَكُمْ فَوْقَ صَوْتِ النَّبِيِّ وَلَا تَجْهَرُوا لَهُ بِالْقَوْلِ كَجَهْرِ بَعْضِكُمْ لِبَعْضٍ ﴿٢﴾
"Enyi ambao mmeamini! Msinyanyue sauti zenu kuliko sauti ya Nabii, wala msiseme naye kwa kelele, kama mnavyosemezana nyinyi kwa nyinyi." (49:2).
Hakika Mwenyezi Mungu anawajua miongoni mwenu wale wanoondoka kwa kujificha.
Yaani kujificha kwa wanafiki wanapotoroka pale wanapoambiwa mambo muhimu, kama jihadi n.k., hakufichiki kwa Mwenyezi Mungu. Baadhi ya mapokezi yanasema kuwa wanafiki walikuwa wakiondoka kwenye vikao vya Mtume(s.a.w. w ) kwa kujiziba na wengine.
Basi na watahadhari wale ambao wanahalifu amri yake isije ikawap- ata fitna au ikawapata adhabu chungu.
Amri yake hapa ni amri ya Mungu na makusudio ya fitna hapa ni balaa duniani. Hii ni hadhari na ahadi ya adhabu duniani na akhera kwa mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake.
Ehee! Hakika ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Hakika yeye anajua mliyo nayo. Na siku watakaporudishwa kwake atawaeleza waliyoyafanya. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi wa kila kitu.
Mwenyezi Mungu hawahitajii walimwengu. Twaa ya mtiifu haimfai chochote, wala uasi wa muasi haumdhuru chochote.
Yeye ni mjuzi wa yanayokuwa nyoyoni na wa siku ambayo watu watakusanyika ndani yake kwa hisabu. Atawapa habari ya matendo yao na makusudio yao na watapata wanayostahiki wala Mola wako hamdhulumu yoyote.
12
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE
Sura Ya Ishirini Na Tano: Surat Al-Furqan.
Imeshuka Makka. Ina Aya 77.
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ
Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu
تَبَارَكَ الَّذِي نَزَّلَ الْفُرْقَانَ عَلَىٰ عَبْدِهِ لِيَكُونَ لِلْعَالَمِينَ نَذِيرًا ﴿١﴾
1. Amekuwa na baraka yule ambaye ameiteremsha Furqani kwa mtumwa wake, ili awe muonyaji kwa walimwengu wote.
الَّذِي لَهُ مُلْكُ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَلَمْ يَتَّخِذْ وَلَدًا وَلَمْ يَكُن لَّهُ شَرِيكٌ فِي الْمُلْكِ وَخَلَقَ كُلَّ شَيْءٍ فَقَدَّرَهُ تَقْدِيرًا ﴿٢﴾
2. Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakufanya mtoto, wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na ameumba kila kitu na akikadiria kipimo.
وَاتَّخَذُوا مِن دُونِهِ آلِهَةً لَّا يَخْلُقُونَ شَيْئًا وَهُمْ يُخْلَقُونَ وَلَا يَمْلِكُونَ لِأَنفُسِهِمْ ضَرًّا وَلَا نَفْعًا وَلَا يَمْلِكُونَ مَوْتًا وَلَا حَيَاةً وَلَا نُشُورًا ﴿٣﴾
3. Na wamechukua badala yake miungu ambayo haiumbi chochote, bali hiyo inaumbwa, haijimilikii dhara wala nafuu, wala haimiliki mauti wala uhai wala kufufuka.
وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا إِنْ هَـٰذَا إِلَّا إِفْكٌ افْتَرَاهُ وَأَعَانَهُ عَلَيْهِ قَوْمٌ آخَرُونَ فَقَدْ جَاءُوا ظُلْمًا وَزُورًا ﴿٤﴾
4. Na wamesema wale ambao wamekufuru: Haikuwa hii ni chochote ila ni uzushi aliouzua, na wamemsaidia haya watu wengine. Basi hakika wamekuja na dhulma na uzushi.
وَقَالُوا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ اكْتَتَبَهَا فَهِيَ تُمْلَىٰ عَلَيْهِ بُكْرَةً وَأَصِيلًا ﴿٥﴾
5. Na wakasema: Hizi ni ngano za wa kale anazoziandikisha anazosomewa asubuhi na jioni.
قُلْ أَنزَلَهُ الَّذِي يَعْلَمُ السِّرَّ فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ إِنَّهُ كَانَ غَفُورًا رَّحِيمًا ﴿٦﴾
6. Sema, ameiteremsha ajuaye siri za mbinguni na ardhini. Hakika Yeye amekuwa ni Mwingi wa msamaha, Mwenye kurehemu.
Aya 1-6
Amekuwa na baraka yule ambaye ameiteremsha Furqani kwa mtumwa wake, ili awe muonyaji kwa walimwengu wote.
Baraka na neema za Mwenyezi Mungu ni nyingi. Katika zilizojitokeza ni hii Qur'an ambayo ameiteremsha kwa mtumwa wake Muhammad(s.a.w. w ) . Kwani inaongoza kwenye msimamo na inatoa onyo la adhabu chungu.
Neno Furqani lina maana ya kufarikisha baina ya haki na batili. Makusudio yake hapa ni Qur'an. Mwenyezi Mungu amemsifu kwa utumwa uliotegemezwa kwake yeye Mungu, kwa sababu ya kumwadhimisha. Kwani aliye adhimu zaidi katika watu ni yule ambaye hamnyenyekei wala kumdhalilikia isipokuwa yule anayestahiki hivyo.
Na dhalili zaidi na mpuzi kuliko watu wote ni yule anayemdhalilikia au kumtukuza asiyekuwa Mwenyezi Mungu. Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (15:1).
Ambaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakufanya mtoto, wala hakuwa na mshirika katika ufalme.
Hii ni kuwarudi warabu wa wakati wa ujahiliya, waliomshirikisha Mwenyezi Mungu na wanaswara waliosema kuwa Masih ni mwana wa Mungu. Njia ya kuwarudi ni kuwa ulimwengu na viliyvomo ndani yake ni miliki ya Mwenyezi Mungu, na anayemilikiwa hawezi kuwa mshirika wa mmliki wala mtoto wake.
Na ameumba kila kitu na akakikadiria kipimo kwa sababu zake, mpangilio wake na nidhamu yake; kwa namna ambayo kitatekeleza wad- hifa wake kwa njia ya ukamilifu. Kimsingi ni kuwa sadfa haina nafasi katika mipangilio, nidhamu na hekima na hawezi kuikimblia isipokuwa mjinga au mwenye inadi.
Na wamechukua badala yake miungu ambayo haiumbi chochote, bali hiyo inaumbwa, haijimilikii dhara wala nafuu, wala haimiliki mauti wala uhai wala kufufuka.
Mambo ya dhahiri yanajulikana na mjuzi na asiyekuwa mjuzi. Kwa maumbile yake mtu, anayatambua tu, bila ya kuhitajia dalili; bali hayo yenyewe ni dalili ya mengine. Miongoni mwa mambo yaliyo wazi ni Mungu. Ni laz- ima awe ni muweza wa kuumba, kunufaisha na kudhuru. Vile vile kuleta uhai, kufisha na kufufua baada ya mauti. Masanamu mnayoyaabudu enyi washirikina hayawezi hayo, basi vipi yanaweza kuwa miungu.
Ilivyokuwa hoja hii inawazima washirikina na kutowapa nafasi ya kukana na kuijadili, walikimbilia kwenye uzushi na wamesema wale ambao wamekufuru:
Haikuwa hii ni chochote ila ni uzushi aliozua, na wamemsaidia haya watu wengine.
Hii wanakusudia Qur'an na aliouzua wanamkusudia Muhammad(s.a.w. w ) .
Qur'an ilipowabana maadui wa haki, walianza kusema kuwa Qur'an imetengenezwa na Muhammad na mkusanyiko wake wa visa unatokana na watu wa kitabu waliomsaidia Muhammad kisha yeye akaipanga kwa ufasaha na kuinasibisha kwa Mwenyezi Mungu, akiwa na lengo la kupata ukubwa na kuwa juu ya watu wote.
Waliozua uzushi huu ndio hasa wapenda makuu, wanaojiweka juu ya watu wote na kuwakandamiza mafukara na wanyonge. Walizua uzushi huu wakiwa na hakika kuwa Muhammad ni mkweli mwaminifu na kwamba Qur'an haifanani na maneno ya binadamu. Hapo mwanzo alishindana nao na kuwaambia walete angalau Sura moja tu inayofanana na Qur'an, lakini wakashindwa.
Ikiwa Muhammad anasaidiwa na watu wa Kitabu, basi wao si ndio wangesaidiwa kwanza na mayahudi, kwa sababu waliungana nao dhidi ya Muhammad na waislamu.
Kwa vile hawana la kufanya, hawana hoja ya kuikabili hoja, sasa wafanyeje, wasalimu amri na kuingia kwenye Uislamu? Wataingiaje Uislamu nao unawamuweka sawa mwinyi wa kiquraishi na mtumwa wa kihabeshi, wala hakuna ubora wa kiumbe juu ya kiumbe mwenzake isipokuwa kwa takua; na unaharamisha dhulma na unyanyasaji, mambo ambayo ndiyo maisha ya wapinzani hawa?
Kwa hiyo basi hakuna nyenzo ya kulinda maisha yao haya isipokuwa uzushi, kusema Muhammad ni mchawi, ni muongo, ni mwendawazimu na kwamba Qur'an ni ngano za watu wa kale alizozikusanya Muhammad kutoka hapa na pale.
Basi hakika wamekuja na dhulma na uzushi.
Wameleta dhulma kubwa kwa Mwenyezi Mungu na Mtume wake na kwa nafsi zao pia. Kwa sababu wameziingiza kwenye maangamizi. Pia wameleta uzushi kuwa Qur'an ni uzushi. Neno dhulma na uzushi linafa- hamisha kwamba wao wamenasibisha uzushi kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) wakiwa wanajijua kuwa wao ni waongo.
Kwa hakika wanavyojasiri leo, maadui wa Uislamu, kusema kuwa chimbuko la Qur'an ni Tawrat na Injil, kumetokana na madhalimu na wazushi waliokuwa wakati wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) na kwamba msukumo wa dhulma hii na kuvunga huku ni kwa aina moja; ambayo ni kuhofia haki kuwafedhehi hawa na wale na kufichua maovu yao.
Na wakasema:Hizi ni ngano za wa kale anazoziandikisha anazosomewa asubuhi na jioni.
Wazushi walipigwa na butwaa wasijue la kufanya. Wakafikiriaje, waeneze uvumi kuwa Muhammad amesoma elimu ya Qur'an kwa mwingine? Lakini ni nani atakayewaamini na watu wote wanajua kuwa Muhammad hasomi wala haandiki (ummiy)?
Ndio wakapata njia nyingine - Qur'an si chochote isipokuwa ni visa vya watu wa kale alivyoandikiwa Muhammad na kusomewa mara kwa mara mpaka akavihifadhi, kisha akavileta kwa mfumo mzuri na kuvitangaza kwa watu kuwa vinatoka kwa Mwenyezi Mungu.
Hivi ndivyo wafanyavyo watu wenye malengo mengine kila wakati. Wanaeneza na kuwazulia watu wema wanaotaka kuleta ukombozi; si kwa lolote ila ni kwa kuhofia chumo lao la kidhalimu, lakini watakimbila wapi? Je, mwangaza wajua unaweza kuzimwa na pumzi za mdomo? Je, uongo unaweza kubadilisha uhakika? Muongo analaaniwa na kila ulimi na atafedheka hata kama atasitiriwa na mapazia elfu.
Sema: ameiteremsha ajuae siri za mbinguni na ardhini.
Sema ewe Muhammad: Hapana! Hii si visa na ngano za watu wa kale, wala haikuchukuliwa kwenye Tawrat na Injil. Ni ilimu na nuru, aliyoiteremsha moyoni mwako ili uwaongoze kwayo, vizazi na vizazi, kwenye haki, heri na uadilifu. Inatoka kwa mwenye hekima, mjuzi wa siri za ulimwengu na yaliyo na masilahi na uharibifu kwa viumbe. Na wewe unawafikishia kutoka kwa Mwenyezi Mungu yale yaliyo na heri yao na shari yao na uokovu wao na maangamizi yao.
Hakika Yeye amekuwa ni Mwingi wa msamaha, Mwenye kurehemu.
Anamrehemu aliyeasi kwa kupuuza, pamoja na kumhadharisha na kumuonya. Wala hamfanyii haraka mkosaji; huenda akarudia kwa Mola wake na kutubia dhambi zake.
Akifanya hivyo atamsamehe yaliyopita; vinginevyo atapata malipo yake na adhabu chungu anayostahiki.
وَقَالُوا مَالِ هَـٰذَا الرَّسُولِ يَأْكُلُ الطَّعَامَ وَيَمْشِي فِي الْأَسْوَاقِ لَوْلَا أُنزِلَ إِلَيْهِ مَلَكٌ فَيَكُونَ مَعَهُ نَذِيرًا ﴿٧﴾
7. Na wakasema: Ana nini Mtume huyu anakula chakula na anatembea masokoni! Mbona hakuteremshiwa malaika awe muonyaji pamoja naye?
أَوْ يُلْقَىٰ إِلَيْهِ كَنزٌ أَوْ تَكُونُ لَهُ جَنَّةٌ يَأْكُلُ مِنْهَا وَقَالَ الظَّالِمُونَ إِن تَتَّبِعُونَ إِلَّا رَجُلًا مَّسْحُورًا ﴿٨﴾
8. Au akaangushiwa hazina, au awe na bustani ale katika hiyo? Na wakasema madhalimu: Hamumfuati ila mtu aliyerogwa.
انظُرْ كَيْفَ ضَرَبُوا لَكَ الْأَمْثَالَ فَضَلُّوا فَلَا يَسْتَطِيعُونَ سَبِيلًا ﴿٩﴾
9. Tazama jinsi wanavyokupigia mfano, basi wamepotea, wala hawataiweza njia.
تَبَارَكَ الَّذِي إِن شَاءَ جَعَلَ لَكَ خَيْرًا مِّن ذَٰلِكَ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ وَيَجْعَل لَّكَ قُصُورًا ﴿١٠﴾
10. Amekuwa na baraka yule ambaye akitaka atakujaalia yaliyo bora kuliko hayo, mabustani yapitayo mito chini yake na akujaalie makasri.
بَلْ كَذَّبُوا بِالسَّاعَةِ وَأَعْتَدْنَا لِمَن كَذَّبَ بِالسَّاعَةِ سَعِيرًا ﴿١١﴾
11. Bali wameikanusha saa. Na tumemwandalia moto mkali mwenye kuikanusha saa.
إِذَا رَأَتْهُم مِّن مَّكَانٍ بَعِيدٍ سَمِعُوا لَهَا تَغَيُّظًا وَزَفِيرًا ﴿١٢﴾
12. Utakapowaona katika mahali pa mbali watasikia hasira yake na mngurumo wake.
وَإِذَا أُلْقُوا مِنْهَا مَكَانًا ضَيِّقًا مُّقَرَّنِينَ دَعَوْا هُنَالِكَ ثُبُورًا ﴿١٣﴾
13. Na watakapotupwa humo, mahali palipo finyu hali wamefungwa, ndipo hapo wataomba mauti.
لَّا تَدْعُوا الْيَوْمَ ثُبُورًا وَاحِدًا وَادْعُوا ثُبُورًا كَثِيرًا ﴿١٤﴾
14. Msiyaombe mara moja bali ombeni mauti mara nyingi
قُلْ أَذَٰلِكَ خَيْرٌ أَمْ جَنَّةُ الْخُلْدِ الَّتِي وُعِدَ الْمُتَّقُونَ كَانَتْ لَهُمْ جَزَاءً وَمَصِيرًا ﴿١٥﴾
15. Sema, je, hayo ni bora au Bustani ya milele, ambayo wameahidiwa wenye takua, iwe kwao malipo na marejeo?
لَّهُمْ فِيهَا مَا يَشَاءُونَ خَالِدِينَ كَانَ عَلَىٰ رَبِّكَ وَعْدًا مَّسْئُولًا ﴿١٦﴾
16. Watapata humo wayatakayo, wakae humo milele. Ni ahadi juu ya Mola wako ya kuombwa.
Aya 7 – 16
Hekima ya Mwenyezi Mungu kupeleka mitume kwa watu ni kuwabainishia yale yaliyo na maslahi kwao na yaliyo na uharibifu, ili waweze kujua mambo yao vizuri na iwe ni hoja ya Mwenyezi Mungu kwao Siku ya Malipo na Hisabu. Hekima hii haiwezi kuhakikika ila akiwa huyo mtume ni wa aina moja na watu katika maisha yake, maumbile yake na hisia zake.
Lau angelikuwa wa jinsi nyingine, basi wangelimkimbia wala wasingelimtegemea; isipokuwa yule anayefanana na wao; akizungumza wanayozungumza wao, akifanya wanayofanya wao na akiathirika kama wanavyoathirika wao.
Hata hivyo, ni lazima Mtume awe na ukamilifu wa juu anaoweza kuufikia binadamu, katika mipaka ya ubinadamu kwa sifa zake na uwezo wake. Kwa sababu ukamilifu ndio nguvu tekelezi ya ujumbe wake na mafunzo yake. Tazama Juz. 16 (20:17 - 35).
Baada ya utangulizi huu, tuangalie kauli za washirikina na kupinga kwao utume wa Muhammad(s.a.w. w ) ambazo ni :
1.Na wamesema: Ana nini Mtume huyu anakula chakula na anatembea masokoni.
Wanataka aishi kwenye nyumba ya kifahari na azungukwe na walinzi; kama wafanyavyo watawala. Hawajui au wanajitia kutojua kuwa mtekelezaji wa risala yoyote, awe Mtume au mwengineo, haiwezekani kutekeleza risala yake ila akiwa pamoja na watu, katika tajruba zao na kazi zao. Vipi watamwitikia ikiwa atawawekea kizuizi au kuwa kwenye ulimwengu mwingine.
2.Mbona hakuteremshiwa malaika awe muonyaji pamoja naye?
Maoni ya washirikina ni kuwa Muhammad(s.a.w. w ) awe pamoja na malaika. Si ajabu hilo kwa wale ambao wanamfanyia Mwenyezi Mungu washirika, sembuse Muhammad, watampinga tu akiwa hana mshirika kati- ka kutekeleza risala yake. Kabla yao Firauni alimsema Musa(a.s ) :
فَلَوْلَا أُلْقِيَ عَلَيْهِ أَسْوِرَةٌ مِّن ذَهَبٍ أَوْ جَاءَ مَعَهُ الْمَلَائِكَةُ مُقْتَرِنِينَ ﴿٥٣﴾
"Basi mbona hakuvikwa vikuku vya dhahabu au kuja malaika pamoja naye wakimwandama? (43:53).
3.Au akaangushiwa hazina au awe na bustani ale katika hiyo.
Haya ndiyo mantiki ya watu wa pesa: Benki na ardhi. Vipi wataweza kumwamini anayesema kuwa hakuna ubora baina ya mwarabu na asiyekuwa mwarabu isipokuwa kwa takua, na wanasema kuwa ubora kwao ni mali, bila ya kutoka jasho? Yule anayetoka jasho kwao ni mtumwa, anatakikana asikilize na kutii amri. Vipi Mwenyezi Mungu amchague Muhammad na kumfadhilisha kuliko watu wengine naye ni fukara? Lau angelikuwa amechaguliwa, kama anavyodai, basi angeliteremshiwa hazina ya pesa au akawa na bustani ambayo hakuitolea jasho.
Hali hii bado inaendelea hadi leo. Serikali katika nchi nyingi ni za wenye mashirika na viwanda au zinasimamiwa na wale waliowachagua kulinda maslahi yao. Tazama Juz. 15 (17: 90 - 96), kifungu cha 'Kufikiria mali.'
4.Na walisema madhalimu -kuwambia waumin- hamumfuati ila mtu aliyerogwa.
Umetangulia mfano wake katika Juz. 15 (17: 101).
Tazama jinsi wanavyokupigia mfano kwamba wewe ni fukara na umerogwa. Basi wamepotea, wala hawataiweza njia ya kubatilisha utume wako na kukurudi kwa hoja na dalili.
Walikadhibisha risala ya Muhammad(s.a.w. w ) wakampa sifa za uzushi, wakawa wao ndio wazushi. Kwa sababu mwenye kumwambia mjuzi kuwa ni mjinga, na mwenye ikhlasi kuwa ni mhaini, basi amejisema yeye mwenyewe kuwa ni mjinga na ni mhaini.
Kwa hiyo basi mifano waliyompigia Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) ni ushahidi na mfano wa ujinga wao, uzushi wao na inadi yao, lakini wao hawatambui; sawa na anayejiangalia kwenye kioo akaona ubaya akafikiria ubaya uko ndani ya kioo, sio katika sura yake.
Amekuwa na baraka yule ambaye akitaka atakujaalia yaliyo bora kuliko hayo, mabustani yapitayo mito chini yake na akujaalie makasri.
Ambaye ameumba ulimwengu pamoja na ardhi yake na mbingu yake, hawezi kushindwa kumpa Mtume wake mtukufu mali nyingi, lakini utukufu mbele ya Mwenyezi Mungu haupimwi kwa mali; isipokuwa unapimwa kwa takua na amali njema na malipo ya wenye takua na wema ni neema na raha ya daima. Maisha ya duniani, si kitu cha maana kwa Mwenyezi Mungu kuwapa mawalii wake.
Kuna Hadith isemayo:"Lau dunia ingelikuwa inapimwa mbele ya Mwenyezi Mungu kwa ubawa wa mbu, basi asingelikunywa kafiri hata tama moja la maji."
Bali wameikanusha saa.
Saa ni saa ya Kiyama. Walikanusha utume wa Muhammad(s.a.w. w ) wakaleta sababu kuwa yeye ni fukara na amerogwa, wakiwa wanajidanganya.
Lengo lao kuu ni kuhofia masilahi na manufaa yao na wakasema hakuna ufufuo, ili wasiaambiwe kuwa wameathirika na yanayokwisha wakaacha yanayobakia.
Kila mwenye kupima ubora kwa mali na akaathirika nayo kuliko radhi ya Mwenyezi Mungu, basi atakuwa katika hukumu ya mwenye kukanusha kukutana na Mwenyezi Mungu hata kama atakuwa anamwamini kinadharia.
Na tumemwandalia moto mkali mwenye kuikanusha saa. Utakapowaona katika mahali pa mbali watasikia hasira yake na mngurumo wake.
Imesekana kuwa utakaoona, kuwa na hasira na kuunguruma ni moto. Wengine wakasema ni watunzaji wa moto. Pia ikasemekana kuwa Mwenyezi Mungu kesho ataufanya moto uwe na uhai na akili. Tuonavyo sisi ni kuwa hicho ni kinaya cha adhabu kali na vituko vikubwa.
Na watakapotupwa humo, mahali palipo finyu hali wamefungwa, ndipo hapo wataomba mauti. Msiyaombe mara moja bali ombeni mauti mara nyingi.
Moto wa Mwenyezi Mungu hauwi finyu; kama ilivyoweka wazi hilo kauli yake Mwenyezi Mungu:
يَوْمَ نَقُولُ لِجَهَنَّمَ هَلِ امْتَلَأْتِ وَتَقُولُ هَلْ مِن مَّزِيدٍ ﴿٣٠﴾
"Siku tutakapoiambia Jahannamu:Umejaa? Nayo itasema: Je, kuna ziada?" (50:30).
Kwa hiyo makusudio ya ufinyu wa moto ni ufinyu wa watu wa motoni watakaona dhiki na kuchukia kuingia humo. Aliulizwa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w. w ) kuhusu Aya hii, akasema:
"Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake! Hakika wao watachukia kama inavyochukia nguzo kwenye ukuta" yaani wataingia kwa kulazimishwa. Umetangulia mfano wa Aya hii katika Juz. 13 (14: 46 -52) kifungu cha 'Jahnnam na silaha za maangamizi.'
Sema, je, hayo ni bora au Bustani ya milele, ambayo wameahidiwa wenye takua, iwe kwao malipo na marejeo? Watapata humo wayatakayo, wakae humo milele. Ni ahadi juu ya Mola wako ya kuombwa.
Neno 'juu ya' linafahamisha kuwa Mwenyezi Mungu (s.w.t) amejilazimishia kutekeleza ahadi yake. Katika Tafsir Ar-Razi kuna melezo haya: "Ikisemwa kuwa adhabu ni bora au Pepo ni kama kumwambia mwenye akili kuwa sukari ni tamu au shubiri (subili)? Tutajibu: Hii inafaa katika hali ya kukaripia; kama vile mtu akimpa mtumwa wake mali kisha akawa na kiburi akampiga pigo la kuumiza huku akimwambia, hii ni tamu au ile."
وَيَوْمَ يَحْشُرُهُمْ وَمَا يَعْبُدُونَ مِن دُونِ اللَّـهِ فَيَقُولُ أَأَنتُمْ أَضْلَلْتُمْ عِبَادِي هَـٰؤُلَاءِ أَمْ هُمْ ضَلُّوا السَّبِيلَ ﴿١٧﴾
17. Na siku atakapowakusanya na wale wanaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu na atasema: Je, nyinyi mmewapoteza waja wangu hawa au ni wao wenyewe walipotea njia.
قَالُوا سُبْحَانَكَ مَا كَانَ يَنبَغِي لَنَا أَن نَّتَّخِذَ مِن دُونِكَ مِنْ أَوْلِيَاءَ وَلَـٰكِن مَّتَّعْتَهُمْ وَآبَاءَهُمْ حَتَّىٰ نَسُوا الذِّكْرَ وَكَانُوا قَوْمًا بُورًا ﴿١٨﴾
18. Watasema: Umetakasika na upungufu! Haikutupasa sisi kuwafanya mawalii badala yako, lakini uliwastarehesha wao na baba zao hata wakasahau ukumbusho na wakawa watu walioangamia.
فَقَدْ كَذَّبُوكُم بِمَا تَقُولُونَ فَمَا تَسْتَطِيعُونَ صَرْفًا وَلَا نَصْرًا وَمَن يَظْلِم مِّنكُمْ نُذِقْهُ عَذَابًا كَبِيرًا ﴿١٩﴾
19. Basi hakika wamewakadhibisha kwa mliyoyasema. Kwa hiyo hamuwezi kujiondolea wala kujisaidia. Na atakayedhulumu miongoni mwenu tutamuonjesha adhabu kubwa.
وَمَا أَرْسَلْنَا قَبْلَكَ مِنَ الْمُرْسَلِينَ إِلَّا إِنَّهُمْ لَيَأْكُلُونَ الطَّعَامَ وَيَمْشُونَ فِي الْأَسْوَاقِ وَجَعَلْنَا بَعْضَكُمْ لِبَعْضٍ فِتْنَةً أَتَصْبِرُونَ وَكَانَ رَبُّكَ بَصِيرًا ﴿٢٠﴾
20. Na hatukuwatuma kabla yako mitume ila kwa hakika walikuwa wakila chakula na wakitembea masokoni. Na tumewajaalia badhi yenu wawe mtihani kwa wengine. Je, mtakuwa na subira? Na Mola wako ni Mwenye kuona.
SIKU ATAKAPOWAKUSANYA NA WANAYOYAABUDU
Aya 17 – 20
Na siku atakapowakusanya na wale wanaowaabudu badala ya Mwenyezi Mungu na atasema: Je, nyinyi mmewapoteza waja wangu hawa au ni wao wenyewe walipotea njia.
Mwenyezi Mungu (s.w.t) katika Aya zilizotangulia, amewataja washirikina na kuli zao kumhusu Mtume wa Mwenyezi Mungu na yale mambo watakayokumbana nayo kesho, ikiwa ni pamoja na adhabu ya kuunguzwa.
Katika Aya tuliyo nayo, Mwenyezi Mungu Mtukufu ametaja kwamba Yeye, siku ya Kiyama, atawakusanya washirkina na wale waliowafanya ni washirika wa Mwenyezi Mungu. Kisha Mwenyezi Mungu (s.w.t) aliulize lile kundi liloabudiwa mbele ya wale waliowashirikisha. Lengo la swali hili ni kuwanyamazisha washirikina na kusisitiza hoja juu yao iliyowalazimu kupitia kwa Manabii na Mitume.
Watasema: Umetakasika na upungufu! Haikutupasa sisi kuwafanya mawalii badala yako.
Kundi lililoabudiwa litajibu: 'Umetakasika na umetukuka na shirki ewe Mola wetu! Vipi tutake tuabudiwe na hali sisi tunakupwekesha wewe, tunakuabudu na kukufanyia ikhlasi?
Pia tunaogopa adhabu na kutaraji thawabu zako wala hatumtaki msaada asiyekuwa wewe? Kwenye jawabu hili pia kuna kutahayariza, kama ilivyo katika swali.
Lakini uliwastarehesha wao na baba zao hata wakasahau ukumbusho na wakawa ni watu walioangamia.
Bado wale walioabudiwa wanaendelea kusema. Maana yake ni kuwa sisi hatukuwapoteza washirikina, lakini hekima yako, ewe Mola wa ulimwengu, imepitisha kuwapa muda wao na baba zao na kuwaneemesha kwa umri mrefu, mali na watoto, ili waweze kutubia na kuomba msamaha, lakini waliuacha, wakaiendea dunia na ladha zake, wakawa ni wenye kuangamia kwa sababu ya uzembe wao na uchaguzi wao mbaya.
Hakika wamewakadhibisha kwa mliyoyasema. Kwa hiyo hamuwezi kujiondolea wala kujisaidia.
Maneno yanatoka kwa Mwenyezi Mungu kuelekea kwa washirikina.
Maana ni kuwa, enyi washirikina! Mlikuwa mkisema kuwa tunawaabudu hao ili watuombee kwa Mwenyezi Mungu na watuwekee karibu naye, sasa je, mmeona? Wamejitenga nanyi na wamewakana mnayoyasema na mambo yenu ya ubatilifu. Adhabu ndio hii sasa inawashukia hakuna wa kuwakinga nayo wala kuwasaidia.
Na atakayedhulumu miongoni mwenu tutamuonjesha adhabu kubwa.
Hakuna kitu kikubwa na adhimu kuliko moto wa Jahannam, na ndiyo malipo ya kila dhalimu na mwenye hatia.
Na hatukuwatuma kabla yako mitume ila kwa hakika walikuwa wakila chakula na wakitembea masokoni.
Washirikina walimkana Muhammad(s.a.w.w) kwa kuwa anakula chakula na kutembea sokoni. Ndipo Mwenyezi Mungu (s.w.t) akawarudi kwa kuwaambia kuwa kuna ajabu gani ya hilo? Mitume wote waliokuwa kabla yake walikuwa wakila chakula na kutembea kwenye masoko, wakiwemo wale mnaoitakidi utume wao; kama Ibrahim na Ismail(a.s) . Rudia Aya 8 ya Sura hii.
Na tumewajaalia badhi yenu wawe mtihani kwa wengine.
Mwenyezi Mungu anawatahini waja wake, akiwa anawajua zaidi, ili visidhihirike vitendo vinavyostahiki thawabu na adhabu; kama alivyosema Imam Ali(a.s) .“Miongoni mwa mambo anayowatahini nayo waja wake na yaliyo wazi zaidi ni kuwapelekea Mitume, kuwabashiria na kuwaonya. Atakayewaamini, kuwasikiliza na kutii, basi atastahiki thawabu na atakayekufuru na kufanya inadi basi atastahiki adhabu.”
Kwa hiyo kupatikana mitume, kama wabashiri na waonyaji ni mtihani kwa waumini na makafiri na ni sababu ya kudhihiri hakika ya makundi hayo mawili.
Vile vile kupatikana makafiri na wanafiki ni mtihani kwa manabii. Kwa vile washari na wafisadi hawawachi wakombozi, bali wanajaribu kuwaudhi kwa kila njia, bali wanawazushia mambo, kuleta uvumi na njama; sawa na washirikina walivyomfanyia Mtume(s.a.w.w) na hivi sasa vibaraka wanaolipwa wanavyowafanyia wakombozi wenye ikhlasi.
Historia ya mapambano baina ya haki na batili inaanzia na mwanzo wa binadamu. Qabil alimuua Habil pamoja na kuwa walitokana na tone moja la manii na mfuko mmoja wa uzazi, si kwa lolote ila ni kwa kuwa Mwenyezi Mungu alikubali amali ya Habil kwa wema wake na hakuikubali ya Qabil kwa ufisadi wake.
Je, mtakuwa na subira?
Yaani enyi waumini kuweni na uthabiti kwenye haki wala msiwajali wabatilifu na uongo wao.
Na Mola wako ni Mwenye kuona yule anayewazulia wema na yule anayethibiti kwenye haki kwa matokeo yoyote yatakayokuwa na atamlipa kila mmoja stahiki yake.
Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)
Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.
MWISHO WA JUZUU YA KUMI NA NANE
YALIYOMO
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE 1
IMEANDIKWA NA: SHEIKH MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYA 1
IMETAFSIRIWA NA: SHEIKH HASAN MWALUPA 1
IMEHARIRIWA NA: USTADH ABDALLAH MOHAMED 1
IMEPANGWA KATIKA KOMPYUTA NA: UKHT PILI RAJABU 1
UTANGULIZI WA MCHAPISHAJI 1
MAKOSA YA CHAPA 2
MUHAMMAD JAWAD MUGHNIYYAH 2
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE 3
HAKIKA WAMEFAULU WAUMINI 3
MAANA 3
KUUMBWA MTU NA MBINGU 5
MWENYEZI MUNGU NA MTU 5
MAANA 6
MAANA YA MBINGU SABA 6
TUKATEREMSHA MAJI KUTOKA MBINGUNI 8
MAANA 8
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE 9
NUH 9
MAANA 10
HUD 12
KISHA BAADA YAO TUKAANZISHA KARNE NYINGINE 12
KILA UMMA ULIKANUSHA MTUME WAKE ALIPOWAFIKIA 13
MAANA 14
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE 16
MAANA 16
TENA SIFA ZA WAUMINI 18
MAANA 18
NYOYO ZAO ZIMO UJINGANI 19
MAANA 19
MWANGA WA JUA NA WANAODEKA NA STAREHE 21
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE 22
UNAWAITA K W ENYE NJIA ILIYONYOOKA 22
MAANA 22
WALISEMA KAMA WALIVYOSEMA WA MWANZO 24
MAANA 24
MJUZI WA GHAIBU NA YALIYO WAZI 26
MAANA 26
KUKINGA MAOVU KWA MEMA ZAIDI 27
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE 29
HAKUNA UJAMAA BAINA YAO SIKU HIYO 29
MAANA 29
MLIKAA MUDA GANI KATIKA ARDHI 31
MAANA 31
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE 33
HUKUMU YA MZINIFU NA MWENYE KUTUSI 33
MAANA 33
KUAPIZANA MUME NA MKE 37
MAANA 37
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE 39
WALIOLETA UONGO 40
KISA CHA UZUSHI KWA UFUPI 40
MAANA 41
MSIFUATE NYAYO ZA SHETANI 44
MAANA 44
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE 46
MAMBO YA UHABITHI NI YA MAHABITHI 46
MAANA 46
HIJABU NA KUINAMISHA MACHO 48
MAANA 49
KUJIWEKA WAZI AU KUJIUZA? 50
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE 53
WAOZENI WAJANE 53
MAANA 53
MATAMSHI NA UELEWA 55
MWENYEZI MUNGU NI NURU YA MBINGU NA ARDHI 56
MAANA 56
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE 59
VITENDO VYAO NI KAMA SARABI (MANGATI) 59
MAANA 59
MAJI 61
MAANA 61
WANAFIKI 63
MAANA 63
IJARIBU DINI YAKO NA IMANI YAKO 64
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE 66
UKHALIFA WA WAUMINI ARDHINI 66
MAANA 66
NJIA NYINGINE YA MUUJIZA WA QUR'AN 67
KUPIGA HODI MTOTO NA MTUMWA 68
MAANA 68
SI VIBAYA KWA KIPOFU 70
MAANA 70
HAWAONDOKI MPAKA WAKUOMBE RUHUSA 72
MAANA 72
TAFSIRI YA QURANI AL-KAASHIF JUZUU YA KUMI NA NANE 74
AMEMTEREMSHIA FURQANI MJA WAKE 74
MAANA 74
ANAKULA CHAKULA NA KUTEMBEA MASOKONI 77
MAANA 78
MANTIKI YA WATU WA PESA NI BENKI NA ARDHI 78
ALIVYO MJINGA ALIYEHADAIKA 79
SIKU ATAKAPOWAKUSANYA NA WANAYOYAABUDU 80
MAANA 81
SHARTI YA KUCHAPA 82
MWISHO WA JUZUU YA KUMI NA NANE 82
YALIYOMO 83