UTENZI WA IMAM HUSEN

MWANDISHI: HEMED BIN ABDALLAH BIN SAID

UTENZI WA KISA CHA SAYYIDNA HUSSEIN

1. Bismillahi Aziza, ArRahmani Mweneza, Ndiye wa Kwanza na kwanza, Wa milele na abadi

2. Ndiye Huyu 'lKayumu, Wa milele na dawamu, Ndiye muumba Adamu, Na wote wake waladi

3. Ndiye muumba 'ssamai, Na wote anbiai, Thumma na auliai, Wote ni wake ibadi

4. Jamii ni wake waja, Wala hawati mmoja, Kula atakae haja, Apata wake mradi

5. Kuumba kwake Jalali, Nabiu na Mursali, Aliyeumbwa awali, Tumwa wetu Muhammadi

6. Huyo alitangulia, Kisijawa vitu pia, Vyote vilivyobakia, Vijile yake baadi

7. Nuru yake yalidanda, Na sifaze zikenenda, Jina aketwa Kipendwa, Kipendo chake 'sSamadi

8. Baada ya kudhukuri, Sifa za Mola Jabari, Na za tumwa Mukhtari, Penda nitunge ishadi

9. Natanga tunga utenzi, Usipate nusu mwezi, Ama kwandika siwezi, Macho yametasawadi

10. Macho yamesawidika, Sioni vema kwandika, Kwa kula siku kushika, Karatasi na midadi

11. Macho yangu wanakwetu, Hayafafanui mtu, Natendea kazi yetu, Ya tangu jadi na jadi

12. Na kuiwacha si vema, Taja dhuriwa nakoma, Hata kwamba si mzima, Afadhali jitihadi

13. Na hadithiye kwambile, Nitakayo nitongole, Bajani moyo mkale, Tena mtuze fuadi

14. Mtoe na wasiwasi, Niwatulie nafusi, Baada ya kujilisi, Na roho kutabaradi

15. Ndipo niweleze shani, Ya Maulana Huseni, Dhuria wake Amini, Vita vyao na Yazidi

16. Huyu Yazidi sikia, Babaye ni Muawia, Kutawafukwe Nabia, Na arubaa Sayyidi

17. Wa kwanza Abubakari, Na Maulana Omari, Na Ally Haidari, Na mmoja taradidi

18. Maulana Athumani, Watu hao sikiani, Kuondoka duniyani, Ndipo hayo yakabidi

19. Kuondoka kwao pia, Kutawala Muawia, Miji yote kuzuia, Asibakie biladi

20. Akashika ufalume, Wala pasiwe muume, Na dhuriaze Mtume, Pendo likenda ahadi

21. Akampenda Huseni, Na watotowe nyumbani, Na angawa sultani, Asiweze kutaadi

22. Kakithiri Muawia, Heshima kamwekea, Na pendo kamzidia, Atakalo lisirudi

23. Akazidi muheshimu, Na wote bani Hashimu, Jamii kawakirimu, Akajifanya abidi

24. Baada hayo rafiki, Akenenda Dimishiki, Na dhuriaze sadiki, Asibakie wahidi

25. Kamtukua Huseni, Na dhuriaze Amini, Rijali na nisiwani, Wakubwa hata waladi

26. Dimishiki kenda nao, Muawia kawa nao, Akawaweka kikao, Kizuri kisikyo budi

27. Baada suu wuadhi, Akapatwa ni maradhi, Muawia kiaridhi, Akajua ni ahadi

28. Akajua ni ajali, Ya roho kunakali, Akamwita tasihili, Mtoto wake Yazidi

29. Akamuweka usoni, Wali wao faraghani, Muawia kabaini, Akamba ewe waladi

30. Ewe Yazidi mwanangu, Nitazama hali yangu, Muwili wote matungu, Na uzito wa jasadi

31. Muwili umezuiwa, Sijiwezi kujinua, Na sisi waja twajua, Mauti hatuna budi

32. Twaijua kwa hakika, Ni faradhi kutoweka, Yazidi akatamka, Maneno akaradidi

33. Baba utakapokufa, Nnani nyuma Khalifa, Mtamalaki taifa, Na ezi ikambidi?

34. Akinena Muawia, Khalifa wewe dhuria, Lakini nakuusia, Usije ukafisidi

35. Sikia ewe mwanangu, Ushike wosia wangu, Wepukane na matungu, Hiyo siku ya mnadi

36. Kwanza nikuusiayo, Ezi ni kutunza moyo, Ujue na marikayo, Na walio kukuzidi

37. Na wote raia wako, Ukae nao kitako, Usikithiri vituko, Utakuja jihusudi

38. Na tena uwashauri, Ijiriapo amri, Ukae nao vizuri, Roho zao ziburudi

39. Pindi hayo ukitenda, Tambua watakupenda, Utakalo utatenda, Neno lako halirudi

40. Baada hayo yakini, Nakusikia Huseni, Na watotowe nyumbani, Alla Alla ya Yazidi

41. Alla Alla uwashike, Tangu waume na wake, Na jambo lisitendeke, Shati apende Sayyidi

42. Jambo asilolipenda, Usije ukalitenda, Tambua umejivunda, Hata kwa Mola Wadudi

43. Wala usimkasiri, Hata kwa jambo saghiri, Mpe kuti na uzari, Kabla wote junudi

44. Alla Alla muheshimu, Umzidie makamu, Kwani sisi tu hadimu, Walidio masayidi

45. Ewe Yazidi yashike, Yule asikasirike, Sisi tu watumwa wake, Na babuye Muhamadi

46. Na ukhalifa si wetu, Wala si wa baba zetu, Wake yeye bwana wetu, Sisi kwao tu abidi

47. Pindi atakapokuwa, Siwate kumtukuwa, Umsalimu ulua, Kuko kwao na urudi

48. Alla Alla ewe mwana, Akuapo Maulana, Enenda naye Madina, Na wote wake waladi

49. Umsalimu eziye, Kwamba atatwaa yeye, Au mtu atakaye, Ushike ndiya urudi

50. Atakalo mfanyie, Wala simzuilie, Na kadiri amriye, Ndiyo itayokufidi

51. Umtie mahabani, Dhahiri na faraghani, Siwe na kitu moyoni, Roho yako isafidi

52. Na pindi umpendapo, Hapana budi na pepo, Utakwenda kaa papo, Pa babuye Muhammadi

53. Pindi usipompenda, Kesho huna la kutenda, Ndia utakayokwenda, Na Majusi na Yahudi

54. Muawia kamaliza, Yazidi asikiliza, Maneno kamrudiza, Manenoyo hayarudi

55. Yote uloniusia, Baba nimeyasikia, Si mwenye kuyawatia, Yote uliyoradidi,

56. Baada hayo nakuli, Isipate siku mbili, Akapatwa na ajali, Mauti yakambidi

57. Alipokwisha toweka, Yazidi kafadhaika, Kasimama akazika, Na kuchawanya nakidi

58. Akaliweka tanzia, La babaye Muawiya, Na vitu vikangamia, Vingi visivyo idadi

59. Akavihasiri vitu, Akawakusanya watu, Si siku mbili si tatu, Ikawa hiyo abadi

60. Akawatinda ghanamu, Na wingi wa bahayumu, Na zakula tamtamu, Na sharubati waridi

61. Matanga akiondoa, Nguo mbaya kazivua, Akavaa za uluwa, Nzuri za kusafidi

62. Akajivika na taji, Lawaka kama siraji, Na wengi watundamaji, Majaria na abidi

63. Akajivika libasi, Hudhuri na sandusi, Zawaka kama shamsi, Rihi ambari na udi

64. Akavaa burukhuti, Akakikalia kiti, Cha lulu na yakuuti, Chema cha zabarijudi

65. Akatungika johari, Na thoria mnawari, Vyandarua vya hariri, Siriri na l'wasidi

66. Sayo yakisha tendeka, Akakutubu nyaraka, Kula nti kapeleka, Akamkua junudi

67. Akaweta asibaki, Kula panapo muluki, Wakutane Dimishiki, Wamkiri usayidi

68. Barua zisibakie, Na kula asikiaye, Akaja na kaumuye, Na nyingi mno zawadi

69. Wakaitika amri, Jamii ya ansari, Wakakutana jifiri, Kuja kwake makusudi

70. Walipokwenda timia, Yazidi akawambia, Jambo alilowetia, Ya maishara junudi

71. Mimi nimetamalaki, Aridhi ya Dimishiki, Na jamii ya muluki, Mje kwangu musujudi

72. Mimi ndimi sultani, Niwetapo nitikani, Pasiwe na ushindani, Wala mwenye kukaidi

73. Mimi ni wenu amiri, Ambaye amenikiri, Tamjaza utajiri, Na kula siku nizidi

74. Ambaye amekubali, Tamjaza mangi mali, Yeye na wake ayali, Na wakewe na abidi

75. Ambaye hakuridhika, Kuwa mimi mamlika, Rasiye itaondoka, Kwa saifi ya hadidi

76. Tamkata yake rasi, Nimwangue kama sisi, Semani hima upesi, Nipate kuyafanidi

77. Jamii wakabaini, Wewe ndiwe sultani, Akubishaye nnani?, Hapo mwenye kukaidi

78. Wewe ndiwe bwana wetu, Uliyemiliki watu, Wala hazumbuki mtu, Kuja kwako na taadi

79. Na ambaye atakuja, Kwa harubu au huja, Shauri letu ni moja, Tambua tutakufidi

80. Haya wakishatamka, Yazidi kafurahika, Akawapa twika twika, Jeshi yote ikarudi

81. Kabaki yeye pekee, Na mjini kaumuye, Akampa ampaye, Wengine akawazidi

82. Akaweka mawaziri, Na aribabu amri, Akadirika hamri, Barazani ikabidi

83. Kinyang'anya masikini, Wenye kupita ndiani, Na wajao barazani, Wengine kiwahusudi

84. Kawakataa tariki, Sipitike Dimishiki, Watu wakataharuki, Kwa mambo yake Yazidi

85. Akaitenda jeuri, Kubwa isiyo kadiri, Raia na mawaziri, Wote wakasitajidi

86. Na kula mtu ambaye, Alipendwa na babaye, Yeye kawa hasimuye, Akija kimtaridi

87. Ali akiwasukuma, Wenye haya na huruma, Akakithiri dhuluma, Na kila siku kuzidi

88. Akautupa wosia, Wa babaye Muawiya, Ukazidi utaghia, Mno akatamaridi

89. Na Maulana Huseni, Asimpe nufaani, Wala kwenda barazani, Asipende mshahidi

90. Na mtu amtajaye, Alosimama mbeleye, Yuamkata nyamaye, Na kumpiga jalidi

91. Kamzia Maulana, Asitake kumuona, Pasiwe neno kunena, Ila la kumuhusudi

92. Akashirabu khamri, Na jilasi ikajiri, Na nyama ya hinziri, Akila na kurajidi

93. Kuonakwe Maulana, Vitendo vyake laana, Na babaye alonena, Yote hayakusuudi

94. Kuonakwe tafauti, Kondoka suu wakati, Kenda kwa wake ukhti, Ili kwenda muradidi

95. Akifika akalia, Nduguye akangalia, Sakina akamwambia, Waliza nini Sayyidi?

96. Akatamka Sakina, Una nini Maulana, Ambalo ni kubwa sana, Jambo lililokuzidi?

97. Kilio chako Huseni, Kitawaliza majini, Na malaika mbinguni, Na baharini swayyidi

98. Na nyama wote barani, Watangia kilioni, Hata maji baharini, Pia yatatujamidi

99. Usilie Maulana, Na uliyo nayo nena, Kwa amriye Rabana, Neo lako halirudi

100. Huseni akamwambia, Ewe Sakina sikia, Yaliyonipa kulia, Ni mambo yake Huseni

101. Ametukiwa na siye, Hapendi atusikie, Ni kheri tumuukiye, Si naye tuwe baidi

102. Sikia ewe Sakina, Twenende zetu Madina, Hapa sipataki tena, Hata kwa saa wahidi

103. Twende zetu Yathiribu, Kunako nyumba za Babu, Tumwondokee harabu, Atakayetuhusudi

104. Ni hayo maneno yangu, Nitakayo roho yangu, Wanenaje nduu yangu, Katika suu mradi?

105. Kamaliza Maulana, Akatamka Sakina, Sayyidi unayonena, Mimi ni bora zaidi

106. Huyu ametakabari, Na kumuasi Jabari, Na kushirabu khamri, Na watu kuwajalidi

107. Na babaye Muawiya, Pia alomuusia, Yote hayakutimia, Hata kwa jambo wahidi

108. Afadhali twende zetu, Kunako majumba yetu, Kwani Yazidi si kitu, Amekwisha tamaridi

109. Walakini kamjibu, Umuarifu kitabu, Nenda zangu Yathiribu, Wala huku sitarudi

110. Mpelekee khabari, Ya kumuaga safari, Tusikize madhukuri, Atakayo kuradidi

111. Kwani tutokapo Kofu, Tusipo kumuarifu, Atasema tuna khofu, Haya atayafanidi

112. Sakina kwisha kalimu, Mara Huseni kakumu, Akaagiza kalamu, Na lauhi na midadi

113. Akawandika waraka, Tasihili kwa kikaka, Ila muhibu pulika, Sikia ewe Yazidi

114. Rohoni nimeazimu, Kwenda Madina kukimu, Au kunako Haramu, Hakae nitaabidi

115. Napenda kwenenda Maka, Au Madina hifika, Hatake pa kuniweka, Katika mbili biladi

116. Nami siwezi safiri, Ila unipe amri, Na ambapo hukukiri, Takaa nitabaradi

117. Nipe rukhusa ya kwenda, Au niambie Vunda, Kula utakalopenda, Siwezi kukukaidi

118. Kashilia Maulana, Kaukunda iyo hina, Kamsalimu kijana, Kenda nao kwa Yazidi

119. Ikiwasili barua, Yazidi kaufungua, Jamii makutubua, Yote akayaadidi

120. Hata akisha usoma, Kaupindua kwa nyuma, Aketa kalamu hima, Kumuarifu Sayyidi

121. Maneno akabaini, Akamba ewe Huseni, Kwangu wataka idhini, Ndiyo uliyoradidi

122. Tumia khiari wewe, Hayo ni yako mwenyewe, Mimi sina haja nawe, Sipendi kukushahidi

123. Ukenenda sikutaki, Wala hu wangu rafiki, Na uwapo Dimishiki, Sikupi hata nakidi

124. Sipendi kushuhudia, Kwamba Rabi ajalia, Kuigauza dunia, Ikawa zabarijudi

125. Ningewapa insani, Watu wote duniani, Wewe ukaitamani, Ujapo kujitahidi

126. Kwangu hupati mahaba, Wala kula ukashiba, Nakuwazia msiba, Na 'ladhabu shadidi

127. Na Maka ukiwasili, Majumba yangu ya mali, Nenda kayakae mbali, Usende ukarajidi

128. Sende ukapanda ngazi, Majumba yangu ya ezi, Akimaa matongozi, Waraka kaujadili

129. Kamsalimu risali, Kenda nao tasihili, Hata alipowasili, Kwa Maulana sayyidi

130. Kausoma kauona, Kenda nao kwa Sakina, Akamba tazama mwana, Maneno yake Yazidi

131. Amesema ni khiari, Kukaa na kusafiri, Wanambiaje shauri?, Mwanamke karadidi

132. Mwanamke kadhukuri, Hapana tena usiri, Na watengeze bairi, Wa kuja panda waladi

133. Hima twandame tariki, Tuitoke Dimishiki, Huseni akasabiki, Kamzaini jawadi

134. Twika kazitengeneza, Ngamia akawatwisa, Kula ambaye apasa, Waungwana na abidi

135. Wakalekea safari, Wakamuomba Jabari, Wakaikabili bari, Yenye nondo na asadi

136. Rabi akawanusuru, Kwenda kheri wa sururu, Pasiwe la kuwadhuru, Dhuria za Muhammadi

137. Kawanusuru Rabuka, Kwa maafa na shabuka, Nondo wote na majoka, Wakuja wakisuudi

138. Jamii watu wazima, Hata watoto yatima, Wakiwasili salama, Badari 'lmakusudi

139. Walipofika Madina, Watu walipowaona, Wakafurahika sana, Furaha kubwa shadidi

140. Wakatelea rikabu, Wakangia Yathiribu, Jamii ya Waarabu, Wakamlaki sayyidi

141. Akafikilia dari, Ya babaye Haidari, Ndiyo aliyokhiari, Kuwatia auladi

142. Baada ya kuwasili, Akenenda tasihili, Kaburini kwa rasuli, Kumzuru wake jadi

143. Kimaa yake zuari, Kaburi iketa nuri, Hata juu ya kamari, Nuru hiyo ikazidi

144. Kwishakwe zuru nabia, Roho ikafurahia, Nyumbani akarejea, Nyumbani kwake kurudi

145. Ali yeye na nduguye, Alokwenda zuru naye, Mtakapo ismuye, Jina ketwa Muhammadi

146. Ni mwana wa Shekhe Ali, Kazawa nyumba ya pili, Naye katika kitali, Kama umeme na radi

147. Jamii zote taifa, Wamwita bunu Khanifa, Wala hafikiri kufa, Atokeapo jihadi

148. Ali simba maalumu, Katika nchi ya Shamu, Ambapo ataranamu, Utamboni akabidi

149. Hakiwa akizumbuka, Awezaye kumfika, Wote wenye kutajika, Kwake wakasitajidi

150. Basi wakarejeea, Na Maulana pamoya, Nyumbani wakenda ngia, Kwa baba yao asadi

151. Na wote 'lAnsari, Na jamii Muhajiri, Pasibakie saghiri, Msifurahi fuadi

152. Wale wakamkirimu, Kwa zakula tamtamu, Wakamuweka makamu, Na pendo likashitadi

153. Jamii wakalingana, Kumwambia Maulana, Kula utakalonena, Kwani ni yako biladi

154. Sisitahi bwana wetu, Roho ikataka kitu, Nafasi na mali zetu, Ni yako wewe Sayyidi

155. Sote tumefurahika, Madina unavyofika, Hatupendi kuondoka, Katika zetu fuadi

156. Basi wakasimulia, Hata kiza kikangia, Wakenenda zao pia, Pasibakie wahidi

157. Ila ni wao theneni, Wao wawili nyumbani, Akatamka Huseni, Kamba Ewe Muhammadi

158. Sababu ya kuja zangu, Ni ghadhabu na matungu, Ya hayo asi wa Mungu, Abdullahi Yazidi

159. Alipokufa babaye, Hamtazama haliye, Sikuweza kaa naye, Kwa jeuri na taadi

160. Yote aliyousiwa, Hata moja halikuwa, Aliposhika ulua, Kangia na kufisidi

161. Nami kanizia sana, Asitake kuniona, Haona sina maana, Kukaa yake biladi

162. Haradhiwa kuondoka, Kuja Madina na Maka, Muhammadi katamka, Ahsanta Sayyidi

163. Hasanta bun Ali, Kuja zako afadhali, Mtu kukaa muhali, Wala asipo mradi

164. Miji yao maghasiki, 'lKofu na Dimishiki, kukaa wewe ni dhiki, mashaka hayana budi

165. Na Yazidi bardhuli, Kuwania udawali, Wala si yao asili, Si ya jadi na jududi

166. Huu ulua ni wetu, Wa baba na babu zetu, Wala hazumbuki mtu, Ambaye ametuzidi

167. Wenyewe tukiutaka, Twenenda tukaushika, Na afanyapo dhihaka, Tukamuonya hadidi

168. Na kwamba hatuutaki, Ya nini kwenda jidhiki?, Kheri kufuata haki, Ya Mola wetu Wadudi

169. Nawe sasa Maulana, Keleti hapa Madina, Kula utakalo nena, Neno lako halirudi

170. Na utakapo Makati, Enenda zako kaketi, Na kwamba wataka nti, Takuwali sina budi

171. Utakapo ukhalifa, Sema niwete taifa, Ahadi ni mimi kufa, Ndipo uone taadi

172. Takawali hivi sasa, Utamalaki kabisa, Pasiwe mtenda kisa, Ukate utabaridi

173. Huseni kamrudia, Ya 'lakhi nisikia, Hayo sikupendelea, Kutamalaki junudi

174. Roho yangu naazimu, Nenende hasitakimu, Maka kunako Haramu, Nimuabudu Wadudi

175. Niabudu Subhana, Kwa usiku na mchana, Nitazame kwa Rabana, Atakalo kunibidi

176. Ezi sina haja nayo, Haimo katika moyo, Wakisha kusema hayo, Wakenda wakarajidi

177. Akaketi Maulana, Siku ashara Madina, Khatima wakandamana, Nduguye akamuwadi

178. Maulana akatoka, Akakusudia Maka, Siku haba zikifika, Akawasili biladi

179. Alipokwisha wasili, Wakatoka kabaili, Wanawake na rijali, Kwenda mlaki Sayyidi

180. Katoka bun Zuberi, Abdalla mashihuri, Pasibakie saghiri, Waungwana na abidi

181. Na Abdalla yuani, Ni ndugu yake Huseni, Wa katika ridhaani, Zamani wali wabidi

182. Ni nduguye hana huja, Walinyonya ziwa moja, Akenda akimngoja, Bara katika 'lwadi

183. Na Abdalla pulika, Zamani hizo hakika, Ndiye khalifa wa Maka, Mtamalaki junudi

184. Wakamlaki Huseni, Na ndugu yake Sakini, Wakamtia mjini, Na furaha za fuadi

185. Abdalla akanena, Twende kwangu Maulana, Kwenda pengine hapana, Kwangu ni bora zaidi

186. Kuwasilikwe fahamu, Ikafanyiwa karamu, Ya hubuzi na lahamu, Na vitu vya kusafidi

187. Twenende kwangu nyumbani, Ukae uje makini, Akatikia Huseni, Asiweze kumrudi

188. Kasimama Abdalla, Akafanyiza vyakula, Na wengine kabaila, Wote wakajitahidi

189. Kula mtu katamani, Kumkirimu Huseni, Vitu launi launi, Vya moto na vya baridi

190. Karamu zikafanyiwa, Na kuliwa zikasazwa, Hata kukangia kiza, Usiku ukasawidi

191. Watu wote barazani, Wakarejea nyumbani, Kabaki yeye Huseni, Na mtoto wa asadi

192. Huseni akatamka, Ya Abdalla pulika, Kisa cha kungia Maka, Na Dimishiki kurudi

193. Ni ibnu Muawia, Mambo alonifanyia, Uasi na utaghia, Jeuri na uhasidi

194. Amekithiri jeuri, Uasi na ujabari, Si mwenye kutafakari, Na kwamba yuko Wadudi

195. Amekithiri uasi, Kupita hao Majusi, Nilipoona jinsi, Hushika ndia harudi

196. Babaye akifariki, Akaushika muluki, Yote hakuyasadiki, Aliyokumradidi

197. Yote alomuusia, Jamii hakuridhia, Sikuweza vumilia, Mji wake kurakidi

198. Nimekuja zangu kwetu, Kuliko majumba yetu, Niabudu Mola wetu, Rakaa na kusujudi

199. Abdalla akanena, Hasanta Maulana, Yamenipendeza sana, Kuja Maka kukaidi

200. Kama wewe kuja Maka, Utakalo ni kutaka, Inshalla litatendeka, Kula utaloradidi

201. Ulitakalo twambie, Hapana alibishaye, Twajua bwana ni wewe, Tangu jadi na jududi

202. Utakapo khalafati, Sasa takitoa kiti, Utamalaki Makati, Na jamii ya biladi

203. Nikuwali ukhalifa, Wa babuyo Musitafa, Na mweye kutaka kufa, Ni mwenye kukukayidi

204. Na asemaye hataki, Sharuti tamuhiliki, Na Yazidi Dimishiki, Tapanda mimi jawadi

205. Nitukue farisani, Wazoefu wa vitani, Kama simba ghadhibani, Walio kama asadi

206. Dimishiki nirikabu, Niuonyeshe barabu, Hadi ni kutaadabu, Yeye na wake juhudi

207. Ningie na bildiye, Nitafute asemaye, Nimuondoshe rasiye, Kula aliye hasidi

208. Pasibaki kabaili, Ambaye hatakubali, Huseni kamba ni kweli, Yote unayoradidi

209. Walakini ndugu yangu, Siupendi ulimwengu, Taka abudu Muungu, Ni huu wangu mradi

210. Sitaki usultani, Taka niwe masikini, Wala hayo sitamani, Kwenda wapiga jihadi

211. Nataka niketi Maka, Nimuabudu Rabuka, Wala sipendi kwondoka, Hata ifike ahadi

212. Hapano Maka sondoki, Na ukhalifa sitaki, Kisha sayo kunatiki, Wakenda wakarakidi

213. Baada hayo yuani, Kaketi Make Huseni, Wote walio mjini, Kupenda wakamzidi

214. Wakampenda sikia, Yeye na wake dhuria, Kula siku kuzidia, Mahaba mangi shadidi

215. Wote wakamjamili, Yeye na wake tifili, Na wake namarijali, Wakubwa na auladi

216. Wasitambike nufaa, Wala nguo za kuvaa, Wala nyumba ya kukaa, Tena akataabadi

217. Roho akaituliza, Akaabudu Aziza, Hata usiku wa kiza, Haramuni kisujudi

218. Kaabudu Mola pweke, Kwa kusafi moyo wake, Yeye na msala wake, Pasiwe na kurakidi

219. Akakithiri saumu, Na yake masitakimu, Yali ndani Haramu, Ikwa hiyo abadi

220. Asitake neno tena, Ila dini ya Rabana, Baada sayo nanena, Mambo baidi baidi

221. Nataka niyakutubu, Niyaweke babubabu, Nisije nikaharibu, Haja hambiwa kusudi

222. Nataka nielekeze, Kula kwa sifaze, Na utenzi upendeze, Nilio kuufanidi

223. Baada kupita hayo, Maneno niwambiayo, Sasa ni kutuza moyo, Niwakhubiri Yazidi

224. Kwondoka kwake Huseni, Kashika usultani, Kamiliki buldani, Kwa nguvu na uhasidi

225. Akawadhiki wenziwe, Wageni raiawe, Jamii wasitongoe, Pasi mwenye kuradidi

226. Watu akiwadhulumu, Na kula mna haramu, Na nguzo za Islamu, Zote asitaamidi

227. Wangine kiwadhurubu, Wala pasipo sababu, Akawa mnoa harabu, Kushinda hao Yahudi

228. Ndia zikafungamana, Pasiwe safari tena, Na ambaye amuona, Humwegema kwa hadidi

229. Kiwapoka watu mali, Wangine kiwakutuli, Ndia zote kazidhili, Za karibu na baidi

230. Pasiwe asafririye, Ala mtu enendaye, Kwa vitendo na haliye, Awatendavyo junudi

231. Kisha sayo nitamke, Katika kaumu yake, Mli mtu jina lake, Akitwa bun Ziadi

232. Jinale Abidallahi, Ali adui asahi, Dhuluma na ukabihi, Apita huyo Yazidi

233. Akichecha watu damu, Kwa jeuri na dhulumu, Hali akisha karimu, Ali jabari anidi

234. Yazidi kumuonakwe, Jeuri na hali yakwe, Kampenda yakwe, Pendo lisilo idadi

235. Kawa mtu maarufu, Tena akamsharifu, Akenda muweka Kofu, Akampa na biladi

236. Kampa katamalaki, Tangu Kofu na Iraki, Neno ambalo hataki, Pasiwe mwinua yadi

237. Akenda akaishika, Kakusa watu mashaka, Viumbe wakadhilika, Ikiwa kheri abidi

238. Jamii watu wa Kofu, Roho zikangia khofu, Kwa mambo yake dhaifu, Aliyo kutaahidi

239. Pasiwe mtu mzima, Wala naye heshima, Na mabaye uasema, Mara yamkaidi

240. Hunyang'anywa mali zao, Huuliwa wana wao, Hutwaliwa nyumba zao, Hali ya nguvu shadidi

241. Mali zao hutwaliwa, Na wao wakauawa, Na wasemalo haliwa, Wa sawa na 'kurudi

242. Wakakeleti mjini, Wakawa kama manyani, Mashekhe na madiwani, Nyuso zikawa sawidi

243. Pasiwe mwenye shauri, Wala anye amri, Kwa kushitadi jeuri, Akaptia Namrudi

244. Wa Kofu wakiyatunza, Dhuluma na miujiza, Wakamba hatutawaza, Dhuluma inatuzidi

245. Wakakutana kabili, Wote wazele wazele, Na mashaibu wa kale, Wasizo na 'lmuridi

246. Mashekhe na madiwani, Wakangia faraghani, Wakauzana yakini, Mwaionaje biladi?

247. Mwaonaje wenye nti, Na hakimu mwenye kiti, Tutaweza kuiketi, 'lKofu tukakhalidi?

248. Mwaonaje wenye kaya, Na huyo mwenye ulaya, Na mambo yake ni haya, Atutendayo abadi?

249. Kwa jamii wamwambie, Bunu Ziadi mamboye, Hapana ayawezaye, Yanatuchoma fuadi

250. Hatuwezi siku moja, Kuvumilia miuja, Kupigwa pasipo huja, Kama tunao jihadi

251. Kupigwa kama watoto, Kwa bakora na makoto, Haya ni mambo mazito, Hatuwenepo abadi

252. Kupigwa tukiuawa, Na mali yakitwaliwa, Wala hakutaadiwa, Si kwamba tuna taadi

253. Katungia kwa batili, Akatunyang'anya mali, Kuno akatukutuli, Mambo yanatupa hadi

254. Shauri na tufanyeni, Tuli hapa faraghani, Wangine wakabaini, Walio wana mradi

255. Wangine wakatamka, Yote yaliyotungika, Ya adhabu na mashaka, Tunayataka kusudi

256. Maana tuna yakini, Ezi na usultani, Si wake huyu laini, Wala babaye Ziadi

257. Wala si ya Muawia, Hawa wanajitwalia, Kutamalaki raia, Kampasaje Yazidi?

258. Sisi tu makabaili, Kutoka majitu mbali, Yakaja na ufedhuli, Katika zetu biladi

259. Wakatenda watakayo, Nasi tukaona ndiyo, Twabasa ni kama hayo, Hata yajapo tuzidi

260. Ezi si ya Marijani, Babuye huyo laini, Wala si ya Sufiyani, Babuye huyo Yazidi

261. Twayajua kwa makini, Ezi mwenyewe Huseni, Kwa babu yake Amini, Na baba yake Asadi

262. Twayajua maarufu, Jamii tulio Kofu, Kwondoka kwake Sharifu, Ezi ya wake waladi


1

UTENZI WA IMAM HUSEN

UTENZI WA KISA CHA SAYYIDNA HUSSEIN

263. Na Huseni kuwasili, Hasha haya hakubali, Ya dhuluma na batili, Zote tungetabaradi

264. Angeitengeza haki, Tangu Kofu na Iraki, Hata huko Dimishiki, Ikafika yake yadi

265. Jamii sote raia, Roho zingefurahia, Angehukumu sharia, Yake Muungu Wadudi

266. Nasi tungekuwa naye, Tukafuata eziye, Tukaola asemaye, Jamii tukamrudi

267. Hayo wakisha yasema, Jamii watu wazima, Wakaona kuwa mema, Kuwa kheri na suudi

268. Jamii wakatamka, Na twandikeni waraka, Na mtu wa kwenda Maka, Tumuarifu Sayyidi

269. Wakataka karatasi, Ikaja hima upesi, Na kalamu ya nukhasi, Na wino mtasawadi

270. Wakatafuta katibu, Fasihi wa kiarabu, Khati wakaikutubu, Maneno wakaradidi

271. Bismillahi Jalali, Ila mtoto wa Ali, Mjukuu wa Rasuli, Tumwa wetu Muhammadi

272. Ila Sayyidi Huseni, Bun binti Amini, Twakuarifu yakini, Kwetu yanayotubidi

273. Ajile mtu kabihi, Jinale Abidallahi, Miji ameifusahi, Kwa hali ya kufisadi

274. Na aliyetuletea, Ni ibunu Muawiya, Mambo yametuzidia, Hatuwezi kujimudi

275. Ameingia 'lKofu, Kwa mambo yake dhaifu, Sote tumetawakafu, Kama tunao baridi

276. Kaziye kula haramu, Na watu kuwadhulumu, Hapana mwenye makamu, Awezaye kuradid

277. Ataka badili dini, Ya babu yako Amini, Sote tuwe taghiyani, Tusujudie Yazidi

278. Mwenye mke si mkewe, Mwenye mwana si mwanawe, Ni kama kuku kwa mwewe, Hali alivyotushidi

279. Na sasa twakuarifu, Twakutaka uje Kofu, Wala usitawakafu, Alla Alla ya Sayyidi

280. Maana ndiwe Khalifa, Wa babuyo Mustafa, Na wasaliao Kofa, Wote ni wako abidi

281. Hima ni kutujilia, Utamalaki raia, Ambaye hakuridhia, Juu yetu kumrudi

282. Tukusalimu eziyo, Ya babuyo na babayo, Na mwenye kufanya payo, Tumuonyeshe hadidi

283. Na Yazidi akitaka, Harubati na shabuka, I juu yetu daraka, Kuwana nae Yazidi

284. Vita vyake twavikifu, Jamii tulio Kofu, Wala usitie khofu, Wajapokuja juradi

285. Twavitosha vita vyake, Yeye na kaumu yake, Bora ni wewe ufike, Uje tukupe biladi

286. Ni hayo maneno yetu, Tafadhali bwana wetu, Twakutaka kuja kwetu, Na haiba tusirudi

287. Wakaukunda waraka, Roho zilifurahika, Tena wakaupeleka, Kwa upesi na juhudi

288. Basi risala akenda, Akizikata ya nanda, Pa milima akipanda, Majimbo yote na wadi

289. Hata akafika Maka, Kwake Huseni pulika, Na rukhusa akitaka, Hodi wenye nyumba hodi

290. Tena kataka idhini, Kuonana na Huseni, Akambiwa pita ndani, Ndiko kunako Sayyidi

291. Yule risala kangia, Kwa Huseni kangukia, Kampa akapokea, Waraka kaufaridi

292. Akayasoma Huseni, Yaliyomo warakani, Kuyaonakwe yuani, Risala kamtwaridi

293. Kautwaa warakawe, Akatowa mkonowe, Akampiga usowe, Khati ikamjalidi

294. Akampiga mateke, Yeye na waraka wake, Yule risala anguka, Toba na toba Sayyidi

295. Akampiga mabawa, Kwa hali ya kutukiwa, Yule risala kaawa, Kakimbia asirudi

296. Kakimbia kenda zake, Yeye na waraka wake, Hata akifika kwake, Wenziwe kawaradidi

297. Faraghani kiwataka, Akawambia hakika, Yaliyompata Maka, Sikuupata muradi

298. Kwa jamii wakanena, Twandike waraka tena, Maana mambo twaona, Kula siku kutuzidi

299. Wakawandika wa pili, Na maneno wakakuli, Bwana wetu tafadhali, Tulitakalo tubidi

300. Ukenda tena waraka, Huseni kaghadhibika, Na watatu wakandika, Kwa shauku za fuadi

301. Mwaka haujatimia, Khati wakamwandikia, Idadi yake sikia, Khati alufu idadi

302. Zote za kumuarifu, Twakutaka uje Kofu, Na Maulana hashufu, Hajali hata wahidi

303. Kula waupelekao, Hupiga risala wao, Katwa wasipate shuo, Wala kukidhi mradi

304. Walipojua yakini, Hataki kuja Huseni, Khati wakaizaini, Maneno wakasanidi

305. Wakawandika waraka, Kumtisha kwa Rabuka, Na kumpa maalaka, Kesho mbele ya Wadudi

306. Barua wakayandika, Ewe Huseni pulika, Khati tumezipeleka, Nyingi hazina idadi

307. Khati haziidadiki, Twakwita uje Iraki, Na wewe kuja hutaki, Na sasa twakuradidi

308. Kesho mbele ya Khaliki, Tutakwenda kushitaki, Ukatupe zetu haki, Hapo mbele ya Wadudi

309. Tutamwambia Manani, Twalimwambia Huseni, Tuli hali duniani, Asitake kutufidi

310. Yote twalimkalimu, Ya kwamba tu madhulumu, Asitake tuhukumu, Akakataa kusudi

311. Nasi leo Mola wetu, Twazitaka haki zetu, Shaurilo bwana wetu, Lipi utaloradidi?

312. Haki zote utatoa, Za wenye kudhulumiwa, Ukae ukitambua, Na kwamba hayana budi

313. Wala huna la kusema, La kumjibu Karima, Hiyo siku ya kiama, Ila kulipa junudi

314. Utawalipa khaliki, Wa Kofu na wa Iraki, Huna utakakobaki, Ibada uloabidi

315. Kwisha kwandika barua, Risala wakamtoa, Barua kaitukua, Kenda hata kwa Sayyidi

316. Alipowasili Maka, Kwa Huseni akafika, Barua akaishika, Kusoma akiadidi

317. Alipokwisha isoma, Muwili ukatetema, Mfano anaye homa, Au la nyingi baridi

318. Huseni katetemeka, Kwa kumkhofu Rabuka, Na matozi kumtoka, Ndia mbele yakabidi

319. Matozi yakamuawa, Kwa kucha kushitakiwa, Na haki kwenda zitowa, Za jamii ya junudi

320. Akalia Maulana, Na kufazaika sana, Kwa kumkhofu Rabana, Watu kwenda mjalidi

321. Akisha kulia mno, Keta dawati na wino, Akayandika maneno, Kwa lafudhi tajididi

322. Waraka kaukutubu, Ila kafa 'lmuhibu, Maneno mulonijibu, Yamenichoma fuadi

323. Khati zalotangulia, Maneno mulonambia, Yote sikuyaridhia, Zote nalizitaridi

324. Wa ama khati ya mwisho, Imekithiri matisho, Kwenda nishitaki kesho, Kwa Mola wetu Wadudi

325. Nami sasa sina huja, Wala sina jambo moja, Litaloniasa kuja, Tasafiri sina budi

326. Nimemleta fahamu, Ndugu yangu Mselemu, Aje akae makamu, Ya sala na kusujudi

327. Akae msikitini, Na kadhi ni Nuamani, Awahukumu mjini, Kula mwenye kutaadi

328. Mselemu na asali, Na Nuamani ni wali, Na karibu tawasili, Kwa amri ya Wadudi

329. Kwisha kwandika fahamu, Kaufunga marukumu, Akamwita Mselemu, Ndoo hima bunu jadi

330. Mselemu kawasili, Maulana akakuli, Ewe ibni Akili, Sikia nakuradidi

331. Nenda ukatwae sefu, Uje nikutume Kofu, Na wendapo tawakafu, Uwasalishe junudi

332. Nenda kasalishe wewe, Nuamani aamuwe, Wala mangine yasiwe, Na mimi najizadidi

333. Nawakusanya ghulamu, Na tweka za bahaimu, Siku haba hazitimu, Ndio yangu makusudi

334. Mselemu ketikia, Marahaba mara mia, Hali ya kufurahia, Utumwa wake Sayyidi

335. Akanena Inshalla, Ewe aba Abdalla, Mimi naona fadhila, Nenolo tajitahidi

336. Hivi sasa nenda kwangu, Nenda twaa uda zangu, Niwaage na wanangu, Farasi tamjalidi

337. Akenenda Mselemu, Kaaga wake ghulamu, Akakaa na hasamu, Sefuye kaikalidi

338. Kamzaini farasi, Akampanda upesi, Roho ina wasiwasi, Kandamana na abidi

339. Wakenda pasi muhula, Yeye na yule risala, Wala pasiwe kulala, Hata kunako biladi

340. 'lKofu wakiwasili, Jamii ya kabaili, Wakafurahi kwa kweli, Furaha kubwa shadidi

341. Wote wakafurahika, Na roho zikasafika, Wakajua ni hakika, Atawasili Sayyidi

342. Hata kukicha yuani, Wakenda kwa Nuamani, Na waraka mkononi, Kapewa kaufaridi

343. Waraka kuusomake, Kafurahi roho yake, Na maneno atamke, Tahukumu sina budi

344. Namshukuru Rabana, Kuwasili Maulana, Tena adhabu hapana, Hana budi kutufidi

345. Akaketi Mselemu, Na watu kumkirimu, Kina wakimuheshimu, Heshima kubwa shadidi

346. Kasali msikitini, Na wote ajmaini, Asubuhi na jioni, Nahari na tasaridi

347. Ali akiwasalisha, Kwa magharibi na isha, Asubuhi huwamsha, Wakenda wakaabidi

348. Wote wakasali naye, Pasiwe akataaye, Akayakini rohoye, Dini watajitahidi

349. Na huyule Nuamani, Akahukumu mjini, Jamii ya khasimani, Kufunga na kujalidi

350. Sasa nyuma turudini, Niwakhubiri Huseni, Kuwatiakwe ndiani, Mselemu na abidi

351. Kimaa kutangulia, Na khati kuwandikia, Asinyamaze kulia, Kula mara akazidi

352. Akondoka hiyo hina, Kenda hata kwa Sakina, Na matozi kumpuna, Usoni yakajamidi

353. Akamwambia mwenzangu, Waliza nini ndu yangu, Huseni hwishi matungu, Daima zote abadi?

354. Huseni akatamka, Nimeletewa nyaraka, Alufu zenye kwandikwa, 'Lhaji hata 'Lkadi

355. Zote hazipurukusha, Ila hino ya kiisha, Ndio iliyonitisha, Kwa mambo yaloradidi

356. Wa Kofu wamenambia, Kesho mbele ya Jalia, Hawatakwenda ridhia, Watakwenda nijalidi

357. Wanitake haki zao, Hao wadhulumi wao, Au niwasili kwao, Hawondolee Yazidi

358. Na sasa tuwasafiri, Na tupandane bairi, Pasiwe tena usiri, Tutawakali Wadudi

359. Tupandeni twende zetu, Na wote watoto wetu, Waama haki za watu, Kesho zitaziadidi

360. Sakina akanatiki, Safari hiyo sitaki, Kwenda Kofu na Iraki, Wakwita kukuhusudi

361. Safari na ivundike, Wala usihadaike, Maneno yao sishike, Wale ni watu fisadi

362. Maneno yao kidhabu, Ndimi zao makilubu, Waweza wapi harubu, Asili yao Hunudi

363. Huseni akatamka, Safari haina shaka, Wala haitavundika, Kwenda zangu sina budi

364. Sakina akakalimu, Na kwamba umeazimu, Na tupishe Muharamu, Hata ingie Jamadi

365. Kwani Tumwa Muungamu, Alisema yako damu, Shahari 'l Muharamu, Ndipo itapomadidi

366. Nae Huseni anene, Sakina tusishindane, Kenda Huseni mwengine, Babu aliyeradidi

367. Na Sakina akakuli, Siku moja Jibrili, Alikuja kwa Rasuli, Na mchanga msafidi

368. Alitukua mchanga, Mzuri uketa anga, Rasuli akiufunga, Kitambaani jadidi

369. Jibrili kabaini, Mtanga wake Huseni, Siku zote uwoleni, Hata ukitasawadi

370. Muuonapo na damu, Tambuani imetimu, Ajali yake ghulamu, Kautwaa Muhamadi

371. Kampa mama Fatuma, Akenda uweka vema, Ningoja tautazama, Sasa hivi tutarudi

372. Sakina akaondoka, Akenda akaushika, Wote umehamirika, Tena umetasawidi

373. Kaja nao hima hima, Akamwambia tazama, Huseni katakalama, Subhana ya Wadudi

374. Huseni akadhukuri, Sina budi tasafiri, Rabi alilokadiri, Siwezi litabaidi

375. Kuona kwake Sakina, Hana budi Maulana, Akondoka iyo hina, Na matozi yakabidi

376. Kenda kwa bunu Zuberi, Akamweleza khabari, Na kushitadi safari, Wala nyuma hairudi

377. Abdalla akondoka, Kwa upesi na haraka, Kwa Maulana kifika, Kalia akaradidi

378. Abdalla akanena, Huseni utatupona, Wala usipo maana, Ya kwenda zako Sayyidi

379. Keti usende Iraki, Wala usitaharaki, Kwamba ni huo muluki, Utakapo maujudi

380. Ulitakalo twambie, Upesi tukufanyie, Huseni amrudie, Tasafiri sina budi

381. Wala sitazuilika, Msijikuse mashaka, Hivino sasa natoka, Nawe Abdalla rudi

382. Abdalla katongoa, Kheri nami nitukuwa, Kula litakalokuwa, Niwepo nilishahidi

383. Kwamba hapano hutaki, Maka kuitamalaki, Shati wenende Iraki, Twenende sote Sayyidi

384. Kwani watuwe jahili, Wala haya si ya kweli, Wakitwa kwenda kudhili, Ndio yao makusudi

385. Tawatukua kaumu, Wana wa bani Hashimu, Wavundao jiwe gumu, Na wenginewe junudi

386. Nende na watu alufu, Wa rumuhi na suyufu, Nende haipande Kofu, Kwa jeuri na taadi

387. Nitukuwe panga kali, Nende mimi hakuwali, Na asemaye si kweli, Nimtoe uritadi

388. Hakusalimishe nti, Pasi kuwa harubati, Niwete makubarati, Na ahali 'l biladi

389. Niwausie maneno, Shekhe Huseni huyuno, Pasiwe na mnong'ono, Wala mwenye kutaadi

390. Nisikize asemaye, Nimuangushe rasiye, Hata nti ituliye, Nishike ndia nirudi

391. Huseni akamjibu, Hasanta ya muhibu, Ama siyo matulubu, Wala si wangu mradi

392. Tatawakali Muungu, Nende mimi peke yangu, Na hawa watoto wangu, Sitaki mtu wahidi

393. Abdalla akalia, Kina akiombolea, Khatima akarejea, Asiweze mkaidi

394. Basi akazipakia, Twika twika za ngamia, Na watu wake dhuria,Katawakali Wadudi

395. Katukua panga kali, Watu sitini rijali, Wasio kucha mahali, Wangiapo hawarudi

396. Na sabaati ashara, Watoto wa watu bora, Sabuini anfara, Na sabaati zaidi

397. Asikari ni sitini, Na watoto wa Hasani, Na wake yeye Huseni, Saba ashara idadi

398. Wali vijana pulika, Wa ithnaashara Maka, Ila panapo shabuka, Wapita hao asadi

399. Kwisha sayo pakhubiri, Huseni akasafiri, Madinati munawiri, Ndipo alipokasidi

400. Sikuhaba kawasili, Madinati ya Rasuli, Akanenda tasihili, Kwa nduguye Muhamadi

401. Akiwasili nyumbani, Nduguye yu kitandani, Yuna maradhi zamani, Hawezi yote jasadi

402. Kumuonakwe nduguye, Akashituka rohoye, Kamba Huseni ni weye, Wenda wapi niradidi

403. Mbona una atifali, Na wake na marijali, Kama wendaye mahali, Tena kuliko baidi

404. Huseni akatamka, Ni kweli hayo hakika, 'l Kofu napenda fika, Ndiyo yangu makusudi

405. Kamwambia moja moja, Na khati zilizokuja, Na jamii ya miuja, Asibakie wahidi

406. Na khati ya kwishilia, Na waliyomwandikia, Nduguye akasikia, Akanena Muhamadi

407. Akanena La Haula, Illa billahi taala, Ewe aba Abdalla, Safari ya Kofu rudi

408. 'lKofu waisa nini, Ewe 'lakhi Huseni, Au kuna haja gani, Ni upi huko mradi?

409. Wa Kofu wakuhadaa, Na wewe yakakutwaa, Huwajui kwamba baa, Tangu jadi na jududi

410. Khasa sisi nyumba yetu, Jamii mauti yetu, Kula atokaye kwetu, Akenda Kofu harudi

411. Wameua baba yako, Na Hasani ndugu yako, Na wewe wenenda huko, Ili kwenda jihusudi

412. Na kwamba wataka kwenda, Safari huwezi vunda, Ngoja Rabi akipenda, Nione vema jasadi

413. Twandamane mimi nawe, Kula mtu upangawe, Tungie Kofu tuawe, Kwa amri ya Wadudi

414. Twenendapo panga mbili, Za wana wa Shekhe Ali, 'lKofu twaikabili, Kuingia na kurudi

415. Ila kwenenda pekeyo, Haunipi wangu moyo, Akisha kusema hayo, Huseni akamrudi

416. Takwenda mimi natosha, Sihitaji mshawasha, Wala sitaki juyusha, Kwandamana na junudi

417. Muhamadi akalia, Kwa kuto amridhia, Abdalla kaawiya, Bun Abbasi Sayyidi

418. Kamuuliza Huseni, Mbona una kharisani, Na wewe waliza nini, Ya 'lakhi Muhamadi

419. Huseni akadhukuri, Yakhi napenda safari, Akamweleza khabari, Kama yaliyo kubidi

420. Kamweleza tangu mwanzo, Khati apelekewazo, Khabari alizo nazo, Abdalla kiadidi

421. Huseni akimaliza, Abdalla akiwaza, Tena akimkataza, Kina akimradidi

422. Kamwambia tawakafu, Sende Iraki na Kofu, Kwa mambo yao dhaifu, Waliyo nayo abadi

423. Wa Kofu ni wanafiki, Uongo hawakutaki, Wala walio Iraki, Hao ndio mahasidi

424. Kwamba umependa moyo, Kusafiri ndia hiyo, Ngoja apoe nduguyo, Mtukue na junudi

425. Nami ningiye ndiyani, Nitukue farisani, Kama watu alufeni, Watambuao hadidi

426. Nende Kofu maridhiwa, Niingie na kuawa, Na ambae ajinuwa, Nimrudishe arudi

427. Nikakuweke Iraki, Hisha handame tariki, Nende zangu Dimishiki, Hamrakidhi Yazidi

428. Wendapo upanga wako, Na wangu ukawa huko, Thama nao ndugu yako, Upangawe Muhamadi

429. Zenendapo panga tatu, Tena hizi panga zetu, Tambua hakuna mtu, Awezaye tujalidi

430. Huseni akatamka, Abdalla pumzika, Hivino sasa natoka, Niombeani Wadudi

431. Sihitaji upangao, Wala huo usemao, Watosha nilio nao, Wa kula litalobidi

432. Akalia Abdalla, Bun Abbasi Fadhila, Na kusema La-Haula, Pamoja na Muhamadi

433. Na watu wote Madina, Jamii wakalizana, Kwa kwondoka Maulana, Yali msiba shadidi

434. Huseni asiridhike, Akenda kwa babu yake, Kenda zuru yeye peke, Khatimaye akarudi

435. Alipokwisha zuari, Kaitengeza safari, Katawakali Jabari, Kamwelekea Samadi

436. Hata bara akifika, Wakashuka malaika, Wana panga wameshika, Na silaha za jihadi

437. Wakamwambia Huseni, Tumeletwa ni Manani, Ili kwenda kuawini, Kwa kula litalobidi

438. Kwamba wataka twambie, Safari yako tungie, Hutaki turejeee, Huseni akaradidi

439. Huseni akawambia, Ni kheri kurejeea, Na apendalo Jalia, Amriye hairudi

440. Malaka wote yakini, Wakarejea mbinguni, Akenda zake Huseni, Hata kafika baidi

441. Akawaona majini, Ambao ni waumini, Wote wamejizaini, Kwa silaha za hadidi

442. Amiri wao kwa mbele, Fijaadumu jinale, Kaja kasimama mbele, Usoni kwake Sayyidi

443. Yule jini akakuli, Ewe ibnu Batuli, Kwenda peke sikubali, Nami nenda sina budi

444. Taichukuwa kaumu, Wenye silaha za sumu, Nende haingie Rumu, Niwachawanye junudi

445. Tawatukua watoto, Wenye dharuba nzito, Na marumuhi ya moto, Na silaha kama radi

446. Nikae usoni kwako, Kwa kula adui yako, Nimuonyeshe vituko, Atakaye tamaridi

447. Huseni akakalimu, Marahaba Fijadumu, Sitaki hata kaumu, Rudi na watuo rudi

448. Natawakali Jalia, Sitaki mtu mmoya, Majini wakarejea, Na matozi yakabidi

449. Katawakali Jabari, Mle katika safari, Akawaona namiri, Na ukuba wa asadi

450. Kaona chui na simba, Na kucha kama vigumba, Usonikwe wamewamba, Jamii wakaradidi

451. Wote kauli walete, Maulana twende sote, Adui tukawakate, Tule nyama tufaidi

452. Wala usitukataze, Sayyidi tutangulize, 'l Kofu tukailaze, Jamii iwe baridi

453. Huseni akawambia, Nyote ni kurejeea, Siwezi kulizuia, Alipendalo Wadudi

454. Hata mbele akifika, Akawaona majoka, Mbele yamejitandika, Wanao sumu shadidi

455. Kaona wamesimama, Majoka kama milima, Wote wakatakalama, Wakamwambia Sayyidi

456. Sayyidi situkataze, Twataka tukawameze, 'l Kofu tusiisaze, Jamii tuisafidi

457. Tutangulie usoni, Tukawatie tumboni, Uje kule na amani, Hakuna tena hasidi

458. Huseni akawajibu, Siyo yangu matulubu, Natawakali Wahabu, Aliye pweke Wahidi

459. Kwisha sayo pakhubiri, Wakamjilia tiri, Mbao wamezinashiri, Sanguri na kanfadi

460. Madege yenye midomo, Wala yasiyo ukomo, Wakaja kwa kitetemo, Akanena hodi hodi

461. Hodi hodi atongoe, Sayyidi wetu ni wewe, Twataka tukawambue, Kufari na mayahudi

462. Twataka tutangulie, 'lKofu tukaingie, Hata ukifika weye, Wote wamesitajidi

463. Maulana kadhukuri, Endani zenu tairi, Sitaki jeshi kathiri, Wa kwenenda nisaidi

464. Huseni asikubali, Wote niliowakuli, Akataka tawakali, Katika yake fuadi

465. Wote asiwaridhie, Pia walosema nae, Kataka yeye pekee, Kutawakali Wadudi

466. Katawakali Rabana, Mwenye ezi Subhana, Kwa usiku na mchana, Kenda akajitahidi

467. Baada hayo kukoma, Ya dhuria wake Tumwa, Natamani rudi nyuma, Niwakhubiri Yazidi

468. Mambo yasichanganyike, Moja moja niliweke, Yazidi kusikiakwe, 'lKofu yanayobidi

469. Akasikia hakika, Wa Kofu wamekwandika, Barua za kwenda Maka, Kumwamkua Sayyidi

470. Khati wamemuarifu, Idadi khati alufu, Wamtaka aje Kofu, Waje wampe biladi

471. Huseni hakuridhia, Na khati ya kwishilia, Yote waliyomwambia, Kesho mbele ya Wadudi

472. Na hivi sasa fahamu, Amekuja Mselemu, Kuwasalisha kaumu, Juu yake Masijidi

473. Na kadhi ni Nuamani, Ahukumuye mjini, Na Huseni yu ndiani, Na akali ya junudi

474. Nao wametangamana, Wa Kofu na Maulana, Na ukitaka pigana, Wao watamsaidi

475. Wakunyang'anye na ezi, Wakutwae wakuhizi, Usitambue makazi, Wala pa kwenda rajidi

476. Wakunyang'anye eziyo, Na jamii ya maliyo, Yazidi kupata hayo, Akili zikasharidi

477. Hayo akiyafasili, Zikamruka akili, Keta wino tasihili, Na lohi njema jadidi,

478. Waraka kaunasihi, Kwa khati njema malihi, Ya akhi Abidillahi, Sikia bun Ziadi

479. Khabari nimepulika, Kofu yanayotendeka, Huseni wamemtaka, Kwa shime na jitihadi

480. Wa Kofu na wa Iraki, Wamwita kutamalaki, Na mimi hawanitaki, Katika zao fuadi

481. Wametukiwa na miye, Watamani nangamiye, Ezi isinijuzie, Ni huo wao mradi

482. Na wote shauri moja, Huseni akisha kuja, Harubu hapana hoja, Na vita hapana budi

483. Na hivi sasa Huseni, Ametoka yu ndiani, Na kadhi ni Nuamani, Ndie kadhi maujudi

484. Na aliye tangulia, Ni Mselemu sikia, Naye wamemridhia, Kuwasalisha junudi

485. Aliyekuja fahamu, Jina lake Mselemu, Mwana wa bani Hashimu, Yumo katika biladi

486. Hayo nilipokwambia, Roho yakinishitua, Na kwamba nawe wajua, Basi u wangu hasidi

487. Kwamba unazo khabari, Hukuwa mtu wa kheri, Labuda mu mashauri, Wewe na hao junudi

488. Kwamba hunazo dalili, Basi enda tasihili, Ukifika kamdhili, Huyo mwenye masijidi

489. Kamuue Mselemu, Ajili mchache damu, Na rasi yake fahamu, Na ije huko baidi

490. Rasi yake niletea, Alla Alla nakwambia, Baada hayo sikia, Kwa Nuamani ubidi

491. Kamwambie Nuamani, Angie mwangu taani, Afanyapo ushindani, Ajili kumuhusudi

492. Umkate rasi yake, Utwae na mali yake, Na mjini uzunguke, Jamii wote junudi

493. Utenze anitakaye, Mali yake muwatie, Na mtu akataaye, Mkutuli asirudi

494. Umngoje na Huseni, Umtiye mautini, Na rasiye iyo hini, Ije na wake waladi

495. Huseni umuuapo, Rasiye na ije papo, Na jamii kilichopo, Wana na wake abidi

496. Ajili kuyafanyiza, Yote nilokuagiza, Nami najua waweza, Hayo na hayo zaidi

497. Najua yatafanyika, Pasipo kuharibika, Nisingali kukuweka, Hakupa na uSayyidi

498. Ni kukujua mamboyo, Waweza kufanya hayo, Na kadiri nitakayo, Wanikidhia mradi

499. Waraka kaukhitimu, Kaufunga marikumu, Kamsalimu hadimu, Kwenda kwa bun Ziadi

500. Akenda hima mtumwa, Pasi kuwa kasimama, Siku haba zikikoma, Kafika kwa jitihadi

501. Kuwasilikwe asahi, Akatoa mansahi, Kampa Abidillahi, Usoni kausujudi

502. Akisha kusujudia, Khati akiangalia, Yaliyokwandikwa pia, Jamii kayaadidi

503. Alipokwisha yaona, Maneno ya wake bwana, Akafurahika sana, Furaha kubwa shadidi

504. Akajua ni hakika, Yazidi ameniweka, Nitakalo lafanyika, Kwa pendo lake Yazidi

505. Baada sayo fahamu, Akaagiza kalamu, Na lohi njema ya Shamu, Khati akaimadidi

506. Ila bunu Muawia, Maneno ulonambia, Na mimi nalisikia, Na watu mtasharidi

507. Haona ni upumbavu, Nisiyashike kwa nguvu, Na kwamba sasa mapevu, Takwenenda sina budi

508. Bwana takutumikia, Kama uliyonambia, Jamii yatatimia, Uyatakayo Sayyidi

Tuliza nafusi yako, Sasa hivi nenda kuko, Najua ezi ni yako, Tangu jadi na jududi

510. Twajua bwana u wewe, Wala hako mwenginewe, Na asemaye welewe, Yuataka jihusudi

511. Rasi mbili utakazo, Naona kama matezo, Na jamii maagizo, Hata moja halirudi

512. Baada ya kuyandika, Kampa tume waraka, Akenda hima haraka, Kama kuvuma baridi

513. Kwa Yazidi kiwasili, Khati akaifasili, Akafurahi kwa kweli, Na mahaba akazidi

514. Baada sayo asahi, Kondoka Abidillahi, Akazipiga siyahi, Kawakusanya junudi

515. Akamba Ya maishara, Mlo mji wa Basara, Ajilini mwa hadhara, Mje tuole taadi

516. Wakakutana sufufu, Sitaashara alufu, Ambao ni mausufu, Watambuao hadidi

517. Wakafika wakasema, Ni wapi penye nakama, Aula penye kilema?, Tukirudishe kirudi

518. Naye akawaarifu, Naweta twende 'lKofu, Ndiko kwenye hitilafu, Wamuasio Yazidi

519. Wakayandama darubu, Kama rihi ya shabubu, Hali ya kutaghadhabu, Na roho kutasawidi

520. 'lKofu wakikaribu, Abidallahi kajibu, Akawambia sahibu, Taka nifanye mradi

521. Ngojani nitangulie, Wa Kofu niwangilie, Kwamba wanipenda mie, Tawaona sina budi

522. Akazifanya hadaa, Nguo nyeupe kavaa, Na ngamia kamtwaa, Na bakora msafidi

523. Kaiwata kaumuye, Akenda yeye pekee, Wa Kofu kumuonaye, Wakadhani ni Sayyidi

524. Wa Kofu na wa Iraki, Wakenda wakamlaki, Na furaha kusabiki, Katika zao fuadi

525. Jamii watu mjini, Wakadhani ni Huseni, Wakangia furahani, Iliyo kubwa shadidi

526. Pasiwe mtu kukaa, Wakatoka kwa fazaa, Kusudi kwenda mtwaa, Waje wampe biladi

527. Kufika wakamuona, Abidallahi laana, Kwa jamii wakanena, Hima upesi nirudi

528. Kumbe ni Abidallahi, Amekwisha tufedhehi, Roho zao zikatwahi, Kwa mara hiyo wahidi

529. Wakambiana ajabu, Mambo tumeyaharibu, Hatukwenda taratibu, Ndipo saya yakabidi

530. Abidallahi kangia, Na watuwe wote pia, Usiku kujilalia, Na wote wake junudi

531. Kulipokucha yuani, Kaamuru maluuni, Kulia mbiu mjini, Wakutane masijidi

532. Basi mbiu ikalia, Mwatakwa jote jamia, Basi jeshi ikangia, Waungwana na abidi

533. Wakenda msikitini, Ma Shekhe na Madiwani, Na wakubwa wa mjini, Na jamii ya muridi

534. Kimaa kukutanika, Abidallahi katoka, Msikitini kifika, Mimbarini akanadi

535. Kwa kweleza mimbari, Kanadi akidhukuri, Ya Maishara jifiri, Sikizani niradidi

536. Tumesikia yakini, Kwamba wenu Sultani, Mmemkiri Huseni, Hamumtaki Yazidi

537. Basi semani sadiki, Wa Kofu na wa Iraki, Yazidi hamumtaki, Kweli mmemtaridi?

538. Kimaa kuwauliza, Jamii wakanyamaza, Na tena likawataza, Neno watakalorudi

539. Jamii wakasakiti, Pasi mtoa sauti, Tena akatoa khati, Itokayo kwa Yazidi

540. Akausoma waraka, Jamii wakapulika, Yote yaliyo kwandika, Wakasikia junudi

541. Tena sapo akakuli, Nambiani tasihili, Maneno haya ni kweli, Nambieni maujudi?

542. Kimya wakanyamazana, Pasiwe mwenye kunena, Abidallahi laana, Kuwambia akazidi

543. Akawambia wa Kofu, Ili kuwatia khofu, Yazidi kaniarifu, Nije kwenu makusudi


2

UTENZI WA IMAM HUSEN

UTENZI WA KISA CHA SAYYIDNA HUSSEIN

544. Nimtazame ambaye, Huseni ampendaye, Nimuangushe rasiye, Na wote wake waladi

545. Na jamii mali yake, Niyatwae niyateke, Dimishiki nipeleke, Ni huo yangu mradi

546. Basi semani upesi, Nijue yenu jinsi, Wote wakenika rasi, Wa khofu nyingi fuadi

547. Jamii wakiolana, Khatimaye wakanena, Aliye bwana ni bwana, Huseni au Yazidi

548. Kwa kula atawalaye, Tutafuata eziye, Hatuna tukataaye, Ali yoyote Sayyidi

549. Kusikiakwe adui, Akaruka kama chui, Kawambia hamjui, Kwamba nyinyi mu abidi

550. Na Yazidi bwana wenu, Aliyemiliki kwenu, Ni haba akili zenu, Ujinga unawazidi

551. Kwamba mmemridhia, Zidi bunu Muawia, Afadhali kutulia, Make mtabaradi

552. Ambaye hakumtaka, Yuwatafuta hilaka, Mimbarini akishuka, Hayo akisha radidi

553. Kitoka msikitini, Akenda kwa Nuamani, Akampa anuwani, Itokayo kwa Yazidi

554. Alipokwisha ijua, Nuamani kamkua, Sisi hatuna uluwa, Wala hatu maSayyidi

555. Ila sisi tu raia, Twawapenda wote pia, Wala hatutakimbia, Kwa amri ya Wadudi

556. Kusikiakwe makali, Abidallahi jahili, Akamnyang'anya mali, Mangi yasiyo idadi

557. Beti asimbakiye, Ila ni yeye rohoye, Sababu asimwambie, Nimpendaye Yazidi

558. Kashukuru Nuamani, Na kuhimidi Manani, Baada sayo yuani, Abidallahi karudi

559. Kenda nyumba ya hukumu, Akawatoa kaumu, Katafuta Mselemu, Katika yote biladi

560. Na Mselemu sikia, Kipindi kilipongia, Ajili kukimbilia, Beti 'l masjidi

561. Akenda akaadhini, Kakaa msikitini, Wote walio mjini, Asimuone wahidi

562. Kasali yeye pekee, Hapo amfuataye, Kataajabu rohoye, Ajabu kubwa shadidi

563. Kwisha kusali yuani, Katoka msikitini, Kamuona ghulimani, Karibu amekaidi

573. Allahumma niauni, Unitie nusurani, Na jeshi ya maluuni, Bi shufaa Muhamadi

564. Mselemu akanena, Nambia ewe kijana, Leo mji nauona, Jamii wote baridi

565. Watu wametaharaki, Gharibi na mashariki, Kusali hawakutaki, Kijana akaradidi

566. Kijana akakalimu, Wailaka Mselemu, Huoni hawa kaumu, Walivyo kujizadidi

567. Jamii wamekuhuni, Hawakutaki mjini, Wala nduguyo Huseni, Hawapendi mshahidi

568. Akamwambia asahi, Mambo ya Abidallahi, Na roho zao kutahi, Na warakawe Yazidi

569. Na wewe wakutafuta, Na pindi wakikukuta, Kitwa chako kitakatwa, Kuuwawa huna budi

570. Ukae ukitambua, Huna budi kuuwawa, Mselemu kamkuwa, Subhana ya Wadudi

571. Akitazama yamini, Asimuone auni, Akiola shimalini, Asione msaadi

572. La haula akasema, Illa billahi Karima, Kamkua Allahumma, Ya Allahu ya Samadi

574. Mara ile kenda zake, Katwaa upanga wake, Ilihamu roho yake, Na matozi yakabidi

575. Silaha kajizaini, Roho haina makini, Akatembea mjini, Makusudi kusharidi

576. Azima ni kukimbia, Hanapo pa kuawia, Mumule katika nyia, Pana nyumba msafidi

577. Na nyumba hiyo yuani, Mwenyewe akitwa Khani, Ali mzee zamani, Wa tangu jadi na jadi

578. Lakini ni Islamu, Yu dini ya Muungamu, Na wote bani Hashimu, Kiwapenda jitihadi

579. Akiwapenda sikia, Dhuria wake Nabia, Na wote 'l Hashimia, Pendo lisilo idadi

580. Kenda kwake Mselemu, Mlangoni akakumu, Kamuuliza khadimu, Yu wapi wako Sayyidi

581. Na kwamba yu humo ndani, Mwambie pana mgeni, Kenda hima ghulumani, Khani akamradidi

582. Mzee Khani kajibu, Na'pite hima gharibu, Akapita Muarabu, Mlango kaukaidi

583. Wakenda wakaonana, Khabari wakauzana, Mselemu akanena, Kama yaliyombidi

584. Khabari akamweleza, Tokea mwanzo wa kwanza, Na jamii miujiza, Hata ya bunu Ziadi

585. Na hivi sasa rijali, Wa kati kunidalili, Wapate kunikutuli, Kwetu Maka nisirudi

586. Kisha sayo kutamka, Khani akaghadhabika, Kwa hayo yalofanyika, Ghadhabu kubwa shadidi

587. Kanena mzee Khani, Na kwamba yali zamani, Sasa ningejizaini, Henda hawa na jihadi

588. Kama banii Hashimu, Huwaje kuwalaumu, Ukataka wadhulumu, Huo ndio wa hasidi

589. Lakini sasa pulika, Hapa umesitirika, Kwa amri ya Rabuka, Watakwisha usitadi

590. Na huyo akutakaye, Rafiki yake ni miye, Labuda asisikiye, Kwamba siwezi jasadi

591. Lakini asikiapo, Hana budi kuja papo, Na pindi hapa ajapo, Kumuua huna budi

592. Ajapo akiwasili, Taja kuweka mahali, Na upangao mkali, Ungoje akikaidi

593. Taja muwekea kiti, Hata akisha keleti, Umuonyeshe mauti, Ahimari na suwedi

594. Akisha kusema hayo, Mselemu kamba ndiyo, Akafurahika moyo, Kwa Khani aloradidi

595. Abidallahi hakika, Siku mbili zikifika, Roho akatia shaka, Khani hajamshahidi

596. Kauliza barazani, Yu wapi mzee Khani?, Kambiwa yuko nyumbani, Ana maradhi shadidi

597. Mara kondoka kitini, Kusudi kwenda kwa Khani, Akipata mlangoni, Kamba wenye nyumba hodi

598. Kisikia sautiye, Wakajua kwamba ndiye, Tena Khani amwambie, Mselemu jizadidi

599. Shika sefu na turusi, Ukae pia nafasi, Hata akisha jilisi, Sikawe kumhusudi,

600. Mselemu kajifita, Paziani akapita, Na sefu kaitafuta, Isiyo shaka na budi

601. Akiweka na siriri, Akitengeza vizuri, Tena kapewa amri, Kupita bun Ziadi

602. Basi akapita ndani, Akaonana na Khani, Mselemu faraghani, Seifi kaikalidi

603. Tena kampa maungo, Khani akamba Muungu, Leo atakata shingo, Ipukane na jasadi

604. Kakaa muda mzima, Khani akaona kimya, Kafazaika mtima, Mbona kimya kinazidi?

605. Basi akatoa fumbo, Kama aimbae wimbo, Akamba mambo si mambo, Si ya jadi na jududi

606. Hino ndiyo kazi yenu, Mliyozoea kwenu, Si kazi yao sununu, Katika zote abadi

607. Kutuka akamuonya, Ni kazi yenu mwafanya, Wala sikukudanganya, Niliyokupa ahadi

608. Nakwambia mara zote, Simama ukiokote, Na lijirilo tu sote, Kwa amri ya Wadudi

609. Khani akisha yasoza, Fumbo la kumuhimiza, Mselemu kanyamaza, Hata saa ikabidi

610. Kasema mara ya pili, Mselemu katwawili, Abidallahi kakuli, Naona mwataradidi

611. Unani mzee Khani, Kwondoa taji kitwani, Ukabanja kitandani, Khatima ukalirudi?

612. Mara wavua kilemba, Na mara nyimbo ukimba, Unani katika nyumba, Jambo lililokuzidi?

613. Mzee Khani kakuli, Ni jua liwapo kali, Hunipungua akili, Na ndwele ikashitadi

614. Ndipo hivi hafanyiza, Fiili na miujiza, Ni ndwele imenikaza, Na akili msharidi

615. Abidallahi kasema, Kwa kheri narudi nyuma, Nijile kukutazama, Khani akenda muwadi

616. Aliporudi nyumbani, Kasema mzee Khani, Mselemu jinsi gani, Usitimize ahadi?

617. Mselemu akakuli, Sefu yali masiluli, Hataka kumkutuli, Hazuiwa yangu yadi

618. Hitaka mwandika sefu, Nimpasue nusufu, Nikasikia khatifu, Na mnada ukanadi

619. Mnada ukatongoa, Usende ukamuua, Na muili hazuiwa, Kujondoa sijimudi

620. Ndipo saya yakajiri, Na zohali na usiri, Na Khani akadhukuri, Kheri ni yake Wadudi

621. Baada sayo asahi, Kondoka Abidallahi, Akili katanabahi, Kuzichawanya nakidi

622. Roho yake kaazimu, Azitoe darahimu, Atafute Mselemu, Kwa akili na juhudi

623. Kamwamkua rijali, Jina lake Muakali, Ubazazi na khitali, Apita wote junudi

624. Dinari kazihesabu, Alufu tatu dhahabu, Na maneno kamjibu, Shime yakhe jitahidi

625. Mtafute Mselemu, Kwa akili na fahamu, Ukampe darahimu, Ukisha mpa urudi

626. Ujue nyumba aliyo, Kwa rai na akiliyo, Muakali kamba ndiyo, Inshallah tajitahidi

627. Akondoka Muakali, Akayatukua mali, Akenda akadalili, Katokea masijidi

628. Akaona msikiti, Kaingia akaketi, Ilipofika salati, Akaja mtu wahidi

629. Jina kitwa Mselemu, Bun Ghaushi fahamu, Kaja kampa salamu, Na heshima kamzidi

630. Kamwambia ndugu yangu, Takupa faragha yangu, Maana humu si mwangu, Mimi natoka baidi

631. Mimi ni mtu wa Maka, Huseni kanipeleka, Nitukuzie waraka, Na mali yaso idadi

632. Nijile na darahimu, Kuja mpa Mselemu, Na alipo sifahamu, Nimekwisha usitadi

633. Na kuuliza siwezi, Mji unavyo makonzi, Na mimi ni mwanagenzi, Sijui mtu wahidi

634. Na wewe kukubaini, Ni kwamba natumaini, Yakhi fanyiza hisani, Na haiba nisirudi

635. Twende ukanipeleke, Hampe amana yake, Hima upesi nitoke, Humu siwezi rajidi

636. Kanionyeshe upesi, Hapo alipojilisi, Roho ina wasiwasi, Mselemu karadidi

637. Kanena bunu Ghausha, Takwenenda kuonyesha, Lakini niaminisha, Kwa mithaki na ahadi

638. Muakali kabaini, Nakuapia yamini, Nami ni msikitini, Ni katika masijidi

639. Kisha apa sura mia, Mara iyo kamwambia, Nyumba alokimbilia, Ya banii 'l Asadi

640. Mselemu yu nyumbani, Huko kwa mzee Khani, Muakali kibaini, Kenda hima na juhudi

641. Alipofika nyumbani, Kabisha kangia ndani, Akamwambia yakini, Nijile nina zawadi

642. Kamtaka Mselemu, Kwa wema na tabasamu, Akampa darahimu, Akisha kamradidi

643. Akamwambia Huseni, Ametoka yu ndiani, Atakuja kuawini, Kama yaliyo kubidi

644. Amenipa diinari, Utakako ushitiri, Kula kipasacho shari, Chombo kilicho jadidi

645. Nami hivi nenda zangu, Nina khofu roho yangu, Nakuhongea mwenzangu, Nawe kujificha zidi

646. Kaamini Mselemu, Kapokea darahimu, Akampa na salamu, Nisalimia Sayyidi

647. Muakali akatoka, Kwa upesi na haraka, Barazani akifika, Kwake ibnu Ziadi

648. Muakali akanena, Kamwambia wake bwana, Umekwisha patikana, Uliotaka mradi

649. Khani bin Ghuruata, Ndiye aliyemfita, Hivi tukimtafuta, Anaye zote abadi

650. Kwambiwa kwake juhali, Kawamkua rijali, Majina yao nakuli, Wa kwanza ni Muhamadi

651. Wa pili etwa asema, Na Omari kawatuma, Akamba nendani hima, Khani mukamkaidi

652. Wakenda na furisani, Wakenda mtwaa Khani, Akifika barazani, Salamu akaradidi

653. Jamii wakanyamaza, Kwa hali ya kutukiza, Abidallahi kauza, Kwani Khani kutaadi?

654. Wamficha Mselemu, Nasi ni wetu khasimu, Wewe u mwenda wazimu, Akili umesharidi

655. Naye Khani atongoe, Mwenda wazimu u wewe, Utakae umuuwe, Bin ami Muhamadi

656. U wewe mwenda wazimu, Utakaye Mselemu, Nikupe umdhulumu, Upate kumhusudi

657. Mara akaghadhibika, Abidallahi karuka, Bakora akaishika, Kitaka kumjalidi

658. Khani alipomshufu, Akaikabili sefu, Kamwegema asikhofu, Kama umeme na radi

659. Dharuba kamsukuma, Akazikata kwa nyuma, Kofia mbili za chuma, Na dirii za hadidi

660. Abidallahi kanguka, Kwa kiwewe kumshika, Roho ikafazaika, Akawambia junudi

661. Kawambia tasihili, Mshikeni mumdhili, Asijesha wakutuli, Khani akaiadidi

662. Akaishika hasama, Jeshini akajitoma, Mithili wimbi la joma, Livumalo na baridi

663. Kawangusha iyo hini, Khamsa wa ishirini, Bi tarafati aini, Kaumu wakamzidi

664. Wakampiga asira, Akafungwa kwa kambara, Na kumpiga bakora, Na dharuba za hadidi

665. Kashahadia Karimu, Kafa ali Islamu, Fi'l janati naimu, Akenda akarajidi,

666. Khabari zilipofika, Nyumani kwake hakika, Mselemu akatoka, Na jitimai shadidi

667. Katoka na jitimai, Hana hila wala rai, Ali katika sarai, Kaona nyumba baidi

668. Nyumba hiyo nitamke, Kamwona mwanamke, Kamuuza hali yake, Yote akamradidi

669. Kasikia nisiwani, Akamba pita nyumbani, Kwani adui mjini, Wa kati kukuadidi

670. Akapita Mselemu, Harume kamuheshimu, Ali na wake ghulamu, Yeye mmoja waladi

671. Kumuonakwe mamaye, Ana fazaa rohoye, Akamuuza haliye, Mama umetasawidi

672. Ni kungia ukatoka, Kitu gani umeweka, Mamaye akatamka, Sikia ewe waladi

673. Nyumbani mna ghulamu, Jina lake Mselemu, Min bani Hashimu, Bin amu Muhamadi

674. Na mimi nimemsiri, Ahadi ni kusafiri, Kijana akadhukuri, Mama kumficha zidi

675. Mara ile akatoka, Barazani akafika, Watu wamekutanika, Kamwita bun Ziadi

676. Yule kijana kasema, Mselemu yu kwa mama, Wapeleke watu hima, Mimi nimemshahidi

677. Kwa mama ndiko aliko, Na mimi natoka huko, Adui keta kacheko, Na kufurahi shadidi

678. Mara ile kasimama, Akawataka kauma, Akamba nendani hima, Na amiri Muhamadi

679. Bun Shiati amiri, Akampa asikari, Khamsamia jifiri, Walio kama asadi

680. Kamwambia tangulia, Mselemu niletea, Basi akashika ndia, Kandamana na junudi

681. Mselemu pakhubiri, Kasikia hawafiri, Na kishindo cha bairi, Kajua ndio hasidi

682. Kamwambia nisiwani, Kanipe maji kuzini, Nisali rakaateni, Nipate omba Wadudi

683 Kasali rakaateni, Akamuomba Manani, Baada sayo yuani, Kamrakibu jawadi

684. Akampanda farasi, Na upanga na turusi, Akamuomba Kudusi, Kawakabili junudi

685. Mbele yao kasimama, Kawauza akasema, Ajili semani hima, Nijue wenu mradi

686. Lililowaleta nini, Msikawe nambiani, Na ambalo mwatamani, Mutafutalo kusudi

687. Mara walipomshufu, Wakamwegema kwa sefu, Wapate kumtilifu, Afungwe kama abidi

688. Kajitia katikati, Akawonesa mauti, Watu khamsamiati, Watu kumi wakarudi

689. Kawapiga kama huwa, Kukata na kuangua, Kama radi ilotia, Shajaria 'l jadidi

690. Akawatawanya damu, Ikenenda milizamu, Wakarejea kaumu, Hata kwa bun Ziadi

691. Wakenda wakimwambia, Kama yaliyo jiria, Sote hatukubakia, Tumebadia suudi

692. Kusikiakwe yuani, Kawatoa shujaani, Idadiye alufeni, Wasioweza taadi

693. Akawambia nendeni, Mselemu mleteni, Msishindwe ni mgeni, Aliyetoka baidi

694. Endani mkamtwae, Upesi muniletee, Tupate hiyo rasiye, Apelekewe Yazidi

695. Wakenenda asikari, Kama rihi na matari, Na kula mtu tayari, Kwa silaha za hadidi

696. Walipomkaribia, Mselemu kawangia, Jeshini kajipakia, Na farasiwe najidi

697. Akamrusha kimatu, Akaja ndani ya watu, Isipate saa tatu, Wote akawasafidi

698. Akaishika hasamu, Mwana wa bani Hashimu, Akawatawanya damu, Nchi yote ikabidi

699. Akinga simba dharia, Damu ikenda milia, Na watu wakangamia, Wangi wasio idadi

700. Yamini kajipeleka, Wanguka kama mataka, Hata akizungumka, Kupigana akazidi

701. Kawatia mautini, Wote watu alufeni, Wakabaki thelathini, Wasihimili hadidi

702. Wakenda kwa bwana wao, Wakampa hali yao, Wakamba siku ya leo, Adui katuhusudi

703. Tulipowasili kando, Katungia kama nondo, Akitutenda kitendo, Hatuwezi kuradidi

704. Katungia kwa upanga, Jeshi yote kaizinga, Pasi muweza kukinga, Wala mkaa baidi

705. Bwana fanyiza shauri, Adui katuhasiri, Kwambiya siyo khabari, Kawakusanya junudi

706. Kawakusanya sufufu, Ambao ni mausufu, Ithnashara alufu, Akaja kawaradidi

707. Akawambia kaumu, Endani kwa Mselemu, Na mrudipo haramu, Mauti yatawabidi

708. Ambapo mwarejeea, Msipo kuniletea, Tawataka vitwa pia, Hayo nimewaahidi

709. Basi ikenenda jeshi, Kama dharuba ya tushi, Na kutaharaki nchi, Kwa hafiri za jawadi

710. Wakamfika alipo, Wakenda muona yupo, Mselemu iwenepo, Ghadhabu akashitadi

711. Upanga kauzungusha, Farasi akamwegesha, Ukinga mwamba kuusha, Na wingu kubwa na radi

712. Muili ukanafiri, Kwa ghadhabu kukithiri, Kiruka kama namiri, Ghadhabu kinga asadi

713. Dharuba akizitoa, Kama umeme na kuwa, Na kipovu kumuawa, Likachemka zubadi

714. Alikikabili mbele, Kusibakie kisele, Akileneza fumole, Watu hamadi hamadi

715. Muili ukamvimba, Kimatu akinga simba, Mara moja kawaramba, Watu mia wakarudi

716. Barazani wakifika, Mtangani wakanguka, Maneno wakitamka, Sikia bun Ziadi

717. Leo tuwene harubu, Iliyo kubwa ajabu, Vita vyake Muarabu, Ataitwaa biladi

718. 'l Kofu itatwaliwa, Ukae ukitambua, Na wewe utauwawa, Ni huyo mtu wahidi

719. Harubu apiganavyo, Hatuwene kama hivyo, Jamii vita twandavyo, Hatuwenepo abadi

720. Muarifu mwenye nchi, Atudirikiye jeshi, Ila sisi hatutoshi, Kupata huo mradi

721. Fisa khati Dimishiki, Watuletee khaliki, Na Basara na Iraki, Na wakutane junudi

722. Na ufanyapo dhihaka, Usipeleke waraka, Tambua unamtoka, Ulua wake Yazidi

723. Kwambiwa hayo asahi, Keta wino na lauhi, Kandika Abidallahi, Sikia ewe Sayyidi

724. Akaikutubu khati, Ya Yazidi mwenye nti, Tu katika harubati, Na vita vimetuzidi

725. Vita vyake Mselemu, Vyapita jabali gumu, Turidikie kaumu, Hima wapate tufidi

726. Wote watu maarufu, Katika nti ya Kofu, Jamii wametilifu, Watambuao hadidi

727. Mselemu atashinda, Na nti ataivunda, Atakalo atatenda, Ni hayo nakuradidi

728. Ulipokwenda waraka, Kwa Yazidi ukafika, Maneno akipulika, Uso ukamsawidi

729. Kanena akitukana, Watu wa Kofu naona, Hawawezi kupigana, Tokea jadi na jadi

730. Huwaje mtu mmoja, Akajirisha vioja, Tena wakatoa hoja, Kwamba avunja biladi

731. Tapeleka farisani, Kama simba ghadhibani, Mselemu na Huseni, Wakawatoe taadi

732. Kawakusanya sufufu, Watu sitini alufu, Ambao ni mausufu, Wasio shaka na budi

733. Kawambia enendani, Mkifika washikeni, Mselemu na Huseni, Upesi hima murudi

734. Basi jeshi ikatoka, Wakapanda wakishuka, Siku haba zikafika, 'l Kofu wakaibidi

735. 'l Kofu wakiwasili, Jamii wote rijali, Wakafurahi kwa kweli, Kwa kuwasili junudi

736. Wakelezana khabari, Za awali na akheri, Na kama yaliyojiri, Wasibakie wahid

737. Hata kukipambazuka, Basi jeshi ikatoka, Kusudi kwenda mshika, Bun amu Muhamadi

738. Alipokwisha waona, Mselemu kakazana, Meno akajitafuna, Mfano kama asadi

739. Kuionakwe shabuka, Mshipa ukamwinuka, Na tauka na tauka, Na kukazana jasadi

740. Jasadi ikahariki, Akinuka na uruki, Wote wakataharuki, Wasiweze mjalidi

741. Kizinga kama umeme, Kushotoni na kulume, Wali papo wasimeme, Na khofu kubwa shadidi

742. Akaipiga siahi, Ikavuma kama rihi, Zikawapuna silahi, Zilizo katika yadi

743. Akamzinga rikabu, Alisimika dhanubu, Na jamii ya ghadhabu, Siku hiyo akazidi

744. Uso ukaghadhibika, Mato yakahamirika, Na kipovu kumtoka, Yeye na wake jawadi

745. Akajitia jeshini, Akawachenga laini, Ali akenda usoni, Na kinyume akarudi

746. Akanenda kwa shimali, Akawachenga rijali, Kija upande wa pili, Ikiwa hivyo abadi

747. Mselemu kiwangua, Kama matone ya mvua, Pasi muweza jinua, Wala enuaye yadi

748. Na ambaye akabili, Mara huwa mbali mbali, Kushotoni na kuvuli, Wote wakatabaadi

749. Wakatamani kimbia, Hapana pa kuawia, Hali ya kuwazuia, Pasiwe muweza rudi

750. Mselemu akawesha, Kuwaua kiwangusha, Wote akawababusha, Wakawa kama rimadi

751. Siku hiyo maarufu, Arubaini alufu, Aliyo kuwatilifu, Wasazao wakarudi

752. Jamii wakakubali, Kuvushwa nchi ni kweli, Wala hataki wa pili, Kutunyang'anya biladi

753. Mashauri wakanena, Na tutoeni vijana, Twende nao mbali sana, Tukawafiche baidi

754. Hana budi Mselemu, Ataimiliki Rumu, Awaue na kaumu, Ashike ndia arudi

755. Wakawatoa kabili, Wana na wao wavyele, Na walio na uwele, Vipofu na makaidi

756. Wakawatoa viwete, Na wenye madonda wote, Mmoja wasimuate, Ila walio jadidi

757. Wakenenda ughaibu, Hata ipite harubu, Baada sayo najibu, Wakakutana junudi

758. Wakakutana kaumu, Thamaanini timamu, Alufu zilizotimu, Isipungue wahidi

759. Basi shauri waseme, Twendeni tukamwegeme, Mmoja asisimame, Ataghumiwa jawadi

760. Farasi akighumiwa, Mara moja atajiwa, Basi sapo wakaawa, Wote wakajizadidi

761. Hata walipomfika, Jeshini kajichomeka, Kupita zote shabuka, Wote wakamsharidi

762. Kawachawanya khumra, Ikenea zote bara, Na mafisi waking'ara, Kwa hali ya kufaidi

763. Akawatenda kitendo, Kuwachawanya uvundo, Kiwopoa kama nondo, Amezaye 'lkurudi

764. Farasiwe apitapo, Hapabaki aliyepo, Kama wingu na upepo, Na dharuba na baridi

765. Akiwangamiza watu, Idadiye wanakwetu, Alufu kumi na tatu, Waliokufa junudi

766. Wote waliobakia, Jamii wakakimbia, Mselemu kawendea, Na sefuye ya hadidi

767. Kiwapiga kwa hasamu, Akawachanganya damu, Wakawa kama ghanamu, Walio katika nadi

768. Kapiga kiwangamiza, Kuno akiwafukuza, Wote wakijelemeza, Masaharati na wadi

769. Wakenda mtashatiti, Kwa kuyakhofu mauti, Wakaikimbia nti, Wote ahali biladi

770. Mselemu akazinga, Akampita kipanga, Mji wote akatanga, Asimuone wahidi

771. Akaizuia Kofu, Thuluthani na nusufu, Na majumba maarufu, Yakawa katika yadi

772. Nusu ya mji baadhi, Yote kaitakabidhi, Pasiwe mtaaradhi, Wala mwenye kutaadi

773. Katamalaki majumba, Mazuri yaliyopambwa, Mwana wa simba na simba, Ni kazi yao abadi

774. Na jamii ya rijali, Kukionakwe kitali, Wakakutanika mbali, Wasiiweze biladi

775. Jamii wakakimbia, Mji wakamuatia, Walipokwisha tulia, Shauri wakafanidi

776. Shauri wakelekeza, Jawabu la kufanyiza, 'lKofu tukakweleza, tukamwondoa hasidi

777. Pana mmoja kanena, Hapana shauri tena, Mji unasha tupona, Na kufa hatuna budi

778. Hawa ni asili yao, Kuwana ni kazi yao, Na ushujaa wa kwao, Jadi zao na jududi

779. Ndio simba wa Mungu, Wanywesa watu matungu, Na katika ulimwengu, Hako aliyewazidi

780. Na roho yangu hiwaza, Yule hatutamuweza, Shauri la kufanyiza, Hapana ila wahidi

781. Na tutimbeni handaki, Ajapo akisabiki, Tufanye kutaharuki, Kinyumenyume turudi

782. Atangia handakini, Tumtie mikononi, Jamii wakayakini, Shauri linalobidi

783. Wakaichimba rijali, Yali usiku laili, Na shimo likenda mbali, Tena wakalisafidi

784. Juu wakalifinika, Farasi akija ruka, Hana budi kuanguka, Kumshika hana budi

785. Kulipokucha sikiza, Wakaitaka baraza, Mselemu katokeza, Mtamboni akanadi

786. Alipokuwatokea, Jamii wakakimbia, Mbele akiwandamia, Na sefuye ya hadidi

787. Kupata punde usoni, Farasi kanguka tini, Akangia handakini, Akaumia jawadi

788. Farasi akavundika, Na Mselemu kanguka, Wakaja wakamshika, Jamii wote junudi

789. Wakakutana asahi, Wakazipiga siahi, Na roho zilifurahi, Furaha kubwa shadidi


3

UTENZI WA IMAM HUSEN

UTENZI WA KISA CHA SAYYIDNA HUSSEIN

790. Wakamfunga kwa kweli, Mikono yote miwili, Wasimbaki pahali, Wasipo kumkaidi

791. Mselemu kamkuwa, La haula wala kuwa, Aladi qalu Molewa, Kujiri halina budi

792. Wakenda naye hakika, Wote walifurahika, Barazani wakifika, Mbele ya bun Ziadi

793. Wakamuweka usoni, Mbele yake maluuni, Abidallahi yuani, Maneno akaradidi

794. Kamwambia Mselemu, Enyi banii Hashimu, Mtakao jidhulumu, Mwatezea maSayyidi

795. Hivi kwenu mkitoka, Kuja Kofu na shabuka, Makusudi kumpoka, Ulua wake Yazidi

796. Mpate usultani, Wewe na huyo Huseni, Mukaishi duniani, Muwe watu maadudi

797. Mtamalaki Iraki, Na Kofu na Dimishiki, Na Yazidi mumdhiki, Ndiyo yenu makusudi

798. Mjile taka matata, Na vitwa vyenu kukatwa, Hayo hamtayapata, Hata mkajitahidi

799. Mselemu kabaini, Wayy-laka maluuni, Wadharauje Huseni, Ukamsifu Yazidi

800. Sakiti ulimi wako, Kwamba si hadaa zako, Ningekuonya vituko, Vikubwa visivyo budi

801. Na kwamba si kunitenga, Nti ningalizipinga, Haziwata nyonganyonga, Hamngojea Sayyidi

802. Hata akija Huseni, Akaikuta amani, Na ambaye mshindani, Akija hamhusudi

803. Mtu wa pili sitaki, Wa 'l Kofu na Iraki, Peke yangu nawadhiki, Mkaitoka biladi

804. Na sasa matungu yangu, Sijutii roho yangu, Nakumbuka ndugu yangu, Yatakayo kumbidi

805. Namkumbuka Huseni, Na jeshi ya maluuni, Wala hanayo yakini, Kwamba wametamaradi

806. Baada sayo nanena, Abidallahi laana, Akawambia watwana, Endani naye baidi

807. Mkamkate rasiye, Ajili mniletee, Watumwa wakenda naye, Wakenda kumuhusudi

808. Akenda akauwawa, Shahada akamkuwa, Ya Rabi wake Molewa, Na Mtume Muhamadi

809. Kashahadia Jalali, Na Mtume Murisali, Wakisha kumkutuli, Roho yake naradidi

810. Roho yake Mselemu, Ikenda fi 'nnaimu, Hurri 'l aini fahamu, Wote wakashua yadi

811. Mikono wakashuua, Rohoye ikapokewa, Fi'l jana ikatiwa, Kunako njema baridi

812. Kisha sayo niwambie, Wakaitwaa rasiye, Na ya Khani rafikiye, Zote wakazijalidi

813. Kitwa chake muumini, Na kile kitwa cha Khani, Vikenda kwa Sultani, Hakimu wao Yazidi

814. Kifika vikatolewa, Yazidi kafurahiwa, Na kaumu kaitoa, Nyingi isiyo idadi

815. Akawambia endani, Mkamngoje Huseni, Mkifika simamani, Nyinyi na bun Ziadi

816. Huseni akiwasili, Upesi kumkutuli, Na rasiye tasihili, Na ije pasipo budi

817. Basi wakenda khaliki, Wana panga kwa mikuki, Wakiwasili Iraki, Na Kofu wakakhalidi

818. Wakaketi kusikiza, Na watu kupeleleza, Kula ndia wakitunza, Kumtazama Sayyidi

819. Hata sikuye kwa mbele, Khabari wazisikile, Kwamba Huseni ajile, Hayuko tena baidi

820. Kaja aba Abdalla, Inshaallah taala, Naye yupo Karabala, Hapo shatii' l wadi

821. Karabala amefika, Na kesho atakondoka, Siku haba zikifika, Aja miliki biladi

822. Abidallahi pulika, Kuipatakwe hakika, Mno akafurahika, Na kutengeza junudi

823. Katengeza asikari, Bi yamini wa yasari, Na kula penye khatari, Kapatengeza jadidi

824. Akazizuia ndia, Mjini za kungilia, Pasiwe pa kupitia, Kwa majiwe kujamidi

825. Tena mbiu ikalia, Katika zote karia, Maneno akiwambia, Abidallahi kanadi

826. Akamba ya farisani, Nnani keno nnani, Mwenda vita vya Huseni, Hamsalimu junudi

827. Nnani aviwezaye, Akenda twaa rasiye, Enzi akapewa yeye, Kwa myaka kumi idadi

828. Akapewa uhakimu, Kwa myaka kumi timamu, Kwisha sayo kukalimu, Pana mmoja hasidi

829. Hayo akayakubali, Huseni kumkutuli, Na jina lake nakuli, Omari bun Saidi

830. Akamba mimi takwenda, Huseni kwenda mtinda, Na utakalo tatenda, Nitimilize ahadi

831. Basi kapewa kaumu, Kuwa yeye mkadamu, Na maamiri fahamu, Majina tawaradidi

832. Wa kwanza bun Hasini, Akapewa alufeni, Kamba simba ghadhibani, Ukali kama asadi

833. Bun Rabia wa pili, Aliopewa rijali, Alufu kumi na mbili, Kandamana na junudi

834. Bun Shiati sikia, Akapewa zikwi mia, Kaambiwa tangulia, Akatoka Muhamadi

835. Alipewa farisani, Watu wa kwenda vitani, Idadi arubaini, Elfu zisizo budi

836. Tena akapewa Hari, Sita alfu jifiri, Walio kama namiri, Akenda bun Yazidi

837. Na Hajari tabaini, Akapewa farasani, Theneni wa ishirini, Alufu wenye hadidi

838. Wakaamrisha mwendo, Na kwenda tenda kitendo, Wakenenda kama nondo, Majimbo yote na wadi

839. Amiri akadhukuri, Endani enyi jifiri, Na amri kwa Omari, Jamii yote junudi

840. Sikizani amriye, Pasiwe ambishaye, Kwa jamii wetikie, Inshallahu Sayyidi

841. Basi wakafuatana, Pasi kuona mchana, Kwa ghubari kufungana, Mchana ukasawidi

842. Wakafika Karabala, Wakazitoa kafila, Wasibakie mahala, Bara yote wakabidi

843. Mito wakaizuia, Ya maji ya kutumia, Pasiwe kuona ndia, Hali ya jeshi kuzidi

844. Wakazuia mitoni, Na maji ya visimani, Kumzuia Huseni, Yeye na wake waladi

845. Huseni akitazama, Kushuka wangi kauma, Na kuzuiwa visima, Na watu kama juradi

846. Kashika yake hasadi, Kawakabili kaumu, Mbele yao akakumu, Kasimama akanadi

847. Akatamka Huseni, Ya kaumu sikiani, Mwanijua ndimi nani, Na baba yangu na jadi

848. Au la jina la mama, Mwalijua ni kusema, Wakatamka kauma, Wakamjibu Sayyidi

849. Ndiwe Huseni rijali, Na babayo Shekhe Ali, Na mama yako Batuli, Na babuyo Muhamadi

850. Huseni akawambia, Kumbe hayo yawelea, Kisa cha kunizuia, Maji na wangu waladi

851. Mwanizuia sharabu, Kesho mbele ya Wahabu, Ndombezi wenu ni babu, Hiyo siku ya mnadi

852. Au maji hamtaki, Siku ya kutaharaki, Jamii wakanatiki, Jamii wakamrudi

853. Twayajua kama hayo, Ndombezi kuwa babuyo, Waama leo rohoyo, Kutoka haina budi

854. Na mngawanya haudhi, Ni babuyo muritadhi, Waama kufa faradhi, Katwaa Maka hurudi

855. Majambo yake babuyo, Yanatupata na moyo, Hayeshi tukili nayo, Yanatuchoma fuadi

856. Kusikiakwe Huseni, La haula kabaini, Illa billahi Manani, Kashika ndia karudi

857. Akarudi akilia, Kwa mambo kumzingia, Hemani alipongia, Wote wakamshahidi

858. Kulia kwake Huseni, Wakalia nisiwani, Na vijana mikononi, Na rijali na abidi

859. Tena wakanyamazana, Basi Huseni kanena, Hema ijengeni sana, Na boma liwe jadidi

860. Basi hema zikakita, Pasi mahali kupita, Na boma kama ukuta, Likawa gumu shadidi

861. Boma lilipotulia, Usiku ulipongia, Huseni akawambia, Wenziwe kawaradidi

862. Wenziwe kawabaini, Afadhali kimbieni, Mtukue nisiwani, Hivi sasa msharidi

863. Tokani hivi laili, Hata kukicha mmbali, Maana hiki kitali, Ni changu mimi wahidi

864. Tokeni enyi wenzangu, Mniwate peke yangu, Na rehema kwa Muungu, Nusura kwake Wadudi

865. Aliposema akesha, Wote wakanena hasha, Ya nini hayo maisha, Ufapo wewe Sayyidi?

866. Twaradhiwa tuyayuke, Ndipo nawe upatike, Ila kukuwata pweke, Sio yetu makusudi

867. Ufapo wewe Huseni, Maisha hayo ya nini?, Twafanyani duniani, Uondokapo Sayyidi?

868. Hayo wakisha mwambia, Huseni kafurahia, Na kumwomba Jalia, Na dua njema kazidi

869. Wakalala ni laili, Wakisoma na kusali, Kabiri na tahalili, Na salatu Muhamadi

870. Hata kukipambazuka, Wakamuomba Rabuka, Kwa kiu ilowashika, Wanawake na waladi

871. Wataka maji ya kunywa, Wayatafuta hawana, Akondoka Maulana, Akawendea junudi

872. Akatamka Huseni, Akamba ya Farisani, Nataka maji nipani, Kwa upesi na juhudi

873. Maji musiyazuie, Nayataka nitumie, Kwani sina nikhofuye, Wala aliyenizidi

874. Nipani maji haraka, Msifanyike dhihaka, Mkatafuta hilaka, Na kwangamia kusudi

875. Na hayo muazimuyo, Yote nayaona siyo, Maneno niwambiayo, Nipani maji nirudi

876. Wakatamka kaumu, Sikia bani Hashimu, Twakuwazia kuzimu, Katika zetu fuadi

877. Wala hapo hatwondoki, Wala maji huyateki, Ahadi ni kuhiliki, Wewe na wako junudi

878. Ewe Aba Abdalla, Katwaa hwendi pahala, Utakufa Karabala, Huna budi huna budi

879. Huseni akipulika, Mno akaghadhibika, Na upanga kaushika, Kawakabili junudi

880. Walipomuona aja, Wasende mbio pamoja, Ila mmoja mmoja, Kwa khofu kuu shadidi

881. Kukimbiakwe kauma, Huseni karudi nyuma, Akenda kunako hema, Na kaumu wakarudi

882. Na jamii watu wake, Wataka maji wateke, Wana waume na wake, Kiu inawashitadi

883. Watoto wamedhikika, Kwa roho kuwakauka, Asimamaye hwanguka, Hapo muweza jasadi

884. Kuyaonakwe yakini, Akondoka farasini, Akamwambia Huseni, Kanena ewe Sayyidi

885. Sayyidi nipa idhini, Nende hangie jeshini, Rabbi ataniauni, Kwa nusuraye Wadudi

886. Na Huseni akakuli, Baraka 'Llahu rijali, Takunusuru Jalali, Bi shufaa Muhamadi

887. Kwambia siyo jinsi, Akenda hima upesi, Dereya kajilabisi, Kanzu mbili za hadidi

888. Na upanga kaushika, Na fumo likigeuka, Farasi kamtandika, Kamkalia jawadi

889. Akajitia jeshini, Kama wingu na tufani, Bi shimali wa yamini, Kwenda huko na kurudi

890. Kiwakata vyao vichwa, Kiwaua kiwangusha, Ukinga mwamba kuosha, Wenye wingu na baridi

891. Kawatia mautini, Alufu na miateni, Kauwawa muumini, Rahema 'Llahu Wadudi

892. Akanguka Islamu, Kashahadia Karimu, Na Mtume Muungamu, Swala 'Llahu wa Sayyidi

893. Roho yake Muumini, Ikenda fi'l janani, Kuona sayo Huseni, Kawakabili junudi

894. Kawangia katikati, Akawanyesha mauti, Yamini na shimalati, Wote wakamsharidi

895. Akawaua Huseni, Jumlaye alufeni, Kampata Muumini, Waliye kumuhusudi

896. Kamfika maitiwe, Kamshika mkonowe, Huseni kapiga yowe, Kulia na kuradidi

897. Akalia akinena, U wapi babu Amina, Leo kwamba waniona, Wanitendavyo junudi?

898. Na baba yangu Alii, Na kwamba leo uhai, Ingalishuka samai, Kwa hurubu kushitadi

899. U wapi baba Sharifu?, Ukaja ukawashufu, Wa Iraki na wa Kofu, Watakavyo nihusudi

900. Akawasili hemani, Kamuweka pale tini, Wakalia nisiwani, Na jamii ya junudi

901. Kulia wakiomboa, Na mikono wakinua, Na kuomba njema dua, Kwa Mola wetu Wadudi

902. Kimaa kunyamazana, Pana mmoja kanena, Nirukhusu Maulana, Nende hawane jihadi

903. Akamba katawakali, Ukamuombe Jalali, Akajifunga kwa kweli, Seifuye ya hadidi

904. Kimaa kushika sefu, Akawangia wa Kofu, Kaua watu alufu, Kama umeme na radi

905. Na yeye wakamuuwa, Kashahadia Molewa, Na Tume wake Rasuwa, Fi'l janna akabidi

906. Akangia Maulana, Akenda akapigana, Hata akenda muona, Kamtwaa akarudi

907. Akatoka na wa tatu, Akenda jeshi ya watu, Yali hivyo wanakwetu, Kwenda wahidi wahidi

908. Na kadiri atokaye, Yuapigana pekeye, Akaua auaye, Alufu au zaidi

909. Na pindi akiuawa, Huseni amtukuwa, Tena akirehemewa, Na Mola wetu Wadudi

910. Kiuawa Muumina, Huseni yuapigana, Hata akenda muona, Hapo alipo shahidi

911. Wakangia mautini, Jamii watu sitini, Kabaki yeye Huseni, Na wale wake waladi

912. Watu sitini fahamu, Wote wakenda kuzimu, Wakabakia ghulamu, Na baba yao Sayyidi

913. Na kiu imekithiri, Watoto wataghayari, Wala hawana shauri, Kupata maji baridi

914. Watoto wamedhikika, Kwa kiu ilowashika, Na maji wakiyataka, Wanazuia junudi

915. Wanawake na vijana, Wapita povu la kanywa, Kazi yao hulizana, Na sala na kusujudi

916. Wamsabihi Jalali, Na sala na tahalili, Kwa mtana na laili, Wa katika kuabidi

917. Huseni akibusiri, Kamtwaa nakhubiri, Mwanawe Ali saghiri, Kijana fi'l mahidi

918. Kijana hajaachishwa, Bado akalinyonyeshwa, Mwana mchanga kabisa, Hazidi mwaka wahidi

919. Kamtukuwa Huseni, Kamuweka mkononi, Akenda naye jeshini, Maneno akaradidi

920. Huseni akabaini, Nataka maji nipani, Kwani huyu ghulimani, Atishi imemzidi

921. Ngawa fanyani huruma, Kwa huyu mwana yatima, Hakumaliza kusema, Mshare ukambidi

922. Mshare ukaja hima, Kapiga yule ghulama, Huseni akitazama, Wanakwisha muhusudi

923. Mshare ukaja mbio, Ukamkata shikio, Kijana keta kilio, Na damu kutamaridi

924. Kijana kafazaika, Kina akipapatika, Kwa shikio kukatika, Naye kijana waladi

925. Babaye akamshika, Kifuani kamuweka, Keno akasikitika, Na kilio akazidi

926. Kenda nayo iyo hina, Akafika kwa Sakina, Ikiwa ni kulizana, Kwa msiba kuwashidi

927. Wakalizana kabili, Wote wana na wavyele, Kwa siaha na kelele, Waungwana na abidi

928. Wakinyamaza yuani, Kondoka katabayani, Mtoto wake Huseni, Jina ketwa Muhamadi

929. Akamwambia amuye, Nipa rukhusa ningie, Naradhiwa nangamie, Kama kuona taadi

940. Alufu wa thamanini, Kawatia mautini, Ndipo akanguka tini, Wakampiga hadidi

931. Akaumba Murisali, Kuwa yeye afadhali, Wa akheri na awali, Bora wao Muhamadi

932. Bora ya watu babuyo, Alomzaa babayo, Akaumbwa na babayo, Akawa yeye asadi

933. Kapewa dhu' l Fukari, Akawapiga kufari, Hata wakataghayari, Pasiwe mwinua yadi

934. Na pepo alowekewa, Ni babu yako Rasuwa, Babayo enda tukuwa, Hiuliwa 'l hamdi

935. Na sisi tu wana wao, Tuzawa ni watu hao, Nnani watupitao, Katika wote junudi

936. Na haya ni makutubu, Yandishiwe ni Wahabu, Kula litalotusibu, Ni amri ya Wadudi

937. Na sasa nipa idhini, Nikaingie jeshini, Huseni akabaini, Naamu wangu waladi

938. Naamu uliyonena, Siwezi kurudi tena, Mtawakali Rabana, Kijana kajizadidi

939. Kajifunga upangawe, Akapanda farasiwe, Kawapoa kama mwewe, Harubu ikashitadi

930. Maana Rabi Molewa, Alimuomba Rasuwa, Kampa haja na kuwa, Kupita wote ibadi

941. Akapiga ukelele, Huseni njoo uole, Hawana wako wavyele, Na babuyo Muhamadi

942. Huyu bibiyo Khadija, Na muombezi wa waja, Na Hasani wa pamoja, Na Fatuma wangu Jadi

943. Na babayo Shekhe Ali, Njoo hima tasihili, Kusikiakwe makali, Sefu kaitakaladi

944. Akaushika upanga, Mwana wa anga kwa anga, Kangia akawachenga, Kama fisi na asadi

945. Hata akamdirika, Miongoni kimweleka, Matozi yakimwaika, Kilio kikashitadi

946. Kufika kunako hema, Huseni kashika tama, Ali papo usimama, Kalia mno Sayyidi

947. Zainabu na Sakina, Zaina 'l abidina, Jamii wakalizana, Pasibakie wahidi

948. Na 'l Umi Kulithumu, Kalia mno fahamu, Na jamii ya ghulamu, Kilio wakaamidi

949. Na Fatuma na Rukia, Wakashitadi kulia, Keno wakipindukia, Kwa kilio kuwazidi

950. Wakashukuru Taala, Akatoka Abdalla, Bin Huseni Fadhila, Kawakabili junudi

951. Jeshini akjitia, Muda wa saa kungia, Alufu wa sita mia, Kawaua asibudi

952. Ndipo naye kauwawa, Kashahadia Molewa, Pepo zimefunguliwa, Mola wetu akanadi

953. Akatamka Manani, Enyi mahuru 'l aini, Simamani simamani, Kwa shime na jitihadi

954. Mpokee roho zao, Viumbe niwapendao, Ni laula baba yao, Kusinge kitu abadi

955. Roho zao zitwaeni, Zisanguke mtangani, Wakaja huru 'l aini, Hapo panapo jihadi

956. Kwa kila auawaye, Wakapokea rohoye, Pasibaki abakiye, Jamii wote waladi

957. Wana sabaa ashara, Wote wakenda akhera, Kwa uwezo wa kudura, Yake Muungu Wadudi

958. Kabaki pweke Huseni, Na upanga mkononi, Akitazama yamini, Asione msaadi

959. Akitazama yasiri, Asione mshauri, Kalia akakithiri, Hata akapita budi

960. Baada kulia kwake, Wakalia wanawake, Kwa Huseni kuwa pweke, Na vita vimeshitadi

961. Junudi yangalizana, Kwa usiku na mtana, Hapana kusikizana, Kwa wangi junudi

962. Ni kamkam malaki, Walioko wanafiki, Hawana walipobaki, Majimbo yote na wadi

963. Wamekutana sufufu, Kamkam maalufu, Kwa mafumo na suyufu, Walizo kutakaladi

964. Kuona bun Imamu, Kuzidi mno kaumu, Kondoka kutayamumu, Kasali akisujudi

965. Akamuomba Rabana, Mwenye ezi Subhana, Baada sayo nanena, Kandoka kajizadidi

966. Kangia kajiwadaa, Pambo ambalo lafaa, Na kofia akavaa, Isiyo shaka na budi

967. Kofia yake kitwani, Ya hadidi mbayani, Ya tokea Adnani, Ya tangu jadi na jadi

968. Akajivika kilemba, Cha maidani kutamba, Ghadhabu akinga simba, Na uso kama asadi

969. Akaishika na sefu, Ka'l bariku khatifu, Ya Abdi 'l Manafu, Izoelee jihad

970. Akalishika fumole, Ukali likinga ghule, Likitisha mlekule, Aliye mbali baidi

971. Akaishika turusi, Ya chuma kingi suwesi, Hata akavuma kusi, Haimpati baridi

972. Dereya sita za chuma, Muili wote mzima, Asiosaze alama, Wote wenele hadidi

973. Na thelatha suruali, Za chuma kingi thakili, Jini na simba wakali, Wote wakamsharidi

974. Kamkali farasi, Kinga umeme wa kusi, Na wingu nene jeusi, Lenye kiza na baridi

975. Akasimama Huseni, Kawaaga nisiwani, Kwa kherini kwa kherini, Nenda zangu sitarudi

976. Kwa kherini wanakwetu, Namuomba Mola wetu, Nasi makutano yetu, Kesho mbele ya Wadudi

977. Kwa kheri ewe Sakina, Zaina 'l abidina, Wake wote na vijana, Na jamii ya waladi

978. Kwa kherini ndugu zangu, Na jamii ya wanangu, Nawaaga nenda zangu, Tena nendako baidi

979. Msikithiri kilio, Tulizani yenu moyo, Kwani Rabi andikayo, Kujiri hayana budi

980. Kwishakwe sema yuani, Wakalia nisiwani, Na jamii ghulmani, Kilio kikashitadi

981. Wakalia na majini, Na nyama wote yakini, Wa bara na baharini, Hata ndege na asadi

982. Kwisha sayo kukalimu, Kamzinza bahaimu, Kaelekea kaumu, Kasimama akanadi

983. Anaa mwana wa enzi, Mwana wa jua na mwezi, Ndiswi waliza walinzi, Na waliotabaradi

984. Ndiswi watenda vitendo, Ndiswi wamwanga uvundo, Ndiswi tumezao nondo, Kula panapo jihadi

985. Ndiswi wavunda milima, Ndiswi wondoa nakama, Ndiswi wondosha kilima, Ndiswi wavunda junudi

986. Kaumu wakisikia, Jamii wakakimbia, Pasi mtu kubakia, Wote wakamsharidi

987. Kwa kumuona haliye, Kifungo na libasiye, Na hayale manenoye, Wakamkaa baidi

988. Huseni akawambia, Haifai kukimbia, Hamna pa kungilia, Hata mahali wahidi

989. Kukimbia hakufai, Kwani zimekwisha rai, Hapana tena uhai, Mimi na nyinyi junudi

990. Basi akajelemeza, Katika wimbi na kiza, Subhana ya Aziza, Ajua yeye Wadudi

991. Akajitia jeshini, Kama wingu baharini, Watu wangukao tini, Huwezi kuwaadidi

992. Sefu ikatenda kazi, Na farasi kanywa wazi, Na awezapo pumzi, Zawalika kama radi

993. Farasi ni Maimuni, Wa Shekhe Aba Huseni, Mzoea upigani, Vita vyote vya jihadi

994. Farasi kaghadhibika, Hako muweza mshika, Yuaruka akiruka, Na kwelemea junudi

995. Farasi akinga simba, Na kivumi kama mwamba, Na maiti wamewamba, Majimbo yote na wadi

996. Akawana Muarabu, Vita vikubwa ajabu, Na uso kutaghadhabu, Ghadhabu kubwa shadidi

997. Pakondoka tushitushi, Kama dharuba ya moshi, Kwa kuwazuia jeshi, Na ghadhabu kumzidi

998. Sefu ikatenda kazi, Kama wembe wa kinyozi, Kumpiga hawawezi, Kwa nguvu aliwazidi

999. Nchi ikafunga kiza, Na damu ikifuaza, Pasiwe na kusikiza, Kwa vita kupita hadi

1000. Dunia ikahamiri, Wakaliona ghubari, Watu walio Misiri, Na walio Baghadadi

1001. Na wa Maka na Madina, Ghubari wakiliona, Wakafazaika sana, Kwa nahari kusawidi

1002. Kharisani na Hijazi, Ghubari li waziwazi, Kwa mwana kutenda kazi, Iliyo katika yadi

1003. Ghubari likisabiki, Basara na Dimishiki, Yemeni na Yarimuki, Sanaa na Sandidi

1004. Na watu walio Rumu, Wakiliona fahamu, Ghubari kubwa adhimu, Wasilijue mradi

1005. Pasiwe asikiaye, Wala mtu aonaye, Wala mwenye akiliye, Zote zikawasharidi

1006. Pasiwe mwenye turusi, Wala mwendesha farasi, Kwa siaha na siasi, Awauavyo Sayyidi

1007. Pasiwe mshika fumo, Wala atokaye humo, Hali ya kiungurumo, Apita wote asadi

1008. Pasiwe mwenye fahamu, Wala akili timamu, Wote wali maghumumu, Wao na wao jawadi

1009. Pasiwe muweza toka, Wala muweza kwondoka, Kwa hali ya kutoweka, Wangi wasio idadi

1010. Kula mtu akadhani, Viumbe hata majini, Mbingu zinakuja chini, Haziko kule baidi

1011. Wakadhani kwa hakika, Samai zimekatika, Na mawingu yameshuka, Hapana shaka na budi

1012. Malaika wa samai, Wote wakatafazai, Hawashuki hawapai, Kwa fazaa na fuadi

1013. Majini na Malaika, Wakamuomba Rabuka, Huseni kunusurika, Allahumma Ya Wadudi

1014. Viwayo na dharubaye, Sawasawa na babaye, Watu wakasema ndiye, Apiganaye jihadi

1015. Wote wakasitatii, Apiganaye Alii, Kumbe hakufa yu hai, Daima zote abadi

1016. Akawatawanya damu, Huseni bun Imamu, Ikenenda milizamu, Kula bara ikabidi


4

UTENZI WA IMAM HUSEN

UTENZI WA KISA CHA SAYYIDNA HUSSEIN

1017. Damu ikenda mafumbi, Ikafuuza mawimbi, Na maiti kama numbi, Wangamiavyo junudi

1018. Wakatazama rijali, Harubu ya bin Ali, Jamii wakenda mbali, Wote wakatabaidi

1019. Maji wakamuachia, Waliyo kuyazuia, Jamii wakakimbia, Masahirai na wadi

1020. Visima wakaviwata, Wakenenda asitata, Kwa msiba kuwapata, Mkubwa usio budi

1021. Akatamka Huseni, Akawambia njooni, Muje mukae mitoni, Haifai kusharidi

1022. Njoni munizuilie, Maji nisiyatumie, Kula amsikiaye, Kukimbia akazidi

1023. Kula msikia hayo, Maneno ayasemayo, Yuazidi kwenda mbio, Kwa upesi na juhudi

1024. Akenda zake Huseni, Hata kafika mtoni, Akashuka farasini, Kwa salama na suudi

1025. Kuona maji farasi, Akenika yake rasi, Kwa atishi na asisi, Kubwa iliyomshidi

1026. Huseni kamkemea, Ya Maimuni sikia, Dhuria wake Nabia, Atishi imewazidi

1027. Haifai kunywa wewe, Sharuti wapelekewe, Ndipo nafusi zituwe, Mimi na wewe turudi

1028. Maimuni kasitahi, Na kuwujuba Illahi, Akaona ni asahi, Maneno yake Sayyidi

1029. Huseni akangalia, Kutaka cha kutekea, Mara ile kasikia, Makelele na mnadi

1030. Wakamwambia Huseni, Wewe u huko mtoni, Lakini huko hemani, Wanakuwako junudi

1031. Wanawake wametekwa, Na buweti na mikeka, Huseni akipulika, Kamrukia jawadi

1032. Kumbe vile ni hadaa, Wamwita kumsawaa, Akatoka kwa fazaa, Kukimbilia waladi

1033. Hata mbele kiwakuta, Wakampiga kwa nyuta, Mishare ikampata, Sabiini kwa idadi

1034. Wakampiga sahamu, Sabaa kumi timamu, Tena akenea damu, Katika yote jasadi

1035. Tena wakamdafiri, Asimuweze bairi, Kashahadia Jabari, Na Tumwawe Muhamadi

1036. Akajua ni mauti, Haihati haihati, Kila kilicho hayati, Na kufa hakina budi

1037. Akashuka farasini, Akanguka pale tini, Wakakutana laini, Ili kuja muhusudi

1038. Pana mmoja kuhani, Jina lake sikiani, Bun Dhu'l Jaushani, Aduwa 'llahi Wadudi

1039. Jina akitwa Shamru, Aduwa 'llahu Ghafuru, Akaikabili nuru, Kwenda yondoa jasadi

1040. Akenda hima upesi, Kwenda iondoa rasi, Akamvua libasi, Na dereya za hadidi

1041. Tena Huseni kanena, Kifunue chako kanywa, Huenda nikayaona, Aliyonambia jadi

1042. Kanywa akakifungua, Huseni akimuoa, Kicheko akakyangua, Kacheka sana Sayyidi

1043. Shamru kamuuliza, Wacheka nini neleza, Naye akamrudiza, Alisema Muhamadi

1044. Alinambia Rasuli, Atakaye kukutuli, Takupa yake dalili, Ajaye kukuhusudi

1045. Kanywani yuna shairi, Mithili kama hinziri, Na mbalanga asfari, Na uso wa l' Kurudi

1046. Nami nimezibaini, Katika mwako kanywani, Ndipo hasema yakini, Babu aliyoradidi

1047. Kwisha sayo nikwambiye, Akaishika sefuye, Akamkata rasiye, Kwa seifi ya hadidi

1048. Akisha akaishika, Fumoni kukitungika, Nchi ikahamirika, Ikazuka na baridi

1049. Yakacheza majabali, Kwa ghadhabu za Jalali, Wakaiona nakili, Hilaki inatubidi

1050. Wakisha sayo yuani, Wakenda kule hemani, Wakatwaa nisiwani, Na vyombo vya kusafidi

1051. Wakavichukua vyombo, Wakawavua mapambo, Wakawavika visambo, Mtu hawezi radidi

1052. Na farasi Maimuni, Aliyepanda Huseni, Akelekea barani, Hata leo hajarudi

1053. Akisha kurambaramba, Na kulia na kusamba, Muungu akamuomba, Akenda zake baidi

1054. Muiliwe sikiani, Akazikwa ni majini, Ambao ni waumini, Wasalio tahajudi

1055. Majini wakikutana, Jumla wakilizana, Akazikwa Maulana, Jamii yake jasadi

1056. Baada hayo nakuli, Walio kumkutuli, Wakesha kutwaa mali, Na wote wake waladi

1057. Kitwa chake muumini, Wakakitia fumoni, Wakarejea mjini, Kwa zumo na kujinadi

1058. Katukuliwa Sakina, Na jamii ya vijana, Zaina'l abidina, Pasibakie wahidi

1059. Wakenda wali mateka, Dhuria wa Nabiuka, Hata Kofu wakifika, Magoma yakashitadi

1060. Wakangia kwa mazumo, Shindo na kiungurumo, Kelele kwa mitetemo, Na furaha za fuadi

1061. Tena ikiwa kuteza, Kwa neno kuwapendeza, Na khabari wakeneza, Tumeupata mradi

1062. Siku tatu wakakumu, Kwa ngoma na baragumu, Kwa siku yane fahamu, Wakenenda kwa Yazidi

1063. Kitwa chake Maulana, Kikenenda na vijana, Kifika kwa wao bwana, Wakafurahi shadidi

1064. Yazidi kafurahiwa, Kwa mradi umekuwa, Na Huseni kuuawa, Ndio yake makusudi

1065. Wakiwasili kaumu, Kwa ngoma na baragumu, Kaitengeza karamu, Kuwakirimu junudi

1066. Wakala wote khaliki, Khabuzi na mishikaki, Yazidi akanatiki, Yajili hima kunadi

1067. Akawambia Nadini, Msibakie mjini, Amtajaye Huseni, Yuataka jihusudi

1068. Huseni amtajaye, Au amkumbukaye, Atachinyanga nyamaye, Hapana shaka na budi

1069. Basi mbiu ikalia, Katika biladi pia, Pasiwe kumsikia, Amtajaye Sayyidi

1070. Katoka mtu mmoja, Huseni akamtaja, Hapana shaka na hoja, Mauti yanambidi

1071. Baada sayo nanena, Akamuweka Sakina, Na wote wake vijana, Nyumba mbovu ya abidi

1072. Kapewa nyumba dhaifu, Pasiwe na masurufu, Na ambaye amshufu, Yuambiwa hima rudi

1073. Pasi kupewa chakula, Wala nyumba ya kulala, Wala kwenenda mahala, Siku nyingi zikabidi

1074. Akawakusa mashaka, Myezi miwili pulika, Wa tatu wakifumbuka, Wapendao Muhamadi

1075. Wakenenda Isilamu, Wapendao Muungamu, Na roho zili na hamu, Hata mbele ya Yazidi

1076. Maneno wakadhukuri, Wakamba ewe Amiri, Tujile kusitajiri, Utukidhie mradi

1077. Huseni ameondoka, Hapana tena shabuka, Lakini hawa mateka, Twataka kwao yarudi

1078. Umekidhi mradio, Kama ule utakao, Hawa ni kurudi kwao, Ya nini kuwahusudi?

1079. Kwani mshindani wako, Umemwondoa hayuko, Kwisha sayo matamko, Aketikia Yazidi

1080. Yazidi akabaini, Na wende watu miteni, Watukue nisiwani, Pamoja na auladi

1081. Wenende hata Madina, Wampeleke Sakina, Kimaa sayo kunena, Safari kaizadidi

1082. Yazidi akawatoa, Dhuria wake Rasua, Wenenda wakizomewa, Kwa ushinde kuwabidi

1083. Wakayandama safari, Kwenda zao ansari, Wakayelekea bari, Kawanusuru Wadudi

1084. Madina wakiwasili, Wakangia kwa laili, Mtana wasikubali, Kwa walivyotasawadi

1085. Kwa hali walivyodhofu, Dhuria wa Muongofu, Wakenda wakawakifu, Nyumba waliyorajidi

1086. Kwa baba yao Alia, Ndio nyumba walongia, Asubuhi wakilia, Kilio kikashitadi

1087. Wakimaa kulizana, Watu walio Madina, Kula mtu akanena, Ni lipi lililobidi

1088. Wakauzana kunani, Wakambiana Huseni, Radhia llahu Manani, Dhuria wake Sayyidi

1089. Huseni ametawafu, Katika nchi ya Kofu, Walipigana kwa sefu, Harubu kubwa shadidi

1090. Walikutana khaliki, Wa Kofu na wa Iraki, Na walio Dimishiki, Kwa amri ya Yazidi

1091. Wakazuia sharabu, Kapigana Muarabu, Vita vikubwa ajabu, Hata wakamuhusudi

1092. Walipokwisha wanawe, Na jamii ya watuwe, Akapigana mwenyewe, Ajali ikambidi

1093. Wakimaa kwambiana, Watu walio Madina, Wakangia kulizana, Wazee na 'l muridi

1094. Kilio kikatawili, Kwa wake na marijali, Kelele zikenda mbali, Zikenda mno baidi

1095. Jamii muhajirina, Na watu walo Madina, Wakimuola Sakina, Sikitiko wakazidi

1096. Wakalia kwa kelele, Kula mtu wangu ole, Wa nyumba henenda mbele, Na wa mbele akarudi

1097. Walikwenda kumngoja, Wakashikana pamoja, Pasiwe shaka na hoja, Kwa machozi kuwabidi

1098. Zikaenea khabari, Madinati mnawari, Na kilio cha fakhari, Kasikia Muhamadi

1099. Bun Khanifa kabili, Akasikia kelele, Kauliza pole pole, Katika wake waladi

1100. Muhamadi akanena, Mnani leo Madina, Mbona watu walizana?, Vijana wakaradidi

1101. Vijana wakamkuwa, Huseni ameuawa, Na watu alotukuwa, Jamii hawakurudi

1102. Kauawawa Maulana, Na wote wake vijana, Aliyekuja Sakina, Hawakubaki junudi

1103. Alipowasili Kofu, Wakakutana sufufu, Ambao ni mausufu, Watambuao hadidi

1104. Wakamzuia maji, Kasimama kawahoji, Akisha zake hujaji, Siku mbili zikabidi

1105. Kiona hawakubali, Kawangia kwa kitali, Wakauawa rijali, Asibakie wahidi

1106. Na wana alotukua, Jamii wakauawa, Naye akakutuliwa, Dhuriawe Muhamadi

1107. Walipigana mahala, Jina lake Karabala, Naye Aba Abdalla, Kaua wengi junidi

1108. Huseni akauawa, Rasi wakaitukua, Kwa baragumu na siwa, Kupelekewa Yazidi

1109. Maneno yakishilia, Muhamadi kasikia, Ghadhabu zikamngia, Zilizo kubwa shadidi

1110. Akangiwa ni ghadhabu, Zilizo kubwa ajabu, Uso wake Muarabu, Wote ukatajamidi

1111. Kutetema munhari, Macho yakatahamari, Mishipa ikanafiri, Katika yake jasadi

1112. Mishipa ikasimama, Na muili ukivuma, Ali akiunguruma, Kama nondo na asadi

1113. Muili ukahariki, Kwa kukazana uruki, Watu wakataharuki, Kwa ghadhabu kushitadi

1114. Muili wake hakika, Wote ukahamirika, Kwa ghadhabu kumshika, Na msiba kumzidi

1115. Damu yali ikijiri, Kwa ghadhabu kukithiri, Muili ukanafiri, Na kucheuka nabidi

1116. Hata akisha kilio, Ghadhabu akali nayo, Kasimama mara hiyo, Kamuagiza jawadi

1117. Kamuagiza farasi, Akija kamlabisi, Pambo kubwa la utesi, Lisilo shaka na budi

1118. Akampamba rikabu, Pambo kubwa la harubu, Liwezalo kughilibu, Kati kati ya junudi

1119. Kitolea farasiwe, Akajipamba mwenyewe, Mkitaka mtajiwe, Pambole taliradidi

1120. Kwanza akajilabisi, Kofia tatu suwesi, Akaifinika rasi, Kwa kofia za hadidi

1121. Kula kofia hakika, Watu kumi kujitwika, Hawawezi kuinuka, Kwa uzito kuwazidi

1122. Akajivika amamu, Ya chuma kingi kigumu, Kinga jabali adhimu, Au wingu la baridi

1123. Na uso akiuwamba, Kwa tamvua la kilemba, Nondo na chui na simba, Yeye ni bora zaidi

1124. Kilemba kikitolea, Singo yote na lahea, Na uso wake jamia, Ila mato kushuhudi

1125. Akavaa muilini, Derea zake yakini, Wahidi wa ishirini, Za hadidi msafidi

1126. Akavaa nakhubiri, Mahazamu ya sifuri, Na hadidi mnawari, Aliyo kujizadidi

1127. Na suruali tisia, Zake alizozivaa, Kuona huwezi kaa, Karibu wala baidi

1128. Suruali za suwesi, Alizovaa mtesi, Na joho kajilabisi, Thamaniati idadi

1129. Kula nguo nakhubiri, Khufu nne mnawari, Akajifunga khanjari, Ya kwenendea jihadi

1130. Akaishika sefuye, Khudumati 'l Hindiye, Na Rumuhi 'l Khatiye, Kama nyoka asawidi

1131. Na ngao kaiwajaza, Ya jadi wao Hamza, Kimaa kujitengeza, Kamrakibu jawadi

1132. Akampanda rikabu, Ali na nyingi ghadhabu, Kimaa kutakarabu, Kasimama akanadi

1133. Kasema ya Ansari, Na jamii Muhajiri, Nawaaga nasafiri, Enyi ahali biladi

1134. Nawaaga kwa kherini, Nyote mulio mjini, Kisasi chake Huseni, Kukitaka sina budi

1135. Nenda Kofu na Iraki, Nende haitake haki, Wala msitaharaki, Wala sitaki junudi

1136. Takwenda ingia Kofu, Niirakibu kwa sefu, Wala msitie khofu, Rabi atanisaidi

1137. Naapa enzi ya Mungu, Kisasi cha ndugu yangu, Ahadi farasi wangu, Damu ikome kabadi

1138. Naapa Rabi Karimu, 'l Kofu taikadimu, Nende haimwaye damu, Majimbo yote na wadi

1139. Naapa Rabi Jalia, 'l Kofu nenda ingia, Ahadi ni kogelea, Mimi na wangu jawadi

1140. Naapa Mwenye Kudura, Nenda imwaya humra, Waitafute nusura, Wasiione abadi

1141. Naapa Rabi Molewa, Damu takwenda itoa, Hata ikome kifua, Katika zao biladi

1142. Naapa Rabi Kudusi, Takwenenda wanukusi, Ahadi wangu farasi, Damu ifike zanadi

1143. Naapa Rabi Manani, Kisasi chake Huseni, Hadi ifike singoni, Damu yao mayahudi

1144. Kaapa mara sabaa, Kiapo cha makataa, Jamii wakashangaa, Pasi mtu kuradidi

1145. Pasiwe amjibuye, Kwa kumuona haliye, Libasi na ghadhubuye, Hali ilivyomzidi

1146. Wote wakamkimbia, Majumbani wakangia, Keno wakajifungia, Kwa kumkhofu Sayyidi

1147. Wakazighaliki babu, Kwa kumcha Muarabu, Mtu aliyemjibu, Khalidi bun Walidi

1148. Yule Khalidi kakuli, Ewe mtoto wa Ali, Nali mimi na Rasuli, Beiti l' masijidi

1149. Tukali msikitini, Akatamka Amini, Huko akhera zamani, Kaja mtu hana budi

1150. Akatokea kijana, Minaye tumefanana, Kwa suraye hata jina, Yuaitwa Muhamadi

1151. Nanyi mutambaini, Siku ya kufa Huseni, Atangia msituni, Kwa ghadhabu kushitadi

1152. Atajifunga libasi, Vao lisilo kiasi, Akatafute kisasi, Biladi zake Yazidi

1153. Atoke kifika bara, Allahu Rabbi Ghafara, Tamshushia sitara, Iliyo kubwa shadidi

1154. Atangia sitarani, Yake Muungu Manani, Hata akheri zamani, Ndipo atakapobidi

1155. Kauli ya Muungama, Katwa hairudi nyuma, Na leo nina tuhuma, Kuwa wewe Muhamadi

1156. Tumwa alitakalamu, Kijana huyo ghulamu, Min banii Hashimu, Asili yao na jadi

1157. Na leo takufuata, Hangia ndani ya vita, Sikubali kukuata, Ukenda pweke Sayyidi

1158. Muhamadi kamjibu, Kite usende shaibu, Huwezi tena harubu, Kwa uzee kukuzidi

1159. Kisha sayo kutamka, Muhamadi akatoka, Kwa ghadhabu kumshika, Zilizo kubwa shadidi

1160. Kamwelekeza jamala, 'l Kofu na Karabala, Pasi kuola mahala, Wala Madina kurudi

1161. Akaikabili bari, Kwenda itafuta shari, Mule katika safari, Kitunza mbele baidi

1162. Akaliona jabali, Mbele limeshitamali, Akamzinsa jamali, Kulumeni akarudi

1163. Kufika akiliona, Jabali limefungana, Pa kupitia hapana, Kwa jabali kujadidi

1164. Kushotoni akifika, Pia limezunguuka, Na nyuma alikotoka, Kataajabu Sayyidi

1165. Hapana pa kupitia, Kwa jabali kuzuia, Kakaa akatulia, Akashukuru Wadudi

1166. Pale alipwakifu, Akasikia khatifu, Mnada wake Latifu, Ukita Ya Muhamadi

1167. Ewe ibnu Khanifa, Bun akhi Mustafa, Wewe hapo hutokufa, Jamii zote abadi

1168. Ya bun Aba Huseni, Kaa hapa jabalini, Hata akheri zamani, Takutoa sina budi

1169. Utakwenda twaa shari, Ya mzawa Haidari, Miongoni mwa kufari, Nasara na mayahudi

1170. Kiapo umekhalifu, Kwenda wangia kwa sefu, Wa Iraki na wa Kofu, Damu ikome kabadi

1171. Nchi wenda ighariki, Tangu Kofu na Iraki, Basara na Dimishiki, Hakutabaki wahidi

1172. Nami ulivyoniapa, Utakayo nimekupa, Damu utamwaya hapa, Hata ikome fuadi

1173. Lakini kwamba saburi, Watamalaki kafiri, Ndipo utakapojiri, Utimilize ahadi

1174. Baada sayo nakuli, Likafungana jabali, Bi yamini wa shimali, Kufungana likazidi

1175. Rabi kamuweka ndani, Kamtia sitarani, Jina lake sikiani, Ndiye etwaye Muhudi

1176. Ndiye Muhudi ajaye, Nyote mumsikiaye, Na awali harubuye, 'l Kofu atakobidi

1177. Hatapigana mahala, Ahadi ni Karabala, Awatie zilizala, Jamii wote junudi

1178. Auwe bina adamu, Awachawanye na damu, Hata ifike lujamu, Alizofunga jawadi

1179. Damu nyingi imwagike, Ahadi farasi wake, Kifua na tumbo lake, Limfinike zabadi

1180. Atapigana pekee, Atimize ahadiye, Ya kisasi cha nduguye, Alichotoa ahadi

1181. Ahadi ikitimia, Farasi akogelea, Ndipo atarejeea, Kwao Madina arudi

1182. Akiwasili Madina, Watu watakimbizana, Hawamtambui jina, Kwa siku nyingi kubidi

1183. Awambie tuliani, Nawauza nambiani, Nani wenu Sultani, Mtamalaki biladi

1184. Nani mmiliki Rumu, Na Maka kwenye Haramu, Na Misiri na Shamu?, Kaumu wataradidi

1185. Watamwambia nasara, Aliyeshika ubora, Haikubakia bora, Mtu aliyetushidi

1186. Katika yote dunia, Hana alipobakia, Hata Maka amengia, Hakuna kutaabidi

1187. Hako mtu ahijiye, Wala mtu asaliye, Kwa nguvu na amriye, Ni huyo wetu Sayyidi

1188. Hayo akishapulika, Ataikabili Maka, Akawakuse mashaka, Kwa sefuye ya hadidi

1189. Awaue makufari, Na damu itanafari, Kama wimbi la bahari, Atamalaki biladi

1190. Wazungu akiwatoa, Ndipo mtazimkuwa, Ndiye tuliyekwambiwa, Ni Mtume Muhamadi

1191. Wote watatanabahi, Ndiye Muhudi asahi, Tena roho zifurahi, Mtabasamu fuadi

1192. Wamfuate kaumu, Aitamalaki Shamu, Akaipigana Rumu, Misiri na Bughudadi

1193. Nchi aitamalaki, Misiri hadi Iraki, Nti moja isibaki, Jamii zote biladi

1194. Ndipo ashuke Jedali, Awaghilibu rijali, Ya akheri na awali, Jamii nimeradidi

1195. Jamii nimeyanena, Yaliyo kutendekana, Ya Huseni Maulana, Vita vyao na Yazidi

1196. Jamii nimewambia, Sina nililobakia, Na kwamba mmesikia, Ni afadhali zaidi

1197. Kusikia afadhali, Na muonapo mahali, Palipo kutajahali, Afadhali kunirudi

1198. Ambapo mumepaona, Palipokoseza vina, Ni afadhali kunena, Ndiyo yangu makusudi

1199. Mwenye kutunga shairi, Mtu mmoja fakiri, Hana tena tadhbiri, Kwa unyonge kumzidi

1200. Afikiri akiwaza, Kwa dunia kumuenza, Kaziye ni kwelekeza, Kula jambo kufanidi

1201. Mwenye kutunga nudhumu, Hemedi yake isimu, Naye ni mtu dhamimu, Asiye shaka na budi

1202. Na Abdalla babaye, Saidi ndiye babuye, 'l Buhuri kabilaye, Asili yake na jadi

1203. Ndiye alokwelekeza, Shairi kulitengeza, Kuweza kutoaweza, Ila amejitahidi

1204. Na yeye muombeeni, Na mikono inueni, Amnusuru Manani, Na 'l adhabu shadidi

1205. Muombeeni Wahabu, Amwepushe na adhabu, Asairi taratibu, Yeye na wake waladi

1206. Mwinue mikono yenu, Mumuombee mwenzenu, Kwani ni malenga wenu, Katika zenu biladi

1207. Siku ya kuja kwondoka, Nyote mutasikitika, Na msiba mtaweka, Katika zenu fuadi

1208. Mtafute atungaye, Msimuone kamaye, Mshike tama mlie, Mpe u wapi Hemedi?

1209. Mumwite asiwetike, Mulie msikitike, Kila siku mukumbuke, Mfanye ile uradi

1210. Ndipo nikawadhukuri, Muombeeni Ghafuri, Uwe tawili umri, Kwa rehemaye Wadudi

1211. Tamati nimemaliza, Sitaweza kuongeza, Kwani hautapendeza, Nendapo mbali baidi

1212. Kwenenda mbali siwezi, Hauharibu utenzi, Ni hayo yangu wapenzi, Niliyo kuwaradidi

1213. Na baiti nadhukuri, Ni alufu nakhubiri, Wa miyateni suturi, Ithnashera zaidi Utenzi wa Hussein

Umetungwa na Hemed Bin Abdallah Bin Said Bin Abdallah Bin Masoud Al Buhry Katika miaka ya mwisho wa 1800.

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU

YALIYOMO

UTENZI WA IMAM HUSEN 1

MWANDISHI: HEMED BIN ABDALLAH BIN SAID 1

UTENZI WA KISA CHA SAYYIDNA HUSSEIN 1

UTENZI WA IMAM HUSEN 13

UTENZI WA KISA CHA SAYYIDNA HUSSEIN 13

UTENZI WA IMAM HUSEN 25

UTENZI WA KISA CHA SAYYIDNA HUSSEIN 25

UTENZI WA IMAM HUSEN 36

UTENZI WA KISA CHA SAYYIDNA HUSSEIN 36

UTENZI WA IMAM HUSEN 46

UTENZI WA KISA CHA SAYYIDNA HUSSEIN 46

SHARTI YA KUCHAPA 54

MWISHO WA KITABU 54

YALIYOMO 55