,MAOBOLEZO YA KIFO CHA IMAM HUSEIN(A.S)

KIMEANDIKWA NA: SAYYID ABDUL HUSAIN SHARAFUDDIN

MTARJUMI: MUSABBAH SHABAN

Mtukufu Mtume(s.a.w.w) Amesema:

1. "Ee Allah! Hawa (Ali, Fatima, Hasan na Husain) ndio AhlulBait wangu, basi watoharishe kwa tohari kamili."

2. "Husain anatokana na mimi na mimi ninatokana na Husain..."

3. "Hao (Hasan na Husain) ni maua yangu katika dunia."

4. "Ewe Mwanangu (Husain)! Mwili wako ni mwili wangu na damu yako ni damu yangu;"

5. (Ewe Husain), wewe u Sayyid, mwana wa Sayyid, na ndugu wa Sayyid; wewe u uthibitisho (wa Mwenyezi Mungu) mwana wa uthibitisho (wa Mwenyezi Mungu) na ndugu wa uthibitisho (wa Mwenyezi Mungu); na baba wa uthibitisho tisa ambao wa tisa wao ni Qaim wao ambaye atakuwa al-Mahdi.

6. "Hasan na Husain ni Masayidi wa Vijana wa Peponi."

7. "Ewe Mola wangu! Mpende yule ampendae Husain."

8. "Adhabu atakayoipewa yule mwuaji wa Husain huko Motoni itakuwa sawa na nusu (nzima) ya adhabu yote watakayoipewa wenye dhambi waulimwengu."

9. " Allah hujirafikisha na wale wajirafikishao na Husain yu adui wa wale walio maadui zake."

DIBAJI

Ahlul-Bayt(a.s) Assembly ya Tanzania (ABATA) ina furaha kutoa kitabu kama hicho cha Majlis kwa watu wazungumzao Kiswahili. Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi, Mwenyekiti wa ABATA, amekichagua kwa ajili ya madhumuni hiyo kitabu kiitwacho "Muqaddamah al-Majalis al-Fakhirah fi Ma'atim al-Itrah at Tahirah" kilichoandikwa na mwanachuoni mashuhuri wa dini na mtunzi, marehemu Allamah Sayyid Abdul Husain Sharafud-din al-Musawi, wa Jabal Amil (Lebanon).

Shaykh Musabah Shaban Mapinda, wa Dar-es-Salaam, kwa ushauri wa Mwenyekiti wa ABATA amefanya tarjuma ya kitabu hiki kutoka Kiarabu kwenda kwenye Kiswahili, knachoitwa "Maombolezo ya Kifo cha Imam Husain(a.s) ."

Hiki ni kitabu cha pili ambacho kinatolewa na Ahlul-Bayt(a.s) Assembly ya Tanzania; na tunayo furaha kubwa kwa kutoa kitabu cha Majlis ambacho ni cha kwanza katika lugha ya Kiswahili.

Allah Subhanahu wa Ta'ala atoe malipo yake kwa mtunzi, mfasir na wale wote ambao wamesaidia katika uchapishaji wake kwa njia yoyote.

Wa ma Tawfeeqi illa Billah


MAOBOLEZO YA KIFO CHA IMAM HUSEIN(A.S)

KIMEANDIKWA NA: SAYYID ABDUL HUSAIN SHARAFUDDIN

MAJLIS YA KWANZA

RUHUSA YA KULIA

Hapana shaka kwamba kuwalilia wafu Waumini ni jambo linalofaa katika Uislamu kutokana na dalili ya kitendo cha Mtume(s.a.w.w) kuhusu jambo hilo.

Mtume kulitenda tendo hili kumekaririka mara nyingi na pahala pengi kama ifuatavyo: Mara ya kwanza ni siku alipofariki ami yake na mlezi wake Bwana Abu Talib. Ya pili ni siku alipouawa kishahidi ami yake Mtume Bwana Hamza katika vita ya Uhud. Ya tatu siku alipopata Shahada (kuuawa) Bwana Jaafar Bin Abi Talib na Bwana Zaid Bin Harith na Bwana Abdallah Bin Ruwah, wote hawa waliuawa katika vita ya Muuta. Mara ya pile, ni siku alipofariki Bwana Ibrahim ambaye ni mtoto wake mwenyewe Mtume(s.a.w.w) .

Mtume(s.a.w.w) alimlilia mwanawe huyu kiasi ambacho kilimfanya Bwana Abdurahman bin Auf amwambie Mtume(s.a.w.w) : "Na wewe unalia Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu "?

Bwana Mtume(s.a.w.w) akasema: "Ewe mwana wa Auf hiyo ni alama ya huruma ".

Kisha Mtume akaendelea kulia na akasema: "Hakika jicho Iinatoa machozi na moyo unahuzinika, wala hatusemi isipokuwa yale anayoyaridhia Mola wetu, na hakika sisi kutengana nawe ewe Ibrahim Wallahi tunahuzunika . "

Na mara ya tano, ni siku Mtume(s.a.w.w) alipozuru kaburi Ia mama yake Bibi Amina, alilia kiasi cha kuwaliza watu waliokuwa karibu yake.

Vitabu vinavyoashiria juu ya Mtume kuwalilia wafu ni vingi mno idadi yake siyo rahisi kuidhibiti.

Kadhalika mapokezi ya kauli ya Mtume(s.a.w.w) na kukiri kwake juu ya kufaa kulia kwa ajili ya wafu ni mengi. Mojawapo ni siku alipopata Shahada Bwana Jaafar bin Abi Talib (At-Tayyaar), Mtume(s.a.w.w) alikwenda kwa mkewe (Jaafar) Bibi Asmaa bint Umais ili kumpa faraja, naye Bibi Fatma aliingia pahala hapo huku analia na kusema: "Ewe Ami yangu". Basi Mtume(s.a.w.w) akasema:

"Na walie wenye kulia kuwalilia mashujaa mfano wa Jaafar ."

Siku nyingine aliyowakubalia watu kuwalilia wafu ni siku alipofariki Ruqaiya binti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , wanawake wakawa wanamlilia (Ruqaiya), basi Omar bin Al-Khatab akawa anawapiga kwa bakora yake, pamoja na kwamba Mtume alikwishawakubalia kulia, basi Mtume(s.a.w.w) akamwambia Omari: "Waache walie " kisha Mtume akasema: "Vyovyote iwavyo, huzuni itokayo Moyoni na jicho kulia, hayo ni kwa ajili ya huruma, ameyaweka Mwenyezi Mungu ".

Pia kuna siku lilipitishwa jeneza mbele ya Mtume(s.a.w.w) ili-hali kuna wanawake wanalia, Omar akawakemea, Mtume akamwambia Omar: "Waache walie ewe Omar kwani nafsi huhuzunika na jicho hutoa machozi ".

Mapokezi ya hadithi kuhusu jambo hili yako mengi kiasi ambacho hatuna nafasi ya kuyakamilisha yote, lakini itoshe kwamba Nabii Yaaqub bin Is-haq bin Ibrahim alimlilia mwanawe Yusufu pale Mwenyezi Mungu alipomuondosha Yusuf machoni pake na akasema (alipokuwa akilia): "Oh majonzi yangu kwa Yusufu! Na macho yake yakawa meupe kwa huzuni naye alikuwa amejawa na huzuni ." Qur'an 12:84.

Kutokana na kilio cha Yaaqub imefikia hadi kusemwa kwamba, "Hayakukauka macho yake (kwa kulia) tangu alipotengana na Yusuf(a.s) mpaka alipokuja kukutana naye, ukiwa umepita muda wa miaka themanini. [1]

Basi je palikuwa na nani aIiyebora mbele ya Mwenyezi Mungu katika zama hizo kuliko Nabii Yaaqub?

Imepokewa kutoka kwa Mtume(s.a.w.w) kwamba yeye Mtume alimuuliza Jibril(a.s) yalifikia kiasi gani majonzi ya Yaquub alipokuwa akimlilia mwanae"? Jibril akaseama: Yalifikia kiasi cha majonzi ya wanawake sabini waliopotelewa na watoto wao.

Mtume akasema: "Je alipata malipo kiasi gani?" Jibril akasema: "Alipata ujira wa mashahidi mia moja.. " [2]

Mimi nasema: "Basi ni mtu gani atakayechukizwa na madhehebu yetu sisi (Shia Ithnashari) katika suala Ia kulia tokana na huzuni, baada ya kuwa jambo hili limethibiti toka kwa Manabii. Ni nani anayechukizwa na mila ya Ibrahim? Hakuna, Isipokuwa yule anayeitia nafsi yake katika upumbavu. Qur'an, 2:130.

Kwa hakika sera ya Maimamu juu ya maombolezo na kulia iliendelea zama baada ya zama, na wakawaamuru wafuasi wao kudumisha mikusanyiko ya huzuni juu ya Imam Husein(a.s) .

Amesema Imam Jaafar As-Sadiq(a.s) : "Hakika Ali bin Husein(a.s) alimlilia baba yake maisha yake yote, hapakuwekwa chakula mbele yake ila hulia, na wala hakuletewa kinywaji isipokuwa hulia.

Kutokana na kulia kwake huko, mmoja wa wafuasi wake alimwambia: "Mimi niwefidia kwako, acha kulia hakika nachelea kwamba utakuwa miaongoni mwa wenye kuangamia kwa kulia sana".

Imam Ali bin Husein (Zainul Abidina) akajibu: "Hapana jambo lolote (linaloniliza sana) isipokuwa mimi nashitakia huzuni zangu kwa Mwenyezi Mungu nami nayajua yaliyoko kwa Mwenyezi Mungu ambayo ninyi hamuyajui ".

Na katika mapokezi mengine Imam Ali bin Husein alisema kumwambia mmoja katika wafuasi wake, "Ole wako hakika Yaaqub(a.s) alikuwa na watoto kumi na wawili, macho yake yalibadilika na kuwa meupe kwa ajili ya kulia sana (kumlilia Yusuf) na mgongo wake ulipinda kutokana na huzuni nyingi, hali yakuwa mwanawe yu hai hapa duniani, lakini mimi nalia sana kiasi hiki kwa sababu niliwaona na kuwashuhudia, baba yangu (Imam Husein), ndugu zangu, ami zangu na watu kumi na saba miongoni mwa watu wa nyumba yangu wakiwa wamenizunguka hali wamechinjwa!"

Pia Imam Ali bin Husein alikuwa kila anapochukuwa chombo ili anywe maji, hulia mpaka chombo kile akakijaza damu.

Akiulizwa kuhusu bali hiyo hujibu: "Basi ni kwa nini nisilie wakati ambapo baba yangu alinyimwa maji ambayo yalikuwa hayana kizuwizi chochote kwa wanyama.........?

Na imepokewa hadithi toka kwa Bwana Rayaan bin Shubaib amesema: "Nilingia nyumbani kwa Imam Ar-Ridha(a.s) katika siku ya kwanza ya Muharram, Imam akaniambia: "Ewe mwana wa Shubaib, hakika Mwezi wa Muharram (Mfungo nne) ni mwezi ambao watu wa zama za Jahiliya (kabla kuja Uislamu) walikuwa wakiharamisha dhulma na mauaji kutokana na utukufu wa Mwezi huu lakini watu wa Ummah huu (wa Kiislamu) hawakuheshimu Utukufu wa Mwezi huu wala heshima ya Mtume wao(s.a.w.w) , kwani walikiua kizazi chake ndani ya Mwezi wa Muharram, na wakawateka wanawake wa kizazi cha Mtume wao, na wakapora vyombo vyao, Ewe mwana wa Shubaib, ikiwa wewe utakuwa ni mwenye kulia, basi mlilie Husein(a.s) kwani yeye alichinjwa kama anayavyochinjwa kondoo, na aliuawa yeye pamoja na watu kumi na nane katika watu wa nyumba yake, ambao hawalinganishwi na ye yote hapa duniani kwa ubora, na kwa hakika Mbingu Saba zililia kwa kuuawa Husein".

Imepokewa hadithi toka kwa Abu Ammarah Al-Munshid amesema: "Hakutajwa Imam Husein(a.s) mbele ya Abu Abdillah As-Sadiq(a.s) katika siku yoyote isipokuwa (siku hiyo) hakuonekana kuwa na furaha mpaka usiku".

Na amesema Abu Ammarah, "Abu Abdillah as-Sadiq alikuwa akisema: Mauaji aliyouliwa Husein(a.s) ni jambo Ia kumpa mazingatio kila Muumini.

Na imepokewa kutoka kwa Imam Jaafar As-Sadiq(a.s) amesema: "Imam Husein(a.s) alisema, mimi nitauawa ili yapatikane mazingatio kutokana na mauaji hayo, hatanikumbuka (kwa kunitaja) Muumini yeyote bali atapata mazingatio.

MAJLIS YA PILl

RUHUSA YA KUOMBOLEZA

Hapana shaka kwamba ipo ruhusa ya kuomboleza vifo vya Waumini, na kwamba jambo hilo ni halali, na hapana dalili iliyo kinyume cha hivi.

Kwa hakika baba yetu Nabii Adam(a.s) aliomboleza kifo cha mwanawe Habil, na maombolezo yakawa yanaendelea mpaka leo kila inapotokea jambo la kifo katika kizazi cha wanaadamu bila upinzani.

Ama Mtume Muhammad(s.a.w.w) aliwaruhusu Masahaba wake kufanya maombolezo kwa wingi kutokana na huzuni, na pia aliruhusu kutaja mema ya waliofariki na kutoa sifa zao katika tabia nzuri na matendo mazuri.

Na wakati Mtume(s.a.w.w) alipofariki, Masahaba walishindana katika kutaja sifa zake walipokuwa wakiomboleza kifo chake.

Katika kifo hicho cha Mtume(s.a.w.w) Bibi Fatma bint wa Mtume(s.a.w.w) pia aliomboleza wazi wazi na kuonesha huzuni yake kwa kusoma beti za Kishairi. [3]

Kadhalika kifo cha Bwana Mtume kiliombolezwa na shangazi yake Mtume(s.a.w.w) Bibi Safia kama inavyoonesha katika Istiiab cha Ibnu Abdil-Bari. Pia lbnu ami yake Mtume Bwana Abu Sufian bin Harith Bin Abdil-Mutalib na Bwana Abu-Dhuarib AlHadh-li, Bwana Abul-Haithami At-Taihani, Ummu Ra-Ala AlQushairiyya na Bwana Amir bin At-Tufail na wengineo wote waliomboleza.[4]

Pamoja na maelezo haya, ili kumkinaisha mtu kuhusu suala la maombolezo yafaa sana kukiangalia na kukisoma kitabu kiitwacho Al Istiiab na pia At-Tabaqat cha Ibn Saad na Usudul Ghaaba na al-Isaba, kwani humo atakuta mambo mengi yanayohusu maomboIezo yaliyofanywa na Masahaba.

Katika Masahaba walioomboleza sana-sana kutokana na vifo ni Sahaba wa Kike Bibi Al-Khinsaa, ambaye aliomboleza vifo vya nduguze wawili, Mabwana Sakhr na Muawiya ambao walikuwa makafiri.

Bibi huyu alikuwa miongoni mwa watu wachamungu kiasi kwamba alitoa wanawe kwa ajili ya kutumikia Uislamu, na wote waliuawa katika njia ya kutumikia Uislamu, kitu ambacho Bibi huyu alikifurahia.

Lakini pamoja na yote hayo hakuacha kuomboleza mauti ya nduguze mpaka alipofariki na wala hakutokea mtu wa kumkemea kwa tendo hilo.

Kwa kifupi suala la kuomboleza ni mashuhuri katika kila zama na kila mahali baina ya Waislamu na wala hawapingani katika hilo.

Sisi tunatosheka na dalili ya kuhalalisha maombolezo yetu tuyafanyayo kama walivyopokea wapokezi wetu kutoka kwa Bwana Zaidi bin As-Shuhaam amesema: "Tulikuwa mbele ya Abu Abdullahi Al-Sadiq(a.s) huku tukiwa na kundi la watu kutoka Al-Kufah, mara akaingia Jaafar bin Af-Fan basi Imam Al- Sadiq akamkaribisha na akamsogeza karibu yake kisha akasema: "Ewe Jaafar nimepata habari kwamba wewe unasoma mashairi juu ya Imam Husein na unayasema vizuri, Jaafar bin Af-Fan akasema: "Ndiyo", Imam Jaafar akasema: "Hebu soma mashairi hayo, nikasoma".

Baada ya Mashairi hayo kusomwa katika hali ya kuomboleza mauaji ya Imam Husein(a.s) , Imam Jaafar Al-Sadiq(a.s) alilia na wakalia watu waliokuwa wamemzunguka kiasi ambacho machozi yalimtiririka usoni mwake hadi kwenye ndevu, kisha Imam akasema: "Ewe Jaafar WalIah wamekushuhudia Malaika Watukufu na wao wanasikiliza maneno yako unapoomboleza kwa ajili ya Imam Husein(a.s) , na kwa hakika wamelia kama tulivyolia sisi na zaidi ya hapo, na Mwenyezi Mungu Mtukufu amefaradhisha kwako Pepo katika muda huu na amekusamehe".

Kisha Imam Jaafar Al-Sadiq akasema kumwambia Jaafar bin Af-Fan, "Je. nikuongezee ubora kwa wenye kuomboleza mauaji ya Imam Husein(a.s) ", akasema Jaafar bin Afan: "Ndiyo Ewe Bwana wangu".

Akasema Imam Jaafar(a.s) : "Hapana yeyote yule atakayesoma Shairi la maombolezo ya Imam Husein(a.s) , na kwa maombolezo hayo akalia na akawaliza wengine isipokuwa Mwenyezi Mungu atamsamehe na kumuwajibishia kupata Pepo".

Imam Muhammad bin Idris As-Shafii (Imam Shafii) ni miongoni mwa watu waliombeleza mauaji ya Imam Husein(a.s) aliposoma mashairi ambayo tafsiri yake ni kama ifuatavyo:

Ulimwengu ulitingishika kwa ajili ya kuuawa kizazi cha Mtume Muhammad(s.a.w.w) , Milima migumu ilikuwa karibu kuyeyuka kwa ajili ya kuuawa kizazi cha Mtume Muhammad(s.a.w.w) , Milima migumu ilikuwa karibu kuyeyuka kwa ajili ya kuwahuzunikia wao (kizazi cha Mtume), Basi nani atanifikishia barua ya huzuni kwa Husein? Nitaomboleza kifo cha Husein japo nafsi za watu na nyoyo zitachukia. [5]

MAJLIS YA TATU YAH:

KUSOMWA HABARI ZA WALIOKWISHA PITA HAPO KALE

Hapana shaka kuwa, upo mkazo na umuhimu mkubwa kusoma na kueleza habari na sifa za Waumini waliokwisha fariki zamani, na pia kutaja matatizo na misiba iliyowafika katika maisha yao ya kueneza Uislamu. Kwani kuyataja mambo yao huwa sawa kama kuwataja wao katika hali ya uhai wao.

Ummah hunufaika kutokana na utukufu walioupata zinapotajwa sifa zao, pia tabia njema walizokuwa nazo na vitendo vyao vizuri huunufaisha Ummah wa Kiislamu.

Iwapo Ummah utatoa umuhimu wa kusimulia historia ya viongozi wao walio wema ndiyo nafasi bora ya kulinda Utukufu wake na huwa ni muongozo mzuri kwa kizazi kitakachofuata.

Kwa hakika mwendo wa vizazi vya tangu hapo zamani na vile vilivofuatia baadaye, upo katika mtiririko wa kutaja na kukumbuka ubora wa watu waliokufa na misiba iliyowafika kwa njia mbali-mbali, ikiwa ni pamoja na kuyakumbuka hayo kwa njia za uandishi, khutba na utunzi wa mashairi.

Maamuzi sahihi ya akili pamoja na mapokezi sahihi ni vitu ambavyo kimsingi vinatoa mwelekeo wa kuboresha hifadhi ya masimulizi ya watu waliopita.

Kadhalika misingi ya maendeleo na maarifa inalazimisha kuweko kumbukumbu za athari za zamani zenye manufaa kwa jamii.

Ukweli ulivyo ni kwamba uhifadhi wa athari hizo huzifanya roho za watu watukufu ziendelee kuwa hai, na kutokana na kumbukumbu zao hutokea mashindano kwa walio hai ili kujaribu kuzifikia sifa zao na wema wao (Hakika katika kutaja habari za watu waliopita kuna kumbukumbu yenye mazingatio kwa wenye akili). Qur'an 12:111

Angalia kitabu cha Mwenyezi Mungu na Sunna ya Mtume wake(s.a.w.w) vimeweka wazi sifa za Manabii na matatizo yaliowapata. Pia vimeonyesha bayana jinsi maadui was Mwenyezi Mungu na Manabii wake walivyofedheheka.

Na lau kama si Qur'an na Sunna ya Mtume tusingefahamu Utukufu wa Manabii wa Mwenyezi Mungu, wala tusingejua uovu wa maadui wa Mwenyezi Mungu.

Basi ni vipi hatufahamu kwamba, lau si Qur'an na Sunna kusimamia maelezo ya mafunzo na miongozo ya Mwenyezi Mungu kwa Manabii na waja wa Mwenyezi Mungu, na pia mafunzo ya kuwausia subira kutokana na kero na usumbufu walioupata katika kupigania haki, tungejuaje vituko vya kina Namruda dhidi ya Nabii Ibrahim, na Firaun dhidi ya Musa na wengineo?

Ifahamike wazi kwamba kauli zitolewazo kuharamisha kusomwa na kutajwa ubora wa watu watukufu, na kutaja matatizo yao na misiba iliyowafika ni lazima ziende sambamba na kuharamisha Qur'an na Sunna ya Mtume visisomwe.

Kadhalika ni lazima kauli hizo kama zitakubalika, basi hakutakuwa tena na haja ya somo la historia wala (Ilmu-R-rijal).

Na hakuna mwenye kuridhia upumbavu huu katika nafsi yake akachagua upofu wakati anatambua haki iko wapi.

(Tunajilinda kwa Mwenyezi Mungu kutokana na ujinga uliopita kiasi).

Ili kuthibitisha kwamba kuyataja mema ya waliopita ni tendo lililoanza tangu hapo kabla, tunasoma ndani ya vitabu vya historia juu ya matokeo ya mwaka wa arobaini Hijriya kama ifuatavyo:

Alipofariki Imam Ali(a.s) alisimama mwanawe Imam Hasan(a.s) akasema: "Hakika leo mumemuuwa mtu ambaye hajakuweko kabl yake wakumfananisha naye miongoni mwenu, na hatapatikana ye yote baadaye wa kufananishwa naye .[6]

MAJLIS YA NNE

VIKAO KWA AJILI YA KUHUZUNIKIA WAFU

Hapana shaka kwamba Mtume(s.a.w.w) alihuzunika huzuni nyingi kwa ajili ya kufiwa na Ami yake Bwana Abu Talib na Bibi Khadija Ummul-Muuminina(a.s) , kwani wawili hawa walifariki ndani ya mwaka mmoja, na Mutume akauita mwaka huo kuwa ni mwaka wa "huzuni".

Kipindi hiki cha msiba huu mkubwa, Bwana Mtume(s.a.w.w) alipunguza kutoka, ikawa muda mrefu hukaa nyumbani, na ikawa Maquraishi wanapomhujumu huomboleza kwa kusema: "Ewe Ammi yangu imekuwa mapema mno kukukosa ." [7]

Na zimethibiti habari kwamba Mtume alifanya kikao ndani ya Msikiti kwa ajili ya kuwahuzunikia Ibn Ammi yake Jaafar na Zaid pamoja na ibn Ruwaha waliouawa katika vita ya Muuta.

Vile vile imethibiti kuwa yeye Bwana Mtume alihuzunika sana na haikuonekana huzuni namna hiyo kwa Mtume baada ya kuuawa wasomaji wake wa Qur'an, na alifanya Qunut kuwaombea msamaha kwa muda wa mwezi mmoja, na pia akawa huwaapiza katika Qunut hiyo waliowauwa.

Kwa hiyo basi kutokana na dalili hizi utakuta zinatoa maamuzi ya kutia nguvu kuwekwa vikao kwa ajili ya kuonesha huzuni kwa kuwakosa watu wema na wenye kumbukumbu nzuri na ukarimu.

Kwani katika kuwapambanua na makundi mengine, huwa na sababu ya kuwahamasisha watu ili waweze kutokea miongoni mwao wenye mfano kama huo. Pia jambo hilo dhahiri yake ni kuwapa haki yao wanayostahiki baada ya kufa kwao, na hupelekea kuwapata watu wengi watakaoiga mienendo yao.

Ama tukija upande wa kufanya vikao kwa ajili ya kumbukumbu ya Masaibu yaliyowapata Maimamu katika njia ya kuleta amani na sul-hu kwa Ummah, jambo hili hufanya nafsi kuwa na imani na uongofu na kuzifanya nyoyo kuwafuata Maimamu, japo zimekwisha kupita siku nyingi na matukio hayo yalitokea sehemu za mbali.

Na maneno ya wanaolaumu mambo haya, wakasema kwamba haifal kufanya vikao kwa ajili ya kuhuzunikia maiti hasa unapokuwa umepita muda mrefu, hayana maana tunapoizingatia misiba iliyotupata kutokana na mambo waliyofanyiwa watu wa nyumba ya Mtume(s.a.w.w) , kiasi ambacho ukweli maneno yao hayaturudishi nyuma katika kuwahuzunikia watu wa nyumba ya Mtume japo ni muda mrefu umepita, na wala hayaondoi huzuni iliyotokana na misiba hiyo, na wala hayazimi joto la huzuni muda wote.

Je hawaioni hadithi iliyoandikwa na Imam Ahmad bin Hambal katika Musnad yake kwamba, Imam Ali(a.s) alipokuwa akienda Siffin, alipofika Nainawa akawa anasema: "Kuwa na subira Ee Abu Abdillah kuwa na subira Ee Abu Abdillah katika kingo za mto Furat ".

Akaulizwa Imam Ali(a.s) maana ya kusema hivyo, naye akajibu kwa kusema: "Siku moja niliingia kwa Mtume(s.a.w.w) nikamkuta analia, basi nikamuuliza sababu ya kulia kwake akasema: "Hivi punde Jibril alisimama mbele yangu akaniambia kwamba hakika Husein atauawa katika kingo za mto wa Furat, akasema Jibril: Je nikunusishe udongo wa sehemu hiyo? Nikamwambia ndiyo, basi akanyoosha mkono wake akachota gao moja la udongo akanipa ". [8]

Na imepokewa kutoka kwa Bibi Aisha UmmuI-Muuminina kwamba siku moja Husein bin Ali(a.s) aliingia nyumbani kwa Mtume(s.a.w.w) hali ya kuwa Mtume anapokeya Wahyi, basi Jibril akasema: "Hakika Ummah wako wataingia katika fitna baada yako na watamuuwa mwanao huyu (Husein a.s), na (Jibril a.s) akanyoosha mkono wake akachukua udongo mweupe na akasema katika ardhi ya udongo huu atauawa mwanao ."

Basi Jibril alipoondoka Mtume wa Mwenyezi Mungu alitoka nje hadi kwa Sahaba zake wakiwemo Abubakar na Umar and Ali na Hudhaifa, Ammar na Abudhar, hali ya kuwa analia, basi wote wakamwambia: "Kitu gani kinakuliza Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu?"

Mtume akasema: "JibriI ameniambia kwamba mwanangu Husein atauawa katika ardhi ya AT-TAF na ameniletea udongo huu akasema kuwa, katika udongo huu ndipo yatakapokuwa malazi yake".

Basi mtu wa kwanza kumlilia Imam Husein katika Ummah huu na wa kwanza kupewa udongo wa malazi ya Imam Husein(a.s) na wa kwanza kuunusa na wa kwanza kuwasomea watu mauaji ya Imam Husein(a.s) katika ardhi ya AT-TAF ni Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) .

Na ni yeye Mtume(s.a.w.w) ndiye wa kwanza aliyewasikilizisha masahaba zake hadith ya mauaji ya Imam Husein(a.s) .

Basi hapana shaka kwamba Masahaba walimliwaza Mtume(s.a.w.w) kutokana na huzuni hiyo na kilio chake (Hakika mnacho kiigizo chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa yule anayemtaraji Mwenyezi Mungu na siku ya mwisho, na yeyote mwenye kupinga basi hakika Mwenyezi Mungu ni mkwasi Mtukufu). Qur'an 33:21

MAJLIS YA TANO

KUMTOLEA SADAKA MAITI

Hapana shaka kwamba, ni jambo zuri kuwatolea sadaka maiti wa Waumini kwani jambo hilo alilifanya Mtume(s.a.w.w) na akaamuru lifanywe.

Ndani ya sahihi mbili (Bukhari na Muslim) imepokewa toka kwa Bibi Aisha amesema: "Sikupata kumuonea wivu mwanamke ye yote miongoni mwa wakeze Mtume kuliko nilivyomuonea wivu Bibi Khadija ambaye hata sikuwahi kumuona, lakini Mtume alikuwa akimtaja sana (Khadija) na wakati mwingine alikuwa akichinja kondoo na kumkatakata vipande vipande kisha huvipeleka kwa jamaa za Khadija kuwa ni sadaka, basi wakati mwingine nilimuambia Mtume(s.a.w.w) , "Kama kwamba katika Dunia hii hakupata kuweko mwanamke isipokuwa Khadija, basi Mtume husema hakika alikuwa ni mwanamke wa pekee bora (katika wake nilioowa) na wala hajakuwepo wa mfano wake na kwake yeye Khadija nilipata watoto". [9]

Hadithi hii inatuonyesha kwamba ni jambo zuri kutowa sadaka kwa marafiki au jamaa wa maiti.

Naye Imam Muslim ameandika kwamba, mtu mmoja alifika kwa Mtume(s.a.w.w) akasema: "Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu hakika mama yangu amefariki na wala hakuacha usia, je, atapata malipo iwapo nitamtolea sadaka? Mtume akasema: "Ndiyo ". [10]

KUZALIWA KWA AL-IMAM HUSEIN BIN ALI(A.S)

Al-Imam Husein(a.s) amezaliwa tarehe tano Mwezi wa Shaaban Mwaka wa nne Hijiriyah.

Baada ya kuzaliwa kwake alishuka Jibril(a.s) akiwa na kundi la Malaika wapatao Elfu Moja, wakampongeza Mtume(s.a.w.w) .

Mtume(s.a.w.w) alifurahi sana kwa kuzaliwa kijana huyu, na akawa amempa jina Ia Husein.

Imepokewa kutoka kwa Ummul-Fadhl mkewe Bwana Abbas Bin Abdil-Mutalib amesema; "Niliota ndoto kabla Husein hajazaliwa, nikaona kama kwamba kipande cha nyama ya mwili wa Mtume kimewekwa mapajani mwangu basi nikamsimulia jambo hilo Mtume wa Mwenyezi Mungu, Mtume akasema: "Naona kuna kheri iwapo ndoto yako itakuwa ya kweli, kwani Fatma atazaa mtoto wa kiume nami nitakupa wewe umlee".

Anaendelea kusimulia Ummul-Fadhli anasema: "Basi mambo yakawa kama alivyosema Mtume(s.a.w.w) na akanipa Husein nimlee".

Siku moja nikaja naye kwa Mtume(s.a.w.w) , wakati Mtume(s.a.w.w) akiwa anambusu Husein, alikojoa na likaruka tone la mkojo kwenye nguo ya Mtume(s.a.w.w) nikamshika Husein (a.s) ili kuepusha asizikojolee nguo za Mtume(s.a.w.w) , Husein(a.s) akalia, Mtume akasema katika hali ya kama mwenye kukemea, "Tulia ewe Ummul-Fadhli, nguo yangu itafuliwa lakini umemuumiza mwanangu ."

Ummul-Fadlili anasema: "Nikamuacha Husein mapajani kwa Mtume na nikasimama kwenda kumletea Mtume(s.a.w.w) maji aisafishe nguo yake.

Basi nikaleta maji na nikamkuta Mtume(s.a.w.w) analia, nikamwambia unalia nini ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu?

Mtume(s.a.w.w) akasema: "Hakika Jibril amenijia na kuniambia kwamba Ummati wangu watamuuwa mwanangu huyu basi ole wao, Mwenyezi Mungu asiwafikishie shufaa (maombezi) yangu siku ya Qiyama watu watakaomuuwa ."

Al-Imam Husein(a.s) alipotimiza mwaka mmoja tangu kuzaliwa kwake, walimshukia Mtume(s.a.w.w) Malaika kumi na wawili, nyuso zao nyekundu huku wanalia na wakawa wanamuambia Mtume(s.a.w.w) kwamba: "Hakika mwanao yatampata masaibu yaIiyompata Habil kutoka kwa Qabil, na kwa ajili hiyo atapewa malipo mema kama alivyopewa Habil, na atakayemuuwa atakuwa na dhambi sawa na dhambi za Qabil.

Hapakubakia Malaika huko Mbinguni ila wote walikuwa wakishuka na kuja kumpa pole na kumuomba awe mvumilivu na pia walikuwa wanamfahamisha malipo atakayolipwa Imam Husein(a.s) , si hivyo tu, bali walikuwa wanamuonyesha udongo wa mahali atakapouawa, na Mtume(s.a.w.w) akawa husema: "Ewe Mwenyezi Mungu mpinge atakayempinga na Umlaani atakaye muuwa... "

Alipotimia Imam Husein umri wa miaka miwili Mtume alitoka kufanya safari na katika safari yake hiyo alisimama mahali fulani, basi aliamua kutoendelea na safari yake na mara macho yake yakawa yanabubujika machozi, akaulizwa sababu gani iliyomfanya alie. Mtume(s.a.w.w) akasema: "Jibril ananieleza kuhusu ardhi iliyoko kando ya mto Furat iitwayo "KARBALA" mahala ambapo atauawa mwanangu Husein, sasa hivi ni kama nauona uwanja wa mapambano baina yake na adui zake, pia kama kwamba napaona mahala atapozikwa.

Kisha baadaye Bwana Mtume(s.a.w.w) aliamua kurudi hali ya kuwa mwenye huzuni na majonzi, akapanda katika Mimbari na akatoa khutba huku Hasan na Husein(a.s) wakiwa mikononi mwake.

Alipoteremka kwenye Mimbari akaweka mkono wake wa kulia juu ya kichwa cha Imam Hasan na nikono wa kushoto akauweka kichwani kwa Imam Husein(a.s) akanyanyua kichwa chake mbinguni akasema: "Ewe Mwenyezi Mungu hakika mimi Muhammad Mja wako na ni Nabii wako na hawa wawili (Hasan na Husein) ni watu bora katika familia yangu na ni wabora katika kizazi changu na atakuwa mbora mtu atakayewafuata hawa katika Ummati wangu, na hakika Jibril ameniambia kwamba mwanangu huyu atapingwa na atauawa. Ewe Mola mpe baraka nyingi atakapouawa na umfanye awe miongoni mwa Mabwana wa Mashahidi. Ewe Mwenyezi Mungu usimbariki atakayemuuwa na atakayempinga."

Basi baada ya maneno hayo watu wakaangua kilio Msikitini, kisha Mtume akatoa tena khutba nyingine fupi hali yakuwa rangi imembadilika na macho yake yanatoka machozi akasema, "Enyi watu hakika mimi ninawaachia vizito viwili, Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu na Kizazi changu watu wa Nyumba yangu, na hakika viwili hivyo havitatengana mpaka vinifikie katika Haudh, fahamuni kwamba hakika mimi ninavisubiri viwili hivyo, na kwa hakika siwatakeni jambo lolote isipokuwa ni lile aliloniamuru Mola wangu. "Muwapende jamaa zangu". (Kizazi Changu).

Mtume akaendelea kusema: "Fahamuni ya kwamba (siku ya Qiyama) yatanijia makundi matatu katika Ummah huu.

Kundi Ia kwanza litakuwa Ia watu weusi sana, wamezingirwa na Malaika, kisha watasimama mbele yangu nami nitasema: "Ni kina nani nyie"?

"Watashindwa kunitambua, nao watasema: "Sisi ni watu wa Tauhidi mongoni mwa Waarabu.

Basi mimi nitawaambia, "Mimi ndiye Ahmad Nabii wa Waarabu na wasio Waarabu".

Kisha wao watasema: "Sisi ni katika ummati wako".

Nami nitawaambia: "Basi ni vipi mulinifuata katika kizazi changu na katika Kitabu cha Mola Wangu".

Watanijibu: "Ama kitabu tulikipuuza na kizazi chako tulikiangamiza kwa kuwauwa".

Basi nitageuza uso wangu, nao watarudi wakiwa na kiu kali hali ya kuwa nyuso zao ni nyeusi.

Kisha litanijia kundi jingine jeusi mao kuliko lile la mwanzo nami nitawaambia: "Vipi mulinifuata katika vizito viwili, kile kikubwa na kile kidogo, yaani Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Kizazi changu"?

Basi hao watasema: "Ama kile kikubwa (Qur'an) tulikipinga, na ama kile kidogo tulikinyanyasa na kukitawanya ovyo ovyo".

Basi nitawaambia niondokeeni mbele yangu hapo wataondoka hali wakiwa na kiu kali makoo yamewakauka na nyuso zao nyeusi.

Baadaye litanijia kundi jingine Ia watu ambao nyuso zao zinangara kwa nuru.

Basi nami nitawauliza, "Ni kina nani ninyi?"

Watasema: "Sisi ndiyo watu wa neno Ia Tauhidi na Uchamungu, sisi ni Ummati wa Muhammad Mteule, nasi ndiyo bora katika watu wa haki, tulikilinda vema Kitabu cha Mola wetu, tukaihalalisha halali iliyohalalishwa na Kitabu na tukaiharamisha haramu iliyoharamishwa na Kitabu, na tuliwapenda kizazi cha Nabii wetu".

Basi nitawaambia: "Furahini hakika mimi ndiye Nabii wenu Muhammad(s.a.w.w) na hakika ninyi duniani muliishi kama hivyo mlivyontajia."

Basi hapo nitawanywesha maji kutoka ndani ya Haudhi langu (alilonipa Mwenyezi Mungu) nao watarejea bali ya kuwa kiu imewakatika tena watakuwa na furaha, na baadaye wataingia peponi waishi humo milele na milele.

KUTHIBITI UIMAM KWA HUSEIN(A.S)

Ulithibiti Uimamu kwa Imam Husein(a.s) baada ya kufariki kwa nduguye Al-Imam Hasan bin Ali bin Abi Talib(a.s) na hapo ikawa ni faradhi kwa viumbe wote kumtii Imam Husein(a.s) .

Na Uimamu wake ulikuwa ni kwa mujibu wa kauli ya baba yake na babu yake(a.s) na pia usia wa nduguye Imam Hasan(a.s) .

Imam Hasan na Imam Husein(a.s) wao ni Mabwana wa vijana wa peponi kwa mujibu wa Mwenyewe Mtume wa Mwenyezi Mungu ambaye ni babu yao.

Miongoni mwa ubora waliokuwa nao Imam Hasan na Imam Husein(a.s) , baada ya kuwa ni wajukuu wa Mtume(s.a.w.w) na vipenzi vyake katika watu wa nyumba yake, pia ni miongoni mwa watu aliotokanao kwenda kuapizana na wakristo wa Najran pale iliposhuka aya ya 61 Sura ya Tatu:

"Basi watakaokuhoji kuhusu Nabii Issa, baada ya kukufikia ujuzi (wa-jambo hili) basi waambie njooni tuwaite watoto wetu na watoto wenu na wanawake wetu na wanawake wenu na sisi wenyewe na ninyi, kisha tuapizane tuombe laana ya Mwenyezi Mungu iwashukie waongo ".

Aya hii inaitwa aya ya Mubahala, na sababu ya kushuka kwake, ni pale viongozi wa Kikristo kutoka Najran walipokuja Madina katika mwaka wa tisa Hijiriya kumjadili Bwana Mtume(s.a.w.w) kuhusu Nabii Isa(a.s) Mtume akawajibu kwamba; "Hakika mfano wa Isa mbele ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa Adam ".

Wakristo hao waliendelea kumjadili Mtume(s.a.w.w) hata baada ya jibu hili, ndipo Mwenyezi Mungu aliposhusha aya hii ya 61 Sura ya Tatu, Mtume akaambiwa kama wataendelea kumhoji, basi awaambie waje waapizane kama ilivyoashiria aya hiyo.

Kutokana na uzito wa suala la kuapizana baina ya Mtume(s.a.w.w) na Wakristo hao, ilibidi Bwana Mtume(s.a.w.w) kwa upande wa Waislamu atoke na watu ambao pia watakuwa na uzito wa kukabili maapizano hayo.

Ndipo alipowachukua Hasan na Husein kama wawakilishi wa watoto wa Kiislamu, na Bi Fatma(a.s) kama muwakilishi upande wa wanawake wa Kiislamu na yeye Mtume(s.a.w.w) na Imam Ali(a.s) wakawa ndiyo nafsi za Waislamu.

Kwa mujibu wa uwakilishi wa Imam Hasan na Imam Husein(a.s) katika tukio hili unadhihiri ubora na utukufu wa vijana hawa wawili ndani ya Uislamu, na inamuwajibikia kila Muislamu kuitambua heshima yao na daraja waliyopewa na Mwenyezi Mungu, kama ambavyo Kiongozi Mkuu wa Wakristo hao kutoka Najran alivyokiri ubora na utukufu uliomo ndani ya nyumba ya Mtume(s.a.w.w) siku hiyo ya mapinzano akasema: Hakika mimi naziona nyuso za watu ambao lau watamuomba Mwenyezi Mungu auondoe mlima mahala ulipo atauondoa, hivyo basi musiapizane nao mtaangmia na hatabakia Mkristo yeyote ulimwenguni baada ya leo".

Pia miongoni mwa hoja zilizowazi kuhusiana na utukufu walio kuwa nao Imam Hasan na Imam Husein ni kuteremka aya zinazothibitisha kuwa wao ni katika watu watakaoingia Peponi hali ya kuwa bado wakiwa ni vijana wadogo, na jambo hili linapatikana katika Surat Ad-Dahr kuanzia aya ya saba mpaka aya ya kumi na mbili.

Kabla ya kuzitaja aya hizo ni bora kukisimulia kisa cha kushuka aya hizo japo kwa mukhtasar.

Imepokewa kwa Ibn Abbas kwamba, Hasan na Husein(a.s) waliugua. Basi Mtume na baadhi ya watu wakenda kuwaona, watu hao wakamwambia Imam Ali(a.s) "Lau utaweka nadhiri itakuwa bora ".

Imam Ali, Bi Fatma(a.s) na Mjakazi wao aliyekuwa akiitwa Fiza, wakaweka nadhiri ya kufunga siku tatu ikiwa Hasan na Husein watapona.

Vijana hawa wawili walipona na ikawa kipindi cha kutekeleza ile nadhiri kimefika, lakini ndani ya Nyumba hamkuwa na kitu.

Hivyo Imam Ali(a.s) alikwenda kwa Myahudi mmoja aliyekuwa akiitwa Sham-uun na akakopa vibaba vitatu vya shayiri.

Bi Fatma(a.s) akaisaga shayiri hiyo na akaoka mikate mitano kwa ajili ya kufuturu kulingana na idadi yao katika nyumba yao.

Chakula hicho kilipowekwa ili waanze kula, alibisha hodi mgeni na akawatolea salam akasema:

"Asalaam Alaikum enyi watu wa Nyumba ya Mtume, mimi ni Masikini wa Kiislamu naomba munipe chakula, nanyi Mwenyezi Mungu atakulisheni chakula cha Peponi ".[11]

Basi wakamuonea huruma wakampa chakula chote, nao wakanywa maji kisha wakalala.

Asubuhi wakaamka na saumu na jioni mwana Fatma aliandaa tena mikate na ilipowekwa tayari kufuturu alibisha hodi yatima na kuomba chakula, wakampa na wao wakanywa maji kisha wakalala.

Asubuhi waliamka na saumu, kisha jioni Bi Fatma alioka tena mikate mitano kwa ajili ya kufuturu.

Walipoketi kufuturu alibisha hodi mtu aliyekuwa mateka akaomba chakula wakampa mikate yote kisha wakanywa maji wakalala.

Kwa ajili ya wao kujinyima kwa muda huo wa siku tatu mfulululizo ndipo ziliposhuka aya zifuatazo katika Sura Ad-Dahr "Wanaotekeleza nadhiri (zao) wanaiogopa siku ambayo shari yake itaenea na wanawalisha chakula masikini na yatima na mateka hali wao pia wanakitaka chakula hicho. (nao husema watoapo chakula hicho) tunakulisheni kwa ajili ya kutaka radhi ya Mwenyezi Mungu, hatutaki kwenu malipo wala shukurani. Hakika tunaogopa kwa Mola wetu siku hiyo yenye taabu na shida. Basi Mwenyezi Mungu atawalinda na shari ya siku hiyo na kuwakutanisha na neema na furaha. Na atawalipa kwa kuwapa Bustani (Pepo) na (Mavazi) ya hariri kutokana na kusubiri kwao.

Zaidi ya hayo ni kwamba Bwana Mtume(s.a.w.w) alidhihirisha wazi Uimamu wao kwa Ummah wake pale aliposema: "Wanangu hawa (Hasan na Husein) ni Maimamu wawe wima au wawe wamekaa ".

Mlolongo wa uimamu wa Maimamu wetu umekuja kwa kila mmoja kumbainisha atakayechukua nafasi ya Imam anayeondoka.

Na jambo hili Ia kubainisha Imamu anayefuata IiIianzia kwa mwenyewe Bwana Mtume(s.a.w.w) kumbainisha Imam Ali(a.s) katika bonde Ia Khum pale alipokuwa akitoka katika Hija ya mwisho. (Mwenye kutaka ziada kuhusu jambo la Uimamu wa Ali bin Abi Talib(a.s) atizame vitabu vya hadithi za Mtume na vitabu vya Historia vinavyotegemewa usahihi wake atalikuta liko wazi). Naye Imam Ali(a.s) alimbainisha Imam Hasan kuwa ndiye atakaye chukua nafasi yake, naye Imam Hasan alimbainisha nduguye Husein(a.s) kuwa ndiyo Imam wa haki baada yake.

Lakini kwa bahati mbaya sana siyo Imam Ali wala Imam Hasan na Husein(a.s) aliyepata fursa ya kuongoza Ummah kama ilivyotarajiwa.

Na hii ilitokana na hali iliyowasibu watukufu hawa baada ya Mtume kuondoka.

Tukimuangalia Imam Husein unakuta matatizo yaliyomkuta ni kama yale yaliyomkuta baba yake hata akasema lmamu Ali kama ifuatavyo: "Nikawa nafikiri baina ya kuwa niupate (Ukhalifa) kwa kuuvuta kwa nguvu au nivumilie uvumilivu wa vipofu wasiojua kitu" Mpaka alifikia kusema, "Basi nikaamua kuvumilia hali ya kuwa jichoni mwangu mna mchanga, na katika koo langu mna dukuduku, nauona urithi wangu umechukuliwa kwa nguvu".

Kwa mwendo kama huu, ndivyo alivyofanya Imam Hasan(a.s) katika siku za uhasama wa Bani Umayya, pindi Mu'awiya bin Abi Sufiyan alipotwaa madaraka ya Ukhalifa kwa nguvu.

Lakini ifahamike wazi sera ya Maimamu wetu kuwa ni sera ya Mtume(s.a.w.w) kwani taabu ilimpata Mtume mwanzo wa kubashiria Uislamu, hakupata utulivu kila alipokuwa akiwaita watu kwenye Uislamu.

Kwa hiyo hali ya Mawasii wake baada yake ni kama ilivyokuwa kwake Mtume(s.a.w.w) hasa itakapokumbukwa kwamba, Maquraishi walipata kumtenga Bwana Mtume(s.a.w.w) na baadaye akalazimika kujificha pangoni wakati akihama Makkah kwenda Madina.

Hali ya matatizo na usumbufu, kama ilivyowapata Manabii ndivyo ilivyokuwa kwa Maimamu.

Muawiyyah bin Abi Sufiyani alipofariki na hali ya vita ikawa imemalizika, hali ambayo ilikuwa ikimzuia Imam Husein(a.s)

kujitangaza Uimamu wake wazi wazi, kipindi hiki walitokea watu wa kumsaidia Imam Husein(a.s) katika kufikisha Ujumbe wa Mwenyezi Mungu, Imam Husein(a.s) alisimama na kujiandaa kufikisha na kusimamia Dini ya Mwenyezi Mungu (s.w.t).

Ili kuanza utekelezaji wa kazi hii, ilimbidi Imam Husein asafiri kutoka Madina kwenda Makkah na hatimaye aelekee Iraq kutokana na wito wa watu wa Al-Kufa waliomtaka aende huko ili akawasaidie na kuwaokoa dhidi ya watawala dhalimu.

Kabla yeye Imam Husein(a.s) kuelekea huko, alimtanguliza Ibn ammi yake Bwana Muslim Bin Aqiil ili akaanze kuwalingania

Dini ya Mwenyezi Mungu na kuchukua kwao baia (kiapo cha utii) kwa niaba ya Imamu Husein(a.s) kwamba watakuwa naye katika Jihadi ya kutetea neno Ia Mwenyezi Mungu, na kuiokoa Dini na Waislamu kutokana na wanafiki waliokuwa wamewakalia Waislainu kwa mabavu.

Muslim Bin Aqiil alipofika huko, watu hao walimpokea na kumuahidi kumsaidia. Lakini haukupita muda mrefu watu hao wakatangua kiapo chao kwa Muslim Bin Aqiil na wakamuacha akauawa mbele yao kifo cha dhulma akiwa ugenini, lakini pia alikufa akiwa ni shahidi.

Na wao hao hao waliomuita Imam Husein wakatoka hapo Al-Kufa kumfuata Imam Husein kwenda kumpiga vita, na wakamtendea mambo ambayo hawakuyatenda Khawarij (Kundi lililomuasi Imamu Ali(a.s) .

Wahinsonga Imam Husein(a.s) , wakamzuia asirudi Makkah wala Madina, wakaweka vizuizi baina yake na maji ya mto Furat mpaka wakamuua hali akiwa na kiu, na wakamdhulumu hali akiwa katika Jihadi, mwenye subira akitaraji radhi za Mola wake.

Hakika ilitenguliwa baia yake na heshima yake ilivunjwa na wala ahadi alizoahidiwa hazikutekelezwa na wakapora mali zake, wakawashika mateka familia yake, wakakidhulumu kizazi cha Mtume(s.a.w.w) hali ya kuwa kimekosa ni mahali gani kitakwenda, njia zote zimefungua.

Kizazi cha Mtume(s.a.w.w) kikawa na huzuni isiyokifani.


1

MAOBOLEZO YA KIFO CHA IMAM HUSEIN(A.S)

SAFARI YA IMAM HUSEIN(A.S) TOKA MADINA HADI MAKKA

Baada ya Imam Hasan(a.s) kufariki. Mashia waliokuwa Iraq walimuandikia Imam Husein kumjulisha kwamba wao waniempa baia na wako tayari kumnusuru.

Imam(a.s) aliwajibu kwa kusema: "Baina yetu ma Muawiya upo mkataba kuhusu jambo hili, hivyo haifai kuuvunja mkataba huo ".

Katikati ya mwezi wa Rajab mwaka wa Sitini Hijiriyah Muawiyyah Bin Abi Sufian alikufa na Yazid mwanawe Muawiyyah akachukua mahali pa baba yake, na ile ahadi na makubaliano aliyoyafanya Imam Hasan na Muawiyyah yakavunjwa, kwani usia wa Muawiyyah ulitaka Yazid ndiyo awe Khalifa kinyume na makubaliano kwamba atakapokufa Muawiyyah ukhalifa urudishwe katika nyumba ya Mtume(s.a.w.w) .

Basi ilikuwaje alipochukua Ukhalifa Yazid yule mlevi asiyejali utu wake, mcheza na mbwa, hana akijuacho katika dini kama alivyokiri yeye mwenyewe ndani ya ibara ziftuatazo baada ya kukalia Ukhalifa akasema: "...na kwa hakika nimetawazwa baada yake (Muawiyyah) na wala sitowi udhuru (wa kuacha jambo hili) kutokana na ujinga (nilionao) na wala sijisumbui kutafuta elimu ".[12]

Kitabu hiki kinatolewa na Wizara ya Elimu ya Saud Arabia kwa ajili ya shule za kati kwa wasichana ndani ya sahi ya tatu."[13]

Jambo aliloona kwamba ndiyo maslahi kwake yeye Yazid, ni kuandika barua kumpelekea lbn Ami yake Walid bin Utba ambaye alikuwa ndiyo Gavana wa Madina siku hizo, akamuamuru achukue baia kutoka kwa watu wote na kutoka kwa Imam Husein(a.s) kwa niaba yake yeye Yazid, akasema katika barua hiyo "Iwapo Husein(a.s) atakataa kutoa baia basi muuwe na uniletee kichwa chake".

Walid bin Utba alipoipata barua hiyo alimtaka ushauri Marwan.

Marwan akamwambia Walid "Hakika Husein(a.s) hawezi kumbai Yazid, lakini Iau mimi ningekuwa na cheo kama chako ningemuua."

Baadaye Walid alimwita Imam Husein(a.s) , naye akaja kwa Walid akiwa na watu thelathini miongoni mwao wakiwa ni watu wa nyumba yake na wafuasi wake.

Imam Husein(a.s) alipofika mbele ya Walid, yeye Walid akamjulisha Imam(a.s) juu ya kifo cha Muawiyyah na pia akawa anamlazimisha ampe baia Yazid.

Imam Husein(a.s) akamwambia "Hakika kiapo cha utii (baia) siyo jambo la siri, basi kesho waite watu nasi pia tuite (tutafanya hiyo baia).

Marwan akasema kumwambia Walid "Ewe Amir usikubali udhuru wake, kama ni baia atowe sasa hivi au sivyo muuwe."

Imam Husein(a.s) akakasirishwa na maneno ya Marwan akamwambia "Ewe mwana wa Zarqaa unaniuwa wewe au yeye? Hakika wewe ni muongo tena umefanya jambo Ia uovu (Kutamka hivyo)". Kisha Imam akamgeukia Walid akasema: "Kwa yakini sisi ndiyo watu wa Nyumba ya Mtume(s.a.w.w) , na kwetu ndiyo kwenye kituo cha Ujumbe (wa Mwenyezi Mungu) na Mwenyezi Mungu alileta nusra kupitia kwetu sisi na akaukamilisha Ujumbe wake kwa Ulimwengu kwetu sisi, na huyu Yazid ni mtu mlevi, muuwaji wa nafsi bila sababu, anafanya maovu wazi wazi, kwa hiyo basi watu kama mimi hawawezi kumpa baia mtu kama yeye". Kisha Imam Husein(a.s) alitoka mahala hapo akaenda zake.

Marwan akamwambia Walid: "Unaona ulipinga ushauri wangu". (Sasa Husein amekukatalia wazi wazi) Walid akamkemea Marwan akasema: "Kefule!!! Ulilokuwa umenishauri ni jambo la kuniharibia Dunia yangu na Akhera yangu, Wallahi sipendi kuona Dunia yote inakuwa yangu wakati nitakuwa nimemuuwa Husein eti kwa sababu amesema hatombai Yazid, walasidhani kama ye yote atakayemuuwa Husein kwamba atakutana na Mwenyezi Mungu akasalimika, bali mtu huyo atajikuta siku ya Qiyama mizani yake ni nyepesi (hana chochote) na Mwenyezi Mungu hatomtazama mtu huyo wala hatamtakasa na atapata adhabu kali". (kwa kumuuwa Husein).

Basi Imam Husein alikaa Nyumbani kwake usiku huo ambao ulikuwa ni usiku wa kuamkia Jumamosi tarehe 27 Rajab mwaka wa Sitini.

Kulipokucha akatoka ili apate kujua habari zilizoko mjini, mara akakutana na Marwan, kisha Marwan akasema: "Ewe Abu Abdillah (Imam Husein) mimi ninayo nasaha kwa ajili yako tafadhali nitii kwa nitakayokuambia utafanikiwa".

Imam Husein(a.s) akasema: "Ni nasaha gani hiyo sema niisikie"?

Marwan akasema: "Hakika mimi nakuamuru umtii Yazid kwani jambo halo ni bora kwako na ni bora katika Dini yako na Dunia yako".

Imam Husein(a.s) akasema: "Hakika sisi ni milki ya Mwenyezi Mungu na hakika sisi kwake tutarejea, Eti mimi kumtii Yazid ndiyo itakuwa ni amani kwa Uislamu? Hakika Ummah umepata mtihani mkubwa kwa kuwa na kiongozi mfano wa Yazid".

Mazungumzo baina yao yalikuwa mengi kiasi ambacho Marwan aliondoka il-hali kachukia.

Jioni ya Jumamosi Walid alituma watu waende kwa Imam Husein(a.s) ili aje afanye baia.

Imam Husein akawaambia: "Ngojeni kutapokucha kesho kisha mtaona ni lipi la kufanya, nasi pia tutaona la kuamua". Wakanyamaza wala hawakuendelea kumlazimisha afanye baia.

Basi Imam Husein alitoka usiku wa kuamkia Jumapili tarehe 28 Rajab kuelekea Makkah, pamoja na wanawe na ndugu zake na kikundi cha watu wa nyumba yake, akaondoka Madina hali anasoma Aya ya Qur'an isemayo: "Akatoka katika mji huo hali anakhofu, anangoja (lipi litamfika) akasema: "Mola wangu niokowe kutokana na watu madhalimu ". Sura Al-Qasas: 21.

Alipita njia kuu iliyo mashuhuri, akaombwa abadili njia kukwepa kufuatwa na adui kama alivyofanya Ibnuz-Zubair, akakataa kufanya hivyo na akasema: "Sitaiacha njia hii mpaka Mwenyezi Mungu aamuwe chochote atakachoniamulia".

Imam Husein(a.s) alifika Makkah usiku wa kuamkia Ijumaa tarehe tatu Shaaban, na aliingia Makkah huku akisoma Aya ifuatayo:

"Na alipoelekea upande wa Madiyan alisema: Huenda Mola wangu ataniongoza njia iliyo sawa ". Sura Al-Qasas Aya 22.

Alikaa hapo Makka kuanzia Mwezi huo wa Shaaban mpaka mfungo pili na siku nane za Mwezi wa mfungo tatu, kisha aliona usalama wake pale Makka in mdogo.

Kwa hiyo Imam Husein hakuwa na utulivu tena wa kumuwezesha kukamilisha Ibada yake ya Hija kwa kuhofia kukamatwa na majasusi ambao wangemkamata hapo Makka na kumpeleka kwa Yazid Bin Muawiyyah.

Hivyo basi akafungua Ihram yake na akaifanya kuwa ni Umra.

Imam Husein(a.s) akautoka Mji wa Makka ambao in Mji wa Mwenyezi Mungu uliotukuka, katika Mji huo ndege na wanyama wanapewa amani waingiapo, basi vipi kwa mjukuu wa Mtume(s.a.w.w) kutishiwa amani yake?

Alitoka Makka kama alivyo uacha mji Mtukufu wa Madina mji wa babu yake ambaye in Mtume wa Mwenyezi Mungu, hali anakhofu mwenye kungojea lipi litamtokea.

MAJLISI YA SITA

YALIYOTOKEA MAKKA BAADA YA IMAM HUSEIN(A.S) KUFIKA HAPO

Ilipofahamika kwa wakazi wa Makkah kwamba, Imam Husein(a.s) yupo Mjini hapo, wakazi wa Mji huo walianza kumtembelea kwa wingi.

Miongoni mwa watu waliofika kwake ni pamoja na wageni kutoka sehemu mbalimbali waliokuja Makka kufanya Umra.

Ikawa watu wanapishana, hawa wanatoka na wengine wanaingia. Pia Abdallah Bin Abbas na Talha Bin Zubair nao walifika kumuona Imam Husein(a.s) .

Wawili hawa walimtaka Imam Husein(a.s) akae hapo Makkah na anyamaze. (Asijihusishe na mambo ya Ukhaiifa).

Imam aliwajibu akasema, "Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu aliniamuru jambo ambalo mimi nitalitekeleza ".

Vile vile Abdallah bin Omar bin Khatab alifika kwa Imam Husein(a.s) na kumtaka afanye mapatano na Yazid bin Muawiya bin Abi Sufiyan.

Imam(a.s) alijibu akasema, "Ewe Baba Abdur-Rahman, unafahamu kwamba Dunia hii kwa uovu uliyomo ni pamoja na kuvinyanyasa viumbe vitukufu vya Mwenyezi Mungu, na elewa pia kwamba kichwa cha Mtume Yahya bin Zakariya kilitolewa na kuwa kama zawadi kwa mtu muovu miongoni mwa watu waovu wa Kiban-Israil?" Akaendelea Imam(a.s) kusema, "Je unafahamu kwamba, wana wa Israil walikuwa wakiwauwa manabii sabini katika kipindi cha kuchomoza Al-fajiri na kutoka jua, kisha baada ya kufanya tendo hili, huenda wakakaa sokoni na kufanya biashara zao za kununua na kuuza kama kwamba hawakutenda chochote cha uovu? Lakini Mwenyezi Mungu hakufanya haraka kuwaadhibu kutokana na maovu yao bali baadaye aliwaadhibu adhabu kali, basi muogope Mwenyezi Mungu ewe baba Abdur-Rahman na wala usiache kunisaidia".

Katika mji wa Al-Kufah, habari za kifo cha Muawiyya zilipowafikia watu wa Mji huo pia kutawazwa kwa Yazid kuwa ndiyo Khalifa wao hawakupendezwa.

Na waIipofahamu kuwa Imam Husein amekataa kumpa baia Yazid na kwamba yuko Makkah, Mashia walikusanyika katika nyumba ya bwana Suleiman bin Surd AI-Khuzai.

Walipokamilika Bwana Sulaiman alisimama akasema, "Kwa hakika Muawiyya amekufa na Husein amekataa kuwatii waliotwaa madaraka na ameondoka Madina sasa yuko Makkah, nanyi ndiyo wafuasi wa baba yake basi ikiwa mnajua kwamba mnaowajibu wa kumsaidia na kumpiga adui yake na kuziangamiza nafsi zetu kwa ajili yake muandikieni barua aje, na kama mtaogopa kushindwa basi musimuite mtu huyu".

Wakajibu kwa kusema; "Sisi tuko tayari kutoa nafsi zetu kwa ajili yake na tutampiga adui yake".

Sulaiman akasema, "Basi muandikieni". Wakamuandikia Imam Husein(a.s) .

BISMILLAAH RAHMAN RAHIM

Barua kwa Husein bin Ali(a.s) kutoka kwa Sulaiman bin Surd na Musayib bin Najiya na Rifaat Shadad na Habib bin Mudhhir na Mashia wake Waumini Waislam katika watu wa Al-Kufah.

Amani iwe juu yake, hakika tunamtukuza Mwenyezi Mungu ambaye hapana Mola ila yeye.

Ama Baad:

Sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu ambaye amemuangamiza adui yako aliyekuwa jeuri na mpinzani wa haki huku anaijua.

Adui huyo aliukandamiza Umma huu kwa nguvu, akapora mali za Umma, akautawala Umma hali yakuwa hautaki kutawaliwa naye, kisha akawa anauwa watu wema katika Umma huu na kubakisha watu waovu mali ya Mwenyezi Mungu akaifanya ni ya kutumiwa na matajiri na wakatili, basi na alaaniwe kama walivyolaaniwa watu wa Thamud.

Kwa hakika sisi hatuna kiongozi wa kutuongoza, basi njoo ili Mwenyezi Mungu apate kutuunganisha katika haki kwako wewe.

Na huyu Nuuman (Gavana wa Muawiyya hapo al-Kufah) sisi hatushirikiani naye kwenye Ibaada ya Ijumaa wala hatutoki pamoja naye kwenye sala ya Idi.

Iwapo tutafahamu tu kwamba tayari umeshafika mjini hapa, basi tutamtoa tumrudishe Shamu Insha-Aallah.

Amani iwe juu yako ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu na pia amani imshukie Baba yako, wala hapana hila wala nguvu isipokuwa vitoke kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu."

Kisha barua hiyo wakapewa Mabwana Abdallah bin Masmaa Al-Hamadani na Abdallah bin Wail waipeleke Makkah na wakawaamuru kwenda mwendo wa haraka.

Baada ya siku mbili kupita tangu walipotuma barua yao, watu wa Mji wa Al-Kufah waliwatuma Mabwana wafuatao.

1. Qais bin Mas-har As-Saidawi

2. Abdalla na Abdur-Rahman watoto wa Shadad Al-ar-habi.

3. Ammarah bin Abdallah Al-Saluli

Waliwapatia barua zisizopungua mia tano kila mtu.

Baada ya siku mbili tena wakawatuma Mabwana Hani bin Haniy As-Subai na Said bin Abdallah Al-Hanafi waende kwa Imam Husein(a.s) kumpelekea barua iliyokuwa na maneno yafuatayo.

BISMILLAHI RAHMAN RAHIM

Kwa Husein bin Ali(a.s) barua kutoka kwa wafuasi wake miongoni mwa Waumini na Waislamu.

Ama baada salaam:

Njoo haraka, kwa hakika watu wanakusubiri, hawana rai nyingine ila kukusubiri wewe.

Basi fanya haraka tena haraka sana"

Barua kwenda kwa Imam Husein(a.s) zilifuatana mfululizo kiasi cha kufikia barua kumi na mbili alfu.

Pamoja na wingi wa barua na kuhimizwa kote alikohimizwa ndani ya barua hizo, Imam Husein(a.s) alikuwa mzito kuwajibu watu hao.

Siku moja ilitokea zikamfikia barua mia sita wajumbe waliotumwa wote wakakutana kwa Imam Husein katika kipindi hicho hicho.

Imam Husein(a.s) akawauliza kuhusu hali ya watu ilivyo huko watokako, kisha akawaambia mabwana Hani na Said bin Abdallah al-Hanafi, "Hebu niambieni ni kina nani hasa waliojumuika kuniandikia barua hii?

Mabwana hawa wakamfahamisha Imam Husein hali halisi ya watu wa Al-Kufah ilivyo na wakamtajia pia watu wenye msimamo na rai ya kumwita yeye Imam(a.s) .

Basi baada ya kutoshelezwa na maelezo ya mabwana hawa, Imam(a.s) alisimama akaswali rakaa mbili halafu akaandika barua ifuatayo.

BISMILLAAH RAHMAN RAHIM

Barua toka kwa Husein Bin Ali, kwenda kwa Watukufu Waumini na Waislamu.

Ama baad, hakika Hani na Said wamenifikia wakiwa na barua zenu, nao ni watu waliofika mwisho miongoni mwa wajumbe wenu niliowatuma.

Kwa kweli niineyafahamu yote mliyoyaeleza, na jambo muhimu mlilozungumza ni kwamba, "Hakika sisi hatuna kiongozi, basi njoo huenda Mwenyezi Mungu akatuimarisha kwenye haki na uongofu kupitia kwako".

Mimi ninanituma ndugu yangu na ibn ammi yangu naye ni miongoni mwa watu wa nyumba yangu (Muslim bin Aqiil) aje huko. Basi iwapo ataniandikia kuniarifu kuwa rai za viongozi wenu na watu bora miongoni mwenu zimeafikiana kama ambavyo wajumbe wenu walivyonijulisha, na nilivyosoma barua zenu, basi mimi nitakuja huko haraka apendapo Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Kwa Yaqin naapa, "Hawi mtu ni Imam (kiongozi wa haki) ila yule anayehukumu kwa mujibu wa Qur'an, mwenye kusimamia haki, anayeishi kwa mujibu wa mafundisho ya dini ya haki (Uislamu) mwenye kuifunga nafsi yake katika dhati ya Mwenyezi Mungu.

Wasalaam.

Baada ya kuandika barua hiyo, Imam Husein(a.s) alimwita nduguye Bwana Muslim bin Aqiil na akamtuma aende Al-Kufah, afuatane na mabwana Qais bin Mas-har As-Saidawi, Ammaarah bin Abdallah na Abdallah na Abdur-Rahman watoto wa Shadad Al-Arhabi.

Imam(a.s) akamuusia nduguye kumcha Mwenyezi Mungu na awe mpole pia asizungumze sababu za yeye kwenda huko.

Mwisho alimtaka afanye haraka kwenda, kwani yaonesha watu wameshikamana pamoja juu ya kumtaka Imam Husein(a.s) kwenda huko.

Muslim bin Aqiil aliondoka kuelekea AI-Kufah kupitia Madina, mahala ambapo alipofika, aliingia katika Msikiti wa Mtume(s.a.w.w) akaswali kisha aliwaaga watu wa nyombani kwake na wangine aliopenda kuwaaga. Baada ya hapo aliondoka mpaka Al-Kufah na akafikia katika nyumba ya bwana Mukhtar bin Ubaid At-Thaqafi. Mashia wa Al-Kufah walipopata habari za kuwasili kwa Muslim bin Aqiil, wakawa wanapishana katika nyumba ya Mukhtar ili waonane naye, na kila wakikusanyika kikundi huwasomea barua ya Imam Husein, kitu ambacho kilikuwa kikiwafanya walie.

Wakampa baia Muslim bin Aqiil watu wapatao elfu kumi na nane.

Muslim bin Aqiil alipoiona hali hiyo kutoka kwa watu wa Al-Kufah, alimuandikia Imam Husein(a.s) kumjulisha na kumtaka aende huko.

Mashia waliendelea kumtembelea Muslim bin Aqiil, mpaka Nuuman bin Bashir aliyekuwa Gavana wa Al-Kufah wakati wa Muawiyya na baadaye katika kipindi cha Yazid, akautambua mkusanyiko huo. Pamoja na kutambua hali hiyo, Nuuman bin Bashiri hakumfanyia lolote Ia ubaya Muslim bin Aqiil.

Lakini baada ya muda kupita, Abdallah bin Muslim bin Rabia Al-Hadhrami ambaye alikuwa mfuasi mkubwa wa bani Ummaya, akamuendea Nuuman bin Bashir akamwambia, "Hakika yote uyaonayo yanatendeka hapa hayana mafanikio kwako ila utapoteza madaraka, na msimamo unaouonyesha baina yako na adui yako ni msimamo wa watu wanyonge".

Kisha huyu Abdallah alimuandikia barua Yazid na akamuambia "Hakika Muslim bin Aqiil amefika hapa Al-Kufah, na watu wamempa baia kwa niyaba ya Husein, basi iwapo wewe unaitaka nchi hii ibaki mikononi mwako, mlete mtu imara atakayesimamia maslahi yako, na atafanya vile ambavyo wewe unamfanyia adni yako, kwani Nuuman ni mtu dhaifu au pengine anajifanya dhaifu."

Nao kina Ammarah bin Uqba na Omar bin Saad, kila mmoja alimuandikia Yazid barua mfano wa ile aliyoandika Abdallah.

Barua hizi zilipomfikia Yazid, mara moja akamuandikia Ubaidullah bin Ziyad aliyekuwa Gavana wa Basra akamjulisha kwamba, kuanzia sasa yeye ni Gavana wa al-Kufah na amemkabidhi nchi hiyo.

Kisha Yazid alimjulisha lbn Ziyad Khabari za Muslim bin Aqiil na akamsisitiza kumkamata na hatimaye amuuwe.

Ubaidullahi bin Ziyad aliyelaaniwa, aliondoka haraka kutoka Basra kuelekea Al-Kufah na akamkabidhi madaraka ya hapo Basra nduguye aliyekuwa akiitwa Athuman.

Ubaidullahi aliingia Al-Kufah usiku, na watu wakadhani kuwa ni Imam(a.s) , wakafurahia na kumsogelea. Walipotambua kwamba kumbe ni lbn Ziyad walitawanyika na kumuacha, naye akaenda hadi kwenye jumba la utawala wa bani Umayya akalala mpaka asubuhi.

Kulipokucha alitoka akaanza kutishia na kuonya kwa ukali wale wanaomuunga mkono Muslim bin Aqiil. Muslim bin Aqiil aliposikia habari za vitisho vya Ibn Ziyad akachelea usalama wake na akaenda nyumbani kwa Bwana Hani bin Urwa mahali ambapo alipewa hifadhi.

Baada ya vitisho na maonyo ya ibn Ziyad hali iligeuka ikawa mbaya sana, kiasi cha kuwafanya watu waliokuwa wamempa baia Muslim bin Aqiil wahitilafiane na wakavunja baia yao, wala hawakuthubutu tena kujitokeza kumtetea Muslim bin Aqiil na ahadi yao ya kumsaidia wakashindwa kuitimiza.

Kwa hakika kilikuwa kipindi kigumu kwa Muslim bin Aqiil, kipindi chenye mateso na tishio la kuuawa. Ni wakati mgumu kwa kuwa waliokuwa wamemuahidi kumsaidia na kumhifadhi walimtelekeza. Kutelekezwa alikotelekezwa Muslim bin Aqiil kulitoa nafasi kwa adui yake kuzidisha uovu wake dhidi yake na ikafikia Muslim bin Aqiil kuwa anasakwa kila mahali na kuzinngirwa barabara katika kila upande hali ya kuwa mpweke hana wakumsaidia.

Muslim bin Aqiil alipata mtihani unaowafika watu wema na alivumilia kungoja matokeo kutokana na vitisho vya panga za maadui zake.

MAJLISI YA SABA

YALIYOTOKEA AL-KUFAH BAADA YA IBN ZIYAD KUFIKA HAPO

Ibn Ziyad alipokwisha wasili katika mji wa AI-Kufah, alijiimarisha kwa kutawanya majasusi kufuatilia nyendo za Muslim bin Aqiil. Matokeo ya ujasusi huo yalimfanya yeye lbn Ziyad afahamu kuwa Muslim bin Aqiil yuko katika nyumba ya Bwana Hani.

Kwa hiyo lbn Ziyad aliwaita mabwana Muhammad bin Al Ashath na Hasan bin Asma bin Kharijah na Amru bin Al-Hajaaj akawaambia, "Ni kitu gani kinamfanya Hani asije kwetu (kutusalimia)?"

Wao wakamjibu, "Hatujui lakini inasemekana ni mgonjwa". lbn Ziyad akasema "Habari hizo nazifahamu, lakini pia nafahamu kwamba kesha pona na kwamba yeye mara kwa mara anaonekana mlangoni kwake amekaa, na lau ningefahamu kuwa bado anaumwa bila shaka ningelimtembelea kumjua hali".

Ibn Ziyad aliendelea kuwaambia, "Nendeni mkamwambie asiache kufanya wajibu wake juu ya haki yetu, (kutoa baia) hakika mimi sipendi kuuona ufisadi mbele yangu unaotokana na mtu mtukufu miongoni mwa Waarabu mfano wake yeye Hani".

Ilipokuwa jioni, mabwana hawa wakaenda nyumbani kwa Bwana Hani na wakasimama mbele ya mlango wa nyumba yake wakamwambia, "Ni kitu gani kinachokuzuia usikutane na Amiri (lbn Ziyad) kwani yeye amekutaja na amesema lau ningefahamu kwamba (Hani) anaumwa ningelimtembelea kumjua hali".

Hani akasema, "Ni maradhi ndiyo yanayonizuia nisiende kukutana naye".

Wale mabwana wakasema kumwambia Hani, "Hakika zimeshamfikia habari kwamba wewe kila jioni unakaa mlangoni nyunbani kwako, naye anakuvumilia kwa hilo, na fahamu kuwa mtawala hawezi kuendelea kuwavumilia watu mfano wako, kwani wewe ni kiongozi wa watu wako, nasi tunakuapia ukweli ulivyo twende pamoja mpaka kwa Ibn Ziyad".

Waliendelea kujadiliana naye mpaka wakamshinda, kisha aliagiza mavazi yake akavaa na hatimaye akaomba aletewe nyumbu wake akapanda na wakaondoka. Walipolisogelea jumba Ia Ibn Ziyad Hani alihisi kutatokea mambo ambayo si mazuri kwake kama ambavyo tangu mwanzo alikuwa akihisi hivyo. Hani akamwambia Hasan bin Asma bin Kharijah, "Ewe mtoto wa ndugu yangu, kwa kweli mimi ninayohofu kubwa juu ya mtu huyu wewe unaonaje"?

Ibn Kharijah akasema, "Ewe ami yangu mimi siogopi chochote juu yako, usianze kutoa nafasi ya mashaka kwa nafsi yako".

Kwa bahati mbaya Hasan alikuwa hakufahamu dhamira na lengo la Ibn Ziyad dhidi ya Bwana Hani. Basi Hani (Mwenyezi Mungu amrehemu) akaja pamoja na jamaa hao mpaka wote wakaingia kwa lbn Ziyad. lbn Ziyad alipomuona Hani akasema, "Muhaini kaletwa na miguu yake mwenyewe".

Hani akasema, "Unakusudia nini kusema hivyo ewe Amir".

Mjadala baina yao ulipokuwa mrefu, na Hani hakukubali madai dhidi yake, lbn Ziyad alimwita Ma-Aqal ambaye alipata kuwa mtumwa wake, akaja akasimama mbele yake.

Huyu Ma-Aqal alikuwa jasusi wa ibn Ziyad na alikuwa akipeleleza nyendo zote za kina Hani na Muslim bin Aqiil hali ya kuwa wao hawana habari kwamba yule ni jasusi, kutokana kuwa akidhihirisha upendo na nia njema kwa kizazi cha Mtume(s.a.w.w) , hivyo basi alifahamu mengi kuwahusu wao.

Hani alipomuona mtu huyo, ndipo alipotambua kwamba alikuwa nijasusi la ibn Ziyad na kuwa mambo yao yote amekwisha yafikisha hapo, na amefaulu kumtumbukiza mikononi mwa ibn Ziyad.

Hali ilivyokuwa hivyo, Hani akasema kumwambia lbn Ziyad, "Mwenyezi Mungu amfanye mwema Amir, naapa kwa jina la Mwenyezi Mwigu kwamba, Muslim bin Aqiil sikumwita mimi lakini alinifikia bali ya kuwa anaomba ulinzi wangu nikamkubalia kumlinda, na niliona haya kumkatalia, na niliingiwa na utu ambao ulimlazimisha kumkaribisha, na sasa hebu nipe nafasi ili nirudi nikamuamuru atoke nyumbani mwangu aende apendako ili nijitoe kuwa mimi ni mdhamini wake, na kisha nitarudi nije nikupe kiapo changu cha utii."

lbn Ziyad akasema, "Wallahi hutoki hapa isipokuwa uniletee huyo Muslim Bin Aqiil". Hani akasema, "Wallahi sitakuletea wataka nikuletee mgeni wangu kisha umuuwe"?

lbn Ziyad akasema, "Wallahi naapa kuwa lazima utaniletea mtu huyo."

Hani naye akajibu, "Wallahi sikuletei hata kidogo".

Majibizano baina ya wawili hawa yalipozidi, bwana mmoja aitwaye Muslim bin Amri Al-Baahili akasema, "Mwenyezi Munga na amfanye mwema Amir, (Amir) hebu niachie nafasi mimi na yeye nizungumze naye. Akasimama yeye na Hani sehemu fulani humo ndani, kiasi kwamba Ibn Ziyad anawaona na anasikia wanachokisema.

Wakati mazungumzo yao yanaendelea, mara sauti zao zikapanda juu zaidi, kisha Bwana Al-Baahili akasema, "Nakuapia Mwenyezi Mungu ewe Hani usijiuwe mwenyewe, na wala usilete balaa kwa jamaa zako, Wallahi hakika mimi nakuona ni mtu muhimu sipendi kuona unanawa, mtoe huyu (Muslim bin Aqiil) uwape watawala, kwani jambo hilo la kumtoa siyo unyonge wala aibu bali unamtoa kwa mtawala (ataamua Ia kumfanya)".

Hani akajibu, "Wallahi kumtoa Muslim bin Aqiil kwangu mimi ni dalili za unyonge na aibu, nimtoe mgeni wangu na isitoshe ni Mjumbe wa mjukuu wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu hali nikiwa ni mzima mwenye nguvu na ninao wasaidizi wengi, Wallahi naapa japo hata ningekuwa peke yangu sina wakunisaidia nisingemtoa (Muslim bin Aqiil) mpaka nife kwa ajili yake".

Al-Baahili akawa anamsisitiza Hani amkabidhi Muslim kwa lbn Ziyad, lakini Hani hujibu, "Wallahi simtoi kamwe".

lbn Ziyad akawa ameyasikia hayo akasema, "Msogezeni hapa karibu yangu", Hani akasogezwa kisha lbn Ziyad akasema kumwambia Hani, "Wallahi lazima uniletee huyo Muslim vinginevyo nitaikata shingo yako".

Hani akasema, "Kama utaniua fahamu wazi utakuwa umewasha moto wa fitna nyumbani kwako".

Akasema: Ooo! Ole wako nakuonea huruma, unanitishia hiyo fitna"?

Kipindi hicho Hani alikuwa akidhani kwamba nduguze na jamaa zake watamsaidia.

Baada ya lbn Ziyad kutamka maneno yale akasema, "Msogezeni kwangu" akasogezwa, kisha lbn Ziyad akatoa fimbo ambayo alianza kumpiga Hani puani na usoni mpaka pua ya Hani ikakatika na nyama za usoni mwake zikachanakanchanika, damu zikawa zinamvuja na kutiririka kwenye nguo zake, na wala hakuacha kumpiga mpaka ile fimbo ikavunjika.

Naye Hani baada ya kutendewa haya, alinyoosha mkono akikusudia kuuchukua upanga wa askari moja aliyekuwa kasimama hapo, yule Askari akauvuta upanga wake kuusalimisha.

Alipoona hivyo lbn Ziyad alipiga kelele akasema "Mshikeni mara moja". Basi Hani akakamatwa na kukokotwa hadi katika moja ya nyumba akafungiwa humo na kuwekewa mlinzi.

Hasan bin Asma bin Kharijah akasimama na kumwambia lbn Ziyad, "Hatujapata kuwa wajumbe wenye khiyana isipokuwa leo ewe Amir, umetuagiza kwa mtu huyu na ukatuamru tumlete kwako, na tulipokuwa tumekuletea umeuchanachana uso wake na umeimwaga damu yake na bado unadai kwamba utamuua".

Maneno haya yakamchukiza Ibn Ziyad, akakasirika sana akasema kumwambia Hasan, "Nawewe uko hapa (kumtetea Hani)"?

Kisha akatoa amri Hasan apigwe, akapigwa na baadaye akafungwa kamba na akatupwa Gerezani. Hapo Hasan akawa anaomboleza kwa kusema "Hakika sisi ni milki ya Mwenyezi Mungu na kwake tutarudi, ewe Hani kwa nafsi yangu ninakusikitikia".

Khabari za tukio hili zikamfikia Bwana Amri bin Al-Hajaaj, na kwamba Hani amekwisha kuuawa.

Bwana Hani alikuwa ni mkwe wa huyu Al-Hajaaj kwa binti yake aliyekuwa akiitwa "Ruwaihah". Hivyo basi Amri bin al-Hajaaj akafika hapo Al-Kufah akiwa na jamaa zake, wakalizunguka jumba Ia Ibn Ziyad, kisha Amri alizungumza kwa sauti kubwa akasema, "Mimi ni Amri bin Al-Hajaaj na hawa nilionao ndiyo viongozi wa jamii ya Madh-haj, nao hawajatoka katika utii wala kupinga umoja, lakini habari zimetufikia kwamba mwenzetu (Hani) kauawa".

Basi Qadhi Shuraih akaja kutoka ndani alimokuwa yeye na Ibn Ziyad na anayaona yote yaliyomfika Hani akamwambia ya kwamba Hani yu katika amani. Basi wakaridhika na kuondoka kurejea kwao.

MAJLISI YA NANE

MAAFA YALIYOMPATA MUSLIM BIN AQIL

Muslim Bin Aqiil zilipomfikia habari za matendo aliyoyatenda Ibn Ziyad kumtendea Hani, alitoka yeye pamoja na watu waliokuwa wakimtii kwenda kumsaidia Hani na kumuokoa, pia kupigana na Ibn Ziyad.

Ibn Ziyad alipogundua jambo hilo alijificha katika jumba hilo la utawala wa Bani Umayya, ikawa wafuasi wake ndiyo wanapigana na watu wa Muslim bin Aqiil.

Wafuasi wa Ibn Ziyad waliokuwa pamoja naye wakawa wanachungulia na kuwatahadharisha wafuasi wa Muslim bin Aqil na wakawaonya kuwa litakuja Jeshi kutoka Sham kwa Yazid nalo litawashambulia.

Waliendelea kufanya hivyo mpaka usiku ukaingia, hapo ndipo wafuasi wa Muslim bin Aqiil walipoanza kutawanyika kumkimbia Muslim, na wakawa wanaambiaana, "Ni kitendo gani tukifanyacho kwa kuikimbilia fitna, inatupasa kujificha majumbani wetu tuwaache hawa jamaa mpaka hapo Mwenyezi Mungu atakapoleta upatanishi baina yao."

Waliendelea kutawanyika mpaka ilipofika jioni, Muslim bin Aqill aliswali Maghrib akiwa na watu thelathini tu ndani ya msikiti. Alipoiona hali hiyo alitoka kuelekea milango ya upande wa Kindah, na hakufika hapo ila alikuwa kabaki peke yake watu wote walikwisha kumtoroka.

Kisha Muslim alitoka kupitia mlangoni, lakini ghafla akajikuta hana mtu wa kumuongoza njia, kumbe alikuwa kabaki peke yake watu wote walikwisha kumtoroka.

Muslim bin Aqiil akaendelea mbele hali ya kuwa akipita katika vichochoro vya mji wa Al-Kufah, hajuwi la kufanya wala hafahamu aendako. Alitembea mpaka akafika kwenye mlango wa nyumba ya mama mmoja aliyekuwa akiitwa "Taua" ambaye alipata kuwa mjakazi wa Ash-Ath bin Qais, alipomuacha huru akaolewa na Usaid Al-Hadhrami akamzalia mtoto aliyeitwa "Bilal".

Huyu Bilal wakati Muslim bin Aqiil anafika kwenye nyumba ya mama yake, alikuwa katoka pamoja na watu fulani, hivyo basi mama yake alikuwa akimngojea pale mlangoni.

Muslim bin Aqiil akamtolea salamu mama yule "akaitikia", kisha akamuomba maji ya kunywa "Akapewa". Yule mama aliporejesha ndani kile chombo cha maji, alitoka na kumkuta Muslim akiwa ameketi chini akamuuliza, "Je, hujanywa maji?" akajibu, "Nimekunywa".

Mama yule akaendelea kumsemesha Muslim, lakini akawa hakujibu, mwisho yule mama akasema "Sub-hana Llah!!'. Ewa mja wa Mwenyezi Mungu simama uende kwenu, haifai wewe kuendelea kukaa mlangoni kwangu wala siwezi kukuruhusu ukae hapa".

Muslim bin Aqiil akasimama na akasema, "Ewe mtumwa wa Mwenyezi Mungu, katika mji huu sina makazi wala ndugu, je wapenda kupata ujira mwema na malipo mazuri, ili nami hapo baadaye nikulipe kwa wema wako baada ya siku hii ya leo?"

Yule mama akasema "Nini makusudio yako Ewe mtumwa wa Mwenyezi Mungu?"

Akajibu "Mimi ni Muslim bin Aqiil, watu wa Mji huu wamenidanganya na wamenihadaa, na sasa wamenifukuza."

Yule mama akasema, "Wewe ndiwe Muslim"?

Akasema "Ndiyo".

Yule mama akasema "Ingia ndani".

Muslim akaingia ndani ya nyumba miongoni mwa nyumba za mama yule isiyokuwa ile anayoishi mwenyewe, na yule mama akamtayarishia Muslim mahali pa kulala, na akamletea chakula ambacho Muslim hakukila.

Mtoto wa yule mama aliporudi na akawa amemtambua Muslim basi haraka alipeleka habari kwa Ibn Ziyad kumjulisha mahali alipo Muslim bin Aqiil.

Ibn Ziyad akamleta Muhammad bin AI-Ash-ath na akamtuma pamoja naye Ubaidullah bin Abbas As-Sulami wakiwa na watu sabini wa Kabila Ia Qais mpaka kwenye nyumba aliyoko Muslim.

Basi Muslim aliposikia sauti ya kwato za farasi na sauti za watu, akafahamu kwamba amefuatwa yeye. Akawatokea akiwa na upanga wake, nao wakamvamia ndani ya nyumba kabla hajatoka, akawashambulia kwa upanga mpaka akawatoa nje. Kisha walimrudia tena naye akawashambulia vikali, na ikatokea mashambulizi yakawa baina ya Muslim na Bakru bin Hamran Al-Ahmari, basi huyo Bakru "Mwenyezi Mungu amlaani" alimpiga Muslim dhoruba Ia Upanga akamkata mdomo wa juu, na akafanya haraka kumkata mdomo wa chini pia, meno ya chini ya Muslim yakabomoka.

Naye Muslim pamoja na hali hiyo alimpiga Bakru dhoruba kali ya kichwani, akamfuatisha nyingine katika sehemu iliyo kati ya shingo na bega, dhoruba ambayo ilikaribia kuingia ndani kabisa ya mwili wa Bakru.

Muslim pamoja na maumivu aliyokwisha yapata, aliendelea kuwashambulia watu wa ibn Ziyad mpaka akafaulu kuwauwa kikundi miongoni mwao.

Walipoona hali ya ushujaa wa Muslim, walianza kumshambulia wakiwa juu ya nyumba kwa kumtupia mawe, na wakawasha vijinga vya moto kisha wakawa wanamrushia kutoka katika paa la nyumba.

Muslim hakukata tamaa bali aliwatokea hali ya kuwa ameutoa upanga wake tayari kwa kupambana nao.

Muhammad bin AI-Ash-ath akawa anamwambia Muslim "Jisalimishe usiiue nafsi yako".

Muslim alimjibu Muhammad AI-Ash-ath hali ya kuwa akiwashambulia akasema: "Nimeapa, siuawi ila niwe katika hali ya uhuru, japokuwa mauti nayaona kuwa ni jambo gumu, nachukia kuhadaiwa au kudanganywa, nitakupigeni wala siogopi madhara".

Ibn Al-Ash-ath akapiga ukelele aksema, "Hakika wewe hudanganywi wala kuhadaiwa".

Lakini kufikia kipindi hiki Muslim akawa ameshehenezwa kwa mawe na akashindwa kuendelea na mapambano, basi akauegemeza mgongo wake ukutani.

lbn Al-Ash-ath akamwambia tena Muslim, "Jisalimishe".

Muslim akajibu, "Mimi nimekwisha salimika".

Akasema ibn Ash-ath, "Vema".

Kisha Muslim akawaambia jamaa waliokuwa wakimshambulia, "Je ninayo amani?"

Wakasema, "Ndiyo".

Akasema "Japo msinipe amani lakini siwezi kuweka mkono wangu mikononi mwenu" (Siwezi kuwatii).

Hapo wakamletea nyumbu, wakampandisha kisha wakamzunguka na wakamnyang'anya panga lake, ikawa kama kwamba Muslim katika kipindi hicho anaihuzunikia nafsi yake, basi ghafla akaaza kujawa machozi machoni mwake akasema: "Huu ndiyo mwanzo wa kuvunja ahadi, uko wapi basi uaminifu wenu?" Hapa Muslim akawa analia.

Ubaidullah As-Sulami akasema kumwambia Muslim bin Aqiil, "Hakika yeyote mwenye kutafuta mambo kama haya uyatafutayo, pindi anapofikwa na hali kama hii ihyokufika wewe hana haja ya kulia".

Muslim akajibu, "Hakika mimi Wallahi silii kwa ajili ya nafsi yangu, wala nafsi yangu siihuzunikii kutokana na kifo, japokuwa siipendelei nafsi yangu kuangamia, lakini (fahamu kwamba) nawalilia jamaa zangu wanaokuja kunifuata mimi, namlilia Husein na watu wa Husein (a.s.)."

Kisha Muslim akamuelekea Ibn Al-Ash-ath akasema: "Hakika wewe utashindwa kunipa amani, basi je kwako kuna wema wowote (unitendee)? Unaweza ukatuma mtu kutoka kwako kwa niyaba yangu akamfahamishe Husein(a.s) , kwani mimi simuoni Husein ila atakuwa leo ametoka au atatoka leo pamoja na watu wa nyumba yake basi akamwambie kwamba "Hakika mwana wa Aqiil amenituma kwako, hali ya kuwa yeye ni mateka mikononi mwa watu (wa Al-Kufah) haoni nafasi yoyote ila jioni atakuwa kisha uawa, naye anasema rudi, wewe na watu wa nyumba yako, baba yangu na mama yangu (nawatoa) iwe fidia kwako na wala wasikudanganye watu wa Al-Kufah, hakika wao ndiyo wale wale watu (waliojidai kushirikiana na) baba yako, ni wao ambao alikuwa akitamani (Baba yako) kutengana nao ima kwa mauti (ya kawaida) au kuuawa, hakika hawa watu wa Al-Kufah wamekudanganya na mwenye kudanganywa huwa hana rai".

lbn Ash-ath akamchukua Muslim mpaka kwenye mlango wa jumba la utawala, akaingia ndani na kumpa khabari zote Ibn Ziyad.

Muslim kiu kali ikawa imemsonga, na hapo kwenye mlango wa jumba hilo kuna watu wengi wanasubiri kupewa ruhusa (kuingia). Mara ghafla likaletwa jagi la maji ya baridi, Muslim akasema "Ninywesheni maji haya".

Muslim bin Amri Al-Baahili akasema, "Wayaonaje, ubaridi ulioje wa maji haya!, Wallahi hutaonja japo tone moja kabisa, mpaka kwaza uonje joto kali liliilomo katika moto wa Jahannam."

Muslim bin Aqiil akamjibu Muslim bin Amri akasema;

"Mama yako kapata hasara (kuzaa mtoto kama wewe) unauovu kiasi gani na moyo mbaya kadiri gani (bali muovu mno) ewe mwana wa Baahilah, wewe ndiyo unastahiki mno kulipata joto hilo kali na pia kuishi milele ndani ya moto wa Jahannam".

Kisha Muslim bin Aqiil akaegemea ukutani.

Bwana Amri bin Huraith akaja na kile chombo kilichokuwa na maji, juu yake kuna kitambaa, pia alikuwa na jagi ambalo alilitia maji yale na akamwambia Muslim bin Aqiil "Kunywa maji", ikawa kila anapotaka kuyanywa maji, basi lile jagi hujaa damu yake inayobubujika kutoka mdomoni mwake.

Akajaribu mara mbili kuyanywa maji hayo bila mafanikio, na alipokusudia kwa mara ya tatu kunywa, meno yake mawili ya mbele yakabomoka na kutumbukia ndani ya jagi la maji.

Muslim bin Aqiil akasema, "Al-hamdulillah (Sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu) lau ningekuwa nayo riziki iliyogawiwa kwangu (kwenye maji haya) ningeyanywa".

Baadaye akaingizwa ndani kwa ibn Ziyad, Muslim hakumtolea salam lbn Ziyad.

Mlinzi wa Ibn Ziyad akamwambia Muslim, "Mtolee salaam Amir (kiongozi)".

Muslim akasema, "Ole wako nyamaza, Wallahi kwangu mimi (huyu) siyo Amiri."

Ibn Ziyad akasema kumwambia Muslim, "Ewe mwana wa Aqiil uliwakuta watu (hapa AI-Kufah) wakiwa pamoja, ukawatenganisha na kuwatawanya (wasikubaliane), pia ukawafanya wagombane wao kwa wao".

Muslim akasema, "Sivyo kabisa, mimi sikuja hapa kwa ajili hiyo, lakini watu wa Mji huu walidai kwamba Baba yako (Muawiyya) amewauwa watu wema (miongoni mwa wenyeji wa hapa) na amemwaga damu zao, na akawatendea matendo ya (Wafalme Kisra ha Kaisar, basi sisi tukawafikia (hapa) ili tuamrishe uadilifu na tuwaite (wote) kwenye hukumu ya kitabu (Qur'an)".

Ibn Ziyad akasema, "Tangu lini nawe (Muslim) ukafaa kuwa (kiongozi) wa hayo uliyoyasema? Kisha lbn Ziyad mwenye kulaaniwa akaendelea kusema kumwambia Muslim "Ewe muovu hakika nafsi yako inakutamanisha jambo ambalo Mwenyezi Mungu kisha kumpa mwingine, na haikukuonyesha mwenye kustahiki".

Muslim akasema, "Basi nani atastahiki jambo hilo (Ia uongozi wa Umma) endapo sisi (tutaonekana) hatufai?"

Ibn Ziyad akajibu akasema, "Mwenye kustahiki jambo Ia (uongozi) ni Amirul Muuminina Yazid".

Muslim aksema, "Kwa kila hali Mwenyezi Mungu ashukuriwe, sisi tumeridhia na tunaridhia kwamba Mwenyezi Mungu ndiye atakayetoa uamuzi baina yetu na ninyi".

Ibn Ziyad akasema, "Mwenyezi Mungu anilaani iwapo sitakuuwa, tena kwa uwaji baya ambalo hajapata mtu kuuliwa katika Uislam".

Muslim akasema, "Ama ilivyo kweli na hakika wewe ni mtu uliyezusha katika Uislamu mambo ambayo hapo kabla hayakuwapo, na kwa tabia yako hutaacha kufanya mauaji ya kinyama, na hutoacha kuwa ni mfano mbaya, mwenye niya mbaya, na kijicho kwa yule mwenye kustahiki mno kwa jambo hili kuliko wewe"

lbn Ziyad akamuelekea Muslim kwa ulimi wa matusi kumtukana yeye na kamtukana Husein na Ali(a.s) pia Aqiil (baba yake Muslim) akamtukana.

Muslim akanyamaza asimsemeshe kitu Ibn Ziyad, bali aliwaangalia watu waliokuwa pamoja na lbn Ziyad, akamuona Omar bin Saad akiwa ni miongoni mwao, akasema kumwambia Omar bin Saad "Ewe Omar bila shaka baina yangu mimi na wewe kuna udugu, basi mimi ninayo haja fulani kwako, na itakupasa wewe ufanikishe haja yangu hiyo, lakini ni siri baina yangu na wewe".

Omar bin Saad (mwenye kulaaniwa) akakataa kumsikiliza Muslim, lakini Ubaidullahi bin Ziyad akamuamuru Omar asikilize ombi Ia Muslim.

Basi wakajitenga wawili hao upande fulani hali ya kuwa Ibn Ziyad anawaona, Muslim akasema, "Hakika kuna baadhi ya watu wa Al-Kufah wananidai Dir-ham miasaba, basi kauze upanga wangu na deraya yangu kisha ulipe deni hilo, na nitakapokuwa nimeuawa uchukue mwili wangu na uusitiri (uuzike) na pia mtume mtu aende kwa Husein amwambie arudi (asije hapa Al-Kufah) bila shaka mimi nilimuandikia kwamba watu wanamuunga mkono (kumbe wamegeuka) nami namuona kuwa anakuja".

Ibn Saad akasema kumwambia ibn Ziyad, "Je wafahamu anasema nini (Muslim) ewe Amiri? hakika anasema kadha kadha". (Akasema yote aliyomwambia Muslim) "Ibn Ziyad akasema kumwambia Muslim bila shaka mtu mwaminifu hawezi kukufanyia khiyana lakini wewe umemuamini mtu mwenye khiyana".

Kisha huyu Ibnu Ziyad "Mwenyezi Mungu amlaani" akaamuru Muslim apandishwejuu ya paa la jumba hilo na akatwe shingo yake huko juu, na itakapoanguka wakitupe kiwiliwili chini kuifuata shingo itakayokuwa imeporomoka chini pamoja na kichwa. lbn Ziyad akamwita Bakru bin Hamran akamwambia "Panda juu ukamkate shingo yake". Akapanda.

Wakati Muslim akipandishwa juu ili akauawe, alikuwa akisoma Takbira na kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu na akimsalia Bwana Mtume(s.a.w.w) na pia akawa husema, "Ewe Mwenyezi Mungu hukumu baina yetu na wale waliotudanganya na wametutweza, basi ghafla akainamishwa chini kisha shingo yake ikakatwa ikadondoka chini na mwili wake pia ukafuatishwa mpaka chini (Muslim bin Aqiil akawa ameuawa kishahidi, ewe Mola iteremshie amani na Rehema roho yake nasi tujaalie vifo vya kishahidi katika kukutumikia - Amin).

Baada ya kuuawa Muslim bin Aqiil, pale pale Ibn Ziyad akaamuru Hani atolewe (alikuwa bado kafungwa) akasema "Mtoeni mumpeleke sokoni kisha muikate shingo yake". Hani akatolewa ilhali mikono yake imefungwa na akawa anasema "Ee!!! jamaa zangu, leo sina jamaa yeyote, wako wapi jamaa zangu"?

Alipoona kwamba hakuna ye yote wa kumsaidia aliutoa kwa nguvu mkono wake katika kifungo alichofungiwa, kisha akasema, "Je hakuna fimbo au kisu au jiwe ambalo mtu anaweza kujilinda nafsi yake"?

Askari wa Ibn Ziyad wakamrukia na wakamfunga barabara na hapo hapo wakamwambia "Nyoosha shingo yako".

Hani akasema, "Sijawa mkarimu kiasi hicho kuwanyooshea shingo yangu, na pia siwezi kuwasaidieni katika kuiua nafsi yangu."

Mturuki ambaye alipata kuwa mtumwa wa lbn Ziyad akaachia dhoruba ya upanga kumkata Hani, lakini dhoruba hiyo haikumfanya kitu Hani.

Hapo Hani aksema, "Kwa Mwenyezi Mungu ndiko kwenye marejeo, Ewe Mola narudi kwenye huruma zako na radhi zako".

Yule mturuki akarudia mara ya pili kumkata Hani akafaulu kumuuwa, hivyo Hani akafa akiwa shahidi kwa kutaraji rehema za Mola wake.


2

MAOBOLEZO YA KIFO CHA IMAM HUSEIN(A.S)

MAJLISI YA TISA

IMAM HUSEIN(A.S) AAZIMIA SAFARI YA IRAQ

Imam Husein (a.s.) alipoazimia kwenda Iraq alisimama akatoa hatuba akasema; "Hamu yangu ya kukutana na wazazi na ndugu zangu waliotangulia (kufariki) ni kama shauku aliyokuwa nayo Yaaqub kwa mwanawe Yusuf (alipopotea) na kifo kitakchonifika kwangu ni jambo bora, kwani naona viungo vya mwili wangu vitakatwakatwa na maadui zangu hapo katika jangwa lililo baina ya Nawasiisi na Karbala.

Wakisha kinuia, lengo lao litakuwa limetimia na hamu yao dhidi yangu itakamilika. Hakuna njia ya kuwepa siku ambayo imekwisha kuandikwa. Alitakalo Mwenyezi Mungu liwe, kwetu sisi watu wa nyumba ya Mtume huwa tumeridhia pia liwe. Jamii ya Mtume wa Mwenyezi Mungu haitatenganishwa naye, bali itakusanywa iwe pamoja naye kesho Akhera mahali patukufu.

Mtume atawakaribisha jamii yake kwa wema na furaha na atawatimizia yote aliyowaahidi. Fahamuni enyi watu ya kwamba, ye yote atakayejitolea roho yake kwa ajili yetu, na akawa amejiandaa kukutana na Mwenyezi Mungu kwa wema, basi na asafiri pamoja nasi, kwani nitaondoka asubuhi pindi apendapo Mwenyezi Mungu Mtukufu."

Usiku wa kuamkia safari, alikuja Muhammad Al-Hanafiyyah ambaye ni mdogo wa Imam Husein (kwa mama mwingine) akamwambia Imam Husein(a.s) "Ewe ndugu yangu bila shaka watu wa Al-Kufah ndiyo wao ambao wewe unafahamu khiyana waliyomfanyia baba yako na nduguyo (Hasan a.s.), nami nachelea kwamba yatakufika yaliyowafika waliokutangulia, basi iwapo utaona ni vema bora ubakie hapa Makkah, kwani wewe ni kiumbe bora mno katika Haram hii ya Makkah nawe ndiyo mlinzi wake".

Imam(a.s) akajibu kwa kusema "Ewe ndugu yangu hakika nachelea Yazid asije ndani ya eneo hili takatifu, nami nikawa ndiyo kiumbe wa kwanza kuhusishwa na uvunjwaji wa heshima ya nyumba hii."

Muhammad AI-Hanafiyya akasema, "Basi ikiwa unachelea hilo, nenda Yemen au sehemu nyingine za nchi, kwani huko utapata hifadhi wala hakuna atakayeweza tena kukusbambulia ukiwa huko".

Imam Husein akasema, "Nitaitafakari rai yako". Kulipokucha alfajiri mapema, Imam Husein(a.s) alifungasha akaondoka.

Khabari zikamfikia Muhammad Al-Hanafiyya kwamba Imam Husein(a.s) ameondoka, akamfuatia, na alipompata akazishika hatamu za ngamia aliyekuwa kapanda Imam Husein(a.s) kisha akasema, "Ewe ndugu yangu hukuniahidi kwamba utalitafakari ombi langu?"

Imam akasema, "Bila shaka nilikuahidi".

Muhammad Al-Hanafiyyah akasema, "Basi jambo gani limekufanya utoke haraka namna hii?"

Imam akajibu, "Ulipoondoka Mtume wa Mwenyezi Mungu alinijia akaniambia, "Ewe Husein toka (wende Iraq) bila shaka Mwenyezi Mungu amekwisha taka kukuona wewe umeuawa".

Akasema Muhammad Al-Hanafiyya, "Hakika sisi ni milki ya Mwenyezi Mungu na bila shaka kwake tutarejea, lakini nini maana yako kuwachukuwa wanawake hawa pamoja nawe ikiwa hali yenyewe ndiyo hii uliyoniambia?"

Imam akajibu "Mtume ameniambia kwamba Mwenyezi Mungu amekwisha kutaka vile vile kuwaona wakiwa ni mateka".

Kadhalika kabla Imam(a.s) hajatoka kuelekea Iraq, alikutana na Mabwana Abu Muhammad Ar-Raaqdiy na Zurarah bin Khalaj, na walimjulisha udhaifu wa watu wa Al-Kufah, na kwamba nyoyo zao ziko pamoja naye na wakati huo huo panga zao ziko juu ya shingo yake.

Imam Husein (a.s.) alinyoosha mkono wake juu mbinguni, ikafunguliwa milango ya mbingu na wakateremka malaika wengi mno, idadi yao aijuaye ni Mwenyezi Mungu kisha akasema, "Lau isingekuwa vitu viko karibu karibu na kama muda wa kifo changu ungekuwa bado Wallahi ningepigana na maadui zangu kwa jeshi na Malaika hawa, lakini nafahamu wazi kabisa kwamba huko niendako ndiko kwenye kifo changu na vifo vya wafuasi wangu, hataokoka yeyote isipokuwa Mwanangu".(Ali bin Husein Zainul-Abidina(a.s) .

Imam Husein(a.s) akawa ameondoka Makkah siku ya Jumanne tarehe nane mfungo tatu mwaka wa sitini. A.H.

Amesema Bwana Maamar katika kitabu kiitwacho "Maqtalul- Husain) kwamba: Ilipokuwa siku ya nane mfungo tatu, Omar bin Saad bin Abi Waqas alifika Makkah akiwa na idadi kubwa ya askari ili kumshambulia Imam Husein hapo Makkah kutokana na amri ya Yazid, na ikiwezekana amuuwe kabisa.

Kumbe Imam naye akawa ametoka siku hiyo hiyo ya tarehe nane mfungo tatu, kwani hakuweza kukamilisha Hija yake kwa kuchelea kuuwa kwake hapo Makkah na itakuwa heshima ya nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu imevunjwa, akafungua Ihram yake na akaifanya kuwa ni Umra "Mufradah".

Imepokewa kutoka kwa Imam Jaafar As-Sadiq(a.s) katika mapokezi ya Sheikh Mufid amesema, "Alipoondoka Imam Husein(a.s) Makkah kwenda Iraq, alikutana na makundi ya malaika waliokuwa na mikuki wamepanda ngamia wakamtolea salamu na wakasema, "Ewe uliye muongozo wa Mwenyezi Mungu kwa viumbe wake baada ya Babu yako na Baba yako na nduguyo, bila shaka Mwenyezi Mungu alimsaidia Babu yako kwa kututumia sisi mahala pengi, na hapana shaka Mwenyezi Mungu amekupa msaada wewe kwa kupitia kwetu".

Imam(a.s) akawaambia, "Makutano yawe katika uwanja wa kaburi langu, mahali ambapo nitapata shahada (nitauwa) napo ni Kar-bala, basi nikishafika hapo njooni ".

Wale Malaika wakamjibu wakasema, "Ewe uliye muongozo utokao kwa Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu ametuamuru kukusikiliza na kukutii, je unayo khofu kutokana na adui kwamba atakutana nawe (njiani) ili tuwe nawe pamoja (tukusaidie)"?

Imam Husein(a.s) akasema, "Hawana uwezo kama huo juu yangu, na wala hawatanifanya lolote la ubaya mpaka nifike kwenye kiwanja changu".

Pia walimjia Imam(a.s) makundi ya majini waumini wakamwambia, "Ewe kiongozi wetu sisi ni wafuasi wako na ni wasaidizi wako, tuamuru chochote ukitakacho (tutakufanyia), na lau utatuamuru kumuuwa adui yako nawe ukiwa hapo ulipo tutakutelezea jambo hilo".

Imam Husein(a.s) akawajibu akasema, "Je hamujasoma kitabu cha Mwenyezi Mungu kilichoteremshwa kwa Babu yangu Mtume wa Allah pale aliposema Mwenyezi Mungu, "Waambie hata kama mngelikuwa majumbani mwenu, wangelitoka wale ambao wameandikiwa kufa wakaenda mahali pao pa kuangukia kifo". Kwa hiyo ikiwa mimi nitabaki hapa basi kwa kitu gani atatahiniwa mja huyu muovu, na ni kwa jambo lipi watu hawa (waovu) watajaribiwa, basi ni nani pia atakayengia katika kaburi langu, kaburi ambalo Mwenyezi Mungu alinichagulia siku aliyoumba ardhi na akapafanya kuwa ni mategemeo ya wafuasi wetu na wanaotupenda, mahala hapo hupokelewa matendo yao na sala zao, na hukubaliwa maombi yao, na wafuasi wetu watakujaishi hapo, basi watapata amani duniani na akhera, lakini pamoja na yote niliyosema njooni siku ya "ASHURA" ambayo nitauawa mwishoni mwa siku hiyo, hatabakia baada yangu mwenye kutafutwa katika watu wangu na ukoo wangu na ndugu zangu na watu wa nyumba yangu, na watatekwa wapelekwe pamoja na kichwa changu kwa Yazid bin Muawiyya.

MAJLISI YA KUMI

IMAM HUSEIN SAFARINI KWENDA IRAQ

Siku aliyotoka Imam Husein(a.s) kuelekea Al-Kufah ndiyo siku ambayo Muslim bin Aqiil alikuwa yumo katika mapambano na askari wa Ibn Ziyad, nayo ilikuwa ndiyo siku ya tarehe nane Dhil-Hija, na Muslim aliuawa siku ya nane tangu Imam Husein(a.s) atoke Makkah, na siku hiyo ilikuwa ni siku ya "ARAFAH".

Kwa hiyo, siku ya kuondoka kwake Imam hapo Makkah, walikusanyika watu mbali mbali kutoka Hijaz na Basra wakaungana na watu wa nyumba ya Imam(a.s) na wafuasi wake.

Wakati akitaka kwenda Iraq Imam Husein(a.s) alitufu na kufanya Saayi, kisha alifungua Ihram yake na akaifanya kuwa Umra Mufradah, ndipo alipoondoka na watu wake na wanawe pia watu ambao walioungana naye miongoni mwa wafuasi wake.

Imepokewa kutoka kwa Farzadaq amesema kwamba, "Nilikwenda Hija pamoja na Mama yangu mwaka wa sitini Hijriya, wakati nilipokuwa namuongoza ngamia wa mama kuingia Al-Haram nilikutana na Husein(a.s) anatoka Makkah akiwa na panga na ngao zake nikasema, msafara huu ni wa nani? Pakasemwa kuwa ni wa Husein bin Ali(a.s) , basi nikamuendea na nikamsalimia kisha nikasema, "Mwenyezi Munga akupe maombi na matarajio yako katika mambo uyapendayo ewe mjukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, ni jambo gani likufanyalo uache Hija kwa haraka namna hiyo?"

Imam Husein(a.s) akasema. "Lau sitafanya haraka nitakamatwa nikiwa hapa hapa, kwani wewe uniulizaye ni nani ?"

Nikasema "Mimi ni mtu miongoni mwa Waarabu, basi Wallahi Husein(a.s) hakunidadisi zaidi ya hivyo nilivyomwambia".

Kisha Imam Husein akasema kuniuliza "Hebu nifahamishe hali ya watu huko utokako ?"

Nikasema "Hakika umemuuliza mtu anayefahamu hali halisi nayo ni kuwa, nyoyo za watu ziko nawe, panga zao ziko juu ya shingo yako na maamuzi yote yanashuka kutoka mbinguni ".

Imam Husein akasema: "Usemavyo ni kweli kabisa, mambo yote ataamua Mwenyezi Mungu, iwapo uamuzi wake utashuka kwa yale tuyapendayo basi tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zake, naye ndiye mwenye kuombwa msaada ili kuitekeleza shukurani tunayo mshukuru, na ikiwa uamuzi wake utakuwa kinyume cha matarajio hatajitenga yeyote ambaye niya yake ilikuwa kutafuta haki, na ucha Mungu ndilo lengo lake ".

Basi nikamwambia Imam Husein(a.s) , "Basi vema, namuomba Mwenyezi Mungu akutimizie yale uyapendayo na atakulinda kutokana na yale unayoyachelea, kisha nilimuuliza baadhi ya mambo ikiwa ni pamoja na nadhiri na ibada mbali mbali nikataka aniambie, Imam(a.s) alimtikisa mnyama aliyekuwa kapanda (Ishara ya kuondoka) na akaniambia amani iwe juu yako na hapo tukaachana".

Wakati Imam Husein(a.s) anaondoka, Yahya bin Said na kikundi cha watu waliokuwa wametumwa na Amri bin Said bin Al-As (Gavana wa Yazid) walijaribu kumzuia Imam Husein(a.s) .

Imam alikataa katakata yeye na wafuasi wake, jambo ambalo lilipelekea kuzuka mashambulizi ya fimbo baina ya pande mbili hizi.

Basi Imam(a.s) aliendelea na safari yake mpaka akafika mahali paitwapo Tan-im, hapa alikutana na msafara fulani unatoka Yemen akanunua kwa watu wa msafara huo ngamia kwa ajili ya matumizi ya safari yake na wafuasi wake. Naye Bwana Abdallah bin Jaafar aliwatuma wanawe wawili Aun na Muhammad wamfuate Imam Husein(a.s) , kisha akawapa na barua ambayo ndani yake alisema kama ifuatavyo:

Ama baad, bila shaka mimi nakuomba kwa Jina la Mwenyezi Mungu (Basi kubali maombi yangu) utapoiona barua yangu usiende rudi, kwa hakika nakuhurumia kutokana na upande unaoelekea, kwani huenda huko kukawa kuna kifo chako na watu wa Nyumba yako kutawanyika ovyo. Na iwapo wewe utauawa leo hii, basi Nuru ya ulimwengu itakuwa imezimika kwani wewe ndiyo bendera ya wenye kuongoka na ndiyo matumaini ya Waumini.

Basi tafadhali usifanye haraka kwenda katika safari yako, bila shaka mimi nitakuja kukufuatia baada ya barua yangu hii.

Wasalaam.

Huyu Bwana Abdallah aliondoka mpaka kwa Amri bin Said (Gavana wa Makkah) akamuomba kwamba amuandikie Imam Husein maandishi ya kumpa hifadhi na amani ili arudi asiendelee na safari yake aliyokusudia.

Amri akamuandikia Imam Husein kama alivyoombwa, na akaituma barua hiyo kwa Imam Husein, na ikapelekwa na Yahya ambaye ni ndugu wa Amri akiwa pamoja na AbdaIIah bin Jaafar, nao wakampa barua hiyo Imam Husein na wakajitahidi kumfanya arudi lakini akasema;

"Hakika mimi nimemuona Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) usingizini na ameniamuru kama hivi ambavyo ninafinya ."

Abdallah alipokwisha kila namna kumrai Imam(a.s) abadili msimamo, alikata tamaa na pale pale akawaamuru wanawe wafuatane na Imam Husein(a.s) katika safari hiyo na wapigane upande wake itapobidi mapambano, naye Bwana Abdallah na Yahya wakarudi Makkah.

Imam Husein(a.s) akaendelea na safari yake kwenda Iraq bila kupinda kushoto wala kulia mpaka akafika mahali paitwapo "Dhat-Irqi". Hapo alikutana na Bwana Bishri bin Ghalib akitokea Iraq, Imam akamuuliza hali ya watu ilivyo huko Bwana Bishri akasema "Huko nimeacha nyoyo za watu zikiwa pamoja nawe, na panga zao ziko pamoja na bani Umayya ".

Imam(a.s) akasema: "Amesema kweli ndugu wa Bani Asad, bila shaka Mwenyezi Mungu anafanya ayatakayo na anaamua mambo ayapendayo yawe ".

Habari zilipomfikia Ibn Ziyad kwamba Husein anakuja (huko al-Kufah) kutoka Makkah, alimtuma kamanda wake aliyekuwa akiitwa Al-Hasin Bin Numair akaja mpaka Qadisiyya na akalipanga jeshi lake kuanzia Qadisiyya mpaka Khifaan na pia kuanzia Qadisiyya hadi Al-Qatqataniyya.

Imam Husein(a.s) alipofika katika kijia cha Batnu-Rumah, alimtuma Bwana Qais bin Mas-har As-Saidawiy- baadhi ya wanahistoria wanasema alimtuma ndugu wa kunyonya Abdallah bin Yaqtar- kwenda al-Kufah.

Wakati Imam anatuma ujumbe huo alikuwa bado hajafahamu yaliyompata Muslim bin Aqiil.

Katika ujumbe huo aliandika bauua ifuatayo:

BISMILLAHI RAHMAN RAHIM

Barua toka kwa Husein bin Ali, kwenda kwa nduguze Waumini wa Waislamu:

Amani ya Mwenyezi Mungu ikushukieni, bila shaka mimi ninaowajibu kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwenu nyinyi, Mwenyezi Mungu ambaye hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa yeye tu.

Ama baad.

Hakika barua ya Muslim bin Aqiil imenifikia ikiwa na maelezo yanayoonyesha uzuri wa rai yenu, na kukubaliana kwenu juu ya kutusaidia na pia kuitetea haki yetu.

Basi mimi nimemuomba Mwenyezi Mungu ayafanye mema mambo yenu na akulipeni kwa yote ya wema mnayokusudia kututendea, wema ulio mkubwa kabisa. Kwa hakika mimi nimeondoka Makkah kuja huko siku ya Jumanne tarehe nane mfungo tatu.

Basi atapokufikieni mjumbe wangu mujizatiti katika maamuzi yenu bila shaka mimi nitafika hivi karibuni.

Wasalaam.

Kabla Muslim hajauawa kwa siku ishirini na saba, alikuwa kamuandikia barua Imam(a.s) .

Watu wa Al-Kufah nao walimuandikia Imam Husein(a.s) katika kipindi hicho wakimjulisha kwamba, "Wapo wapiganaji laki moja hapa kwa ajili ya kukusaidia usichelewe kuja".

Qais bin Mas-har alielekea Al-Kufah akiwa na barua ya Imam Husein(a.s) mpaka alipofika Al-Qadisiyya akakumbana na Al- Hasin bin Numeir (Askari wa Ibn Ziyad) akampokonya barua hiyo na akampeleka yeye pamoja na barua mpaka kwa Ibn Ziyad.

Alipofikishwa hapo, lbn Ziyad akamuamrisha Qais apande kwenye mimbar amtukane Husein na baba yake na nduguye. Qais akapanda juu ya mimbar kisha akamshukuru Mwenyezi Mungu na akamtukuza halafu akasema, "Enyi watu bila shaka huyu Husein bin Ali Iii miongoni mwa viumbe vya Mwenyezi Mungu vilivyo bora mno, naye ni mwana wa Fatma binti ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) , nami ni Mjumbe wake amenituma kwenu, basi muitikieni muungeni mkono."

Kisha Qais akamlaani Ibn Ziyad na Baba yake na akamuombea msamaha Ali bin Abi talib na akamtakia Rehma na Amani.

Kuona hivyo, lbn ziyad akaamuru Qais atupwe kutoka juu ya jumba la Ibn Ziyad, akakamatwa kisha akatupwa kama ilivyoamuriwa mpaka chini akakatika vipande vipande.

Baadhi ya wanahistoria wanasema alifungwa mikono kisha akarushwa kutoka juu na alipoanguka chini akawa bado hajafa, lakini mtu moja aitwaye Abdul-Malik bin Umair Al-Lakhmi akaja akammalizia kwa kumchinja.

Imam Husein(a.s) aliendelea na safari yake kutoka hapo Batnu-Rumah kuelekea Al-Kufah mpaka alifika sehemu fulani iliyokuwa na maji, hapo akakutana na Bwana Abdallah bin Mutii Al-Adawi.

Bwana huyu alipomuona Imam(a.s) alisimama kisha akamwambia "Ewe mwana wa Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ni jambo gani lililokuleta huku?" Imam Husein(a.s) akasema, "Bila shaka habari za kifo cha Muawiyya zimekwisha kukufikia, basi kwa kifo hicho cha Muawiyya watu wa Iraq waliniandikia barua wakiniita niende kwao."

Ibn Mutii akasema "Nakukumbusha Mwenyezi Mungu Ewe mjukuu wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, pia ikumbuke heshima ya Uislamu (uliyonayo) nachelea itavunjika (kwa safari yako hii)".

Aliendelea Ibn Mutii kumwambia Imam Husein(a.s) "Wallahi iwapo utakitaka kilichomo mikononi mwa bani Umayya watakuua, na wakisha kukuuwa wewe hawatamuogopa yeyote baada yako, (kumfanyia uovu) Wallahi heshima ya Uislamu itaporomoka na heshima ya Maquraish na Waarabu kwa jumla, basi usiende huko Al-Kufah na wala usiitoe nafsi yako kuwapa Bani Umayya".

Imam Husein(a.s) alikataa rai ya Bwana Mutii na akaamua kutimiza lengo lake tukufu katika kuunusuru Uislam.

Kwa upande wake Ibn Ziyad alikuwa ameweka askari wake kuanzia Waqisa hadi kwenye njia iendayo Shamu na ile iendayo Basra, na akawamuru wasimruhusu yeyote kuingia wala kutoka.

Imam(a.s) akaendelea na safari yake, njiani akakutana na mabedui akawauliza khabari za huko Iraq, wakamjibu, "Sisi hatuna tukijuacho lakini uwezekano wa mtu kuingia huko au kutoka hakuna".

Hata baada ya kufahamu hilo Imam(a.s) hakukata tamaa bali aliendelea na safari kama alivyokusudia.

Kuna kikundi cha watu kutoka Fizarah na Bajiila walisimulia wakasema, "Wakati tulipokuwa tunatoka Makkah, msafara wetu ulikuwa jirani na msafara wa Husein(a.s) na Zuheri bin Al- Qain alikuwa nasi, lakini tulikuwa tunachukizwa mno kuweka kambi mahali alipoweka Husein(a.s) , cha ajabu ni kwamba kila Imam Husein alipoweka kituo kupumzika nasi tulijikuta tunalazimika kuweka kituo chetu tupumzike, ingawaje tulikuwa tukipumzika upande usiokuwa ule aliyoko Imam Husein(a.s) .

Jamaa wanaendelea kusimulia, "Basi kipindi fulani tulipokuwa tumepumzika tunakula chakula chetu ghafla alitufikia Mjumbe wa Imam Husein(a.s) akatusalimia kisha akasema, "Ewe Zuheri hakika Abu Abdillah Husein(a.s) amenituma kwako anakuita".

Baada ya maneno ya Mjumbe huyu kusemwa kila mmoja wetu alidondosha chakula alichokuwa nacho mkononi hata tukajikuta kama kwamba vichwani mwetu kumetuwa ndege (aliyesababisha mshituko)."

Mkewe Zuheri akamwambia Zuheri (akiitwa Dailam bint Omar) "Sub-hanallah. Mjukuu wa Mtume anakutumia ujumbe nawe hutaki kumuitika basi afadhali uende ukamsikilize maneno yake". (atakayo kukuambia)

Basi Zuheri akaondoka kwenda kwa Husein(a.s) , na wala hakukaa sana akarudi hali ya kuwa mwenye furaha na uso wake unapendeza, pale pale akaamuru hema lake likunjwe na mizigo yake akafunga akahamia kwa Imam Husein(a.s) .

Wakati akiondoka alimwambia mkewe 'Wewe sasa hivi umeachika hivyo basi rejea kwenu, hakika sipendi upate taabu kwa sababu yangu bali nakutakia kheri, na sasa nimeazimia kufuatana na Husein(a.s) na roho yangu nitaitoa iwe ni fidia kwake na nitamlinda kwa nafsi yangu".

Kisha Zuheri akampa mkewe mali zake na akamkabidhi kwa baadhi ya watoto wa Ammi zake wamrejeshe kwao.

Yule mama alisimama kisha akalia na kumuaga mumewe akasema. "Mwenyezi Mungu amekugeuzia (mwelekeo) basi nakuomba unikumbuke mbele ya Babu yake Husein(a.s) siku ya Kiyama".

Kisha Zuheri akawaambia jamaa zake, "Mwenye kupenda kunifuata miongoni mwenu anifuate, vinginevyo hapa ndiyo mwisho wa mahusiano kwangu mimi, lakini sina budi kuwasimulieni hadithi: Hakika tulipata kupigana vita iitwayo Al-Bahr, na Mwenyezi Mungu akatupa ushindi pia tulipata ngawira, Salman Al-Farisi akatuambia, je mmefurahi kwa ushindi aliokupeni Mwenyezi Mugnu na ngawira mlizopata? Tukasema "Ndiyo".

Salman akasema "Iwapo mtakutana na Bwana wa vijana wa kizazi cha Muhammad(s.a.w.w) , furahini mno kupigana mkiwa pamoja naye kutokana na haya mliyoyapata leo". Kisha Zuheri akaondoka na akafaulu kuwa miongoni mwa waliomsaidia Imam Husein(a.s) .

Wamesema Abdallah bin Suleiman na Mundhir bin Mash-al (Mabwana katika kabila la Asadi) "Tulipomaliza Hija yetu hatukuwa na jambo lolote la muhimu ila tulikusudia tumpate Imam Husein(a.s) njiani ili tuone ni jambo gani litamtokea, basi tukaelekea aliko kwa haraka mpaka tukamkuta amefika Zuruud, na tulipomsogelea mara tukamuona mtu katika watu wanaotoka Al-Kufa amegeuza njia baada ya kumuona Husein(a.s) , naye Imam(a.s) akasimama kama kwamba anataka kumfuata mtu yule, lakini akabadili niya na akamuacha aende zake naye akaendelea na safari yake".

Wale mabwana wanaendelea kusimulia wanasema, "Sisi tulipoona hivyo tukamfuata mtu yule mpaka tukampata tukamsalimia "Asalamu Alaika" akaitika "Waa laikumus-Salaam" tukamwambia: "Wewe ni nani?"

Akasema: "Mimi ni katika kabila la Asad".

Tukasema: "Nasi pia ni katika Asadi, basi jina lako nani"?

Akasema: "Mimi naitwa Bakri Bin fulan, kisha nasi tukamtajia nasaba zetu, kisha tukamwambia, "Hebu tupe khabari za watu walivyo huko utokako?"

Akasema: "Bila shaka sikutoka Al-Kufa mpaka alipokuwa Muslim bin Aqiil ameuawa yeye na Hani bin Ur-wah na nimewaona wawili hawa baada ya kuuawa wanakokotwa kwa miguu yao kuzungushwa sokoni" (waonekane kwa kila mtu).

Wale mabwana wanaendelea kueleza kisa chao wanasema, "(Tukamuacha mtu yule) na tukauelekea msafara wa Imam Husein(a.s) , tukaenda naye mpaka alipotua mahala paitwapo Tha-alabiya ikiwa ni jioni. Sisi tukamwendea hapo alipokuwa tukamsalimia naye akaitikia."

Tukamwambia "Tunamuomba Mwenyezi Mungu akupe Rehma, bila shaka sisi tunayo mazungumzo, iwapo utapenda tukuzungumze wazi au kwa siri."

Imam(a.s) akatutazama sisi kisha akawatazama watu wake akasema, "Hakuna siri kwa hawa waliopo hapa."

Basi tukamwambia "Je ulimuona yule msafiri uliyepishana naye jana jioni?"

Akasema, "Ndiyo, na nilitaka kumuuliza khabari fulani."

Sisi tukamwambia Husein(a.s) "Bila shaka Wallahi sisi tutakutosheleza habari zake, na tumemuuliza mambo yake kwa niyaba yako, na mtu huyo ni katika watu wa kabila letu kisha ni mwenye mawazo mazuri tena mkweli mwenye akili timamu".

Wakaendelea kusema, Na yeye ametuzungumza kwamba ametoka Al-Kufah baada ya kuuawa Muslim na Hani, na amewaona wakikokotwa kwa miguu yao wakipitishwa sokoni."

Imam Husein(a.s) akasema, Inna lillahi waina ilaihi Raajiuna - bila shaka sisi ni milki ya Mwenyezi Mungu na hakika kwake tutarudi, Rehma za Mwenyezi Mungu ziwashukie Muslim na Hani, akarudia kusema hivyo mara nyingine".

Baada ya Imam(a.s) kupata habari hizo alikaa akasubiri mpaka kulipokucha, akawaambia vijana wake ongezeni akiba ya maji nanyi mnywe vya kutosha munyanyuke tuendelee na safaari.

Imam akaondoka kuendelea na safari, akaenda mpaka akafika mahali paitwapo "Zubalah", hapo zikamfikia habari za Abdallah bin Yaqtar na yote yaliyomfika, na ndipo alipotoa barua mbele za watu aliokuwa nao na akawaomea kama ifuatavyo:- Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehma Mwenye Kurehemu, ama baad - kwa yakini zimetufikia khabari za kusikitisha, kwamba Muslim bin Aqiil na Hani bin Ur-wa na Abdallah bin Yaq-tar wameuawa, na wafuasi wetu huko Iraq wamtutupa mkono hakuna watakalo tusaidia, basi yeyote miongoni mwenu apendaye kuondoka (kuanchana nasi) basi na aondoke bila ya taabu na wala hatakuwa na lawama.

Basi baada ya tangazo hili, watu wengi wakamkimbia Imam Husein(a.s) wakawa wanakimbia kuelekea kila upande, wengine kulia na wengine kushoto.

Ikawa hapakubaki ila watu wale wale aliondoka nao Madina na wachache katika watu waliomfuata baadae.

Imam alifanya hivyo kwa sababu alifahamu kwamba, Mabedui waliokuwa wamemfuata walifanya hivyo kwa kutaraji kwamba Nchi anayoelekea Imam ataikuta ikiwa na watu wanaomtii yeye Imam Husein(a.s) ndiyo maana Imam(a.s) akaona vibaya kwenda nao hivi bila kuwajulisha hali halisi bali akawatangazia bayana wafahamu ni kitu gani watakachokutana nacho.

Baada ya hapo Imam akasafiri hadi akapita sehemu iitwayo "BAT-NUL-UQBAH akatua hapo.

Mahali hapa alikutana na mzee mmoja katika Bani Ik-Rimah aitwaye Omar bin Luwadhan, na huyu mzee akamuuliza Imam: "Unakusudia kwenda wapi?"

Imam akasema: "Al-Kufah."

Yule mzee akasema "Nakunasihi tafadhali usiende, Wallahi huko hutakutana isipokuwa na mikuki na mapanga, na hawa waliokuita lau wengekuwa ni wenyekukusaidia kwa vita na wakakuanalia mapokezi mazuri, hapo ilikuwa na busara kwako wewe kwenda kwao, lakini kutkana na hali hii unayozungumza mimi naona si vema kwako kuenda."

Imam(a.s) akamwambia yule mzee, "Ewe mtumwa wa Mwenyezi Mungu, kwangu mimi halijifichi lipi la kufanya na lipi la kuacha, lakini fahamu kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu anapoamua jambo hakuna wa kupinga ."

Kisha Imam(a.s) akasema, "Wallahi naapa kwamba, maadui zangu hawataniacha mpaka wahakikishe wanautoa uhai wangu, na wakisha fanya hivyo Mwenyezi Mungu atawapambanisha na watu watakaowanyanyasa mpaka wawe wao ndiyo viumbe dhalili mno katika makundi ya Umma" (Duniyani).

MAJLISI YA KUMI NA MOJA

IMAM HUSEIN(A.S) AWASILI KARBALA

Imam Husein aliendelea na safari yake mpaka ikabaki kiasi cha safari ya siku moja kutoka Al-Kufah hadi hapo alipokuwa.

Mara ghafla alitokea Bwana Huru bin Yazid akiwa na Askari alfu moja wenye farasi na Imam(a.s) akamwambia Huru, "Je hapa nitasalimika au tutaangamia ".

Huru akajibu "Lililopo hapa ni kuangamia tu ewe Abu Abdullahi."

Imam akisema: Lla haula wala Quwwata ma billahi l-aliyyiladhiim" Kisha wakawa wanazungumza baina yao (Imam na Huru) hatimaye Imam Husein(a.s) akasema "Basi iwapo ninyi mmekuwa na mawazo tofauti na zile barua zilizonifikia, pia vile ambavyo wajumbe wenu mlivyowatuma kwangu, basi niacheni nirudi nilikotoka.

Huru na jamaa zake wakamzuia Imam karudi Makkah, bali Huru akamwambia Imam(a.s) "Ewe mjukuu wa Mtume pita njia nyingine yoyote ambayo haitakufikisha Al-Kufah wala Madina, ili nami nipate kisingizio cha kumwambia Ibn Ziyad kwamba wewe umenikwepa njiani ".

Imam Husein(a.s) akaelekea upande wa kushoto, na alipofika mahali paitwapo Udhaibul-Hajanaat, Ubaidullah bin Ziyad (Mwenyezi Mungu Amlaani) akatuma barua kwa Huru akamlaumu kutokana na tendo lake la kumuachia Imam Husein ashike njia nyingine na akamuamuru kuanzia hapo amsonge Imam Husein(a.s) .

Huru na wale askari wake wakamfuata Imam na kumzuia.

Imam Husein(a.s) akamwambia Huru, "Je siyo wewe uliyetuamrisha tubadilishe njia "?

Huru akamjibu Imam(a.s) akasema, "Hakika ni mimi, lakini imenifikia barua ya Amiri (Ibn Ziyad) ananiamrisha nikusonge nisikupe nafasi, na ameniwekea mtu wa kunipeleleza iwapo ninatekeleza jambo hilo au hapana ".

Imam Husein(a.s) akasimama kuwahutubia watu wake, akamshukuru Mwenyezi Mungu na kumsifu, kisha akamtaja Babu yake (Mtume Muhammad(s.a.w.w) na akamswaIia kisha akasema: "Bila shaka yamekwisha kutufika mambo ambayo mnayaona wazi wazi, na kwamba duniya imebadilika na imeyakataa na kuyapa mgongo mema yake, na imeimarika kutenda yasiyokuwa na busara, na hakuna kilichobakia katika dunia isipokuwa ni kama maji kidogo ndani ya chombo, na maisha duni mfano wa malisho yasiyofaa, je hamuoni kwamba ukweli sasa hivi hautumiki na kwamba uovu haukemewi? Basi aliye Muumini na atarajie kukutana na Mola wake kwa kuuawa (na madhalimu) kwani mimi mimi naona kifo (katika njia ya haki) ni mafanikio na kuishi pamoja na watu dhalimu ni unyonge".

Baada ya hotuba ya Imam(a.s) alisimama Bwana Zuhair bin Al-Qain akasema, "Tumesikia usemi wako ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, lau dunia ingekuwa ni yenye kudumu kwa ajili yetu nasi tukawa ni wenye kuishi humo milele, Wallahi tungethamini mno kupambana na udhalimu tukiwa pamoja nawe ili kuitetea haki".

Kisha alisimama Hilal bin Nafii Al-Bajali akasema, "Wallahi hatuchukii kufa ili tukutane na Mola wetu, nasi katika niya zetu na tunavyofahamu ni kwamba tutamtawalisha anayekutawalisha wewe na tutampinga anayekupinga".

Naye Burair bin Khudhair alisimama akasema, "Wallahi Ewe Mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, bila shaka Mwenyezi Mungu ametuneemesha kwa kupitia kwako pale alipo tujaalia kuwa tutauawa mbele yako na viungo vyetu vitakatwakatwa kwa ajili yako, kisha siku ya Qiyama Babu yako (Muhammad s.a.w.w) atakuwa ndiyo muombezi wetu".

Baada ya hapo Imam Husein aliondoka kuendelea na safari yake, lakini ikawa kila alipotaka kuelekea upande fulani Huru na askari wake humzuia na wakati mwingine humsonga wakawa ubavuni mwa msafara wake.

Kutokana na hali hiyo ya kusongwa na majeshi hayo, wanawake waliokuwa pamoja na Imam(a.s) wakaingiwa na woga na watoto nao wakawa na khofu isiyokuwa na kipimo.

Huru na Askari wake walimsonga Imam(a.s) mpaka wakamfikisha Kar-bala ikiwa ni tarehe mbili mfungo nne (Muharram). Walipofika hapo Imam Husein(a.s) akauliza Jina la Ardhi hiyo na akaambiwa, "hapa ni Kar-bala".

Imam(a.s) akasema, "Ewe Mola najilinda kwako kutokana na huzuni na tabu ". (Karb-balaa).

Kisha akasema tena, hapa ndipo mahali penye huzuni na taabu, basi teremkeni kwa kuwa ndicho kituo cha msafara wetu, na ndipo mahali ambapo damu zetu zitamwagika, na ni sehemu itakayokuwa na makaburi yetu, mahali hapa alinisimulia Babu yangu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwa yote niliyoyaeleza".

Watu wote waliokuwa na Imam Husein(a.s) wakashuka kando ya Imam Husein(a.s) .

Imam Husein(a.s) aliketi akawa anauandaa upanga wake huku akisema mashairi yaliyokuwa yanabashiri kifo chake.

Dada yake Imam(a.s) aliyekuwa akiitwa Zainab aliposikia maneno ya nduguye akasema: "Ewe kaka yangu maneno haya usemayo ni ya mtu ambaye tayari amekwisha thibitisha kwamba atauawa ".

Imam akasema: "Hivi ndivyo ilivyo kwangu ewe dada yangu ".

Bibi Zainab akasema: "Aa! hasara iliyoje. Husein anaomboleza mbele yangu kifo chake mwenyewe "!

Kilio cha bi Zainab na maneno aliyoyasema yaliwafanya wanawake wote walie na wakawa wanapiga nyuso zao na kukata mikufu yao. Naye Ummu Kul-thuum akawa anaomboleza kwa kusema "Ewe Muhammad wangu(s.a.w.w) ewe Ali wangu(a.s) Ewe Mama yangu (Fatma a.s) Ewe ndugu yangu Ewe Hasani wangu(a.s) , tumeangamia baada yako ewe Abaa-Abdillah".

Imam Husein(a.s) aliposikia maombolezo ya Ummu Kulthuum akamtaka awe na subira akamwambia, "Ewe dada yangu vumilia ufarijike kwa Mwenyezi Mungu, kwani viumbe vya mbinguni vitakufa, na viumbe wa ardhini nao watakufa, kadhalika viumbe wote watakufa ".

Imepokewa katika mapokezi mengine kwamba Bibi Ummu Kul-thuum alipofahamu madhumuni ya beti za mashairi aliyokuwa akiyasoma Imam(a.s) alitoka kwa uchungu mkubwa huku akikokota nguo zake mpaka akaenda kusimama mbele ya Imam Husein(a.s) akasema, "Ooo! Hasara iliyoje laiti mauti yangenichukua (leo), kwani leo ni sawa na kifo cha mama yangu Fatma, na Baba yangu Ali na ndugu yangu Hasan(a.s) . Ewe uliyebaki baada ya hao waliokutangulia, wewe ulikuwa ndiyo nguzo ya sisi tuliobakia".

Imam Husein(a.s) alimtazama dada yake kisha akasema: "Ewe dada yangu angalia shetani asije akauchukua uvumilivu na subira yako katika machungu yako kwangu ".

Imam Husein(a.s) akashikwa na huzuni kubwa machozi yakawa yanamlengalenga kisha akasema, "Sina njia ya kufanya kuepuka mauti ".


3

MAOBOLEZO YA KIFO CHA IMAM HUSEIN(A.S)

MAJLISI YA KUMI NA MBILI

MAPAMBANO DHIDI YA ASKARI WA IBN ZIYAD

Baada ya Imam Husein kuamua kutua hapo Kar-bala miongoni mwa wafuasi wake waliokuwa bora na wanaombatana naye mara kwa mara ni Bwana Nafii bin Hilal Al-Jamali.

Bwana huyu alikuwa hodari sana wa kupanga mbinu za mapambano ya vita hasa kwa kutokana na ujuzi mkubwa aliokuwa nao kuhusu mambo ya kisiasa.

Basi siku moja Imam(a.s) akatoka nje ya mahema mpaka akawa mbali, Nafii akamuona Imam naye mara akachukua upanga wake na haraka akamfuata Imam(a.s) .

Nafii akamuona Imam akiwa katika harakati za kufanya uchunguzi kwenye mipaka ya maeneo ya mahema ya watu wake, mara Imam(a.s) akageuka na akamuona Nafii akasema, "Nani wewe Nafii?"

Nafii naye akasema, "Ndiyo ewe mwana wa mtume wa Mwenyezi Mungu, mimi ni fidia kwako ".

Imam(a.s) akasema kumwambia Nafii, "Ewe Nafii ni jambo gani Iililokutoa katika usiku huu ?"

Nafii akasema "Ewe Bwana wangu kumeniogopesha kutoka kwako usiku kuelekea upande wa hawa maadui ".

Imam(a.s) akasema, "Ewe Nafii nimetoka ili kufanya uchunguzi wa maeneo yetu kwani nachelea hali ya usalama wetu siku tutapopambana na maadui hawa ".

Nafii anasema: "Kisha Imam hali ya kuwa amenishika mkono wangu kushoto huko akisema "Wallahi hii ni ahadi isiyovunjwa".

Baadaye Imam Husein akasema kumwambia Bwana Nafii, "Ewe Nafii pita baina ya milima hii miwili (Ukimbie) uokoe nafsi yako?"

Nafii bil Hilal aliporomoka chini akaibusu miguu ya Imam(a.s) akalia na huko anasema, "Ewe Bwana wangu, bila shaka upanga wangu thamani yake ni Dir-ham alfu moja kadhalika farasi wangu naye hivyo hivyo, namuapa Mwenyezi Mungu ambaye amenineemesha kwa kuwa pamoja nawe mahali hapa ya kwamba, sitakuacha mimi ni mtumwa wa Mungu naye atanilinda kwa hali yeyote itakayotokea". Nafii anasema: "Kisha Imam aliniacha na akaingia kwenye hema la dada yake Zainab bint Ali(a.s) , nami nikasimama namsubiri.

Bibi Zainab akamkaribisha Imam(a.s) na akampa kiti akakaa na akawa anazungumza naye mazungumzo ambayo sikuwa nasikia kinachozungumzwa.

Basi mara ghafla bibi Zainab alilia na akawa anasema "Bila shaka nitashuhudia kifo chako, na huu ni mtihani mkubwa hasa utakapokuwa umeniacha kuwaangalia wanawake hawa waliojaa hofu na woga ".

"Ewe ndugu yangu, kama unvyofahamu uadui walionao watu hawa toka hapo zamani, kwa hivyo jambo hili ni zito sana kwangu mimi, vifo vya vijana wa Kibanihashim ni msiba mkubwa sana kwangu ".

Kisha Bibi Zainab akasema: "Ewe mtoto wa Mama yangu, hivi wazifahamu niya na dhamira za wafuasi wako? Bila shaka mimi nachelea kwamba watakutelekeza wakati wa mapambano ".

Imam Husein(a.s) akalia kisha akasema: "Wallahi nimewajaribu ili nipate kuwafahamu Imani na niya zao, sikuona miongoni mwao isipokuwa ni watu mashujaa tena hodari wanafurahia kifo kwa ajili yangu na kuliwazika kama anavyoliwazika mtoto mdogo anyonyapo maziwa ya mama yake ".

Nafii akasema, Nikalia kwa kumuonea huruma bibi Zainab, kisha nikamuendea Habib bin Mudhahir na nikamuona amekaa ndani ya hema lake, mkononi mwake ameushika upanga ulionolewa barabara huku anasema kama mtu anayesemesha upanga wake. "Ewe dhoruba ya upanga, jiandae kujibu mashambulizi pindi mapambano yatakapoanza ".

Nafii anaendelea kueleza anasema: "Nikamsalimia Habib na akaniitikia kisha akasema, ewe ndugu yangu ni jambo gani lililokutoa nje usiku huu?"

Basi nikamsimulia mwanzo wa kisa cha mimi kutoka nje mpaka mahali ilipofikia Imam Husein(a.s) kusema kwamba wafuasi wangu wanfurahia kifo kwa ajili yangu na wanaliwazika kama ambavyo mtoto anavyoliwazika pindi anyonyapo ziwa la mama yake".

Baada ya kuambiwa maneno haya Habib alisimama kisha akasema "Aa! Wallahi kama isingekuwa kusubiri amri ya Imam (a.s) katika kuwashambulia adui zetu mimi ningewaanza kuwashambulia usiku huu kwa upanga wangu huu na wala asingemudu yeyote mapambano dhidi yangu "

Kisha Nafii akamwambia Habib "Ewe ndugu yangu nimemuacha Husein(a.s) akiwa na dada yake Zainabu wakiwa na hali ya khofu, nadhani wanawake wengine nao watakuwa tayari wameungana na Bibi Zainab katika hali ya huzuni na majonzi, je waweza kuwakusanya wenzio ili muende mukawatulize nyoyo zao kuwaondolea woga walio nao, kwani nimeshuhudia hali ambayo siamini kama (Huseina.s ) atabakia duniani hapa."

Habib akasema, "Mimi ninatii nakukubali utakavyo ".

Pale pale Habib akaanza kuwaita jamaa zake akasema, "Wako wapi watu wakumnusuru Mwenyezi Mungu, wako wapi watakaomsaidia Mtume wa Mwenyezi Mdngu(s.a.w.w) , wako wapi wasaidizi wa Amiril-Muuminina Ali(a.s) , wako wapi watakaomsaidia Fatma(a.s) wako wapi watetezi wa Husein(a.s) , wako wapi watakaounusuru Uislam?

Wakachomoza kutoka katika mahema yao mfano wa simba wakali wenye kushambulia hali wakiongozwa na Abul-Fadhili Abbas(a.s) (mdogo wake Imam Husein). Walipokwishakusanyika Habib akawaambia bani Hashim, "Rudini mahala penu (katika mahema yenu) hakuna haja ya kukesha".

Kisha akawaambia jamaa zake, "Enyi watukufu na enyi Simba mashujaa, huyu hapa Nafii bin Hilal amenijulisha kitambo kidogo kilichopita (akasimulia mambo yote aliyoambiwa na Nafii kuhusu hali ya Imam(a.s) na Bibi Zainab) kisha akasema, nambieni nanyi niya zenu na dhamiri zenu juu ya haya".

Basi wote wakasema: "Ewe mwana wa Mudhahir Wallahi lau jamaa hawa watatushambulia, tutavikata vichwa vyao na tutawakutanisha na wazee wao nasi tutamlinda Mtume wa Mwenyezi Mungu katika kizazi chake na ukoo wake ".

Habib akawaambia, "Nifuateni, nifuateni". Akasimama akaondoka na kuikanyaga ardhi kwa kishindo, nao wakawa wanarukaruka nyuma yake huko wanamfuata mpaka aliposimama kwenye vigingi vya kamba za mahema ya Imam Husein na watu wa nyumba yake kisha akasema, "Amani ikushukieni enyi mabwana viongozi wetu, Amani ikushukieni Enyi kikundi cha Utukufu wa Mtume wa Mwenyezi Muggu(s.a.w.w) hizi hapa panga za vijana wenu, wameapa kwamba hawatazichomeka panga zao ispokuwa ndani ya shingo ya yeyote anayetaka kuwatendeeni uovu".

Akaendelea kusema: "Hii hapa mikuki ya vijana wenu, wameapa kuwa wataitwika vifua vya wale wanaotaka kutawanyisha umoja wenu ".

Basi hapo Imam Husein(a.s) akawatokea na kusema "Enyi wafuasi wangu, Mwenyezi Mungu akulipeni malipo mema kutokana na (kuwalinda) watu wa Nyumba ya Mtume wenu ".

Imepokewa kutoka kwa Imam Jaafar As-Saadiq(a.s) kwamba yeye amesema, "Nilimsikia Baba yangu akisema, pindi walipokutana Imam Husein na Umar bin Saad na kisha vita vikaanza kupiganwa Mwenyezi Mungu alimteremshia msaada Imam Husein na akampa hiyari baina ya kuwa mshindi dhidi ya maadui zake au auawe katika vita hivyo kisha aende kwa Mola wake, Imam(a.s) alichagua kufa na kukutana na Mwenyezi Mungu".

Baadaye katika kipindi hicho cha kuanza mapambano Imam Husein(a.s) aliita kwa sauti akasema, "Je kuna mwenye kutusaidia (katika vita hivi) kwa ajili ya kupata radhi za Mwenyezi Mungu?"

Basi mara baada ya wito huu Bwana Huru bin Yazid Ar-Riyahi akamwendea Omar bin Saad akamwambia: "Je wewe unataka kupigana na mtu huyu ?"

Omar bin Saad akasema: "Ndiyo niko tayari kupigana naye kwani naapa kwa Mwenyezi Mungu kuwa wepesi na uzuri wa mapambano ni pale vichwa vinaporuka (vikikatwa) na mikono nayo inapokatwa ".

Huru bin Yazid Ar-Riyahi akawa anaondoka huku anatetemeka kwa uchungu mkubwa.

Muhajir bin Ausi akamwambia Huru "Wallahi msimamo wako unatia mashaka, na Iau ningeulizwa ni nani shujaa mno miongoni mwa watu wa Al-Kufah, nisingekutaja wewe kutokana na hali niionayo kwako ".

Huru akajibu akasema: "Namuapa Mwenyezi Mungu, hakika mimi ninahiyarisha nafsi yangu baina ya kuingia peponi au motoni, basi sitachagua chochote kinyume cha pepo japokuwa nitauawa na kukatwakatwa kisha nichomwe moto ".

Kisha palepale alimpiga farasi wake akaondoka kumfuata Imam Husein(a.s) huku ameweka mkono wake kichwani akiwa anasema, "Ewe Mwenyezi Mungu nimerejea kwako basi nisamehe kwani nimekuwa nikizihofisha nyoyo za mawili wako na watoto wa binti ya Mtume wako ."

Kisha Huru akamwambia Imam Husein(a.s) "Mimi ndiye yule niliyekuzuia usirudi ulikotoka na nikakusonga mpaka kukufikisha hapa, kwa hakika sikutarajia kabisa kwamba hawa jamaa watakufanyia haya ninayoyaona sasa hivi, nami kwa yote haya natubia kwa Mwenyezi Mungu, basi je unaona kuwa ninaweza kusamehewa ?"

Imam Husein akamwambia Huru, "Ndiyo Mwenyezi Mungu atakusamehe ".

Kisha Bwana Huru akasema kumwambia Imam Husein(a.s) "Mimi nilikuwa mtu wa mwanzo kutoka dhidi yako, basi nakuomba uniruhusu niwe wa mwanzo kuuawa mbele yako ili niwe miongoni mwa watu watakaopeana mkono na Babu yako Muhammad(s.a.w.w) kesho siku ya Qiyama.

Imam Husein(a.s) akamruhusu Bwana Huru, na mapambano yalipoanza, Huru alipigana kwa ushujaa na uhodari mpaka akawauwa wengi wa waliokuwa mashujaa upande wa maadui kisha baadaye aliuawa na kufa shahidi.

Alibebwa na kupelekwa kwa Imam Husein(a.s) naye Imam(a.s) akawa anampangusa udongo uliokuwa usoni kwake huku akisema "Wewe ni Huru kama alivyokuita mama yako, basi umekuwa Huru duniani na Akhera ".

Imam Jaafar anaendelea kutusimulia "Baada ya Huru kuuawa alitoka Bwana Burair bin Khudhair, na Bwana huyu alikuwa mcha Mungu sana .

Nao upande wa maadui wa Imam Husein(a.s) alitoka Yazidi bin Al-Maghfal ili apambane na Burair.

Kabla ya kupambana watu wawili hawa waliafikiana kufanya "Mubahala" maapizano kwa Mwenyezi Mungu kwamba aliye katika baki na ukweli amuuwe aliye katika uongo na upotofu.

Walipokabiliana kupambana Burair alimuua Yazid, na akaendelea kupigana na wengineo kisha hatimaye aliuawa "Rehema za Mwenyezi Mungu zimshukie."

Baada ya kuuawa kwa Burair Bwana Wahhab bin Hibab Al-Kalbi naye aliingia katika uwanja wa mapambano na akapigana vyema kwa upanga na kuonyesha ushupavu katika Jihadi.

Bwana huyu alikuwa kafuatana na Mkewe pamoja na Mama yake katika safari hii ya kumuunga mkono Imam Husein(a.s)

Ikawa kipindi fulani alirudi kwenye mahema na kumuambia mama yake "Je mama uko radhi nami au hapana"?

Mama yake akasema "Siwezi kuwa radhi mpaka nione unauawa mbele ya Husein(a.s) kwa kumtetea yeye.

Ama mkewe Bwana Wahhab, yeye alisema "Naapa kwa Mwenyezi, nakuonya usije niachia majonzi iwapo utauawa ".

Mama yake akasema: "Mwanangu yapuuze maneno ya mkeo rejea ukapigane kwa ajili ya mtoto wa Binti ya Mtume utapata maombezi ya babu yake siku ya Qiyama".

Bwana Wahhab akarudi na akaendelea kupigana mpaka mikono yake yote miwili ikakatwa.

Mkewe Bwana Wahhab alichukua mkongojo akawa anamfuata mumewe huku akimwambia "Endelea kupigana kuwatetea watu wema upate kuilinda heshima ya Mtume wa Mwenyezi Mungu ".

Bwana Wahhab akamfuata ili amrejeshe mahali waliko wanawake lakini mkewe huyo akaishika sehemu ya nguo zake kisha akasema. "Sirudi mpaka nihakikishe nakufa pamoja nawe ".

Imam Husein alipoiona hali hiyo akasema "Hakika mumekwisha kulipwa mema kutokana na kujitoa kwenu muhanga kwa ajili ya watu wa Nyumba ya Mutme(s.a.w.w) , Ewe mama rudi".

Anaendelea kusimulia anasema: "Kisha alitoka Bwana Muslim bin Usajah, (Mwenyezi Mungu Amrehemu Bwana huyu) yeye alipigana na maadui, na alikuwa mvumilivu kutokana na ukali wa mapambano na shida alizokabiliana nazo mpaka ikafika kipindi fulani alidondoka chini akawa karibu kukata roho. Na ndipo Imam Husein(a.s) akiwa pamoja na Bwana Habib bin Mudh-hir akaenda hapo alipoanguka".

Imam Husein(a.s) akamwambia "Mwenyezi Mungu akurehemu ewe Muslim, katika waumini kuna ambao wamekwisha kufa wakitetea dini ya Mwenyezi Mungu, na wapo wengine wanakisubiri kifo kwa ajili hiyo, na kamwe hawakubadilisha misimamo yao ".

Naye Bwana Habib (r.a) akamsogelea na akasema "Kifo chako kwangu mimi sijaona mfano wake Ewe Ndugu yangu Muslim, basi jibashirie kupata pepo ".

Muslim akajibu kwa sauti ya unyonge (kwani alikuwa karibu kukata roho) akamwambia Habib, "Mwenyezi Mungu nawe akubashirie Pepo".

Kisha Habib akamwambia Muslim "Lau ningalifahamu ya kwamba mimi nitakufuatia, basi ningependa uniusie kila jambo ambalo limekufanya usitulie ila uamue kuingia katika mapambano."

Muslim akamwambia Habib, "Nakuusia juu ya huyu (akamuashiria Imam Husein a.s.) pigana kwa yake mpaka ufe."

Habib akamwambia Muslim "Basi nitakufurahisha kwa kutimiza wasia wako".

Mara Bwana Muslim akakata roho (Mwenyezi Mungu amuwie Radhi). Imam Jaafar anaendelea kusimulia anasema; "Swala ya

Adhuhuri ilipofika Imam Husein(a.s) alimuamuru Zuheir bin Al-Qain na Said bin Abdallah Al-Hanafi wasimame mbele yake, kisha Imam akawasalisha swala ya khofu watu waliobakia.

Ghafla ulitupwa mshale kumlenga Imam Husein(a.s) , Bwana Said bin Abdallah Al-Hanafi akajitokeza kuuzuiya kwa kukinga mwili wake.

Mshale ule ulimpiga Bwana huyu na hakuwahi wala kupiga hatua moja bali alidondoka chini huku akisema, "Ewe Mwenyezi Mungu walaani watu hawa kwa laana uliyowalaani watu wa Aad na Thamud".

Akaendelea kusema Bwana Said, "Ewe Mola mfikishie salamu zangu Mtume wako na umjulishe yaliyonipata kutokana na maumivu ya majeraha, kwani mimi ninataka thawabu zako katika kukitetea kizazi cha Mtume wako".

Kisha Bwaaa huyu alifariki na mwili wake ulikutwa ukiwa na majeraha kumi na tatu ya mishale na mapigo ya panga pia mikuki iliyotokana na mashambulizi yaliyoelekezwa kwake.

Naye Bwana Suwaid bin Amri bin Abil-Mutai alijitokeza kupambana na madhalimu wa jeshi la Yazidi.

Bwana huyu alikuwa mcha mungu mwingi wa kuswali. Alipambana kwa uhodari mfano wa simba aliye shujaa, na alivumilia ukali wa mapigano mpaka alipokuwa kaishaenezwa majeraha mengi alidondoka chini.

Alibakia hapo chini mpaka alipowasikia wakisema; "Husein(a.s) kauawa " alijikakamua na kutoa kissu kilichokuwa ndani ya soksi zake akaanza kupambana nao mpaka akauliwa.

Hapo ndipo wafuasi wa Imam Husein(a.s) walipoanza kupambana kwa ukali huku wakimkinga na kumlindaa Imam Husein(a.s) .

Hali ya vita ilipokuwa imezidi ukali, na maadui wakawa wanamuandama Imam Husein kutaka kumuuwa, Abbas bin Ali bin Abi Talib (mdogo wake Imam Husein kwa mama mwingine) aliwataka maadui hao waahirishe vita mpaka kesho yake.

Imam Husein alitumia fursa hiyo kuwaamuru wafuasi wake wayasogeze mahema yao yawe karibu na kamba zake wazipishanishe kati ya hema na hema jingine.

Pia aliwataka wasimame mbele ya mahema yao na wakamkabili adui kwa mwelekeo mmoja na mahema yawe nyuma yao na mengine yawe kulia kwao na mengine kushoto kwao.

Usiku ulipoingia Imam Husein(a.s) na wafuasi wake walikesha wanaswali na kuomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu, pia waliomba maombi mbali mbali kwa unyenyekevu.

Kifupi walikesha wakiomboleza kwa maombi na sauti zao zilichanganyika na kusikia kama mvumo wa nyuki wengi.

Miongoni mwao walionekana wenye kusimama wengine wamerukuu na wengine wamekaa na wengine wamesujudu, almuradi kila mmoja kwa namna ya ibada yake. Katika usiku huo, askari thelathini na mbili wa lbn Ziyad waliwavamia Imam na watu wake. Askari hao walimsonga Imam Husein(a.s) yeye na watu wake kwa kipindi kirefu.

Ilifika wakati ambao Imam na watu walishikwa na kiu kali ya maji, ndipo Imam(a.s) alisimama akaegemea mpini wa upanga wake, akasema kwa sauti kubwa "Nakuapieni Mwenyezi Mungu, Je ninyi munanifahamu mimi?"

Imam akasema: "Je mnafahamu kwamba Babu yangu ni Mjumbe wa Mwenyezi Mungu ?"

Wakajibu: "Ndiyo tunafahamu".

Akawaambia tena "Je mnafahamu kwamba Baba yangu ni Ali bin Abi Talib?"

Wakajibu: "Bila shaka tunafahamu".

Imam akasema: Je munajua kwamba nyanya yangu Khadija Binti Khuwailid ndiye mwanamke wa kwanza kusilimu?"

Wakasema: "Ndiyo tunajua".

Akawaambia tena, "Je mnafahamu ya kuwa Jaafar At-Tayaar aliyeko Peponi ni Ami yangu?"

Wakajibu: "Hilo pia tunalifahamu."

Imam(a.s) akawaambia: "Je mnafahamu kwamba upanga huu ni upanga wa Mjumbe wa Mwenyezi Mimgu na kwamba mimi nimeurithi?"

Wakajibu: "Hilo tunalijua".

Akasema tena: "Je mnajua kuwa kilemba hiki ni cha njumbe wa Mwenyezi Mungu nami nimekivaa?

Wakasema: "Ndiyo pia tunafahamu".

Akasema tena Imamu(a.s) "Je mnafahamu kwamba Ali bin Abi Talib ndiye Muislamu wa kwanza na ndiye njuzi kuliko wengine (baada ya Mtume (s.a.w.w ) naye alikuwa mpole kuliko wote, na kwamba yeye ndiye Walii wa kila Muumini mwanamume na mwanamke?"

Wakasema: "Pia tunafahamu".

Kisha Imam Husein(a.s) akawaambia, "Basi ni kwanini mnataka kumwaga damu yangu wakati Baba yangu ndiye mlinzi wa haudhi, na Bendera Tukufu ya Mtume itakuwa mikononi mwake siku ya Qiyama?"

Wakasema: "Na hilo nalo twalifahamu".

Kisha wakamwambia Imam(a.s) "Yote hayo uliyoyasema sisi tunayajua vizuri, lakini hatutakuacha mpaka uyaonje mauti hali yakuwa una kiu ".

Baada ya hotuba hii ya Imam Husein(a.s) na ikawa imesikilizwa na mabinti zake pamoja na dada yake Bi Zainab bint Ali, wote hawa walianza kulia na kuomboleza kwa sauti kubwa.

Basi Imam(a.s) alipoiona hali hiyo, akamtuma nduguye Bwana Abbas na Mwanawe Bwana Ali bin Husein akawaambia: "Nendeni mukawanyamazishe watazidi kulia".

Mapambano baina ya Imam Husein na askari hao wa Ibn Ziyad yalikuwa makali kiasi ilifikia Imam(a.s) akabaki yeye na watu wa nyumbani mwake.

Wafuasi wa Imam Husein(a.s) waliuawa wote asibakie hata mmoja. Ilipokuwa Imam kabaki peke yake na watu wa nyumbani mwake, alitoka Ali bin Husein(a.s) akamuomba ruhusa Baba yake ili akapigane na hao maadui.

Imam Husein(a.s) akampa ruhusa mwanawe, kisha akamtazama kwa jicho Ia huzuni na mara macho yake yakaanza kububujika machozi na akasema "Ewe Mwenyezi Mungu shuhudia, hakika amewatokea kupambana nao kijana ambaye kwa umbo na tabia amefanana mno na Mjumbe wako (Muhammad s.a.w.w) nasi tulikuwa kila tukimkumbuka Mtume wako basi humtazama kijana huyu na hamu hutuishia".

Imam Husein alipaza sauti akasema kumwambia Ibn Saad, "Ewe mwana wa Saad Mwenyezi Mungu na aukate ukoo wako kama wewe unavyoikata nasaba yangu.

Basi Ali bin Husein(a.s) akawaelekea hao maadui ili kupambana nao na akapigana nao vikali sana, akawauwa wengi katika wao.

Ali bin Husein(a.s) akarudi hadi kwa Imam Husein(a.s) akamwambia "Ewe Baba hakika kiu ndiyo itakayoniuwa, je naweza kupata maji ya kunywajapo kidogo ili nipate nguvu ya kupambana na maadui hawa ?"

Imam Husein(a.s) akasema "Ewe Mwanangu nitapata wapi maji ya kukupa, nenda kapigane si muda mrefu utakutana na Babu yako Muhammad(s.a.w.w) atakunywesha kikombe cha maji ambacho kitakutosheleza kiu yako na hutahisi tena kiu".

Ali bin Husein(a.s) akarejea kwenye uwanja wa mapambano na akapigana kwa nguvu sana lakini Munqidh bin Murata al-Abadi akamtupia mshale ambao ulimpata na akadondoka chini pale pale akapaza sauti akasema kumwambia Baba yake (Imam Husein a.s) "Ewe Baba pokea salamu toka kwangu, pia huyu hapa Babu yangu (Mtume Muhammad) naye anakutolea salamu na anasema fanya haraka uje huko tuliko," kisha alivuta pumzi ndefu akafariki.

Imam Husein(a.s) alikuja mpaka mahali alipofia mwanawe, akaweka shavu lake juu ya shavu Ia mwanawe akasema: "Mwenyezi Mungu awalaani watu waliokuuwa ewe mwanangu. Akaendelea kusema watu hawa: ni majasiri kiasi gani kuweza kuvunja heshima ya Mtume(s.a.w.w) ".

Baada ya hapo Bibi Zainab bint Ali alitoka akawa anaomboleza kwa kusema: "Ewe kipenzi changu, Ewe mwana wa Ndugu yangu ".

Bibi Zainab alikwenda mpaka akaukumbatia mwili wa Ali bin Husein(a.s) , Imam Husein akamuondoa na kumrudisha waliko wanawake.

Baada ya kuuawa kwa Ali bin Husein(a.s) ikawa sasa anatoka mtu baada ya mtu katika watu wa Nyumba ya Imam Husein(a.s) mpaka idadi yao kubwa wakauawa.

Hali hiyo ilimfanya Imam Husein aseme kwa sauti ya juu "Fanyeni subira Enyi wana wa Ami zangu, vumilieni enyi watu wa Nyumba yangu, Wallahi hamtaona unyonge mwingine baada ya leo ".

Baada ya hali hiyo yuko kijana mwingine katika watu wa Nyumba ya Imam(a.s) alitoka ili akapigane na maadui hao.

Kijana huyu alikuwa na uso wenye kung'ara kama mwezi, na alipoingia katika mapigano alipigwa upanga wa kichani na mtu mmoja aliyekuwa akiitwa Ibn Fudhail Al-Azdi upanga ule ukampasua na akadondoka chini na akaita "Ewe Ami yangu (kumuita Imam Husein).

Imam Husein alipoona kijana huyu naye ameuawa, alijiweka tayari kujibu shambulio hilo, na ndipo akampiga lbn Fudhail kwa dhoruba kali ya upanga. Bwana huyo alijaribu kuzuia kwa mkono wake lakini Imam akamkata katika fundo la mkono. Bwana huyu alipiga makelele kwa nguvu zote mpaka askari wa Yazid wote wakasikia na ikawafanya washituke ili kumuokoa, lakini kuja kwao kwa wingi na kwa haofu kulisababisha wakamkanyagakanyaga kwa miguu ya farasi mpaka akafa.

Kisha Imam Husein alisimama kichwani kwa yule kijana wake ambaye alikuwa karibu kukata roho, akasema "Walaaniwe watu waliokuuwa".

Kisha akasema tena kumwambia kijana wake, "Wallahi limekuwa ni jambo zito kwa ammi yako kumwita asikuitike au akwitike lakini asikusaidie kitu, Wallahi maadui zake ni wengi na ni wachache mno watu wa kumsaidia ".

Imam Husein(a.s) alimbeba kijana huyo (baada ya kufariki) akamuweka mahali walipokuwa maiti wengine katika watu wa nyumba yake.

Hali ya mauaji ya watu wa Imam Husein(a.s) ilipofikia kuwa ya kutisha na kuhuzunisha aliazimia kupambana na maadui zake yeye mwenyewe binafsi.

Imam alianza kwa kutoa mwito akasema: "Je kuna mtetezi atakayeitetea heshima ya Mtume wa Mwenyezi Mungu(s.a.w.w) ?"

"Je kuna mchamungu amuogopaye Mwenyezi Mungu kwa ajili yetu sisi? (Kizazi cha Mtume)."

"Je yupo mwenye kutoa msaada hali ya kuwa anatarajia mema kwa Mwenyezi Mungu katika kutusaidia sisi?"

"Je kuna mwenye kutunusuru ambaye anatarajia radhi ya Mwenyezi Mungu kwa kutunusuru sisi?"

Mwito huu wa Imam Husein(a.s) uliwafanya wanawake waliokuwepo hapo walie kwa sauti na makelele mengi yakasikika.

Imam Husein(a.s) akaenda mpaka kwenye mahema walikokuwa wanawake akamwambia Bibi Zainab binti Ali. "Hebu nipe huyo mwanangu mdogo nipate kumuaga ."

Imam Husein(a.s) akamchukua mtoto huyo akawa anataka kumbusu, lakini Harmulah bin Kahil akamtupia mshale mtoto yule, ukampata shingoni akamuua.

Kuona hivi Imam Husein akamwambia Bibi Zainab mchukue mtoto huyu kisha yeye Imam akakinga viganja vyake, damu ya mwanaye ikawa inatiririka katika viganja.

Pindi viganja vyake vilipojaa damu, Imam aliirusha damu ile juu mbinguni kisha akasema "Si mazito kwangu mimi yaliyonipata kwa kuwa yote yanatendeka mbele ya macho ya Mwenyezi Mungu mtukufu".

Imam Al-Baqir(a.s) amesema "Hakuna hata tone moja la damu lililodondoka chini pale Imam Husein alipoirusha mbinguni damu ya mwanawe ".

Mpokezi wa habari hizi anasema, "Hali ilizidi kuwa ngumu kwa Imam Husein(a.s) kiu kali ilimshika akapanda katika tuta la ukingo wa mto Furat kwa nia ya kwenda kuchota maji yeye pamoja na nduguye Bwana Abbas bin Ali(a.s) .

Lakini wanajeshi wa lbn Saad wakamzuia na mtu mmoja katika Bani Daarama akamtupia Imam Husein mshale ukamchoma Imam(a.s) katika midomo yake mitukufu.

Imam(a.s) akauchomoa mshale huo na akakinga viganja vyake chini ya midomo yake, damu ikiwa inatairirka ndani ya viganja, vilipojaa akairusha damu hiyo juu kisha akasema "Ewe Mwenyezi Mungu nakushitakia mambo anayofanyiwa mtoto wa Binti ya Mtume wako". Kisha maadui hao wakamzuia Abbas bin Ali(a.s) na wakamzingira kila upande mpaka wakamuuwa.

"Imam Husein(a.s) alilia sana kwa kuuawa Abbas(a.s) ".

Baada ya kuuwawa Abbas(a.s) Imam Husein aliwaita watu hao wapambane naye mmoja mmoja.

Alipigana nao kwa njia hii ikawa kila aliyejitokeza Imam(a.s) alimuuwa mtu huyo.

Imam Husein(a.s) aliendelea kupambana nao mpaka walipomzunguka yeye pamoja na farasi wake akasema kwa sauti kubwa "Ole wenu enyi wafuasi wa kizazi cha Abu Sufiyan, ikiwa ninyi hamna Dini na hamuogopi (adhabu) mtakaporudi (kwa Mwenyezi Mungu) basi kuweni watu huru katika dunia yenu hii, na tazameni utu wenu iwapo ni Waarabu kama mnavyodai".

Shimri alijibu kwa kusema: "Wasemaje Ewe mwana wa Fatma?"

Imam(a.s) akasema: "Nasema kwamba, hakika mimi nakupigeni nyinyi nanyi mwanipiga mimi, lakini wanawake hawa hawana kosa lolote, basi hebu wazuiyeni watu wenu hawa waovu na wajinga, wasinivunjie hashima yangu muda wote nitapokuwa ni mzima.

Shimri akasema "Hilo ni jukumu lako Ewe Mwna wa Fatma". Basi wakamuelekea ili wamshambulie, ikawa huwashambulia nao humshambulia huku akitafuta maji azime kiu aliyokuwa nayo lakini hakupata.

Mashambulizi dhidi ya Imam Husein yalizidi mpaka akapatwa na majeraha sabini na mbili yaliyotokana na mishale.

Imam(a.s) alichoka na ikambidi asimame ili apumzike hali ya kuwa mnyonge kutokana na mapambano.

Wakati akiwa amesimama lilitupwa jiwe ambalo lilimpiga usoni mwake.

Imam(a.s) alichukua nguo yake akawa anapangusa damu inayotiririka usoni kutokana na jiwe lililompiga.

Basi ghafla ulimjia mshale wenye ncha tatu uliopakwa sumu ukamchoma moyoni, hapo Imam Husein(a.s) akasema "Nakufa kwa Jina la Mwenyezi Mungu na kwa ajili ya Mwenyezi Mungu na katika mila ya Mjumbe wa Mwenyezi Mungu".

Kisha alinyanyua kichwa chake juu akasema: "Ewe Mola wangu wewe unafahamu kwamba, watu hawa wanamuuwa mtu ambaye ni mtoto wa Mtume hali ya kuwa hapana katika Dunia hii mtoto wa Mtume isipokuwa yeye ".

Imam Husein(a.s) akauchomoa ule mshale kupitia mgongoni, basi damu nyingi sana ikamtiririka mfano wa bomba linavyotoa maji. Hali hii ikamfanya Imam(a.s) asiwe na nguvu kabisa ya kupigana bali akabaki amesimama.

Maadui wale wakawa kila ajaye kutaka kumshambulia Imam(a.s) hukimbia na kurudi kwa kuchelea kwamba jukumu la kumuua Imam Husein(a.s) lisijekuwa juu yake pindi atapokutana na Mwenyezi Mungu (s.w.t).

Baadaye mtu mmoja aitwaye Malik bin Nasir akamfuata Imam(a.s) akamtukana na hatimaye akampiga upanga wa kichwani ukapasua kilemba alichukuwa kavaa nakumjeruhi kichwani.

Kilemba hicho kikajaa damu iliyokuwa inavuja.

Mpokezi wa habari hizi anaendelea kusema:

Imam(a.s) aliomba kitambaa ili afunge kichwa chake, kisha akaomba tena apewe kofia, akapewa na akavaa halafu juu yake akafunga kilemba chake.

Jamaa hao walikaa muda fulani kisha wakamrudia tena Imam wakamzunguka kila upande.

Mambo yalipofikia katika hali hii, Abdallah bin Hasan bin Ali(a.s) kijana ambaye alikuwa hata bado hajafikia umri wa miaka kumi na mitano alitoka mahali walikokuwa wanawake akaenda kusimama karibu na Imam Husein(a.s) .

Bibi Zainab binti Ali(a.s) akamfuata kijana yule ili amzuie asiende alipo Imam kumuepusha asiuawe, lakini kijana huyo akakataa sana sana kurudi na akasema "Wallahi sitamuacha Ami Yangu" (peke yake).

Mara Bahri bin Kaab wanahistoria wengine wanasema Hurmula bin Kahili akarusha upanga kumpinga Imam Husein(a.s) yule kijana akasema "Ole wako Ewe mtoto wa Mwanamke muovu unataka kumuuwa ami Yangu?"

Kijana huyu alikinga mkono wake ili upanga ule usimpate Imam Husein(a.s) , lakini ukampata na kumkata mkono ukabakia unaning'inia kwa kushikiliwa na kipande cha ngozi kilichobaki.

Basi kijana huyu akapiga ukelele kutokana na maumivu akasema "Ewe Ami Yangu!!!" Imam Husein(a.s) akamshika na kumkumbatia kisha akamwambia "Ewe mwana wa Ndugu yangu vumilia kutokana na yaliyokupata na ujihesabu kwamba umokatika wema, kwani Mwenyezi Mungu atakukutanisha na wazazi wako wema."

Mara ghafla, Hurmula bin Kahil akamtupia mshale kijana huyu hali akiwa miguuni mwa Imam Husein akamuuwa.

Watu hawa waliendelea kumshambulia Imam(a.s) , kwa mishale toka kila upande akawa kama nungunungu majeraha mwili mzima, Salehe bin Wahab Al-Mariy alimchoma Imam kwa mkuki kiunoni.

Basi Imam alidondoka kutoka juu ya farasi wake mpaka chini hali ya katanguliza upande wa kulia wa uso wake na akasema "(Nakufa) kwa Jina la Mwenyezi Mungu na kwa Ajili ya Mwenyezi Mungu na katika Mila ya Mjumbe wa Mwenyezi Mungu".

Bibi Zainab binti Ali alitoka kwenye hema huku analia na kusema, "Ooo!!! Masikini ndugu yangu, Ee!!! Kiongozi wangu, Ee!!! Wana hali gani watu wa Nyumba yako, laiti mbingu ingeliifunika ardhi na laiti milima nayo ingeporomoka (yote haya ilikuwa ni maneno ya kuonyesha uchungu na huzuni kwa yaliyomfika nduguye.

Na hapa ndipo yalipotokea yaliyotokea ambayo siwezi kuyataja.

Maombolezo Ya Kifo Cha Imam Husain(a.s)

SHARTI YA KUCHAPA

Sharti ya kuchapa au kusambaza ni kutaja rejeo hili. haki zote zimehifadhiwa na Taasisi ya Al-Hasanain Taasisi ya Imamu Husein(a.s)

Site ya Al-Imaamaini Al-Hassanaini(a.s) ya usambazaji wa utamaduni wa Kiislamu na mafunzo ya Kidini.

MWISHO WA KITABU


YALIYOMO

,MAOBOLEZO YA KIFO CHA IMAM HUSEIN(A.S) 1

KIMEANDIKWA NA: SAYYID ABDUL HUSAIN SHARAFUDDIN 1

MTARJUMI: MUSABBAH SHABAN 1

DIBAJI 1

MAOBOLEZO YA KIFO CHA IMAM HUSEIN(A.S) 2

KIMEANDIKWA NA: SAYYID ABDUL HUSAIN SHARAFUDDIN 2

MAJLIS YA KWANZA 2

RUHUSA YA KULIA 2

MAJLIS YA PILl 4

RUHUSA YA KUOMBOLEZA 4

MAJLIS YA TATU YAH: 6

KUSOMWA HABARI ZA WALIOKWISHA PITA HAPO KALE 6

MAJLIS YA NNE 7

VIKAO KWA AJILI YA KUHUZUNIKIA WAFU 7

MAJLIS YA TANO 9

KUMTOLEA SADAKA MAITI 9

KUZALIWA KWA AL-IMAM HUSEIN BIN ALI(A.S) 9

KUTHIBITI UIMAM KWA HUSEIN(A.S) 11

MAOBOLEZO YA KIFO CHA IMAM HUSEIN(A.S) 16

SAFARI YA IMAM HUSEIN(A.S) TOKA MADINA HADI MAKKA 16

MAJLISI YA SITA 18

YALIYOTOKEA MAKKA BAADA YA IMAM HUSEIN(A.S) KUFIKA HAPO 18

MAJLISI YA SABA 22

YALIYOTOKEA AL-KUFAH BAADA YA IBN ZIYAD KUFIKA HAPO 22

MAJLISI YA NANE 25

MAAFA YALIYOMPATA MUSLIM BIN AQIL 25

MAOBOLEZO YA KIFO CHA IMAM HUSEIN(A.S) 31

MAJLISI YA TISA 31

IMAM HUSEIN(A.S) AAZIMIA SAFARI YA IRAQ 31

MAJLISI YA KUMI 33

IMAM HUSEIN SAFARINI KWENDA IRAQ 33

MAJLISI YA KUMI NA MOJA 39

IMAM HUSEIN(A.S) AWASILI KARBALA 39

MAOBOLEZO YA KIFO CHA IMAM HUSEIN(A.S) 42

MAJLISI YA KUMI NA MBILI 42

MAPAMBANO DHIDI YA ASKARI WA IBN ZIYAD 42

SHARTI YA KUCHAPA 52

MWISHO WA KITABU 52

YALIYOMO 53



[1] . Taz. Tafsirul-Kashaaf ya Az-Zamakhshari.

[2] . Taz. Tafsirul-Kashaaf.

[3] . Taz. Ir-Shad As-Saari cha Al-Qas-Talan Uk.318 Juz. 3.

[4] . Taz. AI-Istiiab na AI-Isaba.

[5] . Taz. Maarij al-Usul.

[6] .Taz. Juz. 2. Uk. 8 Al-Iqdul Farid. Taz. Tarekh Ibn Jarir na Ibn Athir

[7] . Taz. Siratul-Halabiya Uk.462 Juz.1.

[8] . Taz. Musnad Imam Ahmad Juz. 1 uk. 85.

[9] . Taz. Sahihi Bukhari Juz. 2 Uk. 207.

[10] . Taz. Sahihi Muslim Juz. 1 Uk. 372.

[11] . Taz. Tafsiri Al- Kashaaf.

[12] . Taz. Kitabu cha Qawaid AI-Lughatil-Arabiya Juz.3 Uk.48 chapa ya pili mwaka 1973-1393.

[13] . Ibara hii haiko ndani ya Kitabu cha asili bali tumeiongeza tu ili kuonesha udhaifu wa Yazid.